Kufikia mwisho wa somo hili, kila mwanafunzi atapaswa:
(1) Akubaliane na uzuri wa utakatifu wa Mungu na mpango wake wa kutufanya tuwe watakatifu.
(2) Akatae mitazamo inayopotosha kuhusiana na utakatifu, na akubaliane na mitazamo ya kibiblia inayohusiana na utakatifu.
(3) Aimarishwe katika kuweza kumfafanulia mwamini mpya ni nini maana ya kuwa mtakatifu.
(4) Kukariri 1 Petro 1:14-16.
Utambulisho wa Kozi
Utakatifu ni mojawapo ya dhamira kuu ya Biblia. Katika maandiko, Mungu alituonyesha yeye ni nani: kwamba ni Mungu aliye Mtakatifu. Kisha, Mungu akatuonyesha tunawezaje kuwa kwa neema yake: tunaweza kuwa watu watakatifu.
Kwa kila mwamini wa kweli, kuna kiu ya utakatifu. Kama watoto wa Mungu, tunatamani sana kuwa kama yeye. Kwa masikitiko, wengi katika kanisa la wakati huu wa sasa wamekubaliana na mawazo potofu kwamba utakatifu hauwezekani. Badala ya kutafuta kuwa kama Kristo, Wakristo wengi wanakubaliana na kushindwa katika kuishi maisha ya dhambi. Badala ya maisha ya Kikristo yenye ushindi, Wakristo wengi wamejilazimisha kuwa chini ya “utawala wa dhambi.”
Zaidi ya miaka mia moja iliyopita, John Hyde. Mmishenari maarufu kwa ajili ya India, alisema, “Tunachohitaji kwa sasa ni uamsho wa utakatifu.” Kama ndivyo ilivyokuwa, basi ni ukweli usiopingika katika ulimwengu wa dhambi wa karne ya ishirini na moja.
Kama utakatifu ni muhimu sana kwa Mungu, ni lazima tujiulize, “Inamaanisha nini kuwa mtakatifu?” Kama utakatifu umeamriwa katika maandiko matakatifu, tunapaswa tujiulize, “Je inawezekana kuishi maisha ya utakatifu?”
Katika kozi hi, tutajifunza anachomaanisha Mungu anaposema “Kuweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu.” Kama tunavyoelewa ujumbe wa utakatifu katika Biblia, tutaona kwamba maisha ya utakatifu yanawezekana kwa kila Mkristo. Kila somo litahusisha mambo matatu:
Tutajificha maana za maneno ya Biblia kama “utakatifu”, “utakaso”, na “ukamilifu”. Hii ni sehemu ya theolojia ya Biblia inayohusiana na utakatifu.
Tutajifunza mitazamo ya vitendo halisi vya maisha ya utakatifu, moyo ulio safi, na roho inayomfanania Kristo.
Tutayaangalia maisha ya Mkristo anayedhihirisha maana ya kuwa mtakatifu. Tutaangalia ni kwa jinsi gani mtu mtakatifu anatenda katika maisha yake ya kila siku.
Maandiko ya Kusoma na Kujadili
Kabla ya kuendelea na somo, soma maandiko yafuatayo kwa uangalifu na jadili maswali yaliyopo. Hii itatambulisha baadhi ya mada tutakazojifunza katika masomo haya.[1]
► Soma Mambo ya Walawi 19:2. Kutokana na kifungu hiki, Kwanini Israel walitakiwa kuwa watakatifu?
► Soma 1 Petro 1:15-16. Waamini wanatakiwa kuwa na tabia gani?
► Soma Waebrania 12:14. Kutokana na kifungu hiki, ni sifa gani kuu mbili ambazo Wakorintho wanapaswa kuzifanyia kazi kama watataka kumwona Bwana?
► Soma 1 Wathesalonike 4:3-8. Mungu anamwita kila mwamini kukaa mbali na dhambi gani? Mungu amewaita watu wake kwenye nini?
► Soma Ufunuo 20:6. Kuna tabia gani ya kiroho inayoonekana kwa wale wote watakaokuwepo katika unyakuo wa kwanza?
[1] Maswali haya yamekusanywa na Mchungaji Timothy Keep.
Uzuri wa Utakatifu
► Unaposikia mtu akitambulishwa kama “mtakatifu” ni wazo gani linakujia kwenye ufahamu wako? Je wazo lako ni hasi au chanya? Kwa nini?
Mmishenari mmoja wakati fulani alimtembelea chifu wa zamani wa Kiafrika. Chifu alimwuiza, “Mkristo ni nani?” Mmishenari akajibu, “Mkristo hawezi kuiba ng’ombe wa adui yake. Mkristo hawezi kutembea na mke wa adui yake. Mkristo hawezi kuua.”
Chifu akasema, “Nimeelewa. Kuwa Mkristo ni sawa na kuwa mtu mzee! Nilipokuwa kijana, nilimpiga adui yangu, nikamwibia ng’ombe wake na nikatembea na mke wake. Kwa sasa mimi ni mzee sana kuweza kumshambulia adui yangu; mimi ni Mkristo!”
Kwa masikitiko, hivi ndivyo watu wengi wanavyofikiri kuhusiana na ujumbe wa maisha ya utakatifu. Wanafikiri kwamba utakatifu siyo zaidi ya orodha ya majina ya dhambi za kukwepa. Wanakosa uzuri wa Utakatifu kama unavyofundishwa katika neno la Mungu.
Mawazo potofu kuhusu utakatifu
Mungu ni Mtatakatifu. Watu wa Mungu ni lazima wawe watakatifu. Huu ni ujumbe mkuu sana katika Biblia. Hata hivyo, bado kuna imani nyingi potofu kuhusiana na utakatifu.
Watu wengine wanaamini kwamba ni watu wachache tu wanaweza kuwa watakatifu. Wanawagawa Wakristo katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni Wakristo katika imani zao ambao wamemwamini Kristo kama Bwana na Mwokozi wao, lakini hawamtii Mungu kwa uaminifu katika matendo na tabia zao. Kundi la pili linatokana na Wakristo waliofikia kiwango cha juu zaidi wakiwemo- wahubiri, wachungaji, na watu wema sana. Kwa mujibu wa mtazamo huu, ni Wakristo wachache sana walio watakatifu.
Watu wengine wanaamini kwamba tunakuwa watakatifu kwa kujitenga na watu wengine. Miaka mingi iliyopita, baadhi ya “watu watakatifu” walikwenda kuishi jangwani. Mtu mmoja aliishi huko kwa miaka thelathini na saba juu ya jukwaa lilioinuliwa sana juu ya ardhi. Aliamini kwamba tunafanyika watakatifu kwa kujitenga na watu wengine.
Watu wengine wanaamini kwamba tunakuwa watakatifu tu tukishafariki. Wanaamini kwamba kamwe hatuwezi kutimiza makusudi ya Mungu katika maisha haya, lakini tutafanywa watakatifu tukishafariki. Kwa imani hii, kifo siyo adui yetu bali rafiki. Katika kifo, hatimaye tunalipata kusudi la Mungu kwa watu wake.
Watu wengine wanaamini kwamba tunakuwa watakatifu kwa kufuata sheria. Wanaamini kwamba tunakuwa watakatifu kwa kuvaa aina fulani ya mavazi, au kwa kufuata orodha ya vitu vya “kufanya au kutofanya”. Wanaamini kwamba utakatifu ni kwa mambo ya nje tu lakini siyo kubadilishwa kabisa kwa moyo.
Watu wengine wanaamini kwamba ushahidi wa mtu mtakatifu ni pale anapokuwa na karama ya kunena kwa lugha na kufanya miujiza. Wanaupima utakatifu kwamba siyo katika maisha ya utakatifu, bali katika matendo ya ishara na miujiza.
Mwisho, watu wengine wanaamini kwamba utakatifu hauwezekani! Wanaamini kwamba utakatifu ni dhana tu Mungu alioiweka kwetu ili kutupa changamoto ya kufanya mambo mazuri, lakini siyo jambo la uhalisia katika ulimwengu huu. Kwa imani hii, hakuna hata mtu mmoja anayeweza kushika agizo la Mungu la “Iweni watakatifu”.
Hata hivyo, agizo la Mungu la “Iweni watakatifu” ni agizo analotuka sisi tulitii. Mungu ni Baba mwema; kamwe hawezi kutuamuru tufanye jambo lolote ambalo haliwezekani ndani ya neema yake. Kuwa watakatifu ni kuwa katika ile hali Mungu aliyotuumba tuwe nayo. Kwa nguvu zetu wenyewe, haiwezekani kuwa na moyo wa utakatifu, lakini kwa uweza wa Mungu moyo wa utakatifu unawezekana kwa kila mwamini. Utakatifu huja kupitia neema ya Mungu, na siyo kwa nguvu zetu wenyewe.
► Katika haya mawazo potofu yote kuhusiana na utakatifu, ni lipi limekithiri kwenye eneo lako unalohudumu? Je, utakataifu unaonekana kuwa ni mzuri miongoni mwa Wakristo katika jamii yako?
Picha ya Biblia kuhusu utakatifu
Kinyume na mawazo hasi yaliyoorodheshwa hapo juu kuhusiana na utakatifu, Biblia inaonyesha utakatifu kama uwezekano mzuri kwa watoto wa Mungu. Jaribu kufikiria mambo yanayoitwa matakatifu ndani ya Biblia. Hakuna hata moja lililo baya au lisilovutia; yote ni mazuri na yanayovutia. Asili ya Mungu ya utakatifu ni nzuri na inayovutia.
Asili ya Mungu ya utakatifu ni nzuri na yenye utukufu.
Vitu vyote vilivyokuwa kwenye hekalu vilikuwa vitakatifu na vinapendeza.
Israeli iliitwa kuwa taifa takatifu litakalowavuta watu wengine kuja kwa Mungu. Utakatifu wake uliwavutia watu, haukuwafukuza kutoka kwao.[1]
Kanisa linaitwa liwe watu watakatifu. Ndiye atakayekuwa bibi harusi mzuri kwa ajili ya Bwana harusi.
Kila picha hapa inavutia. Biblia inaonesha kwamba utakatifu wa kweli siyo mchafu au wa kuogopesha. Badala yake ni kipawa cha Baba yetu wa Mbinguni. Kama tutauona utakatafu kama ulivyo tutakuwa na kiu ya moyo mtakatifu na maisha matakatifu. Kama tutafundisha utakatifu kama Biblia inavyofudisha watu wetu watakuwa na kiu ya moyo safi na maisha matakatifu. Utakatifu ni kipawa kizuri kutoka kwa Baba mwenye upendo
[1] Unaweza ukasema. “Lakini vipi kuhusu Mafarisayo? Walikusudiwa wawe watu “watakatifu”, lakini waliwafungia wengine nje.” Tutaona katika masomo haya kwamba “utakatifu” wa Mafarisayo haukuwa wa kweli, Kwao haki ilikuwa ni ukiri wa nje tu na siyo utakatifu wa kweli.
Uzuri wa utakatifu unaonekana katika uumbaji wa asili wa Mungu
Aliumba dunia iliyokamilika
Tuanzie kwenye bustani nzuri ya Eden. Fikiria kuhusu matunda matamu ambayo umewahi kula, tunda katika Eden lilikuwa tamu zaidi. Fikiri kuhusu maua mazuri sana ambayo hujawahi kuyaona; maua ya bustani ya Eden yalikuwa mazuri zaidi. Mungu aliumba dunia iliyokamilika, ambayo ilikuwa haina madhara ya dhambi. Aliumba ulimwengu usiokuwa na maumivu, machozi au kifo.
Muhimu kuliko yote, Mungu aliumba ulimwengu wenye urafiki wa ndani kati ya Mungu na mwanadamu. Hakuna kilichomtenganisha mwanadamu na Mungu. Kila siku Mungu alimtembelea Adamu na Hawa. Hakuna kiumbe yeyote aliyekuwa na upendeleo kama huu. Mungu alimwumba mwanadamu kwa ajili ya uhusiano maalumu na yeye. Katika bustani ya Eden, kulikuwa na amani iliyokamilika kati ya Mungu na mwanadamu.
Shetani aliiharibu dunia ya Mungu iliyokuwa Kamilifu
Shetani alitaka aiharibu hii dunia iliyokamilika. Shetani alichukia kila kitu Mungu alichoumba. Juu ya yote, Shetani alichukia urafiki wa karibu uliokuweko kati ya Mungu na mwanadamu. Alikusudia kusambaratisha uhusiano huu wa upendo na uaminifu.
Shetani hakuweza kumharibu mwanadamu moja kwa moja, kwahiyo alidhamiria kuusambaratisha uhusiano uliokuwepo kati ya Mungu na mwanadamu. Shetani alijua kwamba Mungu ni mtakatifu na kwamba alimwumba mwanadamu kwa mfano wake. Shetani alitaka aharibu ule mfano mtakatifu ndani ya mwanadamu. Mungu mtakatifu na mwanadamu mtakatifu wangekuwa na uhusiano usiovunjika, lakini Shetani akaweza kuuharibu uhusiano huu kwa kumdanganya mwanadamu atende dhambi.
Shetani alikuja kwa Hawa kwa sura ya nyoka. Nyoka alihoji amri ya Mungu. Akauliza, “Je ni kweli Mungu alisema ‘Msile matunda ya miti yote ya bustani’?” Alitaka amsababishe Hawa awe na mashaka dhidi ya uzuri wa Mungu. Hawa akamjibu, “Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, ‘Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa.’”[1]
Nyoka alimlaumu Mungu kwa kuwafanyia mema Adam na Hawa. Nyoka akamwambia mwanamke, “Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.” Nyoka akamwingiza Hawa kwenye kiburi: “Mtakuwa kama Mungu.”
Hawa akala lile tunda, akampa na Adam, akala. Adam na Hawa walijitambua kwamba wamevunja sheria ya Mungu. Mungu alipofika bustanini, waliona aibu wakajificha asiwaone. Uhusiano wa karibu uliokuwepo kati ya Mungu na mwanadamu ukavunjika.
Mungu hakuvunjika moyo na uumbaji wake
Kutokana na dhambi yao, Mungu aliwafukuza Adamu na Hawa kutoka katika bustani ya Eden. Dhambi ilivunja uhusiano wa karibu kati ya Mungu na mwanadamu. Dhambi iliharibu mfano wa Mungu ndani ya mwanadamu. Lakini kwa sababu ya upendo wake, Mungu hakumwacha mwanadamu katika hali hii ya kutisha. Mungu angeweza kusema, “Adamu, umesababisha balaa hili lote, ni tatizo lako! Mimi ninaondoka.” Badala yake, Mungu wa upendo akafanyika sehemu ya ulimwengu wetu akatoa tiba kwa ajili ya dhambi zetu.
Tiba hii ilihusisha njia ya kuelekea msamaha. Mungu akatoa njia ya kurejesha uhusiano kati ya Mungu mtakatifu na mwanadamu aliyeanguka. Kanisa limekuwa kila wakati likihubiri kwamba, “Wenye dhambi wanaweza kuhesabiwa haki na Mungu.” Kupitia msalaba, tunaweza kusamehewa dhambi.
Hizi ni habari njema sana! Lakini wakati mwingine Kanisa limesahau upande mwingine wa tiba ya Mungu. Tiba ya Mungu kwa dhambi siyo tu njia ya msamaha bali pia njia ya urejesho. Mungu alitoa njia ya kurejesha sura yake ndani ya mwanadamu.
Mungu hakuridhishwa na kusema, “Mtakuwa huru kutokana na adhabu ya dhambi, lakini kamwe hamtakuwa huru kutokanana nguvu ya dhambi.” Hapana! Mungu alitoa njia ambayo itaweza kumfanya mwanadamu awe mtakatifu. Mungu alitembea bustanini akiwa na watu watakatifu; hawezi kutembea na watu wenye dhambi. Mungu anataka uhusiano na watu wake, kwa hiyo alitoa njia ya kutufanya watakatifu.
Katika maandiko yote, tunamwona Mungu akiwa na kazi ya kuwafanya watu wawe watakatifu ili aweze kuwa na uhusiano nao. Mungu hawezi kusema, “Najua wewe ni mdhambi, lakini nitafunga macho yangu, nisizione dhambi zenu, nijifanye nyie ni wenye haki.” Badala yake Mungu anaahidi kuwafanya watu wake watakatifu.
"Bwana atakuweka uwe taifa takatifu kwake, kama alivyokuapia; utakaposhika maagizo ya Bwana, Mungu wako, na kutembea katika njia zake."[2]
Mungu anataka awafanye watu kuwa watakatifu. Hili ndilo kusudi la Mungu kwa watu wake. Mungu anaahidi kwamba, “watawaita, Watu watakatifu, Waliokombolewa na Bwana.”[3]
Uzuri wa utakatifu unaonekana katika asili ya Mungu
Kutokana na anguko, mwanadamu hakuwa mtakatifu tena. Kwa haraka tunasahau asili ya Mungu ya utakatifu. Mungu alituumba “kwa mfano wake”. Kwa sasa tumejiumbia miungu midogo katika mifano yetu - wivu, chuki, na kiburi.
Wababeli walielezea habari za Marduk aliyekuwa chifu wa mungu kwa kumuua mama yake. Wagiriki walielezea habari za Zeu aliyekuwa anamiliki vimada wengi. Warumi walielezea habari za Bacchu, mungu wa ulevi na ufisadi.
Miungu hii haikuwa mitakatifu. Watu walioiabudu miungu hii walifanana na miungu hii pia. Watu walisema uongo, waliiba, na walidanganywa sawa na miungu yao ilivyosema uongo, ilivyoiba na kudanganywa. Watu waovu walitengeneza miungu waovu. Kinyume chake, miungu hii ikawaruhusu wanadamu kuendelea katika dhambi zetu. Tukawa kama miungu tuliyoiabudu.
Yehova hafanani na hii miungu ya uongo. Mungu ni mtakatifu. Kwa kurudia – rudia, maandiko yameshuhudia utakatifu wa Mungu. Baada ya kuvuka Bahari ya Shamu, watu wa Israeli walimsifu Mungu wao aliye Mtakatifu. Waliimba, “Ee Bwana, katika miungu ni nani aliye kama wewe? Ni nani aliye kama wewe, mtukufu katika utakatifu, Mwenye kuogopwa katika sifa zako, mfanya maajabu?”[1]
Mtunga Zaburi aliimba, “Na Wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli.”[2] Isareli ilimsifu Mungu kwa ajili ya utakatifu wake. Muimba Zaburi, walimwita Mungu, “Mtakatifu, Mungu wa Israeli.”[3]
Manabii walishuhudia kwamba Mungu ni mtakatifu. Sawa na mtunga Zaburi, walimwita Mungu, “Mungu mmoja Mtakatifu wa Israeli.”[4] Isaya akamwita Mungu, “Mtakatifu wa Israeli” mara ishirini na sita. Isaya alimheshimu, “Yeye aliye juu ya vyote na aliyeinuliwa juu, anayeishi miliele, ambaye jina lake ni mtakatifu.”[5] Utakatifu ni sehemu kubwa sana ya tabia ya Mungu kwamba hata kuweza kuapa kwa “utakatifu wake” ilikuwa sawa na kuapa kwa “jina kake mwenyewe.”[6] Habakuki alimshuhudia Mungu, “Wewe uliye na macho safi hata usiweze kuangalia uovu, wewe usiyeweza kutazama ukaidi.”[7] Manabii walijua kwamba Mungu ni Mtakatifu.
Huko mbinguni, kumwabudu Mungu kunasherehekea utakatifu wake. Malaika Maserafi waliimba, “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni Bwana wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake.”[8] Yohana mwona maono aliona viumbe wanne wakimsifu Mungu wakisema, “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja!”[9] Mungu ni Mtakatifu.
Uzuri wa utakatifu unaonekana katika mpango wa Mungu kwa watu wake
Mungu Mtakatifu alimuumba mwanadamu kwa ajili ya uhusiano na yeye, lakini dhambi zetu zilitutenganisha na yeye. Hata hivyo, Mungu alikusudia kuurejesha uhusiano huo na watu wake. Kwa kuwa ni watu watakatifu tu wanaoweza kusimama mbele ya uwepo wa Mungu Mtakatifu, alitengeneza njia ya kutufanya sisi watakatifu. Mungu alifundisha maana ya kuwa mtakatifu kwa watu wake ambao hawakuwa watakatifu. Kuna maeneo mawili katika hatua hii:
Mungu alimfundisha mwanadamu asili ya utakatifu wa Mungu. Marduk, Zeu, na Bacchu walikuwa na nguvu lakini wasio na maadili. Mungu alijidhihirisha mwenyewe kuwa mwenye nguvu na mtakatifu.
Mungu alimfundisha mwanadamu asili ya watu watakatifu. Mungu alisema, “Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu.”[1] Kwa kuwa Mungu ni Mtakatifu, watu wake ni lazima nao wawe watakatifu.
Isaya alihubiri katika taifa la watenda maovu. Dhambi ilikuwa imeharibu kabisa uzuri wa watu wa Mungu. Kutoka kuwa watu waliochaguliwa na Mungu, Israeli ilikuwa imeangukia katika hali ya aibu ya watu walioshindwa na kupelekwa utumwani; walikuwa watumwa waliofedheheshwa. Lakini Isaya aliona katika maono siku ambayo “Haki ya Israeli itakapokwenda kung’aa.” Katika siku hiyo, Israeli “itakuwa taji ya uzuri katika mkono wa Bwana.”[2]
Watu wanaoshindwa kuelewa ujumbe wa utakatifu katika Biblia mara nyingi wanauonesha utakatifu kama sheria, sheria ngumu, na sura za ukali. Huu siyo mtazamo wa kibiblia kuhusiana na utakatifu. Badala yake, kuwa mtakatifu ni kuonyesha uzuri wa utakatifu wa Mungu mwenyewe. Kuwa mtakatifu kunatoa uhuru wa furaha wa kuishi ndani ya uhusiano na Mungu Mtakatifu. Katika Biblia, utakatifu siyo neno la huzuni bali la furaha na uzuri!
Katika Biblia, Mungu anadhihirisha asili yake ya utakatifu. Kisha, Mungu anawafundisha watu wake jinsi ya kuishi maisha matakatifu. Kwa umuhimu mkubwa kabisa, Mungu anaonyesha kwamba atawapa watu nguvu za kuwawezesha kuwa kama yeye anavyotaka wawe. Kupitia neema yake, Mungu anaweza kuwafanya watu wawe watakatifu. Mungu hapuuzi dhambi zilizoko ndani ya watoto wake; badala yake anatufanya tuwe watakatifu. Mungu wa utakatifu anapendelea ushirikiano na watu watakatifu.
Kupitia Neno lake, Mungu amewafundisha watu wake ni nini maana ya kuwa mtakatifu. Wakati Mungu alipoanza kuwafundisha watu wake, hawakujua lolote kuhusu utakatifu. Hawajawahi kumwona Mungu aliye mtakatifu au watu watakatifu. Mungu alifundisha sana kuhusa utakatifu zaidi ya tunapofundisha lugha kwa mtoto.
Tunapomfundisha mtoto mdogo tunanyoosha kidole kueleka kiti na kusema “Kiti”. Tunanyoosha kwenye gari na kusema, “Gari”. Hatua kwa hatua mtoto anajikuta anajifunza maana za maneno. Mtoto huanza kujifunza maana ya neno “upendo” kwa uzoefu wa upendo anaoupata kutoka kwa mama yake. Mtoto anajifunza maana ya neno “haki” wakati mama yake anapomwadhibu kwa kosa la kukosa utii.
Mungu alifundisha maana ya utakatifu kwa njia hiyo hiyo. Tukiwa watu tuliokuwa tumeanguka, hatukujua ni nini maana ya kuwa mtakatifu. Hatua kwa hatua, Mungu akawa anafunua maana ya utakatifu kwa watu wake kupitia maandiko na picha zinazoonyesha ni nini maana ya kuwa mtakatifu. Tunapotafuta maana ya neno Utakatifu ndani ya Biblia tunaona mambo yafuatayo:
Kuwa mtakatifu ni kuwa na ushirika wa karibu na Mungu. Watu watakatifu katika kitabu cha Mwanzo (kama Henoko na Abrahamu) walikuwa ni watu waliokuwa na uhusino wa karibu sana Mungu. Walitembea na Mungu. Kwa kuonesha maisha ya watu watakatifu, Mungu alijifunua kwamba mtu mtakatifu ni yule aliye katika ushirika na Mungu.
Kuwa mtakatifu ni kuakisi mfano na sura ya Mungu. Utakatifu siyo tabia ya asili ya mwanadamu. Utakatifu ni sifa ya Mungu pekee. Israeli walitakiwa wawe watakatifu, “Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu.”[1] Kuwa Mtakatifu maana yake ni kuakisi mfano na sura ya Mungu.
Kuwa mtakatifu maana yake ni kufanana na Mungu. Kwa mara ya kwanza neno “Utakatifu” lianze kwenye Biblia, lilirejea siku ambayo imetengwa kwa makusudi maalumu kwa ajili ya Mungu. Siku ya Sabato ilikuwa takatifu; ilikuwa imetengwa kutoka zile siku nyingine sita. Kama mtoto anayejifunza maana ya “kiti,” Mungu aliilenga siku ya saba na kusema “Ni takatifu.”
Kuwa mtakatifu ni kuwa na moya usiogawanyika. Katika vitabu vya historia, Mungu alitumia neno “ukamilifu” kwa watu ambao “hawana moyo wa kugawanyika.” Kuwa mtakatifu kunamaanisha kuwa na uamuzi usiokuwa na kusitasista katika msimamo wetu na Mungu. Moyo wa utakatifu humpenda Mungu bila mgawanyiko.
Kuwa mtakatifu ni kuishi maisha ya haki. Manabii walihubiri kwa watu waliofikiria tu kwamba, “Tunaenda kuabudu hekaluni na kutoa zaka zetu, kwa hiyo ni watakatifu.” Manabii walionesha wazi kwamba haitoshi tu kufuata matambiko. Kuwa mtakatifu inamaanisha kuishi maisha ya uadilifu kwa ajili ya Bwana na watu wengine. Watu watakatifu “wanatenda haki, wanapenda huruma na wanaenenda kwa unyenyekevu pamoja na Mungu.”[2]
Kuwa watakatifu ni kuwa na upendo kamili kwa Mungu na kwa jirani yetu. Vitabu vya Injili vinaonyesha ufunuo kamili wa utakatifu wa maisha ya Yesu Kristo. Yesu alikuwa na moyo wa utakatifu uliokuwa umejitoa kabisa kwa ajili ya mapenzi ya Baba. Yesu alikuwa na mikono ya utakatifu iliyotenda kwa upendo halisi dhidi ya watu wengine. Yesu alionyesha kuwa kuwa mtakatifu inamaanisha kumpenda Mungu, kumpenda jirani yetu kama tunavyojipenda wenyewe.
Kuwa watakatifu ni kuishi katika utimilifu wa Roho Mtakatifu. Katika kitabu cha Matendo, tunaona mfano wa Wakristo waliokuwa wanajazwa na Roho wa Mungu. Kupitia nguvu za Roho Mtakatifu, waliyaishi maisha matakatifu. Tunakuwa watakatifu tunapoendelea kuishi katika utimilifu wa Roho Mtakatifu.
Kuwa Mtakatifu ni kumfanania Kristo. Yesu alikuwa mfano halisi wa utakatifu wa moyo na mikono. Nyaraka za Mitume katika Agano Jipya zinaonesha kwamba inawezekana kabisa kwa Wakristo wa kawaida kufuata mfano wa Yesu Kristo. Nyaraka hizi hutoa mwongozo wa vitendo wa jinsi ya kuishi maisha ya utakatifu kila siku. Nyaraka hizi zinatufundisha jinsi ya kuishi kama watu tunaomfanania Kristo.[3]
Utakatifu hutuandaa kumwona Mungu. Bustanini Eden, Mungu aliandaa bustani ambayo watu watakatifu wangeishi wakiwa katika ushirika na Baba. Kwa sababu ya dhambi tulifukuzwa kutoka katika ile bustani. Lakini Mungu hakuachana na mpango wake. Katika kitabu cha Ufunuo, tunaona kwamba watu wa Mungu siku moja watauona uso wa Mungu. Hakuna mwenye dhambi atakayeweza kuuona uso wa Mungu, lakini Mungu anawaandaa watu watakatifu watakaoishi kwenye umilele pamoja naye. Huu ni mpango wa Mungu kwa ajili ya watu wake.
[3] “Ni lazima tuwe watakatifu, kwa sababu hii ndio sababu kuu ya msingi iliyomfanya Yesu kuja duniani. Kuzungumza na watu waokoke kutoka kwenye hatia ya dhambi bila kuokolewa kutoka utawala wa dhambi ndani ya mioyo yao ni kujichanganya kwa ushuhuda wote wa Maandiko. Yesu ni mkombozi kamili. Haondoi tu hatia ya dhambi; bali huivunja nguvu yake.” - Nukuu kutoka kwa Askofu J.C. Ryle
Hitimisho: Mungu wa utakatifu anawaita watu wake wawe Watakatifu
Dr. John Stott alikuwa mmoja wa Wainjilisti maarufu sana wa karne ya ishirini. Katika moja ya mahubiri yake ya mwisho, Dr. Stott alizungumza kuhusu mpango wa Mungu kwa watu wake.[1] Tumekombolewa kwa neema kupitia imani; tumetolewa mautini hadi kwenye uzima. Kwa nini? Kusudi la Mungu la kutukomboa ni ili tuwe kama Kristo. Dr. Stott alisema, “Kufanana na Kristo ni mapenzi ya Mungu kwa ajili ya watu wa Mungu.”
Maandiko matatu katika Agano Jipya yanatuonyesha kukua kwetu katika mfano wa Kristo hapa duniani kunatuandaa tukaishi na Mungu. Maandiko haya yanatuonyesha umuhimu wa utakatifu katika maisha ya mwamini.
Warumi 8:29 inarejea wakati uliopita na inaonyesha kusudi la Mungu la umilele kwa watoto wake.
"Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi."
Mpango wa Mungu wa umilele ni kwamba, “tufanane katika sura ya Mwana wake.” Tangu mwanzo mpango wa Mungu ni kutufanya tuwe kama Kristo. Warumi 8:28 inatoka ahadi kwamba, “katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema.” Ahadi hii “ni kwa ajili ya wale wote walioitwa kwa ajili ya kusudi lake.” Kusudi lake ni nini? Kusudi la Mungu tangulizi ni kuwafanya wana wa Mungu katika sura ya mwanae. Mungu alitukomboa ili atufanye watakatifu.
Paulo aliwakumbusha Wakristo wa Kolosai juu ya mabadiliko makubwa ambayo Mungu ameyafanya katika maisha yao. “Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa, tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa; katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake,” Kupitia kifo cha Yesu, hawa watu ambao walikuwa “maadui” kwa Mungu, sasa walikuwa wamepatanishwa na yeye. Kisha Paulo akawakumbusha hawa waamini kuhusu kusudi la Mungu la kuwapatanisha wao na yeye. “ili awalete ninyi mbele zake, watakatifu, wasio na mawaa wala lawama.”[2]
Paulo hasemi tu, “Umepatanishwa na Mungu ili ukautumie umilele wako mbinguni.” Hizo ni habari njema, lakini siyo habari njema zilizokamilika. Paulo anasema, “Umepatanishwa na Mungu ili uweze kuwa Mtakatifu.” Lengo la Mungu ni kuwafanya watoto wake wawe watakatifu wasiokuwa na lawama.”
2 Wakorintho 3:18 inarejea wakati uliopo na kuonyesha jinsi kusudi hili linavyotimia leo katika maisha ya muumini:
"Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano huo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho."
Kupitia nguvu ya Roho Mtakatifu, “tunabadilishwa kutoka kiwango kimoja cha utukufu hadi kingine.” Kusudi la Mungu linatimizwa katika mabadiliko ya watoto wake kupitia nguvu za Roho Mtakatifu. Siku hadi siku tunafanywa ili tufanane na Kristo.
1 Yohana 3:2 inarejea katika wakati ujao na kuonyesha ukamilikaji wa mwisho wa kusudi la Mungu:
"Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo."
Kitabu cha ufunuo kinalenga kwenye siku ambayo tunaweza kumwona Mungu uso kwa uso. Siku hiyo tutafanana na yeye. Kusudi la Mungu litakuwa limetimizwa kabisa na hata milele. John Stott anahitimisha kwamba, “Tutakuwa pamoja na Kristo, kama Kristo, milele.”
Kama Wakristo, kutafuta kwetu maisha ya utakatifu kunatuandaa kwa ajili ya siku ambayo tutamwona Mungu na kusudi lake katika maisha yetu likiwa linatimia. Hii itatufanya sisi tuwe na bidii katika ukuaji wetu wa utakatifu. Kila siku tunabadilishwa zaidi na zaidi katika sura yake.
Utakatifu siyo wazo la mtu fulani; bali ni tabia ya Mungu. Uelewa wetu kuhusu utakatifu unaendana zaidi na tabia ya Mungu ya Utakatifu tunayoipata katika Biblia. Jinsi tunavyotafuta kuwa kama yeye zaidi na zaidi, tukishirikiana na Mungu katika kusudi la umilele. Utakatifu ni kusudio la Mungu la uzima wa milele kwa kila mwamini. Kama watoto wa Mungu, tunapaswa tuwe na uchu wa kuona kwamba hili kusudi linatimizwa ndani ya mioyo na maisha yetu.
[1] Hotuba ya John Stott huko Keswick. (June 20, 2014). Imechkuliwa kutoka https://www.leightonfordministries. org/2014/06/20/john-stott-address-at-keswick/ Desemba 20, 2019.
[3]“Mungu anao mpango mmoja wa hatima ya mwisho ya mwanadamu– utakatifu. Kusudi lake moja ni kuzalisha watakatifu. Alikuja kuwakomboa wanadamu kwa sababu aliwaumba ili wawe watakatifu.” - Oswald Chambers
Aliipata Siri - Samweli Kaboo Morris
Mwaka 1873, Samweli Morris[1] alizaliwa Liberia, Afrika Magharibi kama Mwana wa mfalme Kaboo, mtoto wa chifu wa kabila. Baba yake aliposhindwa kwenye mapigano, Kaboo alikamatwa kwa ajili ya kutolewa kama fidia. Siku moja, Kaboo akaona mwanga uking’aa na akasikia sauti kutoka mbinguni ikimwambia aondoke akimbie. Kamba zilizokuwa zimemfunga mikononi zilifunguka zikaanguka, na Kaboo akakimbilia jangwani.
Alitembea kwenye jangwa kwa siku kadhaa hadi alipofika katika jiji la Monrovia. Akiwa kwenye lile jiji, kijana mmoja akamwalika aende kanisani kwake. Wakati Kaboo alipotembelea lile kanisa, mmishenari alikuwa anaelezea historia ya jinsi Paulo alivyobadilishwa. Alipokuwa akielezea kuhusu mwanga na sauti kutoka mbinguni, Kaboo alitambua kwamba hii ni ile ile sauti aliyoisikia jangwani. Bila kukawia, alimkubali Kristo kama Bwana na Mkombozi wake na akabatizwa kwa jina la Samweli Morris.
Baada ya miaka miwili, Samweli Morris alianza kufanya kazi ya kupaka rangi ili ajipatie kipato cha kuendesha maisha huku akiendelea kujifunza Biblia. Alikuwa anapenda kujifunza zaidi kuhusu Roho Mtakatifu na maisha ya nguvu za Roho. Baada ya mmishenari kumweleza kwamba amefundisha yote aliyojua, Morris alimwuliza, “Je mwalimu wako alikuwa nani”? Akamwlezea kuhusu mhubiri mmoja mtakatifu wa Amerika aitwaye Stephen Merritt. Akiwa hana fedha au usafiri, Morris akajongea karibu na bandari kutafuta meli ya kuzamia ili aende Amerika. Alikuwa amekusudia kujifunza Zaidi kuhusu kuishi katika Roho.
Alilala ufukweni akingojea apate meli. Wakati meli ilipofika, Morris akamwomba kapteni wa meli ampeleke Amerika. Kapteni alikataa, lakini baada ya muda mfupi, mabaharia wake wawili wakatoroka kazi wakakimbia. Kapteni akamwambia Morris kwamba anaweza akamsaidia kufanya kazi kwa kubadilishana na yeye kumpeleka New York. Wakati wa safari, alinyanyaswa vibaya na wale mabaharia wengine, ikiwa ni pamoja na kupewa kazi nzito za kwenye meli. Hata hivyo, Samweli alionyesha moyo wa upendo kwa wale mabaharia waliomsulubu hadi meli ilipokaribia New York, kapteni na baadhi ya mabaharia wakawa wamebadilishwa (wameokoka).
Wakati Morris alipowasili New York, alikutana na Stephen Merritt na akamwelezea shahuku yake ya kutaka kujifunza zaidi kuhusu Roho Mtakatifu. Bwana Merritt alikuwa akahudhurie kikao mahali pengine, lakini akamwacha Morris kwenye misheni yake kwa ajili ya jioni. Aliporejea, alimkuta Samweli akiongoza kipindi cha maombi. Katika usiku wa kwanza nchini Amerika, Samweli Morris aliwaongoza karibu watu ishirini kumpokea Kristo.
Stephen Merritt alimsaidia Samweli Morris kujiunga na Chuo Kikuu cha Taylor kwa ajili ya maandalizi ya kwenda kufanya Uinjilisti katika nchi Liberia. Morris aliwasili chuoni Indiana bila fedha, lakini akiwa na imani kubwa kwamba Mungu atatoa. Alimwomba raisi wa wanafunzi, “Naomba unipe chumba ambacho hakuna mtu mwingine yeyote anayekitaka.” Usiku ule wanafunzi wenzake walimsikia “akizungumza na Baba yake.” Umahiri wake wa kumwamini kabisa Mungu uliwavutia wengi katika chuo na hata kwenye makanisa ya jirani.
Ingawaje Morris alipanga kurudi Liberia, Mungu alikuwa na mpango mwingine juu yake. Katika kipindi cha miaka miwili cha kuwepo katika chuo kikuu cha Taylor, Samuel Morris alikufa kwa ugonjwa wa nimonia. Alikuwa na umri wa miaka ishirini tu, lakini alikuwa na amani kwa kuwa kwenye mpango wa Mungu. Samweli alikuwa amemwambia raisi wa chuo, “Siyo kazi yangu. Ni kazi ya Bwana. Nimeimaliza kazi yangu. Mungu atawatuma watu wengine wazuri kuliko mimi kuifanya kazi hii katika Afrika.”
Maisha ya Morris yalikuwa yamegusa watu wengi sana kiasi kwamba wakati wa mazishi yake mamia ya watu walipangana barabani kwa ajili ya kuhudhuria mazishi yake. Baadhi ya wanafunzi wenzake walikwenda Afrika kama wamishenari, wakitumika kwa “kumkumbuka mtoto wa mfalme Kaboo” Raisi wa chuo kikuu cha Taylor akasema, “Samweli Morris alikuwa mjumbe wa Mungu kwenye chuo kikuu cha Taylor. Alifikiria kwamba alikuja hapa ili kujiandaa mwenyewe kwa ajili ya huduma ya umisheni, lakini badala yake Mungu alikuwa amemtuma kuja kukiandaa chuo kikuu cha Taylor kwa ajili ya umisheni wa dunia nzima. Wote aliokutana nao walivutiwa na utakatifu wake, lakini pia na urahisi wa imani yake kwa Mungu.”
Kwa sasa, mnara wa kumbukumbu kwenye kaburi la Samweli Morris lililoko Fort Wayne, Indiana linasomeka kama ifuatavyo:
Samweli Morris; 1873-1893
Mtoto wa Mfalme Kaboo
Raia wa Afrika Magharibi
Mchaji maarufu wa Ukristo
Mtume wa Imani rahisi
Mwakilishi wa Maisha yaliyojazwa Roho.
Maisha mafupi ya Samweli Morris yanadhihirisha kwamba kila mwamini anaweza kuishi katika uwezo wa nguvu ya Roho Mtakatifu. Moyo wa utakatifu na maisha ya utakatifu ndio kusudi la Mungu kwa kila mwamini.
[1] Image: "Samuel Morris", Samuel Morris: A Spirit Filled Life (1921), retrieved from https://commons.wikimedia.org/wiki/File:JORDAN-READ-MERITT(1921)_Samuel_Morris._A_Spirit_Filled_Life.jpg, public domain.
Tafakuri ya Somo la 1
(1) Uzuri wa utakatifu unaonekana katika uumbaji wa Mungu wa asili. Mungu aliuumba ulimwengu ukiwa mkamilifu na bila dhambi.
(2) Uzuri wa utakatifu unaonekana unaonekana katika asili ya Mungu. Mungu ni Mungu Mtakatifu.
(3) Uzuri wa utakatifu unaonekana kwenye mpango wa Mungu kwa wanadamu. Ingawaje dhambi ilivuruga asili ya mwanadamu, Mungu hakuachana na mpango wake wa watu watakatifu. Kurejesha uhusiano kati ya Mungu mtakatifu na mwanadamu aliyeanguka dhambini, Mungu alifundisha:
Mungu mtakatifu yukoje
Mtu mtakatifu yukoje.
(4) Kuna dhana nyingi potofu kuhusiana na utakatifu. Hizi ni pamoja na:
Ni watu wachache tu wanaweza kuwa watakatifu.
Tunakuwa watakatifu kwa kujitenga na watu wengine.
Tunakuwa watakuwa tukishakufa.
Tunakuwa watakatifu kwa kufuata sheria maalumu.
Ushahidi kwamba mtu ni mtakatifu unaonekana katika vipawa maalumu vya kunena kwa lugha na matendo ya miujiza.
Utakatifu hauwezekani.
(5) Ukweli kuhusu Utakatifu ni rahisi. Ifuatayo ni maana halisi ya kuwa mtakatifu:
Kuwa mtakatifu ni kudumisha uhusiano wa karibu na Mungu.
Kuwa mtakatifu ni kuakisi mfano na sura ya Mungu.
Kuwa mtakatifu ni kutengwa kwa ajili ya Mungu.
Kuwa mtakatifu ni kuwa na moyo usiogawanyika.
Kuwa mtakatifu ni kuishi maisha ya haki.
Kuwa mtakatifu ni kuwa na upendo kamili kwa Mngu na jirani zetu.
Kuwa mtakatifu ni kuishi katika ukamilifu wa Roho Mtakatifu.
Kuwa mtakatifu ni kumfanania Kristo.
Utakatifu hutuandaa sisi kumwona Mungu.
(6) Maandiko matatu katika Agano Jipya yanatuonyesha umuhimu wa utakatifu katika maisha ya mwamini:
Warumi 8:29 inarejea wakati uliopita na inaonyesha kusudi la Mungu la umilele kwa watoto wake.
2 Wakorintho 3:18 inarejea wakati uliopo na kuonyesha jinsi kusudi hili linavyotimia leo katika maisha ya muumini.
1 John 3:2 inarejea katika wakati ujao na kuonyesha ukamilikaji wa mwisho wa kusudi la Mungu.
Kazi ya Kufanya
(1) Hebu fikiria Mkristo mpya anakuambia, “Nilisoma katika Biblia kwamba Mungu ametuita tuwe watakatifu kama yeye alivyo mtakatifu. Hilo haliwezekani! Inamaanisha nini kuwa mtakatifu?” Andika ukurasa mmoja wa majibu kwa ajili ya huyu mwamini mpya. Kwenye kikao kinachofuata cha darasa, kila mwanafunzi asome majibu yake. Jipeni muda wa kujadili haya majibu kama darasa.
(2) Anza kikao kinachofuata cha darasa kwa kunukuu 1 Petro 1:14-16.
(3) Kozi hii imeambatanishwa na Mradi wa Mwisho ambao utatakiwa urejeshwe siku ya mwisho ya darasa. Unatakiwa uanze kuufanyia kazi sasa. Fungua Mpangokazi wa Mwishowa kozi hii kwa maelezo zaidi na ya kina kuhusiana na mradi huo.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.