Viongozi ni kama Yesu wanapokuwa wanahudumia watu wengine.
Utangulizi
“Uongozi” ni neno linalochochea hisia nzito. Wakati watu wenye mawazo ya ulimwengu wanapofikiria kuhusu uongozi, wanazingatia katika nguvu na nafasi. Kuwa kiongozi ni kuwa “bosi”. Viongozi wenye tamaa wanachotaka ni “kupanda ngazi” na kupata cheo kikubwa. Hata wachungaji wanaweza wakachukua mawzo haya. Wanaweza kuzingatia katika mawazo yao jinsi ya kupata makanisa makubwa, nafasi za juu za uongozi na heshima kubwa.
Kwa kukabiliana na mawazo haya ya kidunia, baadhi ya Wakristo huonyesha hisia tofauti na neno hili “uongozi.” Wakati mmoja mchungaji aliniambia. “Sitaki kuwa kiongozi katika kanisa langu. Ninachotaka ni kuwa mtumishi tu.” Hata hivyo, ingawaje kauli hii inaonyesha hali ya unyenyekevu, unaliacha kanisa lake katika kutopambanua mwelekeo au kusudi. Mashirika yote, yakiwemo makanisa, yanahitaji viongozi.
Wachungaji wanapaswa kukumbuka kwamba chimbuko kubwa la neno “mchungaji” ni “mchungaji wa kondoo.” Mchungaji wa kondoo hana kazi inayoonekana kwamba ni ya maana sana! Mchungaji wa kondoo hukamilisha kila siku akiwa na kondoo wanaonuka shombo ya kondoo. Kazi yake ni pamoja na majukumu yanayokinaisha – kutafuta chakula na maji, kufukuzana na wana kondoo wanaotangatanga huku na kule bila mpangilio wake, na kuwahudumia kondoo walioumia.
Mchungaji wa kondoo analo jukumu moja muhimu sana. Mchungaji wa kondoo anafanya kazi zinazoonekana ni za chini sana., mchungaji huyo huyo anabeba jukumu kubwa la kuwaongoza kondoo wake kwenye usalama. Kondoo wanamtegemea mchungaji aliye kiongozi wao.
Yesu hutoa mfano bora wa kuigwa wa kiongozi wa kweli. Alikuwa ni kiongozi wa kondoo aliyetumika kwa unyenyekevu lakini akiwa na fasili ya dhana akilini ya mwelekeo mkubwa na kusudi. Alikuwa na nguvu lakini aliyejaa huruma. Hakutafuta nafasi ya madaraka, lakini alikuwa na uhakika na utume wake. Yesu alifanyika mfano wa kuigwa wa watumishi – viongozi.
► Fikiri juu ya kiongozi mmoja aliyefanikiwa sana ambaye ulimjua au unamjua binafsi. Orodhesha tabia tatu au nne ambazo zilimfanya huyu mtu akawa kiongozi mzuri. Je tabia hizi zinaonekana katika huduma ya Yesu? Je, tabia hizi zinaonekana kwenye huduma yako?
Yesu anaonyesha kwamba uongozi wa kweli unahusisha huduma ya unyenyekevu. Unyenyekevu hauna maana ya kuwa mdhaifu au kukosa maamuzi; Yesu alikuwa mwenye nguvu. Vitabu vya injili kwa kurudia mara nyingi zinaonyesha mamlaka ya Yesu.[1] Hata hivyo, alipata mamlaka hayo siyo kwa kudai heshima, bali kwa kuhudumu. Wakati wanafunzi wake walipouliza kuhusu nafasi za uongozi katka ufalme wa mbinguni, Yesu alijibu:
Wafalme wa Mataifa huwatawala, na wenye mamlaka juu yao huitwa Wenye fadhili; lakini kwenu ninyi sivyo; bali aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye kuongoza kama yule atumikaye. Maana aliye mkubwa ni yupi? Yeye aketiye chakulani, au yule atumikaye? Siye yule aketiye chakulani? Lakini mimi kati yenu ni kama atumikaye (Luka 22:25-27).
Katika somo hili, tutaangalia tabia zilizomfanya Yesu akawa kiongozi mashuhuri. Tutajifunza jinsi ya kuwa viongozi wenye ufanisi kwa kufuata mfano wa Yesu.
[1]Mathayo 7:28-29; Marko 1:22-28; Luka 4:32-36; Luka 20:1-8
Kiongozi wa Kikristo mwenye Ufanisi anajua kuhusu Utume wake
Kiongozi mkuu na mashuhuri ana utume ulio wazi na anazingatia kwa nia moja uzito wa utume alioubeba. Yesu alijua kusudio la utume wake. Utume wa Yesu umejumlishwa kwa pamoja katika Marko 10:45: “Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.”
Katika hotuba yake ya kwanza ya hadharani, Yesu aliwaambia wasikilizaji wake kwamba alikuaja ili kukamilisha ujumbe uliokuwa umetabiriwa na Isaya, kwamba:
Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa (Luka 4:18-19, akinukuu Isaya 61:1-3).
Utume wa Yesu uliongoza maamuzi yake ya kila siku. Alipokuwa akisafiri kutoka Yudea hadi Galilaya, utume wake uliongoza njia yake ya kupitia. Marabi wa Kiyahudi mara nyingi walisafiri kupitia upande wa Mashsriki wa mto Jordani ili kuepuka kukutana na kunajisiwa na Wasamaria. Njia ya Yesu, hata hivyo, iliongozwa na utume wake wa “kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa” Kwa mwanamke Msamaria. Kwa sababu ya hiyo, “ilibidi ni lazima apitie katika nchi ya Samaria” (Yohana 4:4, msisitizo umeongezwa). Kama kiongozi wa Kikristo, utume wako ni lazima ukuongoze katika maamuzi yako ya kila siku.
Kama kiongozi, kuna mambo ya ziada ya kufanya kuliko yale unayoweza kukamilisha. Ni kwa jinsi gani unaweza kupima vipaumbele vyako? Huwezi ukafanya kila kitu, na hutakiwi ufanye kila kitu. Ni lazima ufanye mchanganuo wa nafasi zilizopo katika huduma yako ya umisheni/utume. Kila kiongozi anapaswa awe na orodha mbili: orodha ya “Mambo ya kufanya” na nyingine ya “Mambo yasiyotakiwa kufanyika,” Orodha “Mambo ya kufanya” inakuwa pamoja na mambo yale ambayo unapaswa uyakamilishe. Orodha ya “Mambo yasiyotakiwa kufanywa” inakuwa na mambo yote ambayo yanakukengeusha katika utume au umisheni wako. Mtu fulani anaweza akaitwa kutumika katika mambo kadhaa, lakini wewe usiitwe kwa mambo hayo. Utume wako ni lazima ukuongoze katika vipaumbele vyako vya kila siku.
Mtume Paulo ni mfano wa kiongozi aliyejua kusudi la utume wake. Paulo aliitwa kupanda makanisa katika miji mikubwa ya Dola ya Kirumi. Hakutaka “kujenga juu ya msingi wa mtu mwingine,” lakini alikuwa na wajibu wa kuipeleka injili kwa watu wote ambao walikuwa hawajabahatika kuisikia (Warumi 15:20). Utume huu uliweza kumwongoza Paulo mahali pa kwenda, akae mahali pamoja kwa muda gani, na hata ujumbe aliopaswa kuhubiri.. Utume wa Paulo uliongoza maamuzi yote.
► Jadili maswali haya:
Mungu amekupa wewe utume wa aina gani? Fupisha maelezo ya utume wako kwa maneno machache.
Je, umeshawashirikisha utume wako watu wengine wanaojiunga nawe katika huduma yako?
Je, utume wako unaongoza maamuzi yako ya kila siku?
Kiongozi wa Kikristo mwenye Ufanisi Anafundisha Viongozi Wengine.
Tangu mwanzo wa huduma yake, kwa uangalifu mkubwa Yesu alichagua na kufundisha kikundi cha wanafunzi ambao wangeendeleza huduma yake baada ya kuwa ameondoka kurejea kwa Baba yake. Wanafunzi hawa walijifunza kutoka kwake, walichukua muda mrefu kukaa naye, walitumika pamoja naye, na walisambaza ujumbe wake wa injili kwa dunia nzima. Yesu aliwatia muhuri hawa wanafunzi katika mfano wake, kasha akawatumia katika kulijenga kanisa lake.
[1]Luka aliandika kuhusu shinikizo la huduma. “Wakati huo, makutano walipokutanika elfu elfu, hata wakakanyagana, alianza kuwaambia wanafunzi wake kwanza” (Luka 12:1). Yesu hangeweza kuingiliwa na wasiwasi kutokana na huduma yake hadi kwenye wanafunzi wake,ingawaje hudumakwa maelfu ya watu walio wengi ingekuwa ni ya kushangaza. Alijua kwamba, ili kuujenga ufalme, ni lazima awafundishe wanafunzi wake jinsi ya kuongoza kanisa. Kwa kuwafundisha wanafunzi, tunawaanda viongozi wa kizazi kijacho.
Paulo alifuata mfumo huu wa Yesu. Aliwahubiri makutano, lakini alikazia mawazo yake yote katika kufundisha wanafunzi wachache katika kila mji. Hii inatoa mfano wa viongozi tunaotakiwa tuwe kwa wakati wa sasa. Paulo aliwataka wachungaji “kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke” (Waefeso 4:12). Mchungaji hahitajiki kufanya kazi zote za kanisa; mchungaji anapaswa kuwafundisha na kuwawezesha wafuasi kufanya kazi kwa ajili ya kanisa. Viongozi wenye ufanisi huwafundisha viongozi wengine.
“Yesu kamwe hakuwahi kuandika vitabu. Badala yake, aliandika ujumbe wake juu ya wanadamu, mitume.”
- William Barclay
Mfano wa Yesu wa kuwashauri Wanafunzi
Mshauri ni lazima Achague Wanafunzi kwa Umakini[1]
► Soma Yohana 1:35-51, Yohana 2:1-11, Mathayo 4:18-22, Luka 5:1-11, Luka 6:12-16.
Unaposoma aya hizi, je, unaona mchakato unaotumika? Wakati wa wiki ya kwanza ya huduma yake hadharani, Yesu aliwakaribisha Andrea na Yohana wamfuate. Andrea alimleta Simoni Petro kwa Yesu. Yesu akamwalika Filipo ambaye alimletea Nathanaeli (Yohana 1:35-51). Hii ilikuwa ni hatua ya kwanza katika wito wao. Walimkubali Yesu, lakini bado hawakufanyika wafuasi wa kudumu. Huu ulikuwa ni wito wa kumfuata Yesu. Baadaye, Yesu atawaalika kwenye uanafunzi wa kudumu.
Yohana 2, ni hatua muhimu katika mchakato huu. Kwenye ndoa ya Kana, Yesu “aliudhihirisha utukufu wake” kwa wanafunzi wake. Wageni wengine hawakujua kuhusu mmjiza alioufanya; muujiza ulikuwa ni kwa ajili ya wanafunzi. Yesu alijidhihirisha mwenyewe kwa wafuasi wake ili waweze kuweka tumaini lao kwake. “Na wanafunzi waliamini katika yeye” (Yohana 2:11).
Mathayo 4:18-22 inatokea baada ya Yesu kuondoka Nazarethi kwenda Kapernaumu na kuanza kuhubiri (Matthew 4:12-17). Akiwa anatembea kandokando ya Ziwa la Galilaya, Yesu alimwita Simoni, Andra, Yakobo na Yohana wamfuate. Mara hiyo hiyo waliacha nyavu zao wakamfuata yeye” (Matthew 4:20). Baada ya wito wa kwanza katika Yohana 1, wanafunzi hawa waliendelea na kazi zao kama wavuvi. Sas, Yesu anawaita katika kutumika: “Tangu sasa utakuwa ukivua watu” (Luke 5:10).
Hatua nyingine iliyofuata katika mchakato huu ulikuwa ni Yesu kufanya uteuzi wa wanafunzi kumi na wawili. Miongoni mwa wafuasi wengi (walioitwa “wanafunzi” katika Yohana 6), Yesu alichagua hapo wanafunzi kumi na wawili ambao wangekuwa ni washirika wake wa karibu sana na yeye.
Yesu hakuharakisha katika kuwachagua wanafunzi wake. Inaonekana kama mchakato huu ulichukua miezi kadhaa. Hatua hii ilimpa Yesu nafasi ya kukaa na kila mwanafunzi katika wanafunzi wake Kumi na Wawili. Mara nyingi, kiongozi huwa mwepesi kuharakisha kuchagua mrithi wake bila ya kuchukua muda wa kumjua huyo mtu. Kiongozi mwenye busara hugawa majukumu yanayotoa nafasi ya kumfanyia mtu tathmini kuhusu uwezo wake wa kuwa kiongozi.
Mshauri ni lazima Achukue Muda wa kukaa pamoja na Wanafunzi Wake
► Ni lipi la kusisimua zaidi, kuwafikia wengi au kuwashauri wachache? Ni jambo gani lililo muhimu kwa ajili ya kipindi kirefu? Kwa nini Yesu aliwekeza nguvu zake nyingi sana kwa ajili ya hawa watu kumi na wawili?
Yesu aliutumia muda wake mwingi akiwa na hawa wanafunzi kumi na wawili. “Alichagua Kumi na Wawili (ambao aliwaita Mitume) ili waweze kuwa pamoja naye na ili aweze kuwatuma kuhubiri pamoja na kuondoa mapepo” (Mark 3:14-15). Kwanza, wangetumia muda wao kukaa pamoja na yeye ili wajifunze mbinu zake. Kuanzia hapo ndiyo sasa wangekuwa tayari kutumwa nje kwa ajili ya huduma.
Marko alichukua kumbukumbu mojawapo ya safari za Yesu katikati ya Galilaya: “Naye hakutaka mtu kujua, kwa sababu alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake” (Mark 9:30-31). Lengo kubwa na la msingi la Yesu halikuwa kuanzisha utaratibu wa kuwafikia watu kwa makundi mengi, bali kuwaandaa watu ambao wangeongoza kanisa.
Yesu alihubiri kwa maelfu ya watu, lakini umuhimu wake mkuu ulikuwa katika kuwafundisha watu wachache kwa ajili ya huduma ya baadaye. Yesu alitambua kwamba kufundisha kunaleta matokeo bora zaidi kama mkazo utawekezwa kwenye kikundi kidogo. Robert Coleman anaonya, “Kwa jinsi huduma yako inavyokua, itakuwa ni vigumu zaidi kufanikiwa kupata muda wa kuwahudumia wanafunzi kibinafsi. Lakini jinsi huduma yako inayokua, itakuwa ni muhimu zaidi kufanikiwa kupata muda wa kuwahudumia wanafunzi kibinafsi.”
Unapokuwa unapitia kusoma Vitabu vya Injili, utaona kwamba siyo mara nyingi utaweza kumwona Yesu akihudumu bila ya kuwepo angalao wanafunzi watatu pamoja naye. Mara nyingi, Yesu na wanafunzi wake walijiondoa kwa muda kwenda kwenye maeneo yasiyokuwa na watu kwa ajili ya vipindi vya mafunzo. Kukaribia mwishoni mwa huduma ya Yesu ulimwenguni, aliweza kutumia muda mwingi zaidi kwa ajili ya kukaa na wanafunzi wake. Katika wiki yake ya mwisho Yerusalemu, Yesu hakuwaacha wanafunzi wake wakae mbali na uwepo wake. Kuwafundisha watu hawa lilikuwa ni mojawapo ya majukumu yake muhimu sana.
Mithali ya Kiyahudi inasema, “Mwanafunzi ni mtu anayekula mavumbi ya bwana wake.” Mwanafunzi alitembea karibu sana na bwana wake kiasi kwamba alimeza mavumbi yaliyotifuliwa na mguu wa bwana wake. Mwanafunzi alikula kile alichokula bwana wake; mwanafunzi alikwenda kila alipokwenda bwana wake; mwanafunzi aliwajibika kwa bwana wake kwa mafundisho na kuwa mfano wake. Wafuasi wa Yesu walitumia muda wao na yeye hadi walipochukuana na tabia ya mwalimu wao. Baadaye, wakaja kujulikana kama “Wakristo”; wamekuja kufanana na mwalimu wao.
Kwa njia hiyo hiyo, Paulo alikuwa na wafuasi wake kama Timotheo, Tito, Luka, au Tychicus pamoja naye. Paulo aliwafundisha kuhusu huduma kwa kuchukua muda wa kukaa nao.
Pia, njia hii inatupa mfano wa kuiga sisi wa leo. Unapofanya huduma yako, unaweza kuwatia moyo wafuasi wachanga ya timu yako wakufuate wewe, ili waweze kujifunza jinsi ya kuhudumu. Kiongozi mmoja wa kanisa aliyefanikiwa alisema, “Kamwe sifanyi safari ya huduma bila ya kufuatana na mhudumu mchanga pamoja nami. Kuwafundisha viongozi wa kanisa la baadaye ni muhimu kwangu kama ilivyo huduma ninayoitumikia.” Mchungaji huyu anaelewa kwamba viongozi wenye ufanisi huwafundisha viongozi wengine.
Mshauri ni lazima afanye Huduma kwa Wanafunzi wake
Baada ya kuwaosha miguu wanafunzi wake, Yesu alisema, “Nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo” (Yohana 13:15). Yesu alifundisha kwa kuwa mfano. Alijua kwamba haitoshi tu kusema, “Fanya jambo hili.” Ni lazima tuonyeshe kwa vitendo namna ya kufanya. Yrsu hakuwaelekeza wanafunzi wake kufanya jambo lolote hadi yeye mwenyewe awe ameshalifanya ili kuwaonyesha.
Wanafunzi walimwona Yesu akiomba kisha wakamwambia, “Bwana tufundishe jinsi ya kuomba” (Luka 11:1). Akaomba. Walipokuwa wakimwangalia jinsi anavyoomba, wanafunzi walipatwa na njaa ya kutaka kuelewa maombi. Wakati wanafunzi wanapokuwa na njaa ya kujifunza, wanajifunza vizuri sana!
Wanafunzi walimsikia Yesu akitumia maandiko katika mahubiri yake. Yesu alirejea kwenye Maandiko ya Agano la Kale zaidi ya mara sitini. Aliielezea Biblia jinsi inavyoweza kutumika kimantiki katika kuhubiri na kuandaa mahubiri kutokana na Maandiko yaliyomo. Je, wanafunzi walijifunza somo hili? Kwa hakika ndiyo! Wakati Petro alipohubiri kutoka katika Matendo 2, alirejea katika Yoeli, Zaburi 16, na Zaburi 116. Petro alijifunza kutoka kwa Yesu kuyajenga mahubiri yake kutoka katika Maandiko. Kila andiko la mahubiri katika Matendo linarejea kwenya Agano la Kale.
Paulo alifuata njia hiyo hiyo. Kwa kurudiarudia aliandika, “Mmeona mfano kutoka kwangu. Fuateni mfano wangu.”[2] Paulo alifundisha kwa vitendo. Wanafunzi kama Tito na Timotheo walijifunza uchungaji kwa kufuata mfano wa mshauri wao, Paulo.
Wakati wa leo, tunapaswa kuwa mfano wa huduma kwa wale tunaowafundisha. Katika hili inatupasa sisi tuwe watu tunaoonekana wakati wote. Watayaona yale tunayoshindwa, lakini watatuona tukiyakiri madhaifu yetu. Watatuona kama tunaoyumba, lakini watatuona sisi tukikataa kuacha kusonga mbele. Wanafunzi hujifunza uhalisia wa huduma kwa kuangalia mifano kutoka kwetu.
Mshauri ni lazima Akaimu Majukumu kwa Wanafunzi wake
► Soma Mathayo 10:5-11:1.
Tangu mwanzo, kusudi la Yesu lilikuwa ni kuwaandaa wanafunzi kwa ajili ya huduma. Aliwaita wamfuate ili aweze kuwanya wawe “wavuvi wa watu” (Mathayo 4:19).
[3]Muda mwingi wa wakati wao wa mwaka wa kwanza na Yesu, wanafunzi walikuwa wakiichunguza huduma yake. Walijifunza kutokana na mfano wake. Baada ya kuwa wameshachunguza, Yesu aliwatuma wanafunzi watoke nje kwa ajili ya kwenda kuhudumu. Mathayo 10 anaonyesha jinsi Yesu alivyokaimu majukumu kwa wanafunzi.
Aliwapa Mamlaka (Mathayo 10:1).
Kabla ya kuwatuma nje kwa huduma, Yesu aliwapa mamlaka ya kufanya kazi aliyokuwa awapangie kuifanya. Mara nyingine viongozi wana mashaka ya kuwaamini wale wanaowasaidia kwa mamlaka. Hata hivyo, majukumu bila kuwa na mamlaka kunawalemaza wale uanaowafundisha. Hatupaswi kuwapa wasaidizi wetu majukumu isipokuwa wamepewa mamlaka kamili ya kutimiza majukumu hayo.
Aliwapa maelekezo yaliyo wazi (Mathayo 10:5-42).
Yesu aliwapa wanafunzi wake ujumbe ulio wazi: hubiri kuhusu ufalme. Wajibu wao ulikuwa wazi. Walijua kwa uhakika ni nini Yesu alikuwa anawategemea wafanye.
Yesu aliwaambia wanafunzi wake ni mahali gani waende kuhudumu: “kwa kondoo waliopotea wa Israeli.” Kisha, hawa mitume waende kuhubiri kwa Mataifa, lakini wakati walipokuwa wanajifunza kuhudumu, Yesu aliwataka waanzie karibu na nyumbani. Tunapaswa tufanye kila linalowezekana tuwasaidie wanafunzi wetu wafaulu. Anza na wajibu mdogo ambao ni wepesi kuumaliza. Yesu aliweka malengo yanayoeleweka na yenye maana.
Yesu aliwapa maelekezo wanafunzi wake kuhusiana na mateso. Mateso hayangekujakwa sababu wanafunzi wameshindwa katika huduma yao, bali kwa sababu Yesu mwenyewe huleta utengano kati ya wafuasi wake na wale wanaomkataa yeye.
Aliwatuma wakiwa katika vikundi (Marko 6:7).
Yesu alionyesha umuhimu wa kuwa kwenye vikundi katika huduma. Aliwatuma wanafunzi wake kwa vikundi vya watu wawili wawili. Miezi michache baadaye, Yesu aliwatuma wengine Sabini katika vikundi vya watu wawili wawili. Huu ukafanyika ndio mfumo wa huduma katika kanisa la mwanzo. Petro na Yohana walihudumu pamoja. Barnaba na Sauli walisafiri pamoja. Paulo na Sila walihudumu pamoja.
Mshauri ni lazima Awasimamie Wanafunzi wake
Baada ya wanafunzi kurejea kutoka katika huduma, walitoa taarifa kwa Yesu (Marko 6:30). Ufuatiliaji ulikuwa ni sehemu muhimu katika mafunzo ya Yesu kwa wanafunzi wake. Haitoshi tu kukaimu majukumu; kiongozi mwenye ufanisi atatathmini utendaji wa wanafunzi. Kukaimu wajibu bila kuyafanyia tathmini kunasababisha matokeo hafifu.
► Soma Mathayo 17:14-21.
Howard Hendricks alifundisha kwamba kushindwa ni sehemu sana katika mwendelezo wa hatua za mafunzo. Wanafunzi waliuliza, “Kwa nini sisi tulishindwa kumtoa pepo kutoka kwa huyu kijana?” Yesu aliwajibu kwa kuwafundisha kuhusu imani. Ilikuwa ni vyema sana kushindwa katika hatua za mwanzo za huduma kuliko ingekuwa baada ya Yesu kurejea kwake mbinguni!
Ukaguzi wnye ufanisi wa wanafunzi na lazima uambatane na tathmini. Wakati mwanafunzi anaposhindwa kutimiza wajibu, hatimuliwi “kutoka kwenye kikundi.” Badala yake ni lazima tutafute sababu za kushindwa na tupange tena upya kwa ajili ya maboresho ya baadaye.
Yesu anaonyesha mpangilio huu katika Luka 9:
Luka 9:1-6, Yesu anawatuma nje wanafunzi kumi na wawili.
Luka 9:10, Walitoa taarifa kwake kuhusiana na safari yao.
Luka 9:37-43, Wanafunzi walishindwa kutoa pepo.
Luka 9:46-48, Yesu aliwafundisha kuhusu ukuu katika ufalme.
Luka 9:49-50, Yesu alimkemea Yohana kwa maamuzu mabaya katika huduma.
Luka 9:52, Yesu aliwatuma nje wanafunzi nje kwa ajli ya maandalizi ya kukitembelea kijiji katika Samaria.
Luka 9:54-55, Yesu alimkemea Yakobo na Yohana kwa ajiliya tukio jingine la maamuzi mabaya katika huduma.
Luka 10:1, Yesu alituma kundi kubwa zaidi la watu (Sabini) kwenda kuhudumu.
Yesu alibadilika kati ya mafundisho, kutuma wajumbe, na kufanya tathmini. Hakutaka kuwaacha wanafunzi wake hata pale ilipotokea kwamba wameshindwa. Badala yake alitumia kushindwa kwao huko kama nafasi ya kufundisha.
Paulo alifautilia mapangilio huo huo. Alimchagua Tito kuongoza kanisa katika visiwa vya Krete, na Timotheo kuwa mchungaji katika Efeso. Kisha aliandika nyaraka nyingi kwa ajili ya kuwapa mafunzo zaidi. Baada ya kupanda makanisa kwenye safari yake ya kwanza ya umishenari, Paulo alirudi tena kwenye safari ya pili kwa ajili ya kutoa miongozo kwa makanisa (Matendo 15:36).
Mfumo huu wa mafunzo ni wa ufanisi hata leo. Viongozi wengi wanatuma mhudumu mchanga bila ya usimamizi ulio endelevu au uwajibikaji – na wanashangaa wakati mhudumu anapokuwa ameshindwa. Hatupaswi kufikiri kwamba, “Nimefundisha somo, kwa hiyo watafanya vizuri.” Badala yake, usimamaizi ni mchakato ulio endelevu. Kama unataka kufundisha viongozi, ni lazima uwekeze muda wako katika kusimamia.
Howard Hendricks aliorodhesha hatua nne katika kufundisha wafanyakazi wapya
1. Kuelezea: Wafundishe maudhui. Yesu alifundisha ujumbe wa ufalme kwa wanafunzi wake.
2. Kuonyesha: Onyesha mfano wa huduma. Yesu alionyesha huduma kwa wanafunzi wake.
3. Kufanya majaribio: Huduma chini ya uangalizi wa moja kwa moja. Yesu aliwatuma wanafunzi kwena nje kwa ajili ya huduma kasha akatathmini uzoefu wao.
4. Kutenda: Huduma bila ya uangalizi wa moja kwa moja. Baada ya Pentekoste, wanafunzi walihudumu bila ya uangalizi wa Yesu.
► Unafanya nini katika kuwafundisha wanafunzi kwa ajili ya kuwa viongozi? Kwenye hatua ambazo tumeshajifunza, ni ipi unayoifanya kwa ufanisi? Ni hatua zipi zinahitaji kuboreshwa? Kama kikundi, jadili ni kwa jinsi mnaweza kuwa na ufanisi zaidi katika kuwa washauri wa viongozi wa baadaye. Majadiliano haya yanapaswa yaendelee hadi utakapopata mpango kazi wa kuwaendeleza viongozi katika mpangilio wa huduma yako.
Wanafunzi wetu ni Lazima Wazalishe Wanafunzi wengine
Yesu alisema kwa wanafunzi wake, “Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa” (Yohana 15:16). Yesu aliwafundisha wanafunzi wake kuzalisha wanafunzi wengine zaidi.
► Soma Mathayo 13:31-32.
Mfano wa Yesu wa punje ya haradali unaonyesha kwamba ufalme wa Mungu utakua kupita kiwango chake cha awali. Kama ambavyo mbegu ndogo sana ya haradali inavyoweza kuchipua na kuwa mti mkubwa kupita kiwango kilichotarajiwa, kanisa litaongezeka kupita kiwango ambacho mtu yeyote anaweza kutegemea. Kwenye Agano la Kale, ndege waliofanya makao yao kwenye mti huwakilisha ufalme mkuu yakiwemo mataifa (Danieli 4:12 na Ezekieli 31:6). Yesu aliahidi kwamba kwa jinsi ambavyo wanafunzi watazalisha, kanisa litaongezeka kupita viwango vyake vya mwanzo na litayafikia mataifa yote.
Dr. Robert Coleman aliandika kwamba tathmini ya mwisho ya huduma yetu inaonyesha kwamba huduma yetu inaendelea kuzalisha. “Mwisho wake hapa, sisi sote ni lazima tutathmini ni kwa jinsi gani maisha yetu yanaongezeka. Je, wale watu waliokabidhiwa dhamana kwa ajili yetu wanaweza wakachukuana na maono ya Agizo kuu la Mungu, na je, kwa upande mwingine wanaweza kuliambukiza kwa wanafunzi waaminifu ambao nao pia watawafundisha wanafunzi wengine? Muda unawadia mapema sana ambapo huduma yetu itakuwa mikononi mwao.”[4]
[1]Nukuu kutoka kwa Robert Coleman, The Master Plan of Evangelism. (Grand Rapids: Baker Book House, 1963)
[2]Mifano ni pamoja na 1 Wakorintho 11:1; Wafilipi 3:17; Wafilipi 4:9
Majukumu bila kuwa na mamlaka kunawalemaza wale unaowafundisha.
[4]Robert Coleman, “The Jesus Way to Win the World: Living the Great Commission Every Day.” Evangelical Theological Society, 2003
Angalia kwa kuzingatia: Maombi ya Kuhani Mkuu Yesu
Sehemu ya katikati ya maombi ya Kuhani mkuu Yesu yanaelekezwa kwa wanafunzi wake (Yohana 17:6-19). Maombi yake yanafundisha masomo ya thamani sana kuhusiana na njia ya Yesu ya kuwashauri wanafunzi.[1]
Yesu aliomba, “Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda.” Mara ishirini katika vitabu vya Injili, Yesu anawaambia wanafunzi wake kwamba “wajihadhari” na hatari. Aliwalinda na makosa. Tunapokuwa tunawafundisha wanafunzi, ni lazima tuwalinde kutokana na hatari za ulimwengu wao. Mafunzo yetu ni lazima yawe ya vitendo
► Ni hatari gani wanazopitia wanafunzi wa huduma wachanga katika mila yako? Kama mshauri, utawaandaje watoke katika hizi hatari?
Yesu aliomba, “Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu.” Yesu alijua kwamba wanafunzi watakutana na majaribu, lakini alikuwa na matumaini kwa wale aliokuwa amewafundisha. Ni lazima tujifunze kuwaamini viongozi wadogo tunaowafundisha. Hii inatuhitaji sisi kusalimisha mbinu ya “mamlaka ya kimabavu” ya uongozi na kuwaamini wengine wenye maamuzi muhimu.
Ajith Fernando anaandika kwamba kuna njia mbili ambazo viongozi wanaweza kuwaona wafuasi wao.
Viongozi wadhaifu wanaangalia madhaifu ya wafuasi wao.
Viongozi wenye ufanisi wanaangalia uwezo wa wafuasi wao wakati wakiendelea kufanyia kazi madhaifu yaliyopo. Viongozi wenye ufanisi huwaangalia wengine “kupitia macho ya matumaini.”
(3) Baada ya kuwa wameshafundishwa, tunawatuma wanafunzi wetu nje kwenda kuuhudumia ulimwengu.
Yesu aliomba, “Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni.” Baada ya Pentekoste, wanafunzi walianzisha huduma ya umisheni mkubwa ambao yesu alikuwa amewaandaa. Tunawashauri wanafunzi, ili nao baada ya hapo, wakaipeleke injili kwa ulimwengu wenye kuhitaji.
Yesu aliandika, “Mimi nimetukuzwa ndani yao.” Tunapokuwa tunawatuma nje wale tuliowafundisha, ni lazima tuhakikishe kwamba Yesu anapokea utukufu. Tunaweza kushawishika kujipatia utukufu kutoka kwa wale tuliowafundisha. Tuaweza kushawishika kuupokea utukufu kutoka na uwezo wetu wa kuwafundisha wanafunzi wengine. Badalayake, ni lazima tuhakikishe kwamba utukufu unamrudia Mungu mwenyewe.
[1]Nukuu kutoka kwa Ajith Fernando, Jesus Driven Ministry (Wheaton, Illinois: Crossway Books, 2002), 172-173
Kutumika: Thamani ya Timu za Huduma
Mfano wa Yesu unaonyesha umuhimu wa timu za huduma. Timu ya huduma kwa pamoja inahuska na kuwashauri watendakazi wasaidizi wadogo na kujenga mahusiano na wachungaji wengine. Tuliumbwa kwa ajili ya kuwa na ahusiano na watu wengine. Kwa nini timu za huduma ni muhimu sana?
Timu zinaleta Uwiano
Yesu alichagua watu kutoka katika kaida tofauti za maisha. Petro na Yohana walikuwa wapinzani wa mara kwa mara. Mathayo alikuwa akifanyia kazi zake Roma, Simoni aitwaye Zelote alitaka kuwafurumisha Wayahudi watoke Yudea. Watu hwah walikuwa wanatofautiana. Katika kuchagua wanafunzi wake, Yesu alichagua kundi la watu waliokuwa na tabia na mitazamo tofauti.
Ingawaje mara kwa mara tunaona matatizo ya kuwa na watu wanaopingana na watu wengine katika timu, hatupaswi kudharau faida za tabia na mitazamo hiyo inayotofautiana na wengine. Petro kama Mtume alikuwa mwepesi kufanya matangazo makubwa. Aliwekwa kwenye usawaziko na mitume waangalifu kama Thomasi na Andrea. Kanisa la mwanzo lilifaidika kutokana na kuwa na watu waliokuwa na tabia na mitazamo tofauti katika uongozi.
Viongozi wenye hekima hutafuta watu watakaounda timu kutoka katika kaida tofauti za maisha. Timu yenye nguvu inaleta watu wenye uwezo unaotofautiana kwenye uongozi wa kanisa. Mwanachama mmoja kwenye timu anaweza kuwa na ufahamu mzuri katika mambo ya fedha, mwingine anaweza kuwa na nguvu kwenye mambo ya mahusiano, mwingine anaweza kuwa na ufahamu wa kina wa kibiblia. Wote wakija kwa pamoja wanaleta uwiano wa uongozi kwa ajili ya kanisa.
Timu zinatoa Ushauri wenye Hekima
Alipokuwa akifundisha wanafunzi wake, Yesu alijua kwamba anajenga msingi kwa ajili ya kanisa.Baada ya Pentekoste, kutakuwepo na maamuzi mengi magumu yatakayolikumba kanisa la mwanzo. Yesu alijua kwamba wanafunzi watahitajiana kila mmoja na mwenzake wakati wa kufanya maamuzi haya.
Moja ya maamuzi ya mwanzo kabisa yaliyolikumba kanisa, “Ni kwa jinsi gani Mataifa watakaoamini watafanyika kuwa sehemu ya kanisa? Je, wanatakiwa kufuata vipengele vyote vya sheria ya Kiyahudi? Ingawaje hili linaweza kuonekana ni jambo rahisi kwetu, lilikuwa ni uamuzi mgumu. Hili halikuwa suala la upendeleo wa binafsi; sheria za chakula na kutahiriwa, pamoja na kutahiriwa kwenyewe viliwekwa kwenye msingi wa Agano la Kale. Maamuzi yalikuwa yawe na matokeo yenye madhara ya muda mrefu. Kwa leo, wewe na mimi tunaguswa na uamuzi huu; kama Baraza la Yerusalemu lingeamua vinginevyo, watu wa Mataifa wanaogeukia katika Ukristo wangepaswa wakubaliane na Sheria za Kiyahudi.
Matendo 15 iaonyesha jinsi kanisa la mwanzo lilivyotatua suala hili muhimu. Baada ya kusikia maoni mbalimbali, walifikia kwenye maamuzi. Kwenye barua yao kwenda kwa kanisa la Mataifa, mitume walitumia kauli nzuri ya hekima katika kuelezea maamuzi yaliyoanyika, “Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi” (Matendo 15:28). Roho Mtakatifu aliongoza katika kuwaleta viongozi wa kanisa mahali pamoja, akiruhusu washirikishane maoni yao, na kasha waliongoze kundi kwenye maamuzi sahihi.
Mwandishi wa Mithali anasisitiza thamani ya mchanganyiko wa mawazo wakati wa kufanya maamuzi.
Njia ya mpumbavu imenyoka machoni pake mwenyewe; Bali yeye aliye na hekima husikiliza shauri (Mithali 12:15).
Kwa wingi wa washauri huja wokovu (Mithali 11:14).
Maana kwa mashauri ya akili utafanya vita; Na kwa wingi wa washauri huja wokovu (Mithali 24:6).
Hii ni kanuni muhimu sana kwa viongozi wa kanisa. Kama hauko tayari kuwasikiliza wengine, kwenye Mitahali anasema wewe ni mpumbavu. Mpumbavu siku zote hujifikiria kwamba yeye yuko sahihi, lakini mtu mwenye hekima yuko tayari kuwasikiliza wengine.
Kama kusudi la timu ni kutoa ushauri wa busara, tnahitaji watu wenye kufikiria mawazo tofauti kuliko tunavyofikiria sisi. Ni lazima tuhakikishe kwamba katika kuchagua timu hatuangalii wale wenye kufanana na sisi tu. Hatuhitaji watu wa “Ndio tu.”
Timu zinaleta Kutiwa Moyo
Mhubiri anaelezea faida za timu. “Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao. Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua!” (Mhubiri 4:9-10).
Wakati kanisa lilipokuwa linapitia katika kipindi cha mateso, mitume walitiana moyo wenyewe kwa wenyewe. Luka analitumia neno “kwa umoja” kuelezea msaada wa pamoja miongoni mwa washiriki wa kanisa la mwanzo.
Mmishenari maarufu Hudson Taylor anaelezea hii kanuni. Taylor alikwenda China kwa shauku ya huduma, lakini katika muda mfupi sana alijikuta amekata tamaa. Hata baadhi ya wafadhili wake walisitisha kupeleka misaada ya kifedha. Wamishenari waliokuwa wameshajijenga vizuri kihuduma walikuwa wakimkosoa yeye. Hata serikali ya Uingereza ilipinga huduma yake. Mchumba wake alimwandikia akiwa akiwa Uingereza kwamba alikuwa hana uhakika kama anaweza kuolewa na mmishenari. Taylor alikuwa amekatishwa tamaa sana na alikuwa yuko tayari kurejea nyumbani.
Kwenye kipindi hicho, mmishenari mmoja mzee Mskoti aitwaye William Burns alikaa na Hudson Taylor miezi saba katika safari ya uinjilisti maeneo ya ndani ya China. Hawa watu wawili walisafiri pamoja, waliomba pamoja, na walihubiri pamoja. Wakati huo wa safari, Taylor aliingiwa tena na maono mapya kwa ajili ya China. John Pollock aliandika, “William Burns alimwokoa Hudson Taylor kutoka kwake mwenyewe.”
Hudson Taylor baadaye alianzisha shirika la kimisheni la China Inland Mission na alijulikana kama mmishenari maarufu sana wa kizazi cha sasa; William Burns ni kama hajulikani kabisa. Hata hivyo, William Burns anastahiki kupokea sehemu ya pongezi kwa ajili ya maelfu ya watu waliookoka kupitia shirika la China Inland Mission. Burns alimtia moyo Hudson Taylor wakati akiwa katika mazingira magumu sana. Timu zinaleta kutiwa moyo.
Timu zinaleta Uwajibikaji
Kila mmoja wetu ana kasoro. Tunaleta kwenye huduma zetu madhaifu yanayotokana na kaida za maisha ya familia zetu, yanayotokana na maisha yetu kabla ya kuwa Wakristo, na kutoka katika haiba zetu binafsi. Mambo haya yote huathiri huduma zetu.
Hatuwezi kuziona kasoro hizi ndani yetu sisi wenyewe, lakini wengine walioko kwenye timu wanaweza kutuonya katika maeneo haya ambayo yanaweza kuharibu huduma zetu Mwandishi wa Kitabu cha Waebrania aliwataka Wakristo “Kuhimizana katika kazi nzuri” (Waebrania 10:24). Neno kuhimizana lina wazo la kuchochea au kuleta msukumo kwa mtu. Wakati mwingine, hili halikubaliki. Hakuna hata mmoja wetu anayetaka kuchochewa au kusukumwa, uwajibikaji ni muhimu. Kila kiongozi wa Kikristo angalao mtu mmoja anayeweza kumwambia, “Kitendo hiki siyo cha hekima. Unapaswa ufikirie tena upya,”
Kutokea majumba makubwa ya utawa ya Zama za Kati na mikusanyiko ya madarasi ya Wesley hadi kwenye vikundi vya kisasa kama vile Watunza Ahadi, viongozi wa Kikristo wana msururu mrefu wa uwajibikaji wa mapokeo. Viongozi wa makanisa wa leo wanafaidika na uwajibikaji wa kila wiki. Hii inaweza kufanyika kati ya mtu mmoja na mwingine, kwenye vikundi vidogo, au kwa njia ya simu. Uwajibikaji huu unaweza kutuonya hatari ya kiroho kabla hatujaenda mbali sana.
Uwajibikaji mzuri unahitaji uaminifu kabisa kutoka kwa kila mhusika, na siri kabisa miongoni mwa wahusika. Unaweza ukapata mifano mingi ya maswali ya uwajibikaji. Orodha mojawapo ni hii inayohusisha maswali haya:
Katika wiki hili, je, umeutumia muda wako na Mungu mara kwa mara?
Katika wiki hili, je, umelegeza masharti ya uadilifu wako kwa njia yeyote?
Katika wiki hili, je, mawazo ya maisha yako yamekuwa masafi kabisa?
Katika wiki hili, je, umefanya dhambi yeyote ya uzinifu?
Katika wiki hili, je, umefanya jambo gani la maana kwa mke wako?
Katika wiki hili, je, umeishirikisha imani yako kwa mtu asiyeamini?
Je, umekuwa mwaminifu kwa kila jibu lililotolewa hapa?
Kuwajibika kwa timu ni muhimu katika nyakati za majaribu. Akimwandikia mchungaji kijana, Paulo anampa ushauri wa jinsi ya kujenga huduma ya kudumu. Paulo anamwonya Timotheo, “zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi” (2 Timotheo 2:22). Paulo alielewa kwamba maisha ya kiroho ya Timotheo yatakuwa na faida kama ataungana na watu wengi wanaomfuata Mungu ambao “wanamwita Bwana kutoka ndani ya mioyo iliyo safi.”
► Kama wewe ni mmojawapo katika timu ya huduma, shirikisha baadhi ya faida unazozipata kutoka katika timu yako. Kuna changamoto gani zinazopatikana kwa kuwa mmojawapo katika timu ya huduma?
Kufanya kazi na Timu
Yesu alitengeneza kikundi cha watu wenye sifa zinzotofautiana kabisa kwenye timu yenye umoja.. Yesu alichukuliana na zile tofauti zao na kuunda timu ambayo ingeweza kuongoza kanisa la mwanzo. Kanisa lilihitaji uongozi wa ujasiri wa Petro, na lilihitaji utulivu wa roho wa Filipo. Mojawapo ya changamoto kubwa za kiongozi ni kutengeneza kikundi cha wafuasi ili kuwa timu ya huduma.
Ajith Fernando, kiongozi wa kanisa kutoka Sri Lanka, anaelewa vizuri changamoto za kuijenga timu. Anaandika:
Labda masikitiko makubwa ya kanisa la kiinjili ni kwamba mara kwa mara hisia zinakuwa juu ya theolojia katika kupima jinsi tunavyoamua na kutenda. Mkristo anayeiamini Biblia husema, “Hata kama kuna hisia zozote kuhusiana na mtu huyu. nitamkubalii kwa sababu Mungu ananitaka nifanye hivyo. Na nitamwomba Mungu anipe neema ya kufanya kazi kwa kupatanishwa pamoja naye.” Theolojia yetu inasema kwamba jitihada hii ya kufanya kazi na mtu huyuitafanikiwa, ingawaje hisia zetu zinaweza zikatupa ujumbe mwingine. Theolojia yetu inatutuma kufanya kazi kwa bidii katika mahusuiano haya. Tunaomba kwa ajili ya mtu huo na kuhusu mahusiano yetu na yeye. Tutakutana naye mara kwa mara. Tutatafuta kumwonyesha upendo wa Kristo na kufanya yale yote tunayoweza kwa ajili ya ustawi wake wa binafsi. Tunatengeneza ndoto za kile ambacho mtu huyu anaweza kukifanikisha kupitia katika timu.[1]
1 Wakorintho inafundisha kwamba ndani ya mwili wa Kristo, hatuna haki ya kuwakataa watu kisa tu kwamba hatuwataki. Kama ukijenga kanisa, utakuwa na washirika ambao hutaweza kuwafurahia. Kama kiongozi wa Kikristo, ni lazima useme. “Hata niwe na hisia za aina gani, nitamkubali mtu huyu kwa sababu Mungu amemweka chini ya usimamizi wangu. Nitamwomba Mungu anipe neema ya kufanya kazi pamoja naye, na nitamwomba Mungu ambariki na kumpa mafanikio katika huduma.”
Wakati mmoja nilimwuliza mchungaji mtarajiwa, “Kwa nini unataka kuwa mchungaji?” Kijana huyu akajibu, “Nilipokuwa kwenye uwanja wa ndege nilimwona mtu mmoja akiwa amebeba mkoba wa mchungaji wake. Nami ninataka mtu wa kubeba mkoba wangu!”
Mtazamo wa Yesu ulikuwa tofauti kabisa! Huyu rafiki yangu alikuwa anataka ahudumiwe; Yesu alitaka ahudumie. “Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi” (Marko 10:45). Yesu anatuonyesha sis kwamba uongozi wa kweli unahusisha huduma. Yesu alijinyenyekesha mwenyewe, “akatwaa namna ya mtumwa” (Wafiipi 2:7).
► Soma Yohana 13:1-20.
Kuna maeneo mengi kutoka katika Vitabu vya Injili ambako tunaweza kujifunza aina ya kiongozi mtumishi, lakini moja ya mfano wenye nguvu sana ni maelezo yanayohusiana na Yesu kuwaosha miguu wanafunzi wake. Katika tukio hili, Yesu anaonyesha inamaanisha nini kuwa mtumishi.
Baadhi ya makanisa yanashikilia huduma ya “kuosha-miguu” kama tendo la kuigiza matendo ya Yesu wakati wa Chakula cha Mwisho. Hii inaweza ikawa ni huduma nzuri sana, lakini itakuwa na nguvu zaidi tukitambua kwamba Yesu hakufanya sherehe maalumu. Badala yake, alitimiza wajibu ambao ulipaswa ufanyike.
Kwa sababu mavumbi mengi kwenye barabara za Yerusalemu, ilikuwa ni kawaida kwa mtumishi aliyeajiriwa kuosha miguu ya wageni kwenye chakula rasmi cha jioni. Huu ulikuwa ni wajibu wa unyenyekevu waliokuwa wamepewa watumishi wa hadhi ya chini. Wakati Yesu alipojiunga na wanafunzi wake kwa ajili ya sherehe za Pasaka, hakukuwa na mtimishi katika kile chumba. Hakuna mwanafunzi hata mmoja ambaye angeweza kujitolea kuifanya kazi ya kuosha miguu; walikuwa wanategemea kupata vyeo vikubwa katika ufalme wa Yesu. Yesu akainama akaanza kuifanya kazi iliyokuwa ifanywe na mtumishi wa hadhi ya chini kabisa.
Tukio hili linaonyesha uelewa wa Yesu wa uongozi. Watu wengine huutafuta uongozi kwa ajili ya kupata madaraka na nguvu. Kusudi lao lilikuwa ni kuwa pale juu ya shirika. Yesu tayari alikuwa pale juu; alikuwa Mkuu wa wanafunzi. Lakini kwa hiari yake mwenyewe akajishusha hadi kwenye nafasi ya chini kabisa.
Hii ndiyo inayomaanisha kuwa kiongozi anayemfanania Kristo. Kiongozi anayemfanania Kristo anabeba wajibu ambazo wengine hawazipendi. Kiongozi anayemfanania Kristo huwahamasisha wengine siyo kwa kupitia uwezo wake wa kutoa maamrisho, lakini kupitia mfano wa huduma yake ya unyenyekevu.
[1]Mtu mmoja siku moja akasema, “Kipimo cha roho ya mtumishi ni ‘Ninafanyaje ninapokuwa nimetendewa kama mtumishi?’” Kiongozi anayefuata mfano wa Yesu hakwaziki anapotendewa kama mtumishi wa hadhi ya chini. Katika maisha yake yote, Yesu alitendewa kama mtumishi wa hadhi ya chini, lakini hakutaka kufanya mashambulizi kwa ajili ya hali hiyo. Ususahau kwamba Yesu aliiosha miguu ya Yuda pamoja na wanafunzi wengine. Je, unaweza kufikiria kumwosha mtu kwa unyenyekevu ambaye tayari ameshadhamiria kukusaliti?
Baada ya kuwa amemaliza kuosha miguu ya wanafunzi wake, Yesu aliwaambia hawa watu wanaotafuta nafasi za madaraka, “Nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo” (Yohana 13:15). Miaka thelathini baadaye, Simoni Petro atakuwa amekumbuka unyenyekevu wa Yesu alipoandika, “Jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana” (1 Petro 5:5). Kwa jinsi ile ile ambayo Yesu alijizungushia toweli ili awahudumie wanafunzi wake, sisi nasi tunapaswa tujizungushie unyenyekevu kwa ajili ya kuwahudumia watu wengine.
Kama viongozi wa Kikristo, tunaweza tukashawishika kutafuta madaraka kuliko kutafuta nafasi za kuwahudumia watu wengine. Yesu alionyesha kwamba uongozi ni huduma.
“Meza kuu za watu wa heshima imekuwa ni alama mbadala wa taulo na karai la kunawia kama ishara ya uongozi miongoni mwa watu wa Mungu. Ni wakati wa kurejesha upya utumishi wetu.”
- C. Gene Wilkes
Hitimisho: Umuhimu wa kuwashauri Wahudumu wengine wa Kikristo
Mwishoni mwa maisha yako, athari yako kama mshauri wa wahudumu wengine wa Kikristo inaweza kuwa urithi mkubwa wa huduma yako. Kama utakuwa mshauri wa wahudumu kumi na mbili tu wa Kikristo wakati wa huduma yako, matokeo ya utumishi wako itazidishwa na wale kumi na mbili pamoja na wale ambao wanashauriwa.
Kwa masikitiko, ingawaje viongozi wengi wa Kikristo wanajua umuhimu wa kushauri, viongozi wachache wanatumia muda wao kushauri wengine. Kwa nini tunapuuzia kipengele hiki cha huduma?
Sababu mojawapo ni gharama za kufanya ushauri. Kufanya ushauri kunachukua muda muhimu sana. Mara nyingi tunaamini kwamba muda unaotumika katika ushauri kwa viongozi vijana ungeweza kutumika vizuri zaidi kuhudumia vikundi vikubwa.
Sababu nyingine ni kukatishwa tamaa kunakoambatana na kushauri. Inaonekana kama inaleta mvuto kusema, “Ninafundisha kizazi kingine kijacho cha viongozi.” Ukweli halisi mara nyingi msisimko ni mdogo.
Mara nyingi, yumkini Yesu alikuwa anafikia mahali pa kukata tamaa kutokana na hatua za kuendelea polepole kwa wanafunzi wake. Baada ya miaka mitatu na Yesu, , Filipo aliuliza, “Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha” (Yohana 14:8). Majuma kadhaa baadaye Yesu akawalisha chakula watu elfu tano, wanafunzi walikabiliana na mkutano wa watu elfu nne. Wakaambizana, “Je! Ataweza wapi mtu kuwashibisha hawa mikate hapa nyikani?” (Marko 8:4).
Mtume Paulo alikutana na hali ya kupita kiasi inayofanana na hii ya kukataa tamaa. Yohana Marko aliachana naye kwenye safari yake ya kwanza ya umishenari (Matendo 13:13). Baada ya miezi kadhaa ya kumfundisha Dema, Paulo anaandika akiwa peke yake katika chumba cha gereza, “Dema aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa” (2 Timotheo 4:10).
Kushauri kuna gharama na kunaweza kukatisha tama, lakini ni sehemu muhimu sana ya kazi ya kiongozi.. Kila kiongozi wa Kikristo aliyekomaa anapaswa aweze kufanya ushauri kwa kutengeneza viongozi wa baadaye. Wakati huo huo, kila kiongozi wa Kikristo anahitaji awe na mshauri atakayetoa msaada nyakati za mapambano.
Howard Hendricks alisema kwamba kila mtu anahitaji watu watatu kwenye maisha yake:
1. Kila mtu anamhitaji Paulo, mshauri anayekupa changamoto ya kuendelea kukua.
2. Kila mtu anamhitaji Barnaba, rafiki anayekupenda vya kutosha atakayekuwa mkweli na wewe katika madhaifu yako.
3. Kila mtu anamhitaji Timotheo, kijana mdogo wa kumhudumia kama mwanafunzi na ushauri katika huduma.
► Malizia somo hili kwa kujiuliza:
“Paulo wangu ni nani?”
“Barnaba wangu ni nani?”
“Timotheo wangu ni nani?”
Kazi za Kufanya Somo la 3
(1) Orodhesha mifano minne ya wakati ambapo wanafunzi waliweza kushuhudia huduma ya Yesu. Angalia ni nini wanafunzi walijifunza kutokana na kumwangalia Yesu.
Mfano
Andiko
Fundisho kwa wanafunzi
Yesu akimponya kijana aliyepagawa na mapepo
Mathayo 17:14-21
Nguvu ya imani
(2) Orodhesha watu wawili au watatu unaoweza kuwa mshauri kwa kuwaanda kwa ajili ya huduma ya baadaye. Andika ibara fupi ambayo utajibu maswali mawili yafuatayo:
Ni sifa gani ninazozitaka kuona kwa mtu ambaye namshauri?
Ninataka kuona Mungu akikamilisha nini kwa mtu ambaye namshauri? (Kuwa maalumu)
Anza kuchukua hatua za ushauri kwa watu uliowataja kwa majina. Mwombe Mungu akuonyeshe jinsi ya kuwaandaa kwa ajili nafasi za huduma.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.