Barua kwa Warumi inalezea jinsi mtu anavyoingia katika uhusiano na Mungu ili kupokea wokovu na baraka. Uhusiano na Mungu umejikita katika neema inayopokelewa kwa Imani. Kifugu hiki kinasababisha maswali yanayohusu Israeli. Kunatokea nini katika uhusiano maalumu kati ya Mungu na Israeli? Je, Myahudi nawezaje kuokoka? Je, Mungu bado ana mpango kwa Waisraeli? Sura hizi zinajibu maswali hayo Paulo anapoendelea kuelezea ujumbe wa injili.
"Ee binadamu; wewe u nani umjibuye Mungu?" (Warumi 9:20). Baadhi ya watu wameitumia aya hii katika kukemea mtu yeyote ambaye anajaribu kuihoji au kuipima haki ya Mungu. Wanasema kwamba haki ya Mungu iko juu sana kuliko haki yetu kiasi kwamba hatuwezi kabisa kuifahamu.
[1]Je, kuna aina ya kiwango kingine cha juu cha haki ambacho nyeusi inakuwa nyeupe na uovu unakuwa mzuri? Ikiwa hakimu wa kibinadamu angehukumu watoto wachanga, makosa yaliyohukumiwa na atakuwa dhalimu. Ikiwa angehukumu makosa na uhalifu wa makusudi sawa, atakuwa dhalimu. Lau angewaadhibu watu kwa kufanya yale wasiyoweza kuyazuia, tusingesema kuwa anahukumu kwa kiwango cha juu cha uadilifu, bali alikuwa dhalimu.
Haki ya Mungu ni ya kiwango cha juu lakini haitofautiani na haki yetu. Ufahamu wetu kuhusiana na haki unatoka kwake na uko kwenye misingi ya viwango vyake. Anatuamrisha sisi tuwe watakatifu kwa maana ile ile iliyo sawa kwamba na yeye ni mtakatifu. Kama kwa wakati mwingine hatua zake zinaonekana kutokuwa za haki kwetu ni kwa sababu hatutazami ukweli wote uliopo, kwa sababu maadili yetu ni ya muda sana, na kwa sababu mitazamo yetu imepotoshwa na matamanio yetu wenyewe.
Mungu hajinadi tu kuwa mwenye haki na kukataa kuelezea njia zake kwa viumbe wake. Badala yake, Kitabu cha Warumi kinaweka msisitizo kwamba haki ya Mungu ni kitu kinachoonekana. Wale wanaomkataa Mungu “hawatakuwa na udhuru” (1:20) kwa sababu ya kile wanachokijua kuhusiana na Mungu. Wenye dhambi wanajua kwamba wanastahili hukumu (1:32). Warumi 2 inaeleza wazi kabisa kuhusu kutopendelea na hukumu za Mungu hazibadiliki badiliki. Kazi ya upatanisho iko hivyo kwamba Mungu hana upendeleo ingawaje huwahesabia haki wenye dhambi. (3:26).
Ni jambo lililo wazi kwamba Mungu anataka tumwone yeye kuwa ni mwenye haki. Kwa sababu hiyo, Mungu ameelezea sera zake za wokovu, akielezea ni kwa nini ni za haki. Itakuwa ni jambo lisilowezekana kwetu sisi kumwabudu Mungu katika kweli kama hatutamwona yeye kuwa ni mwenye haki. Kama hatutaweza kumwamini Mungu kwamba ni mwenye haki, utiifu wetu kwake utakuwa ni sawa na utiifu kwa jitu katili au jambazi.
Kwa hiyo, Mungu mwenyewe huruhusu awekwe katika mashitaka, au hata anajiweka mwenyewe kwenye hali hiyo. (3:4). Mungu ana uhakika kwamba matendo yake yanaendana na haki ya kweli. Jaribio la uaminifu la matendo ya Mungu litaonesha kuwa Mungu ni mwenye haki na kuwa mwenye dhambi ni mwenye hatia.
► Je, kwa nini ni muhimu kwetu sisi kuelewa matendo ya haki ya Mungu? Je, tunajuaje kwamba Mungu anatutaka sisi tuelewe kuhusu haki yake?
Mtazamo wa Biblia kuhusiana na ukuu wa Mungu:
Mungu amechagua kuruhusu watu kufanya chaguzi za kweli pamoja na matokeo yake.
Mungu huwaacha watu wakae na chaguzi zao walizozifanya (Warumi 1:24, 26, 28).
Mungu ni mwenye nguvu na hekima ya kutosha katika kukamilisha mpango wake wa mwisho licha ya yale ambayo mtu mwingine yeyote anayafanya.
Kila mtu anaamua aidha kutokuikubali au kuikubali injili na akaokoka au akakataa kuokoka katika msingi huo. Mungu hutoa wokovu, huwapa watu kutambua kuhusu wao kuwa na hatia, huwapa watu matamanio ya neema, na huwapa uweza wa kuamini. Huwatuma wajumbe wake kuwashawishi wasioamini watubu. Lakini mtu binafsi anafanya maamuzi yake mwenyewe kuhusiana na wokovu wake.
"Ili Mungu awe wa milele, ni lazima awe na uwezo wa kusimamia mashitaka yote yatakayohusu mashetani yote, malaika wote, na wanadamu wote. Hakuna yeyote atakayekuwa na uwezo wa lazima wa [haki ya] kumlaumu kwamba hatendi haki.”
- R.G. Flexon, Rudiments of Romans
Kifungu cha kujifunza – Warumi Sehemu 5, kifungu cha 1
Jambo Kuu katika Warumi 9
Mungu amechagua njia ya wokovu, na hakuna njia nyingine yeyote ambayo mtu anaweza akaitumia katika kupata wokovu.
Muhtasari wa Warumi Sura ya 9
Mara nyingi sura hii hufasiriwa kumaanisha kwamba Mungu huwa anachagua ni nani wa kuokoka na ni nani wa kupotea kwa msingi ambao hatuwezi kuujua. Kwa kweli, jambo halisi ni kwamba Mungu amechagua njia ya wokovu, na kwamba hakuna mtu yeyote anayeweza kuokoka kwa njia nyingine yeyote. Ukuu wake Mungu hauonyeshwi kwa kuchagua baadhi ya watu na kukataa wengine bila vigezo vyovyote. Ukuu wake unaonyeshwa kwa uwekaji wake wa vigezo – muundo wa njia ya wokovu.
► Mwanafunzi atapaswa kusoma Warumi 9:1-5 kwa ajili ya kikundi.
Maelezo ya Aya-kwa-Aya
(9:1-3) Paulo alionesha huzuni kubwa kwa ajili ya Israeli kwa sababu kiroho walikuwa wamepotea. Alitaja kwamba alikuwa ndugu yao. Paulo alikuwa ametokana na dini ya Kiyahudi. Aliwaheshimu wanazuoni wake. Alihuzunishwa kwa kutambua kwamba wengi wa waalimu na viongozi na wengi wa watu waliowatumikia walikuwa wamemkataa Kristo.
(9:4-5) Israeli lilikuwa taifa lililokuwa na faida nyingi za kiroho.
Kwanza walikuwa na Mungu kama Baba.
Kwanza walikuwa wameuona utukufu wa Mungu ukifunuliwa.
Walikuwa na
Maagano kama masharti ya baraka zake.
Sheria.
Aina za kuabudu.
Ahadi za wokovu mkuu.
Mababa wa ahadi walikuwa Wayahudi.
Yesu alizaliwa kama Myahudi.
Mwanzoni Paulo alisema katika 3:1-2 kwamba Wayahudi walikuwa na faida nyingi sana.
Uyahudi, Chimbuko la Ukristo
Uyahudi unaweza kusemwa kwamba ndio chimbuko la Ukristo. Hata sasa Uyahudi una mambo yanayofanana zaidi na Ukristo kuliko dini nyingine yeyote. Uyahudi haukuwa kwenye kundi la dini za uongo hadi ilipokuja kumkataa Kristo.
Orodha inayooneshwa hapa chini ni mahusiano yaliyopo kati ya Ukristo na Uyahudi:
1. Wakristo na wafuasi wa Uyahudi wote kwa pamoja wanamwabudu Mungu mmoja wa kufanana na wamepokea ufunuo kutoka kwa Mungu
2. Uyahudi ndio uliotoa msingi wa teolojia na falsafa ya Ukristo. Waisraeli walikuwa wanaamini Mungu mmoja aliye wa milele, asiyekuwa na asili na aliye mtakatifu. Mungu aliumba kila kitu kikiwa kizuri, lakini uovu na mateso vikawepo kwa sababu ya dhambi. Mwanadamu ni kiumbe maalumu kilichoumbwa katika sura au mfano wa Mungu, akiwa na hatima yenye utukufu baada ya kuwa amekombolewa. Tunachukulia hizi kweli zote, lakini zinatofautiana na dini nyingine zote zilizoizunguka Israeli ya kale. Kweli hizi zote mwanzoni zilikuwa zimefunuliwa kwa Waisraeli.
3. Wakristo na wafuasi wa Uyahudi wanakubaliana na Agano la Kale kama ndiyo Maandiko, lakini wafuasi wa Uyahudi hawakubaliani na Agano Jipya.
4. Yesu, mwanzilishi wa Ukristo, alikuwa ni Myahudi na aliithibitisha dini ya watu wake. Alielezea vipaumbele vyake vya kweli na akalaumu uharibifu uliokuwa ukifanywa na Mafarisayo. Hakudai kutaka kuanzisha dini mpya bali kuikamilisha ile ya zamani.
5. Moyo wa Uyahudi ulikuwa unamtarajia Masihi. Wakristo wa kwanza walikuwa ni Wayahudi ambao waliamini kwamba Yesu alikuwa ndiye Masihi wa Wayahudi.
Kifungu cha kujifunza – Warumi Sehemu 5, kifungu cha 1
► Mwanafunzi atapaswa kusoma Warumi 9:6-16 kwa ajili ya kikundi.
Mwendelezo wa maelezo ya Aya-kwa-Aya
(9:6-9) Baadhi yao walikuwa wameokoka; Neno la Mungu lilikuwa limeleta mabadiliko kwao. Watu wa Mungu sio tu wale ambao ni wazao wa kibiolojia wa Ibrahimu. Ni wale watu waliookoka kwa kuziamini ahadi za Mungu.
Tangu wakati ambao Mungu alimchagua Ibrahimu, wokovu ulikuwa umepangwa uwe wa njia hii. Mpango wa Mungu wa wokovu, ambao ulikuwa uendelee hadi kwa Isaka, ilikuwa ni kazi ya Mungu iliyokuwa inategemea mwitikio wa imani. Mfumo wa Mungu wa wokovu ni ahadi, kisha imani, kisha muujiza. Kuzaliwa kwa Isaka kulikuwa ni muujiza.
Ismaili alizaliwa katika hali ya kawaida ya asili, na siyo kimuujiza, na Mungu hakumtumia kwenye mpango wa ukombozi. Kwa kanuni hiyo hiyo, Mungu hakubaliani na wokovu kwa njia ya matendo. Wayahudi waliokuwa wanataka wokovu kwa matendo yao walikataliwa na Mungu kama na vile Ismaili alivyokataliwa kuwa mtoto wa ahadi.
► Je, vipi kuhusu suala la Yakobo na Esau? Baadhi ya watu wanafikiri kwamba aya hizi zinasema kwamba kabla hawajazaliwa, Mungu alishamchagua ni nani atakayetumika. Aya hizi kimsingi zinasema nini?
(9:10-13) Wakati Mungu alipomchagua Yakobo badala ya Esau, hakuwa akichagua mtu yupi wa kuokoa. Alihitaji kuchagua yule ambaye ataweza kumtumia katika kutimiza mpango wa wokovu. Hii ndiyo mada ya sura hii: Haki ya Mungu ya kuchagua njia ya wokovu. Kumbukumbu za maisha ya Esau katika Agano la Kale zinaonyesha kwamba kwa ukweli alikuwa na badiliko la moyo wake na ingewezekana akaokoka. Alikuwa hajakataliwa kwenye wokovu, bali alikataliwa kuwa baba wa taifa teule na Masihi. Neno nimemchukia linamaanisha tu kwamba “kukataliwa kwa ajili ya mtu mwingine,” kama ilivyomaanisha wakati Yesu aliposema kwamba ni lazima kumchukia baba au mama katika kuweka ulinganifu wa utii wetu kwake (Luka 14:26).
Mungu hakumchagua Yakobo kwa sababu ya sifa zake au hakumkataa Esau kwa ajili ya makosa yake. Kifungu hiki kinaweka msisitizo kwamba walikuwa hawajafanya jambo lolote jema au baya wakati Mungu alipofanya chaguo lake. Bila shaka, Mungu alikuwa anajua hatima zao. Jambo la msingi hapa ni kwamba Mungu alichagua kutokana na mpango wake mwenyewe.
► Baadhi ya watu wanasema kwamba 9:14-16 inathibitisha kwamba Mungu huchagua ni nani wa kuokolewa kwa sababu ambazo sisi hatuzijui. Wanasema kwamba matendo yetu na mambo tunayochagua haviwezi kuamua kama tunaweza au hatutaweza kuokoka. Aya hizi kwa uhakika zinasema nini?
(9:14-16) Mungu huchagua ni nani atakayemwonyesha rehema. Hiyo haimaanishi kwamba anafanya bila ya kuwa na msingi au kwenye msingi ambao hatutaweza kuujua. Mungu ameonyesha msingi wa rehema zake: “Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa” (Isaya 55:7).
Anatueleza kwa uwazi kwamba tumechaguliwa kwa ajili ya wokovu kama tutaamini na tutakataliwa kama hatutaamini. Kwa hiyo, siyo kutokana na mapenzi ya mtu atake kujiamulia ni kwa jinsi gani anavyotaka aokoke. Wokovu ni lazima utokane na rehema za Mungu, na upokelewe kama alivyoagiza.
► Mwanafunzi atapaswa kusoma Warumi 9:17-23 kwa ajili ya kikundi. Je, Mungu alimwumba Farao ili awe mtu mwovu na amthibiti ili kwamba aweze kutenda mambo ya uovu?
(9:17-18) Farao hakuzaliwa kwa ajili ya kuhukumiwa, lakini Mungu alimweka kwenye nafasi ya mamlaka kwa sababu Mungu alijua ni kitu gani anakwenda kukifanya. Neno nilikusimamisha halirejelei kwenye uumbaji wake bali kwenye kumsimika mtawala. Mungu ni mwenye rehema kwa wale wanaoamini na huifanya mioyo ya watu wasioamini kuwa migumu. Kufanya moyo kuwa mgumu haina maana kwamba Mungu anambadilisha mtu mzuri kuwa mtu mbaya. Mungu alimpa Farao jukumu la kutekeleza kile ambacho tayari alishakusudia kukifanya.
Wale watu ambao wanafanywa kuwa na mioyo migumu wanafikiriwa kama wenye hatia kwa ajili ya hali zao. Kwa hiyo, kwa mujibu wa haki, kuchagua kwao ni halisi. Mwanzoni, katika Warumi 2:4-5, Wamataifa wanahukumiwa kwa ugumu wa mioyo yao ambako kumeunganishwa na kuukataa ukweli kwa mapenzi yao wenyewe. (Ona pia Yeremia 19:15, Nehemia 9:25-29, Marko 16:14, na Waebrania 3:7-13). Farao hangekuja kuwa na moyo mgumu kama siyo kule kumkataa Mungu kuanzia mwanzo.
(9:19) Hapa mtu anainua upinzani: “Kama Mungu anadhibiti watu, kama alivyofanya kwa Farao, mtu kama huyu atahukumiwaje? Hakuna mtu yeyote ambaye amepingana na mapenzi yake kwa mafanikio.” Mwenye kuinua upinzani anazungumza kana kwamba mtu anapaswa asamehewe kwa kumpinga Mungu kama hatimaye alilazimika kufanya kile ambacho Mungu alikuwa ametaka kifanyike. Lakini Mungu ni mwenye uwezo wa kutofautisha kati ya wale wanaokubaliana naye kwa hiari yao wenyewe na wale ambao hawako hivyo.[1]
(9:20-23) Mungu ni mwenye uwezo wa kuchagua baadhi ya watu kwa ajili ya hukumu na wengine kwa ajili ya rehema, ingawaje mwisho wa siku atatukuzwa na watu wote (kwa sababu yeye anatukuzwa kwa pamoja kwa ajili ya hukumu yake na rehema zake). Ana msingi wa uchaguzi wake na ana haki ya kuchagua. Mungu huweka vigezo vyake kwa ajili ya kukubalika, na havibadiliki.
Mfinyanzi anaweza akaamua afanye nini na udongo. Anaweza akatumia sehemu ya udongo kutengeneza jagi la kuwekea maua na sehemu nyingine ya udongo huo akaamua atengeneze gudulia la kuwekea takataka. Ni kwa njia hiyo hiyo, Mungu huamua kwamba baadhi ya watu wanafaa tu kwa ajili ya hukumu na watu wengine wanastahili rehema. Kitenzi cha Kiyunani hakioneshi ni nani anayefanya tendo. Inaweza kumaanisha kuwa watu wenyewe wanajitayarishia hukumu. Hiyo itakuwa sawa na taarifa kwamba Mungu huvumilia maasi yao hadi wakati ambapo hukumu itakuja. Mungu hakuwaumba kwa ajili ya hukumu au kwa ajili ya kuwafanya wawe watenda dhambi. Hukumu zao zitatokana na jinsi walivyojichagulia wao wenyewe. Ukweli kwamba Mungu ni mwenye mamlaka katika kuchagua kwake haimaanishi kwamba anachagua kwa upendeleo lakini anachagua kwa viwango vyake yeye mwenyewe. Anachagua watu waovu kwa ajili ya hukumu na watu walioamini kwa ajili ya wokovu.
Swali kwamba “Kwa nini Mungu amenifanya niwe hivi?” haimaanishi kwamba “kwa nini umeniumba mimi kwa ajili ya kuhukumu,” bali “Kwa nini uliamua kwamba nilikuwa nafaa kwa ajili ya hukumu?” Lakini Mungu anayo haki ya kuamua na kudhihirisha haki yake.
Mfano wa mfinyanzi unapatikana kutoka Yeremia 18:1-18. Aya muhimu ni 18:7-10. 18:8 inasema, “Ikiwa taifa lile nililolitaja litageuka, na kuacha maovu yake nitaghairi, nisitende mabaya yale niliyoazimia kuwatenda.”
► Je, ni kwa jinsi gani unaweza kuelezea mfano wa mfinyanzi na udongo? Je, Mungu aliwaumba watu wengine kwa kusudi la kuwatumia kuonesha ghadhabu yake? Je, Inamaanisha nini kusema kwamba anatengeneza vitu mbalimbali kutoka katika udongo?
[1]Ona maelezo ya kumbukumbu juu ya kifungu kinachofanana katika Warumi 3:5-8.
Hitimisho Binafsi la Mtume
Baadhi ya watu wamehitimisha kutoka katika sura hii kwamba Mungu huumba watu wengine kwa kusudi la kuhukumiwa na wengine kwa ajili ya kupata rehema. Hata hivyo, Paulo mwenyewe anaelezea kwamba hitimisho lake kuu liko katika sura hii (9:30-33). Ni muhimu kwamba tumwachie mwandishi na jambo kuu alilo nalo kutokana na mfano wake alioutoa mwenyewe. Hatupaswi kubishania matumizi ya maelezo ya mwandishi ambayo yako kinyume na yale ambayo mwenyewe ameyaelezea. Hoja kuu ya Paulo ni hili: Mungu atamhukumu mtu binafsi katika msingi kwamba aidha ameamini au hajaamini. Kama mfinyanzi, ana haki ya kuamua msingi wa kukubalika.
Tunaweza tukafurahia katika ukuu wa Mungu kwa sababu kila siku ni mwenye hekima, ni mzuri, ni mwenye upendo na haki katika kila analolitenda. Ingawaje anayo mamlaka yote kabisa, hafanyi jambo lolote lisilokuwa la haki. Matendo yake siku zote ni sawa na asili yake mwenyewe.
Jambo lililopo kwenye sura hii siyo kwamba Mungu huchagua kila mtu binafsi anayemtaka bila ya kuzingatia vigezo. Jambo kuu katika Warumi 9 ni kwamba Mungu anaweka vigezo vyake ambavyo huamua ni nani amchague kwa ajili ya kuokoka. Kigezo muhimu ni imani inayookoa.
Kifungu cha kujifunza – Warumi Sehemu 5, kifungu cha 1
► Mwanafunzi atapaswa kusoma Warumi 9:24-33 kwa ajili ya kikundi.
Mwendelezo wa maelezo ya Aya–kwa-Aya
(9:24-26) Wamataifa wengi hufanyika kuwa sehemu ya watu wa Mungu, ingawaje walikuwa hawaitwi ni watu wa Mungu kwenye misingi ya utaifa wao. Hali hii inaunganisha mada kuu ya umishenari ya Waraka huu: Injili inaweza kupelekwa kwa mtu yeyote katika ulimwengu huu.
(9:27-29) Wayahudi wengi watakataliwa, na masalia peke yao ndio watakaookolewa. Wayahudi hawataokolewa moja kwa moja kisa tu kwa sababu wao ni Wayahudi. Kama Mungu atakuwa ametenda kwa mujibu wa haki bila ya kuweka hapo rehema yake, wangeangamizwa kabisa kama ilivyokuwa kwa Sodoma.
(9:30-33) Hapa ndio hitimisho la hii sura. Mwandishi anapaswa apewe nafasi ya kutoa hitimisho lake mwenyewe. Mada ya sura hii ni kwamba Mungu ameweka mpango wake wa wokovu. Watu wengine wote waliojaribu kuanzisha njia zao nyingine za haki kwa msingi wa sheria walishindwa. Wale wote wanaotafuta haki kwa njia imani wanafanikiwa. Mtu anayejaribu kuanzisha haki yake wenyewe hujikwaa juu ya jiwe kuu la pembeni ambalo Mungu ameliweka, lakini atakayeamini hatatayarika au hataaibika.
Maswali ya Mapitio Somo la 9
(1) Je, tunajuaje kuwa Mungu anataka tuelewe anavyotenda haki?
(2) Je, ni kwa nini ni muhimu kwetu kuona kwamba Mungu ni wa haki?
(3) Je, mtazamo wa kibiblia kuhusu ukuu wa Mungu ni upi?
(4) Je, jambo kuu katika Warumi 9 ni nini?
(5) Je, manufaa ya kiroho ya Israel ni nini?
(6) Je, kuna mahusiano gani matano kati ya Ukristo na Uyuda?
(7) Je, Warumi 9 inasemaje kuhusu Mungu kumchagua Yakobo?
(8) Je, kwa nini tunafurahia ukuu wa Mungu?
Kazi ya kufanya Somo la 9
(1) Andika ukurasa mmoja ukielezea ni kwa jinsi gani Mungu ni mkuu mno na bado anaitikia uchaguzi wanaofanya wanadamu. Tumia Warumi 9, lakini pia waweza kutumia maandiko mengine.
(2) Unapaswa kuandaa angalau mazungumzo mawili kati yako na waamini wengine kutoka makanisa mengine. Unapaswa uwaulize wafafanue wanafikiri nini kuhusiana na ukuu wa Mungu. Unapaswa uwaelezee kifungu kutoka katika Warumi ambacho kinaendana na mada husika. Unapaswa uandike maelezo ya mazungumzo yenu na kisha yakabidhiwe kwa kiongozi wa darasa.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.