John Wesley aliishi ungereza katika miaka ya 1703-1791. Alihubiri injili kwa wale watu maskini ambao wasingekubaliwa ndani ya makanisa. Aliishi kwa uangalifu, akitafuta kumheshimu Mungu katika kila jambo la maisha yake ikiwemo matumizi ya fedha. Alifundisha ya kwamba wakristo wakipata fedha, wanapaswa kuweka akiba kwa kadiri wanavyoweza na kisha tena kutoa kwa kadri wanavyoweza. Alikuwa mfano mzuri kwenye nidhamu katika kutumia Kanuni za kifedha. Alipunguza matumizi yake ya mwaka, ili awe na fedha za ziada ambazo angezitoa kama sadaka. Mapato yake yalipoongezeka hakuongeza matumizi yake bali alitoa kila kilichokuwa ziada. Hata ingawa mapato yalikuwa paundi 30,000 katika kipindi chake cha Maisha, wakati wa kifo chake alikuwa amebaki na sarafu chache tu kama mali yake. Wesley alitambua kwamba Mungu aliwaaminia wanadamu kusimamia fedha kwa niaba yake, na Wakristo lazima wafuate kanuni za kimungu wanaposhughulika na fedha.
Utangulizi
Agano Jipya linataja fedha mara nyingi zaidi ya masomo mengine mengi, sio kwamba fedha ni ya muhimu zaidi sana kwa Mungu lakini ni kwa sababu watu wengi wamekuwa na shida na fedha.
Mungu muumba ndiye mmiliki wa watu wote na mali zao. Kama Wakristo sisi ni wa Mungu kwa njia ya kipekee kwa sababu ametukomboa. Kama wakristo tunapaswa kujichukulia kama wasimamizi wa mali ambayo inahitajika kutumika kwa utukufu wa Mungu.
Sio makosa kujifurahisha na vitu vizuri. Mungu anafurahia kutubariki kama tutapokea kila kitu kwa shukrani na unyenyekevu.
Lakini fedha ni mojawabo ya hatari za kiroho kwa watu wengi.
Maonyo ya maelekezo kwa matajiri
►Inamaanisha nini kuwa tajiri?
Kuna sababu tofauti tofauti za mtu kuweza kuchukuliwa kuwa Tajiri.
Ukiwa na fedha ya kuweza kunua zaidi ya mahitaji ya msingi wewe ni tajiri kuliko angalau nusu watu duniani. Watu wengi hufanya kazi kila siku kupata chakula cha siku; kama kitu chochote kitafanyika kuwazuia kufanya kazi, basi hawatakuwa na chakula.
Watu humchukulia mtu kuwa ni tajiri kwa sababu ana mali nyingi kuliko watu wengi katika jamii yake. Watu wanamchukulia kuwa yeye ni wa tabaka la juu la kimaisha. Anaweza kufurahia anasa ambazo watu wengi hawawezi kununua. Ana uwezo wa kushawishi watu walio na mamlaka. Watu wako tayari kumtumikia kwa sababu ya mali aliyonayo.
Biblia ina maagizo na maonyo maalum kwa watu kama hao.
Onyo kali ni sentensi ya Yesu kuwa ni vigumu sana kwa tajiri kuingia mbiguni (Mathayo 19:24).
Tunaweza kuelewa zaidi hatari za utajiri kutokana na ujumbe wa Mtume Paulo kwa matajiri.
► Mwanafunzi asome 1 Timotheo 6:17-19 kwa niaba ya kikundi.
Paulo aliwaonya matajiri kutojichukulia kuwa wenye tabaka la juu kuliko wengine. Kuna jaribu la watu matajiri kujiona kuwa hao ni wenye bora zaidi kuliko wengine. Yakobo anaonya kanisa dhidi ya kufanya kosa hilo hilo, kuheshimu watu kwa misingi ya mali au tabaka (Yakobo 2:1-4).
Mtu tajiri hapaswi kuhisi yuko salama kwa sababu ya utajiri wake bali amtegemee Mungu. Ni vigumu zaidi kwa mtu tajiri kufikiri kwamba anahitaji msaada wa Mungu na wakati ana akiba ya fedha. Kuna jaribio lakutojali mambo ya kiroho kwa sababu ya kutohisi haja ya usaidizi wa Mungu (Kumbukumbu la Torati 8:6-18).
Matajiri wanapaswa kuwa watu watoaji kwa ukarimu na watimize mambo mazuri kwa fedha zao.
Moja ya hukumu za matajiri wa kidunia katika Yakobo 5:5 ni kuwa wanaishi kwa kwa anasa wakati wengine wanateseka. Mengi mazuri yanawezwa kufanikishwa kwa kwa utoaji wa busara. Fedha haiwezi kununua furaha lakini inaweza punguza taabu nyingi. Ni makosa kupuuza mateso ya wengine huku ukiishi Maisha ya anasa.
Kupitia Amosi Mungu alidhihirisha moyo wake kwa haki ya binadamu, (rehema na huruma kwa maskini na wanao dhulumiwa) kwa haya maneno: “lakini hukumu na iteremke kama maji, na haki kama maji makuu” (5:24). Mungu alitangaza hukumu juu ya mafanikio wakati wakati ambapo mafanikio ulisababisha kubweteka, kujifurahisha na kutojali kuhusu mahitaji ya maskini (Amosi 6:1; 3-6; Amosi 8:4-7, 11-12).
Kila mkristo anapaswa kujitoa kuwasaidia maskini na wale wanaodhulumiwa, toa fungu la kumi kusaidia kanisa lako la mahali pamoja, na kutoa ili kusaidia kazi Umisheni ili kueneza injili. John Wesley alitoa sababu tatu ambazo zilisababisha kanisa la wakati wake lisilete mabadiliko katika dunia:
1. Kukosa mafundisho yenye uzima
2. Kukosa nidhamu na kuwajibika
3. Kukosa kujidhabihu
Kupenda Fedha
► Mwanafunzi asome 1 Timotheo 6:8-10 kwa niaba ya kikundi.
Maonyo kuhusiana na fedha hayawaendei matajiri pekee. Watu wengi masikini wanafikiri kuwa hawawezi kuwa na furaha kwa sababu wao ni maskini. Biblia inatueleza kwamba kupenda fedha ndiyo chanzo cha uovu wa kila aina. Onyo hilo inatumika kwa kila mtu.
Kupenda fedha kamwe hakutoshelezi. Mtu anayependa fedha hatatosheka na kiwango chochote (Mhubiri 5:10). Biblia inatuambia kuwa tunapaswa tuepuke tamaa ya fedha na tutosheke na mahitaji yetu ya msingi (Waebrania 13:5).
Mtu mwenye hamu ya kuwa tajiri ana majaribio mengi ya kuathiri tabia yake. Katika mchakato wa kuwa tajiri mtu anaweza kuiacha imani yake na kupata huzuni nyingi badala ya furaha aliyotarajia.
Wakati mwingine viongozi wa dini huvutia wafuasi wengi kwa kuwaahidi kupata mali. Wao husema kuwa mtu mwenye imani ni lazima awe na mali. Watu wengi katika jamii maskini wanavutiwa na hizi ahadi kwa sababu ya hali ngumu ya maisha. Hawa viongozi huongea na kuhubiri kuhusu fedha kila mara na wanajivuna kwamba wanaweza kuonyesha alama ya mafanikio kama ambavyo watu wa kidunia huonesha.
Biblia inasema kuwa utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa. Mtu anayetafuta mali kwa njia za kidini yuko katika hatari sawa sawa na mtu yeyote wa kidunia anayetafuta mali. Kanisa ambalo linatoa ahadi ya utajiri huwavutia watu ambao hawajaokoa kwani huvutwa kutokana na matamanio yao binafsi. Hata hivyo Makanisa haya yamejazwa na watu walio na tumaini ambapo hawatapata kitu walichoahidiwa. Watu pekee ambao hutajirika na injili ya mafanikio ni wahubiri wanokusanya sadaka kutoka watu wanaowaamini.
► Mwanafunzi asome Filipi 4:10-13 kwa niaba ya kikundi.
Paulo alikuw anashukuru kwa sababu waamini wa Filipi walikuwa wameta sadaka kwa ajili yake. Aliwaambia kuwa alikuwa amejifunza kuridhika katika hali zote, hata njaa. Sentensi hii inatuonyesha kuwa Paulo hakuwa na wingi wa fedha. Alisema kuwa kwa msada wa Mungu angefanya yote. Muktadha wa sentensi hiyo inaonyesha kuwa alimaanisha kuridhika katika hali yote na kuwa mwaminifu kwa Mungu.
Uaminifu
► Mwanafunzi asome Mithali 11:1 kwa niaba ya kikundi.
Hii aya inaongea kuhusu mizani inayotumika kuuza kitu kwa kipimo cha uzito, kama matunda au mboga au nyama. Wakati mwingine watu wana mizani ambayo imebuniwa kutoa uzani wa uongo ili kupata fedha za ziada. Aya hii inasema Mungu anachukia kutokuwa mwaminifu.
Watu wengi wamefanya vitu vya kutoaminika kwa sababu ya fedha. Somo linalofuata katika kozi hii ni kuwa mwaminifu.
Kumuamini Mungu
Mtume Paulo aliwaandikia wakristo wa Filipi akiwahidi kuwa Mungu atatimiza mahitaji yao. Hii ni ahadi ya ajabu. Tunapaswa kuangalia kifungu cha Biblia pale inapotokea ili kuelewa hali iliyokuwapo.
► Mwanafunzi asome Wafilipi 4:15-19 kwa niaba ya kikundi.
Kanisa lilimtumia Paulo msaada wa kifedha. Alisema ilikuwa ni dhabihu kwa Mungu. Aliwaahidi kuwa Mungu atakutana na mahitaji yao. Hakuwahidi ongezeko kubwa la fedha zao.
Ahadi haikuwa kwa watu ambao hawahajibiki au wabadhilifu. Ilkikuwa ni ya watu ambao walikuwa wasimamizi wa fedha zao kulingana na vipaumbele vya kiroho.
► Mwanafunzi asome Mathayo 6:25-33 kwa niaba ya kikundi.
Yesu aliongoea kuhusu namna ambavyo Mungu anawalisha ndege wa angani na kuyavalisha maua na akaahidi kuwa atashughulikia mahitaji yetu. Anatuambia tusiwe wenye hofu kuhusu kuishi kwetu. Ametuahidi kuwa tukitanguliza ufalme wa Mungu atakutana na mahitaji yetu.
Watu wengi wana hofu sio kuhusu leo bali siku zijazo. Mungu hajaahidi kutoa kila kitu kabla ya wakati husika. Kumbuka katika Agano la Kale wakati mana ilipoanguka, ilikuja kila siku (Kutoka 16). Vivyo hivyo, Yesu akasema tuombe kwa ajili ya “riziki wetu” wa kila siku (Mathayo 6:11). Mungu anataka tumuamini kila siku.
Yakobo alisema kuwa Mungu amewafanya maskini “matajiri kwa Imani” (Yakobo 2:5). Watu maskini wana fursa nzuri ya kumtegemea Mungu kuliko watu ambao wanautoshelevu wa kifedha.
Kumuamini Mungu hakumaanishi kuwa hatuwajibiki. Mara nyingi Mungu ametupatia mahitaji yetu kupitia kazi tunazofanya (Waefeso 4:28). Kama mtu hayuko tayari kufanya kazi, asitarajie Mungu atampa mahitaji yake, na watu wengine wasilazimike kumpa (2 Wathesalonike 3:10).
Tusitarajie riziki toka kwa Mungu kutafanya kuwa matajiri. Mungu anawabariki watu wachache na utajiri, lakini utajiri siyo mapenzi ya Mungu kwa kila mtu. Mtu ambaye ana shauku kubwa ya utajiri atakuwa na shida za kiroho.
Rasilimali Zinazozalisha
Rasilimali zinazozalisha kazi ni vitu ambavyo watu wanavyo kwa ajili ya kuzalisha. Mfano ni ardhi, vifaa vya matumizi au kompuyta. Mtu anaweza kutumia rasilimali zinazozalisha ili kupata faida lakini lazima azitunze bila kuziuza vinginevyo uzalishaji utakoma. Biblia inataja kuhusu rasilimali zinazozalisha katika Mithali 14:4, “Zizi ni safi ambapo hapana ngo’mbe; bali nguvu za ng’ombe zaleta faida nyingi.”
Mtu aliye maskini huenda asielewe dhana ya rasilimali zinazozalisha. Kwa mfano anaweza kudhania kuwa rafiki yake ana fedha nyingi kwa sababu ana vifaa vya bei ghali mno, au compyta, au gari. Anafikiri kuwa rafiki yake au mtu wa jamii yake aliye na kitu kama hicho anapaswa kumpa fedha wakati anahitaji. Hata hivyo chochote kati ya vitu hivi vinaweza kuwa baadhi ya rasilimali zinazozalisha ambazo haziwezi kubadilishwa kuwa fedha bila kumfanya mtu apoteze mapato yake.
► Ni mifano gani mingine ya rasilimali zinazozalisha ambazo zinapatikana katika eneo lako?
Mtu asipoelewa namna rasilimali zinazozalisha zinavyofanya kazi kwa wengine, anaweza asielewe kwamba rasilimali kama hiyo ingeweza kufanya kazi kwake. Hawezi kujua ni nini hasa anachohitaji auni aina gani ya usaidizi ambao anahitaji ili kubadilisha hali yake. Anaweza kuueleza msaada kama hatua ya haraka na fupi ambayo inasaidia katika harakati zake za kila siku badala ya mabadiliko halisi ya maisha.
Sababu moja ya umaskini ni ukosefu wa rasilimali zinazozalisha. Kama mtu ambaye yuko kwenye umaskini haoni haja ya kupata, kudumisha na kuweka akiba ya rasilimali zinazozalisha, hataweza kuondolewa katika hali ya kutegemea msaada.
Katika mila fulani, ni vigumu sana kwa mtu kuweka akiba na kutengeneza rasilimali za zinazozalisha kwa sababu wale wanao mzunguka wanatarajia yeye awashirikishe kila kitu. Hawaelewi kwa nini anakusanya fedha wakati mtu mwingine anahitaji fedha. Wanatarajia kugawana alichonacho hata kama wamekuwa sio wawajibikaji.
Mkristo ni lazima aheshimu matarajio ya mila zake lakini pia atumie kanuni za Biblia. Maandiko yanatueleza kuwa hatulazimishwi kumsaidia mtu ambaye hawajibiki (2 Wathesalonike 3:10). Mtu akitoa rasilimali zinazozalisha na kisha akasaidia wengine ambao hawawajibiki, wote watakuwa maskini.
Maandiko yanadokeza aina ya mafanikio ambayo Mungu hutoa ni kwamba watu wawe na rasilimali zao za zinazozalisha. Nabii Mika alisema kuwa jamii iliyobarikiwa, kila mtu atamiliki vikamilifu “mzabibu wake na mtini” (Mika 4:4). Hiyo inahusu mali ya kibnafsi inayomilikiwa na njia za uzalishaji. Sehemu zingine kilimo kinaweza kisiwe njia halisi ya uzalishaji lakini kanuni kuu ni kuwa watu waliobarikiwa wanapaswa wawe na kile wanachohitaji kuzalisha rasilimali.
Mara nyingi watu maskini ambao wanakuwa wakristo huanza kustawi zaidi, sio kwa sababu ya baraka za moja kwa moja kutoka kwa Mungu lakini kwa sababu ya mtindo wao mzuri wa maisha. Wanaacha kuharibu fedha kwa vitu kama pombe, kucheza kamari na aina mbaya ya burudani. Wanakuwa wafanyakazi wazuri na sifa zao zinakuwa bora. Wanaposaidia Huduma, Mungu anawabariki. Mara nyingi kizazi cha pili cha familia ya kikristo wako katika hali nzuri kulio kizazi cha kwanza.
► Ni njia zipi ambazo watu katika mazingira yako wanaweza kufanya kazi na kuweka akiba ili kuboresha hali yao ya kifedha?
Kamari
Kamari ni kuhatarisha fedha katika jaribio la kupata fedha bila jasho. Mtu yeyote anayeshinda anachukua fedha kutoka kwa mwingine ambaye amepoteza, bila kutoa chochote kama malipo. Watu wengi huwa waraibu wa kucheza kamari, hupoteza fedha zao, na hushindwa kutunza familia zao. Watu wengi wametumia fedha ambayo ilikuwa ya mtu mwingine kucheza kamari wakitumaini kushinda ili waweze kulipa deni lao. Kuna watu wengi wako jela kwa kuiba ili wacheza kamari. Watu wengi ambao ni maskini hucheza kamari kwa sababu wanafikiri hawana tumaini ya kubadilisha hali yao ya maisha ila tu kupata bahati na kushinda fedha.
Kamari ni kinyume cha kanuni nyingine za kikristo:
1. Kanuni ya kupata mali kwa kufanya kazi (Waefeso 4:28)
2. Kanuni ya kuridhika (1 Timotheo 6:6)
3. Kanuni ya kupanda na kuvuna (Wagalatia 6:7).
Pia, Mungu anataka tutoe huduma au uzalishaji wa bidhaa kwa faida badala ya kuchukua fedha kutoka kwa mtu kwa bahati. Kamari inadhurukwa sababu inalevya na inaongeza visa vya uhalifu.
Kamari ni kinyume na kumtegemea Mungu. Mtu anapaswa kujiuliza, “Je namwamini Mungu kwamba ananitunza?” “Naweza kumuomba Mungu ili anipatie utoshelevu wangu?” “Je ninaamini kuwa njia ambayo Mungu ananipa utoshelevu wangu ni kwa kuhatarisha fedha kwa kucheza kamari, nikitumaini kuchukua fedha kutoka kwa mtu mwingine?” “Je ninafikiri kuwa Mungu atanizawadia nikicheza kamari kwa kunifanya nishinde fedha nyingi?” Mtu anayecheza kamari hamtumaini Mungu katika hali yake ya kifedha. Tunapomwamini Mungu kiukweli, tunatii maagizo yake yaliyo wazi kwetu, tukijua ya kwamba atatupatia mahitaji yetu kwa uaminifu tunapotii.
Deni
Mtu anapokopa fedha, yeye hudhani kuwa ataweza kulipa mkopo kutokana na fedha apatazo siku za mbeleni. Kwa hivyo kukopa ni kutumia Fedha ya siku za mbele hata ingawa mahitaji mapya yatakuwepo.
Biblia inasema kuwa mkopaji ni mtumwa wa akopeshaye (Mithali 22:7). Mkopaji anajenga wajibu ambao unapunguza uhuru wake.
Aina fulani ya kukopa ni mbaya zaidi kuliko nyingine. Mtu anapokopa fedha kwa sababu ya mahitaji ya msingi kama vile chakula, anajitia katika hali mbaya zaidi. Chakula kitatumika, na mkopo bado utabaki, na atakuwa maskini zaidi kuliko alivyokuwa awali.
Mtu anapokopa fedha kwa sababu ya kitu kisicho cha lazima, kama vile mapambo ya kibinafsi, mavazi yasiyohitajika, burudani, au mapambo ya nyumbani, anatumia fedha zake za baadaye. Anajipunguzia uhuru wake wa siku za baadaye; siku za baadaye hataweza kuchagua kununua vitu kwa sababu fedha imeshatumika.
Baadhi ya biashara hukopesha fedha kwa riba iliyo juu sana. Watu ambao wamekopeshewa muda usio mrefu hujikuta wanadaiwa fedha zaidi kuliko zile walikopshewa. Baadhi ya maduka yanauza vitu kwa mkopo kwa riba ya juu sana. Watu hatimaye hulipa kwa bei ya juu sana kwa vitu ambavyo vimenunuliwa kwa mkopo kwa sababu hawako tayari kusubiri mpaka wapate fedha za kutosha kulipa kwa bei ya kawaida.
Wakati mwingine watu hukopa kwa sababu yakutaka kuwa na harusi ya kifahari kama inavyotarijiwa na tamaduni zao. Wanaanza ndoa yao kwa deni kubwa. Kanisa kama familia ya imani inapaswa kusaidia washirika wake kujenga tamaduni mpya au kutafuta mbinu za kufanya harusi iwe ya kupendeza bila kuwa na gharama kubwa kupita kiasi.
► Mwanafunzi asome Warumi 13:7-8 kwa niaba ya kikundi.
Mistari hii inateleza kuwa tulipe kile tunachodaiwa na wengine. Tunadaiwa heshima na utiifu kwa mamlaka. Tunadaiwa kodi na serikali. Sentensi ya kwanza ya aya ya 8 inafupisha sentensi katika aya ya 7. Hatupaswi kushindwa kumpa yeyote kile tunachostahili kumpa. Hii haimaanishi kwamba tusikope kamwe, kwa sababu tukilipa kama ilivyokubaliana na mkopeshaji, hatujashindwa kumpa kama inavyotakiwa.
Ni wizi kwa mtu kukopa kama hana nia ya kulipa, au kukopa na kuamua baadaye kutolipa (Zaburi 37:21).
Sheria za Agano la kale kwa sehemu kubwa zinaelekezwa kwa taifa la Isreal kama jamii ya wakulima. Watu wengi waliishi kwa kutegemea ukulima na kuzalisha waliyohitaji nyumbani kwao. Familia zilimiliki ardhi moja kwa vizazi vingi. Kwa hivyo ilikuwa ni vigumu kwa mtu kukopa fedha kununua ardhi au kuanzisha biashara. Kama mtu alikopa fedha, ilikuwa ni kwa sababu alikuwa katika hali mbaya na alihitaji fedha kwa mahitaji ya kimsingi. Mungu alitaka Israel wawe familia ya Imani ambayo ilishughulikia washirika wake. Mungu aliwaambia wakopeshe fedha bila kutoza riba (Kutoka 22:25). Sifa moja ya mtu mwadilifu inavyoelezwa katika Zaburi 15 ni kuwa hakopeshi fedha kwa riba (Ezekieli 18:5-9 inafanana na Zaburi 15).
Sio makosa kwa mwekezaj kuzalisha riba anapokopesha mtu fedha kumsaidia kuanza biashara (Mathayo 25:27). Riba ni zawadi ya mwekezaji kwa kufanya biashara iwezekane.
Watu wanaofanya biashara na maskini hawapaswi kufikiria tu jinsi ya kupata faida (Mithali 22:16a). Ni makosa kuuza vifaa vyenye viwango duni au kutoza bei zisizo za haki, kwa sababu maskini hawana chaguzi. Ni makosa pia kubuni mikopo au kuuza vitu kwa mkopo kwa kusudi ya kutengeneza faida kubwa kutoka kwa watu ambao wamekopa kwa sababu ya hali ngumu. mfanyabiashara anapaswa kutafuta njia ua kuboresha hali ya wateja wake.
Nabii Ezekieli alisema kwamba dhambi ya Sodoma haikuwa tu usherati lakini pia watu walioishi kwa anasa na “walishindwa kuimarisha mkono wa maskini” (Ezekieli 16:49). Mungu anatupa wito sio tu kuwasaidia maskini, bali kusaidia kwa njia ya mikakati ya kuwafanya wawe na nguvu.
Sheria za Mungu kwa Israel ya kale zinatuonyesha vipaumbele vyake. Leo sheria za mataifa yetu sio sawa kama sheria Mungu alizowapa Israel, lakini mapenzi na kanuni zake Mungu hazijabadilika. Kanisa linapaswa kutafuta njia ya kuwapa nguvu maskini, kwanza kujali familia ya Imani, halafu kuleta tofauti katika jamii.
Bajeti
Watu wengine hutumia fedha zao zote mara tu wanapopewa. Mara nyingi wanateseka na ukosefu wa mahitaji kabla ya kupata fedha tena. Hawawezi kuwajibika kwa wengine.
Bajeti ni mpango wa kudhibiti matumizi ya kawaida. Watu wengi hupata matumizi yasiyotarajiwa nyakati za usoni, na hivyo inapaswa kuweka akiba ya fedha kwa ajili ya mahitaji ya siku za mbele. Kwa mfano, mtu anaweza kuwa amepanga nyumba na anaweza kuwa analipa kwa mwezi au mwaka. Anahitajika kutunza mara kwa mara sehemu ya mapato yake ili aweze kulipia kodi ya nyumba wakati unapofika. Kama kodi yake ya nyumba ni ya mwaka, atakuwa ameshikilia baadhi ya fedha kwa muda mrefu, na kuna jaribu la matumizi, lakini anapaswa ahifadhi hizo fedha na afikirie kwamba tayari zimeshatumika.
Fedha za kwanza kuhifadhiwa inapaswa iwe fungu la kumi (Methali 3:9-10). Unapaswa ujitoe kutoa asilimia 10 ya mapato yako kwa ajili ya huduma. Usisubiri kuona kama una fedha ya ziada ya fungu la kumi baada ya matumizi. Mungu atabariki uaminifu wako.[1]
Baada ya mahitaji ya msingi kushughulikiwa na mapato yaliyosalia, mtu lazima ahifadhi fedha kwa mambo ya dharura. Anapaswa kuhifadhi fedha kwa sababu ya kujiboresha, kama vile kutunza fedha kununua nyumba yake binafsi. Anapaswa pia kujaribu kuwekeza fedha katika kuongeza mapato yake. Kununua vifaa ambavyo vitamsaidia alipwe zaidi sehemu yake ya kazi ni mfano wa uwekezaji mdogo.
Mtu ambaye anarasilimali za kuzalisha (kitu kinacho saidia uzalishaji) kama vile gari au jengo ni lazima fedha ikadiriwe (bajetiwe) kwa ajili ya matengenezo ya rasilimali. Kama mtu atapata faida na gari lake lakini hatunzi fedha, hatakuwa na uwezo wa kulipia matengenezo makubwa ya gari au kunua lingine, na faida yake mwishowe itaisha.
Mtu asiyetengeneza bajeti kwa mara nyingi hataweza kutimiza majukumu yake. Anaweza kutegemea wengine na kushindwa kusaidia wengine. Hali yake haitaimarika kwa sababu hajawekeza kwa njia yeyote.
Yesu alisema kuhusu Msamaria Mwema aliyemsaidia mtu aliyejeruhiwa (Luka 10:25-37). Tazama kuwa Msamaria alikuwa na fedha na punda wa kutumia kumbeba aliyejuruhiwa. Ingekuwaje kama Msamari mwema angekuwa ameuza punda wake na kutumia fedha zote? Hata kama angekuwa na shahuku ya kusaidia, angepungukiwa na uwezo wake wa kuingilia kati kwenye hiyo hali.
Kufanya bajeti kunasaidia mtu kujiandaa kwa mahitaji yake, kuwajibikia kwa wale ambao wanamtegemea, kuwekeza kwenye Maisha yake ya baadaye, kabiliana na dharura, na kusaidia huduma.
[1]Mfano wa kina kuhusu fungu la kumi inafanywa katika kozi ya Shepherds Global Classroom Mafundisho na Mazoezi ya Kanisa, inapatikana kwa https://www.shepherdsglobal.org/courses
Familia ya imani
Katika siku za mwanzo za kanisa, muda mfupi baada ya Pentekoste, waumini walijitoa sana kwa familia ya Imani na wakahakikisha kuwa mahitaji ya kila mtu yalitimizwa. Walishirikiana mali zao, na hakuna yeyote aliyesema kuwa chochote kile ni chake. Wengi wao waliuza mali zao na wakatoa fedha kwa kanisa (Matendo ya Mitume 2:44-45). Hata ingawa hatutarajii kuwa Maisha katika kanisa yatakuwa sawa kama wakati huo, tunaona kuwa kanisa likiwa katika ubora wake kama kuna ukarimu na kujitolea kulinda familia.
Waamini wa Thesalonike walihakikisha kuwa washirika wote walipata chakula lakini baadhi yao hawakupenda kufanya kazi. Hao watu walikuwa wanaishi kwa anasa, wakitegemea ukarimu wa kanisa. Paulo hakuambia kanisa kuwa walifanya makosa kuwajali wanafamilia bali alisema mtu asipewe chakula kama hawakuwa tayari kufanya kazi (2 Wathesolanike 3:10). Kwa wengine, kazi inaweza isiwe ya kuajiriwa kwa mshahara, bali ni ya kusaidia waumini kama inavyohitajika. Watu wengine hawana uwezo wa kuajiriwa, lakini kila mtu anaweza kufanya kitu kusaidia.
Katika barua zingine Paulo alitoa maelekezo ya kusaidia wajane na kuwapa msaada Wachungaji (1 Timotheo 5:3-18, Wagalata 6:6).
Kila mkristo anapaswa kuwa sehemu ya familia ya ndani ya imani na anapaswa kujitolea kusaidia washirika wenye mahitaji na kusaidia huduma.
Kushiriki kwa Vikundi
► Ni kwa insi gani kanisa linaweza kuungana kwa pamoja kushughulikia mahitaji kanisani huku wakihitaji watu wawajibike?
► Ni fursa gani zipo katika mazingira yako kwa watu wakanisa kufanya kazi pamoja kujenga rasilimali za kuleta mapato?
Maombi
Baba wa mbinguni,
Ahsante kwa ahadi yako ya kukutana na mahitaji yangu. Nisaidie niwe mwaminifu kwa majukumu yangu kwa kujikimu kwangu na wengine wanao nitegemea. Nisaidie niwe mkarimu na kile nilichonacho. Nisaidie kutosheleza mahitaji ya wengine kwa njia ya hekima.
Nakuomba baraka za kifedha, lakini zaidi ya yote nataka kuweka vipaumbele vya kiroho na nitosheke kwa sababu ya uhusiano wangu na wewe.
Amina
Zoezi la somo la 9
(1) Kwa maombi zingatia kanuni za maandiko zilizotolewa katika somo hili. Jibu kila swali lifuatalo kwa maandishi:
Nimekumbana na majaribu gani linapokuja kwa swala la fedha na rasilimali?
Kwa sasa napataje fedha na/au rasilimali?
Ninatumiaje na kusimamia fedha na/au rasilimali?
Inamaanisha nini kumuamini Mungu na fedha na/au rasilimali?
Nina rasilimali zipi za kuleta mapato?
Kuna rasilimali za kuleta mapato ninapaswa niwe na mpango wa kuzipata siku zijazo? Na kama ni hivyo, ni gani?
Ni kwa njia gani nimekuwa na matumizi mabaya ya fedha na/au rasilimali?
Nitarekebisha kwa namna gani utumiaji wowote mbaya wa fedha au/na rasilimali uliotajwahapo juu?
(2) Andika wasilisho la ukurasa mmoja wa kanuni kutoka kwenye somo hili, ukifanya matumizi mahususi katika mazingira yako. Watu katika mazingira yako wanahitaji kuelewa nini kuhusu ufahamu wa Kikristo kuhusu fedha?
(3) Kariri Mithali 3:13-17 na uandike tafakari ya aya moja juu yake. Mwanzoni wa darasa lifuatalo, andika kifungu hiki kutoka kwenye kumbukumbu na umpe kiongozi wa darasa aya hiyo.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.