Biblia imejaa maana, lakini kwa huzuni, baadhi ya watu wanasoma maandiko pasipo uelewa wa ujumbe wake.[1] Biblia inaundwa na vitabu, sura, vifungu vya maneno, mistari, na maneno. Kuelewa maana za maneno kunatusaidia sisi kutafsiri kwa usahihi kifungu tunachojifunza. Somo hili ni kuhusiana na namna ya kujifunza maneno. Tunajifunza neno ili kuelewa maana yake katika muktadha mahususi wa Biblia.
Wakati mwingine watu wanajifunza maneno ya asili ya kiebrania na kiyunani kwa kutumia vyanzo vya kujifunza Biblia. Vyanzo kama hivyo vinavyotumika havipatikani katika ulimwengu wote, kwa sababu hiyo hatutavijadili katika somo hili. Badala yake, tutajifunza namna ya kujifunza maneno katika tafsiri zetu za Biblia.
Tutatumia mchakato wa hatua tatu wa kujifunza neno:
1. Chagua neno la kujifunza.
2. Orodhesha maana zinazowezekana kwa kila neno lililochaguliwa.
3. Tambua kila neno lina maanisha nini katika muktadha wa kila kifungu.
[1]Nyenzo nyingi katika somo hili zinatoka katika sura ya 9 ya J. Scott Duvall na J. Daniel Hays, Grasping God’s Word (Grand Rapids: Zondervan, 2012).
Makosa ya Yaliyozoeleka katika Kujifunza Neno
Tunapoanza kujifunza neno, kuna baadhi ya makosa ya kuepuka. Makosa haya mara nyingi yanapelekea tafsiri isiyo sahihi.
Kupuuza maana ya awali ya neno
Wakati mwingine namna neno lilivyotunika inabadilika kila wakati. Endapo tafsiri zetu za Biblia zilifanyika miaka kadhaa iliyopita, tunahitaji kufahamu kwamba maana za baadhi ya maneno katika Biblia zetu zinaweza kuwa tofauti na maana ya neno leo. Endapo hatutaelewa namna neno lilivyotumika hapo kabla, tunaweza kuja na hitimisho lisilo sahihi kuhusiana na kifungu tunajifunza. (Hili si suala kubwa sana tunaposoma tafsiri ya Biblia iliyotoka miaka ya hivi karibuni.)
► Zungumza kuhusiana na neno katika lugha yako ambalo lina maana tofauti leo na lilivyokuwa likimaanisha.
Kufikiri kwamba neno lina maana ile ile katika kila muktadha
Waandishi wa Biblia walitumia maneno ambayo yana maana zaidi ya moja. Neno moja linaweza kutumika kwa maana moja katika muktadha mmoja, na maana tofauti katika muktadha mwingine. Ni lazima tuangalie muktadha ambao neno hilo limetumika ili kujua ni maana gani iliyo sahihi katika mstari tunaojifunza.
Mchakato Wa Kujifunza Neno
Hatua ya Kwanza: Chagua neno la kujifunza kutoka kwenye kifungu
Hatuhitaji kujifunza kwa kina kila neno ndani ya Biblia. Wakati mwingine maana ya neno iko wazi. Kwa mfano, Biblia inaposema, Daudi aliokota mawe matano laini (1 Samweli 17:40), hatuhitaji kujifunza neno jiwe ili kutafuta maana yake.
Kuchagua neno la kujifunza, angalia:
Maneno ambayo ni muhimu kwa ajili ya maana ya kifungu.
► Soma Warumi 12:1-2 na zungushia maneno muhimu kwa ajili ya kujifunza. Pembeni mwa kila neno, toa sababu ya kwa nini unalichagua neno hilo:
1 = Neno Muhimu
2 = Neno Lililorudiwa rudiwa
3 = Tamathali ya Semi
4 = Neno lisilo wazi au gumu
Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.
Baadhi ya maneno ambayo unaweza kuyawekea alama ni:
1 = Neno Muhimu: nawasihi, itoeni, msiifuatishe, mgeuzwe, kufanywa upya
2 = Neno lililorudiwa rudiwa: Hakuna katika kifungu hiki
3 = Tamathali ya semi: dhabihu iliyo hai
4 = Neno lisilo wazi au gumu: ibada yenye maana
Hatua ya Pili: Orodhesha maana zinazowezekana kwa kila neno lililochaguliwa
Lugha nyingi zina maneno ambayo hutumiwa kwa namna nyingi, na maana tofauti sana. Kwa kawaida msikilizaji anajua maana ya mzungumzaji kwa sababu ya muktadha. Mara nyingine, ucheshi au kutoelewana sana hutokea wakati msikilizaji ameshindwa kuzingatia muktadha na anakosea kuhusu kile ambacho mzungumzaji anamaanisha.
► Je, unaweza kufikiria juu ya wakati ambapo mtu alifanya makosa kwa sababu hakuelewa nini mwingine alimaanisha kuhusiana na neno fulani?
Katika hatua hii ya pili, tunapaswa kujaribu kufikiria kila njia iwezekanayo ambayo neno hilo linaweza kutumiwa. Ikiwa tafsiri yetu ya Biblia ni ya zamani, tunapaswa pia kufikiria ikiwa neno hilo lilikuwa na maana za ziada hapo awali.[1] Endapo tuna kamusi, inaweza kutusaidia kutengeneza orodha ya maana zote zinazowezekana. Ikiwa tunajifunza na watu wengine, wanaweza pia kutusaidia kufikiria maana ambayo sisi hatukufikiria.
Kama inawezekana, tafuta tafsiri nyingine za Biblia na kuona endapo zimetumia neno lile lile, kama tafsiri nyingine imetumia neno tofauti, linganisha maana ili kuona tofauti ni nini.[2] Je, yanamaanisha kitu kimoja? Kama sivyo, tofauti ni nini? Je, maana ya kifungu itabadilika kwa kutumia neno lingine?
► Itoeni lilikuwa mojawapo ya neno ambalo liliwekewa alama kwa ajili ya kujifunza kutoka katika Warumi 12:1-2. Fanyeni kazi pamoja ili kuorodhesha maana zote zinazowezekana za neno itoeni.
Hatua ya Tatu: Tambua neno linamaanisha nini katika Muktadha
Baada ya kuangalia matumizi mbalimbali ya neno na kutengeneza orordha ya maana zinazowezekana, uko tayari kutambua neno lina maana gani katika kifungu unachojifunza. Muktadha utakuongoza. Kumbuka, mwandishi hakumaanisha kutumia maana maalumu sana ambayo watu wachache wangeweza kufahamu. Mwandishi alitaka wasomaji kuelewa.
Tuliangalia umuhimu wa muktadha katika somo la 5, kwa sababu hiyo hatutajikumbusha tena nyenzo hizo hapa. Kwa kufupisha wajibu wa muktadha: tunaangalia mstari, sura, na kitabu kinachozunguka ili kupata maana bora ya neno.
Yapo maswali ya kuzingatia wakati unaagalia muktadha na kujaribu kugundua maana ya neno.
(1) Je kuna ukinzani au ulinganifu katika kifungu ambao unakusaidia kutoa maana ya neno?
► Soma Yohana 3:16: “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” Kwa pamoja, orodhesheni maana zote zinazowezekana na neno asipotee. (Mnaweza kutumia kamusi yeyote ambayo mnayo.) Sasa, zingatia ukinzani unaotolewa katika mstari. Kupotea kunatofautishwa na kuwa na uzima wa milele. Katika orodha yako, ni maana gani ya neno asipotee iliyokuwa ikimaanishwa na Yesu katika sentensi hii?
(2) Ni kwa namna gani mwandishi ametumia neno hili katika maeneo mengine?
Neno ulimwengu pia limetumika katika Yohana 3:16. Neno ulimwengu linaweza kumaanisha mambo kadhaa:
Ulimwengu wa kifizikia
Watu wote
Mataifa yaliyojulikana kuwa yamestaarabika
Jamii ya jumla ambayo inamkataa Mungu
Mwandishi alitumia neno ulimwengu kurejelea kila kimojawapo kati ya hivi katika sehemu mbalimbali katika Maandiko. Kutambua ni maana gani ya ulimwengu anayo katika Yohana 3:16, tunapaswa kuangalia mifano ya matumizi ya Yohana ya neno.
Yohana 1:10, “Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua.” Mstari huu unazungumza kuhusu Yesu. Ulimwengu haukumtambua Yeye.
Yohana 7:7, “Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi; bali hunichukia mimi, kwa sababu mimi naushuhudia ya kuwa kazi zake ni mbovu.” Yesu anaongea katika mstari huu. Ulimwengu unamchukia Yeye.
Yohana 14:17, “ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.” Ulimwengu hauwezi kumpokea Roho wa Kweli.
1 Yohana 2:15-17, “Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.” Maadili ya ulimwengu na utafutaji wake ni kinyume kabisa na Mungu.
Mtume Yohana mara nyingi ametumia neno dunia kurejelea jamii kwa ujumla ambayo inamkataa Mungu. Hii inaonesha kiwango cha ahadi ya Yesu: Mungu aliwapenda sana wale ambao walitengwa na Yeye kiasi kwamba alimtoa mwana wake ili kwamba wote waokolewe.
(3) Muktadha unaonesha nini kuhusiana na maana ya neno?
► Angalia Luka 1:68-79.
Katika Luka 1:71, Zakaria anaomba ili kwamba Israeli Tuokolewe. Anarejelea nini? Neno Tuokolewe linamaanisha nini katika mstari huu?
Dhana ya wokovu ina maana zaidi ya moja katika maandiko. Mahususi kabisa inaweza kumaanisha:
Kuokolewa na adui au hatari
Kuokolewa kutoka magonjwa
Kuokolewa kutoka dhambini
Muktadha wa karibu (Luka 1:68-74) unaonesha kwamba “Tuokolewe” linarejelea kuokolewa na adui. Ukombozi (wokovu) utatimiza ahadi ambayo Mungu alimwahidi Abrahamu (Luka 1:73).
Mistari michache baade, Luka anatumia neno wokovu katika maana ya ndani (Luka 1:77). Kwa kupitia uongozi wa Roho Mtakatifu, Zakaria atamuona mtoto wake akiitwa kuwa nabii wa aliye juu. Mtoto wa Zakaria atawapa watu wa Bwana ufahamu wa wokovu katika msamaha wa Dhambi zao. Hapa, wokovu umeunganishwa na msamaha wa dhambi.
Maana tofauti tofauti za wokovu zimetumika katika maombi haya. Tunatambua maana kutoka katika muktadha.
[1]Endapo tunatumia tafsiri ya zamani ya Biblia, kuangalia tafsiri mpya ya Biblia kutatupatia mwanga kuhusiana na maana ya inayowezekana ya neno katika muktadha husika.
[2]Rejea Nyongeza kwa orodha ya tovuti ambapo unaweza kusoma Biblia katika lugha na matoleo mbalimbali.
Shughuli za Kufanyia Mazoezi
Angalizo kwa kiongozi wa darasa: Tenga muda wa kutosha darasani kwa ajili ya shughuli hizi za mazoezi kwa vitendo. Ikiwa kipindi chako cha darasani kawaida ni saa moja, tumia kipindi kizima cha darasa kwenye mazoezi haya. Muda uliopendekezwa umetolewa kwa kila zoezi. Kufanya mazoezi pamoja wakati wa darasa kutawasaidia wanafunzi kutumia mawazo wanayojifunza. Kupitia mchakato wa kujifunza neno na watu wengine pia kutawasaidia kuona kwamba mara nyingi kuna mitazamo na maelezo ambayo hawatazingatia ikiwa watafanya kazi peke yao.
Kwa shughuli za vikundi vidogo vidogo, kuwa na wanafunzi watatu katika kila kundi. Kundi zima litakuja pamoja dakika tano za mwisho na kujadili kile walichojifunza.
► Shughuli za vikundi vidogo vidogo (Dakika 20). Katika kundi lako, tafuta mistari kadhaa ambapo neno moja limetumika likiwa na maana mbalimbali. Hapa ni mawazo machache yanayoweza kukusaidia kuanza: nyumba, maono, siku, tunda. Unapotambua baadhi ya mistari inayotumia neno moja kwa namna tofauti, andika orodha ya namna zote ambazo neno hilo linaweza kutumiwa. Je, kujifunza maneno kunasaidia vipi katika tafsiri sahihi ya kila mstari?
► Shughuli ya kundi kubwa (dakika 10). Sasa rudi katika Warumi 12:1 na orodha yako ya maana zinazowezekana za neno itoeni. Tumia maswali yaliyo hapo juu kukusaidia kutambua maana iliyokusudiwa katika mstari huo.
► Shughuli za vikundi vidogo vidogo (dakika 30). Katika kikundi chako, jizoeze kupitia mchakato wa kujifunza neno. Tayari umeweka alama katika maneno katika Warumi 12:1-2 ambayo yanapaswa kujifunza kwa makini. Kwa kila moja ya maneno hayo, orodhesha kila maana inayowezekana na uamue neno hilo lina maana gani katika muktadha huo.
Suala Maalumu: Lugha ya Kitamathali
Katika Somo la 6, tuliangalia kwa ufupi matumizi ya tamathali za semi. Haijalishi tumejifunza neno kwa umakini kiasi gani, hitimisho letu halitakuwa sahihi endapo hatutaelewa lugha ya mwandishi ya kitamathali. Katika tamathali ya semi, jambo muhimu si maana halisi ya maneno, bali dhana inayowakilishwa.[1]
Sisi sote tunatumia lugha ya kitamathali. Fikiria kwamba rafiki wa Marekani anakuonyesha picha za bustani yake. Unastaajabishwa na bustani hiyo na kumuuliza rafiki yako, “Unakuzaje mimea mizuri hivyo?” Anajibu, "Nina kidole gumba cha kijani." Haimaanishi kuwa kidole gumba mkononi mwake ni kijani kibichi. Anatumia tamathali ya usemi ya Kiingereza cha Marekani inayomaanisha, “Nina uwezo usio wa kawaida wa kukuza mimea.”
► Je, ni vishazi gani katika lugha yako ambavyo vinamaanisha kitu tofauti na maana yake halisi?
Wakati mwingine neno hutumiwa kuwakilisha kitu kingine. Hii sio sawa na neno moja kuwa namaana zaidi ya moja. Kwa mfano, katika Biblia watu wengine wanaitwa mbwa (Ufunuo 22:15). Kauli hiyo ni ukosoaji wa watu ambao wana tabia fulani za mbwa ambazo watu hawapaswi kuwa nazo. Neno mbwa bado lina maana ya mnyama tunayemwita mbwa, lakini linatumika kwa njia ya kitamathali kurejelea watu. Yesu alimwita Simoni kwa jina la Petro, maana yake mwamba, kwa sababu Petro alikuwa na tabia ya mwamba ambayo ni nzuri kwa watu kuwa nayo (Mathayo 16:18). Yesu alikuwa akitumia maana ya kawaida ya neno mwamba, akionyesha uhakika kwamba Simoni alikuwa kama mwamba kwa njia fulani.
Yesu alimwita Herode mbweha (Luka 13:32). Hatuhitaji kujifunza maana ya tofauti ya maana ya neno mbweha kisha kuangalia katika muktadha kuangalia ni mnyama wa aina gani Yesu alimaanisha. Ni kauli ya kitamathali, kwa hiyo tunataakiwa kuelewa ni nini Yesu alimaanisha aliposema kuhusu Herode kwa kumwita mbweha. Yesu alimaanisha kwamba Herode alikuwa na akili nyingi lakini hakuweza kuaminiwa kwa sababu ya tabia yake mbaya.
► Ni mnyama gani ambaye anatumiwa kitamathali katika utamaduni wako ili kukosoa watu?
Ni kwa namna gani tunajua kwamba sentensi hii ni halisi au ni ya kitamathali? Hapa kuna miongozi miwili ya kuzingatia:
1. Tumia maana ya Kitamathali wakati kifungu kinakuambia kufanya hivyo. Mwanzo 37 inahusisha ndoto mbili. Katika Biblia, ndoto mara nyingi iliwasilisha ujumbe wa kitamathali. Kwa sababu ya hii, hatutakiwi kutegemea kwamba ndoto ya Yusufu itamaanisha kihalisia kwamba miganda ya ngano itauinamia mganda mwingine, au jua, mwezi, na nyota kumwinamia Yusufu kiuhalisia. Badala yake, sentensi ambayo ni ndoto inatuambia sisi kutegemea lugha ya kitamathali. Katika hali hii, tafsiri inatolewa katika Mwanzo 37:8, 10.
2. Tumia maana ya Kitamathali wakati maana halisi haiwezekani au ni upuuzi. Katika Ufunuo 1:16, Bwana litokea na upanga ukatao kuwili ukitoka kinywani mwake. Katika kitabu kilichojaa lugha ya picha, ni kwa nadra sana kwamba hii itamaanisha picha halisi ya Yesu! Tunapoendelea katika Ufunuo, tunaona kwamba picha ya Yesu akiwa na upanga ukatao kuwili unakaa vizuri katika ujumbe wa ushindi mkuu dhidi ya nguvu za uovu.
Kumbuka kwamba Mungu alitoa Neno lake ili kuwasilisha kweli, si kuficha ukweli. Lugha nyingi za kitamathali katika Biblia zitakuwa dhahiri. Tuliona orodha ya tamathali za usemi katika Somo 6. Hizi hukupa ufahamu mzuri ya jinsi ya kufasiri lugha ya kitamathali. Baada ya kutambua tamathali ya usemi, uliza, "Kwa nini Mungu aliongoza taswira hii mahususi? Ni ukweli gani unaowasilishwa kwa taswira hii?"
Wakati fulani neno linatumiwa kwa njia ya kitamathali na linakuwa alama ya kudumu. Yesu aliposema, “Kondoo wangu waisikia sauti yangu…” (Yohana 10:27), wasikilizaji walijua alimaanisha watu wanaomfuata, na Biblia inatumia alama hiyo nyakati nyingine (Zaburi 23, kwa mfano). Katika Ufunuo 5, Simba aliye wa kabila ya Yuda anatokea mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Kamusi ya Biblia inaeleza kwamba “Simba aliye wa kabila ya Yuda” ni jina la cheo linalomrejelea Masihi. Unapojua hilo, unauliza, “Kwa nini Yohana anatumia jina hili? Jina hili linatuambia nini kuhusu Yesu?” Kwa kutambua tamathali ya semi iliyotumika hutusaidia kuelewa taswira ya Yohana ya nguvu za Yesu za ukombozi.
Ule ukweli kwamba waandishi wa Biblia wakati mwingine walitumia lugha ya kitamathali haimaanishi kwamba hatupaswi kamwe kufasiri maandiko kihalisia. Badala yake, kwa kujua kwamba lugha ya kitamathali ilitumiwa nyakati fulani, tunatakiwa kujaribu kuelewa andiko katika namna ambayo mwandishi alikusudia. Hatupaswi kutumia mawazo yetu kufanya tamko la kibiblia kumaanisha kitu ambacho mwandishi hakuwa anajaribu kusema.
[1]Nyenzo katika sehemu hii zimechukuliwa kutoka sura ya 36 ya Howard G. Hendricks and William D. Hendricks, Living by the Book (Chicago: Moody Publishers, 2007).
Hitimisho
Mwandishi wa Mithali alitoa ahadi hii kwa mtu anayetafuta hekima; “Ukiutafuta kama fedha, Na kuutafutia kama hazina iliyositirika; Ndipo utakapofahamu kumcha BWANA, Na kupata kumjua Mungu” (Mithali 2:4-5). Hakuna chanzo kikuu cha hekima kuliko Neno la Mungu. Kujifunza kwako maandiko kuna malipo ya milele.
(1) Kujifunza neno ni kuchunguza maneno muhimu katika kifungu kwa makusudi ya kugundua maana yake ndani ya muktadha. Kujifunza neno kunatusaidia sisi kutafsiri kwa usahihi kifungu tunachojifunza.
(2) Makosa mawili yaliyozoeleka ya kuepuka unapofanya kujifunza neno:
Kupuuza maana ya awali ya neno
Kufikiri kwamba neno lina maana ile ile katika kila muktadha
(3) Mchakato wa kujifunza neno:
Chagua neno la kujifunza.
Maneno ambayo ni muhimu kwa ajili ya maana ya kifungu
Maneno yaliyorudiwa rudiwa
Tamathali za semi
Maneno yasiyo wazi au ni magumu
Orodhesha maana zinazowezekana kwa kila neno lililochaguliwa.
Tambua kila neno lina maanisha nini katika muktadha wa kila kifungu.
(4) Maswali ambayo yatatusaida kutambua ni nini neno linamaanisha katika muktadha:
Je kuna ukinzani au ulinganifu katika kifungu ambao unakusaidia kutoa maana ya neno?
Ni kwa namna gani mwandishi ametumia neno hili katika maeneo mengine?
Muktadha unaonesha nini kuhusiana na maana ya neno?
(5) Mambo ya kukumbuka unapojifunza lugha ya kitamathali:
Wazo ambalo linawakilishwa ndiyo muhimu.
Picha, kifungu cha maneno, au neno la kitamathali linawakilisha kitu kingine.
Lugha ya kitamathli inataka umakini kwa sifa za kile inayokiwakilisha.
Tunatakiwa kujaribu kuelewa andiko katika namna ambayo mwandishi alikusudia andiko kueleweka hivyo—ama maana ni halisi au ya kitamathali.
(6) Wakati gani tunatafsiri sentensi ya kimaandiko kitamathali:
Wakati kifungu kinakuambia kufanya hivyo
Wakati maana halisi haiwezekani au ni upuuzi
Somo la 7 Mazoezi
(1) Katika Somo la 1, ulichagua kifungu cha maandiko ambayo utayasoma wakati wote wa kozi hii. Kutoka katika kifungu, orodhesha maneo ambayo uanfikiri ni muhimu kujifunza. Angalia maneno muhimu, maneno yaliyorudiwa rudiwa, tamathali za semi, au maneno yasiyo wazi au ni magumu. Jifunze kila mojawapo ya maneno haya kwa kufuata mchakato ulioelezewa katika somo hili. Zingatia muktadha. Tambua maana ya kila neno katika muktadha wa kifungu unachojifunza.
(2) Zingatia kila neno ambalo umekuwa unajifunza. Tafura orodha ya maana zinazowezekana ambazo umezitengeneza katika kujifunza kwako. Ni kwa jinsi gani kutoelewa kwa usahihi maana katika kujifunza kwako kutapelekea kuwa na tafsiri isiyo sahihi ya kifungu? Andika sentensi 2-4 za tafakari.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.