Ayubu alikuwa amepoteza kila kitu. Utajiri wake ulitoweka. Watoto wake waliuawa kwa upepo wenye nguvu. Afya yake iliharibiwa. Alikaa kwenye majivu akikuna majipu yaliyomtoka mwilini kwa kigae. Mke wake alimtaka amlaani Mungu ili afe. Marafiki zake walimlaumu kwamba ni mwenye dhambi za kutisha. Wale waliokuwa wanamheshimu siku za nyuma sasa wakaanza kumdhihaki.
Katika mateso yake, Ayubu haombi kwamba, “Mungu rudisha utajiri wangu,” au “Mungu niponye mwili wangu.” Badala yake Analia, “Laiti ningejua mahali niwezapo kumwona, Nifike hata hapo anapokaa!”[1] Ayubu Analia kwa sababu hamwoni tena Mungu aliyekuwa amekaa naye kwa ukaribu sana. “Tazama, naenda mbele, wala hayuko; Narudi nyuma, lakini siwezi kumwona; Na mkono wa kushoto, afanyapo kazi, lakini siwezi kumwona; Hujificha upande wa kuume, hata nisimwone.”[2]
Ayubu anakumbuka siku za nyuma: “Hapo siri ya Mungu ilipokuwa hemani mwangu.”[3] Lakini sasa:
"Yeye amenibwaga topeni, Nami nimekuwa kama mavumbi na majivu. Nakulilia wewe, wala huniitikii; Nasimama, nawe wanitazama tu. Wewe umegeuka kuwa mkali kwangu; Nawe waniudhi kwa uweza wa mkono wako."[4]
Hiki ni kilio cha mtu anayejisikia kusalitiwa na rafiki yake wa karibu sana. Ni kilio cha mtu aliyempenda Mungu.
Kisa hiki cha Ayubu hakijaishia kwa kukata tamaa. Baada ya Mungu kumjibu Ayubu kutoka katika upepo wa kisulisuli, Ayubu alimjibu, “Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio; Bali sasa jicho langu linakuona.”[5] Ayubu alifarijiwa siyo kwa kurejeshewa kwa mali zake, afya, au hata familia yake, bali kwa kurejea tena uwepo wa Mungu. Ayubu alifarijika alipomwona Mungu. Ayubu alikuwa mtu mtakatifu; Ayubu alimpenda Mungu.
Utakatifu ndani ya Vitabu Vya Mashairi: Kumpenda Mungu
► Inamaanisha nini kumpenda Mungu? Ni kwa vipi kumpenda Mungu kwa uthabiti kunaweza kugusa vipaumbele vyako vya muda na fedha? Ni kwa vipi kumpenda Mungu kunaweza kugusa mtazamo wako wa maagizo yake?
Kitabu cha Ayubu na cha Zaburi vinarudia ujumbe tuliouona kwenye Vitabu vitano vya mwanzo vya Biblia: utakatifu ni mahusiano na Mungu. Sisi tunafanyika watakatifu tu pale tunapokuwa kwenye mahusiano na Mungu. Kuwa mtakatifu maana yake ni kumpenda Mungu kwa ukamilifu wote.
Henoko, Nuhu, na Ibrahimu walikuwa watakatifu kwa sababu walitembea na Mungu. Kwa namna hiyo hiyo, Ayubu na Daudi walikuwa watakatifu kwa sababu walitembea na Mungu. Kitabu cha Ayubu kinaelezea kisa cha mtu ambaye alimpenda Mungu hata kupitiliza. Kitabu ha Zaburi kina maombi na nyimbo za mtu ambaye furaha yake kubwa ilikuwa ni ushirika wa karibu sana uliokuwepo kati yake na Mungu.
Watu Watakatifu wana furaha Ndani ya Mungu
Watu watakatifu wana furaha ndani ya Mungu; wanaipata furaha yao ya ndani kutoka kwake. Matamanio yanayomtawala mtu mtakatifu ni kumpendeza Mungu.
Kwa wale wanaoupima utakatifu kupitia orodha ya vitu vya “kufanya na kutofanya,” inaonekana kama ni rahisi tu. Watu wengi wanafikiri kwamba utakatifu ni jambo tu la kufanya kama wajibu kuliko furaha. Maandiko yanaonesha kwamba watu watakatifu wana furaha ndani ya Mungu. Ayubu hakutaka kitu chochote zaidi ya kurejeshewa uhusiano wake na Mungu. Daudi anashuhudia kuwepo kwa uhusiano wa karibu sana na Mungu. Aliipata furaha yake kubwa ndani ya Mungu.
Nilikuwa nafundisha kwenye jiji moja ambalo maji yake ya kunywa yalikuwa siyo salama. Siku moja ya joto, nilisahau kuchukua chupa yangu ya maji ya kunywa. Wakati nilipomaliza kufundisha, nilikuwa na wazo moja tu, “ninahitaji maji!” Kama ungenipa chaguo la $100 au glasi ya maji masafi, ningelichagua maji. Wakati nilipokuwa na kiu hasa, maji yalikuwa ni muhimu kuliko kitu kingine chochote.
Usiku ule, nilijiulza mwenyewe, “Je, ninayo kiu ya Mungu kama nilivyokuwa na kiu ya maji leo? Je, Mungu ana umuhimu wowote kwangu kuliko kitu chochote katika dunia hii?”
Daudi alimwonea Mungu shahuku. “Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji, vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, Ee Mungu. Nafsi yangu inamwonea kiu MUNGU, Mungu aliye hai.”[1] Daudi alilinganisha kiu yake kwa Mungu na ile ya paa anayekimbia. Matamanio makubwa ya paa anayekimbia ni maji; matamanio makubwa ya mtu mtakatifu ni kuwa katika mahusiano ya karibu sana na Mungu. Mtu mtakatifu “ni mwenye njaa na kiu ya haki.”[2]
Zaburi inalinganisha furaha ya watenda dhambi na ile ya watakatifu wa Mungu. Watenda dhambi furaha yao ni vita; wanafurahia uongo; wanapenda kulaani.[3] Kwa ulinganifu, watu watakatifu wanapata “furaha tele” mbele ya Mungu; wanapenda “makao ya nyumba yako, Na mahali pa maskani ya utukufu wako.”[4] Mtunga Zaburi ameamua, “Wala duniani sina cha kupendeza ila Wewe.”[5] Watakatifu huipata furaha yao ya ndani sana ndani ya Mungu.
Zaburi ya 63 inaonyesha uzuri wa kumtafakari Mungu. Daudi alikuwa anakimbia kutoka kwa Sauli. Maisha yake yalikuwa hatarini. Katika hali hiyo, utafikiria nini? Nitajaribiwa kutafakari juu ya hiyo hatari. Daudi anasema, “Ninapokukumbuka kitandani mwangu, Nakutafakari Wewe makesha yote ya usiku.” Hata katika hatari, mawazo ya Daudi yalimwelekea Mungu. Alijikuta kutafakari huku kukimridhisha “kama kushiba mafuta na vinono.”[6]
Mwimbaji wa Zaburi alikuwa na furaha ndani Mungu; alikuwa na upendo kwa Mungu. Watu wa Mungu hufurahia katika Bwana. Fikiria kidogo: Ni nini kinachokupa kiu? Je, uanayo furaha ndani ya Mungu?
Watu wa Mungu hufurahi ndani ya Sheria za Mungu
Mtu mtakatifu hufurahi ndani ya Sheria za Mungu. Katika Zaburi inaonesha kwamba sheria za Mungu siyo tishio kwa watu wake; watakatifu huzipenda sheria za Mungu. Daudi alisema “Kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu.”[7] Hakuwa na mapambano ya kumwamini Mungu; Alipata furaha katika utiifu wake kwa Mungu.
Furaha katika sheria za Mungu zinaonekana katika kitabu chote cha Zaburi. Zaburi ya 119 ni neno la Mungu. Isikilize furaha ya Daudi:
Unifumbue macho yangu niyatazame Maajabu yatokayo katika sheria yako.[8]
Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu, Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.[9]
Rehema zako zinijue nipate kuishi, Maana sheria yako ni furaha yangu.[10]
Sheria yako naipenda mno ajabu, Ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa.[11]
Ee Bwana, nimeutamani wokovu wako, Na sheria yako ndiyo furaha yangu.[12]
Sheria ya Mungu hudhihirisha Upendo wa Mungu.
“Bwana, dunia imejaa fadhili zako, Unifundishe amri zako.”[13] Mungu huonesha upendo wake kupitia sheria zake: “Kama zilivyo rehema zako umtendee mtumishi wako, Na amri zako unifundishe.”[14] Watu watakatifu hufurahi katika amri za Mungu kwa sababu wanafahamu kwamba sheria ya Mungu hudhihirisha upendo wa Mungu.
Musa alisema kwamba, utii wa Israeli kwa sheria za Mungu kutafanya mataifa mengine yaone wivu kwa hekima yao!
"Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, 'Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili.'"[15]
Musa akauliza, “Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama Torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo?”[16] Sheria ya Mungu haikuwatumikisha Israeli; sheria ya Mungu iliwabariki Israeli.
Leo, ni jambo la kawaida kusikia wahubiri wakifundisha kwamba sheria ya Mungu ilikuwa ni mzigo mkubwa ambao isingewezekana kuutii. Baadhi ya Wakristo wanasema kwamba sheria ya Mungu ni “lengo” mbalo hakuna mtu anayeweza kulifikia. Hata hivyo, Musa, Daudi na watakatifu wengine katika Agano la Kale walifurahia katika sheria za Mungu. Waliamini kwamba ilikuwa ni furaha kuheshimu jina la Mungu na Sabato. Hawakupenda kuiinamia miungu ya sanamu.
Hawakuamini kama wangeweza kuwa na furaha zaidi kwa kutowatii wazazi wao, kufanya mauaji na uzinzi, au kuiba na kusema uongo. Walijua ni vyema mtu kuwa na kitu chake kuliko kuwa na tamaa na alicho nacho jirani yake. Sheria ya Mungu haikuwa mzigo. Mungu alitoa amri yake kutoka ndani ya moyo wa upendo. Sheria iliwaongoza watu watakatifu kwenye mahusiano yao na Mungu. Sheria ya Mungu ilikuwa ni furaha kwa watu wake.[19]
Sheria ya Mungu hudhihirisha Tabia ya Mungu.
Kama tukimpenda Mungu, tutaipenda na sheria yake. Mtunga Zaburi alikiri, “Shuhuda zako ni za ajabu, Ndiyo maana roho yangu imezishika.”[20] Daudi hakusema, “Sheria yako ni ngumu, lakini nitajaribu kuitii.” Hapana. Daudi alisema, “Sheria ya Mungu ni ya ajabu!”
Watu watakatifu hufurahia sheria ya Mungu. Mtunga Zaburi aliipenda sheria ya Mungu kwa sababu alijua kwamba sheria ni zaidi ya msururu wa masharti; Sheria ya Mungu hudhihirisha tabia ya Mungu.
► Soma Zaburi 111 na 112.
Zaburi 111 na 112 ni Zaburi washirika. Kwa pamoja, zinaonyesha umuhimu wa sheria za Mungu kwa mtu mtakatifu. Zaburi ya 111 inaelezea tabia ya Mungu: Mungu ni mwadilifu na mwenye haki, ni wa neema na rehema.
Zaburi ya 112 inaanza, “Heri mtu yule amchaye Bwana, apendezwaye sana na maagizo yake!” Mtu anayefurahishwa na maagizo ya Mungu atabarikiwa. Vipi? Atafanana na Mungu. Atakuwa na “neema, huruma na haki.” Hizi ni tabia zile zile zinazomwelezea Mungu katika Zaburi ya 111. Tunapofurahia katika sheria za Mungu, tunafanana zaidi na Mungu.
Vitabu vitano vya mwanzo vya Biblia vinafundisha kwamba mtu mtakatifu huakisi sura ya Mungu. Zaburi 111 na 112 zinaonyesha kwamba mtu anayefurahia sheria za Mungu hubadilishwa kuwa katika sura ya Mungu. Mtu anyefurahia sheria za Mungu hufanana zaidi na Mungu.
Kama kweli tunampenda Mungu, tutazishika sheria za Mungu. Daudi aliuliza, “Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana? Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?” Ni nani atakayekaa katika uwepo wake? “Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe...”[21] Kuishi kwenye uwepo wa Mungu, kunahitaji utii katika sheria za Mungu. Vitabu vya Mashairi vinaonyesha kwamba Mungu anahitaji utiifu kwa wale wanaofikiri kwamba wao wanampenda Mungu.
Vitabu hivi pia vinaonyesha kwamba Mungu hufanya utii kuwa kitu kinachowezekana. Hii ni ahadi ya Mungu kwa wale wanaompenda.
Kisa cha Ayubu kinaanza na, “Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu.”[22] Wakati Elifasi alipomshutumu Ayubu kama mtenda dhambi, Ayubu alijibu:
"Mguu wangu umeshikamana sana na hatua zake; Njia yake nimeishika, wala sikukengeuka. Sikurudi nyuma kuiacha amri ya midomo yake; Nimeyatunza maneno ya kinywa chake zaidi ya riziki yangu."[23]
Mtu fulani anaweza kuuliza, “Inawezekanaje Ayubu aseme kwamba hajavunja amri za Mungu? Kila siku mtu anatenda dhambi.” Ayubu anajibu, “Ninampenda Mungu na nina furaha ya kuwa mtiifu kwake.” Ayubu alitembea kwa ukaribu sana na Mungu. Aliweka “amri kinywani mwake,” Je, maisha ya utakatatifu yanawezekana? Ayubu anajibu, ”Ndiyo.” Ayubu anatambua kwamba Mungu hufanya utii wa kuaminika uwe ni kitu kinachowezekana kwa wale wampendao yeye.
Maisha ya utakatifu hayategemei nguvu zetu; yanakuja kwa kumtegemea Mungu kila iitwapo leo. Ayubu alikuwa mtu asiyelaumika siyo kwa sababu alikuwa na nidhamu ya kawaida. Alikuwa asiyelaumika kwa sababu ya uhusiano wake wa karibu wa kutembea na Mungu. Ayubu alielewa kwamba Mungu anahitaji utii wa kuaminika na kwamba yeye Mungu hufanya utii wa kuaminika uwe ni kitu kinachowezekana.
Ukweli huu una mguso wa nguvu sana katika maisha ya kila siku ya mwamini. Mungu anahitaji watu wake wawe watakatifu na Mungu huwafanya watu wake wawe watakatifu. Ni kwa kupitia yeye kwamba tunafanywa watakatifu na wasafi. Mungu anataka utakatifu na Mungu hutoa utakatifu. Mungu hutoa kila kitu ambacho Neno lake huhitaji.
Wote wanaofurahi katika Bwana wanapokea haja za mioyo yao
Zaburi ya 37 inaonyesha matokeo ya kufurahi katika Bwana. “Nawe utajifurahisha kwa Bwana, Naye atakupa haja za moyo wako.”[24]
Baadhi ya wasomaji wanafikiri kwamba Zaburi 37:4 hufundisha, “Kama nitamtumikia Mungu, atanipa kila kitu nitakachoomba. Atanifanya niwe tajiri.” Daudi hafundishi injili ya mafanikio inayosema, “Mungu anataka watu wake wawe matajiri.” Daudi anazungumzia jambo lenye maana na umuhimu mkubwa zaidi: “Kama shahuku yako kubwa ni Mungu, Mungu atajitoa mwenyewe kwako.” Kama unamtamani Mungu, utampata Mungu.
Kama utamfuata Mungu ili uweze kupata afya, utajiri, na umashuhuri, utakatishwa tamaa na andiko hili la Zaburi 37:4. Kama unamfuata Mungu kwa ajili ya baraka za mwilini, utakatishwa tamaa utakapokuja kutambua kwamba zawadi yako ni… Mungu!
Kwa mtu mwenye ubinafsi, kumpokea Mungu siyo zawadi kubwa kwake. Mtu mwenye ubinafsi hana tamanio la kumhitaji Mungu. Lakini kwa mtu anayemtamani Mungu, Zaburi 37:4 ni ahadi kubwa kwake. Kwa mtu mtakatifu, Mungu ni zawadi kubwa kwake inayowezekana.
Kwa wale wanaomtamani yeye, Mungu hujitoa kwa uhusiano wa karibu sana na yeye mwenyewe. Siyo kila wakati kufurahi katika Bwana kunaleta baraka za kifedha au uhuru kutokana na mapito. Watu wanaofurahi katika Bwana wanaweza kuchukizwa na maadui zao. Watu watakatifu mara nyingi ni watu wanaopitia katika mapito makali. Hata hivyo, Daudi na Ayubu waligundua kwamba hata katika nyakati za mapito makali, Mungu anawaheshimu wale wanaofurahia katika yeye
Utakatifu ni kumpenda Mungu. Watu watakatifu hufurahi katika Bwana; na Mungu naye, hujitoa mwenyewe kwa wale wenye njaa na kiu kwa ajili yake.
[17]Sala kwa ajili ya Utakatifu “Mungu wangu, Ninaomba kwamba niweze kukujua na kukupenda ili niweze kufurahi katika wewe. Ruhusu akili yangu iweze kutafakari juu ya uzuri wako. Achilia ulimi wangu uzungumzie hayo. Acha moyo wangu uishi kwa hilo. Acha nafsi yangu ione njaa kwa hilo. Acha utu wangu wote utamani hilo, hadi nitakapoingia katika furaha yako.”
- Anselimu wa Canterbury
[18]“Tunafikria kwamba chochote kisichopendeza ni jukumu letu! Hicho chochote siyo kama roho wa Mungu wetu? ‘Ninafurahia kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu wangu.’”
- Oswald Chambers
[19] Kimenukuliwa kutoka: Dennis F. Kinlaw, This Day with the Master (Grand Rapids: Zondervan, 2004).
Utakatifu ndani ya Vitabu Vya Injili: Kumpenda Mungu
Mwanasheria mmoja wa dini alimwuliza Yesu, “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Yesu akarejea kwenye sheria ya Musa kumjibu, “Imeandikwa nini katika Torati? Wasomaje?”
Mwanasheria alikuwa amenukuu kutoka katika Kumbukumbu la Torati 6:5 na Mambo ya Walawi 19:18. Maandiko haya yanatoa muhtasari wa sheria. “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako.” Yesu akamwambia, “Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi.”[1] Utakatifu ni upendo kamili.
Miezi michache baadaye, Yesu alikuwa Yerusalemu. Mwandishi mmoja akamwuliza, “Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza?”[2] Mafarisayo waliorodhesha amri zote 613 kutoka katika Agano la Kale. Mara kwa mara walikuwa wakibishana ni amri ipi iliyokuwa kuu na muhimu zaidi kuliko nyingine. Yesu akawajibu:
"Ya kwanza ndiyo hii, 'Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja; nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.' Na ya pili ndiyo hii, 'Mpende jirani yako kama nafsi yako.' Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi."[3]
Yesu alifafanua utakatifu kama upendo kwa Mungu na upendo kwa watu wengine Utakatifu wa kweli huthibishwa katika upendo. Tunakua katika utakatifu kama tunavyokua katika upendo wa kumfanania Kristo. Kuwa mtakatifu ni kuwa na upendo kama vile naye Yesu alivyokuwa na upendo; huu ni upendo kamili.
Kwenye somo la 5, tuliona kwamba waandishi wa Agano la Kale walitumia neno “mkamilifu” kurejea kwenye moyo ambao haujagawanyika. Kuwa mtu mkamilifu ni kutogawanyika katika kuwajibika kwake kwa Mungu. Waandishi wa Agano Jipya wanatumia neno “mkamilifu” katika maana hiyo hiyo. Yesu aliwaagiza wafuasi wake “kuwa wakamilifu.”[4] Kwenye Vitabu vya Injili, tunaona kwamba kuwa mkamilifu ni kuwa na upendo usiogawanyika kwa Mungu au kwa majirani zetu. Kuwa mkamilifu ni kupenda bila kujibakiza. Huu ndiyo upendo kamili.
Ujumbe wa upendo mkamilifu haukuwa mpya kwenye Vitabu vya Injili. Yesu aliikumbusha Israeli kwamba Mungu siku zote anahitaji upendo kwa ajili yake kama Mungu na upendo kwa ajili ya majirani zetu. Kumbukumbu la Torati 6 inaonyesha kwamba upendo ndiyo msingi wa sheria. Utii bila upendo unasababisha ushikiliaji mno wa sheria. Yesu alifundisha kwamba kuwa mtakatifu ni kumpenda Mungu. Kama tukimpenda Mungu, tutamtii yeye. Utakatifu ni kumpenda Mungu kwa moyo wako wote.
Kumpenda Mungu ni zaidi ya kuwa na mhemuko au hisia. John Wesley alifafanua upendo kwa Mungu:
"….kufurahi katika Bwana, ni kufurahi katika mapenzi yake, kutamani wakati wote kumpendeza yeye, kuomba na kutafuta furaha yetu katika yeye, na kuwa na kiu ya ujazo kamili wa kumfurahia yeye mchana na usiku."[5]
Upendo kwa Mungu huleta mabadiliko kabisa ya mwelekeo wetu wa maisha. Kumpendeza Mungu kunakuwa ndiyo lengo letu la juu na furaha yetu kubwa. Yesu alionyesha inamaanisha nini katika kumpenda Mungu kwa ukamilifu. Ndani ya Yesu, tunaona upendo mtakatifu ambao Mungu anataka uwe kwa kila Mkristo.
Yesu alidhihirisha upendo kamili kwa Mungu katika maisha yake
Yesu alidhihirisha upendo kamili kwa Baba yake. Yesu aliishi katika furaha ya kujikabidhi kabisa kwa mapenzi ya Baba yake. Kujikabidhi huku hakukuwa kwa kulazimishwa kama mtumwa; ilikuwa ni kujikabidhi kwa upendo kutoka kwa mtoto.
Majaribu yalionyesha upendo wa Yesu kwa Baba
Kabla hajaanza huduma yake nje, Yesu alikutana na jaribu jangwani. Kila jaribu lilikuwa limelengwa kuharibu uhusiano kati ya Baba na Mtoto.
Shetani alimjaribu Yesu ili avuke mipaka ya Baba yake na ajitengenezee mkate kwa ajili yake mwenyewe. Shetani alimjaribu Yesu aachane na kumwabudu Baba yake ili achukue mamlaka juu ya falme zote za dunia. Shetani alimjaribu Yesu ili amjaribu Baba yake kwa kuruka kutoka juu ya kinara cha hekalu.[6] Kila jaribu lilikuwa ni kipimo cha upendo wa Yesu kwa Baba yake. Yesu alijibu kwa kuonyesha utiifu wake kamili kwa Baba yake wa mbinguni.
Badala ya kugeuza mawe yawe mkate, Yesu alinukuu andiko la Kumbukumbu ya Torati 8:3: “Imeandikwa, ‘Mtu hataishi kwa mkate tu,’” Musa aliwakumbusha wana wa Israeli kwamba Mungu ametoa mana jangwani; Israeli imwamini Baba yao mtoaji. Kwa njia hiyo hiyo, Yesu aliamini utoaji wa Baba yake.
Badala ya kumsujudia Shetani, Yesu alinukuu andiko la Kumbukumbu la Torati 6:13; “Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.” Kwa kuwa alimpenda Mungu kwa ukamilifu, Yesu alikataa jaribio lolote la kumtaka amsujudie Shetani.
Badala ya kumjaribu Baba yake kwa kuruka kutoka kinara cha hekalu, Yesu alinukuu andiko kutoka Kumbukumbu la Torati 6:16, “Tena imeandikwa, ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’” Kwa kuwa alimpenda Mungu kwa ukamilifu, Yesu alikataa jaribio lolote la kutaka kuvunja ahadi ya Baba yake ya ulinzi.
Utakaso wa Hekalu unaonyesha Upendo wa Yesu kwa Baba yake.
Hata wakati akiwa mtoto, Yesu aliipenda Nyumba ya “Baba yake.”[7] Alimpenda Baba yake, kwa hiyo aliipenda pia nyumba ya Baba yake.
Wakati Yesu alipowakuta wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu kwenye hekalu, aliwajibu kwa hasira ya haki.
"Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng'ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao."[8]
Kwa nini yesu alikasirika? Ni kwa sababu wafanyabiashara hawakuiheshimu nyumba ya Baba yake. Akawaambia, “msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara.”[9] Yesu alimpenda Baba yake na akalipuka kwa hasira ya nyumba ya Baba yake kuvunjiwa heshima.
Yesu pia alikuwa na hisia za kawaida za kibinadamu. Mbele ya maovu, alijisikia hasira, lakini bila kutenda dhambi.[10] Utakatifu haukuondoa hisia za Yesu. Badala yake, kwa kuwa alikuwa mtakatifu, hisia zake ziliakisi hisia za Baba yake. Yesu alikuwa na hasira katika mambo ambayo yanamchukiza Baba yake.
Kutii kwa Yesu kunaonyesha Upendo wake kwa Baba
Kwenye ujumbe wake wa kuaga, Yesu aligusia kuhusu utii wake kama ushuhuda wa upendo wake kwa Baba yake. “Lakini ulimwengu ujue ya kuwa nampenda Baba; na kama vile Baba alivyoniamuru; ndivyo nifanyavyo.”[11] Yesu aliudhihirsha upendo wake kwa Baba kupitia utii wake wa hiari kwenye mapenzi ya Baba. Huu ni upendo kamili.
Hata alipokuwa katika majaribu, Yesu alikuwa mtiifu kwenye mapenzi ya Baba yake. Yesu alijua anaenda kukutana na kesi ya aibu ikifuatiwa na maumivu yasiyoelezeka ya msalaba. Atatengwa na Baba yake kwa sababu ya dhambi ya mwanadamu. Yesu aliomba, “Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki...”[12] Yesu wa Nazarethi alikabiliana na jaribu kubwa la utii wake kwa Baba yake.
Katika ubinadamu wake, Yesu aliomba kwa ajili ya ukombozi. Lakini katika ubinadamu wake, Yesu alionyesha utii wake wa hiari kwa kwa Baba. “…Hata hivyo, siyo kwa mapenzi yangu, bali mapenzi yako yatimizwe.” Yesu alionyesha upendo kamili kwa ajili ya Baba kupitia utiifu wake kwenye mapenzi ya Baba.
Maisha ya Yesu yanatoa mfano wa kuigwa na watu wengine wa upendo kamili. Kuwa mtakatifu ni kumpenda Mungu kama Yesu alivyompenda Baba yake.
Yesu aliwafundisha wafuasi wake kumpenda Mungu kikamilifu
Kumpenda Mungu ni zaidi ya kuwa na hisia. Ni kujikabidhi kwa muda mrefu kunakoleta mabadiliko katika masuala muhimu ya maisha yetu. Yesu alifafanua upendo kwa jinsi hii:
"Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu."[13]
Kwa waalimu wa Kiyahudi, neno “chuki” linamaanisha “kupenda kidogo kuliko kitu kingine.” Mfuasi wa Yesu ni lazima ampende Yesu kuliko vitu vingine vyote, hata kuliko yeye mwenyewe. Hiyo ndiyo inamaanisha kumpenda Mungu – kumpenda Mungu juu ya vitu vingine vyote.
Yesu alisema, “Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana, ama atamchukia huyu na kumpenda huyu, ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu.”[14] Upendo ni wa pekee. Kama unampenda Mungu, anachukua nafasi ya kwanza juu ya kila kitu katika maisha yako.
Yesu alifundisha kwamba, uaminifu na utii wa hiari ni kielelezo cha upendo. “Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye.” Zawadi ya upendo huu wa hiari ni uhusiano wa karibu sana na Mungu. “naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.”[15]
Miaka mingi baadaye, Yohana aliyakubuka maneno ya Yesu katika chumba cha juu. Yohana aliandika, “Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli.”[16] Utakatifu ni upendo mkamilifu kwa Mungu. Watu watakatifu kwa hiari yao hujikabidhi kwenye mapenzi ya Baba. Watu watakatifu huiga mfano wa Yesu wa utii.
Wakati tunapompenda Mungu kwa ukamilifu wote, tunafurahia kuyatii mapenzi yake. Tunapompenda Mungu kwa ukamilifu wote, kwa hiari yetu tunakabidhi mapenzi yetu kwenye mapenzi ya Baba. Tunapompenda Mungu kwa ukamilifu wote, tunaomba pamoja na Daudi:
"Ee Mungu, unichunguze, uujue moyo wangu, Unijaribu, uyajue mawazo yangu; Uone kama iko njia iletayo majuto ndani yangu, Ukaniongoze katika njia ya milele!"[17]
Upendo uliokamilika unatupa shahuku kubwa ya kumfurahisha Baba yetu wa mbinguni. Tunakataa kila kitu kinachoweza kuvuruga uhusiano wetu na yeye. Utakatifu ni upendo mkamilifu kwa Mungu.
Uhusiano kati ya Yesu na Baba ni mfano wa kuigwa kwa Wakristo
► Soma Yohana 17.
Yesu alitoa picha ya utakatifu kwenye maombi yake ya kikuhani mlimani. Katika Yohana 17, Yesu alijiombea mwenyewe, aliombea wanafunzi wake, na aliombea waamini wote. Yesu alionyesha kwamba uhusiano wake wa karibu na Baba ni mpangilio wa uhusiano kati ya Wakristo na Baba yetu.
Yesu alijiombea mwenyewe(Yohana 17:1-5)
Katika kukabiiana na kifo, Yesu alifurahia kwamba amekamilisha kazi ambayo Baba alimtuma kuifanya. “Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye.”
Baadaye katika maombi haya, Yesu akasema, “Najiweka wakfu mwenyewe,” Neno la Kigiriki kutafsiri “wakfu” ni sawa na neno lililokuja baadaye katika tafsiri la “utakaso” katika aya hiyo hiyo. Yesu aliomba: “Uwatakase (hagiazo) kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli; Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni. Na kwa ajili yao najiweka wakfu (hagiazo) mwenyewe, ili na hao watakaswe (hagiazo) katika kweli.”[18]
Hagiazo linaweza kumaanisha aidha “kufanya takatifu” au “kutengwa.” Kwa kuwa Yesu hakuwa na dhambi, hakuhitaji afanywe mtakatifu. Katika sala hii, “utakaso” inamaanisha “kuwekwa wakfu au kutengwa.” Yesu alijitenga ili kuikamilisha kazi ambayo Baba alimpa kuifanya. Yesu alijitakasa mwenyewe kwa ajili ya lile jukumu ambalo Baba alikuwa amemkabidhi.
Yesu aliwaombea Wanafunzi wake (Yohana 17:6-19)
Yesu aliomba kwamba wanafunzi watakaswe katika kweli. “Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli.” Kama vile Yesu alivyotengwa kwa ajili ya kazi duniani, aliomba kwamba wanafunzi watengwe kwa ajili ya huduma. Uhusiano kati ya mtoto na Baba ulikuwa ni mfano wa kuigwa kwa ajili ya mahusiano kati ya wanafunzi na Baba. Kama wanafunzi walivyofuata mtindo wa Yesu, walitengwa ili kushiriki ukweli wake na dunia.
Yesu aliomba kwa ajili ya Waamini wote (Yohana 17:20-26)
Kisha Yesu akaomba kwa wote “wale watakaoniamini kwa sababu ya neno.” Aliomba kwamba Wakristo wote washiriki umoja ule ambao yeye na Baba yake waliufurahia. Yesu aliomba kwamba “wawe wamoja waliokamilika.” Hili neno ni sawa na lile linalotumika katika Mathayo 5:48: “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.” Hili neno linaashiria kukamilika kwa lengo lililokusudiwa. Lengo hilo ni upendo mkamilifu, upendo unaoonekana ndani ya Utatu Mtakatifu wa Mungu.
Sisi kama waamini tunaalikwa kushiriki kwenye upendo mtakatifu wa Baba na Mwana. Yesu aliomba, “ili pendo lile (Baba) ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao.” Upendo kati ya Yesu na Baba ni mwelekeo wa kufuatwa na kila mwamini. Hii ndiyo maana ya kuwa mtakatifu: kuwa na upendo mkamilifu kama ulivyooneshwa na Yesu.
[5] John Wesley, “On Love.” Retrieved from http://wesley.nnu.edu/john-wesley/the-sermons-of-john-wesley-1872- edition/sermon-139-on-love/ December 21, 2019.
George alikuwa na swali kwa mchungaji wake. “Mchungaji, nataka niwe mtakatifu. Kama Ibrahimu, nataka niwe rafiki wa Mungu. Lakini kuna tatizo. Ninafanya mambo ninayojua kwamba ni mabaya. Ninampenda Mungu, lakini sitaki kumtii. Je, ninaweza kuwa rafiki wa Mungu kama sitamtii yeye?”
Yesu alijibu swali la George zaidi ya miaka 2,000 iliyopita. “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.”[1] Hakuna mahali popote Yesu anaposema, “Ukinipenda, unaweza kuendelea kuishi maisha ya kujitakia ya dhambi.” Badala yake, Yesu alisema, “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.” Yesu akaendelea kusema, “Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu.”[2]
Baadhi ya Wakristo waliokwisha kumkiri Kristo, huzungumzia kuhusu upendo wao kwa Mungu ili hali wanaendelea kuishi katika dhambi za kujitakia. Kwa watu hawa, kumpenda Mungu kupo katika mhemuko tu. Wanadai kumpenda Mungu, lakini hawana mabadiliko katika maisha yao. Hata hivyo, kumpenda Mungu ni zaidi ya mhemuko au kuwa na hisia. Kumpenda Mungu kunahitaji utii katika amri zake.
Sally alikuwa na swali kwa mchungaji wake, “Mchungaji, nataka niwe mtakatifu. Kama Ayubu, nataka nisiwe wa kulaumiwa na niwe na msimamo. Niko makini sana katika kuishika kila sheria ya Mungu. Lakini kuna tatizo. Kiuhalisia simpendi Mungu. Ninamtii kwa sababu ya hofu kwamba anaweza kuwa mwenye hasira kama sitatii. Ninamtii Mungu, lakini simpendi. Je, ninaweza kuwa mtakatifu kama simpendi Mungu?”
Yesu alilijibu hili swali la Sally zaidi ya miaka 2,000 iliyopita. Yesu alitoa ujumbe kwa kanisa la Efeso. Aliwapongeza kwa kazi zao nzuri na kwa kuwa na imani inayokubalika. Aliwapongeza kwa uaminifu wao wakati wa kukabiliana na mateso kwa ajili ya imani yao. Lakini, alisema, “Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza.” Yesu alizingatia kwa makini ukosefu wa upendo kiasi cha kuonya kwamba “Nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake,” kama hawatataka kutubu na kuurejesha upendo wao wa kwanza.[3]
Baadhi ya Wakristo huamini kwamba wanaweza kuupata upendeleo wa Mungu kupitia utii, lakini utii wao haukamilishwi na upendo. Wanaamini kwamba utakatifu ni suala la kuwa mtiifu kwa baadhi ya sheria. Wamesahau kwamba chimbuko la utakatifu ni upendo kwa ajili ya Bwana.
Moyoni, wote George na Sally wana tatizo moja la msingi linalowasumbua; hakuna hata mmoja anayempenda Mungu. Ukosefu wa upendo kwa Mungu kutoka kwa George unaonekana kwenye mambo ya kidunia, “Ninaupenda ulimwengu huu kuliko ninavyompenda Mungu.”
Ukosefu wa upendo kwa Sally unaonekana katika kushikilia sheria sana. Kushikilia sheria sana kunasema, “Ninamtii Mungu, siyo katika upendo lakini ni kwa ajili ya matamanio ya kupata upendeleo wa Mungu.” Hakuna hata moja katika haya linalochochewa na upendo kutoka kwa Mungu. Majibu kwa haya yote mawili yanafanana – upendo kwa Mungu.
Jawabu kwa Mambo ya Dunia: Kumpenda Mungu
Inamaanisha nini kuwa wa kidunia? Mara nyingi, tunafafanua mtu wa kidunia kwa kuangalia mavazi, aina za sherehe, kutamani kuthibitika kwa watu, kujionyesha, au alama nyingine za nje. Hizi zinaweza kuwa ni dalili za kuwa kidunia, lakini kuwa mtu wa kidunia ina maana ya ndani zaidi. Hili hapa ni swali la kusaidia kufafanua kidunia: “Ni nini kinachoniletea furaha ya kweli?”
Kuwa wa “kidunia” ni furaha ya ulimwengu huu. Mtu wa kidunia hutafuta utoshelevu mkamilifu katika dunia hii. Kuwa kidunia ni kuthamini mambo ya dunia hii kuliko mambo ya Mungu.
Lutu “akaliona Bonde lote la Yordani, ya kwamba lote pia lina maji.” Alichagua bonde ambalo macho yake yalimvutia.[4] Lutu alikuwa mdunia; Alifurahia sana starehe za dunia hii.
Dema aliiacha huduma kwa sababu aliipata furaha katika dunia hii. Paulo aliandika, “Maana Dema aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa, akasafiri kwenda Thesalonike,” mji wa mafanikio.[5] Dema alikuwa mdunia; aliupenda ulimwengu huu.
Watu wa Mungu hutafuta furaha yao ya ndani kutoka kwa Mungu. Mwimba Zaburi aliandika, “Wala duniani sina cha kupendeza ila Wewe.”[6] Mtunga Zaburi alikuwa mtu wa Mungu; alimpenda Mungu.
Jawabu la u-dunia siyo msururu wa amri. Jawabu sahihi la u-dunia ni upendo wa Mungu. Mchungaji mmoja Mskoti wa karne ya 19, Thomas Chalmers, alihubiri somo juu ya “Nguvu ya Kutosha katika Upendo Mpya.” Mchungaji Chalmers alisema kwamba kuna mambo mawili tunayopaswa kufanya kama tunataka kuachana na kuipenda dunia:
Ni lazima tuachane na kitu fulani. Ni lazima tutambue utupu wa dunia hii. Kama tunavyoona ubatili wa vitu vya dunia hii, upendo wetu kwa dunia hii hupungua. Lakini hilo peke yake haitoshi.
Ni lazima tuwe na kitu fulani. Ni lazima tubadilishane upendo wa dunia hii na kitu kingine kinachopendeka zaidi. Tunapoingia kwenye mapenzi na Mungu, upendo wetu mpya hutimulia mbali upendo wa zamani wa dunia.
Tiba ya kuipenda dunia ni kuingia kwenye urafiki na Mungu. Yesu alitoa mfano wa mfanyabiashara mmoja aliyekwenda kuuza alivyokuwa navyo vyote ili aweze kwenda kununua lulu moja ya thamani.
Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri; naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua.[7]
Fikiria kama ungetamka haya kwa huyu mfanyabiashara, “Ninakusikitikia sana. Inasemekana kwamba ilibidi uuze vitu vyako vyote.” Mfanyabiashara atakucheka! Atakuambia, “Sadaka? Sijatoa sadaka; mimi ninanunua lulu ya thamani kubwa. Vitu nilivyouza siyo chochote ukilinganisha na hii lulu nzuri.” Mfanyabiashara amepata mpenzi mpya. Ameangukia kwenye upendo mpya ambao umefukuza upendo wa zamani.
Jawabu la kuwa wa kidunia ni kuingia kwenye mapenzi mapya na Mungu. Upendo kwa Mungu utafukuza upendo wetu wa kupenda fedha, wa kupigiana makofi, wa kujisifia na kwa mambo yote ambayo dunia inatumia ili kuwashawishi watu wa Mungu. Watu watakatifu wanampenda Mungu – na kwamba upendo wa Mungu huondosha kabisa kuipenda dunia hii.
Wakati tunapokusudia kwa dhati kuishi maisha matakatifu, tunaweza kujaribiwa kuvuka kiwango cha kanuni za kibiblia kutoka kuwa “Mkristo mkamilifu” hadi “nadharia ya ukamilifu” wa kisheria.
“Mkristo mkamilifu” kwa mujibu wa Biblia ni moyo usiogawanyika unaotafuta kumpendeza Mungu katika maeneo yote. Unatambua kwamba hata moyo wa kweli wa upendo hauwezi kutuleta kwenye utendaji uliokamilika. Sisi tumekuwa na mipaka ya udhaifu wa kibinadamu. Mtu mtakatifu hatapenda kuvunja sheria za Mungu kwa makusudi, lakini aliye mtakatifu ataendelea zaidi kutegemea neema ya Mungu katika maeneo yale ambayo kwa kutokukusudia hujikuta tumepungukiwa na viwango vya Mungu vya mema na mabaya.
“Nadharia ya ukamilifu” kwa upande mwingine, inaniongoza mimi kutegemea utendaji mkamilifu kwenye maeneo yote ya maisha. Nadharia ya ukamilifu inanilenga mimi na utendaji wangu kama mtu mtakatifu badala ya kumwelekea Yesu na nguvu zake katika maisha yangu.
Nadharia ya ukamilifu huelekeza kwenye juhudi za kisheria za “kupata” upendeleo wa Mungu kupitia kutengwa. Mara nyingi inapima utakatifu kwa misingi ya orodha ya vitu nisivyovifanya (mimi sivuti sigara, sinywi pombe, sivai nguo za aibu,) au mambo ambayo ninayafanya (ninafunga, ninaomba, ninatoa kanisani).
Kama tulivyoona katika somo la 4, mtu mtakatifu atataka abakie kuwa ametengwa kutoka katika mambo yote yasiyompendeza Mungu. Kwa kusema, “Nampenda Mungu kwa moyo wangu wote” halafu unaishi maisha yanayotafuta kukidhi matakwa ya dunia ni mbaya.
Pamoja na hayo, kamwe tusiruhusu matamanio yetu ya moyo uliotengwa na maisha yaliyotengwa yakatupeleka katika kuamini kwamba tunaweza kupima uhusiano wetu na Mungu kwa orodha za “ninavyovifanya na nisivyovifanya.” Utakatifu ni jambo la kwanza la moyo wa uhusiano wa upendo na Mungu. Uhusiano huu huhamasisha tamaa zetu za kuishi maisha matakatifu, yaliyotengwa. Kinyume chake haitanya kazi: Maisha yaliyotengwa peke yake hayawezi kuhamasisha uhusiano wa upendo na Mungu.
Tunatafuta kuwa wakamilifu kama Mungu anavyoamuru. Tusijaribu kupata upendeleo wa Mungu kupitia nadharia ya ukamilifu. Moyo mkamilifu ni moyo unaompenda Mungu kabisa.
► Ni lipi jaribu kubwa katika kanisa lako, mambo ya dunia au ya sheria? Jadili upanuzi wa uwigo wetu wa upendo kwa Mungu unavyoweza kuleta mabadiliko sahihi katika haya matatizo. Jadili hatua za vitendo za kuhamasisha upendo wa Mungu miongoni mwa watu unaowahudumia.
Ufunguo wa Maisha ya Utakatifu: Kumpenda Mungu
Tunampeda Mungu peke yake kama tutamtii kwa ukamilifu. Tunamtii Mungu peke yake kama kwa ukweli tunampenda yeye. Kama watoto wa Mungu, tunaweza kwenda mbali zaidi kumtumikia Mungu kama wajibu. Tunaweza kufikia mahali ambapo tunaona furaha ya kumtumikia yeye. Furaha hii itapatikana peke yake katika upendo. Mtoto anayemtii baba yake kwa ajili tu ya hofu au kufanyizwa kazi, kamwe haoni furaha katika kutii. Mtoto anayetii kutokana na upendo, atauona utii kuwa furaha.
Wakati mtoto mdogo anapojifunza kupiga violin (fidla), ni lazima afanye mazoezi kila siku. Kwanza, mazoezi haya huonekana kama anafanyizwa kazi badala ya kupata furaha. Lakini baadaye kama mtoto atakuwa mpigaji mahiri, itafikia mahali aanze kujikuta kwamba kupiga fidla ni zaidi ya kufanya kazi. Ni lazima iwe furaha. Kazini wakati mtoto anapofanya mazoezi kwa sababu mama yake anasema, “ni lazima ufanye mazoezi.” Furaha ni wakati mtoto anacheza kwa sababu anafurahia kucheza. Mpiga fidla wa kweli huipata furaha wakati wa kufanya mazoezi kama wajibu.
Hali hii ni sawa na ukweli ulio katika maisha yetu ya kiroho. Mtu mtakatifu hulisoma neno la Mungu kwa nidhamu ya kiroho, lakini pia hufurahi katika hilo neno la Mungu. Utii kwa Mungu huja kwa pamoja kama kazi na furaha.
Fikiria tofauti iliyopo wakati tunapomtumikia Mungu katika furaha kuliko kama kazi. Utii hufanyika furaha, na siyo mzigo. Maombi, neno la Mungu, na taratibu za kinidhamu za maisha ya Kikristo hufanyika furaha. Hii ndiyo maana ya kumpenda Mungu. Watu watakatifu hutii kwa furaha kwa sababu wanampenda Mungu.
[8] Imechukuliwa kutoka John N. Oswalt, “Dangers to Holiness: Perfectionism and Legalism.” Retrieved from https://www. gbs.edu/dangers-to-holiness-perfectionism-and-legalism/ December 20, 2019.
Aliipata Siri - John Sung
John Sung alikuwa mmoja wa wainjilisti mashuri sana katika karne ya ishirini. Alikuwa mtoto wa mchungaji wa Kimethodisti katika Jimbo la Fijian, China, na akawa Mkristo akiwa na umri wa miaka tisa.
Sung alikwenda Amerika kusoma akiwa na umri wa miaka kumi na tisa. Akiwa mwanafunzi mwenye kipaji, John Sung alimaliza elimu yake ya shahada ya kwanza, uzamili, na uzamivu katika kemia ndani ya miaka sita tu. Kwa bahati mbaya, katika kipindi hiki, Sung alianza kutilia mashaka mafundisho ya Biblia aliyojifunza kutoka kwa baba yake.
Sung aliamua kuchukua tena mwaka mmoja kusoma katika chuo cha Union Theological Seminary akitaka kutafuta majibu ya maswali yake. Badala ya kupata majibu aliyotaka, maprofesa wapenda mabadiliko ya wastani katika chuo hicho, walizidi kuididimiza imani yake zaidi.
Mwaka 1926, John Sung alihuduria ibada eneo la Harlem. Usiku ule, msichana wa miaka kumi na tano alitoa ushuhuda wa mabadiliko Mungu aliyomfanyia katika maisha yake. Sung alianza kutafuta kuurejesha tena uhusiano wake na Mungu. Maprofesa wa ile seminari walijiridhisha kwamba John Sung alikuwa mgonjwa wa akili, na raisi wa chuo, Henry Sloan Coffin, akamweka Sung kwenye hifadhi ya watu waliochanganyikiwa akili. Katika muda wa siku 193 alizokuwa amezuiliwa kama aliyechanganyikiwa, aliisoma Biblia mwanzo hadi mwisho mara 40.
Kufuatia kuachiliwa kwake, John Sung alirudi China. Dr. Sung alijua kwamba angeweza kuchukua nafasi ya kufundisha katika chuo chochote nchini China. Hata hivyo, akiwa ndani ya meli, Mungu alikuwa anamwita ayasalimishe zaidi maisha yake. Siku moja, kama alama ya kujisalimisha kabisa, na kwenye kutaka kuondoa mipaka na vizuizi vyovyote vya yeye kufundisha, Dr. Sung alikusanya vyeti vya shahada na stashahada zake zote na zawadi nyingine zote za kitaaluma akazitupa nje ya meli.
John Sung aliwasili China siyo kama “Dr. John Sung, Profesa wa Kemia” bali kama “John Sung, Mtumishi wa Mungu.” Sung alianza kuhubiri na aliweza kuwa na huduma kubwa na yenye nguvu ya uinjilisti. Wanahistoria wanakadiria kwamba chini ya huduma ya Jonh Sung, zaidi ya watu laki moja waliokolewa wakati wa kurudi kwake China mwaka 1927 hadi alipofariki mwaka 1944 akiwa na umri wa miaka arobaini na moja.
Maisha ya John Sung yanadhihirisha kwamba kumpenda Mungu ni zaidi ya mhemuko. Kwa sababu ya upendo wake kwa Mungu, Dr. Sung aliachana na tamanio lake la kuwa na kazi yenye sifa ya kufundisha katika vyuo vikuu vya China, na akaitikia mwito wa Mungu wa kutumika kama mhubiri wa injili. Kwa sababu ya upendo wake kwa Mungu, Sung alikubali kuachana na marupurupu yake yote ya mtu anayelipwa katika nafasi nzuri ya kazi na akaamua kuishi maisha rahisi, akila vyakula vya watu wa kawaida. Kwa sababu ya upendo wake kwa Mungu, John Sung alitumia masaa kadhaa kutoka katika muda wake kila siku kwa ajili ya maombi na kujifunza Biblia. Maisha yake yalimezwa na upendo wake kwa Mungu, na kwa sababu ya upendo wake kwa Mungu, Mungu alimtumia John Sung kuleta maelfu ya watu kwa Kristo.
Tafakuri ya Somo la 7
(1) Kuwa mtakatifu ni kumtii Mungu.
(2) Watu wa Mungu huipata furaha yao kubwa kutoka kwa Mungu.
(3) Kwa sababu wanajua kwamba sheria ya Mungu inaakisi upendo wake, watu wa Mungu hufurahi katika sheria za Mungu.
(4) Wale wote walio na furaha ya Mungu, hujikuta kwamba Mungu amejitoa mwenyewe kwa ajili yao.
(5) Yesu alionyesha mfano halisi wa nini maana ya kumpenda Mungu.
(6) Jawabu kwa maisha ya dunia ni kuwa na upendo wa kina kwa Mungu
(7) Jawabu la kuishi kwa sheria ni kuwa na upendo wa kina kwa Mungu.
Kazi ya Kufanya
(1) Fikiria kwamba Mkristo mpya anakuja kwako na kukuambia, “Nataka niwe na uhusiano wa kina na Mungu. Nampenda Mungu, lakini ni vigumu kujua jinsi ya kukua kwenye uhusiano wangu na yeye. Simwoni Mungu, na inaonekana anakaa mbali sana. Nifanyeje?” Andika insha ya kurasa 2-3 ya kumsaidia huyu muumini mpya aweze kujua ni kwa namna gani anaweza kukua kwenye uhusiano wake na Mungu. Pamoja nayo, uongeze na hatua za vitendo za jinsi ya kusoma Biblia, kuendeleza maisha ya maombi, na kushirikisha Imani yako. Kwenye kipindi kinachofuata cha darasa, kila mwanafunzi atapaswa ayasome majibu yake na hatimaye yajadiliwe na darasa kwa pamoja.
(2) Anza kikao kinachofuata cha darasa kwa kunukuu Marko 12:29-31.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.