Sehemu ya 6 ya Warumi (12:1–15:7) ina maelekezo mengi ya vitendo kwa ajili ya maisha ya kanisa, huduma, mahusiano ya Kikristo, na mahusiano na serikali.
12:1-2 inatambulisha sehemu ya 6, ikituambia kwamba tunapaswa kujitoa kabisa kutumika kwa ajili ya Mungu. Hii inafuatia kutoka maelezo ya Paulo katika sura iliopita: Kwamba tuna deni kwa kila kitu kwa Mungu (11:35), na kwamba njia za Mungu ni za hekima kabisa (11:33).
Paulo anatumia mfano wa dhabihu iliyo hai (12:1). tumejitolea kabisa kama dhabihu inayopaswa kuuawa, lakini badala ya kufa, tunaishi kwa ajili ya Mungu. Hiyo ina maana kwamba msimamo huo ni lazima uzingatiwe. Siku hadi siku ni lazima tukatae kuondoka katika uaminifu wetu. Mfano wa dhabihu iliyo hai unasisitiza kujitoa kwetu kabisa kama sadaka. Hatuwezi tukahifadhi sehemu ya maisha yetu kwa ajili yetu wenyewe nje ya mapenzi ya Mungu. Hatuwezi kulinda baadhi ya matamanio au matarajio kutokana na madai ya kujitolea kabisa kwa Mungu.
Kujitolea huku binafsi kama dhabihu iliyo hai ni ibada ya kiroho, tofauti na mapokeo tu ya dini.[1]
Huduma ya kujitolea kabisa haitawezekana bila ya kuwepo na mabadiliko yaliyoelezwa katika 12:2. Ni lazima tubadilishwe kwa kufanywa upya nia zetu. Hatupaswi kuifuatisha dunia hii katika maadili yake, tabia zake, au maoni yake. Mtu anayetafakari kila swali katika mustakabali wa mapenzi makamilifu ya Mungu atatofautiana na dunia. Hatatoa ruhusa kwa matamanio yeyote ya dhambi; hawezi akayavumilia kana kwamba ni mambo ya kawaida tu.
Tambua kwamba mwili unapaswa uwe mtakatifu. Dhambi siyo kipengele muhimu cha mwili ambacho hakiwezi kutakaswa na Mungu. Mwili siyo wenye kuwa na dhambi wenyewe na hauwezi kutenda dhambi pasipokuwa na mapenzi binafsi ya kufanya hivyo lakini unaweza kutumiwa katika kutenda dhambi.
Aya za kutoka 12:1-15:7 zinaelezea jinsi ya kuishi maisha ya kujitolea kabisa na yaliyobadilishwa.
► Mwanafunzi atapaswa kusoma Warumi 12 kwa ajili ya kikundi.
[1]Ona maelezo ya kumbukumbu yaliyoko katika Warumi 1:9.
Kifungu cha kujifunza – Warumi Sehemu ya 6, kifungu cha 1
Maelezo ya aya kwa aya
(12:3) Neema iliyotolewa kwa Paulo inarejaea mamlaka yake ya kitume na kipawa cha ufunuo.
Tunapaswa kunyenyekea kwa sababu kila tulicho nacho tumepewa na Mungu. Mtu aliye na karama za kiroho anapaswa awe mnyenyekevu akitambua kwamba karama hizo zinatoka kwa Mungu bila malipo na ziko kwa kusudi la kutumikia watu wengine.
(12:4-5) Kama vile katika mwili mmoja, tunawahitaji wengine na tuna wajibu wa kuwahudumia watu wengine. Mfano wa mwili unaelezwa katika 1 Wakorintho 12:12-26.
(12:6-8) Aya hizi zinataja huduma mbalimbali. Kila mtu aliyeamini anapaswa kufuata huduma aliyoitiwa na aliyozawadiwa. Kama mtu hana unyenyekevu wa neema, anaweza akatumia muda na nguvu zake nyingi kwa njia iliyo mbaya, (labda akitafuta kupata kibali cha mwanadamu), na akashindwa katika wito wake halisi.
Watu walio na karama za kiroho wanaonywa wazitumie vizuri. Kwa mfano, mtoaji atoe bila vikwazo, na siyo kwa kusudi la kujipatia heshima yeye mwenyewe. Mwenye kusimamia lazima awe na bidii – makini kwenye mambo ya msingi na yanayotegemewa wakati wote. Mtu anayesaidia watu wengine katika mahitaji yao hapaswi kufanya hivyo kwa kiburi au mtazamo wa chuki ambao humdhalilisha mpokeaji.► Je, ni kwa jinsi gani Wakristo wanatumia karama zao za kiroho tofauti na jinsi watu wa dunia wanavyotumia uwezo wao?
Kifungu cha kujifunza – Warumi Sehemu ya 6, Kifungu cha 2
Maelezo ay Aya-kwa-Aya
(12:9) Pendo lisiwe na unafiki bali liwe katika ukweli na uaminifu. Lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema. Kuongezeka kwa upendo kumeunganishwa na kuboreka kwa ufahamu kuhusu ni jambo gani lililo jema (Wafilipi 1:9-10).
(12:10) Kanisa ni familia ya Mungu, ikiwa na ndugu wengi. Tunapaswa tuwe tayari kwa heshima kwenda kutembelea wengine badala ya sisi wenyewe tu.
(12:11) Tusiwe walegevu kwenye majukumu yetu. Mkristo anapaswa awe mfano wa kuigwa kwenye maadili mazuri ya kazi. Hapaswi awe na muda mwingi wa kupoteza kama anaishi kwenye kusudi la Mungu. Anapaswa awajibikie majukumu kama anayefanya kazi kwa ajili ya Mungu (Waefeso 6:6-7).
(12:12) Furaha yetu haitegemei hali tulizo nazo, kwa sababu tunayo matumaini kwa ajili ya uzima wa milele. Kuwa mvumilivu maana yake ni kuvumilia katika imani. Mtu ni lazima awe na tabia isiyobadilika ya kumtegemea Mungu, na awe tayari kuomba wakati wote.
(12:13) Kusaidia watu wengine walioamini katika haja za mahitaji yao ya kimwili. Ukarimu maana yake ni kukutana na mahitaji ya watu wengine kwa ajili ya chakula na malazi.
(12:14) Usiwatendee watu wanaokuudhi kama wanavyostahili, lakini watendee kama ambavyo Kristo angewatendea. Kuwafanyia watu kile kitu ambacho unafikiri ndicho wanachostahili ni kuhukumu kwa kiwango kikubwa, ambalo ni jukumu la Mungu lililohifadhiwa.
(12:15) Kuwa tayari kushiriki huzuni pamoja na wanaolia, na vivyo hivyo kushiriki furaha pamoja na wengine wafurahio.
(12:16) Usiwe ni mtu wa kusumbuka na vyeo. Tusiwe na upendeleo kwa watu wa daraja la juu la mafanikio. Kuwa mwenye heshima hata kwa watu ambao ni maskini. Usitafute njia nyingine za kujiweka juu ya watu wengine.
(12:17) Siyo jambo sahihi kumwumiza mtu mwingine kisa tu kwa sababu amekuumiza wewe. Hatujaitwa kwa ajili ya kuwapa watu adhabu au kulipa uovu kwa uovu bali kusamehe.
Onesha kwamba wewe ni mwaminifu. Kama unataka uheshimiwe, dumisha sera ambazo zinaonyesha uaminifu kwa kila mtu kuona. Haitoshi wewe na Mungu kujua kwamba wewe ni mwaminifu. Ni rahisi zaidi kudumisha sifa nzuri kuliko kuijenga upya baada ya kuwa imeharibika.
(12:18) Kwa kiwango chochote kile ambacho kitakutegemea wewe, ishi kwa amani na kila mtu. Amani inapokuwa mahali pake halisi inakuwa ni uhusiano wenye mpangilio mzuri. Wakati mwingine amani inahitaji msamaha, hata kwa kosa lisilo la kukusudia. Mara nyingine inahitajika upendo kukabiliana na mtenda maovu, ili kwamba kile kinachozuia uhusiano wako kiweze kutatulika. Aidha kama utakataa kuomba msamaha au kukabiliana inapokuwa inahitajika, maana yake haufanyi kile kinachowezekana katika kudumisha amani.
(12:19) Msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu. Kama mtu anataka awe ndiye mlipiza kisasi, inaonesha hajaamini kwamba Mungu anaifanya kazi yake kwa njia sahihi.
(12:20) Fanya mambo yaliyo mema kwa watu wengine, kuliko kujaribu kuwafanyia mambo wanayostahili kutoka na yale waliyokutendea. Kupalia makaa ya moto kichwani haimaanishi ni kulipiza kisasi kwa njia ya hila zaidi, kwa kuwa mtazamo huo utachanganya jambo kuu lililoko kwenye aya hii. Kwa kufanya hivyo, itawezekana ikawa ni ishara itakayoweza kuuyeyusha moyo na mwenendo wa huyu mtu.
(12:21) Usishindwe na ubaya hata ukatoa nafasi ya kushindwa kiroho. Hata hivyo, usitake kushinda ubaya kwa mabaya, bali ushinde ubaya kwa wema. Kuwa na uchungu na kutaka kushinda kwa njia ya ubaya ni hali ya kushindwa kiroho, hata kama utashinda katika mgogoro huo.
► Jaribu kufikiria kuhusu jinsi ambavyo mtu hataweza kufanya vizuri katika maelekezo haya kama hajajitoa kabisa kwa Mungu. Je, ni kitu gani katika maisha yako unategemea kiwe na mabadiliko kutokana na maelekezo haya?
Kutafsiri Barua za Mtume
Barua za Paulo ziliandikwa kukidhi hali maalumu zilizokuwepo: Kwa kawaida hali yenyewe inaweza ikawa ni aina fulani ya tabia ambayo ilihitaji irekebishwe, au kosa la mafundisho ya imani ambalo lilihitaji maboresho yaliyo sahihi, au kutokuelewana ambako kulihitaji mwanga zaidi."[1] Barua zenyewe haziko katika mfumo wa teolojia inayofuata utaratibu fulani, bali teolojia iliyotokana na kukabiliana na hitaji, Teolojia hii ni ya vitendo kutokea mwanzo. Haijaanzishwa na kutengwa ikae upweke kutoka katika maisha halisi.
Nyaraka za Agano Jipya hazikuwa ni maandishi yaliyoandikwa kwa ajili ya jamii yote kwa ujumla wake, bado yalikusudiwa kwa zaidi ya wapokeaji mmoja na kwa zaidi ya maombi ya papo hapo. Paulo aliwaamba Wakolosai kwamba wanapaswa wabadilishane hizo nyaraka ili zisomwe pia na Walaodikia na hii iwe ni kwa kila waraka uliopokelewa kutoka kwake (Wakolosai 4:16). Mapema kabisa kanisa lilikuwa limeanza kukusanya nyaraka za Paulo na kuzisambaza kwa pamoja. Kwa hiyo, tunajua kwamba waliziona hizo nyaraka zikiwa zinafaa kutumika kwa kanisa katika maeneo yote na kwa nyakati zote.
Ingawaje kuna pengo la muda na utamaduni lililopo kati yetu sisi na wapokeaji wa mwanzo, nyaraka hizi ziliandikwa kwa ajili ya Wakristo wa Agano Jipya waliokuwa wanakabiliwa na matatizo yanayofanana na ya kwetu tuliyo nayo. Kwa hiyo, nyaraka za Paulo ni rahisi kutumika kwenye kanisa la sasa kuliko aina nyingine zozote za maandishi au fasihi kutoka katika Maandiko. Nyaraka hizi hazikuandikwa mahususi kwa ajili ya taifa la Kiyahudi, au hazikuelekezwa kwa watu waliokuwa chini ya sheria ya Agano la Kale.
Hali ya asili ya mwanzo ya uandishi inampa mtafsiri mahali pa kuanzia kwa ajili ya matumizi ya wakati huu wa sasa. Kanuni ya kutafsiri ni kwamba tunaweza tukaelewa maandishi vizuri zaidi kama tutamjua ni nani mwandishi, nani alipokea, na kwa nini kiliandikwa. Nyaraka zinampa mtu anayetafsiri faida ya kujua utambulisho wa mwandishi na wapokeaji wake.
Kitabu cha Warumi ndicho kilicho mahususi na rasmi zaidi katika maandishi ya Paulo. Kinafuata mtiririko uliopangika. Takribani kitabu chote kiko katika tasnifu ya kiteolojia. (Maandiko au makala zenye kuhusu mada moja.) Paulo hakutaja makosa maalumu katika kanisa la Rumi. Hakuzungumzia kuhusu hali zozote maalumu, kama alivyofanya kwenye nyaraka zake kwa makanisa mengine aliyokuwa ameyaanzisha na kuyatembelea.
[1]Gordon Fee and Douglas Stuart, How to Read the Bible for All Its Worth, (Grand Rapids, MI: Zondervan, 1993) 48.
Kifungu cha kujifunza – Warumi Sehemu ya 6, Kifungu cha 3
Jambo Kuu katika Warumi 13:1-7
Watu walioamini wanapaswa wazitii serikali za kiraia kwa sababu serikali zimewekwa na Mungu.
Maelezo kwa kiongozi wa darasa: Pengine kutakuwepo na mjadala zaidi na kutokukubaliana kadri kikundi kitakapokuwa kwenye mafunzo ya kifungu kitakachofuata. Unatakiwa awatake kikundi chako kiruhusu kifungu kisahihishe maoni yao.
► Mwanafunzi atapaswa kusoma Warumi 13:1-7 kwa ajili ya kikundi.
Maelezo ya Aya-kwa-Aya
(13:1-2) Mungu alianzisha serikali. Hiyo haina maana kwamba kila mtawala ni mwenye haki, lakini Mungu anataka mamlaka ya binadamu ianzishwe. Kukataa kuwa chini ya mamlaka ya binadamu ni kumwasi Mungu. Kama vile ambavyo kiukweli tunakuwa hatumpendi Mungu pale tunapokuwa humpendi ndugu tunayemwona, vivyo hivyo hatuwezi tukadai kwamba tuko chini ya mamlaka ya Mungu wakati huku tunakataa kujiweka chini ya mamlaka ya binadamu inayoonekana. Mkristo hapaswi kuwachukulia vibaya watawala wa kisheria kwa kuwavunjia heshima.
(13:3-4) Moja ya kusudi la serikali ni kuwaadhibu watenda maovu. Wakati serikali inapofanya kazi yake kwa ukamilifu, watenda maovu hupata hofu. Katika mazingira ya kawaida Wakristo hawapaswi kuleta mgogoro na serikali kwa sababu sifa ya Ukristo inamfanya Mkristo awe raia mwema. Hata hivyo, mara nyingi katika historia, watawala wamekuwa wakijaribu kudai kupewa heshima ambayo anastahiki Mungu peke yake, na kisha hugeuka kuwa watesaji wa Wakristo.
Serikali ambayo inafanya kazi vizuri na katika misingi ya haki na usawa, iko sawasawa na mamlaka ya Mungu. Aya ya 4 inatuambia kwamba serikali ina mamlaka kutoka kwa Mungu katika kuimarisha sheria ikibidi hata kama ni kuwanyonga watenda maovu.
Wakristo katika baadhi ya Wamataifa duniani wanaamini kwamba ni makosa kwao kuwa na nafasi yeyote ya uongozi katika serikali, hasa nafasi ambayo itaweza kuhitaji wao kutumia nguvu. Wakristo wengi walio na imani hiyo wanaishi katika nchi ambazo serikali zimewatesa na kuwauwa Wakristo na zimesheheni watawala wala rushwa. Hata hivyo, kama serikali inafanya kazi vizuri na katika misingi ya haki na usawa, siyo kosa kwa Mkristo kutumikia nafasi katika serikali kwa sababu serikali imethibitishwa na Mungu.
(13:5) Mkristo anapaswa aitii mamlaka iliyo kuu siyo kwa sababu ya kuogopa ghadhabu ya serikali, bali kwa ajili ya dhamiri nyeupe. Kufanya uasi dhidi ya serikali au kukataa kutii sheria zake ni sawa na kukataa jukumu la serikali. Siyo maamuzi yote yatakayoweza kuamuliwa na watu binafsi ikibidi kuwepo na serikali ya aina yeyote. Uhuru wa mtu binafsi ni lazima uwe chini ya mamlaka ya serikali ambayo inapaswa ilinde haki za watu binafsi, hata kama siku zote hatukubaliani na jinsi ulinzi wa uhuru wetu unavyofanyika.
(13:6-7) Mkristo anapaswa kulipa kodi halali za serikali. Fuata njia za kitamaduni za kuonyesha heshima.
Kifungu cha kujifunza – Warumi Sehemu ya 6, Kifungu cha 4
Jambo Kuu katika Warumi 13:8-10
Upendo hukamilisha sheria kwa sababu inamhamasisha mtu aliyeamini kufanya kile kilicho cha haki kwa ajili ya watu wengine.
Aya hizi zinathibitisha kwamba sheria haziwezekani zikawa hazina maana kwa mtu aliyeamini. Mtu aliyeamini hutimiza sheria, kwani kwa neema anaweza kuwa na upendo unaoelezwa hapa. Neema haiko kwa ajili ya kufunika uvunjaji wa sheria. Neema inachanganya kwa pamoja kazi ya Mungu ndani yetu ili kukamilisha mapenzi yake ndani yetu.
► Mwanafunzi atapaswa kusoma Warumi 13: 8-10 kwa ajili ya kikundi.
Maelezo ya Aya-kwa-Aya
(13:8) Kuwiwa deni katika mantiki hii ni kushindwa kutoa kile ambacho unadaiwa na mtu mwingine. Baadhi ya aina za majukumu zimeorodheshwa kwenye aya iliyotangulia. Siyo kosa kukopa na kulipa katika muda muafaka, kama hiyo ndiyo njia inavyoonekana inafaa katika kukamilisha majukumu yaliyopo. Tunaagizwa, kama ilivyo katika aya ya 7, kumlipa kila mtu haki yake kadri tunavyowiwa kutoka kwetu.
► Je, kunakuwepo na matokeo gani wakati Mkristo anaposhindwa kulipa deni alilokopa?
(13:9-10) Kama kweli unampenda mtu mwingine kama unavyojipenda mwenyewe, hutaweza kumwibia, kumdanganya, kutamani kile alicho nacho, au kumvurugia ndoa yake. Urafiki na upendo tu wa kawaida, kama vile ulivyo wa kawaida katika dunia hii, siku zote haviwezi kuzuia matendo haya maovu; lakini upendo wa Kristo ndani yetu utatuzuia sisi katika kutenda maovu hata kwa wageni, kwa wale wanaotuudhi, au kwa wale wanaoweza kutufanyia maovu dhidi yetu.
Tamaduni nyingi na madhehebu hufundisha kwamba tunadaiwa kiasi cha upendo, labda katika familia zetu na jamii zetu katika kabila. Lakini wanafikiri kwamba kwa wanadamu wengine wote waliobakia, hakuna upendo wa aina yeyote unaodaiwa. Wanaweza wakaona ni ruhusa kuwaibia wageni au waajiri wao na kuwa wakatili kwa watu wasiowajua.
Kristo anatuagiza sisi kuuendeleza upendo wetu kwa kila mtu tunayejikuta tuko naye.
Katika Luka 10:25-37, ili kuonyesha mfano wa jinsi ya kumpenda jirani yako, Yesu alielezea mfano wa Msamaria aliyemsaidia Myahudi aliyeumizwa.
Kifungu cha kujifunza – Warumi Sehemu ya 6, Kifungu cha 5
► Mwanafunzi atapaswa kusoma Warumi 13:11-14 kwa ajili ya kikundi.
Maelezo ay Aya-kwa-Aya
(13:11) Wokovu kwenye aya hii ni marejeo ya wokovu wa mwisho wakati wa kuja kwake Kristo. Hatupaswi tuishi kana kwamba dunia hii itadumu milele. Tunatakiwa tuishi kama watu wanaotegemea kwamba mambo yaliyopo yatapita upesi sana.
(13:12) Usiku ni msemo ambao unaelezea wakati unaoelekea kwenye kuja kwa Kristo (Ona pia 2 Petro 1:19). Giza kwa mujibu wa Agano jipya ni kuhusika katika matendo ya dhambi (Ona pia 1 Wathesalonike 5:4-8 na Waefeso 5:11-14).
(13:13) Hapa maisha ya mwenye dhambi mzembe yanaelezwa. Huyu ni mtu ambaye hajali lolote kuhusu wakati ujao, na zaidi sana hafikirii jambo lolote kuhusiana na umilele. Anaishi maisha ya kujifurahisha bila kujali mambo ya maadili. Maisha ya Mkristo ni kinyume kabisa na mambo hayo.
(13:14) Usiruhusu mambo ya tamaa mbaya yakuingilie. Usitumie asili yako ya ubinadamu kama kigezo cha kuomba radhi kwa ajili ya kutenda dhambi. Ishi kwenye maisha ya nuru na usiruhusu chochote kipenyeze ndani yako ambacho kitakuaibisha.
Kifungu cha Kujifunza – Warumi Sehemu ya 6, Kifungu cha 5
Wakati wote kutakuwa na masuala ya muhimu ambayo waamini watatofautiana. Warumi sura ya 14 inatoa maelekezo kuhusu jinsi wakrsito wanaotofautiana katika baadhi ya mambo wanayoamini na wanayoyaishi lakini bado wanatakiwa kupendana na kuheshimiana, kuabudu na kutumika pamoja.
► Mwanafunzi anapaswa kusoma Warumi 14:1-23 kwa ajili ya kikundi.
Maelezo ay Aya-kwa-Aya
(14:1) Ndugu mdhaifu ni yule anayejihisi kuwa na hatia katika kitendo ambacho kiuhalisisia hakijawahi kukatazwa na Mungu (ona 1 Wakorintho 8:7-12). Ndugu aliye na nguvu ni yule anayafanya kitendo bila kujihisi kuwa na hatia kwa sababu anajua kwamba kitendo anachokifanya kiuhalisia hakihusiki kabisa katika kukosa utii kwa Mungu.
(14:2-3) Sheria ya Kiyahudi ilikuwa imeunganishwa na masharti yaliyohusiana na mambo ya vyakula. Katika kanisa kulikuwepo na Wakristo wengi wa Kiyahudi na Wamataifa ambao walikuwa wameshajifunza kuhusu sheria za Kiyahudi. Mtu aliyekuwa anajisikia yuko huru kutokana na vizuizi vya aina yeyote vilvyohusiana na mambo ya vyakula alikuwa anaweza kushawishika kumnyanyasa mtu mwingine ambaye alijihisi hana uhuru wa kula aina fulani ya chakula na anajisikia kimekatazwa. Yule anayejaribu kufuata sheria kuhusu mambo ya vyakula anaweza akashawishika kuwahukumu wasiofungamana na sheria hiyo kama wenye dhambi.
(14:4) Mungu atawahukumu watumishi wake mwenyewe na kuwapatia ile neema wanayohitaji. Usiwahukumu watu wengine kwa mambo ambayo hayako wazi kwenye Maandiko.
Duniani kote kuna tofauti kati ya watu walioamini kuhusiana na mambo kama ya ubatizo, jinsi ya kuhudumia Meza ya Bwana, chaguo la tafsiri ya Biblia, mavazi, na sherehe. Ndani ya mwili wa Kristo, tunapaswa kudumisha umoja wa Kikristo lakini tusitazamie kila mtu kuwa sawa na mwenzake. Dhima yetu inapaswa iwe: “Katika mambo ya msingi, umoja; katika mambo yasiyokuwa ya msingi, uhuru; lakini katika mambo yote, upendo!”
(14:5-6) Kulikuwa na siku nyingi za kuadhimisha sherehe za Kiyahudi, zikiambatana na tamaduni maalumu kwa kila moja. Kuhusiana na siku ya Sabato hili pia lilikuwa ni suala lililoleta utata. Badala yake kanisa lilianza kukutana na kuabudu katika Siku ya Bwana (Mdo 20:7; 1 Kor 16:2; Ufu 1:10) na baadaye jumapili ikazoeleka kuwa kama sabato ya kikristo. Kanuni ya mapumziko kwenye siku ya Sabato hata sasa ina faida zake ambazo ni wajibu wetu tuzitunze, kwa kuwa ni kanuni ya uumbaji na siyo tu utamaduni ulioanzishwa wakati ilipotolewa sheria ya Musa.
"…Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe” (14:5) inaonesha kwamba maoni ya uhakika ni ya umuhimu. Mtu hapaswi kuwa na mashska katika yale mambo anayoyaamini. Uvumilivu wa maoni au mawazo ya watu wengine haimaanishi kwamba hatujui maoni yetu ni yapi au kwamba tunapuuzia ushahidi na mantiki.
(14:7-9) Hakuna mtu aishiye kwa nafsi yake mwenyewe. Kila aina ya maisha inapaswa imwadhimishe Kristo. Kifo cha Kristo na kufufuka kwake kilitukomboa sisi, na sisi ni mali yake.
(14:10-12) Sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu. Kwa hiyo, maoni yetu kuhusiana na mtu mwingine hayana umuhimu wowote.
(14:13-15) Ni jambo muhimu sana kwetu kwamba mtu asitie kitu cha kumkwaza ndugu au cha kumwangusha. Kwa Mkristo, hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake kwa sababu kila kitu ni mali ya Mungu. Lakini kwake yeye akionaye kitu kuwa najisi, kwake huyo kitu kile ni najisi na kama ataamua kukitumia, atakuwa ametenda dhambi kwa sababu amechagua kufanya jambo baya. Tunamfanya mtu ajikwae ikiwa tunamshawishi afanye jambo analofikiri si sahihi (Andiko lingine kuhusiana na suala hili liko katika 1 Wakorintho 8).
(14:16) Mkristo anaweza kuwa na mafundisho mazuri ya imani na bado akaleta madhara kwa sababu ya kutojali ushawishi wake dhidi ya watu wengine.
(14:17) Ukristo hauna aidha sheria au masharti kuhusiana na mfumo wa maisha au uhuru wake. Ukristo ni ushindi wa kiroho na maisha ndani ya Roho Mtakatifu.
(14:18-19) Mungu huwa anafurahia wakati tunapokabidhi kila kitu tunachofanya kwa Kristo na kufanya lolote linalowezekana katika kuwaimarisha watu wengine.
(14:20-23) Kila kitu ni mali ya Mungu, na mtu yeyote anayekumbuka hivyo anaweza kuwa huru. Hata hivyo, kama mtu akitenda jambo fulani analolifikiria kwamba ni baya, anatenda dhambi kwa kuchagua kufanya hivyo. Ndugu anayejisikia yuko huru anapaswa awe na mpaka wa uhuru wake ili kujizuia asisababishe watu wengine kuanguka.
Hakuna maelekezo yeyote yaliyotolewa kwa ajili ya ndugu aliye dhaifu, isipokuwa tu kwamba hapaswi kumhukumu mtu mwingine aliye na uhuru wake zaidi. Mtu mdhaifu amefungwa na dhamira yake na hawezi akabadili tabia yake, lakini ndugu aliye na nguvu ana chaguo.
Inawezekana kukawepo na majadiliano zaidi wakati wa kushughulikia kukamilisha kifungu kilichotangulia, lakini kuna baadhi ya maswali ya kutafakari yafuatayo:
Kuna mambo gani ambayo kanisa letu linawaachia washirika wake waamue kila mtu kwa binafsi yake?
Je, tunaona tofauti gani kwa waamini wengine kuhusu kile ambacho tulipaswa kuonesha kuvumiliana zaidi?
Je, tunawezaje kuwa waaminifu katika kutumia kanuni za kifungu hiki kwenye maoni yetu na katika kushirikiana na watu wengine?
Kuwatambua wanaotetea ufuatwaji wa sheria za Kiyahudi.
Wayahudi hawkuwa tu ni wafuasi wa Uyahudi, ambayo ni dini ya wayahudi. Hawa ni Wayahudi waliojinadi kuwa wao ni Wakristo lakini wakafikiri kwamba Wakristo ni lazima pia watekeleze matakwa ya dini ya Uyahudi. Halikuwa ni tatizo kwa Wayahudi waliokuwa wameokoka kuendelea katika kutumikia mambo ya Uyahudi. Wengi walifanya hivyo, hasa wakati wa kizazi cha kwanza cha kanisa la Agano Jipya. Tatizo lilikuwa ni wakati Wayahudi hao walipojinadi kwamba wameokoka wakati hawakuwa wanaielewa injili ya neema.
Wayahudi waliokuwa ndani ya kanisa walifikiri kwamba ilikuwa ni muhimu kwa mtu wa Wamataifa aliyeokoka akubaliane na masharti yote ya dini ya Kiyahudi, ikiwemo Kutahiriwa, ili aweze kukamilika kuwa ameokoka. Hawakuhubiri injili kwa watu waliopotea; bali walihubiri mambo mengine kwa wengine waliookoka wakisababisha mtafaruku na mgawanyiko. “Ushindi” wao mkubwa tunauona katika kitabu cha Wagalatia, ambapo walipotosha kanisa lote. Barua ya Paulo kwa Wagalatia ilikusudiwa kuwarejesha wote kwenye ukweli wa injili.
Suala hili la sheria za kiyahudi liliwakilishwa kwenye baraza la uongozi la kanisa, kama ilivyonukuliwa katika Matendo 15. Mitume walitambua kwamba kufuata njia ya Wayahudi waliokuwa ndani ya kanisa ingekuwa ni kuikana injili ya neema ambayo ilikuwa inatolewa kwa kiwango sawa kwa Wamataifa. Maamuzi ya baraza la uongozi yalikuwa ni kuwasahihisha waamini wa kweli ambao kwa ukweli walikuwa wamepotoshwa na hawakuweza kuwazuia wale wote waliokuwa na malengo potofu. Paulo aliwachukulia Wayahudi waliokuwa ndani ya kanisa kama maadui wa injili.
Warumi 14:1-15:12 inahusika na ukweli wa injili ambao Paulo alikuwa ameuelezea kwenye barua yake yote kuhusiana na suala hili la sheria za wayahudi. Watu waliokuwa wameamini hawakupaswa kumhukumu mtu mwingine kutokana na kujishughulisha katika kuzingatia kanuni za kidini za Kiyahudi. Sehemu hiyo ilimalizika kwa msisitizo kwamba injili ni kwa ajili ya dunia nzima
Vifungu vingine kwenye somo hili ni pamoja na Warumi 4; Matendo 15; Wagalatia 2, 3, 5; na Wakolosai 2:11-23.
Kifungu cha Kujifunza – Warumi Sehemu ya 6, kifungu cha 6
Mwendelezo wa maelezo ya Aya-kwa-Aya
(15:1-4) Wale wenye nguvu, ambao wanajiona huru, wanapaswa kuwa tayari kuacha baadhi ya haki zao ili kuwasaidia wale walio dhaifu katika imani na ambao hawajihisi huru kutokana na vizuizi vya ziada.
(15:5-7) Aya hizi zinakamilisha kifungu. Lengo ni umoja wa Kikristo. Upendo wa Kristo ni mfano wetu.
Simulizi inayohusu Umoja, Uamsho na Umisheni.
Katika mwaka a 1722 mmiliki mmoja wa ardhi raia wa Ujerumani aliyekuwa akiitwa Zinzendorf aliwaalika waamini wa Kimoraviani waliokuwa kwenye mateso wahamie kwenye eneo lake la makazina akajenga hapo himaya yake. Hatimaye, watu kwa mamia kadhaa walikuwepo kwenye ile jumuiya. Walijitahidi kupambana na mgawanyiko wa mafundisho kadhaa ya kiimani na taratibu za kuabudu: lakini katika mwaka wa 1727 wakaanzisha “Makubaliano ya Udugu” (ambayo kwa sasa yanaitwa “Agano la Wamoraviani kwa ajili ya Maisha ya Kikristo”) ili kusaidia kuanzisha umoja.
Katika mwaka huo huo, wakaanza kufanya uamsho. Walikuwa na mikusanyiko ya maombi ya usiku na ibada za kuabudu za masaa marefu wakiwa na hisia isiyokuwa ya kawaida ya uwepo wa Mungu, ikiwa ni pamoja na mzungumzaji kulala chini kwa hofu ya Mungu. Wakati wa ibada ya kula sakramenti ya Bwana, Roho Mtakatifu alitembea katikati ya watu katika njia ambayo baadaye katika siku hiyo Zinzendorf alikuja kuona kama ni siku ya Pentekoste ya kufanywa Upya Kanisa la Moraviani. Watu waliokuwa wamegawanyika waliunganishwa tena kwa hisia kuu, na Zinzendorf akongoza sala ya kukiri mafarakano ndani ya kusanyiko. Walianza mkesha wa maombi, waamini mbalimbali wakipeana zamu, na wakaendelea hivyo kwa miaka 100.
Jumuiya ya Kimoraviani ikatokea kuwa ni kusanyiko kubwa sana la kupeleka wamisionari kwa muda wote. Kuanzia mwaka 1733-1742, wamisionari 70 walitumwa kutoka katika jumuiya ya watu 600. Wengi wao walikufa kutokana na kupewa mateso na hali nyinginezo ngumu. Hadi kufikia mwaka 1760, baada ya miaka 28, wamisionari 226 walikuwa wameshatumwa; na idadi ya Wamoraviani duniani ikaongezeka kwa maelfu.
Maswali ya Mapitio Somo la 11
(1) Elezea mfano wa dhabihu iliyo hai.
(2) Je, nini lazima itokee kwetu ili tuweze kuwa waminifu kwa Mungu?
(3) Je, ni kwa nini inatupasa kuwa wanyenyekevu?
(4) Elezea msemo wa ndugu aliye dhaifu na ndugu aliye na nguvu.
(5) Nani walikuwa wanaotetea ufuatwaji wa sheria za Kiyahudi?
Kazi ya kufanya Somo la 11
(1) Andika ukurasa mmoja ukatumia baadhi ya maelekezo ya vitendo yanayopatikana katika Warumi 12:1–15:7 kwa Wakristo wa leo.
(2) Jiandae kwa ajili ya mtihani wa mwisho kwa kujifunza orodha ya maswali yaliyoko kwenye Kiambatisho “A” cha kozi hii. Ni lazima ufanye mtihani huo bila ya kupata msaada kutoka kwa mtu mwingine yeyote na bila ya kuangalia kwenye kumbukumbu zilizoandikwa.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.