Maisha Na Huduma Ya Yesu
Maisha Na Huduma Ya Yesu
Audio Course Purchase

Search Course

Type at least 3 characters to search

Search through all lessons and sections in this course

Searching...

No results found

No matches for ""

Try different keywords or check your spelling

results found

Lesson 1: Maandalizi ya Huduma

28 min read

by Randall McElwain


Ramani ya Palestina wakati wa Yesu

Ramani ya Palestina wakati wa Yesu

Tafadhali fanya marejeo kwenye ramani hii katika mwendelezo wa kozi nzima.[1]

 

[1] “Map of Israel” was created by SGC with open data from NED, SRTM, NASA, and Bible Geocoding

(CC BY 4.0), available from https://www.flickr.com/photos/sgc-library/52344178339, public domain (CC0)

Malengo ya Somo

Kufikia mwisho wa somo hili, kila mwanafunzi atapaswa:

(1) Atambue kwamba Yesu ndiye kielelezo cha kuigwa kwa ajili ya huduma.

(2) Akubaliane na uwezo wa Mungu wa kuwaanda wale anaowachagua kwa ajili ya huduma.

(3) Kujisalimisha kwa ajili ya wito wa Mungu aliokuitia.

(4) Kufuata nyayo za Kristo za ushindi dhidi ya majaribu.

Maandalizi ya Somo

Soma Mathayo 1-4, Luka 1-3, na Yohana 1.

Kanuni ya Huduma

Mungu huwaanda wale anaowaita kwa ajili ya huduma ile aliyowaitia.

Utangulizi

Katika Maisha na Huduma ya Yesu Kristo, tutajifunza kuhusu Yesu kama kielelezo chetu cha kuigwa kwa wakati wa leo. Yesu alisema. “Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo” (Yohana 13:15). Maisha ya Yesu hapa duniani yalikuwa ni kielelezo kwa ajili ya wafuasi wake.

Paulo aliielewa kanuni hii. Aliposikia mgogoro kati ya Wakristo na Wafilipi, Paulo aliwapeleka kwenye mfano wa Yesu. “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu” (Wafilipi 2:5).[1] Paulo alijua kwamba kama Wakristo watafuata mfano wa Yesu, unyenyekevu wao utatatua migogoro ndani ya kanisa.

Katika safari yake ya kuja Afrika, Mwandishi wa Kiyahudi, Daudi Plotz, alikwama kwenye uwanja wa ndege wa Malawi. Akiwa pale alikutana na mchungaji wa Kiafrika ambaye alimpeleka nyumbani kwake, akamtunza kwa siku mbili, na akamshuhudia kuhusu Yesu Masihi. Daudi Plotz baadaye aliandika.”Siamini katika lolote ambalo huyu baba anaamini, lakini ninaogopa kwa msimamo wake. Anajisikia jinsi Kristo anavyotembea ndani yake, ndiyo maana alimchukua mgeni asiyemjua, akamhudumia kwa malazi na chakula, na akamvisha.” Huyu mchungaji wa Kiafrika alielewa kwamba tumeitwa kwa ajili ya kuwa kilelezo cha Yesu.

Kozi hii siyo utafiti wa kina wa maisha ya Yesu. Badala yake, tutajielekeza katika vipengele vinavyohusiana na maisha ya Yesu ambavyo vinatoa kielelezo kwa ajili ya huduma zetu za leo. Tutajifunza jinsi ya kuunda huduma zetu kwa kutumia mfano wa Yesu.

Katika somo hili la kwanza, tutaona maandalizi ya Yesu kwa ajili ya huduma. Hii inaonyesha kanuni kwamba Mungu humwandaa kila mtu anayemwita kwa ajili ya huduma ambazo wameitiwa.


[1]Toleo la Biblia ya Kiswahili (SUBV)

Mungu aliandaa Msingi wa Mwanzo wa familia ya Mtumishi wake.

► Fikiria msingi wa mwanzo wa familia yako na maisha ya awali. Ni kwa jinsi gani Mungu ameutumia mwanzo wako kukuandaa kwa huduma?

Mtiririko wa vizazi katika Vitabu va Injili unaonyesha kwamba Mungu mwenye enzi aliandaa njia kwa ajili ya watu wake karne nyingi kabla Yesu hajazaliwa. Kitambo kirefu kabla ya Yesu kuzaliwa, Mungu aliandaa njia ya kuja kwake.

Mtiririko wa vizazi unajibu swali hili, “Je! Yesu ni nani?” Mtiririko huu wa vizazi unaonyesha umuhimu wa Abrahamu na Daudi. Abrahamu ni muhimu katika ukoo wa Yesu kwa sababu Mungu alimwahidi Abraham kwamba, “katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa” (Mwanzo 12:3). Ahadi hii ilitimia kupitia Yesu wa Nazarethi.

Daudi ni muhimu katika mtiririko wa vizazi kwa sababu Mungu alimwahidi Daudi kwamba, “Nacho kiti chako kitafanywa imara milele” (2 Samweli 7:16). Wakati wa kuzaliwa kwa Yesu, ilikuwa ni zaidi ya miaka 500 imepita tangu utawala wa Daudi ulipokuwa madarakani. Mathayo na Luka wanaonyesha kwamba Yesu alikuwa ni mkamilishaji wa ahadi iliyokuwa imetolewa kwa Daudi.

Yesu alikuwa ni Mwana wa Daudi (Mathayo 1:1-17)

Katika Agano Jipya ya Kiyunani, maneno mawili ya mwanzo ya kitabu cha Mathayo ni biblios genesis, maneno ambayo yangekumbusha wasomaji wa mwanzo wa Mathayo juu ya kitabu cha Mwanzo (Mwanzo 2:4; 5:1). Kama vile kitabu cha Mwanzo kinavyoelezea ukuu wa Mungu dhidi ya uumbaji, kitabu cha Mathayo kinaelzea ukuu wa Mungu dhidi ya historia. Mtiririko wa vizazi katika kitabu cha Mathayo unaonyesha kwamba historia yote ya Israeli ilielekezwa kwenye kuzaliwa kwa Masihi.

Mtiririko wa vizazi katika kitabu cha Mathayo unaonyesha makundi matatu ya watu kumi na nne. Hili lilikuwa ni jambo la kawaida kwa Wayahudi la kusaidia kukumbuka. Makundi mbalimbali ya kawaida ilisaidia wanafunzi kukariri orodha ndefu za majina. Wasomaji wa mtiririko wa vizazi katika kitabu cha Mathayo wanapaswa watambue kwamba orodha hii haikumhusisha kila babu aliyekuweko kati ya Abrahamu na Yusufu. Neno la Mathayo “akamzaa” linaweza kurejewa kwa babu yeyote. Mtiririko wa vizazi wa Wayahudi mara nyingi uliepuka kutaja baadhi ya vizazi vingine. Mathayo anajielekeza kwenye makundi muhimu ya vizazi vya Yesu na kuacha majina mengine.

Kwa kuwa Mathayo aliacha baadhi ya vizazi vingine, majina aliyoingiza kipekee ni ya kuvutia sana. Mathayo aliyachagua majina hayo kwa kusudio maalumu. Kwa mfano, Mathayo anaorodhesha wanawake wanne. Hili lilikuwa siyo jambo la kawaida kwenye mtiririko wa vizazi vya Wayahudi. Majina haya kila moja lilikuwa na hoja ya misingi ya huko nyuma. Rahabu na Ruthi walikuwa wageni. Tamari, Rahabu, na Bathisheba walihusishwa katika aibu ya kashfa ya uzinzi.

Hali kadhalika, baadhi ya wanaume katika orodha hiyo walikuwa wamepatikana na mambo ya aibu. Yuda alimtendea Tamari mambo ya aibu. Kizazi cha Yehokonia kiliondolewa katika uhalali wa kuwa katika kiti cha ufalme cha Israeli (Mathayo 1:12; Yeremia 22:30). Kinachoonekana zaidi, Mathayo anamtambua Daudi siyo katika yale mambo makubwa aliyofanikisha, lakini kama “Baba wa Sulemani kutoka kwa mke wa Uria.”

Majina haya yanamtambulisha Yesu katika ubinadamu wa dhambi. Mungu alimleta Mtoto wake duniani siyo kutoka katika familia ambayo haikuwahi kuwa na doa, bali kama mzaliwa katika ukoo wa watenda dhambi wa kawaida. Wayahudi walidhihaki kuzaliwa kwa Yesu kusikokuwa na heshima, na wakamkataa kama asiyestahili (Yohana 8:41, 48). Mathayo anaonyesha, “Kama Masihi anaweza kuzaliwa kutoka katika kizazi cha ukoo wa aina hii, anaweza akawa mkombozi kwa watu wa aina zote, hata wale ambao wanaonekana hawastahili.”[1]

► Katika mila zetu, ni vipengele gani vya mambo ya nyuma ya mtu vinavyoweza kutufanya tumfikirie kama mtu aliye na uwezo mdogo?

Mara nyingi Mungu huwaita watu kutoka katika mazingira mbalimbali ya nyuma yasiyotegemewa kwa ajili ya huduma yake. Hakuna mtu ambaye ataachwa kutumiwa kutokana na historia ya mambo yake ya nyuma. Vipengele vya mambo ya nyuma vinavyotufanya sisi tumwone mtu kama mwenye uwezo mdogo, havijalishi kwa Mungu.

Yesu alikuwa Mwana wa Adamu (Luka 3:23-38)

Mathayo anafuatilia asili ya mtiririko wa vizazi vya Mfalme wa Wayahudi hadi Abrahamu. Luka anafuatilia asili ya mtiririko wa vizazi vya Yesu hadi Adamu. Hii inakubaliana namkazo wa Luka juu ya Yesu kama “Mwana wa Mtu.” Mtiririko wa vizazi wa Luka unawekea mkazo kwenye ubinadamu wa Yesu. Luka anauweka mtiririko wa vizazi kabla ya kujaribiwa kwa Yesu. Hii inamkumbusha msomaji kwamba Yesu, Adamu wa pili, alifanikiwa mahali ambapo Adamu wa kwanza alishindwa.


[1]Craig L. Blomberg, Jesus and the Gospels. (Nashville: Broadman & Holman, 1997), 199

Angalia kwa kuzingatia: Mtiririko wa vizazi vya Mathayo na Luka

Kitabu cha Mathayo 1 na Luka 3 vinatoa mtiririko wa vizazi vya Yesu unaotofautiana. Mathayo anauchuua mtiririko wake kutoka kwa Abrahamu kuja kwa Mfalme Sulemani hadi kwa Yusufu. Luka anatoa mtiririko wake kutoka kwa Yusufu kuja kwa Nathani (mtoto mwingine wa Daudi) hadi kwa Adamu.

Mtiririko wa vizazi unafanana kati ya Abrahamu na Daudi. Hata hivyo, kati ya Yusufu na Daudi, vizazi viwili vinachukua mikondo mingine. Uwezekano wa maelezo ya tofauti hii ni kwamba Mathayo anachukua kumbukumbu za mtiririko wa ukoo wa Yusufu, na Luka anachukua kumbukumbu za mtiririko wa ukoo wa Mariamu.[1]

Ukoo wa Yusufu katika kitabu cha Mathayo ni wa mtiririko wa vizazi ya “kifalme” ukianzia nyuma kwa mfalme Sulemani. Hii inakubaliana na dhamira ya Mathayo ya Yesu kama Mfalme. Huu ni ukoo halali wa kisheria wa Yesu – ambao ni lazima utoke kwa Yusufu.

Ukoo wa Mariamu katika kitabu cha Luka ni wa mtiririko wa vizazi vya “kimwli” ukianzia nyuma kwa Nathani, mtoto wa Daudi. Mtiririko huu wa uzazi unakubaliana na dhamira ya Luka ya Yesu kuwa “Mwana wa Mtu.” Ili kuonyesha hili, Luka anafuatilia mtiririko wa vizazi kimwili wa Yesu kupitia Mariamu. Na bado anaanza na neno “Mwana wa Yusufu” kwa sababu mtiririko wa vizazi wa Wayahudi ulitumia wanaume, hata pale ilipotakiwa kufuatilia mtiririko wa nasaba za wanawake.

Nasaba ya Mariamu inaonyesha muunganiko wa damu kutoka kwa Daudi. Nasaba ya Yusufu inaonyesha haki za kifalme kupitia kwa Sulemani.


[1]Kwa ufafanuzi mwingine wa ziada tembelea, http://www.gotquestions.org/Jesus-genealogy.html, iliyopatikana March 22, 2021.

Mungu aliandaa Msingi wa Mwanzo wa familia ya Mtumishi wake (Inaendelea)

Yesu alikuwa Mwana wa Mungu (Yohana 1:1-18)

Injili ya Yohana inaanza na mtiririko wa vizazi vya kiungu; Yesu alikuwa Mwana wa Mungu. “Maisha ya Yesu hayakuanza mara tu alipozaliwa.” Alikuja duniani kutoka katika maisha ya roho kabla ya mtu kuzaliwa ili kutimiza kazi maalumu. ”[1]

Katika Agano la Kale, utukufu wa Mungu wa shekinah ulijaa miongoni mwa Israeli katika hema ya kuabudia. Kwa sasa, utukufu wa Mungu unakaa miongoni mwetu katika mtu Yesu Kristo (Yohana 1:14). Utukufu wa kiungu wa Mungu sasa uliachiliwa kupitia mfumo wa kibinadamu.

Neno lilikuwa la milele: “Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu” (Yohana 1:1). Baba na Mwana waliishi katika ushirka wa milele.[2] Kwa nini yesu alikuja katika dunia yetu? Kumdhihirisha Baba. Hakuna mtu aliyewahi kumwona Baba, lakini Yesu “alimfanya afahamike” kwetu (Yohana 1:18 ). Tunapomwona Yesu, tunamwona Baba.

Kwa sasa, watu wengi wanamwona Yesu kama rafiki mwenye upendo, na Baba kama hakimu mkali. Hata hivyo, kitabu cha Yohana 1 kinaonyesha kwamba tabia ya Yesu ni sawa na tabia ya Baba. Tunapomwona Yesu, tumemwona Baba.


[1]J. Dwight Pentecost, The Words and Works of Jesus Christ. (Grand Rapids: Zondervan, 1981), 28
[2]Yohana 1:3 anakataa madai ya mashahidi wa Yehova kwamba Yesu alikuwa kiume aliyeumbwa. Yesu alikuwepo wakati wa uumbaji. “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.”

Mungu Alimwandaa Mtumishi wake kwa kuzaliwa Kimiujiza

Yesu alikuwa amezaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi takribani mwaka wa 5 B.C.[1] Yusufu alikuwa amesafiri hadi Bethlehemu ili kujiandikisha kwa ajili ya kuhesabiwa. Kusudi la zoezi la kuhesabiwa ilikuwa ni kuweka kumbukumbu kwa ajili ya kulipa kodi kwa kila jimbo lililokuwa chini ya mamlaka ya Kirumi.

Utaratibu wa kawaida wa Kirumi wa kuandikisha watu katika miji ulikuwa ni kuwaandikishia pale wanapoishi na kufanyia kazi. Hata hivyo, ili kuimarisha Amani na jamii ya Kiyahudi ambayo ilikuwa wepesi sana kwao kuasi, utawala wa Kirumi uliruhusu jimbo la Yudea kufuata taratibu za uandikishaji za Kiyahudi katika mji wa kabila la mababu zao. Matokeo yake, Yusufu na Mariamu iliwabidi wasafiri kilomita 100 kutoka Nazarethi hadi Bethlehemu. Ingawaje ni mwanaume kiongozi tu wa nyumba aliyekuwa anahitajika kujiandikisha, Yusufu aliambatana na mkewe katika safari hiyo hadi Bethlehemu. Inawezekana kwmba Yusufu hakutaka kumwacha Mariamu nyuma wakati kukiwepo na minong’ono ya majirani zake katika kitongoji chake cha Nazarethi.

Kwa upande mwingine, suala la kuhesabiwa kwa ajili ya kulipa kodi lilikuwa ni wazo la utawala wa Kirumi. Hata hivyo, Mungu alikuwa anaiandaa njia kwa ajili ya mtumishi wake. Mungu hufanya kazi kupitia matukio ya kidunia ili kutimiza kusudi lake. Mungu kwa mamlaka yake alisababisha mfalme wa kipagani “kuchagua” kuwepo na zoezi la kuhesabiwa kwa Wayahudi ili kutimiza kusudi la Mungu. “Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa Bwana; Kama mifereji ya maji huugeuza po pote apendapo” (Mithali 21:1). Kama watendakazi wa ufalme wa Mungu, itupe ujasiri na uhakikakwamba Mungu hutimiza kusudi lake hata pale inapotokea kwamba watu waovu wako madarakani.

Hesabu hii kwa ajili ya kodi ni mfano mmoja katika mifano mingi inayoonyesha jinsi Mungu alivyokuwa ameuandaa ulimwengu kwa ajili ya kuzaliwa kwa Yesu. Mungu alifanya kazi nyuma ya misingi ya kikabila ya Mfalme wa Kiyunani, nyuma ya taratibu za kisheria za Utawala wa Kirumi, na nyuma ya kanuni za kidini za imani ya Wayahudi kuuandaa ulimwengu kwa ajili ya kuzaliwa kwa Masihi. Ili uweze kujifunze misingi hio, tafadhali rejea kwenye somo la kwanza la kozi ya Shepherds Global Classroom, Kuchambua Agano Jipya.

Kutembelewa na Wachungaji wa Kondoo (Luka 2:8-20)

Watu wa kwanza kabisa kupokea taarifa za kuzaliwa kwa Yesu walikuwa wachungaji wa kondoo nje ya Bethlehemu. Hili ni la kutazamwa sana kwani wachungaji wa kondoo walikuwa ni watu wa kutengwa na Wayahudi wengi wa karne ya kwanza. Wachungaji wa kondoo walikuwa wakitazamwa kama watu wa hali ya chini sana katika jamii kiasi kwamba hata ushahidi wao ulikuwa haukubaliki katika mahakama za Kiyahudi. Kwa kuwaangalia hawaa wachngaji wa kondoo, Luka anamaanisha kwamba, “kama wachungaji wa kondoo wameweza kukaribishwa, basi kila mtu anakaribishwa kwenye ufalme wa Mungu!” Malaika alisema kwa Wachungaji wa kondoo, “ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote” (Luka 2:10).

Injili haiko tu kwa ajili ya taifa moja (la Israeli) au kwa ajili ya jamii ya daraja fulani tu; injili ni kwa ajili ya watu wote. Dhamira hii inaonekana katika Injili yote ya Luka. Luka anatoa angalizo maalumu kuhusiana na huduma ya Yesu kwa wanawake, Wasamaria, na kwa watu waliotengwa na jamii kama Zakayo.

Kutembelewa na Mamajusi (Mathayo 2:1-12)

Injili ya Mathayo ilikuwa hapo kwanza imeelekezwa kwa wasikilizaji wa Kiyahudi. Wakati ujumbe wa Luka ulilenga kwa watu wote, ujumbe wa Mathayo ulilenga kwanza kwenye mambo ya ufalme wa Mbinguni. Badala ya wachungaji wa kondoo, Mathayo anaonyesha kukaribishwa kwa watu wenye hekima na akili, mamajusi. Ujio huu ulitokea baada ya familia ya Yesu kuhamia kwenye makazi yao ya kudumu, yumkini miezi michache baada ya kuzaliwa Yesu (Mathayo 2:11). Hili linaungwa mkono na tukio la amri ya mfalme Herode ya kutaka wauawe watoto wachanga wote waliokuwa na umri chini ya miaka miwili.

Mamajusi walikuwa wamefunzwa kusoma mambo ya anga wakichuguza mienendo ya nyota isiyokuwa ya kawaida. Wakati wakiwa katika safari yao ngumu na ya hatari, walitembea umbali mrefu kuchunguza alama ya ajabu waliyokuwa wameiona angani.

Mamajusi walikwenda kwanza Yerusalemu, mahali ambapo ndipo palipotakiwa papatikane mfalme. Wakati habari za kuzaliwa mfalme mbadala zilipomfikia Herode, “alifadhaika, na Yerusalemu (yote) pia pamoja naye” (Mathayo 2:3). Neno “Yerusalemu (yote)” linaashiria kukataliwa baadaye kwa Yesu na viongozi wa kidini wa Yerusalemu.

Kutembelewa na Mamajusi kulikuwa ni ishara ya kwanza ya uwakilishwaji wa Masihi kwa Wamataifa. Ukilinganisha na wale waliokuwa Yerusalemu ambao walikuwa “wamepata shida” kwa kuiona ile alama, Mamajusi waliitikia kwa imani. Yesu alikuja kama mfalme kwa mataifa yote, na siyo mfalme kwa ajili ya Waisraeli tu.

Mathayo hatoi taarifa ni mamajusi wangapi walikwenda kumsujudia Yesu. Mila ya “Watu watatu wenye hekima” inahusiana na zawadi tatu zilizotajwa katika Mathayo 2:11. Kila zawadi ikiwakilisha kipengele kimoja katika huduma ya Yesu.

  • Dhahabu ni zawadi kwa ajili ya malme. Hata hivyo, Yesu hatainukia kutawala kutoka kwenye kiti cha enzi bali kutokea msalabani.

  • Uvumba ni zawadi kwa ajili ya mchungaji. Uvumba ulikuwa unatumika kama manukato. Yesu alikuja kama mchungaji aliyewezesha watu wote waweze kuingia mbele ya uwepo wa Mungu.

  • Manemane ilitumika kama dawa ya kutia kwenye maiti ili isioze.Yesu alizaliwa ili afe kwa ajili ya wanadamu wote.


[1]Kalenda ya Gregori ilikuwa bado haijaanziswa hadi mwaka 1582. Kalenda hiyo iko katika mfumo wa takribani na siyo kwa uhakika. Herode mkuu alifariki takribani mwaka wa 4 K.K. Kwa kuzingatia hili, kuzaliwa kwa Yesu ilikuwa ni takribani kati ya mwaka 5-6 K.K.

Mungu alimlinda Mtumishi wake.

Kabla ya kuzaliwa kwa Yesu, malaika alizungumza na Yusufu katika ndoto ili kumfunulia mipango yake. Baada ya kutembelewa na mamajusi, malaika alimwonya Yusufu akimbilie Misri. Familia hii ilikaa Misri hadi baada ya kifo cha Herode (takribani mwaka wa 4 K.K.)

Kwa namna nyingi Herode Mkuu alikuwa mtawala mzuri. Aliwaheshimu Wayahudi, hata kwa kufuata sheria za vyakula za Kiyahudi nje ya utukufu wake aliokuwa nao kwa wale aliokuwa anawatawala. Alianza kulifanyia ukarabati wa hekalu ambao uliendelea katika kipindi chote cha maisha ya Yesu. Wakati wa njaa ya mwaka wa 5 K.K., alitumia fedha zake mwenyewe kununulia chakula kwa ajili ya walioathirika na njaa ile katika Yudea.

Hata hivyo, Herode alikumbwa na uwazimu usiotibika. Alimwua mmojawapo wa wake zake, Mariamne, na mama yake Alexandra, alipohisi kwamba walikuwa na njama za kumhujumu. Herde alikuwa na watoto watatu waliouawa kikatili walipofikia umri wa kuonekana kwamba wanaanza kuwa tishio kwa utawala wake. Kwa mwanamume aliyefikwa na uwazimu kama Herode, kuchinjwa kwa watoto wachanga Bethlehemu kulikuwa siyo jambo la kushangaza. Mauaji wa dazeni za watoto wachanga kwa ajili ya kulinda nafasi yake ya ufalme lilikuwa ni jambo la usumbufu mdogo sana kwake.

Ukatili wa Herode uliendelea hadi wakati wa kifo chake. Alipokuwa anakaribia kifo chake, Herode aliamuru kwamba raia wote mashuhuri katika Yerusalemu wakamatwe wauawe wakati wa kufa kwake. Aliamini kwamba kwa kufanya hivyo, siku ya kufa kwake ingekuwa siku ya maombolezo makuu. (Badala yake, mjane wake na Herode aliwafungulia wafungwa wote, ikasababisha siku ile iwe ni ya kusherehekewa sana katika nchi yote ya Palestina.)

Baada ya Herode kufa, eneo lake la utawala liligawanywa kwa watoto wake watatu wa kiume. Antipasi alipewa eneo la Galilaya na Perea. Filipo alipewa kutawala eneo la Kaskazini Mashariki mwa Palestina; Arkelau aliteuliwa kuwa mtawala wa Yudea, Idumea na Usamaria. Wanahistoria wa zamani wanasema kwamba Arkelau alikuwa na madhaifu yote ya baba yake na hakuchukua tabia zozote nzuri za baba yake. Alichukiwa na Wayahudi na akaondolewa katika madaraka yake mwaka wa 6 B.K. kutokana na malalamiko ya Wayahudi kwa Kaisari, Baada ya hili, Yudea ilitawaliwa na mawakili wa Kirumi kama Pointio Pilato

Baada ya kifo cha Herode, malaika kwa mara nyingine alimjia tena Yusufu katika ndoto kumpa maelekezo ya kurejea Israeli. Hata hivyo, kwa kuwa Arkelau alikuwa ni mtu wa hatari kama Herode Mkuu, Yusufu aliipeleka familia yake Nazarethi kuliko kurejea tena Yerusalemu.

► Akiwa mtoto mdogo, Yohana Wesley aliokolewa kimiujiza katika nyumba yao iliyokuwa inateketea kwa moto. Aliamini kwamba Mungu alikuwa amemlinda kwa kusudi maalumu. Wesley alijitafakari mwenyewe kama “kijiti kiwakacho kilichonyakuliwa motoni.” Waalike wanafunzi wa darasa lako mshirikishane visa ambavyo Mungu ameweza kuwalinda kwa ajili ya huduma – aidha kupitia ulinzi wa miujiza au kupitia majaliwa ya Mungu.

Angalia kwa kuzingatia: Mathayo 2:23

Zaidi ya Injili nyingine zote, Mathayo anaonyesha kwamba huduma ya Yesu ilitimiza unabii zilizokuwa katika Agano la Kale. Akiwaandikia wasikilizaji wake wa Kiyahudi, Mathayo anaonyesha kwamba Yesu alikuwa ndiye Masihi aliyekuwa ametabiriwa:

  • Kuzaliwa kwa Yesu na bikira (Mathayo 1:22-23) ilitimizwa kutoka Isaya 7:14.

  • Kuzaliwa kwa Yesu Bethlehemu (Mathayo 2:5-6) ilitimizwa kutoka Mika 5:2.

  • Kukimbilia Misri (Mathayo 2:14-15) ilitimizwa katika Hosea 11:1.

  • Kuuawa kwa watoto wachanga Bethlehemu (Mathayo 2:16-18) ilitimizwa kutoka Yeremia 31:15.

  • Kuingia Yerusalemu (Mathayo 21:1-5) ilitimizwa kutoka Zakaria 9:9.

Mojawapo ya mifano migumu kabisa ya kutimizwa kwa unabii uko katika Mathayo 2:23. Mathayo anaandika, ”Akaenda, akakaa katika mji ulioitwa Nazareti; ili litimie neno lililonenwa na manabii, Ataitwa Mnazorayo.”

Tatizo ni kwamba hakuna kumbukumbu yeyote kutoka kwenye unabii wa Agano la Kale unaosema kwamba Masihi ataitwa “Mnazorayo.” Kuna mawazo ya aina mbili nyuma ya hii aya:

1. Kwa wakati ule wa Yesu, Nazarethi kilikuwa ni kijji ambacho kilikuwa hakina uthamani wowote. (Yohana 1:46). Wayahudi walitegemea Masihi angetoka Yudea na siyo katika mkoa wa kibiashara wa Galilayan(Yohana 7:41, 52). Ukweli kwamba Yesu alitoka katika eneo lililokuwa limedharaulika kama Nazarethi ilikamilisha unabii kama wa Isaya 49:7 na 53:3.

2. Isaya 11:1 alitabiri kwamba Masihi takuwa “tawi.” Neno la Kiyunani la tawi (Netzer) linatamkika kama sawa na “Nazarethi.” Wayahudi wasomaji wa kitabu cha Matayo wangelitambua huu ulimbuaji wa maneno.

Mungu aliandaa njia kwa Mtumishi kwa njia ya Mtangulizi wake

Yohana Mbatizaji alikuwa binamu wa Yesu. Maelezo kuhusiana na Yohana yanaanzia wakati baba yake Zakaria alipokuwa anafukiza uvumba kwa niaba ya taifa, mojawapo ya jukumu lililokuwa linaheshimika sana kwa kuhani (Luka 1:9).

Wakati Zakaria alipokuwa akifanya jukumu hili takatifu, malaika alitokea upande wa kulia wa madhabahu wa kufukizia uvumba. Kwa utamaduni wa Kiyahudi hapa ndipo Mungu alipokuwa anasimama wakati wa kutoa sadaka. Malaika Gabrieli alimwambia Zakaria kwamba maombi yake kwa ajili ya kupata mtoto yamejibiwa.

Kwa kuwa Elizabethi alishapitiliza umri wake wa kuweza kuzaa, Zakaria aliionea shaka ahadi ya malaika. Kutokana na kutoamini kwake, malaika alimfanya awe bubu hadi pale alipozaliwa Yohana. Kama kuhani na mwanafunzi wa maandiko, Zakaria alizijua habari za Hana na Raheli na alipaswa kuamini ahadi ya Mungu kwamba kwa miujiza angelilifungua tumbo la uzazi la Elizabethi.

Miaka thelathini baadaye, Yohana alianza huduma yake. Kuliko atumike kama kuhani katika Yerusalemu, Yahana alitumika kama nabii katika maeneo ya jangwa la Yudea. Yohana alikuwa ametumwa kama mtangulizi wa Masihi. Yohana alipokuwa akihubiri, watu walikuwa wakiulizana, “Je! Yohana ndiye yule Masihi aliyeahidiwa?” Yohana alijibu, “yuaja mtu mwenye nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya viatu vyake” (Luka 3:16). Mojawapo ya jukumu la chini sana la mtumwa lilikuwa ni kushughulika na viatu vya bwana wake, lakini Yohana alisema, “anayekuja yuko juu sana kuliko mimi, kiasi kwamba sisitahili kwake hata kwa jukumu hili la chini.” Yohana anawakilisha aina ya utumishi wa unyenyekevu.

Katika maandiko yote, Mungu hutumia watu kuandaa njia kwa ajili ya mtu mwingine. Angalia mfano wa Barnaba na Paulo. Wakati Sauli alipokuwa akiwauawa Wakristo, tayari Barnaba alishakuwa kiongozi wa kanisa anayeheshimika. Barnaba alimwamini Paulo wakati ambapo Wakristo wengine wachache wangeweza kumwamini huyu muuaji na mtesaji wa kanisa.

Wakati walipoanza safari ya kwanza ya kimishenari, Kitabu cha Matendo kinairejea timu hii kama ya Barnaba na Sauli” (Matendo 13:2). Muda siyo mrefu, wakatambulika kama Paulo na Barnaba” (Matendo 13:43 na kuendelea). Barnaba alikuwa “mtangulizi” lakini alikuwa amehiari kumwachia Paulo uongozi.

Wakati mwingine jukumu lako linaweza kuwa ni lile la Yohana Mbatizaji au la Barnaba, la kuandaa njia kwa ajili ya mtu mwingine. Uko tayari kwa hiari yako mwenyewe kuwa “mtangulizi” kuliko kutaka kuwa “mtendaji mkuu”? Wakati wowote Mungu akitaka kukutumia, jitoe kwa kilebora ulicho nacho. Kama Mungu atakuweka kwenye eneo la kutoa msaada, usiikatae huduma hiyo. Unaweza kumwamini Mungu akutumie katika njia ya mafanikio makubwa sana.

Tumeuona unyenyekevu wa Yohana wakati alipowaelekeza wafuasi wake kwa Yesu (Yohana 1:35-37). Lengo la Rabi lilikuwa ni kuwapata wanafunzi ambao wangemfuata na kumheshimu mwalimu wao. Badala yake, Yohana Mbatizaji aliwaelekeza wafuasi wake kwa mwalimu mkuu. Alielewa kwamba jukumu lake ni kuelekeza wengine kwa aliye mkuu kuliko yeye. Yohana alikuwa akiangalia wafuasi wake wakimwacha yeye na kwenda kumfuata Yesu. Lengo laku lilikuwa ni ufalme wa Mungu, na siyo utukufu wake mwenyewe. Kama watumishi wa Kikristo, hatupaswi tusahau kwamba lengo letu ni kuwaelekeza watu kwa Yesu, na siyo kutafuta mafanikio kwa ajili yetu wenyewe.

Angalia kwa kuzingatia: Inamaanisha nini Kutubu?

► Soma Mathayo 3:1-6.

Yohana alihibiri ujumbe wa kutubu. Kwa wakati wa sasa, baadhi ya watu wanasema kwamba kutubu ina maana tu ya kubadili mawazo. Wakristo wengi walioonyesha kuukiri Ukristo huonyesha dalili chache za maisha yaliyobadilishwa.

Hata hivyo, neno “kutubu” linamaanisha jambo muhimu zaidi kuliko uamuzi wa akili tu. Waandishi wa Agano Jipya walitumia neno la “kutubu” sawa na walivyokuwa wanatumia manabii Waebrania. Ilimaanisha kubadilisha kabisa “mfumo wa maisha.” Katika Agano Jipya, kutubu inamaanisha:

  • Kuwa na mabadiliko ya mawazo na imani, na

  • Kuwa na mabadiliko ya matendo a mfumo wa maisha.

Hivi karibuni nilisoma kuhusu muimbaji mmoja nyimbo za miondoko ya polepole aliyejulikana kwa mfumo wa maisha yake ya dhambi. Huyu mwimbaji alisema, “Nimekuwa Mkristo na nimejazwa nguvu za Roho Mtakatifu. Ninandelea kuishi maisha niliyokuwa naya hapo mwanzo, lakini sasa mimi ni Mkristo. Kama nikifa, nitaenda mbinguni.” Hii ina maana kwamba “kutubu” kwa mwanamume huyu hakujaleta mabadiliko yeyote katika mfumo wake wa maisha. Hii siyo toba ya kweli.

Yohana alifundisha kwamba toba inabadilisha mfumo wote wa maisha. Yohana aliwataka wahitimu wake “watoe matunda yapatanayo na toba” (Luka 3:8). Kwa maneno mengine, aliuliza, “Kuna ushahidi gani kwamba umebadilisha maisha yako?” Ubatizo haupaswi ufanyike kuwa ni ibada tupu: “Nimeamini, kwahiyo sasa nibatize.” Ubatizo ni lazima uw ushuhuda wa toba ya kweli na maisha yaliyobadilishwa

Mungu alimwandaa Mtumishi wake kupitia majaribu.

Ushindi wa Yesu dhidi ya majaribu unaonyesha mfano wa kuigwa tunapofikwa na majaribu. “Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na Ibilisi” (Mathayo 4:1). Jaribu lilitokea muda kidogo tu kabla ya kuanza huduma yake rasmi hadharani. Kabla hajaanza kuhubiri kwa watu wengine, Yesu alidhihirisha utii wake kamili kwenye mapenzi ya Baba.

Mathayo anaielezea taarifa hii ya jaribu mara tu baada ya Yesu kubatizwa. Majaribu yetu makuu mara nyingi hufuatiliwa na ushindi wa kiroho. Mara tu baada ya ushindi wa Elia katika mlima Karmeli, Tunamwona akijariwa hadi kufikia kiwango cha kukataa tama na hofu akiwa anakimbia kusalimisha maisha yake (1 Wafalme 18-19).

Luka anaielezea taarifa hii ya jaribu baada ya kufuatilia ukoo wa Yesu kutokea Adamu. Luka anaonyesha kwamba mahali ambapo Adamu alishindwa, Yesu Mwana wa Mtu alikuwa mshindi (Luka 3:38). Yesu alijidhihirisha mwenyewe kwa unyenyekevu na mfano wa kuigwa wa jinsi ambavyo Mkristo wa kawaida anaweza akapata ushindi dhidi ya dhambi.

[1]Majaribu

Jaribu la kugeuza mawe yawe mkate

Shetani alimjaribu Yesu atumie uwezo wake wa kiungu ili aweze kugeuza mawe yawe mkate. Hili lilikuwa ni jaribu la kutumia uhuru wa mtu. Shetani alimjaribu Yesu atumie uwezo wake kwa faida yake mwenyewe badala ya kumtegemea baba yake. Yesu alisalimisha “haki” yake ya chakula kwa Mungu.

Akiwa anakabiliwa na tunda lililokataliwa, Adamu wa kwanza alimwasi Mungu. Akiwa anakabiliwa na mkate uliokatazwa, Adamu wa pili alikuwa mwaminifu.

Jaribu la kuruka kutoka kwenye kinara cha Hekalu

Shetani alimjaribu Yesu kwa kumwambia aruke kutoka kwenye kinara cha hekalu (mita 91 juu ya bonde la Kedari). Hili litawashangaza watu wakati wakiwa katika kujaribu ulinzi wa Mungu.

Shetani alinukuu andiko la ahadi la Zaburi ya 91:11-12 kumjaribu Yesu avunje ahadi za Baba yake. Kwa jaribu hili, Yesu angemfanya Baba yake kwamba ni mtumishi wake – sawa na madai yake na matazamio yake. Hili lilikuwa ni jaribu la ufidhuli.

Yesu alikataa kutumia ahadi ya Zaburi 91 katika mazingira ambayo ahadi haingeweza kutumika. Katika kumjibu Shetani, Yesu alinukuu andiko kutoka katika Kumbukumbu la Torati 6:16, “Msimjaribu Bwana, Mungu wenu.” Kama watoto wa Mungu, hatuwezi kumwingiza Baba yetu wa Mbinguni kwenye jaribu.


[1]

"Tunawapongeza wale wanaosema kwamba, “Nitaithibitisha nguvu yangu kwa kusimamia haki zangu. ‘Lakini mtu mkamilifu huonyesha kwamba nguvu ya kweli inategemea mwanadamu kuachana na mapenzi yake mwenyewe na kutegemea mapenzi ya Mungu.”

- Nukuu kutoka kwa G. Campbell Morgan

Angalia kwa kuzingatia: Imani au Ufidhuli?

Baadhi ya Wakristo husema, “Kila ahadi katika Kitabu ni yangu.” Wakati kila ahadi iliyoko kwenye Maandiko ni kweli, ni lazima kila siku tujiulize, “Je! ahadi hii inaendana na mazingira yaliyopo?” Yesu alijua kwamba ahadi iliyokuwemo katika Zaburi ya 91 haikuwa kwenye mapenzi ya Mungu katika mazingira aliyokutana nayo pale jangwani. Tunawezaje kuwa na uhakika kwamba tunazidai ahadi za Mungu katika imani ya kweli kuliko katika ufidhuli?

(1) Ni lazima tuwe na ufahamu wa Neno la Mungu.

Kwa kiwango kile ninachoweza kujua maudhui ya ahadi za Mungu za kibiblia na mazingira yanayohusiana na ahadi hizo, nitaweza kupima matumizi yake katika mazingira yangu yaliyopo.

Ahadi nyingine zilitolewa kwa watu maalumu na katika mazingira maalumu. Katika Agano la Kale, Mungu aliahidi baraka za mwilini kama Israeli wangekuwa watiifu kwenye agano lake. Ardhi yao itatoa matunda mengi, ghala zao za nafaka zitafurika, na watashinda katika vita vyao. Ahadi za Agano Jipya mara nyingi ni za kiroho katika asili yake. Baadhi ya watu wanakatishwa tamaa wakisikia haya, lakini tunapaswa tuwe na furaha. Mafanikio ya kimwili thamani yake ni ya muda tu; mafanikio ya kiroho ni yenye thamani ya mbinguni. Ufidhuli (kiburi) vinaondoa ahadi za Mungu kutoka kwenye maudhui ya kibiblia na kuzifanya zitumike kwenye matamanio binafsi; imani humtumainia Mungu atimize ahadi zake kama apendavyo.

(2) Ni lazima tutambue tofauti iliyopo kati ya ahadi maalumu na ahadi za ujumla.

Tunaposoma kigezo mantiki cha ujumla, ni lazima tuulize kama Mungu anatoa kigezo mantiki kwa ajili ya mazingira yetu maalumu. Vigezo mantiki vingine ni vya ujumla tu na siyo kwa ajili ya wakati wote.

Zaburi 103:3 inamsifu Mungu “atuponyaye magonjwa yetu yote.” Baadhi ya Wakristo wameichukulia kauli hii kama ahadi ya wakati wote kwa ulimwengu kwamba Mungu ataponya magonjwa yote ya kila Mkristo aliyeamini. Hata hivyo, Maandiko yanaonyesha kwamba siyo kila ugojwa wa mwili unaponywa. Paulo aliomba kwa ajili ya uponyaji, na Mungu akamwambia, “Hapana” (2 Wakorintho 12:7). Mara nyingine Mungu huchagua kuwaponya watoto wake na ugonjwa; mara nyingine huchagua kuwapa neema ya kuhimili maumivu.

Tunapaswa tuwe na majibu kama yale ya vijana watatu wa Kibrania. Wakati mfalme Nebukadineza alipotishia kuwatupa kwenye tanuru la moto, walisema, “Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha” (Danieli 3:17-18). Walijua kwamba Mungu alikuwa na uwezo wa kuwaokoa, lakini kama Mungu atachagua iwe vinginevyo, walikuwa na utayari watumikie kwa uaminifu.

Mungu anaweza kuwaokoa watoto wake, lakini siyo kila wakati anachagua njia ya kupitia. Hadi hapo Mungu atakapoweka wazi kwamba kigezo mantiki cha kibiblia ni maalumu tu kwa ajili yako, mwamini Mungu afanye kama atakavyochagua yeye. Mtume Yohana alitoa kigezo mantiki kwamba, “Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba” (1 Yohana 5:14-15).

Ufidhuli (kiburi) hudhania kwamba kila kigezo mantiki cha kibiblia kinafanya kazi kwa ajili ya mazingira yangu maalumu. Imani inasema, “Nitaomba ‘sawasawa na mapenzi yake.’” Nitashawishika kuingia kwenye ufidhuli kama nitachukulia kwamba kila kigezo mantiki ni changu binafsi. Badala yake napaswa niulize kama kigezo mantiki kimekusudiwa kwa ajili ya mazingira yangu.

(3) Ni lazima tuombe kwa “Jina la Yesu.”

Yesu aliahidi, “Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana” (Yohana 14:13). Kuomba kwa “Jina la Yesu” kunamaanisha kuomba kulingana sawa na mapenzi yake na tabia yake. Inamaanisha kuomba “kwamba Baba aweze kutukuzwa.” Ufidhuli unatafuta mapenzi binafsi, imani inatafuta utukufu wa Mungu.

Kuomba “kwamba Baba aweze kutukuzwa” kunamaanisha kwamba tunajiweka kabisa chini ya makusudi ya Mungu katika maisha yetu. Mungu alitoa ahadi kwa Israeli, “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho” (Yeremia 29:11). Tunapaswa tukumbuke kwamba kigezo mantiki hiki kilitolewa kwa ajili ya Israeli ikiwa inatumikia miaka sabini ya utumwa katika nchi ya Babeli. Hata utumwa ndani ya Babeli utatimiza kusudi la Mungu kwa watu wake; katika dhiki yao, Israeli itamwita Mungu naye atawasikia.

Je, ahadi hii inafanya kazi kwetu leo? Ndiyo! Tabia ya Mungu haijabadilika; analeta mambo mema kwa watoto wake. Siyo kila kitu kitakachofanyika kitakuwa kizuri, lakini tunaweza kuomba kwa uhakika katika “Jina la Yesu” kwa sababu tunajua kwamba Mung analitendea kazi kusudi lake katika yale yote yanayotendeka katika maisha yetu.

Mungu alimwandaa Mtumishi wake kupitia Majaribu (Inaendelea)

Majaribu (Inaendelea)

Kuahidiwa milki za dunia

Jaribu la mwisho la Shetani lilikuwa ni ahadi ya makubaliano, njia ambayo Yesu angekubaliana nayo ili apewe utawala wote ujao bila njia ya msalaba. Kama Yesu atamsujudia Shetani, angeweza kuvuka maumivu makali ya msalaba. Yesu alimjibu kufuatana na andiko la Kumbukumbu la Torati 6:13, “Mwabudu Bwana Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake” (Mathayo 4:10).

Ushindi wa Yesu dhidi ya Majaribu

Ili tufaidike na mfano wa Yesu dhidi ya majaribu, ni lazima tukumbuke kwamba Yesu alikuwa mwanadamu kamili. Alijaribiwa “sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi.”

► Soma 1 Wakorintho 10:13 na Waebrania 4:15. Wanafundisha nini kuhusiana na majaribu?

Katika 1 Yohana 2:16, mtume anatambulisha njia tatu za majaribu, “tamaa za mwili, tamaa za macho na kiburi cha maisha.” Yesu alijaribiwa katika kila eneo.

  • Shetani alimjaribu katika tamaa za mwili wakati Yesu alipokuwa na njaa ya kupata mkate.

  • Shetani alimjaribu katika tamaa za macho kwa kumuonyesha milki za dunia.

  • Shetani alimvutia kwenye kiburi cha maisha kwa kumjaribu Yesu kwa kitendo cha ajabu cha kuvutia ambacho kingeshangaza halaiki za watu.

Ushindi wa Yesu dhidi ya majaribu haukupatikana kwa kutumia nguvu zake za kiungu. Yesu alikuwa mwanadamu kamili na aliyashinda majaribu katika ubinadamu wake. Ushindi wake unatoa mfano wa kuigwa kwetu sisi katika nyakati zote za kujaribiwa. Hapa unatakiwa utambue zana tatu Yesu alizotumia kupata ushindi dhidi ya majaribu:

Nguvu ya Roho Mtakatifu

Yesu alitembea katika uongozi na maelekezo ya Roho Mtakatifu. Alifanya kile ambacho Roho alimwongoza kukifanya. “Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani” (Luka 4:1).

Kwa muda wote wa huduma yake hapa duniani, Yesu alitenda kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Alitoa mapepo kwa uweza wa Roho (Mathayo 12:28). Mungu alimpaka mafuta Yesu wa Nazarethi kwa Roho Mtakatifu na uweza. Alipita kila mahali akitenda mema na kuwaponya wale wote waliokuwa wamegandamizwa na shetani, kwa kuwa Mungu alikuwa pamoja naye” (Matendo 10:38).

Yesu alitimiza huduma yake chini ya uweza wa Roho Mtakatifu. Kama tunataka tuwe na nguvu mbele ya uso wa majaribu, ni lazima tuishi ndani ya uweza wa Roho Mtakatifu.

Nguvu ya maombi

Yesu alijaribiwa kufuatia siku arobaini za kufunga na maombi.Maombi yalimwandaa kwa vita vya kiroho. Kwenye somo litakalofuata, tutaona undani wa maombi kwenye maisha na huduma ya Yesu. Kama Yesu alitegemea maombi, sisi tutategemeaje tupate ushindi wa kiroho nje ya maombi?

Shetani mara nyingi hutupiga vita baada ya kuanza kuwa wazembe katika maisha yetu ya maombi. Anajua kwamba kama hatuimarishi maisha yenye nguvu ya maombi tutakuwa wavivu katika kukabiliana na majaribu yanayotujia mbele yetu

Nguvu ya Neno

Yesu alijibu kila jaribukwa kutumia aya za Maandiko. Aliyajuaje haya maandiko? Watoto wa Kiyahudi walikuwa na desturi ya kukariri Torati kama sehemu yao ya elimu ya utotoni. Wakati Yesu alipojaribiwa, maneno katika maandiko hayo yalikuja haraka kwenye akili yake.

Kama Wakristo, ni lazima tuoteshe mbegu ya Neno la Mungu ndani ya mioyo yetu. Kwenye nyakati za majaribu, maandiko yatatupa nguvu ya kukabiliana na hayo majaribu.

Katika kukabiliana na majaribu, Yesu alitumia zana zinazofanana na tulizo nazo. Tunapaswa kukabiliana na majaribu kama Yesu alivyofanya, Kwa uweza wa Roho Mtakatifu, Kwa uweza wa maombi, na kwa uweza wa Neno. Bila ya kuwa na silaha hizo, tutajikuta tumeangukia kwenye mashambulizi ya Shetani.

Angalia kwa kuzingatia: Kupata mwili kwa Yesu Kristo

Wakristo wa mwanzo duniani kote walikubaliana kwamba Yesu alikuwa na hadhi ya kiungu. Ingawaje wazushi kama Ariasi alikataa uungu wa Yesu, Wakristo wa madhehebu ya Kiothodoksi walifundisha kwamba Yesu alikuwa na uungu.

Wakristo Waothodoksi walifundisha kwamba Yesu alikuwa pia mwanadamu kamili. Imani hii mara nyingi ilikataliwa na wazushi. Hata sasa, waamini wengi wa kiinjili hawauzingaqtii kwa umakini ubinadamu wa Yesu. Wakristo wengi wanajaribu kuwa na hisia kwamba Yesu alikuwa na uungu kamili, lakini ubinadamu wake siyo uliokamilika. Wanafikiri kwamba “aliazima” mwili wa kibinadamu, lakini hakuwa mwanadamu kamili.

Baadhi ya maelezo ya mahubiri yanachangia katika wazo hili potofu. Baadhi ya wahubiri huelezea hadithi ya mfalme aliyejifanya raia wa kawaida akasafiri. Hata hivyo, Yesu hakuwa akijifanya kuwa yeye ni mwanadamu. Alikuwa ni mmoja wetu.

Imani ya Yesu kuwa mwanadamu ni muhimu sana kwa uzoefu wa maisha ya Kikristo. Kama Ysu hakuwa mwanadamu kamili, maisha yake hayawezi kuwa mfano halisi wa kuigwa. Mwanatheolojia aliliweka likae hivi, “Kama Yesu kwa uhalisia hafanani na sisi, basi sisi tunasameheka kwa kutofanana na yeye”[1]

Watu wengi wanaamini kwamba ni lazima mara kwa mara tuanguke katika dhambi za kujitakia. Yesu alionyesha katika maisha yake kwamba, Wakristo wa kawaida wanaweza kudumisha maisha ya ushindi dhidi ya dhambi kupitia uweza wa Roho Mtakatifu.

Kama Yesu alifanyika sehemu ya ubinadamu wetu mdhaifu, kama alipitia katika mahtaji yetu kwa uweza wa Roho Mtakatifu, na kama alijaribiwa kama nasi tunavyojaribiwa, basi ushindi wake dhidi ya majaribu unatuonyesha sisi jinsi ya kuwa washindi dhidi ya dhambi katika maisha yetu ya kila siku. Kwa uweza wa Roho Mtakatifu, tuna uwezo wa kuishi maisha ya ushindi.

► Ni lipi gumu kwako kufahamu, imani ya uungu wa Yesu au imani yay eye kuwa mwanadamu? Jadili ni kwa jinsi gani kila mojawapo ya imani hizi ni muhimu kwetu katika maisha yetu ya Ukristo na huduma.


[1]Cherith Fee Nordling, “Open Question” Christianity Today, April 2015, 26-27).

Hitimisho: Mungu huwaandaa Watumishi wake.

Katika somo hili, tumeona ni kwa jinsi gani Mungu alivyoandaa njia ya huduma ya Yesu. Kutokea ukoo wake, hadi kupitia Utawala wa Kirumi, kupitia kuzaliwa kwa muujiza, kupitia huduma ya Yohana Mbatizaji na hata kupitia katika majaribu, Mungu aliandaa njia kwa ajili ya Yesu.

Tunauona ukweli huu mara nyingi katika Biblia yote. Angalia katika mfano wa Paulo. Paulo alikulia katika jiji la Roma la Taso. Kuanzia utotoni, alikuwa na marafiki mataifa. Tofauti na Wayahudi wengi, Paulo alikuwa ameridhika sana na kuwa na watu a mataifa.

Baba yake na Paulo alkuwa raia wa Kirumi, kwa hiyo Paulo alithamini sana haki za uraia za Kirumi. Mama yake alikuwa Myahudi, kwahiyo Paulo alipata mafunzo ya awali ya Maandiko ya Agano la Kale. Alikuwa na akili sana na alijifunza teolojia ya Kiebrania (Kiyahudi) chini ya mwalimu mkuu Gamalieli. Akiwa na asili yake ya Kirumi, alijifunza Kiyunani na mafundisho ya Wanafalsafa wa Kiyunani.

Kutokana na asili hii, siyo jambo la kushangaza kwamba Mungu alimwita kuwa mmishenari kwa mataifa. Tangu kuzaliwa, Mungu alimwandaa Paulo kuwa mmishenari wa kwanza kwa mataifa. Jaribu kutafakari maandalizi ambayo Mungu aliyafanya kwa ajili ya huduma yake:

  • Kwa Paulo kuwa raia wa Kirumi kulimpa uhuru wa kusafiri bila matatizo.

  • Mafunzo ya Paulo ya Kiebrania na Kiyunani yalimpa nyenzo kubwa ya kuandika vitabu vyenye maarifa mengi vya Agano Jipya.

  • Kwa Paulo kujifunza falsafa ya Kiyunani, kulimwezesha kuzungumza na watu wa maarifa mengi ya kufikiri waliokuwa katika maeneo kama ya Athens.

Yumkini unasema, “Mungu hakunipa elimu kubwa kama ya Paulo. Sina historia kubwa ya nyuma ya familia yangu.” Yote ni sawa! Mwangalie kiongozi mwingine wa kanisa la karne ya kwanza.

Simoni Petro alikulia katika maisha ya uvuvi wa biashara. Hakuwa na elimu au maarifa kama ya Paulo. Kwa hakika, baadaya Petro alikiri kwamba Paulo ameandika mambo mengi “ambayo ni magumu kueleweka” (2 Petro 3:15-16). Lakini Mungu alimtumia Petro kwa kiwango cha nguvu sana. Watu ambao wangeweza kujazwa kwa maneno yenye nguvu na maarifa ya Paulo, walikuwa wanaweza kuelewa mahubiri mepesi ya Petro.

Mungu amekuandalia wewe kwenye sehemu yako ya utumishi. Ukisalimisha mafunzo yako kwake, historia yako ya nyuma, na yote ambayo Mungu amekukirimia, atakutumia wewe katika kutimiza kusudi lake. Mungu huwaandaa wale aliowaita kwa ajili ya huduma.

Kazi za kufanya Somo la 1

Хэвлэх боломжтой PDF
Засварлах боломжтой Word баримт бичиг

(1) Katika somo hili, tumeona mfano wa Yesu wa ushindi dhidi ya majaribu. Orodhesha mifano mitatu ya kibiblia ya watu ambao waliweza kudumisha ushindi wao dhidi ya majaribu. Onyesha jambo moja ambalo liliweza kuwapa nguvu ya kukabiliana na majaribu.

Mifano ya ushindi dhidi ya Jaribu Andiko Nini kilichosababisha ushindi?
Yusufu
(usafi dhidi ya zinaa)
Mwanzo 39 Alimtegemea Mungu
(Mwanzo 39:9)
     
     
     

Orodhesha mifano mitatu ya kibiblia ambayo watu walianguka dhidi ya majaribu. Katika kila moja, onyesha kipengele kimoja kilichosababisha kuanguka kwao.

Mifano ya kuanguka dhidi ya Jaribu Andiko Nini kilichosababisha kuanguka?
Petro kumkana Yesu Luka 22:54-62 Kujiamini kupita kiasi
(Luka 22:31-34)
     
     
     

(2) Kutokana na mifano uliyoorodhesha, andaa andiko la mahubiri au la kujifunza Biblia kuhusiana na majaribu. Unganisha mfano wa Yesu pamoja na hii mingine uliyoorodhesha kwenye jedwali lako.

 

Next Lesson