► Je, imani inayookoa ni nini? Kama mtu atakuwa anayo imani inayookoa, hiyo inamaanisha kwamba ameamini nini?
Je, mtu aliyeamini anaamini nini?
(1) Anaamini kwamba hawezi kufanya lolote katika kujihesabia haki mwenyewe.
"Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu" (Waefeso 2:8-9).
Anatambua kwamba hawezi kufanya lolote (matendo) litakalomfanya astahili kuokoka, hata kwa sehemu kidogo tu.
(2) Anaamini kwamba dhabihu ya Kristo inatosha kwa ajili ya msamaha wake.
" Naye ndiye kipatanisho kwa ajili ya dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote" (1 Yohane 2:2).
Kipatanisho inamaanisha ni dhabihu inayofanya msamaha wetu uwezekane.
(3) Anaamini kwamba Mungu atamsamehe yeye kwa sharti la imani peke yake.
"Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote" (1 Yohane 1:9).
Kama anafikiria kwamba kuna masharti mengine, anategemea kuokoka kwa matendo badala ya kuokoka kabisa kwa neema.
Sehemu ya 3 ina vifungu vitatu. Kifungu cha kwanza (3:21-31) kinaonesha kwamba mwanadamu ni lazima athibitishwe kuwa mwenye haki kwa njia ambayo Mungu hupanga mwenyewe, kwa kuwa mwanadamu hawezi kujihesabia haki mwenyewe katika lolote alilolitenda. Kifungu cha pili (Warumi 4) inamtumia Ibrahimu na Daudi kama vielelezo vya kuthibitisha imani, ikionyesha kwamba fundisho la imani siyo kitu kigeni. Kifungu cha tatu (Warumi 5) kinaelezea jinsi dhabihu ya Kristo inavyoweza kufanya aina hii ya kufanywa mwenye haki iwe kitu kinachowezekana. Katika somo ili tutajifunza aina zote tatu za vifungu hivi.
Jambo Kuu katika sura ya 3:21 - 5:21
Alichokitoa Mungu kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu ni dhabihu ya Kristo, ambayo inaleta kuhesabiwa haki kwa neema kwa njia ya imani.
Kifungu cha kujifunza – Warumi Sehemu ya 3, kifungu cha 1
Jambo Kuu katika sura ya 3:21-31
Njia ambayo Mungu ya kumhesabia mtu haki ni kwa neema kwa njia ya imani, na kuhesabiwa haki kwa njia ya matendo haiwezekani.
Muhtasari wa kifungu cha sura ya 3:21-31
Kwa kuwa hakuna mtu yeyote mwenye haki kwa msingi wa kuhifadhi sheria zote kwa wakati wote, njia nyingine ya kuhesabiwa mwenye haki ni lazima itafutwe. Tatizo (lililotolewa katika 3:26) nikwa ajili ya Mungu kumhesabia haki mwenye dhambi na bado akaendelea kuwa jaji mwenye haki. Tatizo hili linatatuliwa kwa upatanisho; Mungu alitoa dhabihu kama msingi wa msamaha. Anaweza kumsamehe mtu aaminiye, lakini dhabihu huonesha kuwa Mungu huzichukulia dhambi kwa uzito wa hali ya juu sana.
► Mwanafunzi anapaswa asome Warumi 3:21-31 kwa ajili ya kikundi.
Maelezo ya Aya-kwa-Aya
(3:21) Haki inayokubalika kwa Mungu inakamilika mbali na sheria. Mtume anasema kwamba wazo hili siyo jambo geni, lakini lilifundishwa katika sheria hata na mitume. “Lakini sasa” linarejelea kwenye wakati wa ufunuo kamili wa injili katika Kristo, kama aya inayofuata inavyosema. (Ona pia 3:25).
(3:22-23) Hakuna njia tofauti ya kuokolewa kati ya Wayahudi na Wamataifa kwa sababu wote wanahukumiwa sawa. Hata katika Israeli ya kale, wakati walipofuata mila ambayo Mungu aliwapa, hakuna hata wakati mmoja ambao mtu aliokolewa kwa njia ya dhabihu au mila. Mtu yeyote aliyeokolewa, aliokoka kwa kupokea neema kwa njia ya imani. (Ona aya ya 30.)
Wokovu kwa kila mtu ni kwa njia ya imani. Neno wote linatumika mara nyingi hapa. Kama ambavyo wote wametenda dhambi, wote walioamini wanaweza wakaokolewa. Kifungu kinachosema “kwa wote waaminio” msisitizo jinsi unavyopatikana kwa kila mtu. Na "toka imani hadi imani" kinaweka msisitizo wa hali ya imani (1:17).
(3:24) Neema ni ya bure kwa ajili yetu kwa sababu Yesu alilipa gharama ya ukombozi.
(3:25) dhambi zote zilizotangulia kufanywa ni dhambi ambazo zilishawahi kufanywa kabla ya ujio wa Kristo. Hawakulipia makosa kwa ajili ya maadhimisho ya sherehe, bali kwa kifo cha Kristo, ingawaje wakati dhambi zilipokuwa zinatendwa, kifo chake kilikuwa ni cha wakati ujao wa baadaye. Mungu aliwasamehe kwa msingi wa upatanisho wa Kristo kabla haijatokea, kwa sababu ilikuwa imepangwa hivyo tangu mwanzo (ona 3:21).
Upatanisho unaonesha kwamba Mungu alikuwa mwenye haki ingawaje haki yake ilikuwa siyo ya mara moja. Ilionyesha kwamba Mungu huichukulia dhambi kwa uzito wa hali ya juu sana.
(3:26) Aya inaonyesha ufumbuzi wa tatizo kubwa: Ni kwa jinsi gani Mungu anaweza kuwa mwenye haki halafu bado anamhesabia haki mwenye dhambi? Upatanisho ulionesha njia. Mungu alitoa dhabihu kama msingi wa msamaha. Anaweza kumsamehe mtu anayeamini na dhabihu inaonesha kwamba Mungu huzichukulia dhambi kwa uzito wa hali ya juu sana.
► Je, kutakuwepo na tatizo gani endapo Mungu atawasamehe watu bila ya upatanisho?
Mungu ni hakimu wa haki wa ulimwengu huu. Alishatangaza kwamba dhambi ina uzito mkubwa sana kiasi ambacho imewekewa adhabu ya milele. Watu wanatenganishwa na Mungu kwa sababu ya dhambi. Mungu anawajibika na haki ya mwisho ya ulimwengu, thawabu kwa ajili ya wanaotenda mema na adhabu kwa ajili ya wale wote watendao maovu.
Msamaha bila ya kuwepo na msingi wa msamaha huo utaleta mgogoro wa utambulisho halisi wa Mungu. Itaweza kumshushia heshima yake kwa kumfanya aonekane hana msimamo katika kushughulikia dhambi. Ataonekana hana haki kama atawaadhibu baadhi ya watu na watu wengine akawasamehe. Hili siyo tatizo dogo, kwa sababu ulimwengu wote upo kwa ajili ya kumtukuza Mungu. Je, ni kwa jinsi gani watu wanaweza wakamtukuza Mungu kama hawatafikiria kwamba yeye ni mwenye haki?
Suluhu ya hili inabidi kuwepo na kitu ambacho kitaonyesha kwamba dhambi ni hali yenye kuchukuliwa uzito mkubwa sana, kuna sababu ya msamaha, na asili ya Mungu idhihirishwe; ili watu wapate kuendelea kumheshimu Mungu kama mtakatifu na mwenye haki.
Upatanisho ndio unaofaa katika hitaji hilo. Dhabihu iliyotolewa juu ya dhambi ya msalaba inaonesha kwamba dhambi ni hali yenye kuchukuliwa uzito mkubwa sana. Umuhimu wa kutubu unamfanya mwenye dhambi aweze kukiri dhambi zake. Kutolewa bure kwa wokovu kwa ajili ya watu wote kunafanya uchaguzi uwe wa mtu binafsi, ili iwe kwamba ni haki kwa Mungu kuweza kumsamehe mtu anayekubaliana na wokovu na asimsamehe yule anayeukataa wokovu.
Je, ni kwanini Mungu hawezi kuwasamehe wale watu wanaokataa kutubu? Kumsamehe mtu ambaye anaendelea kuwa kwenye dhambi bila kutubu ni kulikosea kusudi la upatanisho: ni kutoa msamaha wakati kuna haki ya Mungu inadai kutimizwa.
(3:27) Mtu hana sababu ya kujisifu kwa ajili ya kupata wokovu. Kumekuweko na baadhi ya watu wanaoamini kwamba mtu anaweza kujivunia kama akijijua kwamba ameokoka. Lakini mtu anayejijua kwamba amesamehewa kwa sababu ya neema anayo sababu ya kuwa na unyenyekevu na siyo kiburi.
(3:28) Kuhesabiwa haki hakutegemei haki iliyokwisha kuwepo nyakati zilizopita. Kuhesabiwa haki inamaanisha kwamba mwenye dhambi anayetubu na kuamini anahesabiwa kuwa mwenye haki kama ambaye hajawahi kufanya dhambi tena. Maisha ya utii kwa Mungu yanaanzia kwenye kuhesabiwa haki, na siyo kabla ya hapo. Mtu hawezi kuyabadillisha maisha yake mwenyewe kwa kusudi la kumfanya yeye binafsi akubalike kwa Mungu. Anakuwa tayari ameshakubalika kwa Mungu kupitia upatanisho wa Kristo, na siyo kwa njia nyingine yeyote.
(3:29-30) Aya hizi zinaunganisha kifungu kwenye mada ya kitabu. Ujumbe ni kwa ajili ya ulimwengu mzima. Matumizi haya ya injili ulimwenguni kote yana msingi wake kwenye imani kwamba kuna Mungu mmoja tu Kwa kuwa kuna Mungu mmoja tu, makusudi yake hufanya kazi kwa wanadamu wote, tofauti na mungu wa kienyeji ambaye huenda akapendezwa na taifa moja tu au ukoo mmoja tu Siku zote Mungu alikusudia kwamba Israeli ishirikishane ufahamu wa Mungu pamoja na Wamataifa (Isaya 42:6, Isaya 43:21, Isaya 49:6).
► Mtume alisema kwamba kuhesabiwa haki kwa njia ya imani hakuharibu sheria, bali kuidumisha. Je, jambo hili likoje?
[1](3:31) Wakati mtu anapotubu dhambi zake na kuanza kuishi maisha ya utii, anakuwa anaidumisha sheria ya kuwa ni kipimo cha haki. dhana yeyote ya upatanisho na kuhesabiwa haki ambayo itaifanya sheria ionekane kwamba haina maana kwa Mkristo haiendani na aya hii.[2] Kama mtu akiomba msamaha lakini hatarajii kuanza kumtii Mungu, inaonesha kwamba haelewi uovu wa dhambi na sababu halisi ya yeye kuhitaji msamaha. Anajitahidi kupata faida za wokovu kwa kujifanya tu kwamba anaheshimu sheria.
"Hakuna mtu anayeweka sheria kwa ukamilifu kama wale ambao wametubu na kugeuka kabisa kutoka katika matendo yao ya dhambi na kumtegemea Yesu ka ajili ya wokovu.”
- George McLaughlin, Maelezo ya Warumii
[2]Mahubiri ya John Wesley yanayohusiana na jinsi sheria inavyoanzishwa kwa imani yanaelezea dhana hizi vizuri zaidi. (Angalia sehemu ya nyumba ya somo hili kuhusu vitabu vingine vinavyopendekezwa kusoma.)
Kifungu cha kujifunza – Warumi Sehemu ya 3, kifungu cha 2
Jambo Kuu katika sura ya 4
Ibrahimu, aliyekuwa amechaguliwa na Mungu kuwa baba wa watu wa Mungu, alihesabiwa haki kwa njia ya imani.
Muhtasari wa sura ya 4
Fundisho la imani kuhusu kuhesabiwa haki kwa neema kwa njia ya imani linapatikana katika kitabu cha Agano la Kale. Ibrahimu, aliyekuwa amechaguliwa na Mungu kuwa baba wa watu wa Mungu, alihesabiwa haki kwa njia ya imani. Mfalme Daudi pia alielewa kuhusu kuhesabiwa haki kwa neema. Kutahiriwa hakukuwa njia ya kupata wokovu lakini baadaye ilifanyika kama ishara ya imani ambayo Ibrahimu tayari alikuwa nayo. Ibrahimu alikuja kuwa baba na mfano wa wale wote ambao baadaye waliokoka kwa njia ya imani.
► Mwanafunzi anapaswa asome Warumi 4 kwa ajili ya kikundi.
Maelezo ya Aya-kwa-Aya
(4:1) Ibrahimu alikuwa baba wa kimwili wa Wayahudi. Swali ni kwamba, je, “Alipokea nini hasa?” Swali hili litajibiwa ili kujibu maswali “Nani anaweza kuwa mrithi?” na “Ni kwa jinsi gani tunaweza kuwa warithi?”
(4:2) Dhana ya wokovu kwa njia ya matendo kwa kawaida husababisha kuwa na kiburi.
► Je, Ibrahimu alikuwa na imani ya aina gani ambayo ilihesabika kama imani inayookoa?
(4:3) Ibrahimu hakuwa anajua mpango mzima wa wokovu, kwa hiyo, hangeweza kuweka imani yake kwenye upatanisho wa Kristo. Hata hivyo, aliamini ahadi ya Mungu kama ambavyo ilikuwa imefunuliwa kwake. Sehemu ya ahadi ambayo imetajwa katika sura hii ni kwamba Ibrahimu atakuwa baba wa mataifa mengi (4:17-18), lakini sehemu nyingine ya ahadi iliyobakia ni kwamba watu wote wa ulimwengu huu watabarikiwa kupitia uzao wake (Mwanzo 12:2-3, Mwanzo 22:17-18). Ahadi hii ilirudiwa tena kwa Yakobo (Mwanzo 28:14). Kupitia uzao wake neema ya Mungu itatolewa kwa watu wote wa ulimwengu huu. Hii ilikuwa ni ahadi ya neema ya Mungu kwa Ibrahim. Iliyotolewa kwa watu wote.
Ibrahimu alihesabiwa haki kwa neema kwa kuwa aliiamini ahadi ya neema Mungu. Kuhesabiwa kwake haki kulikuwa ni sawasawa na inavyokuwa kwetu, ingawaje imani yetu ina maudhui ya zaidi.
(4:4) Kama mtu anafanya kazi ili apate wokovu wake, wokovu siyo zawadi. Badala yake yeye anadaiwa kwamba anajaribu kujifanyia malipo (ona Warumi 11:6).
(4:5) Mtu ambaye hafanyi kazi siyo mtu ambaye hajali kuhusu kumtii Mungu, lakini ni mtu ambaye hafanyi kazi ili kuokoka. Badala ya kutegemea matendo yake ili yampatie nafasi ya kuingia mbinguni, anaamini ahadi ya Mungu ya kumwokoa.
(4:6-8) Daudi pia alirejelea kwenye kuhesabiwa haki kwa imani wakati alipoelezea kukubaliwa na Mungu ambako kunategemea msamaha wa dhambi. Mungu hawezi kumhesabia mtu aliyeamini kuwa mwenye hatia kwa dhambi ya zamani iliyokwishapita. Mtume anaonyesha hapa kwamba fundisho la imani kuhusu kuhesabiwa haki kwa neema kwa njia ya imani sio wazo Jipya – hata mfalme Daudi alilielewa hilo.
Je, ni kwa jinsi gani tutajua kwamba jambo hili linahusika na dhambi ya zamani iliyopita na siyo dhambi inayoendelea? Kwenye Warumi 6:2 panasema kwamba sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi. Ujumbe wote wa Warumi 6 unakataa wazo la kwamba tunaweza tukaishi kwenye dhambi na wakati huo tukiendelea kuhesabiwa haki kwa njia ya imani. (Ona pia Warumi 5:6-8: “tulipokuwa hatuna nguvu” na “tulipokuwa tungali wenye dhambi,” ina maana kwamba sasa tuna nguvu na si wenye dhambi kama hapo awali, lakini tumehesabiwa wenye haki na kubadilishwa.)
(4:9) Swali hili linatambulisha mada kwamba ni kwa jinsi gani mtu anaweza kuingia kwenye nafasi hii ya kuhesabiwa mwenye haki kwa njia ya imani. Je, baraka hizi huja tu kwa watu ambao wametahiriwa?
► Je, ni kitu gani kilitangulia kwanza: sheria au neema?
(4:10-12) Ibrahimu hakuwa ametahiriwa wakati alipopokea neema. Kutahiriwa kulikuja baadaye. Kwa hiyo, inawezekana mtu ambaye hajawahi Kutahiriwa akapokea neema kwa njia ya imani. Ibrahimu ni baba wa imani kwa wale wote wanaofuata mfano wake. (wanaotembea katika hatua zake) za imani, hata kama hawajawahi kutahiriwa. Watu ambao wana imani inayookoa ni Watoto wa kiroho wa Ibrahimu. Waisraeli siyo watoto wake wa kiroho hadi wawe wameamini, ingawaje kibiolojia ni uzao uliotoka kwake.
(4:13-14) Je, ni nani mrithi wa baraka za Ibrahimu? Kama ni wale wanaoshika sheria, basi siyo imani iliyoko kwenye ahadi.
(4:15) Sheria ndiyo inayohalalisha hukumu kwa kuwa inaonyesha dhambi. Siyo sababu ya kupokea neema. Kama hakungekuwepo na sheria, pia hakungekuwepo na uvunjaji wa sheria. Paulo hazungumzii hasa kuhusu sheria ya Musa, bali mahitaji ya Mungu kuhusiana na mwanadamu kwa ujumla. Hakuna mahali ambapo mahitaji ya Mungu hayafahamiki kabisa. (1:20)
(4:16-17) Ibrahimu alikuwa na uzao mwingi wa kibiolojia waliofanyika kuwa mataifa mengi. Hata hivyo, mtume hapa anasema kwamba Ibrahimu alikuwa ni baba wa wengi kwa sababu ni baba wa wale wote walio na imani.
Wokovu unapokelewa kwa imani ili utolewe kwa neema. Kama matendo yeyote yalikuwa yanahitajika ili mtu aweze kuwa na sifa ya kupokea wokovu, haitakuwa tena ni kwa neema. Kwa kuwa ni kwa neema, ni lazima ipokelewe kwa imani peke yake. Mtu anayejaribu kuufanyia kazi wokovu kwa matendo yake haelewi maana ya wokovu.
► Je, ahadi ya Mungu kwa Ibrahimu ilikuwa nini? Ilikuwaje sawa na ahadi ya wokovu tunayopokea?
(4:18-19) Ibrahimu alimwamini Mungu hata wakati ambapo hapakuwepo na mazingira ya kumpa matumaini. Mwili wake ulikuwa sawa na umekufa ukizingatia uwezo wake wa kupata mtoto. Sara alikuwa pia ameshapitiliza muda ule wa mwili kuwa na uwezo wa kubeba mtoto. Lakini imani ya kweli haina utegemezi na aina za mazingira yaliyopo.
Imani hii ni kinyume na kutegemea matendo. Hii inaelezea ni kwa nini Ismaili, mwana wa Hagai, ni mfano wa wokovu kwa njia ya matendo (Wagalatia 4:22-31). Kuzaliwa kwa Ismaili kulifikiwa kwa njia ya kimwili, badala ya imani. Wokovu ni kwa ahadi, kisha imani, halafu miujiza.
(4:20-21) Mungu hutukuzwa zaidi na imani ya mwanadamu kuliko uwezo wa kibinadamu.
(4:22) Ona maelezo katika aya ya 3.
► Je, tunapokea wokovu ule ule ambao Ibrahimu alipokea?
(4:23-25) Imani ya Ibrahimu ni mfano wa kuigwa kwetu sisi. Hakuwa anajua mpango mzima wa wokovu lakini aliamini sehemu ya kile ambacho kilikuwa kimefunuliwa kwake. Ni lazima tuamini kwa undani yale yote yaliyofunuliwa katika mpango wa wokovu ambao Ibrahimu hakuwahi kujua: kifo na kufufuka kwa Yesu Kristo. Aya hizi zinaonyesha kwamba tunapokea kuhesabiwa haki kama vile Ibrahimu alivyopokea, kwa sababu inasema kwamba haki ilihusishwa na yeye na itahusishwa na sisi pia katika msingi huo huo unaofanana.
Kifungu cha kujifunza – Warumi Sehemu ya 3, kifungu cha 3
Jambo Kuu katika sura ya 5
Kristo katika kifo chake na kufufuka kwake alibatilisha matokeo ya dhambi akaleta upatanisho, haki, na uzima.
Muhtasari wa sura ya 5
Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo (5:1). Kifungu kinachosema “kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo” kinatoa utambulisho wa sura hii: ufanisi wa kazi ya upatanisho ya Kristo. Dhambi ya Adamu iliufanya ulimwengu ukawa chini ya dhambi na kifo, na kila mwanadamu baada yake ametenda dhambi. Upatanisho wa Kristo ulipindua madhara ya dhambi.
► Mwanafunzi atapaswa kusoma Warumi 5 kwa ajili ya kikundi.
Maelezo ya Aya-kwa-Aya
[1](5:1-2a) Aya hii inaunganisha sehemu iliyopita pamoja na sehemu hii ya sasa. Somo la sura hii ni ufanisi wa kazi ya upatanisho ya Kristo. Amani inayorejewa inahusika na upatanisho pamoja na Mungu - uadui ukiondolewa na ghadhabu au hasira ikiwa imetupiliwa mbali.
Yesu alisema kwamba yeye ni mlango (Yohane 10:9). Aya hii inasema kitu kinachofanana, kwa sababu kwa kupitia yeye tunayo njia ya kuingia kwenye neema kwa njia ya imani. Yeye ni njia, kweli na uzima (Yohane 14:6).
(5:2b-5) Aya hizi zinaelezea uzoefu wa mtu aliyeamini anapokuwa anaishi kwenye neema.
Paulo alisema kwamba furaha yetu iko kwa sababu ya matumaini kwamba tutauona utukufu wa Bwana. Alisema kwamba tunaweza tukafurahia hata katika nyakati za mateso.
Mkristo anaweza akafurahia na kuvumilia mambo madogo (hali a maisha) kwa sababu mambo makubwa yana usalama. Mtu asiyeamini hujaribu kujipatia furaha yake kutoka katika vitu vya kimaisha. Lakini vitu vya kimaisha kamwe siyo vizuri kwa ajili ya kuleta utoshelevu wa kutosha; vinapita kwa haraka. Hali za maisha siyo mbaya sana kama maisha ni ya safari, lakini hali za maisha huonekana kuwa za kusikitisha sana kama hakuna kitu kingine chochote.
Kuvumilia mateso kwa uaminifu kunakamilisha mchakato kwa ajili ya mtu aliyeamini. (Ona pia Yakobo 1:2-4.) Tunapokuwa tunavumilia mateso kwa imani, tunajenga uvumilivu. Uvumilivu siyo tu uhiari wa kusubiri; ni uwezo wa kuvumilia kwa imani. Tunavyoendelea kufanyia mazoezi imani hii ya uvumilivu, tunaendelea kuwa na mazoea na kuiangalia kazi ya Mungu ambayo inatupa sisi matumaini. Tunajua kwamba makusudi ya Mungu yanakamilishwa hata katika wakati ambapo hali ya mambo yanaonekana kuwa mabaya.
► Je, unajifariji vipi wewe mwenyewe unapokuwa katika hali mbaya?
Tunajua kwamba matumaini yetu hayatakuwa ni ya kukatishwa tamaa, kwa sababu tayari tuna uzoefu wa upendo wa Mungu ndani ya mioyo yetu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Kwenye Waefeso 1:13-14, Paulo alisema kwamba Roho Mtakatifu ni dhamana ambayo Mungu atatumia katika kukamilisha kitu kingine chochote alichoahidi. Roho Mtakatifu ni kama amana ya mkataba.
5:6-10 inaweka msisitizo kwamba wakati wa kuhesabiwa kwetu haki hatukuwa tunastahili na hatungeweza kufanya lolote kukamilisha hilo. Tulikuwa hatuna nguvu, tulikuwa tungali wenye dhambi, na tulikuwa maadui.
(5:6) Kuwa bila nguvu inamaanisha kwamba ni kukosa uwezo wa kujiokoa wenyewe, hasa kwa kutimiza matakwa ya sheria. Tulikuwa hatuna nguvu ya kutimiza matakwa ya Mungu au kujikomboa wenyewe kutoka katika dhambi.
(5:7-8) Ni mara chache sana kwamba mtu anaweza kufa kwa ajili ya mtu mwingine mwema, lakini Kristo alikufa kwa ajili yetu wakati tukiwa wenye dhambi.
(5:9-10) Kristo anaishi kama mpatanishi na wakili wetu. Paulo anatoa sababu kwamba kama Mungu alikuwa tayari kusamehe wakati tulipokuwa wenye dhambi, basi tunaweza kuwa na uhakika hata na zaidi sana kuhusiana na upendeleo wake ambao sasa tunahesabiwa haki kwa njia ya Kristo. Tulipatanishwa kwa kifo chake kwa ajili yetu na kuendelea kukubaliwa na Mungu kwa njia ya kuunganishwa na Kristo aliye hai.
Upendo wa Mungu hauna sababu, hauna kipimo, na haukomi.
Je, sisi ni wenye hatia kwa dhambi ya Adamu?
► Je, sisi ni wenye hatia kwa dhambi ya Adamu? Elezea jibu lako.
Katika Warumi 5:12-19 panasema kwamba watu wote waliingizwa katika hali ya dhambi na kifo kwa sababu ya dhambi ya Adamu. Je, sisi binafsi tunayo hatia kwa dhambi ya Adamu? Je, wenye dhambi wataadhibiwa kwa dhambi ya Adamu?
Paulo hajasema kwamba wenye dhambi wataadhibiwa kwa dhambi ya Adamu. Katika 5:12 alisema kwamba mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi. Kila mtu kwa nafsi yake ni mwenye hatia kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe. Warumi 1-2 tayari ilishatoa msisitizo kwamba watu wanahitaji kuhesabiwa haki kwa sababu ni wenye dhambi ambao wamevunja sheria ya Mungu. Watu hawahukumiwi kwa ajili ya hali waliyozaliwa nayo, bali kwa ajili ya chaguo lao la kutenda dhambi. Hukumu inatokana na matendo (Ufunuo 20:12, Warumi 2:6-16, 2 Wakorintho 5:10).
Hata hivyo, kwa Adamu dhambi iliingia ulimwenguni. Kama baba wa wanadamu wote ambao walikuwa bado hawajazaliwa, alitenganisha wanadamu na Mungu. Watu wote baadaye wakawa wanazaliwa wakiwa tayari wametengwa na Mungu na, kwahiyo, kukasababisha uasi. Kwa sababu ya dhambi ya Adamu, watu wote huwa wanazaliwa wakiwa na tabia ya kutenda dhambi na wote kwa pamoja wameifuata kwa kutenda matendo ya dhambi.
Taarifa zifuatazo zinaweza zikatafsiriwa katika ufahamu huo:
Kwa kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa (5:15)
Hukumu ilikuja kwa njia ya mtu mmoja ikaleta adhabu (5:16)
Kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala (5:17)
Kwa kosa moja watu wote walihukumiwa adhabu (5:18)
Kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi (5:19)
Paulo hakusema kwamba tuna hatia kwa dhambi ya Adamu; lakini Adamu aliileta dhambi, na kila mtu akafuata. Wenye dhambi wanahitaji kusamehewa kwa ajili ya makosa yao mengi (5:16) na siyo kwa ajili ya dhambi ya Adamu.
Kifungu cha kujifunza – Warumi Sehemu ya 3, kifungu cha 3
Mwendelezo wa maelezo ya Aya–kwa-Aya
(5:12) Sababu ya kifo kuenea kwa watu wote siyo kwamba kosa la Adamu liliingizwa kwao, bali ni kwa sababu wote wamefanya dhambi. Adamu ndiye aliyeleta dhambi duniani na alileta uvutano wa dhambi juu ya wazao wake.
(5:13-14) Dhambi haijafunuliwa na kuhukumiwa kwa uwazi bila sheria. Hata hivyo, hata hadi wakati Musa alipopokea sheria, kifo kilikuwa bado kinatawala. Watu walikuwa wanajua kwamba ni wenye hatia kwa ajili ya dhambi, hata bila ya ufafanuzi uliokuwa unatolewa na sheria (Ona 1:20). Uhalisia kamili wa kiwango cha dhambi unaoneshwa na sheria. Kosa kama la Adamu linarejelea kwenye kukosa utii kwa kudhamiria dhidi ya sheria iliyotolewa. Wale waliokuwa hawana ufahamu wowote hawakuwa na chaguo lililo wazi, lakini bado hawakufuata kikamilifu dhamira zao (1:21).
(5:15) Kitendo cha Adamu kilisababisha kifo kwa watu wengi na kazi ya Kristo ikaleta uzima kwa watu wengi. Neno “wengi” linarejelea kila mtu kwa ujumla. Msisitizo ni kwamba matokeo ya upatanisho wa Kristo ulikuwa unafika mbali kuliko dhambi ya Adamu. Aya hii inasema kwamba kama vile dhambi ya Adamu ilivyosababisha kila mtu akawa mwenye dhambi, upatanisho wa Kristo unatoa neema kwa kila mtu. Mungu hutoa neema kwa kila mtu aliyefanywa kuwa mwenye dhambi kutokana na anguko la Adamu.
► Kutoka katika aya ya 15, utawezaje kumjibu mtu anayefikiri kwamba Mungu alitoa wokovu tu kwa asilimia ndogo ya wanadamu?
(5:16) Dhambi ya asili ilikuwa ni kitendo kimoja tu, lakini neema inahitajika sasa kwa ajili ya dhambi nyingi. Neema ni lazima iwe juu zaidi kuliko dhambi ya asili.
(5:17-19) Watu wengi walifanywa watenda dhambi kutokana na madhara ya dhambi ya Adamu. Watafanywa tena wenye haki halisi na Kristo. Maana yake ni kwamba wamebadilishwa.
(5:20) Sheria inazidisha dhambi kwa mantiki kwamba inasababisha msururu mrefu wa makosa wakati ambapo hapo awali dhambi chache tu ndizo zilizokuwa zinatambuliwa. Sheria pia iliongeza dhambi kwa mantiki kwamba kama mtu atakuwa anaijua sheria na akaamua kuikataa, anakuwa ni mtenda dhambi mbaya zaidi kuliko alivyokuwa mwanzo. Hii ni hali inayoelezewa katika 7:5-24. Lakini neema imezidishwa juu sana kupita upeo wa dhambi zote.
Neema ya Kushangaza
John Newton alikuwa na mama wa Kikristo, lakini akaamua kuwa baharia na kapteni wa meli. Akawa mwenye dhambi sana. Aliitabika kwa hali ngumu zikizomkabili katika maisha yake. Alisalitiwa na marafiki zake, kwa muda wa kipindi fulani, akafanywa mtumwa. Wakati hali yake ilipoanza kuonesha ahueni, aliendelea katika dhambi na akasaidia kuharibu maisha ya wengi kwa biashara ya utumwa. Alikuwa ni kapteni wa meli ya watumwa kwa miaka mingi. Wakati fulani alivunjikiwa na meli yake katika kisiwa lakini aliokolewa na kapteni wa meli nyingine ambaye alikuwa rafiki wa baba yake. Alihisi kwamba Mungu alikuwa amemrehemu ingawa alikuwa mwovu. Baadaye ile meli ilikuwa katikati ya dhoruba kali ya mawimbi baharini; akamwita Mungu akiomba rehema. Ile meli ilinusurika na ile dhoruba, na Newton aliendelea kumtumainia Mungu kwa ajili ya rehema. Hatimaye aliachana na mambo ya bahari na kuwa Mchungaji. Mojawapo ya nyimbo alizoandika ni huu ulioimbwa sana na ambao umerekodiwa zaidi kuliko wimbo wowote wa Kikristo uliowahi kuandikwa, “Katika Neema ya Yesu.”
Katika ushuhuda wake, Newton alisema, “Mungu kwa rehema zake amenitoa mimi kutoka katika dimbwi la matope na akaiweka miguu yangu juu ya mwamba, Yesu Kristo. Ameiokoa roho yangu. Na sasa, ni hamu ya moyo wangu kusifia sana, uhuru, ukuu wake na kuheshimu neema yake isiyolinganishwa na kitu chochote kwa sababu ‘Kwa neema ya Mungu niko kama nilivyo’ (1 Wakorintho 15:10). Ni furaha kuu ya moyo wangu ya kuuweka wokovu wangu kwenye neema ya Mungu.” [1]
[1]“John Newton’s Conversion,” kutoka https://banneroftruth.org/us/resources/articles/2001/john-newtons-conversion/ (Ilifikiwa Desemba 29, 2022).
Maswali ya Mapitio Somo la 5
(1) Je, Mtu aliye na imani iokoayo anaamini nini?
(2) Je, ni tatizo gani lilitatuliwa na upatanisho?
(3) Ni jinsi gani upatanisho ulitatua tatizo?
(4) Je, kuhesabiwa haki ina maana gani?
(5) Je, ni kwa njia gani mtu anaiheshimu sheria kama kipimo cha kuhesabiwa haki?
(6) Je, ahadi ya Mungu ya neema kwa Abraham ilikuwa ni nini?
(7) Je, Daudi alisemaje kuhusu kuhesabiwa kwa imani?
(8) Je, nani ni watoto wa kiroho wa Ibraham?
(9) Tunajua nini kutoka katika Warumi 5:15 kwamba wokovu hutolewa kwa kila mmoja?
Kazi ya kufanya Somo la 5
Andika ukurasa mmoja kuhusu kuhesabiwa haki kwa njia ya imani pamoja na kutoa majibu kwa maswali yafuatayo: Je, ni tatizo gani linalotatuliwa na upatanisho? Je, ni kwa nini mwenye dhambi hawezi akaokolewa kwa kutii? Je, ni kwa jinsi gani Ibrahimu amedhihirisha kuhesabiwa haki kwa imani? Je, tunajuaje kwamba wokovu unapatikana kwa kila mtu?
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.