Watu wa Isareli walikuwa tayari kuingia nchi ya Kaanani. Mungu aliwaleta huko kote kupitia jangwani, na walikuwa wamebakiza umbali kidogo tu kutoka nchi ya ahadi. Musa aliwatuma wapelelezi kumi na wawili kwenda kuipeleleza nchi. Baada ya siku arobaini, wapelelezi walirudi na zabibu na taarifa za maajabu ya nchi ya Kaanani. Lakini, walisema, Wakaanani ni watu wenye nguvu sana wanaoishi katika miji. Tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi!
Wapelelezi wawili tu, Yoshua na Kalebu waliamini ahadi ya Mungu ya ushindi. Kalebu akasema, “Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka.”[1] Yoshua na Kalebu waliiona ile nchi kama wapelelezi wengine. Waliiona miji na maboma makubwa sana. Waliwaona wapiganaji wenye nguvu sana.
Lakini Yoshua na Kalebu waliona kitu tofauti ambacho wapelelezi wengine hawakukiona – waliona kwamba Mungu aliyewatoa Israeli kutoka Misri atawaleta Israeli kuingia nchi ya Kaanani. Waliona kwamba Mungu aliyeharibu jeshi la Farao ataharibu na kuta za Yeriko. Waliona kwamba Mungu wa Ibrahimu alikuwa pia Mungu wa Musa. Mungu alisema, “lakini mtumishi wangu Kalebu, kwa kuwa alikuwa na roho nyingine ndani yake, naye ameniandama kwa moyo wote.”[2]
Kwa kuwa hawakumwamini yeye, Mungu alikilaani kile kizazi cha watu wazima kifie jangwani. Miaka arobaini baadaye, Israeli ikaingia Kaanani, na ilikuwa ni wakati wa kuigawa nchi. Kalebu alikuwa na zaidi ya miaka themanini. Akamwambia Yoshua, “Hata sasa mimi nina nguvu zangu hivi leo kama nilivyokuwa siku hiyo Musa aliyonituma…. Basi sasa unipe mlima huu.” Ndiyo, kulikuwa na miji imara iliyokuwa na wapiganaji hodari sana. Lakini Kalebu alikuwa na Imani katika ahadi za Mungu. “Nami nitawafukuza watoke nje, kama Bwana alivyonena.”[3]
Ni kitu gani kilimpa Kalebu Imani kubwa hivyo? Ni moyo usiogawanyika. Kalebu alisema, “Ila mimi nilimfuata Bwana, Mungu wangu, kwa utimilifu.”[4] Kalebu alimwamini Mungu kwa moyo wake wote. Kalebu alikuwa na moyo usiogawanyika.
Vitabu vya Historia vinaelezea anguko la kutisha la Israeli lilivyosababisha watu wake wasiwe kama Mungu alivyotaka wawe. Vitabu vya Hisoria vinaonyesha jinsi Israeli ilivyopotea njia kutoka katika mpango wa Mungu. Israeli ilikuwa imeitwa kumwakilisha Mungu kwa mataifa. Badala yake, ikageukia miungu ya uongo. Kutokana na kushindwa kwake, Israeli ilishindwa na kupelekwa utumwani. Utukufu wake uligeuka kuwa aibu.
Pamoja na picha ya kukosa uaminifu kabisa, Vitabu vya Historia vinaonyesha watu watakatifu waliomtumikia Mungu. Wakati wengi katika Israeli walikuwa siyo waaminifu tena kwa Mungu (Waamuzi), mjane mmoja mdogo Mmoabi alikuwa mwaminifu (Ruth). Hata wakiwa utumwani (2 Wafalme), binti mdogo wa Kiyahudi alikubali mwito wa Mungu akatumikia watu wake (Esta). Watu hawa walimheshimu Mungu kwa mioyo yao yote. Walikuwa watakatifu.
Vitabu vya Historia vinafundisha kwamba kuwa mtakatifu ina maana ya kumtumikia Mungu kwa uaminifu wote. Utakatifu haumaanishi utendaji kamili. Utakatifu unamaanisha kumtumikia Mungu kwa moyo usiogawanyika.
Tafsiri za zamani za Agano la Kale zimetumia neno “kamilifu” kutafsiri neno la Kiebrania shalem. Shalem inatafsiriwa “Kuwa mkamilifu.” Kuwa mkamilifu ni kwamba umekamilika. Kuwa mtakatifu inamaanisha kwamba wewe ni mali ya Mungu kabisa.
Shalem inahusiana na neno la Kiebrania la amani, shalom. Kuwa mkamilifu mbele ya Mungu inamaanisha kuwa na amani na yeye (“mioyo iliyo kamili kwa BWANA”).[1] Kuwa na “moyo mkamilifu” ni kuwa na moyo ambao “umekamilika” au “usiogawanyika,” moyo ulio na uaminifu wa peke yake. Tuangalie mifano ya neno “mkamilifu” au “usiogawanyika” katika Vitabu vya Historia.
Jeshi lenye kusudi lisilogawanyika
Baada ya kifo cha Sauli, makabila ya kaskaini yalimtawaza Ishboshethi kuwa mfalme wakati Yuda ilimfuata Daudi. Kulikuwa na miaka miwili ya vita ambayo Daudi aliiongoza Yuda kupigana na makabila ya kaskazini. Baada ya miaka miwili, Ishboshethi aliuawa na makepteni wake mwenyewe. Majeshi yaliungana kumtawaza Daudi awe mfalme juu ya Israeli wote. Taifa likawa sasa liko chini ya utawala wa mfalme mmoja.
"Hao wote, watu wa vita, askari wastadi, wakaja Hebroni wenye moyo mkamilifu, ili kumtawaza Daudi awe mfalme juu ya Israeli wote; tena wote waliosalia wa Israeli nao walikuwa na moyo mmoja kwamba wamtawaze Daudi."[2]
Jeshi “likaja Hebroni kwa moyo mmoja (shalem) kumfanya Daudi awe mfalme.” Tafsiri za zamani zinatumia maneno “pamoja na moyo makamilifu.”[3] “Mkamilifu” haina maana kwamba hakukuwa na hata mtu mmoja aliyetenda dhambi. Inamaanisha hapa kwamba “taifa lote lilikuwa mwaminifu” kwa Daudi. Walikuwa wameunganishwa chini ya mfalme mmoja. Katika aya hii, shalem siyo neno la kidini; bali la kisiasa. Shalem ikimaanisha kuwa na uaminifu mmoja usiogawanyika kwa mfalme.
Madhabahu iliyo na mawe yasiyochongwa
Wakati Isaraeli ilipoingia katika Nchi ya Ahadi, Yoshua alijenga madhabahu katika mlima wa Ebali. Yoshua alijenga madhabahu ya “mawe yasiyochongwa (shalem) ambayo mtu hakutumia juu yake chombo cha chuma” (Yoshua 8:31). “Yasiyochongwa” ni neno lililo sawa na “yaliyo mazima” au “makamilifu.” Kuwa shalem ni kutogawanyika.
Moyo usiogawanyika
Wakati wa kujitolea kulijenga hekalu, mfalme Sulemani aliwataka watu wa Israeli wamtumikie Mungu kwa mioyo isiyogawanyika.
"Mioyo yenu na iwe kamili (shalem)kwa Bwana, Mungu wetu, kuenenda katika sheria zake, na kuzishika amri zake, kama ilivyo leo."[4]
Hili ni neno lililo sawa na yaliyotumika kuelezea muungano wa jeshi moja chini ya Daudi. Ni neno hilo hilo limetumika kuelezea mawe yasiyochongwa. Sulemani aliwataka Israeli kuwa na uaminifu usiogawanyika kwa Mungu. Kama watu wa Israeli wangekuwa na moyo usiogawanyika, “wangetembea katika amri zake na kuzishika amri zake.” Mtu aliye na moyo usiogawanyika kwa hiari yake humtii Mungu.
Historia ya wafalme wa Israeli inaonyesha kwamba Mungu huwaita watu wamtumike kwa mioyo isiyogawanyika. Mungu anatafuta watu watakatifu. Mungu yuko katika kutafuta mioyo isiyogawanyika.
Mfalme Sulemani: Moyo uliogawanyika
Wakati wa kujitolea kulijenga hekalu, Sulemani aliwataka watu wa Israeli wamtumikie Mungu kwa mioyo isiyogawanyika. Kwa masikitiko, Sulemani hakuutendea kazi ushauri wake mwenyewe. “Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu (shalem) kwa Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake.”[1]
Moyo wa Sulemani ulikuwa umegawanyika. Alitaka awe anaabudu Mungu wa Israeli na wakati huo huo aabudu miungu. Huwezi ukawa mwaminifu kwa Mungu na kwa miungu kwa wakati mmoja. Mwandishi wa kitabu cha 1 Wafalme hasemi kwamba Sulemani aliacha kumwabudu Yehova. Sulemani aliendela kutoa dhabihu kwenye Hekalu, lakini moyo wake ulikuwa umegawanyika. Alljaribu kumtumikia Mungu na moyo uliogawanyika.
Mfalme Daudi: Moyo usiogawanyika
Katika 1 Wafalme 11:4, tunasoma mtazamo wa Mungu kuhusiana na moyo wa Daudi na Sulemani. Moyo wa Daudi haukugawanyika, lakini moyo wa Sulemani uligawanyika. Kwa mtazamo wa kibinadamu tunaweza kufikiria uzinzi na mauaji ya Daudi kama yaliyo mabaya sana kuliko kuasi kwa Sulemani. Kwanini mwandishi wa Wafalme aseme kwamba moyo wa Daudi “ulikuwa mkweli kabisa” kwa Bwana?
Tofauti ni mwitikio wa Daudi kwenye dhambi. Wakati nabii alipokabiliana na Daudi, kwa haraka sana Daudi alitubu. Daudi hakujitetea mwenyewe. Badala yake, alikiri uovu wake kwa Mungu, “Nimekutenda dhambi Wewe peke yako, Na kufanya maovu mbele za macho yako.”[3] Daudi alimtumikia Mungu na moyo usiogawanyika. Moyo wake ulikuwa shalem. Moyo wake haukugawanyika.
Zaburi 86 inaelezea njaa ya Daudi ya moyo usiogawanyika. Katika Zaburi ya 86, Daudi anaomba ukombozi kutokana na maadui zake wanaotafuta kumwua. Katikati ya maombi haya, Daudi analia, “Uunganishe moyo wangu katika kuhofia Jina lako.”[4] Daudi anaomba kwa ajili ya moyo usiogawanyika. Daudi alitafuta kumtumikia Mungu kwa ukamilifu wa moyo wake wote.
Mfalme Asa: Moyo uliogawanyika
Asa aliingia madarakani kuitawala Yuda mwaka wa 910 K.K. Alikuwa amejitoa kabisa kwa Mungu; aliharibu madhabahu zote za miungu ya uongo; alivunjavunja maashera yote yaliyotumika kwa ajili ya ibada za sanamu. Wakati jenerali wa Kushi alipoipiga Yuda na jeshi lake kubwa, Asa alimlilia Mungu kwa ajili ya ukombozi:
"…Bwana, hapana kuliko wewe aliye wa kusaidia, kati yake yeye aliye hodari, na yeye asiye na nguvu; utusaidie, Ee Bwana, Mungu wetu; kwa kuwa sisi twakutegemea wewe, na kwa jina lako tumekuja juu ya jamii kubwa hii. Ee Bwana, wewe ndiwe Mungu wetu, asikushinde mwanadamu."[5]
Mungu alijibu ombi la Asa. “Basi, Bwana akawapiga Wakushi mbele ya Asa, na mbele ya Yuda...”[6] Asa aliweka uaminifu wake wote kwa Mungu, na Mungu akampa ushindi mkubwa.
Miaka ishirini ilipita, Asa akakutana tena na jaribu lingine jipya. Wakati huu, Baasha, mfalme wa makabila ya kaskazini, aliitishia Yuda. Kwa hofu yake, Asa aliamua kuunda muungano wa kijeshi na taifa lingine. Alisaini mkataba na Ben-Hadad, mfalme wa Syria. Badala ya kumtumainia Mungu peke yake, Asa akaweka tumaini lake kwa mfalme wa kipagani.
Katika kujibu, nabii Hanani alimkumbusha Asa kuhusu ushindi wake mkubwa wa nyuma dhidi ya jeshi kubwa la Wakushi. Alimkumbusha Asa kwamba “wakati ulipomtegemea BWANA aliwaingiza mikononi mwako.” Kwa nini Mungu afanye hivyo? Kwa sababu, “macho ya Bwana hukimbia-kimbia duniani mwote, ili ajionyeshe mwenye nguvu kwa ajili ya hao, waliokamilika moyo (shalem) kuelekea kwake.”[7]
Wakati Asa alipomwamini Mungu kwa ukamilifu wote, Mungu alimpa ushindi mkubwa. Lakini sasa Asa anamtegemea mtawala wa Syria. Kwa sababu Asa hamwamini Mungu peke yake tena, Mungu hatamwokoa tena katika hatari yeyote. Hanani alimwonya Asa kwamba atakumbana na vita katika wakati wake wote wa utawala uliobakia.
Miaka ya mwisho ya kutawala kwa Asa ni kivuli tu cha wakati mzuri ujao wa miaka yake ya awali. Mwishoni mwa maisha, Asa akawa mgonjwa, lakini “hakumtafuta Bwana katika ugonjwa wake.”[8]
Utawala wa Asa ulikuwa bora kuliko wa wafalme wengine wengi. Asa hakutelekeza kumsifu Yehova, lakini moyo wake ulikuwa umegawanyika dhidi ya Mungu. Alishindwa kumwamini Mungu kabisa. Asa hakuweza kufikia mafanikio mazuri ya Mungu.
Maisha ya Asa ni kielelezo cha nguvu cha hatari iliyoko katika moyo uliogawanyika. Katika kisa cha kwanza, Asa alimwamini Mungu kabisa. Katika kisa cha pili, aliendelea kutumika kama kiongozi wa watu wa Mungu, lakini moyo wake haukuwa mkamilifu. Badala ya kumtegemea Mungu kabisa, yeye alitengeneza muungano wa kijeshi na adui wa Mungu. Asa alikuwa na moyo uliogawanyika.
Mfalme Amazia: Moyo uliogawanyika
Amazia anaonyesha hatari ya moyo uliogawanyika. Utawala wa Amazia ulianza kwa nguvu kubwa: “Alifanya yaliyo mema machoni pa Bwana.”[9] Kama ilivyokuwa kwa Asa, Amazia alianza vyema.
Hata hivyo, vitabu vyote viwili vya wafalme na Mambo ya Nyakati vinaonya kuhusu hatari iliyopo. Mwandishi wa kitabu cha Wafalme anasema Amazia alifanya yaliyo mema, “lakini siyo kama Daudi baba yake.” Mwandishi wa kitabu cha Mambo ya Nyakati anasema kwamba Amazia alifanya yaliyo adili, “Lakini siyo kwa moyo mkamilifu.” Hakuweza kubomoa “mahali pa juu.” Kwa sababu ya hilo, watu waliendelea kutoa dhabihu zao kwa miungu ya uongo. Kiongozi mwenye moyo uliogawanyika hulipeleka taifa kwenye matatizo.
Kama Asa, Amazia aligundua kwamba kumtumikia Mungu kwa moyo uliogawanyika kunaleta matatizo. Ingawaje utawala wa Amazia ulianza vizuri, baadaye aliabudu miungu ya Edom. Katika hukumu, Mungu aliruhusu ufalme wa Kaskazini kumshinda Amazia. Ahadi ya mwanzo ya utawala wa Amazia kamwe haikutimia kwa sababu alikuwa na moyo uliogawanyika. Moyo wa Amazia haukuwa mkamilifu.
[4]Sala kwa ajili ya Utakatifu “Naomba nife mimi ili niweze kuishi ndani yako; Naomba unifanye mimi mtupu ili niweze kuzidi ndani yako; Naomba mimi nisiwe chochote ili niwe ni yote kwako”
- Erasmus
Utakatifu katika vitendo: Utakatifu huanzia ndani ya Moyo
Yesu alizungumza na viongozi wa dini waliokuwa waangalifu sana kuhusu muonekano wa nje, lakini wanafiki wa moyo.
"Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na Imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache. Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia!"[1]
Hawa wakuu wa dini walikuwa waangalifu sana katika kufuata sheria za dini, lakini hawakufuata sheria ya ndani iliyo muhimu. Yesu aliishutumu dini yao ya uongo. “Unamchuja mbu (uko mwangalifu kwa mambo madogo tu), lakini unammeza ngamia (unadharau matatizo makubwa).” Utakatifu huanzia moyoni.
Kama tufikiria tu muonekano wa nje, tunaweza kusema:
“Mimi ni mtakatifu kwa sababu sivai _______________.”
“Mimi ni mtakatifu kwa sababu siendi _______________.”
“Mimi ni mtakatifu kwa sababu siangalii _______________.”
Tunapodai kuwa watakatifu kwa sababu ya mambo tunayoyatenda au tusiyoyatenda, Tunaweza kuwa kama Mafarisayo. Yesu alielezea kuhusu Farisayo aliyekuwa akiomba, “Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote.”[2] Farisayo huyu aliufafanua utakatifu kwa matendo yake, “Mimi sidanganyi, ninafunga, ninatoa sadaka.” Anadai kuwa mtakatifu, lakini moyo wake haukuwa mtakatifu.
Mafarisayo walikuwa wanajivunia kutengwa kwao na dunia, lakini mioyo yao haikuwa mitakatifu. Yesu alisema, “Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote.”[3] Kwa nje, Mafarisayo walikuwa wametengwa; kwa ndani walikuwa wenye dhambi.
► Ni kipi kinaonekana rahisi kupima – muonekano wa nje au utakatifu wa ndani? Ni kipi rahisi kuigiza – muonekano wa nje au utakatifu wa ndani? Ni kipi tunapenda kuwekea mkazo sana – muonekano wa nje au utakatifu wa ndani?
Mfano kutoka Hezekia
Sheria ya kutengwa ilikuwa muhimu kwa kufundisha kwamba Mungu anahitaji watu watakatifu. Lakini Mungu alikuwa anahusika zaidi na mioyo ya watu wake kuliko ibada zao.
Masimulizi kutokana na uamsho wa Hezekia unaelezea kanuni hii. Baada ya hekalu kutakaswa, Hezekia aliirejesha Pasaka ya Wayahudi. Alilikaribisha taifa “kuja kwenye nyumba ya Bwana Yerusalemu ili kuiweka Pasaka kwa Bwana, Mungu wa Israeli.” Wajumbe kutoka kwa Hezekia walisafiri nchi nzima wakiwakaribisha watu kwenye sherehe hii. Katika maeneo mengi, “watu waliwacheka kwa dharau na kuwadhihaki. Hata hivyo, watu Asheri, Manase, na Zabloni walijinyenyekeza wenyewe na kuja Yerusalemu.”[4]
Walipoanza kuchinja kondoo wa Pasaka, “walikuwepo wengi ndani ya ukumbi ambao walikuwa bado hawajajiweka wakfu wenyewe.” Kwa kuwa taifa lilishakaa muda mrefu sana bila kuwepo na ibada ya kuabudu hekaluni, watu walikuwa wamenajisika na hawakuwa tayari kushiriki Pasaka. Makuhani walipaswa wafanye nini? Mungu aliruhusu watu washiriki Pasaka kwa sababu mioyo yao ilimtaka Mungu, ingawaje bado walikuwa hawajatakaswa.
"Kwani wingi wa watu, naam, wengi wa Efraimu, na wa Manase, na wa Isakari, na wa Zabuloni, hawakujisafisha, lakini wakala pasaka, ila si kama ilivyoandikwa. Naye Hezekia alikuwa amewaombea, akisema, 'Bwana mwema na amsamehe kila mtu, aukazaye moyo wake kumtafuta Mungu, Bwana, Mungu wa babaze, hata ikiwa si kwa utakaso wa patakatifu.' Bwana akamsikia Hezekia, akawaponya watu."[5]
Mungu alikuwa anataka mioyo isiyogawanyika. Hata pale watu waliposhindwa kufuata ibada za kutengwa, Mungu aliangalia mioyo ambayo ilikuwa imejitenga kwa ajili ya kumtafuta Mungu.
Watu watakatifu huitakasa mioyo yao kwa ajili ya Mungu
Utakatifu wakati wote huanza na Mungu. Chochote kilicho kitakatifu ni mali yake. Mungu aliitakasa Sabato, ardhi kwenye kichaka kinachowaka, mzaliwa wa kwanza wa Israeli, Hema ya kuabudia, madhabahu, na Walawi. Mungu alifanya vyote hivi kwa ajili yake mwenyewe. Vilifanywa vitakatifu kwa uwepo wa Mungu.
Utakatifu unaanza na Mungu, lakini Mungu ametuita tujitakase kwa ajili yake. Kama tutaisoma aya ambayo Mungu anasema “Nitawatakasa,” tunaweza tukaamua kwamba utakaso ni tendo la Mungu peke yake. Hata hivyo, Biblia inaonyesha kwamba, utakatifu unahitaji mwitikio kutoka kwa mtu mwenyewe.
Kutoka 19 kunatupa mfano. Mungu anamwagiza Musa, “Enenda kwa watu ukawatakase.” “Kwahiyo, Musa… alitakasa watu.” Musa aliwaweka watu kwa kusudi la Mungu. Baadaye Mungu alisema, “Makuhani nao, wamkaribiao Bwana, na wajitakase.”[6] Makuhani waliagizwa kujiweka kando kwa ajili ya makusudi ya Mungu. Walipaswa wawe watakatifu; walipaswa wajitenge wenyewe kwa ajli ya Mungu.
Moyo usiogawanyika unahusisha masuala mawili:
Mungu aliahidi kuwatenga watu wake: “Mimi ndimi Bwana niwatakasaye ninyi.”[7] Mungu huwafanya watu wake wawe watakatifu.
Mungu huwaagiza watu wake wajitenge kwa ajili yake. “Takaseni nafsi zenu basi; iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni Mtakatifu.”[8]
Tunajitakasa wenyewe kama mwitikio wa neema ya Mungu. Watu watakatifu kwa hiari yao wenyewe hujitakasa kwa Mungu. Wanajitoa wenyewe kwa Mungu kwa moyo mkunjufu.
Katika Walawi 20, amri hii “Jitakaseni wenyewe” inafuatiwa na ahadi, “Mimi ndimi Bwana niwatakasaye ninyi.” Ni jina moja la Kiebrania linalofanana katika aya zote mbili. Zinaweza zikatafsiriwa kama ifuatavyo: “Jitengeni wenyewe… Mimi ni Mungu niwatengaye.”[9]
Utakaso unahusisha kwa pamoja kazi ya Mungu na mwitikio wetu wenyewe. Hatufanyiki kuwa watakatifu kwa juhudi zetu wenyewe, wala hatusemi, “Kama Mungu akitaka niwe mtakatifu, atanifanya niwe mtakatifu bila ya mwitikio wangu.” Tunaitikia neema ya Mungu kwa kujitakasa wenyewe kwa ajili yake. Moyo usiogawanyika unahitaji utakaso.
Utakatifu chimbuko lake ni Mungu mwenyewe. Hata hivyo, Mungu ametuita sisi tujitoe wenyewe kwake. Tunafanywa watakatifu tunapojitoa kwa ajili ya wito wa Mungu. Paulo aliandika, “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.”[11] Paulo ametuita tujisalimishe kabisa kwa kusudi la Mungu. Kwa kuwa Mungu anaahidi kwamba atatufanya watakatifu, lazima tujisalimishe wenyewe. Utakatifu ni agizo (“jitakaseni wenyewe,”) na ahadi (“nitawatakasa”).
Watu watakatifu wanasema “Ndio” iliyokamilika kwa Mungu
Maisha ya Sulemani, Asa, na Amazia yanaonyesha hatari ya moyo uliogawanyika. Moyo uliogawanyika siyo kusudi la Mungu kwa watu wake. Moyo mtakatifu ni moyo usiogawanyika. Kwa hiyo, inamaanisha nini kuwa na moyo usiogawanyika? Inamaanisha nini kuwa na moyo ambao ni shalem au “mkamilifu”?
Wakristo wanaitwa kuwa watumishi wa Mungu. Kazi ya mtumishi ni kufanya kile ambacho bwana wake humwagiza kufanya. Mtumishi mzuri haulizi, “Hiki ndicho nilichochagua?” Mtumishi mzuri hufanya kwa hiari kile ambacho bwana wake ameagiza kifanyike. Wajibu wa mtumishi ni kusema “ndiyo” iliyo kamili na isiyobadilika.
Kwa hali hiyo hiyo, mtu anayemtumikia Mungu kwa moyo usiogawanyika anaitikia “ndio” kwenye wito wa Mungu. Huu ni moyo usiogawanyika. Musa aliwataka Israeli wamtumikie Mungu kwa moyo usiogawanyika:
"Na sasa, Israeli, Bwana, Mungu wako, anataka nini kwako, ila umche Bwana, Mungu wako, na kwenda katika njia zake zote, na kumpenda, na kumtumikia Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote; kuzishika amri za Bwana na sheria zake, ninazokuamuru leo, upate uheri?" [12]
Akiwa mwanafunzi wa chuo, Elisabeth Elliot aliandika kwenye kitabu chake cha kumbukumbu, “Bwana, nimesema ‘ndiyo’ ya milele. Kamwe, baada ya kuweka mkono wangu kwenye plau, nisiangalie nyuma. Ifanye inyooke njia ya msalaba mbele yangu. Nipe upendo, ambao hautatoa nafasi ya wazo la kurudi nyuma au hatua.”[14] Elliot alikuwa na moyo usiogawanyika; alikuwa mkamilifu mbele ya macho ya Mungu.
Miaka iliyofuata baada ya maombi haya, Elizabeth Elliot alikutana na changamoto nyingi. Mume wake, Jim Elliot aliuawa mwaka 1956 alipokuwa akijaribu kufanya uinjilisti kwa kabila la Huaorani nchini Ecuador. Elizabeth baadaye alikuja kuwa mmishenari kwa watu waliomwua mume wake. Ni mtu tu aliyeweza kusema “ndiyo ya milele” anayeweza kwenda kama mmishenari kwa wauwaji wa mume wake.
Mtu mtakatifu humtumikia Mungu kwa moyo usiogawanyika. Mtu mtakatifu husema”ndio ya milele” kwa Mungu. Hii ina maana ya kujisalimisha kabisa kwa Mungu. Mtu mtakatifu anapoyajua mapenzi ya Mungu, kwa hiari hutii. Moyo wake haujagawanyika; ni wa Mungu kabisa. Mtu mtakatifu anasema “ndio” wakati wa kipindi cha kujisalimisha kabisa.
Mtu mtakatifu huendelea kusema “ndio” kila siku. Baada ya Elisabeth Elliot “kusema ndiyo ya milele” aliendelea kukutana na msongo wa maamuzi. Kulikuwa na nyakati nyingine anasema tena, “Ndiyo, Bwana”. Wakristo wengi wanaamini kwamba “ndiyo ya mara moja tu” kutaondoa majaribu ya kujitoa kwako. Kujisalimisha ya mara moja tu ni jambo muhimu sana, lakini bado Shetani ataendelea kuleta majaribu kwenye kujitoa kwako. Zaidi na zaidi sana, utaendelea kusema, “Ndiyo Bwana. Maisha yangu ni yako wewe.” Hii ni “ndiyo” Roho endelevu ya maisha.
[9] Mambo ya Walawi 20:7-8, Tafsiri ya Biblia, New Living
[10]“Tunaweza kutumiwa na Mungu peke yake baada ya kumruhusu atuonyeshe maeneo yaliyofichwa kwa undani ya tabia zetu. Hata hatutambui wivu, uvivu, au kiburi kati yetu tunapokiona. Lakini Yesu atatuonyesha kila kitu tulichoshikilia ndani yetu kabla neema yake haijaanza kufanya kazi.”
- Oswald Chambers
[13]“Nimesema ‘ndiyo’ ya milele. Kamwe sitaangalia nyuma tena.”
- Elisabeth Elliot
[14]Elisabeth Elliot, Passion and Purity (Old Tappan: Fleming H. Revell Co., 1984), 25
Aliipata Siri - George Muller
George Muller[1] alikuwa ni Mkristo aliyekuwa maarufu sana katika karne ya kumi na tisa.[2] Alijenga vituo vitano vya makazi ya watoto yatima na kuhudumia zaidi ya yatima 10,000. Muller alichangisha mamilioni ya dola kwa ajili ya kusaidia yatima na wamishenari wengine. Hadi wakati wa kifo chake, Muller alikuwa ametoa elimu kwa watoto 122,000, aligawa karibu Biblia 2,000,000, na zaidi ya vitabu na vipeperushi milioni 100. Alifanya hivi bila kuomba mchango wowote kutoka kwa mtu binafsi. Alidhamiria kumwomba Mungu tu kwa msaada.
Wakati Mungu alipomwita Muller kujenga makazi yake ya watoto, alikuwa na senti hamsini tu mfukoni mwake! Muller aliitikia wito huu wa Mungu akimtegemea Mungu kwa ufadhili wake wote. Muller alikuwa na senti hamsini tu – lakini aliitoa kwa Mungu na akamwamini Mungu katika mambo mengine yote yaliyosalia. Muller baadaye alikuja kutoa ushuhuda kwamba yatima wake hawakuwahi kukosa chakula; Mungu alitoa kila hitaji.
Muller aliishi maisha ya uovu akiwa kijana mdogo, akiwa ametumikia jela akiwa na umri wa miaka kumi na sita. Hata hivyo, akiwa na umri wa miaka ishirini, George Muller alimpa Yesu maisha yake. Kwa miaka kadhaa iliyofuata, Muller alikuwa na vipindi vya mafanikio ya kiroho, lakini pia akatambua maeneo ya mapambano. Mwishoni, akiwa na umri wa miaka ishirini na nne, Muller aliusalimisha kabisa moyo wake. “Nilijitoa kwa ukamilifu mwenyewe kwa Bwana.”
Akiwa na miaka sabini, Muller alianza kusafiri nchi za nje kuhubiri. Katikati ya miaka sabini na themanini na saba, alikuwa amesafiri katika nchi arobaini na mbili na kuhubiria watu zaidi ya 3,000,000.
Mwishoni mwa maisha yake, George Muller aliulizwa siri ya maisha yake ya huduma. Alijibu, “Kuna siku ambayo nilikufa mwenyewe (mawazo na matamanio yangu), kwa dunia kuidhinisha au kutoidhinisha, na hata kwa kuidhinishwa au kulaumiwa na marafiki zangu. Nilichojali mimi ni kuidhinishwa na Mungu.” George Muller alikuwa na moyo usiogawanyika. Alikuwa mkamilifu mbele ya macho ya Mungu.
[2] Kimenukuliwa kutoka Roger Steer, Spiritual Secrets of George Muller (PA: OMF Books, 1985) and J. Gilchrist Lawson, Deeper Experiences of Famous Christians (Anderson: Warner Press, 1911).
Tafakuri ya Somo la 5
(1) Kuwa mtakatifu ni kuwa na moyo usiogawanyika.
(2) Neno shalem linamaanisha “isiyogawanyika.” Neno hili linalinganishwa na neno shalom, likimaanisha “amani.”Kuwa na “ukamilifu” au “kutogawanyika” moyo ni kuwa na moyo wenye uaminifu mmoja.
(3) Sulemani, Asa, na Amazia wanaonyesha hatari ya moyo uliogawanyika. Kila mmoja alishindwa kumpendeza Mungu kikamilifu kwa sababu mioyo yao ilikuwa imegawanyika.
(4) Utakatifu huanzia moyoni. Yesu aliwaangaliza wale wanaojali ibada ya nje bila ya moyo safi.
(5) Ni lazima tujiweke wakfu wenyewe kwa Mungu. Mungu huwatakasa watu wake. Mungu anawaita watu wake wajiweke wakfu wenyewe kama mwitikio wa neema yake.
(6) Watu watakatifu husema “ndio” iliyokamilika kwa Mungu. Kama mtumishi aliyejitoa, kwa hiari yao husema ndio kwa bwana wao.
(7) Baada ya kusema “ndiyo ya milele” ni lazima tuendelee kusema “ndiyo” kila siku.
Kazi ya Kufanya
(1) Andaa fundisho kuhusu “Kuishi na Moyo Usiogawanyika.” Unaweza ukatengeneza muhtasari wako mwenyewe, au ukafuata muhtasari ufuatao:
A. Mfano wa kibiblia wa moyo uliogawanyika
B. Hatari za kuishi na moyo uliogawanyika
C. Tiba ya moyo uliogawanyika
(2) Anza kikao kinachofuata cha darasa kwa kunukuu Zaburi 86:11-12.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.