Alipokuwa akichunga kondoo jangwani, Musa aliona kijiti kilichokuwa kinawaka lakini hakiteketei. Wakati Musa alipokuwa akisogea karibu na eneo hili la ajabu, alimsikia Mungu akiita, “Musa, Musa!” Musa akasema, “Mimi hapa.” Mungu akamwonya, “Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu.”[1]
Katika ulimwengu wa zamani, kutembea miguu mitupu kuliwakilisha unyenyekevu na heshima kuu. Hakuna mtu ambaye angeweza kuvaa kanda mbili mbele ya Farao. Musa alikuwa mbele ya aliyekuwa mkuu kuliko Farao. Alikuwa mbele ya Mungu mwenye mamlaka yote. Musa alikuwa kwenye nchi takatifu.
Kulikuwa na kitu gani maalumu kuhusiana na eneo alilosimama Musa? Nini kilipafanya pawe patakatifu? Je, kulikuwa na uzio uliokuwa umebandikwa ishara ya “Nchi Takatifu”? Hapana. Kuna mtu yeyote aliyeandaa sherehe za kidini kuashiria kwamba nchi hiyo ni takatifu? Hapana.
Ardhi hiyo ilikuwa takatifu kwa sababu tu ni mali ya Mungu. Mungu alikitenganisha kipande hiki cha ardhi kutoka katika eneo lote la jangwa na kutangaza kuwa ni takatifu; Mungu “aliitakasa” hiyo ardhi. Hii inatoa kielelezo muhimu sana kuhusiana na utakatifu. Ardhi hii ilikuwa takatifu kwa sababu Mungu aliitenga. Kile kilichokuwa kitakatifu kiliwekwa pembeni, kikatengwa na Mungu.
Miaka mingi baadaye, Mungu akakutana na Musa kwenye mlima Sinai. Hapa tena, Mungu akaweka pembeni kipande cha ardhi kama kitakatifu. Musa aliwaambia watu wakae mbali na ule mlima. Hawakutakiwa kuukwea mlima huo au kugusa chochote kilichokuwa karibu kwa sababu ulikuwa takatifu. Uwepo wa Mungu mlimani ulikuwa na nguvu sana hata ikabidi Musa awaonye watu kwamba yeyote atakayeugusa mlima ule “atauawa.”[3] Mlima ni mali ya Mungu. Musa alisimama kwenye nchi takatifu.
[1]Sala kwa ajili ya Utakatifu “Mungu mwenye nguvu zote, Umetuweka sisi kwa ajili yako mwenyewe, na mioyo yetu haitapumzika hadi ipate pumziko kutoka kwako. Tupe usafi wa moyo na nguvu za kusudi lako, na kwamba hakuna hisia za binafsi zitakazotuzuia kuyajua mapenzi yako, na hakuna madhaifu yatakayotuzuia kuyafanya.”
- Augustine wa Hippo
Utakatifu ni tabia ya Mungu. Katika maandiko, neno “utakatifu” linarejea kwamba ni Mungu au chochote ambacho ni mali ya Mungu. Katika kisa cha cha Musa na kichaka kilichowaka moto, ardhi ilikuwa takatifu kwa sababu ilikuwa ni mali ya Mungu. Kuwa mtakatifu inamaanisha kutengwa kwa ajili ya Mungu. Mifano mingi kutoka katika vitabu vitano vya mwanzo vya Biblia inaonyesha kwamba vitu “vitakatifu” hutengwa pembeni na vitu vingine vya kawaida.
Siku takatifu
Kwa mara kwanza neno “utakatifu” kuonekana kwenye Biblia halikuwa limemrejelea kwa mtu bali siku. Katika mwisho wa siku sita za uumbaji. Mungu aliitenga siku ya saba pembeni na zile siku sita.
"Kwahiyo Mungu akaitakasa siku ya saba na kuifanya takatifu, kwa sababu katika hiyo Mungu alipumzika kutokana na kazi zote alizozifanya wakati wa uumbaji."[1]
Siku ya saba ilikuwa takatifu kwa sababu ilitengwa kwa ajili ya Mungu; haikuwa ya kawaida tena. Isaya alisema Sabato ilitengwa kutoka katika siku nyingine zote. Siku hii siyo kwa ajili ya “njia zenu wenyewe” au “anasa zenu wenyewe”; ni mali ya Mungu.[2] Sabato ilitengwa na Mungu kwa ajili ya kuabudu.
Uaminifu wa Isareli kwa ajili ya Sabato ulionyesha uaminifu wake kwa Mungu. Mungu aliyeitenga Sabato pia aliitenga Israeli.
"Bwana akasema na Musa, na kumwambia, 'Kisha, nena wewe na wana wa Israeli, na kuwaambia, "Hakika mtazishika Sabato zangu, kwa kuwa ni ishara kati ya mimi na ninyi katika vizazi vyenu vyote; ili mpate kujua ya kuwa mimi ndimi Bwana niwatakasaye ninyi."'"[3]
Kuwa mtakatifu ni kutengwa na Mungu na kwa ajili ya Mungu. Mungu aliitakasa Sabato; Mungu anawatakasa watu wake.
Vitu vitakatifu
Kipande cha ardhi kilichotengwa pembeni kutoka katika ardhi nyingine kilikuwa kitakatifu; ni mali ya Mungu. Siku iliyokuwa imetengwa pembeni kutoka katika siku nyingine ilikuwa takatifu; ni mali ya Mungu. Chochote kinachotengwa kwa ajili ya Mungu kilikuwa kitakatifu.
Mavazi waliyokuwa wanavaa makuhani yalikuwa matakatifu.[4] Yalikuwa yanatengenezwa kwa maelekezo maalumu kutoka kwa Mungu na yalikuwa mali yake. Sadaka ambazo watu waliziletakwenye hema la kuabudia zilikuwa takatifu; zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya Mungu.[5] Makuhani walitumia mafuta maalumu wakati wa kuabudu. Mungu aliamuru, “Haya yatakuwa ni mafuta matakatifu ya kutiwa kwa ajili yangu mimi katika vizazi vyenu vyote.”[6] Hakuna mtu mwingine yeyote ambaye angeweza kutumia mafuta haya; yalikuwa yametengwa pembeni kwa ajili ya matumizi ya Mungu.
Utoaji kwa ajili ya hema la kuabudia, Mungu alitaka kila mtu wa Israeli alipe kodi iliyoitwa “shekel ya mahali patakatifu.”[7] Fedha hii haikutumika kwa matumizi ya kawaida. Wasomi wengi wanaamini kwamba hii ilikuwa ni sarafu nyingine tofauti kabisa na shekali ya kawaida. Ilikuwa takatifu; ilikuwa mali ya Mungu.
Vitu vya samani katika hekalu la kuabudia vilikuwa vitakatifu. Mungu alimwamuru Musa kutenganisha hizi samani kutoka katika vitu vingine vyote. “Nawe utavitakasa vitu hivyo, ili viwe vitakatifu sana; tena kila kivigusacho vyombo vile kitakuwa kitakatifu.”[8]
Kila kitu kilikuwa aidha kitakatifu au cha kawaida.[9] Kuwa kawaida haikumaanisha kwamba kinahusika na dhambi; bali ilimaanisha kwamba hakikuwa kimetengwa pembeni kwa ajili ya matumizi ya Mungu. Kuna uwezekano wa mambo matatu yaliyoeleweka kwa Israeli kuhusiana na kila kitu:
Kichafu – hakuna ambaye angeweza kukitumia. Kilikuwa ni marufuku kwa wana wa Mungu.
Kisafi – Kilikuwa ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
Kitakatifu – Kilichotengwa pembeni kwa ajili ya matumizi ya Mungu tu. Kilikuwa kinatumika tu kwenye ibada ya Mungu.
Kabla Israeli haijaingia katika nchi ya Kaanani, Mungu alitoa maelekezo kwa ajili ya kupanda miti.
Kwa miaka mitatu ya kwanza, matunda yake “mmenyimwa” msiyatumie. Ni “machafu” kwa ibada.
“Katika mwaka wa nne matunda yake yote yatakuwa ni matakatifu, kwa ajili ya kumpa Bwana shukrani.” Matunda ya mwaka wa nne yalitengwa pembeni na Mungu kwa ajili ya matumizi yake. Yalikuwa “matakatifu”
Kuanzia mwaka wa tano, “mtakula katika matunda yake.” Miti sasa ni “misafi” kwa ajili ya matumizi yake.[10]
Maeneo Matakatifu
Hema ya kukutania ilikuwa takatifu kwa sababu ilikuwa imetengwa pembeni na Mungu. Kila kitu kwenye hema ya kukutania kilikuwa kimetengwa kwa matumizi ya Mungu. Sehemu ambayo Mungu alikuwa akikutana na kuhani mkuu paliitwa Mahali Patakatifu Pa-patakatifu.
Baadaye, hekalu la Yerusalemu lilikuwa takatifu kwa sababu lilitengwa maalumu kwa ajili ya kumwabudia Mungu. Hekalu lilikuwa takatifu tu kwa sababu ni mali ya Mungu. Kwa sababu ya dhambi ya Israeli, Ezekieli aliona maono ya utukufu wa Mungu ukiondoka katika Hekalu.[11]
Baada ya utukufu wa Mungu kuondoka, hekalu halikuwa takatifu tena. Mwaka 63 KK, Jenerali wa Kirumi aitwaye Pompey aliingia Patakatifu Pa-Patakatifu akakuta pako wazi hakuna chochote. Kwa sababu Mungu hakuwa akiishi tena pale, hekaluni.
Kabila Takatifu
Kabila la Walawi lilitengwa maalumu na Mungu. Katika usiku ambao Israeli walikuwa bado hawajaondoka, kila mzaliwa wa kwanza katika kila Mmisri aliuawa. Wazaliwa wa kwanza wa Israeli waliokolewa kwa sababu walitii amri ya Mungu ya kunyunyiza damu juu ya miimo ya milango ya kila nyumba.
Israeli ilikumbuka ukombozi wao kutoka Misri kwa njia mbili. Kwanza, kila familia ya Mwisraeli ilishiriki “Chakula cha Pasaka” kila mwaka. Chakula hiki kilisherehesha ukombozi wa Israeli kutoka Misri
Njia ya pili ambayo Israeli inakumbuka ukombozi wao ni ya kuvutia zaidi. Kuwakumbukusha Israeli kwamba amewakomboa wazaliwa wao wa kwanza wote, Mungu aliamrisha:
"Nitakasie mimi wazaliwa wa kwanza wote. Kila afunguaye tumbo katika wana wa Israeli, wa binadamu na wa mnyama; ni wangu huyo."[12]
Neno “nitakasie” linatokana na neno la Kiebrania “takasa” au “iliyotengwa pembeni.” Kila mzaliwa wa kwanza ni mali ya Mungu. Mungu alilichagua kabila la Walawi kuwakilisha wazaliwa wa kwanza wa Israeli yote. Kabila hili lilitumika badala ya taifa lote.
"Mimi, tazama, nimewatwaa Walawi na kuwatoa kati ya wana wa Israeli badala ya wazaliwa wa kwanza wote wafunguao tumbo katika wana wa Israeli; na hao Walawi watakuwa wangu; kwa kuwa hao wazaliwa wa kwanza wote ni wangu; katika siku ile niliyowapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri nikajiwekea wakfu wazaliwa wa kwanza wote wa Israeli, wa wanadamu na wa wanyama; Watakuwa wangu; Mimi ndimi BWANA."[13]
Katika kitabu cha Kutoka 29, Mungu aliagiza jinsi ya kutakasa makuhani. Jina “utakatifu” linatumika mara tisa katika sura hii. Walawi walitakaswa mahali pa wazaliwa wote wa kwanza; kabila lote lilikuwa ni mali ya Mungu kabisa.
► Kwa nini ilikuwa ni muhimu sana Mungu aweke msisitizo katika ujumbe wa kutengwa kwa Israeli? Kwa nini Paulo awekee msisitizo ujumbe huu kwa makanisa katika Korintho (2 Wakorintho 6:14-7:1) na Thesalonike (1 Wathesalonike 4-5)? Kwa nini ujumbe huu ni muhimu hadi leo?
Mifano hii (siku takatifu, maeneo takatifu, n.k.) inaonyesha kwamba kuwa mtakatifu ni kutengwa kwa ajili ya Mungu. Hii inatusaidia tuelewe maana ya maisha ya utakatifu kwa sasa. Mtu mtakatifu moja kwa moja ni wa Mungu. Ametengwa kwa ajili ya makusudi ya Mungu. Kuwa mtakatifu ni kutengwa kutoka katika dhambina kutengwa kwa ajili ya Mungu.
[9] Tafsiri nyingi hutumia neno “vya ulimwengu” badala ya “vya kawaida” kwenye vitu. Toleo la KJV linatumia “visivyo vitakatifu.” Katika maneno yote hakuna linaloonyesha “kuwepo na dhambi.” Maneno haya kiuhalisia yanamaanisha kwamba hicho chombo “hakijatengwa” kwa ajili ya matumizi ya mambo ya utakatifu.
Kwa sababu Mungu ni mtakatifu, watu wake ni lazima wawe watakatifu. Watu wenye dhambi hawawezi wakawa na mahusiano na Mungu aliye mtakatifu. Watu watakatifu hujitenga wenyewe na chochote kinachomchukiza Mungu.
Mungu Mtakatifu anachukia dhambi
(1) Mungu aliudhihirisha utakatifu wake katika gharika.
Dunia iliyoumbwa na Mungu ilikuwa “nzuri sana,” lakini dhambi ikauharibu uumbaji. Mungu alipomwangalia mwanadamu, aliouna uovu ndani ya moyo wake.
"Bwana akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu siku zote. Bwana akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo."[1]
Nuhu na familia yake waliokolewa kwa sababu waliishi maisha ya utakatifu. “Nuhu alikuwa mtu wa haki, mkamilifu katika vizazi vyake; Nuhu alikwenda pamoja na Mungu.”[2] Alibakia akiwa ametengwa kutoka katika dhambi.
(2) Mungu alidhihirisha utakatifu wake kwenye maamuzi yake juu ya Nadabu na Abihu.
Watoto wakubwa wa Haruni walitengwa kwa ajili ya huduma kwa Mungu. Walipokiuka utakatifu wa hema ya kuabudia, “moto ukatoka hapo mbele za Bwana, nao ukawala, nao wakafa mbele za Bwana.”[3] Kitabu cha Mambo ya Walawi hakikuelezea kumbukumbu za ndani kuhusu dhambi ya Nadabu na Abihu, lakini Mungu alisema, “Nitatakaswa mimi katika hao wanikaribiao, nami nitatukuzwa mbele ya watu hao wote.”[4] Makuhani wa Mungu wanapaswa kuitendea hema ya kuabudia kama takatifu. Nadabu na Abihu walifikiri wangeweza kuutendea utakatifu kama yalivyo mambo mengine ya kawaida.
(3) Mungu alidhihirisha utakatifu wake kwenye maamuzi yake juu ya Musa na Haruni.
Musa na Haruni hawakuingizwa katika Nchi ya Ahadi kwa sababu “hamkuniamini mimi, (Mungu) kama mtakatifu ili kunistahi mbele ya macho ya wana wa Israeli.”[5] Baada ya Mungu kumwamrisha Musa auambie mwamba utoe maji, Musa aliupiga mwamba. Mungu alimhukumu Musa kwa sababu hakumheshimu Mungu kabla ya watu.
Kwa sababu Mungu ni mtakatifu, hawezi kupuuzia dhambi. Mara kumi katika vitabu vitano vya mwanzo vya Biblia, dhambi inaitwa “machukizo mno kwa Mungu,” Jambo ambalo Mungu anachukia. Mungu mtakatifu anachukia dhambi.
Watu Watakatifu wanachukia dhambi
Mungu ni wa utakatifu na Mungu ni wa upendo. Dhambi ya mwanadamu ilisababisha tatizo kubwa. Ni kwa jinsi gani Mungu aliye mtakatifu anaweza kujenga mahusiano na mwanadamu mtenda dhambi? Ni kwa namna gani anaweza kuuonyesha upendo wake kwa mwanadamu na kuwa mkweli kwa utakatifu wake kwa wakati mmoja?
Mungu alitoa Sheria yake kuwasaidia watu wake waweze kuishi kama watu watakatifu. Sheria haikutolewa ili kuyafanya maisha yawe magumu kwetu; ilitolewa ili itusaidie kuishi kwenye mahusiano sahihi na Mungu. Sheria iliwapa watu mfumo wa kuweza kujitenga na dhambi. Watu watakatifu wataichukia dhambi sawa na Mungu mtakatifu anavyoichukia dhambi.
Waandishi wa Agano Jipya walifundisha kwamba kujitenga kwa ajili ya Mungu kunahitaji kujitenga na dhambi. Yakobo alisema, “Hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu.”[7] Haiwezekani ukawa rafiki wa Mungu na wa dhambi kwa wakati mmoja. Haiwezekani ukatembea na Mungu pamoja na dhambi kwa wakati mmoja. Maisha ya utakatifu yanahitaji kujitenga na dhambi.
Paulo aliandika kwa watu waliofikiri kwamba neema ya Mungu kwao inawaruhusu kuendelea katika kuikumbatia dhambi. Aliuliza, “Tufanye dhambi kwa sababu hatuwi chini ya sheria bali chini ya neema?”[8] Jibu la Paulo lilikuwa la kukazia sana, “Hasha! Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii?” Kuna chaguo la mambo mawili tu:
Kama utajitoa mwenyewe kwa ajili ya dhambi, mwisho wake ni kifo.
Kama utajitoa mwenyewe kwa Mungu, mwisho wake ni kuhesabiwa haki.[9]
Huwezi ukajitoa mwenyewe kwenye dhambi na kwa Mungu kwa wakati mmoja. Wakristo “baada ya kuwekwa huru mbali na dhambi, wamekuwa watumwa wa haki.”[10] Kama watoto wa Mungu, tunapaswa tutengwe na dhambi.
Paulo aliyaweka haya katika maneno ya vitendo kuonyesha wajibu wetu wa kuepukana na dhambi za kujitakia. “Kwa kuwa kama mlivyovitoa viungo vyenu vitumiwe na uchafu na uasi mpate kuasi, vivyo hivyo sasa vitoeni viungo vyenu vitumiwe na haki mpate kutakaswa.”[11]
Haiwezekani kuimarisha urafiki na dhambi wakati huo huo ukiishi na Mungu. Kutengwa kwa ajili ya Mungu, kunahitaji kutengwa kutokana na dhambi. Hatuwezi tukaendeleza urafiki na Mungu na dhambi kwa wakati mmoja. Baada ya Adamu na Hawa, kutenda dhambi, walijificha wenyewe kutoka katika uso wa Mungu kwenye miti iliyokuwa kwenye bustani hiyo.[12] Kuunganika na dhambi kumesababisha kutengwa mbali na Mungu.
Wokovu hautufanyi tuwe huru katika kuendelea kutenda dhambi. Wokovu umetuweka huru na dhambi ili tuweze kuwa watakatifu. Lengo la wokovu ni kuwaleta watu wa Mungu kwenye utakatifu. Lengo la Mungu ni kututoa katika dhambi na kututenga kwa ajili ya mahusiano na yeye mwenyewe.[13]
Nilikuwa ninasafiri sehemu ya mlimani huko Taiwan. Mbele ya barabara kulikuwa na mwamba uliomeguka kwenda hadi chini sana kwenye mto. Unadhani niliweza kumwuliza dereva anionyeshe wakati anaendesha gari na kwamba anaweza kuusogelea ule mwamba kwa ukaribu kiasi gani? Hapana! Nilikuwa nataka nikae mbali sana itakavyowezekana na mwamba huo. Vivyo hivyo, mtu mtakatifu hujiweka mbali na dhambi. Katika kila eneo la maisha, mtu mtakatifu huepuka kila aina ya mtindo wa maisha ya dhambi. Mtu mtakatifu anakaa mbali sana na dhambi na anakaa karibu sana na Mungu.
Mtume Petro analiweka jambo hili kama ifuatavyo: “ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu.” Sisi tutafanyaje? Kwa kuishi maisha matakatifu. “Ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho. Muwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa.”[14] Maisha ya utakatifu ya wana wa Mungu ni alama ya kumilikiwa. Watu watakatifu hukaa mbali na dhambi kwa sababu ni wa “milki yake mwenyewe,” watu ambao ni mali ya Mungu. Mtu mtakatifu anataka awe mali ya Mungu kabisa.
Paulo aliwakumbusha watu wa Korintho kwamba “wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu.” Anaorodhesha msururu wa baadhi ya watu ambao hawaturith: “Waasherati, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi hawataurithi ufalme wa Mungu.” Kisha anawakumbusha, “Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii” Wakristo wa kule Korintho walikuwa wamekulia katika mazingira ya maovu na walikuwa wamefanya matendo mengi ya dhambi.
Lakini Paulo anakataa kuwaacha Wakristo katika hali ile. Hajasema, “Sasa ninyi ni Wakristo – mnaoweza kuendelea kuwa waasherati, waabudu sanamu, wazinzi, wafiraji, walawiti, wevi, watamanio, walevi, watukanaji, wanyang'anyi na kadhalika.” Badala yake, Paulo anasema. “lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu.”[15]
Paulo anafurahia, “Hamko tena kama mlivyokuwa! Hamfungwi tena na zile dhambi. Mmetengwa kwenye dhambi na sasa ninyi ni mali ya Mungu.” Kuwa mtakatifu ni kutengwa na dhambi ili tuweze kutengwa kwa ajiliya Mungu.
Uzia alikuwa mfalme mzuri ambaye “alifanya yaliyo ya adili machoni pa Bwana… Akajitia nia amtafute Mungu… Mungu akamsaidia juu ya Wafilisti.”[1] Uzia alifanikiwa kisiasa. Alilipanua eneo la utawala la Yuda na akaikomboa ardhi iliyokuwa imechukuliwa wakati wa utawala wa wafalme dhaifu. “Umaarufu wa jina lake ukaenea mpaka kuingia Misri; kwa kuwa aliongezeka nguvu mno.”[2]
Uzia alikuwa mfalme mwenye nguvu sana, lakini kisa chake kilikuwa na mwisho mbaya. “Lakini alipokuwa na nguvu, moyo wake ulitukuka, hata akafanya maovu, akamwasi Bwana, Mungu wake.”[3]
Ni nini kilicholeta hukumu kwa Uzia? Mfalme aliingia hekaluni kufukiza uvumba kwenye madhabahu. Alikiuka agizo la kutenganisha vitu vya kawaida na vile vitakatifu. Matokeo yake, Uzia alikuwa na “ukoma hata siku ya kufa kwake, na akiwa mkoma akawekwa katika nyumba ya pekee, kwa kuwa ni mwenye ukoma; maana alitengwa na nyumba ya Bwana.”[4]
Mfalme Uzia hakuua, hakuiba, au hakufanya uzinzi. Hakuaudu sanamu au hakwenda kwa waganga. Uzia alitenda dhambi kwa kukiuka sheria ya Mungu ya kutenganisha. Kwa majivuno yake, mfalme Uzia aligusa madhahabu takatifu. “Akawa na majivuno… Hakuwa mwaminifu kwa Bwana Mungu wake.”
Katika majivuno yake, mfalme Uzia alikiuka utakatifu wa hekalu. Sheria ilifundisha watu wa Mungu kwamba wanapaswa kujitenga na dhambi, ili waweze kuishi katika mahusiano sahihi na Mungu. Maisha matakatifu ni Kutengwa kwa ajili ya Mungu.
Vitabu vya historia vya Biblia, vinaelezea mifano ya watu na vitu vilivyokuwa vimetengwa kwa ajili ya Mungu. Kama ambavyo alifanya kwenye kichaka kilichokuwa kinawaka moto, Mungu alitenga sehemu ya ardhi iwe takatifu. “Amiri wa jeshi la Bwana alimwambia Yoshua, ‘Vua viatu vyako miguuni mwako; kwa kuwa mahali hapo usimamapo ni patakatifu.’”[5]
Wakati Israeli walipoishambulia Yeriko, Mungu aliwaamuru waharibu kila kitu kilichokuwa “kimewekwa wakfu kwa Bwana kwa ajili ya uharibifu…. Lakini fedha yote, na dhahabu, na vyombo vya shaba, na chuma, ni vitakatifu kwa Bwana; vitaletwa katika hazina ya Bwana.”[6] Kule Yeriko, vitu vyote hivi havikuwa takatifu; lakini vilikuwa takatifu tu wakati Bwana alipovitaka kwa ajili yake mwenyewe.
Daudi aliwaamuru Walawi, “Jitakaseni, ninyi na ndugu zenu, ili mlipandishe sanduku la Bwana, Mungu wa Israeli, mpaka mahali pale nilipoliwekea tayari.”[7] Kabla ya kulibeba Sanduku la Agano kulirudisha Yerusalemu, Walawi walijitoa wenyewe kwa ajili ya makusudi ya Mungu.
Kujitenga kutokana na dhambi siyo lengo la mwisho kwa watu watakatifu. Israeli ilikuwa imechaguliwa kutoka miongoni mwa mataifa maovu yaliyokuwa yameizunguka ili liweze kutengwa kwa ajili ya Mungu na kuwa milki yake.[8] Wakati wa kuwekwa wakfu kwa hekalu, Sulemani aliomba. “Kwa maana uliwatenga na watu wote wa dunia, wawe urithi wako, kama ulivyonena kwa mdomo wa Musa, mtumishi wako, hapo ulipowatoa baba zetu katika Misri, Ee Bwana MUNGU.”[9] Mungu aliitenga Israeli kutoka mataifa mengine ili iwe mali yake. Israeli ilikuwa na heshima ya kuwa “urithi” wa Mungu.
Akiwaonya Wakorintho kuhusiana kuwa na mahusiano na Mataifa, Paulo alimnukuu Isaya: “‘Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao,’ asema Bwana, ‘Msiguse kitu kilicho kichafu.’”[10] Nikiwa kijana Mkristo, Ninakumbuka kusikia mahubiri kuhusu utakatifu na kutengwa yakimalizia na aya hii. Wahubiri wakiwahusia watu wa Mungu kwa kusema “jitengeni na mambo machafu.”
Ujumbe wa kutengwa mara nyingi ulikuwa hasi (kinyume). Hata hivyo, aya inaendelea na ahadi nzuri sana! Tumetengwa kutoka kwenye dhambi ili kwamba tuweze kutengwa kwa ajili ya Mungu. Paulo anaendelea na ahadi kwamba; “Nitawakaribisha, Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike, asema Bwana Mwenyezi.”
Kutengwa kutokana na chochote kile kichafu hakutunyang’anyi furaha yetu. Badala yake, tumetengwa kutoka dhambini ili tuweze kuwa na furaha ya kutembea na Mungu. Wakristo tunatengwa kutoka katika dhambi ili tuweze kuwa mali ya Mungu kikamilifu. Watu watakatifu kwa furaha hukaa mbali na dhambi kwa sababu wanajua kwamba kutengwa kutoka dhambini kunatoa fursa ya wao kutembea katika mahusiano ya ndani na Baba wa mbinguni.
Kanuni hii inaweza kuonekana katika sheria za chakula na mavazi. Kwa nini Mungu alisema, “Msile aina ya vyakula hivi” au “Msivae aina hizi za mavazi”? Sheria hizi zilikuwa ni mafundisho yaliyokusudiwa kuwafundisha Israeli kwamba ilikuwa ni lazima itengwe kwa ajili ya Mungu. Sheria hizi zilikua ni alama kwamba Israeli kama taifa ni mali ya Mungu. Mungu alisema kwa Israeli, “ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda.”[11] Mawazo gani haya ya kufikirika! Israeli haikutengwa kwa ajili ya Mungu kama adhabu; bali alitengwa kwa ajili ya heshima na upendo. Ilikuwa ni tunu kwake kuliko makabila yote ya watu.[12]
Wazo hili linaonekana katika kielezo cha hema ya kuabudia. Wale ambao kwa mujibu wa kawaida za dini walikuwa siyo wasafi walikaa “nje ya kambi.” Wale ambao kwa mujibu wa kawaida za dini walikuwa safi walikaa “ndani ya Kambi.” Katikati ya eneo la kambi, makuhani walikuwa wakitoa dhabihu “ndani ya hema ya kuabudia.” Kuhani mkuu ndiye peke yake aliyeingia Patakatifu pa Patakatifu. Mpangilio huu uliwapa watu kumbukumbu ya kuona kiuhalisia jinsi kutengwa kutoka katika dhambi kunapotoa fursa ya sisi kutengwa kwa ajili ya Mungu. Hii iliwaonyesha watu ni nini maana ya kuwa karibu na uwepo wa utakatifu wa Mungu.
Kwa jinsi ambavyo watu walikuwa wanafuata sheria za kutengwa, walijifunza kwamba ni lazima kuwa watakatifu katika kila eneo la maisha. Mungu anayo mamlaka juu ya maisha yote.
Mambo ya Walawi 17-26 inaitwa “Kanuni ya Utakatifu.” Kanuni ya Utakatifu iliifundisha Israeli jinsi ya kuishi kama taifa takatifu. Kutoka kwenye kila kitu kidogo hadi kwenye kanuni kubwa, hizi sheria zilipewa nguvu na utakatifu wa Mungu. Ziliwaonesha Israeli ni kwa jinsi gani wanaweza kuwa watakatifu katika ulimwengu wa dhambi. Israeli walifundishwa jinsi ya kutengwa kutoka katika dhambi. Kwa umuhimu zaidi, zilifundisha jinsi Israeli itakavyoweza kutengwa kwa ajili ya Mungu wao, “Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, niliyewatoa katika nchi ya Misri.”[14]
Katika Mambo ya Walawi 20, Mungu alisema, “Nanyi mtakuwa watakatifu kwangu mimi; kwa kuwa mimi Bwana ni mtakatifu nami nimewatenga ninyi na mataifa, ili kwamba mwe wangu.”[15] “Nimewatenganisha ninyi na mataifa.” Kwa nini? “ili muwe wangu.” Hii ilikuwa ni kutengwa kwa ajili ya Mungu.
Neno la Kiebrania lililotafsiri “kutengwa” katika Mambo ya Walawi 20:26 linatumika katika Mwanzo 1:4 wakati Mungu “alipotenganisha” nuru kutoka giza. Huwezi kuchanganya nuru na giza pamoja; vinapingana. Mungu alikusudia kuwepo na kutengwa kabisa kwa Israeli dhidi ya mataifa yote maovu yaliyoizunguka Israeli.
Mungu amewaita watu wake watengwe kabisa kutokana na dhambi. Kwa nini? Ili waweze kuwa mali yake kabisa. Hizi sheria zinaonesha kwamba mifumo ya maisha yote ni mali ya Mungu. Kwa watu watakatifu, mifumo yote ya maisha iko chini ya mamlaka yake. Kuwa mtakatifu inamaanisha kutengwa kwa ajili ya Mungu katika maeneo yote. Tumetengwa katika dhambi ili tuweze kuwa mali ya Mungu.
► Ni lipi linaloonekana kuwa ni ngumu zaidi – kutenganishwa kutoka katika dhambi au kutengwa kwa ajili ya Mungu? Kwa nini?
Utakatifu katika Matendo: “Katika dunia, lakini siyo kwa ajili ya dunia”
Utengwaji wa kibiblia unatoa ushuhuda kwa dunia
Yesu aliomba kwamba wanafunzi wake wawepo ulimwenguni, lakini wasiwe sehemu yake. Danieli alikataa “kujitia unajisi kwa kula chakula cha mfalme, wala kwa divai aliyokunywa.”[1] Katika historia nzima, watu wa Mungu wamekuwa wakijitenga na dhambi katika maeneo yao wanayoishi. Hali hii imeruhusu watu wa Mungu kuwa mashuhuda kwa dunia yao.
Israeli iliitwa kuwa “taifa la makuhani,” taifa takatifu lililoongoza mataifa mengine kwa Mungu.[2] Wakati Israeli ilipokuwa waaminifu kwa Mungu, ilikamilisha umisheni huu. Rahabu alisema, “hofu imetuangukia mbele yenu… mioyo yetu iliyeyuka, wala haukusalia ujasiri wo wote katika mtu awaye yote, kwa sababu yenu.” Kwa nini? Kwa sababu Israeli ilikuwa taifa lenye nguvu na jeshi kubwa? Hapana! Bali ni kwa sababu, “Bwana, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu, katika mbingu juu na katika nchi chini.”[3] Wakati Israeli ilipotengwa kwa ajili ya Mungu, ilifanyika ushuhuda kwa mataifa yote.
Tunaiona kanuni hii kwenye maisha ya Yusufu. Kwa kuwa Yusufu alijitenga mwenyewe na dhambi za Wamisri, alikuwa ni ushuhuda kwa Farao. “Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye roho ya Mungu ndani yake?”[4] Kama Yusufu angekuwa ameishi kama Wamisri, isingewezekana kupatiwa nafasi kubwa kama hiyo ya kuwa shuhuda mbele ya Farao.
Yesu aliomba kwamba wafuasi wake wawe ndani ya ulimwengu, lakini siyo kwa ajili ya ulimwengu. Kifungu hiki mara nyingi kimekuwa hakieleweki kwa Wakristo wanaotaka kuishi maisha ya uangalifu na ya kimungu. Wanafanya makosa kwa kufikiri kwamba kuwepo “katika ulimwengu huu” ni uovu wa lazima ambao watu wa Mungu ni lazima wapitie katika safari ya kuelekea mbinguni.
Hata hivyo, baada ya kufurahia kwamba wafuasi wake “siyo wa ulimwengu huu,” Yesu aliomba “Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni.”[5] Yesu aliomba kwamba wafuasi wake watumike kwa ufanisi mkubwa duniani. Yesu aliomba tusiwe “watu wa dunia” wakati tumetumwa “tuenende duniani.” Kwa kukaa tukiwa tumetengwa na dhambi, tunaweza kutimiza wito wetu wa kuibadilisha dunia. Kama watoto wa Mungu, tunaweza tukawa chumvi na nuru kwa ulimwengu wa dhambi.
Mitume walijua kwamba maisha ya utakatifu ni ushuhuda kwa dunia. Petro aliwataka waamini waishi maisha ya kumcha Mungu kama ushuhuda kwa wasioamini:
"Mwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa."[6]
Paulo aliandika kwa Tito, kiongozi wa kanisa katika kisiwa cha Krete. Waumini hawa walizungukwa na wapagani. Paulo akamwambia Tito kwamba Wakristo “wayapambe mafundisho ya Mwokozi wetu Mungu katika mambo yote.”[7] Wakati Wakristo wakiyaishi maisha ya utakatifu, tabia zao “zitaipamba” Injili. Tabia za watu watakatifu zitaifanya Injili iwe kivutio kwa dunia.
Paulo aliwataka Wakristo wa Filipi kuishi maisha ya kumcha Mungu. Walitakiwa wabakie wakiwa wametengwa katika dhambi. Walitakiwa wawe “wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu.”[8]
Kama watu wa Mungu tunaoishi maisha ya utakatifu, “tunang’ara kama nuru ya dunia.” Maisha ya watoto wa Mungu yanatakiwa yatoe ushuhuda unaong’aa kwa dunia iliyoko gizani. Kutengwa katika dhambi siyo jaribio la kisheria la “kupata wokovu.” Kutengwa katika dhambi kunatuwezesha sisi kutimiza mwito wa Yesu wa kuwa “nuru ya ulimwengu” na “chumvi ya dunia.”[9] Mikono mitakatifu ni ushuhuda wenye nguvu kwa dunia yetu.
Kanuni za Kibiblia za Kutengwa
Kwa watu wengi “kutengwa kutokana na dunia” ni orodha ya “fanya” na “usifanye.” Mara nyingi kutengwa kunafafanuliwa kwa msururu wa sheria nyingi. Watu wengi wanafafanua kutengwa kwa mlolongo wa mavazi wasiyotakiwa kuvaa, maeneo wasiyotaliwa kwenda, na sherehe wasizotakiwa kushiriki.
Ni ukweli usiopingika kwamba watu watakatifu hawataweza kuvaa nguo za aina fulani, au kwenda kila eneo la maisha. Mtu mtakatifu hupenda kumpendezesha Mungu katika kila eneo la maisha yake. Hata hivyo, kutengwa katika dhambi na kutengwa kwa ajili ya Mungu ni zaidi ya msururu wa sheria.
Tatizo moja katika kufafanua kutengwa kwa njia ya msururu wa sheria ni kwamba sheria hizo hubadilika mara kwa mara, mara nyingi kwa maelezo machache sana. Kanisa moja litasimamia kutengwa kwa mfumo wa sheria zake; kanisa lingine nalo litasimamia kwa mfumo wa sheria nyingine. Njia nzuri ya mtazamo ni kufafanua kanuni za kibiblia ambazo ni za kweli kwa nyakati zote na kwa mila zote.
Kama Wakristo, aina ya maisha yetu ni lazima yalenge utii wetu kwa neno la Mungu na uongozi wa Roho Mtakatifu. Kama tutatafuta kuwa watu tuliotengwa kwa ajili ya Mungu kama “watu wa milki yake mwenyewe,”[10] kwa hiari tutayatii mafundisho ya neno lake.
Wakati Biblia haielekezi moja kwa moja mwelekeo wa maisha ya kisasa, inajenga kanuni ambazo zinaweza kutuongoza sisi. Ni kanuni gani zinazoweza kuongoza aina ya maisha ya mtu mtakatifu?
(1) Kanuni ya Staha
Kanuni ya staha inathibitisha kwamba uvaaji na tabia zetu ni lazima zimpe Mungu heshima na lazima kujizuia na yale yote ambayo ni aibu mbele zake. Uvaaji wetu na tabia zetu zinaongozwa na matamanio yetu ya kumpa Mungu utukufu.
Ndani ya Biblia yote, kutembea uchi kulikuwa ni aibu sana. Baada ya kutenda dhambi, Adamu na Hawa waliona aibu kwa sababu “Walifumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi.”[11] Kwa hiyo “wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo.” Wakati Mungu alipokutana nao bustanini, aliwatengenezea “mavazi ya ngozi yaliyokuwa makamilifu zaidi akawavika.”[12]
Kwa mujibu wa muendelezo wa maandiko yote, kukaa uchi ni tendo la aibu.[13] Manabii walitumia kutembea uchi kama ishara ya hukumu ya Mungu.[14] Kama watu wa Mungu, uvaaji wetu ni lazima uonyeshe kwamba tunaheshimu viwango vya Mungu vyenye staha. Tunapaswa tuone aibu kwa uvaaji uchi ambao ulikuwa ni ishara ya aibu kwa manabii wa Mungu. Uvaaji wetu uwe kweli ni uvaaji ambao unawakilisha watu wa Mungu watakatifu na wasafi.
Ustaha katika Biblia ulihusisha tofauti za jinsia. Wakati Biblia haifafanui ni vitu gani maalumu vya mavazi vivaliwe na Waisraeli, Mungu anawaamrisha watu wake wazingatie tofauti za jinsia katika mavazi yao.[15]
Agano Jipya linafundisha kwamba mapambo yetu lazima yaonyeshe kwamba sisi ni wana wa Mungu. Paulo alilinganisha aina mbili za mapambo:
"Wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele,[16] wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani; bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu."[17]
Paulo anakataza mapambo yaliyo juu ya viwango vya kawaida ya kulinganisha mitindo ya nywele, vito vya mapambo, na mavazi. Wakati huo huo, anashauri mapambo “yenye mavazi ya heshima” ambayo ni sahihi kwa wanawake wanaokiri uungu. Haya ndiyo mapambo ya “kazi njema” ambayo Wakristo wanapaswa kutafuta.
Mafundisho ya Paulo yanaonyesha uhusiano uliopo kati ya mapambo ya nje na roho wa ndani. Katika sehemu hii ya barua ya Paulo kwa Timotheo, analenga kuhusu maombi katika kanisa. Anamwambia Timotheo jinsi Wakristo wanavyopaswa kuomba. Anaelekeza kwa kila jinsia.
Paulo anaandika kwamba wanaume wanapaswa waombe “bila ghadhabu au ugomvi.” Hatupaswi kuingia mbele za Mungu na roho ya ghadhabu. Paulo anaandika kwamba wanawake wanapaswa kuomba kwa roho ya staha na unyenyekevu; ikiwa pia ni katika uvaaji na mapambo. Hatupaswi kwenda mbele ya uwepo wa Mungu kwa majivuno na utukufu wa binadamu. Watu watakatifu wanayo staha inayodhirika katika maeneo yote ya maisha.
Petro alitoa uhusiano unaofanana kati ya mwonekano wa nje na roho wa ndani.
"Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi; bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu. Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu, na kuwatii waume zao.…"[18]
Kama Paulo, Petro anatambulisha aina mbili za mapambo. Anakataza mapambo ya nje yanayoonyesha mitindo ya nywele, mapambo ya dhahabu na mavazi. Kisha anaamrisha mapambo ya ndani “roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu.” Watu watakatifu hujali zaidi katika kuwa wa “thamani mbele za Mungu” kuliko kuvutia na kupata uthibitisho wa dunia hii. Hivi ndivyo “wanawake watakatifu wanaomtegemea Mungu walivyojipamba wenyewe.”
Kama Wakristo, burudani yetu lazima ionyeshe kwamba tumetengwa kwa ajili ya Mungu. Paulo anatuambia kwamba Wakristo tunapaswa kujaza fahamu zetu na mambo ambayo yatatufanya tufanane zaidi na Kristo.
"Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo."[19]
Kama watu watakatifu, kila eneo la maisha linadhibitiwa na Mungu. Ukisoma mambo ya Walawi, utaona kwamba hakuna kitu chochote kidogo kinachoweza kuzuia umakini wa sifa njema ya Mungu. Kila kitu ni muhimu kwake! Hii siyo kwa sababu Mungu ni mjeuri anayetaka kutawala kila eneo la maisha. Ni kwa sababu Mungu ni Baba wa upendo anayejali kila kipengele cha maisha ya watoto wake. Baba yetu wa mbinguni hapendezwi watoto wake kuvaa mavazi ambayo yanadhalilisha miili aliyoiumba kwa upendo mkubwa. Baba yetu wa mbinguni hataki watoto wake wajazwe fahamu zao na burudani ambazo zinavutia mawazo ya dhambi na aibu. Sisi ni “watu wa milki yake mwenyewe,” na anajali kila kipengele cha maisha yetu.
► Tumia kanuni ya staha katika mila yako. Ni maeneo gani (ya mavazi na mitindo ya maisha) ambayo ni changamoto katika kudumisha staha kwenye dunia yako?
(2) Kanuni ya Uwakili
Kanuni ya uwakili inathibitisha kwamba kila kitu tulicho nacho ni mali ya Mungu. Kama watoto wa Mungu, tutatumia fedha na mali zetu kwa njia ambayo inamheshimu yeye.
Katika karne ya kumi na nane, baadhi ya Wakristo walifuata kanuni kali ya uvaaji. Walikataa kila aina ya nakshi kwenye mavazi yao. Hawakuvaa vifungo vya kung’ara katika nguo zao; wanaume hawakuvaa tai shingoni; walivaa nguo zilizotengenezwa kwa kitambaa cha kijivu. Inaonekana kwamba walikuwa watu wa kiasi sana.
Hata hivyo, John Wesley alihubiri somo kuhusu mavazi ambapo alilalamika kwamba huo muonekano wa staha ulikuwa wa nje tu. Wakati mavazi yalionekana ni ya kawaida tu, baadhi ya Wakristo walipuuzia kanuni ya uwakili. Walisafiri kutoka Uingereza hadi Paris kwenda kununua vitu vya gharama sana kwa ajili ya uvaaji wao. Ndiyo, walinunua tu nguo za rangi ya kijivu – lakini walinunua nguo za gharama kuonyeshana utajiri wao. Walikuwa watu wa staha, lakini hawakuwa mawakili wazuri wa fedha za Mungu.[20]
Wesley aliweka mkazo kwamba kujitenga na dunia kulimaanisha kuwa wakili mzuri wa fedha Mungu anazotupa. Alihubiri kwamba watu watakatifu hawapaswi kupoteza fedha zao kwa fujo kupita kiasi katika nguo. Inawezekana kuvaa nguo zenye staha lakini tukawa ovyo kwenye chaguo la mavazi. Palo alisema kwamba mapambo yetu hayatakiwi yawe “mavazi ya gharama kubwa.”[21]
Kanuni ya uwakili haimaanishi kwamba kila siku ni kununua vitu rahisi tu. Mara nyingine nguo za thamani zinazogharimu zaidi zinadumu muda mrefu zaidi. Baadhi ya makanisa hutumia $100 kufunga vitu rahisi – na baadaye hutumia mamia ya dola katika kufanya ukarabati wa maeneo yanayoharibika na kuvuja! Huu ni uwakili mbaya.
Kanuni ya uwakili inasema, “Sisi ni mawakili wa fedha ambazo Mungu ametukabidhi. Tunapaswa tuzitumie kwa busara. Sisi ni mawakili wa talanta ambayo Mungu ametupa, tunapaswa tuzitumie kwa utukufu wake. Kila tulifanyalo limpe yeye heshima.”
► Tumia kanuni ya uwakili katika utamaduni wako. Ni kwa jinsi gani makanisa yenu yanaweza kuwa mawakili wazuri kwa rasilimali za Mungu?
(3) Kanuni ya Kuwa na Kiasi
Kanuni ya kuwa na kiasi inathibitisha kwamba hatutaruhusu “vitu” (hata vizuri kiasi gani) vitawale maisha yetu. Mojawapo ya changamoto ya kuishi “humo” lakini siyo “kwa ajili” ya dunia ni kwamba tuko duniani! Kuna vitu vingi sana katika dunia yetu ambavyo tunaweza kuvifurahia. Maisha ya utakatifu yanahitaji kuwa na kiasi hata kama mambo ni mazuri.
Chakula ni mfano. Njaa ni tamaa ya asili, siyo dhambi. Paulo aliandika kwamba tunapaswa kula “kwa utukufu wa Mungu.”[22] Kula siyo dhambi. Hata hivyo, kama mimi ni mlafi ambaye siwezi kujithibiti, sitakuwa ninakula katika utukufu wa Mungu. Dunia inakula kwa kujiridhisha; kama sina kiasi katika tabia zangu za kula, mimi ni “wa dunia.” Badala yake, napaswa kula “kwa ajili ya utukufu wa Mungu.” Hii inamaanisha kwamba nitaimarisha kujithibiti wakati nafurahia chakula alichonipa Mungu.
Wakorintho walisisitiza kwamba, wangeweza kufanya zinaa kwa sababu wao walikuwa watoto wa kiroho wa Mungu haijalishi miili yao iko katika hali gani na inafanya nini. Walisema kwamba, “Vyakula ni kwa tumbo, na tumbo ni kwa vyakula.” Walikuwa na msimamo wa mila yao kwamba mwili unaruhusiwa kupewa chochote unachotaka.
Paulo aliwajibika kujibu kwa kunukuu mafundisho ya Wakorintho na kisha kukanusha kila mapokeo ya uongo kutoka katika mafundisho hayo. “‘Vitu vyote ni halali kwangu,’ lakini mimi sitatiwa chini ya uwezo wa kitu cho chote. ‘Vyakula ni kwa tumbo, na tumbo ni kwa vyakula;’ lakini Mungu atavitowesha vyote viwili, tumbo na vyakula.”[23]Akaendelea, “Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo?” Kisha akahitimisha, “Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu.”
Kanuni ya Paulo hapa ni hii – hata vile vitu ambavyo ni halali havipaswi vitutawale. Mungu anayo mamlaka katika nyanja zote za maisha ya Mkristo, ikiwa ni pamoja na miili yetu. Kila kitu tunachokifanya ni lazima kimletee Mungu heshima. Hii inatutaka tuishi maisha ya kiasi na kujithibiti.
Hii itaonekanaje katika maisha ya kila siku? Inamaaisha kujithibiti katika vile tunavyokula na kunywa. Inamaanisha kujitawala katika burudani zetu. Kama mtu mtakatifu “sitatawaliwa na chochote.” Hata katika burudani ambazo kwazo ni safi na hazina lolote baya kwangu ni mbaya kama zitanitawala. Kanuni ya kuwa na kiasi inafundisha kujithibiti katika maeneo yote.
Nataka nitoe mfano mmoja. Elewa kwamba hii siyo sheria kwako! Ninatumia mfano huu kuonyesha ni jinsi gani kanuni hizi zinaweza kuhusiana na madhaifu binafsi na utu wa mtu.
Nilinunua kompyuta mpya iliyokuwa na mchezo unaoitwa “Tetris.” Hakuna jambo lolote baya kuhusiana na mchezo huu. Siyo ya vurugu au ya kimwili. Ni chemsha bongo rahisi. Baadaye nikajigundua kwamba “nimeshatawaliwa” na ule mchezo. Nitakuwa ninafanya kazi – na kisha nitaanza kucheza mchezo. Kisha ninasema, “Nitachukua mapumziko kazini nikacheze Tetris.” Dakika thelathini baadaye nitasema, “Nataka nimalizie mchezo mmoja zaidi.” Baada ya saa moja, ninajikuta bado naendelea kucheza. Mwishoni, Mungu akanikumbusha kanuni ya kuwa na kiasi. “‘Vitu vyote ni halali kwangu,’ lakini sitatawaliwa na chochote.”
Kwa sababu ya hili, nilijifunza kwamba ni lazima niufute mchezo wa Tetris kutoka kwenye kompyuta yangu. Je, hii ni kanuni ya kibiblia? Hapana! Biblia haijahusisha mchezo wa Tetris mahali popote! Lakini kwangu mimi kanuni ya kuwa na kiasi inamaanisha kuachana na mchezo unaoweza kunitawala mimi.
Kanuni ni pana kuliko sheria. Hakuna fundisho lolote katika Biblia linalohusiana na Tetris. Kama Tetrs ni mchezo pendwa wako, huhitaji kuachana nao kwa sababu yangu. Lakini kwangu mimi, kutokana na udhaifu wangu, Tetris ni mtego kwangu. Kama tunataka kuishi maisha matakatifu, tutamwuliza Mungu, “Niishije katika njia inayokupendeza wewe?”
► Tumia kanuni ya kuwa na kiasi katika utamaduni wako. Ni maeneo gani yana changamoto ya kudumisha uwiano wa kibiblia katika maisha yako?
(4) Kanuni ya Stahili
Wakati Timotheo, mtoto wa Baba wa Kigiriki na mama wa Kiyahudi, alipoungana na Paulo katika safari yao ya umishenari, Paulo alimtaka Timotheo atahiriwe kwa ajili ya huduma yenye ufanisi.[24] Mapema, Paulo alikuwa amekataa kumtahiri Tito, Mgiriki aliyeokoka.[25] Hali hizi mbili za mwitikio tofauti wa Paulo unafundisha kanuni muhimu katika huduma.
Katika suala la Tito, Paulo anasimama kwenye ukweli kwamba tunaokolewa kwa neema katika Imani. Kumtaka mtaifa aliyeokoka afuate sheria za Kiyahudi kungeshusha hadhi ya uhuru wa Mkristo. Paulo alisimama imara dhidi ya wale wote waliotaka Tito atahiriwe.[26] Katika Matendo 15, Kanisa la Yerusalemu lilikuwa linatambua wazi kwamba kutahiriwa kulikuwa hakuhitajiki kwa mataifa wanaookoka.
Katika Matendo 16, Paulo alimtaka Timotheo atahiriwe. Kwa nini? Siyo kwa sababu ya wokovu, bali ni kwa ajili ya ufanisi wa huduma kwenye masinagogi.
► Soma 1 Wakorintho 9:19-23.
Paulo alionyesha tena kanuni hii kwa Wakorintho. Kwa ajili ya Injili, Paulo alikuwa tayari kufanya dhabihu katika maeneo ambayo hayakuhusisha kanuni za kibiblia. Hakuelewana na hukumu za kibiblia, lakini alijitoa dhabihu uhuru wake kwa ajili ya huduma.
Hali hii inapendekeza kanuni muhimu sana kwa Wakristo. Kuna mambo yanayoweza kuonekana ni sahihi katika mazingira fulani, lakini yasionekane ni sahihi kwenye mazingira mengine. Kwa ajili ya ufanisi mzuri wa huduma, kiongozi anaweza kusalimisha sehemu ya “uhuru” wake katika maeneo ambayo hayataathiri maamuzi yake. Maeneo haya siyo yale yenye mafundisho ya Biblia, bali ni yale yenye hukumu za binafsi na mambo ya kitamaduni.
Gary ni mmishenari katika Afrika. Gary amefuga ndevu nyingi sana. Katika nchi yao, kufuga ndevu ni ishara ya umri na mamlaka. Chifu wa kabila siku zote anakuwa na ndevu ndefu. Ndevu za Gary zinampa heshima miongoni mwa watu anaojaribu kuwafikia kwa Injili. Amekubali kubeba ndevu nyingi kwa sababu ya kanuni ya Stahili.
Rick ni mmishenari katika Asia. Katika nchi ya Rick, kufuga ndevu kumefungamana na unyonge na muonekano wa unyonge wa mtu. Mara tu alipokwenda kwenye hii nchi, Rick akahisi kwamba ndevu zake zitakuwa ni kikwazo kwa ufanisi wake. Alinyoa ndevu zake kwa sababu ya kanuni ya stahili.
Kuwa na ndevu ni vibaya au vizuri? Wala! Wanaume wote walijifunza jinsi ya kufuata kanuni ya Stahili. Ni kitu gani kizuri katika mazingira ambayo Mungu ameniwekea?
► Umeshaona maeneo ambayo kanuni ya Stahili inakutaka wewe utoe dhabihu ya uhuru wako ilikuwafikia walio karibu nawe kwa ajili ya Kristo?
(5) Kanuni ya Uwajibikaji: Ninajibu kwa Nani?
Mara nyingi huwa nawauliza wanafunzi wangu chuoni, “Je, mnapendelea sheria au kanuni kwa ajili ya kitabu chenu cha bwenini?” Kwa kawaida watasema, “Tunapendelea Kanuni.”
Kisha nitauliza, “Ni kipi rahisi kutii: sheria inayosema, ‘Taa zote ni lazima zizimwe usiku wa manane,’ au kanuni inayosema, ‘Unajiandaa kwa huduma. Kalale mapema upate mapumziko ya kutosha na uwe tayari kwa kazi ya darasani katika kipindi cha kwanza cha asubuhi.’? Wanafunzi wanatambua haraka kwamba kanuni inahitaji kufikiri zaidi kuliko sheria ya kawaida!
Kanuni zinaweza kuwa ngumu. Mojawapo ya ufunguo ni kutambua kwamba tunamjibu Mungu katika jambo la kutengwa. Huwezi kuwa na sheria inayosema, “_____ gramu za chakula kwa siku ni za kiasi. Zaidi ya hapo ni ulafi.” Hiyo haiwezekani. Badala yake kumbuka kwamba ninawajibika kwa Mungu kwa ajili ya kijitawala.
Mtu mmoja atakuwa ofisini kwa kazi inayohitaji suti nzuri; lakini mtu mwingine atakuwa msimamizi maskini kama atanunua suti ya kuvaa shambani!
Mungu anaweza kutoa mitazamo tofauti kwa watu tofauti kutegemeana na muundo wa huduma zao; maisha ya nyuma; na hata dhambi zinazowakabili. Sisi wote hatufanani; na hatutafanana na mwingine. Kaka na dada zetu wanaweza kuwa na mitazamo tofauti ya aina za maisha. Ili mradi tofauti hizo hazipingani na mafundisho ya Maandiko, tofauti hizi zinaweza kuwa ndio uhuru wa kibiblia.
Kwa sababu hiyo, napaswa kukumbuka mambo mawili:
Sipaswi kuhukumu juu ya moyo wa mtu mwingine. Wanajibu kwa Mungu kwa kutengwa kwao na dunia.[27]
Nitauhukumu moyo wangu mwenyewe kwa uangalifu sana. Ninajibu kwa Mungu kwa kujitenga kwangu na dunia.
[16] Neno “kusuka” mara nyingine huwachanganya wasomaji. Mitindo ya nywele ya kujivunia ya sikuya Paulo ilikuwa ni pamoja na almaria zilizopambwa. Kanuni yake ni “wanawake wanapaswa kujipamba kwa staha na siyo kwa makusudi ya kujionyesha au kujitangaza.”
Katika karne ya kumi na nane, kundi la Wakristo lilikimbilia Ujerumani kukwepa mateso huko Monrovia. Walikaa katika shamba la Count Nikolaus von Zinzendorf,[1] akawa kiongozi wao. Kwa miaka michache walikuwa zaidi ya Wamoraviani 300 wakiishi katika shamba hili eneo la Herrnhut.
Wamoraviani walikuwa wamejitoa kabisa kwa utakatifu wa kweli. Waliishi maisha ya wazi yalioongozwa na kanuni za Maandiko. Walijulikana kwa ustadi wao wa kujifunza Biblia na kwa ajili ya maombi. Mwaka 1727, Wamoraviani walianzisha kutaniko la maombi yaliyoendelea kwa masaa ishirini na nne kwa siku kwa zaidi ya miaka mia moja.
Wamoraviani walichagua kuwa wana wa Mungu kabisa. Kulikuwa na matokeo gani ya uwajibikaji huu wa maisha ya kutengwa? Mungu aliwatumia kwa njia ya nguvu sana.
Wamoraviani walikuwa na ushawishi sana juu ya Wakristo wengine. Mmishenari wa Kimoraviani, Peter Boehler, alikuwa ni muhimu sana katika kuokoka kwa John na Charles Wesley. Wiki chache baada uhakika wa wokovu wa John na Wesley kwenye kanisa la Moraviani, barabara ya Aldersgate, alisafiri hadi Herrnhut kujifunza zaidi kuhusu uzoefu wa kiroho wa waamini waliojitoa kabisa. Kutoka Kwa Wesley hadi William Carey, Wakristo waliojikabidhi kabisa walivutiwa na ufuatiliaji wa utakatifu wa Wamoraviani.
Wamoraviani walibeba ushuhuda mkubwa sana wa Uinjilisti duniani kote. Ndani ya kipindi cha miezi sita ya mikutano ya maombi iliyoanza mwaka 1727, vijana ishirini na sita wa Kimoraviani walishajitolea kwa ajili ya huduma ya kimishenari – wakati ambapo huduma za kimisheni za kigeni zilikua hazijulikani kabisa miongoni mwa makanisa ya Kiprotestanti. Kwenye karne ya kumi na nane, zaidi ya wamishenari 300 walikuwa wametumwa kutoka katika hivi vikundi vidogo vya Wakristo waliokuwa wametengwa. Baadhi ya wamishenari wa Kiprotestanti wa mwanzo kabisa walikuwa wametumwa na Wamoraviani. Wakristo waliotengwa kwa ajili ya Mungu wanaweza kutumiwa na Mungu kuibadilisha dunia.
(1) Kuwa mtakatifu inamaanisha kutengwa au kuwa wa Mungu. Mifano mingine:
Siku takatifu
Vitu vitakatifu
Maeneo matakatifu
Kabila takatifu
(2) Kuwa mtakatifu maana yake ni kutengwa katika dhambi. Kwa kuwa Mungu anachukia dhambi, Watu wa Mungu huchukia dhambi.
(3) Kuwa mtakatifu maana yake ni kutengwa kwa ajili ya Mungu. Kusudi la kutengwa na dhambi ni ili kutengwa kwa ajili ya Mungu.
(4) Watu wa Mungu hukaa mbali na dhambi. Kuishi karibu na Mungu inamaanisha tunaishi mbali na dhambi.
(5) Maisha matakatifu yaliifanya Israeli iwe shuhuda kwa dunia yote. Maisha matakatifu yanawafanya Wakristo waweze kuushuhudia ulimwengu.
(6) Kutengwa Kibiblia kunaanzia moyoni.
(7) Kanuni za kutengwa na dunia ni pamoja na:
Kanuni ya Staha
Kanuni ya Uwakili
Kanuni ya Kuwa na Kiasi
Kanuni ya Stahili
Kanuni ya Uwajibikaji
Kazi ya Kufanya
(1) Chagua suala moja ambalo kutengwa ni tatizo la Wakristo katika jamii yako. Kutumia kanuni zilizopo katika sura hii, andika insha ya kurasa 1-2 ukipendekeza ni jinsi gani Wakristo wanaweza kutengwa na dhambi na kutengwa kwa ajili ya Mungu katika suala ulilochagua.
(2) Anza kikao kinachofuata cha darasa kwa kunukuu 2 Wakorintho 6:16-18.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.