Ezekieli: Mtu aliyeuona mpango wa Mungu kwa ajili ya baadaye
Israeli haikuwa taifa takatifu tena. Iliabudu masanamu; Iligandamiza maskini, ilipuuzia Sabato. Katika hukumu, Mungu aliwapeleka watu wake uhamishoni. Mungu aliruhusu jeshi la Babeli kuipiga Yerusalemu na kuliharibu hekalu. Kwa kuwa watu wa Mungu hawakuwa watakatifu tena, hakuikubali tena ibada yao. Kwa kuwa watu wa Mungu hawakuwa tena wametengwa na dhambi, hakuikubali tena ibada yao.
Hata hivyo, bado Mungu alikuwa na kusudi na watu wake. Miaka kumi baada ya kuharibiwa kwa hekalu, Mungu alimpa maono Ezekieli, nabii aliyeishi kama mateka karibu na Babeli. Ezekieli aliyaona maono ya Mungu kwa ajili ya baadaye.
Katika maono ya Ezekieli, uhamisho umefika mwisho; Hukumu imemalizika; na uwepo wa Mungu umerudi. Hekalu limejazwa na utukufu wa Mungu. Mungu amewanyunyizia maji safi na kuwatakasa na uchafu wote wa nje wa ukosefu wa maadili. Ameondoa “moyo wa jiwe” na kuwapa “moyo mpya na roho mpya.” Ametimiza ahadi yake kwamba, “Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.”[1] Israeli ni safi nje na ndani.
Ezekieli aliona hekalu lililobariki mataifa. Maji safi yakitiririka kutoka katika hekalu lililorejeshwa upya kuelekea Bahari Nyeusi. Miti ilitoa matunda kwa ajili ya chakula na majani kwa ajili ya tiba. Uzuri wa Edeni ulirejeshwa upya.
Sehemu ya kupendeza sana katika maono haya ni katika aya ya mwisho: “…na jina la mji huo tangu siku hiyo litakuwa hili, ‘Bwana yupo hapa’” (Ezekiel 48:35). Kusudi la Mungu kwa watu wake limetimia: watu watakatifu wakiishi mbele ya Mungu mtakatifu!
► Jadili ushahidi mbalimbali wa nje kwamba mtu ni mtakatifu. Tutegemee matendo gani ya nje kutoka kwa mtu ambaye moyo wake ni mtakatifu?
Manabii walileta mashitaka dhidi ya taifa ambalo lilikuwa limevunja agano. Katika Vitabu vya Manabii, kama ilivyo katika Vitabu Vitano vya Mwanzo vya Biblia, neno “mtakatifu” linarejea kitu ambacho ni mali ya Mungu na kilichotengwa kwa ajili ya Mungu. Yerusalemu na hekalu vilikuwa vitakatifu kwa sababu vilikuwa ni mali ya Mungu.
Mungu ni Mtakatifu
Mara ishirini na moja, Isaya alizungumzia kuhusu “Mtakatifu wa Israeli.” Maserafi waliimba: “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni Bwana wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake!”[1]
Mungu ni ambaye “hujidhihirisha utakatifu wake katika haki.”[2] Ezekieli aliiona siku ambayo Mungu ataudhihirisha utakatifu wake kwa mataifa yote. “Nami nitajitukuza, na kujitakasa, na kujidhihirisha, mbele ya macho ya mataifa mengi; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.”[3]
Hukumu za Mungu zinaonyesha asili yake ya utakatifu. Mika alionya kwamba, kutokana na dhambi ya Israeli, “Bwana anakuja akitoka mahali pake, naye atashuka, na kupakanyaga mahali pa dunia palipoinuka.”[4] Mungu aliihukumu Israeli kwa sababu Mungu mtakatifu hawezi kuhurumia au kuachilia dhambi ipite bila kuadhibiwa.
Ukombozi wa Mungu kwa Israeli unaonyesha kwamba yeye ni mtakatifu. Mungu hakuikomboa Israeli kwa sababu alistahili kukombolewa, lakini ni kwa ajili ya jina lake takatifu miongoni mwa mataifa.
"…Bwana MUNGU asema hivi 'Sitendi hili kwa ajili yenu, Ee nyumba ya Israeli, bali kwa ajili ya jina langu takatifu, mlilolitia unajisi katika mataifa mliyoyaendea. Nami nitalitakasa jina langu kuu, lililotiwa unajisi katika mataifa, mlilolitia unajisi kati yao…'"[5]
Mungu asingeweza kukubali jina lake liaibishwe kwa sababu ya dhambi ya Israeli. Aliahidi kuirudisha Israeli katika ardhi yake kuonyesha utakatifu wake mbele ya mataifa mengine.
"Bwana MUNGU asema hivi: 'Nitakapokuwa nimewakusanya nyumba ya Israeli, na kuwatoa katika watu ambao wametawanyika kati yao, na kutakasika kati yao machoni pa mataifa, ndipo watakapokaa katika nchi yao wenyewe, niliyompa mtumishi wangu, Yakobo.'"[6]
Hii ni ahadi ya ajabu. Mungu aliahidi kuonyesha utakatifu wake kwa kuikomboa Isreli na kuirejesha nyumbani. Mungu aliahidi kuudhihirisha utukufu wake kwa watu wale wale alioamua kuwapeleka uhamishoni. Utakatifu ni wa Mungu.
Israeli haikuwa Takatifu
Kwa kuwa utakatifu ni wa Mungu, tunakuwa watakatifu pale tu tunapoishi kwenye mahusiano na Mungu mtakatifu. Manabii walitangaza kwamba Israeli siyo takatifu tena kwa sababu iliishi katika matamanio ya dhambi badala ya kuishi kwa utiifu na mahusiano ya upendo na Mungu.
Katika Isaya, Mungu alisema kwamba alikuwa ametengwa na Yuda kwa sababu ya dhambi yake. Mungu aliikataa Israeli kwa sababu haikukubali kuishi maisha ya haki na uadilifu.
"…kazi zao ni kazi za uovu, na vitendo vya udhalimu vimo mikononi mwao. Miguu yao hukimbilia mabaya, nao hufanya haraka kumwaga damu isiyo na hatia; mawazo yao ni mawazo ya uovu; ukiwa na uharibifu zaonekana katika njia kuu zao."[7]
Mungu alimwamuru Yeremia kuuficha mshipi wake. Kitani cheupe kilikuwa ni ishara ya usafi. Yeremia aliuficha ule mshipi hadi udongo na tope vikauharibu. Hii iliashiria Yuda kuwa mchafu. Mungu aliichagua Yuda iwe ni watu wa haki na uadilifu. Badala yake watu waliishi maisha ya dhambi.[8]
Katika Ezekieli, Mungu aliishutumu Israeli kama taifa la waasi wasumbufu; “walioasi kinyume changu.”[9] Badala ya kumtii Mungu mtakatifu, Israeli iliishi kama mataifa ya kipagani. “Kwa maana hamuendi katika amri zangu, wala hamkuzishika hukumu zangu, bali mmetenda mambo kama hukumu za mataifa wanaowazunguka.”[10] Israeli haikuwa tena yenye maadili na haki.
Wakati wakiwa uhamishoni, Danieli alikiri kwamba watu waliokuwa wamechaguliwa kumheshimu Mungu mbele ya mataifa wamefanyika kuwa ni “aibu ya wazi.”[11] Kwa nini?
"Naam, Israeli wote wameihalifu sheria yako, kwa kugeuka upande, wasiisikilize sauti yako; basi kwa hiyo laana imemwagwa juu yetu, na uapo ule ulioandikwa katika sheria ya Musa, mtumishi wa Mungu; kwa sababu tumemtenda dhambi."[12]
Manabii wadogo waliilaumu Israeli kwa dhambi yake. Hosea aliishutumu Israeli kwa “kuapa kwa uongo, na kuvunja ahadi, na kuua, na kuiba, na kuzini;”[13]Mika aliwahubiri watu “wanaochukia mema, na kuyapenda mabaya.”[14]
Zephania alikuwa ni wa ukoo wa Hezekia. Alikuwa ni wa familia iliyokuwa na nguvu sana katika Yuda, lakini hakusita kuilaumu Israeli kwa dhambi yake.
"Wakuu wake walio ndani yake ni simba wangurumao; makadhi wake ni mbwa-mwitu wa jioni; hawasazi kitu cho chote hata siku ya pili. Manabii wake ni watu hafifu, wadanganyifu; makuhani wake wamepatia unajisi patakatifu, wameifanyia sheria udhalimu."[15]
Kuanzia kwenye watawala wa kisiasa hadi viongozi wa dini, Israeli ilitenda dhambi kinyume na sheria za Mungu. Tatizo lilikuwa ni nini? Israeli ilisahau kwamba utakatifu ni kitu cha ndani mno kuliko kawaida (taratibu) za dini. Israeli ilibadilisha uadilifu na haki ya kweli kuwa sherehe tupu.
Kusudi mojawapo la sheria ilikuwa ni kuifundisha Israeli ijielewe kwamba yeye ni mali ya Mungu. Kwa bahati mbaya, Israeli katika muda mfupi sana ilisahau maana halisi ya sheria. Watu walifuata kawida za dini zilizokuwa sahihi lakini mioyo yao haikuwa mitakatifu. Taifa hili lililokuwa limetengwa na Mungu lionekane ni sura yake sasa limekuwa chafu (najisi). Vitabu vya Manabii vinafundisha kwamba kuwa mtakatifu inamaanisha kuwa mwenye uadilifu na haki ndani na nje yako.
Ezekieli alipelekwa Babeli mwaka wa 597 K.K. Wakati Ezekieli akiwa na miaka thelathini, Mungu alianza kuzungumza naye kupitia mfululizo wa ndoto. Ezekieli aliwaona viongozi wa Yuda wakiabudu sanamu katika Patakatifu pa Patakatifu.[1] Mungu akaamuru malaika kushusha hukumu hadi ua za ndani za hekalu zilipojaa miili iliyokufa. Utukufu wa Mungu uliondoka katika hekalu.[2] Hekalu pamoja na taratibu zake za kidini zilikuwa hazina maana yeyote kwa sababu watu walikuwa sio watakatifu.
Maisha ya utakatifu ni zaidi ya Kawida za Kidini
Israeli ilijinasibu kwamba ni takatifu, lakini ilikuwa ni yenye dhambi na najisi. Watu walifuata kawaida za utakatifu, lakini hawakuishi maisha ya haki na uadilifu ya utakatifu. “Wamemwacha Bwana, wamemdharau yeye aliye Mtakatifu wa Israeli, wamefarakana naye na kurudi nyuma.”[3] Watu walifuata kwa usahihi taratibu za dini, lakini wakaishi maisha ya dhambi. Manabii walifundisha kwamba taratibu za kidini zilikuwa hazina maana yeyote kama watu wa Israeli wataishi maisha ya dhambi. Utakatifu ni zaidi ya matamasha na dhabihu.
Isaya alisema kwamba Mungu amezikataa dhabihu za Yuda kwa sababu ya kutoishi maisha ya uadilifu na haki.
"Msilete tena matoleo ya ubatili…. siyawezi maovu hayo na makutano ya ibada. Sikukuu zenu za mwezi mpya na karamu zenu zilizoamriwa, nafsi yangu yazichukia; mambo hayo yanilemea; nimechoka kuyachukua."[4]
Akiwa amesimama mbele ya hekalu, Yeremia alitangaza, “Msitumainie maneno ya uongo, mkisema, ‘Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana ndiyo haya.’”[5] Hekalu lilikuwa siyo takatifu tena. Kwa nini? Kwa sababu watu wa kuabudu katika hekalu hawakuwa na maisha yenye haki na maadili tena. Mungu alionya, “Wafungapo, mimi sitasikia kilio chao; na watoapo sadaka za kuteketezwa na sadaka ya unga, sitazitakabali.”[6] Mungu anahitaji zaidi ya taratibu za ibada zilizo tupu.
Mungu alimwamiba Hosea, “Nataka fadhili wala si sadaka; na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa.”[7] Israeli ilitoa dhabihu, lakini ikavunja maagano yake na Mungu. Sadaka za kuteketezwa bila ya maisha ya haki na uadilifu hayana maana yeyote. Pamoja na Israeli kutoa dhabihu, Mungu “ataukumbuka uovu wao, na kuwapatiliza dhambi zao.”[8] Kwa nini?
"Hapana neno ila kuapa kwa uongo, na kuvunja ahadi, na kuua, na kuiba, na kuzini; huruka mpaka, na damu hugusana na damu."[9]
Amosi alihubiri kwenye ufalme wa kaskazini muda mfupi kabla ya kutekwa na Waashuru. Amosi aliwapa nafasi ya mwisho ya kutubu. Amosi alikabiliana na Israeli kwa dhambi yake. “Watu wa Mungu” waliokuwa na nadhiri na Mungu walikuwa wenye hatia ya kila dhambi kuanzia kwenye mambo ya ajabu katika jamii hadi kwenye matendo ya aibu ya zinaa. Matajiri wa Israeli waliwatoza watu faini zisizo za haki, na kutumia fedha hizo kununulia mvinyo kwa ajili ya sherehe za kidini.[10] Kwa kuwa maisha yao yalishakuwa ya dhambi, ibada zao zilikuwa hazina chochote.
"Mungu alisema: 'Mimi nazichukia sikukuu zenu, nazidharau, nami sitapendezwa na makutano yenu ya dini. Naam, ijapokuwa mnanitolea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za unga, sitazikubali; wala sitaziangalia sadaka zenu za amani, na za wanyama walionona. Niondoleeni kelele za nyimbo zenu; kwa maana sitaki kuzisikia sauti za vinanda vyenu.'"[11]
Hata baada ya kutoka uhamishoni, Yuda ilijaribu kufanya mbadala wa kawaida za kidini kugeuka kuwa utiifu kamili. Mwaka 516 K.K. watu walianza kulijenga upya hekalu. Ingawaje walikuwa wanaifanya kazi ya Kanisa, mioyo yao haikuwa mitakatifu. Hagai aliwakumbusha watu kwamba kuhani anayekamata kitu kilichokufa anafanyika kuwa najisi. Kwa jinsi hiyo hiyo, uchafu unaosababishwa na dhambi za watu kumeifanya kazi yao katika hekalu kuwa najisi.[12] Kawaida za dini bila haki na uadilifu ni ishara zilizo tupu; Utakatifu ni zaidi ya kawaida (taratibu) za kidini.
Malaki alionya kwamba Mungu ameikataa ibada ya Yuda. “Sina furaha kwenu, asema Bwana wa majeshi, wala sitakubali dhabihu yo yote mikononi mwenu.”[13] Mungu alikataa kupokea dhabihu ya Yuda kwa sababu ya dhambi za watu wake.
Vitabu vya Manabii vinaelezea waziwazi kwamba: Utakatifu ni zaidi ya kawaida za ibada. Mtu asiyeishi maisha ya uadilifu na haki, siyo mtakatifu. Hatuwezi tukamwabudu Mungu kwa mikono michafu.
Maisha ya utakatifu ni zaidi ya kuliita Jina la Mungu
Mungu aliwakataa watu waliokuwa wakiliitia jina lake kwa sababu walikataa kuachana na dhambi zao. Katika Agano Jipya, Yesu alionya:
"Si kila mtu aniambiaye, 'Bwana, Bwana,' atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, 'Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?' Ndipo nitawaambia dhahiri, 'Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.'"[14]
Utakatifu ni zaidi ya kulikiri jina la Mungu. Utakatifu ni haki ya ndani inayojidhihirisha katika tabia ya nje. Mungu anahitaji moyo mtakatifu na mioyo mitakatifu.
Kwa sasa, kama ilivyokuwa wakati wa Yeremia, Mungu anazungumza na wachungaji wanaojijengea majumba ya kifahari kutokana na sadaka za watu maskini. “Ole wake aijengaye nyumba yake kwa uovu. Na vyumba vyake kwa udhalimu.”[16]
Kwa sasa, kama ilivyokuwa wakati wa Amos, Mungu anazungumza na waimbaji makanisani ambao wanaishi katika maisha ya dhambi. “Niondoleeni kelele za nyimbo zenu; kwa maana sitaki kuzisikia sauti za vinanda vyenu.”[17]
Kwa sasa, kama ilivyokuwa wakati wa Mika, Mungu anazungumza na wafanyabiashara wanaojinadi wanaliitia Jina la Yesu lakini wanawadanganya wateja. “Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako.” [18]
Utakatifu ni zaidi ya taratibu za dini au taaluma. Leo, kama ilivyokuwa wakati wa manabii, Mungu hutazama tabia yenye haki na uadilifu.
[15]Sala kwa ajili ya Utakatifu “Bwana mwenye upendo, Nipe moyo imara uliotulia Nipe moyo usioweza kushindwa; Nipe moyo ulio mwadilifu. Nipe ufahamu wa kukuelewa wewe, Bidii ya kukutafuta wewe, na uaminifu wa kukukumbatia wewe.”
- Kutoka Thomas Aquinas
Moyo mtakatifu huonekana katika tabia ya uadilifu. Moyo mtakatifu huonekana katika mikono safi. Israeli isingeweza kujinasibu kwamba ni takatifu wakati inaishi maisha machafu yaliyokosa maadili na haki.
Kwa kuwa Mungu ni mwenye haki, watu wake ni lazima wawe na haki hiyo. Watu wa Mungu wanapaswa kuwa na tabia ya Mungu wao. Wale wanaoabudu miungu wanachukua tabia ya asili ya miungu yao; wale wanaomwabudu Yehova wanapaswa wachukue tabia ya asili ya Yehova. Kusudi la Mungu ni kutengeneza watu watakatifu wenye uadilifu na haki.
Isaya alielezea asili ya Mungu. “Bwana ametukuka; kwa maana anakaa juu; amejaza Sayuni hukumu na haki.”[1] Katika ujumbe huo huo, Isaya anamwelezea mtu mwenye haki na uadilifu anayeweza kuishi mbele za Mungu.
"Ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto ulao; ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto uteketezao milele? Ni yeye aendaye kwa haki, anenaye maneno ya adili; ni yeye anayedharau faida ipatikanayo kwa dhuluma; akung'utaye mikono yake asipokee rushwa; azibaye masikio yake asisikie habari za damu; afumbaye macho yake asitazame uovu."[2]
Ni mtu yule mwenye haki na tabia njema ya Mungu anayeweza kuishi mbele ya uwepo wa Mungu. Watu wa Mungu hutenda kama Mungu anavyotenda; wanaakisi asili ya Mungu mtakatifu.
Utakatifu ni Haki na Uadilifu wa ndani: Moyo
Haki na uadilifu. huanzia ndani ya moyo. Manabii walitambua vizuri sana kwamba kawaida za sheria zenyewe zilikuwa hazijitoshelezi. Utiifu wa nje pasipo haki na maadili ya ndani huo ni unafiki. Haki na uadilifu huanzia moyoni.
Israeli iliikataa sheria kwa sababu ilimkataa Mungu ambaye aliwapa hiyo sheria. Kukosa utiifu kunaanzia ndani ya moyo. Israeli ilivunja amri za Mungu kwa sababu “mioyo yao iliandama vinyago vyao.”[3] Mungu akaona kwamba mioyo yao ilikuwa ya hatia.[4]
Kutokutii kunaanzia ndani ya moyo; haki na maadili huanzia ndani ya moyo. Mungu alizungumza kupitia Isaya, “Nisikilizeni, ninyi mjuao haki, watu ambao mioyoni mwenu mna sheria yangu.”[5] Wanaoijua haki ni wale ambao sheria ya Mungu iko ndani ya mioyo yao.
Yeremia na Ezekieli waliingalia siku ambayo sheria ya Mungu ingesimikwa ndani ya mioyo ya watu wa Mungu.
"Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana; 'Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.'"[6]
"Nami nitawapa moyo mmoja, nami nitatia roho mpya ndani yao; nami nitauondoa moyo wa kijiwe katika miili yao, nami nitawapa moyo wa nyama; ili waende katika amri zangu, na kuyashika maagizo yangu, na kuyatenda; nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao."[7]
Haki na uadilifu huanzia ndani ya moyo. Yoeli aliwaita watu watubu siyo kwa muonekano wa nje tu. Kufunga na kulia kunapaswa kutoke ndani ya moyo wenye toba.
“Lakini hata sasa,” asema Bwana, “nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea; rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu.” Mkamrudie Bwana, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya.[8]
Muonekano wa nje tu hautoshi. Haki na uadilifu vinapaswa vianzie ndani ya moyo.
Utakatifu ni Haki na Maadili ya nje: Mikono
Katika Vitabu vya Manabii, tabia ya maadili ndiyo kijiti cha kupimia utakatifu. Utakatifu unahitaji tabia ya haki na mwenendo mzuri. Ufafanuzi rahisi sana katika Agano la Kale kuhusiana na maisha ya haki na uadilifu yanatoka katika kitabu cha Mika. Mika alifafanua mategemeo ya Mungu kwa watu wake.
"Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako?"[9]
Hii ndiyo inayomaanisha jinsi ya kuishi maisha ya haki na uadilifu: haki na rehema kwa watu, na unyenyekevu kwa Mungu. Katika Vitabu vya Manabii, haki, rehema na unyenyekevu hufafanua maisha ya haki na uadilifu.
Haki na Uadilifu ni Haki na Rehema kwa watu wengine
Baadhi ya watu wanataka kutenganisha moyo na mikono. Wanasema, “Moyo wangu ni mtakatifu, lakini mikono yangu ni ya uovu. Nampenda Mungu kwa moyo wangu wote, lakini siishi maisha ya uadilifu na haki.”
Vitabu vya Manabii havitoi mwanya kwa utengano huu. Moyo mtakatifu utaonekana kwa nje katika uadilifu na haki. Moyo msafi utasababisha matokeo ya tabia njema. Watu watakatifu wana mikono safi.
Zakaria anafafanua uadilifu na haki kama tabia iliyo safi kwa watu wengine.
"Bwana wa majeshi amesema hivi, ya kwamba, 'Fanyeni hukumu za kweli, kila mtu na amwonee ndugu yake rehema na huruma; tena msimdhulumu mjane, wala yatima, wala mgeni, wala maskini; wala mtu awaye yote miongoni mwenu asiwaze mabaya juu ya ndugu yake moyoni mwake.'"[10]
Amosi alihubiri kwa taifa ambalo lilikuwa limesahau uadilifu na haki. Israeli iligeuza “hukumu kuwa uchungu, na kuiangusha haki chini.” Nini suluhisho la uasi wa Israeli? “Hukumu na itelemke kama maji, na haki kama maji makuu.”[11]
Isaya aliishirikisha shauku ya Amosi ya maisha ya uadilifu na haki. Ujumbe wa kwanza wa Isaya kwa Yuda kuhusiana na maisha ya uadilifu na haki:
"Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane."[12]
Mungu alizungumza na Yeremia kuitaka Yuda irudi kwenye hukumu na haki:
"Bwana asema hivi, 'Fanyeni hukumu na haki, mkamtoe yeye aliyetekwa katika mikono ya mdhalimu; wala msiwatende mabaya mgeni, wala yatima, wala mjane, wala kuwadhulumu, wala msimwage damu ya mtu asiye na hatia katika mahali hapa.'"[13]
Kiwango cha Mungu kwa watu wake kilikuwa haki, uadilifu na rehema. Mungu aliwataka watu wake waishi maisha ya uadilifu na haki, watende kama Mungu anavyotenda.
Haki na Uadilifu ni Unyenyekevu kwa Mungu
Mungu huwaangalia watu ambao huwatendea watu wengine kwa haki na rehema; Hii ni lazima iwe msimamo wetu dhidi ya jirani zetu. Mungu anawatafuta watu ambao watatembea mbele yake kwa unyenyekevu; hii ni lazima iwe msimamo wetu na Mungu.
Yuda waliabudu miungu “juu ya mlima mrefu ulioinuka sana.” Mungu alijibu kwa kuwakumbusha Yuda kwamba yeye peke yake ndiye aliye juu sana mahali palipoinuka.
"Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; 'Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu.'"[14]
Tunamfikia Mungu aliye juu kupitia roho iliyopondeka na kuvunjika. Haki na uadilifu ni pamoja na unyenyekevu kwa Mungu. Huu ndio utakatifu wa kweli.
Hosea alihubiria taifa lililokuwa limeasi. Nabii alijua kabisa kwamba taifa lingeukataa ujumbe wake. Lakini pamoja na taifa kukataa kutubu, Hosea aliishia na mwaliko kwa kila Mwisraeli binafsi aliyekuwa anamtafuta Mungu. Ingawaje taifa linaweza likamkataa Mungu, mwenye uadilifu na haki bado anaweza kutembea katika njia za Mungu. Mungu atamheshimu mtu atakaye mheshimu yeye. Mungu ambariki mtu anayetembea katika uadilifu na haki.
"Ni nani aliye na hekima, naye atayafahamu mambo haya? Ni nani aliye na busara, naye atayajua? Kwa maana njia za Bwana zimenyoka, nao wenye haki."[15]
Utakatifu katika Utendaji: Maadili ya Maisha Matakatifu
Utakatifu unaanzia ndani ya moyo, lakini unaonekana kwa tabia za nje. Wakati wa kuliweka hekalu wakfu, Sulemani aliwapa watu changamoto, “Mioyo yenu na iwe kamili kwa Bwana, Mungu wetu, kuenenda katika sheria zake, na kuzishika amri zake, kama ilivyo leo.”[1] Utakatifu wa ndani huleta matokeo ya utakatifu wa nje; kama ni mtakatifu kwa ndani, utaishi kwa uadilifu na haki katika maisha ya nje.
Manabii walipinga mafundisho ya wale waliokuwa katika Israeli zamani wakifundisha kwamba watu wa Mungu walikuwa hawana ulazima wa kutii sheria za Mungu. Manabii wanapinga wale walioko katika kanisa la leo wanaofundisha kwamba Wakristo hawawezi kutimiza maagizo yote ya Mungu kwa ajili ya kuishi maisha matakatifu.
Wahubiri wengi wa leo wanafundisha, “Sheria za Mungu zinasema tuishi maisha ya uadilifu na haki, lakini anajua kwamba huwezi ukatimiza sheria zake.” Huo haukuwa ujumbe wa manabii. Manabii walisema, “Sheria ya Mungu inatutaka tuishi maisha ya uadilifu na haki; hivi ndivyo anavyotaka Mungu. Watu wa Mungu watatii amri za Mungu.”
Mfano kutoka Amri za Musa utaonyesha jinsi moyo mtakatifu unavyogusa maisha yetu ya kila siku. Mungu alisema, “Usimdhulumu jirani yako, wala kumnyang'anya mali yake; ijara yake aliyeajiriwa isikae kwako usiku kucha hata asubuhi.”[2] Katika ulimwengu wa zamani, mfanyakazi alikuwa analipwa kila mwisho wa siku. Hakukuwa na akaunti za hundi au kadi za mikopo. Malipo ya Jumatatu ndiyo ya kununulia chakula cha Jumanne. Kushindwa kumlipa mfanyakazi kila siku kuliwaletea changamoto ya kujinunulia chakula. Sheria ikasaema, “Mlipe mfanyakazi wako kila mwisho wa siku. Mfanya biashara mwenye uadilifu na haki atawatendea wafanyakazi wake kwa haki.”
Tumeona msisitizo juu ya maadili, haki na rehema kutoka kwa manabii. Katika Agano Jipya, Nyaraka za watu wote zinashirikisha ujumbe unaofanana. Hii inaonekana kwa uwazi sana katika Waraka wa Yakobo. Yakobo aliandika kwa wale waliokuwa wakijinadi kwamba ni watoto wa Mungu, lakini hawakuishi maisha ya haki na uadilifu. Anaonyesha kwamba utakatifu wa kweli unaonekana katika kuishi maisha ya haki na uadilifu.
Watu watakatifu wana zaidi ya kufanya kuliko wanaokiri utauwa; wanaishi maisha ya kimungu. “Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.”[3]
Watu watakatifu wanaonyesha huruma kwa yatima na wajane. “Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa.”[4]
Watu watakatifu hawana upendeleo kwa maskini au matajiri. “Bali mkiwapendelea watu, mwafanya dhambi na kuhukumiwa na sheria kuwa wakosaji.”[5]
Watu watakatifu wanatawala kunena kwao. “Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu.”[6]
Wafanya biashara watakatifu watawatendea wafanyakazi wao kwa uadilifu na haki. “Angalieni, ujira wa wakulima waliovuna mashamba yenu, ninyi mliozuia kwa hila, unapiga kelele, na vilio vyao waliovuna vimeingia masikioni mwa Bwana wa majeshi.”[7]
Utakatifu huleta mabadiliko katika kila eneo la maisha tunayoishi, ikijumuisha biashara na kazi zetu. Mtu mtakatifu ataishi kwa uadilifu na haki. Tukiwa watakatifu mbele za Mungu, tutafanya yaliyo sahihi kwa watu wengine. Ujumbe wa manabii na mitume uko wazi: Moyo mtakatifu hubadilisha matendo yetu. Watu watakatifu watakuwa wenye haki na uadilifu katika maeneo yote ya maisha yao. Kusudi la Mungu ni kuwafanya watu wawe waadilifu na wenye haki kwa pamoja katika mioyo na maisha yao ya kila siku.
Haki na uadilifu vinaonekanaje katika maisha yako ya kila siku? Utakatifu unaonekanaje katika mwingiliano wetu wa kila siku na dunia inayotuzunguka? Tuangalie mifano halisi. Mifano yote hii inatokana na watu waliojinasibu kwamba wao ni watakatifu. Majina yamebadilishwa, lakini kwa masikitiko historia zote ni za kweli.
Mchungaji Tom ni mjenzi. Kazi yake ya ujenzi huisaidia huduma yake ambayo yeye ni mchungaji katika kanisala Holiness. Tom alinunua chombo cha kujengea cha $100. Alikitumia kujengea nyumba yake na baadaye akawa hakihitaji tena. Alipokuwa tayari kuuza kile chombo alimwambia mnunuzi kwamba, “Kilipokuwa kipya, nilikinunua kwa bei ya $200. Sasa nitakiuza kwa bei ya $150.”
Mchungaji Tom anasema, “Hii ni biashara nzuri. Nilipata faida kwa kuikuza ile bei niliyonunulia. Hahitajiki mtu kujua. Hata hivyo, nitaitumia hiyo fedha kwa ajili ya kazi ya Mungu.” Mungu anasema, “Watu watakatifu ni waaminifu wanaposhughulika na biashara zao.” Paulo aliandika:
"Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake."[9]
Jane ni karani wa biashara. Wakati mchungaji wake alipomtembelea nyumbani, alisema, “Kama utahitaji vifaa kutoka ofisini kwangu, ninaweza kukupa. Huwa ninaleta kalamu za penseli, vifaa vya kuandikia, na vifaa vingine vya ofisi kutoka kazini kuja nyumbani. Hakuna mtu anayegundua.”
Jane anasema, “Hicho ni kitu kidogo sana.” Mungu anasema, “Watu watakatifu ni waaminifu hata kwenye vitu vidogo.” Paulo aliandika kwamba, “wale wote walioumbwa kwa mfano wa Mungu katika haki, uadilifu na utakatifu” wataishi kwenye njia nyingine nyeupe:
"Mwibaji asiibe tena; bali afadhali afanye juhudi, akitenda kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe, apate kuwa na kitu cha kumgawia mhitaji."[10]
Bill anaendesha biashara. Ni lazima aweke kumbukumbu na kulipa mapato kila mwisho wa mwaka. Mwaka jana, Bill alitengeneza faida ya $50,000 kutoka katika biashara yake, lakini alipokwenda kulipa mapato, alitoa taarifa ya kupata faida ya $40,000. Mara nyingine hutoa rushwa kwa maafisa wa serikali ili apate mikataba mizuri.
Bill anasema, “Ninajua ni namna gani biashara zinafanyika katika nchi yangu. Ni lazima ‘nitie mafuta kwenye magurudumu’ kwa ajili ya biashara yangu. Kando ya hayo, ninalipa zaka na kutumia fedha zangu kwa ajili ya madhumuni mengine.” Mungu anasema, “Watu watakatifu ni waaminifu wanapohusika na serikali yao.” Paulo aliandika kwa wenyeji wa Dola la Kirumi kwamba, “Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu.”[11]
Linda haifurahii kazi yake. Anataka autumie muda wake kwa kufanya kazi za kanisani. Badala yake, ana kazi ya kufanya usafi kwenye majumba ya watu matajiri. Analipwa mshahara kwa kufanya kazi kuanzia saa 8 asubuhi hadi saa 11 jioni, lakini mara nyingi hurejea amechelewa sana na huondoka alfajiri sana. Linda akamwambia mchungaji wake, “Ningependa niweze kutumia muda wangu asubuhi kwa kuomba na niende kazini nimechelewa. Ningependa nitoke mapema kazini ili nije kanisani jioni. Sijali kama nitafanya kazi katika masaa yote ninayolipwa kazini au laa.”
Linda anasema, “Tajiri yangu hawezi kujua kama sifanyi kazi masaa yote.” Mungu anasema, “Watu watakatifu ni waaminifu katika maadili ya kazi. Wanafanya kwa uzuri wote popote pale Mungu anapowaweka.” Paulo aliandika:
"Ninyi watumwa, watiini hao ambao kwa mwili ni bwana zenu, katika mambo yote, si kwa utumwa wa macho, kama wajipendekezao kwa wanadamu, bali kwa unyofu wa moyo, mkimcha Bwana. Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu, mkijua ya kuwa mtapokea kwa Bwana ujira wa urithi. Mnamtumikia Bwana Kristo."[12]
Arthur ni mmishenari. Anampenda Mungu na anafanya kazi kwa bidii sana, lakini ulimi wake ni mwepesi sana. Mara nyingi, watu wa karibu naye wamekuwa wakiumizwa na maneno yake makali.
Arthur anasema, “Ninasema kile ninachokifikiri! Inabidi unikubali jinsi nilivyo. Mungu anasema, “Watu watakatifu hutawala midomo yao.” Yakobo aliandika:
"Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu.… Kwa huo twamhimidi Mungu Baba yetu, na kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mfano wa Mungu. Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo."[13]
► Katika mila yako, ni maeneo gani yenye majaribu ya kimaadili kwa Waristo? Ni maeneo gani Wakristo wana majaribu mengi yanayoonyesha kukosa uaminifu katika maisha yao ya kila siku? Ni kwa jinsi gani ujumbe wa maisha ya utakatifu yanagusa haya maeneo ya majaribu?
[8]“Utakatifu inamaanisha msafi kabisa ninapotembea kwa miguu, msafi kabisa ninapoongea kwa ulimi wangu, msafi kabisa ninapotafakari kwa akili zangu – kila undani wa maisha chini ya uchunguzi wa Mungu.” - Oswald Chambers
Chiune Sugihara alikuwa Mkristo wa Japani akifanya kazi katika Wizara ya mambo ya Nchi za nje Manchuria. Mwaka 1939, alipelekwa Lithuania kuwa balozi wa Japani katika nchi hiyo. Akiwa kule alikutana na dada wa Kiyahudi na akapata kuelezwa jinsi serikali ya Wanazi ya Kijerumani ilivyokuwa inawatendea Wayahudi.
Sugihara aliwasiliana na serikali ya nchi yake akiomba ruhusa ya kuwapa visa wakimbizi wa Kiyahudi waliokuwa wanaikimbia Ujerumani na Poland. Serikali ya Japani ililikataa ombi la Sugihara.
Kwenye majira ya joto ya mwaka 1940, Sugihara alitambua kwamba alipaswa kudhihirisha haki na rehema. Alimwambia mke wake, “Sitaki kuacha kuwa mtiifu kwa serikali yangu, lakini siwezi kukosa utiifu kwa Mungu. Nitaifuata dhamira yangu.”
Sugihara alianza kutengeneza visa za kutoka za wakimbizi. Inakisiwa kwamba, aliweza kuokoa maisha ya zaidi ya Wayahudi 10,000 ambao walikuwa hatarini kuuawa na Hitla. Baadaye, Sugihara alikamatwa na jeshi la Warusi na akatumikia miezi kumi na nane katika jela za Urusi. Alipoachiwa kutoka jela na kurudishwa Japani, Wizara ya Mambo ya nchi za nje ilimfukuza kazi kwa sababu alikiuka maagizo yao.
Baada ya kuwa amefukuzwa kazi, Sugihara alikuwa hana njia nyingine ya kuishi. Alipata matatizo makubwa hata namna ya kuinunulia familia yake chakula. Wakati wazaliwa wa Kiyahudi aliowaokoa walipokuja kumtafuta baadaye, serikali ya Japai ilikanusha kwamba kamwe haijawahi kufanya kazi naye. Mwishowe, katika mwaka 1968, manusura mmoja wa Kiyahudi alimpata Sugihara na akampeleka Israeli.
Sugihara alitambuliwa kidogo sana na dunia kwa jinsi alivyojitoa sadaka, lakini alimtii Mungu kwa sababu alikuwa mwenye haki. Sugihara alitambua kwamba mtoto wa Mungu ni lazima aishi kwa uadiifu na haki. Hakuweza kuvumilia kuona mateso ya wale waliokuwa wanamzunguka. Alijua kwamba kuwa mwadilifu na mwenye haki ni lazima uweze kutenda haki, kupenda rehema na kutembea kwa unyenyekevu pamoja na Mungu. Chiune Sugihara aliishi maisha ya utakatifu.
[1]“Watu wote wa Mungu ni watu wa kawaida ambao wanafanywa kuwa siyo wa kawaida kwa ajili ya makusudi yaliyotengwa kwa ajili yao.”
- Oswald Chambers
Tafakuri ya Somo la 6
(1) Kuwa mtakatifu ni kuwa mwenye haki na uadilifu, kwa pamoja nje na ndani.
(2) Israeli iliruhusu ibada na taaluma kuwa badala ya uadilifu na haki.
(3) Bila maisha ya uadilifu na haki, kawaida za ibada na taaluma hazina maana yeyote.
(4) Haki na uadilifu ni lazima utoke ndani – lazima iwe ni utii kutoka moyoni.
(5) Haki na uadilifu lazima zionekane kwa nje – lazima ziweze kuleta mguso kwa wale walio karibu nasi.
(6) Manabii walifundisha kwamba Mungu anahitaji mambo matatu ya mtu mwenye haki na uadilifu:
Haki kwa watu wengine
Rehema kwa watu wengine
Unyenyekevu kwa Mungu
(7) Nyaraka za Agano Jipya zinajirudia-rudia katika ujumbe wake wa kuishi maisha ya haki na uadilifu. Mtu mtakatifu anapaswa aishi maisha yenye maadili na haki.
Kazi ya Kufanya
(1) Andika insha yenye kurasa 2-3 kuhusiana na “Haki na uadilifu katika dunia ya sasa.” Chukua eneo moja ambalo dhambi ya maadili imekubalika kama jambo la kawaida, na uoneshe Biblia inafundishaje katika eneo hili la dhambi. Toa maelekezo ya vitendo kwa ajili ya watu unaowahudumia.
(2) Anza kikao kinachofuata cha darasa kwa kunukuu Mika 6:8.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.