Yohana: Mtu Aliyeshuhudia Ukamilikaji wa Ahadi ya Mungu.
Tusafiri kuelekea katika kisiwa cha Patmo kwenye bahari ya Aigea. Siyo kisiwa kizuri sana katika bahari ya Karibeani au kisiwa cha Pasifiki ya Kusini. Ni kisiwa na gereza la wafungwa. Patmo ni kisiwa kitupu na cha upweke. Hapo utamkuta Yohana, Mwanafunzi aliyependwa sana, akiishi uhamishoni/kifungoni.
Yohana sasa ni mzee. Amemtumikia Mungu kwa uaminifu na amekuwa mfano wa kuigwa wa maisha ya utakatifu. Amehudumu katika kanisa la Efeso, akimhudumia mama mjane wa Yesu, na akihubiri katika Asia ndogo yote.
Akiwa katika umri ambao angekuwa anapaswa kufurahia heshima ya kuwa mwanafunzi wa mwisho wa Yesu aliye hai, Yohana alikuwa amefukuzwa kwenye nchi yake na kupelekwa katika kisiwa cha Patmo. Yuko mwenyewe mpweke na anaweza kuwa anawaza kwamba yeye hana manufaa tena kwenye kazi ya Mungu. Lakini Jumapili moja asubuhi karibia miaka sitini baada ya Yesu kupaa mbinguni, Yohana alikuwa “katika Roho, siku ya Bwana,” akasikia sauti kuu nyuma yake, kama sauti ya baragumu.
Wakati Yohana alipogeuka nyuma ilikotokea sauti, alimwona Kristo aliyekuwa amemtolea maisha yake. Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu; na macho yake kama mwali wa moto; na miguu yake ilimeremeta kama shaba iliyosuguliwa sana, na sauti yake kama sauti ya maji mengi, na sauti yake kama sauti ya maji mengi, na uso wake kama jua liking'aa kwa nguvu zake. Yohana aliuona “utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”[1]
Katika kitabu cha Ufunuo, tunatembea na Yohana hadi Mbinguni ili tukaone kutimizwa kwa mpango wa Mungu. Watu watakatifu, wataishi kwenye umilele katika ushirika usiovunjika na Mungu aliye mtakatifu.
Kwenye somo la ufunguzi la kozi hii, nilikutaka ufikirie kuhusu bustani ya Edeni wakati wa uumbaji. Ilikuwa ni dunia iliyokuwa imekamilika. Maua, miti, na matunda vilikuwa kila mahali. Ilikuwa ni dunia ambayo haikuwa na dhambi. Ilikuwa ni dunia bila maumivu, machozi, au kifo. Jambo la muhimu zaidi, ilikuwa ni dunia iliyokuwa kwenye mahusiano kamili kati ya Mungu na mwanadanu. Hakuna kilichoweza kumtenganisha mwanadamu na muumba wake.
Kwa masikitiko makubwa, dhambi iliiharibu dunia iliyokuwa kamilifu. Magugu yaliota katikati ya maua. Wanyama waliokuwa hawana matatizo wakafanyika kuwa viumbe hatari. Mwanadamu akaishi kwa mateso, maumivu, na kifo. Kubwa na muhimu kuliko hilo, mahusiano kati ya Mungu na mwanadamu yaliharibika. Kwa sababu ya dhambi. Mwanadamu alifukuzwa kutoka katika bustani ya Eden na akazuiliwa katika kuufikia tena Mti wa Uzima. Ilionekana kwamba Shetani amelishinda kusudi la Mungu alilokuwa nalo kwa ajili ya watu wake.
Ulimwengu kamili ulioahidiwa
Lakini hii haikuwa mwisho wa mambo yote. Katika Maandiko yote, Mungu anaonyesha mpango wake wa kuwafanya watu wake wafanane na yeye; anakusudia kuwafanya watu wake wawe watakatifu. Manabii wa Agano la Kale walitabiri kwamba siku moja Mungu atawafanya watu wake wawe watakatifu na kuwarudisha katika eneo la utakatifu. Akirudia mara kwa mara, Yohana mwona Mafunuo anaonyesha kutimizwa kwa ahadi hizo.
Ezekieli aliiona siku ambayo Mungu atakaa katikati ya watu wake watakatifu:
"Tena maskani yangu itakuwa pamoja nao, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Na mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, mimi niwatakasaye Israeli, patakatifu pangu patakapokuwa katikati yao milele."[1]
Mungu ataitakasa Israeli; atawafanya watu wake kuwa watakatifu. Ataishi katikati ya watu wake. Utabiri wa Ezekieli 37:27 unatimizwa katika Ufunuo 21:3:
"Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu. Naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake, naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao kama Mungu wao."
Kusudi kuu la Mungu litakuwa limetimia wakati atakapokaa katikati ya watu wake watakatifu. Kama Ezekieli, Zakaria naye aliiona siku ambayo kusudi la Mungu kwa watu wake litatimia. Mungu aliahidi, “Nitakaa kati yako.”[2]
Kitabu cha Zakaria 3 kinaonyesha mpango wa Mungu kwa ajili ya watu wake. Katika maono ya Zakaria, Kuhani mkuu alikuwa amevaa nguo chafu sana ikiwakilisha uchafu wa Israeli. Siku moja Mungu atawatakasa watu wake; mavazi machafu ya Israeli na kubadilishiwa hariri mpya.
"Na malaika akasema na wale waliokuwa wamesimama mbele yake, 'Mvueni nguo hizi zenye uchafu.' Kisha akamwambia yeye, 'Tazama, nimekuondolea uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya thamani nyingi.'"[3]
Aya za mwisho katika kitabu cha Zakaria kina picha ya mitazamo mingi ya utukufu katika Agano la Kale.
"Siku hiyo katika njuga za farasi yataandikwa maneno haya, 'WATAKATIFU KWA Bwana.' Navyo vyombo vilivyomo ndani ya nyumba ya Bwana vitakuwa kama mabakuli yaliyoko mbele ya madhabahu. Naam, kila chombo katika Yerusalemu, na katika Yuda, kitakuwa kitakatifu kwa Bwana wa majeshi, nao wote watoao dhabihu watakuja kuvitwaa vile vyombo, na kutokosa nyama ndani yake…."[4]
Katika njuga za farasi yataandikwa maneno kutoka katika kilemba cha ya Kuhani mkuu.[5] Sufuria za kawaida zitakuwa takatifu kama zilivyo “bakuli takatifu mbele ya madhabahu.” Yerusalemu utakuwa kama Mungu alivyoukusudia uwe; jiji lote litakuwa mahali pa Bwana pa kukaa.
Mungu atatimiza kusudi lake; atakuwa na watu watakatifu watakaoishi katika jiji hilo. Maono ya Zakaria yanatimilika katika Ufunuo 21 na 22. Watu wa Mungu wataishi kwenye uwepo wake. “Naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake.”[6]
Ulimwengu kamili Uliorejeshwa
Biblia inaanza kwa kuelezea juu ya ulimwengu kamili uliopotea kwa sababu ya anguko la dhambi. Inamalizia kwa kuelezea juu ya ulimwengu ambao unawangojea wale waliomruhusu Mungu atimize mpango wake katika maisha yao. Mji Mtakatifu unaandaliwa kwa ajili ya watu wa Mungu watakatifu.
Kama ilivyokuwa kwa Bustani ya Edeni, Mji Mtakatifu ni ulimwengu uliokamilika kwa maua, miti, matunda mazuri ya kula kila mahali. Kila kitu ni kizuri:
"Kisha malaika akanionyesha mto wa maji ya uzima, wenye kung'aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwana-Kondoo, katikati ya njia kuu yake. Na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwapo mti wa uzima, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa."[7]
Kwa sababu ya dhambi, mwanadamu alifukuzwa kutoka katika bustani ya Eden na Mti wa uzima. Katika kitabu cha Ufunuo ule mti wa uzima kwa mara nyingine tena unapatika kwa mwanadamu.
Huu utakuwa ni ulimwengu usiokuwa na dhambi. Wasomaji wengi hufadhaishwa na sura za katikati za kitabu cha Ufunuo. Sura hizi huelezea juu ya hukumu zitakazoiangukia dunia. Wasomaji wengi huwa wanapenda kukimbilia kwenye sura za mwisho za kitabu cha Ufunuo zinazozungumzia uzuri wa mbinguni. Hata hivyo, hatuwezi kupuuzia kilichoko katikati ya kitabu hiki. Ili watu watakatifu waweze kuishi katika ushirika usiovunjika na Mungu mtakatifu, nguvu ya dhambi ni lazima ivunjwe.
Kitabu cha Ufunuo kinaonyesha chuki ya Shetani dhidi ya wana wa Mungu. Yohana aliona “mnyama akitoka katika bahari, mwenye pembe kumi, na vichwa saba.”[8] Huyo mnyama “akapewa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda.”[9] Kwa muda, inaonekana kwamba uovu unawashinda watakatifu wa Mungu. Hata hivyo, huyo mnyama kwa vyovyoye vile ni lazima atashindwa.[10] Watu wa Mungu hawana budi kushinda. Kusudi la Mungu litakuwa limekamilika.
Popote katika historia, watu wa Mungu wanaamini kwamba Mungu mtakatifu atafanya kilicho sahihi. Utakatifu wa Mungu ulimpa uhakika mtunga zaburi wakati alipolia kwa ajili ya haki. “Maana huwi Mungu apendezwaye na ubaya; Mtu mwovu hatakaa kwako.”[11] Katika kitabu cha Ufunuo, Yohana alisikia kilio cha wafia Imani, “Ee Mola, Mtakatifu, Mwenye kweli, hata lini kutokuhukumu, wala kuipatia haki damu yetu kwa hao wakaao juu ya nchi?”[12]
Utakatifu wa Mungu unawahakikishia watu wa Mungu kwamba haki itashinda. Yohana aliwaandikia Wakristo waliokuwa wanagandamizwa na utawala wa Kirumi. Aliwaahidi kwamba, mhukumu wa dunia “aliye mtakatifu na mwenye haki” siku moja anakuja kuleta haki kwa watu wake. Kitabu cha Ufunuo kinawataka watu wa Mungu kutulia wakiwa waaminifu, wakijua kwamba Mungu mtakatifu atalipiza kisasi kwa ajili ya watu wake. Kitabu cha Ufunuo kinaangalia muda ambao Shetani atashindwa, na watu wa Mungu wataishi kwa amani.
Mbinguni ni mji mtakatifu. Ni mji mtakatifu usiokuwa na dhambi au na madhila ya dhambi. Ni mji usiokuwa na maombolezo, wala machozi, wala maumivu, na hakuna mauti. Mungu, “atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”[13]
Lakini bado kuna kitu kingine cha ajabu zaidi. Sehemu kubwa ya Bustani ya Edeni ilikuwa ni sehemu kamilifu ya ushirika kati ya Mungu na mwanadamu. Adamu na Hawa walitembea katika bustani hii na Mungu. Walitembea pamoja naye uso kwa uso. Hakuna kilichoweza kumtenganisha Mungu na mwanadamu. Mbinguni, tutaishi katika ushirika mtakatifu na Mungu. Hakuna cha kuweza kutenganisha watu watakatifu kutoka kwa Mungu mtakatifu.
"Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, 'Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.'"[14]
Yohana anailezea mbingu kuwa ni sehemu isiyokuwa na maombolezo, wala maumivu, wala mauti. Vitu vyote vilivyoleta maombolezo katika ulimwengu wa zamani (utajiri usiojulikana kwenye bahari, hatari za usiku, tishio la magonjwa), vyote vitatoweshwa. Amani hii ya mwisho itategemea sana uwepo wa Mungu mwenyewe.
"Wala hapatakuwa na laana yo yote tena. Na kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo ndani yake. Na watumwa wake watamtumikia; nao watamwona uso wake, na jina lake litakuwa katika vipaji vya nyuso zao. Wala hapatakuwa na usiku tena; wala hawana haja ya taa wala ya nuru ya jua kwa kuwa Bwana Mungu huwatia nuru, nao watatawala hata milele na milele."[15]
Watu watakatifu wamekuwa mara zote wakitamani kumwona Mungu. Musa aliomba amwone Mungu, lakini hakuweza kuuona uso wake.[16] Daudi aliomba, “Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu?”[17] Yesu aliahidi kwamba, heri wenye moyo safi; maana hao “watamwona Mungu.”[18] Ahadi hii inatimilika katika kitabu cha Ufunuo. “Nao watamwona uso wake, na jina lake litakuwa katika vipaji vya nyuso zao.”[19]
Dallas Willard alisimulia kuhusu mtoto mdogo aliyefiwa na mama yake. Usiku mmoja, akiwa mwenye mashaka na peke yake, kijana aliomba alale kwenye chumba cha baba yake. Kwenye usiku wa manane, kijana aliamka na kumwuliza baba yake, “Je, umeugeuzia uso wako kwangu?” Baba akamjibu, “Ndiyo, uso wangu umekugeukia wewe.” Hii ilitosha, kijana akalala kwa amani. Mbinguni, watu watakatifu watauona uso wa Mungu. Uso wake utakuwa umegeuziwa kwetu milele; tutakuwa na amani.
Mpango wa Mungu utakuwa umetimilizwa! Bustani ya Edeni itarejeshwa tena. Watu walio na mioyo na mikono mitakatifu wataishi milele na Mungu mtakatifu. Huu ni mpango wa Mungu kwa watu wake.
[20]Sala kwa ajili ya Utakatifu “Ee Bwana, tulete tena kwenye uamsho wa mwisho katika nyumba na lango la mbinguni, kuinga katika lango hilo na kuishi katika nyumba hiyo, Mahali ambapo hakutakuwepo na giza, Bali mwanga mmoja tu; Hakuna kelele bali muziki mmoja tu; Hakuna mwisho wala mwanzo, bali umilele mmoja tu; Kwenye makao ya utukufu na utawala wako, ulimwengu usiokuwa na mwisho.”
- Imenukuliwa kutoka kwa John Donne
Utakatifu ni ushirika pamoja na Mungu usiovunjika
Yohana aliona maono kuhusiana na mpango wa Mungu kwa ajili ya watu wake. Ni maono ya watu watakatifu wanaoishi katika mji mtakatifu. Mara tatu katika kitabu cha Ufunuo Yohana anaelezea maskani yetu ya milele ya kuishi kama “mji mtakatifu.” [1] Hapa ndipo nyumbani pa Mungu Mtakatifu, malaika watakatifu, na watu watakatifu. Mji huu mzuri sana ni mahali pa utakatifu mkamilifu. Ni watu watakatifu tu watakaoishi pale.
Katika Ufunuo sura ya 21 inatoa picha nzuri sana ya kulivyo mbinguni, lakini pia inatoa tahadhari ifuatayo:
"Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili."[2]
Mbinguni ni mji mtakatifu. Mungu hawezi kuruhusu dhambi iharibu usafi wa mji huo. Wahubiri wa zamani walisema, “Mbinguni ni mahali patakatifu palipoandaliwa kwa ajli ya watu watakatifu.” Ni watu watakatifu peke yake watakaoweza kufurahia kuishi katika huu mji mtakatifu.
Mtu binafsi hataweza kupata furaha ya huu mji ambao ndipo penye kivutio cha Mwana Kondoo wa Mungu. Mtu anayeishi maisha ya kufurahia dhambi hataweza kufurahia kukaa katika mji ambao kila kitu ni kisafi. Mtu ambaye hampendi Mungu atachoka sana kukaa katika mji ambapo kusifu na kumwabudu Mungu ni kwa milele. Mji mtakatatifu umeandaliwa mahususi kwa watu watakatifu tu. Kwa kuwa watu wa Mungu ni watakatifu na wasafi, wataishi na yeye milelle katika mji huo.
Ahadi iliyoko katika kitabu cha Ezekieli 40-48 inatimilizwa katika Yerusalemu Mpya. Hata hivyo, msomaji mara moja anaona tofauti iliyoko kati ya Maono ya Ezekieli na utimilifu wake katika kitabu cha Ufunuo. Kwenye maono ya Ezekieli, hekalu limekaa katikati ya mji. Katika mji mpya hakuna “hekalu ndani yake; kwa maana Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo, ndio hekalu lake.” [3] Mungu mwenyewe ndiye hekalu! Mji wote sasa ni “ardhi takatifu” iliyotengwa kwa ajili ya Mungu na watu wake.
Ushirika usiovunjika ambao Mungu na mwanadamu walishirikiana katika bustani unarejeshwa. Aibu na maombolezo yaliyosababishwa na watenda dhambi Adamu na Hawa hata kujificha mbele za Mungu yameondoshwa. Tutauangalia uso wa Mungu. Watu watakatifu wataufurahia ushirika usiovunjika pamoja na Mungu mtakatifu.
Katika Agano la Kale, Mungu aliitenga Israeli kama, “ufalme wa makuhani, na taifa takatifu.”[4] Katika kitabu cha Ufunuo, kanisa ni, “ufalme na makuhani kwa Mungu wetu.”[5] Tofauti na taifa la Israeli, ufalme huu ni, “mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha.”[6] Ahadi katika kitabu cha Mwanzo 12:3 inatimilika katika kitabu cha Ufunuo 7:9.
Kama Israeli ingeweza kutimiza ahadi yake ya kuwa ufalme wa makuhani, na taifa takatifu tu kwa kuwa watakatifu, kadhalika Kanisa linaweza kutimiza ahadi yake kama tu litakuwa takatifu. Watu wa Mungu ni lazima wawe watakatifu. Katika Agano la Kale, Walawi walivaa mavazi meupe kama ishara ya usafi. Kwa jinsi hiyo hiyo, Yohana anaonyesha kwamba watakatifu wanatakiwa wawe wasafi.[7] Ni wale tu “wazifuao nguo zao” watakaoingia katika mji huo.[8] Watu watakatifu wataishi kwa Amani pamoja na Mungu mtakatifu.
Utakatifu katika Mazoezi: Wakati ninapojihisi siyo Mtakatifu
Je, hili ni jambo la kawaida? Unasikia ujumbe unaokupa changamoto ya kuongeza zaidi utakatifu. Unaomba na kujikabidhi mwenyewe kwenye maisha ya utakatifu. Kwa wiki nane zinazofuata, unakuwa katika kiwango chako cha maisha ya kiroho. Unaliona tunda la Roho mtakatifu likiongezeka katika maisha yako ya kiroho. Unajikuta uko kwenye upendo wa ndani na Mungu na jirani yako.
Ghafla, unagonga ukuta. Bado unatembea na Mungu; ukijiagalia unajikuta huna dhambi za kujitakia katika maisha yako; unampenda Mungu na jirani yako. Lakini kutokana na madhaifu ya kimwili, mihemuko ya hisia, au hata shinikizo za huduma, unajigundua kwamba, “Sijisikii kama ninakua katika utakatifu. Kuna tatizo gani?”
Ni kwa jnsi gani utaendelea na maisha ya utakatifu wakati hujisikii kuwa mtakatifu? Je, unakata tamaa na kusema, “Utakatifu kamwe hauwezekani”? Je, huwa unarudi madhabahuni? Ni kwa jinsi gani utaendelea kutembea katika utakatifu?
► Je, umeshakutana na changamoto kama hii? Je, uliishughulikiaje?
“Wakati ninapojihisi siyo mtakatifu, ni lazima nitembee kwa Imani.”
Katika somo la 2, tumeona kwamba utakatifu ni “kutembea pamoja na Mungu.” Ibrahimu alitembea pamoja na Mungu kwenda katika nchi ambayo hakuwahi kuiona. Alitembea pamoja na Mungu kwa utii na Imani. Miaka elfu nne baadaye, bado tunasisimka tunaposoma kuhusu Imani ya Ibrahimu. Lakini hebu vaa kiatu chake – tembea siku hadi siku hadi siku katika ardhi ya mawemawe. Hauoni mwisho, na hata hujui unakokwenda. Je, unadhani kwamba Ibrahimu aliamka kila asubuhi akijihisi kusisimka kwa ajili ya hiyo siku? Sidhani kama ndivyo. Naamini kuna siku ambazo alikuwa akisema, “Sijisikii kutembea leo.” Lakini ibrahimu aliendelea kutembea pamoja na Mungu.
Tunasoma kwamba Nuhu “alitembea pamoja na Mungu” katikati ya dunia iliyojaa dhambi. Alikuwa amezungukwa na wapagani waabudu vinyago, na watu ambao kila mara walishauriana njia mpya za kutenda maovu,[1] Nuhu alitembea pamoja na Mungu. Je, unadhani kwamba aliamka kila asubuhi akijihisi kusisimka kwa ajili ya hiyo siku? Ninahisi kwamba mara nyingine alijisikia kuchoka sana na kukatishwa tamaa. Lakini, Nuhu aliendelea kutembea pamoja na Mungu.
Msingi mmoja wa maisha ya utakatifu ni kukumbuka kwamba tulikombolewa kwa neema kwa njia ya Imani; tulitakaswa kwa neema kupitia Imani, na tunaendelea kukua katika utakatifu kwa neema kupitia Imani. Baadhi ya watu wanaelewa kwamba wameokolewa kwa neema kupitia Imani. Hata wamejifunza kwamba wametakaswa kwa neema kupitia Imani. Lakini, baadaye wanaangukia kwenye mtego wa kuamini kwamba kuendelea kwao kukua kunategemea juhudi zao binafsi.
Je, kunayo nidhamu inayohitajika katika maisha ya utakatifu? Kwa hakika ipo! Je, tunahitajika kuendelea “kuvifisha viungo vyetu vilivyo katika nchi”?[2] Ndiyo. Je, ni lazima “kuyachuchumilia yaliyo mbele” na “kukaza mwendo, kuifikilia mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu”? [3] Hakika!
Lakini kamwe usisahau kwamba “kuvifisha viungo vyetu vilivyo katika nchi” “kuyachuchumilia yaliyo mbele” na “kukaza mwendo, kuifikilia mede ya thawabu” hufanyika kwa nguvu za “Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.”[4] Huyo ndiye peke yake aliyetufanya tutake sana (mapenzi yake); ndiye anayetoa nguvu (za kazi). Anafanya kazi ndani yetu ili kukamilisha kusudi lake la kutufanya sisi watakatifu. Unapojihisi hauko na utakatifu, unapumzika ndani ya neema ya Mungu ambaye kila siku anatubadilisha tuwe katika mfano wake.
“Wakati ninapojihisi siyo mtakatifu, ni lazima nipumzike kwenye utakatifu wake.”
Katika somo la 5, tuliona kwamba ukamilifu siyo kuhusu utendaji usiofaa bali ni kuhusu moyo usiogawanyika katika dhamira yetu kwa Mungu. Katika somo la 7, tulijifunza kwamba agizo la Yesu la “Kuwa mkamilifu” ni agizo kwa upendo usiogawanyika kwa Mungu. Ukristo ulio mkamilifu siyo kuhusu utendaji; bali ni kuhusu upendo.
Sisi ni watakatifu kwa sababu Mungu ni mtakatifu. Utambulisho wetu uko “ndani ya Kristo.” Yeye ndiye anayetufanya tuwe watakatifu. Moja ya kweli za msingi za Injili ni kwamba kwa sasa hatujitaabishi tena kuupata utakatifu kwa juhudi zetu wenyewe. Tuna uhakika katika Kristo. Utambulisho wetu kama Wakristo, utambulisho wetu kama watakatifu, na utambulisho wetu kama watu watakatifu uko ndani yake.
Robert Coleman wakati mmoja alielezea kuhusu ni nini maana ya kumpenda Mungu kwa ukamilifu wakati ambapo hatuwezi kufanya kwa ukamilifu. Dr. Coleman alikuwa anafanya kazi kwenye bustani yake siku moja ya majira ya joto. Kijana wake mdogo alipomwona anatoa jasho kwenye jua, aliamua amletee maji. Alichukua kikombe kilichokuwa kichafu, akakijaza maji kutoka katika birika lililokuwa limejengwa uwani mwa nyumba, akamletea baba yake. Dr. Coleman akasema, ”Kikombe kilikuwa kichafu na maji yalikuwa ya matope. Lakini kinywaji kilikuwa kimekamilika kwa sababu kilikuwa kimetoka katika moyo ulio na upendo.” Hiyo ni taswira ya ukamilifu wetu mdogo. Tunaleta kwa Mungu huduma zetu sizizokamilika na dhaifu, lakini anazikubali kwa sababu zinatoka katika moyo wa upendo.
Mungu huwa anakubali juhudi zetu dhaifu na huzibadilisha ziwe kitu kingine juu ya upeo wetu wa kufikiri – kwa sababu utakatifu wetu ni kitu kidogo tu kutokana na utakatifu wake mwingi usiokuwa na kipimo. Hata upendo wetu mzuri sana unaathiriwa na mapungufu ya kibinadamu. Lakini tunapotulia katika utakatifu wake, tunatambua kwamba kuwa na utii katika maagizo yake ya “Kuwa mtakatifu” kunakamilishwa tu kupitia yeye mwenyewe. Tukiwa na upendo usiogawanyika, tunampelekea glasi yetu ya maji ya matope – na anayabadilisha kuwa kitu kingine kisafi na kinachong’aa. Utakatifu wetu unakamilishwa katika utakatifu wake.
“Ninapojihisi siyo mtakatifu, napaswa nikumbuke kwamba mimi ni sehemu ya watu watakatifu.”
Dhamira kuu kabisa ambayo mara nyingi huwa haizingatiwi katika kitabu cha Ufunuo ni Kanisa. Kitabu cha Ufunuo kinaanza na mfululizo wa meseji za ujumbe kwa makanisa saba. Meseji hizi zinaonyesha umuhimu wa jamii katika kanisa la mahali pamoja ndani ya muundo mkubwa wa mwili wa Kristo. Lakini huu siyo mwisho wa msisitizo wa kitabu cha Ufunuo kwa Kanisa.
Jamii ya watu 144,000 iiyokombolewa inaweza kuwa ni uwakilishi wa Kanisa zima, ambalo ni mwili wa Kristo.[5] Baadaye katika kitabu hicho, kanisa linaonekana kama ni bibi harusi wa Mwanakondoo.[6] Kanisa ni kipengele muhimu sana cha kuzingatia katika kitabu cha Ufunuo.
Kama hivi ndivyo kweli, kuabudu kwetu na ushirika kama kanisa hapa duniani ni maandalizi ya kuabudu na kuwa katika ushirika kama kanisa la mbinguni. Hii inamaanisha nini katika maisha yetu kama Kanisa la leo?
► Kama kitabu cha Ufunuo, ni picha ya bibi harusi wa Kristo, ni kwa jinsi gani kuonyeshwa kwa kanisa kutaathiri maisha ndani ya kanisa? Au niulize kwa njia nyingine – Ni kwa njia gani kanisa lako linafanania na kanisa lililoko katika kitabu cha Ufunuo? Ni kwa njia gani kanisa lako halifananii na kanisa lililoko katika kitabu cha Ufunuo?
Tukio moja la kivitendo la ukweli huu ni kwamba maisha yetu matakatifu yanashabihiana kwa ushirika na kanisa. Katika ulimwengu wa sasa wa mambo ya kibinafsi, Wakristo wengi wanafikiri juu ya wokovu tu katika misingi ya ubinafsi, na uzoefu wa binafsi.
Hata hivyo, wakati kuna mifano ya watu binafsi kama Henoko wakitembea pamoja na Mungu peke yake, kuna mifano mingi ya watoto wa Mungu waliotembea na Mungu kama sehemu ya mwili wao. Sheria za usafi katika Israeli zilikuwa ni kwa ajili ya “watu wa Mungu.” Israeli ilikuwa ni zaidi ya kundi la watu binafsi; ilikuwa ni mwili ulioungana pamoja ukiakisi sura ya Mungu.
Kanisa la Agano Jipya lilikuwa ni zaidi ya kundi la watu binafsi waliotokea kuhusika katika kilabu “moja.” Kanisa lilikuwa – na ni - mwili wa Kristo. Watakatifu wa kitabu cha Ufunuo walikumbana na kuifia dini kama sehemu ya mwili wa Kristo. Hata ilipobidi kufa kama mtu binafsi, waljijua kwamba wao ni sehemu ya Kanisa la ulimwenguni kote. Watakatifu wa kitabu cha Ufunuo waliyaishi maisha matakatifu kamasehemu ya mwili wa Kristo. Ni sehemu ya bibi harusi aliye msafi. Hata wakati Yohana alipofungwa katika kisiwa cha Patmo, alijua wazi kwamba yeye ni sehemu ya kanisa la ulimwenguni kote.
Imekuwa ni jambo la kawaida kusikia watu wakisema, “Nampenda Yesu, lakin silipendi kanisa.” Hii inategemea kutokuelewana kwa kiwango cha kutisha cha kanisa! Kama Kanisa ni bibi harusi wa Kristo, ni lazima nilipende Kanisa. (Kama mume wa mtu, sitapendezwa sana na mtu anayeniambia kwamba, “Nakupenda wewe – lakini simtaki mke wako.”) Kanisa ni mkusanyiko wa waamini wanaokua pamoja katika mfano wa Mungu.
Hatujaumbwa ili tuishi peke yetu. John Wesley alisema, “Utakatifu wote ni utakatifu wa Jamii.” Alimaanisha kwamba tunakua kama sehemu ya mwili. Huo ulikuwa ni msukumo kwa makundi ya Wamethodisti; walisaidia katika kuweka msukumo wa ukuaji wa kila mwanachama wao.
Hii inamaanisha nini kwetu leo? Watu watakatifu ni sehemu ya kanisa takatifu. Tunaukulia utakatifu kama sehemu ya mwili ulio mtakatifu. Wakati ninapokuwa katika kujitahidi sana, Mungu humleta kwangu mwenzangu ambaye naye anapambana kuupata utakatifu ili anitie moyo katika yale maeneo ambayo mimi ni mdhaifu. Kwa upande mwingine, wakati Mungu amenipa msaada katika eneo fulani, mimi nami naweza kumtia moyo ndugu ambaye bado ni mdhaifu. Maisha ya utakatifu yanakusudiwa yawe kwenye jamii ya waamini waliojazwa Roho Mtakatifu wanaoufanya upendo wa Mungu udhihirike katika dunia yetu.
Mwandishi wa kitabu cha Waebrania alilielewa jambo hili vyema:
"Tukaangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na kazi nzuri; wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia."[7]
Kuwatia moyo Wakristo wanaoteswa ili waweze kuendelea kudumu katika Imani anasema, “Tukaangaliane sisi kwa sisi” wakati wa kukutanika pamoja na kutiana moyo mmoja kwa mwingine. Toleo la Biblia ya King James linatumia maneno haya, “Kuchochea mtu mwingine kupenda na kufanya kazi njema.” Sehemu kuu ya utendaji ya Kanisa ni kumtia moyo kila mshirika kuzama zaidi kwenye upendo na utakatifu.
Wakati unapojihisi “hauko kwenye utakatifu” mruhusu Mungu akutie moyo wa kuendelea kukua kupitia Mkristo mwenzako katika mwili wa Kristo pale ambapo amekuweka ukae. Wewe ni sehemu ya “Kanisa la ulimwenguni kote” lakini pia ni sehemu ya jumuiya ya kanisa la mahali pamoja pale ulipo. Mungu amekuweka pale kwa makusudi maalumu. Ruhusu waumini wenzako wachochee ukuaji wako katika maisha ya utakatifu.
[5] Ufunuo 7:4-8; 14:1-5. Watafsiri wanatofautiana kwenye utambulisho wa watu 144,000. Wengine wanaiona namba hii kama namba ya kawaida ya hesabu ya Wayahudi kabla au baada ya dhiki kuu. Wengine wanaiangalia hii kama alama ya Kanisa. Pamoja na hayo, kwa sasa ni mwili wa Kristo unaojumuisha watu, “Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu” (Ufunuo 7:9).
[8]“Wakati mtu anapofikiri kwamba kuyakuza maisha ya utakatifu ni lazima awe peke yake pamoja na Mungu, mtu huyo hawafai tena watu wengine.”
- Oswald Chambers
Aliipata Siri – Fanny Crosby
Wakati Fanny Crosby[1] alipokuwa na umri wa miezi miwili, alipata upofu wa kudumu kutokana na makosa ya madaktari.
Miezi michache baadaye, baba yake alifariki. Mama yake ilibidi aiache familia yake kwa masaa mengi akiwa anafanya kazi kama mjakazi. Fanny aliyajua matatizo ya maisha katika ulimwengu uliolaanika kwa dhambi.
Nyimbo za Fanny Crosby zilidhihirisha uwajibikaji wake kwa Kristo. Alikuwa ameyasalimisha kabisa mapenzi yake kwenye mapenzi ya Mungu. Katika utenzi wake mzuri, Bi.
Fanny Crosby alielewa kwamba utakatifu ni upendo mkamilifu kwa Mungu na kwa jirani yetu. Aliutumia muda wake na fedha zake kwenye umisheni kwa ajili ya walevi na wasio na makazi. Yeye na mume wake walitoa kila kitu ambacho kilikuwa ni muhimu kwa ajili ya wao kuweza kuendelea kuishi. Alimpenda Mungu na jirani zake. Siku hadi siku, Fanny Crosby aliendelea kukua katika kumfanania Kristo na upendo mkamilifu.
Fanny aliiangalia kwa matumaini siku ya ahadi ambayo, “Watauona uso wake” itatimilika. Wakati ikitokea mtu kumwonea huruma katika hali aliyokuwa nayo, Fanny Crosby alikuwa anajibu kwamba anaifurahia hali yake ya kuwa kipofu kwa sababu, “Nitakapoingia mbinguni, uso wa kwanza utakaofurahia kuuona upofu wangu ni ule wa Mwokozi wangu. Nitamwona uso kwa uso.”
[1] Image: "Francis Jane Crosby, 1820-1915" by W.J. Searle, retrieved from the Library of Congress Prints and Photographs Division, http://hdl.loc.gov/loc.pnp/cph.3b17084, "no known restrictions."
Tafakuri ya Somo la 11
(1) Utakatifu ni ushirika na Mungu usiovunjika.
(2) Kuanzia kitabu cha Mwanzo 3 hadi Nyaraka za Mitume, Mungu anaahidi kurejesha tena ushirika wa karibu kati ya Mungu na mwanadamu. Ahadi hii imetimilika katika kitabu cha Ufunuo.
(3) Kitabu cha Ufunuo kinaonyesha watu watakatifu katika ushirika usiovunjika na Mungu mtakatifu.
(4) Ushirika wa Kanisa ni maandalizi ya ushirika wa mbinguni. Kanisa la hapa duniani ni mfano wa kanisa litakalokuwepo wakati wa umilele. Kwa sababu hiyo, ni lazima tutafute sana kuweka maisha ya ushirika wa kanisa la hapa utakaofanana na ule wa kanisa la kule mbinguni.
Kazi ya Kufanya
(1) Jaribu kufikiria mtu anakuambia, “Nampenda Yesu, lakini siyo Kanisa.” Andika barua ya kurasa 1-2 ukimwonyesha huyu mtu kwamba kumpenda Yesu ni lazima kuelekezwe katika kumpenda Bibi harusi wa Bwana Yesu, ambaye ni Kanisa. Onyesha ni kwa jinsi gani moyo wa utakatifu utakavyoweza kuhamasisha upendo kwa ajili ya kanisa la Mungu. Onyesha ni kwa jinsi gani kuwa sehemu ya kanisa kunavyoweza kutusaidia sisi katika kuukulia utakatifu.
(2) Anza kikao kinachofuata cha darasa kwa kunukuu Ufunuo 21:2-3.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.