Utangulizi wa ibada ya Kikristo
Utangulizi wa ibada ya Kikristo
Audio Course Purchase

Search Course

Type at least 3 characters to search

Search through all lessons and sections in this course

Searching...

No results found

No matches for ""

Try different keywords or check your spelling

results found

Lesson 10: Mtindo wa Maisha wa Kuabudu

16 min read

by Randall McElwain


Malengo Ya Somo

Mwisho wa somo hili, mwanafunzi anapaswa:

(1) Kutambua uhusiano kati ya ibada ya ushirika na mtindo wa maisha wa kuabudu.

(2) Kuelewa kwamba mtindo wa maisha wa kuabudu hubadilisha maadili ya mtu.

(3) Kutafuta kuishi kwa utukufu wa Mungu.

(4) Kujitolea kwa mtindo wa maisha wa kuabudu unaofundishwa katika Warumi 12:2.

(5) Kutaja theolojia ya kuabudu yenye msingi wa kibiblia.

Matayarisho kwa somo hili

Kariri 1 Wakorintho 10:31.

Utangulizi

Katika mwaka huohuo, taifa moja la Kiafrika latokea kwenye orodha mbili: “Idadi kubwa zaidi ya Wakristo katika Afrika” na “Taifa lenye ufisadi mwingi zaidi barani Afrika.”

Mchungaji wa mojawapo ya makanisa makubwa zaidi barani Asia apatikana na hatia ya kuiba mamilioni ya dola.

Kiongozi wa kanisa kuu la Marekani ajiuzulu baada ya kukiri kutokuwa mwaminifu katika ndoa.

Tatizo ni nini? Kuna sababu nyingi katika hali hizi, lakini jambo moja ni la kawaida kwa wote: Ibada ya Jumapili haiathiri maisha ya Jumatatu. Jumapili inachukuliwa kuwa "ibada" - hisia na shauku. Jumatatu inachukuliwa kuwa "maisha halisi"- mazoea ya biashara yasiyo ya kimaadili na kujiridhisha. Kwa watu wengi, shughuli za ibada hazileti mabadiliko ya maisha.

► Jadili jinsi ibada inavyoathiri maisha yako ya kila siku. Je, biashara yako inaendeshwa tofauti tofauti kwa sababu ya ibada yako? Je, mahusiano ya familia yako yanaboreshwa kwa sababu ya ibada yako? Maadili yako? Siasa zako? Mazoea yako ya kifedha? Je, unaishi maisha ya mtidno wa ibada?

Ibada: Zaidi ya Jumapili

Tatizo lililoelezewa katika utangulizi wa somo hili si geni. Amosi alizungumza na watu walioleta dhabihu na kufuata taratibu za Hekalu, lakini walishindwa kuishi maisha ya kumcha Mungu (Amosi 5:21-24). Yeremia alihubiri kwa watu waliopaza sauti “Hekalu, Hekalu,” lakini hawakujua uhalisia wa uwepo wa Mungu (Yeremia 7:4). Yesu alieleza wale walioshika kila undani wa sheria, ambao walitoa zaka kwa vitu vidogo zaidi, na ambao walikuwa waaminifu katika maombi, utunzaji wa Sabato na taratibu nyingine za ibada, lakini mioyo yao ilikuwa michafu (Mathayo 23:23). Watu hawa walidai kuwa waabudu, lakini ibada yao ilikuwa ya uwongo. Ibada ya kweli huathiri maisha yote.

[1]Paulo aliwaandikia waumini ambao walikabili suala la nyama iliyotolewa kwa sanamu. Baada ya kushughulikia tatizo hili, Paulo alihitimisha, “Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu” (1 Wakorintho 10:31). Ingawa Paulo alikuwa akizungumzia suala la nyama iliyotolewa kwa sanamu, kanuni hiyo inatumika katika nyanja zote za maisha. Ikiwa tunaabudu kweli, maisha yetu ya kila siku yataishi kwa utukufu wa Mungu.

Moja ya ufafanuzi wa kuabudu ni “…mwitikio wa yote tuliyonayo kwa yote ambayo Mungu alivyo.”[2] Ufafanuzi huu unaonyesha kwamba ibada itahusisha nyanja zote za maisha. Kuna kanuni mbili ambazo lazima ziwekwe kwa usawa wakati wa kufafanua ibada.

Ibada ya Pamoja: Ibada siku ya Jumapili

Ibada ya pamoja inarejelea mkusanyiko wa kundi la kanisa. Mkutano huu unaweza kutokea katika jengo la kanisa, katika nyumba, au katika mazingira mengine. Mpangilio sio muhimu, lakini wakati uliotengwa kwa ajili ya ibada ya pamoja ni muhimu. Wakristo wamepewa fursa na wajibu wa kukusanyika kwa ajili ya ibada ya pamoja (Waebrania 10:25).

Kuabudu kama Mtindo wa Maisha: Kuabudu Katika Maisha Yote

Katika Bustani ya Edeni, kama ungewauliza Adam na Hawa, “Mnaabudu lini?” wangejibu, “Tunaabudu daima. Maisha yetu yote ni ibada.” Hii ni ibada kama mtindo wa maisha.

[3]Kuabudu ni mkutano wa pamoja wa waumini na maisha yanayoishi kwa utukufu wa Mungu. Askofu wa karne ya pili Iraeneus wa Lyons alisema, “Utukufu wa Mungu ni mwanadamu, aliye hai kabisa.” Huu sio ubinadamu unaozingatia mwanadamu; ni utambuzi wa Mungu kwamba kusudi kuu la mwanadamu ni kuishi kwa utukufu kwa Mungu. Hii ndiyo ibada ya kweli.

Kama Wakristo, tunatoa kila kitu maisha yetu, hata mambo ya kawaida, kwa Mungu. Ibada sio Jumapili tu. Kazi zetu, michezo, na kazi zetu za kawaida hufanywa kwa utukufu wa Mungu. Warumi 12:1 inaonyesha kwamba ibada inahusisha kutoa miili yetu kuwa dhabihu iliyo hai; hii ni ibada yetu ya kiroho. Mtazamo wa kibiblia kuhus ibada ni kwamba ibada sio kutaniko la kila wiki tu; ni kutoa maisha yetu yote kwa Mungu.

Mtazamo wa kibiblia wa ibada unajumuisha ibada ya pamoja na maisha ya kila siku. Vipengele vyote viwili ni muhimu. Ikiwa tunasahau kwamba ibada inahusisha maisha ya kila siku, tunaweza kuhudhuria ibada bila kuona matokeo yoyote katika maisha yetu yote. Hii inatupelekea kushiriki katika ibada ya pamoja huku tukishindwa kuishi katika utii wa kila siku kwa Mungu.

Hata hivyo, ikiwa tunasisitiza tu “ibada ni ya maisha yote,” tunasahau umuhimu wa wakati wa kawaida uliotengwa kwa ajili ya ibada ilyojikita. Kushiriki katika ibada ya ushirika hutukumbusha uwakili wa Mungu wa maisha.

Kanuni hii ya uwakili inaonekana katika zaka na Sabato. Uwakili wa Kikristo unamaanisha kwamba pesa zetu zote ni za Mungu; imani yetu katika kanuni hiyo inaonekana kwa zaka yetu. Mtazamo wa Kikristo wa wakati unamaanisha kwamba maisha yote ni ya Mungu; tunadhihirisha hilo kwa kutenga siku moja kwa juma kuabudu na kupumzika. Vivyo hivyo, sehemu zote za maisha yetu ni sehemu ya ibada; tunaonyesha hilo kwa kukusanyika pamoja na waamini wenzetu kwa ajili ya ibada ya pamoja.

Bob Kauflin alionyesha uhusiano kati ya ibada ya ushirika na ibada kama mtindo wa maisha:

Jumapili inaweza kuwa kilele cha wiki yetu, lakini sio kilele pekee. Wakati wa wiki, tunaishi maisha ya ibada tunapopenda familia zetu, kupinga majaribu, kusema kwa ujasiri kwa ajili ya watu wanaodhulumiwa, kusimama dhidi ya uovu, na kutangaza injili. Katika mambo yote hayo, sisi ni kanisa linaloabudu lililotawanyika.

Lakini tunachoka katika vita vyetu dhidi ya ulimwengu, mwili wetu, na shetani na tunahitaji kuimarishwa na kutiwa moyo na Neno la Mungu na uangalizi wa watakatifu wengine. Tunataka kushirikiana na wale ambao Mungu ametuunganisha nao kupitia damu ya Mwanawe. Kwa hiyo, tunakutana ili kuwa kanisa linaloabudu lililokusanyika.[4]

 


[1]

“Kiongozi wa kuabudu anapaswa kuwa mtu wa mfano wa ibada katika nyanja zote za maisha; ambaye humfuata Mungu kwa kila kitu; ambaye huongoza kanisa katika mtindo wa maisha wa kuabudu.”

- Imetolewa na Stephen Miller

[2]Warren Wiersbe, Real Worship. (Grand Rapids: Baker Books, 2000), 21
[3]

“Kutoa maisha yetu katika kumtumikia Mungu kila siku ni wito wetu wa maisha yote. Ibada ya Jumapili asubuhi ni mwendelezo wa wito huo.”

- Barry Liesch

[4]Bob Kauflin, Worship Matters (Wheaton: Crossway Books, 2008), 210

Ibada: Kuishi kwa Utukufu wa Mungu

Ibada huonyesha maadili yetu

Tumeumbwa kwa ajili ya ibada. Sisi sote tunaabudu kitu au mtu fulani. Tunaabudu kile tunachothamini zaidi. Ibada husema, "Hii ndiyo inayo nafasi ya kwanza katika maisha yangu.”

[1]Watu wengi huabudu pesa, kazi, cheo, mahusiano, au mmbo yanafurahisha. Mambo hayo huchukua nafasi ya kwanza katika maisha yao. Unajuaje unachoabudu? Angalia maisha yako. Ni nini kinachopata nguvu zaidi, muda, na pesa? Hilo ndilo uliloamua ni la thamani zaidi kwako; hicho ndicho unachokiabudu.[2]

Mungu pekee ndiye anayestahili kuabudiwa; vitu vingine vinafuata. Mtindo wa maisha wa kuabudu humtanguliza Mungu katika kila jambo. Waabudu wa kweli wamemweka Mungu kwenye kiti cha enzi cha maisha yao; Ana thamani ya juu zaidi. Hiyo inamaanisha kwamba kwa waabudu wa kweli, kila sehemu ya maisha yao inaishi kwa utukufu wa Mungu.

Ibada ya Kweli Hubadili Maadili Yetu

Katika Isaya 6, tunaona kwamba ibada ya kweli inabadilisha. Ibada sio tu inaonyesha maadili yetu, pia inabadilisha maadili yetu.

Kuabudu, kwa Mungu au sanamu, kunabadilisha jinsi tulivyo. Zaburi 115:8 inaonyesha kwamba kuabudu sanamu hutubadilisha na kuwa mbaya. “Wazifanyao watafanana nazo, kila mmoja anayezitumainia.” Waabudu masanamu wanakuwa kama masanamu yao. Wale wanaoabudu pesa wanazidi kuwa wenye tamaa; wale wanaoabudu anasa wanazidi kuwa watumwa wa starehe; wale wanaoabudu umaarufu wanazidi kuwa wabinafsi. Tunakuwa kama chochote tunachoabudu.

[3]Vivyo hivyo, wale wanaomwabudu Mungu wanazidi kuwa kama yeye. “lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu” (2 Wakorintho 3:18). Katika ibada, tunabadilishwa kuwa mfano wake.

Tunapoabudu, maadili yetu yanabadilishwa. Kama waabudu, lazima tuulize, “Je, ibada inabadilisha maisha yangu?”

Kuishi kwa Utukufu wa Mungu Kunahusisha Maisha Yote

Ibada kama mtindo wa maisha humaanisha kwamba maisha yote unaishi kwa utukufu wa Mungu. Wakristo wengi hugawanya maisha yao katika nyanja mbili zilizotenganishwa: takatifu (Jumapili) na ya kidunia (Jumatatu-Jumamosi). Wanaishi kama “Wakristo wa Jumapili.” Wanahudhuria kanisani na kukiri imani ya Kikristo, lakini ibada ya Jumapili haina matokeo kwenye biashara ya Jumatatu, maisha ya familia ya Jumatano, au burudani ya Jumamosi.

Neno la kidunia linamaanisha maisha katika ulimwengu huu. Mkristo ameitwa kuishi maisha ya ulimwengu huu kwa utukufu wa Mungu. Mkristo anatakiwa kuishi siku ya Jumatatu kwa njia inayoonesha matokeo ya ibada ya Jumapili. Mwishoni mwa ibada, lazima tujiulize, "Nitafanya nini kesho ili kuweka ibada ya leo katika vitendo?" Haya ni maisha yanayoishi kwa utukufu wa Mungu.

Je! Kuishi kwa Utukufu wa Mungu Kunaonekanaje?

Kuishi kwa utukufu wa Mungu kunamaanisha kwamba maisha yote yanatawaliwa na shauku kwa ajili ya Mungu. Inamaanisha kumpenda Mungu kiasi kwamba furaha yetu ndiyo inayompendeza. Mtu mmoja alisema kwamba kumpenda mtu kunamaanisha kuwa na wasiwasi naye. "Unampenda mtu (au kitu) ambacho unakifikiria juu yake wakati haufikirii juu ya kitu kingine chochote."

Vivyo hivyo, Louie Giglio anapendekeza kwamba “tunajua kile kilicho kikuu katika nafsi zetu kwa kile kinachotoka vinywani vyetu.”[4] Tunazungumza kile ambacho ni cha thamani zaidi kwetu.

Hiyo inaweza kuonekana kuwa rahisi kupita kiasi, lakini fikiria. Je, watu wanaopenda pesa wanazungumzia nini? Pesa. Wanatukuza pesa. Mshabiki wa michezo anazungumza nini? Michezo. Anaitukuza timu anayopenda ya michezo.

Je, hiyo inamaanisha kwamba Mkristo anapaswa kuzungumza kuhusu Biblia katika kila hali? Hapana; ina maana tu kwamba kila jambo tunalozungumzia litamtukuza Mungu. Tunapofanya uamuzi wa kibiashara, hatuwezi kuwaambia wenzetu, “Uamuzi huu lazima umtukuze Mungu,” lakini utukufu wa Mungu utaathiri uamuzi wetu. Tunapolazimika kumrudi mtoto , huenda tusianze mazungumzo kwa kusema, “Mwanangu, nataka adhabu hii imtukuze Mungu,’ lakini tutajiuliza, Je, nidhamu hii itampendeza Mungu au ninafurahisha hasira yangu tu? Je, hivi ndivyo Baba yangu wa mbinguni angenirudi mimi?’’

Tukiwa Wakristo, tunafanya kila uamuzi katika nuru ya utukufu wa Mungu. Ibada kama mtindo wa maisha kunamaanisha kwamba Mungu na utukufu wake ndio kiini cha kila kitu tunachofanya.

Katika somo la awali, tuliona kwamba bila neema, ibada ya pamoja inakuwa ya kisheria, ambapo tunajiuliza "Je, tunawezaje kuabudu kwa njia ambayo inapata kibali cha Mungu?" Vivyo hivyo, bila neema, mtindo wa maisha wa ibada unakuwa mzigo wa kisheria, ambapo tunajiuliza “Je, ikiwa uamuzi huu sio njia bora ya kumtukuza Mungu? Nikiharibu, je, Mungu atakasirika?”

Tofauti na ibada ya kisheria, kuabudu katika nuru ya neema ya Mungu kunakuwa ni heshima ajabu. Ibada ya pamoja kwa nuru ya neema ya Mungu ni fursa ya kusherehekea Mungu ni nani na amefanya nini. Vivyo hivyo, mtindo wa maisha wa kuabudu (unapoishi katika nuru ya neema ya Mungu) ni fursa ya kumtukuza Mungu katika maisha ya kila siku.

Uamuzi wa kibiashara wa Jumatatu si juhudi isiyo na furaha ya kutii sheria ya Mungu; ni fursa ya furaha ya kumtukuza Mungu na maadili yanayolingana na tabia yake. Kumrudi mtoto si kitu cha kuhuzunisha kinachofanywa tu ili tusimkosee Mungu; ni fursa ya furaha ya kuiga tabia ya upendo ya Mungu kwa mtoto wako. Neema inabadilisha mtindo wa maisha wa ibada.


[1]

“Kila mtu ana madhabahu. Na kila madhabahu ina kiti cha enzi. Basi unajuaje unachokiabudu? Ni rahisi: fuata mkondo wa muda wako, mapenzi yako, nguvu zako, pesa zako, na utii wako. Mwishoni mwa njia hiyo utapata kiti cha enzi, na chochote, au yeyote yule, aliye kwenye kiti hicho cha enzi ndiye aliye na thamani kuu kwako. Kwenye kiti hicho cha enzi. is what you worship.”

- Louie Giglio

[2]Imetolewa kutoka kwa Louie Giglio, The Air I Breathe: Worship as a Way of Life. (Sisters, OR: Multnomah Publishers, 2003).
[3]

Ibada sio tu kitu tunachofanya; 
ibada inatufanyia kitu sisi.

[4]Louie Giglio, "Zaburi 16" katika Matt Redman na Friends, Inside, Out Worship (Ventura: Regal Books, 2005), 78

Kuabudu kama Mtindo wa Maisha: Mfano wa Kibiblia

Katika Warumi 12:1, Mkristo anaitwa kujitoa mwenyewe kama dhabihu iliyo hai, takatifu na ya kumpendeza Mungu. Hii ndiyo ibada yetu ya kiroho. Warumi 12:2 inaonyesha jinsi dhabihu hii itakavyotolewa. Andiko hili ni muhimu sana kwa kuelewa ibada kama mtindo wa maisha.

Baada ya sura 11 ambamo Paulo anaweka msingi wa kitheolojia kwa maisha ya Kikristo, anahamia kwenye vitendo. Kwa kuwa tumehesabiwa haki kwa neema (Warumi 1-11), tunapaswa kuishi kwa namna fulani (Warumi 12-16). Sura hizi zinatoa kielelezo cha mtindo wa maisha wa kuabudu.

Mtazamo Hasi katika Mtindo wa Maisha wa Ibada

Paulo anaanza kwa amri hasi: “Msiifuatishe namna ya dunia hii.” Hatupaswi kuishi kwa kufuata kawaida za ulimwengu huu. Hatuwezi kujisalimisha kwa ulimwengu huu na ufalme wa mbinguni pia; hatuwezi kumwabudu Mungu na roho wa wakati huu.

J.B. Philips alitafsiri agizo la Paulo, “Usiruhusu ulimwengu unaokuzunguka ukufinyange katika mfumo wake.” Wakati udongo unapowekwa kwenye umbo lake, haraka unachukua umbo hilo. Ulimwengu unataka kuwafinyanga Wakristo ili wachukue umbo lake. Ulimwengu unataka kutulazimisha tukubaliane na matakwa yake. Badala yake, tunapaswa kuishi maisha ya ibada, kukataa ushawishi wa ulimwengu huu.

Kishawishi hiki ni hatari sana kwa sababu tunaweza kubadilika bila hata kufahamu umbo hilo. Samaki wanaoishi ndani ya maji hawafikirii, "Haya ni maji." Ni ulimwengu anamoishi tu. Mdudu anayetambaa kwenye uchafu hafikirii, "Huu ni uchafu." Ni ulimwengu anamoishi tu. Tusipokuwa waangalifu, Mkristo anayeishi katika ulimwengu ulioanguka hatafikiri, “Huu ni ulimwengu ulioanguka.” Itakuwa tu ulimwengu anaoishi.

Hii ndiyo sababu ibada ya pamoja ni muhimu. Mwandishi wa Waebrania alionya kwamba hatupaswi kupuuza kukutana pamoja. Kwa nini? Kwa sababu hivi ndivyo tunavyotimiza amri hizi zingine:

  • “Na tukaribie wenye moyo wa kweli, kwa utimilifu wa Imani…” (Waebrania 10:22)

  • “Na mlishike sana ungamo la tumaini letu, lisigeuke…” (Waebrania 10:23)

  • “Tukaangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na kazi nzuri…” (Waebrania 10:24)

Katika ibada, tunakumbushwa kwamba sisi si wa ulimwengu huu. Huko Babeli, akiwa amejitenga na Hekalu, hakuweza kushiriki katika ibada ya pamoja ya watu wake, Danieli aliomba mara tatu kwa siku, madirisha yake yakiwa yamefunguliwa kuelekea Yerusalemu (Danieli 6:10). Ibada ilimtia nguvu Danieli dhidi ya kugeuzwa na ulimwengu wa Babeli. Alipokabili Yerusalemu, Danieli alikumbushwa, “Mimi si mwenyeji wa Babeli; Mimi ni raia wa Yerusalemu. simsujudu Marduk; Ninamtumikia Yehova.”[1]

Mtindo wa maisha wa ibada unamaanisha kwamba tunakataa kufinyangwa katika umbo la ulimwengu wetu. Hii ni zaidi ya kushinda majaribu fulani. Ni zaidi ya kuzingatia sheria fulani. Ni zaidi ya mtindo fulani wa mavazi, kanuni za tabia, au utamaduni wa kidini. Ni njia nzima ya kufikiria na kuishi. Inamaanisha kutathmini kila kitu kulingana na ufalme wa Mungu.

Kama Wakristo, hatuweza kamwe kufaa kwa urahisi katika utamaduni unaotuzunguka. Baada ya darasa nchini China kuhusu Mahubiri ya Mlimani, mwanafunzi mmoja alisema, “Nchini China, ni vigumu kuishi kama Yesu alivyofundisha.” Mwalimu akajibu, “Usishangae. Hata Marekani, pia ni vigumu kuishi kama Yesu alivyofundisha.” Haijalishi utamaduni ni upi, mtindo wa maisha wa ibada utapingana na roho ya ulimwengu huu.

Mtazamo Chanya katika Mtindo wa Maisha wa Ibada

Kufuatia amri hiyo hasi, Warumi 12 inaendelea na maagizo chanya: “bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu.”

Kinyume cha kufuata namna ya dunia hii sio tu kuwa tofauti au kusisitiza utu wako mwenyewe. Badala yake, ni kubadilishwa mpaka utakapojua mapenzi ya Mungu. Wakristo wengine wamefuata mtindo wa maisha tofauti na tamaduni zao, lakini hawajageuzwa kuendana na mapenzi ya Mungu. Badala yake, wametumia mtazamo fulani wa kisiasa, kijamii, au mavazi kwa ajili ya mustakabali wa dunia hii. Hawajabadilishwa kwa kufanywa upya nia zao.

J.B. Phillips alitafsiri, “Usiruhusu ulimwengu unaokuzunguka ukufinyange katika mfumo wake” (hasi), “bali acha Mungu akufanye upya ili mtazamo wako wote wa akili ubadilishwe” (chanya). Sehemu iliyobaki ya kitabu cha Warumi inaonyesha jinsi nia iliyogeuzwa itaonekana.

  • Warumi 12: Muumini aliyebadilishwa hutumia karama zake za kiroho kuwatumikia wengine.

  • Warumi 13: Muumini aliyebadilishwa anaheshimu mamlaka ya kiraia.

  • Waroma 14: Mwamini aliyebadilishwa anaheshimu imani ya waamini wenzake.

Mtindo wa maisha wa kuabudu ni zaidi ya tabia; ibada inabadilisha njia yetu yote ya kufikiri. Fikiria matokeo ya mtindo wa maisha wa ibada:

  • Je, bara la Afrika litakuwaje ikiwa wafanyabiashara na wanasiasa Wakristo watabadilishwa katika mitazamo yao kuhusu pesa na mamlaka?

  • Je! Makanisa ya Asia yatakuwaje ikiwa viongozi watajiona kama mawakili wa pesa za Mungu?

  • Je! Ndoa huko Amerika itakuwaje ikiwa Wakristo wanaona uzinzi kupitia macho ya Mungu, badala ya macho ya Hollywood?

Mtindo wa maisha wa ibada hubadilisha mawazo ya mwamini; akili iliyobadilishwa itaonekana katika maisha yaliyobadilishwa; maisha yaliyobadilishwa yatabadilisha jamii. Mtindo wa maisha wa ibada hatimaye utabadilisha ulimwengu wetu.


[1]Imefafanuliwa kutoka kwa Tim Keep, Misheni za Methodisti ya Biblia. Mahubiri ya kanisa dogo katika Hobe Sound Bible College, Novemba 2013.

Hatari za Ibada: Kuabudu bila Utiifu

Mitume walionya dhidi ya ibada bila utii. Watu wa siku za Yeremia waliamini kwamba Hekalu lingewalinda kutoka katika utumwa wa Babeli. Yeremia alijibu, “Msitumainie maneno ya uongo, mkisema, Hekalu la BWANA, Hekalu la BWANA, Hekalu la BWANA ndiyo haya.’” (Yeremia 7:4) Badala yake,

Mkitengeneza kabisa njia zenu na matendo yenu;

Kama mkihukumu hukumu ya haki kati ya mtu na jirani yake;

Kama hamwonei mgeni, wala yatima, wala mjane, wala kumwaga damu isiyo na hatia mahali hapa, wala kuifuata miungu mingine kwa hasara yenu mwenyewe:

Ndipo nitakapowakilisha mahali hapa, katika nchi hii niliyowapa baba zenu, toke zamani hata milele (Yeremia 7:5-7).

Watu wa Israeli waliamini wangeweza kubadilisha ibada kwa utii. Manabii walihubiri kwamba ibada bila utii haina maana.

Katika baadhi ya mila, utii unabadilishwa na ibada ya liturujia. Vipengele vya ibada vipo. Nyimbo zinasema ukweli. Maandiko yanasomwa na kuhubiriwa. Maombi yanaombewa. Hata hivyo, hakuna utii kwa Neno la Mungu. Maisha hayabadilishwi. Hii ni ibada ya liturujia, sio ibada.

Katika baadhi ya mila, utii hubadilishwa na mwitikio wa kihisia. Lengo la ibada ni kuzalisha hisia fulani. Muziki huchochea hisia. Mahubiri huongoza kwenye mwaliko au muda wa kujitoa kwa Mungu. Hata hivyo, ibada hiyo haifuati maisha ya utii na kujitoa kwa Mungu. Hii ni hisia, sio ibada.

Ibada katika Hekalu ilisherehekea agano la Israeli na Mungu na kuwakumbusha Israeli wajibu wao wa agano. Katika kanisa la kwanza, ibada iliadhimisha agano jipya lililotolewa kupitia kifo cha Yesu na kuwakumbusha Wakristo wajibu wao wa kuishi maisha matakatifu. Ibada ambayo haina matokeo ya utii ni ya uwongo.

Ibada ya kweli humbadilisha mwenye kuabudu. Katika kipindi hiki chote, tumeona kwamba watu wanaoabudu kikweli hubadilishwa. Lengo la kozi hii si tu kwamba utakuwa bora zaidi katika kupanga na kuongoza huduma za ibada, lakini kwamba utakuwa mwabudu ambaye anabadilishwa na ibada. Kisha utaliongoza kanisa lako katika ibada inayombadilisha kila mshirika wa kanisa.

Hitimisho: Ushuhuda wa Mchungaji

Ibada ya kweli ina matokeo gani? Msikilize mchungaji wa kanisa la Uhispania.

“Mnamo 1991, hali ya kiroho ya kanisa letu ilikuwa katika hali ya chini zaidi. Uasherati ulikuwa umenasa baadhi ya washirika wetu. Tulipowaadhibu washirika walioanguka, kanisa liligawanyika. Hatimaye, katika hali ya kuvunjika kiroho na kihisia, mwongofu mpya alipendekeza kwamba tufunge na kuomba siku nzima ya Jumapili. Tulifanya hivi na Mungu akaanza kutembea kati yetu.

“Wiki chache baadaye, tulianza kambi yetu ya kila mwaka. Mgawanyiko fulani kanisani ulikuepo. Mwinjilisti alipoanza mahubiri yake Jumatano usiku, alihisi kwamba Mungu alimtaka aimbe ‘Jinsi Ulivyo Mkuu.’

“Alipokuwa akiimba wimbo huu, utukufu wa Mungu ulishuka juu ya umati wenye njaa. Wengine waliitikia kwa sifa; wengine walianza kumtafuta Mungu madhabahuni. Mwanamke aliyekuwa mzizi wa migogoro kanisani alitokwa na machozi. Akiwa amesimama mbele ya watu 400, alikiri, ‘Mimi ni mwanamke nisiye na furaha zaidi kwa sababu nimemkosea Mungu na kanisa lake kwa kuhifadhi chuki moyoni mwangu. Ninamwomba Bwana anisamehe, na nawasihi ninyi kama kanisa mnisamehe.’

"Maneno hayo yalipotoka midomoni mwake, wengine walipatanishwa. Jioni hiyo, Mungu alirudisha umoja katika kanisa letu. Watu wa Mungu walipojinyenyekeza katika maombi na kufunga, na kama mtumishi wa Mungu alivyokuwa mtiifu kwa uongozi wa Roho Mtakatifu, tuliletwa katika uwepo wa Mungu. Dhambi iliungamwa; umoja ulirejeshwa. Haya ndiyo dmatokeo ya ibada ya kweli.”[1]


[1]Ushuhuda wa Mchungaji Sidney Grant, Hope International Missions

Mapitio ya Somo la 10

Mapitio ya Masomo Yote

(1) Ibada ya pamoja hufanyika Jumapili; mtindo wa maisha wa ibada hutokea katika maisha ya kila siku. Zote mbili ni muhimu kwa mtazamo wa kibiblia wa ibada.

(2) Ibada ya kweli inaonyesha kile tunachothamini hasa.

(3) Ibada ya kweli hubadilisha kile tunachothamini.

(4) Mtindo wa maisha wa kuabudu unamaanisha kuishi kwa utukufu wa Mungu. Hii ina maana kwamba Mungu atakuwa kitovu cha maisha yote.

(5) Mfano wa kibiblia wa mtindo wa maisha wa kuabudu unaonekana katika Warumi 12:2. Inajumuisha

  • Kipengele Hasi: “Msiifuatishe namna ya dunia hii.”

  • Kipengele chanya: “Mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu.”

Jaribio Somo la 10

Majaribio ya Masomo Yote

(1) Andika karatasi ya kurasa 3-4 yenye kichwa "Theolojia Yangu ya Ibada." Karatasi hii inapaswa kuonyesha jinsi ibada inavyoegemezwa kwenye kanuni za Maandiko. Karatasi inapaswa kuwa ya kibiblia na ya vitendo.

(2) Hubiri mahubiri kuhusu ibada ya kweli yanayotegemea Yohana 4:23-24.

(3) Kumaliza mradi wako wa somo: Andika taarifa ya ukurasa mmoja kwa kiongozi wa darasa ambayo inajumlisha kile umejifunza kutoka katika "Safari yako ya Siku 30 ya Ibada." Wala huhitaji kugeuza karatasi yako.

(4) Kwa jaribio lako la mwisho, andika 1 Wakorintho 10:31 toka kwenye kumbukumbu.