Ilikuwa ni siku kubwa kwa maisha ya Musa.[1] Alikuwa amekulia katika kasri la mfalme Farao alikuwa amekutana na watu wenye nguvu sana duniani. Lakini leo, Musa anakutana na mtu mwingine mwenye nguvu kuliko Farao. Anakutana na Yehova, Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo
Musa alikuwa amezungumza na Mungu katika kichaka kinachowaka moto. Aliwahi kumwona Mungu akiliangamiza jeshi lote la Farao katika Bahari ya Shamu. Musa anaenda kumwona Mungu kwa ukaribu zaidi kuliko kwenye kichaka kinachowaka moto au Bahari ya Shamu.
Leo, Musa alikuwa mbele ya uwepo wa Yehova. Musa alikuwa na ombi moja tu, “Nionyeshe utukufu wako.” Mungu alimwambia Musa kwamba hiyo kamwe haiwezekani. “Huwezi ukauona uso wangu, kwa sababu mwanadamu akiniona uso wangu atakufa.” Lakini Mngu akampa Musa upendeleo mwingine:
“Bwana akasema, ‘Tazama, hapa pana mahali karibu nami, nawe utasimama juu ya mwamba; kisha itakuwa wakati unapopita utukufu wangu, nitakutia katika ufa wa ule mwamba, na kukufunika kwa mkono wangu hata nitakapokuwa nimekwisha kupita; nami nitaondoa mkono wangu, nawe utaniona nyuma yangu, bali uso wangu hautaonekana.’”[2]
Musa alikuwa ameona sehemu ndogo tu ya utukufu wa Mungu, lakini aliporejea kambini, uso wake ulikuwa unang’aa. Kila wakati Musa alikuwa mbele ya uwepo wa Mungu, “ngozi ya uso wake Musa iling'aa; naye Musa akautia utaji juu ya uso wake tena, hata alipoingia kusema naye.”[3] Uso wa Musa ulidhihirisha utukufu wa Mungu. Musa akawa mtu mwenye uso wa kung’aa.
Tuliumbwa katika sura na mfano wa Mungu; tuliumbwa ili tuudhihirishe utukufu wa Mungu. Ingawaje dhambi iliharibu sura ya Mungu ndani ya mwanadamu, Mungu anatafuta sana kuirejesha sura yake ndani ya kila muumini. Kuwa watakatifu ni kuwa kama alivyo Baba yetu wa mbinguni. Kusudi la Mungu ni kurejesha sura yake kwa watu wake.
► Fikiria Mkristo anayeigiza mfano wa utakatifu kutoka kwa watu wengine. Ni tabia gani za Baba yetu wa Mbinguni unazoweza kuziona katika maisha ya huyu mtu?
Vitabu vitano vya mwanzo vya Biblia vinaonyesha kwamba Mungu ni mtakatifu, na anawaita watu wake wawe watakatifu. Tulitakiwa tufanane na Baba yetu wa mbinguni; tuliumbwa tuwe watakatifu. Lengo la Mungu ni kuwafanya watoto wake wawe katika sura yake.
Kuwa katika sura ya mtu fulani, inamaanisha kufanana na huyo mtu. Tuliumbwa katika sura ya Mungu. Kama vile kioo kinavyoakisi sura ya mtu, tuliumbwa ili tuakisi sura ya Mungu. Hii haimaanishi kwamba Mungu ana uso unaofanana na sisi; bali roho zetu zilifanywa kamilifu katika asili ya Mungu. Tuliumbwa tuwe mfano wa sura ya Mungu. Kama vile kioo kinavyoakisisura ya mtu, nasi tumeumbwa ili tuakisi sura ya Mungu.[1]
Tuliumbwa tuwe wasafi sana na watakatifu kama Mungu alivyo msafi sana na mtakatifu. Kuwa mtakatifu ina maana ya kuakisi Sura ya Mungu. Mungu anawaamuru watu wake, “Mtakuwa watakatifu.” Kwa nini? “Kwa kuwa mimi ni mtakatifu. Mtafanana na mimi.”[2] Tumeumbwa ili tuwe watakatifu; tuliumbwa ili tufanane na Baba yetu wa mbinguni.
Tumeumbwa katika Sura ya Mungu
Kilele cha historia ya uumbaji kilikuwa pale uumbaji wa mwanadamu ulipotimizwa “kwa kufanywa mfano wa Mungu.”[3] Vyote alivyoumba Mungu vilikuwa vizuri, lakini mwanadamu peke yake aliumbwa kwa sura ya Mungu. Mungu alimwumba Mwanadamu ili afanane na yeye mwenyewe. Mungu "akamvalisha taji la utukufu na heshima.”[4]
Mwanadamu ana uthamani usioisha kwa sababu ameumbwa kwa sura ya Mungu. Paulo anaandika, “kwa sababu yeye ni mfano na utukufu wa Mungu.”[5] Tuliumbwa kuakisi utukufu wa Mungu.
Sura ya Mungu ndani ya mwanadamu iliharibiwa na anguko la dhambi
Dhambi iliharibu kabisa sura ya Mungu ndani ya mwanadamu. Katika Mwanzo 1, mwanadamu aliumbwa “kwa mfanowa Mungu;” Katika Mwanzo 6, “kila mwenye mwili amejiharibia njia yake duniani.”[6] Mwanadamu alijiondoa mapema kwenye mpango wa Mungu kiasi kwamba “kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote.”[7]
Utukufu aliokuwa amepewa mwanadamu wakati wa uumbaji ulibadilika ukawa aibu. Paulo anaweka bayana kile kilichomfanya mwanadamu kupoteza kutokana na kumwasi Mungu na kugeukia miungu mingine. Kutokana na anguko, wanadamu “wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu.…” matokeo yake, Mungu:
Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao na unajisi.
Aliwaacha katika hisia zao kali zisizoweeza kiuwaletea heshima.
Yote haya ni matokeo ya anguko. Kwa sababu ya dhambi utukufu wa Mungu ulifanyika kuwa ni aibu kabIsa. Sura ya Mungu iliharibiwa; mwanadamu hakufanana tena na Muumba wake.
Sura ya Mungu inarejeshwa ndani ya watu wake
Hata hivyo, Mungu hakumwacha mwanadamu mwenyewe. Dhabihu zilikuwa ni njia ya kuthibitisha adhabu ya dhambi na nakurejesha mahusiano kati ya Mungu na mwanadamu. Lakini kusudi la Mungu linaenda mbali zaidi kuliko kulipa adhabu ya dhambi zetu. Mungu anatafuta kumfanya mwanadamu awe mtakatifu kama yeye alivyo matakatifu.
Kusudi la Mungu ni kuturejesha katika sura yake.[9] Sura yake ikisharejea ndani yetu, aibu ya dhambi inafutwa na kwa mara nyingine tena tunauonyesha utukufu wa Mungu. Hii ndiyo mojawapo ya dhamira kuu ya Biblia:
Tulifanywa katika sura ya Mungu (Mwanzo 1-2)
Kupitia dhambi, sura ya Mungu kwa mwanadamu iliharibiwa (Mwanzo 3)
Kuanzia na ahadi ya Masihi katika Mwanzo 3:15 na kilele kitakapofikia mbinguni, Mungu anarejesha sura yake kwa mwanadamu.
Yohana aliahidi kwamba kama tutakaa ndani yake, “tuwe na ujasiri, wala tusiaibike mbele zake katika kuja kwake.”[10] Tutakapokuwa tunabadilishwa katika sura yake, tunaurejesha tena utukufu uliokuwa umepotea kwenye anguko la dhambi. Aibu yetu imefutwa, na tunangojea ujio wake kwa matumaini. Tutakapoendelea kukua katika sura ya Mungu tunafanywa watakatifu. Kama Mungu alivyo mtakatifu, watu wake pia wanafanywa kuwa watakatifu.
Israeli walitakiwa kudhihirisha Sura ya Mungu
Mungu aliita Israeli kuwa watu watakatifu. Kusudi lake lilikuwa kurejesha sura yake kwa Israeli. Mungu aliiteua Israeli kama mwakilishi wake maalumu kwa mataifa mengine. Aliitenga Israeli kama wateule wake ambao wangeuonyesha utakatifu wake kwa mataifa mengine.
Mungu aliita Israeli kuwa “ufalme wa makuhani.” “Nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu.”[11] Jukumu la kuhani lilikuwa ni kumwakilisha Mungu kwa watu. Kazi maalumu kwa Israeli ilikua kumwakilisha Mungu kwenye mataifa yote. Mungu aliita Israeli kudhihirisha asili ya utakatifu wake kwa mataifa mengine. Ili kufanikisha umisheni huo, Israeli alipaswa awe mtakatifu.
Wakati Israeli ilipokuwa mwaminifu kwa Mungu, ilidhihirisha asili ya utakatifu wa Mungu; alifanyika kioo cha Mungu cha utakatifu. Wakati Israeli ilipogeukia miungu, ilidhihirisha asili ya dhambi ya miungu, na alifanyika kioo cha dhambi kwa miungu. Wakati Israeli iliposhindwa kufanana na Mungu, alishindwa katika umisheni wake kwa ulimwengu.
Kanisa linatakiwa kudhihirisha Sura ya Mungu
Katia Agano Jipya, Kanisa linaitwa liwe watu wa Mungu watakatifu. Kanisa linaitwa kuwa “ukuhani wa kifalme” unaomwakilisha Mungu kwa ulimwengu.
“Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu.”[12]
Kama vile Mungu alivyoichagua Isreli kuonyesha sura yake kwa mataifa, vivyo hivyo ameliteua Kanisa “kuwaeleza wengine jinsi Mungu alivyowaita kutoka katika dhambi kuingia kwenye nuru yake kuu.” Mungu alilichagua Kanisa kuwakilisha asili yake kwa wale ambao walikuwa hawajamjua. Kufanya hivyo, Kanisa lazima lidhihirishe sura ya Mungu. Kukamilisha umisheni huu, kanisa ni lazima liwe takatifu.
Wakati Kanisa linapokuwa mwaminifu kwa Mungu; linawakilisha asili ya utakatifu ya Mungu. Wakati kanisa linapogeukia miungu ya umaarufu, utajiri, nguvu na mengineyo, linafanana na miungu hiyo; na linadhihirisha asili ya dhambi ya miungu hiyo batili. Kanisa linaposhindwaa kufanana na Mungu, limeshindwa pia katika umisheni wake kwa ulimwengu.
Sura ya Mungu ni kurejeshwa tena kwa kila mwamini
Tuliumbwa tufanane na Baba yetu wa mbinguni. Tuliumbwa katika sura ya Mungu, lakini sura hii iliharibiwa wakati wa anguko la dhambi. Sura ya Mungu bado iko pale,[13] lakini bado imefichwa na dhambi.
Jaribu kufikiria mtu anayechimba kitu kule China kisha akakuta kitu cha kale cha thamani kubwa. Mwanzoni, hakitaonekana na uzuri wowote kwani kitakuwa kimefunikwa kwa udongo na matope. Mtu mwingine anayekiangalia anaweza kusema, “Kitupe mbali, hakina thamani yeyote!” Lakini mtu mjuzi anajua kwamba chini ya huo uchafu kuna tunu nzuri sana.
Sura ya Mungu kwa mwanadamu iliharibiwa na anguko la dhambi. Sura ya Mungu ilifunikwa na udongo na tope la dhambi, lakini Mungu anafanya urejesho wa sura yake kwetu. “Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake...”[14] Kama vile Yesu alivyofanana na Baba yake, tunapaswa kufanana na Mungu wetu. Utakatifu ni “mfano wa Mungu”; utakatifu ni urejesho wa sura ya Mungu kwa mwanadamu.
Michelangelo, mchongaji wa kinyago kilichoitwa Pieta[15] ni mmoja wa watu maarufu sana wa Sanaa ya uchongaji nchini Italia. Mwaka 1972, mwanamume mmoja kichaa alichukua nyundo akavunja kinyago chake. Wachongaji walichukua miezi kadhaa kukifanyia marekebisho kwenye uharibifu uliofanyika. Kwa sababu kinyango hicho kilikuwa cha thamani sana, walifanya kazi kwa uangalifu mkubwa ili kukirudisha katika sura yake ya awali. Leo hii, huwezi ukaona mahali popote palipoharibika katika kinyago hicho. Mchongaji alirejesha Pieta katika uzuri wake wa asili.
Kwenye anguko, dhambi ilichafua sana uumbaji mkuu wa Mungu. Dhambi iliharibu sura ya Mungu kwa mwanadamu. Kwa kuwa mwanadamu ni wa thamani sana kwa Mungu, alianza kurejesha sura yake ndani yetu. Kuanzia wakati wa anguko hadi sasa, Mungu amekuwa akifanya kazi kwa neema yake kurejesha wanadamu kwenye uzuri wetu wa asili. Kusudi la Mungu ni kuturejesha katika uzuri wa sura yake.
Wetu wengi sana wana uelewa usiokamilika kuhusu Injili. Mtazamo wao kuhusiana na Injili ni:
Nilikuwa mwenye dhambi.
Mungu akaniokoa.
Sasa ninaweza kwenda mbinguni.
Hizi ni habari njema – lakini siyo kwa Injili yote. Habari njema za Injili zinatambua kusudi la Mungu la umilele:
Nilikuwa mtenda dhambi.
Mungu akaniokoa.
Sasa Mungu anarejesha sura yake ndani yangu.
Mbinguni, “nitakuwa kama yeye, kwa sababu nitamwona kama alivyo.”[16] Kusudi la Mungu kwa watu wake litakuwa limetimia.
Je, hii haishangazi? Mungu amekuokoa wewe ili uwe kama yeye. Huu ndiyo uzuri wa maisha ya utakatifu. Kama watakatifu, tunarejeshwa kwenye sura ya Mungu.[17]
Mungu aliwaokoa wana wa Israeli kutoka Misri ili kwamba aweze kuishi pamoja nao katika mahusiano ya upehdo. Mungu hakuwakomboa wana wa Israeli ili waje wakaishi kama Wakanaani. Aliwaweka huru ili waweze kuwa kama yeye.
Kwa njia hiyo hiyo, tumeokolewa tuishi katika uhusiano wa karibu sana na Mungu na tubadilishwe kabisa katika sura yake. Mngu alituokoa katika dhambi zetu ili tuweze kuwa watakatifu kama yeye alivyo mtakatifu. Tuliumbwa tuudhihirishe utukufu wake.
“Bwana, ifanye roho yangu ikufananie wewe,
inga’e kama wewe peke yako ndani yangu,
ili watu waweze kuuona upendo wako na neema yako…”
- Blanche Mary Kelly
[15] Image: "Michelangelo's Pieta 5450 cut out black" taken by Stanislav Traykov on December 4, 2005, edited by Niabot, retrieved from https://commons.wikimedia.org/wiki/File:Michelangelo%27s_Pieta_5450_cut_out_black.jpg, licensed under CC BY 2.5, desaturated from the original.
[17] “Ushahidi unaovuma sana wa Roho Mtakatifu katika maisha ya mtu ni ule uwazi wa mashaka wa familia inayomfanania Yesu, na uhuru kutoka kwa kila mtu ambao haufanani na yeye.”
- Oswald Chambers
Utakatifu katika Matendo - Utakatifu na Hulka za Watu
Watu wengine wanaamini kwamba mtu mtakatifu atakuwa na aina fulani ya tabia na hisia zake. Fikiria nyuma kwenye majibu yako ya mwanzo wa somo hili: “Fikiria Mkristo anayeigiza mfano wa utakatifu kutoka kwa watu wengine. Ni tabia gani za Baba yetu wa Mbinguni unazoweza kuziona katika maisha ya huyu mtu?” Je, umezielezea kimsingi katika tabia au hisia za mtu? Mara nyingi tunafanya!
Hata hivyo, tunaposoma kitabu cha Agano Jipya, tunaona kwamba aina zote za tabia na hisia ziliwakilishwa wakati wa Pentekoste. Watu wa aina mbalimbali walijazwa na nguvu za Roho. Baada ya Pentekoste, wanafunzi hawakubadilika ghafla kuwa watu wa aina nyingine. Badala yake, Mungu alifanya kazi nao kupitia tabia na hisia zao za asili kufanikisha malengo yake kwa njia mpya.
Thomaso hakufanyika mara moja mtu mwenye akili na mwenye matumaini. Hadi kufikia kifo chake, Tomaso labda alikuwa mkimya na wa kujifkiria. Simoni Petro hakuwa kwa ghafla mtu mpole akikaa bila kujulikana na watu kwenye kona. Hata baada ya Pentekoste, Petro alikuwa mmojawapo aliyesema kwa kujiamini, “Hasha, Bwana!”[1]
Mungu alimuumba kilammoja wetu kwa tabia na hisia za kipekee. Utakaso hauharibu hizi tabia au hisia. Badala yake, jinsi sisi wenyewe tunavyojisalimisha kwa Mungu, sura yake inazidi kung’aa ndani yetu kupitia tabia na hisia zetu.
Je, inawezekana Sura ya Mungu ikang’ara kupitia tabia na hisia zetu?
Hii itaonekanaje katika maisha ya kila siku? Mtu “A” mshindani. Mchangamfu ambaye amejisalimisha kabisa kwa Mungu ataendelea kuwa na tabia na hisia za mtu “A”. Mtu mwenye aibu anayeepuka makundi ya watu ataendelea kuwa kuwa na aiu. Hata hivyo, katika hali zote mbili, mtu alitetakaswa humruhusu Mungu “kusakafia maeneo korofi” ya tabia na hisia zake inapoonekana kuna maeneo ambayo hayaakisi sura ya Mungu.
Nitatoa mfano: Wachungaji Greg na Mark walikuwa wenye tabia na hisia zenye nguvu sana. Wote walikuwa na msimamo imara. Wote walikuwa “wasemaji” wazuri waliokuwa na uwezo wa kushindana kwa hoja. Wote walikuwa katika nafasi za uongozi. Kwa sababu ya msimamo wao imara, wote mara nyingine waliweza kulaumiana kwa maneno yao.
Nilimjua Mchungaji Greg alipokuwa anakaribia mwisho wa maisha yake. Aliniambia, “Huwa siombi msamaha. Haijalishi watu wanafikiria nini katika yale ninayoyasema. Ni makossa yao kama wakishindwa kunielewa. Ninajua moyo wangu uko sahihi!” Ingawaje moyo wa Greg ungeweza kuwa wa kweli, watu katika makanisa aliyokuwa akihudumia walikuwa mara nyingi wanaumizwa na maneno yake. Alikuwa hajaweza kujifunza kwa ukamilifu jinsi ya kuachilia sura ya Mungu ing’are kwenye tabia na hisia zake.
Mchungaji Mark pia alikuwa kiongozi mwenye nguvu. Hata hivyo Mchungaji Mark aliojifunza inamaanisha nini kuakisi sura ya Mungu. Alijifunza kusema, “Samahani. Nimezungumza kwa hisia kali sana.” Alijifunza kuonyesha huruma na kutenda haki. Wafuasi wake walikuwa wanasema, “Mchungaji wetu alitutendea kama Yesu.”
Utakatifu haubadilishi aina yako ya tabia na hisia; Utakatifu unakufanya uwe msikivu kwa sauti ya Roho Mtakatifu wakati anaposema, “Unahitajika kuomba msamaha. Ulikuwa na hisia kali sana.”
Kama una tabia na hisia ya kuepuka macho ya watu hadharani, utakatifu haukufanyi ugeuke uwe mchangamfu unayependa kujitokeza mbele ya watu. Hata hivyo, utakatifu unakufanya uwe tayari kuweka pembeni mashaka yako anaposema, “Ninakutaka utoke ukaongoze katika mazingira haya.”
Everett Cattell anatoa mifano mitatu kuonyesha ni kwa jinsi gani Shetani anapenda kupindisha mwelekeo wetu wa asili katika kupiga vita sura ya Mungu katika maisha yetu.[2]
Mfano wa 1: Kula
Njaa ni hamu ya asili. Inawezekana kula “kwa ajili ya utukufu wa Mungu.”[3] Hakuna hata mmoja atakayetafuta uzoefu wa kiroho wa kuharibu njaa.
Kwa watu wengi, hata hivyo, Shetani ameharibu hii hamu ya asili kuifanya ulafi. Badala ya kula ili kutosheleza hitaji la kawaida na la asili, kula kumekuwa ni njia ya kufurahisha tamaa za binafsi.
Suluhisho la kuzuia hivi vita siyo kuondoa kabisa hamu ya kula. Suluhisho ni kujithibiti mwenyewe kunakozuia hamu ya asili isipindishwe kuwa kitu kingine cha hatari na hata cha dhambi.
Mfano wa 2: Wepesi katika kuhisi:
Everett Cattell anatoa tena mfano mwingine mgumu zaidi. Mtu yeyote mwenye mhemuko wa kawaida ana kiwango fulani cha wepesi wa kuhisi maumivu au mateso. Hii ni kawaida na siyo dhambi. Hata hivyo, kama tutaruhusu huu wepesi wa kuhisi ukue kufikia kiwango cha kujionea uchungu, inakuwa ni tabia ya kujifikira mwenyewe tu ambayo inazuia uwezo wetu wa kumtumika Mungu kikamilifu na kuakisi sura ya Mungu kwa wengine.
Hapa tena, suluhisho siyo kuondoa mihemuko ya kawaida au wepesi wa kuhisi na kukosa huruma kwa maneno na vitendo vya watu wengine. Badala yake, tunapaswa tujifunze kusalimisha huu wepesi wa kuhisi kwa Mungu na tumruhusu aongoze na kutawala mwitikio wetu kwa mambo yanayoumiza.
Mfano wa 3: Ulimi:
Inawezekana huu ni mfano mgumu zaidi. Sisi sote ni lazima tutumie ulimi. Hatuwezi kuomba, “Mungu, nakuomba ng’oa ulimi wangu.” Hata hivyo, ulimi hauwezi kuruhusiwa utoke nje ya kujitawala.
Cattell anatoa mfano wa mmishenari aliyekuwa mara kwa mara sahihi katiki maoni yake, lakini akiumiza wengine kwa hisia zake kali. Kwenye maisha ya mabadiliko ya kiroho, alisema maneno ya kuwaumiza watu wake aliowahudumia. Usiku ule, Mungu akamwonyesha yule mmishenari kwamba ana makosa ya ulimi wake kuumiza watu wengine.
Mmishenari aliomba kisha akaenda kwenye mkusanyiko wa asubuhi. Akawaambia watu kwenye ule mkusanyiko, “Kama tatizo langu lingehusiana na pombe, ingekuwa rahisi sana kwangu. Ningeachana nayo kabisa na tatizo lingeisha. Lakini tatizo langu kubwa ni ulimi wangu. Siwezi nikaukata nikautupa kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Lakini nimeukabidhi ulimi wangu kwa Mungu, ninaamini kwamba Roho Mtakatifu atanisaidia niutumie kwa ajili ya utukufu wake.”
Mchungaji Cattell anaonyesha makosa mawili yanayofanana na ya ulimi:
Kusema kwamba, “Mimi ni mwenye dhambi lakini siwezi kuutawala ulimi wangu. Nitaendelea kutenda dhambi, kwa sababu neema ya Mungu haina uwezo wa kuondoa tatizo langu.”
Kusema kwamba, “Nimeomba ili Mungu anifanye mimi kuwa mtakatifu. Kwa hiyo, atautawala ulimi wangu. Sihitajiki kufanya lolote kujiweka katika nidhamu mwenyewe. Nitamwamini Mungu tu.
Tabia iliyo sahihi inasema, “Nimeusalimisha moyo wangu –na ulimi wangu – kwa Bwana. Moyo wangu ni msafi, lakini natambua kwamba napaswa kutiisha matumizi ya ulimi wangu. Nitachukua muda kufikiri kabla kabla ya kuongea. Nitachukua muda wa kuomba kwanza kabla ya kuongea. Na kama ninazungumza sana, nitajishusha mwenyewe na kutubu.” Mtu mtakatifu atakuwa mwepesi kumwendea mtu aliyemkwaza au kumkosea kwa toba ya unyenyekevu.[4]
► Ni sehemu gani yenye hatari kwako? Fikiria tamaa za asli zinazoweza kukuingiza kwenye mitazamo na tabia za dhambi. Toa mfano ni kwa jinsi gani hii hamu mara nyingine imekusababishia matatizo. Kisha toa mfano wa jinsi Mungu alivyokusaidia katika kutiisha hamu hii.
Je, ni kwa jinsi gani Mungu huakisi tabia na hisia za mtu mtakatifu?
Tunapotafuta kuakisi sura ya Mungu katika maisha yetu, Mungu hufanya kazi kwa njia nyingi kututengeneza tuwe watu anaotaka yeye. Kama mwana akiolojia atafutaye sanamu za zamani kule China, na kwa uangalifu mkubwa akakipaka polishi hadi kikang’aa, Mungu kwa utaratibu huwapaka watoto wake polishi hadi wakang’aa na kudhihirisha sura yake.
Ni njia gani Mungu hutumia katika kuwatengeneza watu wake kurejea katika sura yake? Mwanzoni mwa somo hili, tuliona ni kwa jinsi gani Musa aliakisi sura ya Mungu. Tunapoangalia maisha ya Musa, kunatupa vielelezo vya jinsi Mungu anavyotutengeneza sisi katika sura yake.
Mwanzoni mwa maisha yake, Musa hakuwa anaakisi sura ya Mungu kila wakati. Hasira yake ilimfanya akaua mtu, na hii ikatishia kumweka nje kabisa kwa ajili ya kutumika kwenye ufalme wa Mungu.[5] Hata hivyo, Mungu alimtengeneza Musa katika hali ya kuwa, “mnyenyekevu zaidi kuliko watu wote waliokuwa chini ya uso wa dunia.”[6] Musa alikuwa mwepesi kukataa tamaa,[7] lakini Mungu alimtengeneza kuwa mtu mwaminifu wa kuwaongoza watu wake kwa miaka arobaini jangwani. Je, ni kwa jinsi gani Mungu alibadilisha tabia ya Musa?
(1) Mungu hutumia neno lake kutengeneza watoto wake kuwa katika sura yake.
Moja ya kifaa muhimu sana anachokitumia Mungu ni Neno lake. Tuanapoliweka Neno la Mungu ndani ya mioyo yetu, hulitumia katika kutuongoza.[8] Wakati Musa akipokea sheria za Mungu moja kwa moja kutoka mikononi mwa Mungu, kulimtengeneza uelewa wake na tabia yake.
Watu watakatifu ni watu wa dunia. Wanajua katika Neno la Mungu wataiona asili ya Mungu. Wanajua kwamba kwenye Neno la Mungu watajifunza jinsi ambavyo tabia zao zitaakisi tabia ya Mungu. Simjui Mkristo yeyote maarufu katika historia ambaye hajawahi kuwa mwanafunzi wa dunia.
(2) Mungu hutumia mazingira magumu kuwatengeneza watoto wake katika sura yake.
Kwa sababu ya mauaji ya Mmisri, Musa alitumia miaka arobaini jangwani. Mara nyingi, alikuwa anaweza kufikiria, “Nimepoteza nafasi yangu. Siwezi nikafanya jambo lolote la ziada zaidi ya kuchunga kondoo.” Lakini Mungu aliitumia miaka ile arobaini katika kumtengeneza Musa awe kiongozi.
Moja kati ya aya zinazotia moyo katika maisha ya mtume Petro ni wakati Yesu alipotabiri kuhusu anguko lake wakati wa mateso yake. Yesu alimwonya Petro, “Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano;…” Akamtia moyo, “lakini nimekuombea wewe ili Imani yako isitindike.” Kisha baadaye, akaahidi kwamba kutokana na anguko la kushindwa kwa Petro (kwa muda), Mungu atafanya jambo jema. “Nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako.”[9] Mungu alitumia hata mazingira ya uharibifu ya kushindwa kwa Petro kumfanya awe wa kufaa zaidi.
Watu watakatifu huamini utoaji wa Mungu katika nyakati za matatizo. Wanaamini katika Warumi 8:28 kwa sababu wanataka waiishi Warumi 8:29. Mungu anaahidi, “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.” Kisha, anatuambia sisi “kusudi” la Mungu ni kuleta ndani yetu maisha ya mtoto wake: “Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake.”
Siyo kila jambo linalofanyika kwa mtu mtakatifu ni jema! Lakini yote yanayotendeka “hufanya kazi pamoja” katika kutimiza kusudi la Mungu – kututengeneza katika sura ya Mwana wake.
(3) Mungu hutumia watu kutengeneza watoto wake kwa sura yake.
Hii inaweza kuwa ni ngumu zaidi katika zote tatu. Mungu hutumia watu – mara nyingi watu wenye matatizo - ili kututengeneza sisi kuwa katika sura yake. Wakati Musa alipokuwa karibu kuvunjika moyo kutokana na majukumu mazito ya uongozi aliyokuwa nayo, Mungu alimtumia baba mkwe Yethro (ambaye hata hakuwa Mwisraeli) kumpa Musa ushauri uliomfanya awajibike kwa ufanisi zaidi.[10]
Tunaweza kumwangalia tena Simoni Petro. Kupitia kukutana kwake na Yohana, na baadaye kupitia makabiliano yake na Paulo, Petro alitengenezwa zaidi na zaidi katika Sura ya Mungu. Paulo “alikabiliana naye uso kwa uso” kutokana na Petro kushindwa kuishi kwenye mafundisho aliyokuwa amefundishwa na Roho Mtakatifu ya kutokula pamoja na mataifa.[11] Akiwa ni mtume aliyemtangulia, hii ilitosha kumfanya Petro ajisikie kufedheheshwa sana. Alikuwa anamfuata Kristo wakati Paulo alikuwa bado anawauwa Wakristo! Lakini Petro aliruhusu Mungu aendelee kufanya kazi ndani yake ili kumleta karibu na kile ambacho Mungu alikuwa amemkusudia Petro awe.
Watu watakatifu huruhusu Mungu kufanya kazi kupitia watu wengine ili kutengeneza tabia zao katika Sura ya Mungu. Mithali anasema, “Chuma hunoa chuma; Ndivyo mtu aunoavyo uso wa rafiki yake.”[12] Sehemu ya makali ya shoka hupata makali yake kutokana na kunolewa na chuma kingine. Kwa njia hiyohiyo, watu wanapokutana na watu wengine, ustadi wao unanolewa zaidi.
Maisha ya utakatifu ni zaidi ya kipindi kimoja cha mgogoro. Nimaisha ya kubadilishwa kila siku katika sura ya Mungu. Kila tunapojikabidhi kwa kazi ya Bwana katika maisha yetu, anatutengeneza hatua kwa hatua katika sura yake. Haya ni maisha ya vitendo ya utakatifu.
Moyo wa utakatifu haujawekwa kwa ajili ya wachungaji na wamishenari. Mungu anataka ambadilishe kila Mkristo katika sura yake. Frank Crossley alionyesha sura ya Mungu katika maisha ya kawaida sana. Frank Crossley hakuwa mwalimu; alikuwa mmiliki wa injini za Crossley. Hakuishi kwenye pango lililofichwa na majaribu: aliishi Manchester, katika jiji kubwa la viwanda.
Frank Crossley alikuwa mfanya biashara tajiri mkubwa Uingerza katika karne ya 19. Mara tu baada ya kuongoka kwake, Crossley alimsikia msichana mdogo akiimba kutoka Jeshi la Wokovu akishudia kuhusiana na nguvu ya kubadilisha ya Roho Mtakatu. Crossley akasema kwa mke wake, “Ninataka nimfahamu Mungu kama yule msichana anavyomjua Mungu.” Alirudi usiku unaofuata na akaanza kutafuta moyo safi.
Baada ya Mungu kutakasa moyo wake kupitia Imani, Crossley alitaka kufanya zaidi kuliko kutafuta fedha. Aliamua kuwa mhubiri. Aliwasiliana na Jenerali William Booth wa Jeshi la Wokovu, lakini Booth kwa hekima alimshauri Bwana Crossley aendelee na kazi yake ya biashara. Jenereali Booth aliamini kwamba Frank Crossley angekuwa wa ufanisi zaidi katika kumtumikia Mungu kupitia biashara zake.
Bwana Crossley aliuliza, “Ninawezaje kuonyesha sura ya Mungu katia maisha yangu? Ni kwa jinsi gani Yesu anaweza kuwatendea wafanyakazi wangu?” Alihamishia kiwanda chake kwenye eneo lililokuwa maskini sana la jiji ili kuwasaidia wahitaji. Aliwachukulia wafanyakazi wake kama ndugu zake wa Kikristo.
Frank Crossley alidhihirisha moyo wa utakatifu kupitia tabia iliyomfanania Kristo. Siku hadi siku, bwana Crossley aliiakisi sura ya Mungu katika kuhudumia watu wengine. Mwanauamsho mfanya biashara wakati mmoja akakutana na Bwana Crossley kuhusiana na mkataba mgumu. Baadaye alisema, “Bwana Crossley alinitendea kama ambavyo Yesu Kristo angefanya.” Mfanya biashara mwenzake aliiona Sura ya Mungu ndani ya Frank Crossley.
Kwa Frank Crossley, swali muhimu sana kwake halikuwa, “Nitawezaje kupata fedha zaidi?” Swali muhimu sana alilokuwa nalo ni, “Je, ninafanana na baba yangu wa Mbinguni?” Kwa sababu ya hiyo, Bwana Crossley aliudhihirisha uso wa Mungu kwa wale waliokuwa wamemzunguka. Huu ndio utakatifu.
Tafakuri ya Somo la 3
(1) Kuwa mtakatifu inamaanisha kuakisi sura ya Mungu.
(2) Sura ya Mungu kwa wanadamu iliharibiwa katika anguko.
(3) Mojawapo ya dhamira kuu ya Biblia ni kurejesha sura ya Mungu kwa mwanadamu.
(4) Kusudi la Mungu la umilele ni kuturejesha katika sura yake
(5) Wakati Israel ilipokuwa mwaminifu kwa Mungu, ilionyesha sura yake kwa mataifa.
(6) Kanisa linapokuwa na uaminifu kwa Mungu, tunaudhirisha uso wa Mungu kwa ulimwengu unaotuzunguka.
(7) Sura ya Mungu ndani yetu imeharibiwa na dhambi. Hata hivyo, Mungu anafanya kazi ndani ya kila muamini il kutufanya tufanane naye zaidi na zaidi.
(8) Habari njema za Injili ni kwamba:
Nilikuwa mwenye dhambi.
Mungu akaniokoa.
Sasa ninaweza kwenda mbinguni.
Mbinguni, nitafanana na yeye kwa sababu nitamwona kama alivyo.
(9) Mungu yuko kazini akiwatengeneza watoto wake katka sura yake. Bila kujali tabia na hisia zetu, anataka kujidhihirisha mwenyewe kwetu. Mungu hulitumia neno lake, mazingira ya maisha, na watu wengine katika kututengeneza katika sura yake.
Kazi ya Kufanya
(1) Andika insha ya kurasa 2-3 yenye kichwa cha habari: “Sura ya Mungu ndani yangu.” Jibu mawali manne:
Kama watu wa familia yangu wakiniangalia, je, wataiona sura ya Mungu ndani yangu?
Watu wa familia yangu wataona nini watakapoona kwamba hakuna kinachofanana na sura ya Mungu ndani yangu?
Ni hatua gani tatu za vitendo nitakazoweza kuchukua ili kuakisi sura ya Mungu katika maisha yangu?
Ni mazingira gani au watu ambao Mungu huwatumia kunitengeneza katika sura yake kwa sasa hivi?
(2) Anza kikao kinachofuata cha darasa kwa kunukuu 2 Wakorintho 3:17-18.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.