Dr. Robertson McQuilkin alitumika kama misionari katika taifa la Japani kwa miaka kumi na miwili. Baadae akawa raisi wa chuo kikuu cha Kimataifa cha Columbia. Alijulikana kama mwandishi, mnenaji na mkufunzi. Mke wake Muriel aliugua maradhi ya Alzheimer’s (kupoteza kumbukumbu). Ugonjwa ulipozidi kwa kiwango ambacho alihitaji huduma ya karibu, Dr. McQuilkin alijiuzuru kutoka kwenye nafasi yake ya urais wa chuo ili amshugulikie mke wake. Alisema kwamba anazingatia maungamo yake na ahadi alizoahidi mke wake wakati alipomuoa. Aliamini kwamba kumtumikia mke wake kulikuwa kwa maana kuliko nafasi aliokuwa nayo katika chuo kama raisi.
Taasisi ya Ndoa iliyoanzishwa na Mungu
Ndoa ilianzishwa na Mungu kati ya mwanamume na mwanamke wa kwanza ambao Mungu aliwaumba.
► Mwanafunzi asome Mwanzo 2:21-24 kwa niaba ya kikundi. Je Maandiko haya yanatuambia nini kuhusu ndoa?
Ndoa imeumbwa na Mungu ili iwe hasa kile ambacho watu walihitaji. Ilitengenezwa hasa kwa asili ya mwanadamu. Katika kila kitu ambacho Mungu aliumba na kwa kila kitu anachohitaji, Mungu hutaka kutoka kwake kilicho bora zaidi kwetu sisi (Kumbukumbu La Torati 6:24). Mungu anajua kwamba mpango wake wa ndoa utampatia kila mwanandoa hisia nzuri, ushirika, uhusiano na afya ya kiroho.
Ndoa imeumbwa pia iwe mfano wa tabia za Mungu na uhusiano wake. Mungu Baba, Mungu Mwana Na Roho mtakatifu daima wamekuwa na watakuwa daima katika ushirika moja na mwingine. Kila mmoja ni wa kipekee katika jukumu lake, lakini Nafsi zote za Utatu ni Mmoja wa kudumu na ni wa asili moja. Katika uhusiano katika utatu tunaona umoja, urafiki wa karibu, uaminifu na upendo udumuo. Ndoa ya kibiblia inaundwa kwa kufuata kielelezo cha uhusiano huu wa ajabu. Mpango wa Mungu kwa kila mume na mke ni kuwa na upendo halisi na uaminifu kila mmoja kwa mwingine kwa Maisha yote.
Mungu anasema katika ndoa mume na mke watawaacha wazazi wao nao wanaunganishwa pamoja. Ndoa huweka marafiki wawili pamoja katika kushirikiana kwa pamoja kuliko uhusiano mwingine wowote wa kibinadamu.
Ndoa sio tu watu wawili kukaa pamoja katika uhusiano. Maisha yao yameunganishwa ili kwamba wawe kama mtu mmoja. Hii sio kwamba hawana tabia zao za kimaumbile, bali wapo katika muumganiko maalumu.
Kudumu kwa Ndoa
Mungu aliweka ndoa iwe ya kudumu. Katika ndoa mwanaume na mwanamke huahidiana kuwa waamifu kila mmoja kwa mwingine kwa Maisha yao yote.
Biblia inaonyesha maneno ya Yesu a kuhusu ndoa, yaliyosemwa katika mazungumzo na mafarisayo.
► Mwanafunzi asome Mathayo 19:3-8 kwa niaba ya kikundi.
Yesu anasema Mungu alikusudia ndoa iwe ya kudumu. Talaka ni kwa wale ambao hawamjui Mungu.
Kuna sababu nyingi ambazo zinazoonesha Mungu aliitengeneza ndoa ili iwe ni ya kudumu, baadhi ya sababu tumeziona hapo awali katika masomo yetu. Sababu nyingine ambayo huitaka ndoa iwe ya kudumu ni kwa ajili ya watoto. Kutii mpango wa Mungu katika ndoa huleta mazingira mazuri ya kuwalea watoto. Kwa kadri wazazi wanavyomheshimu Mungu kwa kutii kanuni zake katika ndoa na familia, wataweza kulea watoto wa kimungu (Malaki 2:15).
Mungu aliyatengeneza maisha mtu kwa namna ambayo itamchukua mtu miaka mingi kabla hajakomaa na kuwa mtu mzima. Katika wakati huo, watoto hutegemea sana wazazi kwa ulinzi, mahitaji na mafunzo. Hii ni tofauti na wanyama ambao huchukua muda mfupi ili waweze kukomaa mwaka mmoja hadi miwili. Wanadamu wanahitaji muda mwingi ili kujenga tabia ya ukomavu. Mungu ameiweka familia ili iwe ni mahali pa kulea watoto. Matatizo mengi katika jamii hutokana na kukosa familia yenye wazazi ambao ni waaminifu.
Ndoa inahitaji watu kutoa ahadi ya kujitoa kila mmoja kwa mwenzake maisha yao yote. Kila tamaduni ina namna na sherehe ya kuonesha kwamba ndoa ni ahadi nzito. Sherehe ni njia ya hao wawili kusema hadharani kwamba wamejitolea kutunza ahadi yao ya maisha.
Serikali nyingi huweka rekodi za ndoa. Sheria kuhusu ndoa huathili umiliki wa mali, nani atakaa na watoto, na urithi.
Hapa kuna mfano wa kiapo katika ndoa ambacho imetumika katika harusi nyingi:
Nakuchukua wewe uwe mume/mke wangu wa ndoa kuwa nawe kuanzia leo na kuendelea, katika hali njema ama mbaya, katika utajri au umaskini, katika afya njema ama magonjwa, nitakupenda na kukutunza hadi pale kifo kitakapotutenganisha; kulingana na agizo takatifu la Mungu, na kwa hiyo nakupa ahadi yangu.
Hisia za mapenzi hazitakuwepo kila mara. Ndoa haiwezi kuwekwa katika ya misingi hisia za kibinadamu ambazo hubadilika. Kiapo cha ndoa humaanisha ya kwamba mume na mke wameaahidiana kuwa waaminifu kwa Maisha yao yote, na kiapo hiki hakitegemei vigezo na masharti yoyote.
Ndoa kama Ushirikiano wa kikristo.
► Mwanafunzi asome 2 Wakorintho 6:14-18 kwa niaba ya kikundi.
Maandiko haya yanatuambia ya kwamba uwajibikaji wa mkristo hupata vikwazo kutokana na ushirika wa karibu na wasioamini. Kama ambavyo mkristo hawezi kuabudu na mtu anayemwabudu shetani, pia hawezi kufuata mtindo wa maisha na vipaumbele vya wasioamini. Onyo hilo linaweza kutumika katika aina mbalimbali za mahusiano, ikiwa ni pamoja na ushirikiano wa kibiashara.
Ndoa ni ushirika wa karibu zaidi wa mwanadamu. Mkristo asifikirie hata kuingia kwenye ndoa na asieamini (1 Wakorintho 7:39). Mkristo aliyeoa mtu asiyeamini atakumbana na hofu na vikwazo vingi katika kulea watoto na katika kufanya maamuzi ya maisha.
Kama mume na mke wameokoka na wametoka katika makanisa tofauti ni lazima wahakikishe ya kwamba wanaelewana katika mambo kadhaa ya kiroho. Ni vizuri wapange wawe wanaabudu katika kanisa moja baada ya harusi.
► Kwa nini ndoa huanza na kiapo na sio tu maneno ya upendo?
Kiwango cha Maadili cha Mungu.
► Mwanafunzi asome Waebrania 13:4 kwa niaba ya kikundi.
Aya hii inatwambia ya kwamba ndoa lazima iheshimiwe. Dhambi ya kuzini ni ya kutoheshimu ndoa. Mungu atahukumu dhambi ya zinaa.
Dhambi za zinaa zinajumuisha usherati, uzinzi, mapenzi ya jinsia moja, na utumiaji wa filamu za ngono au ponografia. Usherati ni mahusiano ya kindoa kati ya wale ambao hawajaoana tayari. Uzinzi inajumuisha tendo lolote la ndoa kati ya mtu aliyefunga ndoa na mtu ambaye si mwenzi wake. Ushoga ni mahusiano ya kindoa kati ya watu wa jinsia moja. Ponografia inajumuisha maandishi, picha na video zilizoundwa kusasabisha mihemko ya kihisia ya kujamiiana kwa kuonyesha picha za uchi au shughuli za kujamiiana. Mambo haya yote ni ukiukwaji wa mahusiano ya ndoa.
► Mwanafunzi asome 1 Wakorintho 6:9-10 kwa niaba ya kikundi.
Kila jamii ya watu wana mtazamo wa kijamii kuhusu mahusiano ya mwanamke na mwanaume. Viwango vya kijamii viko chini sana kulinganishwa na vya Kimaandiko. Tamaduni nyingi zimeweka sheria tu za kufanya jamii kuishi tu Kwa umoja. Wanavumilia dhambi za zinaa kama zitafanywa pasipo maangamizi au hasara kubwa. Viwango vya maadili ya Mungu ni tofauti.
Kinachohuzunisha ni kwamba, makanisa mengine hufuata maadili ya tamaduni zao badala ya maadili ya Mungu katika Biblia. Huwaadhibu watu ambao makosa yao ni dhahiri na yasiyojali, lakini wanavumilia dhambi hiyo hiyo inapofanywa na watu kwa uangalifu.
Maandiko yanasema mambo haya hufanywa na wale ambao sio wakristo na hawataenda mbinguni. Baadhi ya wakristo katika Korintho walifanya dhambi hizo zamani lakini waliokolewa kutoka huko.
Imani yeyote inayovumilia dhambi yeyote kati ya hizi kwa mtu anayedai kuwa ni mkristo ni Imani potofu. Kama mtu yeyote atajiita mkristo na anafanya dhambi ya zinaa Maandiko yanalitaka kanisa kumtoa kanisani na wasimchukulie kama mkristo (1 Wakorintho 5:11-13).
Viongozi wa kanisa ni vizuri wawe kielelezo kwa tabia njema. Kanisa likiruhusu viongozi wa ibada kuvaa isiyopaswa au kuruhusu namna ya kucheza ambako hakuleti sifa kwa Mungu linamaanisha kwamba tamaa za mwili zinatawala. Hii inamaanisha kwamba dhambi za zinaa hazishughulikiwi ipasavyo.
Labda mivalio ya jamii itaonyesha mwanamke hajavaa vizuri kama hajavaa ili avutie huku akionyesha sehemu zingine za mwili. Washirika wa kanisa wakati mwingine huanguka katika jaribu hili mara kwa mara hasa katika sherehe. Wanafikiri hawajavaa vizuri kama hawajafuata namna ya mavazi katika jamii yao. Kanisa lazima lifundishe ya kwamba hiyo ni mbaya. Mkristo hastahili kusababisha mwingine kuanguka katika tamaa mbaya. 1 Timotheo 2:9-10 inatuambia kwamba mkristo anapaswa avae na aenende kwa namna ambayo wengine wakimuona watajua ya kwamba anaishi maisha ya kujichunga na hakusudii kutenda dhambi wala kufanya mwingine kufanya dhambi. Wanawake wakristo wanapaswa “...kuvaa mavazi ya kusitiri pamoja na adabu mzuri na moyo wa kiasi”
Msaada kwa Mwenye Dhambi
Wagalatia 6:1 inasema kwamba kanisa lina jukumu la kujaribu kumrejesha mshirika ambaye amefanya dhambi. Hii haimaanishi ya kwamba mtu huyu apewe nafasi ya uongozi au kurudishwa haraka katika nafasi ya huduma baada ya kufanya dhambi. Urejesho unamaanisha kukubaliwa tena katika ushirika na kuhudumiwa na kanisa. Mshirika akitubu kwa kumaanisha, anasamehewa na Mungu na kanisa. Kanisa linapaswa kuwajibika kiroho ili kumsaidia awajibike ili awe mshindi na awe shujaa wa kiroho.
Kama msichana ambae hajaolewa akipata mimba, kanisa halistahili kumfukuza kama hawajajaribu kumrejesha kiroho. Kama atatubu na kunyenyekea na pia kuwajibika kwa alichokifanya, atasamehewa. Dhambi yake sio mbaya kuliko ya mwanaume aliyesababisha hilo. Wakati mwingine msichana anatendewa kwa ukali kwa sababu tu matokeo ya dhambi yake yanaonekana sana.
Kanisa ni jamii ya kiimani. Haitoshi tu kanisa kukemea dhambi. Lazima kanisa litunze watu wake. Kwa Mfano, mwamke anapata riziki kupitia njia ambazo hazifai, haitoshi tu kwa kanisa kumwambia kwamba hiyo haifai lakini pia wawe tayari kumpatia njia mbadala anapotubu.
Mfano halisi …
Wasichana kadhaa walikuwa wanahudhuria kanisa fulani kubwa na walikuwa wakiimba katika kwaya. Familia zao zilikuwa maskini. Wasichana hawa walikuwa katika uhusiano potovu na wanaume ili kupata fedha za kusaidia familia zao. Kanisa linapaswa kufanya nini katika hali kama hili?
► Kanisa lako linapswa kufanya nini ili kusaidia wanaoishi katika maisha ya dhambi?
Ponografia
Ponografia ni maadishi, picha na video ambazo zimeundwa kuamsha hisia za kimapenzi kwa kuonyesha picha za utupu na kujamiana.
Mitandao inafanya picha za utupu kupatikana kwa njia rahisi duniani. Hali ya matumizi ya teknologia inafanya picha hizi kuwa jaribu kwa mabo hawajafundishwa kukabiliana nalo kutumia kanuni za kikristo. Wachungaji wengi waliokomaa hawakukabiliana na jaribu hili kwa sababu hapakuwepo na mtandao kama sasa. Wanaweza kosa kuelewa kile ambacho jamii hii changa inakabiliana nacho.
Ponografia ni mbaya kwa sababu imetengenezwa ili kumfanya mtu afurahie kwa kuwaza mambo ya uasherati na uzinzi, na mengine mengi yaliopotoka. Inavutia mtu aliye na tamaa mbaya. Ponografia humfanya mtu kuvutiwa na tabia mbaya ambazo Mungu anachukizwa nazo.
Ponografia ni uraibu. Mtu ambae huona ponografia hupata msukumo mzito wa uhitaji wa kuziona. Hawezi kuishi pasipo kuona zile picha. Kwake maisha yanaonekana matupu na yasiyofurahisha bila mawazo anayopata kutokana na ponografia. Kama aina nyingine ya uraibu inavyofanya kazi, hamu au tamaa inaanza kumla na mwathiliwa huanza kupuuza kile ambacho ni kizuri katika maisha yake.
Ponografia ni Endelevu. Mtumiaji anahitaji zile picha ambazo zinazidi kuwa wazi na potofu. Huanza kupendezwa na mawazo ambayo mwanzoni yangemchukiza na kumtia hofu.
Ponografia Zinaharibu. Mtumizi ya ponografia huaza kusababisha kutopenda mahusiano ya kawaida. Tamaa yake inaaza kuwa isiyokuwa ya kawaida na ambayo haiwezi kutoshelezwa. Anaanza kuacha kujali wengine pasipo kujali.
Wachungaji na wazazi lazima wawaonye vijana kuhusu uraibu. Wazazi wasiwaruhusu watoto wao kuingia katika mtandao bila kudhibitiwa na kama hawana uwezo wa kuzuia jaribu. Mtu yeyote anapambana na hali hii ni vizuri awe na mwingine ambaye anawajibika kwake. Atawajibika kwa huyu mtu mara kwa mara.
► Ni baadhi ya njia/mazoea gani unapendekeza ili kusaidia kulinda watu kutokana na uraibu wa kutazama ponografia? Ni kwa jinsi gani Kanisa linaweza kusaidia?
Ushoga na Usagaji
Jamii za kisasa ambazo zinakataa mamlaka ya Biblia pia wanakataa jinsi ambavyo Biblia inasema kuhusu ndoa. Wanasema wako huru kuchagua kuoana na hata mtu wa jinsia yake.
Biblia inakataa ushoga na usagaji (mapenzi ya jinsia moja).
► Kikundi waangalie Warumi 1:26-27, 1 Timotheo 1:10, and 1 Wakorintho 6:9 kwa pamoja.
Maandiko haya matatu yanahusisha mapenzi ya jinsia moja kama baadhi ya dhambi ambazo ni mbaya sana. Watu ambao hufuata na hufanya Dhambi hizi hukataa mamlaka ya Mungu.
Wengine husema ya kwamba wao kwa asili wana asili ya ushoga. Wanasema wasilaumiwe kwa tabia yao ya ushoga kwa sababu hawakuchagua kuwa na hisia hizo.
Mandiko yanasema ya kuwa ya kuwa kila mmoja ana asili ya dhambi (Isaya 53:6). Mungu anatutaka tuweze kutubu dhambi zetu tulizokusudia (Isaiya 55:7). Kwa sababu tumezaliwa na asili ya dhambi, tamaa zetu za asili haziwezi kuaminiwa kutuongoza. Mtu anaweza kupata hisia nzito na kuvutiwa na mwelekeo wa asili ili kufanya uasherati, au mwenye fujo au vurugu, au kuiba, lakini kuwepo kwa mvuto wa asili haimaniishi kuwa huo mvuto ni sawa.
Kanuni ya kumheshimu Mungu kwa usafi wa tabia kabla ya ndoa.
Vijana hukutana na majaribu makubwa kabla ya ndoa. Ni vizuri wakumbuke ya kwamba wanahitaji mwenza wa Maisha ambaye anaweza ni mwaminifu.[1] Wasiweze kuwakubali wale ambao wanataka kujifurahisha tu kwa muda mfupi tu pasipo ndoa. Wasipendezwe na mahusiano na yule ambae siyo mkristo (1 Wakorintho 7:39). Waweze kuwatambua wale ambao watakuwa waaminifu na wazazi wazuri.
Kijana anayetaka ndoa nzuri lazima awe mwaminifu, mkristo mwaminifu ili avutie yule anayefaa (Mithali 3:4-8). Mtu anayeonesha tabia mzuri na anayevaa vizuri (1 Timotheo 2:9-10). Watu ambao hawana maadili na huvalia visivyo kana kwamba wanawavutia jinsia nyingine wanadokeza kwamba wako tayari kwa mahusiano yenye msingi wa tamaa mbaya (1 Wathesalonike 4:1-7). Mtu anayevaa kusasabisha tamaa mbaya atavutia wale wasiofaa (Mithali 7).
Mungu amewapa vijana wazazi, wachungaji na viongozi wengine wa kiroho ili wawape ushauri katika mienendo, mivao na uchaguzi katika mahusiano. Kama vijana ni vizuri tunyenyekee kwa viogozi hawa na Mungu na watapata Baraka kubwa na Mungu atawalinda kutokana na majaribu na maadhara.
► Mwanafunzi asome 1 Petro 5:5 and Waebrania 13:17 kwa niaba ya kikundi.
Ni jukumu la watoto na vijana kunyenyekea katika hekima na mahusia ya wazazi na viongozi wao wa kiroho. Ni jukumu la viongozi hawa kusaidia hawa vijana ili waishi maisha ya ushindi dhidi ya majaribu.
► Someni Warumi 13:14 and 1 Wakorintho 10:13 kwa pamoja.
Mungu haruhusu wakristo kuwa katika hali ya majaribu ambayo itawashinda bali ile ambayo wanaweza kuipinga na kuishinda. Vijana wana jukumu la kutoroka kwa majaribu (2 Timotheo 2:22). Pia wazazi wanastahili kuwazuia vijana kupata majaribu yasiowafaa iwezekanavyo. Kuna angalau njia tatu ambazo wazazi wanaweza kufanya hivyo:
(1) Kwa kuwapa maelekezo sahihi ya vile Watoto wanavyopaswa kufanya, wakiwa na nani na wapi wanapaswa kwenda (Waefeso 6:1-4).
Wazazi wasiruhusu watoto kuwa katika hali ambayo umri wao hauruhusu kuwalinda kutokana na majaribu. Kwa mfano kijana wa kiume na kijana wa kike wamekaa mahali palipojificha peke yao ni rahisi kupata majaribu ya kutenda dhambi.
(2) Kwa kuwafanya vijana kuwajibika katika maeneo ya majaribu
(3) Kwa kuwapa vijana ushauri wa kimaandiko.
Wazazi wanapaswa kuwasaidia vijana wao kujifunza kufikiria hali kwa kuzingatia kanuni za Biblia (Mithali 4:1-9; Mithali 7:1, 4-5). Waongee na vijana wao kuhusu hatari ambazo wanaziona. Ni vizuri waongee na vijana kuhusu maamuzi ambayo watahitaji kuyafanya. Wanaweza kuwasaidia vijana kufikiria jinsi ya kuepuka majaribu na kile wanachohitaji kufanya wanapokuwa na majaribu.
Kanisa lazima liwe tofauti na utamaduni wake linapotetea maadili ya kibiblia. Tamaduni nyingi hazizingatii dhambi ya zinaa kuwa ni mbaya. Wanatarajia vijana ambao hawajaolewa kuwa na uhusiano wa kindoa kabla ya ndoa. Kanisa lisikubaliane na dhambi. Kanisa halipaswi kufikiri kuwa dhambi ya zinaa miongoni mwa vijana ni jambo la kawaida. Mungu anasema wale wanaofanya uasherati sio wakristo (Waefeso 5:3-7, Waebrania 13:4).
Wakati wa mahusiano kabla ya ndoa sio wakati wa kujamiana. Badala yake ni kipindi cha wakati ambapo mwanamume na mwanamke huhakikisha kwamba wana vipaumbele sawa vya kiroho na kibiblia. Ni wakati ambao wanakuza uelewa wa kila mmoja wao na unaowawezesha kuaminiana vya kutosha kufanya ahadi ya kudumu kwa kila mmoja. Kama hawawezi kuafikia kiwango hicho inabidi waache urafiki wao na wasifunge ndoa.
Watu wengine katika tamaduni zingine hufanya ndoa kuchelewa sana na baadae hufanya harusi kuwa ya gharama mno. Wakati mwingine pia wanaokusudia kuoana hukaa pamoja na wanapata watoto huku wakichelewesha ndoa. Kwa wengine matumizi katika sherehe ya harusi huwa ghamarama kubwa kiasi cha kuteseka baadae kwa sababu walitumia kila kitu kwa ajili ya sherehe na ilibidi wakope fedha. Kanisa linapaswa kuwa mahali ambapo kuna muundo mbadala wa sherehe za ndoa. Ndoa ya kikristo ni kati ya mwamume na mwanamke ambao wamejitoa kila mmoja kwa mwenzake na kwa Mungu na haipaswi kuwa na matumizi mengi yenye gharama kubwa ambazo zitafanya ndoa yao kuumia hapo mbeleni.
► Ni kwa njia zipi ambazo ndoa ya mkristo inastahili kuwa tofauti na ya kitamaduni?
Ndoa ni mpango wa Mungu kwa watu wengi. Hata hivyo mtume Paulo anaeleza sababu ambazo zinaweza kufanya watu wasioe. Katika 1 Wakrintho 7:26 anataja “shida iliyopo”—hali ngumu ya maisha ambayo inaweza kuwa pia mateso. Anasema ni vyema mtu asioe akiwa katika hali hii.
Aya hiyo pia (1 Wakorintho 7:32-35) inasema mtu asiyeoa ana faida ya kipekee. Asiyeoa anaweza kujikita katika kumfanyia Mungu kazi pasipo kujali familia maana hana. Pae ambapo mtu ameitwa na Mungu katika Huduma kabla hajaoa, anaweza kufanya huduma vizuri sana.
Kunazo sababu zaidi anbazo Mungu anaweza kumchagua mtu kubaki bila kuoa (Mathayo 19:10-11). Tusione kwamba hili jambo sio la kawaida. Tusione ya kwamba kila mtu ambaye hajaoa lazima apate mwenzi wake. Tusifikiri kwamba raha kamili hupatikana katika ndoa pekee (Zaburi 107:9).
Mtu ambaye hajaoa lazima awe mwangalifu ili ajiepushe na mahusiano mabaya kwa sabau ya hisia na tamaa ya mwili. Mungu humpa furaha na kutosheka, mtu ambaye amejitoa kikamilifu kwake.
Maelekezi ya kimaandiko katika ndoa
► Someni 1 Petro 3:1-7 na Waefeso 5:22-33 kwa pamoja. Kikundi wafungue maandiko ili kuichunguza wakati wa somo.
Mwanaume ameambiwa ampende mkewe kama vile Kristo anavyolipenda kanisa. Yesu alijitoa kama dhabihu kwa kanisa. Mume atajitoa kwa faida zake mwenyewe, starehe, na matamanio yake ili akutane na mahitaji ya mkewe. Aya inasema kwamba “kaeni na wake zenu kwa akili,” kumaanisha ya kwamba atafanya kila awezavyo ili kumuelewa. Lazima amsome vizuri ili amuelewe. Mwanamke anaitwa “kiumbe dhaifu.” Mke anastahili azingatiwe na mumewe sio tu kwa hatari za huku nje lakini pia kwa hofu na msongo wa mawazo.
Mke anaambiwa anyenyekee kwa mumewe na amheshimu. Mwanamke anastahili kukubali uongozi wa mumewe hata kama mumewe siyo mwamini. Akifanya hivi mumewe ambaye hajaamini anaweza kuvutiwa katika wokovu.
Ni muhimu kukumbuka ya kwamba maandiko haya yanatoa amri. Mwanaume hajaambiwa alazimishe sheria kwa mke wake. Mke ameambiwa amtii mumewe lakini mwanaume hajaambiwa amlazimishe mkewe kufanya hivyo. Anaambiwa ampende mke wake na ajitolee kumtunza. Vivyo hivyo, mwanamke hajaambiwa amlazimishe mwamume kumtunza anambiwa amheshimu.
Kipaumbele cha mume si kuweza kutenda kwa mamlaka bali ni kumtunza na kumpenda mkewe. Kipaumbele cha mwanamke ni sio kumlazimisha mumewe kumtunza lakini kumheshimu.
Mtume anaonya mume ya kwamba maombi yake yanaweza kuzuiliwa kama hatamtunza mkewe vizuri. Hiyo inatuambia tabia zetukatika ndoa inaathiri sana uhusiano wetu na Mungu.
Mtume Yohana anasema kama mtu hatampenda ndugu yake, hawezi kusema anampenda Mungu (1 Yohana 4:20). Vivyo hivyo kwa maneno ya Paulo na Petro mwanaume asiyempenda mkewe impasavyo hampendi Mungu. Mwanamke asiye mheshimu mumewe hamheshimu Mungu kama inavyostahili.
► Mwanafunzi asome 1 Wakorinths 7:1-5 kwa niaba ya kikundi.
Maandiko haya yanatuambia ya kwamba kuna kusudi moja la ndoa nalo ni kutosheleza hisia za kimwili za kimapenzi katika tendo la ndoa. Mume na mke wamejitoa kila mmoja kwa mwingine na hakuna mwenye haki juu ya mwili wake ila mwenzake. Hii inamaanisha kwamba wanandoa hawapaswi kufanya tendo la ndoa wakati tu mmoja anahitaji lakini pia kwa kujali maslahi ya mwenzake. Aya hii haisemi kwamba moja wao anaweza kulazimisha mwenzake. Lakini mstali huo unasema kila mmoja amjali mwenzake.
Aya hii inasema wakristo wasinyimane. Wakati mchache wa kujizuia na tendo la ndoa uwe ni wakati wa saumu na maombi. Lakini isirefushwe huku ikifanya mwingine kuwa katika majaribu kwa sababu ya haja ambayo haijatimizwa. Wakati mwingine wanandoa huchagua kutengana kwa miezi kadhaa au zaidi kwa sababu mmoja huenda kufanya kazi au kusoma katika mahali pa mbali. Kabla ya kufanya maamuzi haya ni vizuri wajiulize kama mpango huu uko katika mapenzi ya Mungu. Wanaweza kupata shida kwa sababu ya kutengana kwa muda.
Kusudi moja la ndoa ni kuwa na familia ambayo itasaidia jamii.
► Mwanafunzi asome 1 Timotheo 5:8 kwa niaba ya kikundi.
Aya hii katika Kifungu hiki inaeleza majukumu ya kanisa na washirika kushirikiana na kusaidiana. Jukumu la mtu la kwanza ni familia yake mwenyewe. Mzazi atahakikisha kwamba mahitaji ya mtoto wake yanatimizwa kama vile, malazi, chakula, mavazi na masomo. Mzazi ni lazima ahakikishe mambo haya anayatenda na sio kuwachia wengine majukumu.
Kushiriki kwa vikundi
Mada ya somo hili italeta mjadala mkubwa.
Mwanafunzi atatakiwa kujaribu kutumia kanuni za kimaandiko katika jibu lake na katika hali yake.
► Ni ukweli upi kuhusu kuhusu ndoa ambao wengi husahau?
► Ni kwa njia gani ambayo kanisa linaweza kuwasaidia vijana wanaopambana na majaribu ya dunia?
► Ni kwa njia gani ambayo washirika kanisani wanaweza kujumuika pamoja (zaidi ya ibada za jumapili tu) ili kuwasaidia watoto kumfuata Kristo.
Maombi
Baba wa mbinguni,
Asante kwa mpango mzuri wa ndoa. Nisaidie niwe mwaminifu kwa mapenzi yako katika kila hatua ya maisha. Nisaidie kuwa mfano mzuri wa uaminifu wa kikristo. Nisaidie niwaambie wengine na niwatie moyo wafuate mapenzi yako.
Nisaidie nitumike kanisani kusaidia familia, vijana, watoto ili wawe na ushujaa katika imani na katika kukutii.
Asante kwa kutupatia nafasi tuwe katika mahusiano ambayo unayabariki.
Amina
Zoezi la somo la 7
(1) Kama hujaolewa, andika aya mbili ya jinsi ambavyo utajitoa kutii kanuni za Mungu katika hali yako na pia katika ndoa baadae. Kama umeoa au kuolewa andika aya mbili na jinsi ambavyo utatii kanuni za Mungu katika ndoa.
(2) Chagua mada moja au zaidi na uandike ukurasa mmoja ukieleza jinsi ambavyo mtu anaweza kutumia kanuni za maandiko katika maeneo anakoishi.
Mfano:
Eleza mahusiano ya wakristo mwanaume na mwanamke ambao wanatazamia kufunga ndoa katika maeneo yako.
Eleza tabia ya mwanaume au mwanamke anyetaka kuonyesha uaminifu katika ndoa katika maeneo yako.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.