Ufanisi wowote wa huduma unafanyika kwa nguvu ya masalaba na kufufuka.
Utambulisho
Kilele cha Injili zote ni maelezo ya mateso ya Yesu. Sura thelathini kutoka katika sura themanini na tisa za Vitabu vya Injili zimejikita kati ya ile wiki ya kuingia Yerusalemu kwa shangwe hadi kufufuka. Takribani nusu ya kitabu cha Yohana imetumika kwa ajili ya wiki hii ya mateso. Hiki ndicho kilele ambacho maisha ya Yesu na huduma vililenga. Katika somo hili, tutajifunza wiki ya mwisho ya huduma ya Yesu hapa duniani ili kujifunza masomo yatakayohusiana na maisha yetu na huduma zetu.
► Kabla ya kuendelea na somo hili, jadili maswali mawili yafuatayo:
Kusulubiwa msalabani kunamaanisha nini kwangu, kitheolojia na kibinafsi?
Kufufuka kunamaanisha nini kwangu, kitheolojia na kibinafsi?
Majibu kwa Yesu: Wiki ya mwisho ya huduma ya Yesu Hadharani.
Moja ya msisitizo mkubwa kutoka kwa wainjilisti ni majibu ya wale waliokuwa wanakutana na Yesu. Kwa mfano, kwenye mwanzo wa maisha ya Yesu, Mathayo analinganisha kuabudu kwa mamajusi na majibu ya Herode, aliyejaibu kumwangamiza huyu mfalme mpinzani. Yohana analinganisha jibu la swali la Nikodemo, Rabi wa Kiyahudi, na la mwanamke Msamaria asiyekuwa na elimu yeyote katika kisima.
► Soma Mathayo 10:32-39.
Hakuna hata mtu mmoja atakayeweza kubakia kwamba hana upande wowote wa kuegemea kwenye ujumbe wa Yesu; aidha tunakubaliana na maelezo yake au tunamkataa yeye. Yesu aliielezea huduma yake kama upanga unaogawa makundi haya mawili. Familia ziligawanyika kwa majibu yao kwa Yesu; hata familia ya Yesu mwenyewe ilikutana na mtihani huu (Mathayo 13:53-58). Hakuna hata mtu mmoja atakayeweza kubakia kwamba hana upande wowote wa kuegemea.
Hali hii ya ulinganifu wa majibu ya Yesu yanakuwa na mvuto wenye hisia zaidi katika wiki la mwisho la huduma yake hadharani. Ulinganifu huu unaendelea hadi kwenye msalaba wenyewe, kwa wezi wawili wakijibizana kwa njia mbili tofauti kabisa kuhusiana na Yesu.
Majibu kwa kufufua Lazaro
► Soma Yohana 11:1-57.
Hata kabla ya kufufuliwa kwa Lazaro. Viongozi wa kidini walikuwa wamempinga Yesu. Mapema kwenye majira ya baridi Yesu alipotembelea hekalu wakati wa Sikukuu ya Kutabaruku, viongozi wa Kiyahudi walimshutumu kwa kukufuru na wakajaribu kumpiga kwa mawe. Kwa kuwa muda wake wa kuwa dhabihu ulikuwa haujawadia, Yesu akatoka mikononi mwao. Akaenda zake tena ng'ambo ya Yordani mbali na mji wa kitovu cha dini wa Yerusalemu (Yohana 10:22-42).
Habari zilipotoka kuhusu kifo cha Lazaro, wanafunzi walijua ni hatari kwa Yesu kurejea Yudea. Wasomaji mara nyingi hufanyia dhihaka shaka na tabia ya kuona mambo yote ni mabaya aliyokuwa nayo Tomaso, lakini mimi ninavutiwa na uaminifu wake aliokuwa nao kwa Bwana wake. Ana hisia (sahihi) kwamba Yesu ataweza kuuawa huko Yudea, lakini Tomaso ni mwaminifu. Wakati Yesu alipokuwa akisisitiza kurudi Yudea, Tomaso anawaambia wanafunzi wenziwe, “Twendeni na sisi, ili tufe pamoja naye.” Bila kujali mashaka ya baadaye ya Tomaso, tusisahau uaminifu wa huyu mwanafunzi aliyejazwa na mashaka. Haileti mshangao wowote kwamba baada ya Yesu kufufuka, Tomaso alikuja kufa kifo kibaya cha wafia dini akiwa anapeleka injili India?
Kwenye kijiji kidogokama Bethania, kufufuliwa kwa Lazaro hakungwezekana kuwe kwa kificho. Hakukuwa na jinsi yeyote ya viongozi wa dini kuficha tukio lenye kuleta msisimko kama hilo. Yohana anaonyesha majibu tofauti katika muujiza huu.
Majibu ya Umati wa Watu
Mara tu taarifa za kufufuka kwa Lazaro zilipoenea, wananchi walijawa na uhakika kwamba Yesu atakuja kuupindua utawala wa Kirumi na kuanzisha upya utawala wa Daudi katika Yerusalemu. Walikuwa na uhakika kwamba Yesu ndiye Yule Masihi aliyekuwa ameahidiwa. “Basi wengi katika Wayahudi waliokuja kwa Mariamu, na kuyaona yale aliyoyafanya, wakamwamini” (Yohana 11:45 na 12:11). “Maana kwa ajili yake wengi katika Wayahudi walijitenga, wakamwamini Yesu” (Yohana 12:19). Kwa hiyo watu wengi walimwamini Yesu ambaye Mafarisayo walisema, “tazameni, ulimwengu umekwenda nyuma yake” (Yohana 12:19). Hili liliongeza shauku ya umma wakati Yesu alipoingia Yerusalemu akiwa amempanda mwana punda.
Majibu ya viongozi wa Dini
Kufufuliwa kwa Lazaro kuliharibu nafasi zote za viongozi wa dini kuweza kukanusha madai ya Yesu kwamba ni Masihi. Wakati umati wa watu ukiwa unageuka kuja kwa Yesu, viongozi wa kidini walikuwa na chaguzi mbili tu:
1. Kukiri kwamba Yesu ni yeye kama alivyojinasibu kwamba ndiye. Pamoja na hayo, hii itawahitaji kusalimisha tamaa yao kwa ajili ya madaraka. Yesu tayari alishalaani tabia yao ya unafiki. Kama watakiri kwamba Yesu ni Masihi, watapoteza nafasi zao kama viongozi wa Wayahudi.
2. Kumkamata na kumwua Yesu. Kama wamekataa kumwamini Yesu kama Masihi, ni lazima watamwua.
Viongozi wa dini walitetea maamuzi yao ya kumwua Yesu kama yaliyokuwa bora sana kwa ajili ya taifa. Kama ilivyo kwa viongozi wote wadhaifu katika historia, walijitahidi kujiridhisha kuhusu uamuzi wao. “Tunafanya nini? Maana mtu huyu afanya ishara nyingi. Tukimwacha hivi, watu wote watamwamini; na Warumi watakuja, watatuondolea mahali petu na taifa letu” (Yohana 11:47-48). Walikuwa na mashaka kwamba Yesu atakuja kuongoza maasi dhidi ya Warumi. Hawakuwa wanajua kwamba ufalme wake ni wa kiroho.
“Mahali petu” yawezekana inarejea kwenye hekalu na “taifa letu” inarejea kwenye uhuru wa aina mbalimbali ambazo Warumi walikuwa wametoa kwa Wayahudi (Ona Matendo 6:13 na 21:28.). Ingawa Yudea ilikuwa chini ya uthibiti wa Warumi, Wayahudi walikuwa wameruhusiwa kuabudu hekaluni, kusimamia sheria za dini, na kupitia baraza lao la Sanhedrini, wasimamie baadhi ya serikali za kiraia. Yote haya yangeondolewa kama Warumi watavunja hayo maasi.
Kayafa alilithibitishia baraza la Sanhedrini kwamba ilikuwa ni heri mtu mmoja afe kuliko taifa lote lisiangamie kwa mateso (Yohana 11:49-50). Kimsingi, Baada ya kumwua Yesu, mashaka yaliyokuwa yamelisibu baraza la Sanhedrini yalikuja kutoweka. Miaka arobaini baadaye baada ya kumwua Yesu, Warumi walilivunja jaribio la maasi lililofanywa na Wayahudi kwa kuvunja lile hekalu, kuwaondolea haki zao zote walizokuwa wamepewa na Warumi, na kufanya kila kitu walichoamriwa ambacho Kayafa alikuwa anajaribu kukikwepa hapo mwanzo.
Kwa kuwa hawakuwa na jinsi ya kuuficha muujiza bila ya kuharibu ushahidi wote, Baraza la Sanhedrini lilifanya shauri kumwua Yesu pamoja na Lazaro. Ili “kulinda taifa” (Yohana 11:53 na 12:10). Miujiza siyo lazima iwashawishi wasioamini. Mara nyingi tunafikiri kwamba, “Kama tu Mungu atajidhihirisha mwenyewe kwa muujiza, kila mtu ataamini.” Hata hivyo, muujiza unaweza kuleta ugumu kwa mwenye kushuku katika hali yake ya kutoamini.
Kwenye hadithi ya Lazaro na maskii (siyo Lazaro aliyefufuliwa na Yesu), tajiri alimsihi Abrahamu amtume Lazaro aende kuwaonya ndugu zake. Abrahamu akamwambia, “Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu akifufuka katika wafu” (Luka 16:31). Maandiko peke yake ni ushuhuda wa kweli unaotosha. Kama tutayakataa maandiko, ushahidi mwingine wowote hauwezi kutushawishi sisi.
Majibu ya Yesu: Mariamu
► Soma Mathayo 26:6-13 na Yohana 12:1-11.
Katika kipindi chote cha huduma ya Yesu duniani, Mariamu, dada wa Lazaro na Martha, walikuwa miongoni mwa wafuasi wake muhimu sana waliokuwa wamejitoa kwake. Katika hadithi ya mwanzo, Martha alilalamika kwa sababu Mariamu alikaa kumsikiliza tu Yesu wakati yeye akihangaika kuhudumia. Katika hadithi hiyo, Yesu alimpongeza Mariamu kwamba, “amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa” (Luka 10:42).
Wiki moja kabla ya kifo chake, Yesu na wanafunzi wake walitembelea nyumbani kwa Simoni aliyekuwa anaugua ukoma. Lazaro na dada zake walikuwa wamealikwa kujiunga katika kundi hilo. Wakati wa chakula, Mariamu mwenye kibweta cha marhamu ya thamani kubwa alimkaribia Yesu akayamimina mafuta ya marhamu kichwani pake hadi miguuni. Marhamu hiyo ilikuwa inagh’arimu takribani dinari mia tatu, kiwango cha mshahara wa mtu kwa mwaka mmoja. Wakati huo ambao hakukuwepo na mabenki, hii inawezekana kwamba Mariamu alikuwa amejihifadhia mwenyewe fedha hizo.
Wanafunzi walikasirika kwa sababu Mariamu alikuwa amepoteza fedha nyingi, (Mathayo 26:8; Marko 14:5). lakini Mariamu alijali tu mawazo ya mtu mmoja, Yesu. Alifanya hayo yote kwa ajili ya upendo wake kwa Yesu uliomfanya kipofu wa kutoona mawazo ya mtu mwingine yeyote. Hakujali marhamu yale yaligharimu fedha kiasi gani na hakujali watu wengine watafikiria nini. Alikuwa anamwabudu Bwana wake, na hakuwa na shughuli na jambo lingine lolote.
Wakati wanafunzi walipopinga matendo ya Mariamu, Yesu aliwakaripia: “Mwacheni; mbona mnamtaabisha? Amenitendea kazi njema” (Marko 14:6). Huku akijua kwamba msalaba ulikuwa unamsubiri siku chache tu mbele, Yesu alitambua ishara iliyokuwemo kwenye kitendo cha Mariamu: “ametangulia kuupaka mwili wangu marhamu kwa ajili ya maziko.” Yesu alimheshimu huyu mwanamke aliyetoa kitu kizuri kuliko vyote alivyokwisha wahi kuwa navyo kwa tendo la kujitegemea la ibada ya upendo.
Tunaposoma taarifa ya Mariamu ya kumpaka Yesu marhamu, tunapaswa kujiuliza, “Je, ni kwa jinsi gani mimi ninampenda Yesu? Je, ninamjali zaidi yeye au ninajali mawazo ya watu wengine wanaonitazama? Hakika Mariamu alimpenda Yesu.
Majibu ya Yesu: Kuingia kwa Shangwe
► Soma Mathayo 21:1-11 na Yohana 12:12-19.
Ilikuwa siku ya Jumapili, Yesu aliingia Yerusalemu akiwa amepanda punda. Katika siku ya kawaida, hakungekuwa na kitu cha kushangaza katika tukio hili; mwalimu kutoka Galilaya akisindikizwa na kikundi kidogo cha wafuasi wakiingia Yerusalemu kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka. Lakini huu haukuwa muda wa kawaida. Kufufuliwa kwa Lazaro kulibadilisha kabisa hija ya Pasaka ijeuke kuwa ni tamko la kidini na kisiasa.
Mathayo anaakisi waziwazi madhara ya kidini yaliyopatikana kutokana na kuingia kwa Yesu Yerusalemu. Mathayo anaonyesha kwamba Kuingia kwa Yesu kulikamilisha unabii wa Zakaria. Maneno yaliyokuwa yakitamkwa na umati wa watu yalitoka katika Zaburi 118, Zaburi ya Pasaka inayoelezea kuingia kwa ushindi katika Yerusalemu (Mathayo 21:4-11; Zakaria 9:9; Zaburi 118:26).
Kuingia kwa Yesu kwa ushindi kulionekana kama gwaride la kisiasa la mfalme:
Umati wa watu ulitandaza nguo kwenye barabara zote ikiwa ni ishara ya kujisalimisha kwa mfalme (Mathayo 21:8; 2 Wafalme 9:13).
Kuanzia kwenye kipindi cha Wamakabayo, matawi ya mitende yalikuwa ni ishara ya ushindi dhidi ya majeshi ya adui (Yohana 12:13; 1 Wamakabayo 13:51).
“Hosiana!” ilimaanisha “tuokoe sisi,” kilio cha kutaka ukombozi,
“Mwana wa Daudi” kilikuwa ni cheo cha kifalme na Masihi.
Watu waliamini kwamba Yesu alikuwa anaingia Yerusalemu kuuangusha utawala wa Kirumi na kuanzisha ufalme wake. Muda mrefu uliokuwa umesubiriwa wa utawala wa kifalme wa Daudi ulionekana sasa umemalizika. Ahadi zilizotolewa na manabii zinaenda kukamilika hivi karibuni.
Ni siku chache tu baada ya hapo, watu hawa - hawa watapiga kelele za kudai, ‘Msulubishe!” Kwa nini? Kwa sababu walikuwa wanamshangilia Yesu kwa sababu potofu. Waliamini atauangusha utawala wa Kirumi, Lakini Yesu hakuwa na mpango wowote wa kuongoza mapinduzi ya kijeshi. Walikuwa wanahitaji utawala wa kifalme wa kisiasa, lakini Yesu alikuwa analeta ufalme wa kiroho. Kwa kukatishwa kwao tamaa, umati wa watu baadaye unamgeuka na kumsaliti Yesu.
Wajumbe wenye uwezo na nguvu za kisiasa na kijamii kwenye baraza la Sanhedrini walishaamua Yesu auawe; wasiokuwa na uwezo au nguvu ghafla wanakuwa kinyume na Yesu na kumsaliti. Akijua yaliyokuwa mbele yake, Yesu akaulilia mji unaokwenda kumkataa (Luka 19:41-44). Hapa tunasema, “kuingia kwa ushindi”; Yesu alijua kwamba hiyo ilikuwa ndiyo “njia ya kuuendea msalaba.” Umati ulinukuu Zaburi 118:26, “Na abarikiwe yeye ajaye kwa jina la Bwana; Tumewabarikia toka nyumbani mwa Bwana!” Yesu aliijua aya nyingine iliyofuatia, “Bwana ndiye aliye Mungu, Naye ndiye aliyetupa nuru. Ifungeni dhabihu kwa kamba Pembeni mwa madhabahu!” (Zaburi 118:27). Yesu aliingia Yerusalemu kama dhabihu ambayo hivi karibuni itatundikwa kwenye “madhabahu,” msalaba wa Kirumi.
Angalia kwa kuzingatia: Yesu anaulaani Mti wa Mtini
► Soma Marko 11:12-25.
Kwenye kila Kitabu cha Injili kinachochukua vidokezo, kinahusisha taarifa za Yesu akiulaani mti wa mtini ambao haukuwahi kuzaa kwenye wiki yake ya mwisho ya huduma ya hadharani. Yesu aliulaani huu mti wa mtini siku ya Jumatatu alipokuwa anarejea Yerusalemu baada ya kulala katika mji wa Bethania. Siku iliyofuata Jumanne, wanafunzi wakauona mti umeshanyauka kwa kipindi cha masaa ishirini na nne tu.
Ingawaje ulikuwa “siyo wakati wa tini” (Mark 11:13), ilimaanisha kwamba majani ya rangi ya kijani yalipaswa yawepo kwenye mti huo. Tunda la mtini hutokea muda mchache tu baada ya hayo majani. Wakati mti ukiwa na majani bila kuwepo na matunda machanga ya mtini, huo mti hautakuwa na matunda katika mwaka huo.
Maelezo haya ya mti wa mtini ni “mfano uliotolewa” kuhusiana na kushindwa kwa Israeli kuzaa matunda.[1] Israeli ilikuwa imechaguliwa na Mungu kuwa Baraka kwa mataifa yote (Mwanzo 12:3). Badala yake, Israeli imeliaibisha jina la Yehova.
Hekalu lilikuwa liwe mahali pa “watu wa aina zote” kwa ajili ya kumwabudu Mungu” (Isaya 56:7). Badala yake, hakalu limekuwa “pango la wanyang’anyi,” mahali ambapo makuhani waliokuwa na nguvu walipatumia kuwadanganya maskini.
Mti wa mtini haukuzaa matunda; Israeli haikuzaa matunda. Mti wa mtini ulikataliwa; Israeli hivi karibuni itakataliwa.
Kulaaniwa kwa mti wa mtini ni moja ya mfululizo wa ujumbe zenye laana za Yesu kwenye siku zake za mwisho za huduma ya hadharani:
1. Mfano ulioonekana wazi wa mti wa mtini usiozaa matunda (Marko 11:12-14, 20-25).
2. Kulisafisha hekalu (Marko 11:15-19).
3. Mfano wa wapangaji waovu wasiokuwa waaminifu (Marko 12:1-12).
4. Mabishano kati yake na viongozi wa kidini (Marko 12:13-40).
5. Yesu anatabiri kubomolewa kwa hekalu (Marko 13:1-37).
[1]Katika Agano la Kale, mara nyingi mti wa mtini huwakilisha Israeli (mfano: Yeremia 8:13; Hosea 9:10; Yoeli 1:7)
Majibu kwa Yesu: Wiki ya mwisho ya huduma ya Yesu Hadharani (Inaendelea)
Majibu ya Yesu: Viongozi wa Dini
► Soma Mathayo 21:23-22:46.
Baada ya kufufuliwa kwa Lazaro, viongozi wa kidini walikusudia kumwua Yesu. Hata hivyo, umaarufu wake na watu wa kawaida ulisababisha mpango huo kuwa mgumu. Walikuwa wanatafuta njia yeyote ya kumshushia hadhi yake mbele ya macho ya umati wa watu. Kwenye siku kadhaa baada ya Yesu kuingia Yerusalemu kwa ushindi, viongozi wa kidini waliratibu msururu wa mahojiano ya kushindana naye ndani ya hekalu. Walikuwa wanajaribu kumtega Yesu, lakini kila wakati walishindwa. Badala yake, umati wa watu uliangalia kila siku Yesu akiwagalagaza kwa aibu kubwa viongozi wa kidini kwa hekima na kwa umahiri mkubwa.
Kwanza, “kuhani mkuu na wazee” walitaka sababu za kuthibitisha uhalali wake wa kulisafisha hekalu na kuhubiri hadharani. Yesu aliwajibu kwa kuwatega kwa swali lililohusiana na Yohana Mbatizaji.
Kisha Yesu akatoa mifano mitatu ambayo iliwashutumu viongozi wa kidini. Mfano wa watoto wawili unaonyesha kwamba utii, na siyo ujuzi, ndiyo uthibitisho wa mahusiano katika ufalme wa Mungu. Mfano wa wapangaji waovu unaonyesha madhara ya kumkataa Yesu kama Masihi. Mwisho, mfano wa sikukuu ya harusi unaonyesha kwamba viongozi wa kidini ambao walikuwa wamealikwa kwenye harusi sasa wamekataliwa na kwa upendeleo wamepewa wale wanaoonekana si chochote, lakini wameitikia mwito wa mwaliko waliopewa.
Wakiwa wamedhamiria kumdhalilisha Yesu, viongozi wa kidini walileta msururu wa maswali kwa ajili ya kutaka kumteka Yesu. Dhamira yao haikuwa katika kujifunza ukweli; dhamira yao ilikuwa ni ili kumsambaratisha Yesu. Yesu alijua kwamba hawakua na haja ya kujua ukweli, kwa hiyo kila swali alivutia upande wake.
Baada ya kushindwa kumtega Yesu, viongozi wa kidini waliachana naye. Mathayo anamalizia sehemu hii akionyesha kushindwa kwao: “Wala hakuweza mtu kumjibu neno; wala hakuthubutu mtu ye yote tangu siku ile kumwuliza neno tena” (Mathayo 22:46). Marko anamalizia kwa kugusia furaha ya watu wa kawaida waliyokuwa nayo wakati wamehudhuria kwenye majadiliano hayo. “Na mkutano mkubwa walikuwa wakimsikiliza kwa furaha” (Marko 12:37)
► Kama mchungaji na kiongozi wa Kikristo, mara kwa mara utakutana na maswali magumu. Je, ni kwa jinsi gani utaweza kutambua tofauti ya watu wanaouliza maswali ya kweli na wale ambao wanataka kukutega? Je, majibu yako kwa aina hizi mbili za watu yanatofautianaje? (Ona Mithali 26:4-5 kama mfano wa ulinganifu huu.)
Miaka ishirini baada ya Yesu kupaa mbinguni, Paulo alianzisha kanisa katika Korintho. Kanisa hili lilikuwa na watu wengi waliookoka kutoka kwenye mazingira mbalimbali ya historia. Kanisa ilihusisha pamoja na Wayahudi waliokuwa wanajua maandiko ya Kiyunani, na Mataifa ambao hawakuwahi kusikia jambo lolote linalohusiana na Mungu wa kweli.
Kanisa la Korintho lilikuwa limepasuka kwa ajili ya migogoro na tishio la mafundisho ya uongo. Akihusika kujibu matatizo haya, Paulo anakumbushia kuhusu ujumbe wake wa kwanza aliohubiri mahali hapo. Mafundisho ya kwanza ya Paulo kwenye jiji ambalo lilikuwa ni la wapagani, yalilenga kwenye matukio manne ya historia:
Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zetu.
Alizikwa.
Alifufuka siku ya tatu.
Alionekana hadharani – kwa Kefa, kwa wale Thenashara, kwa ndugu zaidi ya mia tano pamoja, kwa Yakobo, tena kwa mitume wote, na mwisho wa watu wote Paulo.
Sehemu ya kwanza ya ujumbe wa Paulo katika Korintho ilikuwa juu ya msalaba: “Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu.” Ujumbe kuhusu msalaba ndio kiini kikuu katika imani ya Kikristo.
Kwenye Agano la Kale, mtu aliyeleta kondoo kwa ajili ya dhabihu huiweka mikono yake juu ya kichwa cha kondoo ili kujitambulisha na kifo cha dhabihu. Kwa kuweka mikono yake juu ya kichwa cha kondoo, anayeabudu husema, “Kondoo huyu anakufa kwa niaba yangu. Ninastahili kifo kwa ajii ya dhambi zangu.” Kwa njia hiyo – hiyo, tulistahili kifo kwa ajili ya dhambi zetu, lakini Kristo akafa kwa niaba yetu. Tulistahili kifo; yeye akafa ili sisi tupate kuishi.
Kukamatwa
► Soma Mathayo 26:1-5, 14-56.
Siku ya Jumatano ya Mateso, Yesu alitabiri kifo chake “baada ya siku mbil.” Baraza la Sanhedrini lilikuwa linapanga kumkamata Yesu baada ya umati wa hija ya Pasaka kuwa wamendoka katika jiji hilo, angalao siku tisa kutokea siku ya utabiri huu. Hata hivyo, wakati Yuda alipojitolea kumsaliti Bwana wake, waliamua kumkamata kwa ushirikiano na mfauasi wake mmoja.
Kwa nini makuhani wakuu walimhitaji Yuda? Walijua Yesu ni nani na wataweza kumpata mahali gani. Alikuwa akifundisha hekaluni kila siku. Viongozi wa Kidini walikuwa wanamhitaji Yuda aje atumike kama shahidi dhidi ya Yesu wakati wa kuendeshwa kwa mashtaka. Kwa kosa lolote kubwa lililohitaji hukumu ya kifo, sheria ya Kirumi inahitaji shahidi. Kwa kumsaliti Yesu, Yuda alikuwa anakubali kuwa shahidi wao. Baada ya kukamatwa, Yuda “alibadilisha mawazo yake” na viongozi wa Kiyahudi wakawa wamekosa shahidi wao nyota dhidi ya Yesu (Mathayo 27:3-4, Marko 14:55-56).
Baada ya kushiriki chakula cha Pasaka na wanafunzi wake, Yesu alikwenda katika bustani ya Getsemani kuomba. Akifikiria jinsi ya kukabiliana na mateso ya mwilini katika msalaba na uchungu wa kutenganishwa kutoka kwa Baba yake, Yesu aliomba, “Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.” Hata katika mashtaka haya mazito, Yesu alijikabidhi kwenye mapenzi ya Baba yake.
Baadaye jioni ile ile, Yuda akaja na “kikosi kikubwa” ili kumkamata Yesu.[2] Baada ya Yuda kumtambuisha Yesu kwa njia ya kumbusu, Yesu alizungumza na wale askari. Wakati Yesu alipowaambia, “Ni mimi, walirudi nyuma, wakaanguka chini” (Yohana 18:6). Hili kundi kubwa la askari lilikuwa na wasiwasi dhidi ya mtu aliyekuwa na uwezo juu ya kifo. Katika hili, Yesu ndiye aliyekuwa akisimamia mipango yote, na siyo wale maadui zake. Octavius Winslow, Mhubiri wa karne ya kumi na tisa aliandika, “Ni nani alimtoa Yesu ili afe? Siyo Yuda, kwa ajili ya fedha. Siyo Pilato, kwa ajiliyahofu. Siyo Wayahudi, kwa ajili ya wivu. Ni Baba aliyemtoa, kwa ajili ya upendo!”[3]
Mashtaka
► Soma Mathayo 26:57-27:26; Luka 22:54-23:25; Yohana 18:12-19:16.
[4]Kushtakiwa kwa Yesu kulihusisha kwa pamoja mashtaka ya Kiyahudi na mashtaka ya Kirumi. Sheria ya Kiyahudi ilikuwa inajali ubinadamu zaidi kuliko mifumo mingine yote ya kisheria ya zamani; sheria ya Kiyahudi ilitumia kila linalowezekana kuokoa uhai. Sheria ya Kirumi ilijulikana kwa kuwa na masharti magumu na akili ya kutambua mambo mengi. Hizi zilikua ni sheria kuu mbili za ulimwengu wa zamani, lakini hazikuweza kuwazuia watenda dhambi katika kumwua Mwana wa Mungu.”
Masaa machache baada ya kukamatwa kwake, Yesu alikuwa na makesi ya kisheria sita ya kusikilizwa. Hii ni pamoja na mashtaka ya kidini ya Wayahudi, na mashtaka ya raia ya Kirumi. Wataalamu wa historia wanaelezea kwamba mashtaka ya kidini ya Kiyahudi yalikuwa siyo ya kisheria kwa mujibu wa sheria ya Kiyahudi.
Katika kuharakisha kwao kumhukumu Yesu, baraza la Sanhedrini:
Liliendesha mashtaka usiku (kinyume cha sheria)
Halikufuata taratibu za kawaida za mashtaka kabla ya kumkamta Yesu (kinyume cha sheria )
Hawakuruhusu Yesu kuita mashahidi kwa ajili ya kujitetea (kinyume cha sheria )
Waliharakisha mashtaka yafanyike kwa haraka sana kuliko sheria ya Kiyahudi ilivyokuwa inaruhusu. (kinyume cha sheria)
Kimsingi, haya yote yalifanyika ili Yesu asulubiwe msalabani na maiti yake iweze kuondolewa kabla ya Pasaka. Walimwua mwana kondoo wa Mungu ili kwamba waweze kula kondoo wa Pasaka katika utaratibu wao uliokuwa sahihi!
Mtiririko wa Mashtaka
(1) Kusikilizwa na Wayahudi mbele ya Anasi (Yohana 18:12-14, 19-23)
Anasi alikuwa amechaguliwa kuwa kuhani mkuu wa maisha. Hata baada ya Warumi kumbadilisha Anasi na kumweka mkwewe Kayafa, Wayahudi wengi waliendelea kumwita Anasi kwa cheo chake cha zamani cha “Kuhani Mkuu.” Huu usikilizwaji wa kwanza mbele ya Anasi haukuwa rasmi. Haukuwa na mashtaka au mashahidi.
(2) Kusikilizwa na Wayahudi mbele ya baraza la Sanhedrini (Mathayo 26:57-68)
Kusikilizwa kwa mara ya kwanza na zima la Sanhedrini litakuwa lilifanyika mapema ya saa 8:00 usiku. Ingawaje hawangeweza kuendesha mabhtaka halali ya kisheria kabla ya asubuhi, viongozi wa Kiyahudi walitaka jambo hili lifanyike kwa haraka. Ingawaje uendeshwaji wa mashtaka usiku haukuwa halali kisheria, Baraza la Sanhedrini lilifanya usikilizaji usiokuwa rasmi na likamwona Yesu kuwa na hatia ya kukufuru dini na wakaamua kwamba alistahili adhabu ya kifo.
(3) Mashtaka rasmi ya Wayahudi mbele ya baraza la Sanhedrini (Luka 22:66-71)
“Wakati siku ilipowadia,” baraza la Sanhedrini lilisikiliza rasmi mashtaka kwa mujibu wa sheria, na likaamua rasmi kumhukumu Yesu kwa makosa ya kukufuru dini.
(4) Kusikilizwa mara ya kwanza na Warumi mbele ya Pilato (Luka 23:1-5; Yohana 18:28-38)
Warumi hawakuwa wametoa mamlaka kwa baraza la Sanhedrini kuwahukumu adhabu ya kifo wahalifu (Yohana 18:31). Ili wafanikiwe kupata hukumu ya kifo, viongozi wa Kiyahudi walibadilisha mashtaka yao kutoka kwenye kukufuru dini na kuwa mashtaka ya kisiasa ya kutaka kufanya mapinduzi. Walimshtaki Yesu wakisema, “Tumemwona huyu akipotosha taifa letu, na kuwazuia watu wasimpe Kaisari kodi, akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo, mfalme.”
Wakati wa msimu wa Pasaka, Wayahudi hawataweza kuingia kwenye majumba yeyote ya Warumi kwa hofu ya kunajisika, na kusababisha kuzuiwa kula Chakula cha Pasaka. Kwa kuwa watapaswa kuingia kwenye kasri la mfalme, Pilato aliendesha usikilizwaji wa mashitaka kwenye njia ya waenda kwa miguu nje ya lango la kasri ya mfalme.
(5) Mashtaka kusikilizwa na Warumi mbele ya Herode Antipasi (Luka 23:6-12)
Pilato alijua kwamba Yesu alikuwa hana hatia, lakini hakutaka kuwakasirisha viongozi wa Kiyahudi. Aliposikia kwamba Yesu “Huwataharakisha watu, akifundisha katika Uyahudi yote, tokea Galilaya mpaka huku,” Pilato akaona amepata mahali pa kukwepea ili kutoka katika huu mtanziko. Wakati wa wiki la Pasaka, Herode Antipasi, mtawala wa Galilaya, alikuwa Yerusalemu.[5] Kwa kuwa Yesu alikuwa mtu wa Galilaya, Pilato alitegemea kwamba Herode angetumika kama jaji katika shauri hili. Pilato akampeleka Yesu kwa Herode, lakini Herode alikataa kuingilia kati.
(6) Hukumu ya mwisho ya Warumi mbele ya Pilato (Mathayo 27:15-26; Luka 23:13-25; Yohana 18:39-19:16)
Wakati Yesu aliporejeshwa kwenye mahakama yake, Pilato alitafuta mbadala mwingine wa huo mtanziko. Pilato alijua kwamba Yesu alikuwa hana hatia: “Mtu huyu mmemleta kwangu kana kwamba anapotosha watu; nami, tazama, nimeamua mambo yake mbele yenu, ila sikuona kwake kosa lo lote katika mambo hayo mliyomshitaki” (Luka 23:14). Pilato hakuwa anataka amhukumu Yesu kifo, mtu aliyekuwa hana hatia.
Wakati viongozi walipomtishia kumpeleka Pilato kwa Kaisari kwa kukosa uaminifu, Pilato akahukumu kwamba haja yao ifanyike. Pilato alikuwa mtawala dhaifu. Katika mgogoro wa kwanza, Pilato aliruhusu askari kuingia Yerusalemu na sanamu ya mfalme mkuu. Kusanyiko kubwa la Wayahudi liliandamana mbele ya kasri la Pilato kwa siku tano. Alipotishia kuwauwa waandamanaji, walitangaza kwambawako tayari kufa kuliko kuiona sanamu ya Kaisari ndani ya Jiji Takatifu. Pilato alilazimika kusalimu kwa matakwa yao.
Kutokana na uzoefu huu, Pilato alikuwa na wasiwasi sana na Wayahudi. Zaidi ya hapo, mkubwa wake wa kazi kule Rumi, Sejani, hakuwa anaamini uwezo wa Pilato wa kuthibitiwatu katika nchi ya Yudea. Wakati viongozi walipotishia kumlalamikia Kaisari kama Pilato angemwachilia huru Yesu, “Basi ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulibiwe” (Yohana 19:16). Pilato akamhukumia Yesu adhabu ya kifo, siyo kwa sababu aliamini kwamba Yesu alikuwa na hatia, bali ni kwa sababu ya udhaifu wake mwenyewe.
Wakati shauri likiwa linaendelea, Petro anamkana Yesu.
Kwenye chakula cha Pasaka, Yesu alikuwa amemwonya Petro akimwambia, “Amin, amin, nakuambia, Jimbi hatawika hata wewe utakapokuwa umenikana mara tatu” (Yohana 13:38). Sasa, wakati kesi ya Yesu lilipokuwa inaendelea kusikilizwa, Petro alimkana Yesu mara tatu.
Tunaposoma kuhusu anguko hili la aibu la Petro, tunapaswa tukumbuke kwamba Petro hakuwa peke yake aliyemkosea Yesu katika usiku ule. Ni Petro na Yohana peke yao waliohudhuria kwenye kesi ile usiku ule. Wanafunzi wengine wote walikuwa wamekimbia kwa ajili ya hofu.
Ni wazi kabisa kwamba, Petro alikuwa anampenda Yesu. Lakini ni kwa nini alianguka? Awali, tulijifunza kuhusu kujaribiwa kwa Yesu ili kupata masomo ya kukabiliana na majaribu. Kutokana na anguko la Petro tunaweza kuona mambo ya kutuonya katika kutusaidia sisi kukabiliana na majaribu. Angalau sifa mbili zilichangia katika kuanguka kwa Petro:
(1) Kujiamini kupita kiasi
Wakati Yesu alipoonya kuhusu mashambulizi ya Shetani, Petro alijidai kwamba, “Wajapochukizwa wote kwa ajili yako, mimi sitachukizwa kamwe!” (Mathayo 26:35). Tunapojiamini kupita kiasi, tunakuwa kwenye hatari ya kuanguka. Tunaishi tu kwenye maisha ya ushindi ya Kikristo kupitia uweza wa Roho Mtakatifu. Kujiamini kupita kiasi ni hatua ya kwanza ya kushindwa kiroho.
(2) Ukosefu wa maombi
Akiwa Bustanini, Yesu aliwaonya wanafunzi wake, “Ombeni kwamba msiingie majaribuni” (Luka 22:40). Badala ya kuomba kwa ajili ya kupata nguvu za kukabiliana na jaribu lililokuwa linakuja mbele yake, Petro alilala.
Ukosefu wa maombi kwa vyovyote vile unapelekea anguko la kiroho. Haiwezekani kudumisha maisha endelevu ya ushindi wa Kikristo pasipokuwepo na umahiri wa maisha ya maombi. Shetani hujaribu kuwapata watumishi wa Kikristo wawajibike kwenye majukumu mbalimbali hadi kusiwepo na muda wa kuomba. Anajua kwamba kama tutakuwa hatuna muda wa kuomba kutokana na kuwajibikia majukumu yetu, haitatuchukua muda mrefu bila kuanguka.
► Rejea nyuma na uyaangalie tena maisha yako ya Kikristo na huduma. Fikiri maeneo ambayo ulianguka katika jaribu, au ni mahali gani ulipowahi kuwa karibu sana na kuanguka. Ni sababu zipi zilizokufanya uanguke au ukaribie kuanguka? Je, ulikuwa unakaribia kilele cha mafanikio katika huduma yako hata ukajiamini kupita kiasi? Je, ulikuwa unawajibika na majukumu mengi hata ukashindwa kuutumia muda wako kwa ajili ya maombi? Je, kuna mambo mengine ambayo yanaweza kutumika kama onyo katika dalili zinazoonekana kutuangusha baadaye?
Wakati shauri likiendelea kusikilizwa, Yuda anajiua.
Muda mfupi tu baada ya tukio la Petro kumkana Yesu, Mathayo anatoa maelezo ya kisa cha kujiua kwa Yuda. Alipoona matokeo ya yeye kumsaliti Yesu, Yuda aliamua kubadilisha mawazo yake akarejesha vile vipande vya fedha kwa makuhani wakuu na wazee, akisema. “Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia” (Mathayo 27:3-4). Yuda akavitupa vile vipande vya fedha alivyokuwa amelipwa kwa ajili ya usaliti wake, kisha akaondoka; akaenda akajinyonga mwenyewe (Mathayo 27:5). Yuda alichagua kujinyonga, kuliko akae na hatia katika maisha yake yote.
Maelezo ya Mathayo yanaweka toba ya Petro na majuto ya Yuda kama hali zinazokaribiana. Kaw pamojaPetro na Yuda walijutia matendo yao. Hata hivyo, Kwa ajili ya Yuda, Mathayo anatumia neno ambalo linaonyesha wazo la kubadilisha ufahamu wa mtu, na siyo la kawaida kwa ajili ya toba ya kweli.[6] Tofauti hii ni muhimu sana katika kuelewa jibu la watu wanapojisikia kwa ajili ya kutenda dhambi.
Paulo aliandika kuhusu tofauti ya majuto (huzuni inayoletwa kutokana na matokeo ya dhambi) na toba (huzuni kwa ajili ya dhambi yenyewe na badiliko la mwelekeo). Mtume Paulo aliandika, “Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti” (2 Wakorintho 7:10).
“Huzuni ya kimungu” huleta toba ya kweli, ambayo mwisho wake ni wokovu na maisha. “Huzuni ya kidunia” huleta majuto, ambayo mwisho wake ni kujisikia mwenye hatia na kifo. Wote kwa pamoja Petro na Yuda walihuzunishwa na yale waliyotenda, lakini Petro peke yake alifanya toba ya kweli.
Yuda aliona matokeo ya usaliti wake akachagua kufa kuliko kuendelea kuishi kwa ajili ya aibu na kujisikia mwenye hatia; alikuwa na majuto, lakini hakutubu. Petro aliona matokeo ya kushindwa kwake akachagua kutubu kwa ukweli. Matokeo ya majuto ya Yuda yalikuwa ni kifo; matokeo ya toba ya Petro yalikuwa ni maisha yaliyoambatana na huduma iliyozaa matunda tele.
► Je, umeshawahi kuona watu waliojisikia kujuta kwa ajili ya dhambi, lakini hawakufanya toba ya kweli? Matokeo yake yalikuwaje? Katika mahubiri yetu, tunawezaje kuwaleta watu hadi wafikie kufanya toba ya kweli?
Kusulubiwa
► Soma Mathayo 27:27-54.
Yudea palikuwa mahali pa kusikitisha kwa askari wa Kirumi akipangiwa kazi huko. Watu waliwachukia askari wa Kirumi, na wakereketwa walipanga kuwauwa. Wakati wa Pasaka, jeshi lilikuwa likiwekwa kwenye tahadhari kubwa kwa ajili ya machafuko. Hakukuwa na kazi mbaya kwa askari. Wakati mfungwa wa Kiyahudi akiwa amehukumiwa kifo, wanajeshi huimwaga hasira yao dhidi ya mtu aliyehukumiwa kifo.
Vitendo alivyofanyiwa Yesu – kupigwa, kudhihakiwa, kuvalishwa taji la miiba – kunadhihirisha ukatili wa askari walioichukia kazi yao, waliowachukia watu waliowazunguka, na waliokuwa wanafurahia wanapomwadhibu mtu ambaye hawezi kujitetea. Yesu alifikwa na mateso haya bila ya kutoa neno lolote la chuki kwa askari hawa waliomtesa.
Waandishi wengi wameitafakari taarifa ya kusulubiwa kwa kuangalia matamko saba ya Yesu akiwa pale msalabani. Maneno ya mwisho anayotoa mtu kabla hajafa huonyesha umuhimu wa huyo mtu. Akiwa anakabiliwa na kifo, Yesu alisema nini?
Walipokuwa wakimpigilia kwa misumari msalabani, Yesu aliomba, “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo” (Luka 23:34). Alionyesha upendo na kusamehe hadi mwisho wake
Kwa yule mwizi aliyestahili adhabu ya kifo, Yesu alimwahidi, “Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi” (Luka 23:43).
Maneno ya Huruma
Yesu alimwusia Yohana amwangalie mama yake wakati aliposema, “Mama, tazama, mwanao!” na kwa Yohana, “Tazama, mama yako!” (Yohana 19:26-27). Mapema kabla ya hapo, Yesu alikuwa amefundisha kwamba uhusiano wa kina wa familia ni wa kiroho, “Tazama, Mama yangu na ndugu zangu! Kwa maana ye yote atakayeyafanya mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni, huyu ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu” (Mathayo 12:49-50).
Wakati wa kifo chake, ndugu zake wa kimwili walikuwa bado hawajaamini; hawakuwa sehemu ya familia yake ya kiroho. Kwa hiyo, Yesu alimwacha mama yake chini ya uangalizi wa kaka yake wa kiroho, Yohana Mpendwa.
Maneno yaliyohusiana na kuteseka kwa mwili
Kule kuwa Mwana wa Mungu hakukumwondolea Yesu maumivu ya kimwili ya msalaba. Aliteseka kwa maumivu yote ya kimwili ya mhalifu aliyehukumiwa kifo. Baada ya kukaa kwa masaa bila ya kunywa maji katika lile joto kali, Yesu akasema, “Naona kiu” (Yohana 19:28).
Maneno ya uchungu wa kiroho
Mathayo na Marko wana kumbukumbu ya tamko moja tu, lakini haya maneno yumkini ndiyo yaliyokuwa ya kuumiza moyo zaidi kutokea pale msalabani: “Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” (Mathayo 27:46; Marko 15:34).
Kwa hakika uchungu mkubwa wa Yesu aliokuwa nao ni kutengwa na Baba yake. Baba na Mtoto waliishi kwenye ushirika ambao haujawahi kuvunjika tangu milele. Sasa kwa sababu alibeba dhambi zetu, Yesu alitengwa na Mungu.
Akiwa juu ya msalaba, Mungu “alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye” (2 Wakorintho 5:21). Katika Isaya 53, nabii alizungumzia kuhusu “mtumishi anayeteseka” ambaye atazichukua dhambi zetu (Isaya 53:4-12). Paulo anaelezea kwamba huu mbadala wa upatanisho wa Mungu na binadamu kwa maisha na kifo cha Yesu ulikamilishwa pale juu ya msalaba.
Yesu alifanyika dhambi kwa ajili yetu “ili kwamba kwa kupitia kwake tufanyike wenye haki wa Mungu. Hatupo tena kwenye utumwa wa dhambi; kupitia kifo cha Yesu, tumefanywa wenye haki. Paulo hasemi tu kwamba “katika yeye” tunaitwa wenye haki. Badala yake alisema, “ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye.” Kupitia kazi ya Yesu juu ya msalaba, mabadiliko ya kweli yanachukua nafasi. Yesu alifanyika kuwa dhambi kwa ajili yetu ili sisi tuweze kuwa wenye haki.
Maneno ya kujiweka chini ya madaraka
“Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu!” (Luka 23:46). Katika maisha yake yote, Yesu aliishi kwenye mahusiano ya uaminifu na Baba yake. Akiwa anakabiliana na msalaba, aliomba, akasema, “walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe” (Mathayo 26:39). Wakati huu alitoa tamko hili la mwisho la kujisalimisha kabisa kwenye mapenzi ya Baba yake.
Maneno ya ushindi
“Imekwisha” (Yohana 19:30). Kwa kilio hiki cha ushindi, Yesu alitangaza kwamba amemaliza kazi ambayo Baba alimtuma kuifanya. Adhabu ya dhambi ililipwa; Shetani alishindwa. Upatanisho uliokuwa unafanywa kama kivuli cha upatanisho ujao kupitia kondoo katika Agano la Kale na kuahidiwa katika Isaya 53 ulikamilishwa.
Mazishi
► Soma Mathayo 27:57-61.
Kwenye ujumbe Paulo kwa Wakorintho, alihubiri kwamba Yesu “alikufa kwa ajili dhambi zetu” na “kwamba alizikwa” (1 Wakorintho 15:3-4). Kwa Paulo na kanisa la mwanzo mazishi yalikuwa ni jambo la muhimu sana.
Wachunguzi wengi wa Wiki la Mateso wametoka kwenye Ijumaa ya Pasaka hadi kwenye Jumapili ya Pasaka. Lakini zaidi kwa ajili ya historia ya kanisa, “Jumamosi ya Pasaka” ilitambuliwa kama sehemu muhimu ya Mkesha wa Pasaka. Kuna umuhimu gani katika haya mazishi?[8]
Umuhimu wa kihistoria
Mazishi yanaonyesha kwamba Yesu ni kweli alikufa. Kinyume kabisa na madai ya dini ya Kiislamu kwamba Yesu alikuwa “amezimia” na baadaye akaamka, mazishi yanadhihirisha wazi kwamba Yesu ni kweli alikufa. Warumi walijua sana jinsi ya kumwua mfungwa aliyehukumiwa adhabu ya kifo. Hakuna uwezekano wowote kwamba wangeweza wakamchukua mtu kutoka kwenye mti aliosulubishwa kabla hajakata roho.
Zaidi ya hayo, jiwe kubwa lililokuwa langoni na walinzi wa kaburi ilikuwa ni uhakikisho kwamba hakuna mtu angeweza kutoroka kutoka kwenye kaburi. Hata kama kwa makosa Warumi watakuwa wamemzika Yesu kabla hajafa, ni jambo lisiloweza kufikirika kwamba mtu ambaye alikuwa ameumizwa na kuteseka kwa masaa ya maumivu juu ya msalaba angeweza akajifungua kutoka kwenye sanda, akasukuma jiwe kubwa lililokuwa limewekwa langoni, na kisha kukizidi nguvu na kukishinda kikosi cha walinzi waliopitia mafunzo. Mazishi yanathibitisha ukweli wa historia kwamba Yesu wa Nazarethi alikufa.
Umuhimu wa Kinabii
Akiandika kuhusu kondoo anayepelekwa kwenda kuchinjwa, Isaya aliandika, “Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake” (Isaya 53:9). Mazishi ya Yesu yalihitimisha unabii wa Masihi.
Baada ya Yesu kufa, Yusufu wa Armathaya alikwenda kwa Piato akiomba kuuchukua mwili wa Yesu. Yusufu alikuwa mjumbe katika baraza la Sanhedrini, lakini hakukubaliana na maamuzi ya kumwua Yesu. Hata baada ya kuwa viongozi wengi walimjeuka Yesu wakaenda kinyume naye, “baadhi yao walikuwa “wakiutafuta ufalme wa Mungu.” Yusufu alikuwa mmoja wa hawa wanafunzi wa siri. Yusufu na Nikodemo waliuzika mwili wa Yesu kwenye kaburi la Yusufu (Mathayo 27:57-60; Marko 15:42-46; Luka 23:50-54; Yohana 19:38-42).
Jaribu kufikiria ujasiri waliouchukua. Hata baada ya wanafunzi kuwa wamekimbia wakamwacha Yesu, Yusufu alisonga mbele kujitambulisha na mhalifu aliyehukumiwa kifo. Hii hali ya kujionyesha hivi hadharani kuliatarisha nafasi ya Yusufu kenye baraza la Sanhedrini na msimamo wake katika jamii. Kuna uwezekano mkubwa kwamba alikuja kuondolewa kwenye nafasi yake katika baraza la Sanhedrini kama gharama ya kujitambulisha hadharani na Yesu
Zaidi ya hapo, Yusufu alihatarisha hasira kutoka kwa Pilato. Maafisa wa Kirumi mara chache sana waliruhusu familia kufanya mazishi ya miili ya ndugu zao waliohukuiwa kifo kwa kusulubiwa. Miili yao ilitakiwa ibakie hapo kwa ajili wananchi wote kuona kama onyo kwa wahalifu wengine. Kibali cha Pilato ni ushahidi mwingine kwamba Pilato alijua Yesu hakuwa na hatia ya kosa lolote.
Umuhimu wa Kitheolojia
Paulo alilinganisha ubatizo wetu na mazishi ya Yesu:
[9]Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima (Warumi 6:3-4).
Mazishi yalikuwa ni uthibitisho kwa umma wa kifo cha Yesu. Kwa jinsi hiyo –hiyo, ubatizo ni uthibitisho kwa umma wa ushiriki wetu katika kifo cha Yesu. Katika ubatizo, tunatangaziwa mauti ya mfumo wetu wa maisha ya zamani.
Mazishi ni hatua ya mwisho ya kutambua kifo cha mtu. Katika nchi za Magharibi, waombolezaji hutupa udongo juu jeneza lililoshushwa kaburini ikiwa ni mwisho wa kusema “kwaheri” katika dunia hii. Paulo anaweka mkazo wa kufikia mwisho wa kifo chetu kwa sababu ya dhambi. Kama Kristo alivyokuwa amekufa, na sisi tumekufa kwa dhambi. Kurudia kwenye dhambi baada ya kuwa tumeshazikwa pamoja na Kristo ni sawa na kuchimbua mwili uliokufa. Tumezikwa na Kristo; hatuko tena hai kwa dhambi.
"Ee upendo wa Mungu, umefanya nini! Mungu wa kuishi milele amekufa kwa ajili yangu! Mwana aishiye milele pamoja na Baba aliziweka dhambi zangu zote juu ya mti.
Mungu aishie milele kwa ajili yangu amekufa: Bwana wangu, mpendwa wangu, amesulubiwa!
Amesulubiwa kwa ajili yangu na yako, kuturudisha sisi waasi kwa Mungu.
Amini, amini kumbukumbu ya kweli, wote mmenunuliwa kwa damu ya Yesu. Msamaha kwa mtiririko wote kutoka upande wake: Bwana wangu, mpendwa wangu, amesulubiwa!
Mtazame, kila kitu kinampita, Mwana wa mfalme wa maisha na amani anatokwa na damu, njooni wenye dhambi, mwoneni mkombozi wenu akifa, na mseme, ‘kulishakuwepo na huzuni tena kama yake?’ Njooni, mjisikie pamoja nami damu yake imetumika: Bwana wangu, mpendwa wangu, amesulubiwa!”
- Charles Wesley
[8]Nukuu kutoka kwa, “The Burial of Jesus.” Inapatikana kutoka https://www.alliancenet.org/tab/the-burial-of-jesus-christ-part-one on March 22, 2021
“Kurudia kwenye dhambi wakati umeshaunganishwa na Kristo ni sawa na kuchimbua mwili uliokufa.”
- James Boice
Kufufuka
Paulo alihubiri katika Korintho kuhusu msalaba; Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu na alizikwa. Kisha, Paulo akahubiri kuhusu kufufuka; Kristo alifufuka siku ya tatu na akawatokea mashuhuda wengi (1 Wakorintho 15:3-8). Kufufuka ndio msingi mkuu wa imani ya Kikristo.
► Soma Mathayo 27:62-28:15.
Mathayo 27:62-66 ni sehemu moja wapo ya matukio yangu ninayoyapenda katika maelezo ya Pasaka. Mapema, wakati viongozi wa kidini wa Kiyahudi walipomtaka Pilato abadilishe lile bango lililokuwa juu ya masalaba, aliwakatalia. Alimsulubisha Yesu chini ya bango lililosomeka, “Yesu Mnazareti, Mfalme Wa Wayahudi” (Yohana 19:19). Kwa kutumia tangazo hili kwa mtu aliyehukumiwa kifo kwa uhalifu, Pilato alikuwa akiwadhihaki Wayahudi ambao aliwakasirikia.
Baada ya kusulubiwa msalabani, viongozi wa kidini wa Kiyahudi walirudi tena kwa Pilato wakiomba walinzi wa Kirumi kulilinda kaburi:
Bwana, tumekumbuka kwamba yule mjanja alisema, alipokuwa akali hai, Baada ya siku tatu nitafufuka. Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hata siku ya tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu, Amefufuka katika wafu; na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza.
Charles Spurgeon alitoa maoni yake kwamba Pilato alikuwa akiwadhihaki tena viongozi wa kidini wa Kiyahudi wakati alipowajibu kwamba, ‘“Mna askari; nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo.’ Lakini kama kweli ndiye yeye kama alivyosema ndiye, atatoka kaburini, hata ufanye nini!”
Je, ni kweli viongozi walikuwa na mashaka kwamba wanafunzi watauiba mwili wa Yesu? Inawezekana sivyo. Waliwaona wanafunzi wakiwa wamekimbia kwa ajiliya hofu; walijua kwamba wanafunzi wake hawakuwa na ujasiri wa kuweza kuiba ule mwili. Kama huu ndio uliokuwa wasiwasi wao, baraza la Sanhedrini wangetoa amri ya kukamatwa kwa wale viongozi wa wanafunzi. Suala la wanafunzi kuwa tishio kwao halikuwepo.
Sasa, ni kwa nini waliomba huyu mlinzi? Yesu alishatabiri kwamba atafufuka kutoka katika wafu. Walishaona uwezo wake juu ya kifo wakati alipomfufua Lazaro kutoka katika wafu. Je, inawezekanaje kwamba viongozi wa Kiyahudi walikuwa na mashaka kwamba Yesu atafanya lile ambalo alikuwa ameahidi atalifanya?
Kwa kibali cha Pilato, walilitia muhuri kaburi, na wakaweka walinzi kutoka katika kampuni iliyokuwa imetuma askari kwenda kumkamata Yesu bustanini. Ghafla:
Palikuwa na tetemeko kubwa la nchi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe akalikalia. Na sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji. Na kwa kumwogopa, wale walinzi wakatetemeka, wakawa kama wafu.
Yesu alikuwa amefufuka!
► Soma Yohana 20:1-29.
Vitabu vya Injili vimeandika kumbukumbu ya kuonekana kwa Yesu baada ya kufufuka. Alionekana kwa watu wengi katika mazingira mengi tofauti.
Watu wenye kushuku mambo mara nyingine wanasema, “Wanawake waliokuwa pale kaburini walikuwa wanaota njozi. Waliona walichotegemea kukiona.” Hata hivyo, mashuhuda hawa hawakutegemea kumwona Yesu akiwa hai; walijua alikuwa amekufa. Kwa maana hawajalifahamu bado andiko, ya kwamba imempasa kufufuka (Yohana 20:9). Hata pale mashuhuda wa kwanza waliposema kwamba walimwona Yes, wanafunzi wengine walitilia shaka taarifa hiyo (Marko 16:13). Hawakumtegemea Yesu afufuke kutoka katika wafu.
Hatua kwa hatua, akajionyesha kwa Mariamu Magdalena, (Yohana 20:11-18). kwa wanafunzi wawili waliokuwa wakielekea Emmau, (Luka 24:13-32). kwa Thenashara, (Yohana 20:19-31). Ndugu zaidi ya mia tano pamoja, (1 Wakorintho 15:6). wafuasi wa Yesu walitambua kwamba ni kweli Yesu amefufuka. Kanisa la mwanzo likaanza ibada za kusifu kwa maneno haya, “Amefufuka, Amefufuka kweli kweli!”
“Nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo,” yalikuwa maagizo ya Pilato. Kitambo siyo kirefu, Pilato anatambua kwamba hakuna mtawala yeyote wa dunia hii ambaye angeweza kushinda uwezo wa Yesu wa kufufuka. Amefufuka, Amefufuka kweli kweli!
Matumizi: Huduma katika nguvu ya Msalaba na Kufufuka
Wengi wa wanatheolojia huru wamejaribu kupasisha kwamba ufufuo ni hadithi. Hata hivyo, imani ya wanafunzi ilikuwa haijajengwa kwenye “hadithi nzuri zenye mvuto wa kudumu wa maisha ya Yesu,” bali katika kweli halisi za kifo chake na kufufuka. Mitume walijua kwamba Yesu alikufa na kwamba amefufuka kutoka kwa wafu. Hii iliwapa ujasiri wa kukabiliana na mateso ikibidi hata kama ni kufa. Je, ni kwa jinsi gani kifo na kufufuka kwa Yesu kunagusa huduma zetu leo?
Kufanya Huduma ndani ya Nguvu ya Msalaba
► Soma 1 Wakorintho 1:17-2:5.
Kwenye safari yake ya pili ya umishenari, Paulo alisafiri hado Korintho akitokea Athene alipokuwa amehubiri katika Aeropagi. Inaonekana kwamba Paulo alipata matokeo kidogo sana katika huduma yake pale Athene (Matendo 17:16-34). Hakuanzisha kanisa pale Athene, na wanafalsafa wa Athene walidhihaki ujumbe wake wa kufufuka. Kutoka Athene, Paulo alisafiri kilomita sabini na tano Magharibi mwa Korintho, kwenye mji uliokuwa na ushawishi sana katika jimbo la Akaya.
Paulo alikuja hadi Korintho baada ya upinzani wa mfululilizo wa majiji matatu: Thesalonike, Beroa na Athene. Labda ndiyo maana alisema, “Nami nalikuwako kwenu katika hali ya udhaifu na hofu na matetemeko mengi.” Ingawaje wasikilizaji wa Kiyunani walikuwa wanahitaji lugha ya kushawishi na upeo wa akili inayong’ara, Paulo alikusudia kuhubiri habari za msalaba tu. Nguvu iliyokuwa katika ujumbe wake haikutokana na maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kutoka kwenye msalaba wenyewe. Paulo alihubiri “siyo kwa ufasaha wa maneno, wala kwa hekima, usije msalaba wa Kristo ukapunguzwa nguvu zake.”
Akiwa Korintho, Paulo alisema, “naliazimu nisijue neno lo lote kwenu ila Yesu Kristo, naye amesulibiwa.” Paulo alijua kwamba ujumbe wa Msalaba utawakera watu wengi.
Kwa sababu Wayahudi wanataka ishara, na Wayunani wanatafuta hekima; bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi.
Ujumbe huu ulikuwa ni “kikwazo” au “kashfa” kwa Wayahudi. Walikuwa wanataka “ishara” ambazo zilimhalalisha Masihi. Kwa akili zao, wazo kwamba mtu ambaye amesulubishwa anaweza kuwa ndiye Masihi aliyechaguliwa lilikuwa la kipumbavu. Sheria ilisema, “aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu” (Kumbukumbu la Torati 21:23). Kusema kwamba Yesu aliyeangikwa msalabani alikuwa Masihi ni kashfa nzito kwa wasikilizaji wa Kiyahudi.
Neno la msalaba kwa “mataifa lilikuwa ni upuuzi.“ Wayunani waliheshimu sana adhabu ya kifo cha mateso cha shahidi mfia dini. Ingetokea Yesu kuuawa katika mapambano dhidi ya Warumi, Wayunani mahiri wangemtunuku nishani ya heshima kwake ambaye amekuwa na ujasiri kutekeleza tendo hilo. Lakini kusulubiwa msalabani kulimwondolewa heshima kabisa mhusika; hiki hakikuwa kifo cha kuweza kumtunuku mtu heshima. Waliopatikana na adhabu ya kufa kifo cha msalaba kwa kawaida walinyimwa haki ya kuzikwa kwa heshima kama watu wengine. Miili yao iliachwa iliwe na ndege wa angani au panya, na mifupa yao kutupwa katika shimo la uchafu. Kwa hali hiyo, kudai kwamba raia wa Kiyahudi aliyehukumiwa kufa msalabani alikuwa Bwana” lilikuwa ni jambo la kipumbavu (au upuuzi) kwa wasikilizaji Mataifa.
Msalaba kwa Wayahudi ulikuwa ni “kikwazo” na kwa Mataifa ni “upuzi,” lakini Paulo alihubiri ujumbe wa msalaba bila ya kusita. Mfano wa Paulo ni wa kuigwa na sisi. Kwa wakati huu, kama ilivyokuwa katika karne ya kwanza, msalaba utawakwaza baadhi ya watu, na pia kuonekana kama ni upuuzi kwa watu wengine, lakini ndio ujumbe tunaotakiwa tuhubiri.
Ujasiri wetu kama wahudumu na viongozi wa kanisa hauji kutokana na uwezo tulio nao; ujasiri wetu uko katika msingi wa neno la msalaba. Paulo alikuwa msomi wa elimu ya juu sana, akili ya kipaji, na alikuwa na uwezo wa kuhojiana na wasomi waliobobea wa wakati wake. Lakini ujasiri wake wa mwisho ulikuwa kwenye msalaba. Tunapowapata watu kwa njia ya mahojiano ya kawaida peke yake, imani yao inaweza “kuegemea kwenye hekima ya watu”; lakini tunapowaelekeza kwenye msalaba, imani yao inabakia “kwenye uweza wa Mungu.”
Kuhudumia katika Nguvu Ya Kufufuka
► Soma Matendo 2:22-36.
Kitabu cha Matendo kinaonyesha kwamba kufufuka kulikuwa ndio kiini cha mahubiri ya Wakristoo wa mwanzo. Wakati wa Pentekoste, Petro anaonyesha kufufuka kama ushahidi kwamba Yesu alikuwa ndiye mkamilishaji wa ahadi zilizokuwa zimetolewa na manabii.
Akijitetea mwenyewe mbele ya Agripa, Paulo alitoa kauli kwamba alikuwa kwenye mashtaka “kwa ajili ya tumaini la ahadi baba zetu waliyopewa na Mungu, ambayo kabila zetu kumi na mbili wanataraji kuifikia.” Ahadi hii ilikuwa ni nini? Kufufuka. “Kwa nini limedhaniwa kwenu kuwa ni neno lisilosadikika, kwamba Mungu awafufua wafu?” (Matendo 26:6-8).
► Soma 1 Wakorintho 15:12-34.
Katika 1 Wakorintho, Paulo anaonyesha kwamba huduma yake imejengeka siyo tu kwenye nguvu ya msalaba, bali katika nguvu ya kufufuka. Paulo anatoa msisitizo kwamba mbali na kufufuka, huduma yake itakuwa haina maana yeyote. “Tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure.” Kusingekuwepo na kufufuka, Yesu angekuwa siyo chochote zaidi ya Masihi aliyeshindwa. Pasipokuwepo na kufufuka, Yesu angekuwa ni mfia dini aliyesababisha majonzi, lakini siyo Masihi aliyeahidiwa.
Kufufuka ndio msingi wa imani yetu ya Kikristo. “Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu.” Akiwa juu ya msalaba, Yesu alileta upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu, lakini ilikuwa ni ufufuo uliothibitisha nguvu ya Kristo dhidi ya kifo na dhambi. Kama hakuna ufufuo, Paulo anasema, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu.
Kufufuka ndio msingi wa matumaini yetu ya Kikristo. “Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu. Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa.” Paulo anawahakikishia Wakorintho kwamba wanayo matumaini ya kufufuka kwa sababu Kristo naye alifufuka kutoka katika wafu.
Katika karne ya pili, Lucian, mwandishi wa riwaya wa Kigiriki, aliwadhihaki Wakristo kwa ajili ya Imani yao katika kufufuka.. Alisema, “Ha maskini fukara wanashawishika kwamba wataishi milele. Kwa sababu ya hiyo, wanakidhalilisha kifo na wako tayari kutoa dhabihu maisha yao kwa ajili ya imani yao.” Lucian alikuwa akiwadihaki Wakristo, lakini maneno yake yalikuwa ya kweli. Kama Lucian alivyosema, Wakristo wa karne ya pili waliamini kwamba wataishi milele. Kwa sababu ya imani hiyo, walikuwa tayari kufa kwa ajili ya imani hiyo.
Hii inapasa iwe kweli hata wakati wa sasa. Kama kweli tunaamini kwamba Kristo amefufuka kutoka kwa wafu, itatupa ujasiri wakati wa kukutana na mateso au hata kifo. Kufufuka ndio kiini cha imani yetu ya Kikristo.
Kufufuka ndio msingi wa maisha yetu ya Kikristo. Paulo analeta matumizi ya vitendo ya kushangaza kuhusiana na imani ya kufufuka. “Wasipofufuliwa wafu, na tule, na tunywe, maana kesho tutakufa…Tumieni akili kama ipasavyo, wala msitende dhambi” (1 Wakorintho 15:32-34). Kwa mujibu wa Paulo, kufufuka kunatupa sababu muhimu ya kuishi maisha ya kimungu. Kama hakungekuweko na kufufuka, tungeweza tukaishi kama Epicureans waliosema kwamba, “Tule na tunywe kwa sababu tutakufa hvi karibuni.” Hakuna sababu ya kuishi kwa ajili ya milele kama hakuna kufufuka. Lakini, Paulo anaendelea, kwa kuwa kufufuka kupo, amka na uishi maisha yasiyokuwa na dhambi. Ushindi wetu dhidi ya dhambi unapewa msukumo na matumaini yetu katika kufufuka.
Kisa hiki cha kufufuka kinapaswa kituhukumu sisi kwa sababu ya ukosefu wetu wa imani tunapokutana na changamoto katika huduma zetu. Mara nyingi tunatarajia Mungu hatajibu maombi yetu. Kwa nini? Kwa sababu tumesahau nguvu ya kufufuka. Ni mara ngapi tunakutana na majaribu tukiwa na matumaini madogo ya kushinda? Kwa nini? Kwa sababu tunasahau ahadi ya Paulo: “Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu” (Warumi 8:11).
Kama Kristo anaishi ndani yetu, hatuishi tna katika mwili:hatuko tenakama watumwa wa dhambi. Haya ni maisha yaliyo katika nguvu ya kufufuka. Nguvu ile iliyomfufua Kristo kutoka katika kaburi inatupa ushindi wa kila siku dhidi ya dhambi. Hii ndiyo maana ya kuishi na kuhudumia kwa nguvu za kufufuka.
Hitimisho: Alama za Maisha yanayomfanania Kristo na Huduma
Je, Maisha Yako Yanafanana na Kristo?
Luka aliandika,” Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia” (Matendo 11:26). Jinsi watu walivyokuwa wanawaangalia waamini wa Antiokia walianza kusema, “Hawa watu wanafanya kama Kristo. Tuwaite ‘Wakristo.’” Ninapoisoma aya hii, mara nyingi hujiuliza mimi mwenyewe, “Je, majirani zangu wanaweza kuingia katika jina hili la “Mkristo” kwa kuiangalia tabia yangu, maneno yangu na mwenendo wangu? Je, ninaonekana kama Kristo? Waamini pale Antiokia waliishi maisha ambayo yaliakisi tabia ya Yesu Kristo; walikuwa Wakristo.
Baada ya miakamingi kama mchungaji, Dr. H.B. London kwa sasa anatumika kama mnasihi wa wachungaji vijana. Alionya kuhusu hatari za kiroho ambazo wachungaji hukutana nazo. “Mmoja anaweza kuwa karibu na vitu vitakatiu, lakini yeye mwenyewe asiwe mtakatifu. Inawezekana kuhubiri kuhusu kusamehe, na usiwe mtu wa kusamehe. Watumishi wengi wanaweza kutumia nguvu nyingi sana katika huduma kiasi kwamba wanazembea afya ya roho zao.”[1] Inawezekana kuwahubiria watu wengine kasha ukawa mtu wa kukataliwa (1 Wakorintho 9:27).
Dr. London alipendekeza baadhi ya mambo ya vitendo yanayoweza kuwasaidia wachungaji kuepukana na kushindwa kiroho wakati wanapoongoza watu wengine. Haya ni maeneo ambayo yanaweza kutusaidia kudumisha maisha yanayomfanania Kristo. Aliandika kama ifuatavyo:
Ishi kile unachokihubiri. Usihubirie watu wengine kile ambacho wewe hujakifanyia kazi kwanza kwenye maisha yako mwenyewe
Jali nafsi yako. Madaktari wengine hawana afya. Wanajali kuangalia afya za watu wengine na wanazembea kuangalia afya zao wenyewe. Baadhi ya wachungaji hawana afya ya kiroho. Kama mchungaji, tumia muda wako kutunza afya yako ya kiroho.
Kuwa mnyenyekevu. Kumbuka kwamba mchungaji ni kama mchungaji wa kondoo, na siyo raisi wa benki. Kuwa mtumishi
Jiongeze katika mambo yanayokatisha tamaa. Utakatishwa tama katika huduma. Mtu Yule unayemnasihi atakwenda kinyume chako. Rafiki yako wa karibu atakujeuka. Wafuasi wa kanisa lako watakukataa. Usiruhusu mambo haya ya kukatisha tamaa yakufanye upoteze matumaini. Yuda alimsaliti Yesu. Dema alimsaliti Paulo. Kupitia maombi ya machozi, endelea kukua na kulichunga kundi lako la kondoo.
Je, Huduma yako inamfanania Kristo?
Katika masomo haya ya maisha na huduma ya Yesu, tumeona tabia nyingi zahuduma ya Yesu. Je, tabia hizi zinaonekana katika huduma yako?
Hapa kuna maswali ya kujiuliza katika kufanya tathmini ya huduma yako:
Je, wenye dhambi wanatubu? Wakati Yesu alipohubiri, watu walipokea maisha mapya. Je, wewe unawaleta watu kwenye maisha mapya ya wokovu?
Je, waamini wanajazwa na Roho Mtakatifu? Yesu aliahidi “kumtuma Roho” kwa watoto wake, Je, ahadi hii inakamilishwa miongoni mwa wale unaowahudumia?
Je Shetani anashindwa? Je, ngome kuu za Shetani zinavunjwa? Huduma ya Yesu ilifahamika kwa kuwa na mamlaka ya kiroho.
Je, watu walioumizwa wanapata uponyaji? Je, familia zilizosambaratika zinapata suluhisho la marejeano? Je, maisha yaliyoharibika yanarejeshwa tena kwa upya? Je, mahusiano yaliyoharibika yanarejeshwa? Yesu aliwaponya watu waliokuwa wameumizwa kimwili, kimhemuko na vidonda vya kiroho.
Je watu wanaona neema na ukweli? Je, ninawavutia watu kuja kwa Yesu au ninawatolea nje mbali na Yesu? Yesu alifundisha ukweli ulioleta kujisikia mwenye hatia na neema.
► Unapokuwa katika kujadili maswali haya, angalia maeneo ambayo huduma yako inaweza ikakua katika kumfanania Kristo. Kumbuka kwamba kila mhudumu anao uwanja wa kukulia, kwahiyo chukua orodha hii kama changamoto yako ya kukulia kuliko kuifanya iwe ya kukuhukumu wewe mwenyewe.
[1]H. B. London, They Call Me Pastor. (Grand Rapids: Baker Books, 2000), 145)
Kazi za Somo la 8
(1) Andaa mahubiri au somo la Biblia kuhusu Maneno Saba ya Msalabani. Wekea mkazo wa ujumbe wa maneno haya ya Yesu kwa Wakristo wakati wa sasa.
(2) Andaa mahubiri au somo la Biblia kuhusu maana ya kufufuka kwa maisha ya kila siku ya Mkristo. Tumia kwa pamoja maelezo ya kufufuka kutoka katika Vitabu vya Injili na maneno ya Paulo katika 1 Wakorintho 15:15-17 kwenye maandalizi yako.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.