► Je, unatoa muda gani wa kupanga kwa huduma ya ibada ya kila juma? Je, unalinganisha nyimbo na mahubiri? Je, aina hii ya upangaji ni muhimu au kupanga mapema kunazuia uhuru wa Roho Mtakatifu katika ibada?
Fikiria kuhusu mwanamke anayetayarisha chakula kwa ajili ya wageni maalum. Wageni wanapowasili kwa chakula cha jioni, mhudumu anasema, “Siamini katika kutumia muda mwingi kupika chakula. Hapa kuna mkate uliobaki, nyama na mboga. Mnaweza kuweka pamoja vile mnavyotaka.” Je, wewe ungefanya hivi kwa wageni maalum? Bila shaka hapana! Unataka kutoa kilicho bora kwako kwa ajili ya wageni wako.
Hebu fikiria mchungaji anayeleta ibada kama zawadi yake kwa Mungu. Anasema, “Siamini katika kutumia muda mwingi kupanga ibada. Ninataka kumpa Roho Mtakatifu uhuru wa kuzungumza kupitia mimi, kwa hivyo sitapanga chochote. Namuacha Roho aniongoze.”
Viongozi wengine wanaamini kwamba Roho Mtakatifu hawezi kufanya kazi kupitia mahubiri yaliyotayarishwa vyema au huduma iliyopangwa vizuri. Hata hivyo, Biblia inaonyesha umuhimu wa kupanga kwa ajili ya ibada. Kuanzia kwenye maandalizi makini ya wanamuziki kwa ajili ya ibada hadi maelekezo ya Paulo kuhusu ibada kwa kanisa la Korintho, maandiko yanaonyesha kwamba kupanga ni muhimu kwa kuongoza katika huduma. Hatupaswi kuleta sadaka isiyotugharimu chochote. Kwa kuwa ibada ni dhabihu yetu kwa Mungu, Mungu anastahili toleo letu bora zaidi.
Katika somo hili tutaangalia vipengele viwili vya uongozi wa ibada. Kwanza, tutajifunza umuhimu wa kupanga kwa ajili ya ibada. Kisha, tutaangalia uongozi bora katika huduma ya kuabudu.
Maandalizi ya Huduma ya Ibada
► Soma Kutoka 28-29. Ona maandalizi makini ya wale walioongoza katika ibada ya Israeli. Je, unajiandaa vipi kiroho, kiakili, na kihisia ili kuongoza ibada?
Kuandaa Kiongozi wa Ibada
Kupanga na kuandaa ibada ni muhimu; kuandaa kiongozi wa ibada ni muhimu zaidi. Hatuwezi kuwaongoza watu mahali ambapo hatujafika. Kwa sababu hii, ni lazima tutayarishe mioyo yetu kabla ya kujaribu kuwaongoza wengine katika ibada.
Katika Somo la 2, tuliona matakwa ya Mungu kwa waabudu. Mungu huwaita waabudu wake wawe na mikono safi na mioyo safi. Kabla ya kuanza kutayarisha ibada, tunapaswa kujitayarisha kama viongozi wa ibada. Ni lazima tuwe tayari kiroho kuongoza ibada.
[1]Anza kupanga ibada kwa maombi na usomaji wa Maandiko. Tumia muda katika Neno la Mungu kwa maendeleo yako ya kiroho. Hatari ya mara kwa mara kwa viongozi wa ibada ni kuruhusu maandalizi ya huduma kuchukua nafasi ya maendeleo ya kibinafsi ya kiroho. Tunaweza kujifunza Biblia ili kutayarisha mahubiri kwa wengine huku tukikosa kuruhusu Neno la Mungu lizungumze na mahitaji yetu wenyewe ya kiroho.
Kabla ya kuchagua Maandiko na nyimbo zinazozungumza Neno la Mungu na kanisa, chukua muda kuruhusu Neno la Mungu na Roho ya Mungu kusema nawe kibinafsi. Kisha unapoanza kupanga kwa ajili ya huduma ya Jumapili, mwombe Mungu akuongoze kwa Maandiko, mada ya mahubiri, na wimboi ambao utazungumza na mahitaji ya watu.
Kujipima
Je, unawezaje kusitawisha mtindo mzuri wa ibada ya faragha maishani mwako? Je, unakumbana na vikwazo gani? Je, unashughulikiaje vikwazo hivyo?
Fred Bock alieleza matayarisho ya mchungaji ambaye anatumika chini yake, Lloyd John Ogilvie. Dk. Ogilvie alipanga mahubiri yake kwa mwaka mzima. Mara nyingi, mada ya mahubiri iliyochaguliwa katika Januari ilikuwa inafaa kabisa kwa mahitaji ya kanisa ilipohubiriwa Julai. Kwa nini? “Mungu wetu ni Mungu wa jana, leo na kesho. Anajua mahitaji yetu mapema, muda mrefu kabla ya sisi kufanya hivyo. …Na tunapotayarishwa na kupangwa, hii hutufanya kuwa chombo kinachotumika zaidi na rahisi kwa Roho Mtakatifu.”[3] Roho Mtakatifu anajua ni nani atakuwa katika ibada yako; anaweza kukuongoza kwa nyimbo na maandiko ambayo yatazungumza na mahitaji yao.
Labda hupaswi kupanga mwaka kwa wakati, lakini kupanga ibada ni muhimu. Kupanga kwa uangalifu hutuweka huru kuzingatia kuabudu wakati wa ibada badala ya kuwa na wasiwasi, “Nini kitakachofuata?” Tusipopanga, huwa tunarudi nyuma kwa yale tuliyofanya wiki iliyopita. Mipango hutuweka huru kuwa wabunifu.
Anza na muundo.
Wengi wetu tunapenda utaratibu katika maisha. Tunapendelea kula kifungua kinywa asubuhi na chakula cha jioni usiku. Kwa kawaida tunasoma vitabu kuanzia sura ya 1 hadi mwisho badala ya kusoma kurasa ovyo. Hakuna msafiri anayetaka kupanda ndege ya kimataifa na kumsikia rubani akisema, “Hatujaamua njia ya kuitumia leo. Tutaondoka tu na kuona nini kitatokea." Tunapenda muundo.
[4]Muundo katika ibada hauzuii uhuru wetu wa kumfuata Roho Mtakatifu anapobadilisha mipango yetu! Muundo unatoa mwongozo wa kuabudu, huku ukiendelea kuwa tayari kwa uongozi wa Roho Mtakatifu ikiwa atapita muundo wetu. Wakati wa kuwekwa wakfu kwa Hekalu, kulikuwa na muundo uliopangwa, lakini uwepo wa Mungu ulibadilisha utaratibu wa ibada (2 Mambo ya Nyakati 5:13-14).
Katika Kiambatanisho A kuna muhtasari ambao baadhi ya viongozi hutumia kupanga ibada. Unaweza kuona ina manufaa kurekebisha mojawapo ya haya kwa ibada zako. Hizi sio muundo mgumu lakini zinaweza kutoa muundo ambao unaweza kubadilika kulingana na mahitaji yako.
Baadhi ya miundo ya kawaida ya kupanga ibada ni pamoja na:[5]
(1) Muundo unaozingatia mahubiri
Kutangaza ukweli: nyimbo za ibada, maandiko, mahubiri
Kuitikia ukweli: mwaliko, sadaka, wimbo wa kufunga
Ibada huzungumza na Mungu, lakini pia huzungumza na kanisa. Katika ibada, tunaleta Neno la Mungu kwa waabudu. Unapopanga ibada, inafaa kuuliza, “Mungu anataka kuwaletea watu wake ujumbe gani katika ibada hii?”
Je, umewahi kuhudhuria ibada kama hii?
Mtiririko wa Ibada
Mada/Dhima
Wimbo wa pamoja 1
Faida za maombi
Wimbo wa pamoja 2
Sifa kwa Mungu
Wimbo wa pamoja 3
Tumaini letu la mbinguni
Wimbo binafsi/kwaya
Kumwalika Roho Mtakatifu maishani mwetu
Mahubiri
“Wito wa Yona kwenda Ninawi” – changamoto kwa uinjilisti
Wimbo wa pamoja 4
Sifa kwa Mungu
Ni ujumbe gani waabudu wataupata? Wameimba kuhusu maombi, kumsifu Mungu, mbingu, na Roho Mtakatifu, kisha wamesikia mahubiri kuhusu somo tofauti kabisa. Katika juma linalofuata, je, watu watakumbuka changamoto ya uinjilisti? Pengine; lakini muundo wa huduma haukuimarisha mada hii.
Sasa fikiria ibada iliyopangwa kwa mada ya uinjilisti:
Mtiririko wa Ibada
Mada/Dhima
Wimbo wa pamoja 1
Sifa kwa Mungu
Wimbo wa pamoja 2
Sifa na uinjilisti
Wimbo wa pamoja 3
Mhutasari wa ujumbe wa kiinjilisti
Wimbo wa pamoja 4
Uhitaji wa Uinjilisti
Mahubiri
“Wito wa Yona kwenda Ninawi” – changamoto kwa uinjilisti
Wimbo binafsi/kwaya
Wito wa uinjilisti
Wimbo wa pamoja 5
Mwitikio juu ya wito
Kwa sababu viongozi wamepanga ibada ya kuwasilisha mada moja, watu wanaweza kusikia sauti ya Mungu kwa wiki nzima, wakiwakumbusha juu ya wito wa uinjilisti. Wanapokutana na watu wenye maisha ya shida au upweke, wanaweza kukumbuka kwamba “watu wanamhitaji Bwana.” Wakiwa kazini siku ya Jumanne, wanaweza kufurahi wakikumbuka kuwa Yesu anaokoa. Na kwa sababu “Yesu ametuokoa,” tunapaswa kushirikisha furaha hii na wengine.
Je, Mungu anaweza kufanya kazi kupitia ibada isiyo na mada kuu? Bila shaka! Hata hivyo, tunawasaidia waumini wetu kuzingatia ujumbe tukichukua muda kupanga ibada kwa uangalifu. Je, hii ni muhimu kila wakati? Hapana. Ibada wakati mwingine itakuwa na mada nyingi ambazo Mungu hutumia kuzungumza na mahitaji mbalimbali katika kanisa. Hatupaswi kamwe kuingia katika mtego wa kufikiri kwamba Mungu anafanya kazi kupitia mfumo mmoja tu. Hata hivyo, mada iliyounganishwa mara nyingi huwasaidia waabudu kuzingatia ujumbe wa ibada.
Dumisha usawa katika ibada.
Sote tuna vitu tuvipendavyo: vyakula tuvipendavyo, muziki tunaopenda, vitabu tupendavyo, michezo tuipendayo, na vitabu vya Biblia tuvipendavyo. Katika kupanga ibada, ni muhimu kwamba kiongozi ajumuishe zaidi ya nyimbo anazopenda, maandiko, na mada za mahubiri. Ibada iliyosawazishwa itazungumza injili yote kwa kanisa zima.
(1) Ibada yenye usawa inaonyesha ukuu wa Mungu na uwepo wa Mungu pamoja nasi.
Mungu ni Mungu aliyetukuka anayetawala juu ya dunia yote; Mungu pia ni Mungu aliyepo ambaye anakaa kati ya watu wake. Tunaona usawa huu katika Maandiko yote.
Baada ya kuvuka Bahari ya Shamu, watu wa Israeli waliimba juu ya uwezo wa Mungu; “Ee Bwana, katika miungu ni nani aliye kama wewe? Ni nani aliye kama wewe, mtukufu katika utakatifu, mwenye kuogopwa katika sifa zako, mfanya maajabu?” Waliimba juu a vile Mungu amewatunza; “Wewe kwa rehema zako umewaongoza watu uliowakomboa, Kwa uweza wako uliwaelekeza hata makao yako matakatifu” (Kutoka 15:11-13).
Isaya alimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa. Alikuwa mkuu na mbali sana juu ya dunia. Bwana aliinuliwa, lakini alizungumza kibinafsi kumtuma Isaya “Enenda, ukawaambie watu hawa...” (Isaya 6:1-13).
Mtunga-zaburi alimsifu Mungu aliyetukuka; “wewe Mungu, Bwana wetu jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote! Wewe Umeuweka utukufu wako mbinguni.” Mungu huyu aliyeinuliwa amejinyenyekeza ili kuwa karibu na wanadamu; "Mtu ni kitu gani hata umkumbuke, na binadamu hata umwangalie?" (Zaburi 8).
Katika ibada, tunatilia maanani ukuu wa Mungu na uwepo wa Mungu pamoja nasi. Ibada yetu inaposahau ukuu wa Mungu, anakuwa rafiki wa kawaida ambaye hahitaji tena utii na ibada. Ibada yetu inaposahau jinsi Mungu anavyohusika nasi sasa, tunamwabudu kama Mungu aliye mbali ambaye hajali chochote katika mambo yetu. Katika kupanga ibada, tunapaswa kuzingatia vipengele vyote viwili vya uhusiano wa Mungu na wanadamu. Ni lazima tuwakumbushe waabudu kwamba tunamcha Mungu; lazima pia tukumbuke kwamba tunapendezwa na Mungu. Katika maombi, tunamsifu Mungu kwa matendo yake makuu, pia tunapeleka kwake mahitaji yetu ya ndani ya kibnafsi.
► Tazama mkusanyiko wa tenzi na mapambio katika lugha yako. Tafuta mfano wa wimbo ambao unonyesha ukuu wa Mungu. Tafuta wimbo mwingine unaozungumzia kuhusu Yeye kuwa na uhusiano wa karibu nasi.
(2) Ibada yenye usawa ni ya pamoja na ya kibinafsi.
Kitabu cha Zaburi hujumuisha sifa za pamoja na sifa za mtu binafsi. Zaburi zingine zinazungumza juu ya sifa "zetu"; baadhi ya zaburi huzungumza juu ya sifa “yangu”. Hekaluni, waabudu wa Kiebrania waliabudu pamoja; nyumbani, walisali wakiwa mtu mmoja-mmoja. Yesu mara nyingi alienda kwenye sinagogi kwa ajili ya ibada ya pamoja; pia alienda mahali pasipokuwa na watu ili kukaa peke yake na Baba yake (Luka 4:16 na Marko 1:35). Ibada ya Biblia ilikuwa ya pamoja na ya kibinafsi. Katika ibada, ni lazima tutoe nafasi kwa waamini kuabudu kama kanisa na nafasi kwa waabudu mmoja-mmoja kuonyesha ujitoaji wao binafsi kwa Mungu.
Kuiweka katika vitendo
Ibada ambayo ni ya pamoja na ya kibinafsi itaathiri maeneo yote ya huduma. Kwa Pamoja tutaimba nyimbo kwa kusanyiko lote, kwa Pamoja tutaimba nyimbo za ibada binafsi. Tutasali kwa “Baba yetu uliye mbinguni”; tutakuwa na nyakati za maombi ya kikundi kuruhusu kila mshirika kuomba kibinafsi ndani ya mwili wa Kristo.
Zaidi ya wakati wowote katika historia, ibada ya pamoja ni changamoto. Katika enzi ya simu za mkononi, kompyuta ya mkononi, ujumbe wa maandishi, na upatikanaji wa mtandao mara kwa mara, tunaweza kukaa katika ibada huku tukiwa tumejitenga kihisia na kiroho. Uaminifu kwa ibada ya pamoja unahitaji sisi kujitenga na vikwazo na kuabudu kwa pamoja kama mwili wa Kristo.
► Tazama mkusanyiko wa tenzi na mapambio katika lugha yako. Tafuta mfano wa wimbo ambao umeandikwa katika mtazamo wa kijumuia. Unaweza kujumuisha viwakilishi kama “yetu,” “sisi,” au maneno kama “watu wote.” Kisha, tafuta mfano wa wimbo ambao umeandikwa katika mtazamo wa mtu binafsi. Unaweza kujumuisha viwakilishi kama “yangu,” “mimi”.
(3) Ibada yenye usawa inajumuisha yaliyojulikana na mapya.
Uwiano huu ni wa vitendo badala ya kitheolojia, lakini ni muhimu ikiwa tunataka kushirikisha kikamilifu waumini katika ibada. Katika kupanga kwa ajili ya ibada, tunapaswa kusawazisha yaliyozoeleka na mapya.
Wingi wa mambo mapya husababisha waumini kuwa watazamaji badala ya kuwa waabudu; hawawezi kushiriki kwa sababu hawajui nyimbo. C.S. Isaka alilalamika wakati fulani kwamba wachungaji wengi husahau kwamba “Yesu alimwambia Petro “Lisha kondoo zangu,” sio ‘kuwafundisha mbwa wangu mbinu mpya.’” Mambo mapya kupita kiasi hufanya iwe vigumu kuzingatia ibada.
Mengi ya yale yanayofahamika husababisha utaratibu usio na maana. İbada ambayo imekuwa ya kutabirika kabisa inasababisha waumini kupoteza mwelekeo na kujitenga na ibada.
Upangaji wa ibada unapaswa kujumuisha yote yanayofahamika na mapya. Kwa mfano, kiongozi mmoja wa ibada alichagua kuongoza kusanyiko kwa tenzi mpya kuhusu upatanisho. Wimbo huu unaonesha wazi gharama ya upatanisho. Baada ya wimbo ule kuwa umeimbwa, aliongoza wimbo wa zamani, unaofahamika zaidi ualikao kusanyiko kuitikia sadaka ya Yesu.
Usawa wa yale yanayofahamika na mapya hutia moyo waumini kuabudu kwa bidii.
Kuiweka katika Vitendo
Ibada inayosawazisha ile inayofahamika na mpya itajumuisha nyimbo za zamani na mpya. Itajumuisha usomaji wa Maandiko unaofahamika na usiojulikana sana. Kabla ya kusoma kifungu tunachokifahamu kama vile Yohana 3:1-21 ambamo Yesu anafundisha kuhusu kuzaliwa upya, tunaweza kusoma kifungu kisichojulikana sana kama vile Ezekieli 36:16-38 ambapo Mungu anaahidi kuwaosha Waisraeli kwa maji na kuwapa moyo mpya. Maandiko haya mawili yanahusiana kwa karibu katika mada. Kuzisoma pamoja kutaongeza uelewa wa waumini kuhusu mafundisho ya Yesu katika Yohana 3.
Ikiwa unatanguliza wimbo mpya, zunguka wimbo huo mpya kwa nyimbo zinazofahamika. Tunapofungua ibada kwa wimbo usioufahamu, ibada huanza kwa njia isiyoeleweka. Ni jambo la hekima kufungua kwa wimbo unaojulikana kisha kutambulisha wimbo huo mpya.
Kanisa moja nchini Taiwan lilikuwa na mbinu ya ubunifu ya kutambulisha nyimbo. Wengi wa washirika wao walikuwa waamini wapya na hawakujua nyimbo nyingi zilizoimbwa. Kanisa hili lilikuwa na mazoezi kabla ya kila ibada. Dakika ishirini kabla ya ibada, watu waliimba nyimbo ambazo zingekuwa sehemu ya ibada. Mpiga kinanda alicheza wimbo huo ili kila mtu aweze kujifunza wimbo huo. Kwa kuwa hayo yalikuwa mazoezi, kiongozi angeweza kuacha na kurudia fungu la maneno hadi waumini wajifunze vizuri. Kufikia 10:00, watu waliimba hata nyimbo mpya kwa ujasiri.
► Tazama mkusanyiko wa tenzi na mapambio katika lugha yako. Tafuta nyimbo mbili zenye dhima moja au nyimbo mbili zenye dhima zinazohusiana. Kunatakiwa kuwe na mahusiano dhahiri kati ya nyimbo hizo. Moja uwe wenye kufahamika, mwingine uwe usiofahamika. Kama ungetakiwa kutumia nyimbo hizi mbili kwenye ibada ya kuabudu, ni wimbo upi ungeimba kwanza? Ungebadili vipi kuendea wimbo wa pili?
Panga kama timu.
Mhubiri anatoa ushauri huu unaofaa; “Afadhali kuwa Wawili kuliko mmoja; maana watapata ijara njema kwa kazi yao” (Mhubiri 4:9). Upangaji wa ibada unapaswa kuwa shughuli ya pamoja. Kila mtu anayehusika katika uongozi wa ibada anapaswa kuwa na jukumu katika kupanga.
Mchungaji, kiongozi wa sifa, na viongozi wengine wa kanisa wanapokutana pamoja kutafuta mapenzi ya Mungu kwa ajili ya ibada, karama za kila mtu huunganishwa pamoja. Kwa kufanya kazi kama timu, nguvu za kila mshiriki wa uongozi wa kanisa huchangia katika ibada.
Panga kwa muda mrefu.
Hakuna Ibada moja inayojumuisha ujumbe mzima wa Biblia, lakini baada ya muda tunapaswa kuwasilisha vipengele vyote vya injili kwa waabudu wetu. Kila mmoja wetu ana mada anazopenda; lazima tujitutumue kuhubiri na kuimba mada ambazo hatuzipendi.
Baadhi ya wachungaji na viongozi wa ibada hutumia kalenda inayopanga mada za kufundisha kupitia Biblia katika miaka mitatu.[6] Wengine hupanga kila wiki lakini wako makini kufanyia kazi ujumbe mzima wa maandiko kwa muda fulani.
Hata kama hutafuata kalenda ya mafundisho, ufahamu wa majira ya msingi ya mwaka wa Kikristo utakuongoza kupitia vipengele muhimu vya injili. Majira muhimu katika mwaka wa Kikristo ni:
Majilio (Jumapili nne kuelekea Krismasi): Kuzingatia ujio wa kwanza na wa pili wa Kristo.
Krismasi: Mkazo juu ya kufanyika mwili na kuzaliwa kwa Kristo.
Kwaresima (Jumapili sita zinazoelekea Pasaka): Kuzingatia mateso na kifo cha Yesu, pamoja na mahitaji ya ufuasi kwa kila mwamini.
Pasaka: Kuzingatia ufufuo na kupaa kwa Kristo.
Pentekoste: Kuzingatia Roho Mtakatifu na kanisa.
Iwe unafuata mlolongo rasmi au mpango wa kila wiki, hakikisha kuwa kanisa lako linasikia injili yote kama sehemu ya ibada.
Panga kwa amani.
Ibada sio kuhusu sisi; ibada ni dhabihu yetu kwa Mungu. Upangaji wetu wa ibada ni sehemu ya sadaka hiyo. Tunapanga ibada bila shinikizo linaloongozwa na hatia ya kufikiri, "Je, hii ni nzuri vya kutosha?" Tunamwabudu Mungu wa neema. Sadaka yetu inakubaliwa si kwa sababu ni nzuri ya kutosha, lakini kwa sababu Mungu anakubali sadaka ya hiari ya watoto wake.
Hii ni muhimu katika kuzuia shinikizo kwamba "Lazima tuendane na kanisa la XYZ." Katika ulimwengu wa kisasa wa teknolojia na vyombo vya habari vingi, viongozi wengi wa makanisa wanapata shinikizo la mara kwa mara la kutaka kufanana na makanisa mengine. Wachungaji wanashindana kuwa na teknolojia ya kisasa. Waongozaji wa muziki hushindana kuimba nyimbo mpya zaidi. Waabudu hugeuka kuwa wanunuzi wanaotafuta kanisa linalotoa vivutio vipya zaidi.
Usikubali kuingia kwenye jaribu la kutaka kumvutia Mungu kwa sadaka yako. Usiruhusu zana za ibada, kama vile muziki na teknolojia kuchukua nafasi ya ibada halisi. Mletee kilicho bora zaidi ukijua kwamba Mungu wa neema hufurahia harufu nzuri ya sadaka yako. Mpe kilicho bora zaidi, kisha atakubali sadaka yako. Ibada si mashindano na makanisa mengine; ni zawadi kwa Mungu.
“Utoaji bila utaratibu inaweza kuwa fujo, na utaratibu bila utoaji unaweza kukosa uhai.”
- Franklin Segler na
Randall Bradley
[5]Miundo ninayojumuisha hapa ni ya huduma nzima. Baadhi ya viongozi wa ibada hutumia miundo kwa ajili ya sehemu ya muziki ya ibada pekee. Sijajumuisha hizi kwa sababu hutenganisha ibada na huduma nzima. Katika Biblia, ibada inajumuisha huduma zote, si ibada maalum ya muziki iliyotengwa na mahubiri.
► Je, waumini wana jukumu gani katika ibada? Je, jukumu la viongozi wa ibada ni nini? Nini jukumu la Mungu?
Watu wengi huona ibada kama tamasha. Kusanyiko linasikiliza mchungaji na wanamuziki wakiimba. Patakatifu ni ukumbi wa tamasha.
Barry Liesch alielezea mtazamo huu wa ibada kama mchezo wa mpira:[1]
Viongozi wa ibada ni wachezaji wanaofanya ibada.
Waamini ni watazamaji katika viwanja wakitazama mchezo.
Mungu ndiye kocha anayewaambia viongozi wa ibada nini cha kufanya.
Picha ya kibiblia ya ibada ni tofauti sana. Katika ibada ya kibiblia, mkutano huabudu wakati viongozi wa ibada hufanya kama makocha wanaoongoza ibada:
Kiongozi wa ibada ndiye kocha anayeongoza kanisa.
Waabudu ni wachezaji wanaofanya ibada.
Mungu ndiye hadhira inayopokea ibada zetu.
Katika mchezo wa kuigiza, hutawahi kumwona muongozaji. Muongozaji anajua kila mstari wa mchezo na anaelekeza kila mwigizaji wakati wa kuingia. Hatakama anafanya kazi yake vizuri, watazamaji hawatambui kamwe. Hilo ndilo jukumu la viongozi wa ibada. Kazi yetu si kuabudu kwa ajili ya watu; kazi yetu ni kuongoza watu katika kuabudu. Waumini wanaabudu, pamoja na mchungaji na kiongozi wa uimbaji, katika uwepo wa Mungu. Lengo letu katika ibada ni kumpendeza Mungu. Katika kielelezo cha kibiblia cha ibada, Mungu ndiye hadhira ya ibada yetu.
Hata hivyo, Mungu ni zaidi ya hadhira; Mungu hututia nguvu yote tunayofanya katika ibada. Na, kiongozi wa ibada ni zaidi ya kocha au muongozaji. Kiongozi wa ibada ni muongozaji na mwabudu. Ibada inahusisha mahusiano mengi:
Mungu huwaalika waabudu, hupokea ibada, na huwaongoza viongozi wa ibada wanapohudumu mbele za watu.
Viongozi wa ibada huongoza waumini katika ibada, kusikiliza sauti ya Mungu, na kushiriki kama waabudu.
Waumini humwabudu Mungu, husikiliza Neno la Mungu, na kuzungumza wao kwa wao katika ibada.
Jinsi ya Kuepuka Ibada Kama Onyesho la Utendaji [2]
1. Imba nyimbo ambazo watu wanajua au wanaweza kujifunza kwa urahisi. Ziimbe katika tuni inayoeleweka kwa kanisa. Tumia nyimbo mpya kwa kiasi.
2. Imba na ushangilie uweza, utukufu, na wokovu wa Mungu. Tumikia waumini wako. Wajaze kwa Neno la Mungu. Usiimbe nyimbo zenye maneno mabaya au theolojia dhaifu.
3. Weka taa juu. Punguza kuongea sana. Usiruhusu vitanzi/taa/vielelezo viwe njia yako ya ubunifu kwa gharama ya ukuu wa injili.
4. Badili uongozi wako wa ibada na nyimbo unazochagua zifae watu wengi wa kanisa lako. Ongoza kwa upendo wa kichungaji.
5. Elekeza kwa Yesu. Usijivutie upande wako.
Sifa za Kiongozi wa Ibada
Bila kujali cheo chako, kama kiongozi wa ibada unafanya kazi ya kichungaji. Ikiwa wewe ni mchungaji, tayari unaelewa hili. Ikiwa wewe ni kiongozi wa kawaida, lazima uelewe kwamba jukumu lako linakuweka katika nafasi ya uongozi wa kiroho.
Katika kuchagua kiongozi wa ibada, lazima tuzingatie sifa za kiroho, si tu sifa za uimbaji au za kibinafsi. Mitume walipochagua mashemasi kuwatunza wajane wa Kiyunani, walitafuta wanaume wenye sifa nzuri, waliojaa Roho na hekima (Matendo 6:3). Sifa za kimaadili, za kiroho, na za kiadili zilikuwa muhimu sana.
Katika baadhi ya makanisa, uchaguzi wa viongozi wa nyimbo, wanamuziki, na majukumu mengine ya uongozi hutegemea umaarufu. Ikiwa mashemasi waliohudumu kwenye meza walichaguliwa kwa sifa zao za kiroho, hakika viongozi wa ibada wanapaswa kuchaguliwa kwa sifa za kiroho.
Ikiwa unaongoza ibada katika kanisa lako (kama mchungaji, mwanamuziki, au kiongozi mwingine katika ibada), unapaswa kutafuta kukuza sifa zinazofanya kuwa kiongozi bora wa ibada.
Upambanuzi wa kiroho. “Je, ninaweza kupambanua uongozi wa Roho Mtakatifu?”
Unyeti. “Je, nina wepesi wa kujua mahitaji ya waumini? Je, ninachagua nyimbo na maandiko yanayozungumzia mahitaji hayo?
Ushirikiano. "Je, ninatumikia kwa ufanisi kwenye timu? Je, ninashirikiana na mchungaji anaponiuliza nibadilishe wimbo wa kufunga? Je, ninakubali mahitaji ya timu nzima?”
Maarifa. “Je, ninakua katika ujuzi wangu wa Neno la Mungu? Je, ninalifanya Neno la Mungu kuwa jambo kuu katika ibada?”
Hekima. “Je, ninakua katika hekima ya kuelewa na kutatua mizozo kuhusu ibada? Je, ninajiweka nidhamu ili kuwa mwepesi wa kusikiliza na si mwepesi wa kusema? (Yakobo 1:19).
Unyenyekevu. “Je, niko tayari kuimba wimbo unaozungumzia mahitaji ya waumini walio na mafunzo kidogo? Je, niko tayari kuhubiri kwa mtindo rahisi zaidi unaokidhi mahitaji ya washirika wasio na elimu katika kanisa langu? Je, ninaongoza kwa unyenyekevu, au ninajiona kuwa bora kuliko kanisa ambalo Mungu ameniweka?” Kama kiongozi wa ibada, ubunifu wako lazima upate nafasi katika wajibu wako wa kichungaji. Wajibu wako wa kwanza ni kuwahudumia watu.
Ubunifu. “Je, ninatafuta njia za kufanya ibada iwe na maana? Je, ninaepuka kuangukia katika muundo unaojirudia ambapo kila ibada ni sawa?”
Nidhamu. “Je, nawajibika kudhibiti ubunifu wangu ili usisababishe kuchanganyikiwa katika ibada? Je, najiepusha kufanya kila ibada iwe mpya sana kiasi kwamba watu watashindwa kuongeza umakini kwa Mungu?”
Ubora. “Je, ninatoa kile kilicho bora kila wiki? Je! ninaendelea kukua kama kiongozi wa ibada?”[3]
Hatua Muhimu katika Kuongoza Ibada
Kiongozi hawezi kuwalazimisha watu kuabudu; hata hivyo, kiongozi anaweza kufanya iwe rahisi kwa waumini kuongeza umakini kwa ibada.
Kuongoza kwa mfano
Mojawapo ya mapendeleo ya kuongoza katika ibada ni fursa ya kuabudu pamoja na waumini. Kiongozi lazima aabudu huku akiongoza washirika katika ibada.
Kwa bahati mbaya, ibada inaweza kuwa changamoto kwa kiongozi wa ibada. Tunaweza kuwa na shughuli nyingi sana za kuongoza ibada hadi tukashindwa kuabudu! Ikiwa wewe ni kiongozi wa muziki, unaweza kujikuta ukijaribu kuabudu huku ukiwa na mawazo kama vile:
“Mpiga gitaa amechelewa. Natumaini atafika hapa kwa wakati kwa ajili ya wimbo maalum!”
“Watu hawakuimba vizuri kwenye wimbo wa kwanza. Je, wimbo huo ni mgumu sana kwa kanisa letu?”
“Ninahisi kama tunaimba polepole sana. Je, niharakishe ubeti unaofuata?”
Ikiwa wewe ni mchungaji, unaweza kujikuta ukijaribu kuabudu huku ukifikiri:
“Tumepungukiwa na watu 10 ikilinganishwa na wiki iliopita. Wako wapi?”
“Je, nimalize mahubiri kwa kuwaalika watu madhabahuni?”
“Wimbo huo hauendani na mahubiri yangu! Ninawezaje kuhamia kutoka wimbo kuhusu mbinguni hadi kwenye mahubiri yangu kuhusu Hukumu?”
Hatupaswi kuruhusu uendeshaji wa ibada kuchukua nafasi ya ibada katika maisha yetu. Tunapoongoza ibada, lazima tuabudu. Hii inahamasisha ibada kwa waumini. Msemaji mmoja alisema, “Kama viongozi wa ibada hatuko kama mbwa wa wachungaji wanaouma visigino vya waumini kuwalazimisha waende kwenye mwelekeo tunaoitaka. Sisi ni waabudu tunaowaalika waumini kwenda pamoja nasi katika uwepo wa Mungu.” Waumini hawaabudu wakati kiongozi anawaambia waabudu; wao huabudu wakati kiongozi anaabudu. Kiongozi wa ibada hungoza kwa mfano.
Kuongoza kwa kutia moyo
Susanna alikuwa macho mpaka saa 3:00 asubuhi akimhudumia mtoto mgonjwa. Baada ya masaa matatu ya usingizi, aliamka kuandaa kifungua kinywa na kujitayarisha kwa ajili ya kanisa. Alifika kanisani akiwa amechoka kutokana na kukosa usingizi, akiwa amevunjika moyo kwa sababu alimkemea mwanawe vikali aliposahau kuweka kitu cha kuchezea, na akiwa amepwaya kiroho kwa sababu alikuwa na muda mchache peke yake na Mungu wiki hii.
Mchungaji Joel anataka kuona ushiriki zaidi katika ibada. Baada ya wimbo wa kwanza, anaingia kwenye mimbari, “Mna nini nyinyi watu? Tupo katika uwepo wa Mungu. Tunamwabudu Mfalme, na baadhi yenu mnaonekana kama mngependelea kuwa nyumbani mmelala! mnapaswa kuwa na aibu. Jiunge katika ibada!”
Nia ya Mchungaji Joel ni njema. Anataka waumini wake wawe washiriki kikamilifu katika ibada, lakini Susanna anasikia nini? "Mimi ni mtu aliyeshindwa kama mama; Nilikuwa mkali sana kwa mwanangu. Nimefeli kama Mkristo; Nilikosa ibada zangu binafsi jana. Nimeshindwa hata kuhudhuria kanisani; Mungu anakasirika kwa sababu sikuimba.” Kwa kutumia hatia kama kichochezi, Mchungaji Joel amefanya ibada kuwa ngumu zaidi kwa Susanna.
Kama viongozi wa ibada, tunapaswa kuhimiza ibada; tunapaswa kuwa kielelezo cha ibada katika maisha yetu wenyewe; kisha tun aweza kuacha matokeo mikoni mwa Mungu. Ni neema ya Mungu inayofanya ibada iwezekane; ni neema ya Mungu inayotia nguvu ibada ya kweli; ni neema ya Mungu inayovuta moyo wa mwabudu.
Tunapaswa kuhimiza ibada kwa maneno yenye matumaini, lakini hatupaswi kujaribu kuwahadaa waabudu kwa hatia au kwa kujaribu kuchochea hisia kwa njia isiyo sahihi. Lengo letu ni kuwaelekeza waabudu kwa Mungu. Yeye ndiye anayeleta hamasa ya ibada; ibada haitegemei mbinu zetu za uhamasishaji au udanganyifu wa kihisia. Sisi kama viongozi wa ibada hatuhitaji kufanya kazi ya Mungu!
Sehemu hii ilianza na hadithi ya Susanna. Tumalizie na hadithi ya kweli ya kiongozi mnyenyekevu na mwenye kutia moyo. Daudi alijitahidi kuwahamasisha vijana kushiriki katika ibada. Aligundua kuwa walikuwa wakijikita zaidi kutuma ujumbe wa maandishi kuliko kushiriki katika ibada. Baadhi ya viongozi wangeweza kuanza ibada na kitu kama hiki: “vijana, tuko hapa kuabudu. Wekeni mbali simu hizo na mzingatie ibada. mnamkosea Mungu heshima!”
Daudi alifanya jambo tofauti sana. Mpiga gitaa alipokuwa akipiga wimbo wa utulivu wa ibada, Daudi alisema kwa upole, “Tunapokuja katika uwepo wa Mungu, najua usingependelea kumvuruga jirani yako katika kuabudu kwake. Hebu wote tuweke simu zetu pembeni na kusikiliza sauti ya Mungu asubuhi ya leo.” Kila mtu ndani ya kanisa aliweka simu yake. Daudi kwa unyenyekevu alifundisha ujana wake kuabudu.
Kuongoza au Kuigiza?
Sikiliza ushuhuda wa kiongozi wa kisasa wa ibada:
“Nikiwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza, nilitembelea kanisa karibu na chuo kikuu changu; yake… mwanga mkali na muziki wenye sauti kubwa [zilikuwa] za kusisimua. Kiongozi wa ibada alikuwa na nywele za mtindo, jeans na gitaa la gharama kubwa. Mwanzoni mwa ibada, niliona kipaza sauti kisichotumika kimefungwa kwenye kiuno chake. ‘Hiyo inaweza kuwa na kusudi gani?’ nilijiuliza, kisha nikainua mikono yangu na kuzama katika nyimbo hizo.
"Sauti hiyo ilikuwa nzuri sana, kikundi cha sifa kilikuwa bora, na muziki ulipangwa kwa umakini kuongoza wimbo hadi mwisho. Kiongozi alipoimba maneno ya mwisho napiga magoti, najitoa kwako kikamilifu. Ni wakati huo ndipo nilitambua madhumuni ya kipaza sauti kisichotumiwa. Iliwekwa kwenye urefu sahihi ili kiongozi aweze kuimba na kupiga gitaa akiwa amepiga magoti. Sitaki kuhukumu nia ya kanisa hili, lakini sikuweza kujizuia kuhisi kuwa yalikuwa ni maigizo kuitikia wakati huu wa kihisia, ambao ulionekana wazi kuwa ulipangwa mapema.”[4]
Mfano huu unatoka kwenye ibada ya kisasa, lakini tunaweza pia kutumia mifano kutoka kwa ibada ya kitamaduni. Tatizo la kuigiza haliishii tu kwa mtindo mmoja wa kuabudu. Bila kujali mtindo wetu wa muziki au nia zetu za dhati, tunaweza kulichukulia kanisa kama vibaraka ambao tunawaongoza ili wawe na hisia Fulani maalumu.
Je, hisia katika ibada ni mbaya? Hapana; tunaona mifano mingi ya kibiblia ya athari za kihisia za ibada. Je, ni makosa kujaribu kuhamasisha mwitikio wa kihisia? Hapana; mawasiliano mazuri hugusa akili na hisia zote. Hata hivyo, tusipokuwa waangalifu, tunaweza kufanya kazi ya kuunda athari fulani ya kihisia, mbali na kazi ya Roho Mtakatifu.
Je, tunawezaje kutofautisha kati ya uongozi wa ibada na maigizo? Maigizo huja wakati mwitikio wa kanisa unategemea ufanisi wa matendo ya viongozi badala ya nguvu za Roho Mtakatifu. Labda hatuwezi kamwe kutofautisha kikamilifu kati ya kuongoza na kuigiza, lakini kuna baadhi ya ishara zinazopendekeza kuwa tunaweza kuwa tunafanya maigizo.
1. Tuko katika hatari ya kuigiza kuabudu tunapochanganya hisia na ibada. Tunaanza kufikiri kuwa ni jukumu letu kutengeneza muamko wa kihisia. Baadhi hata ya viongozi wa ibada wamesema, “Fanya hivyo hadi iwe halisi. Tengeneza hisia hadi watu wahisi ukweli. Hii inachukuliwa kwamba kazi yetu ni kutumia hisia kuunda ibada. Viongozi wa ibada huongoza ibada; hatuumbi ibada.
2. Tuko katika hatari ya kuigiza ibada tunapodhania kuwa hali ya hisia kubwa inahitajika kwa ajili ya mabadiliko ya moyo. Mungu anaweza kufanya kazi katika ibada ya kanisa iliyojaa hisia, lakini pia anaweza kufanya kazi katika nyakati tulivu nyumbani. Tuko katika hatari ya kujaribu kuliigizia kanisa ikiwa tunaamini kwamba ni kupitia jitihada zetu tu ndipo Mungu anaweza kuleta mabadiliko katika mioyo ya wale tunaowatumikia.
3. Tuko katika hatari ya kuigiza ibada tunapolinganisha tendo fulani la kimwili na ibada. Wakati fulani kiongozi anataka watu waitikie, kwa hiyo anasema, “Ikiwa unampenda Yesu, utainua mikono yako.” Bila shaka, inawezekana kabisa kwamba mtu fulani kanisani ambaye hampendi Yesu kikweli atanyosha mikono yake! Au, mtu fulani katika kanisa ambaye anampenda Yesu anaweza asiinue mikono yake. Ibada hailinganishwi na tendo fulani la kimwili. Kupiga makofi tunapoimba hakuthibitishi kwamba tunaabudu zaidi ya kukaa kwa utulivu wakati wa maombi kunaonyesha kwamba tunaomba. Mungu pekee ndiye anayeona moyo wa mwabudu. “Viongozi wa ibada wanapofanya vitendo vya nje kuwa kipimo kikuu cha tabia ya ndani, wanakanyaga kwenye ardhi hatari.”[5]
4. Tuko katika hatari ya kufanya maigizo ibadani tunapojaribu kuiga kile ambacho Mungu amefanya wakati mwingine au mahali pengine. Hatupaswi kudhani kwamba kwa sababu Mungu alibariki wimbo fulani wiki iliyopita, ni lazima abariki wimbo huohuo wiki hii. Mungu anapofanya kazi, anafanya kazi kwa njia yake mwenyewe. Viongozi wa kuabudu lazima wamwachie Mungu uhuru kuja kama apendavyo. Hakuna kichocheo cha maajabu ambacho huunda majibu ya kiroho katika kila hali.
5. Tuko hatarini kuigiza ibada tunapopima huduma yetu kwa uwezo wetu wa kupata mwitikio kutoka kwa watu. Mzungumzaji yeyote wa hadhara au mwanamuziki anapenda kupata mwitikio kutoka kwa wasikilizaji; hiyo ni kawaida. Lakini tunapopima ufanisi wa huduma yetu kwa miitikio hii, tuko katika hatari ya kutegemea ujuzi wetu badala ya kutegemea Roho Mtakatifu.
Mada hii ni ngumu. Mara nyingi, maneno yale yale yanayosemwa katika hali mbili tofauti huwakilisha motisha tofauti sana. Kwa upande mmoja, tusipokuwa waangalifu tunaweza kuanza kuigiza ibada. Kwa upande mwingine, ikiwa tuna hofi sana na hisia hatuwezi kutoa uongozi hata kidogo!
Kwa sababu hii, hatupaswi kuwa wepesi kuhukumu uongozi wa ibada wa mtu mwingine lakini wepesi kutathmini uongozi wetu wenyewe. Ni lazima tumwombe Mungu atuonyeshe nia zetu katika kuongoza. Ni lazima tuwe waangalifu kuongoza katika ibada bila kuwaigizia waabudu kwa mwitikio fulani ambao tunatamani.
Maswali ya Kivitendo
Je, tunaanzaje Ibada?
Mfano mbaya:
Saa 4:00, ni wakati wa kuanza ibada. Mchungaji anajaribu kumtafuta kiongozi wa wimbo. Wanawake watatu wanashiriki mapishi. Wanaume wanne wanazungumza juu ya ukosefu wa mvua kwa mazao. Je, tunahamaje kutoka kwa shughuli hizi zote hadi kwenye ibada?
Moja ya majukumu muhimu ya kiongozi wa ibada ni ufunguzi wa ibada. Je, tunawaalikaje watu wa Mungu katika uwepo wa Mungu?
Baadhi ya makanisa huanza na muda wa ukimya. Kiongozi anaanza kwa urahisi, “Jiunge nasi katika muda wa maombi ya utulivu tunapoingia katika uwepo wa Mungu.”
Baadhi ya makanisa huanza na muziki “Wito wa Kuabudu.” Huu unaweza kuimbwa na kwaya au mtu binafsi, au inaweza kuwa kwaya ya kanisa. Katika baadhi ya makanisa, mchungaji atatangulia mbele na kuanza kuimba ubeti kama, “Nitaingia malangoni mwake nikiwa na shukrani moyoni mwangu….”
Baadhi ya makanisa huanza na mstari wa Maandiko, mara nyingi hutolewa kutoka kitabu cha Zaburi.
Njoni, tumwimbie BWANA; tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu! Tuje mbele zake kwa shukrani; tumfanyie shangwe kwa zaburi
(Zaburi 95:1-2).
Zaburi zinazowaalika waabudu katika uwepo wa Mungu ni pamoja na Zaburi 15, Zaburi 66:1-4, Zaburi 96:1-4, Zaburi 100, Zaburi 105:1-3, Zaburi 107:1-3, Zaburi 149:1-2 na Zaburi 150.
Je, matangazo ni ibada?
Mchungaji mmoja wa Hispania aliuliza, “Matangazo yanafaa wapi katika ibada? Tunajaribu kuzingatia ibada na uwepo wa Mungu katika kanisa letu. Tuna Ibada nzuri kisha tunamalizia na orodha ndefu ya matangazo ya kuchosha. Hii inaathiri moyo wa ibada. Je, tunafanyaje matangazo kuwa sehemu ya ibada?”
Bila kujali ni wapi tunaweka matangazo, yanaweza kuharibu ibada. Ni mara chache sana matangazo kuwa ibada; badala yake yanaingilia ibada. Unaweza kufanya nini? Hakuna jibu kamili, lakini mapendekezo machache yanaweza kusaidia:
Inapowezekana, chapisha matangazo badala ya kuyasoma kwa sauti. Inapolazimika kutoa matangazo ya umma, yafanye mafupi.
Tumia projekta ya juu kuonyesha matangazo kabla ya ibada kuanza.
Makanisa mengine yana matangazo, muda wa maombi, na kisha ibada huanza. Kuna kanisa moja ambalo huanza ibada saa 4:00. Kanisa hili hufanya matangazo saa 3:50. Mchungaji alisema, “Hii inatimiza mambo mawili. Kwanza, inahimiza watu waje mapema kwa sababu hawatasikia matangazo ikiwa hawapo hapa kufikia 9:50. Pili, inaturuhusu kuzingatia ibada kwa umakini tangu maneno ya mwanzo ya ibada.”
Usiruhusu matangazo yakatize roho ya ibada. Badala yake, chukulia matangazo kama sehemu ya kufanikisha huduma ya kanisa, toa matangazo, na endelea mbele. Tunapotambua kwamba shughuli za kanisa (maombi ya pamoja, huduma za kijamii, matukio ya nje, na miradi ya kanisa) ni sehemu ya ibada, matangazo ya shughuli hizi ni sehemu ya ibada ya kanisa. Kama vile baba anavyoweza kumalizia ibada ya familia kwa kukumbusha familia juu ya mipango ya wiki, mchungaji anaweza kumaliza ibada kwa kukumbusha kanisa juu ya shughuli za wiki. Matangazo kuhusu shughuli za kanisa hutukumbusha kwamba sisi ni familia; ushirika wa familia ni kipengele muhimu cha ibada.
[1]Barry Liesch, The New Worship, 2nd edition (Grand Rapids: Baker Books, 2001), 123
[2]Imetolewa kutoka kwa Jamie Brown, "Are We Headed For A Crash? Reflections on the Current State of Evangelical Worship." Inapatikana hapa https://worthilymagnify.com/2014/05/19/crash/ July 22, 2020.
[3]Ubora haumaanishi kuwa viongozi waliofunzwa kitaalamu pekee ndio wanaweza kuongoza ibada. Harold Best anafafanua ubora kama "mchakato wa kuwa bora kuliko nilivyokuwa hapo awali." Kwa kuwa ibada ni sadaka yetu kwa Mungu, tunaendelea kutafuta kuwa bora kuliko tulivyokuwa. Harold Best, Music through the Eyes of Faith (San Francisco: Harper Books, 1993), 108
[5]Warren Wiersbe, Real Worship (Grand Rapids: Baker Books, 2000), 215
Hatari za Ibada: “Tunafanya Hivi Kwa Sababu …”
Bibi harusi mpya alikuwa akipika nyama kwa ajili ya chakula cha jioni cha Jumapili. Kabla ya kuweka nyama kwenye jiko la umeme, alikata kwa uangalifu sehemu ya mwisho ya nyama na kuiweka kwenye sufuria ndogo. Mume wake akamuuliza, “Kwa nini unafanya hivyo?”
"Hivyo ndivyo unavyotakiwa kupika nyama ya nguruwe. Mama yangu daima alikata sehemu ya mwisho ya nyama kabla ya kupika. Nadhani inasaidia ladha." Bibi-arusi mpya akaanza kujiuliza, “Kukata kipande cha nyama inaongezaje ladha yake?” Alimwita mama yake kuuliza, "Kwa nini unakata sehemu moja ya mwisho ya nyama?"
Mama yake alisema, “Kwa sababu bibi yako, mama yangu, kila mara alikata sehemu moja ya mwisho ya nyama kabla ya kupika. Lazima iongeze ladha. Hebu tumuulize yeye.”
Bibi arusi alimuita bibi yake mwenye umri mkubwa. Bibi hakupika tena, lakini alijibu swali lao. "Ndio, ninakumbuka kwa nini nilikata sehemu ya mwisho ya nyama. Mimi na babu yako tulipooana, hatukuweza kumudu sufuria nyingi za kupikia. Sufuria yangu pekee ya kuchoma nyama ilikuwa ndogo. Nyama ya nguruwe isingetosha kwenye sufuria yangu isipokuwa niikate sehemu moja!”
Kwa miaka 50 mtoto wake na kisha mjukuu wake walikuwa wameendeleza “desturi” ambayo haikuwa na maana yoyote. Hawajawahi kuuliza, "Kwa nini?"
Kama viongozi wa ibada, wakati mwingine tunafanya mambo bila kuzingatia "Kwa nini?"
Sababu za kanisa kufanya mambo kwa njia maalum:
1. Makanisa ya zamani yalifanya hivyo. Kuna thamani katika mila. Ikiwa makanisa ya zamani yalifanya jambo fulani, hatupaswi kulitupa nje bila kuuliza, “Kwa nini walifanya hivyo?” Tunaweza kupata sababu nzuri ya kuhifadhi mapokeo; lakini ikiwa “makanisa ya zamani walifanya hivyo” ndiyo sababu pekee tu, hakika inaweza isiwe sababu ya kutosha.
2. Makanisa makubwa hufanya hivyo. Kuna umuhimu wa kujifunza kutoka kwa wengine. Ikiwa jambo linafanya kazi vizuri katika makanisa mengine, tunapaswa kuuliza, “Je, jambo hilo lina manufaa kwetu? Kwa nini wanafanya hivyo?” Tunaweza kugundua kwamba kuna sababu nzuri ya kuiga desturi ya ibada; lakini ikiwa “makanisa makubwa yanafanya hivyo” ndiyo sababu pekee tu, hakika inaweza isiwe msaada kwa hali yetu.
3. Watu wanapenda. Kuna faida ya kuwa na ibada inayohamasisha ushiriki wa watu. Hakuna kitu katika Maandiko kinachosema, "Ibada yako inapaswa kuwa ya kuchosha!" Tunaweza kugundua kwamba wimbo unaopendwa na watu wetu ni wa kweli na ni wa kuabudu. kama ndivyo, hiyo ni nzuri; lakini ikiwa watu wanapenda wimbo unaofundisha mafundisho ya uwongo, hatupaswi kuuimba.
4. Inaturuhusu kumwabudu Mungu katika roho na kweli. Hii ndiyo sababu kuu ya kile tunachofanya. Katika kupanga ibada na kuongoza ibada, tunapaswa kuuliza, “Je, wimbo huu unatusaidia kumwabudu Mungu vyema zaidi? Je, utaratibu huu wa ibada unatupeleka katika uwepo wa Mungu? Je, mwaliko utakuwa njia bora zaidi ya kuitikia mahubiri haya, au tumalizie kwa wimbo wa sifa? Je, tunamwabuduje Mungu katika roho na kweli wiki hii?"
Hitimisho: Tunaposhindwa katika ibada
Kanisa liliimba wimbo wa ufunguzi kwa shauku ndogo. Kwaya ilikuwa imefanya mazoezi, lakini waliimba vibaya asubuhi hiyo. Mwimbishaji alisahau maneno. Mpiga kinanda alicheza noti zisizo sahihi. Mahubiri ya mchungaji hayakuonekana kugusa watu. Ibada ilikuwa janga. Je, imewahi kukutokea? Unafanya nini unaposhindwa kuongoza ibada?
(1) Kumbuka, ibada zote ni mazoezi.
Ibada yetu ni mazoezi ya ibada ya mbinguni. Sisi ni watu wasio wakamilifu, na ibada yetu itakuwa isiyokamilika sikuzote. “Tumeitwa kutoa kilicho bora katika ibada, na sio kutoa kilicho kamilika.”[1]
(2) Wiki Ijayo Inakuja.
Usijiuzulu Jumatatu. Subiri hadi Jumanne ili kutathmini Ibada. Jifunze kutokana na makosa na uendelee mbele. Katika ibada iliyoelezwa hapo juu, wimbo wa ufunguzi haukufahamika kwa waumini wa kawaida. Kiongozi alidhani wanaujua wimbo huo; lakini sivyo. Aliandika maandishi katika wimbo wake, “Fundisha kwaya wimbo huu kabla ya mkutano kuuimba tena.” Jifunze kutokana na makosa yako, tafuta msaada wa Mungu, na umruhusu Mungu afanye kazi kupitia wewe Jumapili ijayo.
(3) Kumbuka, kuabudu ni neema.
Viongozi wengi wa ibada ni wapenda ukamilifu; hatutosheki. Ibada haihitaji ukamilifu; kuabudu ni neema. Mungu hufanya kazi hata kwa kushindwa kwetu ili afikie malengo yake. Hivi ndivyo inavyopaswa kuwa! Tunapotambua kwamba ni Mungu anayetuwezesha kuabudu, tunaletwa mahali pa unyenyekevu na utii.
(4) Ikiwa tumejitolea kwa uwezo wetu wote, hatujashindwa.
Jumapili hiyo, kiongozi wa ibada alitoka nje ya kanisa akiwa amekata tamaa. Alipokuwa akiondoka kwenye jengo hilo, Timotheo alikuwa akimngoja. Timotheo alikuwa mwenye aibu na sio mzungumzaji, lakini asubuhi hiyo alisema, “Uliimba wimbo unasema ‘Yesu Ananipenda’ alijitoa dhabihu kwa ajili yangu.” (Ndiyo, kiongozi wa ibada alijua wimbo alioimba - alikuwa ameharibu!) Lakini Timotheo aliendelea, "Nilihitaji kusikia wimbo huo. Wiki hii daktari aliniambia kuwa nina saratani; Nilihitaji kukumbushwa kwamba Yesu ananipenda.”
Ikiwa tumejitolea kwa uwezo wetu wote, hatujashindwa. Mungu anafanya kazi kupitia jitihada zetu dhaifu za kusema Neno lake kwa watu tunaowatumikia.
► Majadiliano ya kikundi. Angalia "Mapitio ya Somo la 8." Je, kuna hoja zozote ambazo hukubaliani nazo? Ni hoja gani unahisi ni muhimu zaidi kwa matumizi yako ya haraka?
[1]Nukuu hii na mapendekezo katika sehemu hii yanatokwa kwa Franklin Segler na Randall Bradley, Christian Worship (Nashville: B&H Publishing, 2006), 274-275.
Maandalizi kwa ajili ya ibada huanza na kujiandaa kwa kiongozi wa ibada kwa kutumia muda wake kwenye Neno.
Utaratibu wa kupanga husaidia kutoa muundo kwa huduma ya ibada.
Mada kwenye ibada husaidia kuwasilisha ujumbe muhimu.
Uwiano hukakikisha ibada yetu huzungumzia injili yote kwa kanisa zima.
Ibada yenye uwiano huonesha ukuu wa Mungu na uwepo wa Mungu kwetu.
Ibada yenye uwiano ni ya pamoja na binafsi.
Ibada yenye uwiano hujumuisha yale yanayofahamika nay ale yasiyofahamika.
Kupanga kwa ajili ya ibada kunapaswa kujumuisha timu ya viongozi wote wa kanisa.
Kupanga kwa ajili ya ibada inapaswa kuangalia muda mrefu.
Tunaweza kupanga bila shinikizo kwa sababu ibada haituhusu; ni kuhusu Mungu.
(2) Ni nini muhimu katika kuongoza ibada?
Msikilizaji muhimu zaidi katika ibada ni Mungu.
Kanisa, viongozi wa ibada, na Mungu wote hushirikiana katika ibada. Viongozi hawafanyi ibada kwa wasikilizaji.
Kiongozi wa ibada lazima aabudu. Huongoza kwa mfano.
Kiongozi wa ibada anapaswa kuwa mwenye kutia moyo, si kuhukumu.
Kiongozi wa ibada lazima aongoze, sio kuigiza.
Matangazo yanapaswa kushughulikiwa kwa njia isiyoleta usumbufu iwezekanavyo.
Baada ya kupanga ibada, tunapaswa kumwachia Mungu aingie katika huduma zetu kwa njia anayochagua kuja.
Somo la 8 Mazoezi
(1) Katika Somo la 6 na 7, ulichagua nyimbo na maandiko juu ya mada tano tofauti. Panga ibada kulingana na kila moja ya mada tano. Kuwa na maelezo ya kina iwezekanavyo katika kupanga ibada ya umoja, ikijumuisha nyimbo za kutaniko, maandiko, mada ya mahubiri na maandishi, pamoja na vitu vingine vyovyote vinavyofaa kwa ibada yako. Tumia muhtasari mmoja au zaidi uliotolewa katika Kiambatisho A kwa mradi huu.
(2) Mwanzoni mwa somo linalofuata, utafanya mtihani kulingana na somo hili. Jifunze maswali ya mtihani kwa uangalifu katika maandalizi.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.