Warren Wiersbe aliandika kuhusu uzoefu wake katika kanisa ambalo lilishindwa kuelewa ibada:
“Hakikisha unarudi kwa ibada ya jioni,” alisema kiongozi wa ibada, akiwa na sauti na tabasamu la mtangazaji wa mchezo wa runinga. "Tutakuwa na wakati mzuri wakufurahia.”
Wakati wa saa za mchana jumapili, nilijiuliza kauli hiyo ilimaanisha nini. “Tutakuwa na wakati mzuri wakufurahia” kauli hii inaeleweka katika mwaliko wa sherehe ya kuzaliwa, lakini inahusianaje na kikundi cha waamini Wa Kikristo waliokusanyika kumwabudu Bwana wa utukufu? Musa na watu wa Israeli hawakuwa na wakati wa kujifurahisha walipokusanyika kwenye Mlima Sinai….
Yohana alipitia mambo makuu yenye kustaajabisha akiwa katika Kisiwa cha Patmo, lakini si rahisi kusema kwamba alikuwa katika wakati wa furaha.[1]
Katika masomo haya, tumeona kwamba ibada ni zaidi ya wakati wa kufurahisha, zaidi ya ibada fulani, na zaidi ya shughuli ya Jumapili asubuhi. Kuabudu ni kumpa Mungu utukufu unaomstahili. Kwenye karatasi, hii ni rahisi; katika maisha halisi, inaweza kuwa changamoto. Katika somo hili, tutaangalia maswali yanayohusiana na ibada. Unapojifunza maswali haya, kumbuka kwamba swali kuu sio, "Ninapenda nini?" Swali kuu la kuabudu ni “Mungu anapenda nini? Ni nini kinachomletea heshima na utukufu?”
[1]Warren Wiersbe, Real Worship (Grand Rapids: Baker Books, 2000), 169-170
Ibada na Utamaduni
► Jadili mtindo wa Ibada wa kanisa lako. Ni vipengele vipi vya ibada yako vimeamriwa katika maandiko na ni vipengele vipi vinavyoamuliwa na utamaduni?
“Suala gumu zaidi kwa ibada katika nchi yangu ni umuhimu wa kitamaduni. Makanisa mengi yanaingiza mtindo wa ibada kutoka nje - iwe ni ya kisasa au ya kitamaduni. Watu wetu huchukua mtindo kutoka nchi za magharibi kwa sababu tu wanataka kuwa wa kisasa, lakini si ibada ya ‘kitamaduni’ wala ya ‘kisasa’ inayowagusa watu kwa sababu zote mbili ni za kigeni. Je, tunaabuduje kwa njia inayomheshimu Mungu na inayozungumza na ulimwengu ambao tunahudumu?”
Utamaduni au Biblia?
Bibi-arusi na bwana harusi walikuwa wanatoka tamaduni mbili tofauti sana. Katika sherehe ya harusi, vyakula vinavyotolewa hutoka katika utamaduni wa bibi arusi. Sahani moja ilipopitishwa, bwana harusi aliuliza, “Ni nini hicho?” Bibi-arusi akamwambia, "Katika nchi yangu, hii ni kitamu." Alijibu akiwa amekunja uso, "Katika nchi yangu, hii ni chukizo!" Tofauti za kitamaduni zinaweza kuwa changamoto.
Sisi sote tunasukumwa na utamaduni wetu. Sababu ya baadhi ya Wakristo kula na uma badala ya vijiti si kwa sababu uma ni wa kibiblia zaidi au wa ufanisi zaidi. Wanakula kwa uma kwa sababu walikulia katika utamaduni wa kutumia uma. Marafiki wao Wakristo katika sehemu nyinginezo za ulimwengu huona vijiti vya kulia kuwa muhimu zaidi kuliko uma.
Ibada yetu inaathiriwa na utamaduni wetu. Mambo mengi ya ibada yetu ni suala la utamaduni. Mtu ambaye alikulia katika kanisa lenye utamaduni wa Marekani anaweza kupenda sauti ya kinanda kanisani. Kuwa na kinanda kanisani sio kibiblia Zaidi kuliko gitaa; ni sehemu ya utamaduni.
Nchini Lesotho, kanisa linaimba kwa kuita na kuitikia kati ya kiongozi na waumini. Katika mtindo huu, kiongozi huimba sentensi na kisha waumini huimba sentensi inayofuata. Mtindo huo mzuri wa uimbaji huenda usisike kamwe katika kanisa la Marekani. Ikiwa muongozji wa muziki katika kanisa la Marekani angejaribu, waumini wangeweza kuchanganyikiwa. Uimbaji wa umoja wa kuita/kuitikia ni suala la kitamaduni, si kanuni ya kibiblia.
Kuna maswali matatu ambayo tunapaswa kuuliza tunapochunguza mtindo wa kuabudu:
1. Je, tunachanganya utamaduni na Maandiko?
2. Je, utamaduni wetu unapingana na Maandiko?
3. Je, ibada yetu inawezaje kuzungumza kwa ufanisi zaidi na watu katika utamaduni ambao Mungu ametuweka?
Je, tunachanganya utamaduni na Maandiko?
Swali hili ni muhimu tunapotathmini uzoefu wa ibada ambao ni tofauti na wetu wenyewe. Katika hali hii, lazima tuhakikishe hatuchanganyi utamaduni na Maandiko. Ni rahisi kwetu kusoma maadili yetu ya kitamaduni katika Maandiko na kisha kusisitiza kwamba kila mtu mwingine asome Biblia kwa njia hiyo hiyo. Tunaelekea kudhani kwamba njia yetu ni njia ya kibiblia.
Mtu anaweza kusema, “kinanda aina ya organi ni chombo sahihi cha muziki kanisani. Gitaa hazina nafasi katika ibada.” Hata hivyo, katika sehemu nyingi za dunia, kinanda cha organi hakitumiki, wakati gitaa linalobebeka ni muhimu sana katika uimbaji. Hakuna mtu anaweza kukataa kwamba makanisa ya nyumbani katika karne ya pili yalitumia vinanda vya bomba! Mtu anaweza kupenda vinanda vya bomba, lakini hawapaswi kuchanganya mapendeleo yao ya kitamaduni na kanuni za kibiblia.
Paul Bradshaw, mwanahistoria wa ibada, ameonyesha kwamba hata katika karne mbili za kwanza za kanisa, kulikuwa na aina mbalimbali za ibada. Kanisa lilipoenea, haikuonyesha kwamba ibada ilibaki vile vile katika kila mpangilio.[1]
Je, ni matokeo yanayofaa ya swali hili? Tunapotathimini mitindo ya kuabudu ya wengine au kuitikia mawazo mapya kutoka ndani ya makanisa yetu wenyewe, hatupaswi kuchanganya utamaduni na Maandiko. Hatupaswi kukataa wazo kwa sababu tu linapingana na matakwa yetu ya kitamaduni. Ikiwa desturi ya kuabudu haipingani na kanuni za kibiblia, basi tunapaswa kuwaruhusu wengine waabudu kwa jinsi wanavyopenda.
Hii haimaanishi kwamba kila mtindo wa ibada ni sahihi kwa kila kanisa. Kiongozi wa ibada mwenye busara ataongoza kwa mtindo ambao unafaa watu ambao yeye anawahudumu.
Kujipima
Je, kuna mazoea ya kuabudu ambayo umeyakataa kwa sababu ya upendeleo wako wa kitamaduni, na si kwa sababu ya kanuni za kibiblia? Ikiwa ndivyo, je, uko tayari kuruhusu waumini wengine kuwa na uhuru wa kuabudu kwa njia yao, mradi tu haikiuki Maandiko?
Je, utamaduni wetu unapingana na Maandiko?
Swali hili ni muhimu tunapojaribiwa kutetea desturi ya ibada kwa sababu tu ni ya kawaida katika utamaduni wetu. Ikiwa tunagundua kwamba kile ambacho ni cha kawaida katika utamaduni wetu kinapingana na Maandiko, ni lazima tutii Maandiko badala ya matarajio ya utamaduni wetu.
Wanamatengenezo walikabiliana na suala hili walipofanya mabadiliko makubwa sana kwenye ibada. Utamaduni wa zama za kati ulisema, “watu wa kawaida hawapaswi kusoma Biblia; hawawezi kuelewa.” Wycliffe, Huss, Luther, na Wanamatengenezo wengine walikuja kutambua kwamba Maandiko yalikuwa kwa ajili ya watu wote. Utamaduni wao wa zama za kati ulipingana na mafundisho ya Maandiko. Wanamatengenezo walihatarisha maisha yao ili kukabiliana na utamaduni wao na ukweli wa Maandiko.
Utamaduni ukipingana na Maandiko, ni lazima tuondoe utamaduni wetu! Neno la Mungu ndilo mamlaka yetu ya mwisho; hatuwezi kuhatarisha uaminifu kwa Maandiko ili kupatana na ulimwengu unaotuzunguka. Muhtasari wa Warumi 12:2 unasema, "Wala msiifuatishe namna ya dunia hii, bali mgeuzwe kwa kufanya upya nia zenu.”[2] Hatuwezi kuruhusu ulimwengu utusukume katika umbo lake.
Kujipima
Je, kuna maeneo ambayo ibada yako inapingana na kanuni za Maandiko?
Je, ibada yetu inawezaje kuzungumza kwa ufanisi zaidi na watu katika utamaduni ambao Mungu ametuweka?
Swali hili ni muhimu kwa ajili ya kuufikia ulimwengu wetu kwa injili. Ikiwa tunataka kugusa ulimwengu unaotuzunguka kwa injili, ibada yetu lazima izungumze katika lugha wanayoelewa.
Yohana Wesley alikabiliana na swali hili alipoanza kuhubiri nje. Kama vijana wenzake wa Kianglikana, mwanzoni Yohana aliamini kwamba kanisani ndio mahali pekee pazuri pa kuhubiri. Chini ya ushawishi wa George Whitefield, Yohana alianza kuelewa kwamba amri kuu ilimtaka ahubiri nje ya kanisa.[3] Yohana alilazimika kujiuliza, “Ninawezaje kuhubiri injili kwa ufanisi zaidi kwa wachimbaji migodi ya makaa ambao kamwe hawataingia kanisani isipokuwa kwa ajili ya harusi na mazishi?” Jibu lilikuwa kuhubiri nje.
Mnamo Aprili 2, 1739, Yohana alienda nje ya mji na kuhubiria watu wapatao 3,000 waliokusanyika uwanjani. Hii ilianzisha huduma ambayo ingebadilisha ulimwengu wa watu wanaozungumza Kiingereza wa karne ya 18.
Yohana alikuwa ameyapinga mahubiri ya nje kwa nguvu sana kiasi kwamba wakati fulani alisema, “ningefikiri kwamba kuokoa nafsi ni dhambi kama isingefayika kanisani.” Alipogundua kuwa chuki zake za kitamaduni zilikuwa kizuizi kwa injili, Yohana alikuwa tayari kubadilisha mazoea yake. Vijana wenzake wakianglikana walikataa badiliko hili. Ndani ya mwezi mmoja baada ya kuanza kuhubiri nje, askofu mmoja alimwambia Yohana kwamba hakubaliwi tena kuhubiri katika makanisa ya Kianglikana. Kuwa tayari kubadilisha utamaduni wako kunaweza kugharimu sana; ilimgharimu Yohana heshima ya wengi wa Waanglikana wenzake. Wito wa Yesu wa kuwa nuru na chumvi ni kipaumbele cha juu kuliko faragha wa kibinafsi.
Michael Cosper anapendekeza maswali matatu ya kuelewa uhusiano kati ya ibada yetu na utamaduni unaotuzunguka.[4]
(1) Nani yupo hapa?
Swali hili linatazama waamini wetu; “ni nani hushiriki ibada zetu?” mara nyingine tunakuwa na wasiwasi sana kuhusu kuwafikia watu ulimwenguni kiasi kwamba tunashindwa kuwahudumia waumini wa kanisa. Ibada yetu inakuwa si halisi tunapojaribu kuwa mtu ambaye sio. Kwa kuwa ibada inapaswa kuhudumia waumini, ni lazima tujiulize, “Ni nani yupo hapa? Mungu amemweka nani katika kanisa letu?”
(2) Nani alikuwa hapa?
Swali hili linaangalia urithi wetu. Kama waamini, tuna urithi unaorudi hadi kanisa la kwanza na kuenea kote ulimwenguni.
Hii ina maana kwamba tutafanya jitihada za kutambulisha nyimbo kuu za zamani kwa kizazi chetu. Ina maana kwamba tutawaunganisha watu leo na historia ya kanisa. Vijana Wakristo wanapaswa kufahamu kwamba wao ni sehemu ya urithi ambao ulianza muda mrefu kabla ya sisi kuzaliwa na utaendelea muda mrefu hata baada ya sisi kuondoka. Sisi ni sehemu ya kanisa zima linaloundwa na waumini kutoka vizazi vyote.
Urithi wetu wa ibada unarudi nyuma hadi Pentekoste, unarudi kwenye ufunuo wa Mungu kwa Musa katika Mlima Sinai, na hatimaye unarudi kwenye ufunuo wa Mungu kwa Adamu na Hawa katika bustani ya Edeni. Ibada yetu inapaswa kuadhimisha historia hiyo. Tunapoimba “Ngome Imara Ni Mungu Wetu,” tunajiunga na ibada ya Mageuzi. Tunapokariri Imani ya Mitume, tunajiunga na ibada ya karne ya pili. Katika ibada tunauliza, "Ni nani aliyekuwa hapa kabla yetu?"
(3) Nani anapaswa kuwa hapa?
Swali hili linaangalia jamii yetu. Tunapouliza, “Ni watu gani wanaopaswa kuwa sehemu ya kanisa letu,” tunauliza maswali kama vile:
Je, tunajaribu kumfikia nani kupitia injili?
Iwapo jamii yetu ingekuja kanisani, ibada yetu ingeonekanaje?[5]
Tunawezaje kuwa waaminifu kwa ujumbe wetu tunapoabudu kwa njia inayozungumza na watu tunaojaribu kuwafikia?
Maswali haya ni magumu katika maisha halisi kuliko kwenye karatasi! Angalia matukio manne. Kila kanisa limekabiliana na changamoto ya kuzungumza na jamii.
Kanisa A: Kanisa ambalo lilishindwa kuuliza, "Ni nani yuko hapa?"
Kanisa A liko katika jamii ya wastaafu. Umri wa wastani katika jamii ni miaka 70, na wastani wa umri katika kanisa ni miaka 70. Miaka miwili iliyopita, mchungaji wao aliamua kufikia familia za vijana. Katika kipindi cha miezi miwili, alibadilisha kinanda, kwaya, na nyimbo na gitaa, timu ya sifa, na skrini ya juu.
Kwa bahati mbaya, mchungaji alisahau kuuliza, “Ni nani yuko hapa?” Kwa sababu hiyo, kanisa la wazee 100 limeshuka hadi kuwa kanisa la wazee 35 wanaoimba muziki ambao hawapendi, kuangalia skrini ambayo hawapendi, na kunung'unika kuhusu gitaa kubwa.
Je, Kanisa A linapaswa kuwafikia watu nje? Kabisa! Lakini watu wanaoweza kuwafikia kwa ufanisi zaidi ni wazee wasio na kanisa katika jamii yao ya wastaafu. Kwa kuwapuuza watu ambao tayari wako kanisani, wanashindwa kuabudu kwa njia inayozungumza na kanisa lenyewe au na jamii inayowazunguka. Kanisa A lilishindwa kuuliza, “Ni nani yupo hapa?”
Kanisa B: Kanisa ambalo lilishindwa kuuliza, “Nani alikuwa hapa?”
Kanisa B lipoo katika mji unakuwa kwa kasi wenye familia nyingi za vijana. Kanisa hilo linazungumza lugha ya jamii yao; ibada yao ni ya kusisimua na yenye shauku.
Kanisa B lina shauku ya uinjilisti. Kwa bahati mbaya, kanisa hilo halijauliza, "Ni Nani alikuwepo hapa?" Kanisa B limesahau urithi wake kama kanisa lililohubiri ujumbe wa moyo safi na maisha ya Kikristo ya ushindi. Mchungaji anaepuka kuhubiri mafundisho kwa sababu anafikiri, “Watu hawataki kusikia mafundisho; wanataka mahubiri ya vitendo.” Kiongozi wa sifa na muziki anaepuka nyimbo zenye kina kibiblia kwa sababu anafikiri, “Watu hawapendi nyimbo zenye maneno magumu; wanapenda nyimbo rahisi.” Kwa hiyo, kanisa limelea kizazi cha “wapagani waliobatizwa.”[6]
Kanisa B linaongezeka kwa idadi, lakini wahirika wachache wanakua katika utauwa. Watu wengi huhudhuria kwa sababu ni kanisa la kuburudisha ambalo linahitaji kujitolea kidogo. Kwa sababu Kanisa B halijui urithi wake, waongofu wengi hivi karibuni wanageukia makanisa mengine ambayo hutoa burudani bora zaidi. Kanisa B lilishindwa kuuliza, “Nani alikuwa hapa?”
Kanisa C: Kanisa ambalo lilishindwa kuuliza, “Nani anapaswa kuwa hapa?”
Kanisa C lilianzishwa karibu miaka 100 iliyopita katika jamii ndogo ya vijijini. Ibada, mahubiri, na muziki viliwasiliana na watu walioishi katika mji huo. Katika miaka ya kati, jamii imebadilika kabisa. Kanisa C sasa limezungukwa na jiji la ndani, lakini ibada yake bado imeundwa kuvutia watu wa tabaka la kati la vijijini.
Cha kusikitisha ni kwamba, watu wengi wanaoishi karibu na Kanisa C hulipita kanisa kila wiki bila kujua kwamba kanisa lina majibu ya njaa yao kuu. Kanisa C lina ujumbe ambao jamii yake inahitaji, lakini haliwasiliani kwa uwazi na jamii. Kama Kanisa C lingeweza kuabudu kwa njia inayowasiliana na Mungu na kwa ulimwengu wenye mahitaji, lingeweza kubadilisha jamii yake. Badala yake, Kanisa C linakufa kwa sababu lilishindwa kuuliza, “Ni nani anayepaswa kuwa hapa?”
Kanisa D: Kanisa linalozungumza na jamii
Kanisa D limeweza kuwa na sifa nyingi za makanisa matatu yaliyotangulia. jamii imebadilika sana tangu kanisa lilipoanzishwa miaka 40 iliyopita. Tofauti na makanisa mengine katika utafiti huu, Kanisa D limejifunza kuwasiliana vyema na jamii yake.
Watendakazi wa wachungaji walipogundua kuwa waongofu wengi wachanga hawaelewi mafundisho yanaliyohubiriwa siku ya Jumapili, walianzisha vikundi vya ufuasi ili kuwaleta waumini wapya kwenye ukomavu. Kiongozi wa muziki alipogundua kuwa muziki huo hauzungumzi na watu wengi katika jamii yao, alianza kujumuisha nyimbo ambazo ni za kweli kimafundisho na zenye kuvutia kimuziki.
Kanisa lilipokua, walipanda makanisa katika miji jirani na kuruhusu makanisa haya kuendana na mahitaji ya jamii zao. Makanisa haya yanachungwa na vijana waliokuwa sehemu ya Kanisa D. Kila kanisa ni tofauti, lakini kila kanisa lina uaminifu kwa injili. Kanisa D linasitawi kwa sababu lilijifunza kuuliza “Ni nani aliye hapa, nani alikuwa hapa, na ni nani anayepaswa kuwa hapa?” limejifunza kusema ukweli wa Biblia kwa jamii ambayo Mungu aliliweka ndani yake.
Kujipima
Je, ibada yako inazungumza na watu wanaohudhuria kanisa lako? Je, ibada yako inaakisi urithi wa kanisa la Kikristo? Je, ibada yako inazungumza na wale ambao Mungu anataka kuwafikia kupitia kanisa lako?
Vipi kuhusu Muziki?
Wanamuziki wa makanisa katika sehemu nyingi za dunia wanakabiliwa na changamoto ya kupata nyimbo zinazofaa kibiblia na zinazozingatia utamaduni. Tunatafuta muziki unaozungumza lugha ya moyoni kwa jamii tunayotaka kufikia. Muziki wa kigeni unaweza usiwe na umuhimu wa kitamaduni, na baadhi ya nyimbo za kitamaduni zinaweza zisiwe za kibiblia. Je, tunachaguaje muziki ambao utaendana na Maandiko na unaozingatia utamaduni ambao tunachunga? Hapa kuna majibu kutoka kwa wachungaji ambao wanakabiliwa na suala hili:
Linapokuja suala la kuchagua nyimbo za kanisa, mtu hahitaji kuchagua kati ya kuwa mwaminifu kulingana na biblia na kuwa mwangalifu kiutamaduni. Kwa kuwa "mwaminifu kulingana naa biblia" natafuta nyimbo ambazo ni za kweli na zilizo wazi. Kwa kuwa "mwangalifu kiutamaduni" ninatafuta nyimbo ambazo ni rahisi kuimba na kushirikisha kanisa.
Uaminifu wa Kibiblia unachukua kipaumbele, lakini hatuhitaji kuchagua kati yao. Ikiwa lengo la kuimba ni mawasiliano, je, si ni vema kuchagua lugha ya muziki inayolingana na utamaduni [mazingira] ya kanisa letu? Tungekuwa wapumbavu tukifikiri kwamba hisia za kitamaduni hazifai, na hatutakuwa na maana ikiwa nyimbo zetu si za kweli au zisizo wazi.
(Murray Campbell, mchungaji huko Melbourne, Australia)
Katika mafunzo ya wachungaji wa Kiafrika, tunawahimiza watafute nyimbo zilizojaa zaidi maandiko, zinazomlenga Mungu, zinazoongozwa na injili, zinazojenga, na za kuimba ambazo wanaweza kupata, za zamani na mpya, na kuziachia! Katika utamaduni wowote, watu wa Mungu wanahitaji nyimbo ambazo zitawafundisha kuishi na kufa kwa ajili ya Kristo.
(Tim Cantrell, mwalimu huko Johannesburg, Afrika Kusini)
Msururu wa nyimbo thabiti za kitheolojia, zinazofaa kimuktadha katika jamii ya Kihindi ni ndogo sana. Nyimbo nyingi ambazo zina theolojia nzuri zimetafsiriwa kutoka kwenye nyimbo za zamani za Magharibi au nyimbo za kuabudu za kisasa. Ingawa maneno yanaweza kuwa ya uaminifu, muziki huo si wa kiasili, na wenyeji wanaona ni vigumu kuuimba. Pia, nyimbo kama hizo zinathibitisha tu tuhuma za watu kwamba Ukristo ni dini ya Magharibi.
Kwa upande mwingine, nyimbo za Kihindi ambazo zina muktadha wa muziki mara nyingi hazina uzito wa teolojia, zinajirudiarudia, na hazina Maandiko. Mara nyingine nyimbo hutumia tuni zinazotumiwa katika mahekalu. Tunaepuka aina zote hizi za nyimbo.
Jambo la kwanza ninaloangalia wakati wa kuchagua nyimbo ni utimilifu wake wa mafundisho. Ikiwa wimbo hauna msingi thabiti wa kitheolojia, hatutauimba, licha ya muktadha wake. Ikiwa maneno ni mazuri lakini wimbo sio wa Kihindi, hatutauimba. Tunachagua nyimbo zenye tuni za Kihindi na maneno ya uaminifu. Kwa kweli, hakuna nyimbo nyingi ambazo ziko katika kitengo hiki, lakini tunaunda mtindo wetu polepole.
(Harshit Singh, Mchungaji huko Lucknow, India)
Kama vile kuna lugha ya moyo ya maongezi ambayo mtu huzungumza kwa kawaida zaidi na anahisi kwa undani zaidi, kuna lugha ya muziki ya moyo ambayo inazungumza na mtu kwa undani zaidi.
Fikiria kuhusu mmishonari anayeshindwa kujifunza lugha ya watu anakohudumu. Anaweza kusema (kwa lugha yake mwenyewe), “Niko hapa kuwaletea injili. Huwezi kuelewa ninachosema, lakini endelea kunisikiliza. Hatimaye, mtaelewa ninachosema, nanyi mtajua habari njema.” Bila shaka hapana hautaweza kujua habari jema! Vivyo hivyo, tunapokosa kutumia lugha ya kimuziki wa utamaduni fulani, tunafanya habari njema kuwa ngumu zaidi kueleweka.[7]
Kwa kusikitisha, kama Mchungaji Singh alivyoandika, katika baadhi ya tamaduni kuna nyimbo chache zenye msingi wa kibiblia zinazotumia lugha ya muziki isiyo ya Magharibi. Hii mara nyingi huwaacha makanisa yakiwa na chaguo mbili: nyimbo zenye nguvu za kibiblia zenye tuni zinazosikika kigeni au nyimbo zenye udhaifu wa kibiblia zenye tuni zinazolingana na muktadha wa muziki. Ikiwa tunataka kutumia muziki kujenga kanisa kote ulimwenguni, tunapaswa kutafuta muziki ambao ni wa kweli kwa Maandiko na ambao unazungumza katika lugha ya muziki ya moyo ya watu. Ninaamini kwamba Mungu anataka kuwaita waandishi wa nyimbo wacha Mungu katika kila utamaduni.
Ikiwa unahudumu katika utamaduni ambapo kuna nyimbo chache za ibada zenye ubora, unaweza kuhamasisha muziki mpya. Hili linaweza kuhitaji ushirikiano kati ya watu wawili; mtu wa kuandika au kutafsiri maandishi bora na mtu wa kuandika muziki. Waandishi wachache wakubwa wa nyimbo waliandika nyimbo zao wenyewe. Tafuta mwanamuziki wa Kikristo aliyejitolea na uwafanye waandike tuni za nyimbo zinazozungumza ukweli wa kibiblia. Kwa kufanya hivi, unaweza kuimba ujumbe wa kibiblia katika lugha ya muziki inayowasiliana na ulimwengu wako.
Ni lazima kila wakati tufikirie Swali la 2 hapo juu: “Je, utamaduni wetu unapingana na Maandiko?” Ikiwa utamaduni wa muziki unapingana na Maandiko, hatupaswi kuutumia. Hata hivyo, wakati hakuna kanuni ya kibiblia inayohusika, tunapaswa kutafuta kuongoza ibada katika lugha ya muziki ya waabudu.
Alipokuwa akiabudu katika kanisa la baba yake, kijana mmoja aliyejitayarisha kwa ajili ya huduma alitambua kwamba watu wachache walielewa nyimbo walizokuwa wakiimba. Badala ya kuabudu, walionyesha uelewa mdogo wa kweli walizokuwa wakiimba. Kijana huyo alipolalamika kuhusu jambo hilo, baba yake alijibu, “Ona kama unaweza kufanya vyema zaidi.” Kijana Isaac Watts alikubali changamoto ya baba yake.
Watu wanaozungumza Kiingereza wanaimba nyimbo za Isaac Watts leo kwa sababu mchungaji kijana aliazimia kuandika nyimbo zinazowasilisha ujumbe wa Biblia katika lugha ambayo watu wanaelewa.[8] Katika kizazi chetu, tunahitaji waandishi wa nyimbo ambazo zinazungumza ukweli wa kibiblia katika lugha inayogusa mioyo ya ulimwengu wa wasiozungumza kiingereza.
[1]Paul Bradshaw, “The Search for the Origins of Christian Worship” in Robert Webber, Twenty Centuries of Christian Worship (Nashville: Star Song Publishing, 1994), 4
[2]E. H. Peterson, The Message (Colorado Springs: NavPress, 2002)
[3]Hii inaelekeza kwa Swali la 2 - "Je, utamaduni wetu unapingana na maandiko?"
[4]Michael Cosper, Rhythms of Grace: How the Church’s Worship Tells the Story of the Gospel (Wheaton: Crossway Books, 2013), 176-179
[5]John Wesley alikabili suala hili. Waanglikana walitambua kwamba ibada iliyohudhuriwa na wachimba migodi ya makaa ya mawe, makahaba waongofu na wenye maduka wasiojua kusoma na kuandika ingekuwa tofauti sana na ibada rasmi ya Waanglikana wa tabaka la juu. Mapadre wengi waliamua kuwa hawakuwa tayari kuruhusu ibada yao kuingiliwa na tabaka za chini. Hii ilisababisha kuundwa kwa jamii za Methodist.
[6]Neno la Mark Dever kwa wanaojiita Wakristo ambao hawana msingi wa kibiblia.
[7]Mfano huu umechukuliwa kutoka kwa Ronald Allen na Gordon Borror, Worship: Rediscovering the Missing Jewel (Colorado Springs: Multnomah Publishers, 1982), 168.
[8]“Furaha kwa Ulimwengu,” “Ninapochunguza Msalaba wa Ajabu,” na “Ee Mungu, Msaada Wetu Katika Zama Zilizopita” ni nyimbo tatu kati ya 750 zilizoandikwa na Isaac Watts.
Baadhi ya Mawazo Ya Kufunga Kuhusu Mtindo wa Muziki
Kwakuwa muziki ni sehemu muhimu katika maisha, wengi wetu tuna Imani kubwa kuhusu muziki. Majadaliano yoyote kuhusu mtindo wa muziki katika ibada yanaweza kupelekea migogoro.
Wale wanaoamini kwamba mtindo fulani wa muziki haufai husema, “mtindo fulani pekee wa muziki unaweza kutumika katika ibada.” Ingawa, Maandiko hayajatoa mwongozo maalumu kuhusu mtindo wa muziki.
Wale wanaoamini kwamba mitindo ya muziki haifungamani na upande wowote wa kimaadili husema, “Tafuta muziki ambao watu wanapenda na uuimbe. Mtindo haujalishi; imba unachopenda.” Hata hivyo, Maandiko yanaweka wazi kwamba ni lazima tuepuke chochote kinachotupeleka kwenye tabia ya kimwili. Kwa sababu ya maana fulani ya kitamaduni na kihisia, muziki fulani haufai kwa ibada.
Akiandika kuhusu uchaguzi wa muziki, Scott Aniol aligawanya mjadala wake katika sehemu mbili:[1]
1. Maandishi: suala sahihi na lisilo sahihi. Bila kujali mtindo wa muziki, ikiwa maneno hayazungumzi ukweli waziwazi haufai kwa ibada. Hili ni suala la sahihi na lisilo sahihi. Kuna nyimbo nyingi zinazotumia mitindo ya muziki wa kitamaduni ambazo zina maneno ambayo hayafundishi ukweli wa kibiblia; haya hayafai kwa ibada. Kuna nyimbo nyingi zinazotumia mitindo ya kisasa ya muziki ambayo ina maneno ambayo hayafundishi ukweli wa Biblia; haya hayafai kwa ibada.
2. Mtindo wa muziki: suala lisilo wazi. Kwa kuwa Maandiko hayasemi waziwazi kuhusu mtindo wa muziki, tunapaswa kufuata kanuni za Warumi 14. Tunapaswa kuepuka muziki unaotiliwa shaka kwa sababu ya muingiliano wake wa kitamaduni. Hata hivyo, hatupaswi kuwahukumu wengine ambao dhamiri yao inawaongoza katika mwelekeo tofauti wa muziki.
Kujipima
Je, kuna maeneo ya kitamaduni katika ibada yako ambayo yanapunguza uwezo wako wa kufikia ulimwengu wako kwa injili? Je, uko tayari kusalimisha mapendeleo yako kwa ajili ya kuufikia ulimwengu wako na injili?
Vipi kuhusu Kupiga makofi?
Vipi kuhusu kupiga makofi ibadani? Je, ni sahihi au sio sahihi? Kupiga makofi hutokea katika miktadha miwili, ikiwa na maana mbili tofauti kabisa.
Kupiga makofi kama sehemu ya ibada
Makanisa mengi hupiga makofi kama sehemu ya kuimba; kupiga makofi ni sehemu ya ibada ya kanisa. Hii ni sehemu ya kipengele cha kimwili cha ibada kinachoelezwa katika Maandiko. “Enyi watu wote, pigeni makofi, Mpigieni Mungu kelele kwa Sauti ya shangwe!” (Zaburi 47:1) waabudu wa kiyahudi walikuwa wenye shauku. Ibada ya kiyahudi ilijumuisha aina mbalimbali za vifaa vya muziki, kuinua mikono, na kupiga makofi.
Ikiwa kupiga makofi ni sehemu ya ibada yako, kiongozi wa ibada lazima ahakikishe kwamba inafaa kwa wimbo unaoimbwa. Kupiga makofi wakati wa wimbo wa maombi hakuleti ujumbe. Kupiga makofi wakati wa wimbo wa sifa za shangwe kunafaa. Swali kwa kiongozi sio kila wakati, "Je, kupiga makofi ni sawa au sio sawa?" Swali bora zaidi linaweza kuwa, “Je, kupiga makofi kunafaa kwa wimbo huu na katika hatua hii ya ibada yetu?”
Makofi kwa kuitikia ibada
Suala gumu zaidi ni kupiga makofi kwa kuitikia wimbo maalum. Hakuna kiashiria katika Maandiko kwamba waabudu Wayahudi au Wakristo walipiga makofi katika kuitikia ibada.
Baadhi ya tamaduni leo ni wepesi wa kupongeza kama kuonyesha shukrani. Katika tamaduni hizi, ni kawaida kutoa sifa kwa Mungu kwa kupiga makofi. Tamaduni nyingine kupiga makofi kunahusiana hasa na kuthamini utendaji mzuri. Katika tamaduni hizi, kupiga makofi kwa mwitikio wa kwaya au mwanamuziki kunaweza kuunda mazingira ya tamasha, badala ya ibada.
Kwa kuwa Maandiko hayazungumzii suala hili moja kwa moja, tunapaswa kuepuka kauli kamilifu. Ikiwa makofi ni itikio la kawaida la shangwe linalomsifu Mungu, huenda likawa tendo la ibada. Makofi yakitangazwa, “Mtu huyu amefanya vyema kwa ajili ya kufurahia kwetu,” huenda ikapunguza ibada.
Kanisa na mwanamuziki wanapaswa kuangalia msukumo wa kupiga makofi. Watu katika ibada wanapaswa kujiuliza, “Kwa nini ninapiga makofi? Je, makofi yangu yanachochewa na sifa kwa Mungu, au makofi yangu yanachochewa na sifa kwa mwimbaji?”
Mwanamuziki anapaswa kuuliza, “Kwa nini waumini wanapiga makofi? Je, wimbo wangu ulichochea tendo la shangwe la kumsifu Mungu, au wimbo wangu ulivuta fikira zao kwenye ustadi wangu wa kuimba? Je, niliongoza katika kuabudu?” Kama viongozi wa ibada tunapaswa kuwa waangalifu kwamba huduma yetu iwe inamuelekea Mungu, na si kwa uwezo wetu.
Kujipima
Ikiwa kanisa lako linapiga makofi wakati wa ibada, je, kweli kwamba makofi hayo huelezea sifa kwa Mungu au ni huelezea sifa kwa mwimbaji?
Warumi 14 na Mitindo ya Kuabudu
► Soma Warumi 14:1-23.
Warumi 14 inatoa miongozo muhimu kwa mambo yenye kutiliwa shaka ambayo Maandiko hayasemi waziwazi. Paulo anahutubia wale ambao hawakubaliani kuhusu kula nyama au kuadhimisha siku maalum. Anatoa kanuni zifuatazo.
(1) Usiwahukumu wengine kuhusu mambo yenye kutiliwa shaka (Warumi 14:1-13).
Katika maeneo ambayo Maandiko hayasemi waziwazi, ni lazima turuhusu uhuru wa dhamiri kwa wale ambao hawakubaliani nasi. Hatupaswi kuwa dhahiri zaidi kuliko Maandiko yenyewe!
Paulo alitambua kwamba mwamini ambaye hajakomaa anaweza kudhuriwa na uhuru unaotumiwa na mwamini aliyekomaa zaidi. Katika hali hiyo, sheria ya upendo inatutaka tuweke kikomo uhuru wetu kwa niaba ya wanyonge. Usimwangamize yeye ambaye Kristo alikufa kwa ajili ya uhuru wako.
Kauli ya Paulo ni kielelezo chenye nguvu kwa maeneo yote ya tabia ya Kikristo; “Kwa hiyo, chakula kikimkwaza ndugu yangu, hakika sitakula nyama hata milele, nisije nikamkwaza ndugu yangu” (1 Wakorintho 8:13).
(3) Tenda kwa imani, na sio mashaka (Warumi 14:23).
Hii ni kanuni muhimu kwa vijana Wakristo. "Kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambi." Hatupaswi kamwe kukiuka dhamiri yetu ili kumpendeza mtu mwingine. "Aliye na shaka, kama akila, amehukumiwa kuwa ana hatia, kwa maana hakula kwa Imani."
Zinapotumika kwenye mitindo ya kuabudu, kanuni hizi hutuonya:
1. Usiwahukumu wale wanaotumia mtindo ambao wewe hujapendezwa nao. Ikiwa Maandiko hayasemi kwa uwazi, lazima usiwe mwepesi kuhukumu.
2. Usitumie muziki ambao unaweza kumuudhi mwamini mpya. Ikiwa mwamini anatoka katika mtindo wa maisha ambamo mitindo fulani ya muziki inahusishwa na mwenendo mpotovu, mtindo huo hauwezi kamwe kuwa wa manufaa kwa mwamini huyo. Upendo kwa ndugu Mkristo unapaswa kukuchochea uepuke jambo lolote linaloweza kuzuia ukuzi wake wa kiroho.
3. Usitumie uhuru wakati dhamiri yako ina mashaka. Haupaswi kujaribu mistari. Kumpenda Mungu kunapaswa kukuchochea uepuke jambo lolote linaloleta shaka katika dhamiri yako mwenyewe.
[1]Scott Aniol, Worship in Song (Winona Lake, IN: BMH Books, 2009), 135-140
Kuwashirikisha Watoto na Vijana katika Ibada.
“Tunawezaje kuwashirikisha watoto na vijana katika ibada? Je, tuwaweke katika ibada tofauti hadi wawe na umri wa kutosha kuelewa ibada ya watu wazima? Je, tunawahimizaje watoto na vijana kuabudu kweli?”
Makanisa mengi hutenganisha watoto, vijana, na watu wazima katika ibada. Kuna sababu mbili za hili: wasiwasi kwamba watoto wadogo watasumbua watu wazima kwenye ibada na wasiwasi kwamba watoto na vijana hawataelewa kile kinachotokea katika huduma ya ibada.
Hakuna kitu katika Maandiko kinachokataza ibada za tofauti kwa vijana na watoto. Hata hivyo, kuna angalau mambo matatu ambayo yanapaswa kuzingatiwa:
1. Katika Maandiko, ibada ilikuwa ya vizazi. Maandiko hayapendekezi kwamba watoto na vijana walitendewa tofauti katika ibada. Katika ibada ya Hekaluni, familia ilibaki pamoja kwa ajili ya ibada ya dhabihu. Hakuna mahali katika Agano Jipya panapopendekeza kwamba kanisa la kwanza lilitenganisha watoto au vijana wakati wa ibada.
2. Ibada kati ya vizazi mbalimbali inaunganisha Mwili wa Kristo. Kama vile kutoa huduma tofauti katika ibada ya kisasa na ibada ya kitamaduni kunaweza kudhoofisha umoja wa Mwili, vivyo hivyo kutoa huduma tofauti kwa watoto na vijana kunaweza kupunguza ufahamu wao wa kuwa sehemu ya familia ya kanisa. Kwa upande mwingine, watoto na vijana wanapojumuishwa katika ibada ya familia ya kanisa, kila mtu anaelewa kwamba wao ni sehemu ya thamani ya Mwili wa Kristo (1 Timotheo 4:12).
3. Kupitia ibada ya vizazi, imani hupitishwa kwa kizazi kijacho. Tunajifunza kuabudu kwa kuabudu. Isipokuwa imepangwa kwa uangalifu, ibada ya watoto inaweza kuwa ni wakati wa kuburudisha watoto ili wasiingiliane na ibada ya watu wazima. Tukifanya hivi, ni lini watoto watajifunza kuabudu?
Vijana na Watoto kama Sehemu ya Huduma ya Ibada ya Pamoja
Vijana na watoto mara nyingi wanaweza kushiriki katika ibada ya pamoja inayozungumza na kila kizazi. Hii inaweza kuhusisha mahubiri mafupi ya watoto juu ya mada sawa na mahubiri makuu.
Tunapodhani kwamba watoto hawawezi kuelewa ukweli wa kina, tunashindwa kuwapa sifa za kutosha kuhusu kupambanua kiroho. Ni Roho Mtakatifu ambaye huangazia nuru yake kwa kila msikilizaji, mtu mzima au mtoto (1 Wakorintho 2:10). Hata katika ibada ya watu wazima, Roho Mtakatifu anaweza kusema ukweli kwa mioyo yao michanga. Kujumuisha watoto katika ibada ya watu wazima inatuhitaji kuwafundisha kuhusu ibada. Tunaweza kuelezea ibada kwa watoto. Tunaweza kufafanua maneno magumu katika usomaji wa Maandiko na nyimbo. Hata watu wazima wakati mwingine wanahitaji maneno hayo kufafanuliwa! Kwa kuwapa watoto nafasi katika ibada, tunawaruhusu wakue kama waabudu pamoja na mwili wote.
Makanisa mengi hutoa ibada tofauti kwa vijana na watoto. Ibada hizi zinapaswa kuwa ibada, sio burudani. Ikiwa watoto na vijana hawatajifunza kuabudu, hawatakua na kufikia ukomavu wa kiroho. Kama vile mtoto hasitawishi afya ya kimwili kwa kula peremende, mtoto hatasitawisha afya ya kiroho kwa kula vyakula visivyofaa vya kiroho.
Ikiwa kanisa linatoa ibada tofauti za watu wazima na vijana/watoto, lazima tuhakikishe kwamba ibada hiyo ni ibada ya kweli. Ibada ya vijana na watoto inapaswa kujumuisha usomaji wa Maandiko. Kwa watoto, vielelezo vya kuvutia vinaweza kuimarisha ukweli wa Maandiko.
Ibada inapaswa kujumuisha mahubiri au somo la Biblia linalotumia Neno la Mungu kwa mahitaji ya vijana na watoto. Biblia yenyewe inapaswa kushikwa kwa upendo mikononi mwa mwalimu. Watoto na vijana hujifunza kuheshimu na kutumia Neno la Mungu kwa kulitazama likitumiwa na watu wazima wanaowaheshimu.
Ibada inapaswa kujumuisha nyimbo zinazozungumza ukweli wa kibiblia. Inapaswa kujumuisha muda wa maombezi, sifa na maombi. Inapaswa kujumuisha sadaka inayoruhusu watoto kuleta zawadi zao kwa Mungu. Vipengele vyote vya ibada vinapaswa kujumuishwa katika ibada ya watoto au vijana.
Kufundisha Watoto Kuomba: “Mkono wa Maombi”
Kidole gumba kinatukumbusha kuwaombea walio karibu nasi (familia).
Kidole cha kuashiria kinatukumbusha kuwaombea wale wanaoelekeza watu kwa Yesu (wachungaji, waalimu, na wamisionari).
Kidole cha kati ndicho kirefu zaidi. Hii inatukumbusha kuwaombea viongozi wa nchi, shule, kanisa na nyumba zetu.
Kidole cha nne ni dhaifu zaidi. Onyesha hili kwa kujaribu kuinua kidole cha nne pekee. Hii inatukumbusha kuwaombea wale walio dhaifu na wanaomhitaji Yesu.
Kidole cha tano ni kidogo zaidi. Hii inakukumbusha kujiombea mwenyewe.
Kuinua mkono mzima kunatukumbusha kumsifu Mungu.
Mkono huu wa maombi unaweza kuwa muundo wa maombi unaoinua kiwango cha maombi cha waabudu wachanga.
Muhtasari
Ikiwa tunataka kuona watoto wetu wakikua na kuwa waumini waliokomaa, ni lazima tuwaandalie chakula cha kiroho. Iwe katika ibada ya umoja au katika ibada tofauti, ni lazima tuwaongoze watoto wetu kwenye ibada.
Kujipima
Iwe una ibada tofauti kwa watoto na vijana au ibada ya umoja kwa kanisa zima, je unawafundisha watoto wako na vijana kuabudu?
[1]Sehemu hii inatumia nyenzo kutoka kwa Bi. Christina Black, Profesa wa Elimu katika Hobe Sound Bible College
Hisia Katika Ibada
“Watu katika nchi yetu wana hisia nyingi sana, na ibada yetu mara nyingi huonyesha maisha yetu ya kihisia moyoni. Muziki wetu wa kuabudu kwa kawaida huwa wa haraka, wenye sauti kubwa na wenye mdundo. Inaturuhusu kushiriki na kueleza hisia. Hata hivyo, ninaogopa kuwa muziki ni hisia tu. Sijui ikiwa muziki wetu unachangia ibada ya kweli.”
Ibada ya kweli ni kuabudu katika roho na kweli. Ibada ya kweli inahusisha hisia, lakini ni zaidi ya hisia. Kuna makosa mawili yanayohusiana na hisia katika ibada ambayo yanaweza kutupoteza.
Baadhi ya waabudu hukana hisia katika ibada. Wanaona kuabudu kuwa ni kukutana na Mungu kiakili; wanashindwa kutambua kipengele cha hisia cha kukutana na Mungu. Ibada ya kweli inazungumza na hisia. Huduma yetu ya kuabudu inapaswa kuwapa waabudu fursa ya kueleza mwitikio wao wa kihisia kwa ufunuo wa Mungu juu yake mwenyewe.
(2) Kosa la kusisitiza zaidi hisia katika ibada.
Hatari iliyo kinyume ni kosa la kuzungumza tu na hisia katika ibada. Ibada inayozungumza na hisia huku ikipuuza akili inakiuka 1 Wakorintho 14:15; "Imekuwaje, basi? Nitaomba kwa roho, tena nitaomba kwa akili pia; mtaimba kwa roho, tena nitaimba kwa akili pia." Kipengele chochote cha ibada kinaweza kuangukia kwenye jaribu hili: mahubiri ya ajabu ambayo yako kinyume na Maandiko; muziki wa hisia unaoshindwa kusema ukweli wa Biblia; mazoea ya ibada yanayokengeusha hisia za waabudu. Ibada inayozungumza tu na hisia sio ibada ya kweli.
Ibada ya Kweli: Ibada katika Roho na Kweli
Mfano wa kibiblia wa ibada huheshimu umuhimu wa hisia huku tukitathmini kwa makini ukweli wa kile tunachohubiri na kuimba. Kwa sababu muziki ni chombo cha hisia, ni lazima tuwe waangalifu hasa ili kutathmini ukweli wa kile tunachoimba. Hata hivyo, muziki ukitumiwa ifaavyo unaweza kuwa wenye matokeo hasa katika kueleza ukweli unaozungumza na akili na hisia pia.
Yohana Wesley alithamini hisia katika ibada. Alielezea moya ya kutaniko moja "Waliokufa kama mawe - tulivu kabisa, na wasiojali kabisa." Aliamini kwamba kukutana na ukweli kunapaswa kuhamasisha mwitikio wa kihisia. Wakati huohuo, alikuwa mwepesi kukosoa maelezo ya kihisia ambayo yaliondoa ibada ya kweli.
Wesley alionya dhidi ya hisia iliyokithiri; kukataa hisia au kuruhusu hisia kututawala. "Je, kuna ulazima wowote wa kuingia katika hali ya kupita kiasi au nyingine? Je, tusiongoze njia ya kati na kujiweka mbali vya kutosha na roho ya upotovu na shauku bila kukataa karama ya Mungu na kuacha mapendeleo makuu ya watoto Wake?”[2] Huu ni mfano mzuri kwetu leo: kuheshimu umuhimu wa hisia katika ibada, huku tukiepuka kupita kiasi na kukengeusha fikira zetu kutoka kwa Mungu na kweli yake.
"Kwa asili, mimi ni mtu mwenye hisia. Muziki unaweza kuwa na ushawishi mkubwa juu ya hisia zangu. Nilijifunza somo miaka michache iliyopita kuhusu kuweka imani nyingi katika mwitikio wangu ya kihisia.
“Nilipokuwa nikisikiliza wimbo wenye sauti nzuri, niliguswa moyo sana. Wimbo ulipokuwa kwenye mabadiliko muhimu ya sauti, nilijikuta nikilia. Kufikia mwisho wa wimbo, nilihisi kana kwamba nilikuwa na uzoefu wa kina wa kiroho.
“Hata hivyo, niliposikiliza mara ya pili, niligundua jambo fulani lenye kushtua: wimbo huu haukuwa ukimuabudu Mungu wa Biblia. Wimbo huo ulikuwa ukiimba sifa kwa mungu wa ibada ya uwongo. Maneno katika badiliko hilo la sauti yalikuwa ni uzushi.
“Siku hiyo nilijifunza kwamba hisia zangu zinaweza kudanganywa kwa urahisi, hasa muziki. Hiyo haimaanishi kuwa kila mwitikio wa kihisia kwa muziki ni batili, lakini inamaanisha kwamba lazima nitathmini maudhui ya nyimbo. Ni lazima ‘nizijaribu roho’ ili kuhakikisha kwamba zinatoka kwa Mungu.”
Kujipima
Je, ibada yako inazungumza na akili na hisia? Je, uko makini kutathmini kile unachoimba na kufundisha ili kuhakikisha kwamba ni sahihi kwa Maandiko?
“Kuimba ni njia ambayo watu wa Mungu hushika Neno lake na kupatanisha hisia zao na shauku zao sawa na Neno la Mungu.”
- Kutoka kwa
Jonathan Leeman
[2]John Wesley, Mahubiri ya John Wesley, “Ushahidi wa Roho”
[3]Barua kutoka kwa Dk Andrew Graham. Mei 29, 2014.
Hatari za Ibada: Kudharau Ibada
Somo hili lilianza na onyo la Warren Wiersbe dhidi ya kuchukulia ibada kama wakati wa kufurahisha.[1] Alionya kwamba tunapodhani ibada ni kuhusu kujifurahisha badala ya kumtafuta Mungu katika ibada zetu, tunaidharau. “Makanisa bado yanatumia neno ibada lakini maana yake imebadilika. Mara nyingi ibada ni neno tu ambalo watu hutumia kutoa heshima ya kidini kwa chochote walichopanga waumini kufanya, bila kujali ikiwa Mungu ndiye kitovu cha mkutano huo. Je, hii hutokeaje?
Tunahama Kutoka Patakatifu Kwenda Kwenye Ukumbi wa Michezo
Ibada inaweza kutokea popote. Wakristo wameabudu katika mapango wakijificha kutokana na watesi au moto kwenye kambi zao wakati wa mapumziko ya kanisa. Wakristo wameabudu katika nyumba za kibinafsi au majengo yenye mapambo. Wakristo wameabudu wakiwa wamelala hospitalini, wakisafiri kwa ndege, au wanapofanya kazi. Ibada inaweza kutokea mahali popote, lakini ibada nyingi za ushirika hufanyika katika jengo la aina fulani. “Waumini wa kanisa lazima wakutane mahali fulani, na ‘mahali fulani’ patakuwa patakatifu au ukumbi wa michezo.”
Tofauti ni ipi? Patakatifu “ni mahali ambapo watu hukusanyika kumwabudu na kumtukuza Bwana wao.” ukumbi wa michezo ni mahali ambapo watu hukusanyika kutazama maonyesho. Je, jengo lako la kanisa ni ukumbi wa michezo au patakatifu?
Tunahama Kutoka Kanisa hadi Kwa Wasikilizaji
“Kanisa la Kikristo hukusanyika ili kumwabudu Yesu Kristo na kumtukuza Yeye. Wasikilizaji hukusanyika ili kuona na kusikia onyesho. Kanisa linaelekezwa kwa Mungu; waikilizaji wanaelekeza umakini kwa mtendaji. Kanisa linaundwa na washirika; wasikilizaji wanaundwa na watazamaji. Je, unaongoza kanisa au wasikilizaji?
Tunahama Kutoka Kwenye Huduma hadi kwenye Maoanyesho
“Tunahudumu kimsingi ili kueleza ukweli wa Mungu; tunafanya onyesho ili kuvutia watu kwa uwezo wetu. Mhudumu anajua kwamba Mungu anatazama na kwamba kibali chake ndicho cha maana; mwonyeshaji anatafuta makofi ya watazamaji." Huduma inaweza kuwa onyesho kwa njia nyingi tofauti: mwanamuziki anayefanya onyesho kwa ajili ya burudani ya wasikilizaji, kikundi cha sifa kinachotafuta mwitikio fulani wa kihisia, au mhubiri anayepima mahubiri yake kulingana na jinsiwatu wanavyoitikia. Je, unahudumu au unafanya maonyesho?
[1]Nukuu katika sehemu hii zimechukuliwa kutoka Warren Wiersbe, Real Worship (Grand Rapids: Baker Books, 2000), 169-174.
Hitimisho: Ushuhuda wa Mmisionari - Warumi 14 katika vitendo
“Nilijifunza somo muhimu kuhusu kuhukumu wengine kwa sababu ya mtindo wao wa kuabudu nilipohudhuria semina ya uongozi na rafiki mmisionari na wachungaji wanane wa Ufilipino.[1]
“Tuliingia kwenye kituo kikubwa cha mkutano na tukapata viti vyetu juu kwenye mabehewa. Skrini kubwa na vipaza sauti vilikuwa vinaning'inia kwenye dari. Kiongozi wa ibada alikuwa mwanamke Mfilipino akiwa na timu ya sifa nyuma yake. Walikuwa wakipiga makofi na kuongoza umati wenye msisimko kwa wimbo wa ‘Ndiyo, Bwana, Ndiyo!’ ulionekana kuwa umechangamka sana kwa ladha yangu.
“Muziki wenye kurudia-rudia, uimbaji wenye sauti kubwa, na harakati za mwili vilinipa wasiwasi sana. Tulikuwa tumewapa changamoto wachungaji wetu wa Ufilipino kuwa viongozi watakatifu, na sasa tulikuwa tunawaleta katika aina hii ya ibada! Mmoja wa wachungaji wa Ufilipino, kiongozi wa kiroho sana, alikuwa amesimama ameinamisha kichwa chake. Alikuwa akiomba kimya kimya na kutokuwa sehemu ya ibada.
“Nilipata shida, ‘Tunafanya nini?’ Baadaye, nilimwona mchungaji huyohuyo akipiga makofi na kuimba kwa moyo wake wote. Uso wake ulikuwa uking'aa, na alionekana kushikwa na ibada.
“Jioni hiyo, tulishirikishana kile tulichojifunza kuhusu uongozi katika mkutano huo. Wakati wa mazungumzo, nilimuuliza kiongozi huyu wa Ufilipino nini kilifanyika kubadili tabia yake. ‘Kwa nini ulitoka katika kutoshiriki hadi kuabudu ghafla na kufurahia uimbaji?’
"Jibu lake lilikuwa na nguvu. 'Nilitatizwa na muziki. Lakini nilipokuwa nikiomba, Mungu alinionyesha kwamba kiongozi wa ibada na watu katika kutaniko hili walikuwa wanamwabudu Mungu kwa mioyo yao yote. Walikuwa wakimpa Mungu kilicho bora zaidi kulingana na wanavyojua. Bwana akasema, “Je, unaweza kuwaacha kwangu? Je, unaweza kuniabudu bila kuwahukumu wengine?”
“Mchungaji huyu alianza kumwabudu Mungu kwa moyo wake wote kama kawaida kuliko kuwahukumu wale walio karibu naye. Je, hii ilibadilisha mtazamo wa kuabudu wa mchungaji huyu? Hapana; aliporudi kanisani kwake, hakuiga mtindo wa kuabudu aliouona mwisho wa juma hilo.
“Akiwa kama kiongozi katika makanisa yetu, mwanamume huyu mara nyingi aliwahimiza wachungaji wenzake kuruhusu uhuru katika ibada bila kuwalaghai washirika. Aliwahimiza wachungaji wenzake kusawazisha kanuni mbili:
1. Fuata kwa uangalifu kanuni za kibiblia za ibada katika kanisa lako.
2. Epuka kukosoa mitindo ya kuabudu ya makanisa mengine.”
[1]Ushuhuda kutoka kwa Mchungaji David Black, mmisionari wa zamani nchini Ufilipino.
Tunapotathimini mitindo ya kuabudu, hatupaswi kuchanganya utamaduni na Maandiko.
Utamaduni wetu unapopingana na Maandiko, ni lazima tutii amri za Maandiko badala ya matarajio ya utamaduni.
Ili kufikia ulimwengu kwa injili, tunapaswa kuuliza jinsi ibada yetu inaweza kuzungumza kwa ufanisi zaidi katika utamaduni wetu.
(2) Maswali matatu yanatusaidia kuelewa uhusiano kati ya ibada ya kanisa la mahali na utamaduni unaozunguka:
Nani yuko hapa? Inaangalia waamini ambao ni sehemu ya kanisa.
Nani alikuwa hapa? Inaangalia urithi wa kanisa.
Nani anapaswa kuwa hapa? Inaangalia jamii tunayoitwa kufikia.
(3) Kwa sababu muziki ni muhimu sana kwa utambulisho wetu wa kitamaduni, makanisa yanapaswa kuchagua muziki unaoaminika kibiblia na unaozingatia utamaduni.
(4) Ikiwa kupiga makofi ni sehemu ya ibada, tunapaswa kuuliza, “Je, kupiga makofi kunafaa kwa wimbo huu na jambo hili katika ibada yetu?”
(5) Ikiwa kupiga makofi ni kuitikia wimbo maalum, tunapaswa kuuliza, “Je, makofi yangu yanachochewa na sifa kwa Mungu au sifa kwa mwimbaji?”
(6) Ikiwa tutawaweka watoto na vijana katika ibada ya watu wazima, tunapaswa kupanga ibada ambayo itazungumza na vizazi vyote.
(7) Ikiwa tuna ibada tofauti kwa watoto na vijana, tunapaswa kuhakikisha kuwa ibada ni ibada, sio burudani.
(8) Hatupaswi kusisitiza kupita kiasi au kukataa hisia katika ibada.
Somo la 9 Mazoezi
(1) Somo hili lilijumuisha maswali kadhaa ya " Kujipima". Andika jibu la ukurasa mmoja kwa mojawapo ya maswali haya. Jibu lako lazima lijumuishe sehemu mbili:
Tathmini ya kile unachofanya hivi sasa katika ibada.
Pendekezo la mabadiliko ambayo yatafanya ibada yako kuwa muhimu zaidi kitamaduni bila kuhama kutoka kwa kanuni za kibiblia za ibada.
(2) Mwanzoni mwa somo linalofuata, utafanya Jaribio kulingana na somo hili. Jifunze maswali ya mtihani kwa uangalifu katika maandalizi.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.