Mambo mengi ya kiteolojia yamefanyiwa mijadala katika kanisa kwa karne nyingi zilizopita. Kitabu cha Warumi kinashughulika na masuala tata ya kiteolojia labda kuliko kitabu kingine chochote cha Biblia. Hapa kuna mifano ya maswali yaliyopata majibu katika barua hii.
Maswali ya kiteolojia yaliyopata majibu katika kitabu cha Warumi
Angalizo kwa kiongozi wa darasa: Somo kila swali na toa nafasi ili kuruhusu wanafunzi kadhaa waweze kutoa majibu. Kikundi hakipaswi kitumie muda wake mrefu kwenye kujibu swali lolote na hakipaswi kijaribu kufikia kwenye hitimisho. Kusudi la orodha hii ya maswali ni kuonesha kwamba kuna maoni mengi kuhusiana na maswali haya.
1. Je, mtu anapaswa aamini kitu gani ili aweze kuokoka kwa njia ya imani?
2. Je, inamaana gani kwamba Mkristo hawezi kuupata wokovu wake kwa njia ya njia ya matendo?
3. Je, Mungu aliamua kuokoa baadhi ya watu, na akaamua kuwaacha wengine?
4. Je, ni kwa jinsi gani Mungu anachagua mtu aliyeokoka na ambaye hajaokoka.
5. Je, ni jambo gani litakalotokea kwa watu ambao kamwe hawajawahi kuisikia injili?
6. Je, ni kwa jinsi gani Mungu anaweza kuwa mwenye haki kama anasamehe baadhi ya watenda dhambi na wengine kuwaadhibu?
7. Je, mtu aliyeamini ataweza kuwa bado mwenye dhambi?
8. Je, ni ushindi gani wa kiroho unaowezekana kwa ajili ya maisha halisi?
9. Je, kuna uwezekano kwa mtu aliyeokoka kupoteza wokovu?
10. Je, Mungu bado anao mpango kwa ajili ya Israeli?
Kusudi la Waraka kwa Rumi
► Mwanafunzi atapaswa kusoma Warumi 1:11-15 na 15:24 kwa ajili ya kikundi. Je, Paulo alitoa sababu gani za kumfanya atake kwenda Rumi?
Kusudi la barua hii lilikuwa ni kumtambulisha Paulo na teolojia yake ya wokovu kwa waamini wa Kirumi, ili kwamba:
1. Aweze kuwatambelea na kuwatia moyo waamini (1:11-12) na kuihubiri injili katika Rumi (1:15).
2. Aweze kuanza matendo mpya ya umisheni kwa kuungwa mkono na wao (15:24).
Paulo alikuwa ametumia miaka ya 47-57 B.K. akifanya uinjilisti kwenye mataifa yaliyokuwa karibu na bahari ya Aigea. Aliandika barua kwa Warumi katika kama mwaka wa 57 B.K.[1] Alipanga kufanya safari ya kwenda Yerusalemu, kisha Rumi. Paulo alitaka kulitumia kanisa katika Rumi kama kituo chake cha kuzindulia jitihada zake za umisheni za kuingia Hispania (15:24), ambayo zamani ilikuwa koloni la Waruni katika upande wa magharibi na kitovu cha ustaarabu wa Warumi katika sehemu hiyo ya dunia.
Kwa kuwa Paulo alikuwa hajawahi kabisa kuitembelea Rumi, barua ilitumika kama utambulisho wake binafsi na maandalizi kwa ajili ya ziara yake. Labda hii ndiyo sababu ya salamu nyingi alizotoa zilizoko katika Warumi 16.
Ziara ya Paulo katika Rumi haikufanyika kama alivyokuwa amepanga. Alikamatwa akiwa Yerusalemu. Ilipoonekana kwamba hataweza kuipata haki yake, alikata rufaa kwa Kaisari. Baada ya safari yake ngumu na ya hatari ambayo ilikuwa ni pamoja na kuvunjika kwa merikebu yao, aliwasili Rumi kama mfungwa kama mwaka wa 60 B.K. Ingawaje alikuwa ameshikiliwa na kuzuiliwa, alikuwa na uhuru wa kupokea wageni na kuwahudumia pamoja na kuhudumia kupitia wao (Matendo 28:30-31). Paulo alisema kwamba matukio haya yalikuwa yanatokea kwa ajili ya injili kuendelea (Wafilipi 1:12). Kulikuwa na waongofu hata ndani ya nyumba ya Kaisari mwenyewe.
Baadhi ya wanahistoria wanamini kwamba Paulo aliachiliwa baada ya miaka miwili ya kuwa kifungoni. Aidha iwe au isiwe kwamba alifanya safari yake ya kwenda Hispania haifahamiki. Tunachojua ni kwamba hatima yake aliuawa huko Rumi, lakini hii inaweza ilikuwa ni kwenye safari yake ya pili kwenye jiji hilo.
[2]Kwa kuelezea teolojia ya wokovu katika kuonyesha msingi wa matendo yake ya umisheni, Paulo alionyesha msingi wa matendo ya umisheni kwenye maeneo yote na kwa wakati wote.
Kwa kawaida maswali kadhaa yatainuka kuhusiana na ombi la Paulo alilotaka asaidiwe katika kuzindua safari yake ya umishenari. Baadhi ya watu wanaweza wakauliza, “Je, kwa nini iwe wewe ndiye unayekwenda?’ Kwa hiyo, Paulo alianza barua yake kwa kutaka kuelezea kujitoa kwake kwa ajili ya matendo ya injili (1:1) Baadaye akaelezea kuhusu wito wake maalumu na mafanikio yake kama mtume kwa Mataifa (15:15-20).
Mtu mwingine anaweza akauliza, “Kwa nini kila mtu ahitaji kuisikia injili? Inawezekana ujumbe huu wa injili hauhitajiki kila mahali.” Lakini Paulo alielezea umuhimu na uzito wa injili kwa wanadamu wote ulimwenguni kote. (1:14, 16, 10:12) na umuhimu wa matendo ya umishenari (10:14-15). Alionesha kwamba ujumbe wa injili unahusika kwa kila mtu aliyeko duniani, na kwamba kila mtu anahitaji sana kuusikia.
[1]Tarehe hizi ni kwa mujibu wa maoni ya wanazuoni, na hatujui kama wako kwenye usahihi kabisa.
"Kwenye ufahamu wa Paulo ilikuwa na kufahamu kwa ufupi katika waraka huu katika ujumla wake kujifunza injili ya Kristo na kuandaa utangulizi kwa yote yaliyohusiana na Agano la Kale.”
- William Tyndale,
“Prologue to Romans”
Kifungu cha kujifunza – Warumi sehemu ya 1
Sasa tuangalie kwenye sura ya kwanza – kuhusu Paulo katika salamu na utangulizi.
► Mwanafunzi atapaswa asome Warumi 1:1-17 kwa ajili ya kikundi.
Maelezo kuhusu Muundo
1:1-17 inaelezea wito wa Paulo na uhamasishaji wake wa kuineza injili. Baada ya hapo, 1:18-3:20 inaelezea ni kwa nini injili ni muhimu, kwa sababu wenye dhambi ambao hawajaokoka wako chini ya laana ya Mungu. Hata hivyo, 1:15-19 kuna kufanyika kwa mpito kati ya sehemu hizi mbili. Yenyewe imejitengenezea hatua, ikielezea injili kwa ufupi: kwamba watenda dhambi wana hatia kwa sababu wanajua zaidi, na kwamba, wako chini ya ghadhabu: lakini mtu aliyeamini ameokolewa.
Jambo kuu katika 1:1-17
Paulo aliitwa na kuhamasika kuieneza injili kwa sababu ni ujumbe wa wokovu kwa kila anayeamini.
Muhtasari wa 1:1-17
Kila kitu kwenye 1:1-14 kinaelekea kwenye taarifa iliyoko katika 1:15. 1:16-18 zinaelezea kwa ufupi injili ni nini na ni kwa nini kila mtu anaihitaji. Kwa kuwa wokovu ni uweza wa Mungu uletao msamaha na watu wanaupokea kwa imani. Sababu ya watu wote kuwa wahitaji wa ujumbe huu ni kwamba wako chini ya ghadhabu ya Mungu.
Kitabu chote cha Warumi ni mwendelezo wa maelezo ya taarifa zilizoko katika 1:16-18.
Maelezo ay Aya-kwa-Aya
(Namba zilizo katika mabano ni namba za kuonesha aya zinazojadiliwa.)
(1:1) Paulo alitoa taarifa tatu zinazohusiana na yeye mwenyewe.
Kwamba alikuwa ni mtumwa wa Yesu Kristo.
Kwamba alikuwa ni mtume kwa sababu wito wa Mungu kwake ulimfanya awe hivyo.
Kwamba alikuwa sehemu ya kazi ambayo alikuwa ameitiwa.
Paulo hapo kwanza alikuwa Mfarisayo, lakini sasa alikuwa amejitolea kwa ajili ya huduma. Paulo alikuwa na uraia wa Kirumi, lakini hakutaja ukweli huo kama sehemu yake ya utambulisho. Kama angefanya hivyo, haingeweza kumsaidia kuchangamana na waamini wengi wa Kirumi. Watu wengi waliokuwa wanaishi Rumi hawakuwa na uraia kwa sababu walikuwa ni wageni au watumwa. Kama ingetokea Paulo akataja uraia wake, ingepelekea yeye kuwekwa katika daraja la juu katika Rumi: ilikuwa ni muhimu kwake kutambulisha jukumu lake la kiroho.
(1:2) Injili haikuwa ni mpya kabisa lakini ilikuwa ndani ya ujumbe wa manabii wa Agano la Kale. Warumi 4 inaonesha hasa kwamba injili ilikuwa inaeleweka kwa Ibrahimu na Daudi.
(1:3-4) Katika hali yake ya asili, mwana wa Mungu alikuwa ni wa uzao wa Daudi kwenye mtiririko wa kifalme ambao ulikuwa umetabiriwa kwa ajili ya Masihi.
Kristo ni neno la Kigiriki linalotokana na neno la Kiebrania Masihi.
Neno Bwana linarejelea uungu wake. Umuhimu wa neno Bwana katika nyaraka za Agano Jipya zinaweza kuonekana zikifanana ukilinganisha Wafilipi 2:10-11 na Isaya 45:23. Ni marejeo kuhusu mmoja aliye mkuu sana juu ya mamlaka nyingine zote. (Ona pia Matendo 2:36.)
Neno Bwana halina ulazima wa kumaanisha kitu kile kile katika Injili za Agano Jipya, wakati ambapo watu wangeweza kumwita Yesu “Bwana” kama neno la heshima bila ya kuelewa kwa uhakika kwamba alikuwa ni Mungu.
Katika Nyaraka za Agano Jipya, neno “Yesu Kristo Bwana wetu” linatoa utambulisho wa aina tatu tofauti. Linasema kwamba yeye ni mtu wa kihistoria aliyeitwa Yesu, yeye ni Masihi wa Kiyahudi, na yeye ni Mungu.
Ufufuo ulithibitisha uungu wa Yesu. Katika Yohane 10:18, alijinadi kwamba anaweza akaurejesha uhai wake tena. Aliufanya ufufuo kama alama ya kizazi kile, na mashuhuda wa ufufuo waliufanya kama ni alama kwa ajili ya vizazi vyote. Mtu ambaye siyo Mungu hawezi akajifufua mwenyewe kutoka katika wafu; aidha Mungu hangeweza kumfufua mtu anayejinadi kwa upotofu kwamba yeye ni Mungu, hasa mtu anayejinadi kwamba ufufuo utathibitisha utambulisho wake.
► Watu wengine waliwahi kufufuliwa kutoka katika wafu, lakini hawakuwa Mungu. Ni kwa jinsi gani utaweza kuelezea kwamba ufufuo ulithibitisha uungu wa Yesu?
(1:5) Wito na karama za kiroho za kitume zilitolewa kwa kusudi la kuwaleta watu wote wa mataifa yote kwenye utiifu kwa Kristo. Njia pekee ya matumizi sahihi ya karama za kiroho ni kwa ajili ya matendo ya Bwana. Lengo pekee la matendo ya huduma ni kwa ajili ya utukufu wa jina la Kristo. Malengo kama ya mafanikio binafsi au umashuhuri wa binafsi ni mambo yasiyofaa kwa mtumishi wa Mungu.
Upekee wa Wito wa Utume
► Je, siku hizi wako mitume walio hai?
Neno mtume wakati mwingine linatumika katika Biblia katika maana yake ya ujumla ya “mtu anayetumwa.” Katika Matendo 14:14, Paulo na Barnaba wanaitwa mitume, ingawaje Barnaba hakuwa mmojawapo katika mitume halisi kumi na mbili wa awali. Katika Wagalatia 1:19, Paulo alisema kwamba katika safari yake moja maalumu hakuwahi kumwona mtume yeyote Zaidi ya Kefa (Petro) na Yakobo nduguye Bwana Yesu, Kwa hali hiyo, alimtaja Yakobo kama mtume, ingawaje hakuwa miongoni mwa mitume kumi na mbili wa awali.
Hata hivyo, mitume kumi na mbili wa awali kwa kawaida walichukuliwa kama ni kundi maalumu, ambalo hakuna mtu mwingine atakayeongezwa katika kikundi hicho. Katika Mathayo 10:2 panasema, “Na majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya…” (Angalia pia katika Luka 6:13). Yesu aliwaambia mitume kwamba wataketi katika viti vya enzi, huku wakiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli, (Luka 22:30). Ahadi inaonekana kuwa ni zawadi maalumu kwa mitume kumi na mbili pekee. Majina ya mitume kumi na mbili yako katika misingi kumi na mbili ya jiji la Mungu, jambo linaloonyesha upekee wa kundi hili la mitume kumi na mbili (Ufunuo 21:14).
Yuda aliyekuwa nduguye na Yesu hakujiita mwenyewe mtume lakini alirejea kwenye mamlaka yao (linganisha Yuda 17 na 2 Petro 3:2). Mitume walikuwa na mamlaka ya kipekee, na lolote waliloandika kwa ajili ya makanisa lilichukuliwa kama ni ufunuo (2 Petro 3:15-16).
Kanisa lilimteua Mathiasi kuwa badala ya Yuda, kwa kutegemewa kwamba kungekuwepo na mitume kumi na mbili (Matendo 1:26); lakini hatuoni kutoka katika historia kwamba kanisa la mwanzo lilikuwa linaendelea kuweka mitume badala ya wale waliokuwa wakifariki.
Paulo aliitwa kuwa mtume (Rum 1:1). Paulo anaashiria kuwa mojawapo ya sifa yake ya kuwa mtume ni kwamba alikuwa amemwona Yesu. (1 Wakorintho 9:1). Hali hiyo inaweka ukomo wa utume kwenye kizazi cha kwanza cha kanisa.
Kifungu cha kujifunza – Warumi sehemu ya 1
Mwendelezo wa maelezo ya Aya-kwa-Aya
(1:6) "Kuitwa" kunahusika na wito wa kuokoka, kuwa watu watakatifu, kama inavyoonekana kwenye aya inayofuata. (Ona pia 8:30). Paulo alikuwa amesema kwamba mitume wana huduma kwa ajili ya mataifa yote; na sasa anaonesha kwamba Wakristo wa Rumi ni waamini waliotokana na ujumbe wa mitume. Kwa hali hiyo anaonyesha kwamba wanapaswa na wanawajibika kuzingatia kwa umakini sana mamlaka yake ya kitume. Waraka huu haukuwa umetokana na mmisionari wa kawaida waliokuwa wamewahi kumsikia. Walikuwa makini katika kumsikiliza na kumheshimu, ingawaje hakuwa mwanzilishi wa kanisa lao.[1]
(1:7) Kuitwa kwenye wokovu ni kuitwa kuwa mtakatifu. Taarifa hii inalinganishwa na iliyoko kwenye aya ya 1, ambapo Paulo alisema kwamba alikuwa ni mtume kwa sababu ya kuitwa kuwa mtume. Haina maana kwamba alikuwa anajaribu au anategemea kuwa mtume, bali alikuwa amefanywa kuwa mtume kwa njia ya wito. Waamini wa Rumi walifanyika kuwa watakatifu kutokana na wito wa kuwa watakatifu. Kama ilivyo kwa wito wa kuwa mtume kuambatana na karama za kiroho na uwezo kwa ajili ya huduma hiyo, wito kwa ajili ya kuwa watakatifu unaambatana na uweza na utakaso unaotufanya sisi tuwe watakatifu. Wito wa Mungu siku zote unaambatana na neema ya kuwezesha kutekeleza huo wito.
Utakatifu uanzapo wakati wa kuokoka huwa haujakamilika katika nyanja zake zote. Mtu aliyeamini anapaswakuwa na mabadiliko endelevu ya maisha yatakayofanania ukweli wa Mungu jinsi atakavyokuwa anaendelea kujifunza ukweli huo. Utakatifu siyo mkamilifu wakati mtu anapookoka; bali utakatifu unaanzia kwenye kuokoka wakati mwenye dhambi anapotubu, anapojiachilia kabisa kumtii Mungu na kufanywa kiumbe kipya (2 Wakorintho 5:17).
(1:8) Neno dunia lilikuwa linatumika kikawaida katika kurejelea kwenye dunia iliyokuwa inajulikana na ambayo ilikuwa ya kistaarabu na siyo ulimwengu wote. Injili ilikuwa bado haijaenda kila mahali ulimwenguni.
(1:9) "Neno latreuo [Ninatumika] liko ndani ya Agano Jipya na siku zote linatumika kwenye huduma za kidini… Huduma hii inaweza ikahusisha aidha kuabudu au kwenye shughuli nyingine za utendaji za nje zinazohusiana na mambo ya kidini."[2] Paulo alimtumikia Mungu siyo kwa jinsi ya shughuli za kidini tu, bali kwa roho yake.
(1:10-12) Hapa Paulo aliwaambia kwamba amepanga kuitembelea Rumi. Alitaka kuwajenga kiroho na alijua kuwa imani ya kila mtu ingefarijiwa.
Maelezo ya Paulo yanatuambia kwamba waamini wanafaidika kiroho kutokana na kushirikiana wenyewe kwa wenyewe. Roho Mtakatifu hukamilisha matendo yake makubwa ndani ya waamini kupitia kwa waamini wengine. Mtu anayepuuzia uhusiano wake na waamini wengine anapoteza neema ya uwezeshwaji inayokuja kupitia ushirika wa pamoja. (Paulo alizungumzia kwa mapana sana kuhusu hitaji alilo nalo kila Mtu aliyeamini kwa ajili ya waamini wengine katika 1 Wakorintho 12.)
(1:13) Paulo alizuiwa katika mpango wake wa kwanza wa kuwatembelea – siyo kutokana na matatizo, bali kutokana na kipaumbele chake cha kuhubiri injili katika mahali ambapo ilikuwa haijawahi kuhubiriwa au kusikika (ona 15:20-22). Kwa kuwa injli ilikuwa tayari imeshahubiriwa katika Rumi, Paulo alikwenda kwanza katika maeneo mengine. Hata hivyo, ujio wake wa sasa haukuwa kinyume na kipaumbele chake kwa kuwa ziara yake ingekuwa ni hatua moja katika kufika kwenye eneo lingine ambalo halijawahi kufikiwa na injili. (15:23-24).
(1:14) Wayunani walikuwa ni watu wa utamaduni na waliokuwa wamestaarabika kutokana na ushawishi wa Kiyunani. Neno mshenzi linamaanisha “mgeni,” likihusisha mtu aliyetoka kwenye utamaduni wa kijahilia zaidi ambao ulikuwa bado haujaguswa na utamaduni wa Kiyunani. Wayunani waliwachukulia hawa washenzi kama watu wasiokuwa na ustaarabu na tena ni wajinga.
Neno hekima linahusika na watu waliokuwa wameelimika, hasa katika falsafa ya Kiyunani; Watu wasiokuwa na hekima walikuwa ambao ni bado hawajaelimika kwa kiwango cha juu. Paulo alionesha kwamba huduma yake haikuwa na ukomo kwa ajili makundi malumu ya watu. Hali hii ilimwezesha kuandaa huduma yake kwa ajili yao, pamoja na kuonesha jukumu lake kama mmishenari.
Paulo alisema kwamba alikuwa na deni kwa kila mtu aliyekuwa na hitaji la kuisikia injili. Paulo hakuwa na deni kwa sababu wenye dhambi walistahili kusikia, bali ni kwa sababu alikuwa amepokea neema na alikuwa na wajibu wa kuitoa neema hiyo.
Kielelezo: Kama endapo mtu atampatia Elifuraha fedha ili ashirikiane na Yohane, Elifuraha sasa anadaiwa deni na Yohane hata kama Yohane hakufunya jambo lolote katika kujipatia fedha hizo. Katika hali kama hii, tunalo deni kwa wale ambao hawajawahi kuisikia injili, kwa sababu Mungu ametupa sisi jukumu la kushirikishana injili hiyo pamoja nao.
► Je, kila Mkristo analo deni analodaiwa la kushirikisha injili kwa wengine?
(1:15) Paulo alikuwa amehubiri kwa wayunani na washenzi, na sasa alikuwa anatamani kuhubiri injili kwa watu wa Rume vile vile.
Anaanza kutoa hoja yake kwa kusema, “mimi ni tayari kuihubiri Injili hata na kwenu,“ kisha akaelezea kwa kifupi injili ni nini na ni kwa nini dunia inaihitaji. Ufafanuzi huu kwa ufupi umepanuliwa vizuri katika waraka wote.
1:14-15 inatuonyesha tena ni kwa nini Paulo alikuwa na sifa za kuja kwao. Alikuwa na ujumbe uliomhusu kila mtu katika ulimwengu huu.[3]
(1:16) Injili ni kwa ajili ya Wayahudi na Wayunani, na mada hii inatambulisha kichwa cha habari juu ya Wayahudi na Wamataifa na msimamo wao mbele ya Mungu. Mada hii inaendelea hadi kwenye Warumi 3. Paulo haionei haya injili hata ingekuwa katikati ya mamlaka ya dola, kwa kuwa injili ni uweza wa Mungu.
Nguvu ya Mungu inatenda kazi katika ujumbe wa injili, ikiufanya ujumbe huo uwe na uwezo wa kuokoa. Amri za Mungu siku zote zinaambatana na nguvu inayohitajika katika kuzitekeleza. Nguvu ya Mungu iko katika matendo wakati yanaposemwa maneno yake.[4] Wapelekaji wa injili wanategemea nguvu iliyoko ndani ya injili kwa sababu wanapokuwa wanawakilisha ujumbe, Roho Mtakatifu huufanya ujumbe huo uwe na ushawishi na uwezeshaji kwa wasikilizaji.
Kwa Paulo, kusimama kwa ajili ya injili hakukuwa na maana tu ya kuitetea injili kama ukweli halisi, lakini pia kuihubiri kama ukweli unaobadilisha. Aliitangaza kwa ujasiri kwamba itawabadilisha wasikilizaji wake.
► Je, kwa nini tunapaswa kuwa na ujasiri wakati tunapohubiri injili?
(1:17) Mtu anafanywa mwenye haki kwa Imani na ataishi kwaimani.[5] Huu ni ukweli mkuu na muhimu katika kitabu cha Warumi.
[6]Waraka wote wa Warumi unashughulika na jinsi ambavyo mwanadamu anaweza kufanywa mwenye haki (kuwa na haki itokanayo na Mungu). Umuhimu wa suala hili unaoneshwa katika aya inayofuata, kwa maana ghadhabu ya Mungu iko tayari kwa wale wanaobakia kuwa wenye dhambi.
Haki ya Mungu inayozungumziwa hapa siyo “ile sifa yake ya kuwa mwenye haki… bali haki inayotiririka kutoka kwake na kukubaliwa na yeye,"[7] haki ya Mungu inayofanya kazi ndani ya wanadamu kupitia katika imani yao. Wazo linalofanana na hili liko katika Wafilipi 3:9: “Haki ile itokayo kwa Mungu, (ek) kwa imani.” Watu hawahesabiwi kuwa wenye haki tu kwa sababu ya msamaha, lakini wanaanza kuwa wenye haki kwa ukweli kwa sababu Mungu amewabadilisha.
[8]Ukiendelea zaidi kwenye hiyo barua (Warumi 3:21-22), Paulo alisema kwamba wenye haki wa Mungu ambao ni kwa njia ya imani katika Yesu ni kwa ajili ya wale wote ambao wataamini. Katika Warumi 5:17-19 tunasoma kuhusiana na karama ya haki ambayo hufanya watu wengi kufanyika wenye haki.
Maneno “kutoka imani hadi imani” yanasisitiza kwamba imani ndiyo njia peke yake ya kupata haki. Msisitizo huu unaendana na dhana ya Kiprotestanti ya imani peke yake kama hitaji la kupata wokovu.
Katika kitabu cha Warumi, neno kifo linahusika na hukumu ya Mungu. Wale tu wanahesabiwa haki kwa Imani wataishi – hiyo ni kusema wataepuka hukumu (angalia 1:18) Laana ya Mungu itamwagwa juu ya watu wote isipokuwa tu kwa wale watakaoepuka kwa njia hii.
► Je, inamaanisha nini kwamba mtu anafanywa mwenye haki kwa imani?
► Kwenye kifungu hiki, je, inamaanisha nini kuishi? Kifo ni nini? Inamaanisha nini kuishi kwa njia ya imani?
“Nia ya jumla ya barua hii ni kuutangaza umilele, kusudi au amri ya Mungu isiyobadilika, ambayo ni: ‘Kila aaminiye ataokoka: Kila asiyeamini ataangamia.’”
- John Wesley,
“Predestination Calmly Considered”
Wanateolojia watatu waliobadilishwa na Kitabu cha Warumi
Waraka bado unahifadhi kusudi lake la awali la kutoa msingi wa matendo ya umishenari. Hata hivyo, waraka huu unafanya zaidi ya hapo. Wakati Paulo alipokuwa akielezea ni kwa nini kila mtu anapaswa asikie ujumbe, alielezea kwa kinagaubaga kwamba ujumbe ulikuwa ni nini na kwa nini watu wanaweza tu kuokolewa kupitia njia hii. Alijihusisha na baadhi ya vipingamizi vya kawaida. Maelezo haya na utetezi wa ujumbe aliouhubiri unachukua sehemu kubwa ya kitabu na unathibiti muundo wake.
Warumi ni maelezo kuhusu teolojia ya wokovu. Teolojia ya wokovu ya Paulo ilitoa utetezi wa haraka dhidi ya Wayahudi,[1] na unatumika pia kufanya masahihisho yaliyopo wakati huu wa sasa kwenye mafundisho ya imani kuhusiana na wokovu.[2]
[3]Kupitia historia, Mungu amekuwa akitumia waraka huu wa Warumi katika kurejesha kweli nyingi muhimu za msingi katika wakati ambapo zilikuwa zimesahaulika.
Akiwa kijana, Augustine alitafuta kuridhika katika uhusiano wa uovu na falisafa na masomo ya taaluma. Aliitafuta kweli na akaipata katika ukristo. Lakini bado kuipenda dhambi kwake kukamfanya kuwa mateka. Akajiona kuwa yeye ndiye mtu anayeelezewa katika Warumi 7. Aliijua kweli lakini akawa hana uwezo kabisa wa kuishi maisha yenye haki.
Augustine
Mwaka 386 BK, baada ya kusoma Rum 13:13-14, katika umri wake mwanzoni mwa miaka thelathini, Augustine aliamua kuacha maisha yake ya dhambi. Mungu alimfungua kutoka vifungo vya dhambi na kumwezesha kuishi maisha ya utauwa katika Yesu Kristo.
Katika miaka iliyobakia ya uhai wake, Augustine[4] Mungu alimtumia Augstine kwa nguvu. Maandiko yake yalitetea mafundisho ya kweli dhidi ya falisafa za uongo. Wazo maarufu lililokuwapo wakati huo ni imani kuwa watu ndani yao wana uwezo kuwa wenye haki na kwa hiyo wanaweza kuchagua kutokuwa wenye dhambi. Kutoka Warumi 5, Augustine alifundisha kuwa watu wanazaliwa wakiwa na dhambi ya asili ambayo huwafanya kutomtii Mungu. Asili hii hufanya kuwa vigumu mtu kumpendeza Mungu kikamilifu usipohitaji neema yake. Augustine alifundisha na akashuhudia neema ya mungu kwamba huwafanya watu kuwa wenye haki mbele ya Mungu.
Martin Luther
Katika mwaka 1515 B.K., Martin Luther alielewa maana ya Warumi 1:17 baada ya kuwa ametafuta kwa miaka mingi kuhusu uhakika wa wokovu.[5] Luther alikuwa ameshajaribu kutafuta amani ya kiroho kwa kufuata maisha ya utawa kwa bidii ya ziada. Aliomba kwa kufunga, alifuata ibada zote za Ukatoliki, na hata alijipiga mwenyewe. Ni wakati alipokuwa akitambaa kwa magoti yaliyokuwa yakivuja damu kwenye ngazi za kuingia kwenye Kanisa la Mtakatifu Petro katika mji wa Roma alipopokea kwa ghafla ufahamu wa neema kutoka kwa Mungu kwa njia ya imani.
Aliona kwamba mtu ambaye ataepushwa na hukumu ya Mungu ni yule tu ambaye anaamini ahadi ya Mungu ya kusamehe. Uhakika huu ulifanyika ni msingi wa ujumbe wake kwamba imani peke yake ndio njia inayoweza kutufanya tuokolewe.
John Wesley
Kwenye mwaka wa 1738 B.K., John Wesley alipata uhakika binafsi wa wokovu aliokuwa ameutafuta kwa miaka mingi.[6] Wesley alikuwa mwanazuoni wa Biblia mwenye bidii kubwa na aliyeishi kwa uangalifu katika Maisha yake ya kidini. Alishawahi hata kwenda kwenye umishenari kwa miaka miwili kwa wenyeji wa Kihindi wa Amerika lakini hakuwahi kupata uelewa sahihi wa injili yeye mwenyewe. Akiwa kwenye meli wakati kukiwepo na mawimbi baharini, aliona familia ya Kimoraviani ambayo ilikuwa imekaa kwa amani kabisa ikimtumainia Mungu na haikuwa na hofu ya kifo, na Wesley alitambua kwamba alikuwa hana imani ya aina hiyo.
Wesley aliona katika Maandiko kwamba kubadilika ni kitendo kinachofanyika kwa haraka. Pia alikutana na ndugu wawili wa Kimoraviani ambao walimshuhudia kwamba walikuwa na uhakika binafsi wa wokovu. Alianza kutambua kwamba alihitaji kupata uzoefu kamili wa kuongoka. Mabadiliko yake yalitokea alipokuwa kwenye kikao nyumba fulani kwa ajili ya kujifunza na kuomba. Wakati mtu fulani akisoma kile Martin Luther alichoandika kuhusu kitabu cha Warumi, Wesley alisikia moyo wake “ukiwaka moto kimaajabu.” Akasema, “Ninajisikia kuwa mtu niliyemwamini Kristo, Kristo peke yake kwa ajili ya wokovu wangu: na nikapewa uhakika kwamba amezichukua dhambi zangu na ameniokoa kutoka katika sheria ya dhambi na kifo."[7]
Kutokana na watu wote hawa watatu, kuelewa ujumbe kulileta uhamasisho wa bidii sana ya uinjilisti. Kitabu hiki bado kinaendelea kukamilisha kusudi lake na kutoa msingi wa huduma za umisheni kwa kuelezea teolojia ya wokovu.
► Je, kuna athari gani unazoweza kufikiria ambazo kitabu cha Warumi kinaweza kuwa nazo kwenye maisha na huduma yako?
[1]Wayahudi wanaelezewa baadaye katika fundisho hili.
[2]Warumi na Wagalatia mara nyingi wanawekwa katika fundisho la pamoja, kwa sababu Wagalatia kwa kiwango kidogo wanahusika kwa kina na baadhi ya mambo ya kufanana ya dhamira mbalimbali za injili.
[7]John Wesley, The Works of John Wesley, Vol. I (Kansas City: Nazarene Publishing House), 103
Maswali ya Mapitio Somo la 1
(1) Je, kwa nini Paulo aliandika waraka kwa Warumi kwa waamini wa Rumi?
(2) Je, kwa nini Paulo alipanga kwenda Rumi?
(3) Je, Maana ya msemo Yesu Krsito Bwana wetu una maana gani katika nyaraka za Agano Jipya?
(4) Je, ufufuo unathibitishaje uungu wa Yesu?
(5) Elezea msemo wasio wayunani (Warumi 1:14).
(6) Kwa nini Mwinjilisti Paulo ana deni la kuhubiri injili?
(7) Je, ni kitu gani kikuu na ukweli muhimu katika kitabu cha Warumi?
(8) Je, kifo kina maana gani katika kitabu cha Warumi?
(9) Kulingana na Warumi, ni nani analindwa asipate hukumu ya Mungu?
Kazi ya kufanya Somo la 1
(1) Kwa kutumia kifungu kutoka katika somo hili, andika ukurasa mmoja kuhusu huduma ya injili. Elezea kuhusu wito kwenye huduma, deni alilo nalo mwinjilisti kwa ajili ya wale wenye hitaji la kuisikia, na kuhusu nguvu ambayo Mungu hutoa kwa ajili ya ujumbe unaotolewa.
(2) Kwenye wiki kadhaa za kozi hii, utaandaa masomo ya mahubiri matatu yenye msingi wake kutoka katika kitabu cha Warumi na uyawakilishe kwenye vikundi vingine visivyokuwa darasa lako. Kila baada ya kuwasilisha, utawauliza wasikilizaji wako ni kwa jinsi gani uwakilishwaji huo unaweza ukaboreshwa. Utapaswa umpe kiongozi wa darasa nakala ya kumbukumbu ya yale uliyowasilisha, maelezo ya kikundi na tukio ulikofanyia uwasilishaji, na mipango yako ya kuboresha uwasilishaji ulioufanya.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.