Upendo unaomfanania Kristo ni hamasa kwa huduma inayomfanania Kristo.
Utangulizi
Maisha yote ya Yesu na huduma yake vilihamasishwa na upendo. Mara kwa mara alionyesha kwamba upendo kwa Mungu na upendo kwa watu wengine vilikuwa katika kina cha ndani cha maisha na huduma yake. Kama tutafuatilia mfano wa Yesu, upendo ni lazima uwe katika kina cha ndani cha maisha yetu na huduma. Hakuna mahali palipowekwa wazi kuhusu hili zaidi ya kwenye mfano wa Msamaria Mwema.
► Soma Luka 10:25-37.
Kabla tu ya kutoa mfano huu, Yesu alikuwa ameshasema kwamba “mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga” (Luka 10:21). Hii inafundisha somo la msingi kuhusu uelewa wa mambo ya kiroho. Kuelewa ukweli wa kiroho kunahitaji jambo lililo zaidi ya utafiti wa akili; kunahitaji ufunuo wa kiroho.Ukweli wa Mngu ni rahisi mno kiasi cha mtoto kuelewa, lakini ni zitosana kwa mwanazuoni.
Hii inatokeaje? Je, Mungu huficha ukweli kwa wale wanaouhitaji? Jibu linahusisha kanuni mbili.
1. Ukweli wa kiroho unafunuliwa tu kupitia Roho mtakatifu. Paulo aliandika kwamba “mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu.” Kwa sababu hiyo, ni lazima tufundishwe na Roho, tukiyafasiri mambo ya kweli ya rohoni kwa maneno ya rohoni kwa watu ambao ni wa kiroho” (1 Wakorintho 2:11, 13).
2. Ukweli wa Kiroho hufunuliwa tu kwa wasikilizaji walio tayari kupokea. Paulo aliendelea kuandika, “Mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni” (1 Wakorintho 2:14).
Mfano wa mpanzi unaonyesha kwamba mtazamo wa msikilizaji unategemea na matunda yatokanayo na hiyo mbegu (Mathayo 13:1-23).[1] Ni wale tu walio tayari kupokea ukweli watakaoweza kuelewa ukweli wanaousikia.
Mwanasheria katika Luka 10:25 ni mfano halisi wa maisha kwenye hii kanuni ya pili. Swalila mwansheria halikutoka kwa mtu mwenye kiu ya kujua ukweli, bali kwenye matamanio ya kumtega Yesu; alitaka “kumweka kwenye jaribu.” Baada ya kusikia jibu la Yesu, jibu la mwanasheria halikuwa jibu la udongo wenye kuzaa matunda. Badala yake, aliuliza tena swali lingine “akitaka kujidai haki.”
Mwanasheria alikuwa tayari ameshapata jibu la swali lake alilouliza, “Nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Jibu lilikuwa limeandikwa kwenye sheria, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako.
Huu ni mfano wa moyowa Yesu kwa ajili yetu. Kuishi na kuhudumu kama Yesu alivyofanya, ni lazima tumpende Mungu, na tumpende jirani yetu kama Yesu alivyopenda. Bila ya kuwa na upendo unaomfanania Kristo, masomo mengine yote katika kozi hii hayatakuwa na maana yeyote. Maombi, uongozi, kufundisha, na kuhubiri – bila kuwa na upendo, hakuna jambo lolote hata moja la ukweli.
Inawezekana hili likaonekana ni rahisi sana. Unaweza ukasema, “Bila shaka, tunapaswa tumpende Mungu na tuwapende watu wengine. Tayari ninalijua hilo! Lakini katika mzigo wa siku hadi siku wa huduma, tunaweza tukapoteza moyo wa upendo. Inawezekana kuhudumia washirika wa kanisa bila kuwapenda. Inawezekana kuhudumia familia zetu bila kuwapenda. Inawezekana kufanya wajibu wa Kikristo bila kumpenda Mungu. Hamasa yetu kwenye huduma ya Kikristo ni lazima pawepo upendo unaomfanania Kristo.
[1]Hasa zaidi angalia katika 13:12. Mtu anayekubali ukweli huupata ukweli zaidi. “Kwa maana ye yote mwenye kitu atapewa.” Mtu anayekataa ukweli ni kipofu hata kwa ule ukweli ambao tayari anao: “lakini ye yote asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa.”
Kumpenda Mungu kama Yesu alivyompenda.
Huduma ya Yesu kwa wanadamu ilihamasishwa na upendo wake kwa Baba. Ili kukwepa kuchoka sana na kuchangayikiwa katika huduma, kuwajibika kwetu kwa watu ni lazima kuwe na msukumo wa upendo wa Mungu. Huduma bila ya upendo kwa Mungu muda si mrefu inakuwa tupu na isiyoweza kuzaa matunda.
Vipengele vitatu vya upendo wa Yesu kwa Baba vitasaidia kuwa mfano kwetu: mahusiano, ufahamu na uaminifu.
Yesu alidumisha Uhusiano wake wa Ndani na Baba yake.
Mara kwa mara, Vitabu vya Injili vinaonyesha uhusiano wa karibu wa Yesu na Baba yake. Hii inaonekana katika:
Tamko la Yesu kwa wazazi wake, “Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu?” (Luka 2:49).
Maombi ya ndani sana ya Yesu katika Yohana 17.
Kilio cha Yesu cha uchungu juu ya msalaba, “Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” (Mathayo 27:46).
Katika Bustani ya Gethsemane, Yesu alimwita Mungu akimwita lugha ya ndani ya kifamilia, “Aba, Baba” (Marko 14:36). Hii ni lugha ya mtoto aliyekuwa salama katika mahusiano na Baba yake.
Maombi ya Kiyahudi ya jadi yalitumia majina mengi ya Mungu: Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo; Mungu wa Baba zetu; Mungu Mbarikiwa; Mungu mmoja Mwenyezi; Mkombozi wa Israeli. Yesu alitumia jina la ndani zaidi la mahusiano Aba. Yesu aliishi katika mahusiano ya ndani na Baba yake.
Kenneth E. Bailey alitumia miaka mingi akifundisha katika Mashariki ya Kati. Anaandika kwamba Aba ni jina la kwanza la mtoto katika nchi za Mashsriki ya Kati. Aba ni jiananalotumia mtoto kwa ajili ya baba yake.
Paulo anatueleza sisi kama watoto wa Mungu kwamba, hata sisi tunayo fursa ya “kulia, ‘Aba! Baba!’” (Warumi 8:15; Wagalatia 4:6). Hatumwabudu Mungu ambaye anakaa mbali. Badala yake, kama Yesu tunaishi kwa usalama na raha ndani ya upendo wa Baba.
Kama wachungaji, tunaweza tukashawishika kujipima wenyewe kwa mafanikio ya huduma zetu. Kama thamani yetu inatoka katika ukubwa wa kanisa, kukubalika kwa kusanyiko letu, au kutambuliwa na wenzetu, tutashawishika kujitoa dhabihu kwa ajili ya uaminifu kwa mafanikio. Tutakuwa tumekatishwa tamaa juhudi zetu zinapokuwa zimeshindwa. Hata hivyo, kama tuna uhakika kwamba Aba wetu anantupenda hata bila ya kujali mafanikio yetu, tunaweza tukayaacha matokeo kwake. Upendo wake hautegemei utendaji wetu.
Yesu aliyajua Mapenzi ya Baba yake.
Mwishoni mwa huduma yake hapa duniani, Yesu alishuhudia, “Nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye” (Yohana 17:4). Yesu alijuani nini baba yake alichomtuma akamilishe na alijitolea maisha yake kwa ajili ya kukamilisha misheni hiyo.
Katika hali ya ubinadamu, Yesu alijifunza mapenzi ya Baba kupitia maombi na kupitia Neno. Kupitia maombi, Yesu aliyapata mapenzi ya Baba.
Yesu pia alijifunza mapenzi ya Baba kupitia Neno. Akiwa Kaperinaumu, Yesu alitoa muhtasari wa umisheni wake kama kukamilishwa kwa unabii za Isaya (Luka 4:18-19). Wakati alipowajibu wajumbe waliokuwa wametumwa kwake na Yohana Mbatizaji, Yesu alitumia maneno ya Yesaya kama ushahidi wa huduma yake ya Kimasihi (Mathayo 11:4-5). Yesu alilijua Neno.
Katika Agano Jipya yote, tunawakuta Wakristo wakirejea kwenye Maandiko kama jawabu kwa matatizo yao. Akiwa anakabiliwa na kifo cha mfia dini, hotuba ya mwisho ya Stefano ilikuwa imesheheni sana Maandiko kutoka katika Agano la Kale na utimilifu wake kwa Yesu Kristo (Matendo 7:1-53). Wakati viongozi wa kidini wa Kiyahudi walipowaamuru waachane kabisa na kuhubiri ujumbe wa Yesu, kanisa lilikutanika pamoja kwa ajili ya maombi. Maombi yao yalikuwa na nukuu ndefu ya Zaburi ya 2 (Matendo 4:24-30; Zaburi 2:1-2). Waamini wa mwanzo waliyajua Maandiko. Ilikuwa ni katika lugha yao ya asili katika kuhubiri na kuomba.
[1]Kupitia historia yote ya kanisa, wahubiri ambao waliweza kuibadilisha dunia ni wale waliokuwa wanaume wa Neno. Martin Luther alishuhudia kwenye kongamano la Chakula cha Minyoo, “Nimefungamanishwa na Maandiko na dhamira yangu ni kuwa mateka wa Neno la Mungu.” John Wesley alijifafanua mwenyewe kama “Mtu wa Kitabu Kimoja.” Charles Spurgeon alisema kwamba wahubiri wanapaswa wajilishe kwa Neno hadi “harufu ya Biblia itoke ndani yako.” Hudson Taylor alitumia muda wake mwingi sana katika Biblia hadi mwandishi mmoja akaandika, “Biblia ni anga ambalo Hudson Taylor aliishi.” Watu hawa waliibadilisha dunia yao kwa sababu walilihubiri Neno kwa mamlaka.
Kama tunapaswa tuhubiri kama Yesu, au kama Wakristo wa mwanzo, au kama wahubiri maarufu katika historia, sisi pia ni lazima tuwe tumefurika Neno la Mungu. Maandiko yalikuwa ndio mamlaka iliyokuwa kuu kwenye huduma ya Paulo (2 Timotheo 3:16-17). Yesu aliomba kwamba wanafunzi wake waweze kutakaswa, na kutengwa, kwa ajili ya huduma. Hili linaenda kukamilishwa kupitia Neno: “Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli” (Yohana 17:17). Neno liliwafanya wanafunzi wakawa wa ufanisi mkubwa katika huduma; Neno linatufanya sisi tuwe na ufanisi katika huduma.
Ajith Fernando ametumia maisha yake kwa ajili ya huduma katika nchi ya Sri Lanka. Anaadika kwamba amefanya mazoea kwamba kamwe hakuna kutoa tamko zito katika mahubiri bila kuwa na msingi wake kutoka katika Maandiko. Hali hii ilimwezesha kuhubiri kwake kuwe kwenye msingi wa Neno. Kama Wakristo, tunamjua Mungu kupitia Neno lake, tunajenga makanisa yenye nguvu kupitia huduma zenye msingi wa Neno la Mungu.
Yesu alimwamini Baba yake
Uhusiano wa Yesu na Baba yake wakati wa huduma yake hapa duniani unaweza kujumuishwa pamoja katika maneno ya maombi yake kwenye Bustani ya Getsemani, “Walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe” (Mathayo 26:39). Hii ni lugha yenye kuonyesha uaminifu wa kutosha na kujikabidhi kabisa.
Ni vigumu sana kujikabidhi kabisa kwenye mapenzi ya mtu ambaye hatumwamini. Tunaweza kwa nje kulazimishwa kumtii, lakini mioyo yetu inapinga kusalimisha uthibiti wetu kwa mtu tusiyemwamini. Yesu alijikabidhi kwenye mapenzi ya Baba kwa sababu alimwamini kabisa Baba yake katika upendo na uzuri wake.
► Soma Yohana 5:1-47.
Huduma yote ya Yesu inaonyesha tabia hii ya kumtegemea Mungu kwa kila kitu. Wakati viongozi wa Kiyahudi walipomwudhi Yesu kwa kumponya mtu aliyekuwa amepooza siku ya Sabato, aliwajibu:
Amin, amin, nawaambia, Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile vile.…Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo; na hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake aliyenipeleka.
Yesu alishajinasibu mapema kwamba yeye ni wa kiungu: “Baba yangu anatenda kazi hata sasa, nami ninatenda kazi.” Lakini ingawaje alikuwa ni wa kiungu kwa ukamilifu wote, Yesu alijikabidhi kwa hiari yake mwenyewe jukumu la chini la misheni ya kidunia. Yeye na Baba wako sawa, lakini alijikabidhi kwenye mapenzi ya Baba.
Wakati waandishi na Mafarisayo walipompinga Yesu miezi michache baadaye, aliweza pia kutetea vitendo vyake kwa kuelekeza maelezo yake kwenye mamlaka ya Baba yake: “sifanyi neno kwa nafsi yangu, ila kama Baba alivyonifundisha ndivyo ninenavyo” (Yohana 8:28). Kwa kuwa alikuwa ameweka tumaini lake lote kwa Baba, Yesu aliweza kujitoa kwa hiari yake mwenyewe kwa ajili ya mapenzi ya Baba.
Uongozi wa kanisa unahitaji uwiano mgumu. Wachungaji wengi na viongozi wa makanisa wana ujuzi wa uongozi wenye nguvu. Kama viongozi, wana maoni mazito na haiba. Hivi vinaweza kuwa ni nguvu yenye thamani sana kwa kiongozi. Hata hivyo, nguvu hii ni lazima iwe na uwiano na kujitoa kwa hiari kwa Mungu. Isipokuwa iwe tumejitoa kwa Mungu kwa uaminifu, tutaweza kulazimisha njia yetu wenyewe badala ya kujitoa kwa ajili ya njia ya Bwana.
Labda mfano bora wa kibiblia ni Musa. Musa alikuwa “Mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi” (Hesabu 12:3). Musa alikuwa na nguvu, lakini pia alikuwa mpole. Alikabiliana na Farao, mtu aliyekuwa na nguvu sana katika Misri. Aliwaongoza watu wa Israeli waliokuwa na usumbufu mkubwa jangwani. Musa alikuwa kiongozi mwenye nguvu. Lakini kwa wakati huo, alikuwa amejitoa kwa ajili ya Mungu. Uongozi wa kanisa ulio na ufanisi unahitaji kwamba tuzitoe nguvu zetu za asili kwa ajili ya Mungu. Hii inawezekana tu tunapokuwa tunatembea na Mungu katika maisha ya imani na uaminifu.
► Katika vipengele hivi vitatu vya upendo kwa ajili ya Baba (mahusiano, ufahamu wa Neno lake, na kujitoa kunakoendana na uaminifu, ni changamoto gani unayokutana nayo wewe binafsi?
"Kamwe usiruhusu vitabu vizuri vikachukua nafasi ya Biblia. Kunywa kutoka kwenye kisima!"
- Amy Carmichael
Angalia kwa kuzingatia: Je, Yesu alijinasibu kuwa ni Mungu?
Dini za uongo kama vile Mormoni na Mashahidi wa Yehova, pamoja na dini myingine zisizo za Kikristo kama vile Uislamu zinakataa kabisa kwamba Yesu alikuwa Mungu wa kweli. Wanamtambua Yesu kama mwalimu wa kiwango cha juu, au mtume, kama kiumbe wa kwanza kuumbwa, na kama Masihi. Lakini wanakataa kabisa kwamba alikuwa Mungu wa kweli.[1]
Wafuasi wa dini hizi maramaranyingi hudai kwamba, “Yesu kamwe hakuwahi kudai kwamba yeye ni Mungu. Alisema yeye alikuwa ni mwana wa Mungu katika njia ile ile ambayo kila mmoja wetu ni wana wa Mungu.”
Je, Yesu alidai kwamba yeye ni Mungu? Ndiyo. Watu waliomsikia Yesu walielewa madai yake. Wakati Yesu aliporejea Mungu kama “Baba yangu,” Wayahudi walijaribu kumwuwa. Kwanini? “Kwa sababu hiyo Wayahudi walizidi kutaka kumwua, kwa kuwa hakuivunja sabato tu, bali pamoja na hayo alimwita Mungu Baba yake, akijifanya sawa na Mungu” (Yohana 5:18).
Katika moja ya madai ya Yesu ya wazi kabisa ya kuwa Mungu, aliwaambia viongozi wa Kiyahudi, “Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko” (Yohana 8:58). Haya ni maneno ambayo Mungu aliyatumia kujidhirisha mwenyewe kwa Musa kwenye kichaka kilichokuwa kinawaka moto: “Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli; MIMI NIKO amenituma kwenu” (Kutoka 3:14). Kwa maneno haya, Yesu alikuwa anajinasibu kwamba alikuwa ni Mungu ambaye alimtokea Musa. Viongozi wa Kiyahudi walijua wazi kwamba Yesu huwa anamaanisha katika maneno yake. Kwa kujibu, ‘walichukua mawe” wakitaka kumwua. Hii ndiyo ilikuwa adhabu sahihi kwa mtu yeyote anayekufuru – kutoa madai ya uongo ya kuwa Mungu (Mambo ya Walawi 24:16).
Kwenye kesi ya Yesu, Kayafa aliuliza, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wake Mtukufu?” Jibu la yesu lilikuwa la uhakika, “Mimi ndiye, nanyi mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija na mawingu ya mbinguni.” Kwa jibu hili, Yesu alijinasibu kuwa mmoja anayeketi mkono wa kuume wa Mungu na Mwana wa Adamu aliyetabiriwa na Danieli ambaye atakuja kuuhukumu ulimwengu (Zaburi 110:1 na Danieli 7:13-14). Kayafa alijua kwamba Yesu alikuwa anajinasibu kwamba yeye ni Mungu. Akararua nguo zake akasema, “Mmesikia kufuru yake” (Marko 14:61-64).
Unaweza kukataa kuyaamini madai ya Yesu, lakini huwezi ukawa unasoma kwa uangalifu katika Vitabu vya Injili bila ya kukiri kwamba Yesu mwenyewe alijinasibu kuwa Mwana wa Mungu. Wasikilizaji wake waliyasikia madai yake na walilazimika aidha kumkubali yeye kama Mungu au kumwua kama nabii wa uongo na mwenye kukufuru.
[1]Ili kujifunza mafundisho kuhusiana na dini za uongo, tafadhali soma kozi ya Shepherds Global Classroom, Dini za Ulimwengu na Ibada
Kuwapenda jirani zetu kama Yesu alivyopenda
Yesu alipokuwa anafundisha, mara nyingi alivuta umati wa “watoza ushuru na wenye dhambi.” Siyo kwamba Yesu aliwafundisha hawa watu tu, bali alikula pamoja nao. Wakati Mafarisayo walipomwona Yesu kwa hiari yake akila pamoja na wenye dhambi, walianza kumshutumu.Yesu aliwajibu kwa hadirhi tatu. Utakapokuwa umezisoma hadithi hizi, utagundua sehemu mbili muhimu za historia ya nyuma.
1. Wakati wa siku za Yesu, kula kwa pamoja na mtu mwingine kulimaanisha unataka kuanzisha mahusiano.[1] Wakati Yesu alipokula na wenye dhambi, alimaanisha kwamba kwa makusudi anaunganishwa nao. Yesu alionyesha kwamba Mungu hangojei watu waende kwake, badala yake, Mungu huwatafuta kwa bidii sana wale waliopotea.
2. Wayahudi wa wakati wa Yesu walitegemea mtu mwenye haki kujizuia kukutana na watu wenye dhambi. Rabi wa Kiyahudi walifundisha kwamba wakati Masihi atakapokuja, ataepukana na mchanganyiko wowote wa watu wenye dhambi na atakula tu na wenye haki.
► Soma Luka 15:1-32.
Huu ni mfanommoja mkubwa katika sehemu tatu: kondoo aliyepotea, shilingi iliyopota, na mtoto mpotevu. Katika kila kipengele, msingi wa mfano ni furaha ya mtu aliyepata tena kile ambacho kilikuwa kimepotea. Yesu anaonyesha furaha ya mbinguni wakati wenye dhambi wanaporejeshwa kutubu.
[2]Rabi wa Kiyahudi walikuwa na methali yao iliyozoeleka: Kuna furaha mbinguni wakati mwenye dhambi mmoja anapoharibiwa mbele za Mungu.” Yesu akabadilisha huu msemo kuwa kinyume chake, ‘Kuna furaha mbinguni wakatimwenye dhambi mmoja anapotubu.” Kulikuwa na tofauti gani kati ya Yesu na hawa Rabi wengine? Upendo. Yesu alionyesha kile kilichomaanisha kuhudumu kutoka ndani ya moyo wa upendo.
Tunapohudumu bila upendo hadhi na nafasi zetu huwa ni muhimu zaidi kuliko watu. Hata hivyo, tunapohudumu kutoka katika moyo wenye upendo, tuko tayari kuweka kando hadhi zetu kwa ajiliya wanaopotea. Yesu alikuwa tayari kuteswa kutokana na shutuma za viongozi wa dini kwa ajili ya kuonyesha upendo kwa wale ambao walihitaji upendo sana.
► Kama tutauliza, “Utaonyesha upendo kwa Mtoto Mpotevu?’ Sisi wote tutajibu, “Ndio.” Tunajua jibu sahihi. Badala yake, uliza, “Ni nani mpotevu ambaye mara ya mwisho nilikutana naye? Ni kwa jinsi gani nilionyesha upendokwa mtu huyo?
Yesu alionyesha Upendo kupitia Huruma yake kwa Waliojeruhiwa
Wakati wa kusoma Vitabu vya Injili, je, umeshagundua kwamba wenye dhambi waliokimbia kutoka kwa viongozi wa dini walikimbia kuja kwa Yesu? Ni nini kilichowafanya wenye dhambi kutafuta uwepo wa Yesu?
Siyo kwamba Yesu alipuuza dhambi zao; alitaka haki iliyozidi viwango vya Mafarisayo (Mathayo 5:20). Wenye dhambi walikimbilia kwa Yesu kwa sababu alikuwa mtu wa huruma. Hakuwa na huruma dhidi ya dhambi, lakini alikuwa na huruma kwa mtu aliyekuwa mateka wa dhambi.
Tunaliona hili kutoka kwa mwanamke aliyekamatwa kwenye tendo la uzinzi. Baada ya waliomtuhumu kuondoka, Yesu alimwambia, “Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena” (Yohana 8:11). Yesu hakusamehe dhambi; alimtaka huyu mwanamke kuachana na maisha ya dhambi. Lakini alionyesha kumhurumia kuliko kumhukumu.
Injili ya Luka inatoa kipaumbele maalumu kwa huruma ya Yesu. Luka anaelezea taarifa inayomhusu Zakayo, mtoza ushuru ambaye angeweza kunyanyaswa na viongozi wa dini. Kwa mshangao wa watazamaji wengi, Yesu alijikaribisha mwenyewe “kuwa mgeni wa mtu ambaye ni mtenda dhambi” (Luka 19:7).
► Soma Luka 5:12-16.
Akitoa taarifa ya uponyaji huu, Luka anatoa maelezo ya kina ambayo yangeweza kuushangaza umati. Yesu “akaunyosha mkono wake, akamgusa.” Hakuna hata mtu mmoja katika ulimwengu wa zamani aliyegusana na mwenye ukoma! Ilikuwa ni hatari kiafya kwa sababu ya uwezekano wa kuambukizwa. Na kwa Myahudi, ilimfanya mtu atambulike rasmi kwamba siyo mwenye haki.
[3]Kwa nini Yesu alimgusa mwenye ukoma? Alijawa na huruma. “Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa” (Marko 1:41). Mtu huyu aliyekuwa na ukoma alihitaji uponyaji wa kimwili, lakini pia alihitaji kuponywa kihisia. Watu waliokuwa na ukoma walihitajika kukaa mbali kabisa na watu wengine. Baada ya kuambukizwa na ukoma, mtu huyu alikuwa hajawahi kuguswa tena na mwanadamu yeyote. Yesu alikuwa na uwezo wa kuuponya huu ugonjwa bila ya kumgusa mwathirika, lakini alijua kwamba mwenye ukoma alihitaji mguso wa mtu mwingine. Yesu alisikia huruma.
Kama tunataka tuhudumu kama Yesu, ni lazima tuwe na mioyo ya huruma kama Yesu. Watu wenye dhambi walipomtizama Yesu kwenye macho yake, waliona upendo wa huruma. Wakati watu wenye dhambi wanapokutizama wewe kwenye macho yako, wanaona nini?
Yesu alionyesha Upendo wake Kupitia Huduma yake kwa Wahitaji
Ni rahisi kusema, “Ninajisikia kuwa na huruma kwa ajili ya wahitaji”; ni vigumu zaidi kushughulikia mahitaji yao. Yesu alionyesha upendo wake kwa kuhudumia mahitaji ya wale waliokuwa pamoja naye. Huduma yote ya Yesu ilikuwa ni kwa ajili ya kuhudumia wengine. Paulo aliandika kwamba Yesu “alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa” (Wafilipi 2:7). Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi” (Marko 10:45).
Miujiza aliyoifanya Yesu inaonyesha huduma yake kwa watu wengine. Miujiza ilikuwa alama yake ya umisheni wa kimasihi, lakini pia ilikuwa ni namna ya kukutana na kuhudumia mahitaji ya watu. Mara nyingine miujiza iifanyika kwa ajili ya kikundi kidogo tu cha watu. Mara nyingine waliwafaidisha watu ambao hawakuwa na nguvu au ushawishi wowote. Mara nyingine, miujiza yake (ya wakati wa Sabato) ilimsababishia kukataliwa zaidi.
Yesu hakufanya miujiza ili kupata kibali kwa watu wenye nguvu; alifanya miujiza kuwahudumia wenye mahitaji. Kulikuwa na matukio mawili tu ambayo Yesu alikataa kufanya miujiza. Mafarisayo walipohojiana naye, “wakitafuta kwake ishara itokayo mbinguni; wakimjaribu” (Marko 8:11). Yesu alikataa kutoa ishara hiyo. Kisha kwenye kesi ya Yesu, Herode “akataraji kuona ishara iliyofanywa na yeye” (Luka 23:8). Yesu alikataa hata kumjibu Herode. Yesu hakuwa wa kufanya miujiza “kwa shinikizo” au kwa ajili ya kuwavutia wasikilizaji waliokuwa na mashaka naye.
Ingawaje Yesu alikataa kufanya muujiza kwa Herode Antipasi, lakini alimponya mkwe wa mvuvi, wenye ukoma, waombaji vipofu, na waliopagawa na mapepo ambao hawakuwa na chochote cha kuweza kumlipa. Aliwalisha watu elfu tano ambao walionyesha ukosefu wa shukrani kwa kumwacha yeye na alimponya mjakazi wa kuhani mkuu aliyekuwa ameenda kumkamata yeye. Yesu alihudumia wahitaji kupitia miujiza yake.
Kama wachungaji na viongozi wa makanisa, ni rahisi kujipa moyo katika maamuzi yetu ya kuwasaidia wale ambao wanaweza kutusaidia sisi. Tunapotumiamuda wtu mwingi na watu wenye uwezo kuliko watumaskini, tunaweza kusema, “Wafanyabiashara wanaweza kusaidia huduma ya kanisa.” Tunapoahirisha safari ya kumtembeleamjane ili kumtembelea afisa mwenye ushawishi mkubwa, tunaweza kutoa udhuru, “Ana ushawishi mkubwa na anaweza kusaidia katika kazi ya Mungu.” Yesu kamwe hakufanya hivyo. Kama tunataka tuwe wahudumu tunaomfanania Yesu, ni lazima tuwe watumishi kama Yesu. Kama yeye alivyokuwa, ni lazima tutafute “siyo kutumikiwa, bali kutumika” (Marko 10:45).
Paulo aliandika, “Kwa maana hatujihubiri wenyewe, bali Kristo Yesu ya kuwa ni Bwana; na sisi wenyewe kuwa tu watumishi wenu kwa ajili ya Yesu” (2 Wakorintho 4:5). Neno mtumishi linaweza pia likatafsiriwa kama “mtumwa.” Watumwa wengi wakati wa Dola ya Kirumi walikuwa wameelimika, wengine walikuwa madaktari na waalimu. Hata kama mtumwa alikuwa na elimu sana kuliko bwana wake, bado alikuwa ni mtumwa tu. Hawezi kuwa na kiburi na kusema, “Sitakutumikia! Mimi ni mkubwa kuliko wewe.”
Baadhi ya wachungaji wanajisikia kwamba, “Nina elimu nzuri. Mimi siyo mtumishi wa mkulima katika kanisa langu!” Paulo kamwe kakusikia hivyo. Paulo alikuwa msomi sana wa elimu ya juu, lakini alifanyika mtumwa kwa Wakorintho “kwa ajiliya Yesu.” Angeweza kusema, “Angalia elimu yangu; Nimefundishwa fasihi ya Kiyahudi, filosofia ya Kigiriki, na theolojia ya Kikristo. Ninaweza kuzungumza kwenye baraza la Kiyahudi la Sanhedrini, la Kigiriki Aeropagi, na baraza la Seneti la Kirumi.” Badala yake alisema, “Mimi ni mtumishi wa watu wa chini sana katika Korintho - kwa ajili ya Bwana wangu, Yesu.”
Kama tunataka tuhudumu kama Yesu, ni lazima tuwe na unyenyekevu wa kuishi kama mtumishi. Kama watumishi, aina ya maisha yetu siyo aina ya maisha ya hali ya juu ya gavana. Kama tunataka tuwe na upendo kama Yesu, ni lazima tuwe watumishi wanyenyekevu.
Yesu alionyesha Upendo kwa kuwa na Rehema kwa Maadui zake
► Soma Mathayo 5:43-48.
Yesu aliwafundisha wafuasi wake kwamba, “Ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.” ikiwa na maana ya kuwa na upendo kama Baba wa mbinguni alivyo na upendo. Inamaanisha zaidi kwamba, “kuwapenda adui zako na kuwaombea wale wanaokutesa.” Unapoonyesha aina hiyo ya upendo, dunia itajua kwamba ninyi ni “watoto wa Baba yenu aliye mbinguni.”
Takribani miaka 200 kabla ya Yesu hajahubiri Hotuba ya Mlimani, mwandishi wa kiyahudi aliandika mkusanyiko wa mafundisho yaliyoitwa Hekaya za Bin Sira. Sikiliza jinsi alivyowafundisha wafuasi wake jinsi ya kushughulika na maadui zao:[4]
Unapofanya jambo jema, hakikisha ni nani anayefaidika kutokana na hilo; kisha utakalolifanya halitapotea bure.
Fanya mambo mema kwa watu wanyenyekevu, lakini usiwape kitu chochote watu ambao siyo wacha Mungu.
Usiwape chakula, vinginevyo watautumia wema wako kinyume chako. Kila jambo zuri unalofanya kwa ajili ya watu hao litakuletea badala yake matatizo mara mbili.
Yeye mwenyewe Aliye Juu sana anachukia watenda dhambi, na atawaadhibu.
Toa kwa ajili ya watu wema, lakini usiwasaidie wenye dhambi.
Maandishi ya Bin Sira yalichukuliwa na Wayahudi kama ni Maandiko wakati wa Yesu. Wakati Yesu aliposema, “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako,” hili ndilo andiko ambalo yawezekana alilirejea. Sira alisema, “Tenda wema kwa wenye haki tu.” Usipoteze mambo yako mema kwa watenda dhambi.” Sasa soma kwa mara nyingine tena Mathayo 5:43-48. Je, unaweza kuona ni kwa nini mafundisho ya Yesu yalileta mshtuko kwa wasikilizaji wake?
Katika Agano la Kale, Mungu alifundisha watu wake kuwapenda adui zao. Hili halikuwa jambo jipya. Kwenye masomo yangu ya Agano la Kale, mara nyingine huwapa “Jaribio” hili kwa wanafunzi wangu.
Jirani yako ni adui wa kanisa. Unapokuwa unapita, anakulaani. Anajaribu kukudanga na hata kukuibia wanyama wako. Siuku moja wakati wa mvua za radi, unamwona ng’ombe wa jirani yako amevunja boma na anakimbia zake. Je, jukumu lako ni nini kwa huyu jirani yako?
1. Je, unachukua fimbo na kumchapa ili apotelee mbali zaidi?
Wanafunzi wangu wanajua kwamba hili siyo jibu sahihi!
2. Je, unapuuzia na kusema, “Hili siyo tatizo langu”?
Wanafunzi wengi hufanya chaguo hili. Wanasema, “Ni ng’ombe wa jirani yangu na siyo ng’mbe wangu. Nitajali shughuli zangu peke yake. Mbali na hilo, jirani yangu hanipendi; hatakubaliana na msaada wangu."
3. Je, unatii andiko la Kutoka 23:4? “Ukimwona ng'ombe wa adui wako, au punda wake, amepotea, sharti umrudishie mwenyewe tena.”
Hata katika Agano la Kale, watu wa Mungu waliitwa kuwapenda jirani zao. Lakini wakati wa Yesu, watu walikuwa hawanukuu sana katika Kutoka 23 bali Hekaya za Bin Sira. Walipenda mafundisho yaliyowaruhusu wawapende jirani zao na wawachukie maadui zao! Yesu alisema, “Wapendeni maadui zenu kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anawapenda watu wote waovu na wema.”
Hii inaonekanaje katika “maisha halisa?” Jaribu kufikiria kisa hiki katika huduma yako:
Kundi la watu ambao wamekuwa wakishiriki pamoja nawe katika mambo ya imani mara kwa mara wanakupinga hadharani. Wanakuuliza maswali yenye lengo la kukutega wewe; wanawaeleza wafuasi wakokwamba wewe ni mwalimu wa uongo; wanategemea utafanya jambo lolote litakalosababisha uingie kwnye mgogoro na wafuasi wako. Je, utawafanyiaje?
1. Kuwafukuzia mbali na kuwaagiza kwamba kamwe msirejee tena?
2. Kuwatendea kama wanavyokutendea wewe?
3. Kuwa mkweli kuhusu makosa yao, lakini uwajibu kwa upendo?
Mafarisayo walitumia kila njia ili kumpinga Yesu. Alikuwa mkweli kuhusiana na makosa yao; alijitahidi kuwafundisha ukweli; lakini siku zote aliwachukulia kwa upendo.
Kama tunataka tuhudumu kama Yesu, ni azima tuwapende maadui zetu. Hilo ni mojawapo ya mafundisho ya Yesu magumu sana. Kwa mtu yeyote anayetusaliti, kwa mtu yeyote anayekataa ujumbe wetu, kwa mtu yeyote anayetutesa, ni lazima tumwonyeshe upendo wa Yesu wa agape.[5] Hiyo ndiyo gharama ya kuwa na upendo kama Yesu.
[1]Hii inaonyeshwa katika kitabu cha Mithali. Mama Hekima anamkaribisha “mtu mjinga” ale pamoja naye mezani pake. (Mithali 9:1-6). Kupitia mahusiano haya na Mama Hekima, huyu mtu mjinga atajeuka kuwa na Hekima
"Mifano hii inaonyesha kwamba injili siyo kwa wale wenye kila kitu kilicho sahihi. Injili ni kwa ajili ya wale wanaojua kwamba hawana kila kitu kilicho usahihi."
Watu hawajali ni kwa jinsi gani unajua hadi pale watakapojua ni kwa jinsi gani wewe unajali.
[4]Hekaya za Bin Sira 12:1-7, Toleo la tafsiri ya Habari Njema
[5]Agape ni neno la Kigiriki lenye maana ya upendo usiokuwa na masharti unaotumika katika Agano Jipya. Ni neno lililotumika katika 1 Yohana na 1 Wakorintho 13.
Matumizi: Tabia ya Yesu katika Maisha ya Mkristo
Ni rahisi sana kuandika kuhusu kumpenda Mungu na kumpenda jirani yetu. Ni vigumu sana kuuonyesha upendo huo katika maisha ya kila siku. Ni pale tu tutakapokuwa tunaipalilia tabia ya Yesu ndani ya maisha yetu tutakapokuwa katika utayari wa kumshirikisha na ulimwengu wetu.
Je, inawezekana sisi kuwa na tabia ya Yesu? Maandiko yanafundisha kwamba Mungu ana uwezo wa kuwawezesha watu wake kufikiri kama eye anavyofikiri. Anataka awape watu wake roho mpya ambayo itatusababisha sisi tupende kile ambacho Mungu naye anakipenda, na tuishi kwa hiari ile anayotuitia tuishi nayo (Ezekieli 36:26-27). Mungu anataka akuze ndani yetu tabia ya Mwanae.
Sikiliza kile ambacho Oswald Chambers alizungumzia kuhusu uaminifu katika huduma ya kila siku:
Unapokuwa huna maono kutoka kwa Mungu, hakuna shauku iliyoachwa ndani ya maisha yako, na hakuna anayekuangalia au kukutia moyo wewe, inahitaji neema ya Mwenyezi Mungu kuweza kuchukua hatua inayofuata katika kujitolea kwako kwa ajili yake…Inachukua zaidi ya neema ya Mungu, na uangalifu wa ziada wa kumsogelea yeye, ili kuweza kuchukua hatua inayofuata, kuliko ilivyo katika kuhubiri injili.
Kitu ambacho kwa uhakika huthibitisha kwa Mungu na kwa watu wa Mungu baada ya hapo ni uvumilivu thabiti, hata pale ambapo kazi haiwezi kuonekana kwa watu wengine. Na njia pekee ya kuishi maisha ya kutoshindwa ni kuendelea kumwangalia Mungu. Mwombe Mungu ayaweke macho yako ya kiroho yawe wazi kwa yeye Kristo aliyefufuka…[1]
Tunawezaje kuimarisha uaminifu huu katika huduma? Tunawezaje kuendelea kumpenda Mungu na jirani yetu wiki hadi wiki, mwaka hata mwaka? Ni lazima tupalilie tabia ya Yesu ndani ya maisha yetu ya kila siku. Hii inatuhitaji kwamba tuwe na ufahamu wa Kristo.
Maelezo kuhusu Ufahamu wa Kristo
► Soma Wafilipi 2:1-16.
Maelekezo ya Paulo kwa kanisa la Filipi ni mwongozo wenye nguvu wa kile kinachomaanisha kuwa na tabia ya Yesu Kristo. Kwa kanisa lililogawanyika kutokana na migogoro, Paulo aliandika, “Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.”
Wangewezaje kufikia hili? Wangeweza tu kama wangetii maelekezo ya Paulo, “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu;
Paulo aliorodhesha tabia nne zisizopatana na maisha ya Kikristo.[2] Tabia hizi zinaharibu ushuhuda wa Kikristo na ufanisi wa mhudumu wa Kikristo. Paulo alisema:
(1) Msitende neno lo lote kwa kushindana (Wafilipi 2:3).
Tamaa ya ubinafsi inauliza, “Kuna nini ndani yake kwa ajili yangu? Nitafaidikaje katika hili? Je, unaweza kufikiria Yesu akiuliza, “nitafaidikaje?” kabla ya kumponya yule aliyepooza au wakati anakabiliana na msalaba? Kwa hakika hapana!
Paulo anasema, “Tukiwa na ufahamu wa Kristo – kama tutafikiri kama Kristo alivyofanya – hatutafanya jambo lolote linalohusiana na kushindana kwa ajili ya tamaa binafsi. Tabia yetu ya ndani itakuwa tabia ya mtumishi. Tutauliza, “Nitawezaje kutumika?’ na siyo “Nitawezaje kutumikiwa?”
(2) Msitende neno lolote kwa majivuno (Wafilipi 2:3).
Majivuno huuliza, “Je, hii inanifanya nionekaneje? Je, watu watavutiwa?” Pia katika hili, jaribu kufikiria Yesu akiuliza, “Watu watavutiwa?” kabla hajamtembelea mwanamke Msamaria kisimani? Kwa hakika hapana!
Paulo anasema, “Tukiwa na ufahamu wa Kristo – kama tutafikiri kama Kristo alivyofanya – hatutafanya jambo lolote linalohusiana na majivuno. Tutatafuta nafasi za kumdhihirisha Kristo, na siyo nafasi kwa ajili ya kujijengea hadhi zetu.
(3) Fanya mambo yote bila manung’uniko (Wafilipi 2:14).
Manung’uniko husema, “Mimi ninastahili zaidi kuliko hiki!” Je, unaweza kufikiria Yesu akisema, “Sikutakiwa niwaoshe wanafunzi miguu yao. Mimi ni mwalimu wao. Ninastahili zaidi. Kwa hakika hapana!
Paulo anasema, ““Tukiwa na ufahamu wa Kristo – kama tutafikiri kama Kristo alivyofanya – tutahudumu bila manung’uniko, hata katika nyakati ngumu sana.” Hapo tutatambua kwamba “hatustahili” chochote. Wakati tunapokumbuka kwamba kila kitu tulicho nacho ni zawadi ipatikanayo kwa neema ya Mungu, inabadilisha mtazamo wetu wa changamoto za huduma.
Helen Roseveare alikuwa ni mmoja wa wamishenari wakuu sana wa karne ya ishirini. Alikuwa daktari wa matibabualiyefundishwa katika Chuo Kikuu Cha Cambridge. Wakati akiwa anatumika kama mmishenari na daktari nchini Zaire, alitaka kujenga hospitali. Kwa sababu kulikuwa hakuna vifaa vya kujengea, hatua ya kwanza aliyochukua ni kutengeneza matofali. Dr. Roseveare alifanya kazi ya kutengeneza matofali ya kuchoma sambamba na wafanyakazi wa Kiafrika.
Alipokuwa anafanya kazi ya kutengeneza hayo matofali, mikono yake iliyokuwa milaini ilianza kububujikwa na damu. Alianza kunung’unika, “Mungu, nilikuja Afrika kama mtaalamu wa upasuaji, na siyo kutengeneza matofali! Bila shaka kuna watu wengine wa kufanya hii kazi ya watu wa chini.”
Wiki chache baadaye, mmoja wa wafanyakazi wa Kiafrika akamwambia, “Daktari, unapokuwa kwenye chumba cha upasuaji unatuogofya sisi kama daktari. Lakini unapokuwa unafanya kazi ya matofali na vidole vyako vinabubujika damu kama vidole vyetu, wewe ni dada yetu na tunakupnda.” Dr. Roseveare ghafla akatambua kwamba, “Mungu hakunituma mimi Afrika kuja kuwa daktari wa upasuaji tu; Alinituma pia kuonyesha upendo wa Kristo.”
(4) Fanya mambo yote pasipo kuwepo na Mashindano (Wafilipi 2:14).
Mashindano yanasema, “Ndiyo, Bwana, lakini…. Niko tayari kutii, lakini….” Pia katika hili, je, unaweza kufikiria Yesu akisema, “Baba, niko hapa kukutumikia; kwanini unafanya kukutumikia kwangu kuwe kugumu kiasi hicho? Haitatokea sisi kufikiria kwamba Yesu anaweza akawa na mashindano na Baba yake.
Paulo anasema, “Tukiwa na ufahamu wa Kristo – kama tutafikiri kama Kristo alivyofanya – hatutashindana kwa jambo lolote katika kutafuta njia rahisi ya kupita.” Hatutaweza kuridhia mapenzi ya Mungu katika maisha yetu kwa ajili ya kujadiliana katika mambo tofauti na yale Mungu aliyokusudia kwetu. Jibu letu kwa Mungu litakuwa, “Ndiyo Bwana.” Kwa njia hii tutakuwa na ufahamu wa Kristo.
Tangu Paulo alipowataka Wafilipi kuwa na ufahamu wa Kristo, aliamini wazi kwamba ingewezekana. Alijua kwamba wangeweza kuwa na roho ya unyenyekevu na utii ambavyo vilikuwa ni alama ya kuonekana katika maisha ya Yesu. Ni kwa jinsi gani tunaupata huu ufahamu wa Yesu?
Fahamu zetu Zinabadilishwa kupitia Maandiko
Mapema katika somo hili, tuliona ni kwa jinsi gani Maandiko hutufundisha kuhusiana na mapenziya Mungu. Yesu alikuwa analifahamu Neno la Mungu. Mitume walilijua Neno la Mungu. Kila uamsho wa kudumu katika historia ya kanisa ulianza kwa kujifunza Neno la Mungu.
Paulo aliwapa changamoto waamini wa Filipi, “kulishika vyema neno la uzima” (Wafilipi 2:16). Ujasiri wao na msimamo wao kwa ajili ya injili kungewafanya wawe nuru ya ulimwengu wao.
Ni kupitia kwenye mafunzo ya kina ya Neno la Mungu kunakotuwezesha tuanze kufikiri kama Yesu, na kuwa na ufahamu wa Kristo. “Kupitia kwenye mafunzo ya kina,” simaanishi kwamba ni lazima ujue Kigiriki na Kiyunani ili kuyaelewa maandiko; simaanishi kwamba ni lazima uwe na maktaba kubwa ya vitabu vya kusherehesha Biblia; kwa wepesi ninamaanisha kwamba ni lazima kutumia muda wa kutosha kujifunza Neno la Mungu. Ni lazima iwe kama ni sehemu yako ya mlo wa kila siku.
Kama Wakristo, Neno la Mungu ni lazima mlo wetu wa kila siku. Itakuwa ni furaha, siyo tu kazi. Hakuna mtu anayeweza kumwambia kijana mwenye njaa kwamba, “Unatakiwa leo ule chakula! Endapo hutakula, hutakuwa na afya,” Kinachotakiwa kufanywa hapa ni kutengeneza mlo mzuri utakaopatikana, na kijana atataka kula! Neno la Mungu linapaswa liwe mlo wa kila Mkristo mwenye njaa.
Tunapokuwa tunajilisha kwa Neno la Mungu, akili zetu zinabadilishwa kuwa kwenye ufahamu wa Kristo. Wakristo wengi wamezaliwa mara ya pili, lakini bado wanaendelea kufikiri kwenye njia ile ile waliyokuwa wakifikiri wakati wakiwa bado hawajaamini. Akili zao bado hazijabadilishwa kuwa kwenye ufahamu wa Kristo. Kwa nini?
Dr. Paul Brand mmishenari na daktari wa upasuaji nchini India. Aliwatibu wagonjwa wengi wa ukoma. Aliwafanyia upasuaji uliotengeneza sehemu za viungo vyao ambavyo vilikuwa vimeharibiwa na ugonjwa wa ukoma. Aliandika kwamba wagonjwa ni lazima wajifunze njia mpya ya kufikiri jinsi ya kujisimamia baada ya kufanyiwa matengenezo upya.
Kwa mfano, angeondoa kano yenye afya kutoka kwenye kidole cha pete ili kurekebisha kano iliyoharibiwa kwenye kidole gumba. Lakini atakaposema kwa mgonjwa, “chezesha kidole gumba,” hakuna kilichotokea. Kisha atasema, “chezesha kidole chako cha pete,” haraka watachezesha kidole gumba! Wanapaswa “kupangilia upya” ubongo wao. Watalazimika kujifunza jinsi ya kukifanyia kazi kidole gumba kwa njia mpya.[3]
Kama waamini wapya, tunapaswa “kupangilia upya” ufahamu wetu ili tuweze kufikiri kama Kristo. Kabla hujawa Mkristo, ulifikiria kwanza kuhusu mahitaji yako mwenyewe. Labda ulimwona mtu maskini, lakini ukafikiria kwamba “mimi mwenyewe ninahitaji fedha. Siwezi nikatoa fedha yangu kumpa mtu Yule.” Kama Mkristo, uliwahi kusoma Neno la Mungu kwamba, “Mwenye kuwagawia maskini hatahitaji kitu” (Mithali 28:27). Unasikia Neno la Mungu, “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa” (Luka 6:38). Unaanza kufikiri mambo ya fedha kama Kristo naye alivyofikiri kuhusu fedha. Unaupata ufahamu wa Kristo kupitia Neno la Mngu.
Kabla hatujawa Wakristo, tulijaribu kuwaumiza wale waliotujeruhi sisi. Mtu alipokuwa mkali kwetu, tulighadhabika kwa hasira. Lakini kama Wakristo, tunasoma, “jivikeni moyo wa rehema” (Wakolosai 3:12). Tunasoma tuwe, “watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi baraka” (1 Petro 3:9). Tunaanza kuwajibu watu wengine kama Kristo alivyokuwa akiwajibu wale waliokuwa wakimuumiza. Tunaupata ufahamu wa Kristo kupitia Neno la Mungu.
Fahamu zetu Zinabadilishwa kupitia Kujisalimisha kila siku.
Paulo aliwataka Wafilipi wawe na ufahamu ambao ulikuwa ndani ya Yesu Kristo. Aliufafanua ufahamu huu kisha akawaeleza jinsi ambavyo hili litawezekana katika maisha yao. Ni lazima waendelee “kuufanyia kazi” wokovu wao kwa utii wa uaminifu na siyo kupata wokovu wao tu – bali kwa sababu Mungu tayari alikuwa kazini kwa “kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema” (Wafilipi 2:12-13). Walipojitoa kwa Mungu kwa unyenyekevu, aliwapa tamanio la (“kutimiza mapenzi”) na nguvu (“ya kufanya kazi”) ili kuishi maisha ya Kimungu.
Tunapoishi maisha ya kujisalimisha, Roho Mtakatifu hupalilia ndani yetu tabia zile zile tunazoziona ndani ya maisha na huduma ya Yesu. Hatuupati ufahamu wa Yesu kwa jitihada zetu wenyewe; tunapata ufahamu wa Yesu kwa kujisalimisha.
Kujisalimisha kunatakiwa kuwe ni kitendo cha kila siku. Paulo ametuambia “itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai” (Warumi 12:1). “Dhabihu iliyo hai” haijafa; inaendelea kuishi. Kuna kujisalimisha ambako tunasalimisha mapenzi yetu yote kwenye mapenzi ya Mungu, lakini pia kuna kujisalimisha kwingi ambako tunaendelea kila siku kujisalimisha kwenye mapenzi yake.
Nancy Leigh DeMoss anatoa picha ya maisha ya kujisalimisha.[4] Utakapokuwa unasoma maelezo aya, jiulize, “Je, ninaishi kwenye maisha ya kujisalimisha kila siku kwenye mazingira haya? Je, ninadhihirisha ufahamu wa Kristo kwenye mazingira haya?”
Wakati mwili wako unapotaka urudie maneno ya kukosoa, Roho Mtakatifu anakuambia, “usimtukane mtu ye yote” (Tito 3:2). Moyo uliojisalimisha unasema, “Ndiyo.”
Wakati mwili wako unapotaka kulalamika kuhusu matatizo, Roho Mtakatifu anakuambia, “shukuruni kwa kila jambo” (1 Wathesalonike 5:18). Moyo uliojisalimisha unasema, “Ndiyo.”
Wakati mwili wako unapotaka kupingana na kiongozi asiyekuwa na busara, Roho Mtakatifuanakuambia, “Tiini kila kiamriwacho na watu, kwa ajili ya Bwana” (1 Petro 2:13). Moyo uliojisalimisha unasema, “Ndiyo.”
[5]Wakati tunapokuwa tumejisalimisha, Roho yule yule aliyekuwa anakaa ndani ya Kristo anakaa ndani yetu. Kupitia Roho Mtakatifu – siyo kupitia makusudi mazuri yetu wenyewe – tumepewa uwezo wa kuchukua hatua kama Kristo dhidi ya mambo ya kuvunja moyo ya kila siku, mambo ya kukatisha tamaa ya huduma, na majaribu ya Shetani.
► Shirikisha muda wa hivi karibuni ambao matamanio ya mwili yaliingiliana na mapenzi ya Mungu. Uliishije katika kujisalimisha kila siku wakati wa kukabiliana na majaribu? Je, lipo jaribu la sasa hivi ambalo itakubidi ujisalimishe tena kwenye mapenzi ya Mungu? Kama darasa, kila mmoja amwombee mwenzake katika maeneo haya.
[1]Oswald Chambers, My Utmost for His Highest (March 6 entry). Yamepatikana kutoka https://utmost.org/taking-the-next-step/ tarehe ya March 22, 2021.
[2]Sehemu hii imenukuliwa kutoka kwa Dennis F. Kinlaw, The Mind of Christ (Anderson, Indiana: Warner Press, 1988), 101-107.
[3]Paul Brand na Philip Yancey, In His Image (Grand Rapids: Zondervan, 1984), 146
[4]Nukuu kutoka kwa Nancy Leigh DeMoss, Surrender. (Chicago: Moody Press, 2008), 223-224
“Siri ya maisha ya utakatifu haiko katika kumuigiza Yesu, lakini iko katika kumruhusu Yesu ajidhihirishe Mwenyewe katika maisha yangu….Utakaso hauleti kutoka kwa Yesu uwezo wa kuwa mtakatifu; ni kuchukua kutoka kwa Yesu utakaso ule ambao ulikuwa umejidhirisha kwake.”
- Oswald Chambers
Hitimisho: Mungu hufanya kazi kupitia Upendo unaomfanania Kristo
Nilipoanza kuandika somo hili, nilijisikia kusitasita. Ingawaje ninajua akilini kwamba tumeitwa kuwapenda adui zetu, ninajua pia kwamba tunaishi kwenye ulimwengu ambao umetatizika. Wengi waliosoma masomo haya, wanaishi kwenye mazingira ambayo kanisa linatishiwa na serikali, dini za uongo, au misongo ya kijamii. Nilipokuwa naandika kuhusu kumpenda adui yako, nilijiuliza mimi mwenyewe, “Je, ni busara kufikiri kwamba kweli tunaweza kuubadilisha ulimwengu wetu kwa kuwapenda adui zetu? Tutampendaje adui yetu wakati adui yetu anajaribu kutuua sisi?”
Wakati nikiwa nashughulka na kuandaa somo hili, nilisoma kipande cha habari kuhusiana na Mkristo mmoja wa Iraq anayeishi Baghdad.[1] Wakati mwandishi wa habari alipokuwa akihojiana naye, wanajeshi wa ISIS walikuwa wamebakiza dakika arobaini tu waingie nyumbani kwake. Mwandishi aliukiza, “Bado kanisa lako linakutana kwa ajili ya kuabudu?” Yule Mkristo akamjibu, “Ndiyo! Kwa kweli, tumeanzisha vikundi viwili vya maombi katika kanisa letu - Kundi mojakwa ajili ya kuombea ndugu zetu waliouawa kwa mateso upande wa kaskazini, na kikundi kingine kuwaombea adui zetu.”
Washirika wa Kanisa la Mtakatifu George huko Baghdad huomba kwa ajili ya adui zao. Wanatoa vifurushi vya chakula kwa wajane wa Kiislamu. Wanawapenda adui zao kwa sababu wanaamini kwamba wameitwa kwa ajili ya kufuata mfano wa Yesu.
Makala hii ilinikumbusha mimi kuhusu ukweli unaoonekana muda wote katika historia ya kanisa. Njia za Mungu za kufanya kazi siku zote hazifanani na njia za wanadamu. Mwanadamu anafanya kazi kwa kupitia mikutano ya uamsho ya kijeshi dhidi ya Waislamu kwenye karne za kati; Mungu anafanya kazi kupitia Raymond Lull aliyekufa akiwa kwenye ziara zake za umisheni kwa ulimwengu wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka themanini na mbili. Mwanadamu anafanya kazi kupitia nguvu za kijeshi; Mungu anafanya kazi kupitia Hudson Taylor aliyejitolea maisha yake kwa ajili ya kupeleka injili kwa watu wa katikati ya Uchina. Mwanadamu anafanya kazi kutumia nguvu zake; Mungu mara nyingi hufanya kazi kupitia udhaifu.
Njia za Mungu kamwe siyo njia za wanadamu. Lakini mwisho wa mambo yote, njia za Mungu siku zote ni lazima zishinde. Dunia yetu inabadilishwa ielekee kwenye umilele kufuatia jinsi ambavyo Wakristo wanavyokuwa na upendo kama Yesu. Mabadiliko yenyewe ni ya polepole lakini mara nyingi yameambatana na maumivu, Lakini hii ndio njia ya Mungu ya kufanya kazi yake katika ulimwengu wetu ulioanguka.
Kufanya huduma kama Yesu kunatuhitaji tuwe na upndo kama Yesu. Mwinjilisti mmoja aliyekuwa mzee aliulizwa kuhusu mafanikio ya huduma yake. Alisema, “Njia pekee ambayo watu watajua ni kwa jinsi gani Mungu anawapenda ni kukuona wewe unawapenda kwa kiasi gani.” Huyu mwinjilisti alielewa kwamba kwa jinsi ile upendo wa Kristo utakavyokuwa unang’aa kupitia sisi, ndiyo hivyo tutakavyokuwa tunauvuta ulimwengu uje kwa Mungu. Hiyo ndiyo maana ya kupenda kama Yesu.
[1]Mindy Belz, “How Does the Church Move the World?” World Magazine, May 27, 2017
Kazi ya kufanya Somo la 7
Katika somo hili, tumeona ni kwa jinsi gani Yesu alikuwa na upendo. Kazi hii inakutaka wewe utafute njia ambazo unaweza kufuata mfano wa Yesu katikakumpenda jirani yako. Haitakiwi ichukue muda mrefu kuifanya kazi hii; Inaweza ikachukua muda mrefu kidogo katika kuiweka kwenye matendo! Usishinwe kuiweka kwenye vitendo. Tumeitwa tuwe na upendo kama Yesu alivyokuwa na upendo
Katika safu ya 1, toa mfano kamili kutoka katika Vitabu vya Injili unaohusiana na upendo wa Yesu kwa ajili ya watu.
Katika safu ya 2, elezea mfano kamili jinsi ulivyoutumia upendo katika maisha yako. Utafuataje mfano wa Yesu wa upendo? Hii kazi ya kufanya ni kwa ajili yako; kuwa mahiri sana kwa jinsi itakavyowezekana.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.