Wakati ule wa Paulo, jiji la Rumi ndilo lililokuwa kubwa kuliko yote duniani, likiwa na wakazi zaidi ya milioni moja.[1] Kulikuwa na mchanganyiko wa makundi mbalimbali ya kikabila, lugha, na dini. Wengi wa watu walikuwa ni watumwa.
Wamisionari wa kwanza katika Rumi
Hatuwezi kujua ni mtu gani aliyekuwa wa kwanza kupeleka injili katika Rumi. Kwenye siku ya Pentekoste, Wayahudi walikuwepo kutokea Rumi (Matendo 2:10). Wale waliokuwa wamebadilishwa na au kuokoka kwa hakika walichukua ujumbe wa injili wakati wa kurejea Rumi. Tangazo lao kwamba Masihi alishakuja lilisababisha mshangao na utata. Injili iliisambaa kwa haraka miongoni mwa Wamataifa ambao tayari walikuwa wanaiheshimu dini ya Kiyahudi.
Kanisa la Wamataifa
Ingawaje Wayahudi wanatamkwa kwenye sehemu za barua hii, kanisa lililokuwa Rumi lilikuwa na wingi wa watu wamataifa. Paulo aliwaita wamataifa (1:13-15) na akasema kwamba kwa sababu alikuwa ni mdeni kwa Wayunani na watu wote waliojulikana kama washenzi, alikuwa tayari kuhubiri kwa Warumi. Hata hivyo, ushawishi wa Kiyahudi katika kanisa la Rumi ulikuwa wenye nguvu sana, kwa kuwa waamini wa kwanza katika eneo hilo walikuwa ni Wayahudi. Inawezekana kwamba injili ilikuwa bado haijaelezwa kwa ufasaha katika njia ambayo ingewaonesha waamini uhuru wao wa kutoka katika sheria za Kiyahudi.
[1]Bruce Wilkinson & Kenneth Boa, Talk through the New Testament, 375
Kwa kuwa kusudi la Paulo lilikuwa ni kuendeleza kazi ya kimisheni, swali ambalo kwa kawaida ni lazima lingejitokeza ni, “Je, kila mtu kweli anahitaji kuhesabiwa haki kwa njia ya imani?” Pamoja na hayo, kuna mambo ambayo siyo kila mtu anayahitaji. Watu walioko sehemu za maeneo ya barafu ya Arctic hawahitaj mtu yeyote awaletee barafu, na watu wanaoishi kwenye majangwa hawahitaji mchanga.
Labda mtu anaweza akafikiria kwamba kuhesabiwa haki kwa njia ya imani siyo kitu ambacho kila mtu katika dunia hii ni lazima ahitaji; inawezekana baadhi ya watu wamekuwa wakiishi kwenye maisha ya haki na tayari wamekubaliwa na Mungu. Sehemu ya 2 ya barua (1:18-3:20) imeandikwa ili kuonyesha kwamba kila mtu anahitaji kuhesabiwa haki kwa njia ya imani na, kwa hiyo, wanahitaji ujumbe unaohusiana na hilo.
Jambo kuu katika 1:18-3:20
Kila mtu katika ulimwengu huu amekiuka matarajio na mahitaji ya Mungu na yuko chini ya laana. Hakuna mtu yeyote anayeweza tena kuokolewa kwenye msingi wa kutimiza matarajio na mahitaji ya Mungu kwa sababau kila mtu tayari alishakuwa mkiukaji wa mambo yote.
Muhtasari wa 1:18-3:20
Kwanza, Paulo anaelezea hali ya Wamataifa wapagani waliokuwa hawana neno la Mungu lililovuviwa kwao na inaonesha kwamba walikuwa wamekataa kuwa na ufahamu wa Mungu aliowaonesha kwenye uumbaji. Kisha, anaelezea hali ya Waisraeli, ambao walikuwa na neno la Mungu lililokuwa limeandikwa lakini hawakulitii. Anahitimisha kwa kuelezea hali ya ujumla ya dhambi ya dunia. Hitimisho ni kwamba dunia yote ina hatia mbele za Mungu. Injili inahitajika kwa sababu hakuna mtu yeyote anayeweza kuokoka kwa kuwa ana stahili mwenyewe.
Kwa ajili ya masomo haya, sehemu ya 2 (1:18-3:20) itagawanywa kwenye vifungu vitatu. Kwenye somo hili, tutajifunza kifungu cha kwanza (1:18-32).
Kifungu cha kujifunza – Warumi sehemu ya 2, kifungu cha 1
1:18 ni aya ya mpito kati ya kifungu hiki na kifungu kilichotangulia.
Jambo kuu katika 1:18-32
Mataifa walikuwa na msingi wa ufahamu wa Mungu, lakini wakaukataa huo ufahamu na kugeukia kwenye kuabudu sanamu, wakawa watu waliokengeuka sana.
► Mwanafunzi atapaswa kusoma 1:18-32 kwa ajili ya kikundi.
Maelezo ya Aya-kwa-Aya
(1:18) Mungu amewapa ufahamu wa msingi kuhusiana na yeye mwenyewe. Wanaukandamiza ukweli. Hii inaonesha kwamba walikuwa na sehemu ya ukweli kama aya inayofuata inavyoelezea. Hukumu yao ni kwamba wameukataa ukweli waliokuwa nao. Neno "Uasi’ linaelezea kosa la kidini na linajieleza lenyewe kama kuabudu sanamu, ibada ya kuabudu zaidi kiumbe kuliko kumwabu Mwumbaji (1:19-23). “Uovu” inamaanisha ukaidi wa maadili na inaoneshwa kwenye suala la uasherati na uovu (1:24-32)."[1]
Ukweli walioukandamiza umebainishwa kwenye 1:20. Unahusisha ufahamu wa malaka ya Mungu uliokuwa juu yao. Mfumo wao wa maisha unadhihirisha kwamba wanayakataa mamlaka ya Mungu. Katika ulinganifu, maisha ya kuishi kwa kumfanania Kristo yanaonesha kujisalimisha na kujikabidhi kwenye mamlaka ya Mungu, kwa pamoja katika yale anayoyatenda na yale ambayo hayatendi.
[1]Imebadilishwa kutoka William Greathouse, “Romans”, in Beacon Bible Commentary, Vol VIII. (Kansas City: Beacon Hill Press, 1968) 50.
Aina za Ufunuo – Maalumu na wa msingi
► Je, kuna baadhi ya njia gani ambazo ukweli wa Mungu hudhihirishwa kwa watu wote?
Kwa kuwa umedhihirisha ukweli kwa njia nyingi, tunazungumzia kuhusu aina mbili: Ufunuo wa msingi na Ufunuo Maalumu. Paulo anarejelea kwenye hizi aina mbili kwenye kitabu cha Warumi, ingawaje siyo kwa kutumia maneno haya.
Ufunuo wa Jumla ni kile ambacho tunaweza kukifahamu kuhusiana na Mungu kwa kuanagalia uumbaji wake. Tunauona ujuzi wa ajabu na wa kushangaza na nguvu za Mungu katika uumbaji wa ulimwengu.
Tunaona umuhimu wa Mungu katika njia ile ambayo mwanadamu ameumbwa. Ukweli kwamba tunaweza kufikiri na kuwa na sababu, tunaweza kukubaliana na uzuri, na tunaweza kuelezea tofauti kati ya jema na baya, (ingawaje siyo ya uhakika) inatuonyesha kwamba Muumbaji wetu anazo sifa hizo katika kiwango cha juu. Tunajua kwamba Mungu anaweza kufikiri na kuwasiliana kwa sababu tunao huo uwezo (Ona Zaburi 19:1-4 na 94:9).
Kwa kuwa Ufunuo wa msingi unaonyesha kwamba Mungu anaweza kuzungumza, tunatambua kwamba Ufunuo Maalumu unaweza ukatokea. Mungu ni nafsi[1] na mwenye uwezo wa kuzungumza na viumbe wake wenye busara. Hiyo inatusaidia sisi kutambua kwamba kunaweza kuwepo na jumbe mbalimbali kutoka kwa Mungu na hata kitabu kutoka kwa Mungu.
Kwa kupitia Ufunuo wa Msingi, hata bila ya Maandiko, watu wanajua kwamba Mungu yupo, na kwamba wanapaswa kumtii, na pia kwamba tayari walishaacha kumtii (Warumi 1:20). Lakini hautuelezei ni kwa jinsi gani tutaweza kuwa kwenye uhusiano sahihi na Mungu. Unatuonesha hitaji maalumu tunalohitaji kwa ajili ya Ufunuo Maalumu kwa sababu unaonesha kwamba watu ni watenda dhambi na wasiwe na udhuru mbele ya Muumba wao.
Ufunuo wa Msingi unatuonesha kwamba utu wa binadamu umeanguka na una hatia. Ufunuo Maalumu unatoa ufafanuzi ni kwa nini utu wa binadamu umefikia kuwa katika hali hiyo. Ufunuo Maalumu ni ukweli unaodhihirishwa kwenye uvuvio wa Biblia na kwenye kuwa mfano halisi wa mwili wa Kristo. Ufunuo Maalumu unaelezea tabia ya Mungu, unafafanua anguko la mwanadamu na dhambi, na ni kwa jinsi gani tunaweza kupatanishwa tena na Mungu.
[1]Hatusemi hapa kumaanisha kwamba Mungu ni mwanadamu; Yeye ni kama mwanadamu – katika uwezo wa kufikiri, dhamira na kuzungumza – badala ya baadhi ya nguvu binafsi isiyokuwa ya kawaida.
Kifungu cha kujifunza – Warumi Sehemu ya 2, kifungu cha 1
Mwendelezo wa maelezo ya Aya-kwa-Aya
► Je, Ufunuo Maalumu unatueleza nini zaidi ya kile tunachokijua kutoka katika Ufunuo wa Msingi?
(1:19) Kwa kuchunguza uumbaji tunauona ukweli kuhusiana na Mungu. Hata wana falsafa wa Kiyunani walikiri kwamba ni lazima kuna aina fulani ya akili za kimungu ambazo zinauongoza ulimwengu. Sehemu muhimu sana ya uumbaji ni ile inayohusiana na asili ya mwanadamu. Tunauona ukweli kuhusiana na uwepo wa asili ya Mungu kwa kuangalia kwamba mwanadamu anao utashi wa kutambua mema na mabaya (Ona 1:32).
► Je, ni jambo gani ambalo tunaweza kulifahamu kuhusiana na Mungu tunapomwangalia mwanadamu?
(1:20) Tangu uumbaji watu wanatambua kwamba wameumbwa na kwamba Mungu anazo nguvu za kiungu na mamlaka juu yao. Huu ni ufahamu wa kutosha wa kufanya kwao kumkataa Mungu kusiwe na udhuru. Watahukumiwa kwa haki ajili ya dhambi zao. Wanajijua kwamba wana hatia kwa ajili ya uasi wao.[1] Ukweli kwamba wanajua mambo haya yote kuhusu Mungu na wao wenyewe kunawaacha bila ya kuwa na udhuru.
Haki ya Mungu inahitaji kwamba dhambi ni lazima ioneshwe kwa uwazi na kwa hiari kabla ya kuadhibiwa. Ni muhimu pia kwamba ufahamu waliokuwa nao ulikuwa unatosha kwa ajili ya wao kuweza kufanya uchaguzi ulio bora zaidi. Kama ingekuwa haiwezekani kwa wao kuchagua kufanya vinginevyo au tafauti na hapo, basi hawangeweza kukaa wasiwe na udhuru. Mungu yuko hapa akijieleza kuhusu yeye mwenyewe.[2]
Takriban kila tamaduni ulimwenguni ina dhana kwamba kuna Mungu mkuu aliyeumba ulimwengu. Kwa kawaida wanaabudu nguvu zingine zisizo za kawaida badala ya Mungu kwa sababu wanajua kwamba wametengwa na Mungu mkuu. Paulo hakujaribu kuthibitisha kuwepo kwa Mungu bali alionyesha kwamba kuwepo na mamlaka ya Mungu yanajulikana katika kila utamaduni. Ujuzi huu unasababisha kuwa na uhakika wa hatia.
Kuna mapungufu kwenye Ufunuo wa Msingi. Kumjua Kristo na injili hakutafahamika ila kwa njia ya Ufunuo Maalumu. Pia, dunia iliyoumbwa haimwoneshi Mungu kwa njia iliyo sahihi kwa sababu iko chini ya laana ya dhambi na haioneshi kabisa muundo wake wa asili. Uumbaji ni kama upakaji mzuri sana wa rangi ambao umewekewa alama ya mguu wa matope juu yake. Umeharibiwa, lakini sehemu yake ya uzuri wa asili bado imebakia, ikionyesha jambo fulani kuhusiana na mchoraji.
(1:21-22) Mungu anastahili kwamba mtu amheshimu kama Mungu (kuabudu) na kuwa na shukrani (sifa). Lakini walikataa mamlaka yake kuliko kuwa na shukrani kwa kile ambacho walikuwa wamepokea kutoka kwake. Walitaka wao wenyewe wawe miungu wakijitwalia sifa kwa yale yote waliyokuwa nayo. Kudai kuwa wao ni miungu ni upumbavu.
Mioyo yao iligeuka kuwa giza. Moyo unawakilisha mapenzi na utiifu wa mtu. Nuru inawakilisha ukweli. Kwa kuwa waliukataa ukweli, walikosa pia na uwezo wa kuuona. Walikosa ufahamu wa kiroho na wa mambo ya milele, kwa hiyo pia hawakuweza kuuelewa ulimwengu wa kimwili kwa usahihi wake.
[3](1:23, 25) Kujitazama wenyewe na kutazama ulimwengu wa kimwili na kumkataa Muumbaji kuliwasababisha kutengeneza miungu ambayo ilitengeneza asili ya maanguko yao wenyewe. Utukufu uliokuwa unamhusu Mungu pekee, waliuhamishia kwenye viumbe wengine Ili kuepukana na uwajibikaji wao kwa Muumbaji, waliukana uwepo wake na wakaheshimu viumbe. Mtazamo huu hasi ndio msingi wa mageuko (evolution) ya kisasa na ya ubinadamu. Kama watu walijitengeneza wenyewe, basi wanaweza wakajiwekea malengo yao, thamani zao na maadili yao wenyewe.
Asili ya ibada ya sanamu ni kutumikia na kuabudu kitu ambacho Mungu amekiumba. Kutumikia kitu ni kule kukipa nafasi ya kwanza katika maisha na kupanga maisha yaende kwa kufuata kipaumbele hicho. Kuabudu kitu ni kukitegemea na kukipa heshima ambazo ni za Mungu peke yake. Ibada ya sanamu hupata utoshelevu wake kutokana vitu ambavyo Muumbaji peke yake anatoa. Hali ya sasa ya kupenda mali na vitu ni ibada ya sanamu. Mtu hawezi akaheshimu mali na vitu bila kupunguza kumheshimu.[4]
►Je, Wamataifa wanajihusishaje na kumfahamu Mungu?
(1:24) Aya hii inatoa utangulizi wa mada ambayo imepanuliwa kwenye 1:26-27. Pendo la kuabudu sanamu kwa kawaida linajielekeza kwenye uasherati, ikiwa ni pamoja na dhambi zote za ngono au kujamiana. Dhambi ya ngono au kujamiana hufanya tamaa za mwili kuwa ni kipaumbele lakini inauvunjia heshima mwili kwa sababu mwili unapaswa uwe mtakatifu na ujikabidhi kwa ajili ya utumishi wa Mungu.
(1:26-27) Uasherati ni matokeo ya asili ya kujitukuza na kuruhusu tamaa za kimwili zitawale. Wakati tamaa zinapotawala, zinakuwa zimepotoshwa. Kwa kuwa mtu hawezi kumpenda mtu mwingine yeyote kwa usahihi au kufurahia kitu chochote kwa usahihi hadi awe amempenda na kumfurahia Mungu kwa hali ya juu sana. 1:24 inatambulisha somo hili na inaonyesha muunganiko ulioko kati ya uasherati na kumkataa Mungu.
Dhambi zote ni upotoshaji wa kitu kizuri alichokifanya Mungu; upotovu wa ngono au kujamiana uko wazi zaidi kuliko baadhi ya dhambi zingine. Kwa jinsi mtu anavyozidi kujiondoa na kuwa mbali na njia za Mungu, hufanyika zaidi kuwa mkatili, mkorofi, na mpotovu. Baadhi ya watu hufikiri kwamba kuna tamaduni na mila zinazoishi maisha mazuri kwa kuwa hazijaingiliwa na ustarabu wa kisasa. Ukweli ni kwamba watu wengi wenye kudumisha mila hizo wanaishi katika hofu ya kifo na mambo ya mizimu; wanatenda matendo ya mila za kikatili; na wanapata mateso ya upotovu yatokanayo na mfumo wa maisha ya upotovu wa dhambi.
Mwanadamu aliumbwa ili atumike kwa ajili ya uhusiano na Mungu. Ikiwa atakuwa ametengwa na Mungu, hawezi akawa vile ambavyo ubinadamu ulikuwa umekusudiwa uwe. Huwa ni mdhaifu hata kwenye maadili yake binafsi. Maadili kuhusiana na uanamume na mwanamke hayawezekani kufikiwa kwa mtu asiye na Mungu. Katika hili upotovu wa dhambi ya zinaa ni wa kupindukia mipaka, lakini kila mtu ameathirika kwa kupotea kwa ubinadamu wa kweli kwa njia nyinginezo pia. Kumkataa Mungu kama Mungu ni sawa na kumkataa binadamu kama binadamu. Kukataa kumwabudu Mungu ni sawa na kuukataa ubinadamu wako mwenyewe.
Jambo lililo kinyume ni kwamba, wale wote wanaoabudu kiumbe wameishia kwenye upotovu hata dhidi ya kiumbe mwenyewe, kinyume na kile kilichokuwa cha asili. Kama watu watajiruhusu wnyewe kutawaliwa na tamaa za mwili, tamaa hizo huingia kwenye hatua ambazo si kawaida za hali ya juu sana.
Ni jambo la ajabu kwamba kama mtu atakuwa na tamaa za mwili bila kumtii Mungu ataukosesha mwili wake heshima. Sehemu za mwili ambazo watu huwa wanaziabudu kwenye dhambi ya ngono au kujamiana ni sehemu zile zile ambazo wanazitaja wanapokuwa wanataka kusemea kitu kibaya au kudhalilisha.
Kwa kawaida wanawake siyo wepesi kiasi cha kufikia wanaume kwa ajili ya uasherati na upotovu. Kwa silika yao wanataka kulinda utimilifu wote wa familia. Neno “hata wanawake wao” linaonyesha kwamba uharibifu wa jamii yao kwa ajili ya uasherati ulikuwa umekamilika.
► Je, kuna aina gani za upotovu ambazo ni za kawaida katika jamii yako?
Hali ya dhambi waliyoingia inaitwa malipo. Ndivyo walivyostahiki kwa haki. Hali ya wenye dhambi ni adhabu ifaayo kwa ajili ya dhambi. Wanapata mateso na aibu inayoongezeka. Tamaa zao haziwezi kutoshelezwa. Kuna matokeo mabaya kwa sababu ya ufisadi wao.
Hakuna ushahidi kwamba Biblia inatambua uhalali wa kupenda “kufanya vitendo vya ushoga (au usagaji).”[1] Kama ingekuwa ndio hivyo, tungetegemea tukute mafundisho katika Maandiko yote kama ilivyofanyika kwenye kila aina ya mahusiano ya kibinadamu (mfano, waume kwa wake, wazazi na watoto, wananchi na serikali.) Badala yake, hakuna aya hata moja katika Biblia inayoonyesha uwezekano wa kuwepo kwa uhusiano wa aina hiyo ambao unakubaliwa kwenye macho ya Mungu.
Siyo majaribu, siyo hisia za upendo au mvuto kati ya wanadamu wawili, au mapambano katika roho zetu ambayo yamekatazwa kwenye Maandiko. Ukweli ni kuwa, Mungu anatuambia kwamba yuko karibu sana na wanaoumia mioyo yao, waliochanganyikiwa, na walioko kwenye majaribu. Dhambi inajitokeza wakati tunapokarisha ndani mwetu mawazo ya tamaa (Yak 1:15) au tunapojihusisha na tabia iliyo nje ya mpango wa Mungu.
Jibu linalofaa kutoka kwa kanisa kuhusiana na ushoga ni lazima lihusishe na upendo wenye huruma, ukweli wenye upole, na unyenyekevu thabiti. Kuwapenda watu wengine inamaanisha kuwajali, na kuuendeleza upendo wa Kristo hata kama watakuwa wamebadilika au hawajabadilika kutoka kwenye hali ya dhambi zao. Kuwapenda watu wengine inamaanisha ni kuwaona kwa jicho la Kristo, kama vile naye alivyotuona (na bado anatuona) katika dhambi zetu. Mara nyinyi, ni uhusiano wetu na mtu binafsi ambao awali utamwongoza mtu huyo kwenye uhusiano wa Kristo uwezao kuokoa. Kitakachofuata baadaye, ni kazi ya Roho Mtakatifu, ambayo kwa kawaida hufanya kazi ndani ya kanisa, ili kurejesha ule ukamilifu.
Na bado, kumpenda mtu pia inamaanisha kuzungumza ukweli, hata kama ukweli huo itabidi kukutana na ukatili au kutojali. Kushirikisha Neno la Mungu kunaweza kumwokoa mwanamume au mwanamke kutoka maisha yote ya maamuzi mabovu, kuchanganyikiwa, dhambi na mateso. Sio kila mtu anakubali maagizo ya Biblia. Uvumilivu na upole unapasa kuongoza mijadala yetu kuhusu ukweli wa jambo hili. Inatupasa kusikiliza kwa mioyo iliyowazi na kutumia Maandiko kwa upendo na upambanuzi. Tunapaswa kuonesha kwa dhati kumjali mtu, ili waweze kuthamini tunachosema.
Unyenyekevu wa kweli ni muhimu kwa ujumbe wa Kristo. Unyenyekevu hutokana na kuwa na mazungumzo na muda pamoja na Mungu; kukubali, kukiri, na kugeuka kutoka katika dhambi zetu wenyewe; na kukubaliana na upendo ulio wa kina wa Mungu kama ulivyojieleza juu ya msalaba. Ni lazima tuachie upendo na huruma viwe ndio nia yetu kuliko hofu, hasira, na chuki.
(1:28) Kwa kuwa walikataa kuwa na Mungu katika fahamu zao na katika mfumo wa maisha, akili zao na falsafa ziliharibiwa pamoja na tabia zao. Kuna msemo wa maneno kwa Wayunani unaoonesha kwamba kwa kuwa walimkataa Mungu, Mungu aliwaacha wawe katika ule ufahamu alioukataa – yaani aliachana na kuwashawishi. Mungu alimpa mwanadamu utashi wa bure na akauruhusu ufanye kazi. Baada ya hatua fulani, Mungu akaruhusu wale ambao wanamkataa yeye kuwaacha huru mbali na ushawishi wake. Hapo ndipo fahamu zao hufuata mkondo wa uharibifu usiozuiliwa na Mungu.
Taarifa kwamba Mungu aliwaacha wafuate tamaa na akili zao (1:24, 26, & 28) inaonesha kwamba watu hawa kiuhalisia walikuwa katika hali mbaya na walikuwa wamefanya kuchagua mambo ambayo haingewezekana kuyabadili tena (Linganisha na 2 Wathesalonike 2:10-12).
Akili za watu na mawazo yao vimedhurika na kuathirika kwa upotovu. Upotovu huwazuia watu wakati wa wanapotaka kufanya maamuzi ya kimaadili. Hii husababisha watu kukumbatia na kutetea tabia na vitendo vyao.
► Je, kuna mifano gani ya udhuru isiyo na maana ambayo watu hutumia kwa ajili ya dhambi zao?
(1:29-31) Katika aya hizi tunakutana na dhambi za kutisha. Mila na serikali vimezuia tabia hizi, lakini zipo ndani ya moyo wa dhambi wa mwanadamu. Kama vizuizi vya mila na serikali vingekuwa vimeondolewa, watu wengi ungekuta wangegeukia kwa haraka kwenye mambo ya ushenzi na ukatili.
Dhambi na maelezo ya wenye dhambi zilizoorodheshwa hapa hazina utofauti mkubwa kwa kila moja. Lakini hapa kuna baadhi ya mawazo makuu yaliyotajwa.
Udhalimu – ni neno la ujumla, ambalo pengine limebeba dhambi nyingine zote.
Uovu – pia ni neno la ujumla linalohusiana na matendo mabaya na tabia mbaya.
Tamaa – Neno linalotumika zaidi katika maandiko ya Kiyunani likirejelea ubinafsi wa ukatili. Linaelezea mtu anayefuatilia mambo yake mwenyewe tu, akiwa na nia ya kutaka kuharibu mambo ya wengine. Hii inahusisha pamoja na matumizi mabaya ya nafasi ya mamlaka kwa ajili ya kujipatia faida.
Ubaya - ni hali ya kuwa mbaya, tabia ya ukatili, uovu, au mwenendo usiofaa.
Husuda – Kutamani vitu vya watu wengine, pamoja na kuwa na chuki kwa wale watu walio na vitu vinavyotamanisha.
Uuaji – kuvunja sheria, kuua mtu kwa kupanga ambayo ni matokeo ya hali ya juu sana ya hasira na chuki.
Fitina – ugomvi, pengine kutokana na ushindani.
Hadaa – ulaghai au udanganyifu, unaweza ukawa chambo cha kuponza mtu aingie kwenye mtego.
Watu wa nia mbaya – kuwa na chuki, tayari kuumiza watu wengine pasipokuwa na sababu yeyote.
Wenye kusengenya– wenye kukashifu kwa siri.
Wenye kusingizia– tabia ya kudhuru hadhi yaw engine kwa kusema mabaya au mambo maovu juu yao.
Wenye kumchukia Mungu – wanamwona Mungu kama adui kwa sababu sheria zake zinawahukumu.
Wenye jeuri –Mtu aina hii ni mwenye kiburi na ukatili. Mtu mdhaifu aliye na tabia hii hupenda kuwatusi watu wengine ambao alistahili awaheshimu. Mtu aliye katika nguvu kubwa ya tabia hii ni mkatili kwa watu wengine na huchukua malipizi ya kupitilza kwa wale wanaoshindwa kuonyesha kwake ile heshima anayoitaka.
Kutakabari – Kiburi ni mtazamo wa mtu kujiinua mwenyewe. Ni shina la maovu yote kwa sababu humshawishi mtu kutawala maisha yake mwenyewe kinyume cha Muumba wake.
Wenye majivuno – Tabia ya kujiinua au kujikweza. Watu hawa ni wabinafsi. Kama ataonekana hapa kwamba anazo sifa nyingine, hujikuza kwa kujidanganya, kwa gharama ya watu wengine, na kuwaumiza wengine.
Wenye kutunga mabaya – Ni wabunifu kwenye mwendelezo wao wa uovu na mambo ya kuumiza
Wasiowatii wazazi wao – Uharibifu wa familia ni matokeo ya dhambi na unaelekeza kwenye kutengana zaidi kwa jamii. Tabia hii ya dhambi hujidhihirisha mapema kwa mtoto ambaye huasi kwa mamlaka yake ya mwanzo anayoijua.
Wasio na ufahamu – Wasio na ufahamu wa thamani ya maadili. Mtu huyu hashawishiki kwa sababu ambazo zimeendana na maadili. Hali hii siyo kukosa werevu, lakini ni ulemavu wa hisia ya kimaadili ambayo ni matokeo ya moyo wa uovu.
Wenye kuvunja maagano – Kukosa uaminifu. Kuachana na maadili na mamlaka, kuuchukia ukweli halisi ambao haufai kwao, na kufanya umimi au ubinafsi kuwa kipaumbele chao, huku wakiwa wanavunja ahadi zao.
Wasiopenda jamaa zao – Kinyume cha kuwa na kinga na silika ya upendo. Wanaweza wakaachana na familia zao na kufuata tamaa zao wenyewe. Silika za msingi za upendo zinaweza zikavurugwa. Wanaweza wakawanyanyapaa watu ambao ni tegemezi kwa ajili ya ulinzi wao.
Wasio na rehema – Bila huruma. Wanaweza wakaangalia mateso bila ya kuwa na huruma. Hawabadilishwi kutoka katika njia ya uovu kwa kuona mateso wanayopitia watu wengine
(1:32) Wanajua kabisa kwamba mambo haya ni mabaya. Wapagani au makafiri hawafuati kwa uaminifu hata ule ukweli ambao wanao. Wanajua kwamba wako chini ya hukumu. Siyo tu kwamba wanaifuata dhambi bali wanaidhinisha dhambi kwa watu wengine. Hamasa ya jamii hushuka kwa kiwango cha chini sana kiasi kwamba kiwango kingine cha mwenedo wa tabia hukubaliana na kuidhinisha uasherati.
Mtu ambaye anakubaliana na dhambi kabisa anajithibitisha mwnyewe kama mtenda dhambi na anawathibitisha wengine kama wenye dhambi. Anaweza akavutiwa na dhambi za watu wengine. Watu walipiga makofi kwa kushangilia mauaji kwenye viwanja vya Rumi. Watu wengi katika nyakati hizi wanafurahia kuangalia vurugu na vitendo vya ngono vya uasherati. Wanafurahia kuona watu wanaoendelea kushamiri kwenye viwango vikubwa vya dhambi wanazoweza kufanya.
"Ni vigumu sana kuelewa uharibifu wote kwa ukamilifu ambao dhambi inafanya kwenye hadhi ya mwanadamu. Mbali na udhaifu wa dhamira ambayo imezaa matunda na kelele za mihemuko kilichojiinua nyuma yake ni akili ambayo imefifia na kufanywa mtumwa kwenye mambo ya tamaa. Imefundishwa kutoa udhuru badala ya kutoa sababu. Inaamua kwanza, na kisha inafikiria baadaye.
Inaangalia mantiki, badala ya sababu. Mara nyingine inaelezea ukweli, lakini siyo katika hali yenye udhabiti. Haiwezi ikawa inayotegemewa… inanadi ukweli kutoka kwenye uongo, inamnadi Mungu kutokea kwenye ibada za sanamu, hekima kwa ajili ya upumbavu….”
- Wilbur Dayton
[2]Maandiko mengi ya Kiyunani hayana neno hili katika orodha hii.
[3]Maandiko mengi ya Kiyunani hayana neno hili katika orodha hii.
Je, kila asiyeokoka yuko hivyo?
Siyo kila mtu ameweza kufanya kwa ukamilifu dhambi hizi zote. Hata hivyo, ubinadamu uliodidimia umekuwa na tabia ya mwelekeo wa kufanya dhambi hizi zote, na inawezekana kila mtu akawa ametenda mojawapo ya dhambi hizi katika hali tofauti.
Seneca alikuwa mwanafalsafa wa Kirumi na afisa wa serikali ambaye aliishi wakati wa Paulo. Hakuwa Mkristo na alikuwa hana ufahamu na Biblia, lakini alifanya utafiti na akaona kwamba nguvu ya kila dhambi iko ndani ya kila mtu. Alisema, “Maovu yote yako ndani ya watu wote, ingawaje maovu yote kwa nje hayawezi kujulikana kwa kila mtu.”[1] Tunaweza tukaona kwamba ufafanuzi wa Paulo kuhusu asiyeokoka unatumika wakati wote na kwenye kila mila.
Serikali na taratibu za kijamii vinazuia tabia ya vitendo vingi vya uovu vya watu binafsi. Watu wengi huijaza mioyo yao na fahamu zao tamaa za dhambi ambazo hazijionyeshi kwa wazi kwa sababu wanataka kukubaliwa na watu wengine. Watu wana tabia za siri za dhambi zilizoorodheshwa katika kifungu hiki na wana hatia ya dhambi hizi katika mioyo yao.
[1]Imenukuliwa na F.F. Bruce, The Epistle to the Romans, in Tyndale Bible Commentaries (Grand Rapids: William B. Eerdmans Pub. Co., 1963), 87
Matumizi ya Kifungu
Kifungu hiki kimsingi ni ufafanuzi wa watu katika jamii ambao hawajawahi kuisikia injili. Walikataa kumjua Mungu ambaye umefunuliwa kwenye uumbaji na katika dhamira zao. Kisha, wakapata kitu kingine cha cha kuabudu ambacho kiliwawezesha kujihusisha na mambo ya tamaa ya mwili; na tamaa zao zikageuka kuwa upotofu. Kifungu hiki kinaelezea ni kwa nini watu hao wanahitaji injili.
Kifungu hiki ni muhimu kwa kila mtu, kwa sababu kinaorodhesha aina nyingi za matendo ya dhambi na kinaonesha kwamba dhambi hizi zinachukiwa na Mungu. Ni onyo pia kwamba dhambi zote zina tabia ya kumpeleka mtu mwenye dhambi mbali zaidi kwenye uovu zaidi. Watu wanaoisikia injili na kuikataa wako kwenye hatari ya kuingia kwenye mchakato unaofanana wa kupoteza ufahamu wa lililo jema na baya.
Kifungu hiki kinaelezea hali tunazoziona katika jamii zetu wenyewe, ingawaje injili imeshahubiriwa huko. Mila hupata nafasi ya kufanya baadhi ya dhambi zikubalike, ikiwa ni kupuuzia kipimo cha Mungu
Ushuhuda
Shmagi alizaliwa katika nchi ya Georgia, katika ulaya mashariki. Wazazi wake walikuwa hawaamini kuwa Mungu yupo, na hakuwahi kuhudhuria kanisani akiwa mtoto. Maana ya jina lake ni “mwepesi wa hasira,” na jina lake linaendana na tabia yake. Mara nyingi alijikuta katika matata akiwa kijana. Baada ya kupatikana kuwa ana hatia, alifungwa Uhurusi miaka miwili. Baadaye alifunguliwa na kurudi Georgia wakati wa Georgia ilipojitenga na Urusi.
Ini la Shmagi lilikuwa limeharibika vibaya kutokana na ulevi, daktari alimwambia kwamba asingeishi muda mrefu. Shmagi akawa hana furaha na akaanza kujisikia na kutafuta kumfahamu Mungu. Akawauliza marafiki wakristo kama wangeweza kumpeleka kanisani. Kwa mara ya kwanza, wakamwambia kanisani sio mahali panapomfaa. Ndipo wakamwambia hata hivyo angeweza kwenda, kama atawaahidi kuwa hatakuwa mtu anatafuta kubishana. Alienda na akaokoka akiwa na umri wa miaka 22. Maisha yake yalibadilishwa kabisa.
Shmagi akaponjwa ugonjwa wake wa ini. Hakuwa ametarajia kuoa kwa sababu ya ugonjwa wake, lakini Mungu kampa hatima mpya. Sasa ana mke na watoto mabinti watatu. Shmagi ni mchungaji na ana huduma ya kufundisha.
Maswali ya Mapitio Somo la 2
(1) Je, ni kwa njia gani watu hupokea ufunuo wa Msingi?
(2) Je, watu wote wanajuaje kuhusu Mungu hata bila Maandiko?
(3) Je, Ufunuo maalumu ni nini?
(4) Je, kuabudu sanamu ni nini?
(5) Taja njia mbili ambazo zinaleta madhara ya upotovu wa fikira kwa watu
Kazi ya kufanya Somo la 2
Andika ukurasa mmoja kuelezea hali ya jamii ambayo haijawahi kusikia injili lakini imemkataa Mungu. Wana ufahamu gani wa Mungu? Imetokea nini kwenye kufikiri kwao? Elezea uovu wao. Fafanua ni kwa nini siyo kila mmoja anaonesha aina moja ya kufanana ya uovu.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.