Fikiria kuhusu mazungumzo na Sauli, wa Tarso katika mwaka 34 B.K.[1] Uliza, “Je, wewe ni mtakatifu?” Sauli angejibu, “Ndiyo, mimi ni mtakatifu! Nilitahiriwa kwa mujibu wa sheria. Mimi ni Farisayo. Mimi ni mwenye kuishika sheria. Mimi ni mwenye haki.” Sauli alijiona kwamba yeye ni mwenye haki kwa sababu ya umakini wake katika kuitii sheria. Alijaribu kupata upendeleo wa Mungu kupitia matendo mema.
Lakini akiwa njiani kwenda Damaskasi, Sauli alikutana uso kwa uso na Bwana mfufuka. Alijifunza kwamba haki yake ni sawa na matambara machafu. Hakupingana na mwalimu ambaye siyo wa uongo, bali Masihi wa kweli. Ameshindwa kutii sheria iliyo kamilifu ya upendo kwa Mungu na jirani yake. Akiwa njiani kwenda Damaskasi, Sauli aliipata njia nyingine ya kumpeleka kwenye utakatifu: “…nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa Imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa Imani.”[2]
Tafakari kuhusu mazungumzo na Sauli, mwaka 60 B.K. “Paulo, sasa unajua kwamba njia pekee ya kupata haki ya kweli ni kwa Imaniiliyo katika Kristo. Je, hii haimaanishi kwamba unaweza kuwa mtakatifu? Je, Ina maana kwamba Kristo atakuhesabia mtakatifu hata kama wewe ni mtenda dhambi?”
Paulo angejibu kwa mshituko. “Hilo ni kosa! Haki inapatikana kwa Imani iliyo katika Kristo – lakini Mungu hatuachi sisi katika hali ya dhambi aliyotukuta nayo. Soma ushuhuda wangu. Lengo langu ni ‘ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake.’ Lengo langu ni kumfanania Kristo. Wokovu kwa Imani hautupi sisi kibali cha kuishi maisha ya dhambi; wokovu kwa Imani unatupa sisi nguvu ya kumfanania Kristo. Mungu wa upendo huwawezesha watoto wake kuishi maisha ya utakatifu kupitia Roho aliyeko ndani yetu!”[3]
► Fanya mapitio ya mambo ambayo umejifunza kuhusiana na utakatifu. Je, unayo taswira halisi ya uzuri wa utakatifu? Je,unaamini kwamba haya maisha ya utakatifu yameahidiwa kwa wana wa Mungu?
Katika kozi hii, tumeona wamba Mungu huwaagiza watu wake wawe watakatifu. Lakini watu wengi husoma maagizo ya Mungu kujibu kwamba, “Hilo haliwezekani. Siwezi nikawa mtakatifu.” Je, Wakristo wanapaswa kuishi maisha ya kushindwa kila siku na matumaini ya kuchanganyikiwa? Je, tushindwe kufurahia maisha ya utakatifu aliyotupa Mungu? Au je, tunaweza kufurahia kusudi kuu la Mungu kwa ajili ya watu wake?
Neno la Mungu linathibitisha kwamba Maisha ya Utakatifu yanawezekana
Kutokea wakati wa Henoko hadi kuongoka kwa mataifa wa Thesalonike, Biblia inafundisha kwamba maisha ya utakatifu yanawezekana.
Katika kitabu cha Walawi na kitabu cha 1 Petro, Mungu anaamrisha, “Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”[1] Hakuna mahali popote ambapo Mungu ametoa maagizo akaacha kutoa na maagizo ya utiifu. Mungu ni Baba wa upendo ambaye hawezi kuwachanganya watoto wake na maagizo yasiyowezekana. Wakati tukiwa hatuna uwezo wa kuyatii maagizo yake kwa nguvu zetu wenyewe, neema ya Mungu hutupa sisi nguvu za kutii maagizo ya Mungu.
Profesa Bill Ury anasema, “Amri au maagizo yanaonyesha picha ya Mungu ni nani na ahadi ya jinsi ambavyo tunaweza kuwa.”[2] Agizo hili kwamba, “Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu” inaonyesha kwamba Mungu ni nani; ni Mungu aliye mtakatifu. Agizo hili pia linaonyesha kwamba tunaweza kuwa; na tunaweza kuwa watakatifu.
Wakristo kwa wakati wote wa Historia wamedhihirisha kwamba Maisha ya Utakatifu yanawezekana
Wakristo katika kila kizazi wamegundua hilo kwamba maisha ya utakatifu ni upendeleo kwa watoto wa Mungu. Watu kutoka katika kila mfumo wa maisha wameiona furaha ya kukaa kwenye uwepo wa nguvu za Roho Mtakatifu. Wameiona amani inayopatikana kwa kumpenda Mungu kwa moyo usiogawanyika na kuwapenda jirani zao kama wanavyojipenda wenyewe.
Njaa ya Mungu kwetu ya Utakatifu inadhihirisha kwamba Maisha ya Utakatifu yanawezekana
Kila muamini anaona njaa ya ndani sana ya kutembea na Mungu. Wakristo wa kweli wanataka watembee kwa ukaribu sana na Baba yao. Wakristo wa kweli wanataka wawe kama alivyo Kristo. Mungu amepandikiza ndani ya mioyo ya watoto wake njaa ya kutaka mahusiano ya kina na yeye mwenyewe. Tunaweza kuwa na uhakikisho kwamba Mungu wa mbinguni wa upendo hawezi akaleta njaa bila ya kutoa njia ya kuimaliza njaa hiyo. Utakaifu ni upendeleo wa furaha kwa kila muamini.
Miaka mingi iliyopita, kulikuwa na mtu mmoja aliyewania kuivuka bahari kwa njia ya meli. Aliwekeza fedha zake kwa miaka mingi hadi zikafikia kununua tiketi. Baada ya kuwa ameilipia tiketi, alibakiwa na fedha kidogo. Alikuwa amesikia kuhusu vyakula vizuri vitamu vinavyopatikana ndani ya meli za baharini, lakini alijua pia kwamba vyakula hivyo vitakuwa ni vya gharama kubwa. Ili kuokoa fedha, mtu huyu alinunua mkate na siagi akaviweka kwenye mkoba wake wa safari.
Kila siku abiria walipokuwa wakiaenda kwenye chumba cha chakula, mtu huyu alikuwa anaingia chumbani mwake na kula mkate wake na siagi. Alikuwa na furaha kuwepo kwenye meli, lakini mara nyingi alikuwa akitamani kama angeweza kula vile vyakula vizuri vinavyopatikana kwenye kile chumba cha chakula. Kwenye siku ya mwisho ya safari, yule mtu aliamua angalao akale mlo mmoja kwenye kile chumba cha chakula. Alikusanya kila senti aliyokuwa amebakiwa nayo, akitegemea kwamba zitatosha kulipia mlo mmoja. Kwa mshangao wake, mhudumu aliuliza, “Wewe ulikuwa wapi? Tumekuwa tukikuandalia meza yako kwa wiki yote! Bei ya chakula imeingizwa kwenye bei ya tiketi yako. Bei ni tayari ilishalipwa.”[1]
Wakristo wengi wamefanana na huyu mtu maskini. Furaha ya maisha, amani ya kuishi kwa kujisalimisha kabisa kwa Mungu, na ushindi wa kuishi katika nguvu za Roho Mtakatifu – vyote vilishatolewa kupitia kifo cha Yesu pale msalabani. Kristo alilipa gharama zote, lakini tunaishi chini ya viwango vya fadhila hizo.
Kama moyo mtakatifu utapatikana kwa kila mwamini, ni kwa nini Mkristo ashindwa kufurahia fadhila hizi? Mara nyingi tumekuwa tukimruhusu Shetani kutudanganya katika kuyaelewa mafundisho ya Biblia. Uongo wa Shetani umetuondoa katika kufurahia fadhila za Mungu alizozikusudia kwa ajili ya watoto wake.
“Moyo wa Utakatifu Hauwezekani”
Wakristo wengi wanafikiri kwamba moyo wa utakatifu hauwezekani. Wanasoma maagizo na ahadi katika Maandiko, lakini wanafikiri kwamba, “Hiyo ilikuwa ni sawa kwa Ibrahimu, lakini kamwe siwezi kuwa ‘rafiki wa Mungu.’”
Baadhi ya wale wanaosema, “Moyo wa utakatifu hauwezekani” wanazungumza kutoka kwenye uzoefu mchungu sana. Wamejaribu kuishi maisha ya utakatifu – lakini wameshindwa. Inawezekana walifuata sheria za nje zilizoambatana na utakatifu; Inawezekana wamejaribu kutawala tabia za dhambi na matendo yanayoharibu nidhamu binafsi; inawezekana hata wametoa ushuhuda wa moyo safi. Kwa sasa, wameamua kwamba haiwezekani “kuwa mtakatifu kama Bwana wetu alivyo mtakatifu.”
Tafakari juu ya mtu anayejaribu kujifunza lugha za ndege. Anafanya majaribio hadi atakapoweza kutoa mlio unaofanana na kasuku. Amekuwa mzuri kiasi kwamba jirani atadhania ni mlio wa kasuku. Lakini huyu mtu siyo ndege! Anaweza akaigiza sauti zao, lakini hajui sauti hizo zinamaanisha nini. Ana uwezo uwezo wa kuigiza sauti, lakini hajui ndege anakuwa anajisikiaje anapotoa mlio wake wa sauti. Mtu huyu ana matendo ya nje; hana uhalisia wa kweli wa ndani.
Wakristo wengi wamejifunza lugha na hata matendo ya mtu mtakatifu. Wanayasema maneno, lakini hayana uzoefu ndani ya mioyo yao. Wamefanya matendo ya nje kuwa mbadala wa uhalisia wa mambo ya ndani. Kwa muda mfupi sana huwaongoza kwenye kukataa tamaa na kuchanganyikiwa.
Ni nini jibu la uongo wa Shetani kwamba, “Moyo wa utakatifu hauwezekani”? Tunapaswa tuwe na Imani katika ahadi za Mungu. Tunapaswa kuamini kwamba Mungu wetu wa upendo atatupa nguvu za kuweza kutii maagizo yake.
Ndiyo, wewe na mimi ni viumbe tuliotengwa ambao kamwe hatuwezi kufikia kiwango cha ukamilifu wa Mungu. Lakini Mungu alituagiza, “Iweni watakatifu.” Mbali na asili yetu ya anguko, tunaweza kumwamini Mungu wetu mwema kutupa neema na nguvu vitakavyotuwezesha kuyatii maagizo yake.
“Sina Njaa ya Moyo wa Utakatifu”
Kwa masikitiko, wako watu wanaodai kwamba wao ni Wakristo lakini kabisa hawana njaa ya utakatifu. Wanadai kuwa Wakristo, lakini wana nia kidogo sana au hawana kabisa nia ya kukua katika mfano wa Kristo.
Jimmy anajishuhudia kwamba yeye ni Mkristo, lakini anaonyesha ana shauku kidogo sana na maisha ya utakatifu. Anaendelea kufanya dhambi za kujitakia; anaishi kama vile alivyokuwa mwanzoni kabla hajamkiri Kristo. Tulipomtembelea, Jimmy alitaja baadhi ya watu ambao walikuwa makini na waangalifu katika maisha wanayoishi. Tabia zao zilikuwa za upendo; matendo yao yanaonyesha nia ya kutaka kumpedezesha Mungu. Walikuwa na mioyo na mikono ya utakatifu.
Jimmy alitoa maoni yake kuhusu njaa yao ya kuutaka utakatifu kisha akasema, “Sijali kuhusu kuwa mtakatifu. Mchungaji wangu aliniambia kwamba, kama nilishatubu dhambi zangu, na kumwamini Yesu kama Mwokozi wangu, nitaenda mbinguni. Kwenda mbinguni ndicho kitu ninachojali tu. Sihitaji kitu kingine zaidi ya hicho!”
Tatizo la Jimmy ni nini? Hana njaa ya utakatifu. Sina shaka kwamba Jimmy ana uelewa mdogo sana kuhusu ni nini maana ya kuwa Mkristo. Mtu yeyote aliyezaliwa mara ya pili atapenda sana kumfanania Kristo. Mkristo wa kweli anapaswa awe na njaa ya moyo wa utakatifu.
Jibu ni nini kama wewe huna njaa ya moyo wa utakatifu? Inawezekana ni kweli umezaliwa mara ya pili, lakini umekuwa ukisumbuliwa na tabia na mazoea ya nyuma, umejichanganya na wanafiki wanaojidai kwamba wao ni watakatifu, au hujawahi kukutana na fundisho la moyo wa utakatifu katika Maandiko. Kama ndivyo, msihi Mungu akupe njaa ya moyo wa utakatifu.
“Mimi ni Mtakatifu wa Kutosha”
Labda uongo wa hatari zaidi tunaoweza kujiambia wenyewe ni, “Mimi ni mtakatifu wa kutosha.” Watu wengine wanajiaminisha kwamba wao ni watakatifu kwa sababu ya jinsi wanavyovaa, ushiriki wao katika kanisa, au wawapo na “karama ya kiroho.” Ninapojiridhisha mimi mwenyewe katika hayo kwamba, “Mimi ni mtakatifu wa kutosha,” hakuna ongezeko lingine tena la kukua katika utakatifu.
Alama isiyoweza kukosewa ya kumtambua mtu mtakatifu ni hamu yake ya kutaka kukua katika utakatifu. Sijawahi kuona mfano wowote au mahali popote katika Maandiko au historia ya Kanisa ya mtu mtakatifu anayesema, “Mimi ni mtakatifu wa kutosha.” Jinsi mtu anavyozidi kukua katika kumfanania Kristo, kwa kiwango hicho hicho anazidi kuwa na njaa ya kukua zaidi.
Mwanamume au mwanamke anayetembea karibu na Mungu husema, “Nina furaha katika kutembea kwangu na Mungu, lakini nataka niendelee kutembea naye karibu zaidi!” Mtu mtakatifu hufurahia kuwa na ushirika na Mungu, lakini hutafuta hata na zaidi jinsi ya kuwa na uhusiano wa ndani kabisa na Mungu. Anafurahia anavyozidi kukua katika kumfanania Kristo, lakini pia huomba kwamba Mungu aendelee kumfanya afanane zaidi na Kristo.
Jibu ni nini kwa ukiri dhaifu wa utakatifu? Kama umejidanganya mwenyewe kwa kujiridhisha, jibu ni udhalilishaji mbele ya utakatifu wa Mungu aliye mkamilifu. Kama utauangalia utakatifu wake mkamilifu, kamwe hutakaa uridhike na ukiri dhaifu wa utakatifu. Wakati Isaya “alimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana,” alitambua hitaji lake binafsi la utakatifu:
"Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana wa majeshi!"[2]
Wakati Isaya alipouona utukufu kamili wa Mungu, alitambua uhitaji wake binafsi wa utakaso. Tiba ya ukiri dhaifu wa utakatifu ni kuwa na uelewa wa kina kuhusu Mungu. Tunapomwona Mungu, tunajiongezea njaa ya kuwa na moyo wa utakatifu. Tunapozidi kumwona Mungu, ndio vivyo hivyo tunavyozidi kuwa na hamu ya kutaka kuwa kama yeye.
[1] Kisa hiki kimechukuliwa kutokakitabu cha John N. Oswalt, Called to be Holy (Nappanee: Evangel Publishing, 1999), 149-150
Ni kwa jinsi gani tunaweza kufanywa kuwa kama Kristo? Unawezaje, wewe kama mwamini mwenye hamu ya kujazwa na utimilifu wote wa Mungu, karama hii ya ajabu? Njia ya kuelekea kwenye moyo wa utakatifu ni ipi?
Hatuhitajiki kupambana sana katika kutafuta njia ya kuuelekea utakatifu. Neno la Mungu latosha kuonyesha njia ya kuelekea maisha ya utakatifu.
Utakaso wa Awali
Kuanzia tu unapozaliwa upya, Roho Mtakatifu amekuwa akiishi ndani yako.[1] Kwa papo hapo, ulihama kutoka gizani na kuingia kwenye nuru. Kuanzia hapo, Agano Jipya linakutambua kama “Mtakatifu.”
Ingawaje unaweza ukapambana na majaribu, Roho Mtakatifu anakupa ushindi wa kila siku dhidi ya dhambi za makusudi. Watu wanaokuzunguka wameona mabadiliko yako kwa jinsi unavyoishi katika maisha mapya ndani ya Kristo. Furahi kwa kile Mungu alichofanya!
Kukua katika Utakaso
Kwa jinsi unavyokuwa unamfuata Kristo, Roho Mtakatifu anabadilisha roho yako ya ndani. Jinsi “unavyoenenda kwa Roho,” wala “hautazitimiza kamwe tamaa za mwili.”[2] Majaribu ya zamani yanasalimu amri juu yako. Utiifu kwa Mungu unakuletea furaha isiyoisha.
Hata hivyo, utakutana na maeneo ya kupambana. Unamtii Mungu, lakini wakati mwingine kuna mapambano kati ya maagizo ya Mungu na matamanio yako ya ndani. Kuna mapambano kati ya kile ambacho Mungu amekuamuru na mapenzi yako ya ubinafsi. Utaona vigumu sana kumpenda Mungu kabisa na kumpenda jirani yako. Unaanza kujitambua kwamba una “moyo uliogawanyika.”
Usafi wa Moyo
Jinsi Mungu anavyodhihirisha maeneo ambayo unayahitaji kwa ajili ya kujiweka msafi kwa kina zaidi, utaanza kusikia njaa ya ahadi iliyoko katika kitabu cha 1 Wathesalonike 5:23. Utatafuta kujua ukweli wa maombi ya Paulo, “Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa.” Utaanza kumwuliza Mungu, “Je, kunalo jambo la zaidi unalotaka kunifanyia katika maisha yangu? Je, naweza kufanywa kuwa msafi? Je, matamanio yangu ya ndani yanaweza kubadilishwa upya hadi kwenye kiwango ambacho sitaweza kupambana tena katika kukutii wewe kabisa?”
Wakristo kwa nyakati zote za historia wameomba sana Mungu awape moyo ulio msafi. Kulingana na 1 Wathesalonike 5:23, wako wachache waliotumia jina “utakaso wote” kwa ajili ya uzoefu huu.[3] Wengine wameuita “maisha ya kina zaidi.” John Wesley alitumia jina “upendo kamili.” Bila kujali maneno yaliyotumika hapa, hii ni kiu ya asili ya mtoto wa Mungu anayetaka kukua katika kumfanania Kristo.
Unapokuwa unaomba kwa ajili ya usafi huu wa ndani sana, unawea kukutana na maeneo matatu ambayo Mungu atakuongoza. Hii siyo hukumu kama ile uliyokuwa unajisikia kama mtu asiyeamini; wewe sasa ni mtoto wa Mungu! Badala yake, haya ni maeneo ambayo Mungu anakuitia kwa ajili ya moyo wa utakatifu.
Mungu atakuita kwa ajili ya utiifu wote
Baadhi ya waumini wanapambana kutafuta moyo wa utakatifu kwa sababu bado wanapambana na maeneo mengine ya ukosefu wa utiifu. Hatuwezi kutembea kwenye mahusiano ya karibu na Mungu isipokuwa tumetembea katika utiifu.
Hakuna Mkristo wa kweli anayeishi katika uasi wa kujitakia kinyume na maamrisho ya Mungu. Hata hivyo, Wakristo wengi wamepata upenyo wa kusamehe au kuacha (hata kwa ajili yao wenyewe) maeneo mengine ya uzembe. Hawatakaa waseme, “Mungu, sitakutii wewe,” lakini husema, “Mungu, sidhani kama hili ni muhimu sana kulitilia maanani.” Kwa kutojali, wanadharau maeneo mengine ambayo wangepaswa kuwa watiifu. Kama tunahitaji kuwa watu watakatifu ambao Mungu anawaita watu wake, ni lazima tumtii Mungu katika kila eneo.
Kama watu tulioanguka, tunajidanganya hata wenyewe kuhusu kina cha uovu wetu. Kwa sababu ya hii, mtunga Zaburi aliomba:
"Ee Mungu, unichunguze, uujue moyo wangu, Unijaribu, uyajue mawazo yangu; Uone kama iko njia iletayo majuto ndani yangu, Ukaniongoze katika njia ya milele!"[4]
Mtunga Zaburi aliomba kwamba Mungu amchunguze na aujue moyo wake. Alijua kwamba hatuna uwezo wa kuyajua yote yaliyomo katika mioyo yetu wenyewe. Lakini kwa jinsi tunavyoendelea kutafuta “kujazwa na utimilifu wote wa Mungu,” tutaomba kwamba Mungu atufunulie kila njia inayohusika na asili yetu ya dhambi.
Daudi aliomba, “Unitakase na mambo ya siri.”[5] Alijua kwamba tunaweza kuficha ukweli wa dhambi zetu hata kutoka ndani yetu sisi wenyewe. Ni Mungu peke yake anayeweza kuangazia mwanga ndani ya mioyo yetu kwa ajili ya dhambi za siri zilizojificha humo.
Unapotafuta kuwa na moyo msafi, utaona kwamba Mungu atakufunulia maeneo ambayo tabia zako na matendo yako haziakisi sura yake. Kwa kuwa unataka umfananie Kristo, kwa hiari yako mwenyewe utayakiri maeneo haya na kutii wito wa Mungu wa kuwa mtiifu kabisa.
Mungu atakuita uusalimishe moyo wako
Unapotafuta kuwa na moyo safi, Mungu atakuita usalimishe kila kipengele cha maisha yako. Hii ni zaidi ya kusema “Hapana” kwa majaribu kutoka nje. Hii ni kujitakasa kamili kwako mwenyewe kwa ajili ya Mungu. Ni kujisalimisha mapenzi yako kwa ajili ya mapenzi ya Mungu.
Paulo aliwaita Wakristo pale Roma kujitoa wenyewe miili yao “iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu.”[6] Hawa walikuwa ni Wakristo waliokuwa wakiishi kwa kumtii Mungu, lakini Paulo aliwaita kwenye kujisalimisha kabisa kwa Mungu. Paulo aliwaita kwa kusudi la kusema “ndiyo ya milele” kwa Mungu. Aliwaita wajisalimishe kabisa.
Oswald Chambers alionyesha umuhimu wa kujisalimisha kabisa kwa ajii ya kusudi la Mungu.
"Ili kuwa pamoja na Yesu Kristo, mtu hatapaswa tu kuachana na dhambi, lakini pia atapaswa asalimishe mfumo wake wote wa jinsi anavyoyatazama mambo. Kuzaliwa upya na Roho wa Mungu inamaanisha kwamba ni lazima kwanza tuachilie mambo mengine ili kuingiza vitu vingine…."
"Kwenye kila hatua ya utaratibu huu, tutapaswa tuachane na malalamiko yetu kwa ajili ya haki zetu wenyewe. Je, tuko tayari kusalimisha ufahamu wetu katika vile vyote tunavyovimiliki, matamanio yetu, na kitu kingine chochote katika maisha yetu? Je, tuko tayari kutambuliwa na kifo cha Yesu Kristo?"
"…Amua kusonga mbele katikati ya mgogoro, ukisalimisha vyote ulivyo navyo na wewe mwenyewe jinsi ulivyo kwake. Na Mungu atakuwezesha wewe kufanya yale yote anayotaka kutoka kwako."[7]
George Matheson alikuwa mchungaji Mskoti wa kanisa la Presibiteri aliyejitambua kwamba ndani ya moyo wake kulikuwa na upinzani mkubwa dhidi ya mapenzi ya Mungu. Alikuwa na njaa ya moyo usiogawanyika ambao ungejitoa kwa hiari kabisa kwa Mungu. Aliomba maombi haya kwa ajili ya kujisalimisha:
Matheson alitambua kwamba katika kujisalimisha kabisa, tunapata ushindi. Tunapojitoa wenyewe kama mateka kwa Mungu, anatuweka huru kutoka katika vifungo na dhambi. Tunapokuwa wadhaifu, anatujaza nguvu. Tunaupata ushindi wetu mkuu tunapofikia kwenye hatua ya kujisalimisha kabisa kwa Mungu.
Mungu atakuita umtii yeye kwa Imani
Kama umejisalimisha kabisa kwa Mungu, unaweza kumwamini yeye katika “kukusafisha moyo kwa Imani.”[9] Tunafanywa watakatifu kwa neema kupitia Imani.
Kama mwenye dhambi, ulikuja kwa Kristo ukiwa huna chochote. Ukajitupa mwenyewe kwenye neema yake. Kwa Imani, ukakubaliana na wokovu wake wa bure, na akakufanya kuwa kiumbe kipya.
Kwa njia hiyo hiyo, utakapokuwa na njaa ya moyo wa utakatifu, ni lazima uende kwa Yesu kwa Imani. Mungu aliyekuita wewe katika utakatifu atakufanya uwe mtakatifu. Unaweza ukaamini kwamba ahadi yake ni kwa ajili yako. Maombi ya Paulo, “Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa.” Inaweza kuwa kweli katika maisha yako. Unaweza ukasadiki ahadi za Mungu. “Yeye ni mwaminifu ambaye awaita, naye atafanya.”[10]
Isaya 6 – Kisa cha Kutakaswa
“Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu,” malaika walikuwa wakisema, wakati huo Isaya akiwa anatetemeka! Isaya alihitaji kujiona mwenyewe kama “mchafu” kabla ya Mungu mtakatifu kumwamini kwa ajili ya roho ya taifa.
Isaya alipojiangalia moyo wake mwenyewe, alisema kwa sauti, “Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu.” Aliona undani wa asili yake ya dhambi. Lakini Mungu hakumwacha katika hali hii ya kutisha.
"Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu; akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, 'Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa.'"
Utakaso mara nyingi huwa mchungu. Je, waweza kusikia nyama inayoungua wakati malaika akigusa kinywa cha Isaya kwa kaa la moto? Hii haikuwa neema rahisi; utakaso haupiti bure bila maumivu.
Hata hivyo, kisa hiki kinafundisha ukweli wa ajabu na unaotia moyo. Tukimruhusu, Mungu atatufanya watakatifu. Kusudi la Mungu halikuwa kwa ajili ya kumtesa Isaya. Kusudi la Mungu lilikuwa ni kumtakasa Isaya. Kusudi la Mungu kwa watu wake linaweza likatimia. Tunaweza kufanywa wasafi.
Ukuaji Endelevu katika Utakatifu
Paulo aliomba, “Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa.” Kisha akaendelea, “nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.”[11] Kukua kwako katika kumfanania Kristo kutaendelea hadi wakati wa “kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.” Utakapokuwa unaendelea kutembea na Mungu, kama vile katika kioo, utabadilishwa ufanane na mfano wa Mungu.[12] Utakomaa katika utakatifu. Utaendelea kujisalimisha kwa furaha kwenye mapenzi ya Mungu. Utakuwa unaendelea kutembea na kujisalimisha kwa uangalifu kwa Mungu.
Jaribu kufikiri juu ya siku yako ya harusi. Kwenye hiyo ndoa, ulitoa ahadi ya maisha. Hujawahi kujiuliza kila asubuhi, “Je, leo nimeoa? Je, agano la ndoa bado linafanya kazi?” Ulifanya tendo la kudumu. Njia pekee unayoweza kuvunja hilo agano ni kugeuka nyuma na kwenda kinyume na nadhiri ulizofanya wakati wa ndoa yako.
Kila siku ya ndoa yako, unaishi kutokana na maagano uliyoahidi kwenye ndoa yako. Unapokabiliwa na kufanya maamuzi, unachagua kufanya kwa upendo kuelekea mwenzi wako. Ile ahadi ya kudumu uliyokiri unaiishi katika maisha ya kila siku.
Hali kadhalika, kujisalimisha kwako kwa Mungu ni tendo la kudumu. Huhitaji kujiuliza kila siku, “Hivi bado nimejisalimisha kwa Mungu hadi sasa?” Badala yake, kila siku unaishi kutokana na ahadi yako uliyofanya wakati ulipojisalimisha kabisa kwa Mungu.
Mhubiri maarufu Mskoti, Horatius Bonar, aliandika kuhusu kuendelea kukua kwa mtu mtakatifu.
"Maisha ya utakatifu yanatokana na wingi wa mambo madogo madogo. Maneno machache, siyo hotuba ndefu au mahubiri marefu; matendo machache, siyo miujiza, siyo mapigano, au tendo moja la kishujaa au kuifia dini kunakofanya maisha ya Ukristo yawe ya kweli. Ni mambo madogo madogo ambayo kwayo maisha hukamilishwa."[13]
Haya ndio maisha ya kila siku ya utakatifu. Unaishi maisha ya utakatifu ambayo siyo kwa ajili yako mwenyewe, bali ni katika utimilifu wa Roho Mtakatifu. Maisha ya utakatifu ni kuhusu mahusiano ya upendo usiogawanyika pamoja na Mungu. Ni kuwa na shauku kwa ajili yake. Ni kumtaka yeye awe juu ya mambo yote. Matamanio haya yatakuongoza wewe kuingia katika mahusiano endelevu ya ndani sana na Mungu.
Katika historia ya mwanadamu, mtu amejaribu kuishi bila kumtegemea Mungu. Shetani alimjaribu Hawa kwa ahadi kwamba, “Mtakuwa kama Mungu.”[14] Katika Babeli, watu waliamua, “na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina.”[15] Katika hali yake ya ubinafsi, mtu anataka aishi maisha ya bila kumtegemea Mungu. Kwa ulinganifu, maisha ya utakatifu ni ya kuishi kwa kumtegemea Mungu kabisa.
Utakatifu ni wa Mungu; wewe na mimi ni watakatifu tu pale tunapoendelea kuishi kwenye mahusiano na yeye. Kamwe hautakaa ufikie kiwango cha kusema kwamba, “Mimi ni mtakatifu kwa nguvu zangu mwenyewe.” Badala yake unapaswa kusema, “Leo, Roho Mtakatifu ananiwezesha nguvu za kuishi maisha ya utakatifu. Leo, ninabadilishwa katika sura yake. Leo, ninamtii Mungu kwa moyo ambao unampenda yeye kabisa. Leo, ninampenda jirani yangu kwa neema ya Mungu. Leo, Roho Mtakatifu ananifanya niwe kile ambacho Mungu alitaka niwe wakati aliponiita.” Haya ndiyo maisha ya utakatifu.
[3] “utakaso wote” ni maana nyingine ya neno “mkamilifu” neno lililotumika katika 1 Wathesalonike 5:23. Haina maana ya “ukuaji mkamilifu;” ina maana ya usafi uliokamilika na utakaso.
[16]“Mgogoro mkubwa uliopo kwenye maisha ya Kikristo ni kusalimisha kabisa mapenzi yetu.”
- Oswald Chambers
Mambo Kumi ya Vitendo ya Kupalilia Maisha ya Kila Siku ya Utakatifu
Maisha thabiti yenye matunda ya utakatifu yanahitaji kipindi katika maisha cha kuyapalilia na kuyatunza.[1] Kutakaswa kwa moyo siyo mwisho wetu wa kufuatilia utakatifu. Sisi ni sawasawa na marubani ambao tumeiweka ndege yetu kwenye usawa wa barabara ya kurukia ndege, lakini tunahitaji kufanya masahihisho mengi kabla ya ndege kutua.
Kifo cha kiroho kwa Wakristo hadi nafsi ni kifo kilicho hai – kufa mara kwa mara. Dhabihu yetu ya nafsi ni dhabihu iliyo hai – dhabihu ya mara kwa mara. Maneno kama “kifo cha nafsi” yapo tu kwa ajili ya kutufundisha kweli za kiroho lakini tunapaswa kuwa waangalifu tusitoke nje ya Neno la Mungu. Kuwa na moyo msafi siyo mwisho wetu wa kuutafuta utakatifu. Moyo msafi na mapenzi binafsi yaliyosalimishwa vinatuwezesha sisi kusonga mbele, lakini tunao muda katika maisha wa kupanda kileleni!
Maisha yaliyojazwa Roho Mtakatifu ni maisha ya kukua na utakaso endelevu. Kwa msaada wa Roho wa Mungu “tunabadilishwa toka utukufu hata utukufu.”[2] Ufuatao hapa ni ushauri wa vitendo kwa wale wote walio na matamanio ya kuwa na maisha ya ndani kabisa ya utakatifu.[3]
(1) Endelea kubakia uliyepondeka kiroho.
Maisha ya kweli ya utakatatifu ni yale yenye toba ya mara kwa mara,[4] wakati Mungu akiendelea kutuponya madhaifu yetu na kuturejesha kwenye tabia kamili ya mfano wa Kristo. Njia ya kuhifadhi kicheko cha Mungu katika maisha yetu ni kukiri kwa haraka makosa yetu na kutembea kwenye nuru ambayo Mungu ameiweka kwenye njia yetu. [5]
(2) Kukubali kuonywa na Mungu.
Mwandishi wa kitabu cha Waebrania anaweka wazi kwamba kukubali kupokea kuliko kuyapuuzia maonyo ya Baba yetu wa mbinguni kutatuwezesha “tuushiriki utakatifu wake.”[6] Hakuna mtu yeyote anayefurahia kukemewa na Mungu, hasa kwa sababu inatokea mara nyingi kwa watu wa kawaida ambao wana matatizo yao ya kushughulikiwa. Kila mmoja wetu ana tabia ya kupuuzia marekebisho machungu hasa inapotokea kwa mwanandoa aliyekosa au viongozi wa kiroho wanaowekwa na Mungu kwenye nafasi za mamlaka juu yetu wanapotenda yasiyofaa. Lakini nidhamu ni mojawapo ya chombo kikuu sana cha Mungu cha kubomoa kabisa maeneo yetu mabovu na kuturejesha tena ndani ya mfano wa Kristo.
Kama itatokea tumefikia mahali ambapo hatuwezi tena kupokea masahihisho, hata kutoka kwa watu ambao kiroho bado ni wachanga, tutakuwa tumeuacha msingi wa njia sahihi ya utakatifu.
(3) Jikabidhi wewe mwenyewe kila siku kama dhabihu kwa Mungu.
Paulo anatukumbusha kwamba tunapaswa kukabidhi miili yetu, pamoja na hamu na tamaa zake zote kwa Mungu kama, “dhabihu iliyo hai.”[7] Miili yetu ambayo hapo mwanzo ilikuwa “silaha za dhuluma kwa dhambi”[8] inabadilishwa kwa neema ya Mungu kuwa “silaha za haki.”
Paulo anaonyesha hii hatua endelevu ya kujitoa kwa Mungu kama ishara ya alama ya maisha ya Kikristo. Alisema, “Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.” Kisha akaendelea kwa kutoa maagizo, “Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi.”[9] Fanya haya, na utakuwa na uzoefu wa kuzidi na zaidi wa vipimo vya neema ya Mungu.
(4) Yatafakari Maandiko kila siku.
Kutakaswa, na tabia inayomfanania Kristo siyo matokeo ya muda mfupi, bali ni matokeo ya kuwa na muda katika maisha ya kutafakari na utiifu kwa Neno la Mungu. Yesu aliwaambia wanafunzi wake kwamba walifanywa wasafi kupitia Neno. “Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia.”[10] Kisha Yesu akaomba kwamba waendelee kuwa watakatifu kupitia Neno. “Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.”[11] Mungu hukamilisha kazi yake ya kututakasa na kutufanya wasafi tunapolitafakari Neno lake mara kwa mara an kulitii.
(5) Kujivalisha mwenyewe kwa Yesu kila siku.
Maisha ya utakatifu yanapatikana kwa kujivalisha wenyewe kwa uangalifu tabia na fadhila za Kristo. “Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo....”[12] Neno “mvaeni” linamaanisha kufikiri kama Yesu, kuiga roho yake, na kuishi kama yeye. Waamini wanapaswa kila siku wachague kuwa kama Yesu katika upendo wake mtakatifu, furaha, amani, msamaha, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi.
(6) Msiuangalie mwili hata kuwasha tamaa zake.
Baada ya kuwa tumemvaa Yesu tunapaswa kuwa waangalifu sana, “msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake.”[13] Je, inawezekana tamaa binafsi zikajitokeza nyuma ya mtu ambaye ana moyo uliojazwa Roho Mtakatifu? Kama ingekuwa haiwezekani, Paulo hangetoa angalizo hilo. Kwa muda wote ambao sisi tunaishi, ni lazima tuchague unyenyekevu. Kila mume au mke anayeongozwa na Roho, ameshajifunza kwamba utauwa unaimarishwa tu kwa kuupalilia kwa uangalifu, umakini wa mara kwa mara, na maombi ya ulinzi. Kama mwili hautaendelea kubakia umesulubishwa, utainuka na kusababisha anguko kubwa la kiroho, mfano wa baba mmoja wa Kiafrika aliyefuga mbwa, akashindwa kuwazuia wasimng’ate miguuni kwa sababu alikuwa anawatembelea mbwa wake akiwa ameweka nyama yao mfukoni!
(7) Isitawishe akili yako kila siku.
Akili yako ndio kituo kikuu cha maamrisho cha maisha yako na siri ya mabadiliko yake. “Maana aonavyo mtu nafsini mwake, ndivyo alivyo.”[14] Akili yako ina mamlaka juu ya maisha yako kwamba utafanyika kuwa kile ambacho umechagua akili yako ikifanye. Paulo alifundisha, “Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”[15]
(8) Vaeni silaha zote za Mungu.
Mpango mkamilifu wa Mungu kwa kila mwamini ni kwamba “mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.”[16] Tunafanya haya kwa kuvaa silaha zote za Mungu – ukweli, haki, utayari, Imani, uhakika wa wokovu, na Neno la Mungu. Vaa silaha zako kwa sababu peke yetu tu, hatuna uwezo dhidi ya adui yetu!
(9) Endelea kuukuza ufahamu wako juu ya Roho Mtakatifu.
Kama unataka kuwa mtakatifu, unapaswa kumwalika Roho Mtakatifu kujaza na kusafisha kila chumba cha maisha yako: sebule yako (chumba ambacho maisha ya kijamii na burudani hufanyikia), chumba cha kulala (chumba chako cha kimaadili na ngono), jiko lako (Chumba chako cha hamu na matamanio), na ofisi yako (chumba chako cha maamuzi ya fedha na kazi mbalimbali). Mara nyingi tunapambana kuwa watakatifu kwa sababu tunashindwa kukuza wakati kwa wakati ufahamu wetu juu ya Roho Mtakatifu na kuuliza kwa dhati “ahadi ya Baba,” ambayo Yesu anayo furaha ya kutoa. Inawezekana hofu ni sehemu ya sababu ya kusita kwetu kuuliza. Hatuhitajiki kuwa na mashaka. Yesu alitoa ahadi hii ya ajabu sana: “Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?”[17]
(10) Ishi kwa neema.
Yesu alisema, “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.”[18] Tumefanywa watakatifu kwa sababu sisi ni mali ya mzabibu. Ni mzabibu ambao unazaa matunda. Tunazaa matunda zaidi na zaidi siyo kwa kujaribu kuwa wazuri bali ni kwa kumng’ang’ania Yesu.
Wakristo wengi wamekuwa wakiumizwa na wasiwasi mkubwa kuhusiana na kutembea kwao na Mungu. Wengine, ambao wamefundishwa kufanya utafiti wa kina wa nafsi, wamekuwa wakijichunguza mno kupita kiasi. Bila kujali viwango vyao vya kukua kiroho, wanakuwa na mashaka kwamba bado wanashindwa kufikia “viwango” anavyotaka Mungu.
Wakristo wengine wamefundishwa kutegemea kupata mihemko maalumu baada ya Mungu kuwa amewatakasa mioyo yao na kuwafanya watakatifu. Wanajiangalia wenyewe pamoja na mihemko yao kuliko kumwangalia Mungu. Hata hivyo, Biblia inafundisha kwamba utakatifu ni tunda la kushikamana na Kristo. Tunapokuwa tunatembea katika Roho, kudumu katika maombi, kujilisha kwa Neno la Mungu, kushiriki katika kuabudu na ushirika wa Kikristo, kukiri madhaifu yetu, na kutembea nuruni, Mungu anatuumba kwenye sura ya Kristo. Tunaweza tusiyaone maendeleo ya haraka kama tulivyotegemea kwa wiki au mwezi, lakini kama tutaangalia nyuma tulikokuwa mwaka mmoja uliopita au mitano iliyopita, kwa vyovyote tutayaona mabadiliko!
Paulo alimtia moyo kila mwamini kujua kwamba Mungu anayeanza kazi ya kutufanya tuwe watakatifu ataikamilisha kazi hiyo: “Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu.”[19]
Utakatifu wa moyo na maisha ni safari. Kanuni hizi kumi za kibiblia zitahifadhi nafsi zetu kupita katika mawimbi ya upepo mkali ya taabu na majaribu na kutufanya sisi tukae kwenye mfungamano mmoja na nyumbani kwetu mbinguni.
[1] Sehemu hii imenukuliwa kutoka katika somo la Rev. Timothy Keep.
Katika kila somo, tumesoma habari za mtu mmoja kutoka historia ya Kanisa aliyenakisi moyo mtakatifu. Wengine ni Wakristo waliokuwa mashuhuri. Wengine ni watu waliojulikana kidogo sana lakini kwa kimya kabisa wakiishi maisha matakatifu.
Sasa ni nafasi yako. Je, unayo njaa ya kuwa na moyo mtakatifu? Je, unayo matamanio ya kushika urafiki na Mungu? Je, unataka umfananie Baba wa Mbinguni? Unaweza kuwa mtakatifu.
Je, unayo njaa ya kuwa mkamilifu katika Roho? Je, unataka kumtumikia Mungu kwa moyo usiogawanyika? Unaweza “kuwa mkamilifu kama kama Baba yako wa mbinguni alivyo mtakatifu.” Unaweza kumpenda Mungu na jirani yako kupitia nguvu ya Roho Mtakatifu katika maisha yako.
Chaguo ni lako. Je, utajisalimisha kikamilifu kwa Mungu? Kama ndivyo, utapata utimilifu wa utajiri wake utakapokuwa umesogea karibu naye. Utapata furaha wakati Mungu atakapokufanya uwe wa sura yake. Utapata amani ya moyo ambayo ni mali ya Mungu kabisa. Utatembea kwa ushindi kila siku katika ukamilifu wa Roho Mtakatifu. Kwa neema ya Mungu, unaweza kuishi maisha ya utakatifu.
Tafakuri ya Somo la 12
(1) Maisha ya utakatifu yanawezekana kwa kila mtoto wa kweli wa Mungu.
Neno la Mungu linafundisha kwamba maisha ya utakatifu yanawezekana.
Wakristo katika historia yote wamedhihirisha kwamba maisha ya utakatifu yanawezekana.
Njaa inayotokana na Mungu ya kutaka utakatifu ni udhihirisho kwamba maisha ya utakatifu yanawezekana.
(2) Neno la Mungu linaonyesha njia ya maisha ya utakatifu.
Wakati tu wa kuzaliwa kwetu mara ya pili, Mungu anaanza kutufanya watakatifu. Huu ndio mwanzo wa utakaso.
Jinsi tunavyomfuata Kristo, tunakua katika utakaso.
Mungu anataka atupe moyo mtakatifu. Mwito kwa ajili ya usafi wa moyo ni pamoja na:
Kuitwa kwa ajili ya utiifu uliokamilika.
Kuitwa kwa ajili ya moyo uliojisalimisha.
Kuitwa kwa ajili ya uaminifu ulio mkamilifu
Baada ya mioyo yetu kuwa misafi, tunaendelea kukua katika kumfanania Kristo.
(3) Njia ambazo tunaweza kuendelea nazo katika kupalilia maisha yetu ya utakatifu ya kila siku:
Endelea kubakia uliyepondeka kiroho.
Kukubali kuonywa na Mungu.
Jikabidhi wewe mwenyewe kila siku kama dhabihu kwa Mungu.
Yatafakari Maandiko kila siku.
Kujivalisha mwenyewe kwa Yesu kila siku.
Msiuangalie mwili hata kuwasha tamaa zake.
Istawishe akili yako kila siku
Vaeni silaha zote za Mungu.
Endelea kuukuza ufahamu wako juu ya Roho Mtakatifu.
Ishi kwa neema.
Kazi ya Kufanya
(1) Soma 1 Wathesalonike 5:23-24.
(2) Katika kila somo, tumeomba maombi ya utakatifu. Mwisho wa somo hili, andika maombi yako mwenyewe kwa ajili ya utakatifu. Andika maombi yako ukimwomba Mungu akuongoze kuendelea kukua katika sura yake. Jisalimishe mwenyewe kabisa kwenye mamlaka na mapenzi yake katika maisha yako. Omba kwa Imani kwamba Mungu aliyekuokoa atalitimiza kusudi la kukubadilisha wewe uwe katika sura yake.
Print Course
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.