Wakati Yesu alipokuwa akitembea kandokando ya bahari ya Galilaya, alipishana na mtoza ushuru. Kwa kuwa alikuwa anawafanyia kazi Warumi, Lawi alikuwa anakwepwa na viongozi wa dini ya Kiyahudi (Rabbi). Kwa mshangao wa wa Lawi, Yesu alisema, “Nifuate.” Rabbi wengine walimwona tu mtoza ushuru; Yesu alimwona mtu wa kumpenda.
Baadaye, Yesu aliketi chakulani pamoja na kundi la watoza ushuru wengi na wenye dhambi nyumbani kwa Lawi. Mafarisayo walishtushwa. Yesu alipaswa awe mtakatifu; kwa nini anatumia muda wake na watenda dhambi? Yesu aliposikia aliwaambia, “Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”[2]
Mfano huu wa Yesu, uliwashangaza wapinzani wake wengi. Mafarisayo walifikiriwa kama watu watakatifu sana wakati wa kipindi cha Yesu. Walisema, “Sisi ni watakatifu, kwa hiyo tunakaa mbali na wenye dhambi.” Yesu anasema, “Mimi ni Mtakatifu, kwa hiyo ninautumia muda wangu na wenye dhambi.”
Yesu alifurahia kuutumia muda wake na wenye dhambi. Kwa jinsi walivyokuwa wanamfuata Yesu, watu wengi waligeuka kuwa watu watakatifu. Yesu alionyesha mfano halisi wa maisha ya upendo mtakatifu unaoweza kuibadilisha dunia. Utakatifu ni upendo kamili kwa Mungu na upendo kamili kwa watu. Utakatifu wa kweli huubadili ulimwengu wetu.
[1]Sala kwa ajili ya Utakatifu “Bwana Nifanye niwe chombo chako cha amani. Palipo na chuki, nionyeshe upendo; Palipo na maumivu, Msamaha; Palipo na mashaka, Imani; Palipo na kukataa tamaa, matumaini; Palipo na giza, palete mwanga; Palipo na majonzi, palete furaha. Ewe Bwana wa Utukufu, Kuwa mpaji wangu, ili nisiwe ombaomba; Nipe kufarijiwa, nami niweze kufariji; Nipe kueleweka, nami nielewe wengine; Nipe kupendwa, nami niweze kupenda. Kwa kuwa katika kutoa, ndipo tunapopokea; Katika kusamehe, ili nasi tuweze kusamehewa; Ni katika kufa, tunazaliwa upya katika maisha ya milele.”
- Mtakatifu Francis wa Assisi
► Ni kwa jinsi gani watu katika ulimwengu wako wanaupima utakatifu? Kiwango hiki unawezaje kukilinganisha na jinsi Yesu alivyoishi?
Watu walioishi kipindi cha dunia ya Yesu waliamini nini kuhusu utakatifu? Walitegemea mtu mtakatifu aishije? Kama tutakavyoona katika majibu ya maswali haya, tutaelewa ni kwa nini watu walishtushwa na maisha na mafundisho ya Yesu.[1]
Walichokiamini Watu wa Wakati wa Dunia ya Yesu
Watu wa wakati wa Yesu walijua kwamba Mungu ni Mtakatifu. Walijua kwamba watu wa Mungu ni lazima wawe watakatifu. Mungu mtakatifu anahitaji watu wawe watakatifu. Mungu aliipeleka Israeli uhamishoni kwa sababu watu wake hawakuwa watakatifu.
Watu wa wakati wa siku za Yesu, walijua kwamba utakatifu unahitaji kutengwa kutoka kitu chochote ambacho ni najisi. Wito wa Agano la Kale ni kuwataka watu wa Mungu kukaa mbali na chochote kinachoitwa dhambi.
Watu wa siku za Yesu walijuaahadi ya Mungu ya kuandika agano jipya ndani ya mioyo ya watu. Mungu aliahidi kuwapa watu wake “moyo mpya” na “roho mpya” itakayowawezesha kuhifadhi lile agano.[2] Watu wa siku za Yesu walikuwa wanaingojea ahadi hii iweze kutimia.
Watu wa siku za Yesu walijua kwamba Mungu mtakatifu hutimiza ahadi zake. Mungu ni mwaminifu katika maagano yake. Ingawaje Israeli imelivunja lile agano, Mungu aliendelea kuwa mwaminifu. Wayahudi waliamini kwamba utukufu wa Mungu ungerejea katika Israeli kama watu wake wangekuwa watakatifu.
Walichokifanya Watu wa Wakati wa Dunia ya Yesu
Watu wa dini wa wakati wa siku za Yesu waliamini katika kanuni hizi, lakini walishindwa kuishi kulingana na mfano wa Mungu wa utakatifu wa kweli. Hawakuwa na mioyo ya utakatifu.
Viongozi wa kidini waliweka Imani yao kwenye hekalu. Waliamini kwamba kama dhabihu zingeweza kutolewa kwa usahihi, utukufu wa Mungu ungerudi. Yesu alijibu, “Nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka.”[3] Yesu alionyesha kwamba sadaka peke yake hazitoshi.
Waliokuwa wanajihesabia haki waliamini kwamba wangeweza kuwa watakatifu kwa kuishi maisha ya kujitenga kuishi na watu wengine. Walitembelea jamii zilizoishi kuzunguka Bahari Nyeusi. Yesu alijibu, “Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu.”[4] “Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”[5] Yesu aliwagusa wenye ukoma; alikula na wenye dhambi. Alionyesha kwamba tunaweza kuwa watakatifu kwenye dunia ya dhambi.
Mafarisayo waliamini katika muonekano wa nje wa mambo yaliyohusiana na sheria, lakini walipuuzia usafi wa ndani. Yesu aliwalinganisha Mafarisayo na makaburi: “Nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote. Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi.”[6] Yesu alionyesha kwamba utakatifu unaanzia kwenye moyo. Huwezi ukawa na mikono mitakatifu kama moyo siyo mtakatifu.
Hawa watu wa dunia ya Yesu waliridhika na utoaji wa sadaka badala ya utakatifu wa kweli. Badala ya kumpenda Mungu, waliupima utakatifu na sheria. Badala ya kuupenda ulimwengu wao, Israeli ilijenga kuta kuzuia dunia iliyokuwa na uhitaji. Yesu anaonyesha kwamba mtu mtakatifu anampenda Mungu na anampenda jirani yake.
[1] Maelezo mengi hapa yanatoka kwa Kent Brower, Holiness in the Gospels (Kansas City: Beacon Hill Press, 2005).
Maisha ya Yesu yalikuwa ni Mfano wa Kuigwa wa Utakatifu
Tunaposoma kuhusu utakatifu katika Agano la Kale, tunaweza kushawishika kusema kwamba, “Hiyo inafanya kuwa ni nadharia nzuri, lakini itafananaje katika uhalisia wa maisha?” Yesu alikuja kutuonyesha utakatifu unafananaje katika maisha ya kila siku. Mtiririko wa Luka wa nasaba (ukoo) ya Yesu unaonyesha kwamba Yesu alikuwa “Mwana wa Adamu, Mwana wa Mungu.”[1] Tunapomwangalia Yesu, mwana wa Adamu, tunaona mfano halisi wa mtu mtakatifu. Vitabu vya Injili vinaonyesha maisha ya utakatifu ya Yesu wa Nazarethi.
Utakatifu ni Kutembea na Yesu
Ndani ya Yesu, tunaona mfano wa kuigwa wa uhusiano wa mtu na Mungu. Maombi ya Yesu yalidhirisha uhusiano wake wa karibu na Baba. Mara kwa mara Yesu alikuwa akijitenga na makundi ili awe peke yake na Baba yake. Yesu alitafuta kuwa na uhusiano wa karibu sana na Baba yake. Alitembea na Mungu.
Labda, picha kubwa ya uhusiano wa Yesu na Baba yake unaweza kuonekana kwenye kilio chake pale msalabani. Alipokuwa amezibeba dhambi zetu pale msalabani, “Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, ‘Eloi, Eloi, lama sabakthani?’ Yaani, ‘Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?’”[2] Kwa kufa badala yetu, na kwa kuichukua adhabu stahili kwa ajili ya dhambi zetu, Yesu alijihisi kuachwa na Baba yake.
Yesu alionyesha uhusiano wa ndani na Mungu. Utakatifu aliokuwa nao Ibrahimu na Daudi ulikamilishwa ndani ya Yesu wa Nazarethi.
Utakatifu ni Kutengwa
Kuwa mtakatifu maana yake ni kutengwa kutokana na dhambi na kutengwa kwa ajili ya Mungu. Akiwa katika hali ya ubinadamu, Yesu alionyesha mfano wa kutengwa kutokana na dhambi. “Hakuwahi kufanya dhambi.”[3] Mwanafunzi aliyekuwa akikaa karibu sana na Yesu wakati wa huduma yake hapa duniani alitoa ushuhuda kwamba, “wala giza lo lote hamna ndani yake.”[4]
Akiwa katika hali ya ubinadamu, Yesu alionyesha mfano wa kutengwa kwa ajili ya Mungu. Aliishi maisha ya kujitoa kwa hiari kwa Baba yake. Yesu alithibitisha, “Naye aliyenipeleka yu pamoja nami, hakuniacha peke yangu; kwa sababu nafanya siku zote yale yampendezayo.”[5] Yesu alikuwa ametengwa kwa ajili ya Baba yake.
Utakatifu ni Sura ya Mungu
Kuwa mtakatifu ni kuakisi sura ya Mungu. Tunapomwangalia Yesu, tunaona kivuli kamili cha sura ya Baba. “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”[6] Wakati Filipo alipomwuliza Yesu, “Tuonyeshe Baba,” Yesu alijibu, “Aliyeniona mimi amemwona Baba.”[7] Ndani ya Yesu, tunaona kivuli kamili cha sura ya Mungu.
Utakatifu ni Moyo Usiogawanyika
Mtu mtakatifu ana moyo usiogawanyika; amejikabidhi kabisa kwa Mungu. Katika bustani ya Getsemane, Yesu aliomba. “Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke.”[8] Moyo wa Yesu ulijisalimisha kabisa kwa Baba. Yesu alionyesha ni nini maana ya kuwa na moyo usiogawanyika.
Utakatifu ni Uadilifu na Haki
Utakatifu wa kweli unahitaji tabia ya uadilifu na haki. Mtu mtakatifu hudhihirishwa na haki, rehema na unyenyekevu. Katika maisha ya Yesu, tunaona mfano ulio mkamilifu wa uadilifu na haki.
Picha ya mwisho ya haki inaonekana wakati Yesu alipobeba hasira ya Mungu msalabani. Yesu hakuikataa hukumu ya kulipia dhambi; badala yake, aliikubali hiyo adhabu kwa ajili yetu.
Yesu alidhihirisha huruma yake wakati aliposhughulika na wenye ukoma, wanawake, watoto, na maskini. Alionyesha huruma kwa mwanawake aliyenaswa katika uzinzi, Zakayo, na kwa yule mwizi pale msalabani. Mara kwa mara, Yesu alikuwa na mwitikio wa huruma kwa wale wote waliokuwa wamekataliwa na watu wengine.
Zaidi ya miaka 700 kabla Yesu hajazaliwa, Isaya alielezea kuhusu unyenyekevu wa Masihi. “Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani.”[9] Isaya alitabiri, “Hatalia, wala hatapaza sauti yake, wala kuifanya isikiwe katika njia kuu. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima.”[10]
Yesu alionyesha huduma yake ya umisheni, ya haki, rehema na unyenyekevu katika mahubiri yake ya kwanza hadharani. Katika hekalu la Nazarethi, alisoma unabii wa Isaya wa mtumishi ajaye:
"Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao. Kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa."[11]
Isaya aliona kabla “mwaka wa Bwana uliokubalika,” muda wa haki kwa watu wote. Yesu alitangaza kwamba alikuja ili kuitimiliza ahadi: “Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu.”[12] Huduma ya Yesu hapa duniani ilionyesha mfano mzuri wa uadilifu na haki.
Utakatifu katika Vitabu vya Injili: Kuwapenda jirani zetu
Katika somo la 7, tumeona kwamba kuwa mtakatifu ni kumpenda Mungu kwa upendo usiogawanyika. Kuwa mtakatifu pia ni kuwapenda jirani zetu. Yesu alitoa maagizo haya mawili, “Mpende Bwana Mungu wako” na “Mpende jirani yako” kama muhtasari wa sheria zote.”[1]
Upendo wa kweli wa Mungu siku zote huleta upendo kwa watu wengine. Kama tunampenda Mungu, tutawapenda na watu ambao Mungu anawapenda. Utakatifu kamwe siyo wa faragha; maisha ya utakatifu ni pamoja ni uhusiano wetu na majirani zetu. Utakatifu ni upendo mkamilifu kwa Mungu naupendo mkamilifu kwa watu wengine. Upendo mkamilifu kwa Mungu hauwezi kutenganishwa na upendo wetu kwa majirani zetu.
Yesu aliliweka liwe hivi: “Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.”[2] Yohana aliunganisha upendo wetu kwa Mungu na upendo wetu kwa majirani zetu:
"Mtu akisema, 'Nampenda Mungu,' naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona. Na amri hii tumepewa na yeye, ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake."[3]
Kutokea kwenye chanzo chake, dhambi ni ubinafsi. Kwenye bustani, Shetani alimwahidi Hawa kwamba anaweza “akafanana na Mungu.”[4] Kule Babeli, watu walidhamiria “wajijengee jina.”[5] Kinyume na mapenzi ya Mungu, Israeli iliomba ipewe mfalme ili “aweze kufanana na mataifa mengine.”[6] Kwenye kila eneo, asili ya dhambi ni ubinafsi.
Kama dhambi ni ubinafsi, basi utakatifu (kinyume cha dhambi) utahusisha kujikita kwa aina nyingine. Kama dhambi inasababisha tutafute mambo mazuri ya kwetu wenyewe, basi utakatifu utasababisha tutafute mambo mazuri kwa watu wengine. Kama dhambi ni kujipenda wenyewe, basi utakatifu ni upendo kwa wengine. Kuwa mtakatifu ni kuwapenda wengine. Amri iliyo kuu inayorudiwa mara kwa mara kwenye Agano Jipya ni ile ya upendo. Neno upendo limerudiwa mara hamsini na tano.
Yesu alifundisha kwamba utakatifu ni kuwa na upendo wenye huruma. Yesu alionyesha kwamba mtu mtakatifu atawavuta wengine kuja kwa Mungu takatifu kupitia maisha ya upendo mtakatifu.
Utii katika sheria ya Mungu ya kuwa mtakatifu kwa sababu Mungu naye ni mtakatifu kunatuhitaji sisi tuwapende jirani zetu. Yesu aliudhihirisha upendo kamili kwa wengine na aliwafundisha wafuasi wake kuwapenda kwa ukamilifu watu wengine.
Yesu aliudhihirisha upendo kamili kwa wengine
Mwanzoni mwa huduma ya Yesu, Yohana Mbatizaji alituma wanafunzi wake kuulizia, “Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?”[7] Farisayo angetegemea Yesu ajibu kwa kujinyooshea kidole cha maisha yake ya kutengwa na mafundisho yake ya hekima. Badala yake, Yesu anagusa huduma yake ya upendo kwa wengine:
"Nendeni mkamweleze Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia: vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakasika, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiriwa habari njema."[8]
Utafiti uliofanywa katika miujiza aliyoifanya Yesu inadhihirisha ukamilifu wa upendo kamili kwa watu wengine. Akida mmoja wa Kirumi alimwomba Yesu amponye mtumishi wake. Makuhani wengi wa Kiyahudi wangelilikataa ombi hili. Yesu siyo tu kwamba alimponya yule mtumishi, bali pia alisifia imani ya yule mmataifa.[9]
Hata wakati miujiza yake ilipoleta upinzani, Yesu aliendelea kutumika kwa upendo. Wakati yule mwanamke kilema alipokuja kwake kwenye siku ya Sabato, alimponya. Ingawaje hakukuwa na sheria yeyote ya kuweza kuzuia uponyaji huu, Mafarisayo hawakuruhusu uponyaji ufanyike siku ya Sabato. Kwa ajili ya upendo, Yesu alisababisha hasira kwa wakuu wa dini.[10]
Yesu alionyesha upendo hata kwa wale waliokuwa wanapitia katika mateso kama matokeo ya matendo ya dhambi zao wenyewe. Yesu alionyesha upendo kwa mwanamke Msamaria aliyeishi maisha ya uasherati.[11] Alimlinda mwanamke aliyekamatwa kwa uzinzi. Yesu hakukataa kwamba hana dhambi; alimwamuru aende, “Enenda zako; wala usitende dhambi tena.”[12] Yesu alijua kwamba utakatifu unahitaji mtu atengwe kutokana na dhambi, lakini alijua pia kwamba upendo una nguvu kuliko nguvu ya dhambi.
Masaa machache kabla ya kifo chake, Yesu aliudhihirisha upendo kwa wengine. Mtumwa wa Kuhani Mkuu alifuatana na bwana wake kwenda kumkamata Yesu kwenye bustani ya Getsemani. Wakati Simoni Petro alipolikata sikio la mtumwa wa Kuhani Mkuu, Yesu alimkemea Petro na akamponya yule mtumwa.[13] Yesu alionyesha ni nini maana ya kumpenda adui yako.
Wakati Yesu akiwa pale msalabani, mwizi aliyekuwa na yeye ametungikwa msalabani alimwomba Yesu rehema. Huyu mwizi alistahili adhabu ya kifo. Alikuwa mhalifu wa ujambazi wa kutumia nguvu. Yesu aliyekuwa anateseka lakini siyo kwa makosa aliyoyatenda, bali kwa ajili ya dhambi za wengine, alimpa ahadi yule mwizi aliyekuwa anangojea kufa.[14] Pamoja na uchungu aliokuwa akiupitia, bado Yesu alimpenda mtu aliyeonekana hawezi kabisa kupendwa.
Yesu alifundisha wafuasi wake kuwapenda watu wengine kwa ukamilifu
Yesu aliwafundisha wafuasi wake ni nini maana ya kupenda kwa ukamilifu. Yesu alionyesha kwamba upendo mkamilifu ndiyo kiwango cha maisha katika ufalme wa mbinguni.
Yesu alifundisha upendo mkamilifu kwenye Hotuba ya Mlimani[15]
Agizo hili, “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu” ndiyo kiini kikuu cha hotuba ya Yesu Mlimani. Agizo hili linafuatiwa na mfululizo wa mifano ya upendo kwa wengine. Kuwa “wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu” ni kuishi maisha ya upendo binafsi dhidi ya watu wengine.
Kama utakatifu usingemaanisha kutengwa na dhambi za nje; Mafarisayo wangekuwa ni watakatifu kuliko watu wengine wote. Waliitwa “Waliotengwa.” Yesu alitaka zaidi ya huku kutengwa kwa Mafarisayo. “Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.”[16]
Kwenye ulinganifu na haki waliyokuwa nayo Mafarisayo, Yesu alionyesha kwamba watu wa ufalme wake ni watu wa upendo. Tabia za nje ambazo haziendani na utakatifu wa ndani ni unafiki na siyo utakatifu. Ni lazima tuwe na mioyo mitakatifu na mikono safi.
Mtu mwenye upendo mkamilifu huenda zaidi ya agizo kwamba. “Usiue.” Upendo hutafuta upatanisho na ndugu aliyekukosea. Mtu mwenye upendo mkamilifu ataenda hata zaidi ya agizo kwamba, “Usizini.” Upendo unakataza hata kumwangalia mwanamke ili kuridhisha matamanio ya mwili.
Mtu mwenye upendo mkamilifu hatafuti sababu za kuachana kwenye ndoa. Anampenda mkewe kiasi cha kutafuta haja za moyo wake. Mtu mwenye upendo mkamilifu huzungumza bila ya kupindisha ukweli. Mtu wa upendo mkamilifu hatafuti kulipiza kisasi.
Yesu alihitimisha kwamba:
"Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki."[17]
Kupenda kama Mungu anavyopenda ni kuwa na upendo kwa adui zako. Yesu hajawahi kupunguza mahitaji ya utakatifu; bali ameyaongeza mahitaji ya utakatifu. “Haki yenu ni lazima izidi” haki ya nje ya waandishi na Mafarisayo.[18] Badala ya kuamua kuwa na tabia za nje peke yake, Mungu huubadilisha moyo. Unapokuwa na upendo kama Mungu alivyo na upendo, unakuwa “mkamilifu kama Baba wa mbinguni alivyo mkamilifu.”
Yesu alifundisha upendo mkamilifu kwenye mfano wa msamaria mwema.[19]
Mwanasheria mmoja wa dini alimwuliza Yesu, “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Yesu akamwambia, “Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje?” Mwanasheria alikuwa anajua jibu sahihi akamjibu, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako.”
Mwanasheria hakutaka kugusia mahitaji ya upendo. Alitafuta kisingizio cha kukwepa kuiweka imani yake kwenye vitendo. “Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu; ‘Na jirani yangu ni nani?’” Yesu alimjibu kwa kutumia mfano wa Msamaria mwema.
Yesu alifundisha kwamba hatupaswi kuwapenda majirani zetu kwa maneno tu, bali pia kwa matendo. Kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema, Wakristo wanaopenda kwa ukamilifu hutafuta fursa ya kuwatumikia wengine – hata aliye adui kwake. Tukiwapenda majirani zetu, tutakuwa na fursa ya kuwahudumia. Yakobo alieleza:
"Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki, na mtu wa kwenu akawaambia, 'Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba,' lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini?"[20]
Upendo mkamilifu unaonekana katika vitendo, na siyo maneno peke yake. Watu watakatifu hupenda kama Yesu alivyopenda. Kupenda kwa ukamilifu ni kupenda kwa kujitoa mhanga.
Yesu alionyesha upendo mkamilifu kwa kuosha miguu ya wanafunzi.[21]
Kwenye usiku wa kukamatwa kwake, Yesu alifundisha somo kuu sana kuhusiana na upendo mkamilifu. Walipokuwa wakila chakula, yakatokea mashindano kati yao, kwamba ni nani anayehesabiwa kuwa mkubwa.
Yesu alijibu: “Maana aliye mkubwa ni yupi? Yeye aketiye chakulani, au yule atumikaye? Siye yule aketiye chakulani? Lakini mimi kati yenu ni kama atumikaye.”[22] Ndipo alipochuka taulo akaanza kutawadha miguu ya wanafunzi wake, kazi ya mtumishi. Yesu alipiga magoti akaosha miguu ya kila mtu aliyekuweko katika chumba kile – hata miguu ya Yuda Iskariote.
Baada ya kuwa amemaliza kuwatawadha, Yesu akawauliza, “Je! Mmeelewa na hayo niliyowatendea?” Alitaka awafundishe hawa wanafunzi wake wanaopigania ukubwa somo la msingi sana:
"Ninyi mwaniita, Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo. Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo hivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi. Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo."[23]
Katika dakika zake za mwisho za kuwa na wanafunzi wake, Yesu alifundisha kwamba upendo ni kujinyenyekeza. Upendo mkamilifu hautafuti madaraka; bali unatafuta fursa za kutumika. Utakatifu ni upendo mkamilifu.
Yesu alisema, “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.”[1] Watu wengi wanapinga kwamba, “hakuna mtu mtakatifu!” Hata hivyo, hatuwezi kupuuzia agizo la Yesu la “Kuwa wakamilifu.” Hii inamaanisha nini? Je, inawezekana Wakristo wa kawaida wakatii hili agizo la Yesu?
Inamaanisha nini kuhusu “Kuwa Mkamilifu”?
Mambo mawili yatatusaidia kuelewa alichokuwa anamaanisha Yesu. Kwanza, tunaangalia tafsiri ya neno la Kigiriki lililofasiri “kuwa mkamilifu” katika Mathayo 5:48. Teleios inamaanisha “kuwa kamili.” Teleios inatokana na nomino inayomaanisha “lengo” au “kusudi.” Kuwa mkamilifu maana yake ni kufikia lengo.
Agano la Kale linaonyesha kwamba mtu mkamilifu ana moyo usiogawanyika kwa ajili ya Mungu. Wazo hili linaendelea hadi kwenye Agano Jipya. Lengo la Mungu kwa watu wake ni “upendo mkamilifu,” upendo unaotoka katika moyo usiogawanyika. Je, kutenda kwa kamilifu kunawezekana kwa nguvu zetu wenyewe? Hapana. Je, upendo mkamilifu usiogawanyika kwa ajili ya Mungu unawezekana? Yesu alisema, “Ndiyo.”
Pili,angalia muktadha ulioko katika Mathayo 5:48. Aya iliyo kabla na baada ya Mathayo 5:48 zinaonyesha kwamba kuwa mkamilifu ni kumpenda Mungu na jirani zetu upendo mkamilifu. Agizo la Yesu linabeba muhtasari wa maisha ya upendo kwa Mungu na kwa jirani zetu.
Agizo la, “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu” linafuatiwa na mifano ya upendo kwa jirani zetu katika Mathayo 5:21-47. Badala ya mauaji, uzinzi, talaka, kuvunja ahadi au kulipiza visasi, watu watakatifu huishi kwa upendo. Amri iliyo kuu kuliko zote ni “Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi.”[2] Watu watakatifu huwapenda hata wale wanaotaka kuwaletea madhara. Kuwa mkamilifu maana yake ni kupenda kama Mungu anavyopenda.
Mara tu baada ya agizo hili, Yesu alitoa mfano wa inamaanisha nini katika kumpenda Mungu katika kweli kabisa katika Mathayo 6:1-18. Wanafiki huwa wanawasaidia maskini kwa ajili ya kutafuta kuonekana na kuheshimiwa na watu wengine; lakini wale wanaompenda Mungu kwa ukamilifu wanatoa ili waonekane na “Baba yao aonaye sirini.”
Wanafiki “hupenda kusimama na kuomba ndani ya mahekalu yao na pembezoni mwa barabara ili waweze kuonekana na watu wengine.” Wale wanaompenda Mungu kwa ukamilifu “wanaenda chumbani kwako, wanafunga mlango, wanaomba na wewe omba kwa Baba yako aliyeko sirini.” Wanafiki hufunga ili kuvutia watu wengine; “wanabadilisha sura za nyuso zao ili waonekane na wengi.” Wale wanaompenda Mungu kwa ukamilifu wote watapenda waonekane tu na “Baba yao aonaye sirini.”
Paulo aliwaagiza waumini wa Kolosai kuishi maisha ya utakatifu. Anaelezea maisha ya upendo na msamaha: “Basi kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa Rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu...”[3]
Juu ya mambo haya yote ni upendo. “Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu.”[4] Kuwa mkamilifu ni “kuuva upendo.” Yesu aliposema “kuweni wakamilifu,” alituagiza sisi “tuuvae” upendo kwa ajili ya Mungu na jirani zetu. Upendo mkamilifu ni upendo unaotoka katika moyo usiogawanyika.
Upendo mkamilifu ni kamilifu kwa kiasi gani?
Katika hali ya kawaida mara nyingine tunatumia neno “kamilifu” katika ufahamu kamili. Tunatumia neno “Kamilifu” kumaanisha kitu ambacho hakiwezi kuongezwa au kupunguzwa. Tukifikiria “ukamilifu” kama kiwango kamilifu cha kupimia mafanikio, tutaupima utakatifu kwa matendo yetu. Kama Mafarisayo, tutauona utakatifu kama kijiti cha kupimia.
Watu wengi huupeleka mtazamo huu kwenye maisha ya utakatifu. Kama Mafarisayo, wana msururu wa mambo ya kufanyia ukaguzi. Kama mambo yote yatawekwa alama ya vema, wanaonekana ni “wakamilifu.”
“Je, amri ninazifanyia kazi?
“Je, ninavaa nguo nzuri?
“Je, ninanena maneno sahihi?
Katika Biblia, neno “mkamilifu” halina mipaka. Halikatai ukuaji endelevu. Ayubu alikuwa “mkamilifu,”[5] lakini aliendelea kukua katika mahusiano yake na Mungu kwa uzoefu aliokuwa ameupata.
Katika Biblia, kuwa “mkamilifu” kunamaanisha “kuwa kamili” katika kila eneo la ukuaji. Mwandishi wa kitabu cha Waebrania aliwaandikia Wakristo ambao hawakuwa wakamilifu katika hatua za ukuaji wao. Walikuwa wameshindwa kukua katika eneo la kukua kiroho.
"Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu. Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga. Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima (teleios), ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya."[6]
Mwandishi wa kitabu cha Waebrania hajajaribu kushauri kwamba waumini waliokua kiroho (au wakamilifu) hawahitaji tena chakula cha kiroho. Badala yake anawasogeza zaidi kwenye kuendelea kukua, ili waweze kula chakula cha kiroho kilicho sahihi katika umri wa maisha yao ya kiroho. Kuwa mkamilifu ni kukua vyema katika hatua za uzoefu wa ukristo wetu. Kuwa mkamilifu ina maana kwamba tumekamilika kwa ujumla wote, na tuko kama Mungu anavyotutaka tuwe.
Badala ya kijiti cha kupimia, picha ya kibiblia ya “ukamilifu” ni mduara. Mduara uko mkamilifu na hauwezi kufanywa ukawa mduara zaidi. Hata hivyo, mduara mkamilifu unaweza kukuzwa umbo lake ukawa mkubwa, na ukapanuka. Ni mkamilifu, lakini bado unaongezeka.
Mtu mtakatifu amejazwa na upendo mkamilifu kwa ajili ya Mungu na jirani zake. Jinsi tunavyokua, uwezo wetu wa upendo unaongezeka. Mduara unazidi kupanuka. Jinsi tunavyokua, pendo letu linazidi “kuwa jingi sana, katika hekima na ufahamu wote."[7]
Katika kila hatua ya ukuaji, Mungu anasema, “Mtu huyu ananipenda kwa moyo mkamilifu wa upendo. Ni mtakatifu.”
Mtu aliyetembea na Mungu kwa miaka arobaini ana uelewa mkubwa zaidi wa kuonyesha upendo kwa jirani zake kuliko mtu ambaye ametembea na Mungu kwa mwaka mmoja tu. Lakini wote wanaweza kuwapenda majirani zao kutoka katika moyo usiogawanyika. Wote wanaweza kuonyesha upendo mkamilifu.
Wakati mtoto wa miaka mitano anavyochora picha ili kumwonyesha baba yake, husema, “Asante, imekamilika.” Hamaanishi kwamba mchoro wake hauwezi kuwa mzuri. Kwenye umri wa miaka kumi na tano mtoto huyu anaweza akachora picha nyingine nzuri na bora zaidi.
“Imekamilika!” maana yake, “Picha hii imetoka katika moyo wa upendo. Ni sahihi katika hatua yake ya kukua.”
Upendo mkamilifu siyo kipimo cha utendaji. Upendo mkamilifu ni upendo usiogawanyika kwa ajili ya Mungu na kwa watu wengine. Upendo mkamilifu ni kufuata mfano wa Yesu, aliyekuja kudhihirsha upendo mkamilifu katika maisha ya kila siku.
Je, upendo mkamilifu unawezekana kwa waumini wa kawaida?
Katika karne ya kumi na saba, watu waliokuwa wasafi wakati ule walitoa kanuni moja ya tafsiri ya Biblia. Walisema kwamba maagizo ya Biblia ni “ahadi zilizofunikwa.” Hawa Wasafi walimaanisha kwamba maagizo ya Biblia “ni ahadi zilizojificha.” Agizo la Biblia inamaanisha ni Ahadi ya Biblia. Kama Mungu akiagiza jambo, atafanya na utii uwezekane. Analolitaka Mungu kwa watu wake, atalifanya kwa watu wake.
Mfikirie baba wa duniani anayempa kijana wake maagizo ambayo hayatekelezeki. “Mwanangu, kama unataka unifurahishe, lazima ukimbie maili moja kwa dakika mbili.” Kwa muda kidogo, kijana anaweza kujaribu kufikia hilo lengo, lakini mategemeo ya baba yake hayawezekani. Mwishowe, huyu kijana atakata tamaa sana na hata kuwa na hasira. Je, huyu ni baba mzuri? Hapana!
Mungu ni Baba mwema. Hawafanyi watoto wake wachanganyikiwe kwa maagizo yasiyowezekana. Wakati Yesu anatuagiza “tuwe wakamilifu kama Baba wa mbinguni alivyo mtakatifu,” anatuwezesha tuweze kutii maagizo yake.
Hotuba ya Mlimani inaonyesha maisha katika ufalme wa Mungu. Hii siyo sheria mpya inayoleta utumwa mkubwa kuliko sheria ya zamani. Siyo seti ya mawazo yasiyofikiwa ya kutuonyesha tuko wapi katika kufikia maagizo ya Mungu. Ni picha ya maisha ya kila siku katika ufalme wa Mungu. Hakuna mahali popote Yesu anasema, “Hili ni agizo langu, lakini hamtaki kutii!” Badala yake, Yesu anasema, “Hivi ndivyo mnavyotakiwa muwe.”
Kama tutayaangalia maagizo ya Yesu kwa jicho la kawaida la kibinadamu, haiwezekani. Kwa nguvu ya kibinadamu, hatuwezi kutimiza maagizo ya Mungu ya kuwa wakamilifu. Kwa nguvu ya kibinadamu hatuwezi agizo la “mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.” Hata hivyo, kwa nguvu za Mungu, tunaweza kutii maagizo ya Mungu. Upendo mkamilifu unawezekana kwa neema ya Mungu.
Kijana mmoja tajiri alimwendea Yesu akamwuliza, “Mwalimu, nitende jambo gani jema, ili nipate uzima wa milele?” Yesu alimjibu kwa kuorodhesha maagizo:
"Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie Uongo, Waheshimu Baba Yako Na Mama Yako, Na, Mpende Jirani Yako Kama Nafsi Yako."[8]
Wakati yule kijana alipojibu, “Haya yote nimeyashika.” Yesu akaongezea amri nyingine, “Ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.” Kuwa mkamilifu kunamaanisha kumpenda Yesu kuliko mali.
Yule kijana alipolisikia neno lile, “akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.” Kijana tajiri hakupenda jirani zake kikamilifu; hawezi kuuza mali zake kisha awape maskini. Hakumpenda Mungu kikamilifu; na hawezi kuondoka nyumbani amfuate Yesu. Huyu kijana alikuwa na moyo uliogawanyika. Alimhitaji Mungu, lakini pia alizihitaji “mali zake nyingi.”
Walipoona matakwa ya uanafunzi, “walishangaa mno, wakisema, ‘Ni nani basi awezaye kuokoka?’” Jibu la Yesu linajibu swali hili, “Je, ukamilifu unawezekana kwa mwamini wa kawaida? Yesu akasema, “Kwa wanadamu hilo haliwezekani; bali kwa Mungu mambo yote yawezekana.”
Kwa nguvu ya mwanadamu, upendo mkamilifu kwa Mungu na jirani zetu haiwezekani. “Bali kwa Mungu yote yawezekana.” Baba mwenye upendo hawezi kuwafadhaisha watoto wake kwa maagizo ambayo hayawezekani kutekelezwa. Maagizo ya Maandiko yanafuatana na neema ya kutii maagizo hayo. “Iweni wakamilifu kama na Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” siyo sheria halali ya kuwaongoza Wakristo katika kukata tamaa. Ni ahadi ya neema ambayo Mungu anaweza kufanya ndani yetu kile ambacho kamwe tusingeweza kufanya sisi wenyewe.
Je, inawezekana kutii maagizo ya Yesu ya kuwa mkamilifu? Kutokana na Hotuba ya Yesu pale Mlimani, jibu ni la kupendeza “Ndiyo!” Kuwa mkamilifu kwenye ufalme wa Mungu ni kuwa na moyo wenye upendo mkamilifu. Kuwa mkamilifu kwenye ufalme wa Mungu ni kuwa na upendo mmoja tu kwa Mungu na jirani yetu. Je, hili linawezekana? Kwa mujibu wa Yesu, upendo mkamilifu pande zote inawezekana na ni muhimu. Upendo mkamilifu ni lengo kuu la Mungu kwa watu wake.
Utakatifu katika vitendo: Upendo unatimizaje sheria?
Huang anasema, “Ninampenda Mungu kwa moyo wangu wote, na ninawapenda watu wengine pia. Lakini siwezi nikawapenda watu weusi. Nadhani watu weusi wote ni wavivu.”
Rafiki yake na Huang akajibu, “Lakini Wakristo wanatakiwa wampende kila mtu! Wakristo hawawezi kuwahukumu watu wengine bila uhalali.” Huang alijibu, “Sitegemei kama Mungu ana nia katika mambo madogo kama haya. Je. kwani siyo jambo la kawaida kuepukana na watu walio tofauti na sisi?”
Mungu anasema, “Watakatifu hushughulika na watu wote – ikiwa ni pamoja na wale wote walio tofauti nasi - walio na huruma na rehema.”
"Lakini mkiitimiza ile sheria ya kifalme kama ilivyoandikwa, 'Mpende jirani yako kama nafsi yako,' mwatenda vema. Bali mkiwapendelea watu, mwafanya dhambi na kuhukumiwa na sheria kuwa wakosaji."[1]
Kipimo kimoja cha tabia yako ni jinsi unavyowatendea wale ambao hawana lolote la kufanya kwa ajili yako. Ni rahisi kuonyesha tofauti na heshima kwa watu wenye nafasi wanaotupatia fedha, kazi, au mamlaka. Upendo unaheshimu wale ambao hawawezi kufanya lolote kwa ajili yetu: maskini, wazee, watoto, na wale wote ambao hawana nafasi katika eneo lolote. “Sheria ya kifalme” ya upendo inagusa jinsi tunavyomtendea kila mtu. Upendo huikamilisha sheria.
Upendo huikamilisha sheria
Dhamira ya upendo mkamilifu ndio kiini kikuu katika ujumbe wa maisha matakatifu. Katika somo la 7, tuliona kwamba upendo kwa ajili ya Mungu ni zaidi ya hisia. Upendo kwa ajili ya Mungu hubadilisha kabisa mwelekeo wa maisha yetu. Sasa tunataka tumfurahishe Mungu zaidi kuliko tunavyotaka tujiurahishe wenyewe. Kwa njia hiyo hiyo, upendo kwa jirani zetu hubadili mwelekeo wa ubinafsi na umimi kwanza kwa ajili ya wengine.
Paulo anawaadikia kanisa la Rumi:
"Msiwiwe na mtu cho chote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sheria. Maana kule kusema, 'Usizini, Usiue, Usiibe, Usitamani' na ikiwapo amri nyingine yo yote, inajumlishwa katika neno hili: 'ya kwamba, mpende jirani yako kama nafsi yako.' Pendo halimfanyii jirani neno baya; basi pendo ndilo utimilifu wa sheria."[2]
Kila Mkristo anawiwa na deni la upendo. Paulo anatuhakikishia kwamba kama tutatimiza vigezo vya vya upendo, tutakuwa pia tumetimiza vigezo vyote vya sheria. Kama tutawapenda watu wengine, hatutafanya uasherati, uuaji, wizi, tamaa na kadhalika. Kigezo cha sheria kitakuwa kimetimizwa nitakapompenda jirani yangu kama ninayojipenda mwenyewe.
Katika sura za mwisho za kitabu cha Warumi, Paulo anaonyesha jinsi upendo unavyokamilisha sheria. Wale wote waliojazwa na upendo wa Mungu:
Watatumika kwa ajili ya mwili wa Kristo na siyo kwa ajili yao wenyewe (Warumi 12:3-5).
Watachukia maovu na kuambatana na yaliyo mema (Warumi 12:9).
Watawatanguliza wengine kwa kuwaonyesha heshima (Warumi 12:10).
Watajali mahitaji ya wengine (Warumi 12:13).
Watakuwa na amani na watu wote, hata na wale walio maadui zao (Warumi 12:14-21).
Watatii mamlaka zinazotawala (Warumi 13:1-7).
Wataheshimu misimamo ya waumini wengine (Warumi 14:1-23).
Watachukuliana madhaifu yao kama Kristo alivyofanya (Warumi 15:1-3).
Upendo kwa ajili ya Mungu hubadili mwelekeo wa moyo kutoka kwenye ubinafsi na kuwa kwa ajili ya Mungu. Upendo kwa ajili ya jirani zetu hubadili mwelekeo wa ubinafsi kwa ajili ya kuwajali wengine. Yote haya ni sehemu ya yale yanayoonyesha ni nini maana ya mtu mtakatifu.
John Wesley alifanya majumuisho ya nini maana ya ukamilifu wa Mkristo:
"Upendo ni zawadi ya hali ya juu kutoka kwa Mungu; unyenyekevu, upole, upendo unaovumilia. Maono yote, unabii wote, au karama zote ni mambo madogo sana ukilinganisha na upendo. Hakuna kitu chochote cha hali ya juu katika dini; kama unatafuta chochote kilicho zaidi ya upendo, unatafuta kisichoeleweka na unatoka nje ya sheria ya kifalme."
"Huwa unawauliza wengine, 'Umeshapokea Baraka hii au ile?' Kama unawauliza ukimaanisha chochote na siyo upendo, unamaanisha vibaya, unawapeleka nje ya njia, na kuwaweka kwenye harufu mbaya. Jifikirie ndani ya moyo wako, kwamba tangu wakati ule Yesu alipokuokoa kutokana na dhambi zote, hujalenga kwenye lolote zaidi ya ule upendo ulioko katika 1 Wakorintho 13. Huwezi kwenda zaidi ya hapo."[3]
Kumpenda jirani yako
Maeneo mawili yanaweza kuelezea jinsi upendo mkamilifu unavyoonekana kwa Wakristo wengine.
Upendo huheshimu mitazamo ya waamini wengine
Akiwaandikia Wakristo wa Korintho, Paulo anazungumzia kuhusu uhuru wa Kikristo. Nitawajibikaje kwa muumini mwingine ambaye atakuwa ameumizwa kiroho na uhuru wangu? Paulo aliandika kwa Wakristo “wenye uwezo” waliokuwa wakisema, “Tunatambua kwamba sanamu siyo chochote. Kula vyakula vya kutambikia havina matatizo yeyote kwetu.” Paulo alijibu:
"Lakini angalieni huu uwezo wenu usije ukawakwaza wale walio dhaifu. Kwa maana, mtu akikuona wewe uliye na ujuzi, umeketi chakulani ndani ya hekalu la sanamu, je! Dhamiri yake mtu huyo, kwa kuwa yu dhaifu, haitathibitika hata yeye naye ale vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu? Na yule aliye dhaifu aangamizwa kwa ujuzi wako, naye ni ndugu ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake. Hivyo, mkiwatenda dhambi ndugu zenu na kuitia jeraha dhamiri iliyo dhaifu, mnamtenda dhambi Kristo. Kwa hiyo, chakula kikimkwaza ndugu yangu, hakika sitakula nyama hata milele, nisije nikamkwaza ndugu yangu."[4]
Paulo angeacha kula nyama maisha yake yote kuliko kusababisha ndugu yake Mkristo dhaifu kuanguka. Upendo mkamilifu unamaanisha kwamba anajali zaidi wokovu wa ndugu yake Mkristo kuliko haki zake. Baadaye, Paulo anasema, “bali twayavumilia mambo yote tusije tukaizuia Habari Njema ya Kristo.”[5]
Wakorintho walisema, “Tuko huru kufanya lolote tunalolipenda. Hatuhitajiki kufikira kuhusu mahitaji ya waumini wengine.” Paulo akasema, “Niko huru kuhudumia mahitaji ya waumini wengine. Mimi siyo mfungwa wa matamanio na haki zangu mwenyewe. Niko huru kuwapenda wengine.” Huu ndio upendo mkamilifu ambao Mungu anataka kumpa kila Mkristo.
► Soma Warumi 14.
Katika kanisa la Roma, kulikuwa na Wakristo “dhaifu” waliokuwa wakila mboga za majani tu. Hawa inawezekana walikuwa ni Waristo wa Kiyahudi walioendelea kufuata sheria za vyakula, na hawakuwa tayari kula vyakula ambavyo havikuwa safi kwao. Kulikuwa pia na Wakristo “wenye uwezo” waliokuwa na ufahamu zaidi, na wakijua kwamba sheria za vyakula hazikuwa kikwazo tena kwa Mkristo.
Paulo alionyesha kila kikundi ni nini maana kupenda kama Kristo naye alivyopenda. Wakristo “dhaifu” wasiwahukumu wenzao wanaokula nyama. Upendo hauhukumu.
Hata hivyo, Mkristo “mwenye uwezo” asimnyanyase Mkristo “dhaifu” na asiutumie uwezo wake kudharau imani ya yule mdhaifu. Badala yake, Mkristo mwenye nguvu, aachane na haki zake ili aweze kuzuia kuharibika kwa imani ya yule muumini dhaifu. Kwa nini? Kwa ajili ya upendo:
"Na ndugu yako akiingia huzuni kwa sababu ya chakula, umeacha kwenda katika upendo. Kwa chakula chako usimharibu mtu yule ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake."[6]
Hii ndiyo maana ya kumpenda jirani yako mkristo. Tunapaswa kupenda kama Kristo naye alivyopenda. Aliyatoa maisha yake kwa ajili ya huyu ndugu mdhaifu; kwa hakika, Paulo anasema, tunaweza kuacha kula nyama ingawaje ni haki yetu.
► Jadili eneo ambalo waamini wa kweli na wa Mungu wanatofautiana. Maeneo ambayo hayako wazi kutokana na mafundisho ya Biblia; maeneo ambayo yanaonyesha tofauti za mitazamo. Tumia kanuni za Paulo kutoka Warumi 14 katika suala hili. Ni kwa jinsi gani makundi haya mawili – Wakristo “dhaifu” na “wenye uwezo” wanaweza kushughulikia eneo hili?
Upendo huwajali wakristo wanaoanguka katika dhambi
Jane ni Mkristo aliyetapeliwa katika biashara yake na mshirika mwenzake wa kanisa. Ivani alimwuzia gari lililokwisha tumika, akijua kwamba gari hilo lilikuwa na matatizo makubwa ya kiufundi. Ivani alimdanganya Jane kwamba, “gari hili limeshakaguliwa na fundi magari, na kwamba limethibitishwa liko katika hali nzuri sana. Unaweza kuniamini. Mimi ni Mkristo.”
Baada ya siku mbili tu baada ya kuwa gari lile limenunuliwa, Jane aligundua kwamba mfumo wa usambazaji umeme kwenye lile gari ulikuwa mbovu – na kwamba Ivani alikuwa analijua tatizo hilo.
► Jane atafanya nini?
Je, umejibu, “Jane atamwonya kila mtu kwamba Ivani siyo mwaminifu”? Je, umejibu, “Jane hatasema lolote katika kujizuia asimdhalilishe Mkristo mwenzake”? Tuangalie jibu la Yesu.
► Soma Mathayo 18:15-17.
Yesu alitoa hatua nne ambazo zinaonyesha upendo mkamilifu unavyoshughulika na mtu aliyeanguka katika dhambi. Tafadhali fahamu kwamba mfano huu unahusiana na tabia ya dhambi. Yesu hapa hazungumzii kuhusu tofauti binafsi za mawazo. Hajasema, “Ondokeni, nendeni mkashughulike na matatizo ya kila mtu.” Yesu anaelezea hali ambayo ndugu mkristo amemkosea mkristo mwenzake. Tuziangalie hatua hizi:
Nitaenda kwa yule ndugu mimi mwenyewe. Upendo mkamilifu “haufurahii udhalimu.”[7] Hautafuti nafasi ya kueneza udhalimu. Badala yake, mtu wa upendo hujaribu kulishughulikia tatizo kwa ukimya yeye mwenyewe. Mtu wa upendo hushughulika na ndugu “aliyeghafilika katika kosa lolote… kwa roho ya upole.”[8] Lengo ni kumrejeza upya ndugu huyo. Kama hakutakuwepo na kutubu…
Nitachukua mtu mmoja au wawili pamoja nami kama mashuhuda. Hapa pia lengo kuu ni kurejeza upya. Mashahidi hawa ni lazima wawe viongozi wa kiroho wa kanisa wanaoweza kutoa ushauri mzuri wa kuleta urejezo upya.[9] Kama hakutakuwepo na kutubu…
Nitaileta dhambi hiyo kwenye kusanyiko la kanisa. Hapa pia lengo kuu ni kurejeza upya. Lengo hapa siyo kulipiza kisasi au kumdhalilisha mtu hadharani. Lengo la Kanisa kuadabisha lazima liwe ni kuleta kutubu na kumrejesha ndugu. Kama mtu huyu ataasi na akakataa kutubu…
Kanisa lichukue hatua za nidhamu dhidi ya huyu mbaya. Kanisa la Korintho lilikuwa na mshirika wa kanisa aliyetenda dhambi ya uzinzi. Paulo aliliagiza kanisa limchukulie hatua za kinidhamu mtu huyu. “Mwondoeni yule mbaya miongoni mwenu.”[10] Hatuwezi kupuuzia matendo ya dhambi katika mwili wa Kristo.
Hata hivyo, tafadhali angalia haya maneno ya Yesu: “Na asipolisikiliza kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru.”[11] Ni kwa jinsi gani wakristo wanatakiwa kuwatendea watu wa mataifa na watoza ushuru? Kwa upendo. Hadi hapa, bado lengo ni kurejeza upya. Katika 2 Wakorintho, Paulo analezea hali ya muumini ambaye anapewa nidhamu na kanisa na ametubu kweli. Paulo anasema,
"Yamtosha mtu wa namna hii adhabu ile aliyopewa na walio wengi; hata kinyume cha hayo, ni afadhali mumsamehe na kumfariji, mtu kama huyo asije akamezwa katika huzuni yake ipitayo kiasi. Kwa hiyo nawasihi kumthibitishia upendo wenu."[12]
Katika 1 Wakorintho, Kanisa lilivumilia dhambi za wazi na halikutaka kuchukua hatua za kinidhamu kwa wale waliitenda dhambi hizo. Paulo akawakumbusha kwamba Upendo wa Mungu unataka watu wote watenda dhambi dhidi ya mwili wa Kristo wachukuliwe hatua za kinidhamu.
Katika 2 Wakorintho, Kanisa lilichukulia hatua za kinidhamu dhidi ya mtu aliyetenda dhambi, lakini wakati mtu huyu alipotubu, kanisa halikutaka kumsamehe. Paulo akawakumbusha kwamba upendo kwa ajili ya jirani yako unahitaji tuwasamehe wale wote wanaotubu.
Lengo la kuchukua nidhamu kwa kanisa lazima siku zote liwe ni toba na marejezo upya. Upendo mkamilifu hautafuti kulipa visasi.
Kumpenda jirani asiyeamini
Ni kwa njia gani tunaweza kuonyesha upendo mkamilifu kwa watu ambao hawajaamini, zaidi sana wale ambao wanatuchukia kwa sababu tu sisi ni Wakristo? Yesu alisema,
"Mmesikia kwamba imenenwa, 'Umpende jirani yako, na, umchukie adui yako,' lakini mimi nawaambia, wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni."[13]
Unapowapenda wale wanaokusababishia wewe mateso, uko “mkamilifu kama Baba yako wa mbinguni alivyo mkamilifu.” Watu watakatifu wana upendo kama Baba wa Mbinguni alivyo na upendo. Hii ndio maana ya kuwa mkamilifu.
Watu watakatifu, “hudhihirisha upendo wao kwa watu wote, siyo tu kwa waamini wenzao, bali pia kwa wale wote ambao siyo waamini wenzao, wale wanaotupinga, na wale wote wanaojihusisha na matendo ya uovu.” Tunapaswa tuwajibike kwa wale wanaotupinga kwa huruma, polepole, kwa uangalifu na unyenyekevu. Mungu anakataza kuanzisha ugomvi, kulipiza visasi, vitisho, au kujitafutia haki mwenyewe. Ingawaje Mungu anatuamuru tuachane na matendo ya dhambi, tunapaswa kumpenda na kumwombea mtu yeyote anayejihusisha na tabia hizi.”[14]
Wakristo siku zote wamekuwa wakiishi katika ulimwengu unaoipinga Injili. Paulo aliwataka watu wa Rumi kuheshimu mamlaka zilizopo na kulipa kodi zao – kwa serikali iliyokuwa inawauwa Wakristo na muda siyo mrefu itamuuwa na Paulo.
Petro aliwaagiza Wakristo, “Waheshimuni watu wote. Wapendeni ndugu. Mcheni Mungu. Mpeni heshima mfalme.”[15] Huyu pia ni mfalme anayetakiwa apewe heshima, lakini muda siyo mrefu naye atamuuwa Petro. Lakini Petro alitaka sana Wakristo wawapende adui zetu. Kwa kuwapenda hata maadui zetu, tunakuwa mashuhuda wa ukweli wa Injili. “Kwa sababu ndiyo mapenzi ya Mungu, kwamba kwa kutenda mema mzibe vinywa vya ujinga vya watu wapumbavu.”[16]
Yoshua ni Mchungaji kutoka Nigeria katika eneo moja la Kaskazini ambako kuna Wakristo wengi lakini wamekuwa wakiteswa vikali na mashambulizi ya wanajeshi wa Kiislamu. Wanajeshi hawa wamekuwa wakichoma makanisa, kuuwa Wakristo, na kuwateka wasichana wadogo wa kike kwa ajili ya kuwauza kama watumwa. Mara ya mwisho nilipoitembela tena Nigeria, Yoshua alinionyesha picha za miili ya marehemu waliokuwa washirka wa kanisa lake waliokuwa wameuawa na washambuliaji wa Kiislamu.
Kisha Yoshua akanionyesha picha zinazoonyesha hatua zilizochukuliwa na kanisa lake baada ya mauaji hayo. Kanisa lake lilijenga shule katika kijiji cha Waislamu; walichimba kisima cha maji kwa ajili ya wanakijiji; walitoa viti vya magurudumu kwa ajili ya Waislamu waathirika wa ukoma; na sasa wanajenga kituo cha zahanati kwa ajili ya kijiji hicho. Wanaonyesha upendo kwa maadui zao.
Mchungaji Yoshua alisema, “Waislamu wengi wanakuja kwa Kristo kwa sababu wanauona upendo wa Mungu kupitia Wakristo. Tunawapata siyo kwa kutumia mitutu ya bunduki au kulipiza kisasi; bali tunawapata kupitia kuishi kwetu sawa na andiko la Mathayo 5:43-48.” Haya ni matokeo ya maisha ya upendo mkamilifu tunayoyaishi kwa sasa duniani.
► Kuna changamoto gani kubwa katika kuwapenda jirani ambao hawajaamii katika dunia yako? Orodhesha baadhi ya hatua za kivitendo za kuonyesha upendo kwa watu ambao hawajaamini katika jumuiya yako.
Mwandishi wa Kirusi Leo Tolstoy aliandika makala fupi kuonyesha nini maana ya kuishi maisha ya upendo mkamilifu. Martini alikuwa maskini mtengenezaji wa viatu aliyempenda Mungu kwa kiwango kikubwa sana.[17] Siku moja usiku, Martini akiwa anasoma Biblia alipitiwa na usingizi akalala. Akawa anaota kwenye ndoto Yesu akisema kwamba, “Kesho, nitalitembelea duka lako.”
Siku iliyofuata, Martini alikaa akiwa anamngojea Yesu. Watu wengine walikuja dukani kwa Martini, lakini Yesu hakutokea. Askari mmoja wa zamani, mzee, alikuwa amesimama nje akitetemeka kwa baridi. Martini alimkaribisha huyu mzee dukani kwake apate kikombe cha chai ya moto. Mwanamke mmoja maskini naye akawa anapita karibu na duka hilo, akijaribu kumfunika mwanae kwa ajili ya kumpatia joto. Martini alimnunulia supu na blanketi kwa ajili ya kumlinda mtoto na baridi. Baadaye Martini alinunua chakula kwa ajili ya kijana aliyekuwa na njaa.
Martini alikata tamaa kwa kuwa Yesu ilikuwa aje, lakini akasema, “Ilikuwa ni ndoto tu. Ilikuwa ni ujinga mimi kufikiria kwamba Yesu angeweza akaja kwenye duka la viatu.”
Usiku uliofuata, Martini akiwa anasoma Biblia, alisikia usingizi akalala. Aliota ndoto kwamba aliwaona watu wakiwa wamesimama dukani kwake. Yule askari akamwuliza, “Martini unanikumbuka? Mimi ni Yesu.” Mwanamke aliyekuwa na mtoto naye akamwambia, “Martini, mimi ni Yesu.” Kijana aliyekuwa na njaa akasema, “Mimi ni Yesu.” Martini aliamka na kuanza kusoma:
"Kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia…. Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi."[18]
Katika karne ya pili, kundi moja la Wakristo liliitwa “Genge la wacheza Kamari” kwa sababu walihatarisha maisha yao kwa kuwatunza watu waliokuwa wanakufa kwa magonjwa ya kuambukiza. Hili kundi liliwatembelea wafungwa, kuwahudumia wagonjwa, na kuokoa watoto wadogo waliokuwa wametupwa na wazazi wao. Genge la wacheza Kamari lilidhihirisha upendo kamili.
Katika mwaka 252 B.K. ugonjwa wa tauni ulitokea katika jiji la Carthage. Madaktari waligoma kuwatembelea wagonjwa; familia zilitupa miili ya wapendwa wao waliofariki barabarani, jiji lilikuwa katika taharuki kubwa. Cyprian, askofu mkuu wa Carthage, aliwakutanisha waumini wake. Aliwakumbusha kwamba Wakristo wameitwa kuonyesha upendo mkamilifu. Wakristo wa Carthage wakaanza kuwazika waliokufa, kuwaganga waliokuwa wagonjwa, na wakaukoa mji wao kutokana na uharibifu. Walikuwa watu wa upendo kamili; walikuwa “wakamilifu” kama Baba yao wa mbingini alivyo mkamilifu.
Esther Ahn Kim[1] alikuwa mwalimu wa muziki aliyeishi katika nchi ya Korea wakati wa utawala wa Wajapani kuanzia mwaka 1937. Wajapani walimtaka kila mkaazi kuinamia sanamu ya mungu jua katika milima ya Namsan. Mwaka 1939, Esther aliamriwa kusujudu kwenye hekalu la mungu jua. Adhabu ya kukataa kusujudu ilikuwa ni kufungwa jela pamoja na mateso makali.
Baadhi ya Wakristo walishaamua kwamba, “Kwa nje tutasujudu, lakini dhamira yetu ya ndani itamwabudu Kristo.” Esther alidhamiria kabisa kwamba hawezi kumsujudia Mungu wa uongo. Alimpenda Mungu kwa moyo usiogawanyika. Siku hiyo, alikataa kusujudu.
Mwishoni mwa mwaka 1939, baada ya kuwa mafichoni kwa miezi kadhaa, Esther Ahn Kim alikamatwa. Kwa miezi yote hiyo aliyokuwa mafichoni alikuwa anajiandaa kwenda jela. Alifunga na kuomba, alikariri Maandiko, na alijiandaa kiakili na kimwili katika kukabiliana na mateso ya jela.
Kim alitumikia kifungo cha miaka sita jela. Alisulubiwa mara kwa mara kwa mateso lakini alibakia kuwa mwamiifu kwa sababu alimpenda Mungu. Lakini Kim alijitambua kwamba alikuwa ameitwa kumpenda jirani yake. Akiwa kule jela, Esther alianzisha kuomba kila siku asubuhi, “Mungu ni mtu gani unataka umpende leo kupitia mimi?” Wakati mwingine alitoa chakula chake cha mgao kwa siku kadhaa kwa mama mmoja aliyekuwa amehukumiwa kunyongwa kwa kosa la kumuua mume wake. Kupitia upendo wa Esther Kim, huyu mama alimpokea Kristo kabla hajafa.
[1] Ilichukuliwa kutoka: Esther Ahn Kim, If I Perish (Chicago: Moody Press, 1977).
Tafakuri ya Somo la 8
(1) Watu katika wakati wa dunia ya Yesu waliamini kile kilichofundishwa na Agano la Kale kuhusu utakatifu. Hata hivyo, walishindwa kuishi kwenye mpangilio wa Mungu kwa ajili ya watu watakatifu.
(2) Mfano halisi wa kuigwa wa utakatifu unaonekana katika maisha ya Yesu wa Nazarethi. Alifuata kila kanuni ya utakatifu kutoka katika Agano la Kale
(3) Kumpenda jirani yetu kwa ukamilifu ni kupenda kama Yesu alivyopenda – kwa kujitoa na unyenyekevu.
(4) Kuwa mkamilifu maana yake ni kuwa kamili. Kuwa mkamilifu haina maana kwamba hakuhitajiki kukua tena.
(5) Agizo au amri, “ni ahadi zilizojificha.”Kama Mungu akiagiza jambo, atafanya liwezekane. Utakatifu unakamilishwa siyo kwa nguvu za kibinadamu bali kwa neema ya Mungu.
(6) Upendo ni ukamilifu wa sheria. Tunapopenda kama Mungu anavyotutaka tupende, tunatimiza matakwa ya sheria.
Kazi ya Kufanya
(1) Andaa andiko kuhusu “Kumpenda adui yako wa karne ya ishirini na moja.” Tumia Mathayo 5:43-48 kama andiko lako. Onyesha inamaanisha nini kumpenda adui yako katika dunia yetu. Hakikisha unajumuisha na habari njema za kile Mungu alichokifanya kupitia Kristo hata kuweza kumpenda adui yako liwe jambo linalowezekana.
(2) Anza kikao kinachofuata cha darasa kwa kunukuu Mathayo 5:43-48.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.