James anathamini ibada ya kimapokeo. Katika mkutano wao wa kila mwezi Enoch, ambaye anaongoza ibada ya kisasa, aliuliza, “Kwa nini usijaribu jambo jipya katika ibada zako?”
“Sisi ni wa kibiblia,” James alijibu. “Ikiwa Biblia haiamuru desturi fulani ya kuabudu, hatuko huru kuiongeza tu kwenye mazoea ya ibada ya kanisa la kwanza. Sisi ni nani kubadili ibada ya kibiblia? Katika kanisa letu, tunaimba zaburi pekee. Nyimbo hizo zilikuwa nyimbo za kanisa la kwanza; zinatufaa!”[1]
Enoch alijibu, “Inaonekana kwangu kana kamba unadhani historia ilikoma mwishoni mwa kitabu cha Ufunuo. Je, tunawezaje kujizuia na mtindo wa kuabudu ambao una miaka 2,000? Maadamu Biblia haijazuia desturi fulani, na desturi hiyo haigawanyi kanisa, tunapaswa kurekebisha ibada kulingana na mahitaji ya kizazi chetu. Katika kanisa langu, tunaimba nyimbo nyingi mpya. Kama Mungu angependa kuzuia nyimbo mpya, Biblia ingekataza waziwazi.”[2]
Jibu la Jason lilikuwa la vitendo. “Tumejifunza yale ambayo Biblia inasema kuhusu ibada. Tunajua kanuni za ibada kutoka kwenye Maandiko. Tunahitaji kuona jinsi Wakristo wengine wametumia kanuni hizi katika kila kizazi. Je, ibada inaonekanaje katika historia ya kanisa?”
Jason anaelewa kanuni muhimu tunapojadili ibada. Ingawa kanuni za kibiblia za kuabudu hazibadiliki, kila uzoefu wa ibada katika Biblia ni tofauti. Maelezo yanatofautiana; vipengele muhimu vya ibada vinabaki vile vile. Tumeona kanuni muhimu za ibada katika masomo mawili yaliyopita, lakini maelezo yanabadilika. Zingatia:
Ibrahimu alikuwa kwenye mlango wa hema lake alipokuwa akiabudu. Mtu anaweza kusoma hii na kusema, “Ibada ya kweli huanzia ukiwa nyumbani.” Lakini …
Isaya alikuwa Hekaluni alipomwona Bwana akiinuliwa. Mtu anaweza kusoma hii na kusema, “Ibada ya kweli hutokea ukiwa kanisani.” Lakini …
Ayubu alifunikwa na majipu kuanzia kichwani hadi miguuni aliposema, “Nilikuwa Nimesikia habari zako kwa kusikia kwa masikio, bali sasa jicho langu linakuona” (Ayubu 42:5). Mtu anaweza kusoma hii na kusema, “Aha! Ibada ya kweli hutokea ukiwa na huzuni.”
Je, unaona hoja? Ibada hufanyika katika hali nyingi tofauti, kwa njia nyingi tofauti, na kufuata mifumo mingi tofauti. Mara nyingi tunachanganya mabadiliko ya hali ya ibada na kanuni zisizobadilika.
Katika somo hili, tutaona jinsi kanisa limetumia kanuni za ibada katika historia. Hilo litakupa ufahamu wa njia mbalimbali ambazo watu wa Mungu huabudu. Tunatumahi hii itakusaidia kuona kwamba hakuna mtindo mmoja wa ibada ambao lazima ufuatwe na watu wote katika hali zote. Badala yake, lazima tutafute mwongozo wa Roho wa Mungu ili kuamua jinsi ya kutumia kanuni za kibiblia za ibada kwa hali yetu.
Katika somo hili, tutaona pia jinsi ibada zetu huakisi imani zetu. Mazoea yetu ya ibada huathiriwa na imani yetu kuhusu Mungu na jinsi tunavyomfikia.
Ufahamu huu ni muhimu unapofanya maamuzi kuhusu ibada. Je, unaendesha ibada yako kwa njia inayowasilisha imani yako, au unaiga tu muundo wa kanisa lingine? Ikiwa unaiga kanisa lingine, lazima uhakikishe kwamba unashiriki imani ya kanisa hilo kuhusu Mungu na jinsi tunavyomfikia. Kuabudu kwetu kunaonyesha kile tunachoamini.
► Kabla ya kuendelea na somo hili, jadili huduma zako za ibada za sasa. Kama mtu hajui chochote kuhusu mafundisho yako, je, mtindo wako wa ibada ungezungumza nini kwao? Wangejifunza nini kuhusu mtazamo wako kwa Mungu, mtazamo wako kuhusu uhusiano wetu na Mungu, na mtazamo wako wa uinjilisti kama matokeo ya huduma yako ya ibada?
[1]Hii inaitwa "kanuni ya udhibiti" ya ibada. Iliyofundishwa na John Calvin, inakataza mazoea yoyote ya kuabudu ambayo hayajaanzishwa katika Maandiko. Hapo awali, hii ilizuia muziki wowote wa ala za muziki (kwakuwa ala za muziki hazijatajwa katika ibada ya Agano Jipya) au matumizi ya nyimbo zozote isipokuwa Zaburi. Baadhi ya makanisa yanayofuata kanuni hii leo yameongeza ala za muziki na nyimbo; lakini wanaendelea kuepuka mbinu mpya zaidi za kuabudu.
[2]Hii inaitwa "kanuni ya kawaida" ya ibada. Mbinu hii inafundisha kwamba ibada zozote ambazo hazijakatazwa katika Maandiko zinaruhusiwa, mradi tu hazivurugi amani na umoja wa Kanisa.
Picha ya Ibada katika Karne ya Pili
Picha yetu ya kwanza ya ibada baada ya Agano Jipya inakuja katika barua kutoka A.D. 113. Pliny, gavana wa Bithinia, alielezea ibada ya Kikristo katika barua kwa Mfalme Trajan.[1] Aliandika kwamba Wakristo, “hukusanyika siku iliyotajwa kabla ya mapambazuko na kuimba kwa kupokezana wimbo kwa Kristo kama kwa mungu, na kwamba waape… Usiibe, usidanganye, wala usizini …. Ni kawaida yao kuachana na kurudi baadaye kula chakula pamoja.”
Kulingana na Pliny, Wakristo walikutana kabla ya jua kuchomoza siku ya Jumapili ili kuimba nyimbo na kuahidi maadili mema, pengine kwa kuitikia usomaji wa Maandiko. Baadaye mchana, walikula chakula, ambacho huenda kilijumuisha meza ya Bwana.
Miaka arobaini baadaye, Justin mfia dini alitoa maelezo ya kina zaidi kuhusu ibada.[2] Justin aliandika ili kutetea ibada ya Kikristo kwa mfalme wa kirumi ambaye aliwatuhumu Wakristo kwa ukosefu wa maadili na ukosa uaminifu kwa mfalme. Justin alimhakikishia mfalme kwamba ibada ya Kikristo haikuwa tishio kwa Warumi. Kulingana na Justin, ibada ya Kikristo ilijumuisha mambo yafuatayo:
1. Usomaji wa Maandiko.
2. Mahubiri kutoka kwa Kiongozi wa Kutaniko.
3. Maombi. Watu binafsi waliomba kimya kimya; kisha kiongozi akaongoza maombi rasm, ambayo watu waliitikia, “Amina.” Mwisho wa maombi, waumini walisalimiana kwa busu takatifu kuashiria uwepo wa Roho Mtakatifu.
4. Ibada ilihitimishwa kwa kushiriki meza ya Bwana. Baada ya ibada, mashemasi wawili walichukua mikate na divai iliyobaki na kupeleka kwa Wakristo waliokuwa wagonjwa au waliokuwa gerezani wakingoja kuuawa.
5. Mwishoni mwa ibada, wale waliokuwa na pesa au chakula walileta zawadi zao kwa kiongozi. Sadaka zilipelekwa kwa “mayatima na wajane, walio na uhitaji kwa sababu ya ugonjwa au sababu nyingine yo yote, na wafungwa na wageni kati yao.”
Moja ya nguvu za ibada ya karne ya pili ilikuwa ushiriki wa waumini. Wote wawili Pliny na Justin Martyr wote walielezea ibada rahisi, itofauti kabisa na mila ya kitamaduni iliyoenea katika dini za siri za kipagani za Rumi. Ibada ilikuwa ya kina, huku vikundi vidogo vilipokusanyika katika nyumba za watu.
Nguvu nyingine ilikuwa uhusiano wa wazi kati ya ibada na maisha. Barua ya Pliny inataja kujitolea kwa Mkristo kuhusu tabia ya maadili; Justin Martyr anataja zawadi za kuwasaidia wahitaji. Ibada ilihusisha maisha yote.
► Ni mambo gani ya ibada katika karne ya pili yanaweza kunufaisha ibada yako? Je, unaona hatari yoyote katika ibada ya karne ya pili?
Kwa ajili ya picha ya pili ya ibada, nenda kwenye karne ya 12. Katika miaka iliyofuata, Ukristo ulikuwa dini rasmi ya Dola Takatifu ya Rumi. Baada ya Amri ya Konstantino ya Milan mwaka 313 B.K., waumini walianza kujenga majengo makubwa ya kanisa. Makanisa mengi makubwa ya Ulaya yalijengwa wakati wa miaka hii 1,000.
Katika zama za Kati, ibada ilizidi kuwa kubwa. Kwa upande mzuri, ibada ya kanisa kuu ilionyesha ukuu wa Mungu. Dirisha za vioo vya rangi zilionyesha matukio ya kibiblia kwa wale ambao hawakuweza kusoma. Kwaya ziliimba nyimbo nzuri. Ibada ilikuwa ya ajabu na nzuri.
Udhaifu wa Ibada katika Zama za Kati
Urembo ulikuwa muhimu zaidi kuliko hali ya kiroho.
Matumizi wa mambo yenye kupendeza kwa ajili ya ibada ulitiliwa mkazo: uvumba, muziki wa fahari ulioimbwa na waimbaji waliofunzwa, kengele, na mavazi ya pekee kwa ajili ya makuhani. Sanaa ikawa muhimu zaidi kuliko ya kiroho.
Watu hawakuweza kuelewa Ibada.
Ibada hiyo ilikuwa katika Kilatini, lugha ambayo watu wachache waliielewa. Wachungaji wengi wa eneo hilo hawakuzoezwa sana kuhubiri mahubiri. Maombi yalikuwa ni sehemu ndogo ya vifungu kutoka vyanzo vingi tofauti na mara nyingi havikuwa vinaeleweka.
Watu walikuwa watazamaji, si waabudu halisi.
Kulikuwa na ushiriki mdogo wa watu. Waumini walikuwa kundi la watazamaji waliokuwa wakitazama tamthilia, yaani Misa. Makasisi walikuwa wakitekeleza matukio ya ibada huku hadhira ikitazama. Kitovu cha ibada kilikuwa Ushirika Mtakatifu badala ya Maandiko Matakatifu.
Kanisa Katoliki lilifundisha kwamba mkate na divai viligeuzwa kuwa mwili na damu halisi ya Kristo (Hili linaitwa fundisho la kugeuka kwa mkate na divai). Watu wengi wa kawaida walifanya meza ya Bwana tu wakati wa Pasaka pekee. Kuhani alikunywa divai na kushiriki mkate tu na waumini.
Injili ilibadilishwa na taratibu.
Ibada zetu hutengeneza imani zetu. Tunaona kanuni hii ikifanya kazi katika Zama za Kati; Ibada ya Kikatoliki ya Kirumi ilitengeneza theolojia yao. Mungu alionekana kuwa mbali na maisha ya wanadamu. Watu wa kawaida hawakuhisi wanaweza kumkaribia Mungu; badala yake, waliweza kuzungumza na Mungu kupitia kuhani pekee. Kuhani akawa mpatanishi kati ya Mungu na mwanadamu.
Nguvu ya ibada katika Zama za Kati ilikuwa katika hali yake ya ukuu na hofu mbele za Mungu. Kupitia usanifu wa majengo, muziki, maigizo, na sanaa nzuri, ibada ilidhihirisha utukufu wa Mungu.
Hata hivyo, udhaifu wa ibada katika Zama za Kati ulizidi nguvu zake. Mkristo wa kawaida alikuwa mtazamaji tu katika ibada. Kwa njia nyingi, ibada ya Zama za Kati ilikuwa ni mkengeuko wa kusikitisha kutoka kwa ibada ya Agano Jipya.
Hatari za Ibada: Ibada Isiyo na Maana
Ni lazima tuchukue muda kufundisha waumini wetu kwa nini tunaabudu jinsi tunavyofanya, vinginevyo mapokeo yenye maana yanaweza kuonekana kuwa hayana maana kwa waabudu.
Muumini mmoja mpya alimuuliza mchungaji wake, “Kwa nini tunasema ‘Amina’ mwishoni mwa maombi? Je, ‘Amina’ ni neno la miujiza linalomfanya Mungu afanye tunachomwomba?” Mchungaji alitambua kwamba anapaswa kutoa melezo kuhusu ibada. Kitu rahisi kama "Amina" kinaweza kukosa maana ikiwa hatufundishi waumini wetu kuhusu ibada.
Sio lazima kuondoa ishara na siri kwenye ibada. Suluhisho ni kufundisha waumini maana ya mazoea yetu kuhusu ibada. Wanapaswa kujua kwa nini tunatumia lugha tunayotumia; wanapaswa kujua kwa nini uimbaji wa pamoja kanisani ni muhimu kwa waumini; wanapaswa kujua nini maana ya Maandiko.
► Ni mambo gani ya ibada katika Zama za Kati yanaweza kunufaisha ibada yako? Je, unaona hatari yoyote katika ibada ya Zama za Kati?
Picha ya Ibada katika Matengenezo ya Kanisa
Wanamatengenezo walijua kuwa ibada yetu inaathiri theolojia yetu. Kwa sababu hii, walijua kwamba kweli za kitheolojia za matengenezo zingepotea kama ibada isingeakisi theolojia ya matengenezo.
Jambo kuu la kitheolojia la Wanamatengenezo lilikuwa ni ukuhani wa mwamini. Hii ina maana kwamba waumini wanamwabudu Mungu moja kwa moja; hatupitii kwa kuhani. Wanamatengenezo pia waliamini sana kwamba Neno la Mungu lazima lipatikane kwa kila mwamini.
Ibada katika Matengenezo ya Kanisa ilihusisha kila mwabudu. Ibada ilikuwa katika lugha ya watu, si Kilatini. Maandiko yalisomwa na kuhubiriwa ili waabudu wote waweze kuelewa Neno la Mungu katika lugha yao wenyewe. Wimbo wa waumini uliruhusu kila mwabudu kushiriki katika ibada. Martin Luther alikuwa mwandishi wa nyimbo, na nyimbo zake zinahesabiwa kuwa zilisaidia kueneza Matengenezo ya Kanisa.
Zaidi ya maeneo haya ya kawaida, kulikuwa na kutokubaliana kwingi kati ya Wanamatengenezo kuhusu ibada. Walutheri na Waanglikana walidumisha sehemu kubwa ya sherehe za Kanisa Katoliki la Roma. Luther aliamini kwamba, isipokuwa kama yamekatazwa katika Maandiko au yalileta migogoro kanisani, desturi mpya ya kuabudu zinapaswa kuruhusiwa.
Kelvin na wafuasi wake walishikilia baadhi ya taratibu lakini walikataa desturi za ibada ambazo hazijazungumziwa haswa katika Maandiko. Kelvin alihimiza uimbaji wa waumini, lakini uimbaji wa zaburi pekee. Aliamini kwamba “Neno la Mungu pekee ndilo linalostahili kuimbwa katika sifa za Mungu.”[1] Alirudi kwenye Ibada ya Ushirika ya waumini, akipendekeza kwamba Meza ya Bwana iandaliwe angalau mara moja kwa mwezi na ikiwezekana kila jumapili.
Waanabaptisti na Wapuritani walikataa sehemu kubwa ya taratibu na kurejea kwenye aina rahisi ya ibada. Wakati mwingine watu hawa waliabudu katika nyumba za kibinafsi na kujiona kuwa wao pekee ndio hufuata ibada ya karne ya kwanza kwa usahihi.
Nguvu ya ibada ya Matengenezo ilikuwa ni kurudi kwa ushiriki wa waumini. Ingawa kulikuwa na tofauti kati ya makanisa mbalimbali ya Matengenezo, Wanamatengenezo wote walitafuta kuiga ukuhani wa mwamini katika ibada.
► Ni mambo gani katika ibada ya matengenezo yanaweza kunufaisha ibada yako? Je, unaona hatari yoyote katika ibada ya Matengenezo ya Kanisa?
[1]Imenukuliwa kwa Donald P. Hustad, Jubilate II (Carol Stream: Hope Publishing Company, 1993), 194.
Picha ya Ibada Katika Makanisa Huru
Kufuatia Matengenezo ya Kanisa, makanisa fulani yalikataa udhibiti wa serikali. Makanisa haya, yanayoitwa "makanisa huru" yalihusisha Anabaptisti, Wapuriti, Wasiofuata kanuni, Wanaojitenga, na Waasi. Wengi wao pia walikataa liturujia na taratibu zilizowekwa.
Vipengele vya ibada ya Makanisa huru:
(1) Kuhubiri kulikuwa kwa sehemu kubwa.
(2) Ushiriki wa waumini ulikuwa muhimu.
Asili ya ushiriki wa waumini ulitofautiana kutoka kanisa hadi kanisa.
Katika baadhi ya makanisa, waumini waliimba nyimbo. Katika makanisa mengine, hakukuwa na uimbaji katika ibada ya pamoja.
Katika baadhi ya makanisa washirika wa ibada waliomba kwa sauti. Katika makanisa mengine padri aliomba kwa niaba ya watu.
Kulikuwa na tofauti ndogo kati ya waumini wa kawaida na viongozi wa kidini. Makanisa mengi ya huru hayakuwa na nguo maalumu za viongozi wa kidini.
(3) Ibada yote ilikuwa katika lugha ya watu.
Muhtasari wa ibada mnamo 1608 ni pamoja na yafuatayo (ibada ilidumu kwa masaa manne):
Maombi
Usomaji wa Maandiko (Sura ya 1-2 zenye maelezo)
Maombi
Mahubiri (ya saa moja au zaidi)
Michango inayozungumzwa na waumini wa kawaida
Maombi
Sadaka
Ibada haikutawaliwa tena na komunio na kuhani. Ibada za makanisa huru zilionekana zaidi kama ibada ya kanisa la Agano Jipya.
Kuna hatari katika njia hii ya ibada. Ijapokuwa makanisa huru yalifundisha ukuhani wa mwamini, katika vitendo mhubiri mara kwa mara alichukua nafasi ya padri kama kitovu cha ibada. Katika baadhi ya makanisa, kulikuwa na ushiriki mdogo wa waumini.
Labda moja ya hatari kubwa zaidi katika ibada ya makanisa huru ilikuwa hatari ya ubinafsi uliokithiri. Iwapo fundisho la ukuhani wa mwamini haliambatani na fundisho la umoja wa kanisa, kanisa linakuwa mkusanyo wa watu binafsi badala ya mwili wa Kristo uliounganishwa katika ibada. Hii inaonekana wakati ibada inahusu "Yesu na mimi" tu bila maana ya kanisa kama mwili.
► Ni vipengele vipi vya Ibada katika makanisa huru vinaweza kunufaisha ibada yako? Je, unaona hatari yoyote katika ibada ya makanisa huru?
Picha ya Ibada katika Uamsho wa Wesley
John Wesley aliathiriwa na mapokeo ya ibada ya pamoja aliyopokea kutoka kwa kanisa la Anglikana na pia kwa msisitizo wa uzoefu wa binafsi wa kiroho aliopata kupitia mapokeo ya Anabaptisti. Wakati ibada ya Anglikana ilipokuwa inafuata Kanisa Katoliki la zama za kati katika ibada zisizo na maana, Wesley na wafuasi wake (walioitwa Wamethodisti) walihuisha uhalisia wa ibada ambao uliwaleta waabudu mbele ya Mungu.
Vipengele vikuu vya ibada ya wamethodist wa mwanzo:
1. Kuhubiri. Kuhubiri ya John Wesley yalichapishwa na kuwa msingi wa mafundisho kwa waabudu wa Methodisti.
2. Ushirika wa mara kwa mara. John Wesley alishiriki meza ya Bwana wastani wa mara tano kwa wiki. Aliwahimiza wafuasi wake kushiriki meza ya Bwana angalau mara moja kwa wiki.
3. Kuimba nyimbo za dini. Nyimbo za Charles Wesley zilieneza mafundisho ya Kimethodisti kupitia Visiwa vya Uingereza na Ulimwengu Mpya.
4. Vikundi vidogo. Mikutano ya darasa ilikuwa muhimu kwa ufuasi wa Kimethodisti.
[1]5. Ibada ya ushirika. Wamethodisti walikutana pamoja mara kwa mara, na hata baada ya wachungaji wengi wa Kianglikana kuwakataa Wamethodisti, Wesley aliwahimiza wafuasi wake kuhudhuria ibada ya Kianglikana.
6. Uinjilisti. Maelfu ya waongofu wapya walimpokea Kristo wakati uamsho wa Kimethodisti ulipoenea kupitia Uingereza na kwingineko.
Ibada ya Kimethodisti ilijumuisha nyimbo ambazo zilimtukuza Mungu, uanafunzi uliojenga waumini waliokomaa, na kuhubiri ukweli uliotangaza kwa kanisa na kwa ulimwengu wenye uhitaji.
► Ni vipengele vipi vya ibada katika uamsho wa Wesley vinaweza kunufaisha ibada yako? Je, unaona hatari yoyote katika ibada ya uamsho wa Wesley?
Umethodisti ulizuka kutokana na kushindwa katika ibada ya karne ya kumi na nane.
“Sakramenti zilipokuwa pembeni
mwa maisha ya kanisa,
umethodisti wa kwanza iliwaweka kwenye
kituo; wakati bidii ya kidini ilikuwa
inapuuzwa, umethodisti alifanya
hamasa kuwa muhimu; mbapo
dini ilikuwa imezuiwa kwenye
makanisa, Umethodisti uliipeleka
mashamba na mitaani.”
- James White katika Robert Webber
Karne Ishirini za Ibada ya Kikristo
Picha ya Ibada katika Amerika ya Kwanza
Waingereza walikaa kwanza kwenye pwani ya mashariki ya nchi ambayo sasa inaitwa Marekani. Mwishoni mwa miaka ya 1700 na zaidi, watu waliendelea kuhamia magharibi katika eneo lisilo na utulivu ili kupata ardhi na kujenga nyumba. Watu walikutana na changamoto nyingi kama vile makanisa, shule, na utekelezaji wa sheria ulivyoendelea polepole. Katika historia, eneo hili ambalo lilitatuliwa polepole linaitwa Frontier ya Amerika.
Kusudi la kujifunza kuhusu ibada katika historia ya awali ya Marekani sio kuunga hoja mtindo wa Marekani kuwa kielelezo cha ibada zote, lakini kuilinganisha na ibada zinazokua za makanisa machanga katika sehemu zingine. Changamoto zilezile zinakabiliwa na makanisa mapya yaliyoanzishwa katika nchi nyingi.
Vipengele vya ibada katika Marekani ya kwanza:
1. Uhuru kutoka kwa madhehebu na aina rasmi za ibada. Makanisa ya mpakani mwa Marekani yalikuwa huru dhidi ya udhibiti wa madhehebu. Yalikuwa na umakini mdogo kuhusu taratibu na maagizo maalum ya ibada (ingawa John Wesley alirekebisha mtindo wake wa kuabudu kwa matumizi katika makoloni). Majengo ya kanisa na huduma za ibada zilikuwa rahisi na wazi.
2. Fursa adimu za meza ya Bwana. Huko Uingereza, akina Wesley walikuwa wamesisitiza umuhimu wa ushirika wa kawaida. Katika mipaka ya Marekani, upungufu wa mapadri waliowekwa rasmi ulionesha kwamba waumini walikuwa na nafasi ndogo ya kushiriki meza ya Bwana.
3. Kuhubiri kwa Neno. Kuhubiri kuliendelea kuwa mkazo wa kimsingi katika ibada. Hata wahubiri ambao hawajazoezwa walisoma mahubiri ya akina Wesley na wahudumu wengine. Kitovu cha kanisa kilikuwa mimbari, si meza ya Bwana. Mkazo mkubwa ulikuwa juu ya kuhubiri Neno.
4. Kuimba kwa uchangamfu. Kuimba kulikuwa kuchangamsha. Makanisa ya Marekani yaliimba nyimbo za Charles Wesley pamoja na nyimbo rahisi za ushuhuda kwa mtindo ambao ulikuwa rahisi kwa waumini wasio na elimu kujifunza.
5. Maombi, uinjilisti, na uamsho. Maombi hayakuwa rasmi na mara nyingi yaliongozwa na watu wa kawaida. Uinjilisti ulikuwa muhimu, na vipindi vya uamsho huko Marekani vilipelekea maelfu kuokoka. Mahubiri kwa kawaida yalifuatiwa na mwaliko kwa watu ambao hawajaokoka kujitokeza na kuomba sala ya toba. Msisitizo kuhusu utakatifu wa Kikristo ulienea Marekani kote, mwaliko uliwaita wasioamini kuokoka na waumini kujitakasa.
Kama ilivyo kwa mapokeo mengine, kulikuwa na uimara na hatari katika ibada hii. Uimara ulijumuisha ushiriki wamtu binafsi na shauku. Hatari ilijumuisha msisitizo kuhusu uzoefu wa kibinafsi na mkazo mdogo juu ya mafundisho. Ilikuwa rahisi kwa mafundisho ya uongo kuenea katika maeneo ya mipakani kwa sababu kulikuwa na uwajibikaji mdogo.
► Ni vipengele vipi vya ibada kwenye mpaka wa Marekani vinaweza kunufaisha ibada yako? Je, unaona hatari yoyote katika ibada ya kanisa la mpaka wa Marekani?
Hatari za Ibada: Kuchanganya Mabadiliko ya Mitindo na Kanuni Zisizobadilika
Mara nyingi tunajaribiwa kuchanganya mitindo ya ibada inayobadilika na kanuni zisizobadilika za ibada ya kibiblia. Fikiria:
Katika makanisa mengine, waabudu hupiga magoti kuonesha unyenyekevu wanaposali. Katika makanisa mengine, waabudu huinua mikono mitakatifu wanapoomba.
Katika makanisa mengine, kinanda hupigwa kwa upole wakati wa maombi. Katika makanisa mengine, kuna ukimya wakati mchungaji anaongoza maombi. Katika makanisa mengine, kila mtu huomba kwa sauti.
Katika makanisa mengine, nyimbo huoneshwa kwenye skrini. Katika makanisa mengine, watu huimba kutoka kwenye kitabu cha nyimbo.
Katika makanisa mengine, mchungaji husoma maandiko mwanzoni mwa mahubiri yake. Katika makanisa mengine, mshirika husoma maandiko kabla ya mchungaji kuhubiri. Katika makanisa mengine, kuna usomaji wa maandiko mawili au matatu.
Hakuna moja kati ya haya lililo kosa; ni masuala ya mitindo, si kanuni. Hatupaswi kufikiria kwamba njia yetu ndiyo njia pekee ya kibiblia. Ibada ya kweli si suala la mtindo; ni uwepo wa Mungu.
Kuna kanuni fulani ambazo hazibadiliki. Tumeziona kanuni hizi katika masomo ya ibada katika Biblia. Kanuni hizi si za hiari. Kama Wakristo, kanuni hizi hutuelekeza katika njia yetu ya kumkaribia Mungu.
Katika masomo machache yajayo, tutatazama mitindo ya ibada. Kanuni hazibadiliki; mitindo hubadilika katika maeneo na nyakati tofauti. Kwa sababu hii, tunapaswa kuwa na uvumilivu kwa wale wanaoabudu tofauti na sisi. Hii haimaanishi kwamba mitindo si muhimu; bali inamaanisha kwamba kuna urahisi zaidi wa kubadilika kuhusu mitindo kuliko kuhusu kanuni.
Oswald Chambers aliandika kuhusu kumpa Mungu nafasi katika maisha yetu. Hii inahusu ibada:
Kama watumishi wa Mungu, lazima tujifunze kumpa nafasi… Tunapanga, lakini tunasahau kumpa Mungu nafasi ya kuingia kama anavyochagua. Je, tutashangaa ikiwa Mungu atakuja kwenye mkutano wetu au kwenye mahubiri yetu kwa njia ambayo hatukuwahi kutarajia? Usimtafute Mungu aje kwa njia fulani, bali mtafute. Njia ya kumpa nafasi ni kumtarajia aje, lakini si kwa njia fulani...
Weka maisha yako katika hali ya kuwasiliana na Mungu mara kwa mara ili nguvu zake za kushangaza ziweze kuvunja mipaka wakati wowote. Ishi katika hali ya kutarajia kila wakati, na mpe Mungu nafasi ya kuja kama anavyoamua.[1]
Ibada inaonekanaje katika karne ya 21? Ni swali ambalo haliwezi kujibiwa kwa urahisi. Ibada katika karne ya 21 inachukua maumbo mengi tofauti. Makanisa mengine yanathamini desturi na mapokeo; makanisa mengine yanakataa desturi kwa ajili ya uhuru wa kibinafsi katika ibada.
► Ibada inaonekanaje katika kanisa lako? Ikiwa unasoma katika kikundi, jadilini tofauti na ufanano kati ya ibada katika makanisa yanayowakilishwa katika kikundi chenu.
Kwa wakati huu katika kozi hii, lengo la maelezo haya si tathmini. Swali si, "Je, tuko sahihi au tumekosea?" Swali ni rahisi, "Tunafanya nini katika ibada yetu?"
Sababu ya maelezo haya ni kuweka msingi kwa masomo yanayofuata. Mara baada ya kuwa na maelezo ya kile mnachofanya kwa sasa katika ibada, mnaweza kuanza kujiuliza, "Kwa nini tunafanya tunachofanya?" na "Tunawezaje kufanya vizuri zaidi?"
Maamuzi kuhusu ibada yanaakisi imani za kitheolojia. Vipengele katika ibada yetu vinaonesha tunachoamini kuhusu Mungu na jinsi tunavyohusiana naye; vipengele katika ibada yetu vinaonesha tunachoamini kuhusu kanisa na jinsi tunavyohusiana na kila mmoja; vipengele katika ibada yetu vinaonesha tunachoamini kuhusu waliopotea na jinsi ibada inavyoweza kuwafikia.
Hebu tuchukue mfano mmoja – kuimba kwa mkusanyiko.
Kutokuwepo kwa kuimba kwa mkusanyiko katika Kanisa Katoliki la Roma kulionesha imani kwamba watu wa kawaida hawakuweza kuelewa maandiko (ikiwa ni pamoja na maandiko yaliyokuwa yakiimbwa). Kama vile mtu wa kawaida hakuruhusiwa kusoma maandiko mwenyewe, mtu wa kawaida hakuruhusiwa kuimba nyimbo za ibada. Ibada ilifanywa na kasisi.
Mkazo wa kuimba kwa mkusanyiko wakati wa Matengenezo ulionesha imani ya Luther kwamba kila Mkristo anaweza kuabudu kama sehemu ya mwili wa Kristo.
Kukataa kwa Calvin kuruhusu nyimbo zaidi ya zaburi kulionesha imani yake kwamba ni Neno la Mungu pekee ndilo lililokubalika katika ibada.
Mkazo wa Wamethodisti katika kuimba kwa mkusanyiko na kufundisha mafundisho kupitia nyimbo ulionesha imani ya Wesleys kwamba kila muumini anapaswa kuimba na kwamba kile tunachoimba kinaathiri kile tunachoamini.
Urahisi wa kuimba kwa waimbaji wa mipakani ulionesha imani ya Wamethodisti kwamba wokovu ulikuwa kwa watu wote. Kwa sababu ya imani hiyo, walihusisha kila mtu katika kuimba kwa shauku.
Tunapoendelea na kozi hii, tutakuwa tukitazama vipengele vingi vya ibada. Swali lako la kwanza kuhusu ibada huenda likawa, "Je, ninapenda?" Hilo si swali muhimu. La muhimu zaidi ni, "Ibada yangu inasema nini kuhusu kile ninachoamini? Je, inaonesha uelewa sahihi wa Mungu na uhusiano wa mwanadamu naye?"
Ibada yetu inaumba kile tunachoamini, lakini pia ni kweli kinyume chake: imani zetu zinaumba jinsi tunavyoabudu.
Uzuri ulikuwa muhimu zaidi kuliko uadilifu wa kiroho.
Watu hawakuweza kuelewa huduma.
Watu walikuwa watazamaji, sio waabudu wanaoshiriki.
Injili ilibadilishwa na desturi.
(3) Katika Matengenezo:
Ibada ilionesha ukuhani wa muumini.
Ibada ilikuwa katika lugha ya watu.
Luther, Calvin, na Wapuritani walitofautiana kuhusu jukumu la desturi katika ibada.
(4) Katika Makanisa Huru baada ya Matengenezo:
Kuhubiri kulikuwa msingi.
Ushiriki wa waumini ulikuwa muhimu.
Mafundisho ya ukuhani wa muumini yalikuwa muhimu.
Ibada yote ilikuwa katika lugha ya watu.
Ubinafsi uliopitiliza ulikuwa hatari.
(5) Ibada za mapema za Wamethodisti zilitambulishwa na:
Msisitizo kwenye kuhubiri.
Msisitizo kwenye Ushirika wa mara kwa mara.
Msisitizo kwenye kuimba nyimbo za kiroho.
Msisitizo kwenye vikundi vidogo.
Msisitizo kwenye ibada ya pamoja.
Msisitizo kwenye uinjilisti.
(6) Ibada katika Amerika Mwanzoni:
Ilikuza ushiriki binafsi na shauku ya uinjilisti.
Wakati mwingine ilisisitiza uzoefu binafsi kwa gharama ya uadilifu wa mafundisho.
(7) Ibada yetu leo inaakisi imani zetu kuhusu Mungu na jinsi tunavyohusiana naye.
Somo la 5 Mazoezi
(1) Katika karne ya pili, Justin Mfia dini aliandika kuhusu ibada ya kanisa kwa mtu ambaye hakuwahi kuona ibada ya Kikristo. Andika aya 2-3 ambazo utaelezea ibada kwa mtu ambaye hajawahi kuhudhuria kanisa la kikristo. Fikiria kwa makini ni nini cha muhimu kuhusu ibada. Je, unawezaje kuelezea ibada zako kwa namna ambayo utawasilisha kile kilicho cha muhimu katika ibada?
Kama unajifunza ukiwa katika kikundi, jadiliana kuhusu majibu ya kila mtu katika kikundi chenu katika darasa litakalofuata.
(2) Kuanzia mwanzo wa somo lijalo, utafanya mtihani uliojikita kwenye somo hili. Jifunze maswali ya mtihani kwa umakini katika maandalizi.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.