Utangulizi wa ibada ya Kikristo
Utangulizi wa ibada ya Kikristo
Audio Course Purchase

Search Course

Type at least 3 characters to search

Search through all lessons and sections in this course

Searching...

No results found

No matches for ""

Try different keywords or check your spelling

results found

Lesson 3: Kuabudu katika Agano la Kale

24 min read

by Randall McElwain


Malengo ya Somo

Mwisho wa somo hili, mwanafunzi anapaswa:

(1) Kuthamini neema ya Mungu inayowezesha ibada.

(2) Kukaribia ibada kwa moyo wa utii.

(3) Kufahamu jukumu la matendo ya ibada.

(4) Kufanya sifa kama kipengele muhimu cha ibada.

(5) Kutambua umuhimu wa kuhubiri Neno la Mungu katika ibada.

(6) Kuepuka hatari ya kutokuwa na uwiano katika ibada.

Matayarisho kwa somo hili

Kariri Mika 6:6-8.

Utangulizi

Kikundi kimoja cha wachungaji hukutana kila mwezi kujadili masuala katika makanisa yao. Hivi karibuni wamejadili ibada. Kuna tofauti kubwa kati ya hawa wachungaji kuhusu suala la ibada. Ingawa wanashiriki imani za doktrini sawa, wanatofautiana sana katika mitindo ya ibada.

Yakobo ni mchungaji wa kanisa linalofuata desturi za zamani katika ibada. Enoki anahudumu katika kanisa linalokua ambalo hutumia mawazo mengi ya kisasa katika ibada. Gideoni bado anajaribu kupata aina ya ibada inayofaa zaidi kwa kanisa lake. Wachungaji hawa wamekuwa na mazungumzo mengi kuhusu ibada, lakini wanahisi kuchanganyikiwa katika juhudi zao za kukubaliana juu ya kanuni za msingi za ibada.

Leo, Jasoni anasema, "Labda tumekuwa tukiliangalia hili vibaya. Tunaendelea kujiuliza, ‘ni aina gani ya ibada tunayoifurahia? Tunataka kufanya ibada vipi?' Labda tunapaswa kujiuliza, 'Mungu anataka tuabudu vipi? Aina gani ya ibada anayoifurahia? Kama Mungu angebuni ibada, ingekuwa vipi?' Ikiwa tutajifunza jinsi ibada ilivyokuwa katika Biblia, hiyo inaweza kutupa mfano wa ibada leo."

► Ikiwa Mungu angebuni ibada, ingekuwa vipi? Eleza kile unachokijua kuhusu ibada kulingana na Biblia.

Utangulizi: Mungu Anahitaji Ibada Sahihi

Katika Somo la 2, tuliona kutoka katika Ufunuo kwamba ibada ya kweli ni ibada kwa Mungu mtakatifu. Tuliona kutoka katika Zaburi 15 kwamba Mungu anahitaji wanaomwabudu wawe watakatifu. Katika Somo la 3, tunajiuliza, "Mwabudu anawezaje kumkaribia Mungu mtakatifu?"

Baadhi ya watu husema kwamba Mungu hajali jinsi tunavyomwabudu; anajali tu kwamba moyo uko sawa. Ni kweli kwamba moyo ni msingi wa ibada. Hata hivyo, tuna ushuhuda wa kutosha kutoka katika Maandiko kwamba Mungu anajali sana jinsi anavyoabudiwa.

Aina ya ibada ni muhimu kwa sababu ibada yetu inaathiri ufahamu wetu kumhusu Mungu. Katika somo lililopita, tuliona kwamba picha iliyopotoshwa ya Mungu husababisha ibada iliyopotoshwa. Ni kweli pia kwamba ibada iliyopotoshwa hupotosha taswira yetu kuhusu Mungu. Wakati Israeli walipomwabudu Yehova kama vile Wakanani walivyoabudu miungu yao, ndipo walianza kuamini kwamba asili ya Mungu ilikuwa kama miungu ya Wakanani. Walianza kuamini kwamba Mungu alikuwa mkali na asiyeaminika, kama miungu ya Wakanani.[1]

Aina ya ibada ni muhimu kwa sababu jinsi tunavyoabudu mara nyingi ni kielelezo cha kwa nini tunamwabudu. Moyo wa upendo unafurahi kuleta ibada inayomheshimu Mungu; moyo wa utii kwa shingo upande unataka kufanya ibada kwa njia yangu badala ya njia ya Mungu.

Madarasa mengi ya vyuo vikuu huwa wanataka aina fulani ya dodoso la karatasi za utafiti. Wanahitaji ukurasa wa kwanza, rejea, na upana fulani wa ukurasa. Maelezo haya si sehemu muhimu zaidi ya utafiti; maudhui ndiyo muhimu zaidi. Hata hivyo, walimu wengi wameona kwamba mwanafunzi anayejali maelezo kiundani huwa mwangalifu kuhusu maudhui; anataka kufanya vizuri zaidi. Kwa upande mwingine, mwanafunzi anayeipuuza matakwa haya mara nyingi ni mkaidi kuhusu maudhui. Aina ya karatasi la dodoso mara nyingi linarefusha maudhui ya karatasi. Njia tunayoabudu mara nyingi inaakisi mtazamo wa mioyo yetu. Jinsi tunavyoabudu mara nyingi inahusiana na sababu yetu ya kuabudu. Kwa sababu hii, Mungu anajali jinsi tunavyoabudu.

  • Kaini alileta sadaka kwa Bwana. Kaini alikuwa mkulima wa ardhi. Alileta matunda ya ardhi, lakini Bwana hakumtazama Kaini wala sadaka yake. Kukosekana kwa Kaini kumwabudu kwa usahihi kulionesha mtazamo wa moyo wake. Sadaka ya Kaini ilikuwa rahisi kwake mwenyewe, lakini Mungu hakukubali ibada yake (Mwanzo 4:1-5).

  • Haruni alijenga ndama wa dhahabu kutumika katika ibada kwa Yehova. Alisema, "Kesho itakuwa sikukuu kwa BWANA" (Kutoka 32:1-5). Labda Haruni alijishawishi kwamba angeweza kumwabudu Mungu kwa njia inayopendeza watu, lakini Mungu hakukubali ibada yake.

  • [2]Nadabu na Abihu walimuona Mungu wa Israeli katika Mlima Sinai (Kutoka 24:1-11). Walikuwa karibu na Mungu kuliko mtu yeyote isipokuwa Musa, lakini siku yao ya kwanza ya huduma ya ukuhani katika Maskani, walitoa moto usio halali mbele za Bwana. Kama jibu, moto kutoka kwa Bwana uliwaangamiza. Musa alieleza hukumu ya Mungu kwa Mungu baba yao mwenye huzuni; "Jambo hili ni hilo BWANA alilolinena, akisema, Nitatakaswa mimi katika hao wanikaribiao, nami nitatukuzwa mbele ya watu hao wote" (Mambo ya Walawi 10:1-7) Makuhani hawa walitoa uvumba kwa njia yao wenyewe, badala ya kufuata amri za Mungu. Mungu hakukubali ibada yao.

  • Uzia alikuwa mfalme mkuu. Alichokifanya kilikuwa kizuri machoni pa Bwana. 2 Mambo ya Nyakati yanahitimisha utawala wake: "... kwa kuwa alisaidiwa mno ajabu, hata akapata nguvu" (2 Mambo ya Nyakati 26:15). Kwa kusikitisha, hii sio mwisho wa hadithi ya Uzia. "Lakini alipokuwa na nguvu, moyo wake ulitukuka, hata akafanya maovu, akamwasi BWANA, Mungu wake; kwani aliingia hekaluni mwa BWANA, ili afukize uvumba juu ya madhabahu ya kufukizia" (2 Mambo ya Nyakati 26:16). Alijaribu kumwabudu Mungu kwa njia yake mwenyewe na akapigwa na ukoma (2 Mambo ya Nyakati 26:1-21). Mungu hakukubali ibada yake.

  • Wayahudi baada ya kuondoka uhamishoni walileta sadaka za vilema Hekaluni. Kukosekana kwao kuleta dhabihu sahihi kulionesha mtazamo wa kutokujali wa mioyo yao. Hawakumpenda kweli Mungu, kwa hivyo Mungu hakukubali ibada yao (Malaki 1:6-14).

Mungu hujali jinsi anavyoabudiwa. Mifano hii inaonesha kwamba, tukiachwa wenyewe, hatutamkaribia Mungu kwa njia inayomheshimu. Kile kinachoonekana kuwa sahihi kwetu kinaweza kutokuwa kinakubalika kwa Mungu. Lazima tuwe na mwongozo wake katika ibada yetu.

Kwa kuwa ibada maana yake ni kumpa heshima Mungu, ibada yetu lazima iwe inafuata tabia za Mungu badala ya tamaa zetu. Hatuwezi kujua wenyewe ni nini kinachompendeza Mungu; lazima tutazame Neno la Mungu ili kujifunza jinsi ya kuabudu kwa njia inayompendeza Mungu.


[1]Katika Mika 6:6-7, "Viongozi wa kidini wanajaribu kumhonga Yehova kwa dhabihu za watoto. Wanadhani kwamba Yehova anatarajia dhabihu za watoto ambazo Moleki alidai.".
[2]

"Kama ungekuwa kuhani wa Agano la Kale, na ukamtumikia Mungu kama unavyomtumikia sasa, itakuwa muda gani kabla Bwana hajakuua?"

- Warren Wiersbe (kutokana na umuhimu wa ibada)

Kuambatana na Mungu: Ibada kama Uhusiano wa Neema

Picha ya kwanza ya ibada katika Biblia inapatikana katika Bustani ya Edeni, "Wakasikia sauti ya BWANA Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga..." (Mwanzo 3:8) Hii inaonyesha kusudi la Mungu kwa ibada: ushirika usiovunjika kati ya mwanadamu na Muumba wake. Kabla ya Kuanguka, ushirika kati ya mwanadamu na Mungu haukuzuiliwa na dhambi. Ibada katika Bustani ilikuwa rahisi na isiyopata utata.

Katika Bustani, tunaona kwamba Mungu anatamani ushirika na viumbe vyake. Hadi Kuanguka, mwanadamu alifurahia ushirika kamili na Mungu; ilikuwa tu baada ya dhambi kuharibu asili ya mwanadamu ndipo mwanadamu alijificha mwenyewe kutoka kwa Mungu.

Katika Agano la Kale, neno "alitembea pamoja na Mungu" hutumiwa kuonyesha kwamba ibada inajumuisha uhusiano na Mungu. Henoko alitembea na Mungu; Nuhu alitembea na Mungu; Ibrahimu aliagizwa kutembea na Mungu (Mwanzo 5:24, Mwanzo 6:9, Mwanzo 17:1). Kila mfano huu unaonesha mtu ambaye alijenga uhusiano kwa kutumia muda pamoja na Mungu. Ibada sahihi inategemea uhusiano sahihi na Mungu.

Mwanzo 3:8 inaonesha kwamba ibada ilikuwa msingi wa uhusiano. Pia inaonesha kwamba ibada inawezekana tu kwa sababu ya neema ya Mungu. Miungu wa kipagani walitarajia mwanadamu apate njia ya kufanya ibada ipasavyo ili kuwafurahisha miungu. Kinyume chake, Yehova kwa neema alitoa njia sahihi ya ibada. Mifano mitatu inaonyesha hili.

Mungu Aliwezesha Ibada Kwa Adamu na Hawa

Baada ya kuanguka, Mungu hakuwa na jukumu la kutafuta au hata kukubali ibada kutoka kwa Adamu na Hawa. Walikuwa wamevunja sheria ya Mungu; walikuwa wameharibu uumbaji wake; hawakustahili chochote ila hukumu.

Baada ya kutenda dhambi, Adamu na Hawa walijificha kutoka mbele za Bwana (Mwanzo 3:8). Hakukuwa na hatua nyingine kwa Adamu na Hawa; hawakutarajia chochote ila kifo. Majibu pekee waliyoyajua ilikuwa kujificha kutoka kwa Mtoaji wa Sheria, lakini kwa neema Bwana Mungu alimwita Adamu. Ibada inawezekana kwa neema ya Mungu. Tukiachwa wenyewe, hatuna njia ya kumkaribia Mungu mtakatifu. Ni kupitia neema yake pekee tunaitwa kwa ibada.

Mungu aliwezesha Ibada kwa Abraham

► Soma Mwanzo 18:1-8.

Katika Somo la 1, tuliona kwamba moja ya maneno ya Kiebrania kwa ibada (Shachah) lina maana ya "kusujudu" au "kuabudu." Neno hili linatumika kwa mara ya kwanza katika Mwanzo 18:2. Bwana na malaika wawili walionekana wakati Abramu alipokuwa ameketi mlangoni mwa hema yake. Abramu alikimbia kutoka mlangoni mwa hema ili kukutana nao na akainama mpaka nchi. Ibrahimu akainama—aliwaabudu.

Kumbuka kwamba Mungu alichukua hatua ya kwanza katika simulizi hii; alikuja kukutana na Ibrahimu. Mungu alifanya ibada iwezekane. Katika Agano la Kale kama ilivyo katika Agano Jipya, ibada inawezekana tu kwa neema. Dhabihu za Agano la Kale si njia ya kumtuliza Mungu mwenye hasira ambaye hataki uhusiano; bali zilipangwa na Mungu mwenyewe kama njia ya upatanisho kati ya Mungu na mwanadamu mwenye dhambi. Hata katika Agano la Kale, ibada inawezekana tu kupitia neema ya Mungu. Ndani yetu wenyewe, hatuna uwezo wa kuabudu ipasavyo.

Mungu aliwezesha Ibada kwa Yakobo

► Soma Mwanzo 28:10-22. Je, simulizi hii inafunua nini kuhusu jukumu la Mungu katika ibada?

Moja ya picha za kushangaza zaidi za ibada katika Biblia inapatikana katika Mwanzo 28:10-22. Hakuna kitu katika maisha ya nyuma ya Yakobo kinachoonesha sifa za mwabudu. Hapitani na sifa za Zaburi 15. Hamtafuti Mungu; kwa kweli, anakimbia matatizo aliyoyasababisha kwa matendo yake ya udanganyifu. Hakuna kitabu chochote kinachohusu ibada kinachosema, "Ibada inayokubalika inatoka kwa wadanganyifu wanaokimbia matokeo ya dhambi zao wenyewe."

Hata hivyo, Mungu alijidhihirisha kwa Yakobo licha ya kutostahili kwake. Neema ya Mungu hufanya ibada iwezekane hata kwa mtu asiye na sifa kama Yakobo. Warren Wiersbe aliandika, "kwa neema Mungu hutuingilia wakati hatutarajii ‒ au hata hatustahili. Wakati ibada inapoacha kuwa jambo la neema, inaacha kuwa suala la utukufu."[1]

Ni kwa neema tu kwamba Mungu anatualika katika uwepo wake. Ibada yetu ni mwitikio wa neema yake. Hakuna kitu tunachofanya katika ibada kinachostahili kwake; isipokuwa ni neema yake tu inayotuwezesha kuabudu.

[2]Simulizi ya Yakobo inaonesha moja ya tofauti kubwa kati ya ibada ya Yehova na ibada ya miungu ya uongo. Waabudu wa miungu ya uongo walijenga madhabahu kwa kujaribu kupata kibali cha mungu wao. Kwenye Mlima Karmeli, manabii wa baali "Wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri, wakisema, Ee Baali, utusikie. Lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu. Nao wakaruka-ruka juu ya madhabahu waliyoifanya" (1 Wafalme 18:26).

► Soma 1 Wafalme 18:20-39 ili kuona tofauti kati ya ibada ya kweli na ibada ya uongo.

Manabii wa baali walijaribu kumshawishi baali ajidhihirishe kwao. Mfano huu unaonekana mara kwa mara katika ibada ya sanamu. Madhabahu na dhabihu ni jaribio la kupata kibali cha sanamu.

Kinyume chake, Mungu kwa neema hujidhihirisha kwa watu wake katika ibada. Eliya alijenga madhabahu yake kwa kujiamini kabisa kwamba Mungu anayemtumikia angejibu maombi yake.

Ee Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako (1 Wafalme 18:36).

Katika kitabu cha Mwanzo, mababa wa imani walijenga madhabahu si kwa ajili ya kuvuta umakini wa Mungu bali kama kumbukumbu za sehemu ambazo Mungu alijidhihirisha. Madhabahu haikupata kibali cha Mungu; ilisherehekea neema yake. Yakobo anatufundisha kwamba ibada inawezekana tu kwa neema. Hatupaswi kamwe kufikiria kwamba ibada yetu inatufanya tustahili kupata kibali cha Mungu; tunaabudu kwa sababu ya neema.

Je, ni kitu gani hutokea Mungu anapofanya ibada iwezekane? Yakobo alibadilishwa. Ilipita miaka 30 kabla ya mabadiliko haya kukamilika, lakini mabadiliko yalianza Betheli. Ibada (hata ibada isiyo kamilifu ya mtu asiye kamilifu kama Yakobo) inatubadilisha na kutufanyia yale ambayo hatuwezi kujifanyia wenyewe.

Kujipima

Hebu jiulize, "Je, ninabadilishwa na ibada, au ninapitia tu hatua zisizo na maana? Ni lini mara ya mwisho nilibadilisha matendo yangu, imani zangu, au mitazamo yangu kwa sababu ya kukutana na Mungu katika ibada?"


[1]Warren W. Wiersbe, Real Worship, (Grand Rapids: Baker Books, 2000), 72
[2]

Katika ibada ya uongo, mtu hujenga madhabahu ili kupata upendeleo wa sanamu (kazi).

Katika ibada ya kweli, mtu hujenga madhabahu kusherehekea upendeleo wa Mungu (neema).

Ibrahimu: Ibada inahitaji Utii

► Soma Mwanzo 22:1-19. Je, ni mahitaji gani ya ibada katika simulizi hii?

dhabihu ya Ibrahimu ya kumtoa mwanawe ilikuwa kitendo kikuu cha ibada. Katika simulizi hii, angalia mkazo juu ya utiifu wa Ibrahimu. Mungu alisema, “Umchukue mwanao… ukaende… ukamtoe sadaka…” Amri tatu. Ibrahimu “alimchukua mwanawe Isaka... akaondoka na kwenda... na akachukua kisu ili amchinje mwanawe.” Ibrahimu alitii kila amri.

Sadaka ya Ibrahimu ya Isaka inaonesha kwamba ibada ya kweli inahitaji utiifu kamili. Ibada ni zaidi ya hisia au mhemko; ibada ni zaidi ya kumsikiliza mwimbaji au mhubiri; ibada ni mwitikio hai kwa Mungu.

Rudi kwenye simulizi ya Ibrahimu katika Mwanzo 18. Mwanzoni mwa simulizi, tunaona ibada kama huduma ya utiifu. Ibrahimu aliona wageni watatu wakikaribia kambi yake. Aliinama mpaka chini. Aliabudu.

Kisha tunaona Ibrahimu akiwa na shughuli nyingi za kuhudumu. Alitoa maji ili kuosha miguu yao; alikimbilia ndani ya hema ili Sara aoke mikate; aliandaa chakula na kuwawekea. Akiwa katika nafasi ya mtumishi anayesubiri, alisimama karibu nao chini ya mti wakati walipokuwa wanakula. Hii yote ni lugha ya mtumishi anayetoa huduma bora kwa bwana wake. Mwabudu wa kweli ana mtazamo wa huduma ya hiari.

Umuhimu wa utiifu katika ibada unaonekana katika Agano la Kale lote. Sadaka ya Abeli ilikubaliwa kwa sababu ilikidhi mahitaji ya Mungu kwa sadaka. Abeli alileta mzaliwa wa kwanza wa kundi lake na sehemu zao za mafuta (Mwanzo 4:4). Abeli alileta kwa utiifu kilicho bora zaidi. Kinyume chake, Kaini alitaka kutimiza wajibu wake kwa njia rahisi iwezekanavyo.

Umuhimu wa utiifu katika ibada unaonekana katika maisha ya Sauli. Wakati Sauli alipokosa kutii amri ya Mungu ya kuharibu wanyama wote wa Amaleki, alijaribu kujisamehe kwa kudai kwamba wanyama bora wamehifadhiwa kwa ajili ya sadaka. “Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia ushauri kuliko mafuta ya beberu” (1 Samweli 15:22).

► Soma 1 Samuel 15:1-23.

Mungu hatakubali ibada kutoka kwa moyo wa uasi.

Ibada ya kweli inachochea uhusiano wa kina na Mungu. Angalia tena simulizi ya Ibrahimu. Mwanzo 18 inaanza na huduma ya Ibrahimu kwa Mungu; sura hiyo inaisha na uhusiano. Bwana aliuliza, “Je! Nimfiche Abrahamu jambo ambalo ninataka kulifanya...?” Baada ya kusikia nia ya Mungu, Ibrahimu alijadiliana kwa ujasiri na Mungu juu ya hatima ya Sodoma. Nini kilitokea? Tunaona kuwa mtumishi wa Mungu pia ni rafiki wa Mungu.

Ni katika ibada tunapomjua Mungu kwa kweli. Ni katika ibada tunapojifunza moyo wa Mungu hadi tunapoweza kuomba kwa ujasiri. Ni katika ibada ya utiifu ambapo uhusiano wetu na Mungu unakua kwa kina. Ibada inayokubalika inajumuisha utiifu (huduma) na uhusiano. Ibrahimu mwabudu ni mtumishi wa Mungu na pia ni rafiki wa Mungu.

Ibada ya Kibiblia Siku Hizi

Je, umewahi kujiuliza kwa nini baadhi ya watu wanahudhuria ibada na kujionea uwepo wa Mungu wakati wengine wanahudhuria ibada hiyo hiyo na hawaoni chochote cha Mungu? Baadhi wanatoa sadaka na kubarikiwa; wengine wanatoa na hawana furaha. Hapo tofauti ni moyo mtiifu.

Haijalishi ibada yetu ni nzuri kiasi gani, haijalishi wanamuziki ni wenye vipaji kiasi gani, haijalishi mahubiri ni yenye nguvu kiasi gani, ikiwa ibada haitoki kwa moyo mtiifu, ni ibada ya Kaini. Ibada ya Kaini inasema, “Ninaweza kuleta sadaka yangu kwa njia yangu mwenyewe. Inatosha.” Ibada ya kweli inatoka kwa moyo mtiifu.

Kujipima

Jiulize, “Je, mimi ni mwabudu mtiifu? Je, ibada yangu inatoka kwa moyo wa Abeli au moyo wa Kaini?”

Dhabihu: Ibada kama taratibu

Kabla ya Anguko, ibada ilifanyika katika uhusiano rahisi kati ya Mungu na mwanadamu. Baada ya dhambi kuharibu asili ya mwanadamu, mwanadamu alihitaji mchakato wa kuingia katika uwepo wa Mungu. Kwa neema, Mungu alitoa mfumo wa dhabihu. Dhabihu ziliwekwa na Mungu bustanini alipoua mnyama na kutumia ngozi yake kutengeneza mavazi kwa Adamu na Eva. Kitabu cha Mambo ya Walawi kiliweka mfumo wa dhabihu kwa ajili ya ibada ya Israeli (Mambo ya Walawi 1-7 na 16).

Tunaposoma katika kitabu cha Kutoka na Mambo ya Walawi, inakuwa wazi kwamba maelezo ya ibada ni muhimu kwa Mungu. Kwa wale wanaosema kwamba “Mungu hajali jinsi tunavyoabudu mradi tu tuabudu,” vitabu vya Kutoka na Mambo ya Walawi vinaonesha kwamba jinsi tunavyoabudu ni muhimu kwa Mungu! Mungu alitoa maagizo ya wazi kwa ajili ya ibada. Hii ni kama ufunuo wa Mungu kwa Adamu na Eva baada ya Anguko, ni ishara ya neema ya Mungu. Yehova alitoa maagizo ya wazi, “Hivi ndivyo mnavyopaswa kunikaribia.” Hili lilikuwa tendo la neema.

Kwa Israeli, ibada ilianza kabla hawajaingia katika nyumba ya Mungu. Mchakato wa kujiandaa kwa ajili ya ibada ulionesha heshima yao kwa Mungu na nyumba yake. Nyimbo za Maandalio katika Zaburi zinaonesha kwamba hata safari ya kwenda Yerusalemu ilikuwa ibada (Zaburi 120-134). Taratibu za ibada hazikuwa tupu; kila kipengele cha dhabihu kilimkumbusha mwabudu umuhimu wa ibada ya kweli.

Dhabihu Ziliwakilisha Kujisalimisha Kikamilifu kwa Mungu

Baadhi ya Wakristo wamekosea kuelewa mfumo wa dhabihu wa Agano la Kale. Wanadhani ni mfumo ambao Waisraeli waliweza kukiuka sheria ya Mungu kwa hiari, halafu wakaleta dhabihu isiyo na maana, kisha mara moja wakarudi kwenye dhambi zilezile bila mabadiliko ya moyo.

Ni kweli kwamba hili lilitokea katika baadhi ya mazingira. Kwa kujibu hilo, Mungu alisema, “Mimi nazichukia sikukuu zenu, nazidharau, nami sitapendezwa na makutano yenu ya dini. Naam, ijapokuwa mnanitolea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za unga, sitazikubali” (Amosi 5:21-22).

Hata hivyo, hii ilikuwa ni kushindwa kwa mwanadamu, si kwa Mungu. Mfumo wa dhabihu ulishindwa wakati mwanadamu aliposhindwa kufanya kile ambacho Mungu aliamuru. Mpango wa Mungu ulikuwa ni dhabihu ambazo zinaakisi toba ya kweli ya moyo.

Taratibu zinazohusiana na sikukuu zilionesha Israeli umuhimu wa matendo ya ibada. Kila kila kitu kilionesha heshima ya Israeli kwa Yehova. Ibada ya Israeli haikuwa taratibu tupu; taratibu hizi zilionesha ukweli wa kujisalimisha na utiifu wao. Kwa kuweka mikono yake juu ya kichwa cha mnyama, mwabudu alijitambulisha na kifo cha sadaka. Kwa kufanya hivyo, alikuwa anakiri, “Huyu anapaswa kuwa mimi. Dhambi yangu inastahili kifo” (Rejea Mambo ya Walawi 1:4).

Mungu Alitukuza Ibada ya Kweli kwa Uwepo Wake

Kwa kujengwa kwa Hekalu, Ibada ya Israeli ilipangwa zaidi. Kama Maskani ilivyo, kila jambo katika Hekalu liliashiria utiifu wa heshima ya Israeli kwa Mungu (2 Mambo ya Nyakati 1-7). Uzito wa dhabihu na umakini wa ibada ya Hekalu uliwakumbusha Israeli ukuu wa Yehova na unyenyekevu ambao walipaswa kumkaribia.

Mipango makini ya taratibu za ibada kwa ajili ya Hekalu haikuzuia uwepo wa Mungu. Mojawapo ya ibada zilizoandaliwa zaidi katika historia, yaweza kuwa ni ile ya kuweka wakfu Hekalu. Daudi alikuwa amepanga Hekalu miaka mingi kabla. Baada ya Hekalu kukamilika, Sulemani aliongoza ibada nzuri ya kuweka wakfu jengo kama iliyoelezewa katika 2 Mambo ya Nyakati 5. Wanamuziki walipiga matoazi, vinubi, na vinanda. Makuhani 120 walipiga tarumbeta. Kwaya iliimba nyimbo za sifa. Walipoimba, “ndipo nyumba ikajawa na wingu, naam, nyumba ya BWANA, hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya lile wingu; kwa kuwa nyumba ya Mungu imejaa utukufu wa BWANA” (2 Mambo ya Nyakati 5:13-14).

Ibada ya Kibiblia Siku hizi

Baadhi ya watu wanapinga muundo na namna yeyote katika ibada. Wanaamini kwamba liturujia yoyote iliyoandaliwa inazuia ibada ya moyo. Hata hivyo, tunaona ibada ya Kibiblia ilikuwa na muundo.

Ikiwa tunajitahidi kumletea Mungu kilicho bora, ibada yake inastahili kupangwa kwa umakini. Tunapanga ibada si kwa ajili ya kuwashangaza wengine kwa uzuri wa ibada yetu, bali kumletea Mungu dhabihu bora ya ibada.

Katika Biblia ibada zote, ibada iliyo na muundo uliopangwa kwa umakini (kama kuweka wakfu Hekalu) na ibada isiyokuwa na muundo (kama mikutano ya makanisa ya nyumbani katika karne ya kwanza) zilibarikiwa na uwepo wa Mungu. Na pia, ibada yenye muundo uliopangwa kwa umakini (kama ibada ya Hekalu wakati wa Yeremia) na ibada isiyo na muundo (kama ibada yenye machafuko ya Korintho) inaweza kufanywa bila uwepo wa Mungu. Swala si kiwango cha muundo; swala ni utii kwa Mungu na njaa ya uwepo wa Mungu.

Kujipima

Jiulize, “Je, ibada yangu ya pamoja na wengine (bila kujali ni ya kawaida au isiyo ya kawaida) inatoka kwa moyo mtiifu?”

Zaburi: Ibada kama Sifa

Kitabu cha Zaburi ni kitabu cha ibada cha Israeli. Kilikuwa kitabu cha nyimbo za sifa; kilikuwa mkusanyiko wa maombi; kilikuwa mwongozo wa ibada sahihi; kilikuwa mwongozo wa maisha ya haki. Kitabu cha Zaburi kilikuwa muhimu katika ibada ya Israeli.

Sifa katika Ibada

[1]Kitabu cha Zaburi kinaonesha kwamba ibada ya kweli inajumuisha msisitizo mkubwa juu ya sifa. Isipokuwa Zaburi ya 88, kila zaburi ina kauli fulani ya sifa. Taratibu za Mambo ya Walawi zinatukumbusha uzito wa ibada ya Kibiblia; zaburi zinatukumbusha furaha ya ibada ya Kibiblia. Zaburi 120-134 zinaonesha furaha ya mahujaji Wayahudi walipokuwa wanakwenda Yerusalemu kwa ibada. Sifa ni kitovu cha ibada.

Sifa iliyopatikana katika kitabu cha Zaburi inaonesha furaha ya ibada ya kweli. Sifa inaonesha furaha yetu katika Mungu. Ibada ya kweli inajumuisha sherehe ya Mungu na matendo yake.

Maombolezo katika Ibada

Zaburi za maombolezo zinaonyesha upande mwingine wa ibada ya Kibiblia; ibada inaruhusu ukweli kamili kati ya mtoaji wa ibada na Mungu. Katika zaburi za maombolezo, mwandishi wa zaburi anaelezea kuchoshwa na udhalimu wa ulimwengu huu. Katika Zaburi 10:1, mwandishi wa zaburi aliuliza, “Ee Bwana, kwa nini wasimama mbali? Kwani kujificha nyakati za shida?” Kwa nini Mungu anaruhusu wafanya mabaya kufanya uasi na kiburi. Kwa sababu ibada inategemea uhusiano na Mungu, mtoaji wa ibada anaweza kusema kwa uaminifu na wazi.

Zaburi ya 10 inamalizika na tangazo la imani katika Mungu.

“Bwana ndiye Mfalme milele na milele; Mataifa wamepotea kutoka nchi yake. Bwana, umeisikia tamaa ya wanyonge, Utaitengeneza mioyo yao, utalitega sikio lako. Ili kumhukumu yatima naye aliyeonewa, Binadamu aliye udongo asizidi kudhulumu” (Zaburi 10:16-18).

Tangazo hili linategemea imani katika Mungu. Ingawa watenda mabaya wanaendelea kutenda udhalimu, mwandishi wa zaburi anazungumza kwa ujasiri kwamba Mungu atafanya yaliyo haki.

Tunaona ukweli huo huo katika kitabu cha Ayubu. Ukweli kama huu unategemea uhusiano wa karibu na Mungu. Hii ni ibada ya kweli, ibada ambayo ni ya kukubaliwa na Mungu.


[1]

“Hakikisha unaendelea kumfurahia Mungu kila wakati.”

- Richard Baxter

Ibada ya kibiblia Siku hizi

Zaburi zinajumuisha aina mbili za nyimbo za sifa. Kanisa letu linapaswa kujumwisha vyote.

  Nyimbo za Sifa ya kutangaza Sifa za Maelezo
Maana Sifa au agizo la kusifu lisiloelekezwa kwa mhusika maalum. Sifa mahususi kwa tabia na matendo makuu ya Mungu
Sentensi ya mfano “Haleluya. Mwimbieni BWANA wimbo mpya, Sifa zake katika kusanyiko la watauwa” (Zaburi 149:1). “Yeye, BWANA, ndiye Mungu wetu; Duniani mwote mna hukumu zake.” (Zaburi 105:7).
Faida ya sifa ya aina hii Inamwalika mwabudu kumtukuza Mungu Humfundisha mwabudu kweli za kina kuhusu asili ya Mungu.
Kwa kawaida hupatikana katika mtindo huu wa wimbo Mapambio Nyimbo za tenzi
Mifano kutoka katika Zaburi Zaburi hizi zinaagiza sifa bila kutoa sababu mahususi: Zaburi 148-150 Zaburi hizi zinaeleza sababu nyingi mahususi za kutoa sifa Zaburi 19, 105, na 136

► Tazama kila mojawapo ya Zaburi sita zilizoorodheshwa hapo juu. Linganisha aina za sifa zinazopatikana katika kila moja

► Tazama mkusanyiko wa tenzi na mapambio katika lugha yako. Tafuta mifano 2–3 ya kila aina ya sifa.

Kujipima

Sifa za mwandishi wa zaburi zinaonesha furaha yake kwa Mungu. Jiulize, "Je, kweli ninamfurahia Mungu?"

Manabii: Ibada kama Kutangaza

Sheria za dhabihu, Maskani, na Hekalu zinaonesha thamani ya utaratibu katika ibada. Hata hivyo, manabii wanaonesha kuwa taratibu ambazo haziendani na ibada ya moyo ni bure. Wakati watu wa Israeli walipoanza kufuata taratibu bila mioyo ya utii, manabii walileta ujumbe wa hukumu kutoka kwa Mungu. Walitangaza kwamba Mungu hakubali tena dhabihu za taifa lililoasi.

Manabii wanaonesha kwamba kutangaza la Neno la Mungu ni ibada. Katika huduma zetu, hatupaswi kutenganisha ibada na mahubiri. Tangazo la Neno ni ibada katika ukweli. Mahubiri yanathibitisha mamlaka ya Mungu juu yetu na hekima yake kwa maisha yetu. Hii ni ibada; inamheshimu Mungu.

Ujumbe wa Manabii

Taratibu bila ukweli si ibada.

Amosi alitangaza kuwa Mungu alikuwa amekataa dhabihu za Israeli. Kwa nini? Kwa sababu maisha ya waabudu yalikuwa ya dhambi (Amosi 5:21-22). Isaya alitangaza kwamba sikukuu za Israeli zilikuwa mzigo wa kuchosha kwa Mungu. Kwa nini? Kwa sababu mikono yake ilikuwa imejaa damu.

Kabla ya kuabudu, waabudu wanaamriwa: “Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane” (Isaya 1:13-17).

Mungu hafurahii taratibu ambazo hazioneshi ukweli wa moyo.

Ibada ya kweli inahitaji bora yetu.

Ibrahimu alimtoa mwanawe kwa Mungu; alitoa bora yake. Habili alileta mzaliwa wa kwanza wa kundi lake; alitoa bora yake. Mambo ya Walawi yalihitaji wanyama bora kwa dhabihu. Daudi alikataa kutoa sadaka ambayo haikumgharimu chochote (2 Samweli 24:24). Katika kila mfano hapo juu, ibada inahitaji bora yetu.

Ujumbe huu unaendelea katika manabii. Malaki aliwaonya dhidi ya kuleta wanyama duni kwa dhabihu (Malaki 1:6-8). Hagai alionya juu ya hukumu kwa sababu watu walijali zaidi hali ya nyumba zao wenyewe kuliko nyumba ya Mungu (Hagai 1:8-11). Ibada ya kweli inahitaji bora yetu.

Ibada ya Kweli Inahusisha Maisha yote.

Amosi alitoa majibu ya kivitendo kwa uasi wa Israeli. Suluhisho halikuwa dhabihu zaidi; suluhisho lilikuwa maisha ya haki. “Lakini hukumu na itelemke kama maji, na haki kama maji makuu” (Amosi 5:24). Manabii hawakupinga ibada ya Hekalu na dhabihu.[1] Walipinga ibada isiyoambatana na maisha ya haki.

Katika Biblia nzima, tunaona kwamba ibada ya kweli inahusisha maisha yote. Katika Pentateuki, sheria kuhusu ibada ziko karibu na sheria kuhusu tabia ya kimaadili; hakuna utengano kati yao. Katika vitabu vya kihistoria, kutotii kwa Israeli katika maisha ya kila siku kunasababisha uharibifu wa mahali pa ibada ya Israeli, Hekalu. Manabii wanatangaza kwamba Mungu amekataa ibada ya Israeli kwa sababu ya kutotii kwake. Katika Agano Jipya, Yesu anakumbusha Mafarisayo kwamba desturi za ibada kama vile utunzaji wa Sabato hazina maana bila maisha ya rehema (Mathayo 12:7).

Mfano wa Manabii: Mahubiri na Kutangazo ni Ibada

Manabii wanaonesha kwamba kutangaza la Neno la Mungu ni ibada. Fikiria upuuzi wa Yeremia kusimama mbele ya Hekalu na kusema, “Nendeni Hekaluni kuimba Zaburi na kutoa dhabihu zenu. Hiyo itakuwa ibada. Mkimaliza, nitawahubiria ujumbe wa Mungu.” Hapana! Tangazo la Yeremia lilikuwa lenyewe ni kitendo cha ibada. Yeremia alihubiri kwamba Mungu alikuwa amekataa ibada ya Israeli kwa sababu ya maisha yao ya dhambi. Hii ilikuwa ibada. Ilitambua usafi wa Mungu mtakatifu; ilitambua thamani ya Mungu.


[1]"Baadhi ya wasomi wanasema kwamba manabii walikataa mfumo wa Hekalu. Hata hivyo, manabii wengi walihusishwa sana na Hekalu. Isaya alimuona Bwana ndani ya Hekalu. Ezekieli alitabiri Hekalu lililorejeshwa lililojaa utukufu wa Mungu. Hagai alimhimiza Zerubabeli kujenga upya Hekalu. Manabii hawakukataa dhabihu; walikataa matumizi mabaya ya dhabihu.".

Ibada ya Kibiblia Siku hizi

Baadhi ya makanisa hutenganisha ibada na mahubiri. Wanatangaza, “Tutaanza na muda wa ibada.” Baada ya ibada kukamilika, wanahama kwenda kwenye mahubiri. Hii ina hatari mbili.

1. Inamaanisha kwamba ibada inahusishwa na muziki tu. Mtazamo huu wa ibada unalenga tu hisia. Ibada ya kweli lazima iwe zaidi ya muziki na wimbo.

2. Inatenganisha tangazo kutoka kwa ibada. Kila kitu tunachofanya katika huduma ya kanisa kinapaswa kuwa ibada. Muziki, sala, maandiko, mahubiri, na hata sadaka ni sehemu ya ibada.

Kujipima

Jiulize, "Je, mahubiri yangu ni kitendo cha ibada? Ninapohubiri, je, ninaongea kama mjumbe wa Mungu anayemheshimu Mungu?"

Hatari za Ibada: Kutokuwa na Kiasi katika Ibada

(1) Hatari ya ibada ya kimazoea

Tunaposahau kwamba ibada ya kibiblia inahitaji utii, tunaweza kuanza kumchukulia Mungu kama rafiki wa kawaida ambaye hapewi heshima. Ibada ya kimazoea huhamasisha mtazamo huu. Hatupaswi kamwe kusahau kwamba Mungu ni Mungu wa ajabu anayehitaji utii kamili. Yeye ni " Mfalme wa milele, asiyeweza kuona uharibifu, asiyeonekana, Mungu peke yake" (1 Timotheo 1:17). Baadhi ya makanisa yanasahau ukuu wa Mungu; ibada inakuwa kama kunywa kikombe cha kahawa na rafiki wa zamani mnayekutana naye.

(2) Hatari ya ibada inayozingatia desturi

Tunaposahau kwamba ibada ya kibiblia ni ibada kwa Mungu anayetamani kujenga uhusiano nasi, tunaweza kuanza kumchukulia Mungu kama mungu wa mbali. Mtazamo rasmi sana wa ibada unaweza kuhamasisha mtazamo huu. Baadhi ya makanisa hayatoi nafasi kwa mwamini kupata urafiki na Mungu; mkazo wote uko kwenye ukuu na ukubwa wake.

Katika ibada, tunapaswa kupata uzoefu wa mamlaka ya Mungu juu ya uumbaji wake na urafiki wake wa karibu na watoto wake.

Kujipima

Fikiria ibada yako ya hivi karibuni. Jiulize, "Sehemu gani za ibada ziliwahimiza waabudu kumheshimu Mungu kwa ukuu wake? Je, walitoka kwenye ibada wakiwa na hisia za Mungu wetu mkuu?" Kisha jiulize, "Sehemu gani za ibada ziliwahimiza waabudu kupata urafiki wa karibu na Mungu? Je, walitoka kwenye ibada wakijua kwamba Mungu anawapenda sana?"

Hitimisho: Ushuhuda wa Shahidi wa Kuzinduliwa kwa Hekalu

Je, ingekuwaje kama ungekuwa kwenye uzinduzi wa Hekalu? Labda inaweza kuelezwa hivi:

"Nilikuwepo kwenye uzinduzi wa Hekalu. Sitausahau siku hiyo. Tulikuwa tumeisubiri ibada hiyo kwa miaka mingi.

"Miaka? Ndiyo, miaka! Mfalme Daudi alikuwa ametengeneza mipango ya kujenga Hekalu na akampa Solomoni kabla ya kifo chake. Sasa Hekalu lilikuwa limekamilika, na ibada iliyosubiriwa kwa muda mrefu ya uzinduzi ilifanyika.

"Ilikuwa ni mazingira mazuri na ibada yenye msisimko. Fikiria...

  • Dhabihu za maksai 22,000 na kondoo 120,000

  • Kwaya ya mamia ya watu ikiiimba Zaburi za Daudi

  • Bendi ya matoazi, vinubi, zeze, na tarumbeta 120

  • Makuhani na Walawi wamevaa mavazi meupe mazuri

  • Moja ya majengo mazuri zaidi yaliyowahi kujengwa

  • Vyombo vya dhahabu na fedha kwa kila tendo la ibada

"Ilikuwa ni ibada nzuri, lakini uzuri wa mipangilio siyo jambo muhimu zaidi katika kumbukumbu yangu. Ninachokumbuka zaidi ni kwamba wanamuziki walipoanza kupiga na kuimba, 'utukufu wa Bwana ulijaza nyumba ya Mungu.' Uwepo wa Mungu ulijaza Hekalu hadi makuhani hawakuweza kufanya kazi zao. Ibada kwa Mungu ilitawaliwa na Mungu!

"Imepita miaka tangu ile ibada ya kukumbukwa. Sidai kwamba kila ibada niliyohudhuria tangu siku ile imekuwa na ishara zile zile za wazi za uwepo wa Mungu; ile ilikuwa siku maalum. Hata hivyo, katika kila ibada ninayohudhuria, natarajia uwepo wa Mungu.

"Wakati mwingine, uwepo wake ni wa kusisimua; wakati mwingine, ni kimya. Wakati mwingine, uwepo wake unauhisi kwenye uimbaji; wakati mwingine, anazungumza kupitia mahubiri. Wakati mwingine, hisia zangu huguswa; wakati mwingine, ukweli wake unazungumza kwa akili na nia yangu. Wakati mwingine, natoka nikiwa nimehamasishwa; wakati mwingine, natoka nikiwa nimehukumiwa.

"Bila kujali jinsi Mungu anavyochagua kuwepo, nauthamini uwepo wake. Huenda nisije kuona tena tukio la wazi la uwepo wa Mungu kama lile, lakini ninaweza kuingia kwenye uwepo wake kila wakati ninapoabudu."

Majadiliano ya kikundi

► Kwa matumizi ya vitendo vya somo hili, jadili yafuatayo:

Esther ni Mkristo mkweli na anapenda kuhudhuria ibada za kanisani kijijini kwake. Muziki wenye nguvu na ushirika vinatoa mabadiliko mazuri kutoka kwenye matatizo ya maisha ya kila siku. Anapenda hisia na mihemko anayopata anapomwabudu Mungu kwa moyo wake wote. Hata hivyo, Esther anakutana na ugumu wa kuweka bidii sawa kwenye ndoa yake na majukumu ya maisha ya kila siku kama anavyoweka kwenye ibada za Jumapili asubuhi. Ungewezaje kumshauri Esther?

 

Mapitio ya Somo la 3

Mapitio ya Masomo Yote

(1) Mungu anajali jinsi tunavyoabudu kwa sababu:

  • Namna ya ibada yetu inaathiri ufahamu wetu juu ya Mungu.

  • Namna ya ibada yetu inaonesha sababu ya kuabudu kwetu.

(2) Ibada ni uhusiano - kutembea na Mungu.

  • Mungu alitoa njia za ibada kwa Adamu na Eva.

  • Mungu alichukua hatua ya kufanya ibada iwezekane kwa Abrahamu.

  • Neema ya Mungu ilifanya ibada iwezekane kwa Yakobo.

  • Tunapotembea na Mungu, maisha yetu yanabadilika.

(3) Ibada inaanza na utiifu.

  • Ibada ni zaidi ya hisia au mihemko.

  • Ibada ni mwitikio kwa amri za Mungu.

  • Utiifu kwa Mungu unazidisha uhusiano wetu naye.

(4) Ibada inajumuisha desturi (dhabihu za Agano la Kale).

  • Dhabihu zilionesha kujisalimisha kikamilifu kwa Mungu. (Warumi 12:1)

  • Mungu aliheshimu ibada ya kweli kwa uwepo wake. (2 Mambo ya Nyakati 5)

  • Taratibu za ibada za pamoja lazima zitoke kwa moyo mtiifu.

(5) Ibada inajumuisha sifa (Zaburi).

  • Kitabu cha Zaburi kinaonesha kwamba ibada inajumuisha sifa.

  • Kitabu cha Zaburi kinaonesha kwamba ibada inajumuisha maombolezo.

(6) Ibada inajumuisha kutangaza (Manabii).

  • Ibada ni zaidi ya sifa; ni pia kutangaza ukweli. Mahubiri ni ibada.

  • Manabii walifundisha kwamba taratibu za ibada bila ukweli siyo ibada.

  • Manabii walifundisha kuwa ibada ya kweli inapaswa kuwa ya kiwango cha juu kabisa.

  • Manabii walifundisha kwamba ibada ya kweli inajumuisha maisha yote.

Somo la 3 Mazoezi

(1) Orodhesha kanuni tatu kuhusu ibada ambazo umejifunza kutoka kwenye somo hili la ibada za Agano la Kale. Andika ukurasa mmoja ukielezea njia za vitendo za kutumia kila kanuni katika ibada ya kanisa lako.

(2) Mwanzoni mwa somo lijalo, utafanya mtihani kulingana na somo hili. Soma maswali ya mtihani kwa uangalifu katika maandalizi.

Jaribio Somo la 3

Majaribio ya Masomo Yote

(1) Kutoka kwenye somo hili, orodhesha mifano miwili ya kibiblia ya ibada iliyokataliwa na Mungu.

(2) Neno “alitembea pamoja na Mungu” linaonesha kwamba ibada inahusisha __________ na Mungu.

(3) Kutoka kwenye somo hili, taja watu watatu wasiofaa ambao Mungu kwa neema aliwawezesha kumwabudu.

(4) Sadaka ya Ibrahimu ya Isaka inaonyesha kuwa ibada ya kweli inahitaji__________ kamili.

(5) Tofauti ilikuwa nini kati ya ibada ya Abeli na ibada ya Kaini?

(6) Umuhimu wa muabudu kuweka mikono yake juu ya kichwa cha mnyama wa sadaka ulikuwa nini?

(7) Eleza maana ya sifa za kutangaza na sifa za maelezo.

(8) Manabii wanaonesha kwamba__________ la Neno la Mungu ni ibada.

(9) Orodhesha vipengele vitatu vya ujumbe wa manabii kuhusu ibada.

(10) Taja mambo mawili ya hatari ya kutokuwa na uwiano katika ibada.

(11) Andika Mika 6:6-8 kwa kumbukumbu.

Next Lesson