Maisha Na Huduma Ya Yesu
Maisha Na Huduma Ya Yesu
Audio Course Purchase

Search Course

Type at least 3 characters to search

Search through all lessons and sections in this course

Searching...

No results found

No matches for ""

Try different keywords or check your spelling

results found

Lesson 9: Kuacha Urithi

24 min read

by Randall McElwain


Malengo ya Somo

Kufikia mwisho wa somo hili, kila mwanafunzi atapaswa:

(1) Kuelewa urithi wa mwisho wa Yesu kwa wanafunzi wake na kanisa.

(2) Kutambua umuhimu wa umisheni ulioko katika urithi wa Yesu

(3) Kukubaliana na matokeo endelevu ya huduma ya Yesu kupitia wanafunzi wake katika Kitabu cha Matendo

(4) Kukuza hatua za vitendo za kuacha urithi wa huduma yako wenyewe.

Kanuni za Huduma

Kipimo cha huduma yetu ni kile tunachokiacha nyuma tutakapokuwa hatupo tena kwenye huduma.

Utangulizi

Tim alikuwa anakaribia kustaafu baada ya miaka mingi ya utumishi kama mchungaji aliyepata kuheshimiwa. Nilimwuliza, “ Unaliandaaje kanisa katika kustaafu kwako? Ni nini maono ya kanisa kwa miaka kumi ijayo? Jibu lake lilinifanya nikapigwa na bumbuazi. “ Sitakuwepo tena hapa. Kwa hiyo sina cha kujali ni nini kitakachotokea baada ya kuwa nimendoka.” Huyu mchungaji :hakuwa ameelewa kanuni muhimu ya huduma: kipimo cha mwisho cha huduma zetu ni kile kinachofanyika baada ya sisi kuondoka.

Fanya ulinganifu wa huyu mchungaji na mchungaji mwingine aitwaye Pete. Pete alifariki ghafla baada ya miaka ishirini na tano ya huduma. Wakati wa miaka hiyo, Pete alikuwa ameongoza huduma nyingi katika kanisa lake. Alikuwa ameanzisha huduma kwa watu wasio na makazi, programu ya kuhudumia walioathirika na madawa ya kulevya, na makongamano kwa ajili ya viongozi wa wafanyabiashara. Kwenye mazishi ya Pete, kiongozi wa huduma ya kushughulikia waathirika wa madawa ya kulevya alisema, “Mwezi uliopita, Pete na mimi tulijadiliana kuhusu bajeti ya mwaka ujao.” Kiongozi wa huduma ya wasiokuwa na makazi alitoa ramani ya jengo jipya kwa ajili ya makazi ya familia hizo. Kwa uangalifu mkubwa, Pete alikuwa ameweka mipango ya baadaye ya huduma. Alikuwa ameacha urithi.

Katika somo hili la mwisho, tutajifunza kuhusu mafundisho ya mwisho ya Yesu kwa ajili ya wanafunzi wake, kukabidhi wanafunzi wake majukumu kwa mara ya mwisho, na huduma za wanafunzi wake baada ya kupaa mbinguni. Tutajifunza masomo yanayohusu jinsi ya kuacha urithi.

► Je, kama ulikuwa ufariki usiku wa leo, utaacha urithi gani?

  • Nini urithi wako kwa familia yako?

  • Nini urithi wako kwa jamii yako?

  • Nini urithi wako kwa huduma yako?

Mihadhara ya Yesu ya Kuaga

Yohana 13-16 inaweza kulinganishwana na “mihadhara ya kuaga” kwenye Agano la Kale ya Yakobo, Musa, Yoshua na Daudi.[1] “Mihadhara ya kuaga” ya Yesu inatoa baadhi ya mafundisho yake ya ndani sana na ya mwisho.

Yohana 13:1 inatoa muundo wa mafundisho haya ya kuaga: “Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba.” Kama wewe ungejua utakufa katika kipindi cha masaa arobaini na nane yajayo, ungesemaje kwa wale ambao utawaacha kuendeleza huduma yako? Maneno hayo yatawakilisha kile ambacho ulikuwa umeamini kwamba ni muhimu sana kwa wafuasi wako.

Kwenye Chakula cha jioni cha Mwisho, Yesu alionyesha upendo wake wa mwisho kwa wanafunzi wake kwa matendo yake (ya kuwatawadha miguu) na kwa maneno yake kawa pamoja. Yesu ”aliwapenda watu wake katika ulimwengu.” Na sasa, “aliwapenda hadi mwisho” (Yohana 13:1). Neno “Hadi mwisho” linabeba nadharia kuu mbili:

1. Inamaanisha kwamba Yesu “aliwapenda hadi mwisho” wa muda wa kukaa nao.

2. Inaamaanisha kwamba “Yesu aliwapenda kwa upeo wake wote wa mwisho.” Yesu aliwapenda kabisa.

► Soma Yohana 13:31-14:31.

Maamrisho na Ahadi katika Mihadhara ya Yesu ya Kuaga

Amri: Mpendane (Yohana 13:34).

“Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. ”Kwa kikundi cha wanafunzi kilichojulikana zaidi kwa kubishanabishana kuliko kupendana, amri hii ilikuwa ngumu.

Ilikuwaje hii “ikawa amri mpya?” Hata Agano la Kale liliamrisha watu wa Mungu kwamba “Mpende jirani yako.” Kuna vipengele viwili “vipya” vya Yesu kufundisha kuhusu upendo.[2]

Kipengele cha kwanza, Yesu alitoa aina ya upendo ambao aliuamrisha. Walikuwa wapendane kama yeye alivyowapenda. Baada ya kuwatawadha miguu yao kwa unyenyekevu mkubwa, Yesu aliwaambia, “Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo.” Aliingiza upendo ambao unadhihirishwa kwenye huduma ya unyenyekevu. Wanafunzi, kwa wakati ule na hata sasa, ni lazima wawe na uwezo wa kupenda kama Yesu alivyopenda. Upendo huu unachukua kitambaa cha kujifutia ili kutumika. Upendo huu unatumikia hata msaliti. Upendo huu unadumu hata kama ni kufikia mahali pa kufa.

Kipengele cha pili, Upendo kati ya Wakristo ulitakiwa uwe ushuhuda wa aina yake wa ukweli wa ujumbe wa Yesu. “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.” Baada ya hapo, Yesu anaomba “Wote wawe na umoja; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma” (Yohana 17:23). Upendo na umoja katika kanisa ni lazima uwe ushuhuda kwa ujumbe wa Yesu.

Wakristo wengi wamegundua kwamba ni rahisi zaidi kumpenda jirani ambaye bado hajaamini kuliko kumpenda ndugu wa Kikristo ambaye amejaa tele makosa ya kibinadamu. Lakini kama Wakristo, tumepewa amri “Mpendane.” Miaka hamsini baadaye, Yohana akalikumbusha kanisa kuhusu ujumbe huu:

Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona. Na amri hii tumepewa na yeye, ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake (1 Yohana 4:20-21).

Yesu alianza na ujumbe wake wa kuaga kwa amri ya mpendane. Amri hii ndio msingi wa kila kitu alichozungumza katika ujumbe huu.

Amri: Msifadhaike, Aminini (Yohana 14:1).

Kama alivyokuwa anafanya mara kwa mara, Petro aliingilia kati kumwuliza Yesu, “Bwana unaenda wapi?” Katika jibu lake, Yesu alitabiri kuhusu Petro kumkana. Kisha Yesu akaendelea na ujumbe wake kwa Petro, kwa ajili a wanafunzi wake na kwa ajili yetu sisi wa leo. “Msifadhaike mioyoni mwenu.”

Kwa kuwa kuna kituo cha sura baada ya Yohana 13:38, mara nyingi tunasoma Yohana 14:1 kana kwamba ndiyo tunaanza aya mpya. Yohana 14:1 ni sehemu ya jibu kwa Petro. Lisome kwa njia hii:

Petro, utanikana mara tatu. Wewe ni mdhaifu kuliko unavyojifikiria. Lakini usikate tamaa; nina ujumbe wa matumaini kwa ajili yako, Petro, na kwa ajili ya wale wote ambao katika muda mfupi tu ujao watakimbia kwa hofu ya kukamatwa. “Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi.”

Petro alihitajika kujua kwamba pamoja na kushindwa kwake, Yesu alikuwa na ujumbe wa matumaini. Wanafunzi walihitaji kujua kwamba pamoja na kuwa na hofu, Yesu alikuwa na ujumbe wa matumaini. “Msifadhaike mioyoni mwenu” ni kwa wakati uliopo. Wakiwa wamepewa maonyo pamoja na upinzani wa viongozi wa kidini, wanafunzi tayari walishakuwa na mfadhaiko. Yesu anasema, “Acheni kufadhaika ….mnamwamini Mungu; niaminini na mimi.”

Njia pekee tunayoweza kuepuka kuwa na “mfadhaiko” kutokana na msongo wa huduma ni “kuamini.” Ninaandika somo hili katika siku ya Jumatatu asubuhi. Katika Jumatatu yeyote, kuna wachungaji duniani kote ambao wamekata tamaa. Jana, ulifundisha kwa uaminifu – na mmoja wa wafuasi wako akakasirika. Ulihubiri ujumbe wa kutubu – na hakuna hata mmoja aliyejitokeza. Uliita ambao hawajaokoka – hakuna hata mmoja aliyekuja.

Katika baadhi ya nchi, Kanisa linakabiliwa na upinzani wa serikali. Katika baadhi ya nchi, Kanisa linagubikwa na vitisho vya wajahidina wa Kiislamu. Katika baadhi ya nchi, kania linakabiliwa na vitisho vya tofauti za kijamii – hakuna anayejali. Yesu anasema, “Msifadhaike. Mnamwamini Mungu; niaminini na mimi.”

Ahadi: Mimi ndimi njia. (Yohana 14:6).

Yesu aliwapa matumaini wanafunzi wake kwamba yeye anaondoka kwenda kuwaandalia makao. Tomaso akaingilia kati, “Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia?”

Jibu la Yesu linafundisha kanuni muhimu sana ya maisha ya Mkristo. Yesu hakusema, “Hapa ndipo ninapokwenda.” Badala yake alisema, “Mimi ndimi njia.” Yesu hakuonyesha njia ya kupitia; alijionyesha yeye mwenyewe. Hakuna tamko lingine lililo wazi zaidi katika Maandiko linaloonyesha kwamba njia pekee ya kwenda kwa Baba ni kupitia kwa Yesu. Kinyume na madai ya wanatheolojia wanaopendelea mabadiliko ya wastani, Yesu alitamka wazi kwamba yeye peke yake ndiye njia ya kupitia kwenda kwa Baba.

Ahadi: Kazi kubwa kuliko hizo Mtafanya (Yohana 14:12-14).

Yesu aliahidi kwamba, “Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba.” Hizi kazi zitakuwa nyingi siyo kwa sababu zina mambo ya kushangaza zaidi, lakini ni kwa sababu zitakuwa kwenye uwigo mpana zaidi wa kufika. Wakati wa huduma yake duniani, kazi za Yesu zilikuwa zimesambaa katika eneo moja tu la kijeografia. Sasa, kwa sababu Yesu alikuwa anatuma Roho Mtakatifu, kazi zitakazofanywa na kanisa zitaufikia ulimwengu wote.

Yesu akaendelea, “Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.” Kuna nadharia kuu mbili zinazofungamana na ahadi hii:

(1) “Mkiomba lo lote kwa jina langu.”

Hii ni zaidi ya kuongezea “Kwa jina la Yesu” katika kila mwisho wa maombi yetu. Siyo kila kitu tunachokiweka katika maombi kitakachomlazimisha Yesu atoe majibu ya maombi yetu. Katika Biblia nzima, “jina” la Mungu linawakilisha tabia yake. Kuomba “Kwa jina la Yesu” inamaanisha ni kuomba kwa namna inayoendana na tabia ya Yesu na mapenzi yake.

Kuomba “kwa jina langu” inaweza ia ikamaanisha ni “kuja kwa Baba kupitia kwa mamlaka ya Yesu.” Kwa maana tangu Musa “alipokwenda kwa Farao, kusema naye kwa jina lako,” alikuja kwa mamlaka ya ya Mungu aliyemtuma (Kutoka 5:23). Kuomba kwa Jina la Yesu inamaanisha kuomba katika kibali na mamlaka yake. Tunamwendea Mungu kupitia maombezi ya Mwanae ambaye “yu hai sikuzote ili awaombee” (Waebrania 7:25).

(2) “…ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.”

Maombi yetu ni lazima yawe kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Yakobo aliwaonya wale ambao “Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu” (Yakobo 4:3). Tunapodai ahadi za Mungu, ni lazima tuwe na hakika kwamba tunaomba kwa ajili ya utukufu wa Mungu, na siyo kwa ajili ya makusudi yetu binafsi.

Amri: Mtazishika amri zangu (Yohana 14:15).

Yesu alitoa kiwango ambacho tunaweza kuupima upendo wetu kwake. “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.” Yohana akakumbuka kauli hii wakati alipoandika barua yake ya kwanza: “Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli” (1 Yohana 2:5). Kinyume na jinsi ambavyo wahubiri wengine wa wakati huu wanahubiri, Yesu kamwe hakufundisha kwamba wanafunzi wake wanaweza kuishi katika kutokutii kwa hiari amri zake. Upendo unaonekena katika utii wa hiari.

Ahadi: Naye atawapa Msaidizi mwingine (Yohana 14:16).

Neno lililotafsiriwa “Msaidizi” katika Yohana 14:16 ni Paraclete.[3] Neno hili linarejea kwa “wakili anayemtetea mtu mwingine kwenye shauri.” Linarejea kwa “Msaidizi” au “Mfariji anayetoa huduma yake ya faraja wakati wa matatizo.”

Yesu alisema kwamba, “Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele.” Hii inaonyesha kwamba huduma ya Roho Mtakatifu itafanana na ile huduma ya Yesu. Roho Mtakatifu hakuja kama “nguvu” ya mtu binafsi lakini kama nafsi hai, sawa na vile Yesu alivyokuwa nafsi hai.

Paraclete ni “Roho Mtakatifu wa kweli” ambaye “anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.” Yeye “atawafundisha mambo yote ambayo niliwaambia ninyi.” Huduma yake itakuwa na nguvu sana kiasi cha Yesu kutangaza kwamba, “yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu” (Yohana 16:7).

Itakuwaje kwa faida ya wanafunzi kama Yesu ataondoka? Robert Coleman anafafanua:

Wakati wanafunzi wake walipokuwa naye katika hali ya mwili wa kawaida, waliona umuhimu mdogo sana wa kumtegemea Roho Mtakatifu, kwa sababu hiyo walikuwa hawajawahi kujua kwa undani ukweli unaohusiana na maisha yake. Alipokuwa hayupo, hata hivyo, hawakuwa na msaada unaoonekana. Ili waweze kuendelea kuwepo, walipaswa wajifunze siri ya mahusiano yake ya ndani na Baba. Nje ya umuhimu wao, watapata uzoefu wa ushirika mkuu na Kristo kulikoni hata walivyokuwa wamejua kabla ya hapo.[4]

Maisha katika Mzabibu

► Soma Yohana 15:1-16:37.

Yesu aliendelea na moja ya sura zake zenye nguvu sana. “Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima.” Agano la Kale limekuwa likiirejea mara nyingi Israelini kama mzabibu.[5] Hata hivyo, kwa sababu ya dhambi yake, Israeli kamwe haikutimiza kusudi la Mungu la uzuri wa mzabibu alioupanda. Badala yake, jinsi Israeli ilvyofanikiwa kwa mali nyingi, alijenga madhdbahu kwa miungu ya uongo (Hosea 10:2). Badala ya kuzaa matunda ambayo yangekuwa ni baraka kwa ulimwengu, Israeli akazaa “mzabibu mwitu.”[6] Israeli ilfanya maovu mengi kiasi kwamba Mungu hangeweza kufanya lolote na huu mzabibu isipokuwa kuchoma kuni kwa ajili ya mafuta (Ezekieli 15:1-6).

Yesu alikuja kama mzabibu wa kweli.” Alikuja kutimiza kile ambacho taifa la Israeli lilishindwa kufanya; alikuja kukamilisha wito wa Israeli wa kufanyika baraka kwa ulimwengu wote.

Yesu aliwaambia wanafunzi wake kwamba yeye alikuwa ni mzabibu, na wao ni matawi. Ujumbe wa Yesu ulikuwa wazi: Matunda hutegemea kabisa nia yetu ya “kukaa ndani yake.”

Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.

Mbali na mzabibu, wanafunzi hawangeweza kufanya jambo lolote; mbali na mzabibu, sisi hatuwezi kufanya jambo lolote katika wakati wa leo. Tunapojaribu kufanya huduma kwa nguvu zetu wenyewe, tunajitafutia kuchanganyikiwa na kukosa nguvu kabisa. Kwa nini? Kwa sababu kamwe hatujakusudiwa kuzaa matunda tukiwa sisi wenyewe.

Maisha yetu ya kiroho yenyewe yanapatikana kutokana na mahusiano yetu na mzabibu. Mtu yeyote asipokaa ndani ya mzabibu, “hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea.” Wakati aya hii ni onyo, lakini pia ni faraja kubwa. Mbali na mzabibu, hatufai wala hatuna thamani. Lakini kama tutaendelea kukaa ndani ya mzabibu, tunayo maisha na uzao wa matunda tele. Maisha yetu ya kiroho hayategemei nguvu zetu wenyewe; tunaishi ndani ya “mzabibu.”

Dhamira hii inaonekana tena katika Waebrania. Kuhani wetu mkuu, Yesu, “yu hai sikuzote ili awaombee” wale “wamjiao Mungu kwa yeye” (Waebrania 7:25). Howard Hendricks aliwafariji wachungaji wanaojitahidi na ambao wanajisikia kama walioachwa: “Kama huna mtu yeyote anayekuombea, usisahau kwamba Kristo anakuombea.” Yeye ni mwombezi wetu; yeye ni chanzo cha maisha yetu ya kiroho.

Yesu aliwakumbusha wanafunzi kwamba ni lazima wakae ndani ya mzabibu. Hiyo ni kweli hata sasa. Kama wachungaji na viongozi wa makanisa, hufanyi huduma kwa nguvu zako mwenyewe. Unaishi ndani ya nguvu ya msalaba na ndani ya Kuhani mkuu ambaye anakuombea wakati unapojikuta huna nguvu za kujiombea mwenyewe.

Kupitia mihadhara ya wazi yote ya mwisho ya Yesu, aliwafundisha wanafunzi wake tena kwamba ni lazima wapendane. Aliwaandaa katika kukabiliana na machukizo ya ulimwengu huu. Ulimwengu ulimchukia Yesu; ulimwengu huo huo utawachukia wafuasi wa kweli wa Yesu.

Kisha Yesu akafafanua zaidi kuhusu kazi za Roho Mtakatifu. Mwanzoni mwa mihadhara yake, alishaahidi kumtuma Roho. Sasa anawafundisha zaidi kuhusu kazi za Roho Mtakatifu. Roho atauhukumu ulimwengu; atawaongoza wanafunzi awatie katika kweli yote; atamtukuza Mwana.

Yesu pia aliwafafanulia kuhusu kuondoka kwake katika “kitambo kidogo kijacho.” Akazungumza nao tena kuhusu amani kuwa matatani. Mapema katika mhadhara huu, Yesu aliagiza, “Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi” (Yohana 14:1). Aliufunga mhadhara pamoja na kuwapa maneno ya kuwatia moyo: “Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu” (Yohana 16:33).

Kumbuka kwamba katika matukio yote kwa pamoja, matumaini yetu yako ndani ya Kristo peke yake. Hatupaswi kufadhaika kama pia tunaamini “ndani yake.” Ni lazima “tuwe na moyo mkuu” kwa sababu anasema “mimi nimeushinda ulimwengu.” Maisha ndani ya mzabibu ni maisha yenye amani ya uhakika. Matumaini yetu hayategemei hali za kidunia; matumaini yanamtegemea Kristo na ushindi wake dhidi ya dunia.


[1]Mwanzo 49; Kumbukumbu la Torati 32-33; Yoshua 23-24; 1 Mambo ya Nyakati 28-29
[2]Darrell L. Bock, Jesus According to Scripture (Grand Rapids: Baker Book House, 2002), 498
[3]Msaidizi, English Standard Version; Mfariji, King James Version; Wakili, New International Version
[4]Robert Coleman, The Mind of the Master (Colorado Springs: WaterBrook Press, 2000), 29
[5]Zaburi 80:8-9; Isaya 5:1-7; 27:2-6; Hosea 10:1-2
[6]Isaya 5:2. “Mwitu” lina maana sawa na ladha “chungu” badala ya ladha tamu ya mvinyo utokanao na mizabibu iliyostawishwa mashambani

Angalia kwa kuzingatia: Chakua cha Mwisho

Mishnah ni kumbukumbu ya mila za kale za Kiyahudi.[1] Sehemu moja ya Mishnah inaonyesha jinsi Wayahudi walivyoshiriki chakula cha Pasaka. Kwenye Chakula cha Mwisho, Yesu na wanafunzi wake yumkini walifuata mtindo huu ambao bado unaendelea miaka 2,000 baadaye.

Mvinyo wa mzabibu uliochanganywa na maji kwenye kikombe cha kwanza unatolewa utumike. Baraka juu ya kikombe cha mvinyo ni pamoja na ahadi iliyopo katika kitabu cha Kutoka “Nami nitawatoa ninyi mtoke.”

Mvinyo wa mzabibu umechanganywa na maji kwenye kikombe cha pili, lakini bado haujatolewa utumike. Kijana mdogo anauliza, “Kwa nini usiku huu ni tofauti na usiku nyingine zote?’ Baba anamjibu akitumia maelezo ya ukombozi wa Israeli kutoka Misri.

Baada ya maelezo hayo, familia inaimba Haleluya ya kwanza ya Pasaka, Zaburi 113-114. Kisha wanakunywa kikombe cha pili pamoja na ahadi hii: “Nami nitawaokoa na utumwa wao.”

Baada ya Baraka, chakula kinagawanywa kitumike. Chakula kimechanganywa pamoja na mimea michungu, mikate isiyotiwa chachu, kondoo, na mchuzi mzito wa matunda ya msimu uliochanganywa na viungo na siki. Baba anaosha mikono yake, humega na kuombea mikate, anachukua kipande cha mkate, anakifungia kwenye mimea michungu, anakichovya kwenye mchuzi mzito kisha anakula. Baada ya hapo anashukuru na kula kipnde cha kondoo. Ndipo kila mwanafamilia naye hula.

Kikombe cha tatu kimebarikiwa na ahadi za Pasaka: “nami nitawakomboa.”

Kikombe cha nne kimebarikiwa na ahadi za Pasaka: “nami nitawatwaeni kuwa taifa langu.”

Kisha familia inaimba Haleluya ya mwisho ya Pasaka, Zaburi 115-118.[2]

Wakati wa chakula cha Pasaka, Wayahudi wanakumbuka jinsi Mungu alivyoikomboa Israeli kutoka utumwani. Zaidi ya hapo, wana mategemeo ya ukamilishwaji kamili wa ahadi za Mungu wakati Masihi atakapowakomboa kutoka kwenye utumwa kwa mara nyingine na ya mwisho kabisa.

Siku moja baada ya Pasaka, Yesu alikufa kama kondoo wa Pasaka kamili. Juu ya msalaba, ahadi ya ukombozi ilikamilishwa.


[1]Unaweza kuangalia video kuhusu chakula cha Pasaka ya Masihi ya Kiyahudi kutoka https://www.youtube.com/watch?v=bVolBDlWloQ, iliyopatikana mwezi Marchi 22, 2021. Unaweza kusoma zaidi kutoka http://www.crivoice.org/haggadah.html, iliyopatikana mwezi Marchi 22, 2021
[2]Hii ni Zaburi ya mwisho ambayo Yesu aliimba pamoja na wanafunzi wake kabla ya kwenda (Mathayo 26:30)

Maombi ya Kuhani Mkuu

► Soma Yohana 17.

Maombi ya mwisho ya Yesu yaliyonukuliwa akiwa na wanafunzi wake ni muhimu sana katika kuelewa urithi wake kwa wanafunzi na kanisa la leo. Maombi haya yanaitwa “Patakatifu pa Patakatifu pa maombi ya Yesu.” Ni maombi yake ya ndani sana.

Yesu alijiombea mwenyewe (Yohana 17:1-5)

Yesu aliomba akasema Baba, “Mtukuze Mwanao, ili Mwana wako naye akutukuze wewe.” Wakati wanafunzi hawakuelewa maombi haya, baadaye wanakuja kujifunza ukweli wa kushtusha kwamba majibu ya maombi haya yanakuja kujibiwa juu ya masalaba wa Warumi.

Siku ya Jumatatu ya wiki la mateso, Yesu alisema, “Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu.” Yohana akafafanua, “Aliyanena hayo akionyesha ni mauti gani atakayokufa” (Yohana 12:32-33). Yesu alitukuzwa siyo kwa kupitia ushindi, bali kwa njia dhahiri ya kushindwa. Yesu alitukuzwa kupitia msalaba.

Yesu Aliomba kwa ajili ya Wanafunzi wake (Yohana 17:6-19)

Yesu aliombea mambo matatu kwa wanafunzi wake. Aliomba kwamba, Baba, “kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa,” na akaomba tena kwamba “uwalinde na yule mwovu,” na akaomba tena kwamba Baba,“Uwatakase kwa ile kweli.”

Yesu Aliomba kwa ajili ya Waamini wote (Yohana 17:20-26)

Yesu aliomba kwa ajili ya “wale watakaoniamini” baadaye. Aliomba kwamba, “wote wawe na umoja.” Umoja huu ni kwa ajili ya ushuhuda kwa ulimwengu kwamba, “wewe ndiwe uliyenituma.”

Yesu hakuomba kwa ajili ya ulimwengu: “mimi siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa.” Badala yake aliomba kwa ajili ya Wakristo ili ulimwengu upate kusadiki. Kwenye maombi yake ya mwisho kwa ajili ya kanisa, Yesu aliomba kwamba tuweze kuwa mashuhuda kwa ulimwengu kupitia umoja na uaminifu wetu.

Urithi wa Yesu ulikuwa ni kundi la watu walioamini ambao wataenda kukamilisha kusudi lake hapa duniani. Katika Agano la Kale, Israeli ilibarikiwa na Mungu ili iwe ni gari la kupeleka baraka kwa mataifa mengine yote (Mwanzo 12:1-3 ). Katika Agano Jipya, Kanisa lilibarikiwa na Mungu ili liwe ni gari la kupelaka Baraka kwa watu wote. Yesu aliomba kwamba tutatimiza jukumu letu la kuwa Baraka kwa watu wote.

Agizo Kuu la mwisho la Yesu kwa Wanafunzi wake.

► Soma Mathayo 28:16-20; Marko 16:15; Luka 24:44-49; Matendo 1:6-11.

Ushawishi wa wisho wa kiongozi kwa sehemu kubwa unapimwa na uwezo wake wa kushirikisha maoni yake kwa watu wengine. Siku hizi tunasema ni “kutoa maono.” Yesu anatoa mfumo wa kutoa maono katika njia ambayo itawahamasisha wafuasi waliojidhili kabisa. Kwa sababu ya maono yake, wanafunzi walijitolea maisha yao kusambaza injili ya ufalme wa Mungu katika Dola yote ya Kirumi.

Vitabu vya Injili vinashirikisha matamko matatu ya agizo kuu la Yesu. Kila tamko linalenga katika kipengele tofauti cha agizo kuu. Mathayo anasisitiza kuhusu mamlaka ambayo ni muhimu kwa ajili ya agizo kuu hilo. Marko anabainisha agizo kuu linakotakiwa lifike: “kwa kila kiumbe.” Luka anatoa kwa muhtasari maudhui ya ujumbe ambao mitume wanapaswa kuhubiri.

Tamko kamili lililokamilika la agizo kuu la Yesu la mwisho liko katika Mathayo 28:18-20.

Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.

Amri kuu ya msingi iliyoko katika hili agizo kuu ni “mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi.” Ili kukamilisha amri hii kunatuhitaji sisi tuende, tubatize waamini wapya na kuwafundisha waamini wachanga. Shughuli hizi ndizo zinazounganisha amri kuu ya, “mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi.” Uinjilisti, kazi za kijamii, elimu, na vipengele vyote katika huduma vinaongozwa na hii amri kuu: tumepewa agizo kuu la kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi.

Kusudi la kufanya Huduma ya Kichungaji

Ed Markquart, mchungaji wa Kimarekani, alikula chakula cha jioni na mchungaji Richard Wurmbrand kutoka Romania ambaye alikuwa amefungwa miaka mingi katika gereza la kikomunisti. Wakati wa chakula hicho cha jioni, Wurmbrand akamgeukia mfuasi mmoja wa kanisa la Markquart na kumwuliza, “Je, mchungaji wako ni mzuri?” Yule mfuasi alijibu, “Ndiyo.”

Wurmbrand akauliza, “Kwa nini unaona ni mchungaji mzuri?” Yule mfuasi akajibu, “Kwa sababu anahutubu mahubiri mazuri.”

Kisha Wurmbrand akamwuliza tena, “Lakini huwafanya watu kuwa wanafunzi?” Mchungaji Markquart akasema swali hilo limebadilisha kabisa mwelekeo wa huduma yake yote. Akasema, “

Kusudi la Mungu kwa kwa wachungaji wote ni kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi wa Yesu Kristo. Watu wanaompenda Yesu Kristo, wanaomfuata Yesu Kristo, wanaomwita Yesu Kristo Bwana wao. Hiki ndicho tulichoitiwa kukifanya: kufanya wanafunzi kwa ajili ya Yesu Kristo. Siyo kuwafanya watu wawe wafuasi wa kanisa. Siyo kutengeneza shule za Jumapili. Siyo kujenga majengo. Tunapaswa kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi wa Yesu Kristo. Hilo tu ndilo linalohitajika.

Angalia kwa kuzingatia: Kazi Maalumu ya Yesu

Matukio ya wiki ya mwisho ya huduma ya Yesu yanaonyesha kazi yake maalumu ya kuanzisha ufalme unaohuzsisha mataifa yote, rangi zote, na watu wa aina zote. Sehemu za matukio ya wiki ya mwisho ya huduma ya Yesu zinaonyesha kazi yake maalumu kwa mataifa yote.

  • Yesu aliingia kwenye jiji kwa kupanda punda. Mathayo na Yohana walinukuu unabii wa Zakaria, “Tazama, mfalme wako anakuja kwako; Ni mnyenyekevu, amepanda punda.” Zakaria alielezea utawala wa huyu mfalme. “atawahubiri mataifa yote habari za amani; na mamlaka yake yatakuwa toka bahari hata bahari” (Mathayo 21:5; Zakaria 9:9-10; Msisitizo umeongezwa).

  • Alipousafisha uwanja uliokuwa mahali pa kuabudia kwa Mataifa, Yesu alimnukuu Isaya akasema, “Je! Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote?” (Marko 11:17, Ikinukuu Isaya 56:7; Msisitizo umeongezwa). Viongozi wa kidini wa Kiyahudi walikuwa wamegeuza uwanja ambao watu wa Mataifa walikuwa wakiabudia kuwa eneo la soko kwa ajili ya kubadilishana fedha na kuuza njiwa.

  • Wakati wanafunzi walipomshutumu Mariamu kwa “kutumia” marhamu ya gharama kubwa, Yesu aliwajibu: “Amin, nawaambia, Kila ihubiriwapo Injili katika ulimwengu wote, na hili alilotenda huyu litatajwa kwa kumbukumbu lake” (Marko 14:9; Msisitizo umeongezwa).

  • Kwenye hotuba ya Oliveti, Yesu alitoa unabii wa siku ambayo “Habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja” (Mathayo 24:14; Msisitizo umeongezwa). Kwa hawa wanafunzi wa Kiyahudi ambao walikuwa wanafikiri kwamba ufalme ulikuwa ni kwa ajili ya watu waliochaguliwa peke yao, Yesu alisema kwamba habari njema za ufalme zitahubiriwa duniani kote.

Manabii wa Agano la Kale walishaonyesha kwamba Masihi atakuja kwa ajili ya mataifa yote. Katika wiki ya mwisho ya huduma yake, Yesu alifundisha wanafunzi wake kwamba ufalme wa Mungu utahusisha watu kutoka mataifa yote. Ahadi za manabii zilikuwa zikamilishwe kupitia kanisa.

Urithi wa Yesu: Kanisa katika Matendo

Vitabu vingi kuhusiana na maisha ya Yesu vinamalizikia kwenye kupaa kwake. Hata hivyo, Kupaa kwake hakukuwa mwisho wa huduma ya Yesu duniani. Huduma ya Yesu haikuwa tu kuuendea msalaba au kuiacha kaburi wazi; huduma yake iliendelea hata wakati wa Pentekoste. Yesu alitoa ahadi kwamba “atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele” (Yohana 14:16). Ahadi hii ilitimizwa kwenye Matondo. Sehemu mbili za matukio katika Matendo zinaonyesha ukamilishwaji wa urithi wa Yesu.

Kanisa Wakati wa Pentekoste

► Soma Matendo 1:4-11 na 2:1-41.

Kitambo kidogo kabla Yesu hajapaishwa, wanafunzi walimwuliza, “Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme?” Walikuwa wanategemea Yesu aanzishe ufalme wa kisiasa wa duniani. Kwa akili zao, kufufuka kwake kuliimarisha matumaini yao ya kuwepo ufalme wa kidunia. Alichohitaji tu Yesu kukifanya, walivyofikiria, ni kutumia uwezo wake kuwapindua Warumi. Yesu akawajibu,

Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.

Yesu anamaanisha “Nyakati na majira ya ufalme siyo jukumu letu.” Badala yake, nilazima ukamilishe kazi maalumu niliyawapeni.: tumikeni kama mashahidi wangu hadi miisho yanchi. Lakni kabla hamjaenda, ni lazima mngojee. Katika Luka, Yesu alisema, “lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu” (Luka 24:49).

Siku hamsini baada ya Pasaka, wanafunzi wapatao 120 walikuwa wamekusanyika kwenye chumba cha juu, ambako ndiko ahadi ya Roho Mtakatifu ilipokamilishwa. Walianza kuzungumza kwa lugha za watu mbalimbali waliokuwa wamekusanyika kutoka kila taifa kwa ajili ya Sikukuu ya Kiyahudi ya Pentekoste.

Hii iliashiria kukamilika kwa mpango wa Kristo wa kuanzisha kanisa lake kutoka mataifa yote. Orodha ya mataifa iliyoko katika Matendo 2 inatukumbusha sisi orodha ya mataifa iliyoko katika Mwanzo 10. Katika Mwanzo 11, Yesu alihukumu jaribio la mwanadamu la kuanzisha ufalme mmoja wa dunia nzima katika mji wa Babiloni kwa kuwachanganya wasisikilizane katika lugha zao. Katika Matendo 2, Mungu alianza kuujenga ufalme wake kwa kuugeuza ule mkanganyiko uliokuwepo wa kutoelewana lugha.

Pentekoste ulikuwa mwanzo wa “kazi kubwa kuliko hizo” ambazo Yesu aliahidi (Yohana 14:12). Kwa sababu ya kazi ya Roho Mtakatifu, watu wengi waliamini kuliko wakati wa huduma ya Yesu hapa duniani. Utimilifu wa urithi wa Yesu umeanza. Roho Mtakatifu aliyeahidiwa sasa anafanya kazi kupitia hudumaza mitume. Kuanzia wakati huu, kanisa litaanza kukamilisha kusudi kuu la Mungu la kuanzisha ufalme wake. Kama mahubiri ya Petro yalivyojifafanua kwa uwazi, ahadi za Agano la Kale sasa zinakamilishwa kupitia kanisa.

John Stott alielezea vipengele vinne vinavyohusiana na siku ya Pentekoste.[1]

  • Siku ya Pentekoste ilikuwa ndiyo ya kitendo cha mwisho cha Yesu kuhudumu katika ulimwengu.

  • Siku ya Pentekoste iliwapa mitume uwezo kwa ajili ya kutekeleza Agizo Kuu.

  • Siku ya Pentekoste ilizindua enzi mpya ya Roho Mtakatifu. Kwenye Agano la Kale lote, Roho Mtakatifu aliwawezesha watumishi wa Mungu katika nyakati maalumu tu za huduma. Baada ya Pentekoste, Wakristo kwa nyakati zote na katika maeneo yeyote wanafaidika kutokana na huduma yake.

  • Huduma ya uamsho ya kwanza ya Wakristo ilianza wakati wa Pentekoste.

Matokeo ya Pentekoste yanaonekana katika kitabu chote cha Matendo. Ishara zilizotokea wakati wa Pentekoste zilikuwa “ni maalumu na za kipekee.” Furaha, ushirika wa waumini, uhuru wa kuabudu, ujasiri wa kushuhudia, na nguvu ya huduma viliweza kuwa ni ushahidi wa “kawaida” wa huduma katika uweza wa Roho Mtakatifu.

Maisha ya kila siku katika Kanisa la Mwanzo

► Soma Matendo 2:42-47.

Sehemu ya pili ya tukio la ukamilishwaji wa urithi wa Yesu liko mwishoni mwa matendo 2. Sehemu hii inaonyesha maisha ya kila siku ya kanisa la mwanzo.

Katika maombi yake ya Kuhani Mkuu, Yesu aliomba umoja kwa ajili ya wafuasi wake. Aliomba kwamba, “wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja” (Yohana 17:22). Jibu kwa ajili ya ombi hili linaanziakatika Matendo 2. Wote walioamini “walikuwako wote mahali pamoja”; kwa pamoja walidumu ndani ya hekalu pamoja na kumega mkate nyumba kwa nyumba”; Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa.”

Katika Matendo, neno “pamoja” linawakilisha umoja wakanisa la mwanzo. Licha ya matatizo ya kuanzisha kanisa moja la Wayahudi na watu wa Mataifa, mateso kutoka kwa viongoziwa Kiyahudi, na migogoro binafsi miongoni mwa mitume, kanisa liliendelea kubakia kuwa moja. Kinyume na magumu yote, maombi ya Yesu kwamba, “waweze kuwa wamoja” yalitimilizwa.

► Je, picha ya kanisa katika Matendo 2:42-47 inafanana na iliyopo kwenye kanisa lako? Je,unahudumu katika uweza wa Roho Mtakatifu? Kama sivyo, kuna vizuizi gani vinazuia kazi ya Roho Mtakatifu ndani na katika huduma yako yote? Je, ni ukosefu wa utii? Je, ni ukosefu wa maombi? Je, ni ukosefu wa imani? Je, ni ukosefu wa umoja? Je, unawezaje ukaona mmiminiko mpya wa Roho Mtakatifu katika huduma yako?


[1]John W. Stott, The Message of Acts (Westmont, Illinois: InterVarsity Press, 1990), 60-61

Matumizi: Kuacha Urithi

Katika kuandaa sehemu hii, niliwafanyia usaili viongozi mbalimbali wastaafu wa huduma.[1] Niliwahoji kuhusu urithi wao, maandalizi yao ya kustaafu uongozi, na masomo ya kuwavusha. Sehemu hii inategemezwa na majibu kutoka kwao.

(1) Viongozi wanaoacha urithi hupanga mpango ya baadaye.

Fikiria unamwuliza mtu anayejenga, “Je, unajenga nini?” Utashangaa kama huyu mjenzi atakujibu, “Sijajua bado. Nategemea kuona kitakachotokea.”

Kabla hajaanza kujenga, mjenzi huwa na mipango ya matokeo ya mwisho ya ujenzi anaoufanya. Viongozi wanaoacha urithi wanajua wanachotaka kuacha baada ya wao kuondoka.

Viongozi wanaomaliza vizuri wanajua urithi wanaotaka kuacha baada ya wao kuondoka. Hawaendelezi huduma zao kama vipofu. Viongozi hawa waliamini kwamba, “Hili ndilo kusudi Mungu aliloniitia mimi kukamilisha kama sehemu yangu ya huduma.”

Urithi wa Yesu ulikuwa ni kundi la wanafunzi ambao walitayarishwa kwa ajili ya kuliongoza kanisa. Tangu mwanzo wa huduma yake, alitoa mudawa kutosha na nguvu zake katika kuwaandaa hwa watu kama urithi wake.

[2]Kama unataka kuacha urithi, ni lazima uwe na mipango ya baadaye. Kwa masikitiko, watu wengi wanajenga maisha yao pasipokuwepo na umakini katika malengo. Kama utawauliza wakiwa katika umri wa miaka 30, 50 au hata 70 kwamba, “Unajenga nini na maisha yako?” Jibu litakuwa, “Sijui. Nangojea nione kitakachotokea.”

(2) Viongozi wanaoacha urithi hujiandaa kikamilifu kwa kipndi cha mpito

Fikiria kumtembelea fundi ujenzi anayekaribia kumalizia ujenzi wa mradi mkubwa wa ujenzi. Kuta zimekamilika; paa limekamilika; liko tayari kuanza kutumika. Uliza, “Ni hatua gani zimebakia kabla jengo halijakamilika kabisa?”

Utashikwa na mshangao kama atajibu, “Sijui! Sina muda wa kufikiria kuhusu hatua za mwisho.” Hapana! Fundi ujenzi anaacha kitu ambacho kitaendelea kudumu na kuwepo hata baada ya yeye mwenyewe akiwa hayupo hai tena. Anapanga kwa uangalifu kila hatua. Anaweza akakuambia, “Hii ni siku ambayo tutakamilisha ujenzi. Hii ni siku ambayo mwenye jengo anaweza kuingia kukaa.” Kila kitu kimepangwa kwa ajili ya mpito.

Viongozi wanaoacha urithi hujiandaa kikamilifu kwa ajili ya kipindi cha mpito. Inapowezekana, wanapanga mapema kuhusu kustaafu kwao, kutoa nafasi kwa shirika kuchagua atakayekuwa badala yake, na hawa wapya kujiandaa kwa ajili ya majukumu mapya. Katika baadhi ya matukio, viongozi wanaoingia na wanaoondoka wanakuwa na kipindi cha “kufanya pamoja” ambacho kiongozi mpya anaanza kufanya maamuzi wakati kiongozi aliyekuwepo anayeondoka anakuwepo kwa ajili tu ya kutoa usia na ushauri.

Viongozi wanaoacha urithi huiandaa huduma wanayoiongoza kwa ajili ya kipindi cha mpito. Viongozi wanaoondoka wenye ufanisi wanawasilisha kujiamini katika utoaji wa Mungu kwa ajili ya baadaye. Wanawaanda watu kufanya kazi vizuri chini ya kiongozi wao mpya anayefuata. Wanahakikisha kwamba watu katika shirika wanajisikia kuwa salama kwenye kipindi cha mpito. Kiongozi mmoja aliandika, “Lengo langu lilikuwa ni kufanya mabadiliko yaliyotulia kiasi kwamba hata wafanyakazi hawangetambua kuondoka kwangu.”

(3) Viongozi wanaoacha urithi wanajua ni lini wataondoka.

Viongozi ni lazima wawe na hiari ya kubadilishana majukumu na viongozi wanaoondoka na “waondoke bila ya kuwepo na majuto.” Viongozi wa zamani wanatakiwa waweze kupatikana kwa ajili ya kutoa usia, lakini iwe ni pale tu anapoombwa na mrithi wake.

Katika kozi hii, tumeonajinsi Yesu alivyowaandaa wanafunzi wake kuchukua nafasi za kuongoza makanisa. Mapema, aliwapa mafunzo kwa uangalifu. Baadaye, aliwatuma nje kwenda kufanya huduma na baadaye kurejea kwa ajili ya kufanyiwa tathmini. Kwenye Chakula cha Mwisho cha Pasaka, aliwapa maelekezo ya mwisho kwa ajili ya huduma. Muda mfupi kabla ya kupaa, aliwapa ukumbusho wa mwisho kuhusiana na agizo kuu. Yesu aliwaandaa kwa uangalifu kwa ajili ya kipindi cha mpito.

Kwa masikitiko, viongozi wengi wa Kikristo hutumia muda mfupi kwa ajili ya kipindi cha mpito. Wanachukulia kwamba, “Nitafanya kazi yangu hadi nitakapopewa mtu wa kunibadilisha. Baada ya hapo, itakuwa tatizo lamtu mwingine.“ Bila shaka, kuna nyakati ambazo kunatokea dharura za maradhi, vifo, au mabadiliko makubwa ya huduma jambo ambalo hufanya maandalizi ya kipindi cha mpito kuwa finyu. Lakini kila inapowezekana, tunapaswa tupange kwa uangalifu kipindi cha mpito kwa ajili ya kiongozi mpya anayekuja. Hii ni moja ya hatua muhimu sana katika kuhifadhi urithi kwa ajili ya baadaye.


[1]Usaili kwa ajili ya sehemu hii ulihusisha viongozi wafuatao:
+ Dr. Michael Avery, raisi wa zamani katika God’s Bible School and College, Cincinnati, OH
+ Rev. Paul Pierpoint, mchungaji wa zamani katika Hobe Sound Bible Church na raisi wa FEA Missions, Hobe Sound, FL
+ Rev. Leonard Sankey, mchungaji mstaafu na kiongozi wa mashirika ya huduma mchanganyiko za kimisheni
+ Dr. Sidney Grant, raisi wa zamani wa huduma za umisheni za FEA, Hobe Sound, FL
[2]

“ Unauandaa urithi wako kila siku, na siyo pale kwenye mwisho wa maisha yako.”

- Alan Weiss

Kazi za kufanya Somo la 9

Andika insha ya kurasa 3-5 kwa ajili ya kujibu maswali matatu yafuatayo:

(1) Fikiria kuhusu kiongozi mmoja wa huduma ambaye ameacha urithi ambao ulishawishi maisha yako ya Ukristo na huduma. Katika ukurasa mmoja, toa kwa muhtasari ushawishi wao kwenye maisha yako. Jibu maswali mawili yafuatayo.

  • Ushawishi wao ulikuwa ni nini kwenye maisha yako?

  • Walifanya kitu gani au walisema nini hata vikafanya kuwepo na matokeo muhimu kama hayo?

(2) Unataka kuacha urithi gani kwa wanaobakia wakati utakapofariki? Kuwa makini kwenye majibu yako. Jibu kwenye kurasa 1-2.

  • Unataka uache urithi gani kwa familia yako?

  • Unataka uache urithi gani kwa jamii yako?

  • Unataka uache urithi gani kwa huduma yako?

(3) Kwa kila kipengele katika vipengele vitatu vya jibu la 2, tambulisha mambo maalumu utakayopaswa kufuata sasa ili uweze kuacha urithi unaotaka uuache. Jibu kwenye kurasa 1-2.

Ihifadhi karatasi hii na kila wiki ifanyie marejeo kwa kipindi cha miezi sita ijayo kwa mfululizo. Itumie katika kuanza kupanga urithi wako kwa kizazi kijacho