Mathayo anataka kujiuzulu wadhifa wake wa uchungaji katika kanisa lake. Alifika katika Kanisa la Lakeside First akiwa na msisimko na matumaini makubwa. Anapenda kusoma na kuandaa mahubiri. Anafurahia kutembelea watu na kuleta faraja kwa wale wanaoumia. Anafurahi kupata fursa ya kuhubiri injili kwa wasioamini. Washirika wa kanisa lake wanapenda mahubiri yake. Washirika wapya wanaongezeka. Mathayo anapaswa kufurahi kama mchungaji. Lakini kuna kitu hakiko sawa. Na hii inatokana na mgogoro kuhusu muziki.
Kila Jumatatu asubuhi, Yosia hupiga simu kwenye ofisi ya kanisa. “Mchungaji, muziki wa jana ulikuwa mbaya! Sikuuelewa wimbo wa mwisho. Kibodi ilikuwa na sauti kubwa sana. Siwezi kustahimili. Inabidi ufanye kitu kuhusu muziki katika kanisa hili!
Mathayo hukutana na Thomasi kiongozi wake wa muziki kila jumanne. Thomas ana malalamiko tofauti. “Mchungaji mbona bado tunaimba nyimbo nyingi za kizamani? Wanakwaya wamechoshwa na nyimbo hizi. Jumapili, tuliimba nyimbo mbili za zamani na wimbo mmoja tu mpya. Kwa nini hatuwezi kuondokana na nyimbo hizi za vitabuni? Makanisa yote makubwa yamebadilika. Tafadhali niruhusu nibadilishe muziki!”
Kufikia Jumanne usiku, Mathayo anahisi kuacha kazi yake kwakuwa sehemu ya Kanisa la Lakeside First inapenda nyimbo za zamani; wanalalamika kila wimbo mpya unapoanzishwa. Sehemu nyingine ya Kanisa inachukia nyimbo za zamani; wanataka kuimba nyimbo za kusifu na kuabudu pekee. Mathayo hawezi kupata suluhu.
► Je, ushauri gani unaweza kumpa Mchungaji Mathayo? Je, mziki wa kanisa utahudumiaje kila kundi katika kanisa lake?
Sababu Muhimu za Mziki katika Ibada
Katika mahojiano kuhusu mziki kanisani, mchungaji alisema, “hatuhitaj mziki katika ibada. Kama nitahubiri neno la Mungu kwa ufanisi, uimbaji sio lazima.” Mchungaji huyu hakuona thamani yeyote ya mziki katika ibada.
► Ungemjibu vipi huyu mchungaji? Je, kwa nini mziki ni muhimu katika ibada zetu?
Wakristo ni watu wa kuimba. Waislamu wanapokutana hawaimbi. Wabudha wakikutana hawaimbi. Wahindu wakikusanyika hawaimbi. Wakristo wakikusanyika huimba. Sio kila mkristo anahubiri, anaongoza maombi, au kusoma Maandiko katika ibada. Wakrsito wote wanapaswa kuimba. Hapa chini kuna sababu chache ambazo zinaonesha kuwa mziki ni muhimu katika ibada ya kikristo.
Sababu za kibiblia za umuhimu wa mziki katika Ibada
Mziki ni muhimu katika Ibada kwa sababu ni muhimu katika Biblia. Kuna takribani rejea 600 za uimbaji na muziki katika Maandiko. Vitabu arobaini na nne vya Biblia hurejelea muziki.
Nyimbo za kibiblia zinahusu matukio mbali mbali:
Waisraeli walimsifu Mungu kwa ushindi dhidi ya jeshi la Farao (Kutoka 15).
Waisraeli walimsifu Mungu baada ya ushindi wa Debora dhidi ya Yabini (Waamuzi 5).
Waimbaji waliabudu wakati wa kuwekwa wakfu kwa hekalu. (2 Nyakati 5:11-14).
Waimbaji waliongoza ibada katika ujenzi wa Hekalu (Ezra 3:10-12).
Kitabu cha Zaburi ni mkusanyo wa nyimbo za ibada ya Kiyahudi na Kikristo.
Yesu na wanafunzi wake waliimba nyimbo wakati wa karamu ya mwisho (Mathayo 26:30).
Paulo na Sila waliimba nyimbo za sifa gerezani (Matendo 16:22-25).
Yohana aliona kuwa uimbaji ni sehemu ya ibada mbinguni (Ufunuo 4 and 5).
Sababu za Kitheolojia za Muziki katika Ibada
Waabudu wa Kiyahudi waliimba walipokuwa wakiabudu. Wakristo wakwanza waliimba huku wakitoa shukrani za mioyo yao kwa Bwana (Wakolosai 3:16). Muziki ulikuwa ni sehemu muhimu ya ibada za kikristo.
Kwa bahati mbaya, wakati wa Enzi za Kati, nafasi ya muziki katika ibada ilibadilika. Makanisa yaliruhusu waumini kuimba nyimbo za sifa kwa nadra sana. Badala yake, waumini walitazama na kusikiliza wakati vikundi vya waimbaji waliobobea vikiimba nyimbo ngumu za sifa.
Martin Luther alirudisha muziki wa ibada kwa waumini. Muziki wa kusanyiko unaeleza kanuni ya kitheolojia ya ukuhani wa mwamini. Kanuni hii ilifundisha kwamba kila Mkristo anaweza kumwendea Mungu moja kwa moja; hatuhitaji kuhani kuwa mpatanishi kati yetu na Mungu. Hii ina maana kwamba kila muumini ana haki na wajibu wa:
Kuomba moja kwa moja kwa Mungu.
Kusikiliza Mungu akinena kupitia Neno lake.
Kuimba katika ibada.
Martini Luther aliona uhusiano kati ya usomaji wa Maandiko na uimbaji. Alisema, “Acha Mungu aseme moja kwa moja na watu wake kupitia maandiko, na watu wake waitikie kwa nyimbo za shukrani za sifa.”[1]
Kanuni ya pili ya kitheolojia inayoonyeshwa na muziki ni umoja wa kanisa. Marejeleo mengi ya kibiblia ya uimbaji ni uimbaji wa kusanyiko, uimbaji wa watu wote. Paulo aliwaamuru Wakristo wa kwanza kufundishana na kuonyana kwa wimbo (Wakolosai 3:16). Kanisa linapoimba pamoja, tunadhihirisha umoja wa kanisa.
[1]Imenukuliwa kwa David Jeremiah, Worship (CA: Turning Point Outreach, 1995
Hatari za Ibada: Kupotea kwa wimbo wa Kanisa
Wimbo mkubwa wa Isaac Watts unasema,
“Wasiimbe wale ambao hawakumjua Mungu wetu,
Lakini watoto wa Mfalme wa mbinguni na watangaze furaha yao duniani!”.[1]
Martin Luther alisema, “Ikiwa yeyote hataimba na kuzungumza juu ya yale ambayo Kristo ametufanyia, anaonyesha kwamba haamini kabisa.[2] Fursa ya wimbo wa kanisa uliopotea katika Enzi za Kati ilirudishwa na Wanamatengenezo. Waliamini kuwa kuabudu kwa nyimbo ni mali ya watu. Cha kusikitisha ni kwamba katika makanisa mengi fursa hii inapotea tena.
Usemi wa kimuziki wa ukuhani wa mwamini unaharibika kutokana na muziki ambao haufahamiki kwa mwimbaji wa kawaida. Hii hutokea wakati kwaya zilizofunzwa zinaimba muziki ambao ni mgumu sana kwa watu wengi. Inatokea wakati timu za sifa huimba nyimbo mpya ambazo watu wachache wanaweza kujifunza. Hatupaswi kamwe kuruhusu vikundi vidogo kuchukua nafasi ya nyimbo za kanisa.
Usemi wa muziki wa umoja wa kanisa uko hatarini katika makanisa ambayo yanagawanya kusanyiko katika huduma tofauti kulingana na mitindo tofauti ya ibada au tofauti za vizazi. Ni vigumu kuona kanisa kama mwili mmoja wakati washirika wa muda mrefu wa kanisa hawazingatii washiriki wachanga.
Hebu fikiria maelekezo ya Paulo kwa kanisa la Efeso yaliyotafsiriwa upya kwa baadhi ya makanisa ya kisasa.
Wale wanaoimba zaburi watakutana Jumapili saa 2:30 asubuhi.
Wale wanaoimba Nyimbo za vitabu watakutana Jumapili saa 5:00 asubuhi.
Wale wanaoimba nyimbo za kiroho watakutana Jumamosi saa 1:00 Jioni.
Hapana! Paulo alikuwa anazungumza na washirika wote wa kanisa alipowasihi wajazwe na Roho, wakisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za kiroho, huku wakiimba na kumshangilia Bwana (Waefeso 5:18-19).
Katika vitendo, hii ina maana kwamba kila sehemu ya mwili wa Kristo inasalimisha baadhi ya mapendekezo yake kwa ajili ya umoja wa mwili. Kijana anaimba wimbo wa kitabu kwa tuni ambayo haisisimui sana. Na kwa sababu yeye ni sehemu ya mwili wa Kristo, kanisa pia wanaimba wimbo huo wa kitabu. Mzee pia anaanzisha wimbo mpya wa sifa ambao haufurahishi. Na Kwa sababu yeye ni sehemu ya mwili wa Kristo, na kanisa wanaimba wimbo mpya.
Mwanamuziki aliyefunzwa katika kanisa dogo la kijijini anaimba nyimbo ambazo hazina changamoto kimuziki. Kwa nini? Kwa sababu yeye ni sehemu ya mwili wa Kristo, na mwili wa Kristo unajumuisha washirika ambao hawafahamu muziki mzuri. Mshirika wa kanisa ambaye hana taaluma ya muziki anaweza kusema “Amina” mwishoni mwa wimbo unaoimbwa kwa mtindo ambao hauthamini kabisa. Kwa nini? Kwa sababu yeye ni sehemu ya mwili, na mwili unajumuisha washirika wanaoimba muziki zaidi ya uthamini wake.
Kanuni hii huenda mbali zaidi ya muziki. Mchungaji anayarahisisha mahubiri yake ili yaweze kueleweka kwa watoto na washirika wapya. Waumini wapya hujifunza ili kuelewa kifungu cha mahubiri ambacho kinafaikia uelewa wao mdogo wa Biblia.
Vijana huketi katika ibada ambayo inaonekana kuwa ndefu sana. Kwa nini? Kwa sababu wao ni sehemu ya kanisa na wanajua kwamba baadhi ya vipengele vya ibada vinaweza kuwa juu ya ufahamu wao. Wazee wanamkaribisha mtoto mchanga ambaye analia kwa sauti katika ibada. Kwa nini? Kwa sababu wao ni sehemu ya mwili wa Kristo, na wanafurahi kwamba mwili wa Kristo unajumuisha watoto, wenye kelele.
Je, hii ni sehemu ya ibada? Kabisa! Theolojia ya kibiblia ya ibada inajumuisha kuthamini umoja wa kanisa. Hii inamaanisha kuacha vipaumbele binafsi kwa ajili ya mwili wa Kristo. Inamaanisha kuimba wimbo ambao haupendi. Kwa viongozi, ina maana ya kuchagua nyimbo zinazohudumia sehemu zote za mwili wa Kristo, si tu nyimbo zinazopendwa. Nyimbo za ibada lazima zihudumie kanisa zima, si kwa vikundi vichache tu.
► Fikiria juu ya muziki ulioutumia katika ibada wiki nne zilizopita. Je, uliimba wimbo ambao unahudumia kila mmoja ibadani? Kama kiongozi, je, umewahi kuchagua kwa hiari nyimbo ambazo hupendi, lakini zinahudumia kanisa? Je, muziki wako unaonyesha ukuhani wa mwamini na umoja wa kanisa kwa kuhimiza ushiriki wa kila mwamini ibadani?
[2]Imenukuliwa kwa Ronald Allen and Gordon Borror, Worship: Rediscovering the Missing Jewel (Colorado Springs: Multnomah Publishers, 1982), 165.
Sababu Muziki ni Muhimu katika Kuabudu (Inaendelea)
Sababu za Kivitendo za Muziki katika Ibada
Pamoja na sababu za kibiblia na kitheolojia, kuna sababu za kivitendo za kuthamini muziki katika kuabudu. Nguvu ya muziki inatokana na uwezo wake wa kuhudumia vipengele vyote vya utu wetu.
Muziki huzungumza na akili.
Walimu wa shule wanajua kwamba kuweka sheria ya sarufi kwa tuni rahisi huwarahisishia watoto kukariri. Kuimba maandiko hurahisisha kujifunza. Baadhi ya watu wanaosema, “Siwezi kukariri Biblia” tayari wanajua mistari mingi ya maandiko; wanaziimba kwa nyimbo za sifa. Baadhi ya nyimbo bora za sifa ni mistari ya maandiko iliyowekwa kwa nyimbo za kukumbukwa.
Kanuni mbili zinazoonyesha uhusiano wa muziki na akili ni muhimu.
(1) Muziki unapaswa uzungumze na akili, sio hisia peke yake.
Muziki ni hisia; hiyo ni sehemu ya nguvu zake. Hakuna kitu kibaya na nguvu ya kihisia ya muziki, lakini muziki lazima pia uzungumze na akili zetu.
Baadhi ya waabudu hufikiri kwamba wanaweza kuzima akili wanapoimba. Sauti ya gitaa ni kubwa, mdundo ni mkubwa, muziki ni hisia, hivyo wanadhani wanaabudu. Hatupaswi kamwe kusahau kwamba Paulo alisema, “Mtaimba kwa roho, tena nitaimba kwa akili pia” (1 Wakorintho 14:15).
Ikiwa muziki wetu huzungumza na hisia bila kuzungumza na akili, tunakuwa katika hatari ya ibada ya uongo. Hakuna kibaya kuhusu muziki unaozungumza na hisia; Hatari ni muziki ambao unaozungumza na hisia bila kuzungumza na akili. Wachungaji wenye busara watahakikisha kwamba muziki wa kuabudu haupitwi na akili.
(2) Ujumbe tunaoimba lazima uwe wa kweli.
[1]Muziki huzungumza na akili, kwa hivyo nyimbo ni zana yenye nguvu ya kufundisha mafundisho.
Katika karne ya 18, Mungu aliwatumia ndugu wawili, Charles na John Wesley, kutangaza kweli za kibiblia ambazo watu wengi walihitaji kusikia: Watu wote wanaweza kuokolewa kutoka dhambini, na kila mtu anaweza kuwa na uhakika binafsi wa wokovu. Ndugu hawa walieneza kweli hii kwa njia mbili: John alihubiri kweli hiyo kupitia mahubiri, wakati Charles aliandika nyimbo za tenzi zilizofundisha kweli hiyo. Tenzi zake zilikuwa rahisi kuimbwa na mtu yeyote kwa sababu muziki haukuwa mgumu. Wale waliomsikia na kuimba nyimbo za Charles waliweza kuelewa na kukumbuka kweli za Mungu, hata kama hawakuweza kusoma. Nyimbo zetu leo pia zinapaswa kufundisha kweli thabiti za kibiblia kwa waimbaji na wasikilizaji.
Wachungaji, mkiruhusu nyimbo zisizo za kibiblia, mnadhoofisha ufanisi wa huduma yenu. Watu watakumbuka wimbo muda mrefu baada ya kusahau muhtasari wa mahubiri yako. Tumia muda kupanga muziki kwa ajili ya ibada. Hakikisha nyimbo zinaunga mkono ukweli wa mahubiri.
Kujipima
Je, nyimbo zako za kuabudu ziko sambamba na mafundisho ya Biblia? Makanisa mengi huimba nyimbo ambazo ama zinafundisha makosa au hazifundishi chochote (maneno ni tupu). Je, nyimbo zako zinafundisha ukweli wa ushindi dhidi ya dhambi? Je, nyimbo zako zinafundisha kwamba wokovu unapatikana kwa wote? Je, nyimbo zenu zinafundisha kwamba Mungu anakusudia kumpa kila muumini moyo safi?
Muziki huzungumza na moyo
Jonathan Edwards alisema kwamba tunaamriwa kumwimbia Mungu sifa kwa sababu kuimba “huchochea hisia zetu.” “[2] Ingawa kuzingatia hisia kwa ajili yake mwenyewe ni hatari, hisia ni jibu la kawaida na linalostahili kwa muziki. Kuimba huleta mwitikio wa kihisia kuhusu ukweli. Muziki huzungumza na akili na moyo.
Wakristo wengine wa magharibi wanaogopa muziki ambao unazungumza kwa undani na hisia, lakini wahusika wa kibiblia ambao waliingia kwenye uwepo wa Mungu walihisi mwitikio wa kihisia. Muziki bora wa kuabudu huzungumza na akili na hudai jibu kutoka moyoni:
► Tazama mkusanyiko wa tenzi na mapambio katika lugha yako. Tafuta mfano wa wimbo ulioandikwa kama sala binafsi ya kujitoa kwa Mungu.
Muziki huzungumza na mwili.
Tazama mtoto akiwa kwenye tamasha; ikiwa muziki una mdundo, wataanza kucheza. Muziki huzungumza na mwili.
Muziki unaozungumza na mwili pekee ni wa kimwili. Hata hivyo, Biblia inapozungumza juu ya ibada, mara nyingi inazungumza kuhusu nafasi ya kimwili ya waabudu: mikono iliyoinuliwa, magoti yaliyopigwa, miili ya kusujudu, na harakati za kimwili. Mkao wetu na ishara za kimwili wakati mwingine huwasiliana kwa nguvu zaidi kuliko maneno yetu.
Katika Zaburi 149:3, Israeli inaitwa “walisifu jina lake kwa kucheza, Kwa matari na kinubi wamwimbie” Ingawa baadhi ya tamaduni za kisasa hucheza tu katika suala la mwendo wa kimwili; Biblia inatumia neno dansi kufafanua harakati zozote za kimwili katika ibada. Mtunga-zaburi alitambua kwamba hata mwili unahusika katika sifa.
Hii sio dansi ya kimwili mwili inayofanyika katika vilabu vya usiku, lakini pia sio ya kukaa kwa utulivu kwenye viti vilivyo rasmi. dansi ya Kibiblia ilihusisha kiwango fulani cha miondoko wakati wa nyimbo za ibada. Tunapoinua mikono yetu wakati wa kusifu au kufanya miondoko fulani inayoendana na muziki, Hii inalingana na neno dansi la kibiblia.
Ingawa maana ya ishara za kimwili hutofautiana kutoka tamaduni hadi tamaduni na kizazi hadi kizazi, hatupaswi kamwe kuruhusu ibada takatifu ya Mungu iwe na kielelezo cha mazoea machafu ya utamaduni unaotuzunguka.
► Pitia Kutoka 32 kuhusu ibada takatifu inayojulikana kama “sikukuu kwa Bwana” (32:5) na sanamu za ibada ya Wamisri (32:4) na mazoea ya aibu ya utamaduni wa kipagani (32:25). Ibada yetu lazima iathiri utamaduni unaotuzunguka kupitia uinjilisti. Utamaduni unaotuzunguka haupaswi kuamua mazoea yetu ya kuabudu.
Wachungaji na viongozi wenye hekima watapata muziki unaoepuka kuchafua ibada, lakini ambao pia unazungumza na watu wote, na kuruhusu kusanyiko kuabudu kwa nyimbo katika kweli.
Kujipima
Je, muziki wako wa kuabudu unahudumia mwili wa Kristo kwa namna sahihi ya ibada? Je, watu wako wanasifu na kuabudu bila kuharibu maana ya ibada kwa mazoea ya kimwili?
Muziki huongea na moyo wa ndani
Muziki mara nyingi hujibu matakwa ya mtu. Paulo aliwaamuru wakolosai kuonyana kila mmoja kwa zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni (wakolosai 3:16). Kuonya ni kusahihisha kosa. Karipio linauliza jibu; masahihisho hutaka mtu afanye mabadiliko katika tabia yake. Paulo alitarajia muziki uwe sababu ya mabadiliko. Muziki huigusa nafsi na kuamsha utashi kutoa mwitikio.
► Tazama mkusanyiko wa tenzi na mapambio katika lugha yako. Tafuta mfano wa wimbo ulioandikwa kama sala binafsi ya kujitoa kwa Mungu.
Muziki katika kuabudu ni muhimu kwasababu unazungumza na mtu mzima, kwasababu hii, muziki ni wa thamani na hatari. Ni wa thamani kwasababu unaweza kuwasilisha ukweli kwa njia yenye nguvu. Ni hatari kwasababu inaweza kufanya mafundisho ya uongo yavutie. Warren Wiersbe alionya, “Nina hakika kwamba watu wanapokutanika kuabudu hujifunza theolojia zaidi (nzuri na mbaya) kutoka katika nyimbo wanazoimba kuliko kutoka katika mahubiri wanayosikia…. [Muziki] unaweza kuwa chombo kizuri katika mikono ya Roho au silaha ya kutisha mikononi mwa Adui. Waumini wasio na ufahamu wa kina wanaweza kuingia katika mafundisho ya uongo kwa njia ya nyimbo kabla hata hawajagundua kinachoendelea.”[3]
Muziki una nguvu; utumie kwa busara.
Kujipima
Fikiria nyimbo ambazo umeimba katika wiki nne zilizopita. Je, uliimba nyimbo zilizozungumza na nafsi nzima?
Taja wimbo ambao ulitoa mafundisho kwa washirika wakati wa kuabudu.
Taja wimbo ambao uligusa hisia za washirika wakati wa kuabudu.
Taja wimbo ambao ulitoa changamoto kuhusu kujitoa kwa kina mbele za Mungu wakati wa kuabudu.
Sababu za waumini kuimba: kuchochea ibada yao kwa Mungu, kuimarisha imani yao, kuhamasisha tumaini lao, na kuongeza upendo wao kwa Mungu na kwa watu wengine.
- Umetoholewa kutoka kwa John Wesley
[2]Imetoholewa kutoka Bob Kauflin, Worship Matters (Wheaton: Crossway Books, 2008), 98
Tulianza somo hili kwa hadithi ya mgongano juu ya muziki wa kuabudu. Ikiwa wewe ni mchungaji ambaye unakabiliwa na aina hii ya migogoro, tambua kwamba hili si tatizo jipya! Katika kila kizazi, kanisa limejitahidi kuamua aina ya muziki unaofaa kwa ibada. Kwa makanisa mengi, muziki umekuwa chanzo cha migogoro badala ya kuwa njia ya ibada ya kweli.
Muziki ni muhimu katika ibada za kuabudu. Katika makanisa mengi, nusu ya ibada inahusisha muziki: muziki wakati wa kufungua ibada, kanisa nzima kuimba wakati wa sifa, nyimbo maalum, muziki wakati wa kumaliza ibada, na muziki laini wakati wa maombi. Kwa sababu muziki ni muhimu katika kuabudu, migogoro kuhusu muziki inakua zaidi.
Watu wana mapendekezo tofauti kuhusu mitindo ya muziki. Watu wengi hawataki kuvumilia mitindo ya muziki ambayo hawafurahii.
Migogoro inatokana na tofauti za maoni kuhusu maadili ya mitindo ya muziki. Hapa kuna mitazamo mitatu ya kawaida:
1. Watu wengine wanaamini kwamba mitindo fulani ya muziki ni mibaya. Wanachagua kutumia mitindo ya muziki ambayo wanaamini kuwa safi.
2. Wengine wanaamini kwamba mitindo ya muziki haiwezi kuwa mizuri au mibaya, na hivyo kila mtindo unakubalika. Watu hawa kwa kawaida wanataka kutumia mitindo ya muziki ya kitamaduni kwa ajili ya kuabudu.
3. Wengine wanaamini kwamba mitindo ya muziki haiegemei maadili ilhali ina husisha hisia na tamaduni ambayo huathiri manufaa yao katika kuabudu. Watu hawa hutathmini kila mtindo ili kuona ikiwa utasaidia washirika kuabudu kwa njia inayomletea Mungu heshima.
Katika sehemu hii, tutaangalia kanuni za kibiblia zinazohusu muziki katika kuabudu kwetu.
Maneno ya muziki wa ibada lazima yaweze kuwasilisha ukweli kwa uwazi.
Lengo kuu la Maandiko ni juu ya maudhui ya ujumbe wa wimbo, sio mtindo wa muziki.
[1]Bila kujali mtindo wa muziki, nyimbo zilizo na ujumbe wa uongo (au hazina ujumbe) hazifai katika kuabudu. Warren Wiersbe huonya kwamba maneno mengi katika wimbo “hayaeleweki na hayana hisia, sio ya kitheolojia.”[2] jaribio moja la ujumbe wetu wa muziki ni, "Je, mtu asiyeamini, Mhindu, au Mwislamu anaweza kuimba maandishi haya bila kubadilisha maneno?" Ikiwa unaweza kubadilisha jina la Buddha bila kubadilisha ujumbe wa wimbo, huo wimbo haufai katika kuabudu. Kama wimbo hauzungumzi ukweli kwa uwazi, tunapaswa kuuliza umuhimu wake katika kuabudu. Nyimbo zetu zinapaswa kuwasilisha Imani yetu. Kama hazifanyi hivyo, nyimbo zetu hazitawaelekeza watu wanaoabudu kwa Mungu.
Sikiliza wimbo kutoka katika Maandiko:
Haleluya.
Msifuni BWANA kutoka mbinguni;
Msifuni katika mahali palipo juu.
Msifuni, enyi malaika wake wote;
Msifuni, majeshi yake yote.
Msifuni, jua na mwezi;
Msifuni, nyota zote zenye mwanga.
Msifuni, enyi mbingu za mbingu,
Nanyi maji mlioko juu ya mbingu.
Na vilisifu jina la BWANA,
Kwa maana aliamuru, vikaumbwa.
Amevithibitisha hata milele na milele… (Zaburi 148).
Linganisha hii na wimbo maarufu wa hivi karibuni:
“Ni sahihi kucheza unapocheza kwa jina la Yesu
Ni sahihi kucheza unapocheza kwa ajili ya Bwana…”[3]
Wimbo gani unatangaza Neno la Mungu? Paulo alionya juu ya ibada zisizoeleweka. Alisema, “Mtaimba kwa roho, tena nitaimba kwa akili pia” (1 Wakorintho 14:15). Tunaposoma nyimbo zinazopatikana katika Maandiko, tunagundua kwamba zinafundisha kwa uwazi. Maandishi ya muziki wa kuabudu yanapaswa kuzungumza kweli za kibiblia.
Je, maandiko haya ni ya kweli kwa mujibu wa mafundisho ya imani?
Je, maneno ya wimbo yana muktadha wa kikristo
Je, watu waliokusanyika kuabudu wataelewa ujumbe wa wimbo?
Je, mtindo wa muziki unalingana na maneno?
Je, tuni ya wimbo ni rahisi kwa wanaoabudu kuimba?
Kujipima
Je, nyimbo zako za kuabudu ni za kibiblia kweli? Je, mshirika mpya atamjua Mungu sawasawa na Biblia kupitia nyimbo za kanisa lako?
Mitindo ya Muziki wa ibada Inaweza Kutofautiana
Mungu ni Mungu wa aina mbalimbali. Alivuvia injili nne katika Agano Jipya, sio moja. Alizungumza kwa namna pekee na kila mwandishi. Aliumba maelfu ya aina mbalimbali za Samaki, sio mmoja. Aliumba jicho la mwanadamu lenye uwezo wa kujua tofauti za rangi milioni 8. Uumbaji huonyesha utukufu wa Mungu katika aina yake na uzuri wake. Aliumba watu wa pekee, si aina moja tu ya utu. Mungu anaonyesha utofauti usio na kikomo.
Muziki wetu unapaswa kuakisi aina mbalimbali za ubunifu wa Mungu tunayemwabu. Katika Wakolosai 3:16 Paulo anaorodhesha aina tatu za nyimbo ambazo zinapaswa kutumika kwa ajili ya kuabudu: zaburi, nyimbo, na tenzi za rohoni (Tazama pia Waefeso 5:19). Paulo hakutoa maana ya aina hizi tatu. Waandishi wengi wamefafanua aina hizi tatu kama.
Zaburi huenda zinarejelea kitabu cha zaburi.
Nyimbo pengine ni nyimbo zilizotungwa na binadamu. Waandishi wengi huweka neno hili kuwa ni nyimbo zinazomuimbia Mungu au kuhusu Mungu. Hii inaweza kuhusisha nyimbo za biblia tofauti na kitabu cha zaburi.
Tenzi za rohoni ni ngumu zaidi kufafanua. Waandishi wengine hufafanua hizi kama nyimbo zisizo rasmi; wengine huzingatia tenzi za rohoni kuwa ni nyimbo kuhusu Maisha ya Kikristo na nyimbo kuhusu ushuhuda binafsi.
Bila kujali ufafanuzi, mistari hii inaonyesha kwamba kanisa liliimba aina mbalimbali za muziki tangu siku zake za kwanza.
Warren Wiersbe anazungumzia kanuni ya uhalisia. Anaandika, “Maelezo ya kuabudu lazima yawe ya kweli, yakifichua tofauti za kitamaduni za watu.”[5] Ibada halisi huzungumzia Neno la Mungu katika lugha ya kila tamaduni. Katika kila kizazi, wakristo wameandika nyimbo ambazo zinamsifu Mungu katika mtindo wa muziki wa tamaduni zao. Hatupaswi kudhania kwamba muziki wa tamaduni yetu ni muziki pekee mtakatifu na halisi. Badala yake, isipokuwa mtindo unapingana na kanuni ya wazi ya Maandiko, tunapaswa kuruhusu kila tamaduni na kila kizazi kumsifu Mungu katika lugha zao.
Kujipima
Je, muziki wa kanisa lako unaonyesha aina mbalimbali za ubunifu wa Mungu wetu?
Sio Kila Mtindo Unafaa kwa Kila Hali
Ingawa watu wengi wamejaribu kufafanua kuhusu mtindo wa muziki kibiblia, Biblia haijaamuru aina fulani ya mtindo wa muziki. Baada ya kusoma Falsafa ya mtindo wa muziki, Francis Schaeffer aliandika, “Wacha niseme kwa uthabiti kwamba hakuna kitu kama mtindo wa kimungu…”[6]
Sauti za muziki haziwasilishi maudhui ya maadili. Muziki wa noti zilizopangwa pamoja si wa kiroho wala si wa kidunia. Je, hii inamaanisha kwamba kila mtindo wa muziki unafaa kwa ajili ya ibada? Hapana. Mitindo mingine inahusishwa sana na utamaduni wenye dhambi ambao hautawasilisha ujumbe wa kimungu katika ibada.
Wanamuziki na wamishonari wamepata kitu kimoja: watu huitikia sauti za muziki kwa njia tofauti. Ikiwa watu wawili wanasikiliza muziki uleule, mtu mmoja anaweza kuanza kulia kwa sababu ya jinsi anavyoathiriwa na wimbo huo. Na huenda mtu mwingine asihisi chochote katika kuitikia muziki.[7]
Kipimo kikuu cha muziki wa ibada hakiwezi kuwa, "Je, ninaupenda?" au “Je, unanivutia?” Kipimo kikuu ni utukufu wa Mungu. Hii ina maana kwamba ni lazima tutathmini mtindo gani wa muziki unawasilishwa ndani ya muktadha wetu wa kitamaduni. Ni lazima tuulize, “Katika muktadha wangu wa kitamaduni, je mtindo huu wa muziki unamtukuza Mungu?”
Ijapokuwa vitu vyote ni halali, bali si vitu vyote vijengavyo (1 Wakorintho 10:23). Ikiwa lengo la muziki wa kuabudu ni kuwajenga waumini, mtindo tunaotumia lazima usizuie kusudi hili. Muziki huohuo unaweza kuwa msaada wa kuabudu katika utamaduni mmoja, na pia kizuizi katika utamaduni mwingine. Kiongozi makini wa ibada atachagua muziki unaofaa kwa watu anaowaongoza.
Tunawezaje kujua kama mtindo fulani wa muziki unafaa? Kama kiongozi, unawajibika kusaidia watu wako kujibu swali hili katika mazingira yako ya kitamaduni. Kinachofaa katika utamaduni mmoja huenda kisifae katika utamaduni mwingine. Kwa sababu ya uhusiano wa kidini wa mtindo fulani au kwa sababu mtindo fulani umehusishwa na mazoea ya dhambi ya utamaduni unaozunguka, mtindo wa muziki hauwezi kufaa kwa ajili ya ibada. Lazima utathmini muziki kulingana na kufaa kwake katika hali yako.
Paulo alituamuru tujaribu mambo yote na kushika sana lililo jema (1 Wathesalonike 5:21). Bila kupima na kuthibitisha hatupaswi kukubali kitu chochote. Hii ni pamoja na muziki tunaoimba.
Kujipima
Je, unaimba nyimbo zisizoendana na utamaduni wako? Je, muziki unawasilisha mtindo wa kimwili au wa kilimwengu katika utamaduni wako? Je, ujumbe wa muziki unapingana na ujumbe wa maneno?
Panapaswa kuwa na usawa katika muziki wetu wa ibada.
Kitabu cha Zaburi kinaonyesha kuwa Mungu anathamini utofauti katika ibada. Kitabu cha Zaburi kina sifa, maombolezo, vilio vya kuomba msaada, na shukrani kwa ajili ya ukombozi. Zaburi zinazungumza na mahitaji ya ibada ya waabudu wote.
Alama moja ya ukomavu katika kanisa ni utofauti (1 Wakorintho 12:4-6). Mwili wa Kristo unajumuisha tamaduni tofauti, lugha tofauti, haiba tofauti, na karama tofauti. Ibada yetu, pamoja na muziki wetu, vinapaswa kuzungumza na washirika wote katika mwili wa Kristo. Kwa kweli, ibada yetu inapaswa kuzungumza zaidi ya kanisa lenyewe ili kutoa injili kwa wasioamini. Nyimbo katika Biblia huzungumza na hadhira tatu.[8]
Muziki unapaswa kutangaza sifa kwa Mungu: "Mwimbieni na kumshangilia Bwana" (Waefeso 5:19).
► Soma Zaburi 92:1-4.
Zaburi ya 92 inaonyesha kwamba tunamwimbia Bwana. Muziki unapaswa kueleza sifa kwa Mungu. Kuanzia kwenye wimbo wa sifa katika Kutoka 15 hadi nyimbo za mbinguni katika Ufunuo, nyimbo za kibiblia zinamsifu Mungu kwa ukuu wake. Kusudi kuu la muziki katika Biblia ni sifa. Zaburi za maombolezo, maombi, au sifa mara nyingi huelekezwa kwa Mungu. Ukiimba Zaburi zote, utaimba kuhusu:
“Nilimlilia Bwana kwa sauti kuu…”
“Niitikie ninapoita, Ee Mungu wa haki yangu!”
“Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote.”
“Nitamwimbia Bwana.”
“Nakupenda, Ee Bwana.”
Muziki unapaswa kutangaza ukweli kwa kanisa: “Mkifundishana na kuonyana” (Wakolosai 3:16).
Viongozi wengi wa ibada wamesema, “Hatupaswi kuwaimbia watu wengine; tunamwimbia Mungu pekee.” Hata hivyo, zaburi nyingi huimbia Israeli. Ingawa ni kweli kwamba nyimbo nyingi za Biblia humwimbia Mungu, Pia ni kweli kwamba nyimbo nyingi za Biblia huzungumza na kanisa.
Waefeso 5:19 inawaagiza waamini wasemezane wao kwa wao kwa zaburi, tenzi na nyimbo za kiroho. Wakolosai 3:16 huzungumza zaidi kuhusu kusudi la uimbaji wetu: “Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu.”
Paulo anaonyesha kwamba neno la Kristo linatangazwa kupitia uimbaji wa kanisa. Tunapoimba, tunasema kweli ya Mungu kwa waabudu wenzetu. Kupitia wimbo, kanisa linafundishana. Kupitia wimbo, waamini wanajengwa na mwili wa Kristo unajengwa.
Muziki unapaswa kutangaza injili kwa ulimwengu: “Wahubirini mataifa habari za utukufu wake…” (Zaburi 96:3).
Mtunga Zaburi anatuita kuimba kama ushuhuda kwa mataifa:
Mwimbieni BWANA wimbo mpya, Mwimbieni BWANA, nchi yote. Mwimbieni BWANA, libarikini jina lake, Tangazeni wokovu wake siku kwa siku. Wahubirini mataifa habari za utukufu wake, Na watu wote habari za maajabu yake (Zaburi 96:1-3).
► Soma 1 Wafalme 8:41-43.
Mungu anaposifiwa, injili inatangazwa kwa mataifa. Wakati wa kuwekwa wakfu kwa Hekalu, Sulemani aliomba kwamba hata watu wa mataifa wangeabudu kwenye Hekalu; aliomba kwamba jina la Bwana lijulikane kwa watu wote wa dunia. Tunapoabudu, injili inatangazwa kwa ulimwengu unaotazama.
Muziki wetu wa kuabudu unapaswa kuzungumza na Mungu na kuhusu Mungu; muziki wetu wa kuabudu unapaswa kuzungumza na kanisa; muziki wetu wa kuabudu unapaswa kutangaza injili kwa ulimwengu.
Tunaposahau mojawapo ya wasikilizaji hawa, ibada yetu inashindwa kufikia kusudi kamili la Mungu kwa kanisa. Tunaposahau kwamba Mungu ndiye msikilizaji mkuu wa ibada, ibada yetu inashindwa kusema na Mungu kimsingi. Tunaposahau kuwa kanisa ni wasikilizaji wa ibada, tunashindwa kufundishana na kukumbushana kwa muziki wetu. Tunaposahau kwamba ibada inapaswa kutangaza injili kwa ulimwengu, tunashindwa kuhubiri na kutimiza Agizo Kuu.
Kujipima
Je, katika nyimbo zako unazungumza na Mungu, kanisa, na wasioamini? Sio kila wimbo unazungumza na kila mmoja kati ya haya; lakini katika ibada yote, tunapaswa kuzungumza na kila mmoja wa wasikilizaji hawa.
Kuiweka katika Vitendo
Tumeona kwa nini muziki ni muhimu katika ibada. Tumechunguza kanuni za kibiblia za muziki katika ibada. Tutamaliza somo hili kwa kuangalia mawazo ya kivitendo kuhusu muziki katika ibada. Unaweza kuyachukua haya ili kuendana na kanisa lako na mpangilio wa kanisa.
Kwa kujibu kanuni zilizoorodheshwa hapo juu, mwanafunzi aliuliza, “Ikiwa mitindo ya muziki wa kuabudu inatofautiana na ikiwa mitindo ya muziki kwa asili si nzuri au mbaya, je, kuna miongozo yoyote inayoweza kutusaidia katika kuchagua muziki wa kanisa letu?”
Ndiyo, kuna miongozo yenye kutumika ambayo inaweza kutusaidia. Lazima uamue jinsi ya kutumia hiyo katika eneo lako mahususi, lakini baadhi ya kanuni za kimsingi zinapaswa kuongoza maamuzi yetu kuhusu muziki wa kanisa.
Muziki Muhimu Zaidi Wa Kanisa Ni Uimbaji Wa Waumini Wote.
Kwa kuwa muziki wa kanisa unaonyesha umoja wa kanisa na ukuhani wa waumini, muziki wetu muhimu zaidi ni uimbaji wa washirika wote. Ingawa kwaya, waimbaji binafsi, kikundi cha sifa, na vikundi vya ala na muziki mingine ni vya thamani, muziki wa kanisa nzima ni muziki muhimu zaidi katika ibada ya Kikristo. Kuna baadhi ya hatua zinazofaa tunazoweza kuchukua ili kusitawisha uimbaji wa waumini wote.
Kumbuka:
1. Upigaji wa muziki haupaswi kuwa wa kifahari wenye sauti kali hivyo ukaondoa umakini kutoka kwa uimbaji. Katika Agano Jipya, uimbaji ni muziki wa msingi wa kanisa. Wapiga kinanda, wapiga gitaa, wapiga ngoma sio muziki wa msingi wa kanisa. Acha kanisa liimbe.
2. Baadhi ya nyimbo huimbwa vizuri bila vyombo za muziki. Nyimbo za sala mara nyingi huweza kuwasilishwa vizuri kwa kuimba kimya kimya bila vyombo vya muziki. Hii huwawezesha waumini kuzingatia ujumbe wa wimbo bila vurugu yoyote.
3. Muziki haupaswi kuwa mgumu sana au mpya hivi kiasi kwamba waumini wasiweze kushiriki. Nyimbo mpya ni nzuri, lakini tunapaswa kuwaruhusu waumini muda wa kujifunza wimbo mpya vizuri kabla ya kuongeza nyimbo mpya zaidi. Matumizi ya mara kwa mara ya nyimbo mpya yanakuwa mengi hadi hatuwezi kuelewa ujumbe vizuri. Mbinu nzuri ni kuongeza nyimbo mpya huku tukiendelea kuwa na zile tunazozoea.
4. Wachungaji wanapaswa kuimba pamoja na waumini. Ikiwa kuimba kwa pamoja ni ibada, basi lazima uabudu. Mchungaji anapofanya mambo mengine wakati wa uimbaji wa wote, matendo yake yanasema, “Ni mahubiri yangu pekee ndiyo muhimu katika ibada.” Wachungaji wanapaswa kuwa kielelezo cha ibada kwa waumini wengine.
Muziki Lazima Uhudumie Maandiko
Kwa kuwa muziki wa ibada unakusudiwa kutangaza sifa kwa Mungu, kusema ukweli kwa waumini, na kutangaza injili kwa ulimwengu, maandiko ndiyo kiini muhimu zaidi. Bila kujali mtindo wa muziki, ikiwa muziki unazuia mawasiliano ya maandiko, hatusemezane kwa zaburi, nyimbo, na nyimbo za kiroho.
Hii haimaanishi kuwa muziki wa ala sio muhimu. Vyombo vinaweza kutusaidia kuzingatia akili, hisia, na mapenzi yetu kwenye ibada. Muziki wa ala unaweza kuwa na thamani katika ibada, lakini katika uimbaji wa pamoja, lengo kuu linapaswa kuwa maandiko.
Kiongozi Lazima Awasaidie Waumini Kuzingatia Maana Ya Maandiko.
Viongozi wanaweza kufanya maandiko kuwa na maana zaidi kwa jinsi wanavyoongoza. Mifano miwili itaonyesha jinsi kiongozi anavyoathiri ujumbe wa wimbo.
Yohana hakufikiria kwa makini kuhusu ujumbe wa nyimbo za ibada za waumini. Wiki iliyopita, Yohana aliongoza nyimbo mbili kuhusu utatu. Beti za wimbo wa kwanza kila mmoja unajikita kwenye mambo tofauti: ubeti wa 1 ni sala kwa Baba; ubeti wa 2 ni sala kwa Mwana; ubeti wa 3 ni sala kwa Roho Mtakatifu; na ubeti wa 4 ni sala kwa utatu.
Kabla ya kuimba, Yohana alisema, “Tutaimba ubeti wa 1, 2, na 4.”
Nini kibaya na kuacha ubeti wa 3? Ni wimbo kuhusu Utatu; ujumbe unahisiwa kupunguzwa ikiwa utaacha ubeti.
Katika wimbo wa pili, beti zote tatu ni ibada na sifa kwa mtu maalum katika Utatu. Yohana alisema, “Tuimbe beti mbili.” Tena, Yohana alisahau kwamba wimbo wa Utatu lazima ujumuishe watu wote watatu. Kuacha ubeti wa wimbo bila kuzingatia maandiko kunazuia ibada ya waumini.
Daudi anajua kwamba uimbaji wa waumini wote ni muhimu katika ibada. Siku ya Jumapili, aliongoza wimbo usiojulikana. Alianza kwa kusema, “Wimbo huu ni mpya kwetu. Sikiliza Zaburi ya 150, zaburi ambayo wimbo huu umeegemezwa.” Kwa maneno machache, Daudi alisaidia waumini kuzingatia maana ya wimbo mpya.
Baadaye katika ibada, Daudi aliongoza wimbo unaoelezea ukuu wa Mungu kama mfalme. Kabla hawajaimba, Daudi alisoma 1 Timotheo 1:17; “Sasa kwa Mfalme wa milele, asiyeweza kuona uharibifu, asiyeonekana, Mungu peke yake, na iwe heshima na utukufu milele na milele. Amina.” Wimbo ambao waumini walikuwa wameimba mara nyingi ulifanywa kuwa mpya waabudu waliposikia andiko lililoongooza wimbo huo. Kuunganisha wimbo na msingi wake wa kibiblia kunahamasisha ibada ya waumini.
► Tazama mkusanyiko wa tenzi na mapambio katika lugha yako. Chagua wimbo na kifungu cha Andiko ambacho kinautambulisha.
Ikiwa unatumia kinasa picha (projekta), mtu anayesimamia kinasa picha ni sehemu ya uongozi wa ibada.
Maneno kwenye skrini yanaweza kuwasaidia waabudu kuzingatia maandiko au yanaweza kuwachanganya. Mtu anayesimamia uonyeshaji anapaswa kuwa mwangalifu katika uongozi wake. Ipuka matatizo yafuatayo:
Kuandika neno kimakosa
Kuweka kimakosa alama za kusomea mf nukta na koma.
Kugawa mistari ya wimbo katikati ya vifungu badala ya kuigawa kati ya vifungu
Kuweka slaidi katika mpangilio usio sahihi
Kutobadilisha slaidi kwa wakati unaofaa
Matatizo haya yote huvuruga ibada. Wakati kuna makosa, watu huanza kuyafikiria badala ya kuzingatia ibada. Kuonekana kwa maneno kwenye skrini huathiri uimbaji wa waumini.
Katika muziki wa ibada, muziki huhudumia waabudu. Kwa kuwa hii ni kweli, viongozi wa ibada lazima wasaidie waumini kuimba kwa maana. Hakuna chochote kati ya hii inaunda ibada; Ibada hutoka moyoni. Hata hivyo, kuondoa vikwazo kunawatia moyo waabudu kuzingatia lengo la kweli la ibada, ambalo ni Mungu.
“Ikiwa mtu angekua akiimba nyimbo zetu kwa miaka ishirini, angemjua Mungu vizuri kiasi gani? Je, wangejua kwamba Mungu ni mtakatifu, mwenye hekima, muweza yote, na mwenye enzi kuu? Je, wangeelewa utukufu na umuhimu wa injili?”
- Bob Kauflin
in Worship Matters
[2]Warren Wiersbe, Real Worship (Grand Rapids: Baker Books, 2000), 137
[4]Imechukuliwa kutoka kwa Constance M. Cherry, The Worship Architect. (Grand Rapids: Baker Academic, 2010), 202-203.
[5]Warren Wiersbe, Real Worship (Grand Rapids: Baker Books, 2000), 139
[6]Francis Schaeffer, Art and the Bible (Downers Grove: InterVarsity Press, 1973), 51
[7]Gerardo Marti, Worship across the Racial Divide: Religious Music and the Multiracial Congregation. (England: Oxford University Press, 2012)
[8]Imechukuliwa kutoka kwa Herbert Bateman, editor. Authentic Worship (Grand Rapids: Kregel Publications, 2002), 150-155.
Hatua za Kivitendo za Kuboresha Wimbo wa Waumini Wote
1. Fundisha umuhimu wa kuabudu katika wimbo. Kama vile Wakristo lazima wafundishwe umuhimu wa maombi na nidhamu zingine za kiroho, vivyo hivyo lazima wajifunze jinsi Mungu anawavyokusudia kuimba.
2. Hakikisha waumini wanajua kwanini wanaimba wimbo. Ikiwa ni maombi, wakumbushe. Ikiwa ni wimbo wa kujisalimisha kwa Bwana, eleza hiyo. Ikiwa inaakisi ujumbe uliohubiriwa, weka wazi hilo. Watu wataimba kwa shauku zaidi ikiwa wanajua kwanini wanaimba wimbo.
3. Chagua nyimbo za waumini wote badala ya nyimbo za maonyesho. Nyimbo za kushiriki wote huwa na melodi rahisi zinazoweza kukumbukwa na na kuimbwa kwa urahisi. Ikiwa unataka watu wote kuimba, fikiria, "Je! Watoto wanaweza kuimba wimbo huu wanapokuwa njiani kurudi nyumbani?"
4. Punguza sauti nyingi za muziki. Usiruhusu gitaa, kinanda, ngoma, au kwaya kuzidi sauti ya waumini wote. Sauti kubwa katika chumba inapaswa kuwa sauti za waumini.
5. Tafuta usawa kati ya nyimbo mpya na nyimbo za zamani.
6. Tumia nyimbo ambazo zinaakisi uzoefu mpana wa kikristo. Ikiwa muziki wote ni wa furaha, hautawakilisha waumini ambao wanapitia wakati mgumu. Kama zaburi, nyimbo zetu za ibada zinapaswa kuwa na maneno kwa wakristo wenye furaha, wakristo wenye huzuni, na wakristo wanaopitia wakati mgumu.
7. Mchungaji na viongozi wa kanisa wanapaswa kuwa mfano wa kuimba kwa shauku hata kama hawana ujuzi mzuri wa kuimba. Kuimba nje ya toni ni bora kuliko kutokuimba kabisa. Mchungaji ambaye anatazama maelezo ya mahubiri yake wakati wa kuimba anasema, “kuimba katika ibada si muhimu sana.”
8. Wakumbushe waumini kuwa wao ndio chombo kikuu katika ibada ya pamoja. Ikiwa watu hawaimbi kwa shauku, muziki wa waumini unafeli katika lengo lake. aumini lazima wafundishwe kuwa ni haki yao na jukumu lao kuimba kama tendo cha ibada.
Hitimisho: Ushuhuda wa Gloria
Je, Mungu huzungumza kupitia muziki wa ibada? Sikiliza ushuhuda wa Mchungaji kutokea Taiwani.
Wakati Gloria alipoingia kanisani kwetu, alikuwa hajawahi kusikia injili. Hakuwa akitafuta mahubiri; Hakuwa na nia ya kuwa Mkristo. Gloria hakuwa akimtafuta Mungu, lakini Mungu alikuwa akimtafuta Gloria!
Gloria alitembelea kanisa letu ili kuboresha lugha yake ya Kiingereza. Alikuwa amesikia kwamba kanisa letu lilikuwa linatoa kozi za Kiingereza bure, kwa hivyo alikuja kujifunza Kiingereza. Katika ziara yake ya kwanza, Gloria alifika kwa kuchelewa. Alipoingia patakatifu, kanisa lilikuwa likiimba wimbo rahisi kulingana na Zaburi 42: 1, "Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji. Vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, Ee Mungu."
Mwaka mmoja baadaye wakati wa ubatizo wake, Gloria alitoa ushuhuda huu:
"Sikumbuki chochote kuhusu ibada ile isipokuwa wimbo ambao mlikuwa mnaimba nilipokuwa nimeketi. Niliposikiliza wimbo huo, nilianza kulia. Kwa miaka 30, nimekuwa na kiu ya Mungu kama ayala anavyotamani maji, lakini sikuwahi kujua kile nilichokuwa nikihitaji. Nilijaribu elimu; Nilijaribu pesa; Nilijaribu burudani; Nilijaribu kila kitu - na bado nilikuwa tupu. Niliamua kujaribu kujifunza Kiingereza, kwa hivyo nilikuja kanisani kwenu.
"Badala ya Kiingereza, nilipata maji niliyohitaji. Nilipokuwa nikiketi katika ibada, nililia nilipogundua kuwa Mungu ndiye utimilifu wa kiu ya moyo wangu. Yeye ndiye mtoaji wa furaha ya kweli. Siku hiyo, niliamua kumpa Mungu moyo wangu. Leo hii, yeye ndiye mboni ya jicho langu. "
Kwasababu muziki ulikuwa muhimu katika ibada ndani ya biblia.
Kwasababu inaelezea kanuni ya kitheolojia ya ukuhani wa mwamini.
Kwasababu inaelezea kanuni ya kitheolojia ya umoja wa kanisa.
(2) Muziki
Huzungumza na akili, hivyo ujumbe tunaouimba ni laizma uwe wa kweli.
Huzungumza na moyo na hugusa hisia.
Huzungumza na mwili na haupaswi kuigwa kwa mazoea machafu.
Huzungumza na nia na huuliza mwitikio.
Huzungumza na mtu mzima. Hii inafanya kuwa ya thamani wakati inafundisha ukweli na hatari wakati inafundisha uzushi.
(3) Misingi ya Maneno kwa muziki wa ibada ni pamoja na:
Maneno ya muziki wa ibada lazima yawe wazi katika kuwasilisha ukweli.
Mitindo ya muziki wa ibada inaweza kutofautiana. Paulo anarejelea zaburi, nyimbo, na tenzi za rohoni. Tangu siku zake za mwanzo, kanisa liliimba aina mbalimbali za muziki.
Sio kila mtindo unafaa kwa kila mazingira. Tunapaswa kujiuliza, “katika muktadha wa tamaduni yangu, je, mtindo huu wa muziki unampa Mungu utukufu?”
(4) muziki unapaswa kuzungumza na wasikilizaji watatu:
Muziki unapaswa kutangaza sifa kwa Mungu.
Muziki unapaswa kutangaza kweli kwa kanisa.
Muziki unapawwa kuhubiri injili kwa ulimwengu.
(5) Kanuni za muziki wa kanisa ni pamoja na:
Muziki muhimu zaidi wa kanisa ni wimbo wa pamoja.
Muziki ni lazima uhudumie maandiko.
Somo la 6 Mazoezi
(1) Ili kufahamu aina ya muziki unaopatikana kwa ibada, tengeneza orodha ya nyimbo 4 au zaidi ambazo zinashughulikia kila mada zifuatazo. Orodha yako itatumika wakati unapanga ibada katika somo la baadaye. Tafuta nyimbo ambazo zinazungumza na akili, moyo, na nia.
Nyimbo 4 kuhusu asili ya Mungu
Nyimbo 4 kuhusu Yesu, kifo chake na kufufuka kwake
Nyimbo 4 kuhusu Roho Mtakatifu na kanisa
Nymbo 4 ambazo zinawaalika watu wa Mungu kuwa na maisha matakatifu
Nyimbo 4 kuhusu injili na umisheni
Ikiwa unasoma katika kikundi, shirikisha orodha zako na kisha ujadili, "Je! Ni nyimbo ngapi ambazo tumeimba katika mwaka uliopita? Je! Tunatangaza injili nzima katika uimbaji wetu?
(2) Mwanzoni mwa somo linalofuata, utachukua mtihani kulingana na somo hili. Soma maswali ya mtihani kwa uangalifu katika maandalizi.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.