Kufikia mwisho wa somo hili, kila mwanafunzi atapaswa:
(1) Kutambua kiini cha utakatifu katika nyaraka za Agano Jipya.
(2) Kufurahia utoaji wa Mungu wa kuwafanya watu wake wamfananie Kristo.
(3) Kutambua uwiano uliopo kati ya kile ambacho Mungu tayari ameshatufanya tuwe watakatifu na kile Mungu anachoendelea kukifanya jinsi tunavyoendelea kukua katika utakatifu.
(4) Kukubaliana na uwezekano wa maisha yenye ushindi endelevu juu ya dhambi ya makusudi.
Ni mapema Jumapili asubuhi karibia miaka thelathini tangu kupaa kwa Yesu mbinguni. Kundi la Wakristo wamekusanyika kwa ajili ya kumwabudu Mungu kwenye nyumba moja ya binafsi katika mji wa Filipi. Wana msisimko kwa sababu wamepata barua kutoka kwa Paulo, Mchungaji wao. [4]
Kiongozi anaanza kuisoma ile barua ya Paulo. Paulo anaandika kutoka katika moyo uliojawa na furaha. Ingawaje yuko kizuizini katika gereza la Rumi, anamfurahia Kristo. Paulo hajui kama ataachiliwa huru au atafungwa, lakini ana Amani. Kwa nini? “Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida.”[1]
Akiwa ni baba yao wa kiroho, Paulo anawatia moyo Wakristo wa Filipi waendelee kukua katika imani ya Kikristo. Anataka awaone hawa waamini wakikua kama watu watakatifu ambao Mungu amewaita wawe hivyo. Paulo anaandika, “Lakini mwenendo wenu na uwe kama inavyoipasa Injili ya Kristo,”[2] Mwenendo wenu na uwe kama inavyoipasa Injili? Hili linawezekanaje?
Jibu la Paulo ni kwamba: “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu.” [3] Kama Wakristo wa Filipi wana akili ya Kristo, watakuwa kama Kristo. Siri ya maisha matakatifu ni kuishi na akili ya Kristo. Utakatifu ni kumfanania Kristo.
[4] Sala kwa ajili ya Utakatifu “Siko tena mwenyewe, bali ni wako. Niweke katika lolote unalotaka, nipe cheo chochote unachotaka. Niweke katika kutenda, Niweke katika mateso. Naomba niajiriwe na wewe Au niwekwe akiba kwa ajili yako. Niinuliwe kwa ajili yako, Au nishushwe chini nawe. Nifanye nijae, Nifanye niwe mtupu. Nifanye niwe na kila kitu, Nifanye nisiwe na chochote. Kwa uhuru na kwa moyo wangu natoa vitu vyote kwako Kwa furaha yako na uwazi wako. Na sasa, Ewe Mungu wa utukufu na Baraka, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, wewe ni wangu, nami ni wako.”
- John Wesley
Ujumbe wa Nyaraka: Wakristo wawe Watakatifu
Nyaraka za Agano Jipya zinawaita Wakristo wawe Watakatifu
Kila Mkristo anaitwa awe mtakatifu. Mungu “alituchagua sisi ndani yake [Kristo] kabla ya kuwepo misingi ya dunia ili kwamba tuwe watakatifu na tusiolaumika mbele zake.”[1] Kusudi la Mungu la milele katika wokovu ni kutufanya tuwe watu watakatifu.
Hakuna Mkristo wa Kiyahudi wa karne ya kwanza aliyeshangaa kusoma kwamba wanatakiwa wawe watakatifu. Mungu aliamuru utakatifu katika kitabu cha Walawi. Wayahudi Wakristo walitambua kwamba Mungu aliwategemea watu wake wawe watakatifu.
Hata hivyo, Mataifa walizidi kuabudu miungu ya kipagani ambayo haikuwa mitakatifu. Ujumbe wa utakatifu kwa wapagani ulikuwa mgeni kabisa. Petro aliwaandikia Wakristo waliotoka kwenye upagani ambao si muda mrefu umepita tangu “kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu.”[2] Watu hawa wamekuwa wapagani bila dhana ya kuwepo kwa haki ya kweli, lakini Petro aliwaita waje kwenye maisha ya utakatifu.
Mitume walifundisha mataifa waliobadilishwa jinsi ya kuishi maisha ya utakatifu. Walifundisha ujumbe chanya: “Hili ndilo unalopaswa kufanya.” Walifundisha ujumbe hasi: “Hili ndilo hupaswi kufanya.”
Mara arobaini, Mitume waliwaita waamini “watakatifu.” Mtakatifu wa Agano Jipya siyo mtu aliyekufa zamani za kale na anayechukuliwa kama kioo cha rangi cha Hekalu kubwa la Ulaya. Mtakatifu ni mtu yeyote anayeishi kama Mungu alivyowataka watu wake waishi. Kila Mkristo ameitwa kuwa mtakatifu; kila Mkristo anatakiwa awe mtakatifu.
Mitume waliwaagiza waamini kufuatilia utakatifu
Paulo aliwakumbusha waamini wa Korintho kwamba wao ni “hekalu la Mungu aliye hai.”[3] Hekalu lilikuwa sehemu takatifu ya kuabudia. Kwa kuwa sisi ni hakalu la Mungu, “na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu.”[4]
Watu wa Mungu mmeitwa “mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu.”[5] Paulo aliandika kwamba, Kristo “alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema.”[6] Mwandishi wa kitabu cha Waebrania aliwaelekeza wasomaji wake: “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao.”[7] Watu wa Mungu wameitwa wawe watakatifu.
Mitume waliomba Wakristo, waweze kuwa watakatifu
Paulo aliomba kwamba watu wa Mungu wafanywe kuwa watakatifu.
► Soma 1 Wathesalonike 1:2-10. Elezea Wakristo wa Thesalonike wakati wa mwanzo wa barua ya Paulo.
Watu waliopokea barua ya Paulo katika kanisa la Thesalonike walikuwa ni Wakristo wa kweli. Walijulikana kwa Imani yao, upendo wao, uthabiti wa matumaini yao. Walikuwa ni “ndugu waliopendwa na Mungu.” Injili ilikuja kwao “siyo kwa maneno tu, bali kwa nguvu na kwa Roho Mtakatifu na kwa uhakika kamili.” “Walilipokea neno na mateso mengi kwa furaha ya Roho Mtakatifu.” “Walikuwa mfano kwa waamini wengine wote katika Makedonia na Akaia.” “Wamegeuka kutoka waabudu sanamu hadi kuwa watumishi wa Mungu wa kweli.”
Hata hivyo, hawa Wakristo bado walihitaji uzoefu mzito zaidi na Mungu. Walikuwa watakatifu. Walipozaliwa upya, Mungu alianza kuwafanya watakatifu. Hata hivyo, Paulo aliwaombea:
"Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo."[8]
Maombi haya yalikuwa ni muhimu sana kwa Paulo. Alikuwa akiomba, “usiku na mchana tunapoomba kwa juhudi tupate kuwaona nyuso zenu, na kuyatengeneza mapungufu ya Imani yenu.”[9] Watu hawa walikuwa ni Wakristo wa kweli; lakini Paulo alijua kwamba kuna kitu kimepungua. Hii haimaanishi kwamba walikuwa Wakristo wenye “mabaya,” Paulo alikuwa tayari ameshawapongeza kwa uzoefu wao mzuri katika Ukristo wao.
Hakukuwa na “ubaya” wowote kwenye uzoefu wao wa Ukristo, lakini Paulo alijua kwamba wanahitaji kukua zaidi. Walikuwa wametakaswa, lakini Paulo anawaombea Mungu “awatakase kabisa.” Aliomba kwamba Mungu awafanye watakatifu zaidi na zaidi. Aliomba Mungu awasafishe “mwili, nafsi na roho.”
Mitume waliahidi kwamba Wakristo wanaweza kuwa watakatifu
Wakati alipoomba kwamba Waefeso “wapate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu” Paulo alikuwa na uhakika kwamba Mungu atajibu maombi yake kwa sababu alikuwa anaomba kwa Mungu “yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu….”[10] Wito wa Mungu kwa moyo mtakatifu siyo agizo lisilowezekana. Wito wa Mungu ni kwa ajli ya kila mwamini.
Wakati alipoomba kwa kwa Wakristo wa Thesalonike, alikuwa na uhkika kwamba Mungu angejibu maombi yake, Paulo aliifuatilia sala yake, “Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa” kwa ahadi kwamba, “Yeye ni mwaminifu ambaye awaita, naye atafanya.”[11] Mitume wanaahidi kwamba tunaweza kuwa watakatifu.
Kwenye Agano la Kale, Mungu alifunua ujumbe wa moyo mtakatifu na mikono mitakatifu kupitia Sheria na mitume. Katika maisha ya Yesu Kristo, Mungu alitoa mfano wa upendo mkamilifu. Katika kitabu cha Matendo, Wakristo wa mwanzo walionesha kwamba ni jambo linalowezekana kwa mwamini wa kawaida kuishi maisha ya utakatifu kwa uweza wa Nguvu za Roho Mtakatifu. Katika Nyaraka za Agano Jipya, ujumbe wa utakatifu unatumika katika maisha ya kila siku ya mwamini.
Utakatifu ni Moyo na Akili vinavyomfanania Kristo
Nyaraka za Agano Jipya zinafundisha kwamba utakatifu ni kumfanania Kristo. Waamini wanapaswa wafanane na Kristo. Kuwa mtakatifu ni zaidi ya tabia ya nje. Utakatifu unaanzia moyoni. Kuwa mtakatifu ni kuwa kama Kristo ndani ya mioyo yetu na akili zetu.
Paulo hasemi kwamba, “Utaigiza kama Yesu Kristo.” Anasisitiza kwamba, “Utakuwa kama Yesu Kristo.” Haitoshi kumwigiza Yesu kwa nje; tunatakiwa tufanane na yeye kwa ndani. Mpango wa Mungu ni kuwabadilisha kabisa watu wake wawe katika mfano wa Kristo. “Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake.[1] Kusudi la Mungu la milele ni kutufanya sisi tuwe kwenye mfano wa Kristo. Hii ndiyo maana ya kuwa mtakatifu.
Mfano mmoja unaoshangaza sana wa wazo hili unapatikana kwenye barua ya Paulo kwa Wakorintho. Kanisa hili lilikuwa na matatizo mengi sana, lakini bado Paulo aliwataja kama “watakatifu” na akawataka wageukie maisha matakatifu. Inawezekanaje kundi hili la waamini wachanga, linalopigania kuachana na tabia zao za zamani za kipagani, litegemee kuwa takatifu? Paulo alijibu, “Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye.”[2]
Kwa kuwa Kristo alikuja kwa ajili ya dhambi zetu, tunaweza tukawa “wenye haki wa Mungu.” Katika Agano la Kale, dhabibu kwa ajili ya dhambi zilifunika wingi wa dhambi kwa wale waliomwendea Mungu kwa Imani. Hata leo, damu ya Kristo inafunika wingi wa dhambi kwa wale wote wanaomwendea kwa Imani. Lakini Paulo anaahidi jambo lingine lililo zaidi ya kufunika. Siyo kwamba tu “tunafunikwa,” bali tunabadilishwa. “Kwa kuwa tumepatanishwa na Mungu,” tumefanyika “wenye haki wa Mungu.” Paulo anaandika:
"Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya. Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo."[3]
Yesu hakufa ili kufunika uovu wetu unaoendelea dhidi ya Mungu. Kupitia Kristo, sisi ni uzao mpya. Sisi siyo waasi tena; ni viumbe vipya ambavyo vimepatanishwa na Mungu mtakatifu.
Hali hii ya kubadilishwa inaenda mbali zaidi kuliko tabia ya nje peke yake. Paulo aliomba kwa ajili ya Wathesalonike:
"Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo."[4]
Neno “Kabisa” linabeba wazo la kufanywa mtakatifu katika maeneo yote yanayohusika. Aya hii inaweza kutafsiriwa kama “utakaswe wewe kila eneo.” Paulo aliomba kwamba hawa waamini wabadilishwe kwenye hali zao zote za “nafsi, mwili, na roho.” Aliahidi, “Yeye ni mwaminifu ambaye awaita, naye atafanya.”[5]
Mabadiliko haya huathiri maeneo yote ya maisha. Kwa Wafilipi, Paulo anaandika kuhusu njia mpya yakufikiri. Anaiita “Akili ya Yesu.” Paulo anaelezea juu ya kujitoa kwa Kristo kwa hiari yake mwenyewe na kwa ajili ya mapenzi ya Baba. Yesu “alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.”[6]
Paulo hajasema, “Unyenyekevu wa Kristo ndio njia nzuri ya kuishi, lakini bila shaka haiwezekani kwa wewe na mimi.” Badala yake anasema, “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu.”[7] Wazo hili ni lako; unaweza kumfanania Kristo!
Tunaweza kuwa na roho ileile ya kupenda kujitoa kama ilivyomwongoza Yesu kujitoa kwa ajili ya mapenzi ya Baba yake. Tunaweza kuwa na ufahamu wa Kristo. Tunaweza kuyaangalia maisha kupitia macho ya Yesu Kristo. Hii haitokei kupitia maazimio mazuri, bali kupitia mioyo iliyobadilishwa. Tunaitwa tuwe kama Kristo, siyo kwa matendo peke yake bali kutoka ndani ya moyo. Tunaitwa tuwe na akili ya Kristo.
Utakatifu ni Tabia inayomfanania Kristo
Watu wengine wanaweza wakanena, “Moyo wangu unamfanania Yesu, lakini matendo yangu sivyo. Kwa ndani, nia zangu ni njema, lakini kwa nje siishi kama Kristo.” Mitume hawakuweza kukubaliana kuhusu huu mgawanyiko wa asili yetu ya ndani na ya nje. Asili yetu ya ndani itadhirishwa kwenye matendo yetu ya nje. Kuwa mtakatifu maana yake ni kuwa kama Kristo katika tabia zetu.
Ujumbe huu unaonekana kwenye Nyaraka zote za Agano Jipya. Paulo alizungumzia kwamba Kristo alijitoa mwenyewe kwa ajili ya Kanisa “ili makusudi alitakase.” Kristo alijitoa mwenyewe ili amfanye bibi harusi wake mtakatifu. Kristo anamwandaa bibi harusi. Analiandaa Kanisa “apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa.”[8]
Je, unaweza kufikiria bibi harusi wa duniani amwambie mume wake, “Sitakuwa mwaminifu kwako kwa mwili wangu, lakini moyo wangu utakuwa safi?” Kwa hakika haiwezekani! Hata Paulo hawezi kufikiria bibi harusi wa Kristo aseme, “Moyo wangu ni msafi, lakini matendo yangu hayatakuwa masafi.” Kanisa linaitwa liwe bibi harusi “liwe takatifu lisilo na mawaa.”
Paulo aliandikia Wakristo wa Thesalonike. Kanisa hili lilikuwa na mchanganyiko wa waamini waliotokana na Wayahudi na waamini wapya waliobadilishwa kutoka madhehebu ya kipagani ya Wathesalonike. Waamini waliotokana na Wayahudi walizijua amri za Agano la Kale kuhusiana na tabia ya utakatifu, lakini wapagani wamekuwa wakiishi katika mazingira ya uasherati.
Paulo aliwafundisha hawa waamini wapya ni nini maana ya kuishi maisha ya utakatifu. Aliomba Mungu ili, “apate kuifanya imara mioyo yenu iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu.”[9] Waamini hawa wapya walipaswa wawe watakatifu ndani ya mioyo yao, na walitakiwa wawe watakatifu katika tabia zao. “Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu.“ Utakaso haugusi mioyo yao tu, bali unasababisha watu kuishi katika hali tofauti:
“Mwepukane na uasherati”
“Kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima; si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua Mungu.
“Mtu asimpunje ndugu yake wala kumkosa katika jambo hili.”[10]
Kuwa mtakatifu ni kuwa na moyo unaomfanania Kristo na ambao unahamasisha tabia inayomfanania Kristo. Kuwa mtakatifu ni kufanana na Kristo.
Utakatifu ni Upendo unaomfanania Kristo
Vitabu vya Injili vinaonyesha kwamba utakatifu ni upendo kwa Mungu na kwa jirani zetu. Paulo anaunganisha tabia inayomfanania Kristo na Upendo unaomfanania Kristo. Anawapa changamoto Wakristo wa Efeso, “mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa.” Watamfuataje Mungu? Kwa kuishi katika upendo unaomfanania Kristo. “Mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato.”[11]
Wanapokuwa wakitembea kwenye maisha ya upendo wa kujitoa bure, Wakristo wanadhihirisha sura ya Mungu. Kuwa mtakatifu ni kupenda kama Kristo alivyopenda. Katika Warumi 14, Paulo anadhihirisha kwa vitendo upendo huu unaomfanania Kristo. Anawataka waamini kujitoa dhabihu ya uhuru wa dhamira yao kwa ajili ya ndugu aliye mdhaifu. Kwa nini? Kwa sababu, “Ndugu yako akiingia huzuni kwa sababu ya chakula, umeacha kwenda katika upendo.”[12] Kama uhuru wangu utasababisha ndugu yangu (katika Kristo) kuanguka, nitakuwa sitembei katika upendo. Kristo alisalimisha uhuru wake kwa sababu ya upendo kwa ajili ya wengine; tumeitwa ili kusalimisha haki zetu kwa sababu ya upendo kwa wengine. Huu ndio upendo unaomfanania Kristo.
Ufafanuzi muhimu sana wa Paulo wa nini maana ya kupenda kama Kristo uko katika
1 Wakorintho 13. Kwa kanisa lililokabiliwa na mgawanyiko, tabia za kujiona, wivu, na majivuno, Paulo aliandika:
"Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli."[13]
Katika kitabu cha 1 Yohana, mtume anasisitiza mambo ya vitendo kuhusu upendo unaomfanania Kristo. 1 Yohana inaonesha upendo unaomfanania Kristo ukoje.
Upendo huhitaji utiifu. Kama tunampenda Mungu, tutamtii yeye.[14] Hatuwezi kutenganisha upendo na utii.
Upendo unahitaji nia moja. Kama tunampenda Mungu, hatutaupenda ulimwengu. “Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.” [15] Hatuwezi kwa wakati mmoja kumpenda Mungu na huku tunataka kuupenda ulimwengu ambao unapingana na Mungu. Mtu mtakatifu anampenda Mungu kwa moyo usiogawanyika.
Upendo unahitaji mahusiano. Kama tunampenda Mungu, tutawapenda na Wakristo wengine. “Yeyote anayempenda Mungu anapaswa pia kumpenda na ndugu yake.” Hakika,“Mtu akisema, ‘Nampenda Mungu,’ naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo….”[16] Yohana anafundisha kwamba haiwezekani mtu ampende Mungu wakati akiwa anamchukia ndugu yake wa Kikristo.
Ni nini matokeo ya huu upendo wa kumfanania Kristo? Ni kuwa na Imani na Mungu. “Tukipendana, Mungu hukaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani yetu.”[17] Upendo huu mkamilifu unatupa “tuwe na ujasiri katika siku ya hukumu,” na “huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu.”[18]
Tutauishije huu upendo mkamilifu? “Kwa kuwa tunajua kwamba maisha yetu katika dunia hii, ni maisha yake tunayoyaishi ndani yetu.”[19] Tunaweza peke yake kuwa mfano wa upendo unaomfanania Kristo kwa kupitia Kristo aishiye ndani yetu.
Maisha ya Utakatifu: Wewe ni mtakatifu; fuata utakatifu
Tommy alikuwa na hamu ya kuwa mtu mtakatifu. Kwa bahati mbaya, uelelewa wa Tommy kuhusu utakatifu ulikuwa zaidi kwenye msingi wa mihemuko na hisia kuliko Maandiko. Kwa sababu ya hilo, Tommy alivuka kiwango cha fundisho moja hadi lingine.
Kwa muda, Tommy alifunga mara kadhaa, aliomba kwa masaa, na alijaribu kujiweka katika nidhamu ya utakatifu yeye mwenyewe. Alikuwa na uhakika kwamba tunakuwa watakatifu kwa kupitia nidhamu yetu wenyewe.
Tommy baadaye alivunjika moyo na akaachana na juhudi hizo. Akaanza kuukulia uzembe katika nidhamu ya utakatifu na kurudia kwenye dhambi. Nipomwuliza kuhusu eneo la dhambi linalomsumbua, Tommy alisema, ”Ninaishi kwa neema na sihitaji kuwa na nidhamu. Mungu atanifanya niwe mtakatifu atakapokuwa tayari.”
Kwa wakati mwingine, Tommy akaomba sana kwa ajili ya kipawa cha kiroho cha ajabu. Aliamua kwamba utakatifu ni juu ya vipawa vya kiroho na nguvu za nje.
Utafiti wa Tommy kuhusu utakatifu uliwekwa kwenye msingi wa mhemuko kuliko usomaji kwa makini wa Maandiko. Hakusoma Biblia ili aweze kuelewa jinsi ya kuishi maisha ya utakatifu kila siku.
Nyaraka za Agano Jipya zinafundisha mambo ya ukweli na muhimu yanayohusiana na maisha ya utakatifu. Kama tutazisahau kanuni hizi, tutakuwa hatuna msimamo katika uelewa wetu kuhusu utakatifu. Mitume waliandika kutuonyesha jinsi ya kuishi maisha ya utakatifu kila siku ambayo Mungu ametuitia.
Ulifanywa kuwa mtakatifu; Unafanywa kuwa mtakatifu
Wakati Paulo alipowaandikia “watakatifu,” alikuwa anasema, “wewe ni mtakatifu.” Mtakatifu ni mtu ambaye tayari ni mtakatifu, lakini Paulo aliwaandikia hawa watakatifu akiwaambia, “Ni lazima muwe watakatifu.” Ninyi ni watakatifu, mnapaswa muendelee kuukulia utakatifu.
Uwiano huu unaonekana ukijirudia-rudia katika hizi Nyaraka. Kama Waamini, tayari sisi ni watakatifu, lakini tuendelee kukua katika utakatifu na kutembea na utii kwa Mungu.
Mwandishi wa kitabu cha Waebrania anaonyesha kwamba tulifanywa watakatifu kwa kifo cha Yesu. “Hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.”[1] Tumetakaswa kupitia kifo cha Yesu.
Mwandishi anaendelea, “Maana kwa toleo moja amewakamilisha hata milele hao wanaotakaswa.”[2] Aya hii inahusisha maneno mawili yaliyofanana kwa ajili ya mandhari ya utakatifu, Kupitia kifo chake, Kristo “amewakamilisha” (teios) wale wote ambao “wametakaswa” (hagiazo). Aya hii inatuambia kwamba:
Tulifanywa kuwa Watakatifu; “Alitufanyia ukamilifu kwa nyakati zote…”
Kristo alikufa ili tuweze kuwekwa huru kutokana na nguvu ya dhambi. “Kwa ajili hii Yesu naye, ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa nje ya lango.”[3] Kusudi la Mungu kuwafanya watu wake wawe watakatifu lilitimilika kupitia kifo cha Yesu. Tumefanywa kuwa wakamilifu.
Tumefanywa kuwa Watakatifu: “Wale Ambao Wanatakaswa”
Kifo cha Yesu kimekamilisha kusudi la Mungu la utakaso kwa nyakati zote, lakini ukuaji wetu katika utakatifu unaendlea katika maisha yetu yote. Ni ukuaji ulio endelevu. Kupitia kifo cha Yesu, sisi ni watakatifu; kupitia kifo cha Yesu, sisi tunafanywa kuwa watakatifu.
Ushuhuda binafsi wa Paulo unaelezea kanuni hii. Katika Wafilipi 3, Paulo anaandika kwamba yeye bado hajawa mkamilifu, lakini katika aya nyingine baadaye anasema, anajirejea mwenyewe kama ambaye amekamilika (“wale wote miongoni mwetu ambao wamekua”). Maneno yaliyokuzwa kwa weusi katika dondoo ifuatayo, kwa pamoja yanatokana na teleios. Maneno yote mawili yanaweza kitafsiriwa kama “mkamilifu.”
"Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu (teleios); la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu… Basi sisi tulio wakamilifu (teleios) na tuwaze hayo; na hata mkiwaza mengine katika jambo lo lote, Mungu atawafunulia hilo nalo."[4]
Paulo anasema, “Mimi bado siyo mkamilifu.” Kisha anaendelea, “Wale miongoni mwetu walio wakamilifu.” Paulo bado hajafikia kwenye malengo yake; anakua katika utakatifu wake. Kwa hali hiyo, bado hajawa mkamilifu. Lakini, Paulo anajaribu kukaza kila msuli ili aweze kulifikia lengo. Amejipanga kumaliza mbio. Kwa ufahamu huu tayari Paulo ni mkamilifu. Paulo anaweza kusema “Bado mimi siyo mkamilifu” na “Mimi ni mkamilifu” katika ibara hiyo moja.
Kuwa mkamilifu haina maana kwamba tumepanda ngazi ya kazi inayotufanya sisi tuwe wakamilifu. Badala yake, ina maana kwamba tumejisalimisha kwa neema ya Mungu katika maisha yetu. Ni kwa wakati huo huo kwamba kuna wakati ambao Mungu anaelekeza mioyo yetu kuelekea upande wake. Ni mchakato kwamba nyendo zetu kumwendea yeye zitaendelea katika maisha yetu yote.[5]
Mfikirie mchezaji wa golfu anayepiga mpira kuelekea kwenye shimo; ni shuti kamili. Shuti haliwi kamili tu mpira unapotua kwenye shimo. Unapokuwa angani ukienda, shuti hilo tayari ni kamilifu; ukiwa kwenye mkondo wa kuelekea shimoni. Shuti hilo liko kamilifu tangu wakati mchezaji alipoupiga mpira.[6]
Kwa njia hiyo hiyo, Paulo alikuwa anaelekea kwenye lengo la mwisho. Alishaanda mwelekeo wake na alikuwa akisonga mbele kukaribia lengo lake kwa moyo usiogawanyika. Alikuwa bado hajawa mkamilifu, lakini alikuwa kwenye njia ya kufikia kwenye lengo lake. Hakuwa bado amekamilika, lakini tayari alikuwa mkamilifu.
Kama waamini, ni watakatifu “watakatifu” ambao wamekubalika na Mungu kupitia kwa Kristo, lakini tumeitwa tujitoe wenyewe kama “dhabihu iliyo hai” inayoendelea kukua kila siku katika utii na kujisalimisha. [7] Tayari tumeshafanyika watakatifu; tunaendelea kufanywa watakatifu.
Ninyi ni Watakatifu; Lazima muishi kama Watakatifu
Paulo aliandika kwa “watakatifu” walioshi Korintho. 1 Wakorintho imeelekezwa kwa watu watakatifu, “waliotakaswa katika Kristo.”[8] 2 Wakorintho imeelekezwa kwa “Kanisa la Mungu lililoko Korintho, likiwa na watakatifu wote wa eneo lote la Akaya.”[9] Walikuwa watakatifu – lakini walikuwa na mengi ya kujifunza jinsi ya kuishi kama watakatifu.
Kuna njia mbili ambazo Wakristo wanashindwa kuelewa ukweli. Kwanza, baadhi ya Wakristo husema, “Ninaitwa mtakatifu kwa sababu Mungu anaona haki ya Kristo ndani yangu kuliko anavyoiona dhambi yangu. Utakatifu wangu ni ‘uongo wa kisheria.’ Kamwe siwezi kuwa mtakatifu katika dunia hii, lakini hata hivyo, Mungu ananiita niwe mtakatifu.” Kitabu cha Warumi 6 kinaweka wazi kwamba hili jibu haliwezi kabisa kukubaliwa na Paulo. Watu watakatifu ni lazima wayaishi maisha matakatifu.
Pili, Wakristo wengine husema, “Mimi ni mtakatifu. Kamwe sishuki kwenye viwango vya chini vya Mungu alivyoweka kwa ajili ya kuwa mkamilifu. Kamwe situbu kwa sababu mimi sina makosa. Mimi ni mtakatifu!” Paulo anakataa msimamo huu wa pili kama pia alivyokataa msimamo wa kwanza. Paulo aliandika kuwafundisha “watakatifu” wa Korintho kuishi maisha matakatifu. Wanachokosa ni ufahamu na ukuaji wa kiroho, kwa hiyo Paulo anawafundisha hawa watakatifu jinsi ya kuishi kama watakatifu. Watu watakatifu ni lazima wayaishi maisha matakatifu.
Jiji la Korintho lilijulikana sana kwa tabia chafu zisizo za kimungu kwa wakazi wake. Paulo anawataka waamini waishio katika jiji hili la maovu wawe na tabia ya utakatifu. Wajiepushe na tabia ya uasherati kwa sababu “miili yao ni viungo vya Kristo.”[10] Paulo anaorodhesha tabia chafu ambazo hazitakiwi kabisa kwenye ufalme wa Mungu:
Baada ya orodha hii ya dhambi, Paulo anahoji, “Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii.” Paulo anawaandikia watu wake ambao wameshiriki sana kwenye haya matendo ya dhambi. Kama waamini, Paulo anawategemea waachane na mfumo wa maisha ya zamani! Inapokumbukwa hali yao ya dhambi ya zamani, je, watu hawa wanawezaje kuishi maisha masafi? Paulo anatoa jibu:
"Lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu."[12]
Dhambi za 1 Wakorintho 6:9-10 zimefutwa kwa mabadiliko ya 1 Wakorintho 6:11. Mabadiliko haya siyo ya utaratibu wa kisheria; hakuna mahali popote Paulo anapendekeza kwamba, “Mtaendelea kutenda dhambi hizi, lakini Mungu ataendelea kuwahesabia haki hata pamoja na madhaifu yenu ya tabia.” Hapana! Anasema, “Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa.” Wakristo wa Korintho kamwe hawatarejea kwenye dhambi zao za zamani. Paulo anasema, “Ninyi ni watakatifu. Fanyeni kama utakatifu unavyowataka mfanye!” Walikuwa wameoshwa; walikuwa wametakaswa; walikuwa wamefanywa watakatifu. Ni watakaifu; ni lazima waishi kama watakatifu.
Wakati kijana anavyojiunga na jeshi, anapewa sare ya jeshi inayomtambulisha kwamba yeye ni mwanajeshi. Wakati huo huo, anapewa mwongozo ambao unaelezea Msimbo wa Maadili ya Jeshi. Sare peke yake haitoshi; ni lazima aweze kuishi kulingana na msimbo wa maadili.
Inachukua muda mrefu zaidi kujifunza msimbo/kanuni za maadili kuliko kuvaa sare. Mwanajeshi mpya ni lazima ajifunze kuishi katika mazingira yanayoendana na ile sare ya jeshi aliyovaa. Ni lazima aweze kukomaa kama mwanajeshi. Mara nyingi, huyu mwanajeshi mpya inabidi akumbushwe kuhusu sheria za kijeshi. Je, utendaji wake ni mkamilifu? Hapana. Lakini, dhamira yake ya kuwa mwanajeshi iko kamilifu? Ndiyo. Kwenye siku ya kwanza jeshini, yeye ni mwanajeshi; lakini atachukua siku nyingi akijifunza jinsi ya kuishi kama mwanajeshi.
Jaribu kumfikiria kijana anayesema, “Nataka niitwe mwanajeshi, lakini sitataka nifuate Msimbo wa Maadili.” Ananunua sare ya kijeshi, lakini haishi kwa mujibu wa Msimbo wa Maadili. Je, huyu ni mwanajeshi wa kweli? Hapana. Anajifanya tu kuwa mwanajeshi lakini sivyo.
Nyaraka za Agano Jipya zimendikwa kwa waamini ambao “wamemvaa Kristo.” Sasa wanajifunza jinsi ya kuishi maisha matakatifu. Katika Waefeso 4-6 tunajifunza maisha ya utakatifu yakoje kwenye mahusiano ya kifamilia, mahusiano na kanisa, na katika maadili ya biashara. Katika Wagalatia 5, tunajifunza tunda la maisha yaliyofuatana na hatua za Roho Mtakatifu. Katika 1 Petro, tunajifunza jinsi ya kuishi maisha ya utakatifu wakati wa kukabiliana uso kwa uso na mateso. Tunaposoma kitabu cha Yakobo, tunajifunza jinsi mtu mtakatifu anavyopaswa kuutawala ulimi wake.
Paulo aliandika kwa waamini wa Kolosai, “Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.” Waamini hawa walikuwa wamekufa katika dhambi; wako hai katika Kristo; siyo watumwa wa dhambi tena; ni watakatifu. Lakini Paulo anaendelea, “Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi.”[13] Mmekufa katika dhambi; achilieni dhambi zife. Mmekuwa watakatifu; lazima muishi kama watakatifu.
Kanuni imeelezwa mwanzoni mwa ibara.
"Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi."[14]
Paulo anasema, “Siku hadi siku, endelea kutafuta vitu vya mbinguni. Siku hadi siku, endelea kuweka akili yako kwenye mambo ya Mungu.” Msingi wa maisha ya utakatifu ni kuweka akili yako kwenye mambo ya Mungu. Umefanywa kuwa mtakatifu (“umeinuliwa na Kristo”), kwa hiyo kuwa mtakatifu, (“weka akili yako kwenye mambo yaliyo juu”).
Ni nini matokeo ya haya maisha matakatifu? “Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu.”[15] Maisha ya utakatifu yanakuandaa wewe ukaishi milele na Mungu aliye mtakatifu. “Henoko akaenda pamoja na Mungu, naye akatoweka, maana Mungu alimtwaa.”[16] Kutembea kwa utakatifu katika dunia hii kulimwandaa Henoko kwa ajili ya maisha ya umilele na Mungu. Kutembea na Mungu kwenye utakatifu katika ulimwengu huu kunatuandaa sisi “kuonekana na Kristo katika utukufu.”
Nyaraka katika Agano Jipya zimeandikwa kwa ajili ya watakatifu. Tumefanywa watakatifu kupitia damu ya Yesu Kristo. Tumemvua mtu wa kale na kumvaa mtu mpya. Sasa tunajifunza siku hadi siku ni nini maana ya kuwa mtakatifu. Tunabadilishwa siku hadi siku kuwa katika sura ya Mungu. Je, utendaji wetu ni mkamilifu? Hapana. Je, ahadi yetu ya kuwa watakatifu iko kamili? Ndiyo. Sisi ni watakatifu. Tunajifunza kuishi kama watakatifu.
Mungu anakufanya uwe Mtakatifu; Lazima ufuate Utakatifu
Katika kitabu cha Walawi, Mungu anasema, “Jitakaseni basi, iweni watakatifu.” Hili ni agizo ambalo kila mtu alipaswa kulifuata. Katika aya inayofuata, Mungu anaahidi, “Mimi ndimi Bwana niwatakasaye ninyi.”[17] Hii ilikuwa ni ahadi ya Mungu ya kile ambacho angefanya. Kuuelewa utakatifu, ni lazima tuweke kwenye uwiano kweli mbili zifuatazo:
Utakatifu ni zawadi kutoka kwa Mungu. Mungu huwafanya watu wake wawe watakatifu.
Utakatifu ni agizo la Mungu; Mungu anawaagiza watu wake “wafuate utakatifu.”
Mafarisayo walikumbuka tu, “Ni lazima kufuata utakatifu.” Waliamini kwamba wanaweza kuwa watakatifu kwa nguvu zao wenyewe. Majibu ya Nyaraka za Agano Jipya, “Mungu anawafanya kuwa watakatifu.”
Baadhi ya Wakristo katika Kanisa la mwanzo walikwenda kinyume tena mbali zaidi. Waliamini, “Kama Mungu anataka kutufanya sisi tuwe watakatifu, atafanya. Sisi hatuna la kufanya.” Majibu ya Nyaraka za Agano Jipya, “Lazima kufuata utakatifu.”
Kujisalimisha na kufuata yote kwa pamoja ni muhimu katika utakaso. Mungu anatufanya tuwe watakatifu; lazima kufuata utakatifu. Tunajisalimisha kwa Mungu na kumruhusu atubadilishe, lakini tunakaza mwendo, tuifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu kwetu.[18] Paulo alielewa kwamba kuziamini ahadi za Mungu haina maana kwamba hatupo tena katika kukaza mwendo ili tuifikie ile mede ya thawabu. Tumepewa nguvu za kufuata utakatifu kwa sababu Mungu anatufanya tuwe watakatifu.
Wakati watoto wangu walipokuwa wadogo, walikuwa wanaweza kusoma Andiko kwa sauti kwenye kipindi chetu cha maombi ya familia. Siku moja, msichana wetu akautana na andiko la Wafilipi 2:12. Kwa hamasa kubwa, Stacey (binti yetu) akapaaza sauti, “Utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka!” Alikuwa amevutiwa sana na agizo hili la “utimizeni wokovu wenu wenyewe.” Lakini Paulo anaendelea, “Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu.” Kazi yetu imekamilika kwa sababu ya kazi ya Mungu.
Kinyume na Imani ya Wakristo wengi, Kazi ya Mungu inakamilishwa wakati “tunapoufanyia kazi wokovu wetu.” Ina maana kwamba tunapata utakatifu kutokana na kazi zetu? Hapana kabisa! Paulo anaendelea, “Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.”[19] Ni Mungu atoae hamu ya (kutaka kutenda); ni Mungu anayeiwezesha kazi. Bila Mungu afanyaye kazi ndani yako, kazi zetu ni bure. Hatuwezi kujifanya wenyewe watakatifu, lakini Mungu hatatufanya tuwe watakatifu mbali na ufuatiliaji wetu wenyewe wa utakatifu.
Paulo aliwakumbusha Wakorintho juu ya ahadi za ajabu za Mungu. “Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike.”[20] Kisha akawaagiza kuishi maisha ya utakatifu. “Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu.”[21] Kwa sababu ya ahadi za Mungu “tunajitakasa nafsi zetu na uchafu wote.” Ahadi za Mungu za kutufanya tuwe watakatifu zinatupa uhakika wa kufuata utakatifu.
Akiwaandikia Wakristo wa Thesalonike, Paulo aliomba kwamba Mungu “aifanye mioyo yenu isiwe ya lawama ndani ya utakatifu.”[22] Hii ni kazi ya Mungu. Kisha, Paulo akaanza kufundisha, “Jinsi gani utembee na kumpendeza Mungu.” Kwanini? “Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu.”[23] Mungu alikuwa anawafanya Wakristo wa Thesalonike kuwa watakatifu, kwahiyo ni lazima wafuatilie maisha matakatifu.
Kitabu cha Wagalatia kimeandikwa kwa waamini waliokuwa wanajaribu kurejea kwenye wokovu kwa matendo ya sheria. Paulo aliwakumbusha kwamba “mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali kwa Imani ya Kristo Yesu; maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki.“[24] Kama kuhesabiwa haki kwa Imani ndiyo mwisho wa injili, huu ungekuwa waraka sahihi kwa Paulo kwa kusema, “Mmethibitishwa kwa imani. Kwahiyo sasa mnaweza kuishi kama mpendavyo na mtaingia mbinguni. Sehemu yako mbinguni ni ya uhakika.” Lakini Paulo hasemi hivyo, badala yake anasema:
"Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake. Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho."[25]
Kuweka hatua, maana yake ni “kutembea bega kwa bega na kiongozi.” Inaelekeza nidhamu na kujitawala binafsi. Inaelekeza kuishi kwenye uongozi wa Roho Mtakatifu na siyo kwa matamanio yetu. Mungu aliwafanya Wagalatia wawe watakatifu, lakini ni lazima waendelee kufuata utakatifu.
Mwandishi wa kitabu cha Waebrania aliandika kwamba Mungu “huturudi kwa faida yetu, ili tuushiriki utakatifu wake.” Huu ni ukweli wa kushangaza! Mtu aliyeanguka anaweza kushiriki kwenye utakatifu wa Mungu. Huu siyo aina ya muungano wa siri kama ilivyo kwa ibada za kipagani. Haya ni mafundisho kamili ya kimatendo kuhusiana na nidhamu ya kiroho. Anaandika kuhusu “tunda la haki,” kuhusu amani, na kuhusu dhambi kama vile uchungu na uasherati.[26] Haya siyo mafundisho ya kumfikia Mungu kwa mafumbo, bali ndiyo Ukristo wa kawaida. Mungu anawaita watoto wake wawe watakatifu; anawategemea watoto wake washiriki katika utakatifu wake.
Tunawezaje kushiriki katika utakatifu wa Mungu? Tunashiki utakatifu wa Mungu pale tunapokuwa “washirika wa tabia ya asili ya Uungu.”[27] Petro anaonyesha kwa pamoja nguvu za Mungu za kutufanya tufanane naye na juhudi zetu za kukulia katika sura ya Mungu.
Kwanza, Petro anaahidi kwamba tunaweza kuwa washirika wa tabia ya Uungu:
"Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya asili ya Uungu, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa."[28]
Mungu anatufanya tuwe watakatifu. “Uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote” vipasavyo kwa ajili ya “maisha na utauwa.” Utauwa siyo ndoto isiyowezekana; Mungu “alishatupa ahadi zake za thamani na kubwa mno.” Moja ya ahadi hizi ni kwamba “tutakuwa washirika wa tabia ya asili ya Uungu.” Ahadi kwamba tunaweza kufanana na baba yetu wa mbinguni kwa ajili ya kila mtoto wa Mungu. Jambo hili halitimizwi kupitia juhudi zetu wenyewe; utauwa ni zawadi inayotokana na neema ya Mungu. Kupitia uwezo wa Mungu, tunaweza kuishi kwa upatanifu na tabia ya Mungu. Mungu anatufanya watakatifu.
Kisha, Petro anaendelea:
"Naam, na kwa sababu iyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika Imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa, na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa, na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo. Maana mambo hayo yakiwa kwenu na kujaa tele, yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na matunda, kwa kumjua Bwana wetu Yesu Kristo."[29]
Kwa kuwa nguvu ya Uungu ya Mungu imetufanya sisi tuwe washirika wa tabia ya asili ya Uungu, inatupasa “tufanye kila jitihada” kukua katika wema, maarifa, kiasi, utauwa, upendano wa ndugu, na upendo. Kwa sababu ya yale ambayo Mungu ametenda, tunapaswa kufuata utakatifu.
Petro hajajaribu kutushauri kwamba tujifanye wenyewe watakatifu kwa “kufanya kila jitihada.” Hapa hafundishi ushikiliaji mno wa sheria. Hatupati upendeleo wa Mungu kupitia nguvu zetu wenyewe. Hata hivyo, Petro anatutaka sisi tuelewe kwamba hatuwezi kuyaishi maisha ya utakatifu pasipo nidhamu binafsi.
Tunafuata utakatifu kwa sababu ya neema ya Mungu. Neema yake inatuwezesha katika kufuata maisha ya utakatifu. Kwa sababu ya Uweza wake wa Uungu (2 Petro 1:3-4), “tunafanya kila jitihada” kukua (2 Petro 1:5-8). Kufuata kwetu utakatifu siyo takwa la kisheria; ni hamu ya asili ya moyo uliobadilishwa. Kama sisi kwa ukweli ni watoto wa Mungu tutapenda tukulie ndani ya utakatifu. Kama kweli sisi ni watoto wa Mungu, tutapenda kuona kusudi la Mungu likitimia katika maisha yetu.
[30]“Paulo alisema, ‘Nimesulubiwa pamoja na Kristo....’ Hajasema, ‘Nimefanya maamuzi ya kumuigiza Yesu Kristo,’ au, ‘Kwa hakika nitafanya juhudi za kumfuata Yeye’ — lakini ‘Nimekubaliwa na yeye katika mauti yake.’”
- Oswald Chambers
Nitayaishije Maisha ya Utakatifu? “Siyo Mimi, Bali Kristo”
Akiwaandikia Wakristo wa Filipi, Paulo anamlenga Yesu kama mfano wa tabia wanayopaswa kuionyesha. “Kristo akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.”[1] Paulo alitaka hawa waamini waelewe kwamba njia ya watoto wa Mungu ni njia ya unyenyekevu, na siyo njia ya kujikweza. Tunapaswa kuwa na “akili ya Kristo.”
Inawezekana tukashawishika kusema, “Ni kweli, Yesu aliishi maisha ya utakatifu. Alikuwa ni Mwana wa Mungu. Hiyo hainisaidii mimi. Mimi siyo Yesu!” Lakini tunawezaje kufuata mfano wa Yesu? Paulo alifundisha kwamba Roho wa Kristo huishi ndani ya mwamini.
Paulo aliandika kwa Wakristo wachanga, “Ninyi hamuufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake.”[2] Tunaishi maisha matakatifu siyo kwa nguvu zetu bali kwa nguvu za Roho Mtakatifu.
Ushuhuda wa Paulo mwenyewe unaonyesha ushuhuda wa mabadiliko yake. Paulo anayaona maisha yake yaliyopita kama ya Mfarisayo anayejaribu kutimiza maagizo ya sheria kwa nguvu zake mwenyewe. Anakumbuka wakati ambao alikuwa na nia ya kufanya yaliyo mema, lakini hakuwa na uwezo wa kutenda mema. Anasema, “Basi sasa si mimi nafsi yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.”[3] Jitihada za Paulo za kuwa mwenye haki kwa nguvu zake mwenyewe ziliongozwa na kushindwa.
Baada ya kukutana na Kristo, ushuhuda wa Paulo ulibadilika kutoka “siyo mimi, bali dhambi” hadi kwenye “siyo mimi, bali Kristo.”[4] Paulo ataweza kuishi maisha ya Kikristo ya ushindi kwa sababu sasa Kristo anaishi ndani yake.
Paulo aliwatia moyo Wakorintho, “Au hamjijui wenyewe, kwamba Yesu Kristo yu ndani yenu?”[5] Tunaweza kumfanania Kristo kwa sababu anaishi ndani yetu. Mtheolojia wa Kilutheri aitwaye Dietrich Bonhoeffer aliliweka hivi: Kuwa Mkristo inamaanisha kwamba “nafasi ambayo wakati mmoja ilikuwa imekaliwa na mzee, sasa imekaliwa na Yesu Kristo.”[6]
Kristo anaishi ndani yetu, au kuelezea kanuni hii kwa njia nyingine inayofanana na hiyo, “Tunaishi ndani ya Kristo.” Mojawapo ya maneno ambayo Paulo amekuwa akitumia sana katika huduma yake ni “ndani ya Kristo.” Paulo anatumia fasiri nyingine ya “ndani ya Kristo,” “ndani yake,” “ambaye” na “ndani ya mwana” zaidi ya mara 150 katika nyaraka zake. Paulo akirudia mara kwa mara huelekeza kuhusu sehemu yetu ndani ya Kristo kama siri kwa maisha ya Mkristo. Ushindi wa kila siku unakuja kwa sababu tuko ndani ya Kristo.
Maisha yetu ya zamani yalikuwa “ndani ya Adamu” kwenye anguko la nafsi yetu ya dhambi. Maisha yetu mapya yako “ndani ya Kristo,” katika nguvu ya Bwana aliyefufuka ambaye anatupa ushindi wa kila siku dhidi ya dhambi.
Ndani ya Adamu, tulitembea katika giza; ndani ya Kristo tunatembea katika nuru.
Ndani ya Adamu, tulikuwa watumwa wa dhambi; katika Kristo sisi ni watumwa wa uadilifu na haki.
Ndani ya Adamu, tulifurahi katika dhambi za mwili; ndani ya Kristo tulivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba.”[7]
Uelewa huu ni muhimu sana kwa ajili ya maisha ya ushindi. Tunapojiona tuko ndani ya Adamu (“watenda dhambi waliosamehewa” wanaoishi kwenye kifungo cha dhambi), tutaendelea kuangukia kwenye majaribu. Tunapojiona wenyewe ndani ya Kristo (“Watakatifu waliobadilishwa” ambao wana nguvu kupitia Kristo), tutaishi kwa ushindi dhidi ya dhambi. Paulo aliwaambia Wakristo wa Kolosai siri iliyoko ya maisha ya utakatifu: “Basi kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye.”[8] Jinsi tunavyotembea na Kristo, tunafanywa kuwa watakatifu.
Watu wengine wanadhani kwamba utakaso ni kama dozi ya mafua anayokupa daktari ili kuzuia ugonjwa. Wanafikiri kwamba, tunapomwomba Mungu atufanye watakatifu, anatupa “dozi takatifu” ya kutuzuia tusiwe watenda dhambi. Wanaamini kwamba baada ya Mungu kuwa ametutakasa, tunaishi maisha ya utakatifu kwa nguvu zetu wenyewe.
Hakuna mahali popote Biblia inapotoa picha kama hii. Badala yake, tunaishi “ndani ya Kristo.” Sisi ni watakatifu “ndani ya Kristo.” “Sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti.”[9] Sisi ni wale “waliotakaswa katika Kristo Yesu.”[10] Hatufanywi watakatifu kupitia majaribio yetu ya kukata tamaa ya kumuigiza Yesu kwa nguvu zetu wenyewe. Tunakuwa watakatifu kwa kumruhusu Yesu aishi ndani yetu. Kwahiyo, “Yeye aonaye fahari na aone fahari juu ya Bwana.”[11]
Paulo alishuhudia,
"Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika Imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu."[12]
Ushuhuda wa Paulo unaweza kutafsiriwa kama ifuatavyo: “Maisha ninayoishi kwa sasa katika mwili ninaishi kwa Imani ndani ya Yesu Mwana wa Mungu.” Paulo haahirishi mwito wa utakatifu hadi kifo. Paulo anashuhudia kwamba anaishi maisha ya utakatifu “sasa.” Anaishije maisha ya utakatifu? Kwa Imani ndani ya Mwana wa Mungu. Paulo aliyaishi maisha ya utakatifu kwa sababu “wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu.”
Lugha ya Paulo inaendana sambamba na mafundisho ya Yesu katika Yohana 15.
"Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote."[13]
Utakatifu siyo kitu cha kupokea mbali na maisha yetu ndani ya Kristo; utakatifu ni uhusiano unaotakiwa udumishwe. Sisi tuko hai kwa ule muda wote ambao tutakuwa tumebaki tumeunganika na mzabibu. Tunaishi maisha ya utakatifu peke yake kupitia maisha yetu ndani ya Kristo. Mungu mtakatifu anakaa ndani yetu na tuko watakatifu tunapotembea naye.
“Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.”[14] Maisha ya utakatifu hayapatikani kwa nguvu zetu; maisha matakatifu “yamefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.” Tunaishi maisha matakatifu kwa kuishi kila siku na akili ya Kristo. Jinsi tunavyotembea “ndani ya Kristo” tunayo nguvu ya kuishi maisha matakatifu katika dunia hii yenye dhambi. Tunazo nguvu za kuwa watakatifu katika maisha yetu ya kila siku. Hii ndiyo maana yaku mtakatifu.
[15]“Siri ya maisha ya utakatifu haiko katika kumuigiza Yesu, bali katika kuachilia utakatifu wa Yesu ujidhihirishe wenyewe ndani yangu.”
- Oswald Chambers
Utakatifu katika Vitendo: Kuishi Maisha ya Ushindi
Ujumbe wa maisha matakatifu ni ujumbe mzuri. Hata hivyo, Imani ambayo haiwezekani kuiishi katika maisha ya kila siku ni ya thamani ndogo sana kivitendo. Je, inawezekana kuishi maisha ya ushindi dhidi ya dhambi za kukusudia, au je, ujumbe wa maisha matakatifu ni ndoto tu?
Je, ushindi dhidi ya dhambi inawezekana?
Paulo aliahidi kwamba “katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.”[1] Kwa hakika, ahadi hii ya maisha ya ushindi katika Kristo inahusisha pamoja na mambo mengine, ushindi juu ya nguvu ya dhambi. Kama inawezekana kuishi maisha ya ushindi wa kila siku dhidi ya dhambi za kukusudia, kwa nini Wakristo wengi sana wanashindwa kuishi kwa ushindi? Kuna sababu gani za kushindwa kiroho?
Tutashindwa kama hatutaamini kwamba maisha ya ushindi yanawezekana
Ninaridhikakwamba baadhi ya Wakristo hawaishi maisha ya ushindi kwa sababu wamejiridhisha kwamba maisha ya ushindi hayawezekani. Wamesikia mafundisho yakinena kwamba mara kwa mara ni lazima kuanguka kwenye dhambi za kukusudia – na wamekata tamaa ya ushindi wowote dhidi ya dhambi. Kama tunataka tuishi maisha ya ushindi dhidi ya dhambi, ni lazima tuchukue kwa kumaanisha wito wa Yohana: “Nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi.”[2] Yohana aliwaandikia Wakristo kwa uhakika kwamba ilikuwa inawezekana kwao kuishi maisha ya ushindi. Ni lazima tukiri tumaini hili kwa Imani ili kutupa uhakika wa ushindi wakati wa kukabiliana na majaribu.
Tutashindwa kama tutang’ang’ania uzoefu wa zamani wa kiroho au hadhi ya kanisa
Watu wengine wanayaona maisha ya utakatifu kama ni uzoefu wa maramoja tu ambao hauhitaji nidhamu au juhudi endelevu. Wanaamini kwamba wakishashuhudia tu kwamba, “Mungu amenitakasa moyo wangu na kunifanya msafi” hakuna kitu kingine tena kinachotakiwa kifanyike. Hata hivyo, kama Paulo alivyoonyesha, ni lazima tuendelee “kukaza mwendo katika kuifikilia mede ya thawabu.” Ushindi dhidi ya dhambi unahitaji nidhamu endelevu katika maisha. Nitaendelea kusema ”hapana” kwa dhambi na “ndiyo” kwa Mungu.
Baadhi ya mafundisho yanayohusu kujaribiwa kwa Yesu yanamalizia na ushindi wa Yesu dhidi ya majaribu ya Shetani. Hata hivyo, Luka anamalizia maelezo yake kwa kauli muhimu sana ya kuhitimisha kwamba, “Basi alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda.”[3] Hii haikuwa ni mara ya mwisho Yesu kujaribiwa. Ingawaje vitabu vya Injili havijanakili taarifa kamili ya kumbukumbu za majaribu ya mwisho, Luka anabainisha kwa uwazi kwamba Shetani alipanga kumjaribu tena Yesu.
Kamwe hatupaswi kuwa na dhana kwamba tumefikia kilele cha kukua kiroho ambacho hatuwezi kuanguka tena. Badala yake, tunatakiwa tuendelee kujilinda mwili na akili zetu. Shetani anapenda sana kufanya mashambulizi wakati tunapotoka kwenye ulinzi wetu. Maisha ya utakatifu yanahitaji sana umakini wa tahadhari.
Wachungaji na viongozi wa makanisa wanaweza kuingia kwenye majaribu ya kutumainia hadhi zao katika jamii ili kupata ushindi wa kiroho. Tunaweza kuwa na dhana hiyo kwamba kwa sababu tunahubiri ukweli na kujisikia kuwa na upako wa Mungu kwamba hatuwezi kuanguka. Hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa wa kuhubiri ibada ya Jumapili na kuanguka kesho yake Jumatatu. Kamwe tusikae tukitumainia uzoefu wetu wa nyuma au nafasi zetu katika kanisa.
Tutashindwa kama tutajaribu kuishi maisha ya Kikristo kwa nguvu zetu wenyewe
Maisha ya ushindi hayaji kwa nguvu zetu wenyewe bali kwa nguvu za Roho Mtakatifu. Maisha ya utakatifu tunayaishi kila siku kwa nguvu endelevu za Roho Mtakatifu. Hatuwezi kufikia kiwango ambacho kwa nguvu zetu wenyewe tunaweza kuyashinda majaribu ya Shetani. Petro alijisifu, “Hata wajapokunguwazwa wote, lakini siyo mimi…Ijaponipasa kufa nawe, hata hivyo sitakukana kamwe.”[4] Alijiamini sana kwamba angeweza akakabiliana na mashambulizi ya Shetani kwa nguvu zake mwenyewe. Haikuchukua muda alishindwa.
Hata hivyo, tunavyoishi ndani ya nguvu za Roho Mtakatifu, anatupa ushindi dhidi ya majaribu. Kwa njia hiyo hiyo ambayo Yesu alifikwa na majaribu akiwa na nguvu za Roho Mtakatifu, nasi pia tunaweza kukabiliana na majaribu tukiwa na nguvu za Roho Mtakatifu.
Hali kadhalika, wachungaji na viongozi wa makanisa wanaweza kujaribiwa kutegemea nguvu zao wenyewe. Tunapoongoza maombi ya hadhara, tunaweza tukajikuta tunashindwa kuchukua muda binafsi wa maombi na Mungu. Tunapojifunza na kulihuburi Neno la Mungu hadharani, tunaweza kushindwa kuchukua muda wa kumsikiliza Mungu akisemanasi binafsi kupitia Neno lake. Hatupaswi kabisa kuruhusu juhudi zetu katika huduma zetu zidumaze kutembea kwetu binafsi na Mungu pamoja na Roho Mtakatifu kwa ajili ya ushindi wa kiroho.
Kama tukishindwa
Yohana aliwataka waamini waishi maisha ya utakatifu dhidi ya dhambi. “Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi.”[5] Kuna uwezekano mkubwa wa kuishi bila ya kuwepo kushindwa kiroho. Hata hivyo, Yohana alitoa angalizo kwa wale wanaoangukia kwenye dhambi, “Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki.”[6] Uwiano huu ni muhimu - lakini mara nyingi ukipuuzwa.
Kwa upande mwingine, kuna wale wanaowekea mkazo sehemu ya kwanza tu ya aya hii: “Nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi.” Wanafundisha kwamba tunaweza kuishi maisha ya uhuru bila dhambi za kukusudia. Hata hivyo, hawana ujumbe kwa ajili ya wale wanaoshindwa katika dhambi wakati wa kipindi cha madhaifu.
Kwa upande mwingine pia, kuna wale wanaowekea mkazo tu kwenye sehemu ya mwisho ya aya hii: “Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki.” Wanamaanisha kuwa maisha ya ushindi hayawezekani, kwa hiyo tutaendelea kushindwa katika dhambi.
Yohana anatoa uwiano sahihi. Kwanza, maisha ya ushindi yanawezekana; Siwezi kujiachilia tu kwenye majaribu. Lakini la pili, nikianguka katika nyakati za majaribu, ninaye wakili wa kunitetea. Sihitaji kuachana na msimamo wangu wa Kikristo. Sihitaji kukata tamaa. Ndiyo, Mungu ataniadabisha. Lakini ananiadabisha kama Baba wa upendo anavyomuadabisha mtoto – ili kusudi “kuwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani.” Yeye “anatuadabisha kwa faida yetu, ili tuushiriki utakatifu wake. ”[7]
Shetani hutaka kuwashawishi Wakristo watumainie utendaji wao kama njia ya kumfurahisha Mungu. Anataka tujisahau kwamba sisi tulishapatanishwa na Mungu na kwamba sisi sasa ni watoto wake. Tulipokuwa watenda dhambi, “tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake.” Kisha tafakari kwamba, “zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake.” [8]
Kama watenda dhambi, hatukupata kibali cha Mungu; alitupatanisha sisi na yeye mwenyewe kwa kifo cha mwanae. Sasa Paulo anasema, “zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake!” Baadhi ya Wakristo wametokea kuamini kwamba, “Nimeokolewa kwa neema kupitia Imani, lakini ninabakia kuwa nimeokolewa kwa kuwa mzuri sana kustahili upendo wa Mungu.”
Hii ni sawa na mzazi anayesema, “Ndiyo, Nilikupenda sana kiasi cha kukuleta wewe duniani – lakini kwa sasa upendo wangu utaupata kupitia utendaji wako wa kila siku.” Huyu siyo mzazi mwenye upendo! Na huyu siyo Baba yetu wa mbinguni mwenye upendo.
Badala yake, kama nilivyotegemea kwa mara ya kwanza neema ya Mungu inilete kwenye maisha ya kiroho, ninategemea pia neema iiweke hai hali yangu ya kiroho. Na kama nitaanguka, ni lazima nitegemee tena neema ya Mungu inirejeshe upya kwenye afya ya kiroho.
Hudson Taylor ni mmoja kati ya wamishenari wa zama za kisasa aliyekuwa na ushawishi mkubwa sana, na alikuwa mwasisi wa shirika la kimisheni la China Inland Mission.[1]
Taylor aliongoka akiwa na umria wa miaka 17 kupitia maombi ya mama yake wa Kimethodisti. Alijifunza udaktari na alisafiri kwenda China kama mmishenari katika umri wa miaka 21.
Alipokuwa na umri wa miaka 28 alirejea Uingereza kwa sababu ya ugonjwa wa kisukari. Miaka mitano baadaye iliyofuata, alitafuta sana uongozi wa Mungu, na akiamini kwamba Mungu alimtaka aajiri kundi la wamishenari kwa ajili ya kwenda kufanya uinjilisti katikati ya nchi ya China. Akiwa na umri wa miaka 34, Hudson na Maria Taylor na watoto wao walisafiri pamoja na kundi la wamishenari kumi na sita, likiwa ni kundi la kwanza la wamishenari kutoka katika shirika hilo la China Inland Missionary.
Moja ya misemo maarufu sana ya Hudson Taylor ilikuwa, “Kazi ya Mungu inayofanyika katika mpango wa Mungu kamwe haiwezi kukosa mahitaji.” Mara nyingi tunatafsiri kauli hii kwamba ni kuhusiana na fedha, lakini kwa Taylor ilikuwa ni zaidi ya hapo. Yeye aliamini kwamba Mungu atatoa fedha, uhakikisho, Imani, nguvu, na chochote kile ambacho kingehitajika kutimiza mapenzi yake. Kwa muda wote wa kipindi cha miongo mitano akiwa kiongozi wa China Inland Mission, Hudson Taylor aliiona ahadi hii ya Mungu ikitekelezwa mara nyingi zisizohesabika.
Mwaka 1869, Taylor alijikuta kwenye mgogoro mkubwa katika maisha yake ya kiroho. Amepambana na majaribu na kushindwa. Alimwandikia mama yake, “Sikuwa nimejua nilikuwa na moyo mbaya wa aina gani.” Lakini pia aliandika, “Ninajua kwamba ninampenda Mungu na kazi yake, nina tumaini la kumtumikia yeye peke yake na katika mambo yote. Mungu anisaidie katika kumpenda yeye zaidi na kumtumika vyema.”
Mnamo Septemba 4, 1869, Hudson Taylor alitoa ushuhuda kwamba Mungu alimimina Roho wake kwa njia mpya katika maisha yake. Taylor alimwandikia mtumishi mwenzake, “Mungu amenifanya kuwa mtu mpya!” Msingi wa uhakikisho wa uwepo wa Mungu katika maisha mapya ya Taylor ulikuwa ni sentensi moja katika barua aliyoandikiwa na mmishenari mwenzake John McCarthy. Taylor alikuwa akitafuta kwa nguvu zake mwenyewe kuongeza Imani yake na uhakika wa uwepo wa Mungu. McCarthy aliandika, “Ni kwa jinsi gani Imani yetu inapata kuimarishwa? Siyo kujitahidi kuipata Imani, bali kutulia kwa huyo aliye Mwaminifu.”
Taylor alimwandikia dada yake,
"Jinsi ninavyosoma, ninaona yote hayo! 'Kama tusipoamini, yeye anabakia kuwa mwaminifu.' Nilimwangalia Yesu nikaona, (na nilivyoona, uh, furaha yangu ilibubujikaje)! kwamba alishasema, 'Kamwe sitamwacha yeye.'
'Ah, kuna mapumziko!' niliwaza. 'Nilijisumbua bure kutaka kukaa kwake. Sitajisumbua tena. Kwa kuwa hajaahidi kuacha kushikamana nami – wala kuniacha, wala kunifanya nishindwe.' Na mpendwa wangu, hafanyi hivyo.
Sijaona tu kwamba Yesu kamwe hataniacha, bali kwamba na mimi ni mmoja wa mwilli wake, nyama yake, na mifupa yake. Mzabibu siyo mzizi tu, bali ni vyote – mizizi, shina, matawi, vitawi, majani, maua na matunda. Na Yesu siyo mwenyewe tu - Yeye ni udongo, nuru, hewa, manyunyu, na yuko mara elfu kumi zaidi kuliko tunavyomwazia, tunavyomtakia au tunavyomhitaji. Uh, hii ndiyo furaha ya kuuona ukweli! Ninaomba kwamba macho yetu ya kuona pia yawe na ufahamu na yaangaziwe nuru, ili tuweze kujua na kufurahia utajiri tunaopewa bure katika Kristo."
Kwa wakati huu, Taylor anaelewa kwamba kumfanania Kristo hakupatikani kwa juhudi binafsi bali kupitia muunganiko wa mzabibu ambao unatoa uhai. Unakuja kupitia kutambuliwa na Kristo. Mtoto wake baadaye aliandika kwamba, “Kwa muda mrefu alijua ni nini kujisalimisha, lakini kwa hili ilikuwa ni zaidi; ilikuwa ni kukubali kwa upya, furaha na kukabidhi bila kubakiza ubinafsi na vitu vyote kwake.”
Hii haikuwa ni kwa muda mfupi tu wa uzoefu wa mhemuko. Miaka thelathini baadaye, Taylor alirejea nyuma na kuandika, “Kamwe hatutasahau baraka tulizopokea kutoka katika maneno, Yohana 4:14, ‘walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele.’ Tulikuja kutambua kwamba Kristo alimaanisha kila alichokisema kwa ufasaha – kwamba ‘hataona’ anamaanisha hataona, ‘milele’ anamaanisha milele, na ‘kiu’ anamaanisha kiu – mioyo yetu ilifurikwa na furaha mno kwa kupokea kipawa hicho.” Angalia maneno haya, “kwa kupokea kipawa hicho.” Taylor alielewa kwamba neema ya Mungu inayotakasa ni karama inayopaswa kupokelewa, na siyo mafanikio ya kuchuma.
Uzoefu wa neema ya Mungu, haukufanya maisha yaliyobakia ya Taylor kuwa rahisi. Mwaka uliofuata ulikuwa ni mwaka mgumu kwake kuliko miaka mingine yote katika maisha yake. Katika mwaka huo, watoto wake wawili walikufa na Maria alikufa akiwa na miaka 33. Baadaye, Taylor akaliongoza shirika la kimisheni la China Inland Mission katikati ya vitisho vya mashambulizi ya waasi. Wamishenari wapatao sabini na tisa kutoka katika shirika hilo waliuawa katika siku hizo za kutisha sana.
Lakini pamoja na kupitia mambo haya yote, Taylor alibakia na uhakika wa utii wake kwamba Mungu ataendelea kumpatia mahitaji yote yaliyohitajika. Mhubiri mmoja askofu aliyemtembelea Taylor katika nyakati zile ngumu kwake aliandika. “Hapa kuna mtu mwenye umri unaokaribia miaka sitini, akibeba mizigo mizito ya ajabu, lakini bado alikuwa mtulivu na asiyetaabika.” Kwa nini? Kwa sababu alikuwa ni kitu kimoja na Mzabibu na alikuwa ametulia ndani ya Kristo. Alikuwa, “mmoja wa watu ambao wamehudumu kwa nguvu kubwa ambayo Mungu alimpa - ili Mungu atukuzwe katika mambo yote kwa Yesu Kristo.”[2]c
Uzoefu huu haukua ndio mwisho wa kukua kiroho kwa Taylor. Hata “kupumzika kwake chini ya Kristo” haimaanishi kwamba hakukuwa na juhudi zilizofanyika. Kila asubuhi, bila kujali shinikizo la huduma, Taylor alitumia masaa mawili ya maombi na kujifunza Biblia kabla ya kuanza kazi za siku. Yeye na Paulo walielewa kwamba, “ni lazima kusonga mbele katika kufikia malengo.” Lakini hii ni juhudi ambayo inategemea nguvu za Mungu, na siyo za Hudson Taylor. Taylor alitambua kwamba hata nguvu inayomwezesha kuondoka kitandani kwenda kuanza kujifunza Biblia ilikuwa karama ya neema ya Mungu yenye kuwezesha. Angemfanania Kristo kwa sababualikuwa ‘ndani ya Kristo.’
Mtoto wa Taylor alikumbuka maisha yake ya maombi na Neno. Kutulia ndani ya Kristo hakuna maana kwamba Taylor alipuuzia umuhimu wa nidhamu ya Kiroho.
"Kwake yeye, siri ya kushinda ilikuwa katika masaa ya kila siku ya ushirika na Mungu; na kwa hili, aligundua, lingeweza kudumishwa kwa maombi ya siri na kujilisha kwa Neno ambalo Mungu hujidhihirisha mwenyewe kwa nafsi inayongojea. Haikuwa rahisi kwa Bwana Taylor, katika maisha yake yaliyobadilishwa, kuwa na muda wa kufanya maombi na kujifunza Biblia, lakini alijua kwamba ni muhimu."
"Mara nyingi katika chumba kimoja kikubwa, wangetenga pembe moja kwa ajili ya baba yao, na pembe nyingine kwa ajili yao wenyewe, kwa mapazia tofauti; kisha baada ya kulala pakawepo na ukimya, watasikia njiti ya kiberiti ikiwashwa na wataona nuru ya mshumaa, ikiashiria kwamba Bwana Taylor, hata kama amechoka kiasi gani, alikuwa anafungua Biblia yake tayari kuanza kuyatafakari maneno ya Biblia. Kuanzia saa 8 hadi 10 alfajiri ulikuwa ndio muda wake wa maombi; muda ambao alikuwa na uhakika wa kutokuwepo na usumbufu wowote wakati wa kumngojea Mungu…. Sehemu ngumu sana katika huduma ya umishenari aliyoiona Bwana Taylor, ni kudumisha mara kwa mara maombi ya kujifunza Biblia. 'Shetani mara zote atakutafutia wewe kitu cha kufanya,' Atakusemesha, 'wakati ule ambao ndio unataka kuzama' kwenye maombi na kujifunza Maandiko."
Hadi sasa, wamishenari 1600 wanafanya kazi katika shirika la umisheni la OMF International, mrithi wa shirika la China Inland Mission. Mamilioni ya waamini wa China walioongozwa kumwamini Kristo wanatokana na huduma ya shirika hili la umisheni. Haya ni matunda ya mtu aliyeishi katika umoja na Kristo. [3]
[3] Maelezo yanatokana na Dr. na Bibi Howard Taylor, Hudson Taylor’s Spiritual Secret
Tafakuri ya Somo la 10
(1) Mitume walimtaka kila Mkristo awe mtakatifu.
(2) Kuwa mtakatifu ni kufanana na Kristo.
Kuwa mtakatifu ni kuwa na moyo wa utakatifu:moyo na akili vinavyomfanania Kristo.
Kuwa mtakatifu ni kuwa na mikono mitakatifu: Tabia inayomfanania Kristo.
Kuwa mtakatifu ni kuwa na upendo unaomfanania Kristo.
(3) Mitume walionyesha utakatifu unavyotakiwa uwe kwenye maisha ya kila siku.
Umefanywa kuwa mtakatifu; unaendelea kufanywa mtakatifu.
Ninyi ni watakatifu; lazima muishi kama watakatifu.
Mungu anawafanya muwe watakatifu; lazima kufuata utakatifu.
(4) Tumepewa uwezo wa kuyaishi maisha matakatifu kupitia Roho wa Kristo aishiye ndani yetu.
(5) Tunaishi maisha matakatifu tukiwa “ndani ya Kristo.” Maisha yetu ya kale yalikuwa “ndani ya Adamu.” Maisha yetu mapya tunayaishi “ndani ya Kristo.”
(6) Maisha ya Utakatifu yako kwenye msingi endelevu wa uhusiano na Mzabibu.
Kazi ya Kufanya
(1) Andaa fundisho kuhusu “Maisha yanayomfanania Yesu.” Linganisha njia mbili za kuishi: Maisha yetu ya zamani ndani ya Adamu na maisha yetu mapya ndani ya Kristo. Onyesha jinsi ambavyo kuwa “ndani ya Kristo” kunatuwezesha sisi kuwa washindi juu ya dhambi.
(2) Anza kikao kinachofuata cha darasa kwa kunukuu Wafilipi 2:1-5.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.