Baadhi ya usomaji si wa muhimu; tunasoma riwaya ili kupitisha muda wakati tunasafiri. Baadhi ya usomaji una umuhimu mdogo; tunasoma maganeti ili kufahamu yanayoendelea katika ulimwengu wetu. Baadi ya usomaji una umuhimu wa milele; tunasoma Maandiko ili kusikia sauti ya Mungu. Paulo aliandika kwamba kila andiko lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki (2 Timotheo 3:16-17). Kwa sababu hii, tunasoma Biblia kwa umakini, ili kumsikia Mungu akisema.
Katika somo la 2, tulifanya uchunguzi kuhusiana na mstari husika. Katika somo hili, tutaviangalia vifungu kikubwa. Hivi vinaweza kuwa kifungu cha andiko, sura, au hata kitabu chote. Katika simulizi za kihistoria, kifungu kikubwa kinaweza kuwa ni habari yote. Katika injili, tunaweza kujifunza mfano, muujiza, au mahubiri. Kifungu kikubwa kinaweza kuwa ni sehemu kuwa ambayo inajikita katika wazo au dhana moja.
Kwa asili, Biblia ilikuwa haijagawanywa katika sura na mistari. Katika karne ya 13, Stephen Langton aligawanya Biblia katika sura ili iwe rahisi kujifunza. Katika karne ya 16, Robert Estienne alichapisha Biblia ilkiwa imegawanywa katika mistari. Mgawanyo wa sura na mistari inatusaidia sisi kujifunza Biblia; hata hivyo, wakati mwingi mgawanyo haukubaliani na mgawanyo wa asili wa andiko. Usiruhusu mgawanyo wa sura kudhibiti kujifunza kwako; fuata mgawanyo wa asili wa andiko na mtiririko wa wazo katika kifungu cha maneno.
Katika somo hili, tutajifunza kifungu cha andiko, Nehemia 1:4-11. Hiki kitakuwa kielelezo kwa ajili ya kujifunza kwako hapo baadae. Tutajifunza njia kadhaa za kujifunza kifungu. Tambua kwamba si kila aina ya ujifunzaji itafanya kazi katika kila kitabu. Somo hili litakupa sanduku za zana au vifaa vya kutumia. Unapojifunza kitabu cha Biblia, utahitaji kuamua, “ni zana gani ni sahihi kwa kitabu hiki?”
Kutafuta Muktadha wa Kifungu cha Maandiko
Nehemia 1:4-11:
Hata ikawa niliposikia maneno hayo, nikaketi, nikalia, nikaomboleza siku kadha wa kadha; kisha nikafunga, nikaomba mbele za Mungu wa mbinguni.
Nikasema, Nakusihi, Ee BWANA, Mungu wa mbinguni, Mungu mkuu, mwenye kuogofya, mwenye kutimiza agano lake na rehema zake kwa hao wampendao na kuzishika amri zake; tega sikio lako, macho yako yakafumbuke, upate kuyasikiliza maombi ya mtumishi wako, ninayoomba mbele zako wakati huu, mchana na usiku, kwa ajili ya wana wa Israeli, watumishi wako; hapo ninapoziungama dhambi za wana wa Israeli, tulizozifanya juu yako; naam, mimi na nyumba ya baba yangu tumefanya dhambi. Tumetenda maovu mengi juu yako, wala hatukuzishika amri, wala sheria, wala hukumu, ulizomwamuru Musa, mtumishi wako.
Nakuomba, likumbuke neno lile ulilomwamuru Musa, mtumishi wako, ukisema, Mkikosa, nitawatawanya kati ya mataifa; bali mkinirudia mimi, na kuzishika amri zangu na kuzitenda, watu wako waliofukuzwa wajapokuwa katika pande za mwisho za mbingu, hata hivyo nitawakusanya kutoka huko, na kuwaleta mpaka mahali pale nilipopachagua ili kuliweka jina langu hapo.
Basi watu hao ni watumishi wako na watu wako, uliowakomboa kwa uweza wako mwingi, na kwa mkono wako hodari. Ee Bwana, nakusihi, litege sikio lako, uyasikilize maombi ya mtumishi wako, na maombi ya watumishi wako, wanaofurahi kulicha jina lako; nakuomba sana; unifanikishe mimi, mtumishi wako, leo, ukanijalie rehema mbele ya mtu huyu.
Maana, nalikuwa mnyweshaji wa mfalme.
Tunapojifunza Kifungu cha andiko, tunahitaji kuutambua muktadha ambao kifungu cha andiko kinapatikana. Nehemia 1:4 inarejelea mwanzoni mwa sura
Hata ikawa niliposikia maneno hayo....
“Maneno hayo” yanatuhitaji sisi turudi katika mistari ya nyuma ili kutafuta ni maneno gani ambayo Nehemia aliyasikia yaliyosababisha mwitikio wake.
Nehemia 1:1 inatoa muktadha wa kitabu cha Nehemia:
Habari za Nehemia, mwana wa Hakalia. Ikawa katika mwezi wa Kisleu, mwaka wa ishirini, nilipokuwapo Shushani ngomeni.
Somo la 2 lilitupa maswali ya kuuliza tunapojifunza mstari.
Nani? “Nehemia, mwana wa Hakalia.” Kuna Nehemia mwingine aliyetajwa baadae katika kitabu hiki (Nehemia 3:16). Jina la familia (“mwana wa Hakalia”) linaonesha ni Nehemia yupi anayerejelewa hapa.
Lini? “…katika mwezi wa Kisleu, mwaka wa ishirini.” Kutoka katika Kamusi ya Biblia, tunajifunza kwamba mwezi wa Kiebrania wa Kislev ni sawa na mwezi Novemba kwenda wa Desemba.[1] “katika...mwaka wa ishirini” haituelezi kwa uwazi kwa sababu hatujui kama mwandishi alirejelea mwaka wa ishirini wa Maisha ya Nehemia, mwaka wa ishirini wa matukio ya kihistoria, au rejea nyinginezo. Katika wakati huu, tunaweza kuwekea alama ya kuuliza pembezoni mwa kifungu hiki. Katika Nehemia 2, tunajifunza jibu; “mwaka wa ishirini wa mfalme Artashasta.” Nehemia alianza Novemba/Desemba mwa mwaka wa ishirini wa utawala wa mfalme Artashasta.
Wapi? Nehemia alikuwa “Shushani ngomeni.” Kutoka katika atlasi au kamusi ya Biblia, tunajifunza kwamba kulikuwa na ikulu mbili katika Uajemi. Ikulu ya wakati wa kiangazi ilikuwa Ek-batana. Ikulu ya masika ilikuwa ya kifahari na ilikuwa Shushani Ngomeni. Kitabu kinaanza wakati Nehemia alikuwa na mfalme Artashasta katika ikulu yake ya wakati wa masika huko Shushani Ngomeni.
Endapo unajifunza neno katika kompyuta yako, inaweza kuwa ya msaada sana endapo kompyuta yako itakitengeneza kwa mtindo mwingine kifungu cha andiko ili kuonesha mahusiano kati ya vishazi hivi. Kifungu cha andiko cha (Nehemia 1:1) kitaonekana kama hivi;
Habari za Nehemia, mwana wa Hakalia. Ikawa
katika mwezi wa Kisleu,
mwaka wa ishirini,
nilipokuwapo Shushani ngomeni...
Mstari wa 1 unatoa mazingira ya kitabu cha Nehemia. Mistari ya 2 na 3 zinaonesha mazingira kwa ajili ya maombi ya Nehemia. Akiwa Shushani Ngomeni, “Hanani, mmoja wa ndugu zangu, akanijia, yeye na watu wengine waliotoka Yuda.” Nehemia aliulizia habari ya mambo mawili.
Nami nikawauliza
habari za Wayahudi waliopona, hao watu wa uhamisho waliosalia; na habari za Yerusalemu.
Katika mwitikio, watu kutoka Yuda waliripoti matatizo mawili:
“Watu wa uhamisho, waliosalia huko katika wilaya ile, wamo katika hali ya dhiki nyingi na mashutumu.”
“Tena ukuta wa Yerusalemu umebomolewa, na malango yake yameteketezwa kwa moto.”
Hii inaonesha matatizo ambayo yalimsukuma maombi ya Nehemia. Baada ya kujifunza muktadha, tupo tayari kufanya uchunguzi kuhusiana na maombi yenyewe.
Uchunguzi wako katika kifungu utategemea mtindo wa kifungu. Simulizi ya kihistoria itajumuisha maswali ya nani, nini, lini, na wapi. Kifungu cha mafundisho kitajumuisha maswali yanayohusiana na mafundisho.[1]
Nehemia 1:5-11 ni maombi. Maombi yake yanajumuisha:
Sifa kwa Mungu “Mungu mkuu, mwenye kuogofya, mwenye kutimiza agano lake.”
Toba kwa ajili ya “dhambi za wana wa Israeli, tulizozifanya juu yako.”
Maombi kwa msingi wa ahadi za Mungu “mkinirudia mimi…nitawakusanya kutoka huko, na kuwaleta mpaka mahali pale nilipopachagua ili kuliweka jina langu hapo.”
Katika hatua hii ni muhimu kuwa makini na taarifa ambazo si za kawaida. Maombi ya Nehemia yanafuatiwa na taarifa ya wasifu: “Maana, nalikuwa mnyweshaji wa mfalme.” Hii kwa mara ya kwanza inaonekana si muhimu, lakini taarifa hii inakuwa ya muhimu kwa kadiri habari inavyosimuliwa.
Kama tukisoma neno mnyweshaji katika kamusi ya Biblia,[2] tunajifunza kwamba mnyweshaji alikuwa ni zaidi ya mtumishi wa kawaida; alikuwa ni afisa wa juu na kwa ujasiri aliaminiwa na mfalme.[3]
Taarifa gani tunaweza kuzichunguza katika kifungu? Angalia:
Mahusiano ya Jumla kwenda Mahususi
Vifungu vingi vinaanza na mtazamo wa jumla ambao baadae unaendelezwa kwa kutumia taarifa mahususi. Taarifa hizi zinaunga mkono tamko la jumla kwa maelezo zaidi.
Mahusiano ya jumla kwenda mahususi ni ya kawaida katika nyaraka za Paulo. Wagalatia 5:16 inatoa ukinzani wa maisha katika Roho na maisha katika mwili; “Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.” Tamko hili la jumla baadae linaumgwa mkono na mfuflulizo wa mambo mahususi. Wagalatia 5:19-21 inatambulisha matendo ya mwili; Wagalatia 5:22-23 inatambulisha tunda la Roho.
Baadhi ya simulizi zinafuata kielelezo cha jumla kwenda mahususi. Mwanzo 1 na 2 inafuata kielelzo hiki, kutembea toka tamko la jumla kwenda kwenye taarifa mahususi. Hii inakuja katika hatua tatu:
1. Mwanzo 1:1 inatoa tamko la jumla: “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi.”
2. Mwanzo 1:3-31 inatoa taarifa za kina kuhusiana na uumbaji. Siku ya kwanza, Mungu aliumba Nuru, siku ya pili Mungu alitenganisha maji na anga; na kuendelea.
3. Mwanzo 2 ni mahususi zaidi. Msimuliaji anatembea kutoka uumbaji wa jumla wa ulimwengu kwenda uumbaji mahususi wa mwanadamu. Habari inajikita kutoka ulimwengu wote na kwenda mahali mahususi, bustani ya Edeni. Hata jina la Mungu limebadilika. Mwanzo 1 inatumia jina Mungu, jina la jumla la nguvu. Mwanzo BWANA MUNGU, jina la kibinafsi kuonesha mahusiano yake ya ndani na Adamu na Eva.[4]
Mara nyingi kielelezo kinaenda kutoka jumla kwenda mahususi. Wakati mwingine hubadilika, kutoka mahususi kwenda jumla. Katika 1 Wakorintho 13, Paulo anatoa mambo mahususi kuhusiana na upendo katika mstari wa 1-12. Sura inamalizika kwa Paulo kutoa tamko la jumla ambalo linafupisha fundisho la Paulo: “Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.”
Sehemu za swali na jibu
Kifungu kinapoanza na swali, swali linaonesha umuhimu wa sehemu iliyobaki ya kifungu. Mfumo huu ni wa kawaida katika kitabu cha Warumi. Kwa wanaofundisha kwamba neema inaruhusu maisha ya dhambi, Paulo anauliza, “Tuseme nini basi? Tudumu katika dhambi ili neema izidi kuwa nyingi?” (Warumi 6:1). Kisha anaonesha kwamba neema ya Mungu inampa nguvu mkristo ya kushinda dhambi, “Hasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi?” (Warumi 6:2).
Injili ya Marko mara kwa mara imetumia muundo huu. Katika Marko 2:1–3:6, matukio matano yameanza na mswali. Mara nne, wapinzani wameuliza swali. Kila wakati, Yesu alijibu kwa utetezi. Katika tukio la mwisho, Yesu anauliza swali ambalo mafarisayo walishindwa kulijibu. Kuwa makini namna ambavyo hii inatoa muundo wa sehemu kubwa. Pasipo hii, tunasoma habari tano binafsi. Tunapoona muundo unaoundwa na maswali na majibu, habari tano zinatoa ushuhuda kwa mamlaka ya kimasihi ya Mwana wa Adamu.
Jibu: Yesu anaonesha mamlaka yake kwa kumponya mtu aliyepooza.
2. Kula na wenye dhambi (Marko 2:13-17)
Swali: “Mbona anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?”
Jibu: “sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”
3. Kufunga (Marko 2:18-22)
Swali: “Kwani wanafunzi wa Yohana na wanafunzi wa Mafarisayo hufunga, bali wanafunzi wako hawafungi?”
Jibu: “Muda wote walipo na bwana-arusi pamoja nao hawawezi kufunga.”
4. Sheria za Sabato (Marko 2:23-28)
Swali: “mbona wanafanya lisilokuwa halali siku ya sabato?”
Jibu: “Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato pia.”
5. Uponyaji siku ya Sabato (Marko 3:1-6)
Swali: “Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya?”
Jibu: Wapinzani wa Yesu alibaki kimya.
Mahojiano
Injili mara nyingi zinaonesha mahojiano kati ya Yesu na wale wanaomzunguka. Tunaweza kupata uelewa zaidi wa mafundisho ya Yesu kwa kuuliza maswali kama:
Washiriki ni kina nani katika mahojiano?
Nani walikuwa watazamaji waliokuwa wanasikiliza mazungumzo hayo? Waliitikia kwa namna gani?
Ni mgogoro gani ambao ulisababisha mahojiano?
Mathayo 21:23–22:46 inaonesha mfululizo wa mahojiano kati ya Yesu na wapinzani wake. Kila kundi liliuliza maswali ili kumnasa Yesu.
Kwanza, viongozi wa kidini walihoji mamlaka yake (Mathayo 21:23-46).
Mafarisayo na maherode (mara nyingi walikuwa maadui) waliungana pamoja ili kumnasa Yesu kwa kuuliza maswali kuhusiana na kodi (Mathayo 22:15-22).
Masadukayo (ambao hawakuamini ufufuo) walimuuliza Yesu swali kuhusiana na ndoa baada ya ufufuo (Mathayo 22:23-32).
Mafarisayo walijaribu tena kwa swali lingine kuhusiana na amri (Mathayo 22:34-40).
Mwisho, Yesu anamaliza mgogoro kwa kuuliza swali ambalo hawakuweza kujibu (Mathayo 22:41-46).
Makutano walikuwa wakiangalia wakati makundi yote yalipokuwa yanajaribu kumnasa Yesu, na walikuwa waliangalia wakati Yesu alipowafumba vinywa kila wauliza swali. “Na makutano waliposikia, walishangaa kwa mafunzo yake” (Mathayo 22:33).
Mahojiano ni muhimu katika kitabu cha Ayubu. Kitabu hiki kinajumuisha mazungumzo kati ya Mungu na Shetani, kati ya Ayubu na marafiki zake, na kati ya Ayubu na Mungu.
Kitabu chote cha Habakuki kinajumuisha mahojiano kati ya nabii na Mungu. Kitabu kimeundwa kama hivi:
Habakuki anauliza maswali: Kwa nini Mungu anavumilia dhambi ya Yuda (1:1-4)?
Mungu anajibu: Babeli watawashinda Yuda (1:5-11).
Habakuki anauliza maswali: Mungu anawezaje kuwatumia Babeli waovu ili kuhukumu Yuda (1:12-2:1)?
Mungu anajibu: Habakuki lazima aishi kwa imani katika makusudi ya Mungu (2:2-20).
Toni ya Kihisia
Toni ya kihisia inarejelea hisia ambazo mwandishi anaonesha. Maandiko ni zaidi ya habari ya kufikirika; ni hadithi ya uhusiano kati ya Mungu mwenye upendo na watu aliowaumba. Uhusiano huo wa karibu unahusisha hisia. Wasomaji makini huzingatia hisia za mwandishi.
Ili kutafuta toni ya kihisia ya kifungu cha andiko, angalia maneno ambayo yanaonesha hisia (furaha, dharau, maombolezo) au mahusiano (baba, mwana, binti). Sikiliza roho ya mwandishi na ya wapokeaji katika simulizi.
► Soma Wafilipi 1:1-8 ikifuatiwa na Wagalatia 1:1-9. Ni toni gani za hisia zinazoonekana katika kila kifungu? Kutoka katika utangulizi, unaweza kuhitimisha nini kuhusu uhusiano wa Paulo na kanisa la Filipi na makanisa ya Galatia?
[1]Nyenzo nyingi katika sehemu hii yamechukuliwa kutoka katika Sura ya 4 ya kitabu cha J. Scott Duvall and J. Daniel Hays, Grasping God’s Word (Grand Rapids: Zondervan, 2012).
[3]J. D. Douglas, New Bible Dictionary, (2nd edition), (Wheaton: Tyndale House, 1982)
[4]Jina la Kiebrania Elohim linatafsiriwa Mungu katika Biblia za Kiswahili; ni jina la jumla, lenye utisho. Jina la Kiebrania Yahweh is limetafsiriwa “BWANA” katika Biblia za Kiswahili; ni jina la kibinafsi lililofunuliwa katika in Kutoka 3:14.
Nini cha kuangalia unaposoma kitabu chote
Tunaposoma kitabu chote, tunaangalia muundo na dhana kuu katika kitabu. Mambo ya kuchunguza katika hatua hii yanajumuisha:
Mambo Yanayosisitizwa
Tunaweza kupata kile kinachosisitizwa na kitabu kwa kuchunguza:
Kiwango cha Nafasi
Kiwango cha nafasi ambacho kitabu kinatoa kwa mada mara nyingi kinaonesha nini ni muhimu kwa mwandishi. Katika Mwanzo, watu wanne (Ibrahimu, Isaka, Yakobo, na Yusufu) wamesomwa katika sura ya 12-50. Hii ikilinganishwa na sura 11 tu ambazo zinaelezea habari ya Uumbaji, Anguko, gharika, na mnara wa Babeli. Kuwa makini na taarifa hizi katika hatua ya Uchunguzi kutatuandaa sisi kujiuliza “kwa nini?” katika hatua ya kutafsiri.
Tunaposoma kitabu cha Nehemia, tunagundua kwamba maombi yamechukua nafasi kuu katika kitabu. Katika kila wakati muhimu katika maisha ya Nehemia, aliomba. Kwa kutambua hili, tunaandaliwa kuelewa vizuri tabia ya Nehemia.
Kusudi Lililotamkwa
Katika baadhi ya vitabu, mwandishi anatuambia kusudi la kiandika kwake. Mithali inaanza na tamko refu la kusudi la Sulemani katika kuandika mkusanyiko wake wa hekima (Mithali 1:2-6). Injili ya Yohana inatamka kusudi lake: “ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake” (Yohana 20:31).
Mpangilio wa Nyenzo
Katika simulizi ya kihistoria, mpangilio wa nyenzo unaweza kuonesha kusudi la mwandishi. 2 Samweli 1-10 inaelezea habari ya ushindi wa ufalme wa Daudi. 2 Samweli 11 inarekodi dhambi ya Daudi na Bathsheba. Kutoka hapo, 2 Samweli inafuatilia matatizo yaliyokuja katika ufalme wa Daudi. Mwandishi wa 2 Samweli anaonesha kwamba matatizo ni hukumu ya Mungu kwa dhambi ya Daudi.
Nehemia imegawanywa katika sehemu kuu tatu. Katika Nehemia 1-6, Nehemia anajenga tena ukuta wa mji. Nehemia 7-12 inaorodhesha watu waliorudi Yerusalemu na inasimulia kufanya agano upya. Nehemia 13 inaangazia matatizo yaliyotokea baada ya Nehemia kurudi Yerusalemu mara ya pili. Mpangilio huu unaonesha kwamba ujenzi wa ukuta haukutosheleza; Yuda walihitaji uamsho ili kuangazia tatizo la asili ambalo lilipelekea uhamisho.
Mambo Yaliyorudiwa Rudiwa
Kujirudia rudia ni njia ambayo waandishi wa Biblia wanaweza kuitumia kusisitiza nyenzo.
Maneno na vishazi vilivyorudiwa rudiwa
Neno kumbuka limerudiwa rudiwa katika kitabu chote cha Nehemia. Nehemia anamuuliza Mungu “likumbuke neno lile ulilomwamuru Musa, mtumishi wako” (Nehemia 1:8). Wakati watu wa Yerusalem wametishiwa, Nehemia anawauliza “mkumbukeni Bwana, aliye mkuu mwenye kuogofya” (Nehemia 4:14). Mara tatu, Nehemia anaomba Mungu amkumbuke yeye na uaminifu wake. Kumbukumbu ni muhimu kwa Nehemia; kile Mungu amefanya huko nyuma kinatoa ujasiri katika uaminifu wa Mungu huko mbeleni.
► Soma Zaburi 119:1-32. Kila mstari unatumia baadhi ya maneno yanayorejelea Neno la Mungu. Kutokana na hili, tengeneza orodha inayoonesha kile ambacho mzaburi anaamini kuhusiana na umuhimu wa Neno la Mungu.
Watu waliorudiwa rudiwa
Barnaba ametokea tena katika maeneo muhimu sana wakati wote katika kitabu cha Matendo ya Mitume. Kila wakati Barnaba alipotokea, aliliishi jina lake alilopewa, “Mwana wa faraja” (Matendo ya Mitume 4:36). Barnaba anamleta Paulo kwa mitume na kushuhudia ukweli wa badiliko la Sauli (Matendo ya Mitume 9:27). Akiwa na Paulo, Barnabas analijenga kanisa la Antiokia (Matendo ya Mitume 11:22-26). Pasipo kujali mashaka ya Paulo, Barnaba anamtia moyo kijana mdogo Yohana Marko (Matendo ya Mitume 12:25 na Matendo ya Mitume 15:36-39). Barnaba kuonekana kwa kujirudia katika kitabu cha Matendo ya Mitume kunaonesha ni kwa namna gani kanisa la kwanza lilitimiza Agizo kuu la kufanya waamini kuwa wanafunzi.
Matukio au Mazingira yaliyorudiwa rudiwa
Kitabu cha Waamuzi kinajumuisha mfululizo wa habari za kuanguka kwa Israeli kutoka ushindi mkuu chini ya uongozi wa Yoshua hadi kwenye ghasia za kijamii. Mara saba mzunguko umerudiwa ambapo wana wa Israeli wanafanya yaliyo mabaya mbele za Mungu na wanashindwa na adui zao. Kila wakati Mungu alimwinua mwamuzi ili kuwakomboa. Habari hii inayorudiwa rudiwa inaonesha kuanguka kwa taifa la Israeli.
Kuhama kwa Mwelekeo
Kuhama kwa mwelekeo ni mabadiliko katika msisitizo wa mwandishi. Kwa mfano, mwelekeo wa Paulo mara nyingi hubadilika karibu na katikati ya kitabu. Waefeso inaanza na msisitizo wa nini Mungu amefanya kwa watu wake; sehemu ya pili ya Waefeso inasisitiza nini watu wa Mungu wanatakiwa kufanya kama utii kwa Mungu.
Katika Waefeso 1-3, vitenzi vielezi vinaonesha nini ambacho Mungu amefanya kwa watu wake. Mungu:
Aliyetubariki (Waefeso 1:3, 6)
Alivyotuchagua (Waefeso 1:4)
Alitangulia kutuchagua (Waefeso 1:5)
Kuanzia Waefeso 4:1, Paulo anaangazia wajibu wa mwamini wa kuishi katika namna inayopasa kazi ya wokovu ndani yetu. Katika Waefeso 4–6, vitenzi vingi vinaonesha maagizo. Paulo anatuagiza sisi:
Mkaseme kweli (Waefeso 4:25)
Msimuhuzunishe Roho Mtakatifu (Waefeso 4:30)
Mkaenende katika upendo (Waefeso 5:2)
Mnavyoenenda (Waefeso 5:15)
Waheshimu baba yako na mama yako (Waefeso 6:2)
Vaeni silaha zote za Mungu (Waefeso 6:11)
Mabadiliko ya mwelekeo kutoka kufurahia kile ambacho Mungu amefanya kwa ajili yetu kwenda kwenye vile ambavyo sisi tunatakiwa kuishi kama mwitikio wa neema yake unaonekana katika vitenzi. Kuchunguza kwa makini mabasiliko hayo kutatuandaa sisi kutafsiri kwa usahihi ujumbe wa Paulo katika Waefeso.
Muundo wa Uandishi
Ingawa kuna njia nyingi tofauti tofauti ambazo kitabu kinaweza kupangwa, aina tatu za muundo wa uandishi ni rahisi kutambua.[1]
Muundo wa Kiwasifu
Vitabu vya historia mara nyingi vimepangwa kuzunguka watu mahususi. Habari inamsingi katika matukio ya maisha ya mtu. Kwa mfano:
Mwanzo 12-50: Watu Wanne Mashuhuri
Sura
Mtu
Mwanzo 12-25
Ibrahimu
Mwanzo 25-26
Isaka
Mwanzo 27-36
Yakobo
Mwanzo 37-50
Yusufu
Samweli wa 1 na 2 inafuatilia kupanda na kuanguka kwa wafalme wawili wa kwanza wa Israeli, Sauli na Daudi.
1 & 2 Samweli: Wafalme wa Kwanza wa Israeli
Sura
Kupanda/kuanguka kwa wafalme
1 Samweli 1-8
Nabii Samweli
1 Samweli 9-12
Kupanda kwa Sauli
1 Samweli 13-31
Kuanguka kwa Sauli & Kupanda kwa Daudi
2 Samweli 1-10
Mfanikio ya Daudi
2 Samweli 11-24
Mapambano ya Daudi
Muundo wa Kijiografia
Jiografia inatoa muundo wa baadhi ya vitabu. Habari inaendelea kwa kadiri matukio yanavyotokea katika maeneo tofauti tofauti ya kijiografia. Atlasi ya Biblia itakusaidia kuweka muundo wa yaliyomo katika vitabu hivi.
Kutoka: Safari ya Israeli
Kifungu
Eneo
Kutoka 1:1-3:16
Israeli Misri
Kutoka 13:17-18:27
Israeli jangwani
Kutoka 19-40
Israeli katika mlima Sinai
Yesu aliwaagiza wanafunzi wake kuwa mashahidi wake “katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi” (Matendo ya Mitume 1:8). Kitabu cha Matendo ya Mitume kinafuatilia kanisa la kwanza linavyotimiza Agizo hili.
Matendo ya Mitume: Injili Inafikia Mataifa
Sura
Eneo
Matendo ya Mitume 1-7
Yerusalemu
Matendo ya Mitume 8-12
Yudea & Samaria
Matendo ya Mitume 13-28
Mwisho wa nchi
Muundo wa Kihistoria au Kiwakati
Baadhi ya vitabu vimeundwa kwa kuzingatia mpangilio wa matukio muhimu ya kihistoria, mara nyingi ni mpangilio wa muda. Kuwekea alama matukio haya kutatupatia mtazamo wa jumla wa kitabu.
Kitabu cha Yoshua kinafuatilia kuteka na kukaa Kanaani. Muundo wa Yoshua unafuata matukio ya msingi ya kuteka (nchi ya Kanaani).
Kuvuka kwenda Kanaani (Yoshua 1–5)
Kuuteka Yeriko (Yoshua 6)
Kushindwa kule Ai (Yoshua 7–8)
Kufanya agano upya huko Shekem (Yoshua 9)
Kampeni ya vita ya kusini (Yoshua 10)
Kampeni ya vita ya Kaskazini (Yoshua 11–12)
Mgawanyo wa ardhi na makazi (Yoshua 13–23)
Kufanya agano upya huko Shekem (Yoshua 24)
Kusudi la Yohana kuandika injili yake limetamkwa mwishoni mwa kitabu. “Basi kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki. Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake” (Yohana 20:30-31). Injili ya Yohana imepangwa kuzunguka miujiza saba ambayo inatimiza kusudi lake. Ishara hizi saba zinatoa muundo wa kitabu chote:
Kubadili maji kuwa divai (Yohana 2:1-12)
Kumponya mwana wa Afisa (Yohana 4:46-54)
Uponyaji katika Bethzatha (Yohana 5:1-47)
Kulisha watu 5,000 (Yohana 6:1-4)
Kutembea juu ya maji (Yohana 6:15-21)
Kumponya mtu aliyezaliwa kipofu (Yohana 9:1-41)
Kumfufua Lazaro (Yohana 11:1-57)
[1]Nyenzo hizi zimechukuliwa kutoka katika sura ya 15 ya Howard G. Hendrick na William D. Hendricks, Living by the Book (Chicago: Moody Publishers, 2007).
Kuona Picha Kubwa
Hadi sasa, tumechunguza taarifa kuhusiana na mstari, kifungu kikubwa cha maandiko, na vitabu vyote.[1] Hatua ya mwisho ni hatua ya Uchunguzi ni kupanga taarifa ya uchunguzi katika mfumo ambao ni rahisi kutumia. Njia mojawapo nzuri ya kutumia ni kuweka nyenzo katika jedwali la ufupisho. Hii inaonesha muunganiko baina ya sehemu kubwa katika maandiko. Pia inatoa ufupisho katika maandalizi ya hatua ya tafsiri katika kujifunza Biblia.
Zipo njia nyingi tofauti tofauti za kupanga jedwali hili. Mgawanyo katika jedwali unategemea mtindo wa kifungu unachojifunza. Katika sehemu hii, tutatumia aina kadhaa za majedwali ili kuonesha namna ambavyo jedwali linaweza kukusaidia kujifunza Biblia.
Kuweka Kwenye Jedwali Matukio Yanayohusiana
Ilikuwa imetajwa hapo awali kwamba mgawanyo wa sura mara nyingine hauendani na muundo wa kitabu. Jedwali linaloonesha mahusiano baina ya matukio linaonesha umoja wa mfululizo wa matukio ambayo yanatokea katika sura kadhaa. Mara nyingi hii itaonesha ulinganifu au ukinzani baina ya matukio.
Marko 4:35—Marko 5:42 inaonesha mfululizo wa Miujiza minne. Kama ukilinganisha habari nne, utaona kwamba habari zinaonesha kukosa imani kwa wanafunzi wa Yesu katikati ya dhoruba na imani ya watu ambao hawakutegemewa: mtu aliyepagawa na pepo, mwanamke aliyetokwa na damu, na kiongozi wa sinagogi. Marko inaonesha kwamba wanafunzi walikuwa mashuhuda wa kuona kwa macho kwa kila habari hizi kubwa za imani kubwa. Zitazame habari hizi upande kwa upande:
Miujiza Minne
Muujiza
Watu katika Habari
Jukumu la Imani
Kutuliza dhoruba
Yesu
Wanafunzi
Wanafunzi hawakuwa na imani (Marko 4:40).
Kumponya aliyepagawa na pepo
Yesu
Mtu aliyepagawa na pepo
Watu wa mji
Wanafunzi (wakishuhudia)
Mtu alimwabudu Yesu (Marko 5:6) na kumshuhudia Yesu (Marko 5:18-20).
Watu wa mji walimkataa Yesu (Marko 5:10).
Kumponya mwanamke aliyetokwa na damu
Yesu
Mwanamke
Wanafunzi (wakishuhudia)
Mwanamke alikuwa na imani na akachukua hatua ya kumgusa Yesu (Marko 5:28, 34).
Kumfufua binti Yairo
Yesu
Yairo na binti yake
Waombolezaji
Petro, Yakobo, na Yohana
Yairo alikuwa na imani (Marko 5:23).
Zamu Yako
Andaa jedwali kwa msingi wa Mathayo 13:1-23.
1. Soma habari mara tatu.
2. Wekea alama Uchunguzi kwa kadiri unavyopata.
3. Jaza jedwali na mawazo wa msingi katika mfano.
Kumbuka kwamba Jedwali sio lengo; jedwali ni nyenzo ya kukuwezesha wewe kujifunza na kulitendea kazi neno la Mungu katika maisha yako. Lengo la kujifunza Biblia ni kubadilika. Katika kujifunza mfano huu, uliza, “Mimi ni udongo wa aina gani? Je, ninaliruhusu neno la Mungu kuzaa matunda katika maisha yangu?”
Soma Marko 5:21-43. Ni habari moja ambayo ina miujiza miwili. Habari ya mwanamke aliyetokwa damu inaingilia kati habari ya Yairo na binti yake. Ni nini ulinganifu na ukinzani kati ya habari hizi mbili? Muundo unaonekana kama hivi:
Jedwali linaweza kukusaidia kufupisha kitabu chote. Hili linaonesha picha kubwa ya kitabu. Katika kuandaa jedwali, soma kitabu chote mara kadhaa. Angalia sehemu kubwa. Unaposoma, wekea alama maneno yaliyorudiwa rudiwa, maswali na majibu, na mahusiano mengine yanaoonesha muundo wa kitabu.
Kujifunza 1 Petro – Kutia Moyo kwa Watakatifu Wanaoteseka
Wokovu (1:1–2:10)
Kutii (2:11–3:12)
Mateso (3:13–5:11)
Nafasi ya Wokovu
(1:2-12)
Matokeo ya Wokovu (1:13-25)
Mchakato wa Wokovu (2:1-10)
Katika serikali (2:13-25)
Katika familia (3:1-12)
Kama mwananchi
(3:13–4:6)
Kama mwamini (4:7-19)
Kama mchungaji
(5:1-11)
Hatma ya Mkristo
Wajibu wa Mkristo
Maadili ya Mkristo
Sehemu tatu kubwa za 1 Petro zinahusiana. Hatutaweza kuelewa mateso (3:13–5:11) hadi tuwe tumejitiisha katika mapenzi ya Baba (2:11–3:12); hatutaweza kujitiisha kwa Baba hadi tuwe tumeelewa nguvu yake ya kuokoa (1:1–2:10).
Zamu Yako
Andaa jedwali lako kuhusiana na Waefeso. Jedwali hili litakusaidia kufuatilia dhana katika waraka wa Paulo. Mfano mmoja umetolewa. Unapomaliza, jiulize:
Kuna mahusiano gani kati ya kila mada kuu?
Je, kuna mada moja kati ya hizi ambayo imezungumzwa sana kuliko zingine?
Ni kwa namna gani kila mada inahusiana na muundo mzima wa kitabu?
[1]Nyenzo katika sehemu hii yana msingi katika sura ya 24-25 ya Howard G. Hendricks na William D. Hendricks, Living by the Book (Chicago: Moody Publishers, 2007).
(1) Unaendelea na mchakato wa Uchunguzi kwa kusoma kifungu cha maandiko na kisha kitabu chote. Kwa asili, Biblia ilikuwa haijagawanywa katika sura na mistari. Ni lazima uhakikishe kwamba unafuata mgawanyo wa asili wa andiko katika kujifunza kwako.
(2) Unaposoma kifungu cha maandiko, angalia:
Mahusiano ya jumla kwenda mahususi
Sehemu za swali na jibu
Mahojiano
Toni ya kihisia
(3) Unaposoma kitabu chote, angalia:
Mambo Yanayosisitizwa. Mwandishi anaweza kusisitiza mambo akijumuisha:
Kiwango cha Nafasi
Kusudi lililotamkwa
Mpangilio wa nyenzo
Mambo Yaliyorudiwa Rudiwa
Maneno na vishazi vilivyorudiwa rudiwa
Watu waliorudiwa rudiwa
Matukio au mazingira yaliyorudiwa rudiwa
Kuhama kwa Mwelekeo
Muundo wa Uandishi
Muundo wa Kiwasifu
Muundo wa Kijiografia
Muundo wa Kihistoria au Kiwakati
(4) Kutengeneza jedwali katika sehemu ya maandiko au kitabu chote kunaweza kuelezea muundo.
Somo la 3 Zoezi
Katika Somo la 1, ulichagua kifungu cha maandiko ambayo utayasoma wakati wote wa kozi hii. Kwa kufuata hatua zilizotolewa katika somo hili, fanya uchunguzi kwa kiasi kikubwa juu ya kifungu ulichochagua. Kumbuka, haujaanza kutafsiri mstari au hauandai muhtasari wa ujumbe. Unaangalia tu taarifa za kina katika kifungu. Ikiwa ni muhimu, tayarisha jedwali linalofupisha Uchunguzi wako. Ikiwa unasoma kwenye kikundi, shirikisha Uchunguzi wako kwenye mkutaniko wenu unaofuata.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.