Utangulizi wa ibada ya Kikristo
Utangulizi wa ibada ya Kikristo
Audio Course Purchase

Search Course

Type at least 3 characters to search

Search through all lessons and sections in this course

Searching...

No results found

No matches for ""

Try different keywords or check your spelling

results found

Lesson 2: Mungu na Muabuduji

19 min read

by Randall McElwain


Malengo ya Somo

Mwisho wa somo hili, mwanafunzi anapaswa:

(1) Kutambua taswira ya kibiblia ya Mungu na jukumu lake katika ibada yetu.

(2) Kuelewa matakwa ya Mungu kwa wanaomwabudu.

(3) Kutafuta kuthibitisha matakwa ya Mungu kwa wanaomwabudu.

(4) Kuthamini neema ya Mungu kwa kuruhusu mwanadamu kuingia katika uwepo wake kwa ajili ya ibada.

Matayarisho kwa somo hili

Kariri Ufunuo 5:9-14.

Utangulizi

Kikundi kidogo kiliketi kuzungumzia somo la Biblia la wiki. Swali la majadiliano lilikuwa, "Mungu yukoje na tunamwabudu vipi?"

Sara alianza kusema kwanza. "Nikifikiria kuhusu Mungu, nafikiria kama ni babu mwenye ndevu ndefu nyeupe. Yeye anatuona kama wajukuu. Inamsikitisha anapotuona tukifanya dhambi, lakini anatupenda na anaelewa kuwa tunajitahidi. Sioni kama Mungu anajali tunavyomwabudu, mradi tuoneshe kwamba tunampenda."

Anna akajibu. "Mimi nafikiria kuhusu Mungu kama ni baba mwenye madai sana. Haji karibu sana na watoto wake, lakini anatazama ili aone ikiwa tunatii. Katika kuabudu, tunahitaji kuonesha kwamba tunanyenyekea na tunatii. Sipendi nyimbo zinazomwambia Mungu kuwa yeye ni rafiki yetu; lazima tukumbuke kwamba yeye ni Bwana wetu wa mbinguni na sisi ni watumishi wake! Naenda kanisani ili kujua Mungu anatarajia nitende nini."

Abigaili hakuridhika na majibu yote ya watu hawa. "Mimi nafikiria kuhusu Mungu kama rafiki. Biblia inasema kwamba Mungu anapenda kutoa zawadi njema kwa watoto wake. Naenda kanisani ili kujua Mungu anataka kunifanyia nini. Ninamwomba na kumwambia ninahitaji nini. Nasikiliza mahubiri na muziki ili kujifunza jinsi Mungu atakavyonibariki maishani mwangu. Mungu anataka kutoa zawadi njema; naenda kanisani kupokea hizo zawadi."

Kila mmoja wa hawa wanamke kati yao ana dhana tofauti kuhusu Mungu. Kwa sababu hiyo, kila mmoja ana matarajio tofauti kuhusu kuabudu.

Sara anamtarajia Mungu babu mwenye huruma ambaye hajali sana kuhusu vipengele vya kuabudu kwetu. Kwake yeye ibada bora, ni ile ambayo kila mtu atamwabudu kwa namna ambayo inamfanya ajisikie anafarijika zaidi. Sara atashangaa kama ibada itafanyikia Hemani. Huko angeona kuwa kumbe Mungu anajali kila kipengele cha ibada.

Anna anamwona Mungu kama yuko mbali na mkali. Angekuwa na wasiwasi na uhusiano wa kina unaopatikana katika Zaburi na malalamiko ya kweli ya Ayubu kwa Mungu. Kwake ibada bora itaendeleza umbali kati ya mwabudu na Mungu. Maombi yatakuwa rasmi na yaliyopangiliwa. Muziki utakuwa mzuri, lakini usiogusa hisia. Anna hangependa ushirika wa karibu uliopatikana katika makanisa ya nyumbani katika karne ya kwanza.

Katika mawazo ya Abigaili, Mungu ni mtumishi ambaye yupo kwa ajili ya kutoa mahitaji ya binadamu. Anapoondoka katika ibada, swali lake ni, "Nilipata nini katika ibada?" Muziki lazima uwe na uguse hisia zake binafsi. Maombi lazima yaelekee mahitaji yake binafsi. Mahubiri lazima yawe na uhalisia wa vitendo na lazima yaseme mahitaji yake halisi. Abigail angeweza kuudhika na ibada ya Hekaluni. Ibada ya Hekalu ilikuwa inahusu kuleta dhabihu kwa Mungu, sio kuhusu Mungu kuleta zawadi kwa mwanadamu.

Kila mmoja wa wanawake hawa anatafuta ibada inayohusisha dhana yake kuhusu Mungu. Uelewa wetu kuhusu Mungu una athari kubwa kwa ibada yetu.

► Jadili dhana yako kuhusu Mungu. Jinsi gani dhana yako kuhusu Mungu inaathiri ibada yako? Katika somo hili tutaangalia maswali mawili.

(1) Je, tunamwabudu nani?

Kwa kuwa ibada ni kumpa Mungu heshima anayostahili, kadiri tunavyomjua Mungu, ndivyo tutakavyokuwa tumejitayarisha vizuri kwa ajili ya ibada ya kweli. Sura ya Mungu iliyopotoshwa husababisha ibada iliyopotoshwa.

Picha ya ibada ya sanamu kibiblia inaonesha kanuni hii. Baali alikuwa mungu wa uzazi, mungu wa mazoea yasiyodhibitiwa. Manabii wa Baali walikuwa wakimwabudu vipi? Kwa hisia na desturi zisizodhibitiwa. " Wakapiga kelele, wakajikata-kata kwa visu na vyembe kama ilivyo desturi yao, hata damu ikawachuruzika" (1 Wafalme 18:28).

(2) Je, Mungu anahitaji nini kwa wanaoabudu?

Kwa kuwa Mungu ni mtakatifu, tunawezaje kuingia mbele zake? Mungu anahitaji nini kutoka kwa wale wanaomwabudu?

Miungu wa uongo kama Baal na Moleki hawakuwa watakatifu; waabudu wao hawakuwa na haja ya kuwa watakatifu. Waabudu wa Baal walikuwa kama Baal, hawakuwa watakatifu kimaadili. Tunakuwa kama vile tunavyomwabudu.

Mungu wa kweli ni mtakatifu. Kwa sababu hii, anahitaji watu watakatifu. Waabudu wa Yehova walikuwa kama Yehova; walipaswa kuwa watu watakatifu wanaomwabudu Mungu mtakatifu.

Je, tunamwabudu nani?

[1]Fikiria unavutiwa na machweo mazuri ya jua.[2] Ghafla unaacha kuangalia machweo ili kupiga picha yako: "Mimi Nikiangalia Machweo." Hii inaitwa "selfie," picha yako mwenyewe. Umakini wako umehamia kutoka machweo kuja kwako mwenyewe. Mtu anayechukua selfie anavutiwa zaidi na uwepo wake kuliko na tukio analoliona.

Mungu anastahili ibada yetu bora. Lakini tunapojikita katika ubora wa ibada yetu badala ya katika Mungu tunayemwabudu, tunakuwa tunapiga picha ya kidini ya 'selfie' ("Mimi Nikiabudu Mungu"). Hatupaswi kamwe kuruhusu mahangaiko yetu kuhusu ubora wa ibada yetu ya kuabudu kuchukua nafasi ya umakini wetu kwa Mungu tunayemwabudu!

C.S. Lewis aliandika kuhusu sanamu ya kuwa na uangalifu zaidi kwa ibada ya kuabudu kuliko kwa Mungu. Hivi karibuni, D.A. Carson alionya kwamba tunaweza kushawishiwa "kuabudu ibada badala ya kumuabudu Mungu."[3]

Ibada haiwezi kuwa ibada ya kweli mpaka nimepoteza nafsi yangu katika kumwabudu Mungu. Katika ibada ya kweli, natoa umakini zaidi kwa Mungu kuliko kwa ubora wa jitihada zangu za kuabudu. Ibada ya kweli inajikita kwa Mungu, si katika ubora wa uzoefu wangu wa kuabudu.

Kama tulivyoona katika Somo la 1, amri ya kwanza inatuambia tunamwabudu nani. "Mimi ndimi Bwana, Mungu wako... Usiwe na miungu mingine ila mimi" (Kutoka 20:2-3). Kwa kuwa kuabudu inamaanisha kumpa Mungu heshima anayostahili, kujifunza kuabudu kunapaswa kuanza kwa kujiuliza Mungu ni nani? Kuna nyimbo nne katika kitabu cha Ufunuo hutoa jibu la sehemu kwa swali hili.

Tunamwabudu Muumbaji (Ufunuo 4)

► Soma Ufunuo sura ya 4 kwa sauti. Chukua muda kufikiria mandhari ya kimbingu. Kitabu hiki kinatuambia nini kuhusu Mungu tunayemwabudu?

Na dirisha lake kuelekea mbinguni, Ufunuo 4 hutoa mtazamo wa Muumba tunayemwabudu.

Muumbaji ni mwenye enzi.

Mungu anaketi katika kiti cha enzi juu ya ulimwengu. Neno "kiti cha enzi" hutumiwa mara 14 katika sura hii. Yeye ni Bwana Mungu Mwenyezi; yeye ni mwenye enzi. Ibada lazima iutambue daima uweza wa Mungu. Katika ibada, tunaelezea utii wetu kwa Mungu mwenye enzi. Yeye ni Baba mwenye upendo, lakini yeye ni mwenye enzi.

Muumbaji ni Mtakatifu.

Mungu anaonekana kama Mungu mtakatifu katika maandiko yote.

  • Mungu anawaambia Waisraeli, "Mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu" (Walawi 19:2).

  • Mungu anasifiwa, "Na Wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli" (Zaburi 22:3).

  • Nabii Isaya anaona malaika wakiabudu karibu na kiti cha enzi, "Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu, ni Bwana wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake" (Isaya 6:3).

  • Mtume Yohana anaona mbinguni, ambapo wazee wanapaza sauti, "Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja!" (Ufunuo 4:8).

Tunamuabudu Mungu mtakatifu.

Muumbaji ni wa Milele.

Yeye alikuwako na yupo na atakayekuja (Ufunuo 4:8).

Daudi alielekeza kwa mshangao wa uumbaji kama dirisha la utukufu wa Mungu. "Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, Na anga laitangaza kazi ya mikono yake" (Zaburi 19:1). Sura ya kwanza ya Mwanzo inaanza na Mungu kama Muumbaji; kitabu cha mwisho cha Biblia kinatukumbusha tena kwamba Mungu ni Muumbaji na kwamba atatawala milele juu ya viumbe vyake.

Kusisitiza huku kunadhihirisha umakini sahihi wa kuabudu. Sisi tuliumbwa kumwaabudu Mungu Muumba. Ibada ni sahihi kumhusu yeye, si sisi. Tunapojizamisha katika kumwabudu Muumbaji, mbingu zinaendelea kutangaza utukufu wake.

Tunamwabudu Mkombozi (Ufunuo 5)

► Soma Ufunuo 5 kwa sauti. Je, Ni nini kinachotueleza kuhusu Mungu tunayemwabudu katika mandhari hii yenye utukufu?

Kama Wakristo, hatupaswi kamwe kupoteza hisia za kustaajabu tunapokumbuka kwamba Mfalme wa ulimwengu ametupatia ukombozi wetu. Katika Ufunuo 5, tunatazama jinsi Mwana-Kondoo wa Mungu, Mkombozi wa ulimwengu, anavyoabudiwa. Yesu anaitwa "Mwana-Kondoo" mara 28 katika Kitabu cha Ufunuo. Hii ni mojawapo ya picha kuu katika Ufunuo.

Tunamuabudu Mkombozi kwa sababu ya yeye ni nani.

Yeye ni Simba wa kabila la Yuda. Yeye anatokana na Daudi. Yeye ni Mwana-Kondoo aliyechinjwa. Yeye ni Mwana-Kondoo mwenye pembe saba na macho saba (Ufunuo 5:6), ishara ya ukamilifu. Katika kuabudu, tunamtukuza Yesu kwa sababu ya yeye ni nani. `Ibada ni "karamu ya utukufu wa ukamilifu wa Kristo" (John Piper).

Tunamuabudu Mkombozi kwa sababu ya mahali alipo.

Katika Ufunuo 5:6, Yesu yuko katikati ya ibada ya mbinguni. Yeye yuko kati ya kiti cha enzi na viumbe hai wanne na kati ya wazee. Mwandishi wa Waebrania anatoa ahadi nzuri kwamba mtetezi wetu ameketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mungu (Waebrania 12:2).

Tunamuabudu Mkombozi kwa sababu ya kile alichofanya.

Katika hali ya kuzingatia thamani ya Mungu, baadhi ya walimu wamependekeza kimakosa kwamba tunapaswa kumuabudu Mungu tu kwa ajili ya yeye ni nani, si kwa ajili ya yale anayotufanyia. Yohana Mfunuliwa anaonesha kwamba ibada ya mbinguni inamtukuza Mwana-Kondoo kwa yale aliyoyafanya. " Astahili Mwana-kondoo aliyechinjwa..." (Ufunuo 5:12).

Huu mfano unaonekana katika Zaburi. Zaburi 134 inatuamuru kumbariki Bwana. Haitupi sababu; tunamtukuza kwa sababu yeye ni Mungu. Hii inafuatwa na Zaburi 135-136, ambazo zinamtukuza Mungu kwa sababu ya yale aliyoyafanya katika historia ya Israeli. Tabia ya Mungu, lakini pia matendo yake makuu, yanastahili sifa. Tunapaswa kumsifu Mungu kwa ajili ya yeye ni nani na kwa ajili ya yale aliyoyafanya.

Tunamuabudu Mfalme (Ufunuo 11:15-18)

Ufunuo 11 hutoa mtazamo mwingine wa ibada ya mbinguni. Katika tukio hili, wazee wanamtukuza Mfalme ambaye amechukua kiti chake cha enzi kwa haki. Ingawa falme za dunia zinampinga, mwishowe lazima zitii mamlaka yake. "Ufalme wa dunia umekwisha kuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake, naye atamiliki hata milele na milele" (Ufunuo 11:15).

Katika wimbo huu, Mfalme anatukuzwa kwa hukumu yake ya haki juu ya ulimwengu. Wimbo huu hutukumbusha kwamba Mungu anatawala kwa nguvu kuu. Ingawa mataifa walikuwa na ghadhabu, Mungu aliwahukumu kwa haki.

Ibada ni kuabudu katika ukweli. Ibada ya kweli haipunguzi hukumu za kweli za Mungu. Tena, ibada ya Ufunuo inalingana na ibada ya Zaburi. Zaburi 96 ni wimbo mpya kwa Bwana. Katika wimbo huu, Mungu anatukuzwa miongoni mwa mataifa. Anahofiwa kuliko miungu yote. Anatukuzwa kwa sababu atawahukumu watu kwa haki. Ibada ya kweli inajua kwamba lazima tumwogope Mungu; tunamtukuza kama Mfalme.

Tunamuabudu Bwana Arusi Mshindi (Ufunuo 19:1-9)

Katika darasa la masomo ya uchunguzi wa Biblia, mwalimu aliuliza, "Je, ni wangapi miongoni mwenu wanafurahia Kitabu cha Ufunuo?" Wanafunzi wachache sana waliinua mikono yao. Mwalimu alipouliza, "Kwa nini mnachukia kitabu cha Ufunuo?" mwanafunzi mmoja alijibu, "Unatisha!". Wanafunzi hawa wanapata woga kutokana na Ufunuo kwa sababu wanapuuzilia mbali sehemu bora za kitabu hicho. Wanazingatia hukumu zinazowapata wale wanaopinga Mungu. Hilo bila shaka ni ujumbe muhimu katika Ufunuo. Lakini kwa Wakristo, ujumbe mkuu wa Ufunuo ni ushindi wa mwisho wa Mungu wetu!

Ufunuo 19 unafafanua ujumbe huu. Sura hii inajumuisha maelezo ya ziwa la moto linalowaka kwa kiberiti (Ufunuo 19:20) na ndege wanaokula nyama ya wafalme, nyama ya makapteni, na nyama ya wanaume wenye nguvu... (Ufunuo 19:18). Hii ndiyo hatima ya wale wanaopinga Mfalme. Kwa wale wanaomtukuza Mfalme kwa unyenyekevu wenye heshima, Ufunuo 19 ni wimbo wa furaha. Kahaba mkuu ambaye aliufanya ulimwengu uharibike kwa uasherati wake (Ufunuo 19:2) anaharibiwa. Bwana Arusi mshindi anawashinda adui zake na kumpokea bibi arusi wake mtakatifu kwenye karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo (Ufunuo 19:9).

Kama mwitikio wa ushindi huu mkubwa, Yohana alisikia " sauti ya makutano mengi, na kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi yenye nguvu, ikisema, Haleluya; kwa kuwa Bwana Mungu wetu, Mwenyezi, amemiliki. Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari" (Ufunuo 19:6-7).

Katika ibada, tunamtukuza Bwana Arusi Mshindi. Ibada yetu inatarajia siku za usoni ambazo Yesu anaandaa kwa ajili ya bibi Arusi wake. Moja ya sababu kuu ya umuhimu wa ibada ni kwamba ibada inatupa nguvu ya kuishi maisha ya Kikristo yenye ushindi katika ulimwengu wenye upinzani. Katika ibada, tunakumbuka kwamba " wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo; atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake" (Wafilipi 3:20-21).

Nyimbo hizi nne kutoka kwenye Ufunuo zinatupatia taswira ya Mungu tunayemuabudu. Katika ibada, tunahamisha mawazo yetu wenyewe kutoka kwetu na kuyaelekeza kwa Mungu. Katika ibada, tunapiga magoti mbele ya Muumbaji; katika ibada, tunamtukuza Mkombozi; katika ibada, tunasherehekea Kristo Mfalme; katika ibada, tunatarajia umilele mbele za Bwana Arusi Mshindi.

Huyu ndiye Mungu tunayemuabudu. Hii inasababisha swali, "Nani anaweza kuabudu? Mungu anahitaji nini kutoka kwa wale wanaomwendea mbele ya uso wake?"


[1]

"Mungu, Wewe ni...

Mkuu kuliko wote, mwenye sifa kuu;

mwenye huruma zaidi na mwenye haki zaidi;

aliyefichika zaidi na yupo karibu zaidi;

mzuri zaidi na mwenye nguvu zaidi;

daima akifanya kazi, daima akistarehe;

akikusanya, lakini hana haja ya chochote;

akishikilia na kulinda;

anayeumba na kudumisha;

akutafutaye, ingawa anamiliki vitu vyote."

- Imetokana na Augustine

[2]Sehemu kubwa ya haya yamechukuliwa kutoka kwa Warren Wiersbe, Real Worship, (Grand Rapids: Baker Books, 2000), Sura ya 5.
[3]Imechukuliwa kutoka kwa D.A. Carson, Worship by the Book, (Grand Rapids: Zondervan, 2002), 31.

Je, Mungu anahitaji nini kwa wanaoabudu?

Katika mazungumzo yake na mwanamke Msamaria,[1] Yesu alitoa kauli ya kushangaza. Baada ya kumwambia kwamba waabudu wa kweli watamuabudu Baba kwa roho na kweli, Yesu alisema kwamba Baba anatafuta watu kama hao wamuabudu (Yohana 4:23). Mungu anatafuta aina fulani ya mwabudu, yule anayeabudu kwa roho na kweli. Mungu anatafuta waabudu.

Je, ni tabia gani ambazo Mungu anatafuta kwa wale wanaomwabudu? Mtu yeyote anaweza kuhudhuria ibada; mtu yeyote anaweza kuimba nyimbo za sifa; mtu yeyote anaweza kuomba. Hata hivyo, Mungu ametoa mwongozo maalum kwa tabia za mwabudu wa kweli. Mahali pekee pa kuona hili ni Zaburi 15.

► Soma Zaburi 15. Je, inasemaje kuhusiana na Maisha ya mwabudu?

Zaburi 15 ni zaburi ya utaratibu wa ki-ibada. Inaelezea mazungumzo kati ya kuhani na mwabudu kwenye mlango wa Hekalu. Mwabudu anatafuta lango la kuingia katika Hekalu takatifu la Mungu. Katika kujibu swali la mwabudu " ni nani atakayekaa Katika hema yako?" kuhani anataja mahitaji ya kuingia. Mtindo huu huo hutumiwa katika Zaburi 24:3-6 na Mika 6:6-8. Zaburi 15 inagawanyika katika sehemu tatu:

1. Swali: Nani awezaye kuabudu?

2. Jibu: Maelezo ya mwenye kuabudu

3. Hitimisho: Ahadi kwa mwenye kuabudu

Swali: Nani Anaweza Kuabudu? (Zaburi 15:1).

Mlangoni mwa Hekalu, mwabudu anauliza, ‘Bwana, ni nani atakayekaa Katika hema yako? Ni nani atakayefanya maskani yake Katika kilima chako kitakatifu?’ Maswali haya yanamaanisha sifa tatu za mwabudu.

Mwabudu wa kweli anajua hofu ya Mungu.

Zaburi hii inaonesha kwamba kuingia katika uwepo wa Mungu kamwe si jambo la kawaida. Mwabudu wa kweli anaelewa kwamba Mungu ni mtakatifu na sisi tumetengwa naye.

Katika Maandiko, kuna hisia ya hofu inayohusishwa na uwepo wa Mungu. Katika Mlima Sinai, watu walionywa kuwa mbali na mlima ambapo Mungu aliongea na Musa (Kutoka 19:7-25). Juu ya Mlima ambaye Yesu aligeuka sura, wanafunzi walikuwa na hofu sana (Mathayo 17:6).

Kwa muumini, hofu ya Mungu si hofu inayomfanya mtu kutoroka kutoka kwa uwepo wa Mungu. Badala yake, ni heshima inayomfanya anayeabudu kumkaribia Mungu kwa unyenyekevu. Mwabudu haipaswi kuingia katika uwepo wa Mungu bila maandalizi.

Mwabudu wa kweli anamwabudu kwa unyenyekevu.

Mwabudu aliuliza, "Nani atakayeishi katika hema yako?" Wageni ni wageni wa kudumu katika nchi nyingine. Wao ni wageni, ambao hawana haki ambazo raia wanazo.

Zaburi 15 inahitaji mwabudu kutambua kwamba sisi ni wageni katika uwepo wa Mungu. Kwa sababu Mungu ni mtakatifu na nyumba yake ni takatifu, hatustahili kuwa hapo. Kwa hali yoyote katika maisha, lazima tuingie katika uwepo wa Mungu kwa nia ya unyenyekevu. Sisi ni wageni wake.

Mwabudu wa kweli anasherehekea neema ya Mungu.

Kwa sababu tunatambua utakatifu wa Mungu, tunasherehekea neema ya Mungu anapotukaribisha katika nyumba yake. Mwabudu aliyeuliza, "Nani atakayekaa katika kilima chako kitakatifu?" aliuliza swali hili kwa ujasiri kwamba wangealikwa katika nyumba ya Mungu. Mungu alikuwa ameanzisha uhusiano na Israeli; ibada ya Kiyahudi ilisherehekea uhusiano huu wa neema.

Zaburi 103 ni mwaliko wa kuabudu, "Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana " Zaburi 103 ina kumbukumbu nzuri ya neema inayoturuhusu kuingia katika uwepo wa Mungu.[2]

"Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, Ndivyo BWANA anavyowahurumia wamchao. Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi" (Zaburi 103:13-14). Mungu ambaye alitufanya kutoka mavumbini ametuita kwa neema ya kuabudu! Tunapoingia katika ibada, tunakumbuka neema ya Mungu. Ni neema inayouhusu mavumbi kuingia katika uwepo wa Muumba wa ulimwengu.

Kuabudu kweli kunahusisha hofu ya Mungu, unyenyekevu, na neema. Kila moja ya vipengele hivi vya ibada vilionekana katika ibada ya Hekaluni. Waabudu wa Kiyahudi waliliheshimu Hekalu kwa sababu ilikuwa ni nyumba ya Mungu mtakatifu.[3] Walijiandaa kwa makini kwa ajili ya ibada ili kuonesha unyenyekevu sahihi mbele ya Mungu. Pia walisherehekea katika ibada. Ibada ya Kiyahudi ilijaa kuimba, vyombo vya muziki, harufu nzuri, na hali ya kusherehekea neema ya Mungu kwa watu wake.

Leo, tunapaswa kuingia katika nyumba ya Mungu na hisia ya hofu ya Mungu. Lazima tukubali kutokuwa wa thamani mbele ya Mungu. Lakini ibada yetu pia inapaswa kusherehekea neema ya Mungu inayotukaribisha katika uwepo wake. Liturujia ya zamani ya meza ya Bwana husema, "Hatuji kwa sababu tunastahili, bali kwa sababu tumekaribishwa." Hii ni ibada inayosherehekea neema ya Mungu.

Jibu: Maelezo ya Mwabudu (Zaburi 15:2-5)

Katika kujibu swali, "Nani awezaye kuingia katika nyumba ya Mungu?" kuhani alitoa maelezo kuhusu mwabudu. Mwabudu anatembea bila lawama mbele za Mungu. Yeye ni mwangalifu wa jinsi ya kuwatendea wengine. Anakataa wale wanaomkataa Mungu, lakini anaheshimu wale wanaomcha Mungu. Anajaribu kuiga tabia yake Mungu. Mtu ambaye kweli anamwabudu Mungu atakuwa kama Mungu zaidi na zaidi.

Jibu hili linatukumbusha kwamba ibada inagusa maisha yote. Kuingia katika uwepo wa Mungu kunahitaji utii kamili. Daudi hawezi kukumbuka mtu aliyewahi kusema, "Mimi ni mwana wa Mungu, lakini siishi chini ya sheria ya Mungu." Maandiko hayaruhusu mtu kusema, "Yesu ni mwokozi wangu, lakini yeye si Bwana wa maisha yangu." Kuingia katika uwepo wa Mungu kunahitaji kujitolea kwa mamlaka ya Mungu.

Muabudu wa kweli anaishi maisha ya kimungu

Zaburi 15:2 kwa kweli inatupa kanuni muhimu ya mwabudu. Wale wanaoingia mbele ya uwepo wa Mungu wanapaswa kutembea bila lawama; hii inamaanisha maisha yenye uadilifu katika maeneo yote. Wanapaswa daima kufanya yaliyo sawa. Wanapaswa kusema ukweli kutoka moyoni. Maneno haya yanafafanua maisha endelevu ya mwabudu. Maisha yote yanaguswa na ibada.

Muabudu wa kweli anaishi katika uhusiano sahihi na jamii.

Kama vile Daudi hawezi kumkumbuka mtu aliye wahi kusema, "Mimi ni mtoto wa Mungu, lakini siitii sheria ya Mungu," vivyo hivyo hawezi kumkumbuka mtu anayesema, "Mimi ni mwenye haki mbele za Mungu, lakini siwatendei jirani zangu kwa haki."

Mtu anayeingia mbele za Mungu ni mtu anayeishi katika uhusiano sahihi na jamii. Yeye:

  • Hachongei watu kwa ulimi wake.

  • Hawatendei mabaya jirani zake.

  • Hasemi mabaya dhidi ya rafiki yake; hasambazi uvumi.

  • Anapinga wale wanaomkataa Mungu.

  • Anawaheshimu wale wanaomcha Mungu.

  • Anashikamana na neno lake.

  • Hakandamizi au kuwadhulumu maskini kwa mikopo isiyo ya haki.

  • Hawatendei vibaya wasio na hatia kwa kupokea rushwa.

Mtu anayeishi katika hema la Mungu ni mtu mwenye haki, ndani na nje. Mwabudu wa kweli ni mtu wa uadilifu. Mwabudu wa kweli haruhusu desturi za ibada kuchukua nafasi ya maisha ya kila siku ya utii.

Hitimisho: Ahadi kwa Mwabudu (Zaburi 15:5c)

Zaburi 15 inamalizia kwa ahadi kwa mwabudu; “Mtu atendaye mambo hayo hataondoshwa milele” (Zaburi 15:5). Mtu anayeishi kwa kutii amri za Mungu ameahidiwa ulinzi wa Mungu. Zaburi 15 inafanana na Zaburi 1 kwa maelezo yake ya uchaji Mungu na ahadi yake ya baraka za Mungu kwa mtu mcha Mungu.

Zaburi 15 inaonesha kile ambacho Mungu anahitaji kwa wale wanaomwabudu. Zaburi 15 inapaswa kusomwa kama amri (“Hivi ndivyo Mungu anavyotaka”) na pia kama ahadi (“Hivi ndivyo Mungu atakavyowafanyia wale wanaomuomba”). Kwa kuzingatia Isaya 6, tunaelewa kuwa Mungu ndiye anayempa mwabudu uwezo wa kutii; Mungu ndiye anayetakasa midomo michafu; Mungu ndiye anayefanya mahitaji ya Zaburi 15 yawezekane. Ibada ya kweli inategemea neema ya Mungu. Inapatikana si kwa juhudi zetu dhaifu, bali kwa neema ya Mungu katika maisha ya wale wanaotafuta kumwabudu. Usisahau kamwe neema ya Mungu katika ibada; Baba anatafuta waabudu wa kweli, na Baba ndiye anayefanya ibada iwezekane.

Kujipima

Jiulize, “Je, nina moyo na mikono ya mwabudu wa kweli?” Soma Zaburi 15 kama kipimo. Baada ya kila kifungu, jiulize “Je, hii inanielezea mimi? Je, niko tayari kwa ibada?”

Soma Zaburi 15 tena, kama sala ya kibinafsi. “Bwana, nipe uwezo wa kutembea bila lawama na kutenda yaliyo haki…. Nipe neema ya kuepuka majungu na kashfa…” Maliza kwa kusikia ahadi ya Mungu, “Atendaye mambo hayo hatatikisika kamwe.”


[1]Kiasi kikubwa cha haya kimechukuliwa kutoka“The Worshipper’s Approach to God” by Ronald E. Manahan, kinachopatikana katika Sura ya 2 ya Authentic Worship, kilicho haririwa na Herbert Bateman. (Grand Rapids: Kregel Books, 2002).
[2]Uchunguzi huu unatokana na Richard Averbeck, “Worshipping God in Spirit.”
[3]Kwa wakati wa Yesu, heshima hii ilikuwa imepotea na mlango wa Hekalu ulikuwa umekuwa soko. Yesu aliwafukuza wabadilishaji wa fedha waliokuwa wamelidhalilisha Hekalu, na kulifanya kuwa 'pango la wanyang'anyi'. (Mathayo 21:12-13).

Hatari za Ibada: Unafiki

Yesu alizungumza na watu waliodhani kuwa wao ni wataalamu wa ibada. Waandishi na Mafarisayo walikuwa makini kutii kila undani wa ibada, amri za kibiblia na pia mapokeo ya Kiyahudi. Walikuwa wepesi wa kumlaumu yeyote aliyeshindwa kufuata kila undani wa taratibu zao. Hata hivyo, Yesu aliukosoa ibada yao kwa sababu walikuwa wanafiki.

Mafarisayo walilalamika kwamba wanafunzi wa Yesu hawakufuata taratibu za kiibada za kunawa mikono. Yesu alijibu, “Enyi wanafiki, ni vema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu, akisema, Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu. (Mathayo 15:7-9) Mafarisayo, kama waabudu wa uongo wa wakati wa Isaya, waliitwa wanafiki na Yesu kwa sababu ya makosa mawili:

1. Ibada yao ilikuwa ya nje, si kutoka moyoni (Mathayo 15:8).

2. Ibada yao ilitegemea mapokeo ya kibinadamu, si amri za Mungu (Mathayo 15:9).

Tunapaswa kuwa waangalifu kuepuka hatari ya ibada ya kinafiki. Ibada yetu lazima itoke moyoni, na ibada yetu lazima iongozwe na Mungu, si kwa mapokeo ambayo yameinuliwa kuwa sawa na Neno la Mungu.

Hitimisho: Ushuhuda wa Mwabudu

Tukisoma Zaburi 15 bila kukumbuka nafasi ya neema katika maisha ya Kikristo, tunaweza kupata wazo potofu kwamba lazima tujitahidi kupata haki ya kuabudu. Hata hivyo, Zaburi 15 inaonesha kile ambacho Mungu anatufanyia, si kile tunachofanya, ili kupokea makaribisho katika nyumba yake.

Nani anaalikwa kuabudu? Sikiliza baadhi ya ushuhuda wa waabudu. Wanaonesha kuwa ibada si suala la kuwa unastahili; ibada ni kuhusu kuja kwa unyenyekevu mbele za Mungu na kubadilishwa na neema yake.

Farisayo anasema:

“Nina hakika unaweza kuelewa kwa nini nimekasirishwa na mafundisho ya Yesu. Mimi ni mtu mwema. Sivunji amri. Ninafunga na kutoa zaka. Ikiwa kuna mtu anayestahili kibali cha Mungu, ni mimi! Naenda nyumbani kwa Mungu kuonesha kuwa mimi ni mtu mwema. Inawezekanaje Mungu kukataa ibada yangu?”

Mtoza ushuru anasema:

“Kusema kweli, mimi nimeshangazwa kama Farisayo! Sikujua kama ningekubaliwa kuingia Hekaluni. Nilikaa mbali na watu wema kadiri niwezavyo. Nilitarajia mtu yeyote asinionee. Nilitafuta rehema ya Mungu ingawa sistahili rehema. Kwa mshangao wangu, nilienda nyumbani nikiwa nimetakaswa. Maisha yangu yalibadilishwa katika ibada.”

Tajiri anasema:

“Natoa pesa nyingi kwa Hekalu. Nadhani Yesu anapaswa kuvutiwa na sadaka yangu. Hiyo ndiyo ibada yangu. Ninapoweka sadaka yangu kwenye kisanduku, kila mtu anajua 'Bw. Pesa' yupo. Natumaini Mungu ataona jinsi ninavyotoa nyingi!”

Mjane maskini anasema:

“Nilikua na aibu kuweka sadaka yangu kwenye kisanduku. Nilikuwa na sarafu mbili ndogo tu. Kila mtu alikuwa akitoa michango mikubwa; mimi nilikuwa kama sina chochote. Lakini ibada ni kuhusu kumpa Mungu kilicho bora zaidi. Haikuwa nyingi; lakini nilitoa vyote nilivyokuwa navyo. Nilitumaini hakuna atakayeona sadaka yangu ndogo, lakini mtu aliona. Yesu aliona nilichotoa! Na alisema kuwa nilitoa zaidi ya mtu yeyote. Sijui Yesu alimaanisha nini kwa kauli hiyo, lakini ninafuraha nilitoa bora yangu!”

Majadiliano ya kikundi

► Kwa matumizi ya kivitendo ya somo hili, jadilini yafuatayo:

Yohana amekuwa Mkristo kwa miaka kadhaa. Anajua kuwa kwenda kanisani, kusoma Biblia, na kuomba ni muhimu, lakini ni vigumu kwake kuhisi uwepo wa Mungu katika shughuli hizi. Inaonekana kuwa ni taratibu tu. Unawezaje kumsaidia Yohana kumwona Mungu katika ibada yake?

Mapitio ya Somo la 2

Mapitio ya Masomo Yote

(1) Uelewa wetu wa Mungu ni muhimu kwa ibada kwa sababu taswira potofu ya Mungu itaongoza kwenye ibada potofu.

(2) Ibada lazima ilenge kwa Mungu, si kwa ubora wa uzoefu wetu wa ibada.

(3) Ufunuo unatupa picha ya ibada ya mbinguni:

  • Ibada ya mbinguni ni ibada kwa Muumba ambaye ni mkuu, mtakatifu, na wa milele.

  • Ibada ya mbinguni ni ibada kwa Mkombozi.

  • Ibada ya mbinguni ni ibada kwa Mfalme.

  • Ibada ya mbinguni ni ibada kwa Bwana Harusi Mshindi.

(4) Zaburi 15 ni zaburi ya ibada inayofupisha mahitaji ya Mungu kwa waabudu. Waabudu wa kweli:

  • Wanajua hofu ya Mungu.

  • Wanaabudu kwa unyenyekevu.

  • Wanasherehekea neema ya Mungu.

  • Wanaishi maisha ya ucha Mungu.

  • Wanaishi katika uhusiano sahihi na jamii.

  • Wanapokea ahadi ya Mungu ya ulinzi na baraka.

 

Somo la 2 Mazoezi

(1) Zaburi 120-134 ni mkusanyiko wa nyimbo za wanaohiji wanaosafiri kuelekea Yerusalemu. Zaburi hizi zinafundisha kuhusu ibada katika hali mbalimbali. Soma zaburi hizi wakati unajibu maswali katika jedwali hapa chini.

Zaburi Swali la Kujibu
120 Mesheki na Kedari ziko wapi? Kwa nini ibada Yerusalemu ni muhimu kwa hija anayeishi Mesheki au Kedari?
122 Je, Zaburi hii inatufundisha nini kuhusu mtazamo wa kuabudu?
123 Je, mstari wa pili unafundisha nini kuhusu uhusiano wa mwabudu na Mungu?
124 Unajifunza nini kuhusu sifa katika hali ngumu kutoka kwa zaburi hii?
126 Je, kuabudu kunahusianaje na umisheni miongoni mwa mataifa? Angalia mstari wa pili.
130 Zaburi hii inafundisha nini kuhusu jukumu la maungamo katika ibada?
131 Je, mwandishi wa zaburi anajiandaa vipi kwa ibada? Ni hatua zipi za kivitendo unazoweza kuchukua kufuata mfano huu?
133 Zaburi 133, Yohana 17:20-23, na Waefeso 4:1-16 zote zinazungumzia umoja na zote zinahusiana na maisha ya kanisa kwa namna fulani. Je, umoja unahusianaje na ibada na maisha ya kanisa?
134 Je, Zaburi 134 inafaa vipi kama mwisho wa mfululizo huu wa zaburi za ibada?

(2) Mwanzoni mwa somo linalofuata, utafanya mtihani unaotokana na somo hili. Soma maswali ya mtihani kwa makini ili kujiandaa.

Jaribio Somo la 2

Majaribio ya Masomo Yote

(1) Orodhesha mambo matatu tunayojifunza kuhusu Mungu Muumba katika wimbo wa Ufunuo 4.

(2) Orodhesha sababu tatu za kumwabudu Mkombozi katika Ufunuo 5.

(3 Ujumbe mkuu wa Ufunuo kwa Wakristo ni nini?

(4) Zaburi 15 ni zaburi ya liturujia iliyogawanywa katika sehemu tatu. Orodhesha sehemu hizo tatu.

(5) Mtazamo wa muabudu anayeelewa kuwa yeye ni mgeni katika uwepo wa Mungu ni nini?

(6) Tabia mbili muhimu za mwabudu wa kweli kutoka Zaburi 15:2-5 ni zipi?

(7) Kwa nini Yesu aliwaita Mafarisayo wanafiki?

(8) Andika Ufunuo 5:9-14 kwa kumbukumbu.

Next Lesson