Kanuni katika somo hili ni msingi kwa ajili ya kujifunza maandiko. Hizi ni kanuni ambazo waalimu wa Biblia wenye busara wamezitengeneza ili kuongoza ujifunzaji wao. Kanuni hizi zinatakiwa kuwa msingi wa njia zako za kujifunza Biblia. Tafadhali chukua muda kuzielewa kanuni hizi na kisha uzitumie katika kujifunza kwako.
Zingatia Kusudi la Mwandishi
Mwandishi alikusudia kitu kwa wasomaji wake. Maana ile iliyokusudiwa ndiyo maana ya andiko. Tafsiri ni kazi inayojaribu kuuelewa ujumbe uliokususduwa na mwandishi. Hatutakiwi kutumia maandiko kama nyenzo kwa ajili ya ujumbe ambao ni tofauti na maana iliyokusudiwa na mwandishi.
Tamko la kimaandiko linaweza kumaanisha zaidi ya vile mwandishi alivyokusudia. Ibrahimu alipomwambia Isaka kwamba “Mungu atajipatia mwana-kondoo…” (Mwanzo 22:8), anaweza asijue kuwa Mungu atatimiza maneno haya katika namna kubwa zaidi katika ujio wa Yesu. Musa alipoandika maneno hayo ya Ibrahimu, musa anawezakuwa hakuwa anaelewa maana ya tamko hilo. Hata hivyo, kutumia tamko kwa ajili ya ujio wa Yesu si kutumia maana tofauti na iliyokusudiwa na Musa; ni matumizi mapana, yaliyokamilika ya kanuni ambayo Mungu anatoa kile ambacho kinatakiwa kwa ajili ya wokovu.
Kila mwandishi wa Biblia alikusudia kwamba wasomaji wake wa kwanza wautumie ujumbe wake katika matendo. Matumizi yetu ya ujumbe yanaweza kuwa tofauti na matumizi ya wapokeaji wa kwanza, lakini yanafuata kanuni zile zile. Kwa sababu tunatumia kanuni za kibiblia katika mazingira tofauti, matendo yetu yanaweza kuwa tofauti. Kwa mfano, watu wa Israeli waliambiwa waweke kingo katika dari za nyumba zao (Kumbukumbu la Torati 22:8). Dari za nyumba za wakati huo zilikuwa tambarare na zilitumika kama sehemu ya kuishi. Kama hauishi katika nyumba ambayo ina dari tambarare ambapo watu hawaendi, hauhitaji kingo. Hata hivyo, tunatakiwa kutumia kanuni ya kufanya mali zetu kuwa salama kwa ajili ya watu.
Mtafsiri hatakiwi kutengeneza tafsiri ya kufikirika kwa ajili ya taarifa katika kifungu. Hapa ni mfano wa tafsiri ya kufikirika ya Habari ya Yesu ya Masamaria mwema aliyemsaidia mtu aliyejeruhiwa (Luka 10:30-35):
Msamaria ni mwinjilisti, mtu aliyejeruhiwa ni mwenye dhambi ambaye ametubu, nyumba ya wageni ni kanisa, na dinari mbili ni ubatizo na meza ya Bwana.
Tafsiri hii inapuuza dondoo ambayo Yesu alikusudia kutengeneza kuhusiana na kuwapenda Jirani zetu (Luka 10:27-29, 36-37): tunatakiwa kuonesha upendo kwa wale tunaokutana nao ambao wana uhitaji.
Yapo matatizo matatu katika tafsiri za kufikirika:
1. Zinatokea katika mawazo ya mtafsiri.
2. Haziongozwi na kanuni nzuri za kutafsiri.
3. Haziwezi kutathiminiwa na njia zozote za kawaida na za kimantiki.
Anza na Andiko, na si Hitimisho Lako
Shujaa aliangalia ramani ili kufika anakokwenda, lakini Shujaa alisema, “Ramani hii si sahihi.” Abiria wa Shujaa wakauliza, “Unajuaje kwamba ramani si sahihi?” Shujaa alijibu kwa ujasiri, “Ninafahamu njia ya kupita. Ramani si sahihi.” Masaa machache baadae, akiwa amepotea kabisa, Shujaa akakiri kwamba ameshindwa na akaanza kujaribu kuielewa na kuifuata ramani. Kosa lake lilikuwa ni nini? Alianza na hitimisho. Alikuwa na uhakika kwamba ana jibu sahihi, kwa hiyo alikataa kuisikiliza ramani ambayo ilitoa jibu tofauti.
Baadhi ya watu wanasoma Biblia kwa namna hii. Wakati mmoja mhubiri anaposoma mstari wa andiko asilolipenda. Akasema, “Sifahamu huu unamaanisha nini, lakini halimaanishi kile linachosema.” Alianza na hitimisho (“Sikubaliani na fundisho hili”) na kisha anasoma andiko. Hakupata andiko linaloendana na hitimisho lake, kwa sababu hiyo aliamua tu kulipuuza andiko (“Halimaanishi kile linachosema”).
Ili kutafsiri andiko, tunatakiwa kuanza na andiko na kisha kutafuta hitimisho letu. Kila mmoja wetu ana nadharia fulani. Tunaanza na mtazamo fulani. Hii ni sawa. Tatizo ni pale nadharia zetu zinapotusababisha kupuuza fundisho sahihi la maandiko. Tunapaswa kuhakikisha tunaanza na andiko, na si hitimisho zetu. Hatutakiwi kuruhusu nadharia zetu kutusababisha sisi kupuuza andiko.
Mfano
“Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu” (Mathayo 5:48).
Baadhi ya watu wanasema, “Hakuna aliye mkamilifu!” Kwa hiyo, wanapuuza agizo la Yesu. Wameanza na hitimisho lao (“Hakuna aliye mkamilifu!”) na hata hawajaribu kuelewa kile Yesu alichokimaanisha.
Unapojifunza Mathayo 5:48, lazima tuulize, “Yesu alimaanisha nini kwa kusema ‘wakamilifu? Ni kwa namna gani tunatakiwa kuwa kama Baba yetu wa mbinguni?” Mistari michache kabla ya Mathayo 5:48 inatoa majibu: Tunapaswa kuwapenada adui zetu na kuwatendea mema kwa namna ile ile ambayo Baba yetu wa mbinguni “…huwaangazia jua lake waovu na wema …” (Mathayo 5:45).
Mafundisho ya Maandiko Hayakinzani na Mafundisho ya Maandiko
Tunaposoma kitabu cha mwandishi wa kibinadamu, kinaweza kujipinga kwa namna fulani. Waandishi wawili wa kibinadamu wanaweza kupingana katika hoja fulani. Hata hivyo, Biblia ni neno la Mungu; haliwezi kujipinga.
Mungu habadiliki (Yakobo 1:17). Kwa sababu ya hili, neno lake ni sawasawa na hata kama liliandikwa kwa kipindi cha miaka mamia na waandishi kadhaa wa kibinadamu. Neno la Mungu haliwezi kujipinga lenyewe.
Kanuni hii ni muhimu kutokana na mafundisho ya uvuvio: “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu…” (2 Timotheo 3:16-17). Kama chanzo kikuu cha maandiko ni Mungu, Biblia haiwezi kujipinga yenyewe. Hii ni muhimu kwa tafsiri nzuri ya Biblia. Pale ambapo vifungu vinaonekana vinajipinga, tunatakiwa kuuliza kama hatukuelewa vizuri andiko mojawapo. Tunapoelewa kwa usahihi kila kifungu, tunaona kwamba kila kifungu ni sahihi.
Mfano
“Basi, twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria” (Warumi 3:28).
“…mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali kwa imani ya Kristo Yesu” (Wagalatia 2:16).
“Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake” (Yakobo 2:24).
Baadhi ya waandishi wanafikiri kwamba Yakobo na Paulo hawakukubaliana kuhusiana na kazi ya imani na matendo. Paulo anasisitiza kwamba mtu anahesabiwa haki pasipo matendo ya sheria. Yakobo anaandika kwamba mtu anahesabiwa haki kwa matendo, na si kwa imani peke yake.
Pasipo kuangalia muktadha wa mistari hii mtu anaweza kufikiri kuwa Yakobo alimpinga Paulo. Hata hivyo, muktadha wa kila kifungu unaonesha ni nini Paulo na Yakono walikuwa wanasema. Paulo anazungumzia namna ambavyo mtu anaokolewa na kufanywa mwenye haki. Mtu anakuwa mwenye haki kwa imani. Yakobo anazungumzia kuhusiana na namna ambavyo mtu anaonesha kuwa ameokoka. Mtu anaonesha haki yake kwa matendo. Wote wawili Paulo na Yakobo wanakubaliana kwamba mtu anakuwa mwenye haki kwa imani, na kisha anaonesha haki yake kwa matendo.
Maandiko ni Mtafsiri Bora wa Maandiko
Kanuni hii ina mahusiano makubwa na kanuni iliyopita. Kwa sababu maandiko hayajipingi yenyewe, tunaweza kutumia vifungu vyenye maana zilizo wazi ili kutusaidia kuelewa vifungu ambavyo maana zake haziko wazi sana. Tunatumia mistari ambayo iko wazi ili kuelezea mistari migumu zaidi; hatupindishi mistari rahisi ili kufaa tafsiri zetu za mistari migumu.
Kitabu cha tafsiri kinasema hivi: “Mara nyingi kile ambacho kimefichika katika sehemu moja ya Biblia, kimewekwa wazi katika sehemu nyingine.”[1] Kwa kujifunza maandiko yote, tunaruhusu mistari iliyowazi kutoa mwanga kwa mistari ambayo ni migumu zaidi.
Mfano
“Au je! Wenye kubatizwa kwa ajili ya wafu watafanyaje? Kama wafu hawafufuliwi kamwe, kwa nini kubatizwa kwa ajili yao?” (1 Wakorintho 15:29).
Kwa sabau ya mstari huu, baadhi ya watu wanafikiri kwamba walio hai wanatakiwa kubatizwa kwa ajili ya watu waliokufa kabla kubatizwa. Hata hivyo, hakuna sehemu yeyote ambapo Biblia inatuambia hivyo. Paulo alitaja utamaduni huu ambao wasomaji wake walikuwa wanaufanya, lakini hatujui utamaduni huu ulikuwaje.
Maandiko ni mtafsiri bora wa maandiko. Kanuni hii inatuongoza sisi kutafsiri 1 Wakorintho 15:29. Tunaposoma Mathayo 28:19, Matendo ya Mitume 2:41, Matendo ya Mitume 8:12, na Matendo ya Mitume 19:5, tunaona kwamba ubatizo ulikuwa kwa ajili ya waamini wanaoishi. Kwa kuwa 1 Wakorintho 15:29 haiagizi kwa wazi ubatizo kwa ajili ya wafu na kwa sababu mistari mingine inaonesha kwa wazi matendo ya kanisa la kwanza, hakuna sababu ya kuamini kwamba 1 Wakorintho 15 inaagiza ubatizo kwa ajili ya wafu.
[1]Walter Kaiser na Moises Silva, An Intoduction to Biblical Hermeneutics (Grand Rapids: Zondervan, 1994), 132.
Maandiko Yaliandikwa ili Kueleweka
Maana ya neno la Mungu inaweza kupatikana katika maandiko yenyewe, kwa kutumia njia za kawaida za kutafsiri. Neno la Mungu halikuandikwa kwa kutumia herufi za siri.
Tangu mwanzo wa kanisa, kweli zote za injili zimepokelewa na kufunuliwa kwa uwazi kwa kila mtu, si tu kwa washirika maalumu wa kanisa. Yesu alisema kwamba hakuwa na mafundisho yeyote ya siri kwa ajili ya wafuasi wake (Yohana 18:20). Mtume Paulo alimwambia Timotheo kufundisha wengine kweli ambayo Paulo aliifundisha hadharani (2 Timotheo 2:2). Paulo alieleza kwamba kama watu hawawezi kuona kweli, si kwa sababu imefichwa kwa makusudi, bali ni kwa sababu Shetani amewapofusha (2 Wakorintho 4:1-6). Utume wa kanisa wakati wote umekuwa ni kushirikisha kwa wazi kweli ya Injili.
[1]Ni kweli kwamba maandiko mengi ni lazima yasomwe kwa umakini ili kupata maana yake, lakini kweli yake haijafichwa. Kweli kuu ya maandiko haijazikwa katika mistari iliyojificha isiyoeleweka. Mzaburi anasema, “Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu” (Zaburi 119:105). Kusudi la neno la Mungu ni kutuongoza sisi, na si kuficha ukweli.
Hakuna funguo maalumu ili kufungu ujumbe wa neno la Mungu. Usiamini vitabu ambavyo vinadai kufungua mfumo maalumu uliofichwa wa Biblia. Mungu aliongea ili kwamba sisi tuelewe neno lake.
Mfano
Kwa miaka michahe, mtu mmoja angedai, “Mungu amenifunulia mimi kwamba Yesu angerudi mwaka unaofuata.” Kitabu maarufu mwaka 1987 kilitabiri ujio wa Yesu mwaka 1988. Mwandishi alidai kwamba amegundua kweli hii baada ya kusoma sherehe za kale za Kiyahudi. Mwandishi yule yule aliandika kitabu mwaka unaofuata akitabiri unyakuo mwaka 1989. Hatutakiwi kumwamini mtu ambaye msingi wa mafundisho yake muhimu ni njia za siri au zilizofichika za kutafsiri Biblia. Yesu alisema, “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake” (Mathayo 24:36).
“Mara nyingi Tafsiri za Kipekee si sahihi.”
- Gordon Fee, How to Read the Bible
Maagizo ya Biblia yanaonesha Ahadi za Biblia
Kanuni hii inafundisha kwamba kama Mungu alitoa agizo, anatengeneza utii kuwezekana.
Fikiria baba ambaye anasema, “Mwanangu, ili kunipendeza unatakiwa kukimbia maili mbili ndani ya dakika mbili.” Kwa mara kadhaa, mtoto atajitahidi kwa uwezo wake wote, lakini kila wakati atashindwa kufikia matarajio ya baba yake. Mwishowe, mtoto anakata tamaa na ataacha kujaribu. Je, huyu ni baba mzuri?
Baadhi ya watu wanafikiri kwamba Mungu ni baba asiye na mantiki. Mungu anaposema, “Iweni watakatifu,”[1] wanasema, “Mungu anafahamu kwamba hatuwezi kuyatii maagizo yake.”
John Calvin alisema kwamba hatuwezi “…kupima nguvu ya wanadamu kwa [maagizo] ya Mungu.”[2] Calvin aliamini kwamba Mungu anatupa maagizo ambayo hatuwezi kutatii kwa uwezo wa kibinadamu, lakini kwamba Mungu hutoa nguvu ya kutii kwa wale wanaookoka. John Wesley alifundisha kwamba kila agizo la Mungu ni ahadi kwamba nguvu za Mungu zitatimizwa ndani ya mwamini.
Mtu hawezi kutimiliza maagizo ya Mungu katika nguvu za kawaida za mwanadamu. Lakini tunaweza kutimiliza maagizo ya Mungu kwa nguvu zake. Baba wa mbinguni mwenye upendo anawawezesha Watoto wake kutii agizo lake. Baba mwenye upendo hawezi kufachachafya Watoto wake kwa maagizo yasiyowezekana. Kila agizo la maandiko linasindikizwa na neema ya kutii agizo.
Yesu aliagiza, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote” (Mathayo 22:37). Hili ni vyote viwili agizo na ahadi. Agizo la Mungu la kupenda kwa moyo wote linaonesha ahadi yake ya kutupa sisi moyo usiogawanyika kama tutamwamini Yeye.
Mfano
“Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu” (Mathayo 5:48).
Kutoka katika muktadha, tunaelewa kwamba Yesu alikuwa anarejela upendo, na si ukamilifu katika kila njia. Na pia tunaelewa kwamba hili si jambo ambalo tunatakiwa kulikamailisha sisi wenyewe kwa nguvu zetu. Mungu anayetuagiza sisi kuwa wakamilifu ni Mungu anayetimiza agizo. Mzaburi anashuhudia, “[Ni] Mungu ndiye anifungaye mshipi wa nguvu, Naye anaifanya kamilifu njia yangu” (Zaburi 18:32).
Agizo la Yesu ni lazima lieleweke. Ni lazima lisomwe katika mwanga wa muktadha wa karibu wa mafundisho ya Yesu, na katika mwanga wa mafundisho kuhusu watu kuwa wakamilifu (kutogawanyika) moyo na kuwa watakatifu (kutengwa). Mara baada ya kuelewa hili, agizo la Yesu linakuwa ahadi yenye neema, na si kipimo kisichowezekana kwa ajili ya juhudi ya wanadamu.
[1]Mungu ameagiza hili mara kadhaa, sio tu mara moja. (Ona Mambo ya Walawi 11:44, 45, Mambo ya Walawi 20:7, na 1 Petro 1:16.)
[2]John Calvin’s mafafanuzi juu ya 1 Wathesalonike 5:23 kutoka The Epistles of Paul to the Romans and Thessalonians.
Lenzi Tatu juu ya Biblia
Kama wakristo wa kiinjili, tunaamini Biblia ni mamlaka ya mwisho kwa ajili ya mafundisho na mwenendo. Biblia ina maarifa yote yanayohitajika kwa ajili ya wokovu.
Hata hivyo, ni muhimu kutambua kwamba tunatafsiri kile ambacho tumekisoma kupitia njia tofauti tofauti. Kwa wainjili wengi, zipo lenzi ambazo kupitia hizo tunasoma Biblia. Lenzi hizi haziwi mbadala wa mamlaka ya Biblia kwa namna yeyote. Ni namna tu ambayo tunasoma na kuelewa maandiko.
Ili kupata uelewa kamili ya maandiko, tunapaswa kutumia lenzi zote tatu. Endapo tutapuuza lenzi moja, tunaweza kutafsiri maandiko isivyo sahihi. Kusoma Biblia kwa kutumia lenzi hizi kunatusaidia sisi kuelewa vema ujumbe wa neno la Mungu.
Picha hii inaweza kukusaidia kuona mahusiano ya lenzi hizi juu ya Biblia. Tunaangalia Biblia kupitia lenzi.[1]
Lenzi ya 1: Utamaduni
[2]Lenzi ya kwanza kupitia hiyo tunayaangalia maandiko ni utamaduni. Lenzi ya utamaduni inauliza, “Ni kwa namna gani wakristo katika historia walilielewa andiko hili?” Utamaduni unajaribu uelewa wetu wa andiko kwa kulinganisha na katika mwanga wa uelewa wa wakristo wengine katika kipindi chote cha historia.
Utamaduni unajumuisha matamko ya kanisa la kwanza, mafundisho makuu ambayo yamewaunganisha wakristo huko nyuma, na mafundisho wa vivazi vya mwanzoni. Utamaduni unaonesha namna ambavyo Biblia imetafsiriwa katika kipindi chote cha historia ya kanisa.
Tamaduni za kanisa hazikubaliani kwa kila kitu, utamaduni ambao unategemewa sana ni ule uliofundishwa na kanisa kila mahali na kila nyakati. Utamaduni wa dhehebu unaweza kuzingatiwa, lakini si kwa kiwango cha mamlaka kama utamaduni wa kanisa la ulimwengu mzima.
Mungu anazungumza kupitia utamaduni ili kutusaidia sisi kuelewa neno lake. Kama tafsiri yako inatoa maana ya andiko ambayo hakuna mwingine yeyoye aliyewahi kuiona, lazima ufikirie kwamba umekosea!
Lenzi ya 2: Mantiki
Mantiki ni lenzi ya pili ambayo tunatumia. Lenzi hii inauliza, “Uelewa wa kimantinki wa andiko hili ni nini?” Lenzi ya mantiki inatutaka sisi kutumia akili zetu kuelewa kile tunachokisoma katika maandiko. Inatambua kwamba maandiko yanaweza kueleweka kwa kutumia akili zetu. Tunatumia mantiki kuelewa maandiko; hata hivyo; hatupaswi kuukataa ukweli wa Biblia kwa sababu tu hatuwezi kutumia mantiki kuuthibitisha kwamba ni kweli. Watu wengi wanakataa rekodi za Biblia za miujiza kwa sababu wanafikiri kwamba miujiza ni kinyume cha uelewa wa kimantiki. Hata hivyo, miujiza si kinyume cha mantiki kwa sababu kimantiki tunaelewa kwamba Mungu anazo nguvu za kufanya miujiza.
Baadhi ya wakristo wanapinga matumizi ya mantiki; wanasema kwamba akili zetu katika anguko haziwezi kutumika kuelewa Neno la Mungu. Ni kweli kwamba wanadamu wana mipaka katika uwezo wao wa akili. Hata hivyo, Paulo mara kwa mara ameomba kutmia mantiki anapoleta hoja zake. Katika Warumi, kwa mfano, Paulo anauliza mfululizo wa maswali ambayo yanawaongoza wasomaji wake katika uelewa wa kweli kuu kuhusiana na wokovu. Wakati mantiki na akili zetu si mamlaka ya mwisho, hatuwezi kupuuza maana za kimantiki za maandiko.
Lenzi ya 3: Uzoefu
Uzoefu ni lenzi ya mwisho. Lenzi hii inauliza, “Je, uelewa wangu unashabihiana na uzoefu wa wakristo wengine?” Uzoefu binafsi haupaswi kuaminiwa zaidi ya kweli kuu. Hata hivyo, uzoefu ni wa thamani sana endapo utasawazishwa na utamaduni na mantiki.
Kila lenzi hizi ni muhimu. Kana tunatumia utamaduni pekee, tutaangukia katika makosa ya kanisa la Rumi ambalo linayachukua mafundisho ya kanisa kama yako sawasawa na maandiko kimamlaka. Kama tutatumia tu mantiki, tutaangalia akili kama mamlaka ya mwisho. Endapo tutatumia uzoefu pekee, tafsiri zetu zitakuwa na mipaka na zitategemea hisia za mtu binafsi, mtazamo, na mawazo ya watu. Lenzi hizi ni njia za sisi kuelewa maandiko, lakini hazitakiwi kutumika katika namna ambayo inakinzana na mamlaka ya maandiko.
Mfano
“Kwa hiyo nampigia Baba magoti… mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu” (Waefeso 3:14, 19).
Paulo anaomba kwamba Waefeso wakue sana katika mahusiano yao ya ndani na Mungu. Anaomba kwamba wapate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu. Tunapata nini tunaposoma maombi haya kupitia lenzi hizi tatu?
Utamaduni. Wakristo wa vizazi vyote wamefundisha kwamba Mungu ameahidi kuwatakasa kabisa waamini. Wakristo hawajaweza kukubaliana na undani wa kina wa taarifa uhusiana na namna ambavyo Mungu analikamilisha kusudi hili ndani ya waamini, lakini katika nyakati zote za historia ya kanisa, wakristo wa historia mbalimbali wamekubaliana kwamba Mungu anawaita Watoto wake katika mahusiano ya ndani sana na yeye.
Katika karne ya pili, Irenaeus aliandika kwamba Kusudi la Mungu kwetu ni “kwamba tufanywe katika sura na mfano wa Mungu.”[3] Irenaeus aliamini kwamba kila mwamini anaweza kujazwa na ukamilifu wa Mungu. Katika karne ya nne, waandihi wa mashariki kama vile Gregory wa Nyssa alifundisha kwamba wakristo wanatakiwa zaidi na zaidi kujazwa na ukamilifu wa Mungu. Katika karne ya 17, mkatoloki wa Kifaransa Francois Fenelon aliandika kwamba, kupitia nguvu ya neema ya Mungu, tunaweza kuishi “kama Yesu alivyoishi, kufikiri kama alivyofikiri.…”[4] Kupitia neema ya Mungu, tunaweza kufanywa katika mfao wake.
Mantiki. Tunapozingatia maombi ya Paulo, akili zetu zinauliza, “Je, tafsiri yangu ya maombi haya ni sawasawa na maandiko mengine?” Je, ni mantiki kutafsiri maombi haya kama ahadi ya Maisha ya ndani sana kwa wakristo? Kwa kuangalia maandiko mengine, tunaona kwamba Warumi 12:1, 1 Wathesalonike 5:23, na maandiko mengine yanashauri Maisha ya ndani sana ambayo yapo kwa ajili ya waamini. Uhalisia wa kujazwa na utimilifu wote wa Mungu ni wa kimantiki.
Uzoefu. Uzoefu wa wakristo wengi wakubwa katika kipindi chote cha historia kinaonesha njaa ya kuwa na Maisha ya ndani sana. Kila mkristo aliyejikita anashahuku zaidi na Mungu. Shuhuda za wakristo wakubwa zinaoesha kwamba njaa hii ilitimizwa kwa neema ya Mungu.
Maswali ya Kuuliza wakati Unafikiri Kuhusiana na Vifungu vyenye Mjadala
Kuna vifungu vya maandiko ambavyo vimetafsiriwa tofauti tofauti katikati ya makanisa na wakati mwingine katikati ya marafiki. Unapoangalia kimojawapo kati ya vifungu hivyo, badala ya kutetea tu mawazo yako, fikiria maswali yafuatayo:
Je, ninaanza na hitimisho? Je, tayari nimeshaamua kile ninachofikiri kwamba andiko linasema kabla sijasoma?
Je, tafsiri yangu inakinzana na vifungu vingine vya maandiko?
Je, vifungu vingine vinatoa maana ya wazi ya kifungu hiki?
Je, tafsiri yangu inajikita katika ujumbe uliofichwa, au ninajaribu kutafsiri kifungu katika namna wazi kwa kadiri inavyowezekana?
Je, kifungu hiki kinatoa agizo? Kama ndivyo, kuna ahadi gani ambayo inaoneshwa katika agizo hili?
Tamaduni gani ya kanisa la kikristo katika kipindi chote inasema nini kuhusiana na kifungu?
Uelewa wa wazi na wa kimantiki wa andiko hili ni nini?
Uzoefu wa wakristo wengine unasema nini kuhusiana na kifungu hiki?
Maswali haya hayakuhakikishii wewe kwamba utaweza kupatana katika tafsiri ya kifungu. Hata hivyo, yanaweza kukusaidia kutafuta maeneo mnayokubaliana. Kama sivyo, maswali yanaweza kukusaidia kutambua sababu ambazo zinawafanya wakristo halisi ambao wamejikita katika mamlaka ya neno la Mungu kutokukubaliana juu ya tafsiri ya baadhi ya vifungu vya maandiko.
(1) Uelewa wa kanuni za msingi za tafsiri ya Biblia utakusaidia kukuzuia kuja katika hitimisho lisilo sahihi katika kujifunza.
(2) Anza na andiko, na si hitimisho lako. Usiruhusu nadharia zako kukusababisha wewe kupuuza andiko.
(3) Mafundisho ya Maandiko hayakinzani na Mafundisho ya Maandiko. Kama vifungu viwili vinaonekana kukinzana, fikiri kwamba pengine haukuelewa vizuri mojawapo ya kifungu.
(4) Maandiko ni mtafsiri bora wa maandiko. Ruhusu vifungu vilivyo wazi kuelezea vifungu vigumu.
(5) Maandiko yaliandikwa ili kueleweka. Tafuta maana ya kawaida ya andiko.
(6) Maagizo ya Biblia yanaonesha ahadi za Biblia. Mungu anayetupatia maagizo anatuwezesha sisi kutii.
(7) Biblia ina maarifa yote yanayohitajika kwa ajili ya wokovu.
(8) Tunaangalia maandiko kupitia lenzi tatu ambazo zinatusaidia sisi kuelewa neno la Mungu:
Utamaduni: uelewa wa wakristo wengine katika kipindi chote cha historia
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.