► Jadili uhusiano kati ya tafsiri na matumizi katika ujifunzaji wako wa Biblia wa sasa. Unapohubiri au unapofundisha kipi ni rahisi: kutafsiri andiko au kutumia katika ulimwengu wa leo? Unapojifunza andiko au unaposikiliza mahubiri, Je, unaweza kupata matumizi katika maisha yako?
Amani alisema, “Mchungaji, tunaweza kukutana? Nina swali kubwa kuhusu Biblia” Baadae katika juma lile, mchungaji alikutana na Amani na waliangalia vifungu mbalimbali ambavyo vilizungumzia suala ambalo alilipitia Amani. Baada ya dakika chache, Amani alifunika Biblia yake na kusema, “Ngoja niwe muwazi. Tayari ninajua Biblia inasema nini lakini sitaki kufanya hivi. Ni ngumu sana kwangu.”
[1]Tatizo la Amani halikuwa tafsiri, tatizo lilikuwa matumizi. Haitoshi kuangalia tu nini andiko linasema na kutafsiri maana yake ni lazima tulitumie katika maisha yetu. Mara nyingi sana, kujfunza Biblia huishia kwenye hatua ya tafsiri.
Tunaanza kwa kuchunguza andiko linasema nini; tunaendelea kwa kutafsiri linasema nini; lazima tuishie kwa kulitumia kwenye maisha yetu. Tunaweza kufupisha mchakato huu kwa maswali matatu:
Andiko linasema nini? (Uchunguzi)
Andiko linamaanisha nini? (Tafsiri)
Ni kwa namna gani andiko linafanya kazi katika maisha yangu? (Matumizi)
“Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.”
- Yakobo 1:23-24
Mbadala wa Matumizi
Mzaburi aliandika kuwa, mtu ambaye anapendezwa na sheria ya Bwana na kuitafakari sheria yake, atakuwa “kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake” (Zaburi 1:2-3). Shetani anajaribu kutuweka nje na neno la Bwana. Anafahamu kuwa tutadhoofika na kufa kiroho kama hatutajilisha neno la Mungu.[1]
Endapo hatatutoa nje na neno la Mungu, Shetani atajaribu kutufanya tusitumie ukweli huo katika maisha yetu. Kwa kadiri ambavyo hatutumii neno la Mungu, hatutazaa matunda. Endapo shetani hataweza kutufanya tusisome Biblia, atatujaribu ili kukubali mbadala wa matumizi.
Tafsiri inakuwa mbadala wa Matumizi
Inawezekana kujifunza maandiko kwa makini na kupata maana pasipo kuweka katika matendo. Daudi aliposikia hadithi ya Nathani kuhusu tajiri aliyeiba kondoo wa masikini, alijibu kwa tafsiri sahihi. “…Aishivyo BWANA, mtu huyo aliyetenda jambo hili, hakika yake astahili kufa; naye atamrudishia yule mwana-kondoo mara nne, kwa sababu ametenda neno hili, na kwa sababu hakuwa na huruma” (2 Samweli 12:5-6).
Tafsiri ya Daudi ilikuwa sahihi. Alijibu kwa jina la Bwana akisisitiza haki, alihitaji fidia. Hakuna anayeweza kuipinga tafsiri ya Daudi, lakini Daudi alishindwa kuutumia mfano katika maisha yake. Nabii ndiye alifanya matumizi, “Wewe ndiwe mtu huyo” (2 Samweli 12:7).
Hii ni hatari ya kipekee kwa wahubiri na waalimu. Tunaweza kufundisha maandiko kwa wengine wakati tukipuuza kutotii kwetu wenyewe. Yakobo alionya kuhusu tafsiri pasipo utii. “Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi” (Yakobo 4:17). Baada ya kuwa tumetafsiri maandiko sawasawa, hatupaswi kushindwa kuyaweka katika vitendo. Hatupaswi kufanya tafsiri kuwa mbadala wa matumizi.
Utii Kwa Sehemu unakuwa mbadala wa Utii Kamilifu
Inawezekana kujifunza kifungu cha maandiko, kutambua maana yake, na kutafuta matumizi ya baadhi ya maeneo pasipo kuruhusu kutubadilisha kikamilifu. Tunaweza kutafuta baadhi ya maeneno ambayo tutatii andiko, lakini tunaweza kupuuza maeneo ya ndani na muhimu kabisa ya kutotii katika maisha yetu.
Pengine tumekuwa kukijifunza Waefeso 4:29, “Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia.” Katika hatua ya matumizi, tunapima mahusiano yetu ya umuhimu. Tunauliza:
“Je, ninatumia maneno ya kujenga kwa watoto wangu?” “Ndio; Mimi ni mzazi mwenye upendo.”
“Je, ninamjenga mwenzi wangu?” “Hapana; mara nyingi nina mtazamo hasi katika majibu yangu.”
Mawasiliano yako na mwenzi wako ni mahali ambapo Roho wa Mungu anataka kukubadilisha. Shetani anakujaribu ili uweke mbadala wa utii katika maeneo mengine yanayobadilisha maisha, kuhusiana na matumizi ya andiko hili katika uhusiano wako na mwenzi wako. Anakujaribu kukubali utii kwa sehemu badala ya kujitoa kwa utii kamilifu.
Tunafanya Visingizio kuwa Mbadala wa Toba
Mwana sheria alimuuliza Yesu, “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” (Luka 10:25). Mwanasheria alikuwa tayari anafahamu jibu: “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako” (Luka 10:27).
Mwanasheria aliyaelewa maandiko “Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu, Na jirani yangu ni nani?” (Luka 10:29). Tatizo lake halikuwa tafsiri; tatizo lake lilikuwa matumizi. Mwanasheria alihalalisha ukosefu wake wa upendo.
Pengine Roho wa Mungu anasema na wewe, “Maneno yako hayamjengi mwenzi wako; hayo ni mawasiliano mabovu yanayoharibu.” Umesoma neno, umetafsiri neno, sasa ni muda wa kutumia neno. Badala yake, unaweza kufikiri, “mwenzi wangu kila mara ana mtazamo hasi. Kama nina mtazamo hasi, ni kwa sababu mwenzi wangu ana mtazamo hasi. Siyo kosa langu!” Je, umefanya nini? Umeihalalisha tabia yako badala ya kutubu kwa sababu ya wewe kushindwa kulitii neno la Mungu.
Tunafanya Hisia kuwa Mbadala wa Kubadilishwa
Yakobo aliandika kuhusu mtu anayesikia neno lakini halifanyii kazi (Yakobo 1:23-24). Wakati mwingine mtu anasikia neno na anaguswa kabisa, lakini anaruhusu mwitikio wa hisia kuwa mbadala wa badiliko la kweli. Kila mchungaji anajua kukatishwa tamaa katika kuhubiri ujumbe juu ya mada fulani, hasa watu wanaposema “Mahubiri yale yalinigusa sana,” na kisha kuona mabadiliko yasiyodumu
Huenda unasikia Waefeso 4:29 ikifundishwa kwenye semina ya ndoa. Wakati wa muda wa kuweka ahadi mwishoni mwa semina, unamwambia mwenza wako, “Samahani. Ninataka kuzungumza maneno chanya. Nitafanya vizuri!” Lakini punde, unarudi tena katika tabia za zamani za maneno makali, hasi, na mazungumzo yanayoumiza.
Nini kimetokea? Kulikuwa na mwitikio wa kihisia, na siyo mabadiliko ya kweli. Hii ni hatari, baada ya kushindwa kunakojirudia rudia, tunaamini kwamba mabadiliko hayawezekani. Mwitikio wa kihisia juu ya kweli lazima unaambatana na mabadiliko ya kweli na utii, ambavyo vinawezekana tu tunapojinyenyekeza kwa kazi ya Roho Mtakatifu.
[1]Nyenzo katika somo hili zimechukuliwa kutoka Howard G. Hendricks na William D. Hendricks, Living by the Book (Chicago: Moody Publishers, 2007).
Hatua za Kutumia Maandiko
Baada ya kumwelezea mtu anayejitazama katika kioo na akasahau jinsi alivyo. Yakobo amwelezea mtu ambaye analitumia andiko katika maisha yake. “Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake” (Yakobo 1:25). Haitoshi kulisikia neno la Mungu, tunatakiwa kulitendea kazi Neno. Kipi ni kinahitajika ili kutendea kazi andiko?
Ili kulitendea kazi kikamilifu Neno la Mungu, unahitaji kufanya mambo matatu.
Hatua ya 1: Fahamu maana ya Andiko
Ndiyo maana somo kuhusus uchunguzi na tafsiri ni muhimu sana. Iwapo hatufahamu andiko, matumizi yetu hayatakuwa sahihi. Tunaanza hatua ya matumizi kwa kuuliza, “Ni kwa namna gani Wakristo wa karne ya kwanza waliweza kutumia andiko hili katika ulimwengu wao?”
Kwa mfano, Paulo aliandika, “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu” (Wafilipi 4:13). Baadhi ya waalimu wamelichukulia ndiko hili kama ahadi kwamba tunaweza kupata chochote tunachokihitaji kwa sababu, “Kristo ananitia nguvu.” Mwanariadha anatangaza, “Nitashinda mchezo wa leo kwa sababu ‘Ninayaweza mambo yote katika Kristo.’” Waponyaji wa kiimani wanawahakikishia wasikilizaji wao, “Kama una imani ya kutosha, utaponywa, kwa sababu ‘Unayaweza mambo yote katika Kristo.’” Wahubiri wa mafanikio yasiyo ya kweli wanatangaza, “Mungu anataka kukufanya wewe kuwa tajiri. Unachotakiwa kufanya ni kushirikiana na Mungu. ‘Unayaweza mambo yote katika Kristo.’”
Tunapouliza, “Ni kwa namna gani Wakristo wa Filipi walilitumia andiko hili?” Tunagundua kuwa hii haikuwa ahadi ya mafanikio ya kidunia, bali ni ahadi ya kuvumilia kiroho. Paulo alikuwa gerezani kule Rumi; wapokeaji wake walikuwa wanapitia mateso. Hakumaanisha kwamba alikuwa na mafanikio ya kidunia, bali kwamba alikuwa na uwezo wa kuvumilia katika hali zote kwa imani na utii. Paulo alijifunza kuridhika katika hali zote katika Kristo, angeweza kufanya chochote ambacho Mungu alimtaka kufanya. Hii haikumaanisha maisha ya anasa; ilimaanisha kwamba hakupoteza roho ya kuridhika akiwa anapitia magumu.
Hatua ya 2: Elewa ni kwa namna gani Andiko linatumika katika maisha
Paulo alimuonya Timotheo kwamba ni lazima yeye mwenyewe afahamu kwanza ili aweze kuwahudumia wengine kwa ufanisi. “Jitunze nafsi yako, na mafundisho yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikiao pia” (1 Timotheo 4:16). Kwa kadiri Timotheo anavyoweka umakini kwake na kwa mafundisho ayayoyahubiri, ndivyo atakavyo watumikia kwa ufanisi wasikilizaji wake.
Baada ya kufahamu andiko na namna lilivyotumika kwa wasomaji wa kwanza, ni lazima nijifahamu mwenyewe na kuona namna linavyotumika katika ulimwengu wangu. Pengine ninajiangalia mwenyewe na kuona kwamba mara zote sitarajii Mungu kunibariki na kunisaidia. Wafilipi 4:13 inaniambia kukabialiana na changamoto kwa ujasiri kwa sababu “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.”
Sasa matumizi yanakuwa wazi na mahususi. Kama mstari pembeni mwa mstari huu, ninaweza kuandika hivi, “Ukiwa unafanya kazi katika mazingira ambayo yanapinga maadili ya kikristo, nitaiamini neema ya Mungu ili kunitia nguvu kuwa mwaminifu. Ninayaweza mambo yote katika Kristo.” Hii imechukua mstari toka karme ya 1 hadi karne ya 21.
Matumizi sahihi ya andiko yanafanya kazi katika ulimwengu halisi. Neno la Mungu linahusiana na maeneo yote ya maisha. Ninapotendea kazi andiko, siulizi, “Ni matumizi gani ya kidini ambayo yapo katika andiko hili?” Badala yake, Ninauliza, “Ni kwa namna gani nitaliishi andiko hili katika maeneo yote ya maisha?”
John Wesley aliandika, “Injili ya Kristo haijui dini yeyote bali jamii; hakuna utakatifu bali utakatifu wa kijamii.”[1] Tunaiishi Injili si kama watawa waliotengwa kutoka kwa wengine, bali kama waamini katika mahusiano na wengine. Tunakua katika utakatifu siyo kwa kujitenga na wengine bali ndani ya muktadha wa jumuiya ya kanisa.
Hapo awali, tuliangalia katika Waefeso 4:29. Ninapozingatia matumizi ya mstari huu, ninatakiwa kuutumia katika mahusiano na wakristo wenzangu: “Je, maneno yangu yanamjenga mwamini mwenzangu au yanavunja vunja?” Ninatakiwa kuhusianisha mstari na familia yangu: “Je, mazungumzo yangu yanajenga familia yangu, au yanaondoa nguvu ya ujasiri ya mwenza wangu na watoto?” Ninatakiwa kuhusianisha mstari na kazi yangu: “Je, mimi na mwajiriwa ambaye niazungumza maneno chanya, au ninasambaza mawazo hasi?” Waefeso 4:29 inahusiana na kila eneo la maisha.
Hii ndiyo sababu Paulo aliandika kwamba watumwa ambao wanaishi vema katika mahusiano na bwana zao wanayapamba mafundisho ya Mungu mwokozi wetu katika mambo yote (Tito 2:10). Matumizi sahihi ya kina ya maandiko yatafanya Injili kuwa ya kuvutia kwa watu wanaotuzunguka sisi.
Hatua ya 3: Tii Maandiko
Kusudi la juu zaidi la kujifunza Biblia kila siku ni Matumizi. Katika 2 Timotheo 2:3-6, Paulo anaelezea Wakristo kama askali, wanariadha, na wakulima. Picha hizi zinaelezea mtu ambaye anaendelea bila kuchoka ili kufikia lengo. Askali hapumziki wakati wa vita; wanariadha hapumziki katikati ya urefu wa riadha; mkulima hapumziki kulima hadi pale atakapomaliza kazi. Maisha ya Ukristo yanahitaji uvumilivu. “Tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu” (Waebrania 12:1).
Unapojifunza maandiko, uliza, “Je, kuna eneo la maisha yangu ambapo ninahitaji kuutendea kazi ukweli huu?” Mwombe Mungu akusaidie kutumia kweli katika maisha yako kwa utaratibu mzuri uliopangwa. Unapofanya hivi, Mungu atakufunulia kweli zaidi. Na hata utakuwa na shahuku kubwa ya chakula cha kiroho.
Endapo Mungu anazungumza na wewe kupitia Waefeso 4:29 ili kukuonesha kuhusiana na mazungumzo yako, unapaswa kujitoa ili kufanyia mazoezi mazungumzo yanayojenga. Hii inaweza kuwa rahisi endapo unamwomba Mungu akupe fursa kila siku ya kunena neema katika maisha ya mtu fulani. Inaweza kumaanisha kumwomba rafiki unayemwamini akuonye anapokusikia ukitumia mawasiliano yanayoharibu. Hii inaweza kuwa njia ya kutendea kazi Neno la Mungu kila siku.
Chuoni, palikuwa na kijana mmoja ambaye alikuwa anahangaika na majaribu katika maeneo fulani. Tahir alipenda muziki, pamoja na mtindo pamoja na maneno ya wimbo ambayo yangeweza kumjaribu katika udhaifu wake. Tahir alitaka ushindi dhidi ya jaribu, lakini hakuweza kuyatumia maandiko kwa uthabiti katika maisha yake.
Septemba, shule ilikuwa na ibada za uamsho. Tahir angeenda madhabahuni. Angerudi bwenini kwake na kutupa muziki wake ambao si sahihi. Kwa majuma kadhaa, angekuwa na ushuhuda mzuri. Baada ya muda mfupi angevunjwa moyo; Novemba, angesema, “Nimerudi nyuma.”
Febriari, shule ingekuwa na kongamano la Biblia. Tahir angeenda mbele madhabahuni. Angezitupa tena rekodi zake na angekuwa na ushuhuda mzuri kwa majuma machache. Kisha, Aprili, angenunua tena baadhi ya muziki na mchakato ungeanza tena!
Tahir alihitaji nini? Tafsiri nzuri? Hapana! Alifahamu maeneo ya udhaifu wake; alifahamu nini Biblia Inasema kuhusiana na kuwa na kutunza akili njema; alifahamu madhara ya baadhi ya muziki katika maisha yake ya kiroho. Tatizo la Tahir halikuwa tafsiri; alitakiwa tu kutendea kazi kile alichokifahamu.
Ni maeneo gani ya matumizi unayotakiwa kuyatendea kazi?
[1]Dibaji na John na Charles Wesley’s 1739 toleo ya Hymns and Sacred Poems.
Mswali ya Kuuliza
Itakuwa na msaada zaidi kuuliza maswali haya matano wakati unatafuta njia za kutendea kazi andiko katika maisha yako.
(1) Je, kuna dhambi ya kuepuka?
Wakristo wengi hukata tamaa wakati wanapoona kwamba eneo fulani katika maisha yao limeshindwa kufuata matakwa ya maandiko. Mungu anaposema na sisi kupitia neno lake kuhusiana na eneo la dhambi katika maisha yetu hatutakiwi kukata tamaa. Badala yake, tunatakiwa kuwa tayari kulitii neno lake.
(2) Je, kuna ahadi ya kuidai?
Wakati mwingine matumizi ni kuidai tu ahadi ya Mungu. Tunatakiwa kuwa makini na kutafsiri ahadi kwa usahihi. Baadhi ya ahadi zilikuwa ni kwa ajili ya watu fulani au kwa taifa la iasraeli. Tunatakiwa kuwa makini ili tusiichukue ahadi nje na muktadha. Hata hivyo, tunapokuwa tumetafsiri kwa umakini ahadi katika muktadha wake na kufahamu kwamba ni ahadi kwa waamini wote, tunaweza kuzidai ahadi hizo katika maisha yetu.
(3) Je, kuna hatua ya kuchukua?
Uliza, “Nifanye nini kwa sababu ya kifungu hiki cha andiko. Ni kweli gani ambayo kifungu hiki kinafundisha? Je, kinanionya kuhusiana na fundisho langu lisilo sahihi? Je, ninahitaji kubadilisha kufikiri kwangu ili kuwa sawa na maandiko? Ninatakiwa kufanya nini kwa sababu ya andiko hili?”
Mfano mmoja ni maombi. Tunaposoma maombi ya Daudi, Paulo, Nehemia, na Yesu, tunaona kielelezo kwa ajili ya maisha yetu ya maombi. Ni kujifunza vizuri kiasi gani kama kuyachukua maombi ya Paulo au Yesu na kuyafanya yangu! Ninaposoma, ninaweza kuchukua hatua katika kutendea kazi kwa kuchukua maombi ya hayo katika maisha yangu.
(4) Je, kuna Agizo la kutii?
Mara nyingi sehemu ya pili ya nyaraka za Paulo zinaundwa na maagizo. Maagizo haya mara nyingi ni rahisi na ya moja kwa moja. Wakati mwingine Wakristo wanatafuta kweli kuu, huku wakipuuza matumizi rahisi ya kile ambacho tayari wanafahamu!
Mtu mmoja aliandika kuhusiana na kutafuta kweli wa ndani zaidi huku ukipuuza ukweli ulio wazi. Alieleza kuhusu mafunzo yake ya kwanza juu ya Kiyunani cha Agano Jipya. Katika Mathayo 16:24, Yesu alisema, “Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.” Kiyunani cha asili hakina maana ya tofauti, inayoshangaza. Maana hii ni sawa kabisa na kile inachomaanisha. Siyo ngumu kuelewa maana. Badala yake, ni vigumu kutii.[1]
Wakati mwingine kinachohitajika ni rahisi sana, “Ndiyo, Bwana. Nitatii.”
(5) Je, kuna mfano wa kufuata?
Maandiko mengi yanajumuisha wasifu wa watu. Tunapososma wasifu, tunauliza, “Je, kuna mfano wa kufuata?”
Tunaposoma kuhusu Abrahamu katika Mwanzo 18, tunaweza kufuata kielelezo cha Abrahamu kwa kuuombea ulimwengu wetu. Mwalimu alikuwa anafundisha Nigeria. Nigeria imekuwa inasumbuliwa na mgogogro kati ya Waislamu na Wakristo. Mmoja wa wanafunzi akawaomba wanafunzi wenzake, “Kwa nini tunagombana na Waislamu kuliko tunavyowaombea? Je, tunaamini kwamba Mungu anaweza kuwaleta katika wokovu? Kama ni hivyo, tunatakiwa kufuata kielelezo cha Abrahamu na kuwaombea ili wapate wokovu!” haya ni matumizi.
Tumefanya uchunguzi kutoka katika Warumi 12:1-2. Tumejifunza neno juu ya maneno muhimu katika mistari hii. Tumejifunza muktadha wa kihistoria, kiutamaduni, na kibiblia ili kutafsiri kwa usahihi ujumbe wa Paulo.
Sasa tupo tayari kwa ajili ya hatua muhimu sana. Ni kwa namna gani utatendea kazi Warumi 12:1-2 katika maisha yako?
► Rejea tena nakili juu ya Warumi 12:1-2 ambazo ulizitengeneza hapo kabla katika somo llililopita. Kisha orodhesha mambo matatu mahususi utakayoyatenda ili kufanyia kazi andiko katika maisha yako.
► Endapo unajifunza somo hili katika kundi, shirikisha matumizi yako katika kundi. Endapo mtakuwa mnakutana tena hapo mbeleni, tengeneza uwajibikaji. Mfanye mtu awajibike na omba kundi kufuatilia kwa kukuuliza wewe namna unavyofanya matumizi yako.
Hitimisho
Kozi hii ni kuhusu kutafsiri Biblia ili kwamba tuweze kuwafundisha wengine. Huu ndio wito tulioitiwa kama waalimu wa neno la Mungu. Hata hivyo, kuna hatari katika hili. Kama hatutakuwa makini, tunaweza kujifunza Biblia kwa ajili ya kuhubiri na kufundisha tu. Tunaweza kushindwa kuutumia ukweli wa Biblia katika maisha yetu.
Kujifunza Biblia si kwa kusudi la kujifunza na kufundisha. Neno la Mungu linawea kulinganishwa na chakula kwa ajili ya kutujenga kimwili. Kula chakula kuna matokeo ya kila siku na ya muda mrefu. Hauwezi kushusha kiwango cha cholesterol yako kwa mlo mmoja wenye afya, haujengi afya ya kiroho kwa kujifunza Biblia siku moja. Inachukua mlo wa wenye afya wa mara kwa mara ili kujenga afya ya kimwili, na itachukua mlo wa muda mrefu wa neno la Mungu ili kujenga nguvu za kiroho. Lakini bado, mlo wa siku moja wa neno la Mungu ni muhimu kwa chochote utakachokutana nacho siku hiyo, kama ambavyo chakula cha asubuhi kinavyokusaidia katika kazi ya siku husika.
Kama wachungaji, waalimu, na viongozi wa kanisa, hatupaswi kusahau kwamba maisha yetu ya kiroho ni lazima yajengwe kila siku. Katika juhudi zetu za kuwafundisha wengine, kamwe tusisahau kuilisha mioyo yetu na mkate wa neno la Mungu. Ni hadi pale tu tutakapojijenga wenyewe ndipo tutakuwa na nguvu ambayo tunahitaji ili kuhudumia watu wa Mungu.
Paulo alikuwa anafahamu hatari hii. Aliandika kuhusiana na hofu yake kwamba asije kukataliwa baada ya kuwahubiri wengine (1 Wakorintho 9:27). Ni jambo baya sana sisi kuwafundisha wengine wakati tunaikataa neema ya Mungu katika mioyo yetu. Jifunze ili kufundisha wengine, lakini pia jifunze ili kumsikia Mungu akizungumza na moyo wako.
Weka katika Matendo
► Luka 14:25–17:10 ni mfululizo wa mifano na maelekezo. Yesu anaposafiri kwenda Yerusalemu kwa mara ya mwisho, alitoa maelekezo ya mwisho kwa wanafunzi wake. Unaposoma maelekezo ya Yesu, tafuta matumizi mahususi kutoka katika mistari hii. Uliza:
(1) Haitoshi tu kwa sisi kutafsiri kwa usahihi Neno la Mungu; tunapaswa kulitendea kazi katika maisha yetu ya kila siku.
(2) Shetani anatujaribu sisi ili kuwa na mbadala wa matumizi:
Tafsiri inakuwa mbadala wa Matumizi
Utii Kwa Sehemu unakuwa mbadala wa Utii Kamilifu
Tunafanya Visingizio kuwa Mbadala wa Toba
Tunafanya Hisia kuwa Mbadala wa Kubadilishwa
(3) Ili sisi kufanyia kazi maandiko katika maisha yetu, tunatakiwa kufuata hatua hizi tatu:
Fahamu maana ya andiko.
Elewa ni kwa namna gani andiko linatumika katika maisha.
Tii Maandiko.
(4) Ili kupata njia za kutendea kazi maandiko katika maisha yako, uliza maswali haya:
Je, kuna dhambi ya kuepuka?
Je, kuna ahadi ya kuidai?
Je, kuna hatua ya kuchukua?
Je, kuna Agizo la kutii?
Je, kuna mfano wa kufuata?
Somo la 9 Zoezi
Katika Somo la 1, ulichagua kifungu cha maandiko ambayo utayasoma wakati wote wa kozi hii. Kwa kutumia nakili ambazo umeziandaa katika Uchunguzi na tafsiri, tengeneza orodha ya hatua ya matumizi ya kivitendo kwa ajili ya andiko unalojifunza.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.