Unamkumbuka Tinghao kutoka Somo la 1? Tinghao alisoma Biblia kila siku, lakini hakuweza kusikia sauti ya Mungu kupitia kile ambacho anakisoma. Shida ilikuwa ni nini? Tinghao hakuwa na mchakato wa kutafsiri kile ambacho anakisoma. Alisoma, lakini hakuweza kuelewa.
[1]Matendo ya Mitume 8 inatueleza habari ya mtu mwingine alikuwa anasoma lakini hakuweza kuelewa. Filipo, shemasi katika kanisa la kwanza, aliongozwa na Roho Mtakatifu katika njia ya jangwa kutoka Yerusalemu kwenda Gaza. Huko alikutana na towashi mwenye mamlaka wa Kushi ambaye alikuwa anatoka hekaluni Yerusalemu kuabudu. Afisa yule alikuwa anasoma kutoka kitabu cha Isaya alipokuwa anasafiri.
Filipo alimuuliza towashi, “Je! Yamekuelea haya unayosoma?” (Matendo ya Mitume 8:30). Towashi alijibu, “Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza?” (Matendo ya Mitume 8:31). Filipo alipokuwa analielezea neno la Mungu, yule mtu alimwamini Yesu kwamba ni mwana wa Mungu na akabatizwa kama mwamini mpya.
Kufahamu jinsi ya kutafsiri kile unachokisoma ni muhimu. Katika masomo machache yajayo tutajifunza mchakato wa kutafsiri maandiko. Tutajifunza hatua za kivitendo kwa ajili ya kutafsiri.
“Unifahamishe nami nitaishika sheria yako, Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote.”
- Zaburi 119:34
Umuhimu wa Tafsiri
Mahakimu watatu walikuwa wanajadiliana kuhusiana na kazi zao mahakamani. Hakimu wa kwanza anasema, “Kuna watu wenye hatia na kuna watu wasio na hatia. Ninawatambua kwa jinsi walivyo.” Hakimu huyu anaamini kuwa kuna ukweli kuu. Kuna watu wenye hatia na watu wasio na hatia, na kazi ya hakimu ni kutangaza kile kilicho ukweli.
Hakimu wa pili anasema, “Kuna watu wenye hatia na watu wasio na hatia. Ninajaribu kutambua endapo mtu ana hatia au hana hatia. Hakimu huyu anajua kwamba kuna ukweli kabisa, lakini pia anatambua kwamba anaweza kuwa na makosa katika maoni yake kuhusu mtu fulani.
Hakimu wa tatu alisema, “Mtu ana hatia au hana hatia hadi nitakapotoa tamko langu.” Hakimu huyu haamini juu ya kweli kuu. Anafikiri kwamba tamko lake ndilo linafanya kitu kuwa kweli.
Kwa huzuni, wakristo wengi hawaamini kwamba maandiko ni kweli kuu. Kisha wanasema, “Kile kilicho kweli kwako kinaweza kisiwe kweli kwangu.” Katika mtazamo huu, kila msomaji anatengenza “kweli” yake. Wanafikiria kuwa matamko ya kibiblia yanamaanisha vyovyote ambavyo yeyote anataka yamaanishe.
Kama hakimu wa pili katika habari. Wakristo wanahitaji kuelewa kweli mbili muhimu:
1. Maana ya maandiko ni kweli, na wajibu wetu ni kujaribu kuielewa kweli ya Mungu katika andiko.
2. Uelewa wetu una mipaka. Kwa sababu, tafsiri zetu zinaweza kuwa si sahihi. Tunatakiwa kuwa wanyenyekevu.
Katika hatua ya Uchunguzi, tuliuliza, “Ninaona nini katika andiko?” Katika hatua ya Tafsiri tunauliza, “Andiko linamaanisha nini?” Baadae, tunaangalia matumizi ya andiko katika maisha yetu.
Tunaanza mchakato wa tafsiri kwa kuuliza, “Mwandishi alikusudia kusema nini?” hii itatuandaa sisi kuuliza, “Maandiko yanamaanisha nini kwangu?”
Changamoto Zinazokabili Tafsiri Sahihi
Zipo changamoto nyingi kwa wasomaji wa leo wanaotafsiri maandiko ya kale kama Biblia. Muda na nafasi inayotutenga sisi kutoka kwa waandishi wa asili inafanya kutafsiri kuwe kugumu. Tunazungumza lugha tofauti. Tamaduni zetu ni tofauti na tamaduni za waandishi wa Biblia.
Picha hii inaonesha changamoto inayohusika katika kutafsiri Biblia katika siku zetu. Biblia iliandikwa kwa ajili ya ulimwengu wa kale (1). Wasomaji wa kwanza waliishi katika utamaduni tofauti na msomaji wa leo. Mto (2) ambao unatenganisha ulimwengu wao na wetu unafanya iwe ngumu kwa sisi kuelewa Biblia. Mto huu unaundwa na utofauti kati ya tamaduni zetu na ulimwengu wa Biblia. Ni tofauti gani kati ya msomaji wa leo na mwandishi?
Tofauti ya Lugha
Biblia iliandikwa katika lugha tatu: Kiebrania, Kiyunani, na Kiaramu. Leo, wengi wetu husoma Biblia katika lugha yetu wenyewe. Hii inatengeneza umbali mkubwa kati yetu na mwandishi. Yeyote anayezungumza lugha ya pili anaelewa ugumu wa lugha.
Tofauti ya Utamaduni
Ikifanana na ugumu wa lugha ni ugumu wa utofauti wa tamaduni. Waandishi wa maandiko walikuwa sehemu ya utamaduni ambao ni toauti na ulimwengu wetu. Tunaposoma maandiko, tunatakiwa kujiuliza, “Ninajifunza nini kuhusiana na utamaduni wa ulimwengu wa kale ambacho kitanisaidia mimi kuelewa na kuutafsiri ujumbe wa Biblia?”
Jiografia Isiyojulikana
Matukio ya Biblia yalitokea kwa watu halisi wanaoishi katika maeneo halisi. Kadiri tunavyoelewa jiografia, ndivyo tunavyoweza kuvuka vizuri mto unaogawanya ulimwengu wetu na ulimwengu wao.
Kujua kwamba barabara kati ya Yeriko na Yerusalemu inapita katika eneo hatari la milimani inaeleza tahadhari ya kuhani na Mlawi (Luka 10:31-32). Pia inatoa shukrani kwa ajili ya huruma ya Msamaria ambaye alihatarisha usalama wake ili kusaidia mgeni aliyejeruhiwa (Luka 10:33-34).
Wasomaji wameuliza, “Kwa nini wanafunzi walitilia shaka uwezo wa Yesu wa kulisha 4,000 katika Marko 8 baada ya kuwalisha 5,000 katika Marko 6?” Ramani inatoa jibu. Katika Marko 7, Yesu anasafiri hadi Dekapoli, eneo lenye watu wa Mataifa. Swali kwa wanafunzi halikuwa, “Je, Yesu anaweza kuwalisha watu hawa?” lakini “Je, atawalisha?” Hawakuamini kwamba watu wa mataifa mengine walistahili muujiza huo. Bado hawakuelewa kwamba Yesu amekuja kwa ajili ya watu wote.
Marko 6
Marko 7
Marko 8
Nafasi
Galilaya
SAFARI
Dekapoli
Watu
Wayahudi
-
Wamataifa
Marko 4 inazungumza namna ambavyo Yesu alituliza dhoruba kwenye Bahari ya Galilaya. Katika atlasi ya Biblia, tunajifunza kwamba Bahari ya Galilaya ni ziwa kubwa, mita 210 chini ya usawa wa bahari. Kwa sababu sehemu iliyoinuka kuzunguka ziwa huelekeza upepo kama mtaro mwembaba, upepo hutengeneza dhoruba kali ndani ya dakika chache. Wakiwa ni wavuvi waliotumia maisha yao kwenye bahari hii, wanafunzi walizoea dhoruba kali. Ule ukweli kwamba walihofia maisha yao unatuambia kwamba dhoruba hii haikuwa ya kawaida. Hii ilikuwa dhoruba yenye nguvu isiyo ya kawaida, lakini ilichukua maneno machache tu kwa Yesu kuituliza bahari. Ndio maana walisema, “Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?” (Marko 4:36-41).
Aina ya Fasihi Isiyofahamika
Kila aina ya uandishi ni lazima isomwe kwa namna tofauti. Tunaposoma Warumi, ni lazima tufuatilie kwa makini hoja ya Paulo anapoonyesha jinsi tunavyofanywa kuwa sawa mbele za Mungu. Tunaposoma mfano, tunamsikiliza anayesimulia habari akifundisha kupitia habari ya ajabu.
Hitimisho
Angalia tena picha. Hata kama mto wa lugha, tamaduni, jiografia, na fasihi unatutenga sisi, Biblia ina ujumbe ambao unazungumza katika tamaduni zote. Hili ni daraja (3) linalounganisha mto. Daraja linaundwa na kanuni ambazo Biblia inafundisha. Kanuni hizi ni kweli kwa tamaduni zote katika vizazi vyote.
Ramani (4) inatuuliza sisi wapi tupo katika habari ya Biblia. Ujio wa Kristo umetimiliza unabii na sheria za Agano la Kale. Kwa kukumbuka hili tutabadilisha namna ambayo tutatafsiri na kutumia vifungu hivi vya maandiko.
Mwisho, tunafika katika ulimwengu wetu leo (5). Katika hatua hii, tunauliza ki kwa namna gani kanuni tulizozipata (3) zitatumika katika ulimwengu wetu.
Tutakuja tena katika picha hii katika masomo yanayofuata. Kwa sasa, unatakiwa kuelewa hatua.
[1]Picha: “Interpreting the Bible” imechorwa na Anna Boggs, inapatikana katika https://www.flickr.com/photos/sgc-library/52377290578, licensed under CC BY 2.0. Concept from J. Scott Duvall and J. Daniel Hays, Grasping God’s Word (Grand Rapids: Zondervan, 2012)
Makosa Yaliyozoeleka ya Watafsiri wa Biblia
Yapo makossa kadhaa yaliyozoeleka ambayo watafsiri wa Biblia wanaweza kufanya.
Kusoma Andiko Kimakosa
Baadhi ya wahubiri wamehubiri kwamba Paulo alisema, “Fedha ni shina la mabaya yoye.” Lakini Paulo hakusema hivyo. Alisema, “Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha” (1 Timotheo 6:10). Inawezekana kuwa na fedha pasipo kuzipenda, na inawezekana kuipenda fedha, hata kama hauna fedha nyingi. Onyo la Paulo kimsingi si kuwa na fedha; ni kuhusiana na moyo ambao unatawaliwa na fedha.
Baadhi ya wakristo wanasoma kimakosa Zaburi 37:4 ikisema, “Mungu amehaidi kunipa haja za moyo wangu. Ninataka kuwa tajiri, kwa hiyo Mungu atanifanya mimi kuwa tajiri” Mzaburi anasema, “Nawe utajifurahisha kwa BWANA, Naye atakupa haja za moyo wako.” Zaburi inahaidi kwamba kama tutajifurahisha kwa Bwana, Bwana atatupatia haja zetu – Bwana. Baadae, anaahidi kwamba kama tukiwa na njaa na kiu ya haki, tutajazwa - na haki (Mathayo 5:6). Hii si ahadi kwa mafanikio ya kiuchumi; ni ahadi kwa ajili ya jambo zuri zaidi – mafanikio ya kiroho.
Hatua ya kwanza tuliyojifunza katika kozi hii ni Uchunguzi. Uchunguzi wetu ni lazima uwe sahihi au tafsiri yetu haitakuwa sahihi. Kuwa makini usisome andiko kimakosa. Mtu mmoja alisema kwamba hatua tatu za kwanza za kujifunza Biblia ni:
1. Kusoma andiko.
2. Kusoma andiko tena.
3. Baada ya hatua ya pili, soma andiko tena!
Kupindisha Andiko
Katika historia yote, waalimu wa uongo wamekuwa wanapindisha maandiko ili kutetea makossa yao. Paulo alionya kwamba baadhi ya watu watapindisha mafundisho yake ya kuhesabiwa haki kwa imani pekee ili kutetea shahuku zao za kuendelea katika dhambi kwa makusudi (Warumi 6:1-2). Kumekuwa na nyakati ambapo maandiko yametumika kutetea utumwa au serikali kuuwa kundi la watu wa utamaduni fulani. Leo, baadhi ya wahubiri wamepindidha kweli ya Mungu kuwa Injili ya mafanikio ambayo ni kiyume na kweli ya maandiko.
Petro anawaonya wale wanaopindisha maandiko kwenda katika uharibifu wao wenyewe (2 Petro 3:16). Vilevile, Yakobo alizungumza sana juu wa wajibu wa wale wanaofundisha (Yakobo 3:1). Sisi tunaofundisha maandiko tunatakiwa kuwa makini kwamba tusipindishe maandiko ili kutetea mawazo au dhana potofu.
Kutoa Maana ya Kufikirika
Habari ya mahakimu watatu inaelezea kosa lingine llililozoeleka la watafsiri wa Biblia: dhana kwamba tafsiri ya maandiko inatoka katika fikra za msomaji. Baadhi ya watu wanajiuliza tu, “Ninahisi Biblia inamaanisha nini?” Wakati hisia na kujisikia ni kwa muhimu, kweli kuu ya maandiko ni ile ambayo mwandishi aliandika, na sio kile ambacho ninahisi ameandika.
Kujiamini Kupita Kiasi
Mtafsiri anaiamini akili yake sana kiasi kwamba anafikiri hawezi kukosea kabisa. Tunajifunza neno ili kufikia hitimisho la maana ya andiko; hata hivyo, tunatakiwa kuwa wanyenyekevu kukiri wakati hitimisho letu sio sahihi. Hakuna mwenye majibu yote.
Unyenyekevu katika tafsiri ni muhimu. Unapojifunza Biblia, utakutana na maeneo ambayo wakristo wacha Mungu wanatofautiana mawazo. Hii haina maana kwamba mara zote kuna upande mmoja ambao umepindisha andiko; unaweza kuwa ni utofauti kati ya pande mbili ambazo zimejikita katika kweli ya Mungu. Tunatakiwa kuendelea kuwa wanyenyekevu kwa kuzingatia tafsiri zetu ili kuweza kuvumuliana na wenye mtazamo tofauti.
Zamu Yako
Hapa chini ni baadhi ya matamko ambayo si sahihi ambayo watu wamekuwa wanayasema, wakifikiri wananukuu maandiko. Ili kuthamini usomaji makini, tafuta kifungu cha andiko ambalo limepindishwa katika kila mfano na nukuu kile ambacho Biblia inasema. Mfano wa kwanza umekamilishwa kwa ajili yako.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.