Utangulizi wa ibada ya Kikristo
Utangulizi wa ibada ya Kikristo
Audio Course Purchase

Search Course

Type at least 3 characters to search

Search through all lessons and sections in this course

Searching...

No results found

No matches for ""

Try different keywords or check your spelling

results found

Lesson 1: Kuelezea maana ya Ibada

26 min read

by Randall McElwain


Malengo ya Somo

Mwisho wa somo hili, mwanafunzi anapaswa:

(1) Kuelewa maana ya Ibada katika kibiblia.

(2) Elewa kwamba ibada ya kweli inaathiri maeneo yote ya maisha yetu.

(3) Tambua aina ya ibada inayokubalika na Mungu.

(4) Thamini umuhimu wa ibada katika maisha ya Kikristo.

Matayarisho kwa somo hili

Kariri Yohana 4:23-24.

Utangulizi

Ni asubuhi ya Jumapili nchini Marekani. Wakristo waliopendeza hukusanyika kwa ajili ya ibada katika patakatifu pazuri. Wanaimba nyimbo za ibada wakisindikizwa na muziki pamoja na kwaya, wanaimba tenzi kuu zenye utukufu. Muziki unapigwa wakati sadaka zinakusanywa. Washirika wanaomba kimya kimya huku mchungaji akiwaongoza katika maombi. Wakati wa mahubiri yake, mchungaji ananukuu maneno ya waandishi tofauti kutoka kwenye maktaba yake kubwa. Baada ya mahubiri, kanisa wanashiriki meza ya Bwana kwa kutumia sahani yenye rangi ya fedha, mikate, na vikombe kwa kila mtu binafsi. Hii ni kuabudu.

Ni jumapili asubuhi huko China. Waumini 30 waliovaa mavazi ya kawaida hukusanyika katika chumba cha kupanga. Wanaimba nyimbo za sifa na za kitabuni wakiimba bila ala za muziki. Kiongozi anahubiri ukweli wa neno ambalo amelipata kwa siku za karibuni kwa kupitia usomaji wa Maandiko. Wakati wa kipindi cha maombi ya muda mrefu, washirika wa nyumba hii wanaomba kulingana na mahitaji ya kila mmoja. Baada ya maombi, washirika wa nyumba hii wanakula ushirika mtakatifu huku mkate na divai ikiwa kwenye kikombe cha plastiki. Watu wanapoondoka, wanaweka sadaka zao kimya kimya katika kikapu kilichopo mlangoni. Wenye mahitaji maalumu watapewa sadaka hii. Hii ni kuabudu.

Ni jumapili asubuhi kule Nigeria. Wakristo wanavaa mavazi ya kumeremeta wamekusanyika wakiwa na hamasa ya ibada. Timu ya kuimba na kuabudu ikiwa na magitaa, vinanda, na ngoma inaongoza ibada kwa nyimbo ambazo zinaoneshwa katika kioo kikubwa cha projecta. Kwaya hii inaimba wakati watu wanaenda kutoa sadaka katika sanduku la sadaka mbele ya kanisa. Ujumbe wa mahubiri unaendana na mahitaji yaliyopo ya watu wa Nigeria. Ibada inaisha kwa kubusiana mikono, kukumbatiana, na sherehe za furaha. Hii ni kuabudu.

Kuabudu kuna namna tofauti. Kwa kila nchi na kila utamaduni, kuabudu kuna tofautiana. Kuabudu ni zaidi ya ibada aina fulani. Kusema kweli kuabudu ni zaidi ya ibada yenyewe; kuabudu inahusisha maeneo yote ya maisha ya mkristo. Katika somo hili, tutaangalia maana ya kuabudu kibiblia.

► Soma Yohana 4:1-29. Jadili maana ya kuabudu katika roho na kweli.

Vipengele vya Kuabudu vya Kibiblia

Kuabudu ni kutambua na kuheshimu thamani ya Mungu. Inamaanisha kumpa Mungu heshima anayostahili.

► Hapa chini kuna maana tatu za kuabudu. Kariri maana ambayo ina maana muhimu zaidi kwako.

  • “Ibada ni mwitikio wa kuabudu wa mwanadamu kwa Mungu wa Milele.” - Evelyn Underhill

  • “Ibada ni kuinua moyo wetu kwa mwitikio wa hiari kwa Mungu.” - Franklin Segler

  • “Ibada ni mwitikio wa yote tuliyo kwa yote Mungu alivyo.” - Warren Wiersbe

Ibada ni utiifu wa heshima.

Kwa lugha ya Kiebrania na Kiyunani neno “kuabudu” lililotafsiriwa katika Biblia lina dhana ya kuinama chini mbele ya Mungu.[1] Htii inaonesha kuwa kujisalimisha kwa heshima kunahusishwa katika kuabudu. Tendo la kuinama lina akisi heshima ya moyo. Kuanzia ngalau karne ya pili, Wakristo walipiga magoti wakati wakiomba.

Katika Ufunuo 4:10-11, Mtume Yonana aliona tukio la kuabudu mbinguni:

Ndipo hao wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi, nao humsujudia yeye aliye hai hata milele na milele, nao huzitupa taji zao mbele ya kile kiti cha enzi, wakisema, Umestahili wewe, Bwana wetu na Mungu wetu, kuupokea utukufu na heshima na uweza; kwa kuwa wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumbwa.

Wakati wa Rumi mfalme aliyeshindwa vita akiletwa kwa Kaisari, alitakiwa kutupa taji lake la kifame chini ya miguu ya Kaisari na kuinama kwa kujisalimisha. Yohana anaonesha kuwa Mungu, ambaye ana nguvu na anastahili kuliko Kaisari, anastahili heshima yenye kujisalimisha ya wanaoabudu.

Katika Agano la Kale, Mungu Mungu alikataa sadaka za walioasi. “Watu hawa hunikaribia na kuniheshimu kwa vinywa vyao, bali mioyo yao wamefarakana nami, na kicho chao walicho nacho kwangu ni maagizo ya wanadamu …” (Isaya 29:13). Kwa nje, wnaonekana kana kwamba ni watu wanaoabudu; walisema maneno sahihi na kufuata utaratibu wa ibada. Kwa ndani, mioyo yao ilikuwa mbali na Mungu. Kuabudu yenye kweli ni kujisalimisha kwa heshima kutoka moyoni.

Ukweli ule ule unaonekana katika Agano Jipya. Mwanamke Msamaria anahoji kuhusu mahali pa kuabudia, ni Yerusalem au Mlima wa Gerizim. Yesu akaonesha moyo, kuwa ni mahali pa kiroho pa kuabudia. “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli” (Yohana 4:24). Kuabudu yenye ukweli inahitaji kujisalimisha kwa Mungu.

Kuabudu yenye ukweli inamheshimu yule anayeabudiwa. Katika baadhi ya makanisa, kuabudu kunashindwa kutambua heshima anayomstahili Mungu. Kama tutakavyoona maana nyingine baadaye, kuabudu kunajumuisha kusherehekea, lakini pia kuabudu ni kunamheshimu Mungu. Hii haina maana kuwa mtindo moja wa kuabudu ndio unaofaa. Walakini, maana hii ya kwanza inatukumbusha kwamba pale tunapoamua kuhusu vitendo vya vyetu vya kuabudu, tunapaswa kujiuliza, “Je, mimi ninaonesha heshima kwa Mungu ninayemwabudu?”

Ibada ni huduma

Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana (Warumi 12:1).

Mstari huu unaunganisha kujisalimisha kwetu kwa heshima na maisha ya kila siku. Ni pale tu tunapojisalimisha kama dhabihu iliyohai ndipo huduma zetu, au kuabudu kwetu, kunakubalika na Mungu. Kukutana mara kwa mara kanisani ni muhimu; kanisa la kwanza walithamini kuabudu pamoja.[2] Walakini, kuabudu hakuishii pale mkusanyiko wa kanisa unapomalizika. Kuabudu ya ukweli huendelea katika nyanja zote za maisha.

Ibada ni sifa.

Neno sifa limetumika zaidi ya mara 130 katika kitabu cha Zaburi. Kuna maneno matatu ya kiebrania yanayotafsiriwa “kusifu.” Neno la kwanza, halal, lina maana ya kusherehekea au kujivunia. Neno la pili, yadah, maana yake kusifu, kutoa shukrani, au kukiri. Neno la tatu, zamar, maana yake “kuimba” au “kuimba sifa.”

Maneno haya, hususani halal, linaashiria furaha ya kuabudu. Halal ni neno ambalo Myahudi angelitumia kujivunia mtu fulani. Katika kuabudu, tunajivunia Mungu; katika kuabudu, tunasherehekea wema wake; katika kuabudu, tunafurahia ukuu wa Mungu.

Kuabudu kwa ukweli kunamheshimu Mungu; walakini, kuabudu kwa ukweli vile vile ni kumsherehekea Mungu! Katika kuabudu, tunafurahia wema wa Mungu. Katika somo la 6, tutajifunza kazi ya mziki katika ibada. Muziki ni muhimu kwa sababu unatengeneza njia kwa kusanyiko kuungana katika kusherehekea na kumsifu Mungu.

Ibada ni ushirika.

Kuabudu ni ushirika kati ya Mungu na mwanadamu. Kuabudu pia ni pamoja na ushirika kati ya wanaoabudu. Neno la Kigiriki (koinonia) lenye maana ya ushirika au kushirikiana mara nyingi hutumiwa katika muktadha wa kuabudu. Wakristo walijitolea kwa mafundisho ya mitume na ushirika (koinonia), kwa kuvunja mkate na maombi (Matendo 2:42). Kama waamini, tumekaribishwa katika ushirika (koinonia) wa Mwana wa Mungu, Yesu Kristo Bwana wetu (1 Wakorintho 1:9).

Kielelezo cha kufahamu kuabudu kama ushirika ni Utatu. Kwa njia ile ile ambayo Utatu unavyohusiana kati yao katika ushirika, sisi pia tunahusiana kati yetu na kwa Mungu katika kuabudu. Katika baraka inayohusisha kuabudu ya kidunia na Utatu wa milele, Paulo aliandika, " Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu, na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote” (2 Wakorintho 13:14). Tunapokuwa umoja na Kristo, tunashiriki kwa njia ya Roho katika ushirika wa Mwana na Baba. [3] Katika kuabudu, tunakutana na ushirika tajiri wa Utatu. Kuabudu kwetu duniani kumeigwa kulingana na ushirika kamili wa Utatu.

Kuabudu kwa namna ya Utatu ni uzoefu wa neema, si matendo. Kuabudu inawezekana kupitia kuhani wetu mkuu, Yesu Kristo. Yeye huchukua kuabudu yetu isiyostahili, anaitakasa, na kuileta mbele ya Baba bila doa wala mawaa. Kuabudu kwetu hukubaliwa na Baba kwa ajili ya Yesu, na sisi tunaungana na Yesu katika maisha yake katika Roho.

Tunaabudu si kwa sababu tujipatie kibali cha Mungu, bali kwa neema tumepewa heshima ya kushiriki katika ushirika na Mungu.

Koinonia yetu ambayo sio kamili leo (ushirika na Mungu katika kuabudu na ushirika na waamini wengine) ni kionjo cha kuabudu mbinguni. Kama waabudu, tunatafuta ushirika na waamini wenzetu kwa sababu kuabudu duniani ni mazoezi ya kuabudu milele.

Ibada inajumuisha maisha yote.

Neno lingine linalotumiwa kwa kuabudu katika Agano Jipya mara nyingi hufasiriwa kama "dini":[4]

Mtu akidhani ya kuwa anayo dini, wala hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hali akijidanganya moyo wake, dini yake mtu huyo haifai. Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa (Yakobo 1:26-27).

Neno hili linaonesha kuwa kuabudu ni zaidi ya yanayotokea Jumapili. Kuabudu kwa kibiblia ni pamoja na maisha yote. Ibada ya kuabudu ni kielelezo kilichojikita katika kuabudu, lakini ibada ya kuabudu pekee haitoshi. Lazima kudumisha mtindo wa maisha ya kuabudu. Ibada yetu ya kikundi kila wiki lazima ionekane katika maisha yetu ya kila siku.

Kuabudu halisi huonekana katika kumtii Mungu kila siku. Yakobo anaonesha kwamba ikiwa ninaimba nyimbo za sifa Jumapili, lakini ninashindwa kudhibiti ulimi wangu Jumatatu, ibada yangu haijakamilika. Kuabudu safi na isiyo na taka pamoja na huduma ya vitendo (kutembelea mayatima na wajane) na utii wa kila siku (kujitunza mwenyewe usichafuke na ulimwengu).

Katika Isaya 6, Nabii aliona maono ya Mungu akiwa katika kiti chake cha enzi. Huduma ya Isaya kama Nabii ilibadilishwa kwa kuona hili. Isaya alimsikia Bwana akiuliza “Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu? Ndipo niliposema, Mimi hapa, nitume mimi” (Isaya 6:8). Kuabudu ya kweli hubadilisha maisha yetu na kutufanya kuwa tayari na watumishi wa mungu wenye ufanisi.

► Soma Malaki 1:6-9, 1 Samweli 13:8-14, Walawi 10:1-3, na Matendo 5:1-11. Je, Maandiko haya yanafundisha nini kuhusu kuabudu?


[1]Neno la kiebrania ni shachah, katika Agano la kale limetafsiriwa “kuabudu,” “kuinama chini,” “anguka chini,” au “kuheshimu.” Neno la kiyunani ni proskuneo, katika Agano jipya limetafsiriwa “kuabudu” au “inama chini.”
[2]Kuabudu pamoja imeamriwa katika Maandiko kama Waebrania 10:25. Inasadikika kuna kuabudu kwa pamoja katika Matendo 2:46-47.
[3]James B. Torrance, Worship, Community, and the Triune God of Grace (Downers Grove: InterVarsity Press, 1996), 20-21
[4]Neno la Kiyunani kwa kawaida linarejelea kipengele cha nje cha kuabudu. Matendo ya Mitume 26:5, Wakolosai 2:18, and Yakobo 1:26-27.

Je, Kwa nini Ibada ni Muhimu?

A.W. Tozer aliita Ibada "lulu iliyopotea" ya kanisa la kisasa. Alisema kwamba tunajua jinsi ya kuhubiri, jinsi ya kushuhudia, na jinsi ya kuwa na ushirika. Hata hivyo, licha ya nguvu zetu zote, mara nyingi tunashindwa katika kuabudu. Tunamtazama mhubiri akihubiri; tunasikiliza kwaya, kikundi cha sifa, au msanii akisoma; tunatoa sadaka. Lakini mara nyingi tunashindwa kuabudu kweli; tunaruhusu shughuli kuchukua nafasi ya Ibada ya kweli.

Kuabudu kunapaswa kuwa muhimu kwetu kwa kuwa ni muhimu kwa Mungu.

► Soma Kutoka 20:1-5 ili kuona umuhimu ambao Mungu anauweka katika Ibada.

Amri mbili za kwanza zinahusiana na kuabudu. Amri ya kwanza inatuambia tunamwabudu nani. "Usiwe na miungu mingine ila mimi" (Kutoka 20:3). Amri ya pili inatuambia tunavyoabudu. "Usijifanyie sanamu ya kuchonga..." (Kutoka 20:4). Kisha, katika mstari wa mwisho wa Kutoka 20, Mungu anarudi kwenye somo la kuabudu. Mistari hii inafundisha Israeli jinsi ya kujenga madhabahu yao na jinsi ya kukaribia madhabahu kwa njia ya heshima.

► Soma Kutoka 20:23-26. Kuabudu ni muhimu kwa Mungu!

Kuabudu ni jukumu muhimu katika Maandiko. Kitabu cha Kutoka na Walawi hutoa maelekezo maalum kwa ibada ya Israeli. Zaburi ni kitabu cha nyimbo kwa ajili ya kuabudu. Katika Injili, tunaona watu wakianguka chini kumwaabudu Yesu.

► Soma Mathayo 2:11, Mathayo 8:2, Mathayo 9:18, Mathayo 14:33, Mathayo 15:25, Mathayo 28:17.

Katika kitabu cha Matendo, kanisa linakusanyika kwa ajili ya ibada.[1] Katika barua zake, Paulo anazungumzia mazoea ya ibada katika kanisa (1 Wakorintho 11 na 1 Timotheo 2). Ufunuo unatupa fursa ya kuangalia mbinguni kupata mtazamo wa kuabudu ambao tayari unafanyika kwenye kiti cha enzi cha Mungu. Kuabudu duniani ni mazoezi kwa ajili ya kuabudu mbinguni (Ufunuo 4-5). Kuabudu ni muhimu kwa Mungu.

Ibada ni Muhimu kwa sababu katika Kuabudu tunamwona Mungu

► Soma Isaya 6:1-8. Jadili uzoefu wa Isaya katika hekalu.

Isaya 6 inatoa kielelezo muhimu cha kuabudu. Inaonesha kuwa katika ibada tunamuona Mungu. Katika Hekalu, Isaya alimwona Bwana ameinuliwa.

Ukweli huu unarudiwa mara kwa mara katika Maandiko. Alipokuwa akiabudu siku ya Bwana, Yohana aliona maono yake ya mbinguni (Ufunuo 1:10). Paulo na Sila walipokuwa wakiabudu kwa maombi na wimbo, Mungu alifunua nguvu zake (Matendo 16:25-26). Daudi alivumilia mateso yaliyomsababisha kulia, "Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?" (Zaburi 22:1) Katikati ya mateso yake, Daudi alimwona Mungu kupitia kuabudu na sifa; " “Na Wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli” (Zaburi 22:3). Katika kuabudu, tunamuona Mungu.

Ibada ni Muhimu kwa sababu katika Kuabudu Tunajiona na Kubadilishwa

Katika hekalu, Isaya aliona si tu Bwana aliyeinuliwa, alijiona mwenyewe pia. Alipomwona Mungu kwenye kiti chake cha enzi, Isaya alipiga kelele, "Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu..." (Isaya 6:5). Kuabudu ya kweli huturuhusu kujiona sisi wenyewe kama Mungu anavyotuona.

Ndiyo maana jadi za liturujia zimekuwa zikijumuisha maombi ya kutubu. Maombi ya kutubu hayasemi, "tumeasi sheria ya Mungu na kutenda dhambi kwa makusudi." Maombi ya kutubu yanatambua kuwa, "Hata moyo wa mwanadamu uliye safi kabisa ni mchafu ukilinganishwa na utakatifu kamili wa Mungu mtakatifu. Tuna uhitaji wa daima wa neema ya Mungu."

Katika kuabudu, tunajiona kwa macho ya Mungu mtakatifu. Kusingekuwa kuabudu, mtazamo huu ungekuwa ni wa kutisha. Hata hivyo, kwa sababu tayari tumemwona Mungu, tunasafishwa, si kuhukumiwa. Kwa sababu tumemwona Mungu na neema yake, tunajiona kwa uaminifu, kukiri hitaji letu kwake, na kupokea neema yake katika maisha yetu.

Kuabudu huonesha sisi ni nani, lakini haituachi kama tulivyo. Katika mwanga wa utakatifu wa Mungu, Isaya alijiona kama mchafu. Hata hivyo, badala ya kusababisha kukata tamaa, kuabudu kulileta mabadiliko.

Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu; akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa (Isaya 6:6-7).

Isaya alibadilishwa kupitia kukutana kwake na Mungu mtakatifu.

Kuabudu ya kweli hubadilisha mwabudu—Isaya Hekaluni, mwanamke Msamaria kando ya kisima, na wanafunzi juu ya Mlima wa Yesu kubadilika sura. Kukutana na Mungu hubadilisha mwabudu.

Ibada ni Muhimu kwa Sababu katika Kuabudu Tunauona Ulimwengu Wetu

Katika kuabudu, Isaya alimwona Mungu; alijiona mwenyewe; aliona mahitaji ya ulimwengu wake. "Nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu" (Isaya 6:5). Kwa kuitikia, alisema, "Mimi hapa, nitume" (Isaya 6:8). Ni katika kuabudu ambapo tunajiandaa kwa huduma yenye ufanisi kwa ulimwengu wenye uhitaji.[2]

Mapema, tuliona kwamba kuabudu halisi huathiri maisha yote. Baadhi ya makanisa yamegawa kuabudu na kuhubiri Injili. Wanasema, "Fikira kuu ya kanisa letu ni kuhubiri Injili. Makanisa mengine yanaweza kujikita katika kuabudu." Au wanaweza kusema, "Lengo letu ni kuabudu. Tutawaachia kuhubiri Injili na misheni wengine." Hii inaonesha kutokuelewa kuabudu. Katika kuabudu, tunamruhusu Mungu atuoneshe mahitaji ya ulimwengu wetu. Katika kuabudu halisi kutatokea kuhubiri Injili.

Kuabudu halisi ilifunua hitaji la Isaya—na alibadilishwa na kuabudu. Kuabudu halisi ilifunua hitaji la ulimwengu wa Isaya—na yeye alijitolea kwa kubadilisha ulimwengu huo. Katika kuabudu, tutapata hamu ya kutumikia ulimwengu wetu. Jibu muhimu kwa kuabudu halisi ni, "Hapa nipo! Unitume mimi."

Oswald Chambers aliwaonya wamisionari watarajiwa, "kama umekuwa huabudu katika matukio ya kila siku, unapojihusisha na kazi ya Mungu, sio tu hautakuwa wa maana wewe mwenyewe bali pia utakuwa kizuizi kwa wale walio karibu nawe."[3]

Chambers alitambua umuhimu wa kuabudu kama maandalizi ya huduma yenye ufanisi. Katika kuabudu, Mungu huonesha mahitaji ya ulimwengu unaotuzunguka na kutuandaa kukutana na mahitaji hayo.

Ibada Ni Muhimu Kwa sababu Kukosa kuabudu kunatutenganisha na Mungu

► Soma Warumi 1:18-25. Je, kuna uhusiano gani kati ya kuabudu kwa udanganyifu na dhambi?

Mwanzoni mwa Warumi, Paulo anaonyesha sababu kwa nini mwanadamu amehukumiwa mbele za Mungu. Anaonesha kwamba hali ya kupotoka mwanadamu ni matokeo ya kukataa kuabudu Mungu wa kweli. Tazama mchakato ambao Paulo anaelezea katika Warumi 1:21-25.

1. Hawakumwabudu Mungu. “Kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru” (Warumi 1:21). “Waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa” (Warumi 1:25).

2. Matokeo yake “…bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza. Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika; wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo” (Warumi 1:21-23).

3. Katika hukumu “Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu…” (Warumi 1:24).

Paulo anaonesha kwamba kuanguka kwa binadamu katika upumbavu, uharibifu, na tamaa ilikuwa ni matokeo ya watu kukataa kuabudu Mungu. Hawakuabudu Mungu; walikuwa wakiabudu na kutumikia kiumbe badala ya Muumba.

Kila mtu anaabudu. Wakristo wanamwabudu Mungu. Muislamu anamwabudu Allah. Mtu asiyeamini anaabudu hekima yake mwenyewe. Kila mtu anaabudu. Ikiwa tunakataa kuabudu Muumba, tutamwabudu kiumbe. Kuabudu ni muhimu. Kuabudu kweli ya Mungu wa kweli hutubadilisha kulingana na mfano wake. Kuabudu kwa mungu wa uongo hutubadilisha kulingana na mfano wa mungu huyo. Tunakuwa kama kile tunachokiabudu.


[1]Waumini wa kwanza walizidi kushiriki ibada katika Hekalu na sinagogi (Matendo 2:46-47, Matendo 3:1-11, Matendo 5:12, 21, 42). Aidha, walikusanyika nyumbani kwa sala, mafundisho, na ushirika, kama ilivyoonekana katika (Matendo 2:46-47, Matendo 4:31, Matendo 5:42).
[2]

“Ingia Uabudu -
Ondoka Utumike”

- Alama juu ya mlango wa kanisa

[3]Oswald Chambers, My Utmost for His Highest, (September 10 entry). Imepatikana kutoka tovuti ya https://utmost.org/missionary-weapons-1/ on July 21, 2020.

Malengo Matatu ya Kuabudu

Marva Dawn anataja malengo halisi matatu ya kuabudu.[1] Katika ibada, tuna:

(1) Katika Ibada, tunakutana na Mungu

Ibada yoyote ambayo haituleti kwa Mungu inaupungufu wa kuwa ibada ya kweli. Hii haimaanishi kuwa kila ibada itakuwa ya kihisia au ya kusisimua. Hata haijalishi kuwa kila ibada itakuwa sawa na mada yake iliyotangazwa. Lakini katika kila ibada, tunapaswa kujikuta tukiwa mbele ya Mungu. Hii inaweza kuwa kupitia ukweli uliopatikana kutoka kwenye mahubiri; inaweza kuwa kupitia kusoma Neno la Mungu; inaweza kuwa kupitia wimbo unaomsifu Mungu; inaweza kuwa wakati wa sala ambapo tunapata nguvu mpya kwa safari yetu na Mungu. Kwa njia fulani, kila ibada inapaswa kutuleta katika kukutana na Mungu.

(2) Katika Ibada, tunachonga tabia ya kikristo

Katika ibada tunajiona wenyewe na tunabadilishwa. Katika ibada, tunajifunza ukweli ambao unachonga tabia yetu ya Kikristo. Tunapomwabudu Mungu, tabia yetu inarekebishwa zaidi na zaidi kufanana na sura yake. Tunakuwa kama kitu chochote tunachokiabudu.

(3) Katika Ibada, tunajenga jumuiya ya kikristo

Katika ibada, tunatazama ulimwengu unaotuzunguka na kujitolea kutumikia mahitaji ya ulimwengu huo. Tunapofanya hivi, kanisa linajengwa, na waamini wanakua katika kila njia kuwa kama yeye aliye kichwa, yaani, Kristo (Waefeso 4:15). Ibada ya kweli ni chombo cha kujenga jumuiya ya kweli ya Kikristo.


[1]Marva Dawn, Reaching Out Without Dumbing Down (Grand Rapids: Eerdmans, 1995)

Je, ni aina gani ya Ibada inakubalika kwa Mungu?

► Je, ni aina gani ya kuabudu unafikiri Mungu anaikubali?

Yesu alimwambia mwanamke Msamaria kwamba waabudu wa kweli wanamwabudu kwa roho na kweli (Yohana 4:23-24). Kuna ibada ya kweli ambayo ni ya kukubalika kwa Mungu; hii inamaanisha kwamba kuna ibada ya uongo ambayo si ya kukubalika.[1]

Viongozi wa kuabudisha mara nyingi hujitambulisha kwa kuuliza, "Je, kuabudu kwetu ilihamisha kanisa? Je, tulifanya kwa mtindo ambao watu wanafurahia?" Maandiko yanatuonesha kuwa maswali muhimu zaidi ni, "Je, ibada yetu ilimheshimu Mungu? Je, tulimwabudu Mungu kama anavyohitaji? Je, ibada yetu ni ya kukubalika kwake?"

Ibada Ambayo Mungu Huikataa

Mungu hakubali Ibada isiyo na uelewa

Mwanamke Msamaria hakujua alichokuwa anakiabudu (Yohana 4:22). Kule Athene, Paulo aliona watu ambao waliabudu Mungu asiyejulikana (Matendo 17:23).

Katika somo la pili, tutajifunza asili ya Mungu ambaye tunamwabudu. Tunapokuwa hatumjui Mungu wa kweli, ibada yetu inakuwa haina uelewa; ni ibada ya Mungu asiyejulikana. Tunafuata desturi za liturujia,[2] lakini ibada yetu ni ya Mungu asiyejulikana. Ibada lazima ifunue asili ya Mungu kwa anayemwabudu. Lazima tuimbe nyimbo zinazotoa sifa za Mungu; lazima tusome maandiko yanayosema ukweli kuhusu Mungu; lazima tufundishe mahubiri yanayofunua asili ya Mungu. Hatupaswi kukubali ibada ya Mungu asiyejulikana.

Mungu hakubali ibada ya sanam

Sanamu ni kitu chochote kinachochukua nafasi ya Mungu na kuwa mamlaka ya juu katika eneo lolote la maisha. Katika baadhi ya maeneo ya ulimwengu, masanamu ni sanamu za miungu ya kipagani. Katika maeneo mengine ya dunia, masanamu ni kazi, akaunti za benki, nyumba, na burudani. Kitu chochote kinachochukua nafasi ya Mungu katika maisha yetu ni sanamu. Ikiwa tunakwenda kanisani jumapili lakini tunaruhusu vitu vingine viwe na mamlaka ya mwisho katika maisha yetu ya kila siku, tunatumikia sanamu.

Mungu hakubali ibada isiyokuwa ya kiwango cha juu.

► Toa mfano wa ibada ya kiwango cha chini.

Nabii Malaki alionya kwamba ibada ya Israeli ilikuwa inamkera Mungu. Walipinga, "Tumemkosea vipi Mungu?" Malaki akajibu,

“Tena mtoapo sadaka aliye kipofu, si vibaya? Na mtoapo sadaka walio vilema na wagonjwa, si vibaya? Haya! Mtolee liwali wako; je! Atakuwa radhi nawe? Au atakukubali nafsi yako? Asema Bwana wa majeshi” (Malaki 1:8).

Hawangeweza kupeleka zawadi ya mnyama mlemavu kwa gavana wa jimbo lao, lakini walileta wanyama walemavu kama dhabihu kwa Mungu Mwenyezi wa dunia yote.

Baadhi ya watu wanaamini kwamba vipengele vya nje vya ibada si muhimu kwa sababu Mungu huangalia moyo. Ni kweli kwamba Mungu huangalia moyo. Hata hivyo, ni dhahiri katika Maandiko kwamba vipengele vya nje vya ibada ni muhimu kwa Mungu. Kitabu cha Kutoka na Mambo ya Walawi hutoa maelekezo ya kina kuhusu mahitaji ya Mungu kwa ibada. Maelekezo kuhusu Hema yalikuwa ya uhakika. Mungu alitoa maelekezo ya kina kuhusu mavazi yaliyovaliwa na makuhani. Katika Kutoka 39-40, neno "kama Bwana alivyomwagiza Musa" linarudiwa mara 13 kuonyesha utii wa Israeli. Maelezo ya ibada yalikuwa na umuhimu kwa Mungu. Alikuwa anahitaji kitu bora kutoka kwa Israeli.

Tunaabudu kwa uduni tunapompa Mungu kitu kilicho chini ya ubora wetu. Kanuni hizi bado ni muhimu, ingawa hatuleti tena dhabihu za wanyama kwa Mungu. Maswali yaliyoulizwa katika kitabu cha Malaki ni kielelezo cha maswali ambayo tunapaswa kujiuliza kuhusu ibada yetu leo.

  • Wachungaji: "Je, ningetayarisha mahubiri yangu kwa uangalifu zaidi ikiwa gavana angekuwepo kwenye ibada? Je, ninamletea Mungu dhabihu iliyo lemavu?"

  • Wanamuziki: "Je, ningejifunza kwa uangalifu zaidi ikiwa mwanamuziki maarufu angekuwepo kwenye kanisani? Je, ninamletea Mungu dhabihu iliyo lemavu?"

  • Waumini: "Je, ningesikiliza kwa uangalifu zaidi mahubiri haya ikiwa rais angekuwa anayatoa? Je, ninamletea Mungu dhabihu iliyo lemavu?"

Mungu hakubali kuabudu kwa kiburi

Mungu haikubali dhabihu ambayo haina ubora. Hata hivyo, kuna hatari ambayo tunapaswa kuepuka. Mungu haikubali dhabihu ya moyo wenye kiburi na majivuno. Ingawa tunamletea Mungu kilichobora, tunapaswa kutambua kwamba hakuna chochote tunachomletea ambacho kweli kinamstahili Mungu. Dhabihu yetu bora ni ishara ndogo tu ya kile ambacho Mungu anastahili. Tunakaribia mbele za Mungu kwa unyenyekevu, kamwe si kwa mtazamo wa kiburi na thamani yetu wenyewe.

Ibada ambayo Mungu anaikubali

Ikiwa hizi ni sifa za kuabudu ambayo Mungu hakubali, ni aina gani ya kuabudu ambayo Mungu anakubali?

Ibada inayokubalika inajikita katika Mungu.

Kama ilivyo katika Isaya 6, Ufunuo 4 inafungua dirisha kuelekea mbinguni. Katika Ufunuo 4, tahadhari ya wanaomwabudu inaelekezwa kwa yule aliyeketi juu ya kiti cha enzi. Ibada ya kweli inazingatia Mungu. Ibada ya kweli inamweka Mungu kuwa yule anayestahili kuabudiwa.

Ibada inayokubalika inampa Mungu utukufu anaostahili.

Zaburi 96:7-8 inaonesha kusudi la kuabudu:

Mpeni Bwana, enyi jamaa za watu, Mpeni Bwana utukufu na nguvu.
Mpeni Bwana utukufu wa jina lake, Leteni sadaka mkaziingie nyua zake.

Kuabudu humpa Mungu utukufu anaostahili. Bila kujali nyimbo tunazotunga, hisia tunazozua, au majibu tunayopokea kutoka kwa watazamaji, kuabudu ambako hakupeleki utukufu kwa Mungu imeshindwa kutimiza lengo lake.

Lengo la kuabudu siyo kupata baraka kwa ajili yangu mwenyewe; lengo la kuabudu ni kumheshimu na kumpa utukufu Mungu. Tunapomwabudu, mara nyingi tutabarikiwa - lakini baraka yetu siyo msukumo wa ibada. Msukumo wa ibada ni kumheshimu Mungu.

Kutambua lengo la ibada kunabadilisha swali tunalouliza mara nyingi kuhusu ibada. Badala ya kuuliza, "Je, nilifurahia ibada ya leo?" tutauliza, "Je, ibada ya leo ilimheshimu Mungu?" Tunapoelewa vizuri lengo la ibada, tutabadilisha mwelekeo wetu kutoka nafsi yetu kwenda kwa Mungu.

Ibada inayokubalika ni ibada katika roho na kweli.

Katika mazungumzo ya Yesu na mwanamke Msamaria katika Yohana 4, alimwambia kwamba wale wanaomwabudu Mungu lazima wamuabudu kwa roho na kweli (Yohana 4:24). Hii ndiyo namna sahihi ya kuabudu.

Kawaida tunapojadili mifumo ya ibada, tunazungumzia mitindo ya muziki, utaratibu wa liturujia, na masuala mengine ya muundo. Wengi wamekasirika kwa kutokuwepo taarifa za kina kuhusu walivyofanya ibada katika kanisa la Agano Jipya. Fikiria kuhusu mambo yote ambayo hatujui kuhusu ibada ya Agano Jipya:

  • Tunajua walikuwa wanaimba zaburi. Hatujui tuni gani walizotumia; hatujui vyombo gani walivyotumia; hatujui nyimbo mpya walizoimba.

  • Tunajua walikuwa wakiomba. Hatujui ikiwa wote walikuwa wakiomba kwa sauti, ikiwa walikuwa wanaomba kwa vikundi vidogo, au kama mtu binafsi aliongoza maombi. Hatujui ikiwa walitumia maombi yaliyoandikwa tu (zaburi) au maombi ya papo kwa papo.

  • Tunajua walikuwa wanahubiri. Hatujui walihubiri kwa muda gani, ni mtindo gani wa kuhubiri walitumia, au ikiwa kila ibada ilikuwa na mahubiri.

Mbali na Agano Jipya na andiko moja lililoandikwa miongo kadhaa baadaye, tunazo taarifa chache kuhusu mfumo wa ibada ya kanisa la kwanza.[3]

Kwa wasomi, ukosefu huu wa taarifa ni kero. Hata hivyo, labda hii inaonesha kwamba masuala tunayoyaona kuwa muhimu zaidi siyo muhimu kwa Mungu! Yesu alipozungumza kuhusu mfumo wa ibada, Alielekeza katika masuala mawili: roho na kweli. Masuala haya ni muhimu zaidi katika ibada ya kweli.

Ibada katika roho labda inahusiana na roho ya binadamu. Ibada haipaswi kuwa desturi isiyo na maana; inahusisha roho. Hii ni ibada halisi; inatoka moyoni.

Kuabudu katika roho?
Mwaka wa 1994, Kanisa la Vineyard huko Toronto liliripoti kuhusu uamsho ambapo watu walicheka, wakalia kama simba, na "kukandamiza" (kutapika kama mchakato wa kuondoa hisia). Wakati wa "kucheka takatifu," mara kwa mara watu walipoteza udhibiti wa hisia zao. Badala ya kuweka msisitizo kwenye kuruhusu Neno la Mungu kutenda kazi kwa kina mioyoni mwa watafutaji, "Baraka ya Toronto" ililenga tu jibu la kihisia. Je, hii ni ibada katika roho? Je, ni ibada halisi?

Ibada katika kweli inalingana na mafundisho ya Biblia. Ni zaidi ya hisia nzuri au jibu la kihisia. Kama wachungaji na viongozi wa ibada, tunachunguza kila sehemu ya ibada yetu, tukijiuliza "Je, hii ni kweli?" Maneno tunayohubiri, nyimbo tunazotunga, na maombi tunayotoa lazima yawe ya uaminifu kwa Maandiko. Mungu haguswi na maneno matupu; anatafuta ibada katika roho na kweli (Yohana 4:24).

Kuabudu katika kweli?
Mchungaji Bill anaelewa umuhimu wa muziki katika ibada. Anathamini nyimbo za kitabuni, lakini pia anakaribisha nyimbo mpya. Wimbo ambao umekuwa maarufu katika makanisa mengi unafundisha kwamba waamini huendelea daima kuanguka katika dhambi za kukusudia na kisha hutafuta marejesho. Wimbo huo hautoi ahadi ya maisha ya Kikristo ya kushinda. Kusikiliza wimbo huo, Bill alisema, "Wimbo huu si wa kweli kulingana na Maandiko, lakini ni wimbo tu. Watu wanapenda muziki; maneno si muhimu." Je, hii ni ibada katika kweli?

[1]Baadhi ya sehemu hizi zimechukuliwa kutoka kwa David Jeremiah. Worship. (CA: Turning Point Outreach, 1995), 20-24.
[2]Liturujia ni mpango unaotumiwa wakati wa ibada ya Pamoja. Liturujia inaweza kuwa imepangiliwa kwa mwongozo ulioandikwa. Unaweza pia usiwe na mwongozo ulioandikwa. Katika kozi hii neno “liturujia” linarejelea mpango wowote katika kuabudu. Baadhi ya watu hulaumu liturujia yote, wakidhani kuwa ibada iliyopangiliwa sio ibada ya kweli. Tutatumia neno “liturujia” katika dhana ya kiujumla. Ibada iliyopangiliwa inaweza kuwa isiwe na kitu, au inaweza kuwa na uwepo wa Mungu.
[3]Maandiko ya Didache (Mafundisho) ni maandiko mafupi ya mwishoni mwa karne ya kwanza au mwanzoni mwa karne ya pili. Didache inajumuisha ya maadili ya kikristo, ibada za kanisa, na uongozi wa kanisa.

Hatari za Ibada: Mbadala wa Ibada ya Kweli

Yesu aliongelea kuhusu ibada ya kweli. Kama kuna ibada ya kweli basi, kutakuwa na ibada ya uongo. Martin Luther mara nyingi alinukuu methali ya Kijerumani, "Popote ambapo Mungu anajenga kanisa, Shetani hujenga kanisa jirani." Shetani anapenda kututia moyo kuweka mawazo ya uongo badala ya ibada ya kweli. Mara nyingi tumekubali ibada ifuate mahitaji ya utamaduni badala ya kufuata mahitaji ya Mungu tunayemwabudu. Je, baadhi ya mbadala wa ibada ya kweli ni nini?

Ibada ya chapuchapu

Hii ni ibada inayojikita katika urahisishaji binafsi, badala ya kumfurahisha Mungu. Mfano Kuna migahawa 35,000 ya McDonald's duniani. Wateja milioni 68 hula katika McDonald kila siku. Hii si kwa sababu McDonald inatoa chakula bora kilichopo. Si kwa sababu wanatoa lishe ambayo ni ya kipekee kwa afya. Ni kwa sababu McDonald inatoa urahisi, wepesi, na mazingira ya kuvutia. Katika ibada za chapuchapu, shughuli kuu ni urahisi, wepesi, na burudani.

McDonald's na ibada chapuchapu hupima mafanikio kwa idadi. McDonald's hujivuna kuwa, "watu zaidi ya bilioni 300 wamehudumiwa." ibada ya chapuchapu hujivuna, "tuliongezeka kwa 17% kuliko mwaka uliopita." Idadi badala ya utakatifu huwa kigezo cha mafanikio.

Kuna mahitaji machache kwa wa ibada za chapuchapu. Ibada hizo zinatoa muziki mzuri, wazungumzaji wenye burudani, na vivutio vizuri - yote kwa gharama ndogo. Chapuchapu huvutia umati, lakini chakula cha kiroho mara nyingi hakina maana na hakisaidii afya ya kiroho. Ni vyema kutafuta kuvutia watu kwa Injili, lakini chapuchapu sio ibada ya kweli.

Ibada ya Makumbusho

Hali katika makumbusho ni kinyume cha McDonalds. Katika makumbusho, kuna mkazo mkubwa katika kuhifadhi utamaduni. Watu huonesha heshima wanapotazama maonesho. Zaidi ya hayo, makumbusho mengi hayasisitizi ushiriki na ahadi ya kibinafsi. Huwa hauombwi kuweka michoro yako kwenye ukuta wa Makumbusho ya Sanaa ya jengo la makumbusho!

Katika Ibada ya Makumbusho, shughuli kuu ni utamaduni na mfumo. Tunaimba nyimbo ambazo kanisa limekuwa likizimba daima. Tunajivunia uaminifu wetu kwa utamaduni. Lakini ni jambo linalowezekana watu kuhudhuria wiki baada ya wiki bila kukabiliana na mahitaji ya Mungu kwa ahadi ya kibinafsi. Ni jambo linalowezekana kuhudhuria kanisa kila Jumapili na kutazama maonyesho (hotuba, nyimbo, maombi) bila kufanyika mabadiliko ya maisha. Ni jambo zuri kuuthamini urithi wetu, lakini Ibada ya Makumbusho sio ibada ya kweli.

Ibada ya Darasani

Katika darasa, mwalimu ndiye anayesimamia. Mwalimu ndiye anayeamua kile ambacho darasa linajifunza. Mwalimu huendesha mihadhara; wanafunzi husikiliza na kuchukua maelezo. Ushiriki unadhibitiwa na mwalimu.

Katika Ibada ya Darasani, mchungaji ndiye mtu muhimu. Mahubiri ni kitovu cha ibada; kila kitu kingine ni kama maandalizi tu. Waumini wako hapo kusikiliza na kuchukua maelezo. Ibada imepunguzwa kuwa shughuli ya kiakili. Ni jambo zuri kutafuta kuwasiliana ukweli katika ibada yetu; tunapaswa kufafanua ukweli kwa waabudu wetu, lakini Ibada ya Darasani sio ibada ya kweli.

Ibada ya Kweli

Ibada ya kweli inazingatia Mungu. Ibada ya kweli inauliza, "Mungu anataka nini?" Ibada ya kweli husaidia kuona mwenyewe kupitia macho ya Mungu - na hilo ni gumu kwa mtu ambaye hataki kubadilishwa na Mungu. Ibada ya kweli ni kumhusu yeye. Ibada ya kweli inahusisha msalaba, sadaka, kujisalimisha. Ibada ya kweli hubadilisha mwabudu.

Hitimisho: Ushuhuda wa Martha

Je, ibada ina umuhimu gani? Sikiliza ushuhuda wa Martha.

"Mimi ni mtu wa vitendo. Mtu lazima apige deki sakafu, apike chakula, na ajali mambo ya nyumbani. Hiyo ni nguvu yangu; nina karama ya huduma.

"Ninakumbuka siku Yesu alipotembelea nyumba yetu ndogo huko Bethania. Nilikuwa na wasiwasi kumkaribisha mwalimu muhimu hivyo katika nyumba yetu. Nilitaka kila kitu kiwe kamilifu. Baadaye Luka aliandika, 'Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi ' (Luka 10:40) Nilikuwa ninajizatiti kufanya kila kitu kiwe kamili.

"Wakati nilikuwa nikijishughulisha nyumbani, Maria alikaa chumba kingine akimsikiliza Yesu. Sikufurahishwa; nilihitaji msaada! Zaidi ya hayo, yeye ni mwanamke; hahitaji kujifunza kutoka kwa Rabbi.

"Nikaingiwa na hasira kiasi kwamba niliingia ndani na kusema, Bwana, hujali kwamba dada yangu ameniacha nisaidie peke yangu? Mwambie basi anisaidie.' (Luka 10:40) Sitakuja nisahau jibu lake. Yesu alinitazama na kutikisa kichwa chake. Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi, lakini kinatakiwa kitu kimoja tu, na Mariamu amelichagua fungu lililo jema ….' (Luka 10:41-42).

"Ulikuwa ujumbe gani Mwalimu alikuwa akinipa? Hakumaanisha kwamba huduma si muhimu. Muda mfupi kabla ya kututembelea, Yesu alitoa mfano wa Msamaria Mwema - simulizi kuhusu huduma (Luka 10:25-37). Yesu hakumaanisha kwamba huduma si muhimu; alikuwa akinifundisha kwamba huduma yangu inapaswa kutiririka kutoka katika abudu yangu. Kitu muhimu ni ibada. Ikiwa ninaabudu, huduma itatiririka yenyewe; sitakuwa 'na wasiwasi na kuhangaika.' (Luka 10:41).

"Siku hiyo, nilijifunza somo katika maisha. Tangu siku hiyo, huduma yangu haijawahi tena kuwa kipaumbele kuliko ibada yangu. Tangu siku hiyo, nilichukua muda kushiriki na Maria miguuni mwa Yesu; nilitumia muda katika kumwabudu."

Kujipima

Jitathmini mwenyewe, "Ninawezaje kuwa mwabudu bora zaidi?" Tafuta maeneo ambapo unaweza kufanya ibada yako ifanane zaidi na maana ya ibada ya Biblia.

Mapitio ya Somo la 1

Mapitio ya Masomo Yote

(1) Je, kuabudu ni nini?

  • Ibada ni kujisalimisha kwa heshima (Ufunuo 4:10-11).

  • Ibada ni huduma (Warumi 12:1).

  • Ibada ni sifa (Zaburi).

  • Ibada ni ushirika (Matendo 2:42).

  • Ibada inajumuisha maisha yote (Yakobo 1:26-27).

(2) Je, kwanini Ibada ni muhimu?

  • Katika Ibada tunamwona Mungu (Isaya 6:1-8).

  • Katika Ibada tunajiona na kubadilika (Isaya 6:1-8).

  • Katika Ibada tunatazama ulimwengu wetu (Isaya 6:1-8).

  • Kushindwa kuabudu kutatutenga na Mungu (Warumi 1:18-25).

(3) Malengo ya Ibada:

  • Katika Ibada, tunakutana na Mungu.

  • Katika Ibada, tunajenga tabia ya Kikristo.

  • Katika Ibada, tunajenga jumuiya ya Kikristo.

(4) Je, ni ibada gani inayokubalika na Mungu?

  • Ibada inayokubalika inajikita katika Mungu (Ufunuo 4).

  • Ibada inayokubalika inampa Mungu utukufu anaoustahili (Zaburi 96:7-8).

  • Ibada inayokubalika ni katika roho na kweli (Yohana 4:23-24).

Somo la 1 Mazoezi

(1) Je, Biblia inaelezeaje kuhusu Ibada? Andika jibu lako katika ukurasa moja ukizingatia mistari ifuatayo:

  • Zaburi 111:1-2

  • Zaburi 147:1

  • Zaburi 150

  • Isaya 6:1-8

  • Ufunuo 4

Kama unajifunza ukiwa katika kikundi, jadiliana jibu lako na wengine katka darasa linalofuata.

(2) Mwanzoni mwa somo linalofuata, utafanya jaribio kufuatia somo hili. Kwa kujitayarisha soma maswali ya jaribio kwa uangalifu.

Mradi wa kozi

Mchakato wa Siku 30 wa Ibada [1]

Utashughulikia mradi huu kipindi chote cha kozi hii. Mwishoni mwa kozi, utaripoti kwamba umekamilisha mradi huu. Hutawasilisha jarida lako kwa kiongozi wa darasa.

Kila siku kwa siku 30, utatumia dakika chache kutafakari moja ya sifa za Mungu. Ni bora kufanya mradi huu asubuhi ili uweze kutafakari kuhusu sifa hiyo mchana mzima. Maana ya kutafakari ni kufikiria kwa kina kuhusu kitu fulani.

Uwe na kitabu cha kumbukumbu utakachokitumia kwa matukio ya kila siku. Anza kila siku kwa maombi ukimwomba Mungu ajifunue kwako. Kisha, fungua kitabu cha Zaburi na anza kusoma. Lengo la mradi huu ni kutafakari, sio kusoma kwa wingi. Unaweza kusoma aya moja au Zaburi nzima.

Unaposoma, tafuta sifa moja ya Mungu au Mungu kufananishwa na mtu au kitu kingine. Sifa ni sehemu ya tabia ya Mungu - huruma yake, utakatifu wake, utunzaji wake. Mifano ya kumfanisha Mungu na kitu kingine ni kama vile –yeye ni mchungaji, mwamba, kimbilio letu au ngao yetu.

Ukipata sifa au mfananisho wa Mungu ambao unakugusa, andika sifa hiyo juu ya ukurasa wa jarida lako. Chini ya yake, andika aya inayohusiana na sifa hiyo.

Fikiria kuhusu sifa hiyo na inamaanisha nini kuhusu Mungu. Baada ya kuomba, andika mawazo yako kuhusu Mungu na sifa hii. Hii si karatasi ya kisomi; ni jarida la kibinafsi la ibada. Kupitia siku nzima, tafakari kuhusu Mungu na tabia yake. Msifu kwa ajili ya yeye ni nani. Unapofanya hivi kwa siku 30, utakuwa na maarifa ya kina zaidi kumhusu Mungu.


[1]Mradi huu umechukuliwa kutoka kwa Louie Giglio, The Air I Breathe: Worship as a Way of Life (Sisters, OR: Multnomah Publishers, 2003).

Jaribio Somo la 1

Majaribio ya Masomo Yote

(1) Ulipewa maana tatu za kuabudu mwanzoni mwa somo hili. Andika maana unayoikumbuka.

(2) Orodhesha vipengele vinne vya ibada ya kibiblia.

(3) Mwanamke Msamaria alipojadili kuhusu mahali pa kimwili pa ibada, Yesu alionyesha mahali pa ________ pa ibada.

(4) Katika Zaburi, neno __________ mara nyingi linatumika kupendekeza furaha ya ibada.

(5) Kulingana na Yakobo, ibada safi na isiyo na doa inajumuisha nini vipengele viwili?

(6) Orodhesha sababu nne kwa nini ibada ni muhimu.

(7) Kulingana na somo hili, ni tabia zipi tatu za kuabudu ambazo ni za kukubalika kwa Mungu?

(8) Andika Yohana 4:23-24 kwa kumbukumbu.

Next Lesson