[1]► Pata mwanakikundi mmoja au wawili kutoka katika kundi lako waelezee safari yao ya kufika katika eneo mnalokutana kwa ajili ya kozi hii. Wajumuishe taarifa nyingi kwa kadiri inavyowezekana. Je, mlipita karibu na migahawa, makanisa, au biashara? Je, mlipita vibao vingapi vya kusimama au mlipita taa za barabarani ngapi? Mlikatisha kona mara ngapi? Je, mlikutana na chochote ambacho si cha kawaida, kitu chochote ambacho kwa kawaida hakiko katika safari yenu? Kila mmoja atakapomaliza kuelezea, jadilini ni kiasi gani kimechunguzwa na kiasi gani hakikuchunguzwa.
Juma anapomaliza kusoma Biblia, humalizia na picha akilini. Ukimuomba Juma asome na kufupisha Marko 1:29-31, angesema, “Yesu aliondoka kwenye Sinagogi kule Galilaya akiwa na wanafunzi wake wanne (Simoni, Andrea, Yakobo na Yohana). Walikwenda nyumbani kwa Simoni ambapo Mama mkwe wake na Simoni alikuwa anaumwa na homa kali. Yesu akamuinua kwa mkono wake na homa ikamwacha mara. Alikuwa mzima sana kiasi kwamba aliwaandalia chakula. Hakuhitaji hata muda wa kupumzika ili kupona.”
Yusuf akisoma Biblia, yeye husoma maneno lakini huona taarifa chache. Ukimwambia Yusuf asome na kufupisha Marko 1:29-31, angesema, “Yesu alitembelea nyumbani kwa Simoni na kumponya mtu mmoja.”
Ni msomaji gani kati ya hawa wawili alichunguza? Ni msomaji gani ataikumbuka habari kwa muda mrefu? Ni msomaji gani ana taarifa za kutosha ambazo zinaweza kuwa msingi wa tafsiri ya habari hii? Jibu liko wazi. Juma aliona kile kilichotokea katika Marko 1:29-31. Yusuf alisoma sura, lakini hakuchunguza.
Hatua ya kwanza ya kujifunza Biblia ni uchunguzi. Katika hatua hii, tunauliza, “ni nini ninachokiona katika sehemu hii ya maandiko? Msingi wa ufanisi katika kutafsiri Biblia ni kuchunguza sana kwa kadiri inavyowezekana. Katika somo hili, tutajifunza kuchunguza taarifa muhimu katika mstari. Uwe na subira unapofanya hivi, unapochunguza zaidi, ndivyo unavyopata nyenzo kwa ajili ya tafsiri yako.
“Unifumbue macho yangu niyatazame Maajabu yatokayo katika sheria yako.”
- Zaburi 119:18
Uchunguzi kutoka katika Mstari
Matendo ya Mitume 1:8:
Lakini mtapokea nguvu
akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu,
nanyi mtakuwa mashahidi wangu
katika Yerusalemu
na katika Uyahudi wote
na Samaria,
na hata mwisho wa nchi.
Ni nini tunaweza kuchunguza katika mstari mmoja?
Neno la kwanza ni lipi?
“Lakini.” Lakini ni kiunganishi ambacho kinaunganisha mstari uliopita. katika Matendo ya Mitume 1:6, wanafunzi walimuuliza, “Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme?” Sasa kwa sababu umefufuka kutoka wafu, je, utausiamaisha ufalme wako? Yesu anajibu kwa matamko mawili:
“Si kazi yenu kujua nyakati wala majira…” (Matendo ya Mitume 1:7). Huu ni wajibu wa Baba.
“Lakini mtapokea nguvu… nanyi mtakuwa mashahidi wangu.” Huu ni wajibu wenu.
Nani Wanahusika?
“Nanyi.” Yesu anazungumza na nani? Mitume (Matendo ya Mitume 1:2, 4). Chukua muda kuuliza, “Mitume hawa ni nani?” Orodhesha kila unachofahamu kuhusiana na mitume. Nani katika mstari huu unahusiana, inaonesha nguvu ya ajabu ya kubadilisha ya Pentekoste.
Wao ni Wayahudi; Yesu anawatuma Samaria!
Hawakuwa na uwezo wa kumponya kijana aliyepagawa na pepo (Marko 9:14-29); watapokea nguvu.
Walikimbia kwa hofu wakati Yesu anakamatwa (Mathayo 26:56); watakuwa mashahidi wake hadi mwisho wa nchi.
Kitendo cha Sentensi ni nini?
“Mtapokea.” Kitendo kinatuambia ni nini kitatokea. Katika hali hii, wakati wa kitendo unaagazia kitu ambacho watakipokea baadae.
Watapoka nini?
“Nguvu.” Kitabu cha Matendo ya Mitume kitaonesha nguvu hii katika huduma za mitume.
► Hii inakufanya wewe uanze. Fanyia kazi mistari inayofuata, kwa kujibu maswali haya:
Watapokea lini?
Nani atawapa nguvu?
Matokeo ya nguvu ni nini? (Nguvu inatangulia ushuhuda. Matokeo ya asili ya nguvu itakuwa ni shahuku ya kushirikisha Injili na wengine.)
Watakuwa mashahidi wa nani?
Watashuhudia wapi? (unafahamu nini kuhusiana na maeneo hayo manne? Ni nini maalumu kuhusiana na Samamria, je, mitume hawa wa Kiyahudi wangetaka kwenda huko?)
Kuza Nguvu zako za Uchunguzi
Neema alikuwa na uoni hafifu. Alipokuwa shuleni, alikuwa hawezi kumuona mwalimu wake vivuri. Alikuwa hawezi kusoma maneno katika ubao wa chaki akiwa mbele kabisa ya darasa. Kisha siku moja, akaanza kuvaa miwani ya macho. Ghafla, aliona vitu ambavyo hakuviona hapo kabla! Aliweza kuona uso wa mwalimu wake vizuri. Aliweza kusoma kwa urahisi kile kilichoandikwa katika ubao. Alikuwa na furaha!
Uchunguzi makini ni sawa na kuvaa miwani ya macho ili kurekebisha uoni hafifu. Kujifunza jinsi ya kuchunguza maandiko kunakuza uelewa wako wa kile ambacho maandiko yanasema.
Kufanyia mazoezi Matendo ya Mitume 1:8 inaonesha ni kwa umakini kiasi gani umechunguza kile unachokisoma. Hebu tujadili maadhi ya dondoo kwa ajili ya kukuza nguvu zako za uchunguzi. Utajifunza maswali ya kuuliza ambayo yataleta maandiko katika uelewa wa wazi. Kisha utafanya mazoezi ya kusoma mistari mingine.
Unaposoma mstari katika Biblia, tafadhali usiseme, “tayari ninaufahamu mstari huu!” badala yake, muulize Mungu afungue macho yako kwa neno lake kwa namna mpya. Stadi katika somo hili zitakusaidia kusoma kwa uelewa mpya.[1]
Soma ili Kupata Uelewa
Mvulana wa miaka 10 aliamua Kamba atasoma Biblia yote kwa mwaka kila mwaka. Alikuwa ameamua vizuri; kwa bahati mbaya, alikuwa hajui namna ya kusoma Biblia kwa ufanisi. Alikuwa na kalenda inayoonesha kiasi gani cha kusoma kila siku, lakini mara kwa mara aliachwa nyuma. Jumapili mchana, alijaribu kukimbizana nayo. Angeangalia kalenda ili kuona kwamba amechwa nyuma kwa sura 20 (katika Mambo ya Walawi!). Kwa hiyo, angesoma Mambo ya Walawi yote mchana huo. Angesoma kwa haraka kwa kadiri alivyoweza, akijaribu kufika mwisho. Dakika 10 baada ya kumaliza, asingeweza kukuambia ujumbe wa Mambo ya Walawi. Alikuwa anasoma bila uelewa.
Kusoma ili kuelewa ni kazi ngumu. Biblia inaelezea Kuutafuta ukweli kama hivi: “Ukiutafuta kama fedha, Na kuutafutia kama hazina iliyositirika; Ndipo utakapofahamu kumcha BWANA, Na kupata kumjua Mungu” (Mithali 2:4-5). Soma andiko kwa makini. Uliza maswali. Andika nakili. Soma na akili yako.
Wakati mwingine unaweza kupata uelewa kwa kuyasema maandiko kwa maneno yako. Wakati kuyasema maandiko kwa maneno yako sio kutafsiri, kunaweza kukusaidia kufikiri kwa kina kuhusiana na maana ya andiko.
Uliza Maswali Unaposoma
Ufunguo wa kusoma na akili yako ni kuuliza maswali.
► Soma Luka 24:13-35 kabla ya kuendelea na sehemu hii. Wakati unajifunza hili somo, rejea tena katika Luka 24 ili kujibu kila swali.
(1) Nani?
Watu hawa ni nani katika andiko? Unafahamu nini kuhusiana na kila mtu?
Watu katika Luka 24:13-35 ni nani? Cleopa na mwenzake ambaye hajatajwa kwa jina[2] walikuwa wanasafiri kwenda Emau siku ya ufufuo. Walikuwa ni wafuasi wa Yesu ambao waliifahamu Miujiza yake na mafundisho yake. Jumapili hii, walikuwa ni watu wa kwanza kuelezewa mateso na ufufuo na Yesu mwenyewe; walikuwa mashuhuda wa kwanza wa ufufuo.
(2) Nini?
Nini kinatokea katika andiko? Endapo ni andiko la kihistoria, ni matukio gani yametokea? Endapo ni waraka, mwandishi anajaibu kufundisha nini?
Katika Luka 24, tukio lilikuwa ni kufunuliwa kwa Yesu. Macho ya watu hawa wawili yalifunuliwa kuona uhalisia wa ufufuo wa Yesu (Luka 24:31).
(3) Lini?
Kama swali lililopita, muda unatoa muktadha katika kujifunza kwetu. Katika hatua ya Uchunguzi ya kujifunza Biblia, tunaangalia kuhusiana na muda ndani ya andiko lenyewe. Kutoka Luka 24:13, tunajifunza kwamba safari ya kwenda Emau ilikuwa siku ile ile ambayo waligundua kaburi liko tupu.
Wanafunzi hawa wawili walikutana na Yesu masaa machache tu baada ya kaburi tupu kugundulika. Hii inatueleza kitu kuhusiana na hisia zao wanapozungumza na kuhojiana (Luka 24:15). Fikiri kuhusiana na hisia zao zilizokuwa juu na chini katika siku tatu zilizopita.
Alhamisi, walijisikia kukata tamaa walipomuona Yesu amekamatwa. Ijumaa, matarajio yao ya ufalme wa kimasihi yalivunjika walipomuona Yesu amekufa. Sasa ni Jumapili, na kaburi liko tupu. Wakiwa wanasafiri kwenda Emau, walikuwa wanajaribu kuelewa uajabu wa mfululizo wa matukio.
(4) Wapi?
Inasaidia kuuliza, “haya yalitokea wapi?” Atlasi ya Biblia inakusaidia kutafuta majibu ya swali hili. Baadhi ya Biblia zina ramani nyuma yake.
Katika Luka 24, Cleopa na mwenzake ambaye hajatajwa kwa jina wamesafiri kutoka Yerusalemu kwenda Emau, kijiji kilichokuwa kilometa 11 magharibi kwa mji. Walipokuwa wamemaliza kutembea umbali huu, tayari ilikuwa jioni. Lakini baada ya macho yako kufumbuliwa, watu hawa walirudi Yerusalemu kwa furaha. Habari hizi zisingeweza kungoja hadi siku inayofuata!
(5) Kwa nini?
Tunaona kwa nini wanafunzi hawa walikuwa wamevunjika moyo tulipokuwa tunajibu swali la muda. Walikuwa wamevunjika moyo kwa sabau matumaini yao yote kuhusiana na Masihi yalipotea Yesu alipokufa.
(6) Kwa namna gani?
Ni kwa nana gani maisha ya wanafunzi hawa yalibadilika baada ya kukutana (na Yesu)? Walirejea Yerusalemu kwa ujasiri kwamba Yesu amefufuka kutoka kwa wafu. Kama watu mamilioni baada ya hapo, maisha yao wamebadilika milele baada ya ufufuo.
Soma kifungu cha andiko au kitabu hicho mara nyingi
G. Campbell Morgan alikuwa mmoja wa wahubiri wakubwa sana wa karne ya 20. Morgan hakuwahi kuhudhuria chuo cha Biblia, lakini alikuwa mwalimu mwenye ufanisi wa Biblia. Kabla hajahubiri andiko, Morgan alisoma kitabu chote kilichokuwa na andiko alilolichagua angalau mara 40. Kupitia mchakato huu, Morgan alijifunza ni kwa namna gani kila mstari unakaa vizuri katika kitabu chote. Alijua dhana muhimu katika kitabu; aliuelewa ujumbe wa mwandishi. Kuna wakati Morgan alisema, “Kamwe Biblia haijiachi kwa mvivu.” Kujifunza Biblia ni kazi inayohitaji bidii.
Unaweza kujiuliza, “Ni kwa namna gani naweza kukisoma kitabu mara 40? Sitamaliza Biblia.” Inaweza kuwa sio ngumu kama unavyofikiria. Watu wazima wengi husoma maneno 200 kwa dakika moja; wanaweza kusoma maneno 12,000 kwa saa moja. Vitabu 44 vya Biblia vina chini ya maneno 12,000. Hii inajumuisha nyaraka za Paulo, nyaraka za watu wote, manabii wadogo, na vitabu vya Agano la Kale vya Ruthu, Ezra, Nehemia, Esta, na Danieli. Kwa saa moja kila siku, unaweza kusoma kitabu cha Waefeso, Wafilipi, Wakolosai, na Wathesalonike wa 1 na 2 mara 40 katika siku 40.
Kusoma kitabu chote kunaonesha namna kitabu kilivyopangwa. Hapo kabla tulisoma Matendo ya Mitume 1:8 ambapo wanafunzi walitumwa kuwa mashahidi Yerusalemu, Yudea, Samaria, na hata mwisho wa dunia. Unaposoma Matendo ya Mitume mara kwa mara, hii Inatoa kielelezo kwa ajili ya kitabu chote. Katika sehemu ya mwanzo ya Matendo ya Mitume, mateso yaliwachukua wanafunzi kutoka Yerusalemu hadi sehemu nyingine za Yudea; katika Matendo ya Mitume 8, Filipo anachukua Injili hadi Samaria; hadi mwisho wa Matendo ya Mitume, Paulo anahubiri Rumi, kutoka hapo Injili itakwenda hadi mwisho wa ulimwengu uliokuwa unajulikana.
Baadhi ya Dondoo za Kusoma kwa Kurudia Rudia.
1. Soma Biblia kwa sauti au sikiliza ikiwa inasomwa. Watu wanaoishi katika utamaduni wanaotegemea sana maandishi wanasahahu kwamba wakristo wengi wa kwanza walisikia Biblia ikisomwa. Kanisa la Efeso lilipopokea waraka wa Paulo, hawakutoa nakala kwa kila mwamini! Kiongozi angesoma waraka huo kwa waamini. Kupitia historia, watu wengi walipokea neno la Mungu kwa kusikia kuliko kusoma. Nyaraka za Paulo zilisomwa kanisani; manabii walizungumza jumbe zao. Kwa kusoma waraka kwa sauti au kwa kusikiliza kitabu kilichorekodiwa kwa sauti, utalisikia neno la Mungu likizungumzwa kama vile kanisa la kwanza walivyosikia maandiko.[3]
2. Soma Biblia katika tafsiri tofauti tofauti (Endapo kuna tafsiri Zaidi ya moja katika lugha yako). Baadhi ya tafsiri ni ngumu katika njia iliyotumika; nyingine zimelenga katika uelewa kwa urahisi. Kwa kusoma zaidi ya tafsiri moja, utapata uelewa zaidi wa ujumbe. Kama unafahamu zaidi ya lugha moja, inaweza kuwa ya msaada endapo utasoma maandiko katika lugha ya pili.[4]
3. Kila wakati unaposoma kuwa makini na vitu tofauti tofauti. Kwa mfano, mtu anaweza kusoma Mwanzo 3 mara moja kila siku kwa juma moja, kuiangalia habari katika mtazamo tofauti tofauti kila wakati:
Jumatatu: Soma Mwanzo 3 katika mtazamo wa Baba wa mbinguni. Baba anajisikiaje anapoona dhambi ya watoto wake?
Jumanne: Mstari muhimu katika sura hii ni upi?
Jumatano: Soma Mwanzo 3 katika mtazamo wa Shetani. Ni kwa namna gani anajaribu kuharibu mahusiano ya Mungu na watoto wake?
Alhamisi: Soma Mwanzo 3 ukiwa unaiangalia sadaka ya Yesu msalabani.
Ijumaa: Soma Mwanzo 3 katika mtazamo wa Adamu na Eva. Walijisikiaje walipokuwa wanapokea hukumu ya Mungu?
Jumamosi: Soma Mwanzo 3 katika mtazamo wa mtu ambaye anasoma Biblia kwa mara ya kwanza. Ni kwa namna gani habari hii ni muhimu ili kuelewa sehemu nyingine yote ya Biblia?
Machaguzi ya mpango yanapatikana katika www.bible.com ili kukusaidia wewe kusoma Biblia mwaka mzima. Mpango mwingine, unajikita katika Muundo wa G. Campbell Morgan, ni wa kusoma kitabu kimoja mara kadhaa katika mwezi mmoja. Kwa sababu vitabu 44 vya Biblia vinaweza kusomwa chini ya saa moja au ndani saa moja kila siku, unaweza kusoma kitabu chote mara 30 katika mwezi kwa saa moja kila siku. Wakati mchakato huu unaweza kuonekana ni wa polepole, kurudia rudia kusoma kitabu kutakupa uelewa wa Neno la Mungu. Kusoma kwa namna hii, unaweza kusoma Biblia yote mara 30 ndani ya miaka sita.[5]
Jifunze Sarufi
Mungu anawasiliana na sisi kwa njia nyingi, kuu ni kupitia neno lilioandikwa. Ni kweli hauhitaji kuwa mwana lugha ili kuelewa maandiko, lakini kwa kadiri unavyoelewa lugha iliyoandikwa, ndivyo utakavyopata ukweli wa Neno la Mungu kwa usahihi.
Kama mfano, tutajifunza sarufi ya moja kati ya mistari wa Paulo inayojulikana sana. “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana” (Warumi 12:1). Katika kuchunguza sarufi ya andiko, tunaangalia:
Vitenzi
Vitenzi vinawasilisha kitendo au hali ya kuwa. Kuna vitenzi viwili vinavyoonesha matendo katika Warumi 12:1:
Nawasihi inamaanisha “kuomba” au hata “kusihi.” Je, unaona uharaka wa ombi la Paulo? Hili si pendekezo la kawaida; kuna hisia nzito wakati Paulo anawasihi wasomaji wake wajitoe kikamilifu kwa Mungu.
Itoeni ni kitenzi kinachoonesha tendo. Inahitaji kuweka ahadi. Paulo anawataka wasomaji wake waitoe miili yao, wajitoe wao wenyewe kwa Mungu.
Majina
Katika Warumi 12:1, majina ambayo ni muhimu katika kujifunza kwetu yanajumuisha:
Ndugu. Pauo anawaandikia waamini. Hawaiti wenye dhambi kubadilika; anawaita waamini katika kujitoa kikamilifu.
Miili. Sehemu iliyobaki ya Warumi 12 inaonesha kwamba miili inawakilisha utu wetu kwa ujumla. Tunaweza tukalisema kwa namna nyingine kama hivi, “Jitoe utu wako wote.”
Huruma. Wito wa Paulo unamsingi katika huruma za Mungu. Katika kifungu kilichotangulia kabla ya mstari huu, Paulo amekuwa anauelezea wema wa Mungu unaoneshwa kwa watu, wote wawili Wayahudi na Wamataifa (Warumi 11:32).
Dhabihu. Chini ya sheria ya Musa, anayeabudu alileta mnyama kama sadaka. Katika Ufalme wa Kristo, tunaitwa kujitoa wenyewe kama sadaka inayoshi.
Vivumishi
Vivumishi na vielezi ni maneno ya ufafanuzi ambayo “hukuza maana ya maneno wanayoyavumisha na kuyaelezea.”[6] Katika Warumi 12:1, dhabihu inaelezewa kwa mfululizo wa maneno.
Dhabihu yetu ni hai. Hatutoi tena dhabihu mnyama aliyekufa; tunatoa maisha yetu kwa kujisalimisha kila siku.
Sadaka zetu lazima ziwe takatifu. Mwabudu wa Agano la Kale asingeweza kuleta sadaka ambayo ni kilema au hata isiyofaa; mwamini wa Agano Jipya hawezi kuleta sadaka ya maisha machafu, yasiyo na utii kama dhabihu.
Ni dhabihu iliyokamilika tu na iliyo tayari ndiyo ya kumpendeza Mungu.
Vishazi Vihusishi
Vihusishi ni maneno kama vile ndani, juu, kupitia, ndani ya, na kwa. Maneno haya madogo yanabeba maana kubwa. Katika Warumi 12:1, vishazi vihusishi viwili ni muhimu:
“Kwa huruma zake Mungu” Inatoa msingi wa kusihi kwa Paulo. Hapa si kama mwanajeshi anamlazimisha adui kujisalimisha; badala yake, ni mtoto kujisalimisha kwa furaha kwenye mapenzi ya baba yake anayependa.
Dhabihi zetu ni lazima ziwe za kukubalika “kwa Mungu.” Kwa mkristo, kukubalika na Mungu ni zawadi kuu sana.
Maneno Yanayounganisha
Maneno yanayounganisha na au lakini yana nguvu sana. Mwandishi mmoja analinganisha maneno yanayounganisha na udongo wa kujengea unaounganisha matofali pamoja.[7] Katika Matendo ya Mitume 1:8, tuliona kwamba lakini inarejelea nyuma katika kutoelewa kwa mitume.
Katika Warumi 12:1, Basi inarejelea nyuma katika kifungu kilichopita. Endapo utasoma kitabu chote cha Warumi, kwa haraka utaona kuna migawanyo mikubwa miwili:
Warumi 1-11 inafundisha mafundisho: hukumu ya dhambi, kuhesabiwa haki kwa imani, utakaso wa mwamini, kutukuzwa kama lengo kuu la Mungu kwa watoto wake, na kuchaguliwa kama njia ya Mungu kutimiliza kusudi hili.
Warumi 12-16 inaonesha matumizi ya kivitendo ya mafundisho haya. Kwa sababu tumekuwa sawa na Mungu, tunatakiwa kuishi kwa namna hii. Kwa sababu ya kile tunachokiamini (Warumi 1-11), hivi ndivyo tunatakiwa kufanya (Warumi 12-16). Mstari unaounganisha ni Warumi 12:1.
Basi ni kiashiria muhimu cha alama katika nyaraka nyingi za Paulo. Baada ya kuwakumbusha waamini wa Galatia kuhusiana na kweli kuhusu kuhesabiwa haki kwa imani pekee, Paulo anawaita kuiishi haki yao katika maisha yao ya kila siku; “Katika ungwana huo Kristo alituandika huru; kwa hiyo simameni” (Wagalatia 5:1). Baada ya kuwafundisha Waefeso kweli mkuu ya mafundisho ya kuchaguliwa kwao katika Kristo Yesu, Paulo anawaita wao kuishi maisha yanayostahili wito wao; “Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa” (Waefeso 4:1). Paulo aliwaambia Wakolosai kwamba wao walikuwa wamekufa na maisha yao yamefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Ni kwa namna gani wao wanatakiwa kuishi kama matokeo? “Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi” (Wakolosai 3:5).
Kutambua stadi ambazo waandishi wa Biblia wanazitumia kuonesha wazo kuu katika andiko kunaweza kuleta uelewa mpya katika kujifunza kwako. Taarifa za kina za kuziangalia ni pamoja na:
Maneno Yaliyorudiwa Rudiwa
Mwandishi anaporudia maneno mara kwa mara, inaonesha wazo muhimu. Katika hatua ya uchunguzi, hautaweza kwenda kwa kina sana kutafuta maana za maneno yaliyorudiwa rudiwa, lakini unaweza kuliwekea alama neno na kujiuliza, “Kwa nini neno hili limerudiwa rudiwa?”
► Soma vifungu vifuatavyo na wekea alama maneno yaliyorudiwa rudiwa:
2 Wakorintho 1:3-7. Ni mara ngapi neno faraja limerudiwa katika kifungu hiki? Mifano ya maswali ambayo unaweza kuyauliza wakati unapogundua kurudiwa rudiwa katika kifungu:
Je, neno faraja limetumika kwa namna ile ile kila wakati?
Ni vielezi vipi vimetumika? (faraja yote; faraja yetu; faraja yenu.)
Yohana 15:1-10. Ni mara ngapi neno kaeni nimerudiwa katika kifungu hiki? Mifano ya maswali ambayo unaweza kuyauliza wakati unapogundua kurudiwa rudiwa katika kifungu:
Ni masharti gani ya kukaa ndani yake?
Je, maonyo katika kifungu hiki yanaonesha kwamba inawezekana kwa mtu kutokaa ndani yake?
Ni nini matokeo ya kutokaa ndani yake?
Ni nini Baraka za kukaa nadani yake?
Ukinzani
Waandihi wengi wa Biblia walikinzanisha watu na mawazo. Unaliona neno lakini katikati ya mstari, linaweza kuwa linaunganisha mawazo mawili tofauti. Mithali nyingi zinatumia aina hii ya ukinzani.
Kuna namna mbili za kukabiliana na ukosoaji: “Jawabu la upole hugeuza hasira; Bali neno liumizalo huchochea ghadhabu” (Mithali 15:1).
Kuna namna mbili za kufanya maamuzi muhimu: “Pasipo mashauri taifa huanguka; Bali kwa wingi wa washauri huja wokovu” (Mithali 11:14).
Namna tunavyowatendea masikini inaonesha mitazamo yetu kuhusiana na Mungu: “Amwoneaye maskini humsuta Muumba wake; Bali yeye awahurumiaye wahitaji humheshimu” (Mithali 14:31).
Waandishi wa Agano Jipya pia wanatoa ukinzani. Paulo alitoa tofauti kati ya maisha yetu ya kale (giza) na maisha yetu mapya (nuru); “Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika Bwana…” (Waefeso 5:8).
Katika 1 Yohana 1:5-7, Yohana anatofautisha kati ya giza na nuru katika namna mbili:
Mungu ni Nuru na hamna giza ndani yake.
Endapo tunaushirika na Mungu, tutatembea nuruni, na si gizani.
“Kama siki menoni, na kama moshi machoni, Ndivyo alivyo mtu mvivu kwao wamtumao” (Mithali 10:26).
“Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika Bwana” (Mithali 25:25).
► Soma Yakobo 3:3-6. Ulimi unalinganishwa na mambo gani matatu? Unajifunza nini kutokana na ulinganifu huu?
► Kila mstari wa Mithali 26:8-11 unajumuisha neno kama. Kwa kila mstari, jifunze ulinganifu. Kwa mfano, kama unaangalia Mithali 26:8, unaweza ukajiambia mwenyewe: “Kama mfuko wa vito katika chungu ya mawe kadhalika mtu amheshimuye mpumbavu kwa sababu….” Ni mfanano gani unaouona katika ya mithali iliyozungumzwa na kumuheshimu mpumbavui?
Orodha
Unaposoma Biblia, unatakiwa kuonesha orodha na kujifunza hizo kwa ajili ya sifa muhimu.
► Kabla ya kuendelea na somo, chukua muda kusoma orodha ifuatayo:
Katika 1 Wakorintho 3:6, Paulo anaonesha kazi za huduma yake huko Korintho.
1 Yohana 2:16 inaorodhesha mambo ambayo yanatokea katika ulimwengu na si yanayotoka kwa Baba.
Wagalatia 5:19-21 inaorodhesha matendo ya mwili.
Wagalatia 5:22-23 inaorodhesha tunda la Roho Mtakatifu.
Tamko la Kusudi
Maneno kama kwamba, ili kwamba au kwa mara nyingi yanaelezea msukumo kwa ajili ya tendo au matokeo ya; kitendo. Chukua muda kufikiri mahusiano kati ya makusudi na matokeo; uliza ni kwa nini maandiko yanatupa maelekezo.
“Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka,” (kwa nini?) “mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa” (Yohana 15:16).
“kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu” (kwa nini Mungu alituchagua sisi?), “ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake” (Waefeso 1:4).
Wakati mwingine, tamko linaonesha ni kwa namna gani kusudi linatimizwa:
“Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako” (Zaburi 119:9).
Ni kwa namna gani tunaweza kupata uhakika wa maisha? “kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi” (Warumi 8:13).
Vishazi Masharti
Vishazi vinavyoanza na kama vinatoa sharti. Wakati mwingine msomaji wa Biblia anatarajia ahadi zitimilizwe pasipo kutimiza masharti; hata hivyo, ahadi yenye sharti inategemea kutimilizwa kwa masharti mahususi. Hii inaonekana mara kwa mara kupitia vishazi masharti.
Sharti: “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo,”
Matokeo: “amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya” (2 Wakorintho 5:17).
Sharti: “Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu,”
Matokeo: “nitalifanya” (Yohana 14:14).
Omba Unaposoma
Maelekezo haya ya mwisho yanaonekana ya kawaida, lakini ni muhimu. Mkristo kujifunza Biblia na maisha ya maombi hayatakiwi kutenganishwa. Kutenganisha kusoma Biblia na maombi ni kutenganisha nyanja mbili za maisha yetu ya kila siku ya mawasiliano na Mungu.
Yakobo anatuhakikishia sisi kwamba tunaweza kuomba msaada wa Mungu tunapopungukiwa hekima; “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa” (Yakobo 1:5). Hii ni ahadi ya ajabu sana tunapohitaji msaada wa Mungu ili kulielewa neno la Mungu.
Zaburi 119 inaonesha daraja au muunganiko kati ya maombi na andiko. Mzaburi anarudia rudia kumuomba Mungu kuongoza kujifunza kwake neno la Mungu. Katika namna hiyo hiyo, tunaweza kutafuta usaidizi wa Mungu tunapojifunza.
“Unifumbue macho yangu niyatazame Maajabu yatokayo katika sheria yako” (Zaburi 119:18).
“Unifahamishe njia ya mausia yako” (Zaburi 119:27).
“Ee BWANA, unifundishe njia ya amri zako” (Zaburi 119:33).
Watu wengi wamejifunza nguvu ya kugeuza maneno ya maandiko na kuwa maombi. Jaribu kugeuza vifungu hivi ili kuwa maombi binafsi:
Zaburi 23 – ombi kwa ajili ya uongozi wa Kimungu na ulinzi
Isaya 40:28-31 – ombi kwa ajili ya nguvu za Kimungu
Wafilipi 4:8-9 – ombi kwa ajili ya akili njema ya kimungu
[1]Hatua katika somo hili zinatoka katika Sura ya 8-17 ya Living by the Book, by Howard G. Hendricks na William D. Hendricks (Chicago: Moody Publishers, 2007). Unaweza kupata mazoezi ya nyongeza na maelezo kwa kusoma sura hizo.
[2]Tamaduni moja Inasema kwamba Luka ndiye aliyekuwa mtu ambaye hakutajwa, ambayo Inatoa maelezo kuhusiana na kiasi cha undani wa habari.
(1) Anza mchakato wa Uchunguzi kwa kujifunza mstari mmoja. Jiulize maswali mengi kwa kadiri unavyoweza kuhusiana na mstari.
(2) Hatua za kukuza nguvu zako za uchunguzi zinajumuisha:
Soma ili kupata uelewa.
Uliza maswali unaposoma.
Nani?
Nini?
Lini?
Wapi?
Kwa nini?
Kwa namna gani?
Soma kifungu cha andiko au kitabu hicho mara nyingi.
Jifunze sarufi. Angalia:
Vitenzi
Majina
Vivumishi
Vishazi Vihusishi
Maneno Yanayounganisha
Tafuta Taarifa Maalumu katika Andiko. Angalia:
Maneno yaliyorudiwa rudiwa
Ukinzani
Ulinganifu
Orodha
Tamko la kusudi
Vishazi Masharti
Omba unaposoma.
Somo la 2 Mazoezi
(1) Tengeneza orodha ya uchunguzi wa Yoshua 1:8. Andika mstari katika karatasi na kisha uanze kujiuliza maswali: “Nani? Nini? Lini? Wapi? Kwa nini? Kwa namna gani?” Kwa kutumia mfano uliopewa katika sehemu ya mwisho na mwongozo katika somo hili, fanya uchunguzi mwingi wa kina kwa kadiri utakavyoweza. Katika hatua hii, hautafsiri mstari au hauandai muhtasari wa ujumbe. Unaangalia tu taarifa za kina katika mstari.
(2) Kwa mazoezi zaidi, fuata mchakato ule ule kwa Mathayo 28:18-20.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.