Utangulizi wa ibada ya Kikristo
Utangulizi wa ibada ya Kikristo
Audio Course Purchase

Search Course

Type at least 3 characters to search

Search through all lessons and sections in this course

Searching...

No results found

No matches for ""

Try different keywords or check your spelling

results found

Lesson 4: Ibada katika Agano Jipya

22 min read

by Randall McElwain


Malengo ya Somo

Mwisho wa somo hili, mwanafunzi anapaswa:

(1) Kuelewa jinsi Yesu alivyotimiza ibada.

(2) Kutambua aina za ibada za uongo katika injili, Matendo na Ufunuo.

(3) Kutoa ahadi binafsi kwa ibada na uinjilisti.

(4) Kujua vipengele vya msingi vya ibada katika kanisa la kwanza katika nyaraka.

(5) Kupata uzoefu wa ibada inayolenga Mungu.

Matayarisho kwa somo hili

Kariri Warumi 12:1-2.

Utangulizi

[1]Mchungaji James, Enoch, Gideon, na Jason walikutana tena kujadili walichojifunza kuhusu ibada kutoka Agano la Kale.

James, anayethamini ibada za tamaduni za zamani, alisema, “Nadhani Agano la Kale linathibitisha kuwa kanisa langu linafanya ibada kwa usahihi. Ibada katika Hekalu ilikuwa rasmi na iliyopangwa. Hicho ndicho tunajaribu kufanya.”

Enoch alicheka, “Ndiyo, lakini ulisoma manabii walivyosema? Ibada rasmi ya Hekalu haikumaanisha chochote! Ibada inayompendeza Mungu ni ibada kutoka moyoni. Hicho ndicho tunachofanya katika ibada yetu ya kisasa; tunagusa mioyo ya kizazi kipya.”

Kwa hasira, Gideon alisema, “Hatuko mbali zaidi kuliko tulipoanza kujifunza kuhusu ibada. Kwa nini Mungu asiseme tu, 'Hivi ndivyo mnavyopaswa kuniabudu'?”

Jason alisema. “Tusikate tamaa. Sisi ni Wakristo wa Agano Jipya; labda Agano Jipya litajibu maswali yetu. Hebu tujifunze ibada katika Agano Jipya na tuone linasema nini.”

► Je, ibada ilibadilika vipi katika Agano Jipya? Ibada ya kanisa la kwanza ilikuwa tofauti vipi na ibada ya Hema na Hekalu? Fupisha unachojua tayari kuhusu ibada ya Agano Jipya.


[1]

“Ibada ni shughuli kuu na ya kipekee isiyoweza kuepukika ya kanisa la Kikristo. Ni ibada pekee itakayoendelea…hadi mbinguni, wakati shughuli nyingine zote za Kanisa zitakuwa zimekoma.”

- W. Nicholls

Injili: Ibada Inatimizwa katika Yesu Kristo

Jumla ya neno ibada katika Agano jipya, nusu yake iko katika vitabu vya injili. Injili zinaonesha kwamba Yesu ndiye utimilifu wa mwisho wa ibada. Anatimiza ibada kwa njia mbili.

Katika Ubinadamu Wake, Yesu Alikuwa Mfano Mkuu wa Ibada

Yesu aliweka mfano wa ibada ya kweli. Yesu alimwambia mwanamke Msamaria kwamba Mungu anatafuta wale wanaomwabudu kwa roho na kweli (Yohana 4:24). Katika desturi zake za ibada (kusoma Biblia, kuomba, kuhudhuria sinagogi na Hekalu), Yesu alionesha maana ya kuabudu kwa roho na kweli.

Yesu alipenda mahali pa ibada.

Luka anaonesha upendo wa Yesu kwa mahali pa ibada. Hata akiwa mtoto, Yesu alitambua Hekalu kama nyumba ya Baba yake (Luka 2:41-49). Alikuwa na shauku kwa usafi wa ibada ya Hekalu; mara mbili aliwafukuza wale waliokuwa wakinyanyasa Hekalu.[1]

Mwanzoni mwa huduma yake kwa umma, Yesu alikwenda katika sinagogi huko Nazareti siku ya Sabato kama desturi yake (Luka 4:16). Katika huduma yake yote duniani, Yesu mara nyingi alitembelea masinagogi.

Yesu alikataa kumwabudu yeyote au chochote isipokuwa Mungu.

Katika jangwa, Yesu alikataa jaribu la ibada ya uongo.

► Soma Mathayo 4:9-10.

Jaribu la kuabudu kiumbe badala ya Muumba ni mada ya mara kwa mara katika maandiko. Ni mzizi wa sanamu katika Agano la Kale. Ufunuo unaonesha tofauti kati ya ibada ya joka na mnyama, na ibada ya Mungu na Mwana-Kondoo. Yesu alikataa kuabudu kiumbe.[2]

Yesu alizoea kuomba.

Maombi yalikuwa muhimu katika huduma yote ya Yesu. Mara kumi na tano, injili zinaripoti kwamba Yesu aliomba. Katika baadhi ya nyakati hizi, alitumia usiku kucha akiwa peke yake na Baba yake. Kabla ya kuchagua mitume kumi na wawili, alitumia usiku kucha katika maombi (Luka 6:12). Katika masaa yake ya mwisho na wanafunzi wake, Yesu aliwaombea wanafunzi na wote watakaokuja kuamini ndani yake (Yohana 17). Akikabili msalaba, alikwenda Gethsemane kuomba (Mathayo 26:36-42). Maombi yalikuwa muhimu katika ibada ya Yesu.

Yesu alielezea ibada ya kweli.

Mbali na kuonesha ibada kupitia matendo yake mwenyewe, Yesu alifundisha mara kwa mara kuhusu ibada. Alifundisha mwanamke Msamaria kuhusu ibada ya kweli. Yesu aliwafundisha wanafunzi maombi ya mfano na alifundisha kuhusu maombi kupitia mifano (Luka 11:5-8, Luka 18:1-14).

► Soma Luka 11:1-4.

Maombi ya mfano ya Yesu yanaonesha kwamba maombi lazima yatoke katika moyo wa ibada. Maombi yanaanza, "Jina lako litukuzwe." Kutukuza ni kuheshimu kama takatifu. Katika maombi, tunamtambua Mungu kama mtakatifu.

Yesu alikemea ibada ya uongo.

Kama ibada ya kweli ni ibada katika roho na kweli, basi ibada ya uongo ni chochote kinachokosa haya. Yesu alikataa:

(1) Ibada ya kinafiki

Katika Mahubiri ya Mlimani, Yesu alionya kwamba inawezekana kufanya mambo sahihi kwa sababu zisizo nzuri. Kutoa kwa maskini, maombi, na kufunga ni vipengele vyote vya ibada. Yesu alionya dhidi ya wale wanaofanya matendo haya ili kuwavutia wengine; wao ni wanafiki (Mathayo 6:1-18). Waabuduo wa kweli hufanya matendo haya kwa nia ya kufanya ibada kwa Mungu.

Katika Mathayo 23, Yesu aliwalaani viongozi wa kidini ambao hufundisha mambo sahihi kuhusu ibada, lakini mioyo yao iko mbali na Mungu. Yesu alisema kwamba mafundisho yao yalikuwa sahihi, lakini mioyo yao ilikuwa mibaya; wao ni wanafiki.

(2) Ibada ya kisheria

Hatari moja ni ibada ya kinafiki; ibada inayokusudiwa kuwavutia watazamaji badala ya kumpendeza Mungu. Hatari nyingine ni sheria; ibada inayokusudiwa kupata kibali cha Mungu kupitia kutimiza masharti fulani. Tunapojaribu kupata kibali cha Mungu kwa matendo yetu ya ibada, tunapoteza ukweli wa ibada ya kweli. Ibada inakuwa kazi ambayo tunapata kibali cha Mungu badala ya jibu la furaha kwa wema wa Mungu.

Yesu aliwakera viongozi wa kidini wa Israeli alipozivunja desturi zao [3] Yesu hakuvunja sheria au hata roho ya sheria; alivunja desturi za kibinadamu zilizokuwa zimejengeka kupitia miaka ya uhalali wa Kifarisayo. Kwa Mafarisayo, desturi hizi zilikuwa muhimu kama sheria yenyewe. Waliamini kwamba kuzingatia sheria kunapata kibali kwa Mungu. Hii inafafanua sheria: jaribio la kupata kibali cha Mungu kwa kutimiza masharti. Yesu alikataa sheria kwa nguvu kama alivyokataa unafiki.

Katika Uungu Wake, Yesu Anaabudiwa

Baada ya kifo na ufufuo wake, Yesu anakaa mkono wa kuume wa Baba na kwa haki anapokea ibada (Ufunuo 5:12-14). Paulo aliandika kuhusu mabadiliko haya katika Wafilipi 2. Kwa sababu ya kujinyenyekeza kwa hiari ya Yesu, sasa anatukuzwa na kuabudiwa.

Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba (Wafilipi 2:9-11).

Katika Mathayo 18:20, Yesu alishuhudia kwamba anastahili kuabudiwa. Katika desturi ya Kiyahudi, wanachama wa kiume 10 walihitajika kabla ya sinagogi kukutana kwa maombi na ibada. Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Kwa kuwa wawili au watatu wamekusanyika kwa jina langu, hapo nipo kati yao.” Katika Kanisa, uwepo wa Yesu, si idadi ya watu waliohudhuria, ndio huamua ibada.

Kwa kupitia makundi ya watu waliotazama miujiza yake, Yesu anaonesha kwamba anastahili kuabudiwa. Walipoona miujiza yake, watu walimtukuza Mungu, kitendo cha ibada. Watu waliouona uponyaji wake wote walishangaa (Marko 1:23-27).

Usiku wake wa mwisho na wanafunzi, Yesu alikula Pasaka. Wakati mlo huu ulifuata mpangilio wa kawaida wa mlo wa Pasaka ya Kiyahudi, Yesu aliupa maana mpya alipowaambia wanafunzi kwamba mkate "ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu" na kikombe "ni agano jipya katika damu yangu" (Luka 22:19-20).

► Soma Luka 22:13-20.

Aliwaamuru wafanye hivi kwa ukumbusho wake. Meza ya Bwana inamlenga Kristo, utimilifu kamili wa Pasaka.


[1]Yohana 2:13-16 anazungumzia kutakaswa kwa kwanza. Mathayo 21:12-27, Marko 11:15-17, na Luka 19:45-46 wanatoa taarifa kwa kutakaswa pili wakati wa juma la mwisho la huduma yake duniani.
[2]Yesu hakuwa kama watu wanaotajwa katika Warumi 1:25.
[3]Mathayo 12:1-14, Luka 13:10-17, na Yohana 5:8-18, kati ya wengine.

Ibada ya Kibiblia Leo

Karipio la Yesu dhidi ya ibada ya uongo na mfano wake wa ibada ya kweli unaonesha kwamba ibada yetu lazima iwe ya dhati, siyo kwa ajili ya kuwavutia wengine. Ibada ya kweli lazima ilenge kumpendeza Baba, siyo kuwafurahisha wengine.

Jaribu hili ni la mara kwa mara kwa viongozi wa kanisa. Kwa sababu kuhubiri na kuongoza ibada kunafanywa hadharani, tunaweza kushawishika kufanya maonesho badala ya kuabudu. Tunapolenga kuwafurahisha watu badala ya kumheshimu Mungu, tunafanya maonesho badala ya kuabudu.

Je, nini jaribu la ibada ya uongo kwa kiongozi?

  • Kuchagua andiko la mahubiri kwa sababu tunajua litapendwa na wasikilizaji

  • Maombi yanayozungumzia zaidi wasikilizaji badala ya Mungu

  • Sadaka inayotolewa kwa namna inayovutia umakini kwa mtoaji

  • Muziki unaomletea utukufu mwimbaji badala ya Mungu

Mafundisho na mfano wa Yesu yanatukumbusha kwamba ibada ya kweli ni ya Mungu pekee. Ibada ni kuhusu yeye, siyo kuhusu sisi.

Kujipima

Jiulize, "Je, nani anaheshimiwa katika uongozi wangu wa ibada? Je, ninahubiri, kuimba, kuomba, na kutoa kwa utukufu wa Mungu, au kwa ajili ya kutambuliwa kwangu? Je, kweli ninaabudu?"

Matendo ya Mitume: Ibadan a Uinjilisti

Ibada inahusiana kwa karibu na uinjilisti. Wasioamini wanakuwa waabudu wanaposikia na kuipokea injili. Kitabu cha Matendo ya Mitume kinaonesha uhusiano kati ya ibada na uinjilisti.

Isaya 6:8 inaonesha kwamba ibada husababisha uinjilisti; jibu la Isaya kwa ibada lilikuwa "Mimi hapa! Nitume mimi." Tunapoabudu kiukweli, tunapata shauku ya uinjilisti. Katika ibada, tunamwona Mungu na tunayaona mahitaji ya dunia yetu kupitia macho ya Mungu. Ibada huumba wainjilisti.

Ibada huwahamasisha kanisa kwa uinjilisti. Kanisa linapowaongoza wasioamini kwa Kristo, waumini wapya wanakuwa waabudu. Waabudu hawa wapya kisha wanahamasishwa kwa uinjilisti.

Kitabu cha Matendo ya Mitume kinaonesha mchakato huu kwa vitendo. Baada ya Paulo kuhubiri huko Efeso, watu waligeuka kutoka kwa mungu Diana na ibada ya miungu iliyotengenezwa kwa mikono na kuelekea kwa ibada ya Mungu wa kweli (Matendo 19:26-27). Tunapomhubiri Kristo, waumini wapya wanavutwa katika ufalme; wanakuwa waabudu. Uinjilisti huumba waabudu.

Ibada ya Kweli huhamasisha Uinjilisti

Matendo ya Mitume yanaanza na wanafunzi wakiabudu; walikuwa pamoja wakijitoa kwa maombi (Matendo 1:14). Matendo yanaisha na Paulo akihubiri huko Rumi; alikuwa " akihubiri habari za ufalme wa Mungu, na kuyafundisha mambo ya Bwana Yesu Kristo, kwa ujasiri mwingi, asikatazwe na mtu " (Matendo 28:31).

Ibada ya Wakristo wa mwanzo iliongoza kwa uinjilisti. Wito wa Paulo na Barnaba ulitokea katika mazingira ya ibada.

Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, “Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia.” Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao (Matendo 13:2-3).

Ibada ya kweli inahamasisha uinjilisti.

Uinjilisti Wa Ufanisi Huunda Waabudu

Katika kitabu chote cha Matendo, wanafunzi walikuwa wakijishughulisha na ibada. Siku ya Pentekoste, watu 3,000 waliokolewa. Waumini hawa wapya wakawa waabudu; walijitoa kwa mafundisho ya mitume na ushirika, kwa kumega mkate na maombi (Matendo 2:42).

► Soma Matendo 2:42-46 kwa picha ya ibada katika kanisa la mwanzo.

Wakristo wa Kiyahudi waliendelea kuabudu katika Hekalu.[1] Zaidi ya hayo, Wakristo wa Kiyahudi na watu wa Mataifa waliokoka walikutana kwenye sinagogi kwa ibada. Katika miji mingi, Paulo alianza huduma yake katika sinagogi, akionesha kuwa Yesu ni utimilifu wa ahadi za Agano la Kale.[2] Ibada pia ilifanyika katika nyumba za faragha. Waumini walitembeleana nyumba kwa nyumba kwa ushirika na ibada (Matendo 2:46). Barua za Paulo zinajumuisha salamu kwa makanisa yanayokutana nyumbani.[3] Jitihada za uinjilisti za kanisa la mwanzo ziliunda kundi jipya la waabudu.

Uinjilisti katika Areopago

Ujumbe wa Paulo kwenye Areopago ni maandiko ya kawaida yanayoonesha uhusiano kati ya uinjilisti na ibada (Matendo 17:16-34). Huko Athene, Paulo alikabiliana na utamaduni uliojaa sanamu za miungu. Paulo alionesha tofauti kati ya ibada ya uongo ya sanamu na ibada ya kweli ya Yehova.

Waathene walikuwa washika dini sana (Matendo 17:22).

Watu wa Athene walikuwa waabudu, lakini hawakuabudu Mungu wa kweli. Ibada yenyewe haitoshi; ibada lazima ilenge kwenye kitu sahihi.

Waathene waliabudu kwa ujinga (Matendo 17:23).

Hawakujua nani wanayemwabudu. Paulo aliwatangazia Bwana ambaye walikuwa wakimtafuta. Aliwaambia kwamba Mungu ameumba mataifa yote kwa namna yao ili kumtafuta na kumpata. Hii ni kauli ni ya mtu papasa gizani. Njaa ya mwanadamu kwa Mungu ilitoa nafasi ya injili.

Waathene waliabudu mungu asiyeweza kutosheleza.

Yehova haabudiwi kwa mikono ya wanadamu, kana kwamba anahitaji chochote. Yeye ndiye anayewapa watu wote uhai, pumzi, na vitu vyote (Matendo 17:25). Ibada ya Waathene ilikuwa ya uongo kwa sababu mungu wao asiyeweza kutosheleza. Mungu wa kweli anawapa wote uhai; hahitaji chochote. Tunamwabudu Mungu kwa sababu anastahili ibada yetu, si kwa sababu anahitaji ibada yetu.

Paulo alilinganisha sanamu na Mungu wa kweli.

1. Mungu ni Muumbaji. Alifanya ulimwengu na kila kitu ndani yake... Yeye ni Bwana wa mbingu na dunia (Matendo 17:24). Tofauti na sanamu zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu, Mungu aliumba mwanadamu. Yeye si mungu mgeni; (Matendo 17:18) yeye ni muumbaji wa ulimwengu wote.

2. Mungu yuko karibu. Yeye hayuko mbali na kila mmoja wetu (Matendo 17:27). Ingawa Mungu ni mtukufu, ameuingia ulimwengu wetu na yuko karibu na kila mwabudu.

3. Mungu atawahukumu wale wanaokataa kutubu (Matendo 17:30-31). Ibada katika ukweli inatambua kwamba Mungu ni hakimu mwenye haki ambaye hatavumilia uasi. Katika ibada yetu, tunajisalimisha kwa enzi yake.

4. Mungu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu, akionesha kwamba Yesu anastahili kuabudiwa (Matendo 17:31). Yesu alijinyenyekeza kwa hiari hadi kufa; sasa ameinuliwa na Baba, " ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba" (Wafilipi 2:10-11).

Ujumbe wa Paulo huko Athene ulikabiliana na ibada ya uongo ya sanamu kwa injili ya ibada ya kweli ya Yehova. Uinjilisti wenye ufanisiwa kweli huunda waabudu.


[1]Matendo 2:46, Matendo 3:1, 11-26; Matendo 4:2, Matendo 5:12, 42
[2]Matendo 13:14-15, Matendo 14:1, Matendo 17:1, 10; Matendo 18:4, 19; Matendo 19:8
[3]Warumi 16:5, 1 Wakorintho 16:19, Wakolosai 4:15, Filemoni 1:2

Hatari za Ibada: Ibada Bila Uinjilisti

Makanisa mengi hutenganisha ibada na misheni na uinjilisti. Makanisa mengine husema, "Tumejitolea kwa kufanya uinjilisti. Shauku yetu ni kuwafikia waliopotea." Makanisa haya hayazingatii sana ibada. Wanajiona kama makanisa ya uinjilisti. Makanisa mengine husema, "Tunaamini lengo kuu la kanisa ni ibada. Watu wengine wanaweza kufanya uinjilisti; lengo letu ni ibada."

Matendo yanaonesha kwamba kanisa lazima lijitolee kwa ibada na uinjilisti. Ibada ya kweli hutupa shauku kwa uinjilisti. Uinjilisti wa kweli huunda waabudu wapya.

Hatuwezi kutenganisha ibada na uinjilisti. Ibada ambayo haihamasishi uinjilisti ina uwezekano wa kuwa ibada ya kujitakia yenyewe ambayo hufanywa kwa ajili ya msukumo wetu wenyewe. Uinjilisti ambao hauongozi kwa ibada utatengeneza Wakristo wa juu juu ambao wanashindwa kumwona Mungu kweli.

Katika ibada ya kibiblia, tunapata shauku mpya kwa uinjilisti. Kama Isaya, mtazamo wetu wa Mungu utaambatana na mtazamo wa dunia yenye uhitaji. Kama Isaya, ahadi yetu ya ibada kwa Mungu itatuongoza kusema, "Mimi hapa! Nitume mimi."

Kujipima

Jiulize, “Je, ibada inanihamasisha kushiriki injili na wasioamini? Je, nina shauku ya kuwaleta waabudu wapya kwa Mungu?”

Waraka: Ibada ya Kanisa la Kwanza

Tofauti na Agano la Kale lenye maelekezo maalum kwa ajili ya ibada ya Kiyahudi, Agano Jipya halitoi maelekezo mengi kwa ajili ya ibada kanisani.[1] Hakuna maelezo kamili ya ibada katika Agano Jipya, lakini nyaraka zinaonesha baadhi ya vipengele vya ibada ya Kikristo vya kanisa la kwanza.

Kusoma Maandiko

Kusoma maandiko kulikuwa muhimu katika ibada ya Kikristo ya kwanza. Wakolosai 4:16 na 1 Wathesalonike 5:27 zinaagiza makanisa kusoma barua za Paulo kwa pamoja. Katika 1 Timotheo 4:13, Paulo anamkumbusha Timotheo kuzingatia usomaji wa maandiko wa pamoja.

Umuhimu wa kusoma maandiko unaoneshwa katika Wakolosai 3:16, “Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu… katika hekima yote.” Mwandishi wa zaburi anamwelezea mtu aliye barikiwa; anafurahia na kutafakari sheria ya Bwana (Zaburi 1:2). Ibada yetu ya hadhara inaonesha thamani tunayoweka kwenye Maandiko.

Kuhubiri Neno

Pamoja na kusoma maandiko, kiongozi alikuwa na jukumu la kuhubiri Neno (2 Timotheo 4:1-4, Tito 2:15). Tangu wakati wa Ezra, waandishi walifafanua Maandiko kwa watu. Ezra na wenzake walisoma kutoka kitabu, kutoka Sheria ya Mungu, kwa uwazi, na wakafafanua maana, ili watu waelewe usomaji (Nehemia 8:8). Masinagogi ya Kiyahudi katika enzi ya Agano Jipya yaliendeleza desturi hii (Matendo 13:14-15). Kutoa ufafanuzi wa maandiko ni msingi wa mahubiri ya Kikristo ya kwanza.

Mahubiri katika Matendo yanaonyesha yaliyomo katika mahubiri ya Kikristo ya kwanza.[2] Mada muhimu katika mahubiri haya ni pamoja na:

  • Yesu alitimiza unabii wa Agano la Kale.

  • Yesu alifanya kazi kuu kwa nguvu za Mungu.

  • Yesu alisulubiwa na kisha kufufuka kutoka kwa wafu.

  • Yesu sasa ametukuzwa na kufanywa Bwana.

  • Wote wanaosikia wanapaswa kutubu na kubatizwa.

Maombi ya pamoja

Maombi ya Pamoja yalikuwa muhimu katika ibada za Kikristo za kwanza (1 Timotheo 2:1-3). Wanazuoni wengi wanaamini kwamba maombi yalijumuishwa katika barua za Paulo zilitumika katika ibada za pamoja. "Amina" ya mkusanyiko ilionesha kukubaliana kwao na maombi.[3]

Kuimba

Kuimba kulikuwa muhimu katika Hekalu na kuliendelea kuwa na nafasi katika ibada za Kikristo za kwanza. Pamoja na Zaburi ambazo Wakristo walileta kutoka kwenye ibada zao za Kiyahudi, nyimbo mpya zilimsifu Yesu kama Masiya. Hii inashauriwa na Waefeso 5:19 na Wakolosai 3:16. Wanazuoni wengi wa Biblia wanaamini kwamba Wafilipi 2:5-11 ilikuwa wimbo wa Kikristo wa kanisa la kwanza. Zaidi ya hayo, wimbo wa Maria katika Luka 1:46-55 na maombi ya Simeoni katika Luka 2:29-32 huenda zilikuwa zinaimbwa katika ibada.

Sadaka

Katika baadhi ya nyakati, sadaka ilikuwa sehemu ya ibada ya pamoja. 1 Wakorintho 16:2 na 2 Wakorintho 9:6-13 zinaelekeza kanisa la Korintho kukusanya sadaka kwa ajili ya Wakristo wanaoteseka huko Yerusalemu.

Ubatizo na Meza ya Bwana

Ubatizo na Meza ya Bwana zilikuwa sehemu ya ibada. Paulo aliandika kurekebisha matumizi mabaya katika sherehe za Meza ya Bwana za Wakorintho. Badala ya kuwa ukumbusho wa dhabihu ya Kristo, ilikuwa imekuwa karamu. Paulo alionya juu ya uzito wa Meza ya Bwana. Ushirika unakumbuka tukio takatifu zaidi kwa Mkristo; haupaswi kuchukuliwa kwa wepesi.[4]

Zaidi ya viashiria hivi vya vipengele vya ibada, tunajua kidogo sana kuhusu ibada za Kikristo za kwanza. Nyaraka hazielekezi utaratibu maalum wa ibada, mazingira ya ibada, au maelezo mengine kuhusu ibada za pamoja katika kanisa la kwanza. Kwa sababu ya aina mbalimbali za asili za kidini na kitamaduni zilizowakilishwa katika kanisa la kwanza, inawezekana kwamba ibada za pamoja zilionekana tofauti kutoka mahali hadi mahali. Wakristo wa Kiyahudi huenda waliendelea kuabudu kwa namna inayofanana na ibada za sinagogi. Wakristo wa Mataifa wasingekuwa na mazoea ya Kiyahudi na huenda waliabudu kwa namna tofauti. Hata hivyo, ni wazi kwamba kanisa la kwanza liliweka msisitizo mkubwa juu ya maandiko na kuhubiri na kufundisha Neno la Mungu.


[1]Sehemu kubwa imechukuliwa Franklin M. Segler na Randall Bradely, Christian Worship: Its Theology and Practice. (Nashville: B&H Publishing, 2006), Chapter 2.
[2]Mahubiri muhimu katika Matendo yanapatikana katika Acts 2, 7, 10, 17.
[3]1 Wakorintho 14:16 inamsingi katika utendaji huu.
[4]Mathayo 28:18-20, Matendo 2:38-41, 1 Wakorintho 11:20-34

Ibada ya kibiblia Siku hizi

Katika makanisa mengi, kusoma maandiko pamoja kumekuwa nadra. Si jambo la kushangaza kuona makanisa ya kiinjili ambapo ni mistari michache tu ya maandiko husomwa wakati wa ibada. Maandiko yanapaswa kuwa kipaumbele katika ibada yetu. Kupitia nyimbo zinazotokana na maandiko, usomaji wa Biblia, au ufafanuzi makini wa maandiko katika mahubiri, tunapaswa kujulikana kama “watu wa Kitabu.” Biblia lazima iendelee kuwa na nafasi ya katikati katika ibada yetu.

Kujipima

Jiulize, “Je, ibada yangu inajumuisha kila kipengele kilichokuwa sehemu ya ibada ya kanisa la kwanza?”

Ufunuo: Ibada kama Kumuabudu Mungu kwa Upendo wa Dhati

Ibada ni kiini cha ujumbe wa Ufunuo.

  • Yohana alikuwa katika Roho siku ya Bwana aliposikia sauti ya Alfa na Omega (Ufunuo 1:10).

  • Mojawapo ya mada kuu za Ufunuo ni tofauti kati ya wale wanaomwabudu Yehova kwenye kiti chake cha enzi na wale wanaomwabudu mnyama.

  • Ufunuo unaahidi kwamba Mungu atashinda maadui zake, na mataifa yote yatakuja na kumwabudu mbele zake (Ufunuo 15:4).

[1]Kuelewa ibada katika Ufunuo, ni muhimu kupitia hali ya kihistoria ya kitabu hiki. Wakristo wa karne ya kwanza walikabiliana na madai mawili yanayopingana. Kwa upande mmoja, walijua kwamba Yesu Kristo ni Bwana (Wafilipi 2:11). Imani kwa Kristo inahitaji kujitolea kwa mamlaka na ubwana wa Yesu Kristo. Kwa upande mwingine, Ruma ilihitaji kila mtu chini ya mamlaka ya himaya kushuhudia kwamba Kaisari alikuwa bwana na mungu wao.

Ilikuwa haiwezekani kwa Wakristo kutoa utii wa mwisho kwa yeyote isipokuwa Mungu. Mizizi ya mgogoro kati ya Roma na Wakristo wa karne ya kwanza ilikuwa, "Nani anastahili kuabudiwa?" Katika hali hii, Ufunuo unasema, "Yesu ni Bwana." Hata katika dunia isiyotambua mamlaka yake, Yesu ni Bwana. Anastahili kuabudiwa. Ufunuo unatoa picha ya ibada ya kweli.

Ibada ya Kimbinguni Ikilinganishwa na Ibada Iliyoshindwa

Ufunuo unaanza na ujumbe kwa makanisa saba ya Asia Ndogo. Asia Ndogo ilikuwa mojawapo ya vituo vikali vya ibada ya mfalme. Kulikuwa na mahekalu ya kifalme katika kila mojawapo ya miji iliyotajwa katika Ufunuo. Ibada ya mfalme ilikuwa ni karibu ya kila mahali katika Roma.

Ujumbe kwa makanisa saba unaonesha kushindwa kwa ibada katika makanisa kadhaa. Ingawa makanisa yote saba yanamwabudu Mungu, makanisa matano yanakaripiwa. Karipio hizi zinaonesha kwamba makanisa haya yalishindwa kumwabudu Mungu kwa namna inayokubalika.

1. Ukosefu wa upendo unazuia ibada ya kweli. Waefeso walifanya mambo mengi vizuri, lakini walikuwa wameacha upendo wao wa kwanza. Kuwa na mikono mitupu katika ibada kunaweza kuwa ishara kwamba tumepoteza upendo wetu kwa Mungu tunayemwabudu.

2. Mafundisho ya uongo yanazuia ibada ya kweli. Pergamo na Thiatira walivumilia mafundisho ya uongo. Hatari hii inaweza kuonekana katika makanisa yanayobadilishana ishara na maajabu kwa ukweli wa kibiblia.

3. Matendo yaliyokufa yanazuia ibada ya kweli. Mji wa Sardi ulikuwa umeshindwa mara mbili wakati walinzi waliolala walishindwa kuona adui anayekuja.[2] Yohana alionya kwamba kanisa la Sardi lilikuwa linalala kwa sababu lilitegemea kazi zake nzuri. Kukutana na Mungu katika ibada kungeamsha Sardi kutoka kwenye utepetevu wake.

4. Ukosefu wa shauku unazuia ibada ya kweli. Laodikia ilionesha roho ya uvuguvugu ambayo kanisa limeona mara nyingi katika nyakati za ustawi. Ukosefu wa shauku wa Walaodikia ulisababishwa na utajiri wao na kujitegemea. Ibada ya kweli inatukumbusha utegemezi wetu kwa Mungu.

Ibada ya Mbinguni Inamlenga Mungu

Ufunuo 4-5 inaonesha kwamba ibada ya mbinguni inamlenga Mungu na utukufu wake. Waabudu wa mbinguni wanamwabudu Mfalme wa Milele na Mwanakondoo aliyefufuka.

Je, unaweza kumwazia malaika akimwambia Yohana, “Kuna kitu chochote tunaweza kubadilisha ili uwe na faraja zaidi katika ibada?” Bila shaka hapana! Ibada inamhusu Mungu, sio mimi. Ibada inambariki mwabudu lakini hilo siyo lengo kuu la ibada. Lengo la ibada ni kumheshimu Mungu. Waabudu waliomzunguka kiti cha enzi cha Mungu wanaimba wimbo wa kumsifu Mungu:

Matendo yako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi; Ni za haki, na za kweli, njia zako, Ee Mfalme wa mataifa. Ni nani asiyekucha, Ee Bwana, na kulitukuza jina lako? Kwa kuwa wewe peke yako u Mtakatifu; kwa maana mataifa yote watakuja na kusujudu mbele zako; kwa kuwa matendo yako ya haki yamekwisha kufunuliwa (Ufunuo 15:3-4).

Ibada ya mbinguni hufanyika mbele za Mungu. Tangu wakati Adamu na Hawa walipofukuzwa kutoka bustanini, mwanadamu ametenganishwa na Mungu. Mbinguni, ibada itafanyika tena mbele za Mungu bila ushawishi wowote wa uovu.

Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. (Ufunuo 21:3).

Ibada ya Mbinguni Inaonesha Ukweli Halisi

Yohana alikuwa uhamishoni kwenye kisiwa cha Patmo, alipoandika Ufunuo. Wakristo kote katika Dola la Roma walikuwa wakiteseka kwa ajili ya imani yao. Kutoka mtazamo wa duniani, siku zijazo zilikuwa na giza. Hata hivyo, Ufunuo unaonesha mtazamo wa mbinguni juu ya matukio ya duniani.[3]

Duniani, tunaona upande mmoja tu wa historia. Tunajaribiwa kufikiri kwamba dunia inayotuzunguka ndiyo ukweli halisi. Ibada na mbingu zinaonekana kuwa mbali na mapambano ya dunia halisi. Mionekano ya ibada ya mbinguni inayoonekana katika Ufunuo 4, 5, na 15 inaonesha picha ya dunia halisi.

Kwa wafanyakazi wa Kikristo, Ufunuo ni ukumbusho muhimu kwamba mapambano ya dunia hii ni ya muda mfupi. Ibada siyo kimbilio la kila wiki kutoka kwenye ukweli; badala yake, ibada inaonesha ukweli kutoka mtazamo wa Mungu - na hili linabadilisha mtazamo wetu wa dunia yetu. Katika Ufunuo, Mungu anasema, “Mambo siyo kama yanavyoonekana kuwa. Mambo hayapo nje ya udhibiti, Shetani hajashinda, uovu haujashinda. Tazama kupitia mlango na upate kuona ukweli. Mungu yuko kwenye kiti chake cha enzi.”[4]


[1]

"Kamilisha uumbaji Wako mpya,
Utu safi usio na doa utufanye tuwe;
Tuweze kuona wokovu wako mkuu,
Ulio timilika kikamilifu ndani Yako:
Tukibadilishwa kutoka utukufu hadi utukufu,
Hadi tupate nafasi yetu mbinguni,
Tukiimba na kutupa taji zetu mbele Yako,
Tukizama katika mshangao, upendo na sifa!"

- Charles Wesley

[2]Hii ilitokea Koresh aliposhambulia mwaka 547 K.K. na tena Antiochus III alishambulia mwaka 214 K.K.
[3]Kwa mfano: 6:1-7:8 yapo duniani; 7:9-8:6 ni mbinguni. 8:7-11:14 ni duniani; 11:15-19 ni mbinguni.
[4]David Jeremiah. Worship. (CA: Turning Point Outreach, 1995), 72

Ibada ya kibiblia siku hizi

“Amefufuka!” “Yeye ni Bwana!” Matamko haya ni muhimu kwa ibada. Ni ufufuo uliomtangaza Yesu kuwa Bwana (Warumi 1:4).

Kanisa la kwanza liliitambua kila Jumapili kama sherehe ya Ufufuo; kila Jumapili ilikuwa Pasaka. Wakristo hawakufunga siku ya Jumapili; Jumapili ilikuwa siku ya sherehe.

Leo, ibada yetu inapaswa kuwa wakati wa sherehe. Ndiyo, kuna uzito unaohusishwa na kuingia mbele za Mwenyezi, lakini pia kuna furaha tunaposherehekea Bwana aliyefufuka. Ibada yetu inapaswa kujumuisha fursa za kusherehekea.

Ibada inajumuisha nyimbo za sifa na shuhuda za neema ya Mungu katika maisha ya washiriki. Kanisa moja nchini Nigeria husherehekea wanapotoa sadaka. Washiriki huandamana kuzunguka kanisa sadaka inapo kusanywa. Waabudu hawa wanajua furaha ya Ufufuo. Ibada lazima ijumuishwe na fursa za kusherehekea ushindi tuliopata kupitia ushindi wa Kristo juu ya kifo.

Kujipima

Jiulize, "Je, ibada yangu ni sherehe au ni wajibu tu? Je, ninafurahia kuingia kwenye ibada, au nahudhuria ibada kwa sababu tu ni wajibu wangu kama Mkristo?"

Weka katika Vitendo

"Chukua muda kutafakari juu ya Mungu tunayemwabudu. Fikiria kile maandiko yanayotuambia kumhusu."[1]

Mungu ni Nani katika Maandiko
Katika Mwanzo Yeye ni Muumba wa Ulimwengu.
Katika Kutoka Yeye ni Mwanakondoo wa Pasaka.
Katika Mambo ya Walawi Yeye ni Dhabihu Kamilifu
Katika Hesabu Yeye ni Wingu
Katika Kumbukumbu la Torati Yeye ni Nabii wa Kweli.
Katika Yoshua Yeye ni Jemadari wa Jeshi la Bwana
Katika Ruthu Yeye ni Mkombozi wa Ukoo.
Katika 1 na 2 Samweli Yeye ni Nabii.
Katika Mambo ya Nyakati Yeye ni Hekalu la Mbinguni
Katika Ayubu Yeye ni Mpatanishi
Katika Zaburi Yeye ni Mchungaji.
Katika Isaya Yeye ni Mkuu wa Amani.
Katika Ezekiel Yeye ni Mwana wa Adamu.
Katika Hosea Yeye ni Mponyaji wa Wale Wanaorudi Nyuma.
Katika Hagai Yeye ni Tamaa ya Mataifa Yote
Katika Malaki Yeye ni Jua la Haki.
Katika Mathayo Yeye ni Masiya Aliyeahidiwa.
Katika Marko Yeye ni Mtumishi.
Katika Luka Yeye ni Mwana wa Adamu.
Katika Yohana Yeye ni Neno.
Katika Warumi Yeye ni Yule Anayehesabia Haki.
Katika Wafilipi Yeye ni Furaha Yetu.
Katika Wakolosai Yeye ni Utimilifu wa Uungu.
Katika Waebrania Yeye ni Kuhani Mkuu.
Katika 1 & 2 Petro Yeye ni Mchungaji Mkuu wa Kondoo
Katika Ufunuo Yeye ni Mwanakondoo Aliyechinjwa, Mfalme wa Wafalme, na Bwana wa Mabwana!

[1]Jedwali lifuatalo limechukuliwa kutoka kutoka kwaVernon Whaley, Called to Worship. (Nashville: Thomas Nelson, 2009), 331-333.

Hitimisho: Ushuhuda wa Mtume Yohana

Jina langu ni Yohana. Maisha yangu yamebadilishwa na ibada. Tangu nilipokutana na Yesu wa Nazareti kwa mara ya kwanza, nimekuwa mwabudu.

Nilikuwepo kwenye Mlima wa Mabadiliko. Tulisikia sauti kutoka mbinguni, tukaona utukufu wake, na tukaanguka kifudifudi kwa hofu (Mathayo 17:6). Tuliabudu bila ukamilifu. Matendo yetu wakati wa Wiki ya Mateso yalionesha kwamba hatukuelewa kabisa yale tuliyoona mlimani.

Nilikuwepo mlimani Galilaya Yesu alipoonekana baada ya kufufuka. Tuliabudu, ingawa wengine walikuwa na mashaka (Mathayo 28:17). Tuliabudu kusiko na kamilifu. Tulijua kwamba amefufuka, lakini hatukuwa tumeelewa kikamilifu maana yake yote.

Nilikuwepo katika chumba cha juu tulipojitolea kwa maombi kwa moyo mmoja (Matendo ya Mitume 1:14). Tulipoabudu, Roho Mtakatifu alitujia. Ibada ikawa kichocheo cha uinjilisti; tulipeleka injili Yerusalemu, Yudea na Samaria, na hata mwisho wa dunia.

Nilipokuwa uhamishoni katika kisiwa cha Patmo, nilikuwa katika Roho siku ya Bwana niliposikia sauti kuu kama tarumbeta. Ilikuwa sauti ya Alfa na Omega, wa kwanza na wa mwisho (Ufunuo 1:10-11).

Nilikuwepo wakati Mungu alipofungua mlango mbinguni na kuniruhusu kuona ibada kuzunguka Kiti cha Enzi cha Mungu.

Nitakuwa milele katika Yerusalemu mpya, ikishuka kutoka kwa Mungu kutoka mbinguni (Ufunuo 21:2). Katika mji huo, ibada yetu hatimaye itakuwa kamilifu kwa sababu tutauona uso wa Yule tunayeabudu. Mbinguni, “maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao” (Ufunuo 21:3).

Mimi ni Yohana. Na nitatumia umilele wote kumwabudu Mungu wangu na Mkombozi wangu!

Weka katika Vitendo

Kabla ya kumaliza somo hili, chukua muda kuabudu. Soma nyimbo za Ufunuo 4, 5, na 15 au Zaburi 19. Imba wimbo unaomsifu Mungu. Omba maombi ya kumsifu Mungu. Sikiliza Mungu anapozungumza nawe. Chukua muda wa kumwabudu Mungu hasa.

Majadiliano ya kikundi

► Kwa matumizi ya vitendo vya somo hili, jadilini yafuatayo:

Tim anachunga kanisa ambalo lina shauku kubwa ya uinjilisti. Waamini wapya wanabatizwa kila mwezi. Ni wakati wa kusisimua katika kanisa.

Hata hivyo, Tim anahofia kwamba kanisa halijaabudu hasa. Mahubiri mengi yanalenga wasioamini na waongofu wapya. Ni vigumu kutumia nyimbo kuu za kitabuni kwa sababu watu wapya hawazijui nyimbo hizo. Tim anaogopa kwamba kanisa lake litakuwa kubwa kwa ukubwa lakini lina kina kidogo kiroho. Anataka kujikita zaidi kwenye ibada. Jadili jinsi Tim anavyoweza kudumisha msisitizo wa uinjilisti huku pia akikuza kina cha ibada katika kanisa.

Mapitio ya Somo la 4

Mapitio ya Masomo Yote

(1) Injili zinaonesha kwamba ibada inakamilishwa katika Yesu Kristo:

  • Yesu alitoa mfano wa ibada.

  • Yesu alikataa majaribu ya ibada ya uongo.

  • Yesu alionyesha umuhimu wa maombi.

  • Yesu ataabudiwa milele.

(2) Matendo ya Mitume yanaonesha uhusiano kati ya ibada na uinjilisti.

  • Ibada ya kweli inachochea uinjilisti.

  • Uinjilisti wenye ufanisi huunda waabudu.

  • Ibada ambayo haituongozi kwenye uinjilisti itakuwa ya kujishughulisha binafsi.

(3) Nyaraka zinaonesha vipengele muhimu vya ibada katika kanisa la kwanza. Ibada katika kanisa la kwanza ilijumuisha:

  • Kusoma Maandiko

  • Kuhubiri Neno

  • Maombi ya pamoja

  • Kuimba

  • Sadaka

  • Ubatizo

  • Meza ya Bwana

(4) Ufunuo unaonesha kwamba ibada ni kumsifu Mungu.

  • Ibada inabariki mwabudu, lakini hiyo si lengo kuu la ibada.

  • Lengo kuu la ibada ni kumletea Mungu heshima.

  • Ibada ya mbinguni inatukumbusha kwamba dunia tunayoiona haina ukweli wa mwisho.

Somo la 4 Mazoezi

(1) Orodhesha kanuni tatu za ibada kutoka somo hili. Kwa kila kanuni, andika aya moja ikijadili njia za vitendo za kutumia kanuni hiyo katika kanisa lako.

(2) Mwanzoni mwa somo lijalo, utapewa mtihani unaotokana na somo hili. Soma maswali ya mtihani kwa makini ili kujiandaa.

Jaribio Somo la 4

Majaribio ya Masomo Yote

(1) Orodhesha njia tatu ambazo Yesu alionesha ibada ya kweli.

(2) Mafundisho na mfano wa Yesu yanatukumbusha nini kuhusu ibada ya kweli?

(3) Kauli mbili zinazofupisha uhusiano kati ya ibada na uinjilisti ni zipi?

(4) Ibada ya uongo ya Athene inaelezwaje katika Matendo 17?

(5) Mungu wa kweli anaelezwaje katika Matendo 17?

(6) Orodhesha vipengele vitano vya ibada ya kanisa la kwanza katika Nyaraka.

(7) Orodhesha mifano miwili ya vizuizi vya ibada vilivyopatikana miongoni mwa makanisa ya Asia Ndogo.

(8) Andika Warumi 12:1-2 kwa kukariri.

Next Lesson