Hata kama itatolewa dhabihu, mwenye dhambi hawezi kuwa na matumaini bila ya neema ya Mungu kuwa inafanya kazi ndani ya moyo wake. Mwenye dhambi huwa amekufa kiroho katika dhambi yake, akiwa anatawaliwa na tamaa mbaya, na akiwa chini ya utawala wa shetani. (Wafeso 2:1-3). Hana uwezo wowote wa kubadilisha mwenendo wake (Warumi 7:18-19). Je, ni kwa jinsi gani anaweza kukubaliana na injili kwa toba na imani?
Wanateolojia wamejaribu kuelezea jinsi neema ya Mungu inavyotenda kazi kwenye hali ya uenye dhambi ya mwanadamu.
John Calvin
John Calvin aliamini kwamba kwa sababu mwanadamu amepotoka au amekengeuka kabisa hawezi akawa na chaguo la kuwajibika kwa Mungu.[1] Kwa hiyo, Mungu ndiye anayechagua ni nani atakayeokoka na ni nani ambaye hataokoka. Kwa kuwa Mungu huchagua watu wachache tu kwa ajili ya kuokoka, upatanisho unatolewa kwa ajili yao peke yao na siyo kwa watu wote. Watu hawa hawawezi kuchagua. Kwa neema ambayo haiwezi kuzuiliwa, Mungu huwafanya waweze kutubu na kuamini. Kamwe hawawezi wakaanguka na kutoka kwenye wokovu kwa sababu mapenzi yao yako chini ya uongozi wa Mungu. Hii ilikuwa ni dhana ya John Calvin kuhusiana na mamlaka aliyo nayo Mungu.
Calvin hakuamini kwamba neema iokoayo inapatikana kwa ajili ya kila mtu. Aliamini kwamba hakuna mtu yeyote anayeweza kutubu na kuamini bila ya neema maalumu, na aliamini kwamba neema hiyo haikutolewa kwa watu walio wengi.
Calvin aliamini kwamba mtu hawezi akafanya jambo lolote zuri, kama vile kutunza ahadi, kuipenda familia yake, bila ya kupata msaada wa Mungu. Aliamini kwamba Mungu huwapa watu wote neema inayowawezesha kufanya mambo mazuri. Anaiita neema hii “neema ya kawaida.” Hakuamini kwamba neema ya kawaida inaweza kumpeleka mtu kwenye kuokoka.
John Wesley alikuwa na mtazamo tofauti kuhusiana na neema ya Mungu. Aliona kwamba Biblia kwa mara zote inawaita watu kuwajibika kwa Mungu. Kwa sababu ya hiyo, aliamini kwamba mwanadamu ana uweza wa kuchagua. Aliamini kama Calvin kwamba mwanadamu amepotoka na hawezi kupokea injili bila ya msaada wa Mungu, lakini aliamini kwamba Mungu hutoa huo msaada kwa kila mtu. Aliamini kwamba Mungu huwapa watu nia na uwezo wa kuwajibika, lakini hawalazimishi kuokolewa. Mungu hufanya chaguo la mwanadamu liwe kitu kinachowezekana. Hii ni neema ya mwanzo inayokuja kwa kila mtu. Wanateolojia wameiita “neema ya awali,” ikimaanisha kwamba ni ”neema inayokuja kabla.”
Neema ya Mungu huingia hadi ndani ya moyo wa mwenye dhambi, ikimhukumu kutokana na dhambi zake na ikimwonyesha kwamba yeye mwenyewe ajilaumu kwa kutengana kwake na Mungu. Neema ya Mungu husababisha awe na nia ya msamaha na anampa uwezo wa kumwitikia Mungu.
Bila ya neema, mwenye dhambi hawezi hata kuja kwa Mungu. Neema ya Mungu huja kwa kila mtu kabla hajaanza kumtafuta Mungu, ingawaje huwa hajafanya lolote ili aweze kustahili.
Kumbuka katika Waefeso 2:1-3, je, inatoa maelezo gani yasiyokuwa na matumaini? Lakini angalia aya mbili zinazofuata baada ya maelezo hayo.
Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda; hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; (yaani, tumeokolewa kwa neema) (Waefeso 2:4-5).
Kama mtu akiwa hajaokoka, siyo kwa sababu hakuwa na neema, bali ni kwa sababu hakutaka kuwajibikia neema aliyokuwa nayo.
► Je, ni kipi kinachotangulia kwanza, mwanadamu kumtafuta Mungu au kazi ya Mungu ndani ya mwanadamu? Ni kwa jinsi gani utaielezea hii?
Kifungu cha kujifunza – Warumi Sehemu ya 2, kifungu cha 3
Kwenye somo hili, tunamaliza sehemu ya 2 ya Waraka kwa Warumi. Tumeona ni kwa jinsi gani Wamataifa walivyokataa kuwa na ufahamu wa Mungu na wakageukia sanamu. Wayahudi walikuwa na sheria ya Mungu lakini hawakuitii. Sasa, mtume anatoa muhtasari wa hali ya ujumla ya watu wa dunia
Jambo Kuu katika sura ya 3:1-20
Kila mtu katika dunia hii ni mtenda dhambi na atasimama kwenye mahakama ya Mungu kwa ajili ya hukumu.
Muhtasari wa sura ya 3:1-20
Kifungu hiki kinatoa muhtasari wa kifungu kikubwa cha 1:18-3:20. 3:19-20 vinatoa muhtasari wa kifungu kidogo, pamoja pia na kifungu kikubwa. Sheria inaonyesha kwamba ulimwengu wote una hatia; kwa hiyo, hakuna mtu yeyote anayeweza kuhesabiwa haki kwa msingi wa matendo yake.
Maana ya kusema hivyo ni kwamba kila kila kinywa kifumbwe (3:19), ikimaanisha kwamba hakuna mtu yeyote ambaye atakuwa na sababu ya kutoa udhuru au sababu ya kujihesabia haki. 3:9 inaonyesha mtiririko wa hoja ya Paulo: Amewaonyesha kwa pamoja Wayahudi na Wamataifa kwamba wako chini ya dhambi. Kwa kuwa hakuna hata mtu mmoja mwenye sababu ya kutoa samahani, Mungu anashughulika na watu wote kama watenda dhambi.
► Mwanafunzi atasoma Warumi 3:1-20 kwa ajili ya kikundi.
Maelezo ya Aya-kwa-Aya
(3:1-2) Paulo ameonyesha kwamba Wayahudi hawataokolewa kwa sababu tu wao ni Wayahudi; watahukumiwa kwa matendo yao sawasawa na Mataifa watakavyohukumiwa. Swali la kawaida sasa litakuwa, “Je, kweli kuna faida yeyote kwa Myahudi?” Faida kubwa ni kwamba wao ndio waliokuwa wamepewa Maandiko. Takribani Biblia yote imeandikwa na Wayahudi ambao Mungu aliwavuvia. (Faida nyingine zimeorodheshwa katika 9:4-5.)
Swali hilo hilo lingeweza likaulizwa kuhusiana na aina yeyote ya dini, au maana ya neema, kama vile ubatizo, ushirika wa kanisa, meza ya Bwana, au aina nyingine za mila za kidini. Haviwezi kutoa uhakika wa wokovu, kwa hiyo mtu anaweza akauliza, “sasa vina uzuri gani?” Jibu ni kwamba ni aina za ibada kama hizo zimetolewa kwa ajili ya kutusaidia katika imani yetu. Tunapovitendea kazi kwa imani, tunapokea neema. Lakini kama tutavifanyia kazi pasipo kuwa na imani na kama mbadala wa utii, havina thamani yeyote.[1]
(3:3) Je, itakuwaje kama wengine hawakuwa waaminifu? Je, kutokuwa kwao waaminifu kutaufanya uaminifu wa Mungu uonekane hauna maana yeyote? Swali linaloulizwa linaashiria kwamba kama Mungu hakuwaokoa Wayahudi ambao hawakutii, basi ahadi ya Mungu haikutimizwa.
Walifikiri kwamba upendeleo wa Mungu haungekuwa na masharti kwa Wayahudi. Walifikiri kwamba wangeweza wakamlaumu Mungu kwa kutokuwa mtu aliyeamini fu ingawaje walishindwa kutimiza matakwa yaliyohitajika.
(3:4) Sehemu hii ni kama kuonyesha kwamba Mungu na mwanadamu wanatofautiana katika mahakama. Uaminifu wa Mungu ukilinganishwa na mtu, kutokuwa mwaminifu kwa mtu kunathibitika. Mtume hasemi kwamba hatupaswi kupima haki ya Mungu. Anasema kwamba wakati tunapoyapima matendo ya Mungu, tutatambua kwamba yeye hapendelei na ni mwenye haki katika mambo yote aliyokwishafanya.[2]
Baadaye katika barua, tunaona kwamba kwa sababu wokovu ni wa masharti, haki ya Mungu inadhihirishwa kwa pamoja wakati anapookoa na wakati anapohukumu.
(3:5) Mtume anaibua swali kwamba mtu anaweza akauliza: Kama katika dhambi yetu inaonyesha kwamba Mungu hapendelei, basi inatimiza jambo lililo jema. Kisha, je, ni vibaya Mungu kutuadhibu sisi kwa ajili ya hiyo dhambi?”
► Je, ni kwa jinsi gani utajibu swali lililoko katika 3:5?
(3:6) Hapana, kwa sababu kama dhambi ya mwanadamu itabidi iwe udhuru kwa sababu inaonesha haki ya Mungu, hakuna dhambi itakayoweza kuhukumiwa. Hii ingekuwa inakana kuwa kuna hukumu ya mwisho, ambayo ni fundisho muhimu kwa kila mtu anayeamini katika Mungu asiyekuwa na upendeleo. Zaidi ya hapo, haki ya Mungu inadhihirishwa kwenye mwanga ulio wazi wakati anapoadhibu dhambi, lakini hangeweza akaadhibu dhambi kama dhambi inakubalika kwa msingi kwamba inaonesha kuwa na haki yake. Kipingamizi hiki kinajikanusha chenyewe.
(3:7) Tena wazo hilo linapendekezwa kwamba kwa kuwa hata dhambi zetu zitatumika kuleta utukufu kwa Mungu, mwenye dhambi hapaswi kupewa adhabu. Hili ni jaribio la kutaka kutathmini vitendo kulingana na matokeo yake ya mwisho. Hata hivyo, hii ni kinyume na ukweli kwamba hukumu itakuwepo kulingana na sababu ya kutenda jambo (2:15-16). Hata hivyo, wajibu wa kuleta matokea mazuri kutokana na matendo mabaya unahusiana na Mungu peke yake. Mwenye dhambi hawezi kukamilisha mambo mema kwa dhambi yake. Dhambi huleta matokeo mabaya isipokuwa tu pale ambapo Mungu atakuwa ameingilia kati.
(3:8) Paulo anasema tu kwamba wenye dhambi na wale wanaotaka radhi kwa dhambi zao wanastahili hukumu. Pia anakanusha mashtaka ya uongo kwamba wakristo hufundisha hivyo hivyo kwa sababu dhambi zetu zaweza kuleta mema kupitia neema ya Mungu, tunapaswa tu tuikiri na kubakia wenye dhambi. Kukiri tu hali yako ya dhambi haitoshi. Mtu ni lazima atubu; lakini ili aweze kutubu kwa ukweli, ni lazima aione dhambi yake kuwa kweli ni uovu.
(3:9) Neno "Sisi" inarejelea Wayahudi. Hawana hadhi ya kiroho inayojileta yenyewe. Wote wako chini ya dhambi; wametenda dhambi na wako chini ya hukumu yake.
(3:10-18) Aya hizi ni nukuu kutoka Zaburi na manabii wa Agano la Kale.[3] Baadhi ya watu hunukuu 3:10 na kusema inamaanisha kwamba hakuna mtu mwenye haki, hata yule ambaye ni Mkristo. Hata hivyo, 3:10-18 haiwezekani kuwa inamwelezea Mkristo. Kama mtu yeyote atafikiri kwamba hii inamwelezea Mkristo, jaribu kufikiria kuweka jina la Mkristo unayemjua kwenye sentensi hizi. Kwa mfano, kinywa cha Mchungaji Petro kimejaa laana, miguu yake ni miepesi kwenda kuua, na hana hofu ya Mungu.”
Aya hizi zinaelezea hali ya ujumla ya wale ambao hawajaokoka. Ni sawa na maelezo yaliyoko kwenye 1:29-31. Kusudi la Paulo ni kuonyesha kwamba hakuna mtu anayeweza kupata wokovu kwa matendo yake. Rum 3:10-18 inaonesha kuwa hakuna mtu mwenye haki bila ya kuwa amepata haki ya Mungu.
► Je, ni kwa jinsi gani unaweza kujibu taarifa hii: “Hakuna mtu atakayeweza kujinadi kwamba anaishi kwa ushindi dhidi ya majaribu kwa sababu Biblia inasema kwamba hakuna mtu yeyote mwenye haki”?
3:19-20 hazitoi tu muhtasari wa 3:1-20, bali 1:18 - 3:20.
(3:19-20) Sheria haikuwa imetolewa kwa ajili ya kuwaonesha watu jinsi ya kuhesabiwa haki, bali kuonesha kwamba kila mmoja tayari ni mwenye hatia. Sheria siyo kwa ajili ya kuhesabiwa haki, bali hukumu. “Kwamba kila kinywa kiweze kufumbwa” inamaanisha kwamba hakuna mtu mwenye udhuru au msingi wa kujihesabia haki yeye mwenyewe. Hawezi kujitetea mwenyewe katika mahakama ya Mungu.
Mtu afikiriaye kwamba anapaswa kushika sheria ili akubaliwe na Mungu yuko chini ya sheria. Kuwa chini ya sheria haina maana ya kurejea kwenye kipindi cha historia cha Agano la Kale. Mtu yeyote yuko chini ya sheria kama hatakua amepokea neema inayookoa.; kwa sababu kama ilikuwa aende kwenye hukumu ya Mungu, atakuwa amehukumiwa kwa kuvunja sheria. Mtu huwa hayuko tena chini ya sheria kama anakuwa ameokoka kwa sababu amekubaliwa na Mungu kwa msingi wa neema.
Ni lazima kila mmoja kuelewa jinsi menye dhambi naweza kusamehewa mbele ya Mungu. Hapatakuwa na Amani au kupata furaha tukiwa maadui wa Mungu, ikiwa ni wakati wa sasa au katika umilele unaokuja[1]
Watu waliumbwa kwa sura ya Mungu na walikuwa watakatifu, kama vile Mungu muumba wao alivyo mtakatifu. Kama Mungu alivyo mwenye upendo, ndivyo alivyo mtu mme na mke, wakiishi katika upendo, waliishi katika Mungu na Mungu akiwa ndanbi yao. Walikuwa watakatifu, kama Mungu alivyo, mbali na kila doa la dhambi. Hawakujua dhambi ndani na nje walikuwa bila dhambi. Walimpenda Bwana Mungu wao kwa mioyo yao yote, akili, nafsi na nguvu zao.
Mungu akampa Adamu, mtu mwenye haki na mkamilifu, na sheria kamilifu. Mungu akahitaji kwake utii kamili, ambao Adamu angeuweza. Hata hivyo Adamu na Hawa walimwasi Mungu (Mwanzo 3:6).
Mara moja Adam akahukumiwa kwa hukumu ya haki ya Mungu. Mungu alikuwa amemwonya Adamu kuwa adhabu ya kutokutiii ingekuwa ni kifo (Mwanzo 2:17). Mara Adamu alipoonja tunda lililokatazwa, alikufa. Roho yake ilikufa kwa sababu alitengwa na Mungu. (Bila Mungu nafsi inakosa uhai). Kadhalika, na mwili wake unakufa. Kwa kuwa amekufa rohoni, amekufa kwa Mungu, na amekufa kwenye dhambi, aliingia katika kifo cha milele; aliingia kwenye hukumu ya milele; kwenye adhabu ya mwili na roho katika jehanamu ya moto, ambayo haizimiki.
“dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi (Warumi 5:12). Dhambi ilikuja kupitia Adam, ambaye alikuwa ndiye baba na mwakilishi wetu sote. Kwa sababu ya hili, watu wote walikufa —wafu kwa Mungu, wafu kwenye dhambi, kuishi katika mwili wa kufa ambao sio muda mrefu unasambaratika, na unakuwa chini ya hukumu ya kifo cha milele. Kwa kutokutii mtu moja watu wote wakafanywa wenye dhambi (Warumi 5:19) na “…kama kwa kosa moja watu wote walihukumiwa adhabu…” (Warumi 5:18).
Watu wote wakawa katika hali hii ya uenye dhambi na kuhukumiwa—Mungu akaupenda ulimwengu, hata akamtoa mwana wake pekee, ili kwamba tusipotee, bali tuwe na uzima (Yohane 3:16). Mwana wa Mungu akawa mtu, kichwa cha pili cha familia za wanadamu . kwa namna hiyo akachukua huzuni zetu (Isaya 53:4), Na Bwana akaweka juu yake Maovu yetu sisi sote (Isaya 53:6). alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu (Isaya 53:5). Akafanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi (Isaya 53:10). Alitoa damu yake kwa ajili ya wenye dhambi. Akafanya sadaka kamili na kamilifu kwa ajili ya dhambi za ulimwengu wote
Kwa sababu mwana wa Mungu alionua mauti kwa ajili ya kila moja (Waebrania 2:9), yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao (2 Wakorintho 5:19). “…kama kwa kosa moja watu wote walihukumiwa adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki watu wote walihesabiwa haki yenye uzima” (Warumi 5:18). Kwa sababu ya mateso ya mwana wake kwa ajili yetu, Mungu sasa anatupa uhakika wa kufuta adhabu ya dhambi tuliyoistahili kwa ajili ya dhambi zetu, ili kuturudisha kwake, na kutufanya upya roho zetu mfu na kuzipa uzima, huku akitupa uhakika wa uzima wa milele. Ahadi hii ina sharti moja, ambayo anatuwezesha kuifikia.
► Je, sharti moja linalotajwa katika aya ya mwisho ni nini?
► Je, kulikuwa na neema na uzoefu gani wa kiroho uliokuwa unapatikana kwa ajili ya watu walioishi wakati wa Agano la Kale? Kwa nini swali hili ni muhimu?
Baadhi ya watu wanaamini kwamba watu kwenye Agano la Kale hawakuweza kubadilishwa au kuokoka na kupata uzoefu wa Roho Mtakatifu. Kwa hiyo, hawaoni umuhimu wa Agano la Kale kwa ajili ya waamini wa leo. Wanafikiri kwamba wokovu kwa njia ya neema kupitia imani ilianza na Agano Jipya. Wanafikiri kwamba watu kwenye Agano la Kale wangeweza wakaokoka kwa kutumia sheria na dhabihu.
Ukweli ni kwamba kamwe hakuna mtu yeyote aliyewahi kuokoka kwa kuishika sheria au kwa kutoa dhabihu (Waebrania 10:4). Kwa hiyo, walikuwa wanaokokaje? Kwa njia ya neema kupitia imani.
(1) Agano Jipya linasema kwamba Injili iko kwenye Agano la Kale
Agano la Kale linafundisha kuhusu wokovu kwa njia ya imani kupitia Yesu Kristo (2 Timotheo 3:15).
Ibrahimu alikuwa na injili na alihesabiwa mwenye haki kwa njia ya imani (Warumi 4:1-3; Wagalatia 3:6, 8).
Daudi alielezea kuhusu kuhesabiwa haki kwa njia ya imani (Warumi 4:6-8).
Injili ilikuja mwanzo; sheria ikafuata baadaye (Wagalatia 3:17).
Watu wa Agano la Kale walikuwa na injili ikihubiriwa kwao kama inavyofanyika kwetu (Waebrania 4:2).
Yesu alionyesha kwamba Nikodemo alikuwa ameshajua kuhusu uzao mpya kutokana na kujifunza kwake Agano la Kale (Yohane3:10).
Haki hutolewa kwa sababu ya Imani (Warumi 1:17), inashuhudiwa na sheria na manabii (Warumi 3:21).
(2) Elimu nyingi siyo muhimu katika kupokea neema kwa njia ya imani.
Yesu alihubiri kuhusu toba na msamaha lakini hakuelezea kuhusu upatanisho. Watu walikuwa wanaokoka kwa kuamini ujumbe wake (kwa mfano, mwanamke Msamaria pale kisimani, Yohane 4:39-42).
Waamini wa Agano la Kale hawakuwa wanaelewa kuhusu upatanisho, lakini walichokuwa wanahitaji ni kuamini tu kwamba Mungu alikuwa anatoa njia ya msamaha kwa ajili yao. Kisha wangeweza wakaokoka kwa neema kwa njia ya imani, na siyo kwa matendo yao au kwa kutoa dhabihu. Dhabihu zao na utii wao zilikuwa ni udhihirisho wa imani yao, kama ilivyo kwetu.
Endapo mtu atamtii Mungu, Mungu atamwonesha njia ya kumleta kwenye uhusiano naye Zabu 25:14 inasema “Siri ya Bwana iko kwao wamchao, Naye atawajulisha agano lake.”
(3) Amri za Mungu hufanya neema iwe muhimu.
Yesu alisema katika Mathayo 22:37-40 kwamba amri zilizo muhimu ni kumpenda Mungu kwa namna yeyote ile ulivyo (Kumbukumbu la Torati 6:5) na kumpenda jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe (Walawi 19:18). Haiwezekani kuzitii amri hizi bila ya neema. Je, Mungu aliamuru mambo yasiyowezekana kwa ajili ya watu katika Agano la Kale, au aliwezesha utii kwa njia ya neema?
Usilipe uovu kwa uovu (Mithali 24:28-29). Watendee mema wale wanaokutendea maovu (Mithali 25:21-22). Ukimwona ng’ombe au punda wa adui yako amepotea mrudishe (Kutoka 23:4-5). Usifurahi, adui yako aangukapo (Mithali 24:17).
(4) Mungu alitegemea watu wa Agano la Kale waishi maisha ya utii.
Kumbukumbu la Torati 27 na 28 pameorodheshwa baraka zinazotokana na kutii na laana zinazoambatana na kutokutii. Laana hizi zinahusisha kila kitu kinachoweza kufikirika. Kama ingekuwa hakuna neema ya kufanya kutii kuwe ni kitu kinachowezekana, watu hawa walitengwa kupokea laana za aina zote na kupoteza baraka zote.
(5) Mungu alitoa kazi ya neema kubadilisha mioyo yao.
Katika Kumbukumbu la Torati 30:6 panasema kwamba kwa pamoja wao na madhuria wao wanaweza wakatahiriwa kwenye moyo, ili waweze kutii na kuishi. Katika 30:11-20 tunaona mambo yafuatayo: Walikuwa hawapaswi kusema kwamba ilikuwa ni vigumu kupokea, kwa sababu ilikuwa ndani ya midomo na mioyo yao ‒ taarifa iliyonukuliwa na Paulo katika Warumi 10:6-8 inarejelea kwenye neema iliyopokelewa kwa imani. Suala litaamuliwa ndani ya mioyo yao (Kumbukumbu la Torati 30:17). Upendo kwa Mungu utaongoza kwenye utii (Kumbukumbu la Torati 30:20).
(Ona pia Kumbukumbu la Torati 10:12, 16.) Alichokuwa anakihitaji Mungu ni upendo mkamilifu na utakaso wa moyo. Kutahiriwa kwa moyo kungefanya hili liwezekane kufanyika.
(6) Watu wa kweli wa Mungu kwa wakati wowote – ni wale wanaompenda na kumtumikia.
Warumi 2:28-29, Wakolosai 2:11-12, na Wafilipi 3:3 kwa pamoja panasema kwamba Myahudi wa kweli ni yule aliye wa kiroho. Mitume walisema jambo kama hilo linalofanana. Wokovu unategemea utii wa moyo, na dhabihu hazikuweza kuhalalisha mioyo ya uovu. Stefano aliwalaumu Wayahudi wa wakati wake kwa kuwa kama mababu zao wa Agano la Kale ambao Walikuwa hawajatahiriwa mioyo yao na masikio (Matendo 7:51). Hakuna wakati ambapo Mungu aliwataka tu watu wafanye namna za ibada.
Daudi aliomba, "Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele zako" (Zaburi 19:14).
(7) Kuna mifano mingi ya neema katika Agano la Kale.
Ayubu alikuwa na hofu ya Mungu na aliukataa uovu (Yobu 1:1).
Nuhu alikuwa mwenye haki na mkamilifu (Mwanzo 6:9).
Isaya alikuwa na uzoefu wa kutakasa moyo (Isaya 6).
Daudi aliomba kwa ajili ya utakaso kwa ajili ya dhambi zake (Zaburi 51).
Ushahidi unaonesha kwamba wokovu na moyo ulio mweupe ulikuwa unapatikana katika Agano la Kale. Hii inamaanisha kwamba Agano la Kale ni muhimu kwetu. Maelekezo ya Mungu kwa ajili ya maisha ya haki kwenye Agano la Kale yalikuwa ni maelekezo kutoka kwa Mungu aliye Mtakatifu kwenda kwa watu wake ambao walikuwa wanapaswa waishi kwenye neema. Bila shaka, amri nyingi zilikuwa ni maalumu kwa wakati na hali ile na haitendi kazi tena nasi kwa njia ile ile iliyokuwa inatumika kwa wakati ule. Katika somo la 7 ni sehemu inayoelezea jinsi ambavyo tutatumia Maandiko ya Agano la Kale kwenye maisha yetu.
Maswali ya Mapitio Somo la 4
(1) Elezea dhana ya Calvin ya “neema ya kawaida”.
(2) Elezea dhana ya Wesley ya “neema ya awali” yaani neema inayotangulia.
(3) Katika Warumi 3:19, maneno “kila kinywa kufumbwe” yana maanisha nini?
(4) Je, ni manufaa gani mabwa yanatajwa kwa Wayahudi katika Warumi 3?
(5) Je, aina mbali mbali za kuabudu zinatunufaishaje?
(6) Je, Warumi 3:10-18 inaonesha nini?
(7) Je, ni nani aliyeko chini ya sheria? (Warumi 3:19-20)
Kazi ya kufanya Somo la 4
(1) Andika ukurasa mmoja kuhusiana na mmoja mada zifuatazo:
Neema ya awali
Neema katika Agano la Kale
Sababu zinazopelekea wenye dhambi kuhitaji kuhesabiwa haki kwa njia ya imani
Unaweza ukatumia mchangayiko wa maandiko mbalimbali tofauti na kitabu cha Warumi endapo itahitajika.
(2) Kumbuka kwamba unahitajika kuhubiri mahubiri matatu au kufundisha vipindi vitatu kwa vikundi vingine wakati kozi hii ikiwa inaendelea.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.