Kifungu cha kujifunza – Warumi Sehemu ya 4, Kifungu cha 3
Katika somo hili tunaendelea na Sehemu ya 4 ya Kitabu cha Warumi. Tumejifunza Warumi 6, kuhusu “ushindi dhidi ya dhambi,” na Warumi 7, kuhusu “mtenda dhambi mwenye hatia.” Katika somo hili tutajifunza Warumi 8, ambayo inaelezea maisha ya Mkristo kwenye hali ngumu za dunia.
Jambo Kuu katika Warumi 8
Ingawaje mwamini anaishi kwenye dunia iliyoanguka, akipata mateso kutokana na hali ya dunia na kutokana na udhaifu wake mwenyewe, Roho Mtakatifu humpa ushindi juu ya dhambi na katika hali zote anazopitia.
Muhtasari wa Warumi Sura ya 8
Sura hii inarejea mara nyingi katika nafsi tatu zilizoko kwenye Utatu Mtakatifu wa Mungu. Nafsi hizi zote tatu zinahusiana kwa karibu sana katika wokovu wetu wa sasa na wa baadaye. Tunaweza kuishi kwa ushindi tukiwa katika hali ya mwili, tunaweza kufurahia kwa uhakika wokovu wetu binafsi, tunaweza kuhimili hali mbalimbali za maanguko zilizopo, tunaweza kuomba kwa msaada wa kiroho zaidi ya akili zetu wenyewe, na tukaendelea kudumu katika uhusiano wetu wa wokovu na Mungu.
8:1-13 zinaunda kifungu ambacho kinaweza kikaitwa “Siyo katika Mwili tena.”
Utangulizi wa Warumi 8:1-13
Wale watu wote ambao hawahukumiwi ni wale ambao hawafuati tena mambo ya mwili. Kuwa katika hali ya kimwili haimaanishi ni kuwa mwanadamu; bali inamaanisha ni kuwa chini ya mamlaka ya hali ya asili ya anguko la dhambi.[1]
Kuwa katika hali ya kimwili inatofautisha na kuwa katika hali ya kuokoka. Hali ya kimwili ni kifo (8:6) na ni uadui na Mungu (8:7). Mtu aliyeko katika hali ya kimwili hawezi akampendeza Mungu (8:8) na lazima atakufa (8:13). Kuwa katika hali ya kimwili ni hali moja inayofanana na ile iliyoelezwa katika 7:7-25 (ona 7:14, 18, 25).
8:12-13 ni hitimisho. Hatupaswi tuishi katika hali ya kimwili, kwa kuwa mtu anayeishi katika hali ya kimwili atakufa, hii ikiwa na maana kwamba ni kupokea hukumu ya Mungu (ona 1:17). Ni lazima tuue matendo ya dhambi ya mwili. Kwa kuwa mtu anayefuata matendo ya kimwili ni mwenye dhambi, sio mfuasi wa Yesu, dhambi ni lazima isambaratishwe kabisa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.
► Mwanafunzi atapaswa kusoma Warumi 8:1-13 kwa ajili ya kikundi.
[1]Mwangalizo katika somo la 7 kuhusu “Kufafanua Mwili/Nyama” ni muhimu sana katika kukielewa kifungu hiki.
(8:1) Mtu anayefuata mambo ya Roho hayuko chini ya hukumu. Mtu anayefuata mambo ya kimwili yuko chini ya hukumu –na hayuko ndani ya Kristo.
(8:2) Sheria ya Roho kuhusiana na maisha ni kwamba mtu aliyesamehewa anakubaliwa kwa neema na anakuwa na maisha ya kiroho. Sheria ya dhambi na kifo ni kwamba mtu ambaye ataonekana kuwa na hatia kupitia hiyo sheria atahukumiwa adhabu ya kifo.
(8:3) Sheria imetoa mahitaji. Haikutoa nguvu. Mwenye dhambi hakufuata sheria; kwa hiyo, sheria haikuwa ndiyo njia ya wokovu. Mungu alimtuma Mwanaye kama Mkombozi.
[1](8:4) Hatuisahau sheria ya Mungu lakini tunaitii kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
(8:5) Kila mtu hufuata asili yake mwenyewe. Kama hajapokea maisha ya kiroho, basi anatawaliwa na hali ya kimwili.
(8:6) Kutawaliwa na hali ya asili ya dhambi ni kuwa chini ya hukumu. Mbadala wake ni kutembea katika Roho na kumtii Mungu. Hakuna njia nyingine ya mkato ya kupata msamaha wakati mtu anapoendelea kufuata matendo ya dhambi.
(8:7-8) Mtu aliye katika asili ya hali ya kimwili kwa kawaida ni adui wa Mungu, kwa sababu kwa jinsi anavyoendelea kutawaliwa na hali ya asili ya dhambi hawezi akajitoa kuwa chini ya Mungu. Katika hali hiyo hakubaliki kwa Mungu.
► Orodhesha baadhi ya mambo yanayoelezea kuhusu mtu ambaye yuko katika hali ya kimwili.
[2](8:9) Kuwa katika hali ya kimwili maana yake ni kuwa chini ya mamlaka ya hali ya asili ya anguko la dhambi; mtu aliyeamini hayuko tena katika hali ya kimwili. Bado ataendelea kukumbana na majaribu, lakini hatakuwa chini ya mamlaka, na anao uwezo wa kuzuia jaribu. Aya hii inatuambia kwamba uwezo huu uko hapo kwa sababu Roho wa Mungu naye yuko hapo. Mtu hawezi kudai kwamba anaongozwa na amepakwa mafuta ya upako na Roho Mtakatifu kama hana ushindi dhidi ya dhambi.
(8:10-11) Mwili wa mwanadamu bado umeathirika na dhambi ya Adamu pamoja na dhambi zetu zilizopita. Kwa hiyo, matamanio ya mwili yanaweza yakaenda kwenye mwelekeo mbaya. Hatuwezi tukayaamini matamanio ya miili yetu kutuongoza. Lakini nguvu ile ile ambayo ilimfufua Yesu kutoka kwa wafu inafanya kazi ndani yetu, na inatupa uhai ili kwamba miili yetu iweze kuletwa kwenye utii kwa Mungu. Udhaifu wa mwili hauwezi kuwa ni sababu ya kutenda dhambi. Hatupaswi kutenda dhambi, kwa sababu uweza wa Mungu ni mkuu kuliko udhaifu wa miili yetu.
(8:12-13) Kufuata hali ya kimwili kunasababisha kifo cha kiroho. Kupitia Roho Mtakatifu tunayaua matendo yote ya kimwili, na kuyasambaratisha hadi mwisho. Watu wanaofanya hivyo huepuka hukumu ya Mungu. Maandiko haya hayaruhusu mtu aliyesamehewa na kukubaliwa na Mungu kuendelea kutenda dhambi.
“Wanadamu wanaridhika na kile kilicho nje, kinachoonekana, vitu na vilivyo vya juu. Kilicho muhimu kwa Mungu kina kina, cha ndani, ni kazi ya siri ya Roho Mtakatifu katika mioyo yetu”
- John R.W. Stott, Ujumbe wa Warumi:
Habari njema ya Mungu kwa dunia
"Hamu nzuri, iliyo chini ya uthibiti, inasaidia afya na ina manufaa. Hamu hiyo hiyo, inayomweka mtu katika utumwa na kutawala maisha yake, inaleta kifungo na dhambi.”
- Wilbur Dayton
Sheria ya Mungu kwa Mkristo
Baadhi ya watu husema kwamba sheria ya Mungu haina umuhimu kwa maisha ya Mkristo. Mambo wanayosema ni kama vile, “Mungu hajali lolote kuhusu matendo yako,” na “wakati utakapoingia mbinguni matendo yako yatakuwa siyo chochote.” Kwa mawazo yao, neema huchukua nafasi ya utii. Lakini Paulo alisema, “Basi, je! Twaibatilisha sheria kwa imani hiyo? Hasha! Kinyume cha hayo twaithibitisha sheria (Warumi 3:31). Kama tutafundisha injili itakayoiona sheria kwamba siyo kitu chochote, hiyo siyo injili ambayo Paulo aliihubiri.
Sheria ambayo Paulo aliizungumzia siyo tu utaratibu wa sheria za Musa. Sheria ya Musa ilikuwa ni utendaji wa mapenzi ya Mungu kwa wakati na mahali maalumu. Mambo yake mengi hayafanyi kazi kwenye maeneo yote na kwa muda wote kwa njia inayofanana, hasa kwenye hali za ibada na sheria zilizotolewa kwa Waisraeli kwa taifa. Kanuni za sheria ya Musa bado zinafanya kazi hata sasa kwa sababu tabia ya Mungu haibadiliki.
Kwa ujumla, sheria ya Mungu ndiyo inayohitajika kwa ajili ya mwanadamu. Sheria ni takatifu, haina upendeleo, na ni nzuri, (7:12) kwa sababu inatoka kwenye asili ya Mungu mwenyewe. Sheria ya Mungu ni ya kiroho (7:14).
Haki ya sheria inakamilika kwa wale watu ambao wanatembea na Roho Mtakatifu badala ya kutembea katika hali ya kimwili (8:4) kwa sababu wanaishi kwa kumtii Mungu.
Biblia inatoa taarifa zifuatazo kuhusiana na sheria ya Mungu:
1. Utii wa sheria unapaswa uwe ni udhihirisho wa upendo kamili kutoka ndani ya moyo (Mathayo 22:37-40).
2. Kusudi la Amri maalumu za Mungu ni kuonyesha hitaji la upendo kutoka katika moyo ulio safi, dhamira njema, na imani ya uhalisia wa kweli (1 Timotheo 1:5). Ni jambo lisilowezekana kwa mtu kuweza kutimiza kwa ukweli kabisa mahitaji yote ya Mungu isipokuwa kwa nia ya upendo, hivyo, kutotii unaonyesha kukosekana kwa upendo.
3. Mtu mwenye upendo huu anatimiza sheria yote; yaani, anatimiza yote ambayo Mungu anahitaji kutoka kwa mtu (Warumi 13:8-10). Kwa hiyo, kuwa na upendo kamili ni kuwa na utii kamili.
4. Upendo hudhihirishwa kwenye utii (1 Yohane 5:2-3). Upendo siyo tu hisia au uaminifu uliotabiriwa kwa Mungu. Upendo hauwezi kuwa badala ya utii lakini unachochea utii.
5. Yesu hakuja kuitangua sheria, na alisema kwamba kama mtu atawafundisha watu wengine kuivunja sheria, ataitwa mdogo sana katika ufalme wa mbinguni. (Mathayo 5:17-20).
Uelewa mzuri wa sheria ni muhimu kwa injili kwa sababu watu kwa ajili ya umilele wameshahukumiwa kwa kuvunja sheria ya Mungu. Mtu hawezi akatubu hadi akubaliane na Mungu kuhusiana na dhambi na sheria. Baadhi ya watu wanatambua mwenye dhambi anastahili kwenda motoni kwa kuvunja sheria ya Mungu, lakini bado wana mawazo ya ajabu kwamba Mungu hajali tena kuhusu sheria baada ya kuwa mtu ameamini.
Sheria siyo kigezo cha kukubalika kwetu na Mungu. Lakini inatupa sisi ufahamu wa kujua ni kwa jinsi gani Mungu anatutaka tuishi.
► Kwa mtu aliyeamini, kuna uhusiano gani kati ya kumpenda Mungu na sheria ya Mungu?
Kifungu cha kujifunza – Warumi Sehemu 4, kifungu cha 3
Utangulizi wa Warumi 8:14-27
8:14 inaunganisha aya zilizotangulia kwenye mada muhimu ya uhakika wa wokovu kwenye aya zinazofuata. Utambulisho wa watoto wa Mungu ni kwamba wanamfuata Roho Mtakatifu na wanaishi kwa ushindi badala ya kufuata hali ya mwili na kuishi katika dhambi.
8:14-27 ni kifungu ambacho kinaweza kupewa kichwa cha habari “Msaada wa Roho Mtakatifu katika Ulimwengu Ulioanguka.”
► Mwanafunzi atapaswa asome Warumi 8:14-27 kwa ajili ya kikundi.
Maelezo ya Aya-kwa-Aya
(8:14) Utambulisho wa mtoto wa Mungu ni kwamba anamfuata Roho Mtakatifu na anaishi kwa ushindi badala ya kufuata hali ya mwili na kuishi katika dhambi.
8:14-17 inaelezea uhakika wa wokovu binafsi unaoletwa na Roho Mtakatifu.
(8:15) Kama watu ambao tumeamini, hatupaswi kurudi tena kwenye hofu ya sheria. Badala yake, tunaishi na uhakika wa wokovu kwa neema. Tumerithiwa kama watoto wa Mungu. Utii wa Mkristo siyo suala la kurudi nyuma na kuwa chini ya sheria kama njia ya wokovu bali ni suala la uhusiano na Mungu.
Ni sehemu ndogo tu ya Wakristo wa sasa wanaojinasibu kuwa waumini ambao kwa kweli wanachukua kwa umakini kazi ya kuhesabiwa haki kupitia Kristo katika maisha yao. Wengi wao wana ufahamu hafifu sana wa utakatifu wa Mungu na uzito wa dhambi zao kiasi kwamba kwa dhahiri hawaoni haja kubwa ya kuhesabiwa haki, ingawa katika undani wa maisha yao wanajawa na hisia za hatia na kutokuwa na usalama. Wengine wengi wanajitolea kinadharia tu kwa mafundisho haya, lakini katika maisha yao ya kila siku wanategemea utakaso wao kwa ajili ya kuhesabiwa haki, kwa mtindo wa Augustino, wakipata uthibitisho wa kukubalika kwao na Mungu kupitia unyofu wao, uzoefu wao wa zamani wa kugeuka, utendaji wao wa hivi karibuni wa kidini, au mara chache kwa makosa yao ya dhahiri na ya makusudi. Wachache wanajua vya kutosha kuanza kila siku kwa kusimama thabiti juu ya msingi wa Luther: kwamba wamekubaliwa, wakiangalia nje kwa imani na kudai haki ya Kristo, ambayo si yao wenyewe, kama msingi pekee wa kukubalika kwao, na kupumzika katika aina hiyo ya imani ambayo italeta utakaso unaozidi kuongezeka kadri imani inavyofanya kazi kwa upendo na shukrani.[1]
(8:16) Aya hii inaelezea kitu ambacho wainjilisti walioamini wanaita “ushuhuda wa Roho.” Roho wa Mungu anatuthibitishia kwamba tuko kwenye uhusiano wa upendo na utii pamoja na Mungu na ni shuhuda kwamba tumeokoka. Roho zetu wenyewe zinatambua kuhusu ukweli huo. Mkataba huo wa Roho wa Mungu na roho zetu ndio msingi wa uhakika tulio nao ili kwamba tusiwe watu wa kuishi kwa mashaka, tukijifikiria kama kweli tumeokoka.
Dini na madhehebu ambayo hayahubiri kuhusu uhakika wa wokovu wanawaweka watu wao kwenye mashaka. Watu wanakuwa na mashaka kwamba hawajafanya lolote la kutosha ili waokoke. Injili inaleta ukombozi wa kutoka kwenye mashaka kwa sababu tunajijua kwamba tumesamehewa. Utii wetu umejikita katika kumfuata Roho Mtakatifu ili kumpendeza Mungu ambaye tayari ameshatukubali sisi, kuliko kushika sheria kama njia ya kuweza kukubalika kwake.Tunaweza tukajijua kwamba tumeokoka kwa sababu tunaishi kwa utii kwenye uhusiano pamoja na Mungu na kuwa na ushuhuda wa Roho Matakatifu kwamba ni kweli tumeokoka. (Ona 1 Yohane 2:3, 29; 1 Yohane 3:14, 18-21, 24 kwa ajili ya msingi wa kimaandiko kuhusu uhakika wa wokovu.)
► Ni ushauri gani utakaoweza kumpa mtu ambaye hana uhakika kwamba ameokoka?
(8:17-18) Tutarithi pamoja na Kristo utukufu na ufalme wa Mungu. Utukufu wake utadhihirishwa ndani yetu kwa mambo mengi na makubwa ambayo amefanya ndani yetu, akibadilisha asili yetu iwe kama vile alivyopanga tuwe. Tutarithi uzima wa milele, ikimaanisha tutaishi maisha ya Mungu. Tutatawala pamoja na Kristo. Hata hivyo, siyo marupurupu yetu yote yatapatikana kwa sasa. Utukufu unaotajwa hapa bado ni siku za baadaye. Mateso ni sasa, na utawala ni baadaye. Hata hivyo, utukufu wa mwisho ni mkuu mno kiasi kwamba hali zetu za sasa siyo muhimu ukilinganisha na hatima yetu.
8:19-25 zinaelezea kuendelea kudumu katika imani wakati tukiwa tunamsubiri Mungu arejeshe tena uumbaji wake kwa ukamilifu.
(8:19) Kila kitu kilichoumbwa bado kinasubiri muda ambao Mungu atawatukuza kikamilifu watoto wake. Mtume Yohane anasema kuwa hatujaona muundo wa miili yetu tutakayokuwa nayo mbingunini (1 Yohane 3:2).
(8:20-21) Kila kitu kilichoumbwa bado kinateseka na matokeo ya dhambi. Mungu ameruhusu laana iendelee kubakia kwa mategemeo kwamba wenye dhambi watatubu kwa sababu ya kuona matokeo ya dhambi. Viumbe vilivyoumbwa hatimaye vitarejeshwa na kuletwa kwenye ukamilifu wa mwisho wa mpango wa Mungu. Hii haitawahusu wale watu ambao hadi mwisho wameyakataa mapenzi ya Mungu, wakikataa kutubu.
(8:22) Laana ya dhambi ilivuruga uumbaji wote. (Mwanzo 3:17-19). Kazi ni ngumu. Ardhi haizalishi tena kwa ajili ya mwanadamu kama ilivyokuwa kabla ya anguko. Magonjwa, uzee na kifo huja kwa viumbe vyote vinavyoishi.
(8:23) Hata watu walioamini bado wanateseka kwa matokeo ya dhambi kwa sababu miili yao bado haijarejeshwa kwenye hali ilivyokuwa kabla ya anguko. Tunaye Roho Mtakatifu kama sehemu ya kwanza, aliye mfano, na shahidi wa mwisho wa urejeshaji wa Mungu. Mwisho wa yote, urejeshaji mkamilifu wa uumbaji utakuwa wokovu wa mwisho. Tunaweza kusema kwamba tayari tumeokoka, lakini bado tunangojea kwa ajili ya wokovu wa mwisho.
► Je, ni mambo gani unayoona ni dalili zinazoonesha kwamba uumbaji uko chini ya laana ya dhambi?
Sera ya Shetani kwa wenye dhambi ni kuwapa kitu kilicho kizuri sana atakachoweza pale mwanzoni, kisha kwapa kibaya na kibaya tena, akiwahadaa na ahadi ambazo hawezi kuzitekeleza na mwisho wake kuishia motoni. Mungu anatupa sisi mfano wa mbinguni kwa sasa na anaweka akiba ya vitu vizuri zaidi kwa ajili yetu baadaye.
(8:24-25) Aya hizi zina ujumbe kwamba tunangojea kuona vitu ambavyo bado hatujawahi kuviona au kuvipokea.
Kufufuliwa kwa mwili ni fundisho la imani muhimu la Kikristo, na kulikataa kunapelekea kuishi maisha ya dhambi.
Baadhi ya watu katika kanisa la Korintho walikana ufufuo. Katika hilo ikaotokea misimamo miwili mikali.
1. Msimamo mkali wa kukandamiza tamaa za kimwili kwa sababu walifikiri kuwa wao ni waovu.
2. Msimamo wa uzembe na kudekeza tamaa za mwili kana kwamba hazina madhara yeyote
Baadhi walifikiri kwamba ikiwa mwili utaenda kutupwa kama kitu kisichofaa na kiovu, basi kuwa na tamaa za mwili ni dhambi. Kwa hoja hii, walisema mtu asioe bali awe bikira. Wengine walikuwa wazembe na waliachilia na walitii tamaa zao za kimwili, kwa sababu walifikiri hazikuwa na madhara. Mikazo hii inapitiliza kiwango na siyo ya Kikristo. Imani hizi zenye uharibifu, za uongo zinatokana na kukana fundisho la ufufuo wa mwili.
8:26-27 zinaelezea kazi ya Roho Mtakatifu kwenye maombi ya mtu aliyeamini.
(8:26-27) Hali yetu ya kuanguka inaleta madhara kwenye mtazamo wa akili na kiroho. Hatuwezi tukaelewa kwa ukamilifu wote kweli zote za kiroho. Hatuwezi tukaelewa kwa ukamilifu wote ni nini Mungu anachokusudia kukifanya kwa ajili ya dunia. Tunapoomba, Roho Mtakatifu hufidia udhaifu wetu kwa kuomba pamoja nasi maneno ambayo hatuwezi kuyasema. Anajua jinsi ya kuomba kulingana na mapenzi ya Mungu.
Aya hizi hazina maana ya kuomba katika lugha isiyojulikana. Taarifa ni kwamba Roho Mtakatifu anasema maombi kwa ajili yetu kwa sababu hatuwezi kuyasema. Aya hizi hazisemi kwamba tunaomba katika njia fulani isiyokuwa ya kawaida.
Utangulizi wa Warumi 8:28-39
Kifungu hiki kinaelezea kwamba waumini wako kwenye mpango wa Mungu, na anakusudia kuwapa neema ya kumaliza safari yao ya Ukristo na kubadilishwa kuwa katika sura ya Kristo. Hakuna hali zozote ambazo ziko duniani zinazoweza kututenganisha na Mungu kwa sababu neema na nguvu zake ni kuu mno.
Kifungu hiki kinaweza kikapewa kichwa cha habari “Usalama wa Kiroho wa Mtu Aliyeamini.”
► Mwanafunzi atapaswa kusoma Warumi 8:28-39 kwa ajili ya kikundi.
Maelezo ay Aya-kwa-Aya
(8:28) Kifungu cha maneno “mambo yote " kinahusisha mambo yote ambayo tunapitia katika mateso. Haimaanishi kwamba Mungu ametoa amri kwa mambo yote yanayotokea, ikiwemo dhambi. Inamaanisha kwamba Mungu huleta matokeo mazuri kutoka katika mambo hayo yote kwa ajili ya watu walioamini. Katika 8:37, baada ya kuorodhesha aina zote za mateso, akasema kwamba, katika mambo hayo yote sisi ni zaidi ya washindi. Mungu huyatumia mateso kwa ajili ya makusudi yake mwenyewe na hutujenga sisi kwa kupitia hayo.
Mungu hatoi amri au maagizo kwa kila kitu kinachotokea. Huwa anaruhusu mapenzi huru yafanye kazi, anaruhusu uthubutu wa kweli uweze kuchukuliwa ambayo yanategemea uwepo wa nafasi, na hata wakati mwingine anaruhusu dhambi itendeke. Lakini bado kwa mtu aliyeamini, Mungu huleta matokeo mazuri kutoka katika matukio yote – ikiwa ni kutoka hata katika dhambi za watu wengine walizozifanya kwa madhumuni mabaya ya kusababisha madhara.
(8:29) Tunatambua kwamba siyo kila mtu katika ulimwengu huu ameokoka. Kwa hiyo, wale aliowajua tangu asili ni wale ambao aliwajua kwa mambo maalumu. Tunatambua kutoka katika muktadha wa kitabu cha Warumi kwamba Mungu huchagua wale watu ambao wanaamini. Anajua mambo ya mbeleni ni mtu gani atakayeitikia wito wake wa wokovu kwa imani. (Ona pia 11.2 na maelezo yake.) Ni jambo la muhimu kuelewa kwamba Mungu alijua kwanza ndipo alikuja kuchagua au kupanga. Mungu alipanga kuokoa watakatifu (Ona Zaburi 1:6, 1 Wakorintho 8:3, Wagalatia 4:9, na 2 Timotheo 2:19 kwa ajili ya mifano ya Mungu “kujua.”)
Alipanga kwa ajili yao kufanana kama Kristo. Kufanana kama Kristo inamaanisha kwamba tutatafanywa tufanane na Kristo katika mwenendo wetu.
(8:30) Ni kazi ya Mungu inayotuleta kutoka kote huko tuliko hadi kwenye wokovu wa milele. Hakuna chochote kinachohitajika kutoka kwetu isipokuwa nia yetu tu.
(8:31-32) Hakuna hali zozote zinazoweza kuwa ngumu za kumshinda Mungu. Tayari alishafanya dhabihu ya hali ya juu sana, kwa hiyo sasa atatupa sisi kila kitu kinachohitajika kwa ajili ya ushindi wetu.
(8:33) Hakuna mtu yeyote anayeweza kutuhesabia wenye hatia ya dhambi katika kumbukumbu zetu kwa sababu zimefutwa kwa kuhesabiwa wenye haki kulikotolewa na Mungu.
(8:35-39) Kifungu hiki kinatoa matumaini makubwa na faraja kwa wale wanaomfuta Yesu. Hakuna kinachoweza kukutenganisha na Mungu. Paulo anasema kwamba tunalindwa kiroho kutoka kila kitu ambacho tunaweza kukabiliana nacho katika ulimwengu huu. Usalama wa mtu aliyeokoka ni ahadi ambayo kamwe Mungu hawezi kushindwa kumpa nguvu ya kuvumilia katika imani yake na hakuna nguvu nyingine yeyote itakayoweza kumtoa kutoka kwa Mungu.
► Je, nii kwa jinsi gani unaweza kuelezea namna amabavyo Mungu humsaidia mwamini kukabiliana yote kwa imani
[1]Richard Lovelace, The Dynamics of Spiritual Life, (Downers Grove, IL: Intervarsity Press, 1979) 101.
Maswali ya Mapitio Somo la 8
(1) Kwa nini haiwezekani sheria iwe ni njia ya wokovu?
(2) Je, ina maana gani kusema mwamini hatawaliwi tena na mwili?
(3) Je, ni kwa jinsi gani sheria inaelekeza maisha ya mkristo?
(4) Je, ushuhuda wa Roho ni nini?
(5) Wokovu wa mwisho ni nini?
(6) Je, kama watu watakana ufufuo wa mwili matokeo yake ni nini?
(7) Je, ni nini usalama wa mwamini?
Kazi ya kufanya Somo la 8
Andika ukurasa mmoja kuelezea matatizo ya kuishi kama Mkristo katika ulimwengu ulioanguka na pia toa maelezo ni nini Roho Mtakatifu anafanya kwa Mkristo.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.