Utangulizi wa Maandiko yahusuyo siku za mwisho (Apocalyptic)
Maandiko yanayohusu siku za mwisho yanahusu kutunza imani badala ya kulemewa na uovu na kutotenda haki katika dunia wakati wa siku za mwisho. Yanaelezea muda ambao Mungu kwa ghafla ataingilia kati duniani, akiadhibu uovu na akiwasaidia watu wake.[1]
Neno ambalo mara kwa mara linatumika kwa ajili ya muda wa mwisho wa Mungu kuingilia kati ni Siku ya Bwana. Baadhi ya vifungu kwenye Agano la Kale huelezea siku ya Bwana kama ni ule muda ambao Wamataifa wataadhibiwa kwa yale waliyokuwa wameifanyia Israeli.[2] Wayahudi wengi walianza kudhania kwamba Wayahudi hawakuwa na haja ya kuhofia chochote kuhusiana na hukumu ya Mungu. Manabii walijitahidi kuwaonesha kwamba hata wao watapaswa kuhukumiwa kama watakuwa watenda dhambi. (Zefania 1:12, Amosi 5:18-27) na kwamba hawataepuka kwa sababu wao ni Wayahudi; lakini dhana hii iliendelea kubaki.
Ilikuwa ni vigumu kwa Wayahudi kukubali ukweli kwamba walihitaji kuokoka. Kwa mfano, ubatizo ulikuwa ni sherehe waliyoitumia kuwaingiza Wamataifa kwenye Uyahudi. Hawakuwabatiza Wayahudi. Yohane Mbatizaji aliwabatiza Wayahudi, na kitendo chake hicho kiliwaghadhibisha Wayahudi ambao walifikiri kwamba hawakuwa wanahitaji ubatizo au msamaha. Walidhania kwamba walikuwa wamependelewa na Mungu kwa sababu walikuwa ni uzao au watoto wa Ibrahimu (Mathayo 3:9).
Kwenye kitabu cha Warumi, Paulo anarejelea kwenye maneno haya ya “siku ile ya hasira” (2:5) na “katika siku ile Mungu atakapozihukumu” (2:16). Marejeo haya yanatokana na mada iliyoko katika 1:16-18, kwamba injili huleta wokovu unaotuepusha na siku ile ya hasira. Katika 2:2-3 anawashangaza Wayahudi wanaojihesabia haki ambapo ukweli ni kwamba walikuwa pia na sababu ya kuwa na hofu na siku ile ya Bwana. Kwani hata Wayahudi wanahitaji wokovu.
[1]Maandiko ya siku za mwisho katika Agano la Kale ni pamoja na kitabu cha Danieli, Zekaria, Yoeli, Ezekieli 37-39, na Isaya 24-27. Kwenye Agano Jipya, tunapata kitabu cha Mathayo 24, Luka 21, Marko 13, 2 Wathesalonike 2, na Ufunuo.
Kifungu cha kujifunza – Warumi sehemu ya 2, kifungu cha 2
Katika somo hili, tutaendelea kujifunza sehemu ya 2 ya kitabu hiki cha Warumi. Katika somo lililotangulia, tulisoma kifungu kinachoelezea kuhusu kosa la Wamataifa. Kifungu hiki cha (2:1-29) kinaelezea kosa la Waisraeli.
Sehemu ya 2 ni 1:18-3:20. Jambo kuu katika sehemu hii ya 2 ni kwamba kila mtu katika dunia hii amekiuka mapenzi ya Mungu na yuko chini ya hukumu. Hakuna mtu anayeweza kuokoka kwa kufuata yale anayoyataka Mungu kwa sababu kila mtu tayari ameshayakiuka matakwa hayo.
Kwanza Paulo anatoa ufafanuzi kwamba Wamataifa wamekataa kuwa na ufahamu wa Mungu na wakageukia kwenye sanamu na tamaa za dhambi. Kisha, anaelezea hali ya Waisraeli, amabao walikuwa na sheria ya Mungu lakini hawakuifuata au hawakuitii. Sasa tutajifunza kifungu kinachohusiana na Waisraeli.
Hapa Paulo anabadilika kutoka katika nafsi ya tatu (wao) na kugeukia katika nafsi ya pili (wewe). Anazungumza na mtu yeyote aliyefikiria kwamba injili haikuwahusu kwa sababu tayari walikuwa wamefikia katik kutimiza viwango vya kuwa wenye haki. Wayahudi wengi walikuwa katika kundi hilo, na sehemu hii inazungumza kwa ajili yao (2:17); lakini Wamataifa walio na maadili ya viwango vya juu wanaweza pia wakawa kwenye kosa linalofanana. Anaonyesha kwamba mtu anayejifikiria kwamba ni mwenye haki bila ya neema ni mnafiki na mwenye hatia.
Jambo Kuu katika sura ya 2
Wayahudi wana hatia ya dhambi zinazofanana na wanazofanya Wamataifa na kwa sababu hiyo watahukumiwa vilevile na Mungu.
Muhtasari wa sura ya 2
2:1, 11 ndizo zinazofanya jambo kuu. 2:1 inaelezea kwamba Wayahudi wote kwa pamoja wana hatia inayofanana; 2:11 inaelezea kwamba Mungu hana upendeleo. Sehemu nyingine inayoendelea katika sura hii inajenga hoja inayotokana na taarifa zilizoko katika aya hizo. Yaliyopo hapo hayana kisingizio au udhuru, kama vile ambavyo wapagani au makafiri hawana pia cha kusingizia au udhuru (1:20).
2:13, 17 inaonyesha ni kwa nini Wayahudi wana tegemeo la kupewa upendeleo – kwa sababu walipokea Ufunuo wa Mungu na walikuwa na dini inayozingatia mafunuo hayo. Kwenye Warumi 1, Paulo alieleza ukweli kwamba Wamataifa wanastahili hukumu. Kila Myahudi angekubaliana na hili. Kisha kwenye 2:1, Paulo anawaogofya Wayahudi kwa kuonesha hatia yao. Wao pia walivunja sheria na wanastahili hukumu ile ile kama Wamataifa!. Walitegemea kwamba wangesamehewa kwa sababu walikuwa Wayahudi ambao waliifahamu sheria ya Mungu na walikuwa na dini iliyo sahihi.
Mamilioni ya watu leo wako katika kundi hili. Wanafikiri kwamba wanakubalika na Mungu kwa sababu wanaamini katika Mungu na wanatekeleza taratibu na mifumo ya dini wakati huku wakiendelea kutenda dhambi.
► Je kuna watu wengi katika jamii yako ambao kimakosa wanajifikiria kwamba wao ni Wakristo? Ni kwa nini wanafikiria hivyo?
► Mwanafunzi atapaswa asome Warumi 2:1-29 kwa ajili ya kikundi.
Maelezo ya Aya-kwa-Aya
(2:1) Kwamba wayahudi hawakuwa na “kisingizio au udhuru” inalingana na hali ya Wamataifa ambao walikuwa hawana kisingizio au udhuru (1:20). Wazo hilo lingeleta mshtuko kwa Myahudi anayejihesabia mwenye haki, kama ambavyo ingekuwa kwa binadamu wa sasa anayejidhania kwamba yeye ni mzuri wa kutosha.
Kwa kuwahukumu wengine, walijihukumu wenyewe pia, kwa sababu walikuwa wana hatia katika dhambi zile zile zinazofanana. Wajibu wao uliongezeka kwa kuwa walikuwa na Ufahamu wa ukweli. Yesu alisema kwamba miji mingine ya Israeli itahukumiwa vibaya kuliko hata ilivyokuwa kwa Sodoma na Gomora (Mathayo 11:21-24).
Aya hii inarejelea kwa mtu anayefikiria kwamba anaweza akawahukmu wengine na kisha akajihesabia yeye kwamba ni mwenye haki. Sehemu nyingine ya sura iliyobakia inamweka Mungu kwenye jukumu la kuwa jaji na inaonesha ni kwa jinsi gani hukumu yake ni tofauti na ya wale wanaohukumu katika njia ya kujipendelea wenyewe.
(2:2-3) Hukumu ya Mungu iko katika viwango vya uhakika. Mungu hatoi hukumu yake kwa kutumia viwango vinavyobadilika na visivyo sahihi vya kibinadamu.
(2:4) Mungu ametoa mwangalizo maalumu kwa Wayahudi, kwa hiyo walifikiria kwamba atapinda haki kwa ajili ya kuwapendelea. Ni kweli, wema wake kwao ulikuwa ni wa kuwaongoza kwenye toba, na siyo kuiondoa haki. Kwahiyo watu wengi “hudharau” wema wa Mungu kwa kuona kwamba ni sawa na suala la kawaida tu la ukarimu na uvumilivu. Kile ambacho mtu wa dunia anataka kutoka kwa Mungu ni mafaniko ya mali pamoja na kumvumilia wakati anaendelea kutenda dhambi. Kuuona wema wa Mungu katika njia hii ni kudharau wema wake. Wale ambao wamesikia habari za Mungu wana hatia zaidi kwa sababu wema wake Mungu uliwapa nafasi ya kutubu.
(2:5) Kuchelewa kwa muda wakati wanapoendelea kutenda dhambi badala ya kutubu kulikuwa kunalimbikiza ghadhabu. Kwa kuwa walikuwa wanajua ukweli, wanakuwa watu wa kuwajibika zaidi, na, kwa hiyo, ghadhabu ya Mungu iliongezeka dhidi ya kutokutii kwao.
(sehemu inayofuata ni muhimu sana kwa ajili ya kuelewa sehemu iliyobakia ya sura hii.)
Hukumu ya Matendo
► Tunapokuja kwenye eneo la hukumu, je, mambo tuliyotenda duniani yatakuwa muhimu?
Hukumu ya mwisho itakuwa ni kutathimini matendo. Mungu ataadhibu na kuwazawadia watu kutokana na matendo yao waliyofanya. Kutakuwepo na madaraja ya adhabu na thawabu kwa ajili ya watu wa aina mbalimbali (Waebrania 2:2, Waebrania 10:28-29, Mathayo 10:42, Luka 12:47-48, 2 Wakorintho 5:10).
Wazo kwamba wenye dhambi wanahukumiwa tu kwa ajili ya kutoamini sio la kimaandiko. Katika Ufunuo 20:12, watu wanahukumiwa kutokana na kumbukumbu za matendo yao. Katika 2 Wakorintho 5:10 panasema watu wote, ikiwa ni pamoja na watu waliookoka, watahukumiwa kwa matendo yao. 1Wakorintho 3:12-15 inaonyesha kwamba Wakristo watapokea thawabu tofauti tofauti kulingana na nia, bidii, na ubora (“dhahabu, fedha, mawe ya thamani, miti, majani, manyasi”), wa matendo yao. Wakristo wote watapata thawabu kwa sababu Wakristo wote wa kweli wanafanya matendo mazuri, lakini siyo matendo yao yote yatakayokuwa na usawa unaofanana. Matendo ya watu walioamini ambayo hayatapita kwenye jaribio la viwango vya ubora yatateketezwa kwa moto.
Kwenye Warumi 2 inaonesha kwamba baadhi ya watu ambao hawajawahi kusikia injili ya Agano Jipya hawatahukumiwa kwa ajili ya matendo yao. (ona 2:7, 10, 13, 26-27). Hiyo haimaanishi kwamba kuna watu ambao hawajawahi kutenda dhambi na kwahiyo wanaweza wakakubalika kwa matendo yao bila ya neema; kwa kuwa kwenye 3:19-20 panasema kwamba watu wote wametenda dhambi. Watu ambao matendo yao yanakubalika ni wale ambao wamejionea neema inayoitwa kutahiriwa moyo. Matendo yao yamethibitishwa na Mungu (2:29).
Hii neema ya upasuaji kwenye moyo ilikuwa imeahidiwa kwenye nyakati za Agano la Kale:
Bwana, Mungu wako, atautahiri moyo wako, na moyo wa uzao wako, ili umpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, upate kuwa hai (Kumbukumbu la Torati 30:6).
Kwa hiyo, tunatambua kwamba Wayahudi waliokolewa kwa neema, na siyo kwa matendo yao.
Neema hii ilipatikana pia kwa Wamataifa, aidha wawe au wasiwe wamepokea Ufunuo Maalumu.
Petro akafumbua kinywa chake, akasema, “Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye” (Matendo 10:34-35).
Matendo ya haki hufuatana na mabadiliko ya moyo, kukiwa na uthibitisho wa utii kwa Mungu. Ushahidi huu ndio msingi wa kuhesabiwa haki ya mwisho uliozungumzwa katika Warumi 2:13, 16, kuhesabiwa haki kwenye hukumu ya mwisho.
Kifungu hiki hakifundishi kwamba mtu ataweza kuokolewa kwa matendo yake, bali utii wa kweli ndio unaohitajika, na siyo tu ujuzi wa sheria. Jambo hli linaungwa mkono nakifungu hiki: kwamba Wayahudi pia wanahitaji wokovu kwa sababu hawakutii.
Kifungu cha kujifunza– Warumi Sehemu ya 2, kifungu cha 2
Mwendelezo wa maelezo ya Aya–kwa-Aya
(2:7) Mungu hutoa uzima wa milele kwa wale wote wanaotafuta kupata heshima itokanayo na Mungu kwa kuishi katika matendo yanayompendeza Mungu.
(2:9) Hapa fursa ya myahudi inaleta uwajibikaji mkubwa. Kwa kuwa injili ilikuja kwake kwanza, anastahili kupata hukumu ya kwanza.
(2:11) Hii ndio aya ya msingi ya sura hii. Wale wote wanaoishi kwa kumwasi Mungu watahukumiwa, bila ya upendeleo kwa sababu wamekuwa ni watu wa dini.
Mtazamo kutoka kwa Yakobo
Yakobo anasema kwamba mwanadamu hahesabiwi haki kwa imani tu, lakini pia kwa matendo yake (Yakobo 2:24). Lakini Paulo anasema katika Waefeso 2:8 kwamba mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria. Katika Warumi 3:28 anasema kwamba mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani mbali na matendo ya sheria.
Kwahiyo, je, tunahesabiwa haki kwa matendo na imani kwa wakati moja, au tunahesabiwa haki kwa imani tu? Je, Paulo na Yakobo wanajichanganya wenyewe? Ukweli ni kwamba hawakuwa wanazungumzia kuhusu jambo linalofanana.
Paulo anaelezea jinsi mtu anavyohesabiwa haki mbele ya Mungu. Mtu anakuwa mwenye haki kwa neema kwa njia ya imani.
Yakobo anaelezea jinsi mtu anavyohesabiwa haki mbele ya watu wengine. Mtu huonesha kuwa anayo imaini iokoayo kwa kuishi kwa uaminifu.
Jambo kuu katika Waraka wa Yakobo ni kuthibitisha kwamba imani ya kweli inatumiwa katika maisha ya kila siku. Anasema kwamba Ibrahimu alikuwa “amehesabiwa haki,” kwa matendo yake. Mtu anaonyeshwa kuwa mwenye haki kwa imani na matendo kwa pamoja. Tunatambua kwamba mtu ni Mkristo kama anakiri kuwa hivyo na pia kama anaishi maisha yanayofanana na Mkristo.
Paulo anatoa uthibitisho kwamba matendo mema hufuata baada ya imani. Katika Waefeso 2:10, baada tu ya tamko lake kwamba tunaokolewa kwa njia ya imani, Paulo alisema kwamba “tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema.”
Yakobo na Paulo hawajichanganyi. Wote wanakubaliana kwamba imani iokoayo humfanya mtu akubalike kwa Mungu, na kwamba matendo hufuata baada ya mabadiliko na kudhihirisha kwamba mtu huyo ameokoka.
Kifungu cha kujifunza– Warumi Sehemu ya 2, kifungu cha 2
Mwendelezo wa maelezo ya Aya-kwa-Aya
(2:12) Sheria iliyoandikwa haiwezi ikawa ndio kipimo cha hukumu kwa wale ambao hawajawahi kabisa kuisikia. Watahukumiwa kwa sheria ile ambayo Mungu alikuwa ameidhihirsha kwao kwa njia nyingine (Ona 1:20 & 2:15).
(2:13) “Watakao hesabiwa haki” inalenga kwenye hukumu ya mwisho. Baadhi ya watu wanategemea kuhesabiwa haki kwa sababu wameishika sheria. Lakini ufahamu wa sheria bila utiifu haukubaliki.
(2:14) wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati Ukweli ni kwamba wanaweza kufanya jambo la haki “kwa tabia zao” haimaanishi kwamba kwa asili ni wazuri bila Mungu. 2:15 inaonesha kwamba ni kwa sababu ya sheria ambayo Mungu ameandika ndani ya mioyo yao na dhamiri zao kwamba wanaweza kufanya jambo lililo jema. “kwa tabia zao” inamaanisha kwamba wanafanya kwa kile Mungu anachowafunulia kwenye asili yao bila ya Maandiko yaliyoandikwa.
(2:15) Wale ambao hawana sheria iliyoandikwa bado wanayo sheria iliyo ya maadili iliyoko dani yao na wanaweza wakafanya maamuzi yao maalumu. Hiyo haina maana kwamba dhamiri ni ya kutegemea kabisa. Dhamiri haiko sahihi kwenye kila jambo kwa kina, ikiwa inashawishiwa na mazingira na elimu; lakini ni mwongozo kwa kile kitu ambacho ni sahihi kwa ujumla. Hata hivyo, watu wote ni watenda dhambi, hata katika kipimo hicho, kwa sababu siku zote hawajaweza kufanya kile ambacho walijua kwamba ni sahihi.
2:15, 16 inaonyesha kwamba hukumu haitakuwa tu ni kwa ajili ya matendo ya nje, bali kimsingi hata nia ya kutenda jambo. (mistari hii inazungumzia mioyo, mawazo, dhamiri, na siri.)
(2:16) Kuhesabiwa haki kunakojadiliwa katika kifungu hiki (Imetajwa kwenye 2:13) siyo mbadala wa kuhesabiwa haki kwa njia ya imani. Ni udhihirisho wa mwisho, wa kuhesabiwa haki katika hukumu ya mwisho.
Kanuni hizi za hukumu ni za msingi kutokana na injili aliyoihubiri Paulo. Habari njema za injili kuhusiana na msamaha siyo muhimu kama hakuna uelewa wa hukumu ya Mungu itakayokuja dhidi ya wale ambao hawana msamaha. Kosa lolote ambalo linadhoofisha mtazamo sahihi wa haki ya Mungu litapotosha pia injili.
Tumaini kwa Wapagani au Makafiri ambao hawajafikiwa.
► Je, ni nini kitakachotokea kwa wapagani au makafiri ambao hawajawahi kuisikia injili? Ni kwa jinsi gani wanaweza kustahili hukumu kwa ajili ya dhambi kama hawajui vizuri?
Kwenye Warumi 2:14-16 panaonesha kwamba kuna baadhi ya watu ambao huchagua kutenda mambo ya haki, na, kwahiyo, hawatahukumiwa. Hata hivyo, tunajua kwamba hakuna mtu atakayeokoka kwa matendo yake. Kila mtu ameivunja sheria na anastahili hukumu. (3:9-10, 19-20). Hakuna mtu anayeweza kuokoka kwa sifa njema za matendo yake. Kwa hiyo, mtu ambaye hajawahi kusikia injili akiokoka, itakuwa ni kwa neema kupitia upatinisho, kama atakuwa hajaisikia injili.
Kama mtu anamcha Mungu, Mungu atamonesha njia ya kumleta kwenye uhusiano naye. Zaburi 25:14 inasema "Siri ya Bwana iko kwao wamchao, Naye atawajulisha agano lake." Agano la Mungu linatuonesha kitu kinachohitajiwa katika ushirika naye. Uhusiano na Mungu huhitaji neema kwa sababu watu wote wametenda dhambi.
Kulikuwa na watu kama akina Ayubu, Balaamu, na Nuhu ambao walimjua Mungu ingawaje hawakuwa na Maandiko. Kulikuwepo na Melkizedeki, aliyekuwa kuhani wa Mungu, ingawaje alikuwa hana uhusiano na kile ambacho Mungu baadaye alifanya kwa Israeli. Mungu anaweza akajidhihirisha mwenyewe kwenye utamaduni wa aina yeyote na kwa wakati wowote. (Ona pia Zaburi 19:1-4, Warumi 10:18). Waabudu sanamu katika Warumi 1 hawakuwa katika hali ya kukengeuka kwa sababu kamwe walikuwa hawajawahi kumjua Mungu, lakini kwa sababu walikuwa wamekataa kile walichokuwa wanakijua.
Je, inawezekana mpagani au kafiri akaokoka bila ya kuisikia injili? Kama mtu atafuata ukweli anaoujua, Mungu atamwongoza katika kuelewa zaidi jinsi ya kutafuta na kupata msamaha. Hiyo ndiyo wokovu kwa njia ya neema na siyo kwa matendo. Hii ni tofauti ya ulinganifu wa wokovu kwa njia ya matendo ambao ndio unaoelezwa na dini nyingi.
Hivyo, kama mtu anaweza akaokoka bila ya kusikia injili, kwa nini jambo muhimu kwetu kueneza injili? Swali hili litajibiwa zaidi mbeleni.
Kifungu cha kujifunza – Warumi Sehemu ya 2, kifungu cha 2
Mwendelezo wa maelezo ya Aya–kwa-Aya
(2:17-20) Wayahudi walikuwa wanafiki kwa sababu walikuwa wanafundisha sheria huku wakiivunja wao wnyewe. Walifurahia jukumu lao la kuwa ni watu waliomiliki sheria, watu wanaotambua haki, na waalimu wa wajinga. Kuna maelezo ya kejeli hapa wakati Paulo anapoorodhesha madai yao makubwa.
Biblia inaweza ikawa kitabu kinachouzika hata katika jamii ambayo inaenda kuwa siyo ya kumcha Mungu. Inaonesha kwamba watu wanaona thamani kuwa na sheria za Mungu hata kama hawawezii kuzitii.
Mara nyingi watu wanashikilia namna za kidini kama kisingizio cha kufunika dhambi baada ya kupoteza ukweli wa kiroho kwenye uhusiano wao na Mungu.
(2:21-24) Wayahudi walifurahia kuwahukumu Wamataifa kwa kutumia sheria, lakni wao wenyewe walikuwa hawaitii kwa ukamilifu. Walimvunjia Mungu heshima kwa kujisifu juu ya wema wao huku wakiishi maisha ya dhambi. Vivyo hivyo, kipingamizi kikubwa kwenye Ukristo ni kwamba Wakristo sio mfano mzuri wa kuigwa katika yale mambo wanayojinadi nayo kwamba wanaamini.
(2:25) Hawakuweza kudai kuwa wenye haki mbele za Mungu kwa msingi wa kutahiriwa isipokuwa kama wangeishika sheria yote. Kama walivunja sheria, walikuwa sawa tu na watu ambao walikuwa hawajatahiriwa.
Msamiati wa Kutahiriwa
► Je, kutahiriwa kulikuwa kunaashiria nini?
Kwa fikira ya Wayahudi kulikuwa na aina mbili za watu duniani: wale wenye sifa ya kukaa kwenye agano na Mungu na wale ambao hawakuwa na haki hiyo. Kutahiriwa kulikuwa ni kama ishara ya Agano kati Israeli na Mungu, lakini hatimaye ikaja kuwakilisha msururu mzima wa mahitaji yote kwa ajili ya agano. Kwa hiyo, Wayahudi wakaita hizi aina mbili za watu wa dunia kwamba ni waliotahiriwa na wasiotahiriwa. Ili uweze kutahiriwa, kwa mujibu wa malezo ya Paulo, kwa kawaida ina maana ya kufuata mfumo mzima wa Uyahudi kama njia ya kuwa kwenye Agano. (Ona Wagalatia 5:2-3 kama mfano wa matumizi ya maelezo hayo). Kutahiriwa katika maana hiyo ya ufahamu ilkuwa ni jaribio la kuokolewa kwa njia matendo kuliko kwa njia ya neema.
Kifungu cha kujifunza – Warumi Sehemu ya 2, kifungu cha 2
Mwendelezo wa maelezo ya Aya-kwa-Aya
(2:26) Kama mtu asiyetahiriwa akitimiza makusudi ya kweli ya sheria, Mungu hatamhukumu kwa kutotahiriwa.
(2:27) Ulinganifu kati ya Mmataifa mwenye haki na Myahudi mtenda dhambi unaonesha kwamba Myahudi ni mwenye hatia, ingawaje anayo asili ya Uyahudi. Kwa ufahamu unaofanana, Nuhu aliihukumu dunia kwa hali yake ya kuwa mwenye haki kwa sababu alionesha utii wa kweli ni nini (Waebrania 11:7).
(2:28-29) Kutahiriwa kulikuwa ni alama ya utambulisho kwa Myahudi, kwamba alikuwa ni mmoja wa watu wa Mungu. Kwa Mkristo (Katika Kumbukumbu la Torati 30:6 na katika maeneo kadhaa ya Agano Jipya) inaashiria kazi ya Roho Mtakatifu wakati anapobadilisha moyo wa mwenye dhambi kwa kumpenda na kumtii Mungu.[1] Huu ni umuhiku wa tohara kwa mkristo
► Mwanafunzi atapaswa asome Kumbukumbu la Torati 30:6 kwa ajili ya kikundi.
Mungu aliwaahidi Waisraeli wa mwanzo kwamba atafanya kazi ya neema ndani ya mioyo yao. Hii haikuwa ni kwa ajili ya uzao wao tu, lakini ni kwa ajili ya watu wote waliousikia ujumbe kwa wakati ule.
Mtu anayezungumziwa katika sura hii ambaye anafanya matendo mema bila ya kujua Maandiko ni mtu ambaye ameipokea neema kwa njia ya imani, kwa kuiamini kweli aliyo nayo.
[1]Kumbukumbu la Torati 30:6, Wafilipi 3:3, Wakolosai 2:11-12
Mtazamo kutoka kwa Isaya
Mungu siku zote anantaka utii kutoka ndani ya moyo, kuliko urasmi na ushikiliaji mno wa sheria, na anatoa neema kwa Wamataifa wote. Kumbuka mistari hii kutoka Isaya 56:6-7.
Na wageni, walioandamana na Bwana ili wamhudumu, na kulipenda jina la Bwana, kuwa watumishi wake; kila aishikaye sabato asiivunje, na kulishika sana agano langu; Nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote.
Maswali ya Mapitio Somo la 3
(1) Je, Maandiko yanayohusu siku za mwisho yanaelezaje?
(2) Je, kwa nini Wayahudi walitarajia kupata Upendeleo?
(3) Je, mtu anahesabiwaje haki?
(4) Je, mtu huoneshaje kwamba anayo imani iokoayo?
(5) Je, tohara ina umuhimu gani kwa Myahudi, na ina mfano gani kwa Mkristo?
Kazi ya kufanya Somo la 3
Andika ukurasa mmoja kuelezea kuhusu kutokuelewa kwa Wayahudi ambao kwa makosa hufikiri kwamba wanapaswa wakubaliwe na Mungu. Elezea watu wengine ambao wana kutokuelewa kama hawa Wayahudi leo.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.